SIMULIZI

Mikononi Mwa Nunda – EP01

SIMULIZI Mikononi Mwa Nunda
SIMULIZI Mikononi Mwa Nunda – EP01

IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA

*********************************************************************************

Simulizi : Mikononi Mwa Nunda
Sehemu Ya Kwanza (1)

SURA YA KWANZA

UKEKE Maulana alikuwa mzee ambaye siku zote alipingana na uzee, mzee ambaye hakukubali uzee umtawale hata mara moja. Alikuwa vitani akiupinga na kuudhihaki hadi uzee ukaelekea kumpigia magoti. Kama si kwa ajili ya mvi chache ambazo zilikataa kuitii kanta, hata wewe ungemwondoa katika orodha ya wazee na kumwita kijana. Kumwita hivyo kungekufanya akupende, na watu wote wamjuao wasingekulaumu. Wangekulaumu vipi wakati hata chembe moja ya ndevu haikuthubutu kujitokeza katika kidevu chake?

Wakati mavazi yake yalikuwa yale ya vijana? Wakati mienendo yake yote ilikuwa katika kumbi na vipenyo vilevile ambavyo vijana walipenda kupita? Si hayo tu, zaidi ni jinsi alivyokuwa akienda sehemu hizo, dansini, baa, sinema na kokote; akiwa amefuatana na msichana mwenye umri ambao haukuwa mbali na wajukuu zake. Naam, Ukeke alikuwa Ukeke.

Sifa zake hizo zilitajwa na zilizosahauliwa, ziliwafanya watu watundu waanze kumwita majina kadha wa kadha. Mara “Mzee kijana,” mara “Kizito”, ama “Mwenyewe” pamoja na yote waliyodhani yangemfaa. Yote hayo yalimpendeza Ukeke. Lakini hakuna lililomfaa zaidi ya “Ukeke.” Hivyo, Ukeke akabaki Ukeke na kuendelea kuwa Ukeke.

Alichukia jinsi uzee ulivyotishia kumpokonya nafasi yake ya kustarehe. Na aliupenda na kuung’ang’ania ujana kwa ajili ya ile ahadi ya kuwa huru katika harakati za anasa na starehe, anasa ambazo zilimjaza furaha na hamu ya maisha. Hiyo ndiyo sababu iliyomfanya augande ujana akifurahi na kustarehe pamoja na vijana.

Starehe aliipata kama alivyopenda. Fedha haikuwa kipingamizi. Alikuwa na kazi yenye cheo katika moja ya kampuni za umma, kazi ambayo, licha ya kumlipa vizuri, ilikuwa nafasi nyingine iliyomwezesha kujipatia chochote nje ya mshahara, kwa njia moja au nyingine. Hivyo, starehe zake hazikupotoshwa na aina yoyote ya kipingamizi cha fedha au “watoto watakula nini.” Bali alistarehe alivyopenda; huku kaandamana na binti yeyote aliyempenda.

Hata hivyo, jioni hii aliiona “mbovu.” Kama kawaida, tatizo halikuwa pesa. Hizo alikuwa nazo. Tatizo lilikuwa ampate nani wa kula naye pesa hizo. Aliwapigia simu wasichana wote aliodhani wangestarehe naye jioni hii, hakufanikiwa. Kila mmoja alitoa udhuru ambao haukuweza kupingika.

Kwa mara ya kwanza akawaza kutembea na mama watoto wake. Lakini wazo hilo aliliponda mara moja alipowaza kuwa mama huyo hakujua chochote juu ya dansi na pombe. Kisha angeweza kusababisha zogo la bure katika mabaa kati ya mke wake na wapenzi wake. Na zaidi, hakuona kama alikuwa mwanamke anayefaa kuwekwa hadharani.

Ni hali hiyo iliyomfanya jioni hii atoke peke yake na kupanda gari lake ambalo alilitia moto, likamchukua hadi Buguruni. Huko aliingia West Bar na kujipatia meza ya mbali ambako alijiwashia sigara polepole, macho yake yakiangaza huku na huko kumsaka mhudumu ambaye angestahili kumhudumia. Kustahili, si kwa usafi bali sura na umbo ambalo macho yangevutiwa kutazama, mikono istarehe kumgusa na roho iridhike kuwa naye. Mbele yake walipita wengi, wengine hata walidiriki kumchochea walipomuuliza angehitaji nini. Wote aliwapuuza baada ya kutoa dosari za umbo, umri, na kadhalika katika maumbile yao.

“Nikusaidie nini mzee?” sauti hiyo ilitokea nyuma yake.

Alipogeuka kumtazama mwenyewe alishangaa kuona ikitoka katika kinywa cha msichana mzuri kuliko wote aliopata kuwaona wakiuza baa, mzuri tosha; akiwa na sura inayovutia, umbo linaloumiza na macho yanayoshawishi. Alikuwa kasimama kwa namna ya mwigizaji mzuri wa sinema ambaye alisubiri kufotolewa, picha ambayo ingepamba jalada la gazeti kiasi cha kulifanya lipendeke kuliko mengine.

Kilichomvutia Ukeke si sura na umbo tu, hasa ni ujana ambao aliuona ulikuwa wazi kabisa katika sura hiyo. Ikamshangaza kuona vipi mtoto mwenye umri mdogo kama huo, aangukie katika baa na kuuza baa. Alivyoamini yeye ni dhiki tu ambayo ingemfanya mtu kuuza baa. Vinginevyo, hakuiona sababu. Hakuona kama umbo na sura ya msichana huyo inaweza kumfanya apate dhiki ya aina yoyote duniani.

Mawazo hayo hakuacha yapokonye nafasi njema iliyomjia, ya kujipatia mwanamke mwingine mzuri, siku ya leo, siku ambayo alidhani ingekuwa na kasoro. Hivyo, badala ya kujibu alitega paja lake na kumwashiria msichana huyo kuketi huku akisema, “Keti hapa, kimwana. Keti tustarehe; mengine yatafuata baadaye.”

“Samahani nipo kazini, Bwana Ukeke,” msichana huyo alimjibu kwa upole. “Endapo una haja nami sema niombe ruhusa ili tuondoke baa hii na kwenda popote tuwezapo kustarehe.”

Ukeke akajisikia kucheka kwa furaha. Bahati ilioje! Kirahisi namna hii! Asingeipoteza nafasi kama hii, nafasi nyingine ya kujiburudisha kwa damu changa yenye afya. Ni hayo aliyomjibu msichana. Kisha akataka kumletea chupa moja ya bia. Wakati akiinywa alikumbuka kuwa binti huyo alimtaja jina. Alijuaje? akajiuliza.

Halafu akajikumbusha kuwa yeye yu mtu mkubwa, mtu maarufu mitaani, mtu mwenye hadhi ofisini. Lazima watu wamjuao ni wengi kuliko aliowajua yeye. Hivyo, haikuwa ajabu kwa msichana huyo kumfahamu ingawa leo ilikuwa mara ya kwanza kuingia baa hii.
Alipomaliza chupa moja alimkonyeza binti huyo ambaye alitulia kaunta, akimtazama kwa utulivu.

Walikutana nje. Wakapanda gari na kuliondoa. “Twende wapi?” Ukeke aliuliza wakati akikanyaga mafuta.

“Popote.”

“Waonaje tukienda kwanza ufukoni, tupigwe na upepo mzuri, kisha twende hoteli nzuri, kupata chochote; halafu tupate chumba kizuri kitakachotuhifadhi hadi kesho?”

“Sawa.”

Wakaianza safari ya ufukoni. Njiani Ukeke alizungumza hili na lile. Ikamshangaza kuona binti huyo akiendelea kumpa majibu ya mkato, “Ndiyo” au “Hapana.”

Yale maongezi ya kike, maongezi yenye upuuzi unaofariji, hayakumtoka binti huyo angalau kwa kukosea. Si hilo tu!

Kadhalika, tabasamu, kitu ambacho kingeustahili kabisa uso wa mrembo kama huyo, halikujitokeza hata chembe. Maneno yote ambayo Ukeke aliyatamka kwa nia ya kumliwaza yakapita bila kuzaa matunda. Kwa nini? Ukeke alijiuliza. Akajikuta akiwaza kumfukuza binti huyo nje ya gari lake, arudi zake kwake Mnazi Mmoja, akalale. Lakini tamaa ilimnyima uwezo, tamaa ya kujiburudisha kwa mara nyingine. Hivyo, akaendelea na safari hadi ufukoni.

Ufuko ulikuwa mtulivu kuliko walivyotarajia, utulivu mzito kiasi cha kumtisha kidogo Ukeke. Akamgeukia msichana huyo na kumtazama. Akashangaa kumkuta akitabasamu. “Mpenzi…” alitaka kusema zaidi. Lakini akasita alipomsikia msichana huyo akisema kwa sauti yenye furaha kinyume cha ile aliyokuwa akiitumia huko mbeleni.

“Utulivu ulioje huu bwana Ukeke? Natumaini utatufaa sana. Nibusu, tafadhali.”

Tamaa iliyomwingia ilimfanya ajisogeze karibu zaidi na binti huyo huku akijitayarisha kuupokea ulimi uliokuwa ukimjia. Mshangao wa pili ulimjia pindi alipoona bapa la kisu likimeremeta na kujitokeza ghafla katika mkono wa binti huyo. Kabla hajajua la kufikiri jisu hilo lilichomwa kwa nguvu ubavuni mwake. Likang’olewa na kuchomwa tena.

Ingawa maumivu aliyoyapata yalikuwa makali kiasi cha kuifanya sauti yake isisikike alipopiga kelele, lakini hayakumzuia kushangaa. Aliendelea kushangaa akimtazama binti huyo alivyokuwa akiendelea kuchomoa na kumchoma kisu hicho mwilini mwake kama mtoto achezavyo na mgomba wa ndizi. Mshangao wake wa tatu ulimjia wakati alipoona akikoma kusikia maumivu na badala yake kuanza kudidimia katika shimo refu lisilo na mwisho, shimo lenye kiza kizito zaidi ya kiza. Akaendelea kushangaa. Hata hivyo, huo ulikuwa mshangao wake wa mwisho.

***
Joto la mchana katika Jiji la Dar es Salaam humfanya mzee Mohamed Matoke kubarizi nje ya nyumba yake kila baada ya mlo wa usiku. Huketi juu ya msingi wa nyumba yake, shati jepesi likiwa kifuani na kikoi kiunoni, upepo mwanana ukiupepea uso wake; na nuru hafifu ikimwezesha kuwaona wapita njia ambao mara nyingi hutokea kuwa wapenzi watokao ama kuelekea katika majumba ya starehe. Huketi hapo huku akijihisi burudiko na starehe. Huongeza uzito wa burudani lake hilo kwa kujivutia sigara zake za Safari, moja baada ya nyingine.

Watu waanzapo kuadimika katika mtaa huo ndipo huinuka na kukiendea chumba chake ambako humkuta mkewe akijiandaa kulala.

Jioni ya leo haikutofautiana sana na nyingine zilizotangulia. Alikuwa kakaa mahala pake pa kawaida, sigara yake ya kawaida ikiungua mdomoni na watu wa kawaida wakiendelea kupita njiani. Tofauti pekee ni kwamba usiku wa leo asingemkuta mke wake chumbani. Angekuwa peke yake nyumba nzima. Mkewe na wanawe waliondoka jioni ya leo kuelekea kwao, Kilwa, kuwasalimu wazazi. Ilikuwa safari fupi tu, baada ya siku tatu wangerudi. Hivyo, mzee Matoke hakuona dhiki kubaki peke yake kwa kipindi kifupi kama hicho.

Hata hivyo, hisia za upweke ambao angepambana nazo ndani ndizo zilizomfanya achelewe nje zaidi ya muda wake wa kawaida. Alipoitazama saa yake mshale wa dakika ulikuwa mbele kidogo ya saa sita kamili. Akaendelea kustarehe, sigara zikiendelea kuteketea.

Watu sasa walipita kwa uchache mno, wawili tu walikuwa wamempita baada ya dakika tano nzima, vijana; mvulana na msichana. Walikuwa katika mavazi yao ambayo yeye huyaona ya kihuni, wakitembea huku wameshikana viuno. Aliwafuata kwa macho hadi walipotokomea.

Wakati akifikiri kuyainua macho yake, yakavutwa na mtu mwingine aliyetokea chini ya mtaa. Alikuwa akija polepole. Alipokaribia, mzee Matoke aliweza kuona kuwa alikuwa msichana, peke yake! Hilo lilimshangaza. Hakuzoea kuwaona wasichana wakitembea kwa upweke saa kama hizo, hasa msichana kama huyu ambaye umbo lake, ingawa kwa mbali, aliliona kama zuri, liwezalo kumshawishi mwanaume yeyote kuvunja safari yake na kufuatana naye. Ni hayo yaliyomfanya ahairishe kwenda zake ndani na badala yake aendelee kutulia akimtazama. Kila msichana huyo alivyozidi kumkaribia ndivyo mzee Matoke alivyozidi kuvutiwa na umbo lake.

Hatimaye binti akamfikia. Nuru hafifu ya taa ya umeme iliyokuwa ikitoka katika nyumba zake na zile za jirani ilimfanya mzee Matoke auone uso wa msichana huyo vyema zaidi. Sura nzuri! aliwaza. Sura hiyo ililandana na umbo lake! Sura inayofaa kabisa kumfariji mwanaume, sura ambayo ni nuru katikati ya kiza, sura hiyo ni zaidi ya ua zuri bustanini. Naam, sura hiyo ikamfanya mzee Matoke asahau kuvutiwa na badala yake ahusudu. Husuda nayo ilimezwa ghafla na tamaa. Akajikuta akimtamani.

Kuna watu ambao wana tabia ya kupendapenda ovyo, tabia ambayo imewaganda kiasi cha kugeuka kuwa maradhi, ambayo humfanya mzee na mvi zake kusimama na binti mwenye umri wa binti yake hadharani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mohamed Matoke hakuwa mmoja miongoni mwa wazee hao. Yeye alijiheshimu na kuuheshimu mno umri wake. Zaidi ya heshima aliuogopa mchezo huo kwaajili ya kuipenda mno fedha. Kwake fedha ilikuwa zaidi ya kila kitu. Zaidi ya mwanamke, zaidi ya mahaba. Kuipenda huko kulimfanya aanze kuikusanya tangu akiwa mdogo mno.

Wazazi wake walicheka kwa hasira na mshangao walipomwona akitoroka shule kwa ajili ya kuuza karanga mitaani. Haikusaidia kitu walipojaribu kumlazimisha masomo. Wakazidi kushangaa alipoacha kuuza karanga na kuanza kuuza mayai. Mayai nayo walishtukia akiyaweka kando na kuuza kuku. Kuku zilifuatwa na mbuzi. Mbuzi zikamezwa na ng’ombe. Tahamaki akawa maarufu katika minada yote ya ng’ombe. Sasa alikuwa na nyumba tatu za kupangisha sehemu hizo za Mnazi Mmoja, hoteli mbili na lori ambalo lilimsaidia kuingiza biashara zake katika Soko la Kariakoo.

Siku zote za kutafuta kwake alijiepusha vilivyo na starehe. Nje ya chakula na mavazi hafifu kitu pekee kilichodokoa senti zake ni sigara. Hizo alijifunza kuzivuta kwa “bahati mbaya” na juhudi zake za kuacha hazikufua dafu. Mwanamke ni kitu ambacho hakukijaribu, “… ni sumu ya biashara,” mara kwa mara alisikika akiwanong’oneza wenzake. Maelezo hayo yalifuatwa na masimulizi ya “fulani na fulani” alioanza nao biashara ambao walikwama kwa ajili hiyo. “Hadi leo wanaishi kwa kutegemea vibarua.” Alimalizia hadithi zake. Pengine asingeoa na kujipatia watoto wanane alionao, iwapo wazazi wake wasingemwita nyumbani na kumlazimisha mke, mke ambaye aliondokea kuridhika naye.

Hata hivyo, pamoja na ushujaa wake wa kuyashinda mapenzi, msichana huyu aliyekuwa akipita peke yake, saa kama hizi, alimtia wazo ambalo awali halikuwahi kumpitia akilini, wazo la kujiburudisha naye kwa muda mfupi tu, aisikie damu changa inavyoweza kuiburudisha nafsi iliyozeeka, auone ujana uwezavyo kufariji. Kwa mara nyingine! Kwani tangu alipoutokomeza usichana wa mkewe, miaka mingi iliyopita, alikwishasahau kabisa kilichomo katika usichana.

Wakati mawazo hayo yakitambaa katika fikra zake, kuenea katika ubongo wake na hatimaye, kuneemeka katika nafsi yake yule binti alikuwa mbele yake, akikaribia kumpita.

“Waonaje bibie,” alisema akiinuka kumsogelea; sauti yake akiitoa kwenye amri kama alivyozoea na kuiweka katika hali ya kibiashara. “Waonaje,” alirudia. “Kama ungepumzika kidogo tuzungumze machache.”

Binti akasimama. Mzee Matoke alipomfikia, alishangaa kujikuta amesahau yote aliyopanga kuyazungumza, yote yale ambayo amewasikia wazee wenzake wakizungumza na watoto wa kike. Alichoweza kufanya ni kusimama mbele ya binti huyo, huku moyo ukimdunda na mwili kutetemeka.

“Najua unachotaka. Unanitaka. Au sio?” binti alihoji alipoona kimya kinazidi. Mzee Matoke sauti yake ilizidi kumkwama. Sauti ya huyu binti ilikuwa moja ya zile ambazo wahenga walisema zaweza kumtoa nyoka pangoni.

“Hasa, ni hivyo,” alijikuta akijibu.

“Huna mke?” msichana aliuliza tena.

“Mke ninaye. Lakini hayupo. Yupo shamba pamoja na wanangu. Niko peke yangu leo…”

“Basi twende zetu ndani.”

Wakaongozana hadi ndani. Humo walifuatana chumbani.
Wakiwa chumbani, binti alisimama mbele ya kitanda akimtazama mwenyeji wake, mwenyeji ambaye alisimama katikati ya chumba kama mgeni katika chumba chake mwenyewe; akimtazama msichana huyo. Maadamu sasa walikuwa chini ya nuru kali, mzee Matoke aliweza kumwona msichana huyo kwa uzuri zaidi.

Bahati iliyoje! Mdogo kuliko alivyotarajia! Sura ikiwa na dalili zote za usichana, macho yakiwa na nuru yote ya ujana. Pua iliyonyooka! Mashavu laini! Meno… utafiti wake ulikwama hapo alipoona kitu kimoja tu kikiadimika kuufanya uzuri uchanue, tabasamu. Alizoea kuwaona wasichana wa aina hiyo wakiwachekea wateja wao mara kwa mara , vicheko ambavyo huwa kama sabuni katika roho za wateja. Kwa nini asitabasamu? Labda hamjamkirimu kikamilifu. Aliwaza hayo huku akianza tena kuutafiti mwili wa binti huyo.

“Si unan’taka? Njoo basi,” binti alisema akikaribia kuvua nguo.

Mzee Matoke alizitazama nguo hizo, nzuri, za kihuni kabisa! Tazama zilivyoruhusu sehemu kubwa ya mapaja kuonekana! Tazama… akasita ghafla alipoona kitu cha ziada katika nguo hiyo. Kitu zaidi ya mapambo. Damu! Damu mbichi!

“Una nini bibie?” aliuliza kwa mshangao.

“N’na nini?”

“Damu.”

“Damu! Damu ya nini? Ya mtu! Iko wapi?”

“Hii hapa,” mzee Matoke alisema akimsogelea na kuinama kuligusa gauni, juu kidogo ya paja ambapo damu ilianza kuganda.
“Tazama. Imetoka wapi…”

Swali lake halikupata jibu kwani pindi akiinuka kumtazama msichana huyo aliambulia kuona nuru ya kisu ikimeremeta ghafla na kupotelea katika mwili wake, mgongoni. Maumivu makali yakamlegeza kiasi cha kumfanya aanguke kifudifudi. Pigo la pili likamfuata tena mgongoni.

“Unaniua… Ah… usiniue,” alilia au kulalamika. “Yakhla!… tafadhali usiniue… sema utakacho nikupe… kama ni fedha sema… tene…” kisu kikaendelea kumchoma mgongoni.” …Ohh! Tafadhali… chukua pesa niachie roho yangu…”

“Ziko wapi?”

“U… u… uvungu wa kitanda cha watoto… ndani ya sanduku kuu kuu… Oh! Niachie tafadhali… Oh!…” aliendelea kutapatapa, akisema lile na hili hadi alipoona ulimi ukishindwa kutamka chochote, macho yakishindwa kuiona nuru kali ya umeme na hatimaye, masikio yakitokwa na uwezo wa kusikia.

*****SURA YA PILI******

TAARIFA ya vifo hivyo iliwafikia polisi alfajiri ya siku ya pili. Iliyotangulia ilikuwa habari ya kifo cha Bwana Ukeke Bin Maulana. Maiti yake yaliokotwa na wavuvi wa samaki waliokuwa wakirejea toka baharini walikokesha wakivua. Walivutiwa na kuliona gari likiwa limesimama sehemu za ufukoni saa hizo. Wakaliendea. Walipokaribiawaligundua kuwa halikuwa na matairi wala injini.

Vyote vilikuwa vimeibiwa usiku. Walipochungulia ndani walijikuta wakizidiwa na mshangao ambao uligeuka kuwa hofu kwa kuyaona maiti ya mtu, mwanaume, yakiwa yamelalia usukani kama dereva yeyote aliyechoka, ama kulewa kiasi cha kusahau wajibu wake. Wangeweza kumfikiria hivyo kama si sababu ya damu nyingi ambayo iliganda juu ya shati na suruali. Ndipo walipoiarifu polisi.

Kifo cha mzee Mohamed Matoke kiliripotiwa na mtumishi wake aliyefika katika nyumba hiyo saa moja za asubuhi, kama ilivyokuwa kawaida yake. Ikamshangaza alipoukuta mlango ukiwa wazi. Hivyo, akaingia akiwa na mashaka ya kuibiwa au ukatili mwingine.

Naam, alipofika chumbani tu mashaka yake yalikamilika au kutoweka alipomkuta bwana wake kaikumbatia sakafu kama anayeibusu, akiwa katika dimbwi la damu kavu, kikoi chake kikiwa kimesahau kusitiri mapaja yake, na utulivu aliokuwa nao vilimwashiria mtumishi huyo jambo moja tu; kifo. Kwa mkono unaotetemeka, akakiinua chombo cha simu na kuzungusha 999. Polisi wakaipokea na kuishughulikia kikamilifu.

Mkuu wa kituo maalumu cha polisi, ndugu Mkwaju Kombora aliipokea habari hiyo kwa hasira kali. Hakuna kitu kilichomtisha kama mauaji. Wala hakuna mtu aliyemchukia kama mwuaji. Mtu kama huyo, alimchukia kama shetani mwenyewe na kumsaka kwa ari zote ili ampate na kumpeleka gerezani ambako alikuita “jehanamu.”

Mwuaji au wauaji hawa aliwaona kama watu walioelekea kumletea kazi ya kutosha. “Watu wawili kwa usiku mmoja!”alijikuta akiropoka bila mategemeo. “Wote kwa kisu! Mmoja ufukoni, wa pili mjini! Ni nani hawa! Na kwanini wafanye hivi!” alijiuliza. Hakutegemea kupata majibu haraka kiasi hicho. Alikuwa akisubiri uchunguzi uliokuwa ukifanywa na vijana wake maarufu ambao aliwatuma katika shughuli hizo.

Subira ilikuwa ikimtesa kama adhabu. Alihisi kila dakika aliyoendelea kusubiri ikimjeruhi juu ya jeraha bichi. Kiti pia alihisi chawaka moto. Alipoondoka na kuliendea dirisha alijikuta hana hamu ya kukaa hapo kwa kukiona kikundi cha watu ambao walikuwa wakibishana na polisi. Aliwajua watu hao. Walikuwa watu wa habari, waandishi wa magazeti na watangazaji wa redio.

Bila shaka kisa cha ubishi wao kilikuwa kutaka kuonana naye. Waandishi hao walidai kumwona hali askari hawataki. Aliwaagiza askari hao kutomruhusu mtu yeyote mwenye nia ya kutangaza chochote juu ya vifo hivyo kuonana naye kwa sasa kwani hakuwa na chochote ambacho kingeeleweka kwa taifa.

Baada ya subira ambayo Kombora aliiona ndefu kupindukia, hatimaye, ripoti ikamwasilia mezani kwake. Aliipokea upesi na kuanza kuisoma kwanza harakaharaka na kisha polepole; kwa tuo na tahadhari.

Kwa mujibu wa daktari kifo cha Bwana Ukeke bin Maulana kilisababishwa na majeraha ya kisu au visu ambavyo vilichomwa ubavuni na kifuani mara kadhaa. Kifo hicho kimetokea kati ya saa tano na sita za usiku wa leo. Mwuaji au wauaji hao wameiba injini, vioo na matairi ya gari na kumwacha kalalia usukani. Uchunguzi umeonyesha kuwa Bwana Maulana hakufanya machachari yoyote katika kufa kwake.

Mwuaji aweza kuwa mtu yeyote ambaye ama ni mwizi ama anamchukia. Uchunguzi bado unaendelea juu ya mienendo ya marehemu siku yake ya mwisho.

Nayo taarifa juu ya marehemu mzee Matoke haikutofautiana chochote na hiyo isipokuwa,… amefariki baina ya saa nne na tano. Majeraha ya kisu ndiyo yaliyomwua. Hakuna hakika kama ni kisu kilekile au kingine ambacho kimewaua marehemu hawa. Lakini inaonyesha kama iko tofauti basi ni ndogo sana kwani mzee Matoke pia anaonyesha kuwa amefariki katika hali ya utulivu.

Alikuwa kalala sakafuni hali hakuna chombo chochote, wala kitu chochote ambacho kilianguka au kuonyesha dalili ya mapambano. Kwa mujibu wa mtumishi wake sanduku lake la pesa ambazo alikuwa akizihifadhi kabla ya kupelekwa benki lilikuwa limetoweka. Kwa hesabu za harakaharaka kiasi cha shilingi elfu hamsini zinakisiwa kuwemo katika kasha hilo…

Pamoja na taarifa hizo zilikuwepo picha za marehemu wote wawili ambazo zilifotolewa kabla ya maiti zao kuguswa na mtu yeyote. Picha ya mzee Matoke pindi kalala katika dimbwi la damu kavu, ilimfanya inspekta Kombora ashindwe kuuona uso wake na, hivyo, kuukisia umri wake. Lakini ile ya Bwana Ukeke, ikionyesha nusu ya sura yake, katika mavazi yake mazuri, ilimfanya Kombora kumdhania kama mwenye umri wa miaka arobaini. Hakujua kuwa alikuwa kampunguzia miaka kumi. Alizitazama picha hizo kwa muda zaidi, kisha akairejea tena taarifa ya vifo vyao, halafu akashika kichwa na kuanza kuwaza kwa nguvu.

Wazo kuu lilikuwa moja tu, ampate vipi mwuaji au wauaji hao wasio na hata chembe ya huruma, wauaji ambao hupenda kuichafua amani na kufurahia kumwagika kwa damu isiyo na hatia. Angependa sana kuwapata haraka watu hao. Tatizo lilikuwa atawapataje upesi. Jiji lilifurika watu, wema kwa waovu, wenye hatia kwa wasio na hatia. Vipi awaopoe watu hao wenye hatia miongoni mwa maelfu yasiyo na hatia?

Jibu lilikuwa moja tu, muda, yaani subira. Asubiri hadi hapo atakapokusanya habari muhimu ambazo zingemwongoza hadi mbele ya mwuaji. Habari kama kuifahamu mienendo ya marehemu jioni hiyo, wapi alikopita, watu gani alikutana nao, mambo gani aliongea nao na mambo mengine ambayo yangejitokeza. Ni hayo ambayo yangetengeneza njia ya kumwendea mwuaji.

Na ni hayo yaliyohitaji muda, subira.

Subira hiyo ilimtisha zaidi ya mwuaji mwenyewe. Hakuipenda kwasababu nyingi, sababu moja ikiwa ile ya kutojua mwuaji atafanya nini katika kipindi hicho, pengine aongeze ukatili, pengine aitoroke sheria. Sababu nyingine ni ile ya raia wema kuwa katika hofu na mashaka juu ya uhai wao. Hali hiyo haikumpendeza hata kidogo. Yeye kama mlinzi wa amani katika jiji hilo, aliyepewa dhamana hiyo na taifa zima, asingestarehe hata kidogo kuiona amani hiyo ikitoweka.

Mawazo hayo ndiyo yaliyomfanya ashindwe kuwakabili waandishi wa habari, badala yake akamtuma msaidizi wake akawaambie kuwa “uchunguzi unaendelea.”

***
Kesho yake habari zilitapakaa nchi nzima. Watu wa mikoani waligutuka na kushangaa huku baadhi walizoziwahi ndimi zao wakiropoka, “Ni nini kilichotokea Dar?” wakazi wa hapa jijini walizipokea habari hizo kwa kitu zaidi ya mshangao, hofu. Hofu ilipenya katika fikra zao kwa kule kusikika kwamba haikuwepo fununu yeyote juu ya kupatikana mwuaji. Kila mtu alimtazama mwenziwe kwa macho yanayoitangaza hofu hiyo iliyojificha rohoni. Kila mmoja alitamka lile au hili, yote yakidhihirisha neno moja tu; hofu.

Mtu mmoja tu aliipokea habari hii kwa tabasamu, mtu mmoja katika jiji zima, kijana mrefu, mwenye maungo yenye nguvu, uso mzuri na macho maangavu, kijana ambaye mikasa yote ya aina hii huipokea kwa kicheko ambacho huwa si cha furaha bali hasira dhidi ya ukatili. Hakuna asiyemfahamu kwani sifa zake si haba katika visa vya kuwatia mbaroni wahalifu wa jinai ambao huwababaisha polisi, nusura wasalimike na kubaki raia watakatifu machoni mwa jamii. Yeyehutumia mbinu zake, akifuata njia azijuazo mwenyewe hata akahakikisha kila mhalifu akipokea tuzo ya madhambi yake. Natumaini umekwishamfahamu sasa. Kwa jina ni Joram Kiango.

Alizipata habari kwa njia ya gazeti la Daily News. Alikuwa amezikosa kwenye kipindi cha Majira na taarifa ya habari kwani asubuhi kama hiyo yeye huitumia kwa mazoezi ya viungo ambayo humchukua hadi saa moja unusu za kila asubuhi. Baada ya hapo huoga, hufungua kinywa na kisha kulifuata gari lake Peugeot 504 ambalo humchukua hadi Mnazi Mmoja iliko ofisi yake.

Asubuhi hii haikutofautiana sana na asubuhi zote zilizotangulia, isipokuwa kwamba baada ya kununua gazeti hilo na kukutana na habari za mauaji, ukurasa wa kwanza, alisimamisha gari kando na kuzisoma habari kwa tuo. Hivyo, aliingia ofisini mwake akiwa amechelewa dakika tano zaidi ya muda wake wa kawaida. Tabasamu lilikuwa bado liko wazi usoni mwake wakati alipoingia ndani na kulakiwa na katibu wake, Neema Iddi.

“Ya nini furaha yote hiyo asubuhi kama hii?” Neema alimwuliza baada ya salamu za kawaida. “Ah, sijui kwa nini nimeuliza. Kama sikosei nadhani umekwishasoma gazeti la leo.”

“Ni kweli dada yangu,” Joram alimjibu akimsogelea Neema. “Inashangaza watu wanavyozidi kupenda unyama zaidi ya utu.”
Kimya kifupi kikafuata. Katika kimya hicho tabasamu la Joram lilitoweka na sura yake kuvaa sura ya kikazi, sura isiyo na mzaha. Kisha, ghafla, hali hiyo ilitoweka na tabasamu kuchukua tena nafasi yake aliposema, “Kitambo kirefu mno kimepita tangu nilipopata nafasi ya kuichangamsha akili na mwili wangu. Nadhani wakati huo umewadia tena.”

Neema aliukunja uso wake kidogo, macho akiyakaza kumtazama Joram. Kama ilivyo kwa msichana yeyote mwenye sura nzuri, kwa Neema pia kukunja uso haikuwa chochote. Nia yake ya kuufanya uso wake uonyeshe ama hasira ama huzuni haikuzaa matunda yoyote. Badala yake iliifanya sura izidi kuvutia, izidi kutamanika, jambo ambalo ilifanya tabasamu la Joram ligeuke kuwa kicheko.

“Usicheke Joram. Nilichotaka kusema ni kwamba unadhamiria tena kujiingiza katika mkasa huu wa kutisha? Kwa nini siku zote unakuwa na kiu ya kuyaweka maisha yako hatarini? Nadhani hujui. Hivyo nitapenda kukufahamiisha kuwa vile vitendo vyako vya kumnasa mwuaji wa kule Arusha yuko mtu mmoja ambaye ameyaandikia kitabu matukio yote muhimu yaliyotokea. Nimekisoma kitabu hicho Joram. Nimeona ulivyoponea chupuchupu ingawa ulinilaghai kuwa kumnasa mtu huyo kwako ulikuwa kama mchezo tu.”

“Nini? Kuponea chupuchupu?” Joram aliuliza, “Nadhani watu hawajanielewa bado. Yote yaliyotokea ni mbinu ambazo zilipangwa hatua kwa hatua, kwa hadhari na uangalifu…” alisita kumeza mate. “Mbinu hizohizo zitatumika kumnasa mtu huyu ambaye ameua watu wawili wasio na hatia. Na zitaendelea kutumika katika harakati zangu zote za kusafisha mbegu chafu isiyostahili kuota katika jamii hii, jamii ambayo inakusudia kuinua haki na usawa si ukatili na vitisho. La, sistarehe kamwe.”

Mzaha ulikuwa mbali na sauti ya Neema aliporudia tena tamko ambalo humtoka mara kwa mara, “Jihadhari Joram.”

“Kujihadhari kutasaidia nini? Kama kutanisaidia mimi kamwe hakuwezi kuisaidia jamii inayotishwa na kuonewa. Na kama ujuavyo, kila mtu aliyezaliwa katika jamii fulani hakuzaliwa kwa manufaa yake binafsi bali kwa manufaa ya jamii nzima. Wazo hilo, likijengwa na ushirikiano ndio msingi wa maendeleo yote duniani. Bila hivyo hadi leo bado dunia ingekuwa pori na watu tusingetofautiana na wanyama. Utakubaliana na mawazo yangu endapo utawafikiria wanasayansi waliotuletea matibabu na nyanja za kurahisisha maisha, mafundi ambao wametengeneza vitu mbalimbali; watunzi ambao hutuburudisha kwa riwaya na mashairi ya kuvutia, n.k. bila juhudi zao tungekuwa katika hali gani? Mimi pia nina wajibu wa kuisaidia jamii kwa njia zangu, au siyo mpenzi?

“Mh!” Neema aliguna badala ya jibu.

Ingawa Joram alimweleza Neema nia yake na kujishirikisha katika harakati za kumsaka mwuaji wa vifo hivyo, lakini bado hakuwa na fununu wala mwanya wowote ambao ungemwezesha kumtia mkononi mwuaji huyo. Habari pekee aliyokuwa nayo ni ile ya vifo tu, kifo cha ‘Bwana Ukeke Maulana, Meneja Mkuu wa kiwanda cha kutengeneza rangi za nguo’ na ‘mzee Mohamed Matoke, aliyekuwa mfanyabiashara maarufu jijini,’ pamoja na kujua kuwa Bwana Matoke aliibiwa maelfu ya fedha yake na Ukeke kuibiwa injini na vyombo kadhaa vya gari. Ni hayo tu aliyoyafahamu. Hakujua chochote zaidi ya gazeti lilivyomweleza. Hivyo, bado alihitaji kujua mengi.

Tatizo lilikuwa aanzie wapi, kuutafuta mkondo. Hakumfahamu yeyote kati ya marehemu hao kwa sura wala picha. Hakuyafahamu makazi yao wala makazini kwao. Yote hayo yalikuwa na umuhimu mzito kumwezesha kuanza uchunguzi wake. Aanzie wapi! Alijiuliza. Akajiketisha vyema kitini mwake na kujiwashia sigara.

Baada ya kuwaza sana alijikuta akilazimika kuanzia uchunguzi wake palepale ambapo hakupenda kuanzia, polisi. Ni wao ambao walifahamu mengi ambayo angependa kuyafahamu. Kadhalika, ni wao waliokuwa na uwezo wa kuweza kufahamu kwa urahisi zaidi mambo mengi wanayohitaji kuhusu mienendo ya marehemu. Ugumu aliouona katika kuwakabili ni ile hofu ya kutoshughulikiwa kikamilifu. Vilevile yeye machoni mwa polisi si lolote zaidi ya kijana “mtundu apendaye kuyahatarisha maisha yake bure!” hivyo, uwezekano wa kuyapata yote aliyoyataka ulikuwa hafifu mno. Hata hivyo, maadamu haikuwepo njia nyingine aliamua kuwafuata.
Aliitupa sigara yake iliyokuwa imeungua nusu. Katika kasha la taka na kuinuka kutoka nje.

“Nafika polisi mara moja,” alimweleza Neema alipoona akimtazama kwa macho yanayouliza.

“Polisi tangu lini?”

“Leo, naanza.”

Isikupite Hii: Pasipoti Ya Gaidi ‘hujuma Na Uzandiki’ – EP01

Akatoka na kuingia katika gari lake. Akalitia moto. Lilipoondoka aliliendesha kwa mwendo wa polepole, kichwani akipanga kwa uangalifu vipi afaulu kupenya hadi katika siri za polisi juu ya vifo hivyo.

Kituoni alipokelewa kama mtu yeyote ambaye alikuwa na shitaka au kesi. Polisi wanne waliokuwa nyuma ya meza kubwa wakisubiri matatizo walimtazama, wakavutiwa na ubora wa sura, umbile na mavazi yake. Kisha waliyasahau haya na kumhoji kwa sauti za kikazi. “Tukusaidie nini?” mmoja wao alitamka.

“Nina tatizo kubwa,” Joram alimjibu. “Tatizo ambalo linahusiana na kifo cha mjomba wangu. Anaitwa mzee Matoke…”

“Alaa kumbe ni wewe?” mwingine alidakiza. “Pole sana, ndugu yangu. Amekufa kifo cha ajabu sana.” Akasita. Kisha alibadili sauti na kuirejesha katika mfumo wa kikazi. “Lakini sijui tunaweza kukusaidia nini. Au unahitaji barua ya kwenda jumba la maiti hospitali kumchukua? Ama…”
“Hapana si hilo lililonileta kwasasa,” Joram alisema tena, akiruhusu tabasamu la namna ya msiba kuuvaa uso wake. “Nadhani yanipasa kujieleza kwa urefu kidogo ili nieleweke. Nina miaka mnne tangu nilipoonana na marehemu mjomba wangu kwa mara ya mwisho. Mnionavyo hapa ndio kwanza nawasili toka Nairobi ambako nasomea shahada ya pili Chuo Kikuu. Ya kwanza niliipata Moscow, Urusi. Jana tu ndio nimepata simu ya kifo hiki. Kwa hiyo, ninachoomba ni kufahamishwa mmefikia wapi katika juhudi zenu za kumpata mwuaji.”
“Hilo ni jambo gumu, ndugu yetu,” aliyesema ni askari mwingine ambaye alikuwa kimya muda wote. “Kifo chenyewe ni cha ghafla sana na jiji hili ni kubwa kiasi. Si rahisi kumpata mhalifu kwa saa chache kama hizi.”
“Hayo nayafahamu,” Joram alimjibu. “Ninachohitaji ni fununu yoyote ile, kwani naona ikibidi nitamwajiri mpelelezi wa kulipwa alishughulikie suala hili.”
“Nimekuelewa. Lakinji ukweli ni kwamba hatuna fununu yoyote ya haja.”
“Hata juu ya yule mwingine? Nani vile jina lake?” Joram alijitia kusahau.
“Yule Meneja? Ukeke…”
“Oh, yes. Kitu kama hicho.”
“… hatuna lolote tujualo. Isipokuwa tumepata fununu kuwa gari lake lilionekana kwa mara ya mwisho mbele ya West Bar huko Buguruni. Hilo tu. Wala sioni kama hilo lina msaada wowote.”
“Huyu bwana naona awaone jamaa wa upelelezi huenda wakamsaidia. Mwone mzee, Inspekta Kombora, ambaye atakuwezesha kuyapata yote unayoyahitaji,” Yule askari aliyemkaribisha alisema. “Pita hapa uende huko juu. Utaona chumba kilichoandikwa MKUU WA KITUO.”
Joram akalifuata dole hilo.
Alipoufikia mlango wa chumba alichohitaji aliugonga na kuufungua. Macho yaliyomlaki hayakuwa ya mwingine zaidi ya Kombora mwenyewe. Alikuwa mchovu kwa mawazo kiasi kwamba aliduwaa akimtazama Joram alivyojikaribisha mwenyewe na kujiketisha juu ya kiti kilichomwelekea.
“Samahani mzee. Mimi ni mjomba wake marehemu mzee Matoke. Ninahitaji kufahamu chochote mlichokwishapata juu ya mauaji hayo. Yaani…” Joram alilazimika kusita pindi mwenyeji wake alipoangua kicheko na kusema.
“Wewe ni nani? Mjomba wake marehemu? Naona umejisahau. Nitakukumbusha. Wewe ni Joram Kiango unayejitia mpelelezi na kujidanganya kuwa una hekima za kiupelelezi zaidi ya polisi. Nakufahamu sana kijana. Huwezi kunilaghai hata kidogo. Labda ningekutupa ndani kidogo kwa kosa la kulaghai na kujaribu kuiba habari hata polisi ili ujue kuwa ujanja wako ni duni na hafifu. Leo nitakusamehe kwa kuwa ni mara yako ya kwanza.” Akasita na kumeza mate kidogo. “Nia yako ilikuwa chafu, uibe habari za kesi hii na kesho ujitangaze kuwa umempata mwuaji ambaye polisi wameshindwa kumpata. Mbinu hafifu.”
“Pamoja na kukusamehe, nakuonya ujiepushe na kesi hii. Hii si kesi ya kuingilia papara kwa mbinu zako za kujihatarisha na kubahatisha ambazo unaita upelelezi. Hii ni kesi ya hatari. Kwa usiku mmoja tu, kufa watu wawili, kifo cha aina moja! Jihadhari sana. Sawa?
Joram hakujibu chochote.
“Sasa nenda zako. Nenda ukijikumbusha kuwa polisi haihitaji msaada wako katika kazi hii,” alimaliza na kumfukuza Joram kwa kujiinamia katika mafaili yake yaliyotapakaa mezani.
Joram akainuka na kutoka nje.
Joram alilisahau onyo la Kombora, mara tu alipotoka nje ya jengo hilo la polisi. Hakuwa tayari kutii amri hiyo kwasababu kadha wa kadha, moja ikiwa ile njaa yake ya siku zote; kucheza na hatari. Njaa hiyo huifanya damu yake kuchemka na kutopoa hadi anapokipata akitakacho. Sababu nyingine ni kule kuamini kuwa , kama raia mwema, ilikuwa haki na wajibu wake kushiriki katika kitendo chochote ambacho kilidhamiria neema kwa taifa. Wala sio kwamba alimlaumu Inspekta Kombora kwa maneno aliyompa, la. Alijua kabisa kuwa, kama polisi mwenyewe hadhi ya ujuzi, hakuwa na sababu ya kufurahia Joram anapompata adui hatari ambaye jeshi zima la polisi limeshindwa. Ni kweli kuwa kupatikana kwa adui huyo ni kuzuri, lakini vilevile kwa polisi ni aibu.
Wakati akiyawaza hayo alikuwa safarini kuirejea ofisi yake. Alipofika jengo ambalo ofisi yake ilikuwemo aliliegesha gari lake katika sehemu yake ya kawaida na kuiendea lifti ambayo ilimpeleka hadi mlangoni kwake. Maandishi yake ambayo yaliandikwa na msanii hodari yalimlaki yakisema “JORAM KIANGO – PRIVATE INVESTIGATOR. Akafungua mlango na kumwona Neema akijaribu kuficha kitambaa alichokuwa akifuma.
“Mara hii umerudi?” Neema alimwuliza.
“Ndio. Nina kazi moja ambayo nataka uifanye mara moja.”
“Kazi ipi?”
“Chukua kitabu cha orodha za simu, unifahamishe makazi ya marehemu Ukeke na Matoke. Ukeke Maula alikuwa meneja wa…”
“Najua. Nimesoma gazeti,” Neema alimjibu akiinuka kuiendea safu ya vitabu.
Joram alimtazama kwa muda. Kisha akampita kuiendea ofisi yake ya ndani. Huko alijiwashia sigara na kutulia miguu juu ya meza akiwaza.
Baada ya muda Neema alimletea namba za simu pamoja na maelezo yote kama alivyohitaji. Ofisi ya Ukeke ilikuwa katika barabara ya Pugu. Mara moja akamuaga Neema kwa tabasamu na kuondoka ofisini kuelekea huko. Baada ya kupita viwanda kadha wa kadha kama Tegry, KIUTA, Bora na Sigara akafikia ofisi aliyohitaji. Akasimamisha gari na kuiendea.
“Nahitaji kumwona Kaimu Meneja,” alimweleza askari wa mlangoni.
“Tatizo gani? Kama ni kazi andika barua,” alitamka bila ya kumtazama Joram.
“Naonekana kama mwomba kazi? Joram alihoji baada ya kicheko cha hasira.
Askari huyo akamtazama kwa makini. Ndio kwanza akayaona mavazi yake yaliyomkaa kitanashati, umbile lake lenye nguvu na uso wake wenye dalili za madaraka na kutosheka. Nuru iliyokuwa ikitoka katika macho yake ikamfanya askari huyo ajikute akimwomba radhi. “Samahani sana. Nenda mlango huu hadi utakapoiona ofisi yake,” hatimaye Yule askari alimwelekeza.
Joram akaufuata mkono wake.

Kaimu meneja alikuwa mtu mcheshi, hasa baada ya Joram kujitambulisha kama mpelelezi. Hakudai kitambulisho wala kuuliza maswali. Badala yake alieleza yote ambayo Joram alihitaji kufahamu juu ya maisha na mienendo ya marehemu Ukeke. Akafahamishwa kuwa marehemu alikuwa ameoa na kuzaa watoto kadhaa, kwamba miaka miwili iliyopita alikuwa ametumwa ng’ambo kuongeza ujuzi wake na aliporudi akawa mroho wa anasa zote; pombe, wanawake nakadhalika. Ingawa kaimu huyo hakusema, lakini katika maelezo yake Joram aligundua kuwa mapenzi ya starehe yalimfanya marehemu kupokea aina yoyote ya rushwa toka kwa mtu yeyote anayehitaji chochote toka kwake.
“Nakushukuru sana ndugu. Lakini kabla ya kuondoka naomba unifahamishe ilipo nyumba ya marehemu,” Joram alisema akiinuka.
“Iko mbali kidogo. Sehemu za Upanga. Nyumba namba ishirini na moja. Mtaa…”
“Nakushukuru tena ndugu yangu,” alisema huku akitoka.

ITAENDELEA

SOMA: Mikononi Mwa Nunda – EP02

Ngoma 10 Bora za Mwezi may, 2020.

Leave a Comment