SIMULIZI

Mikononi Mwa Nunda – EP03

SIMULIZI Mikononi Mwa Nunda – EP03
SIMULIZI Mikononi Mwa Nunda – EP03

Simulizi : Mikononi Mwa Nunda
Sehemu Ya Tatu (3)

Wakaendelea na safari yao, peke yao, katikati ya usiku mzito, usiku ambao ungeweza kutisha sana kama mwezi usingekuwa mpevu kiasi cha kutoa nuru ya kuvutia.

Kutembea na msichana huyo, usiku kama huo, akiwa na kanga moja bila dalili yoyote ya nguo za ziada ndani, kulimfanya Makonko asahau tatizo aliloliacha nyuma na badala yake kujikuta akiwaza vipi aitumie nafasi hiyo pekee kumfaidi binti huyo.
Aliwapenda sana wanawake wa aina hii, wanawake wenye dhiki, kwani hawana nafasi ya kutoa amri wala kukataa amri yake. Hakuwapenda wanawake wa kudumu kwa ajili ya hofu ya kuupoteza uhuru wake na kuwa mtu wa kupangiwa saa za kurudi nyumbani, watu wa kuzungumza nao, na mambo mengine kadha wa kadha ya kike.

“Ulikuwa umejificha wapi, msichana mrembo kama wewe?” alianza maongezi baada ya kipindi cha ukimya.

“Dar kubwa hii, ndugu yangu.”

“Ni kweli.”

Kimya kikawameza tena. Safari hii ni msichana huyo aliyeizima kimya hiyo kwa kusema polepole, “Baridi!”

“Kweli, inatisha.”

“Unajua kaka, sina hamu ya kurudi nyumbani saa hizi,” msichana aliongeza.

“Kwanini?” Makonko aliuliza huku moyo ukimdunda kwa shahuku.

“Tatizo ni dogo tu. Nilipoondoka nilimwaga rafiki yangu tunaye lala naye chumba kimoja, kwamba nisingerejea hadi kesho. Naye aliposikia hivyo akamwalika mpenzi wake. Kwa hiyo, nikienda itakuwa usumbufu kwao na kwangu. Unayajua maisha ya mjini yalivyo siku hizi, watu wawili; chumba kimoja; kitanda kimoja.”
Makonko hakujua ajibu nini. Ilikuwa bahati yake pekee. Tatizo lake pia lilikuwa malazi. Asingethubutu kurejea chumbani kwake ambako aliacha maiti mbili. Hakujua ampeleke wapi binti huyo.

“Tuna tatizo la aina moja, dada yangu,” akalaghai. “Kinachonifanya nitembee usiku kama huu ni kitendo alichonifanyia rafiki yangu tuliyekuwa tukichangia chumba. Kamleta mwanamke na kuanza kufanya naye mapenzi mbele yangu bila angalao kuzima taa. Nilipoamka na kuzima nimesababisha ugomvi ambao umeishia kututenganisha. Hivi unionavyo sijui niendako.”

“Pole sana.”

“Ni tatizo dogo sana. Kesho asubuhi nitapata chumba changu binafsi.”

Binti huyo aliguna tu. Wakaendelea na safari yao, hatua moja baada ya nyingine. Kwa mara nyingine tena, binti huyo akanong’ona kitu fulani kuilaani baridi. Halafu alisimama ghafla na kuuelekezea mkono mbuyu mkubwa uliokuwa hatua kadhaa kando ya barabara. “Unaonaje kaka?” akasema, “Pale panaweza kutuhifadhi hadi kesho alfajiri tutakapoachana. Tutaishinda baridi kwa kukumbatiana na kustareheshana. Miili yetu ina afya na uhai. Au siyo kaka?”

Makonko akasita kujibu.

“Usihofu kaka. Utakuwa usiku mtamu wenye mapenzi na mahaba kuliko yote niliyowahi kuyafanya. Sitausahau usiku huu kamwe. Twende zetu. Hakuna mtu atayepita hapa saa hizi. Twende,” mkono wake ulimkumbatia Makonko shingoni na kumzidishia njaa aliyokuwanayo.

Bila kauli akamfuata. Walipofika chini ya mbuyu binti huyo alimkumbatia vyema Makonko na kumbusu. Kisha akamwachia na kuifungua kanga yake moja. Akaivua na kuitupa kwenye moja ya mizizi ya mbuyu huo iliyotambaa juu ya ardhi.

“Njoo,” akanong’ona.

Alikuwa kama alivozaliwa, uchi; uchi wa mnyama. Makonko akajikuta akimsogelea huku vidole vyake vikitetemeka katika kufungua vifungo vya suruali yake. Ghafla akaona kitu kikimeremeta katika mkono wa kuume wa msichana huyo, kitu ambacho hakutegemea kukiona wakati huo.

“Ni nini hi…” alijaribu kuuliza. Sauti yake ikamezwa kwa mshtuko wa maumivu makali yaliyosababishwa na kitu hicho,chenye baridi, kikipenya ghafla kifuani mwake. Ndipo alipojua ni kitu gani, kisu. Kabla hajajua afanye nini kikapenya tena ubavuni mwake. Kilipopenya kwa mara ya tatu alihisi kikimpokonya uwezo wa kusimama. Kwa mara ya kwanza alijikuta akiitii amri, amri ya kisu; na kuanguka kifudifudi.

SURA YA NNE

ILIKUWA ikikaribia kukamilika saa nane za usiku. Kombora alikuwa hajatongoa hata lepe moja la usingizi kwaajili ya mawazo juu ya kushindwa kwa mpango wake wa kumnasa mmoja wa majambazi haya ambayo yaliua bila huruma kwa haja ya kujipatia fedha. “kwa nini mpango ule haukufaulu? Kwanini mmoja wao hakutokea kuchukua fedha iliyotengwa? Kwa nini?” alijiuliza maswali hayo kwa mara ya elfu…

Tendwa alikuwa kamthibitishia kuwa hakuzungumza na mtu yeyote alipokuwa akienda polisi. Kadhalika, ilikuwa dhahiri kuwa hakumwambia mtu yeyote mpango ule, kwa hofu ya kuhatarisha maisha yake. Vipi basi majambazi hayo yakahofu kujitokeza? Kwa vipi?… kushindwa kujibu maswali hayo kukamfanya aamini kuwa kikundi cha majambazi hayo kilikuwa kikubwa sana, chenye nguvu na mbinu ambazo si za kuchukulia mzaha. Vinginnevyo isingekuwa rahisi kugundua siri ya polisi, siri ambayo ilifanyika katika taratibu zote za kipolisi na ikiwa baina ya polisi wachache wenye vyeo vinavyostahili.

Jambo jingine linalomwuma rohoni kama jipu lililowiva ni kule kusoma habari zote hizo, za barua aliyoipata Tendwa, katika magazeti; Habari kamili zikiwa zimeeleza yote yaliyoandikwa katika barua hiyo,kuitaja dhamira ya barua na kumtaja mwandishi wake; NUNDA MLA WATU. Hakujua waandishi hao walizipataje habari hizo.

Alikuwa amewaonya askari wake wote, hata mmoja asizungumze chochote juu ya barua hiyo. Lakini kwa mashangao wake, alipoamka kesho yake tu alikutana na gazeti ambalo lilipambwa kwa habari hizo. Hata hivyo, kilichomtatiza si vipi habari hizo zilifika gazetini bali matokeo yake baada ya kusomwa na kila mtu, pamoja na majambazi yenyewe. Jambo ambalo yangefanya majambazi hayo ingekuwa kutumia mbinu mpya baada ya mbinu yao ya awali kufahamika, ama yaamue kutoweka kabisa, yasikamamtwe tena. Hilo hakupenda litokee, alichohitaji kuliko chochote ni kuyapata yakiwa hai au maiti.

Simu ikalia. Akaitazama kwa hasira bila nia yoyote ya kujibu. Hakuzipenda asilani simu za usiku kama huu. Mara nyingi zilimletea habari mbaya, habari ambayo humlazimu kukiacha kitanda chake na kwenda mitaani. Angeweza kuiacha iendelee kulia. Hata hivyo, kwa kuwa kelele zake hazikumruhusu kustarehe, alinyoosha mkono wake na kuichukua. “Kombora hapa, nani mwenzangu?”

“Inspekta. Hapa ni kituoni,” upande wa pili ulijibu.

“Enhe?”

“Kuna mauaji yametokea, mzee.”

“Mauaji!” akafoka kwa hofu. “Nani aliyekufa? Tendwa? Usiniambie…”

Kicheko kidogo kikasikika upande wa pili. “Sio Tendwa, Inspekta,” sauti iliongeza. “Tendwa yuko hai kabisa nyumbani kwake. Hii labda tuseme kidogo ni habari njema…”

“Nani aliyekufa?” Kombora alimkatiza kwa kufoka.

“Majambazi wawili ambao tulikuwa tukiwahitaji kwa muda mrefu. Nadhani unawafahamu. Kwa majina ni Togo na Matoro, magaidi wa kikundi cha White Satans. Wamekutwa maiti, matundu ya risasi yakiwa katika vichwa vyao,” akasita kidogo kusubiri swali kwa Kombora. Alipoona kimya, akaongeza, “Wameokotwa huko Buguruni na raia ambao walisikia mlio wa bastola toka katika nyumba hiyo. Walipokiendea chumba hicho walikuta maiti hizo mbili bila ya mwuaji wala silaha iliyotumika. Ndipo wakapiga simu polisi.”

“Umefanya nini zaidi ya kunipigia simu?”

“Nimeiarifu hospitali pamoja na kuwatuma makachero wetu wa zamu. Sasa hivi naamini wanapima alama za vidole. Kuna la zaidi, mzee?”

“Nadhani umefanya yote,” Kombora alisema akiweka simu chini na kuduwaa wima kwa muda mrefu.

‘Habari njema!’ aliwaza akiyarudia maneno ya yule askari. Habari njema wakati bado watu wanachukua sheria mikononi mwao na kuhukumu mpaka adhabu ya kifo! Habari njema? Kwa vipi wakati muuaji huyo bado yuko hai na huru mahala fulani katika jiji hilihili, tayari kufanya lolote ambalo linaweza kuhatarisha usalama. La, kwake haikuwa habari njema kamwe. Ilikuwa habari mbaya kama zote zilizotangulia, habari ya kuchukiza, habari ambayo hakuipenda hata chembe.
Kwake habari njema ingekuwa kumnasa kiongozi wa kikundi hicho, pamoja na wafuasi wake na kuhakikisha mahakama ikiwaelekeza kwenye adhabu moja tu, kitanzi. Hilo tu. Tatizo lilikuwa afanye lipi kuhakikisha watu hao wananaswa upesi.
Wazo hilo liliupokonya usingizi wake wote. Ingawa alijilaza kitandani, akifanya hili na lile asinzie, lakini usingizi haukumjia.
Kunako mapambazuko, usingizi hafifu ulimjia. Alipojaribu kuubembeleza simu nyingine ililia tena na kuupokonya kabisa usingizi wake. Kwa hasira aliamka kabisa, akavaa nguo zake za kikazi na baadaye kuijibu simu hiyo kwa sauti nzito.
“Kombora hapa. Nani mwenzangu?”
“Ni mimi, mzee. Samahani kwa kukusumbua tena. Kuna…”
“Wewe nani? Askari wa zamu tena!… kuna nini?… Enhe! La…”
Alisikiliza kwa makini sana kisha akakitua chombo cha simu na kujitupa juu ya kochi akiwaza. Kifo kingine tena! Mtu wa tatu katika usiku mmoja! Mwanaume vilevile. Jambazi lililokuwa likitafutwa sana vilevile. Limekutwa maiti. Chini ya mbuyu, uchi! Silaha iliyomwua ikiwa kisu kama walivyokufa Ukeke na Matoke! Buguruni kulekule! Na huyu mwuaji anayeua wauaji wenzake? Na kwa nini anafanya hivyo? Ama ni vikundi vya majambazi ambavyo viko vitani vikipigania kitu fulani? Pengine! Ama… Au…
Aliwaza lile na hili. Mawazo yake yote alihisi yakiwa hayana jibu alilohitaji. Hatimaye, akatoka nje na kupanda gari lake ambalo alilielekeza kituoni.

***
Na sasa Nunda alitukuka mfano wa mvua katika nchi kame. Jina lake lilitawala maongezi yote, akitajwa kwa sifa zote za unyama na ukatili usiokadirika. Usiku na mchana maiti ya watu waliokotwa huko na huko katika jiji la Dar na vitongoji vyake. Kila maiti yalikutwa yakiwa na waraka ulioandikwa kwa wino mwekundu ukimtaka ama kutoa fedha ama kumwua fulani.
Hofu ilivyotawala katika mioyo ya wananchi ilifanya waanze kuamini kuwa Nunda alikuwa jambazi aliyekubuhu ambaye aliongoza jeshi zima la majambazi. Vinginevyo angewezaje kulitetemesha jiji zima, akiepuka kila mtego wa polisi kama mzaha? La, hasha Nunda ni Nunda kweli, Nunda mla watu!
Polisi walifanya yote ambayo wangeyafanya. Yote, mema kwa mabaya, wakimkamata yeyote aliyedhani angeweza kuwapa walao fununu kwa kashfa hiyo. Kila mmoja alihojiwa kwa maneno na vitendo lakini jibu lilikuwa moja tu, kwamba hawakuwa watumishi wa Nunda; pia, hawakujua chochote juu yake. Zaidi, wote walimwogopa kama raia wengine.
Hata Joram, ambaye hupenda kupambana na visa vya aina hii, alijikuta akigutuka kidogo kwa mafanikio ya huyo kiumbe aliyejiita Nunda. Juhudi zake zote za kumfahamu, amfikishe mbele ya polisi, zilielekea kutomzalia matunda. Alijitahidi kuchunguza maisha ya marehemu wote kwa makini. Aligundua mengi ya kusisimua. Lakini alichohitaji hasa hakukipata.
Kesi hii ilianza kumsisimua mara alipoisoma gazetini ile barua toka kwa Nunda ikimwendea Tendwa, ikidai fedha. Barua hiyo aliiona kama hatua ya kwanza ya kumfahamu mwuaji. Hilo likamfanya arejee tena majumbani kwa akina Ukeke na Matoke akapeleleza iwapo kulikuwa na fununu yoyote ya marehemu hao kupokea barua kama ile. Jibu lilimshangaza sana, kwamba haikuwepo dalili ya kitu kama hicho. Aliliamini haraka jibu hilo. Si kwa kuwa alitafuta kila mahala na kutoona nyaraka hizo tu, la, sababu kubwa ilitokana na jinsi alivyoyaona maiti ya Ukeke katika picha. Yalikuwa yamelalia usukani kwa utulivu mno. Kadhalika, uchunguzi wake ulimwonyesha kuwa kutwa nzima ya mwisho, katika maisha ya marehemu hao, hakikutokea kitu chochote kisicho cha kawaida katika tabia na mienendo yao. Hata huko West Bar ambako marehemu Ukeke alikunywa chupa yake ya mwisho, wahudumu walikuwa na hakika kuwa aliinywa katika hali ya kawaida na kuondoka kwa mwendo wa kawaida.
Kwa bahati mbaya, Joram hakufanikiwa kuzungumza na msichana ambaye inasemekana alimhudumia marehemu huyo hapo baa. Aliambiwa kuwa binti huyo aliziacha bia zake na kutojulikana alikokwenda, kama ilivyo tabia ya wauza baa wote. “Nawezaje kumpata?” alihoji.
“Nani atajua? Aweza kuwa amempata wake wa kumweka ndani. Ama amepata baa nzuri zaidi,” lilikuwa jibu la mwisho alilolipata hapo West Bar.
Mchana huu alitulia katika ofisi yake, kimya, kinyume cha kawaida yake. Ingawa macho yalikuwa yakitazamana na yale ya Neema Iddi ambayo, kama kawaida, yalikuwa kama yachekayo; Joram Kiango hakuwa tayari kukipokea kicheko hicho. Uchungu mkali uliyameza yote ambayo angependa kusema. Uchungu huo ulitokana na hasira ya kuona ikishindikana kumpata mhalifu mchafu kama NUNDA na kundi lake. Kwake lilikuwa tusi. La, zaidi ya tusi kwa nchi nzima, mtu kama NUNDA kuendelea kuishi miongoni mwa raia wema. Aliamini kuwa haki ya mtu au watu kama hao ilikuwa kuishi gerezani akisubiri kitanzi. Ni hilo alilolipenda kuliko yote. Tatizo lilikuwa alifanikishe vipi? Vipi angalau amjue huyo NUNDA? Mbinu zake zote za kupeleleza, alihisi zikielekea kukwama. Afanye nini zaidi? Ni kutokuwa na jibu la swali hilo ambako kulimtia uchungu na hasira kiasi cha kuipokonya tabia yake ya ucheshi na uchangamfu.

Sigara iliyokuwa mdomoni mwake ikielekea kuteketea bila ya kuvutwa angalao mkupuo mmoja. Aliitupa katika kasha la takataka na kuiwasha nyingine. Hiyo aliivuta na kuurusha moshi mwingi angani kwa mkondo mnyoofu. Macho yake yaliufuata mkondo huo wa moshi hadi ulipotoweka angani. Wakati akiusukuma mkupuo wa pili alisikia mlango ukibishwa. Alipogeuka kutazama alimwona Neema akisimama kando ya mlango kumruhusu yeyote aliyebisha kuingia.
Mgeni alikuwa mwanamke. La. Msichana, msichana ambaye haikuwa rahisi kumwita mfupi au mrefu, wala mwembamba au mnene. Alikuwa katikati ya yote hayo. Umbo hilo likiwa limejaliwa mkatiko wa kike kiunoni, mjao wa kuridhisha nyuma na ngozi nyekundu inayomeremeta lilimfanya Joram Kiango ajikute ameinuka kitini kutaka kumlaki. Lakini alijiketisha hima mara alipojikumbusha hadhi inayostahili mbele ya wateja wake. Polepole, akavuta faili lililokuwa karibu na kuanza kulipekuapekua akijitia kazini.
“Sijui hii ndio ofisi ya Joram Kiango?” iliuliza sauti ya msichana huyo. Joram aliipima na kuona kuwa haikuwa na dosari. Ililistahili vilivyo umbo lake.
“Ndio hii,” Neema alimjibu.
“Yupo?”
“Yupo.”
“Nahitaji kumwona.”
“Karibu ukae basi,” Neema alimkaribisha akielekeza mkono kwenye kochi lililokuwa likiwasubiri wateja. “Kumradhi nimwulize kama yu tayari kuonana nawe,” Neema aliongeza akiuendea mlango uliokuwa wazi muda wote.
Neema aliufunga mlango nyuma yake na kumsogelea Joram, tayari kutamka neno ambalo Joram alilikatiza mara moja kwa kusema, “Mwache aingie.”
Msichana alipoingia ofisini humo na kuketi mbele yake, Joram alijikuta akitazama sura nzuri kuliko nyingi alizowahi kuzitazama, sura yenye kila kitu ambacho kinahitajika katika sura ya msichana mzuri, macho maangavu ambayo si kwamba yanavutia tu; bali pamoja na kushawishi; mashavu yaliyoumbwa kwa namna ya matunda pacha yanayostahili kubusiwa; pua iliyokamilika katika unyoofu na kinywa ambacho kilihifadhi meno… utafiti wa Joram ulikomea hapo kwa kutoyaona menohayo. Tabasamu dogo tu katika uso huo lingemfanya Joram ajisikie faraja na kusahau usumbufu wa kutwa nzima.

“Jisikie nyumbani dada,” Joram alitamka kumtoa ugeni.
“Ahsante.”
Ghafla Joram alihisi sura hiyo haikuwa ngeni sana kwake. Lazima amewahi kuiona mahala. ‘Wapi vile?’ alijiuliza. Msichana mzuri kama huyo, amemwona wapi? Katika majalada ya magazeti? Gazeti lipi! Sinema? La. Mara akakumbuka wapi alikomwona. “Dada nadhani uso wako si mgeni kwangu. Niliwahi kukuona mahala?” Joram alilazimika kusita alipoona mabadiliko ya ghafla yakiutokea uso wa msichana huyo. Uzuri wake ulitokomea na badala yake kuvaa dalili za taharuki.
“Wapi? Sidhani kama inawezekana. Mimi sio mwenyeji sana hapa,” alikana kwa sauti ambayo masikioni kwa Joram ilikuwa kama kujitetea badala ya kukataa kwa kawaida.
Joram akaruhusu moja ya vicheko vyake ambavyo aliamini humfanya kila msichana avionaye kuburudika. “Pengine nilikufananisha ingawa sio rahisi kwani ni wasichana wachache sana ambao wamebahatika sura na umbo kama hilo lako.”
“Lazima umenifananisha.” Msichana huyo alijibu. Tabasamu na maneno ya Joram havikumfanya atokwe na hali ya tahayari iliyoikumba sura na sauti yake.
“Si kitu dada yangu. Macho pia hukosea,” Joram alimjibu akimtazama kwa makini. “Unaonaje kama ukiniambia kilichokuleta hapa ili niweze kukusaidia.”
Msichana huyo alishusha pumzi kwa nguvu kabla ya kumjibu akisema, “Nina tatizo kubwa Bwana Kiango, tatizo ambalo ni la hatari mno katika maisha yangu. Niko hatarini. Nadhani nitakufa.”
“Huwezi kufa,” Joram alimjibu akimtazama kwa makini. “Sioni vipi msichana mzuri kama wewe ufe kirahisi. Itakuwa kama kuteketeza mbegu ya maua bora na kuacha hafifu. La, hufi kamwe, maadamu umefika kwa Joram Kiango.
Kama alikusudia kuona tabasamu, au angalau dalili za faraja kujitokeza katika uso wa msichana huyo, hakuiona. Uliendelea kuwa uso mzuri lakini uliopotoshwa kwa upungufu wa utulivu. Tahayari ilikuwa bado wazi machoni mwake. “Nitakufa Joram. Hujui tu. Tatizo lenyewe si dogo kama unavyowaza. Labda nikueleze kwa ufupi. Ni NUNDA anayehitaji roho yangu.”
“Nunda!”… Joram aliropoka kwa mshangao. Moyo ulimdunda na shahuku kumteka fikara zake zote, hata hivyo, aliuficha hima mshangao au shahuku iliyomkumba kwa kusema, baada ya kicheko kingine, “Nunda nini? Huyo mwendawazimu anayeangamiza watu? Usihofu chochote dada yangu. Changamka, jisikie furaha…”
Mgeni huyo alimkazia Joram macho yenye hasira. “Nadhani nimekosea kuja kwako,” alisema baada ya kitambo kirefu cha kimya. “Naona nimeupoteza bure muda wangu. Huelekei kuwa mtu anayemfahamu Nunda kikamilifu.”
“Simfahamu lakini nimemsikia tosha. Kwa kadri ninavyosikia visa vyake nimegundua kuwa yu mtu mwoga na punguani. Kila jambo analotenda linamwelekeza katika mikono ya sheria.”
“Kwa vipi?” sauti ya kike ilihoji.
“Kwa jinsi alivyo. Kujiita kwake Nunda kusichukuliwe kuwa kweli ni Nunda awezaye kula jiji zima la Dar es Salaam kama alivyofanya Yule Nunda wa hadithini. Hilo ni jina ambalo ametumia kuficha uoga wake tu. Nawafahamu watu wa kawaida, wafupi kama mbilikimo, ambao hujiita akina Twiga, Tembo au Simba. Ni majina tu.”
Wakati wote huo wa maongezi hayo Joram alikuwa kayakaza macho yake akimtazama mgeni wake. Aliona na kushuhudia jinsi macho ya mgeni yalivyokodoka kumtazama, katika hali yenye dalili za mshangao na hofu. Hofu hiyo ilitoweka polepole na nafasi yake kuchukuliwa na kitu kama tabasamu, tabasamu lisilo kamili, tabasamu la kwanza tangu walipoanza maongezi.
“Nadhani wewe ndiye mtu nimtakaye. Mtu shujaa asiyeogopa chochote,” msichana huyo alisema baada ya kutoweka kwa tabasamu hilo. “Nahitaji msaada wa kuokoa maisha yangu. Nunda amenitumia moja ya barua zake zinazodai roho yangu endapo sitampa fedha anayohitaji. Amenionya nikienda polisi kesho nitakuwa marehemu. Nikaona heri nije hapa kwako. Nasikia huna uhusiano na polisi. Tafadhali, nisaidie kabla ya kuingia katika mikono ya Nunda.”
“Bila tafadhali,” Joram alimkatiza akinyoosha mkono kuipokea barua iliyokuwa wazi mikononi mwa msichana huyo. “Niko hapa kutatua matatizo kama hayo, kuondoa vitisho na ukatili wa kiendawazimu miongoni mwa jamii. Ebu niitupie jicho barua yenyewe.”
Akaanza kuisoma. Ilikuwa barua kama zile nyingine ambazo zilitolewa katika magazeti. Barua fupi, iliyojaa vitisho na majisifu. Kama nyingine zilizotangulia hii pia iliandikwa kwa mashine ya chapa. Aliipitia harakaharaka, kisha akamgeukia mgeni wake na kusema, “Nimeuona uendawazimu mwingine wa huyu mwendawazimu ajiitaye Nunda. Sina shaka kuwa nitamtia mbaroni hivi karibuni.”
“Unaweza Joram!” Yule msichana alisema kwa furaha iliyojaa mshangao.
“Usihofu nitampata tu. Kwasasa nadhani umewadia wakati wa kufahamiana zaidi. Yaani unitajie jina lako, unakoishi, kazi yako na yote ambayo yanaweza kumfanya Nunda akuchague wewe kama mwanamke wa kwanza katika hatua yake ya umwagaji damu.”
Msichana huyo aliukunja kidogo uso wake. Kisha aliukunjua na kusema, “Labda nina mkosi zaidi ya wanawake wote. Kwa kweli, inashangaza, mimi, mtoto mdogo, kuwa wa kwanza katika mkasa huu. Lakini hii isikushangaze sana. Nadhani nia ya Nunda ni pesa. Amepata fununu ya urithi nilionao. Anauhitaji…”
“Urithi! Umerithi utajiri mkubwa?”
“Sio mkubwa sana. Lakini unanitosha kula maisha yangu yote bila ya kufanya kazi.”
“Nadhani ingebidi unieleze polepole, hatua kwa hatua. Anza kwa kunitajia jina lako.”
“Jina langu ni Adela Msufi mzaliwa wa Mwanza. Mama yangu alifariki nikiwa bado nanyonya. Baba amefariki miaka miwili iliyopita. Wote walikufa kwa magonjwa yasiyoelezeka. Jirani wakanieleza kuwa walirogwa. Wazo hilo nilielekea kulipuuza lakini ikanilazimu kulikubali baada ya kujiona nikipata maradhi ya ajabuajabu mara tu ilipofahamika kuwa mimi ndiye niliyeachiwa urithi wote. Hakukuwa na mtu mwingine wa kurithi mali hizo kwani mimi ni mtoto wao pekee,” Adela alisita kidogo kuiacha hadithi yake izame katika fikra za Joram.
“Hivyo nikaamua kuuza mali zote za wazazi wangu na kuondoka mkoani hapo hadi Dodoma ambako niliishi miezi kadhaa. Mazingira ya Dodoma hayakuniridhisha. Nikajivuta tena hadi hapa Dar. Mpaka sasa bado naishi mahotelini, sijapata nyumba inifaayo.” Akapumua kwa nguvu na kumgeukia Joram. “Nadhani hayo yanakutosha.”
“Kidogo yanatosha,” Joram alimjibu. “Inasikitisha sana msiba uliokupata, ndugu yangu. Pole sana. Unaishi hoteli ipi?”
“Nilikuwa nikiishi Afrikana. Lakini mara tu baada ya kuipokea barua hiyo nimehamia hoteli moja ndogo hapo Kariakoo. Inaitwa Mzalendo.”
Joram alifurahia kuisikia hoteli hiyo. Alikuwa anaifahamu ilipo. “Una hakika hakuna mtu aliyejua kuwa umehamia hoteli hiyo?” akamwuliza.
“Hakuna. Niliwaaga wote wanijuao kuwa nakwenda Zanzibar. Nadhani waliniamini.”
“Inawezekana. Na barua hii, uliipataje?”
“Yaani… Sijakuelewa.”
“Ilikufikiaje?”
“Aha! Nadhani ilipenyezwa chini ya mlango wangu. Niliiona asubuhi nilipokuwa nikitaka kufungua mlango.”
Kikafuata kimya kirefu. Katika kimya hicho Joram alinukuu mambo kadhaa katika daftari lake, akitumia hati mkato. Hivyo, ingawa Adela aliiona michoro yote, lakini kwake ilikuwa haina maana yoyote. “Vizuri dada Adela,” alisema baada ya kimya hicho. “Nitahakikisha nayaokoa maisha yako. Usihofu chochote. Nenda zako hotelini ukapumzike. Nitakutembelea jioni ya leo, nione hali ya usalama wako katika hoteli hiyo.”
Msichana huyo aliinuka na kuanza kutoka. Alipokaribia mlango, kama ambaye alikumbuka jambo akageuka na kumwuliza Joram, “Una hakika na maneno yako? Kwamba utaniokoa na huyu mwendawaazimu mwenye kiu za watu wasio na hatia?”

“Bila shaka,” Joram Kiango alimjibu baada ya kucheka kidogo. “Wala sio kukuokoa tu, bali pamoja na kumtia mbaroni. Hiyo ni ahadi na haijatokea hata mara moja nikashindwa kuitimiza ahadi yangu.”
Adela aliduwaa kwa muda, mdomo ukiwa wazi kama aliyetaka kusema neno ambalo hakulifahamu. Kisha kama aliyejikumbusha akageuka na kutoka nje.
Joram alimsindikiza kwa macho yanayocheka.

ITAENDELEA

SOMA: Mikononi Mwa Nunda – EP04

Ngoma 10 Bora za Mwezi may, 2020.

Leave a Comment