SIMULIZI Pumbazo - Ep 2
SIMULIZI

Ep 2: Pumbazo

SIMULIZI Pumbazo – Ep 2

Simulizi : Pumbazo
Sehemu Ya Pili (2)

Baada ya hapo nikasikia hatua zikisogea kisha zikatulia, nikawa najiuliza mtu anayenihoji yu upande gani wa mwili wangu.
Hapohapo ghafla taa zenye mwanga mkali zikawashwa na kunimulika machoni.
Ile najaribu kujiziba macho yangu hapohapo nikawa nimefanya kosa kubwa kuuacha mgongo wangu wazi. Mjeledi ukapenya!
Nikapiga mayowe makubwa sana ya uchungu, mayowe yale yakawa kama yameuzima ule mwanga mkali.
Giza likarejea na mbu nao wakachukua utawala wao wa kunishambulia bila kupeana zamu ya kung’ata.
“Silijui jina hilo afande!” nililia huku nikimsihi mtu nisiyemuona.
Kwa sauti ya utaratibu kabisa kana kwamba hakuna kilichotokea mtu yule alinijibu.
“Rama… mimi sijakuuliza iwapo unalijua jina ama la… maana hata majambazi huwa hawajuani kwa majina bali matendo yao. Nahitaji tu unieleze ni wapi tutampata huyo shetwain muuaji mwenzako” alizungumzan huku akimalizia kwa kupiga kite cha ghadhabu.
Alipotaja jina ‘Shetwain’ akili yangu ikafanya kazi upesi na hapo nikagundua kuwa aliyekuwa akinihoji ni mtu niliyekuwa namfahamu.
Nasema nilikuwa namfahamu ila si kwamba tulikuwa tunafahamiana.
Huyu alikuwa ni mpelelezi ambaye alikuwa akihusika na kesi nzito nztito.
Ukisikia kesi imefikia hatua ya kukabidhiwa kwake basi utambue wazi kuwa muhusika akikamatwa ni lazima huyu bwana amalize hasira zake kwanza ndipo mambo mengine yaendelee.
Usoni alionekana mpole sana lakini hakuwa na utu katu!
Kwa muonekano wake huu maafande wenye vyeo vya kawaida wakambatiza jina lililoanza kimasihara akalikataa lakini baadaye akalikubali.
Walimuita sajini PILIPILI!
Wakimaanisha kuwa anawasha na kuumiza lakini haui!
Nilikuwa mikononi mwa sajini Pilipili!
Moyo wangu ulipiga kwa nguvu sana huku mwili ukiingiwa ubaridi!
Nikiwa bado katika hali ileile ya ubaridi na hofu kuu ikiwa imenitawala nikifahamu fika kuwa yule bwana wa kuitwa pilipili anakwenda kunisulubisha. Nilikuwa katika majuto makubwa sana nikijiuliza ilikuwaje hadi nikamkaribisha yule binti ambaye sasa ni marehemu katika meza yangu.
Laiti kama nisingemkaribisha basi nisingekubwa na balaa hili ambalo nipo nalo sasa.
Kimya kilitanda bila kumsikia Sajini Pilipili wala kiumbe chochote pale ndani.
Ukimya ule ukazidi kuniweka katika mashaka nikijiuliza amepanga kunifanya nini bwana yule katili.
Lakini hakuna kilichotokea baada ya hapo… ukimya uliendelea kutanda huku mbu pekee wakipiga kelele za kushangilia chakula kilichokuwa mbele yao.

Niling’atwa na mbu kwa kiasi kikubwa sana… hadi mwanga ulipoonekana tena nilikuwa nimewazoea.
Nilichukuliwa na kupelekwa mbele ya sajini Pilipili. Sasa niliweza kuonana naye ana kwa ana.
Alikuwa anatabasamu kama kawaida yake, huwezi kujua tabasamu lake lina maana gani.
Neno la kwanza alilosema kwangu ni kunipa pole kwa usiku uliopita, hakusubiri nijibu pole yake badala yake akaendelea kuzungumza huku akifanya juhudi ya kukikuna kidevu chake kisichokuwa na ndevu.
“Umekataa kumtaja Vonso anapopatikana sivyo?” aliniuliza… sasa alisubiri jibu langu.
Nikamueleza kwa kuapa mbele ya Mungu kuwa katu sijawahi kukutana na mtu huyo, na hapo upesi nikauunganisha mkasa wa mimi kukutana na yule binti ambaye ni marehemu kwa sasa.
“Kwa hiyo zile alama za vidole mikononi, mabegani na shingoni zimejiweka zenyewe ama?” alinisanifu. Nikarejea maelezo yangu na kumweleza kuwa ni kweli nilimgusa binti yule wakati wa kumsaidia.
“Wakati wa kumsaidia kuutoa uhai wake ama?” alinisanifu tena huku akiacha kukikuna kidevu chake.
“Sajini… hakuna ninachokuficha naomba tu uniamini lakini kama wewe hautaniamini basi sina jingine la kufanya lakini nilichosema ni kweli tupu….” Sasa niliamua kumjibu kwa jazba tu kwa sababu sikuona dalili yoyote ya kunielewa na nilijihisi kukata tamaa.
“Ramadhani… huna haja ya kupaniki….. unatakiwa utulie kuna jambo zito katika mkasa wako huu… na ukileta ujuaji na kujifanya una hasira na mihemko ya kipuuzi itakugharimu tena sana….”
Alisita na kisha akapiga simu yake na kuzungumza maneno machache, halafu kimya kikatanda hadi pale askari wawili wasiovaa sare walipofika wakiwa pamoja na Nasra pacha wa marehemu.
“Keti” sajini alimuelekeza kwa ishara ya mkono naye akatii.
Kimya kikatanda nikamtazama Nasra usoni.
Ama! Alikuwa anatisha haswa, uso wake ulikuwa umewiva kwa hasira kali na chuki ya waziwazi dhidi yangu.
“Nilijaribu kumwokoa dada yako laki…” nilimweleza lakini kabla sijamaliza alinigeukia na kunitandika kibao kikali usoni kisha akaendelea kumtazama Sajini.
Sajini akatokwa na tabasamu hafifu.
“Rama…” aliniita bila kuzungumzia lile tukio la mimi kuchapwa kibao na yule binti.
Niliitika akaendelea kuzungumza.
“Mtashirikiana na Nasra….” Akapiga kimya kisha akaendelea.
“Mtashirikiana kuanzia sasa ninavyozungumza nawe.” Akasita tena.
“Majibu ya ushirikiano wenu ndo hatma ya mkeo….. mkeo yupo salama lakini ukifanya ujanja wowote ule wa kujioana unajua sana hautawaona mke na mtoto wako tena maishani mwako.” Alisita na kunikazia macho akinitazama jinsi nilivyokodoa macho yangu.
Nilitaka kusema neno lakini akanipungia mkono kuwa ninyamaze.
“Mtaondoka hapa pamoja, mtazungumza kila kinachotakiwa kuzungumza. Mkihitaji msaada wangu nitakuwepo kwa ajili ya kuwasaidia… tafadhali msiwasiliane na mtu mwingine tofauti na mimi…. Sababu nazijua mimi.” Akatoa kadi yake na kumpatia Nasra.
Mara simu yake ikaita, akapokea na kuzungumza huku akiondoka… tukamsindikiza kwa macho. Akageuka na kusema neno la mwisho kwa siku ile.
“Huyo sio aliyemuua pacha wako….. zungumza naye. Atamtaja muuaji”
Akatoweka akituacha mafahali wawili tukishindwa namna ya kutazamana.
Sasa sikiwa namuwaza tena Nasra bali nilikuwa nawaza juu ya mke na mtoto wangu.
Nilifikiria kwa muda kiasi na kisha machozi yakaanza kunitoka kwa kasi, nilikuwa najenga picha jinsi nitakavyokuwa ikiwa tu mke na mtoto wangu sitawatia tena machoni.
Baada ya kilio cha dakika kadhaa nilinyanyau macho yangu na kumtazama Nasra.
“Dada Nasra, mke na mtoto wangu wakiuwawa na damu yao iwe juu yako…. Sijawahi kuua… sijawahi hata kufikiria juu ya hilo umeamua kunishtaki kuwa mimi ni muuaji wa pacha wako? Ukweli wangu kwako umenilipa haya? Kwanini lakini… eeh kwanini Nasra… ni kweli nastahili haya…. Nitazame ngozi yangu… nimechapwa mijeledi nimeliwa na mbu wenye dhiki kuu ya damu… nimeishi maisha ya hofu. Lakini sikumuua wala kumjeruhi dada yako… nilimwokoa…” hapo sasa sikuweza kuendelea kuzungumza nikajikuta katika kilio tena.
Ule mwonekano wa chuki ukageuka kuwa wa huruma na hapo akanifikia akanishika mkono tukaondoka.
Huu ulikuwa mwanzo wa safari ndefu ambayo sikuitarajia kamwe.

Baada ya kilio cha dakika kadhaa nilinyanyau macho yangu na kumtazama Nasra.
“Dada Nasra, mke na mtoto wangu wakiuwawa na damu yao iwe juu yako…. Sijawahi kuua… sijawahi hata kufikiria juu ya hilo umeamua kunishtaki kuwa mimi ni muuaji wa pacha wako? Ukweli wangu kwako umenilipa haya? Kwanini lakini… eeh kwanini Nasra… ni kweli nastahili haya…. Nitazame ngozi yangu… nimechapwa mijeledi nimeliwa na mbu wenye dhiki kuu ya damu… nimeishi maisha ya hofu. Lakini sikumuua wala kumjeruhi dada yako… nilimwokoa…” hapo sasa sikuweza kuendelea kuzungumza nikajikuta katika kilio tena.
Ule mwonekano wa chuki ukageuka kuwa wa huruma na hapo akanifikia akanishika mkono tukaondoka.
Huu ulikuwa mwanzo wa safari ndefu ambayo sikuitarajia kamwe.
MSIMULIZI ANAINGIA.
MAMA JOSE aligutuka kutoka usingizini majira ya saa nane na nusu.
Usiku wa maneno, hii ni baada ya Jose kuanza kulia.
Mama Jose akakumbuka kuwa Jose hakunyonya vizuri siku hiyo basi pasi na shaka kile kilio kilikuwa cha njaa.
Mama Jose akakurupuka na kumkwapua mwanaye wa pekee huku akitokwa na maneno ya huruma topka kwa mama kwenda kwa mwana!

Jose alipoisikia sauti ya mama lile deko la kitopto likaongeza kilio chake.
Mama Jose hakuhangaika akampatia ziwa mwana akaanza kunyonya kwa fujo.
Baada ya muda akasinzia, ni hapo ndipo mama Jose akagutuka kuwa pale kitandani mumewe waliyelala pamoja usiku hakuwepo.
Akamlaza Jose wake na kisha kwa kunyemelea akaanza kwenda sebuleni.
Wazo lake la kwanza akafikiria kuwa Rama atakuwa sebuleni akazungumza na simu ya siri.
Siri gani zaidi ya kuzungumza na vimada wake?
Mama Jose alijiwazia huku akizidisha umakini katika mwendo wake wa kunyata.
Alipokaribia sebule upesi akaufungua mlango ili aweze kumfumania mumewe.
Holaa! Hakuna mtu….
“Baba Jose….. we Rama….” Mama Jose alianza kuita,badala ya kupata majibu aliisikia sauti yake mwenyewe ikijenga mwangwi!
Hapo sasa ule wivu ukatimua mbio, nafasi yake ikachukuliwa na hofu.
Mama Jose akaufikia mlango.
Akajaribu kuufungua akaukuta umefungwa kwa funguo.
Hilo halikuwa tatizo kwa sababu alikuwa na funguo zake za ziada.
Hapo sasa akaiendea taa na kuwasha.
Chumba kile kidogo kikaabnza kumtisha, na akili yake ikamfikiria yule mwanamke aliyenyongwa vibaya sana na kisha anakuja kuonekana tena katika mfumo wa pacha.
Sasa Mama Jose alitimua mbio kali kuelekea chumbani huku akipiga mayowe.
Mayowe yale yakamwamsha Jose akaanza kusaidiana naye kupiga mayowe.
Mama Jose akamkumbatia mwanaye huku akifanya sala kwa kurudiarudia.
Hakutoka kitandani hadi jogoo wa kwanza alipowika huku akiwa bado bandani.
Kumekucha!
Mama Jose alijisemea huku nafsi yake ikiamini kuwa mumewe amechukuliwa na jini Nasra ama kwa jina jingine Hajrati.
Mama Jose akamweka mwanaye mgongoni, wakatoka nje.
Hata kabla hawajazungumza na majirani mara macho yake kwa mbali yakaona jambo lililompa tafsiri moja tu.
Mumewe alikuwa hajachukuliwa na jini bali alikuwa ameenda kwa kimada.
Alimuona kwa mbali akiongozana na msichana.
“Baba Jose ameniolea mke wa pili…. Uuuuwi sikubali nasema naondoka mimi….” Alijisemea mama Jose huku akimweka sawa mwanaye mgongoni.
Akatazama kwa makini zaidi, kweli alikuwa baba Jose na mwanamke ambaye alikuwa hajamtambua bado.
“Heeh! Tena ameenda kuoa wa dini yake…. Eeh! Baba Jose si ungesubiri mwanao walau akue kidogo jamani….” Alizidi kuzungumza huku akisononeka. Alimwona kwa mbali jinsia ya kike akiwa amejitanda kichwani huku akiwa amemshika mkono mumewe.
Mapigo ya moyo yakamwenda mbio sana, akaanza kuugulia uke wenza hata kabla hajatambulishwa rasmi katika uhalali wa ndoa ile.
Mara ghafla, akaanza kupiga hatua nyuma mama huyu mwenye shahada ya wivu wa kimapenzi!
Hatua moja ikazaa nyingine, mwishowe akajikuta amegusa ukuta.. akatokwa nay owe la hofu.
Yowe hili likamfikia mumewe, Rama akaachana na yule mwanamama aliyejitanda…. Akatimua mbio kumwelekea mkewe.
Alimkuta Mama Jose akiwa katika uoga mkubwa sana, macho akiwa ameyakodoa, si kumuelekea Rama bali binti aliyejitanda ambaye alikuwa anakuja hatua moja baada ya nyingine.
Rama akaufuata uelekeo wa macho ya Mama Jose akatambua alichokuwa akikihofia. Lakini wakati huohuo naye alikuwa katika namna ya pumbazo, aliyakumbuka maneno ya Sajenti Pilipili kuwa mkewe amekamatwa, lakini sasa anamuona tena!
“Si kitu mama Jose… kuwa mtulivu. Tena mtulivu haswa…. Kuna jambo la…” kabla hajasema neno lolote la ziada mara gari ya polisi ikafunga breki kwa fujo nyumbani kwake. Wakashuka maaskari wasiopungua sita…. Hawakusema neno bali waliwavamia mama na baba Jose, wakamsukuma kando Rama, akapepesuka na kutua chini kama gunia.
Wakamtwaa mama Jose na Jose akiwa analia katika mgongo wa mama yake.
Wakamwingiza katika karandinga kisha kama walivyoingia kwa fujo, wakaondoka hivyohivyo!
Huu ikawa ushuhuda wa kwanza kabisa katika safari ya Ramadhani!
Mkewe na mtoto walikuwa wametoweka!
Hakujua kilichokuwa kinaendelea…..
Akabaki mkiwa huku akitakiwa kufanya awezavyo kuhakikisha anamtambua Vonso ilimradi tu aweze tena kuungana na familia yake.
Kwa sababu Rama aliwahi kuwa polisi kabla, alitambua wazi kile kilichotokea pale kuwa ni kitisho cha awali ili atambue wazi kuwa mkewe na mwanaye wapo matatani na ili kurejesha amani hana budi kupambana.
Hapo akamgeukia Nasra!
“Vonso ni nani kwani?” alimuuliza kiutulivu kabisa huku akijaribu kuidhibiti ile hali yake ya kutetemeka kutokana na hofu.
“Ni mimi natakiwa kukuuliza wewe kaka… na sio wewe kuniuliza mimi?” alijibu kwa ukali kiasi fulani.
Rama hakusema neno badala yake akamkaribisha ndani.
Alizungumza naye mengi sana akilielezea upya tukio la kukutana na Hajrati na kisha kuzipata taarifa za kifo chake kwa kushtukiza.
Na hapa ndipo Nasra alipoinamisha kichwa chake kisha akakinyanyua na kumtazama Rama machoni moja kwa moja na kumwelezea jambo ambalo lilizidi kuisogeza safari yao mbele.
ILIKUWA MNAMO MWAKA 1997, ikiwa ni miaka kadhaa tangu uchaguzi wa kwanzqa kabisa nchini Tanzania unaohusisha vyama vingi ulipofanyika.
Pia ile ruksa iliyoasisiwa na mzee Mwinyi ikizidi kuchukua nafasui yake.
Mwanamama Hadija, mama wa watoto wane alikuwa amenuia kufanya jambo kwa ajili ya familia yake. Uzito kimajukumu ulikuwa umemzidi… akawaweka chini watoto wake japokuwa walikuwa wadogo akawakabidhi kwa dada yake yaani mama yao mkubwa na kuaga kuwa anakwenda kufabnya kazi mahali na atakuwa akiwatumia pesa za matumizi…….
Akawaaga wanawe kwa kuwakumbatia huku akimsihi dada yake awatunze wanawe kama ambavyo angeweza kuwatunza watoto wake wa kuwazaa japokuwa hakuwahi kubarikiwa kupata watoto.
Hadija akawakumbatia kwa mara ya pili watoto wake wadogo ambao walikuwa pacha, akawaasa wapendane kwa dhati.
Watoto hawa hawakuelewa lolote lakini huu ulikuwa mwisho wa kumuona mama yao ambaye katika ukubwa wao wanaambiwa kuwa alienda nchi za ugenini kufanya kazi za ndani.
Historia hii ikawa haina uhakika sana ikaenda kushoto ikarudi kulia kisha kushoto tena ikapinduka na kupotea katika kumbukumbu zao.
Walichoamini ni kwamba waliwahi kuwa na mama kwa kutazama picha chache za mama yao alizowahi kupiga enzi za uhai wake.
Ikawa mwaka na hatimaye miaka mapacha wale hata kabla ya kufikia makamo ya kuitwa wasichana wakaanza majukumu ya kufanya kazi kama wasichana, kazi gani nyingine wangefanya zaidi ya kazi za ndani?
Hawakuiwa na elimu walau ya darasa moja!

Wakatumbukia katika ajira hii kwa ajili ya kumsaidia mama yao mkubwa ambaye alikuwa anasumbuliwa na kansa ya matiti akiwa kitandani hajiwezi.
Kansa ambayo ilisababisha mgawanyo, wale watoto wane kila mmoja akichukuliwa na ndugu ambaye angeweza kumsaidia.
Mama mkubwa akabaki na pacha mmoja aliyeitwa Hajrati.
Na alikuwa ni Hajrati aliyemletea mama yake mkubwa jambo ambalo alihitaji ushauri wa kina.
Hajrati alikuwa amekutana na kijana nadhifu ambaye alimweleza kuwa kuna kazi amempatia inalipa kwa kiasi kikubwa sana.
Mama mkubwa akashindwa kukubali kirahisi hadi alipomwomba Hajrati akutanishwe na huyo kijana.
Kweli kijana akafika akiwa nadhifu vilevile na maneno yaliyonyooka vyema katika kinywa chake, maneno matamu ya kuvutia haswa.
Ushawishi ukachukua nafasi hatimaye mipango ikaanza kufanyika, kijana yule mwema alisema kuwa yeye ni mwakilishi kutoka kampuni inayohusika na mambo ya ajira inaenda kwa jina la VONSO ALMEIDA & CO. Limited. Jina ambalo Hajrat alilikariri kwa sababu ya kulisema kila siku akiwa anamshawishi mama yake mkubwa.
Ikapatikana hati ya kusafiria na mambo yote stahiki, Hajrati akiwaza kupanda ndege na kwenda kufanya kazi yenye kuingiza kipato kikubwa.
Siku moja kabla hajaondoka alienda kumwaga pacha wake…… alimkumbatia na kumpa ahadi kedekede.
“Nakupenda Nasra! Nitakutumia nauli na wewe uje nitakapokuwa…” Hajrati alimwambia pacha wake wa kufanana.
“Usijali Nasra nawe nitakutafutia kazi sawa…Vonso anahitaji wafanyakazi wengi ila kwa hatua ya awali ngoja aende mwenzako” ilisikika sauti ya kijana yule nadhifu.
Na ule ukawa mwisho wa Nasra kuonana na Hajrati hadi siku ile alipokuja kufananishwa katika daladala na hatimaye kufikia hatua ya kushuhudia maiti ya pacha wake katika namna ya kutisha sana.
Kesi ikamuangukia Rama na sasa Nasra anatakiwa kushirikiana naye ili waweze kutatua jawabu.
Jawabu juu ya Hajrati aliyetoweka miaka saba iliyopita na kisha kurejea kimyakimya na kushuhudiwa akiwa maiti!
Zaidi ya yote jawabu juu ya Vonso na kampuni yake.
ULIKUWA NI UTATA WA AINA YAKE…..

RAMADHANI alikumbuka kuiwasha simu yake masaa kadhaa baada ya kuwa amerejea nyumbani akitokea mahabusu katika namna asizoweza kuzielezea , punde baada ya kuiwasha alikumbana na ujumbe kutoka katika nambari mpya lakini iliyoanza kwa kujitambulisha.
Ulikuwa ni ujumbe kutoka kwa Sajenti Pilipili.
Ujumbe mfupi kabisa uliomkumbusha kuwa familia yake inahitaji maarifa yake zaidi kuliko kuchanganyikiwa kwake.
Ujumbe huu ulimchanganya upya Rama, kitendo cha kusikia juu ya familia yake kilikuwa ni sawa na kuliona bomu asilolijua na anatakiwa kulitegua na iwapo atashindwa katika mbinu zake basi litamlipukia.
Rama akaiweka simu yake kando, akaingia jikoni na kuandaa maakuli kwa ajili yao wawili yeye na Nasra.
Wakati wanapata chakula, kwa mara nyingine Rama akamuuliza Nasra juu ya mama yake mkubwa ambaye alimruhusu Hajrati kwenda kusikojulikana kufanya kazi na kisha kupotea moja kwa moja.
Nasra akamueleza Rama kuwa mama yake mdogo alipotea katika mazingira ya kutatanisha na akahisiwa huenda alikufa katika ajali ya treni iliyotokea Dodoma na kuua watu wapatao mia nane na ushee.
Rama akachukua kalamu na kuandika kitu katika kitabu chake kidogo.
Kisha wakaendelea kupata chakula, kimyakimya hadi kila mmoja aliporidhika.
Rama akaagana na Nasra kwa makubaliano ya kukutana siku inayofuata.
Nasra alipoondoka Rama hakubaki kichwa wazi asiwe na la kufanya, alikuwa ameingia kazini rasmi.
Akamfuatilia binti yule nyendo zake.
RAMA ANASIMULIA.
UCHUNGU wa mwana hakika aujuaye mzazi, lakini uchungu wa mwana jumlisha na ule wa mke unapowekwa pamoja hakika nyongo ya mamba ina utamu wake.
Tafakuri tupu isingeweza kuwa mbadala wa tatizo langu, nilitakiwa kuamua… na ipo hivyo katika maisha ukihitaji kufikia kilele cha mafanikio katika jambo fulani basi huna budi kunyanyua mguu wako na kupiga hatua mbele.
Nilijkua kuwa jambo hili haliwezi kuwa jepesi hata kidogo na nilitambua kuwa serikali yetu isokuwa na dogo haitakuwa na msalia mtume ikiwa sitapambana mimi kuusaka ukweli.
Labda ungeweza kunishauri kwa wakati huo niende mahali kushtaki kuwa sijatendewa haki, lakini ni yupi namshtaki haswa wakati ile kesi ya mauaji nilikuwa naimiliki mimi?
Nikaona ni heri nijaribu kuliko kuketi na kusubiri muujiza.
Nilimfuatilia Nasra na kupafahamu nyumbani kwake…..
Hiyo ilikuwa siku ya kwanza, sikutaka kujua la ziada kwa siku ile….
Sikurejea nyumbani mapema, badala yake nilielekea katika ofisi inayohusika na kusajiri makampuni. Lengo langu ni kujua juu ya hiyo kampuni ambayo Hajrati aliwahi kufanya kazi na hatimaye kupotea kwa miaka kadhaa na kisha kurejea na kukumbwa na umauti.
Nia yangu kuu ni kumjua mkurugenzi ambaye angenisaidia kujua kampuni ile inahusika na mambo yapi.
Niliafikiana na wazo langu lile ambalo nililiona kuwa ni sahihi na ambalo lingenipa mwanga, hatua ya kumjua tu ambaye anamiliki kampuni ile kwangu ingekuwa hatua kubwa ya awali.
Kweli nikafika na kuulizia juu ya kampuni ile huku nikijifanya kuwa nahitaji kusajili kampuni ya jina lile ikiwa hamna ambaye amewahi kusajili kwa jina lile.
“Kwanini unahitaji kusajili kwa jina hili?” yule bwana alinitazama kivivu vivu huku akiwa anaendelea kupekua jina hilo katika kompyuta yake.
“Ni muunganiko wa majina ya wenzangu tunaoshirikiana..” nilibumba uongo upesi.
Hakujibu kitu… baada ya muda akanieleza kuwa jina lile halijawahi kutumiwa na mtu yeyote yule hivyo kama nahitaji kulitumia nifuate taratibu za kusajili kampuni kisheria.
Majibu yake yalinifanya nikaishiwa nguvu!!
Hajrati alipewa ajira na kampuni ya VONSO ALMEIDA. CO. LTD halafu leo hii naambiwa kuwa hakuna kampuni kama ile imewahi kutokea nchini?
Nikamuaga yule bwana na kumweleza kuwa nitarejea tena nikiwa tayari.
“Una uhakika unahitaji kusajili kampuni kijana?” alinihoji nikiwa nimesimama nataka kutoka.
Sikuelewa maana ya swali lake, nikatikisa kichwa kukubali.
“Haya karibu tena sisi tupo kuwahudumia watu kama wewe.”
Nilitoweka nikiwa mnyonge sana, pahali nilipotegemea kuwa patanipa mwanga mpya pameniingiza katika giza nene. Kipi kingine ningefanya zaidi ya kurejea nyumbani kulala niwaze na kuwazua upya?
Nilitembea kwa mwendo mfupi kiasi fulani kabla sijafika kituoni.
Kama ilivyo kawaida ya jiji la Dar es salaam. Magari ni mengi lakini watu ni wengi zaidi hivyo vurugu za kuwania magari huwa haziishi kirahisi.
Nilisubiri likapita gari la kwanza, waliowania wakawania mi nikawa mtulivu, likapita la pili likiwa limejaa sana hili sikujishughulisha nalo kabisa.
Nikiwa bado nimesimama pale mara akafika mpiga debe akilinadi gari aina ya Noah ambalo linapakia kwa bei mara mbili ya ile ya daladala za kawaida.

Maneno yake ya ushawishi yakanivuta, nikaona ni heri hasara lakini nisafiri kwa raha.
Nikaufuata uelekeo wa mkono wake, nikaingia katika Noah.
Walikuwemo abiria wawili, mke na mume. Nikaingia kimyakimya bila kuwajulia hali.
Mara akafika yule mpigadebe, akaingia na kuufunga mlango!
Kisha gari likaondoka kwa kasi sana, nikabaki katika pumbazo nikijiuliza inawezekana vipi gari linaondoka bila abiria?
Niliwatazama abiria wenzangu ikiwa walikuwa katika mshangao lakini wao walikuwa na maongezi yao mengine kabisa jambo hili halikuwagusa kabisa.
Gari lilizidi kwenda huku yule bwna niliyemtambua kama kondakta akiwa hajihusishi kudai nauli yake wala kunadi lile gari kila kituo. Alikuwa yu mtulivu haswa…..
Gari lilitembea kwa kasi ileile hadi maeneo ya Magomeni, hapo likasimama kisha yule mtu mzima ambaye alikuwa akizungumza na mwanamke pekee katika lile gari akanitazama. Jicho lake likaniweka hatiani kuwa wakati naingia ndani ya lile gari hakuna niliyekuwa nimemsalimia. Nikakurupuka na kumsalimia.
Badala ya kunijibu aliniuliza umri wangu.
“Miaka Thelathini mzee…” nilimjibu kwa adabu zote.
“Wewe bado ni kijana mdogo sana, je una mke na watoto….” aliniuliza kwa utulivu sana.
Nikamweleza juu ya kuwa na mke na mtoto mmoja.
Jibu hili nililompa lilipita na kinywani huku likiniachia kumbukumbu kichwani kuwa mke na mwanangu hawakuwa mikononi mwangu.
“Tumia muda wako mwingi kujali na kuhudumia familia yako, achana na mambo ya VONSO…. ni mazito kuliko unavyodhani… achana nayo. Siku hii ya leo huruma yangu ipo juu yako…. shuka!!” alizungumza maneno yale na hata aliposema nishuke, mlango ukafunguka bila kuguswa na mtu yeyote yule. Sikuuliza swali nikashuka upesi nikiwa nimekodoa macho nisiamini nilichokuwa nakisikia.
Niliposhuka gari likaondoka kwa mwendo wa kawaida, nilipolitazama nikagundua kuwa gari lile halikuwa na namba za usajili.
NILICHOKA!!

NILITEMBEA hatua kubwa kubwa huku kila mara nikigeuka nyuma kutazama ikiwa kuna watu ambao walikuwa wakinifuata.
Lakini baada ya muda nilijikuta najicheka mwenyewe huku nikijisonya.
“Sasa kama waliweza kunifuatilia hadi kunipandisha katika gari lao kisha wakaniacha, sasa hivi nakwepa kitu gani labda…”
Baada ya kubaini udhaifu wangu walioutumia kunifuatilia, hapo nikarejea katika unyonge wangu wa awali nikatembea hadi kituo cha daladala, nikakwea gari kuelekea nyumbani.
Kichwani mwangu nikiwa sina maswali mengi sana, nilijua wazi kuwa yule afisa wa kusajiri makampuni alikuwa yu nyuma ya jambo hili kwa asilimia zake. Lakini kilichoniumiza kichwa ni kwa nini sasa nimepewa onyo mapema kiasi kile.
Nilijiuliza pia ikiwa wakuu katika idara ya upelelezi tena chini ya konkodi Sajenti Pilipili waliweza kufuatilia hili jambo, ina maana nao waliwahi kupewa onyo kama nilivyopewa mimi?
Na kama waliwahi kupewa onyo, ina maana basi wameamua kuniugeuza mimi chambo nijipeleke ili waupime ukali wa Vonso ama?
Fikra hizi zikanifanya niingiwe na hofu.
Nilipogeuka nje kutazama mazingira ili kujisahaulisha mawazo yaliyokuwa yananikabili nikatanabai ya kwamba zamani sana nilishapitishwa katika kituo nilichotakiwa kushukia.
Nikasimama upesi na kujifanya kuwa sijapitishwa kituo, nikampigia kelele konda anishushe kituo kinachofuata.
Konda akatii nikashuka na kuanza kutembea kwa miguu kurejea nyumbani kwangu!!!
Nikiwa barabarani nikapata wazo la kuwasiliana na Sajenti Pilipili nimueleze bayana kuwa mtihani alionipa ulikuwa mgumu sana na laiti kama nikiendelea kuufanya basi utanigharimu maisha yangu.
Nikajaribu kuwasiliana na ile nambari iliyonitumia ujumbe, iliita kwa muda kisha ikapokelewa.
“Nikusaidie nini?” iliniuliza kikakamavu.
“Mimi ni Ramadhani…. bila shaka nazungumza na Afande Pilipili…”
“Tazama nambari uliyopiga kwa makini….” alijibu yule bwana na kunikatia simu.
Nilibaki kuitazama simu ile huku nikichelewa kuiingiza mfukoni kana kwamba mpigaji angeendelea kuzungumza, lakini haikuwa hivyo.
Nilitembea hadi nyumbani, nilipofika niliukuta mlango upo wazi. Nikasita kuingia kwa muda huku nikijaribu kuvuta kumbukumbu nikifikiria ni nani ambaye angeweza kuwa katika chumba changu.
Hata kabla sijapata jawabu mara mlango ukafunguliwa.
Alikuwa ni Nasra!
Macho yake yalionyesha hofu ya waziwazi, akaingia ndani huku akinipa ishara nimfuate, nikaingia huku masikio yangu yakitarajia kupokea kitu ambacho kitanishtua.
Nasra alifungua mkoba wake na kisha akanionyesha albamu ya picha, sikumuuliza kitu nikaanza kufunua. Nusu ya macho yangu yakiangalia picha na nusu nyingine nikimtazama Nasra na jinsi alivyokuwa anatetemeka kwa hofu, mikono yake ikiwa haijatulia sehemu moja.
Nilikuwa naziona picha zake mbalimbali, akiwa sehemu za starehe na watu mbalimbali.
Nikamaliza kuangalia zile picha nikiwa sijaambulia kitu chochote.
Hapo nikauvunja ukimya nikamuuliza kulikoni.
“Sijaelewa maana yako…” nilimuuliza.
Akanitazama na kujaribu kusema neno, midomo yake ikitaka kufunguka na kusema neno lakini anashindwa kutoa kauli yoyote.
“Nasra kwani hizi picha zina nini… nakuona wewe ukiwa sehemu mbalimbali…”
“Huyo sio mimi… ni Hajrati… nimetumiwa bahasha na mama yetu mkubwa siku kadhaa nyuma…. na leo nimeambiwa kuwa amekutwa amekufa kama…. kama alivyokutwa Hajrati…..” alishindwa kuendelea akaanza kulia, nikamsogelea na kumbembeleza na kumsihi kuwa huo haukuwa wakati wa kuomboleza.
Baada ya kutulia kidogo akaniambia nifungue zile picha kwa nyuma….. hapa nikaanza zoezi la kufungua picha moja baada ya nyingine. Kuna baadhi hazikuandikwa kitu chochote na nyingine zilikuwa zimeandikwa maandishi ya kiarabu ama kichina. Sikuweza kuielewa lugha ile kwa sababu bila kificho japokuwa niliwahi kusoma Madrasa na kumaliza Juzuu kadhaa lakini mambo mengi yalikuwa yananichenga katika kusoma kiarabu.
“Maandishi haya yanamaanisha nini?” nilimuuliza Nasra.
Akabaki mdomo wazi, akaniuliza ikiwa sijasoma madrasa.
“Nasra!! huu si wakati wa kuulizana mambo ya Madrasa nieleze yana maana gani?” nilikuwa mkali kidogo baada ya kuona anataka kuniumbua.
Nasra akaanza kunitafsiria maneno yale picha kwa picha.
Zilikuwa ni picha sita.
1. Ewe Mungu uliye hai litazame chozi langu.
2. Ipo siku dunia itajua na mtasaga meno.
3. Ukipata nafasi ya kuyasoma haya nifikishie ujumbe kwa raisi.
4. Eeh Tanzania yangu damu yenu inateseka huku.
5. Nina mpango wa kutoroka ukiipata picha hii kabla yangu basi nimeshindwa
6. Nikifa naomba uwe shuhuda

Maneno haya yalizua utata mkubwa sana, yalikosa muunganiko sahihi, Nasra alichanganyikiwa na mimi nikibaki katika kuchanganyikiwa vilevile.
Kwa kauli moja mimi na Nasra tukakubaliana kuwa ni lazima jambo hili tulifikishe kwa Sajenti Pilipili na kumwomba msaada wake iwapo itawezekana, wakati huo nikiwa nimemsimulia Nasra jinsi nilivyotekwa na kuachiwa ndani ya muda mfupi huku nikisindikizwa na onyo kali.
Tuliondoka wakati uleule kwa kutumia usafiri wa taksi hadi kituo kile cha polisi.
Hatukumkuta Afande Pilipili, hivyo tulilazimika kumngoja kwa muda zaidi hadi alipopigiwa simu.
Alipofika nilichukua jukumu la kumueleza kinaga ubaga kuanzia mwanzo hadi mwisho juu ya kilichojiri kwangu na kwa Nasra pia.
Afande akasema kuwa anatambua juu ya kifo ambacho Nasra alikielezea, ilipofikia suala la yale maandishi hapa sasa Pilipili alitilia maanani zaidi. Akachukua ile bahasha na kuitazama kwa makini kuliko umakini alioutumia kusikiliza maana ya maandishi yale ya kiarabu.
Baada ya kuitazama ile bahasha alinivuta pembeni kisha akanitazama machoni.
“Afande unarejea kazini kwa kazi moja maalumu….. sahau kuhusu kesi sahau kuhusu mkeo ni kwa masilahi ya taifa letu…” akameza mate kisha akanieleza kuwa alilosema sio ombi bali narejea kazini bila hiari yangu.
“Kesho asubuhi ufike ofisini kwangu kwa ajili ya….. aahm ukifika utajua… tutazungumza….” alimalizia kisha akanyanyua simu yake.
“Naomba unichukulie mtuhumiwa wangu hapa mara moja…” alipotamka maneno yale kwenye simu nikaingiwa mchecheto nikitambua kuwa ni mimi natakiwa kuwekwea rumande, sehemu ambayo sikuitaka tena asilani.
Punde wakafika askari wawili wasiovaa sare, wakamchukua Nasra na kuondoka naye.
Nikatambua kuwa alikuwa anaenda kuhifadhiwa kwa sababu ya usalama wake.
Laiti kama ningekuwa sijawahi kupitia maisha ya uaskari ningeweza kusema kuwa ule ni unyanyasaji wa hali ya juu, lakini kwa sababu nimewahi kuwa mmoja wao nilielewa.
Kama alivyowaza kiusahihi Sajenti Pilipili, ilikuwa hivyo.
Saa tano usiku alinipigia simu na kuniuliza nipo wapi. Nikamjibu kuwa nipo kitandani lakini si katika nyumba yangu. Akaelewa ninachomaanisha, akanieleza kuwa chumba cha Nasra kimevamiwa na kupekuliwa sana na watu wanaodhaniwa kuwa ni mtandao mkubwa wa huyo kiumbe ama yeyote ajiitaye Vonso.
“Upo kazini Ramadhan… na si kazi ndogo ni kubwa na nzito. Kuwa makini sasa kwa kila hatua yako” alinieleza na kisha bila kuaga akakata simu.
Nikakiri kimoyomoyo kuwa hakika palikuwa na kazi kubwa. Nikasimama kutoka kitandani kikakamavu nikapiga saluti.
Ishara kuwa nimerejea kazini upya!!
Baada ya kupiga saluti ile nikajihisi kama nipo imara na nina utayari mkubwa sana.
Asubuhi kama tulivyoahidiana na Pilipili, nikakutana naye ofisini.
Nilipofika kwa katibu muhtasi wake na kujitambulisha, akanipatia vijana wawili wakaniongoza hadi katika ukumbi mmoja na kuniambia niingie ndani.
Kwa mawazo yangu nilitarajia kukutana na Pilipili peke yake, hivyo nikitazamia kuzungumza kwa kujiamini mbele yake kwani nilikuwa nimeanza kumzoea.
Nikaingia mlango ule wa kwanza, nikapokelewa na askari wawili, wakanisabahi na kisha wakanisihi niwafuate.
Nilianza kuingiwa nma hofu, maana tabia za Pilipili nilizitambua wazi, ni jambo la kawaida kukuua ama kukutesa huku anacheka. Hapa sasa hofu ikanivamia upya na kijasho chembamba kikanitoka licha ya hewa safi iliyotawala katika jengo lile.
Askari wale walinifikisha mahali wakafungua mlango na kunisihi niingie…..
Macho yangu yakatua katika vazi la kipolisi lililosheheni nyota lukuki, nikatazama kushoto na penyewe vilevile.
Ama! nilipagawa.
Sikuwahi kuingia katika kikao kikubwa na kizito kiasi hiki, niliwashuhudia wakuu wa kazi ambao nilikuwa nikiwaona magazetini pekee bila ndoto ya kuonana nao hata siku moja.
Mkuu wa jeshi la polisi alikuwa mbele yangu, niliduwaa lakini sikusahau kupiga saluti baada ya kuingia pale ndani. Hakuijibu bali alinipungia mkono niketi.
Hapakuwa na muda zaidi wa kupoteza, maongezi yakachukua nafasi yake.
Alifungua maongezi yale sajenti Pilipili na kisha akapokelewa na mkuu wa jeshi la polisi.
Yalizungumzwa mengi sana, na kisha mzizi wa mazungumzo ukaguswa, VONSO!
Mkuu wa jeshi la polisi akaelezea kuwa jina hilo lipo katika midomo yao kuanzia mwaka 1990 na suluhu haijawahi kupatikana. Miaka yote mwanga ulikuwa mbali lakini sasa mwanga umeanza kupatikana kwa kiasi fulani. Hivyo ni wakati wa kulitafuta jibu la miaka mingi!
Na jibu hilo nitatakiwa kulitafuta mimi…… bila kuchelewa.
Nilitamani kukataa wajibu huu lakini hapakuwa na kifungu walichokitenga kwa ajili ya mimi kujieleza ikiwa nipo tayari ama la.
Baada ya ya kukabidhiwa jukumu hilo na watu ambao nitaweza kuwaomba msaada itakapobidi.
ghafla nikatajiwa tarehe yangu ya kusafiri, safari ya kwenda nje ya bara la Afrika.
Ambapo waliamini kuwa ndipo jibu lilipojificha.
Nilipagawa jinsi mambo yalivyokuwa yanapelekwa upesiupesi, lakini kitu ambacho sikuweza kufanya kwa wakati ule ni kupinga. Kumbukumbu ya mke na mwanangu mikononi mwa jeshi la polisi ilinitesa.
Kichwani nikajiuliza, ni kitu gani cha ajabu wameona kwangu hadi kunipa jukumu lile?
Binafsi sikujiona na lolote la ziada, badala yake nikajipatia jibu tena kuwa jamaa wameamua kunifanya mimi CHAMBO…..
Baada ya siku tatu nilikuwa navuta na kutoa hewa nje nikiwa nje ya Afrika.. mahali ambapo watu wa rangi yangu ni wa kutafuta.
Na huko ndipo nilipokutana na balaa jipya, ajabu ni kwamba hata huku Vonso alikuwepo lakini hakujulikana!!
Nikaendelea kubaki katika PUMBAZO!
Mara mapenzi nayo yakaingilia kati…

Nilipokelewa nchini Oman na mwanamke refu, alikuwa amejihifadhi ndani ya juba jeusi na uso wake ukifichwa katika nikabu iliyofanya nishindwe kumtambua ikiwa alitabasamu wakati wa kunipokea lakini hilo halikunizuia kumpokea.
“Asalam aleykum Ramadhani, karibu Muscat! Umekuja wakati sahihi kabisa na jina lako….” Alinikaribisha na masikio yangu yakiipokea vyema lafudhi yake ile ambayo huenda ilikuwa ya Zanzibar.
Nikaijibu salamu yake huku nikikumbuka kuwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ulikuwa njiani!
Aliniongoza hadi katika taksi na kumweleza wapi pa kutupeleka.
Ama! Jiji hili la Muscat nilikuwa nikiliona tu katika runinga, lakini kwa macho yangu nilikiri kuwa lilikuwa jiji lenye hekaheka nyingi.
“Naona huku vazi lenu ni moja… ukinipotea nitapata tabu kukupata…..”
“Asilimia sabini na tano ya wakazi wa hapa ni waumini wa dini ya kiislamu….. hili nd’o vazi letu sahihi.” Alinijibu na kwa hisia nikahisi alikuwa anatabasamu wakati anazungumza maneno yale.
“Inakuwaje juu ya wanaume kuchagua mabibi zao sasa… maana nyote mnafanana?” Nilimuuliza na hapa nikakisikia kicheko chake.
Aliishia kucheka tu na hakutoa jibu.

Isikupite Hii: Pumbazo – Ep 1

Safari yetu iliishia katika hoteli ambayo sikujua kama ni bei ghali ama la kwa sababu mlipaji sikuwa mimi.
“Nimekuwa katika nchi hii kwa miaka minne sasa… naamini siku moja nitarejea Zanzibar!” alinieleza wakati tukiwa mapokezi.
“Rama muhudumu atakupa maelekezo zaidi, mimi siruhusiwi kuingia chumbani kwako pasi na cheti cha ndoa.” Aliniambia huku akitoa mkono wake na kunipatia.
Nikahisi kuna kitu ananiachia nami nikakipokea kana kwamba hakuna lolote lililotokea kati yetu.
Akaniaga na kuahidi kurejea siku ifuatayo kwa ajili ya kunipa maelekezo zaidi.
Kwa mara ya kwanza nikaingia katika hoteli kwa ajili ya kulala nikiwa nje ya bara langu, nje ya nchi yangu ya Tanzania.
Yule binti akaondoka bila kunipatia hata jina lake.
Kuondoka kwa binti yule ukawa mwisho wa kuzungumza Kiswahili, sasa nikaanza kuhangaishana na muhudumu anayezungumza kiingereza kibovu chenye lafudhi ya kiarabu.
Hatimaye nikamalizana naye na kubaki nikiwa nimejifungia chumbani.
Nilijaribu kujilaza lakini kichwa kilikuwa kizito sana, jambo la kufanya upelelezi nisioujua mwanzo wake katika nchi hii ya kigeni liliniweka katika hofu ya namna yake. Nikasimama na kukizunguka chumba kile kikubwa, hadi nilipolifikia dirisha na kutazama kwa umakini mji huu wa Muscat!
Hakuna nilichoambulia zaidi ya maghorofa marefu ya kifahari na hekaheka za kutosha zilizoonekana kwa macho.
“Kama Kariakoo vile!” nilijisemea kwa sauti ya chini, na neno lile likanifanya niuhisi ukiwa wa kupakosa Tanzania.
Ama hakika nyumbani ni nyumbani.
Macho yangu yaliendelea kutalii, mara yakalifikia jengo refu sana, jengo hili liliufanya moyo wangu ushtuke na kuongeza umakini kulitazama.
Jengo lile halikuwa mara ya kwanza kuonekana katika macho yangu.
Nikabaki kujiuliza ni wapi nimewahi kuliona?
Dar? Arusha? Mbeya? Mwanza au wapi……
Bado sikupata mfanano wa wapi nimewahi kuliona lakini akili ilinisihi kuwa nimewahi kuliona jengo lile kabisa, tena si mara moja!!
Nilijaribu kutuliza kichwa sana ili nipate jawabu lakini mambo yaliniwia magumu.
Mwishowe nikapuuzia na kujiona najiumiza akili kwa mambo yasiyokuwa na maana.
Yaani nina jukumu la kuzijua hila za Vonso halafu natumia akili nyingi kujiuliza ni wapi nimeona jengo fulani.
Nikiwa katika kupuuza kule walau akili ikapata kitu cha kukumbuka, nikakumbuka juu ya kile alichoniachia yule mwanadada asiyekuwa na jina.
Nikaipekua suruali yangu nikautoa ujumbe ule.
Alikuwa ameandika kiarabu!
Ebwana eeh!
Nilichachawa na kuingiwa na hatia ya kutotilia maanani niliyokuwa nafundishwa madrasa…. Sasa naumbuka.
Itakuwaje kama ni ujumbe wa hatari ama dharula?? Nilijiuliza na hapo nikajikuta namkumbuka Nasra, pacha wa marehemu Hajrati mtalamu wa lugha ya kiarabu.
Nikatamani sana kama angekuwepo anipe tafsiri.
Nikakumbuka kuwa nilipoondoka alikuwa yu mikononi mwa polisi kwa usalama wake.
“Mungu wangu!” mara nikajikuta napiga kelele na kisha upesiupesi nikakimbia kuelekea kule dirishani, nikalitazama tena lile jengo.
Hatimaye, hatimaye nilikumbuka ni wapi niliwahi kuliona lile jengo.
Nililiona katika zile picha za marehemu Hajrati zilizoambatana na jumbe mbalimbali za kushangaza na zisizokuwa na majibu.
“Ina maana Hajrati aliwahi kuishi Muscat?” hili lilikuwa swali la kwanza lenye uhai katika kile kilichokuwa kimenipeleka kule.
Jumbe zile na maisha yake ya Muscat zinahusiana vipi? Ina maana Vonso naye yupo Muscat?? Kama yupo Muscat na afande Pilipili anajua kuiwa yupo Muscat ni kwanini ameniagiza mimi nije huku, kwanini asimkamate??
CHAMBO!!! Nageuzwa chambo……
Nilijisemea huku nafsi ikiingiwa na simanzi sana…… nilitamani sasa kumuuliza afande Sajenti Pilipili juu ya kwanini mimi nipewe jukumu lile. Lakini nikatambuakuwa atanikumbusha kuwa jeshini hakuna kuchagua kazi…..
“Kanuni gandamizi sana hii…” nililalamika.
MASAA niliona hayaendi huku nikiishi na ujumbe hatari kama ule mkononi mwangu nikiwa sielewi maana yake.
Nikakata shauri nimuulize tu muhudumu wa kile chumba ili niwe na amani.
Nikachukua simu na kupiga nambari iliyoandikwa kwa kimombo…. RECEPTION!
Mpokeaji akaanza kuzungumza kihindi ama kiarabu, mi sijui…. Nikamkatisha kiingereza, akabadili lugha bila kunitaka radhi.
Nikamweleza kuwa nina shida na ninahitaji kuonana na muhudumu.
Akakata simu bila kusema lolote.
Baada ya dakika sita ama saba, chumba kikagongwa akaingia yule muhudumu wa kiume mwenye kiingereza kibovu.
“Nimeukuta huu ujumbe bafuni, je nimeandikiwa mimi mteja ama ni wa nani? Napenda kujua maana yake nikiwa kama mteja wenu…” nikampatia kile kikaratasi.
Akakisoma kisha akanitazama na kukisoma tena.
“Are you sure?” aliniuliza huku akikisoma tena kwa mara ya tatu. Nikamtazama kwa ghadhabu huku kwa sauti ya chini nikitokwa na tusi kwa lugha ya Kiswahili.
Alitaka kuondoka na kile kikaratasi, nikamkwapua na kumuuliza kwa nini anaondoka kana kwamba ameitatua shida yangu tayari.
“Si kitu, ni uchafu tu….” Alisema huku nikimwona kama anayejawa na hofu na asiyekuwa na uhakika na maneno yake. Na hapo akashika hamsini zake aweze kuondoka. Akaufungua mlango na kutoka kwa kasi akiniacha katika taharuki ya aina yake.
Sekunde ishirini badaye nikiwa nimeganda vilevile katika sintofahamu mara mlango ukafunguliwa kwa nguvu sana, nikaruka pembeni upesi!
Na pale nilipotoka kikapita kiumbe kwa kasi kubwa na kutua chini kikijibamiza kitandani.
Nikakitazama kiumbe kile na kutambua kuwa alikuwa ni yule muhudumu aliyekuja kunihudumia.
Nikiwa sijapata pumzi za kusema neno, akaingia mwanadada akiwa amevalia suruali na fulana ya kiume.
Akaingia na kuufunga mlango, kisha upesi akamvamia yule mtu pale chini na kumyanyua.
“What’s wrong..” niliuliza kwa kujitutumua hatimaye huku nikitoa katika hatia.
“Huyu fala umempa zawadi gani mbona ametoka nje anachekelea hivyo?” badala ya kujibu kiingereza alijibu Kiswahili.
Nikashtuka zaidi.
“Naitwa Zainabu niite Zay B… sikujitambulisha awali eeh….” Aliendelea kuzungumza.
Na hapa nikaitambua sauti yake ile yenye lafudhi ya kizenji. Alikuwa ni mwanadada aliyenipokea.
“Nilimwita anitafasirie ulichoniandikia…” nilimjibu.
Akanitazama kwa mshangao mdomo wake ukiwa wazi kabisa. Akataka kusema neno lakini halikutoka.
“Jeshi la Tanzania ndo linafundisha hivyo siku hizi… kuamini amini watu hovyo katika jambo zito kama hili….. ama unadhani umekuja huku kwa jambo la kitoto. Wenzako kumi na ushee kuanzia mwaka 1990 hakuna anayerudi akiwa hai. Tafadhali sana tusifanye makosa safari hii….” Alinijibu. Majibu yake yakazidi kunipagawawisha maana ni kweli sikuwa najua kilichoniweka kule, zaidi ya kufahamu juu ya jina Vonso.
“Ningechelewa dakika moja zaidi ungekuwa maiti….” Alinambia na mara ghafla akaizungusha shingo ya yule muhudumu ikaelekea upande usokuwa wa kawaida.
Huo ukawa mwisho wa uhai wake……

Tukatoweka kwa njia mbili tofauti, mimi kwa njia ya kawaida mapokezi, na yeye akiruka dirisha. Tukakutana mbele ya hoteli ile na kutoweka.
MKASA ukaanzia hapo rasmi!!
Huku mimi bado nikiwa sina mwanga, bali kiza kikizidi kuchukua nafasi.

Kuna nyakati hutupitia katika maisha yetu nasi kuzitafsiri kama mkosi lakini ndani yake zimebeba maajabu ambayo huwezi kuyatambua ikiwa hautavumilia kile ulichokiita mikosi.

Baada ya kutoweka eneo lile Zay B aliita taksi na kumpa maelekezo ya wapi anapaswa kutupeleka, alimwambia jina ambalo sikulishika vizuri zaidi ya kumsikia yule dereva akimuuliza ikiwa wapite njia ya mnara wa saa ama kwingineko.
“Pitia mnara wa saa we jamaa” Zay alimwambia kwa Kiswahili, maksudi kabisa yule mwarabu akaduwaa akauliza kiingereza ni nini Zay ana maanisha, kwa pamoja bila kupeana taarifa tukajikuta tunacheka huku nikipata muda wa kuitazama sura ya mwarabu yule jinsi ilivyokuwa imebadilika kwa hasira, ndevu zake aina ya mustachi zikimfanya azidi kuchekesha.
Sisi tuliendelea kuzungumza Kiswahili. Mimi nikiwa mjibu maswali na Zay B akiwa ananiuliza mambo kedekede juu ya Tanzania yetu!!
Ilifurahisha hakika, na kwa wakati huo nikajikuta nikisahau juu ya hatari ya kumfuatilia Vonso kadri nilivyoonywa na yule mzee wa Tanzania.
“Ule kule ndo mnara mashuhuri wa Oman, mnara ule ni mkongwe haswa na ni kivutio kwa watalii….” Akasita akiniacha nikiutazama mnara ule kisha akaendelea.
“Sijui kinachowavutia kipi sasa hapo… si huu ni kama ule mnara wa saa wa Arachuga ama Mbeya…” akasita akiniacha nikicheka kutokana na kauli yake kisha akaendeleza vijembe.
“Bora nikashangae sanamu la posta limeshika bunduki miaka lukuki lakini halipigi risasi hata moja kuliko huu mnara….” Hapa tena tukacheka kwa pamoja.
Mwarabu akazidi kukunja sura, mustachi nao ukasisimka na kusimama.
Alifurahisha!!!
Hatimaye akatushusha baada ya kufika, Zay B akamlipa. Nikamwambia Zay ampe na nyongeza.
Zay akanipa habari kuwa nchini Oman hakuna uswahili wa namna hiyo, iwe kwa wahudumu wa mahoteli ama hao madereva wa taksi, Bakhshishi ni kitu kisichokubalika kabisa.
Kauli hii ikanifanya niipende nchi ya Oman hasahasa jiji hili la Muscat. Maana Tanzania yangu rushwa imegeuzwa kuwa bakhshishi
Sikujua kabisa kuna nyakati huja na furaha tele na kisha kugeuka ghafla!!
____
MSIMULIZI ANATOKA KATIKA PUMZIKO! ANAINGIA
ZAY B pamoja na Ramadhani waliingia katika mgahawa kwa ajili ya kupata chakula.
Ramadhani hakutaka kuonekana ‘wakuja’, akaishika karatasi iliyokuwa na orodha ya vyakula na bei zake.
Macho yake yakiwa yanaibia kumtazama Zay, akiutathmini urembo wa mwanamke yule mwenye mikono yenye uwezo wa kuua.
Rama alitumia kidole chake akawa anashuka chini hadi akalifikia neno ‘MISHKAK’
Badala ya kuchagua chakula Rama akaanza kucheka.
“Hawa majamaa nao wanaita Mishkaki… eti ili kujitofautisha wameondoa ile ‘i’ wanaita Mishkak… watu bwana”….. Zay aliyekuwa amejikaza asicheke akajikuta anacheka kwa sauti ya juu kidogo.
Uchangamfu wa Rama ulikuwa umemkosha, hakujua Rama alikuwa amepagawa na urembo wake tayari.
“Vipi nikuagizie SHUWA?” Zay alimuuliza Rama huku akiwa anamalizia kicheko.
“SHUWA?? CHURAAA? Sijakusikia vizuri….” Rama alihoji kimasikhara.
“SHUWA…. Hii ni nyama inaokwa taratibu hadi siku mbili chini ya ardhi kwa moto mdogo kabisa…..inapendwa japokuwa nasikia inaleta kitambi.” Alitoa maelezo yale.
“Sitaki SHUWA wana Chura… niletee Mishkak…” alijibu Rama huku akigeza lafudhi ya kiarabu.
Zay B akampungia mkono muhudumu, akampa maelekezo pamoja na pesa.
Baada ya dakika arobaini na tano, Rama alikuwa anashambulia mishkaki pamoja na Zay B huku kila mmoja akiwa na kinywaji baridi.
Wakiwa katikati ya mlo, simu ya Zay iliita. Akaipokea na kusikiliza kwa sekunde kadhaa…
“Simu muhimu afande… nikukute maeneo hayahaya..” alisema Zay akimwambia Rama, sasa hakuwa na tabasamu lolote usoni.
Akatoweka akimwacha Rama akimsindikiza kwa macho yaliyochanganyika nusu mshangao na nusu matamanio.
Baada ya kumaliza chakula, Rama alitoka nje ya mgahawa na kuangaza huku na kule huku akipiga mluzi kana kwamba ni mwenyeji sana.
Mara akajikuta akilikumbuka tukio la usiku ule, tukio la kukutana na Hajrati na sasa yu Muscat Oman kwa upelelezi.
Kitendo cha kumkumbuka Hajrati akakumbuka ladha ya ile bia yake ya mwisho kabisa.
Mawazo haya yakamletea kiu kikali cha bia.
Rama akaamua kuitafuta pombe, alipita mitaa kadhaa huku akijitahidi kukumbuka njia ya kwenda mgahawani na jina lake.
Hatimaye akafika alipohitaji, akaagiza chupa mbili za bia.
“Leseni ipo wapi? Maana sura yako ni ngeni hapa” akaulizwa kiingereza na muhudumu huku akimsaili vyema.
Leseni?? Rama akashtushwa!
Leseni kwake huja ikiwa anaendesha gari, sasa hapa ni baa anaulizwa leseni.
Akamwomba yule bwana amweleze vyema anachomaanisha.
Muhudumu yule mkarimu, akamweleza kuwa nchini Oman pombe ni haramu kwa waumini wa dini ya kislamu na hairuhusiwi kabisa lakini kwa watalii na wasiokuwa waislamu basi umri wa kunywa pombe ni miaka 21 na kuendelea tena katika baa ambazo zina leseni ya kuuza pombe, na mnywaji pia awe ameruhusiwa kunywa pombe.

Rama akatulia kwa sekunde kadhaa kisha akatokwa na tusi zito la nguoni kwa lugha mama ya Kiswahili huku akimlaani yeyote yule aliyepitisha sharia ile ya kikatili dhidi ya wapenda pombe kama yeye.
Aikainama kwa muda huku akilisikia koo likizidi kukauka, akamuita yule bwana aliyekuwa anataka kuondoka.
“Nisaidie walau chupa moja tu nakuomba…..” alibembeleza.
Yule bwana kwa kumsaidia akamuelekeza katika baa isiyofuata sheria mtaa unaofuata.
Looh! Amakweli kimfaacho mtu chake, Rama hakujali kuhusu kupotea akakatiza mitaa na kufika alipotakiwa kufika.
Kweli akaipata huduma, akanywa pombe chupa tatu.
Ile anaifungua chupa ya nne, likazuka balaa.
Alikuja mtu kuketi pahali alipokuwa amekaa, kama alivyokuja hajrati usiku ule, sema huyu hakuomba kuketi pamoja na Rama.
Akamsabahi Rama naye akajibu.
Huku akimimina ile pombe katika glasi yake.
“Samahani naweza kuona leseni yako ya unywaji pombe?” yule bwana akamuuliza.
Rama hadi wakati huo aliichukulia Oman kama Tanzania kuwa mikwara ni mingi kuliko vitendo.
Akatabasamu tu huku akiipeleka glasi mdomoni.
Mara akadakwa mkono na kuzuiwa kuinywa, akaulizwa tena swali lilelile.
Safari hii akajibu.
“Sina leseni ila ni mnywaji mzuri tu!”
Ile anamalizia jibu lile yule mtu akapuliza kipyenga, ghafla watu kadhaa wakamzingira Ramadhani ambaye alikuwa hajaijua vyema Oman.
Mmoja kati ya watu waliomzunguka alikuwemo yule dereva taksi mwenye mustachio.
Sasa alikuwa anatabasamu wakati huio Rama akifungwa pingu.
Ilikuwa bahati kubwa sana kwa Rama alikana kuwa yeye sio muislamu, na hili lilimsaidia kupatiwa hukumu ya mtu wa kawaida.
Alikaa rumande siku tatu, siku ya nne akasimamishwa mahakamani.
Akasomewa vifungu vya sheria.
Nchini Oman ukinywa pombe, ama kuuza kilevi bila kuwa na kibali unapelekwa jela miezi sita, ama unalipa faina ya reali mia tatu ama vyote kwa pamoja.
Miezi sita ikamuangukia Rama, reali 300 hakuwa nazo na wala hakuulizwa kama hanazo.
Bora hata angekuwa ni mwarabu angefikiriwa lakini ni mweusi tena kutoka Tanzania akashangaa anaingia jela bila kupewa nafasi ya kutafuta wakili wala kuujulisha ubalozi wake juu ya kinachomsibu.
Rama akiwa na masaa yasiyozidi sabini na mbili katika jiji la Muscat nchini Oman, akajikuta hajajua jina la mtaa hata mmoja badala yake akalijua jina la gereza kuu lililo katika jiji hilo.
Gereza la SUMAYIL (Sumayil Central Prison).
Lazima alijue kwa sababu ilikuwa ni nyumba yake.
Kama Zay B alivyobaki na pumbazo siku ilipopita bila kumwona Rama kisha zikawa siku tatu, hivyohivyo kwa sajini Pilipili na wenzake akiwemo inspekta jenerali mkuu wa polisi.
Wote hawa waliingia katika pumbazo baada ya kufikishiwa taarifa za Rama kutoweka.
Heri yao walikumbwa na jinamizi hili la pumbazo wakiwa mtaani, Ramadhani alikuwa ni mfungwa halali kabisa.
Kifungo cha miezi sita!
Harakati za kuutafuta mwili wa Rama zikaanza kufanyika chinichini bila kuushirikisha ubalozi wa Tanzania nchini Oman.
Wangeanza vipi kuushirikisha ubalozi ikiwa ubalozi ulishawakanya kabisa kujihusisha na harakati za kumnyamazisha Vonso?
Wangejibu nini? Kwamba hawakuelewa maana ya ‘mwacheni Vonso?’ ama ni kiherehere kimewaponza?
Sajini Pilipili akageuka kuwa mpole na mtulivu kama maji yaliyotiwa katika mtungi na kuachwa kama yalivyo ama mwanaume aliyekamatwa ugoni.
Jeuri yake ikayeyuka, na sasa akajikuta yu upande wa hatia dhidi ya mke wa Rama pamoja na mtoto wake. Ataanza vipi kuwaeleza kuwa Ramadhani amepoteza maisha lakini hata nguo yake aliyokuwa ameivaa haijaonekana?
Wangeanza vipi kuipokea taarifa hii na kuielewa kisha maisha yaendelee.
Sajenti pilipili alichanganyikiwa, akampigia simu inspeikta Zay B na kumuuliza kama kuna lolote ambalo amesikia juu ya mtu mweusi kuuwawa.
Akajibu ndio!
Pilipili akapata matumaini mapya kabla Zay B hajaua Tumaini lile kwa kuelezea kuwa aliyeuwawa sio Ramadhan.
Pilipili akakata simu na kujitupa kitandani!

ITAENDELEA!!!

Ep 3: Pumbazo

Leave a Comment