Ninah Sehemu ya Tano
IMEANDIKWA NA: CHANDE ABDALLAH
********************************************************************************
Chombezo: Ninah
Sehemu ya Tano (5)
“sikia, sipo kwa ajili ya fedha kwa mr Edgar, na nitakuthibitishia hilo, kwa kuwa nitaolewa naye akiwa hivyohivyo, na sitataka hata robo ya mali zenu,”nilisema Tsoza akanitazama vizuri kisha akasema: “ nakupa fursa ya mwisho, wewe kahaba, nitakuongeza dollar 2000.”
Aisee kusikia neno hilo nilikasirika na kutaka kumvaa, lakini nilianza kulia, Mama Sele akaingilia na kuuliza kulikoni, Tsoza akaondoka zake kwa dharau.
Muda si mrefu nikiwa naugulia tusi la Tsoza tukaitwa kumtazama mgonjwa maana alikuwa ameanza kuongea, na mtu wa kwanza kuniulizia ilikuwa ni mimi.
NINAH 43
Niliingia mle wodini kwa aibu Mungu tu ndiye aliyekuwa akifahamu kilichokuwa kikiendelea ndani ya nafsi yangu. Nilimkuta Mr Edgar amelala kitandani, madripu yakimmiminikia kwenye mishipa yake ya damu, alinitazama na kuongea kwa shida huku mdomo wake ukiwa umepinda kwa pembeni.
Aliongea kwa tabu sana lakini nilimsikia vyema.
“Ninah..nenda kamtafute Brighton..” wakati anasema hivyo nikajikuta naangusha michozi mfululizo.
“siwezi Mr Edgar, siwezi, nitakuwa na wewe zaidi sasa kuliko muda wowote,” nilisema kwa tabu.
“sikutaki Ninah ondoka!” aliongea kwa hasira kidogo Mr Edgar, lakini sikutaka kuondoka wala nini, na hapo hapo Tsoza akaingia mle ndani, alionekana kunichukia wazi kutokea mwanzo.
“Nadhani hataki hela anataka roho yako, brother!” aliongea Tsoza akimwambia Mr Edgar.
Niligundua Mr Edgar alimtazama Tsoza kwa jicho kali mno Tsoza hakuonekana kujali sana kuhusu kaka yake kuugua, maana alikuwa akiniandama mno.
“nimeshangaa sana, jinsi gani mtu mwenye nguvu zake, kuanguka kisa kahaba huyu, kwani umri wako wote huo hujawahi kuona wanawake wazuri?” Tsoza alianza kuongea kwa dharau, akimwambia kaka yake.
“Sio kahaba, kuwa na heshima Tsoza!” alisema Mr Edgar akijitahidi kuongea kwa sauti yake ya mwisho.
“Niambie nielewe brother; hivi mwanamke gani atakayekubali kuwa na wewe ambaye huwezi hata kupanda mtungi, kama siyo kwa ajili ya hela zako! Niamini kaka ulikuwa unachunwa! Kama siyo niambie ni nini kilichokufanya ukapoteza fahamu na kupata stroke, kama siyo umemkuta na mwanaume mwingine,” aliongea Tsoza alikiwa anaukaribia ukweli kabisa, isipokuwa tu hakuwa ananitendea haki kwa sababu mwanzoni niliangukia kwa Mr Edgar kwa sababu ya Brighton, lakini nilipoamua kumpenda, Brighton akaibuka tena. Ndiyo anaweza kuniita kahaba, lakini siyo kahaba ; Ananionea.
Wakati huo Mr Edgar alionekana kujaa hasira lakini mwili wake uligoma kufanya chochote, akatulia tu akimtazama Tsoza kwa ghadhabu, iliniuma maana japo kuwa alikuwa amelala kitandani kwa ugonjwa niliomsababishia lakini alionekana kuwa tayari kunitetea tena na tena.
Ninah 44
“Tsoza, nimefanya kosa kama msichana, kiasi cha Mr Edgar kuishia hapa kitandani, nastahili kulaumiwa, lakini sipo tayari kuitwa kahaba na nitafanya chochote ili kulipia makosa niliyomfanyia kaka yako ili usinione kahaba machoni mwako!” nilisema kwa hasira lakini kwa kulalamika.
“utafanya kitu gani?” aliongea Tsoza kwa kebehi.
“kwanza tulikuwa tumepanga kuvishana pete na baada ya hapo tulipanga tuoane, na yote hayo nitayafanya,” nilisema huku nikiwa najua fika kuwa ni mtihani mkubwa najipa lakini sikuwa na budi, maana nimelikoroga lazima nilinywe hata kama halina sukari.
“wooh subiri kwanza, najua unapoelekea, unataka uoane na kaka yangu ukijua kuwa ukiwa naye kama mkewe utaingia kwenye mirathi kirahisi ndiyo? Nasikia wanawake wa kitanzania ndiyo biashara yenu siku hizi! Hamjui kutofautisha kati ya penzi na hela. Ndiyo maana ukawaacha wanaume wote saizi yako ukamchagua mzee kama huyu, ukijifanya kumvumilia matatizo yake yote kisa tu upate hela si ndiyo! Sitaki hiyo ndoa wala uchumba wenu. Kesho namchukua kaka naondoka naye Sauz na wewe nimekupa ofa ya hela, umekataa it’s over goldigger!” alifoka Tsoza.
“Sikia, sipo kwa ajili ya hela zozote wala mirathi yenu, kama huamini tuwekeane makubaliano kabisa kuwa sitataka kuingia kwenye mirathi yenu kivyovyote, tafadhali Tsoza, Mr Edgar alikuwa mkarimu na mwema kwangu, nikamkosea, naomba nilipie makosa yangu!” nilisema na kulia juu, huwezi amini Tsoza alinitazama kwa mshangao mno.
“Ooh sawa nimekubali tutasaini makubaliano yote, hata hivyo wewe unatufaa kuwa mdada wa kazi, maana hatuna mtu wa kumuangalia akiwa nyumbani, huko ndiyo tutaona umetengenezwa kwa udongo gani!” alisema Tsoza na kuondoka.
Mr Edgar akashangaa maneno yangu, nikamsogelea kwa sababu alikuwa akiongea kwa sauti ya chini.
“Ninah, sitaki… ondoka, unafanya nini?”
“hapana, MR Edgar nitatumia muda wangu kuhakikisha unatimiza ndoto ulizotaka kuzitimiza ukiwa na mimi, umeshateseka sana na mapenzi, sitaki moyo wako uniorodheshe na mimi pia kama mtesi wako!” nilisema kwa kauli thabiti.
“Hapana, Ninah; usiwe kama mimi, tumia muda wako kufurahia penzi lako na unayeamini unampenda, siyo mimi tafadhali. Huoni sina umbo tena?.” Alisema Mr Edgar.
“nimejifunza kitu kimoja Mr Edgar, siyo kila unayempenda utampata, wengi wametengana na wanaowapenda na mioyo yao inawauma hadi hivi leo, mimi ni nani hadi nijifanye nayajua mapenzi zaidi?” nilisema na kuondoka nikiwapisha wafanyakazi wenzake walioonekana kuwa na shauku kweli ya kumuona bosi wao.
“Ninah kila kitu kipo sawa!” aliniuliza Mama Sele wakati tunaondoka na kuelekea hotelini maana Mr Edgar alilipia mwezi mzima mbele hivyo hakukuwa na gharama yoyote zaidi.
Ikabidi nianze kumuhadithia Mama Sele kuanzia mwanzo hadi nilipofikia, alishangaa mno. Akanipa moyo kuwa hata yeye angekuwa katika hali ngumu wakati ule angefanya uamuzi kama wangu wa kutembea na Mr Edgar, isitoshe aliniambia hakuna mwanamke ambaye angefanya tofauti na nilivyofanya mimi kutokana na mazingira yaliyonikuta.
Nikapata moyo, tena akaniambia kwa muda huo sikupaswa kumtelekeza Mr Edgar kwa ajili ya Brighton ambaye yeye kwa kosa moja tu hata hakunisamehe.
“Usijifikirie vibaya hata kidogo, ni makosa ya Brighton pia lakini kwa sababu mwanamke wa kutupiwa lawama za usaliti siku zote, ndiyo maana amekuwa mgumu kukusamehe, lakini usijali achana naye na kwa sasa hutakiwi kufanya kosa lolote, mjali Mr Edgar Mungu atakulipia, hata kama huyo mdogo wake atakuvunja moyo kiasi gani,” alisema mama Sele.
Nilimshukuru mno maana kiukweli sikuwahi kudhania kuwa atawahi kuongea na mimi maneno yenye busara na kutia moyo kama hayo.
Asubuhi yake kama kawaida nilienda hospitali kumuona Mr Edgar, kama kawaida nilikutana na Tsoza aliyenisalimia angalau vizuri kidogo tofauti na siku iliyopita.
“Aaah Ninah! Kesho tutasafiri kuelekea Sauz, kaka atatibiwa kule, na kama umeazimia kufanya ulichokuwa unakitaka, niambie nikakate tiketi na kufanya utaratibu mwingine ukiwemo kusaini zile karatasi tulizoambiana kuwa hautapata chochote hata kama utaolewa na kaka yangu,” alisema Tsoza.
“Nimesema nitakuwa na Mr Edgar popote, na hizo karatasi nipe nisaini hata sasa,” nilisema kwa uhakika zaidi.
NINAH 46
“Ooh okey, tutaandaa utaratibu tukifika Sauz, kwa sasa kaongee na mpenzi wako,” alisema kwa kebehi Tsoza, nikaingia kwa Mr Edgar lakini hakuwa akiongea chochote, zaidi ule mdomo wake na uso mzima upande wa kulia ukiwa umemshuka kuashiria kuwa haufanyi kazi.
Ilinitisha mno. Jioni ile nakumbuka Brighton alinipigia na kuniuliza kulikoni, nikamtaarifu kila kitu kilichotokea. Akaonekana kunisikitikia, nikamshukuru kwa kuniunganisha na ndugu wa Mr Edgar na kukata simu nikiwa sijamwambia mipango yangu niliyoazimia kuifanya.
Zaidi kuanzia siku hiyo nilihakikisha sitaongea tena na Brighton, nikabadili kila kitu na kujipanga kufuta kichwani kumbukumbu zote za Brighton nilizokuwa nazo.
Nikakumbuka mateso yote niliyopitia Tandale, nilivyogombana na ndugu zangu kwa sababu yake, lakini hadi kufikia hatua ya kutembea na Mr Edgar kwa ajili yake, roho ikanitumbukia nyongo kuhusu Brighton japo nilishindwa kumfuta akilini nikaweza kumuwekea kama alama ya ghadhabu zangu na siyo kama mpenzi wa moyo wangu tena.
Kweli ilipofika siku iliyofuata, tulisafiri kuelekea Johannesburg na moja kwa moja kuingia katika jumba la kifahari ambapo Tsoza aliniambia kuwa hiyo ni moja ya nyumba za Mr Edgar.
Wakati huo Mr Edgar, akiwa kwenye kiti cha gurudumu nilimburuza mwenyewe kutoka kwenye gari hadi ndani ya jumba hilo lililokuwa kimya na pekee akiwa mlinzi tu mlangoni tu.
“Ninah, umetaka mwenyewe hii, sasa, wewe ndiye utakuwa ukimtazama Mr Edgar kwa kila kitu, ukiwa na tatizo lolote nipigie. Kila siku nitajitahidi kuja.” Alisema Tsoza kama nilivyokwambia taratibu alianza kuniongelesha kistaarabu tofauti na mwanzoni.
Nilikagua jumba zima na kujionea utajiri wa Mr Edgar hadi nikashangaa. Nakumbuka kipindi hicho ilikuwa baridi mno hivyo nikajifunza kuzoea mazingira haraka na kuhakikisha namhudumia Mr Edgar kuanzia kumuogesha kumfulia, kumsafisha, kumfanyisha mazoezi, kumlisha kumpikia kusafisha nyumba na mambo mengi mno. Kifupi kama Tsoza alivyosema nilikuwa msaidizi, yaani zaidi ya Hausigeli.
NINAH 47
Sikukataka kukata tamaa wala kukimbia, nikajipa moyo kama niliteseka kwenye shida huko Tandale miezi kibao hadi kufikia hatua ya kuuza miguu ya kuku na mlo mmoja, sitaweza kukata tamaa kwa Mr Edgar.
Nilikuwa mimi tu na Mr Edgar peke yetu yapata wiki sasa, Tsoza hakuja pale nyumbani na mimi wala sikumpigia simu, siku nzima nikiongea na Mr Edgar tu nikijitahidi kumchekesha na kumsahaulisha kuwa alikuwa akiumwa chochote. Mwenyewe mara kwa mara alikuwa akinishukuru na kuongea kwa tabu kuwa amekuwa na furaha mno katika kipindi hicho kigumu cha maisha yake tena alidai kuwa ni zaidi ya ndoto ya kuoana aliyokuwa anaiota kila siku.
Na mimi nilimhakikishia kuwa sitaondoka karibu yake. Akafurahi na kulala kwa amani nikiwa nimemkumbatia nyuma yake.
Nilimaliza wiki ya pili sasa, na ikabidi nimtafute Tsoza ili nimkumbushe ile ahadi ya mimi na Mr Edgar kuoana kama tulivyopanga ikiwa pamoja na kusaini hayo makubaliano kama tulivyopanga kuwa sitataka chochote kutoka kwao.
Nilipompigia alikuwa kama vile amesahau hivi, ikabidi nimkumbushe vizuri akaniambia nisijali kwani angeshughulikia jambo hilo haraka.
Na mimi nikatulia tu kusubiri, siku ya pili yake tu nilishangaa mlinzi anamfungulia mlango mama mmoja mtu mzima kidogo, ambaye aliingia ndani na gari yake na kushuka harakaharaka akitembea kuingia mle ndani.
Nilimsalimia lakini alinitazama vizuri kuanzia chini hadi juu kwa jicho kali, akanisonya na kumuulizia Mr Edgar, nilishangaa lakini kwa heshima tu nikamuonesha chumba alichopo akatangulia harakaharaka tena akionekana anaijua vizuri ramani ya jumba hilo. Nikamfuata kwa nyuma ili nihakikishe yeye ni nani hasa na ana shida gani na Mr Edgar.
Yule mama alipofika alimtazama Mr Edgar akimzungukazunguka na kuongea maneno ya Kizulu ambayo mimi sikuwa nafahamu, Mr Edgar naye akamjibu. Yule mama bado alikuwa akinitazama kwa jicho kali akizungumza kama vile alikuwa akiniongelea mimi. Kisha akaondoka zake haraka.
Ikabidi nimuulize Mr Edgar aliyefika hapo ni nani.
Akaniambia kuwa ni mtalaka wake yaani aliyekuwa mkewe wa ndoa.
NINAH 48
Ndiye yule aliyeniambia kuwa mara kadhaa alikuwa akimsaliti na kutoka nje ya ndoa hadi kufikia hatua ya kuomba talaka.
“Ameshangaa kukuona, alidhania ni uongo. Ameuliza nakulipa shilingi ngapi ili uwe na mimi katika hali hii! Nimemwambia sikupi chochote ndiyo amekasirika na kuondoka. Usimjali achana naye na tafadhali niitie mlinzi nimwambie huyu asiingie tena hapa,” alisema Mr Edgar.
Nikajichekea moyoni kuwa kumbe habari zangu zimesambaa hadi kumtikisa mtalaka wake! Lakini ni kweli inabidi akate mguu wake asije tena hapa kwa sababu Mr Edgar sasa ni wa kwangu na alikuwa akiniuma vilevile.
Basi baada ya tukio hilo, siku ya pili yake Tsoza alifika, kwanza alishangaa nyumba ikiwa safi, halafu na kaka yake akiwa anaendelea vizuri tu ingawa bado alikuwa akitembelea kile kiti cha magurudumu, akanitazama kwa muda nadhani alikuwa akinishangaa kwa vile nimesimamia kauli yangu kuwa nimeamua kuwa na kaka yake bila kuhitaji chochote.
“Ninah nilikuwa sikuamini na nimekuwa nikikuchukulia vibaya, leo naomba mbele ya kaka hapa nikuombe msamaha,” alisema Tsoza, lakini Mr Edgar kama kawaida alionekana haongei sana mbele ya mdogo wake na hata walivyoangaliana kulikuwa kama kuna kitu kinaendelea kati yao, lakini niliwaacha tu maana mambo mengine ni ya ndugu si yangu kuyaingilia.
“Nimekusamehe shem, usijali,” niliongea kwa tabasamu pana nadhani ni kwa mara ya kwanza tangu matatizo ya Mr Edgar yatokee.
Siku ile Tsoza akaniambia atanitembeza mjini kuona mazingira na mimi nilikubali kwa sababu ni kweli tangu nifike Sauz sikuwahi hata kukanyaga nje ya jumba la Mr Edgar na nilitamani kutoka kwa kweli japo Mr Edgar alionekana kutaka kupinga lakini mdogo wake akamsisitiza kuwa haitachukua muda mrefu.
Hivyo basi nilijiandaa na kuvaa nguo zangu tukaondoka tukitalii Johanesburg na kuzungukia vivutio kadhaa, jiji ni kubwa na zuri mno, nilipiga picha kadhaa kwenye simu yangu kuweka kumbukumbu, giza lilipoingia tu nilimuomba Tsoza anirudishe nyumbani, lakini wakati tunarudi, kuna watu wawili waliokuwa na silaha mkononi walituvamia mimi nikawekwa chiniya ulinzi na Tsoza pia.
Itaendelea..
NINAH 49
Nilifunikwa kitambaa cheusi na kupakizwa kwenye gari nikiwa sielewi moja wala mbili, kote huko nikisikia wakiongea kizulu tu na kucheka; niliogopa mno.
Nilishushwa kwenye jumba moja hivi bovubovu, nikafungwa kwenye kiti na kutolewa kitambaa usoni nikashangaa kuona nimezungukwa na wanaume kadhaa wengine wakinishikashika mwilini, huku wakiongea kilugha chao, nikajua moja kwa moja walitaka kunibaka.
Wakati huo kwa mshangao nilimuona yule mama ambaye Mr Edgar alisema ni mkewe akija pale ndani lakini cha ajabu alikuwa na Tsoza kwa kuwatazama tu walionekana wamenichezea mchezo.
“Ninah, wewe ndiye msichana unayetaka kuchukua urithi wa wanangu kutoka kwa baba yao, si ndiyo?” aliniuliza kwa kiingereza yule mama akionekana ana ghadhabu mno.
“Hapana, mbona nilishasema kuwa sitataka chochote?” nililia na kwa hofu.
“hutaki chochote? Hahaaa! Sikia mimi siyo mpumbavu,unajua sheria wewe?” aliniuliza.
Nikatikisa kichwa nikiwa sijui hata nimesema hapana au ndiyo.
“Mimi siyo mjinga unajifanya sasa hivi unakataa lakini najua ukiolewa tu na Mr Edgar hata kama utasaini hizo karatasi za kusema hautachukua mirathi, bado unaweza kutugeuka na kwenda mahakamani ukapata haki yako, kwa sababu mahakama inamtambua mke wa halali kama mrithi wa lazima hata kama hajajumuishwa kwenye mirathi. Ulijua ukiwa mke lazima apate urithi wake ndiyo maana ulijipanga kusafiri hadi huku ukijifanya unampenda, mshenzi wewe. Ulidhani utapunguza urithi wa wanangu kwa mtindo huo si ndiyo?” alisema yule mama, nikashangaa maana hata sheria yenyewe sijui kama ilikuwa hivyo.
Nilitoa macho na kuishia kukataa tu, machozi yakinitiririka kwa uoga. Nikamtazama Tsoza ambaye ndiye pekee niliyekuwa namjua nikamuomba amueleweshe huyo mama kuwa sikuwa na nia mbaya, lakini Tsoza alinicheka tu.
Yule mama akanisogelea karibu na kulichana gauni langu kuanzia kifuani, akaanza kunikagua matiti na kunipapasa ngozi yangu, akamtazama Tsoza na kuongea maneno fulani wakacheka wote. Nilishindwa kujistiri kwa sababu nilifungwa kwa nguvu sana pale kwenye kiti hivyo nikawa video ya burebure kwa wale wanaume mle ndani maana nilikuwa kifua wazi na hiyo ilinidhalilisha mno.
NINAH 50
Nikajua tu hapo lazima kinachofuatia ni kubakwa na kundi lote hilo la wanaume kisha wakanitupa mtaani.
Niliomba Mungu hilo lisitokee, lakini kila saa zilipoenda nikawa nazidi kuwa hatarini, maana yule Mama aliondoka na Tsoza na kuniacha na lile kundi la wahuni;niliogopa hadi nikajikojolea nikafumba macho kwa nguvu sikutaka kuyafumbua hata kidogo.
Nilishangaa tu nikichomwa sindano sijui ilikuwa na nini ndani yake. Nikapoteza fahamu taratibu.
Nilikuja kushtuka nikiamshwa na mtu niliyekuwa na uhakika ninamfahamu.
He! alikuwa ni binamu yangu, Rose yule aliyenizima mkufu, nikashangaa mno. Tena niliamka nikiwa kwenye kitanda ndani ya chumba ambacho ndani yake niliona vitanda vingi mno vingine vikiwa na wasichana kama mimi.
“Rose!” niliongea kwa mshtuko mno nikawa sielewi nipo Bongo au Sauz na hiyo ilikuwa siku gani.
“Shiiii! Ninah, sikia na unisikilize kwa makini sana, sijui yalikukuta mambo gani, lakini umeletwa hapa na mwanaume mmoja rafiki wa mume wangu, hapa siyo pazuri kabisa hivyo leo hiihii natakiwa nikutoroshe urudi Tanzania, Sawa!” aliongea Rose kwa kunong’ona tena akionekana ana wasiwasi mno.
“Rose kwani mbona unanitisha!” nilisema nikiingia uoga tena kwa maneno yake, kuwa pale sio pazuri tena na yeye mwenyewe alivyokuwa akizungumza kwa kunong’ona huku akitazama kila upande alizidi kunitisha mno.
Kabla hajamaliza nikasikia sauti ya kiume ikimuita:“Rose” akaitika lakini alichofanya akaniambia nisimame akanimwagia maji machafu ya mapovu yaliyokuwa pembeni sabuni ikaniingia machoni huku baridi likinipiga ile mbaya, nikawa siwezi kutazama mbele nikabakia nalia tu, bila kujua kwanini Rose amenifanyia vile.
Kidogo hatua za huyo mtu aliyekuwa akimuita Rose ziliingia mle ndani.
“Rose! Huyu ndiye aliyeletwa na Tsoza?” ilisema sauti ile ya kiutuuzima, ikabidi nitulie sasa na kusikiliza kwa makini.
“Ndiyo lakini ni mbaya sana ana makovu uso mzima, halafu ni mchafu, sidhani kama ataweza kuwa klabu aagh!,” alisema Rose nikajua alikuwa akitunga uongo.
“Agh shit! Basi sawa achana naye,” alisema yule mtu na kuondoka zake.
NINAH 51
Wakati huo Rose akanichukua hadi bafuni na kunipa maji nikanawa akanipa na nguo, kisha akaniomba radhi kwa alichokifanya na kusema ilikuwa ni lazima afanye hivyo ili yule mwanaume aliyeingia mle ndani ni ambaye kumbe ndio mumewewe, asinione usoni.
Kwa mujibu wa maelezo yake kumbe huyo mumewe ambaye ni mtu mzima aliyemuoa, ni mfanyabiashara mkubwa wa Club za usiku, Sauzi na Dubai, na kwenye biashara zake mara nyingi huwatumia wasichana wazuri kama mastripper, yaani wacheza uchi.
Wengi wao ni wasichana wanaotekwa kutoka nchi mbalimbali Africa na yeye huwanunua na kuwatumikisha kwa muda fulani kwa fedha kidogo na makazi, kisha baada ya muda huwabadilisha ili biashara yake izidi kufanya vizuri kwa kila siku kuwa na warembo wapya.
Kwa hiyo hata mimi nilikuwa mmoja wao isingekuwa sijakutana na Rose. Sasa kibaya zaidi alinichana wazi kuwa huyo mumewe ana tabia ya kutembea na wasichana wowote wazuri atakaowaona na hakuwa akimheshimu kwa lolote na mara kadhaa alimnyanyasa sana kutokana na hela zake, hivyo akaniambia kama huyo mumewe angeniona nilivyo mzuri asingeniachia.
Nikashangaa mno jinsi watu wanavyoteswa na mapenzi, yaani inamaana huyo mumewe japokuwa mtu mzima lakini alikuwa akifanya ngono na wanawake wengine mbele ya Rose na Rose alivumilia kisa ameolewa na tajiri,Loh! nikajiona bora yangu mara mbili zaidi.
“Ninah tuondoke hapa haraka sitaki ujulikane kama ulikuwa humu, maana kwanza akijua wewe ni ndugu yangu na umejua siri yake ndio hatari zaidi. Bora tu nifanye mpango urudi nyumbani; lakini umefikaje hapa, Brighton yupo wapi?” aliniuliza Rose wakati huo tukitembea haraka kuhama jengo moja korido moja hadi nyingine mpaka tukatoka nje nikiwa nimeinamisha kichwa chini.
Kusema kweli, bado nilikuwa kwenye mshtuko hivyo sikuweza kumsimulia zaidi ya kumwambia neno moja tu: “Mkufu.”
“Ninah mkufu ndiyo nini, umefanyaje?” aliniuliza akishangaa mno.
“Mkufu wako Rose ndiyo umenifanya niwe hapa,” nilisema kinyonge.
NINAH 52
“Nini? sikuelewi Ninah,” alishangaa Rose ikabidi nimuelezee kuanzia mwanzo hadi mwisho jinsi mkufu ulivyotusotesha mimi na Brighton hadi nilivyopata vishawishi na kuingia kwenye penzi la mtu mzima, nilivyoachana na Brighton, nilivyoingia Sauz na kuuzwa hapo.
Kote huko Rose alikuwa kimya tu akiguna palipomstaajabisha; akasikitika palipomsikitisha na kulia palipomliza.
“Hahaa Ninah, ungejua loh, nakusikitikia,” alisema Rose akitikisa kichwa na kucheka humohumo.
Nikawa hata mimi sielewi maana ya yeye kufanya mambo yale.
Alichonielezea nilitamani kuzimia.
“Ninah ule mkufu ile siyo dhahabu halisi ni English Gold na lile jiwe siyo Ruby ni kichupa, thamani yake kutengeneza haizidi laki mbili, Umefanya nini Ninah, kwanini hukusema! Jamani polee sana Ninah polee!” alisema Rose nikashtuka mno nikitamani kulia, kucheka, kujizomea na kila kitu kwa pamoja.
“Hapana Rose siyo kweli niliuona ule mkufu kwa macho yangu na najua Replica, lakini siyo uleule ni Original,” nilisema, ingawa Rose akazidi kucheka,machozi yakimtoka na kunipa pole zaidi na zaidi.
“Ninah, ule mkufu mimi ndiyo nilimlipia mama dukani, naujua thamani yake,” alisema kwa uhakika Rose nikashushuka dunia nzima ikinizomea.
Kumbuka hapo tulitumia milioni 78 na kufikia hatua ya kujifilisi kabisa mali zetu zote, hata kupelekea matatizo yote yaliyonikuta, halafu Rose anasema nini?
Nilichanganyikiwa kwa kweli, lakini nikapata wazo palepale.
“Basi Rose hakijaharibika kitu, naomba basi nipe huo mkufu nikauuze nikanunue huo wa Replica niwarudishie,” nilisema kwa shauku hapo nikapiga mahesabu harakaharaka kichwani pindi nitakapopata huo mkufu,nitarudisha heshima yetu na kumwambia Brighton pengine tuta.. tutaaa….; kabla sijamaliza kufikiria unajua Rose alichonijibu? maana alinikata maini kabisa na kuyamenyea vitunguu saumu.
“Jamani Ninah, mkufu wenyewe niliutoa kama zawadi kwenye engagement kwa wifi yangu yaani dada yake mume wangu, Anaitwa Bokamoso. Halafu.. loh! aliyemvisha pete mwenyewe ndiye Tsoza huyu aliyekuleta kwa mume wangu. Mungu wangu, Ninah!hapana lazima ule mkufu tuupate,” alisema Rose akiwa ametoa macho.
THE END
Also, read other stories from SIMULIZI;