Roho ya Paka Sehemu ya Tano
NEW AUDIO

Ep 05: Roho ya Paka

SIMULIZI Roho ya Paka
Roho ya Paka Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA


Simulizi : Roho Ya Paka

Sehemu ya Tano (5)

Si kawaida ya ninja kukodiwa kwa kazi ya aina hii. Lakini dunia ilikuwa imebadilika kitambo. Akiwa ametulia hotelini kwake mjiniCalifornia, asubuhi hiyo alifuatwa na ajenti wake ambaye alimwambia kuwa kuna kazi ya kufanya nje ya nchi.

“Wapi?”

“Afrika”

“Nchi gani?”

“Tanzania”

Hakujua Tanzania. Kwa ujumla nchi za Afrika alizozifahamu ni Naijeria na Cameroon kwa ajili ya mpira; Uganda kwa ajili ya vituko vya Idd Amin, Kenya kwaajili ya utalii na Afrika Kusini kwa ajili ya Mandela Tanzania haikuwemo kabisa katika ramani ya kichwani.

Lakini baada ya kukutana na watu hao waliomuhitaji, ambao nusura wamfanye aangue kicheko kwa maumbile yao, alijikuta akiijua Tanzania. Ilikuwa baada ya kutajiwa jina la mtu ambaye alitakiwa wamkamate, Joram Kiango, alikuwa hajamsahau. Hakuwa na uwezo wa kusahau kipigo ambacho “nyani” huyo anayejiita Joram Kiango alimpa, kipigo cha kwanza katika maisha yake. Hivyo, aliafiki mara moja.

Kumkamata Joram lilikuwa jukumu la pili la kwanza lilikuwa kumfuta duniani “nyani” mwingine anayeitwa Kakakuona, kwa kosa la kushindwa kumpata Joram na kuhatarisha harakati zao kwa kufanya mauaji kwa fujo, kimachomacho. Jukumu hilo alilitekeleza kwa urahisi sana, hasa baada ya kuandaliwa silaha safi ya aina yake, ambayo alikuwa akiisikia tu katika simulizi za kihistoria. Kidole chake cha shahada kilipoifyatua bunduki hiyo na kumfanya binadamu, ambaye alikuwa kando ya barabara, atoweke kama tufe la barafu, lililoyeyuka ghafla, alijisikia kama mungu.

Baada ya kazi hiyo ndipo alipotakiwa kumnasa Inspekta Kombora ambaye waajiri wake walidai kuwa anajitia “kimbelembele” ambacho kinawea kuwaharibia mipango yao kabla hawajampata Joram. Haikuwa kazi kubwa kumtia mikononi. Wakiwa na hakika kuwa makachero wake wanaichunguza nyumba hiyo kwa uficho, na wakiyasikiliza maongezi yake baina yake na vijana wake, ingawa walitegemea mfasiri kuwafahamisha kwa kiingereza, iliwagharimu kutumia hila za kizamani, ya kupakia sanduku katika pick up na mara wakamsikia akimwambia kachero wake kuwa anakuja.

Tatizo pekee katika kumnasa Kombora ni pale alipotokea mtu ambaye hakujulikana na kuanza kupambana naye. Number one hakumtegemea. Na zaidi alishangazwa na uwezo wake wa kupigana ambao ulimfanya ashindwe kuamini kuwa anapambana na binadamu wa kawaida kwani hakuna binadamu wa kawaida ambaye alipata kumpa shida kama huyu. Wingi wa watu ambao walianza kujazana na ufupi wa muda aliokuwa nao, vilimfanya Number one atumie njia ya uoga, ya kupiga lile bomu la moshi unaowasha, na kuitumia fursa hiyo kuwachukua mateka wake na kuwarejesha mjini.

Ni wakati alipokuwa akiendesha pick up hiyo kurudi mjini, ndipo ilipomjia akilini kuwa aliyekuwa akipambana naye hakuwa mwingine ila ni Joram Kiango. Miaka mingi waliyotengana ilimfanya aanze kumsahau lakini asingeusahau upiganaji wake usio kifani. Alijilaumu kuruhusu, kwa mara nyingine, aponyoke toka mikononi mwake kama samaki aliyepenya toka kinywani mwa mamba. ‘mwanaharamu yule, ama zake ama zangu,’ aliwaza akiwageukia Philip na Paul ambao walikuwa wakiendelea kusema kitu ambacho hakuwa amekisikia.

“Tunasema twende huko ghalani tukaone madhara yaliyosababishwa.” Paul alisema akiingia nyuma ya benzi lao na kufuatiwa na Philip. Number one ambaye jina lake lingine la bandia katika hati ya usafiri lilikuwa Newton Kelly, aliingia mbele na kulitia moto gari.

Ingawa alikuwa na siku tatu tu tangu alipoingia Dar es Salaam, lakini ramani alizopewa na jinsi alivyoutumia muda huo mfupi kulivinjari jiji tayari alikwishakuwa mwenyeji. Hakuhitaji kuelekezwa, wala hakusubiri kuamriwa afuate njia ipi. Badala yake alikanyaga petrol na kuacha gari liteleze kuifuata UWT na baadaye, Maktaba, hadi Samora ambako aliichukua uhuru na kuambaa nayo hadi Buguruni. Alipofika Mandela alipinda kulia na kuelekea Tabata.

Toka hapo macho yao yalivutwa na moto mkubwa ambao uliufanya usiku huo uonekane mchana. Philip na Paul hawakuyaamini macho yao walipoona kuwa moto huo ulikuwa ukiiteketeza hazina yao yote, hazina ambayo pia ilikuwa ndoto yao pekee ambayo waliiweka akilini kwa miaka zaidi ya sita na kuigharamia kwa kila senti waliyokua nayo. Waliutazama moto huo kwa huzuni, hisia zao zikionyesha ni miili yao inayoteketea katika majengo hayo, badala ya mafuta ya kujipaka na vipodozi. Mmoja wao alitokwa na sauti ya kilio bila machozi, hali mwingine alitokwa na machozi bila kilio.

Number one aliwatazama kwa mshangao jinsi walivyobadilika. Alitamani kucheka lakini hakuthubutu. Alitamani kuwahurumia, lakini hakujisikia. Hakuona vipi tukio kama hilo, kwa wafanyakazi wakubwa kama wao, liwe kama mwisho wa dunia. “Kwani hamna bima?” aliwauliza. Hakuna aliyemjibu. Badala yake Philip alimgeukia na kumkazia macho. Baada ya muda, kama anayezungumza peke yake, alisema, “Najua hii ni kazi ya Joram Kiango. Mwanaharamu, kwa mara nyingine ametutia kilema. Kwa bahati mbaya safari hii ametutia kilema cha moyo badala ya mwili. Unasemaje Paul?”

Paul aliendelea kulia.

Philip akamrudia Number one, “Kelly” kwa mara ya kwanza alimwita kwa jina lake, kinyume na maafikiano yao.

“Tumekuhaidi ngapi kwa kutuletea Joram Kiango?”

Number one hakukumbuka. Tangu alipojua kuwa mtu wake ni Joram kiango alijikuta amesahau malipo ya kazi hiyo na kuifanya yake binafsi, kwa nia ya kulipa kisasi.

“Ngapi?” Philip alirudia. “Okey pengine hamna haja ya kutaja. Ninachosema ni hiki. Tunamtaka Joram Kiango usiku huu huu; awe hai au amekufa. Tutakulipa mara kumi ya chochote tulichokuhaidi. Upo?”

Number one alikubali kwa kichwa.

“Usiku wa leo.” Philip alisisitiza. Kabla ya kesho tutakuambia wapi amejificha. Unasemaje Paul?


Joram Kiango pia alikuwa ameapa kuwa usiku huohuo angemaliza “unyama huu wa kipuuzi.” Mara tu alipohakikisha moto aliouanzisha umepamba moto, alifika mjini na kuliegesha gari lake mbele ya kiwanda cha printpak. Kisha, akatembea kwa mguu kurudi hotelini kwake ambako alikisikiliza chombo chake cha kupokelea ujumbe wa simu zake.

Akafahamu kuwa Inspekta Kombora alikuwa hajarudi na kwamba vijana wake walikuwa wakitapatapa kwa “kutoweka” huko kwa afande wao. Aidha, mtu wake wa kampuni ya simu alimwarifu kuwa bado ilikuwa vigumu kunasa maongezi ya ofisi ya Kangaroo kutokana na mitambo iliyotengwa kuepusha jambo hilo. Habari alizotegemea toka nje juu ya wakurugenzi wa Kangaroo zilikuwa bado hazijapatikana. Akakitegesha tena chombo hicho na kusimama.

Uchovu aliokuwa nao haukuwa na kifani; alitamani kuingia bafuni aoge. Alikitamani kitanda chake, lakini hakuweza kufanya lolote kati ya hayo kila alipokuwa akiitazama saa yake ilikuwa ikimkera kuona mapambazuko yakikaribia. Hivyo, alijinyoosha, akachunguza vifaa vyake vyote vilikuwa kamili katika mifuko yake ya siri. Kisha, akakifunga chumba chake na kutoka.

Hakuhitaji gari, alipenya vinjia vya uchochoroni na akiiendea ofisi ya Kangaroo. Nyumba mbili kabla ya kuifikia ofisi hiyo, alitafuta uchochoro na kujificha, macho yake yakiwa kazini kulitazama jengo hilo kwa makini.

Matumaini ya Joram yalikuwa kwamba taarifa za kuungua kwa maghala yao zitakapowafikia wakurugenzi hao wasingesita kutoka kwenda kutazama uharibifu uliotokea. Fursa hiyo alihitaji ili aingie katika jengo hilo na kumtoa Nuru kabla hajawashughulikia wendawazimu hao.

Kama alivyotegemea, haikupita robo saa kabla hajaona benzi likitoka eneo hilo kwa mwendo wa kasi kuifuata UWT. Aliwapa dakika tano kisha aliiendea ofisi na kushughulikia geti ambalo halikumchukua dakika mbili. Alilifunga nyuma yake na kuliendea lango akipenya katika kivuli cha michongoma.

Joram alikuwa na taarifa zote jinsi jengo hilo linavyolindwa kwa umeme. Alifahamu fika kuwa kwa kugusa mlango au dirisha ovyo angekuwa amejichongea kwa kutoa ishara ambayo ingeweza kuwafikia wakurugenzi hao huko huko waliko na hata kituo cha polisi. Hali kadhalika, alijua kuwa ndani ya jengo hilo kuna milango ya siri ambayo isingeweza kufunguka bila ya kujua hila ambazo hutumiwa. Ni hayo ambayo yalimfanya Joram ahitaji ramani za jengo hilo au mhandisi aliyelishughulikia. Lakini baada ya kusikia kilichomtokea mhandisi huyo, na kunasa maongezi ya kikosi cha Kombora juu ya ramani ya jengo hilo, hakuona kama alikuwa na muda wa kutosha zaidi ya kufanya kile ambacho waingereza ukiita short in the dark, kujituma kazini.

Kwa mujibu wa taarifa za kikosi cha Kombora, na kile alichokiona mwenyewe Kakakuona alipojituma kupitia jengo la Sunrise na kutokea Kangaroo, Joram alikuwa na uhakika kuwa nyuma au chini ya meza kulikuwa na njia ya siri ambayo ama ilifunguka kwa kubonyeza tufe lililofichwa ukutani au kwa chombo maalumu cha mkononi. Joram hakupenda kupitia njia hiyo kwa kuhofia kupotezewa muda na makachero wa Kombora ambao pia wangeweza kumharibia mambo. Hali kadhalika, alijua jicho la adui linatazama upande huo baada ya Kakakuona kukorofisha. Hivyo, aliamua kutumia mlango wa mbele.

Akiwa amejiandaa kwa vifaa vya umeme, Joram alitafuta hadi alipopata nyaya za umeme. Alizifuata hadi zinapoungana na zile za ndani. Akashughulika nazo kwa dakika kadhaa na kufanikisha kutegesha chombo chake maalumu ambacho kina nguvu ya kuvuruga mpangilio wote wa vifaa vya umeme katika jengo kiasi cha mitambo iliyotegeshwa kushindwa kufanya kazi. Baada ya hapo alitumia funguo zake malaya kufungua ofisi hiyo na kuingia. Alihofia kuwasha taa za umeme ambazo zilikuwa zimezimwa. Akatumia tochi yake ndogo yenye ukubwa wa kalamu kumulika hapa na pale hadi alipoipata ofisi ya wakurugenzi. Alihangaika na makasha mbalimbali na kupekua nyaraka hizi na zile hadi alipoona kuwa alikuwa akiupoteza bure muda wake. Akageuka ukutani na kumulika hapa na pale, akipapasa hapa na kutomasa pale hadi alipata kitu alichokuwa akikihitaji. Picha moja ukutani hapo ilikuwa imficha tufe moja lenye namba toka 0 hadi 9. Joram alicheza na namba hizo kwa dakika kama kumi. Wakati akikaribia kukata tamaa, kama ndoto, aliona nusu ya ukuta huo ikimeguka na kumruhusu kuingia katika chumba kipana, cha siri. Hicho ndicho chumba alichokihitaji.

“wewe malaya, inuka hapo ulipo, kuja hapa,” sauti yenye mkwaruzo , iliyojaa chuki na hasira ilimwashiria Nuru.

Ilikuwa sauti Philip, Paul akiwa nyuma yake. Ndio kwanza walikuwa wamerejea toka kushuhudia hasara kubwa waliyoipata. Wakiwa wamejawa na hasira, akili yao ilikuwa najambo moja tu akilini, kuua, hawakuweza kushuku chochote walipoingia katika jengo lao hilo; kupita katika ofisi ya siri hadi katika chumba cha mateso.

Nuru alijikongoja kuinuka toka sakafuni alipolala, kando ya Kombora. Akawaendea na kusimama mbele yao akitetemeka. Hasira zilimjaa moyoni, lakini macho yake yalijaa upole yakiomba kitu ambacho akili yake haikumruhusu kutamka. Kilio chake kilikuwa wazi machoni mwa Philip na Paul. Pamoja na hasira zilizowajaa rohoni, walitazamana, wakacheka.

“Unataka chakula chako sio?” Philip alimkebehi, “Leo hutapata chakula chako, mama. Tunakutaka uwe mzima na akili zako zote ili ufe huku unaona. Usikie kila ladha ya kifo hadi roho yako itakapokutoka. Upo mpenzi?”

“Na nitakuambia jambo jingine la kupendeza,” Paul aliongeza. “Kabla hujafa utashuhudia kifo cha hawara yako Joram Kiango. Wakati wowote kuanzia sasa ataletwa hapa akiwa hai au maiti. Tutapenda umpatie busu la mwisho kabla hamjaagana na kuanza safari yenu ya mwisho ya kwenda motoni.”

Inspekta Kombora aliyasikia yote hayo hali kalala chali juu ya sakafu. Alikuwa akilaani kila dakika ambayo ilikuwa ikimfanya aendelee kuwa shahidi wa unyama huo bila uwezo wa kufanya lolote. Aliiona bastola moja iliyoshikwa kizembe katika mkono mmoja wa Paul. Angeweza kabisa kuipokonya bastola hiyo kirahisi na kisha kuvifumua vichwa vyao wote wawili kabla hawajajua kinachowatokea. Kilichomzuia kufanya hivyo ni hali aliyokuwa nayo. Sindano waliyomchoma mara tu alipozinduka baada ya lile joto la kutisha ilimlegeza kila kiungo na kumlegeza akili. Alijiona kama dubwana ambalo lingeweza kuambiwa “lala vizuri tukuchinje” likalala bila kipingamizi. Pamoja na ukweli kwamba alijaribu kupambana na hali hiyo, bado alijua fika kuwa anajidanganya. Hakuwa na hali.

Hilo Kombora alilifahamu tangu alipoona miili ya vijana wake ikiburuzwa kama mizoga ya mbwa na kutumbukizwa ndani ya shimo chumbani humo. Shimo hilo, mara tu lilipofunuliwa liliruhusu harufu mbaya isiyostahimilika ambayo iliashiria kuwepo kwa maiti nyingine nyingi zilizoachwa kuozea humo. Alijaribu kuinuka awatetee vijana wake. Hakuweza. Alipojaribu kufoka sauti haikutoka. Alichoambulia ni kutoa macho tu, kama kondoo.

“Unajua kwanini mnakufa leo?” Philip aliendelea kumsimanga Nuru, “Mnakufa kwaajili ya roho zenu mbaya. Mnakufa kwaajili ya tamaa yenu ya fisi. Mnakufa kwakua nyie sio watu, ni mijibwa tu isiyostahili kuishi.”

“Inatosha Philip, inatosha sana. Huna haja tena ya kuendelea kumnyanyasa msichana huyo asiye na hatia yoyote,” Sauti kubwa, iliyowazi na inayojiamini ilisikika ghafla chumbani humo na kuwafanya Philip na Paul watazamane kwa hofu kubwa.

Ilikuwa sauti ambayo kamwe Nuru asingeweza kuisahau, sauti ya mtu aliyempenda zaidi ya alivyojipenda mwenyewe. Sauti ya Joram Kiango. Ilimfanya Nuru ahisi akipata nguvu mpya.

Mara sehemu ya ukuta chumbani humo ikamenyeka. Umbo refu, lililokakamaa; la Joram Kiango likaingia taratibu, hatua moja baada ya nyingine. Akiwa amevaa suti yake nyeusi, iliyochafuka kwa mavumbi machoni mwa Nuru alionekana mchovu kupita kiasi, lakini macho yake yalikuwa maangavu yakitoa nuru ambayo Nuru asingeweza kuisahau kila aionapo; Nuru ya ushindi. Mkononi alikuwa na bastola ambayo ilimwelekea Philip, lakini hakuijali sana. Alimwendea taratibu na kusimama mbele yake. Akamtazama kwa muda mrefu. Kisha alikizungusha kichwa chake na kumpokonya bastola hiyo ambayo aliitumbukiza katika moja ya mifuko yake. “wewe, umeingiaje humu ndani?” Philip alifoka baada ya kupigwa na butwaa muda mrefu.

“Wewe ni Joram kiango?” Paul naye alipata sauti yake.

“Naam, nadhani mlikuwa mkinitarajia kwa muda mrefu. Sioni kwanini mshangae kuniona,” Joram aliwajibu kwa kebehi huku akiwatazama.

Macho yao yalijaa chuki, hasira na kisasi kwa kiwango ambacho Joram hakupata kukiona. Hata hivyo, ilikuwa dhahiri kuwa hawakuwa na uwezo wa kufanya lolote, hasa baada ya ngao yao kubwa, ambayo ilitokana na mitambo yao ya umeme waliyoiamini kubomolewa. Walitazamana. Kisha, wakatazama huko na huko kama wanaotarajia msaada. Mmoja wao alifyonza na kutema mate.

Joram aliwapuuza akamwendea Nuru na kumkumbatia. Alichokiona katika macho yake kilimtisha. Hakuwa Nuru aliyemfahamu, Nuru ambaye siku zote alikuwa sharp kwa maneno na vitendo. Nuru huyu macho yake yalionekana kana kwamba yuko maili elfu moja nje ya chumba hicho. Ingawa alimtambua Joram lakini alionekana kama amemwona katika ndoto, si katika dunia halisi. Hata mwili wake, Joram alipomkubatia ilikuwa kama aliyekumbatia zombie au maiti yanayotembea.

Hali hiyo iliamsha upya hasira za Joram “Mmemtendea haya msichana huyu?” alimwuliza kwa sauti ndogo ambayo, kwa anayeifahamu ilikuwa kali, yenye hasira zake siku zote. Mmemfanya nini mpenzi wangu? Vizuri. Muda si mrefu baadaye mtajuta kuzaliwa. Nilitegemea niwafikishe katika vyombo vya sheria, lakini sioni kama kuna haja ya kufanya hivyo. Nitawaadhibu mimi mwenyewe, kwa njia ninazofahamu mimi.”

Alimwendea inspekta Kombora na kumtazama machoni. Hali yake haikutofautiana sana na ya Nuru. Kombora aliduwaa, akamtazama Joram bila kuonyesha dalili zozote za kuelewa kama amekuja kummaliza au kumwokoa.

Joram hakuhitaji kuambiwa kuwa walikuwa wamepewa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya,Sedative Hyprotics, kama Mandrax na mengineyo ambayo yaliwapumbaza miili na akili. Baada ya kuitazama hali yao kwa muda, Joram alijikuta akibuni njia ya kuweza kuwachangamsha walao kwa muda. Miongoni mwa vitu vyake vya siri ambavyo hutembea navyo siku zote ni pamoja na vidonge vya kuongeza nguvu, kuhamasisha mwili na kutoa maumivu, vichocheo ambavyo ni mchanganyiko wa Cocaine, Amphetamine, Heroine na mengineyo. Ingawa matumizi ya dawa hizo pia hayaruhusiwi bila ushauri wa daktari, Joram, kwa nadra sana alizitumia kila ilipobidi; na mara nyingi zilimsaidia. Alitoa vidonge viwiliviwili kati ya hivyo na kuwapa Nuru na Kombora.

“Samahani, mkitoka hapa mtakwenda Muhimbili, watarekebisha afya zenu.” Aliwaeleza wakati akiwashawishi kumeza.

Philip na Paul walijaribu kutumia fursa hiyo kutoroka. Walinyata kuiendea sehemu ya kubonyeza tufe ili wafungue lango na kutoka. Hawakujua jinsi Joram alivyo mwepesi. Aliwaona bila kugeuza kichwa chake. Na kabla hawajabonyeza tufe hilo, alikwisha ruka na kuwachota teke moja ambalo liliwapeleka chini wote wawili, kama magunia.

“Bado nina shughuli na nyinyi,” aliwaambia akiwaburuza katikati ya chumba.

Alipowarejea Nuru na Kombora walionekana wakianza kuchamgamka. Dakika moja baadaye Nuru alitamka kile ambacho roho yake ilitamani kukitamka muda mrefu “Joram!”

Alisogea na kumkumbatia tena, machozi yakianza kumtiririka.

Joram alimbusu na kumfuta machozi huku akisema, “Wewe ni msichana mkubwa Nuru. Unafahamu kabisa kuwa huu sio muda wa kutokwa na machozi. Bado tuna kazi ya kufanya.”

Pamoja na kuanza kuchangamka, Inspekta Kombora alionekana mnyonge sana. Alijitahidi kukwepa macho ya Joram, kila alipomtazama. Joram akiwa mtu anayemfahamu fika mzee huyo, alijua kuwa alikuwa akikionea aibu kitendo chake cha kupatikana kirahisi na maadui hao kuruhusu vijana wake wauwawe mbele yake na kuaibishwa mbele ya Joram na Nuru. Joram alimpa maneno ya mzaha ambayo yalimfanya asahau aibu hiyo, aamke na kuanza kuwachunguza maadui hao. “Viumbe duni na dhaifu hawa wamewezaje kufanya unyama wote huu” Kombora aliuliza na kumtazama Joram kwa mshangao.

“pesa.”

“pesa?”

“Wanapesa nyingi sijapata kuona. Katika ofisi yao nimepata akaunti yao ya siri ambayo ina pesa inayotosha kulisha jeshi letu zima kwa miaka miwili.”

Alimsimulia Kombora uchunguzi alioufanya katika chumba hicho ambao ulimfanya atetemeke baada ya kugundua kuwa walikuwa wakipambana na watu ambao wanaweza kuiharibu Tanzania na kuiweka katika msiba usiomithilika hapa duniani.

“Sijapata kuona binadamu wenye mioyo ya kinyama kama hawa, Inspekta Kombora. Wangeifanya Tanzania liwe taifa la kusikitisha, lenye machozi na majonzi yasiyo na mwisho kwa miaka nenda rudi. Mbinu waliyobuni, ambayo haijapata kutumiwa na mtu yeyote duniani, kwa kiwango kikubwa, ilikuwa imekwishafanikiwa. Hasira na chuki waliyonayo dhidi yangu pengine ndiyo iliyowaharibia. Walitaka wahakikishe wanashuhudia kifo au maiti yangu kabla hawajaanza rasmi harakati zao za kishetani,” Joram alieleza na kumwuliza Kombora, “Inspekta si unawakumbuka wale marehemu ambao mlipata maiti zao na kukuta nyuso zao zikiwa zimeliwa nyama na kubakia mafuvu?”

Kombora aliitikia kwa kichwa.

“Basi yale yalikuwa majaribio tu. Ama yalifanywa kimachomacho mno ili kufikisha ujumbe kwangu. Hali ya marehemu wale ndio ingewatokea watanzania wengi, wake kwa waume, katika sura na miili yao. Lakini ingetokea taratibu, hatua kwa hatua, baada ya miezi mitatu au minne ya matumizi ya perfume, mafuta, sabuni, poda na vipodozi vingine mbalimbali ambavyo viumbe hawa wameingiza nchini.” Joram alisita kidogo na kutazama jinsi taarifa hiyo ilivyopokelewa na Kombora kwa hasira iliyochanganyika na hofu.

“Vipodozi hivyo ambavyo wamevipa jina Glamour ni sumu kali sana ambayo imefanyiwa utafiti wa miaka mingi, kwa gharama kubwa, hadi ilipoonekana ipo tayari ndipo imewekwa katika mafuta, perfume, cream, sabuni n.k ambazo zina harufu nzuri sana tofauti kabisa na matokeo ambayo yatafuata baada ya miaka mitatu, yasiyo na dawa, ikizingatiwa kuwa tayari sumu hiyo itakuwa imeenea mwilini na hakuna daktari ambaye amejiandaa.”

Kwa Kombora ilikuwa kama ambaye tayari ameshuhudia maafa hayo, kama ambaye tayari anauona msululu wa watu waliokata tamaa mbele ya madaktari walioduwaa, huku vilio vikisikika toka katika kila nyumba na kila mtaa. Aidha, aliona majeneza mengi yakipelekwa katika viwanja vya makaburi ambayo tayari vilikuwa vimefurika.

Kombora aliweza hata kuhisi harufu iliyotapakaa katika kila nyumba harufu ya uozo, harufu ya nyama, sura na miili ya wasichana wazuri ambao wanaoza taratibu huku wakiwa hai, hadi pale wanapokata tamaa na kusalimu amri ya kifo. Kana kwamba anayasoma mawazo yake, Joram kiango aliongeza ghafla, “Naamini mpango wao haukufanikiwa. Maghala yao mawili ambayo yalikuwa yamefurika mali zikisubiri zianze kutawanywa kote nchini, baada ya matangazo mengi katika vyombo vya habari, nimeyateketeza kwa moto. Kila kitu kimegeuka jivu, mizigo yao ambayo ipo bandarini, ambayo nashuku pia ina bidhaa za aina hii, kama nilivyoona katika hati zao za siri, pia haitawafikia wananchi. Itateketezwa kabla vibaka hawajaiba hata kopo moja.”

Kombora alishusha pumzi kabla hajasema, “Mambo yote umenieleza, Joram, kama ilivyokawaida yako umenitafunia na umeacha nimeze tu. Hata hivyo, kuna mawili hujaniambia. La kwanza hujaniambia adui yangu mkubwa zaidi ni nani, Kakakuona yuko wapi. Usiniambie kuwa amekuponyoka kwasababu ningependa kushuhudia kifo chake kwa macho yangu, kama si kumwua kwa mkono wangu.”

“Kakakuona tayari amekufa,” Joram alimjibu.

“Amekufa! Amekufa lini?

“Ni hadithi ndefu Inspekta. Tutaizungumza baadaye. Kuhusu swali lako la pili, nadhani unataka nikwambie hawa viumbe ni kina nani na wanahusika vipi na mkasa huu wa kutisha. Au sio Nuru?” alisita akimtazama Nuru na Inspekta Kombora kwa zamu, kisha akaendelea, “Hiyo ni hadithi nyingine ndefu, ningeshauri tutoke katika chumba hiki cha mauti twende katika ofisi ya kifahari ya wakurugenzi hawa ambamo tutaketi na kuzungumza kwa utulivu kabla hatujawakabidhi watu hawa kwa vijana wako ambao watajua la kuwafanya.”

“Kuwakabidhi?” Kombora alifoka ghafla. “Niwakabidhi kwa mtu mwingine watu kama hawa! Sikiliza Joram, mwanangu. Naweza kuwa mtu ninayeheshimika sana kisheria. Naweza pia kuwa mtu aliyeajiriwa kwa kuhakikisha sheria zinafuatwa. Lakini sio kwa suala la mashetani kama haya. Hawa, niliapa nitawauwa kwa mikono yangu,na ni hilo nitakalolifanya.” Aliwatazama Nuru na Joram kwa zamu. kisha, akauelekeza mkono wake kwenye shimo ambalo lilikuwa likiendelea kutoa harufu mbaya za maiti.

“Mnaliona shimo lile? Watu hawa wamelitumia shimo lile kuangamiza watu wengi wasio na hatia. Shimo lilelile litakuwa kaburi lao. Na nitawazika ili waisheherekee kila kila dakika ya safari yao kuelekea kuzimu.” Baada ya kusema hayo, bila kutaka ushauri wa Joram wala Nuru, alimwendea Philip na kumpiga teke moja ambalo lilimfanya aanguke kando ya shimo hilo, damu zikimvuja puani na mdomoni. Teke la pili, ambalo bila shaka liliuvunja mguu wake mzima, lilimfanya aviringike na kutumbukia shimoni humo kuungana na maiti nyingine.

Paul alianza kutetemeka hata kabla ya Kombora hajamfikia. Kwa jicho lake kali, ambalo lilijaa kisasi, alimtazama Joram kwa muda mrefu hadi Kombora alipompiga ngumi iliyomfanya ateme meno mawili na kuvunjika pua. Huku bado akimtazama Joram, badala ya Kombora aliyekuwa akimwadhibu, aliangukia shimoni kama mzoga. Kwa msaada wa Joram, Kombora aliitoa miili ya vijana wake wawili. Kisha, wakafunga mlango wa shimo hilo ambao ulifanya ionekane kama sakafu ya kawaida.

“Msijali” kombora aliwaambia, akiwatazama Jorama na Nuru. “Kwa hili nipo tayari kujieleza hata mbele ya mungu.”

Nuru na Joram walitazamana kisha, kwa sauti ndogo Nuru akamwambia, “Tuondokeni katika chumba hiki. Ni chumba cha mauti, hakitufai.”

Joram aliendea tufe la ukutani na kulibonyeza. Ukuta ukafunguka na kuwaruhusu kuingia katika ofisi safi ya wakurugenzi hao ambao walikuwa wakitapatapa chini ya ardhi kwa kukosa hewa safi. Wakaufunga nyuma, Joram akiwa amemshika Nuru mkono, aliwaongoza hadi juu ya viti ambako waliketi.

Ndio kwanza wakafahamu kuwa kulikuwa kumepambazuka. Nuru toka nje kupitia katika vioo, ambavyo viliruhusu kuona nje hali mtu wa nje hawezi kuona ndani, iliwawezesha kuona kundi dogo la polisi wenye silaha wakiwa wamelizingira jengo hilo. Kiongozi wao, akiwa na kipaza sauti mkononi, alikuwa akizungumza kitu fulani mara kwa mara kabla hawajalivamia. Kundi kubwa la raia walionekana wakiwa wamesimama nyuma ya askari hao wakitazama kwa macho yanayouliza, kulikoni!

Joram aliwapuuza watu hao wa nje. Akainuka na kuiendea ofisi ya mkurugenzi mtendaji na kuketi juu ya kiti chake cha starehe. “Kisasi ni kitu cha ajabu sana” Joram alianza kuamini.

“Nuru” alimwita akimtazama. “Unaweza kuamini kuwa hawa watu wawili ni binadamu pekee walionusurika katika jengo ambalo lilikuwa na ile mitambo iliyokuwa ikiendesha satelaiti ya ajabu ya Afrika Kusini ambayo ilikuwa isababishe ile mioto ya ajabu ajabu katika nchi za mstari wa mbele?”

“Philip na Paul walikuwa miongoni mwa mainjinia waliokuwa wakiiongoza mitambo hiyo. Ni wao pekee walionusurika kufa, baada ya moto tuliouanzisha kuteketeza kila mtu na kila kitu,” aliogeza.

Hakuna mtu ambaye angeweza kulisahau tukio hilo. Kombora asingesahau jinsi yeye, na kila Mtanzania, alivyokuwa roho mkononi, akisubiri maafa ambayo yaliandaliwa na serikali ya kidhalimu iliyokuwa ikiongoza nchi wakati huo. Nuru asingeweza kusahau yaliyomkuta. Asingesahau alivyoonja kifo baada ya mateso na kudhalilishwa kusiko na kifani. Ingawa yeye na Joram walitoka kama washindi na mashujaa wa Afrika na dunia nzima, bado tukio hilo ambalo limeandikwa vitabuni kwa lugha mbalimbali kama Tutarudi na Roho Zetu? Na Zero Hour bado kila anapolikumbuka, Nuru hujisikia kichefuchefu.

“Kwa nini hukuniambia kabla Joram?” aliuliza taratibu. “Nisingeacha wabakie hai humo shimoni.”

“Hawako hai.” Kombora alijibu. “Wamekufa taratibu, kifo ambacho kinawastahili kabisa.”

Joram aliendelea, “Ilivyotokea ni kwamba, baada ya wale jamaa kupona majeraha yao walijaribu kujihusisha tena na mipango ileile. Na kwakuwa jambo lile lilikuwa la siri sana likiwa limetengewa mamilioni ya pesa ambazo wao walikuwa miongoni mwa walioruhusiwa kuzitumia benki, walichofanya ilikuwa kuhamisha pesa hizo na kuziweka Marekani kwa majina yao. Wakati huo harakati za ukombozi nchini humo zilizidi kupamba moto, na hatimaye Mandela kuchukua urahisi baada ya kutoka kifungoni. Hasira zao juu ya mtu mweusi zilizidi. Na walizielekeza hasira hizo kwangu kwa kudhani kuwa nimesaidia kuwafanya washindwe na Watanzania wote kwa kuamini kuwa wamechangia kuwezesha ubaguzi utokomezwe, hivyo, wakabuni njia mbalimbali hadi walipopata msaada wa wanasayansi ambao walifanikisha jaribio la kutengeneza sumu ambayo ilikuwa almanusura iangamize Tanzania.”

“Nadhani wameona kuwa Tanzania bado si nchi ya kuchezea,” Kombora alisema.

“Nadhani,” Joram alisema akijiuliza mangapi zaidi amweleze Kombora. Katika uchunguzi wake alipata namba za akaunti za watu hao ambazo alikuwa tayari kumpa Kombora. Pia alipata nyaraka nyingi za siri ambazo angempa ili zimsaidie kukamilisha kazi yake.

Lakini katika uchunguzi huohuo aligundua uficho wa siri katika ofisi hiyo, ambao ulikuwa na mamilioni ya pesa taslimu za nje na za kigeni. Hilo asingemwambia Kombora kwani alipangakuzihamisha usiku utakapoingia. Aidha, kwa kumuhurumia mzee huyo alivyochoka hakupenda kumsimulia muda huo juu ya kiumbe wa hatari kuliko Kakakuona, mwenye taaluma kamili ya ninja, ambaye yuko mahali fulani, akisubiri. Joram aliamua kuwa hilo pia liwe siri yake hadi atakapolishughulikia.

Akiwa na hakika kuwa Kombora na jeshi lake hata wapekue jengo hilo mara ngapi wasingeweza kuzifikia pesa hizo aliinuka na kumshika Nuru mkono. “Nadhani huyu msichana amechoka. Anahitaji kupumzika. Kila kitu unachohitaji kiko humu. Kwa hiyo, nadhani utaturuhusu twende zetu.” Alipiga hatua mbili tatu kuuendea mlango, kisha akamgeukia Kombora na kumwuliza, “Kwa jinsi watu walivyojaa huko nje, unaonaje, nani aanze kutoka. Wewe au mimi na Nuru?”

Mamia ya watu walioduwaa nje ya jengo hilo walishangaa kuona mlango ukifunguka taratibu na kumruhusu kijana mmoja mkakamavu na msichana kuanza kuondoka. Mvulana akiwa katika suti yake nyeusi, isipokuwa kwa vumbi kidogo, katika mavazi yake alionekana mtanashati kama ambaye anatoka katika jumba la starehe kinyume na watu waliokuwa nje walivyoamini. Lakini msichana alikuwa taabani, kachakaa mwili na mavazi kama aliyetoroka kuzimu. Alitembea kwa kujikongoja huku akipata msaada wa mkono wa mvulana uliomshika kiuno.

Sura za vijana hawa zilikuwa maarufu nchini kama zilivyomashuhuri kote duniani. Haukupita muda kabla ya watu waliokuwa hapo nje hawajaanza kunong’ona, “Ni joram Kiango!”

“Ndiyo. Na Nuru”

Polisi ambao walianza kuziweka silaha zao sawa kuwaelekea, walipowafahamu walizirudisha makwapani na kusimama kwa utulivu. Mmoja wao saluti ilimtoka, na Joram akapokea kwa kutabasamu kidogo. Kabla askari hao hawajajua wafanye nini na Joram, bosi wao, Inspekta Kombora, alitokea, na askari wote wakamkimbilia.

Yeye pia alikuwa taabani kama Nuru. Nguo zake zilichakaa na kuchafuka, mwili wake ulijaa marejaha, macho yake yalilegea kana kwamba alikuwa amekesha akinywa pombe kali. Akiushikilia ukuta alitembea taratibu na kuzipuuza saluti ambazo zilielekewa kwake.

“Pole sana mzee.”

“Nipelekeni ofisini… hapana nyumbani,” alisema kwa udhaifu

“Tukupeleke hospitali afande?”

“Nimesema nyumbani.”

Dereva mmoja alimsogezea gari. Kabla hajalipanda alitoa maelekezo kwa askari hao, akiwataka wahakikishe jengo hilo linalindwa kwa makini usiku na mchana hadi atakapokuwa tayari kukamilisha suala hilo ambalo alidai limekwisha!

Joram alitumia fursa hiyo kuutoroka umati wa watu. Alimfuata mtu mmoja aliyekuwa ameketi ndani ya gari lake, Toyota Saloon, na kumwomba lifti. Mtu huyo, kwa furaha, aliwafungulia milango na kuwakaribisha ndani. Joram akamwingiza mgonjwa wake kisha yeye akaingia na kumtaka awapeleke hotel ya Mawenzi.

“Nina bahati sana leo” msamaria alisema.

“Bahati gani?” Joram alimwuliza

“Kukutana ana kwa ana na wewe. Ni jambo ambalo sikulitegemea kabisa. Nimekuwa nikikusoma katika vitabu na magazeti tu. Hivi huko ndani kulikuwa na nini?”

“Ngoja gazeti la kesho utaelewa, ni hadithi ndefu sana”

“Hivi haya wanayoyaandika juu yako ni ya kweli? Sio kwamba waandishi wanatia chumvi sana ili magazeti na vitabu vyao vinunuliwe?”

Joram, akiwa hana hamu na magazeti, alijikuta akimwambia, “Hayo unayoyasikia yazidishe mara nne, utoe nane na kuongeza mbili ndipo utapata ukweli wenyewe”

Akiwa amechanganyikiwa, dereva huyo aliendesha gari bila maongezi zaidi mpaka alipowafikisha mbele ya hoteli yao.

Joram alimshukuru kwa ukarimu wake, akamzoa Nuru ambaye alianza kulala na kumwingiza hotelini. Watu waliokuwa mapokezi walitokwa na macho ya mshangao, hasa kutokana na hali ya Nuru, lakini Joram hakuwapa nafasi ya maswali. Badala yake alichukua ufunguo wake na kwenda chumbani kwake, akiwa bado amemshikilia Nuru kiuno. Hakuhitaji funguo huo, chumba kilikuwa wazi, kinyume na alivyokiacha. Jicho lake moja chumbani humo lilimfanya afahamu kuwa alikuwa ametembelewa. Ingawa karibu kila kitu kilikuwa kama alivyokiacha, lakini bado dalili zilimwonyesha kuwa kila kitu kilikuwa kimekaguliwa na kuvurugwa kwa uangalifu mkubwa.

Joram akamtua Nuru kwenye kitanda na kumlaza taratibu. Alipovuta mto ili amweke vizuri, aligutuka kuona mto huo ulikuwa umetumiwa kuficha maiti ya paka mnene, aliyenawiri, ambayo yalilazwa kitandani hapo. Kando ya mzoga huo, Joram aliona maandishi mekundu yalioandikwa juu ya shuka kwa lugha ya kiingereza ‘you’re next’ yakimaanisha kuwa ni yeye Joram atakayefuatia.

Alipomgeukia Nuru kuona kama naye pia alikuwa ameuona mzoga huo, alifurahi kumwona tayari kalala kwa utulivu, akikoroma taratibu. Akainama na kumchunguza paka huyo kwa makini zaidi. Akabaini kuwa aliuawa kwa kunyongwa kwa kwa mkono muda mfupi uliopita kwani alikuwa bado ana joto. Lakini Joram alipozidi kumchunguza aligundua kuwa bado alikuwa akipumua taratibu. Badala ya kumtupa dirishani kama alivyokusudia, Joram alimwinua polepole na kumweka nje ya chumba, upande wa mapumziko.

Baada ya kuduwaa kwa mara ya pili, Joram alimnusisha paka huyo dawa ya kulevya, jambo ambalo lilimfanya mnyama huyo mdogo apige chafya na dakika chache baadaye ainuke na kujikongoja taratibu kuelekea nje.

Joram hakuhitaji kuambiwa paka huyo ameletwa na nani chumbani humo. Adrian!… Ni yeye pia aliyekipekua chumba chake ambamo dalili zilimwonyesha Joram kuwa alikaa muda mrefu akimsubiri.

Kitendo cha kupata uhai kwa paka huyo, ambaye Joram alijua fika aliwekwa hapa kwa njia ya kumtisha huku adui huyo akiamini kuwa ni mzoga, kilimdhihirishia Joram kuwa mapambano bado yalikuwa yanaendelea. Hata hivyo, ilimtia matumaini makubwa ya kuibuka mshindi akizingatia uhai wa paka huyo ulivyorejea baada ya muuaji kuamini kuwa ametimiza kazi yake.

Akifahamu fika jinsi roho ya Adrian ilivyolemaa kwa chuki na fikra zake zilivyomezwa na kiasi Joram alijua kuwa alikuwa na wajibu mkubwa kumteketeza kiumbe huyo kabla hajafanya madhara zaidi. “Ni yeye, au mimi!” aliwaza akiondoka kurudi kitandani ambako Nuru alilala kwa utulivu.

Joram alimtazama msichana huyu alivyolala na mavazi yake yote. Aliitazama sura yake nzuri na umbo lake la kuvutia lilivyopendeza katika mavazi hayo yaliyochakaa na kuchafuka.


Pamoja na hasira zake, Adrian alichukua wasaa wa kujilaumu kimoyomoyo. Kwa kiasi kikubwa alihisi alishiriki kuwaangusha waajiri wake ambao alikwisha amua kuwa wana aina fulani ya kichaa. Kitendo chake cha kupenya toka katika eneo hilo la ofisi hadi katika hoteli ya Joram Kiango ili akammalize hukohuko, badala ya kumsubiri, kama wenyeji wake walivyomwelekeza, kwa kila hali kimechangia kumfanya awe hai hadi sasa na awaokoe mateka wake.

Jambo hili, limezifanya jitihada zake zote, za kupenya katika uchochoro wa hoteli hiyo, hadi nyuma ambako alitumia kamba kupanda hadi juu na kisha kwa kutumia tundu la moshi kujipenyeza hadi ndani ziwe za bure.

Chumbani mwa Joram, Adrian alipekua kila sehemu bila kujua anatafuta nini. Hakupata chochote. Hata hivyo, ili asiondoke bila zawadi yoyote, ndipo alipochukua mkufu wa dhahabu uliokuwa kama umesahauliwa katika begi mojawapo.

Adrian alijua ingemchukua muda Joram kugundua upotevu huo, lakini kwake ingekuwa fahari kubaki na kumbukumbu ya kumfuta duniani.

Ni wakati alipokuwa akitoka nje ya chumba hicho alipokutana na paka yule ambaye alipita akinusa huko na huko. Adrian hakuchelewa kumdaka na kumminya koo kwa vidole viwili hadi paka alipokata roho, kisha akamlaza juu ya kitanda cha Joram kama salamu ambazo alijua zitamsisimua zaidi ya kupotea kwa mkufu mdogo wa dhahabu.

Adrian akaamua kurudi kwa waajiri wake. Akiwa nje ya jengo hilo la Paul na Philip, alimwona inspekta Kombora, pamoja na uchovu wake mwingi, akitoa maelekezo juu ya ulinzi wa jengo hilo. Akiwa na hakika kuwa mambo yalikuwa yamewaendea kombo waajiri wake, Adrian alitazama kwa makini jengo hilo huku rohoni akijua wazi kuwa japo jeshi zima la polisi liletwe kulinda usiku huo lazima angeingia katika jengo hilo na kuchukua kila kilicho chake.

Hakukuwa na mtu yeyote, duniani na mbinguni, ambaye angemzuia.

Kwa miji yote mikubwa ilivyo kote duniani, jiji la Dar es Salaam pia halijui usiku. Mara tu jua linapozama na kiza kutanda, wako baadhiya watu ambao huona kana kwamba ndio kwanza kumepambazuka. Hivyo, wakati wenzao wakijiandaa kulala wenzao hujiandaa kutoka tayari kwa shughuli zao mbalimbali, baadhi wakiwa wafanyakazi wa zamu za usiku, baadhi watumiaji tu wa pesa zao, hali wengine wakiwa waviziaji tu, wezi na Malaya wa bandarini.

Usiku wa leo Joram alikuwa mmoja wao. aliporejea toka muhimbili akiwa na aina mbalimbali za dawa ambazo alielekezwa jinsi ya kumpa Nuru, alimwamsha na kumshurutisha kuzinywa.

Kama alivyokuwa ameambiwa na daktari yule, mara tu baada ya kuzinywa, Nuru alichukuliwa tena na usingizi, usingizi mzito ambao ungempumzisha kwa saa ishirini na nne wakati dawa zikifanya kazi.

Baada ya kuhakikisha Nuru amelala kwa utulivu, ndipo Joram pia alipolala kando yake na usingizi mnono, usio na ndoto, kumchukua. Alizinduka saa moja usiku. Akafanya haraka kuoga, kisha kuvaa suti yake.

Baada ya hapo aliichukua bastola yake, bomu moja la mkono, kisu na silaha zake nyingine akazitokomeza katika mifuko yake ya siri. Alipojitazama katika kioo na kuridhika kuwa hata askari mdadisi kiasi gani asingemshuku kuwa anakwenda vitani badala ya kwenda kufanya matumizi, ndipo alipombusu Nuru, akamfunika vizuri na kisha kuondoka baada ya kuufunga mlango vyema nyuma yake.

Hakuwa na haraka. Alipita katika chumba cha maakuli ambako aliagiza ugali kwa kuku wa kuokwa. Wakati akisubiri chakula hicho alijipongeza kwa bia mbili za stella. Chakula chake kilipofika alikula kwa utulivu, huku akiteremsha kwa kopo la tatu la stella. Alipomaliza aliwasha sigara na kuivuta taratibu huku kopo la nne lilkikoza moshi. Saa yake ilipomwashiria kuwa imetimia nne kasorobo za usiku ndipo alipolipa bili yake na kuingia mitaani.

Kwa mwendo ule ule wa taratibu, alivuta hatua moja baada ya nyingine kuziendea ofisi za Kangaroo. Alijua fika kuwa watakuwepo na silaha zao mikononi. Hata hivyo, akiwa amedhamiria kuingia alikwishajiandaa kwa njia moja au nyingine ambayo ingemwezesha kuingia. Hivyo, hilo hakulitilia wasiwasi. Ambalo lilimtia wasiwasi na kumwongezea shahuku ya kufika aendako ni Adrian. Alikuwa na hakika kuwa Adrian, alivo kichwa maji, lazima pia angebuni kuingia katika jengo hilo. Na ni hilo lililomfanya awahi. Alitaka awe wa kwanza kufika katika jengo hilo ili amsubiri na kumpokea. Alijua fika kuwa mkutano wao wa ana kwa ana ulikuwa na maana moja tu, ya kumwacha mmoja hai, mwingine maiti. Joram alikuwa na uhakika kuwa huyo maiti asingekuwa yeye.

Wakati akikaribia ofisi hiyo, Joram aliichomoa tai yake nyeupe na kuisokomeza mfukoni. Kuondolewa kwa tai hiyo, kulimfanya abadilike ghafla na kuwa kama kivuli au sehemu ya kiza. Aliubadili pia mwendo wake na kuanza kunyata kwa uangalifu, toka ukuta hadi ukuta; kichaka hadi kichaka. Wapita njia waliomtazama kwa macho ya udadisi aliwapumbaza kwa kujifanya ama anajisaidia haja ndogo au anafunga kamba za viatu vyake, ama amelewa na hivyo, anakwenda bila mpangilio wowote.

Alipofika mbele ya Kangaroo, kama ivyotegemea, alimwona askari mmoja mwenye silaha na magwanda akiwa amesimama kuuegemea ukuta, bunduki yake kaishika mkono mmoja, wa pili ukiwa mfukoni. Joram alimtazama kwa makini. Akashangazwa na utulivu wa askari huyo. Alipotupa macho kutazama huko na huko hakumwona askari mwingine.

Akaitazama saa yake ambayo ilimuashiria saa nne na dakika kumi. Alihitaji kuwa katika jengo hilo mapema. Hivyo, alipoona askari huyo hatoki hapo aliposimama, aliamua kumfuata. Aliiwasha sigara yake na kuipachika mdomoni, akakohoa, kisha akaanza kumsogelea. Alitegemea kuambiwa simama au kupewa amri yoyote ile. Haikutoka. Joram alizidi kumsogelea hadi alipomfikia na kumsalimu. Hakuitikia.

“Hujambo, brother?” Joram alisalimu tena.

Bado hakuitikiwa, jambo ambalo aliona halikuwa la kawaida. Alimtazama askari huyo kwa makini zaidi na kubaini kuwa alikuwa hatingishiki, haoni wala hasikii. Alipojaribu kumtikisa aliporomoka na silaha yake na kuanguka sakafuni.

Ndio kwanza Joram akabaini kuwa alikuwa anaongea na maiti. Akainama na kumshika kifuani ambako alimkuta kapoa kitambo. Kiasi Joram alitahayari. Alitegemea ukatili. Lakini hakutegemea ukatili wa kiasi hicho. Kwa ujumla, aliondokea kuamini kuwa kipindi cha mauaji ya kinyama kilikuwa kimepita, wazo ambalo sasa alilijutia.

Hakuhitaji kuambiwa kuwa mauaji hayo yamefanywa na nani. Wala hakuiona haja ya kujiuliza kwanini yamefanyika. Adrian alikuwa amemtangulia. Akamwua askari huyo, bila shaka kwa hila, ili asiwe kipingamizi cha kumfanya ashindwe kuingia ndani. Hivyo, ama alikuwa ndani ama ametoka.

Wakati akiyafikiri hayo Joram Kiango tayari alikuwa ameusimamisha mzoga huo wa askari kama alivyoukuta na kuirejesha bunduki mkononi mwake na kuanza kunyata akielekea mlangoni. Kando ya mlango huo, kwenye kibanda kidogo cha mapokezi, Joram aliikuta maiti ya askari wa pili. Huyu alikuwa ameketishwa juu ya kiti na kuiinamia meza, bunduki mkononi. Joram hakuitaji kumgusa kujua kuwa amekufa.

Aidha, hakuwa na haja ya kumshika shingo ili kubaini kuwa lilikuwa limevunjwa kwa pigo kali la judo. Alichofanya ni kukimbilia ndani, ambako aliukuta mlango ukiwa wazi, kama unaomsubiri. Harakaharaka bastola yake ikiwa mkononi, alinyata toka chumba hadi chumba. Akitumia tochi yake yenye ukubwa wa kalamu, alichungulia kila kona, kila uvungu wa meza, kila kabati, kila uvungu wa friji, bila mafanikio. Kila dalili ilimwonyesha kuwa Adrian amekuja na kuondoka.

Joram akaziacha ofisi za kawaida na kuzifuata zile za siri ambako waliwazika hai Paul na Philip. Huko pia Adrian alikuwa amemtangulia na alichokifanya hakikustahili kutazamwa. Mateka hao wawili ambao yeye na Kombora waliamua kuwafungia hai, Adrian alikuwa amewachoropoa toka shimoni humo na kuwachinja kama kuku, mmoja baada ya mwingine. Miili yao, aliitupa juu ya sakafu na kuwafanya walale wakiwa wamekumbatiana ndani ya dimbwi la damu yao wenyewe.

Joram alikiacha chumba hicho na kukimbilia kile ambacho kilihifadhi mamilioni ya pesa za kigeni. Alisogeza sefu ambalo liliwekwa kwa geresha na kulifikia lile la siri ambalo liliunganishwa na ukuta kwa hila. Alipojaribu kulifungua alishangaa kulikuta likiwa wazi. Pale ambapo palikuwa na vitita vya noti za ndani na nje sasa hapakuwa na kitu chochote. Hapana, palikuwa na kitu fulani, kitu kidogo, cheusi. Joram aliisogeza tochi yake na kutazama. Kama macho yake yalichelewa kumwashiria yanatazama nini, pua yake haikuchelea kufanya hivyo. Kitu hicho kilikuwa kinyesi. Baada ya kuchukua pesa hizo, kwa kuonyesha dharau, Adrian, akijua mtu yeyote angetamani kuzipata pesa hizo ndipo alipoamua kufanya hivyo.

Mara ya kwanza maishani mwake hasira hizo zilimfanya atetemeke mwili mzima. “Mshenzi” aliropoka kwa mara ya pili. “Haendi popote! Kamwe haondoki nje ya nchi hii akiwa hai,” alinguruma akigeuka kuanza kutoka nje ya chumba hicho taratibu kwa mwendo wa sismba aliyejeruhiwa mwili na roho.

MWISHO

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment