SIMULIZI

Ep 5: Pumbazo

SIMULIZI Pumbazo – Ep 5
SIMULIZI Pumbazo – Ep 5

Simulizi : Pumbazo
Sehemu Ya Tano (5)

Geza alimnyanyua Zai akajipima kama anaweza kumbeba vyema Zai, kisha akamtua na kutazama namna watakavyotoka eneo lile.
Funguo zilikuwa pale mlangoni, Geza akafungua mlango na kutazama mazingira.
Eneo lilikuwa tulivu kabisa, bila shaka waliwapuuzia sana wawili hawa kuwa hawataweza kuleta athari yoyote ile.
Geza akarejea na kumchukua Zainabu, akamweka mgongoni na kutoka kwa mwendo wa kawaida kabisa.
Moyoni akiwa na wasiwasi mkubwa sana juu ya usalama wao!!
Ilikuwa kama wasiwasi wake ulivyomtuma……
Walipolifikia geti la mwisho ili kutoka nje walisikia amri ikiwalazimisha kusimama palepale.
Kijasho kikaanza kumtoka Geza!!
_____
Nchini OMAN
RAMA ANASIMULIA
BARIDI lilianzia miguuni likanitafuna huku likipanda kwa kasi kuja mapajani, wakati huo mikono ilikuwa imekufa ganzi tayari.
Kumbuka nilikuwa uchi wa mnyama wakati huo.
Kuendelea kukaa katika ukiwa ule niliouita uhuru sikuona maana kubwa, nikaamua kupiga hatua mbele ili nielewe ni njia ipi nitaitumia kutoka pale. Kwa sababu usiku ulikuwa unakaribia kuaga ili jua nalo lichukue nafasi ya utawala wa masaa kadhaa yaitwayo asubuhi na mchana.
Nilitazama huku na kule lakini eneo lilikuwa kimya sana.
Baadaye nikaona taa kwa mbali, sikujua zilikuwa ni taa za chombo gani lakini upesi nilichukua tahadhari, nikatembea juu ya kile chuma kisha nikaingia majini eneo ambalo halikuwa na kina kirefu sana.
Sikulihisi baridi kali la maji yale kwa sababu tayari mwili ulikuwa umekufa ganzi.
Kile chombo kilizidi kukaribia eneo lile, niliweza kuyasoma maandishi ya ubavuni katika chombo kile ambacho sasa nilibaini kuwa ilikuwa ni meli.
Ilipiga honi mara moja, ikafika na kutua nanga, hapo sasa nikawa katika ushuhuda mwingine.
Chimbo la mauti lilikuwa linahamishwa kama sio kuvunjwa.

Nikahusisha simu ile kutoka Tanzania aliyokuwa anazungumza nayo bwana yule kwa lugha ya kiingereza nikahusisha na haya niliyokuwa nayaona.;
Aisee mateka walikuwa wengi sana, kiasi cha kutia huzuni.
Nikajiuliza vipi kuhusu wazazi wao? Je walikwisha amini kuwa ndugu zao wamepoteza maisha ama vipi….
Kupatwa na fikra hizi nikaikumbuka familia yako, hapa nikaingiwa na hofu kuwa huenda familia yangu imetangaziwa kuwa mimi ni marehemu tayari.
Nilimwomba Mungu isije kuwa kama nidhaniavyo!
Nilidumu katika maji hadi nikaanza kujihisi ninaishiwa nguvu na njaa nayo ilikuwa imenikamata vilivyo.
Baada ya saa zima, ile meli iliondoka.
Chozi la huruma likanitoka, nikawafikiria wale mateka ambao ndugu zao wanafahamu fika wapendwa wao walikwenda kujaribu maisha na hatimaye kupoteza maisha huko, tena kwa namna ya kuteseka hasawa.
Meli ile ilitoweka, sikuwa jasiri kuifuatilia na badala yake nilitaka niifikie dunia nitoe ushuhuda na baada ya hapo nitaungana na wengi katika katika kuikomesha biashara hii huku wahusika wa kifikishwa mbele ya sharia.
Meli ilipoondoka likafuata zoezi la kusaka nguo za kuustiri mwili wangu, kuhusu kurudi kule juu ambapo zilikuwepo nguo sikuwa tayari hata kidogo kucheza mchezo ule wa hatari kisa nguo yangu!
Nikiwa najiamini kabisa kuwa hali ni shwari, mara nikasikia kitu cha ubaridi sana kikigusa shingo yangu.
Bunduki! Nikatanabahi!
Nikatulia tuli, nikasikia naulizwa swali kwa kiarabu.
Sikujibu nikawa kimya tu. Alipouliza tena nami nikamjibu Kiswahili.
Lengo langu aghadhabike, na ikawa hivyo!
Nikawa naishi kwa hisia nikahesabu sekunde kadhaa za kufoka kwake kiarabu kisha upesi nikageuka alikuwa anataka kunipiga na kitako cha bunduki.
Mara moja nikawahi kuidaka ile bunduki kisha nikawahi kumfyatua teke kali katikati ya miguu yake, akalia kwa uchungu huku akiiachia ile bunduki. Nami nikaiachia nikapambana naye ana kwa ana. Hakuwa na ujuzi kuniacha mimi…
Nikafanikiwa kumdhibiti……
Japo haikuwa rahisi!
_____
BADA YA SIKU KADHAA.
HALI ya hewa ilikuwa tulivu kabisa, na hatimaye siku ilikuwa imefika.
Siku aliyoingoja kwa muda mrefu sana….
Yawezekana siku kumi zikaonekana chache kwa mtu aliye katika uhuru thabiti, tena asiyekuwa na msongo wa mawazo katika kichwa chaake. Lakini kwake yeye siku kumi zilikuwa sawa na mwana mzima.
Aliishi kwa tahadhali kubwa sana, akiwa na utaratibu wa kuvaa kofia muda wote hata pindi anapokuwa peke yake amejifungia chumbani kwake.
Alijijengea utaratibu wa kutojiamini hata yeye mwenyewe!
Siku hii alitoka katika chumba chake kwa sababu moja tu!
Kuuvunja ukimya na kutazama namna ya kuupata tena uhuru wake ili aweze kuzungumza anachopaswa kuzungumza.
Kabla ya kutoka chumbani alijitazama katika kioo kikubwa kilichokuwa pale chumbani, akaona jinsi mavazi yale aliyokuwa ameyavaa yalivyokuwa yamembadilisha.
Aliondoka kwa mwendo wa kawaida kabisa ili asimtie mtu yeyote mashaka ya kumfuatilia, alitembea kwa kujiamini kana kwamba ni mkazi wa pale tena mzoefu.
Akatembea hadi alipofika katika kibanda cha kupigia simu za malipo, alitazama foleni iliyokuwa pale naye akajiunga!
Baada ya dakika ishirini ilikuwa ni zamu yake.
SIMU iliita kwa muda mrefu sana, haikupokelewa mara ya kwanza ikaita tena mara ya pili. Hapa ikapokelewa baada ya miito mitatu.
Mpigaji alikuwa akitegemea sauti ya kike itapokea simu ile, lakini ajabu ikapokea sauti ya kiume yenye majibu ya karaha.
“Yupo bafuni anaoga mpigie baadaye…..”
“Mimi ni mume wake!” haya yalikuwa majibu mawili yenye uzito mkubwa sana kwa mtu aliyekuwa amepiga simu. Kwa unyonge kabisa akaikata simu…..
Kisha akazungumza kwa ghadhabu.
“Mama Jose ameolewa? Haiwezekani!! Haiwezekani nasema…”
Mzungumzaji akabaki kwa sekunde kadhaa katika kibanda kile kabla hajashtuliwa na muhitaji huduma mwingine.
Akampisha bila kumwomba radhi……
Akasimama pembeni kwa dakika takribani tano akitafakari juu ya jibu alilopewa na mwanaume juu ya mkewe kipenzi.
“Yaani kidogo hivyo ameshindwa kuvumilia anasahau kuwa bila yeye nisingeingia katika hali hii ya hatari iliyokuwa inaenda kugharimu maisha yangu?” alijiuliza kwa sauti ya chini kwa lugha ya Kiswahili.
Kufikia hapo mapenzi yakazidi nguvu mpango wake kamambe aliokuwa ameusuka kuanzia alipokuwa chimbo la umauti na sasa akiwa huru.
Yote aliyoyakusanya katika kichwa chake akayaona hayana maana akayaweka kando na kumjaza amama Jose katika fikra zake.
Akafikiria magumu yote aliyopitia hadi kuwa pale huru, akakumbuka hata mara ya mwisho alivyopambana kishujaa dhidi ya yule mwarabu na hatimaye kumdhulumu uhai wake na kumvua nguo kisha kutokomea na mtumbwi wake.

Mwisho wa safari anapata bahati ya aina yake, bahati ya kukuta kitita cha pesa katika nguo alizomvua yule mwarabu.
Baada ya utulivu mkubwa katika nyumba ya kulala wageni aliyojichimbia, hatimaye anaamua kutoka nje na kuwasiliana na namba ambayo hata akiwa usingizini katu hawezi kuisahau.
Namba ya mama Jose!
Anakutana na majibu ya kukatisha tamaa.
Rama akajikuta anatokwa machozi.
Na hapo MAPENZI yakamzidi nguvu!
Mpango ukabadilikia hapo.
Wakati Rama akibadilisha mpango wake, huku akiwa amepumbazika na kile alichosikia..
Nchini Tanzania pia mambo yalibadilika….
Ni kama tatizo lilikuwa katika chungu na sasa kuni zinachochewa kwa kasi!

FAMILIA hutazamwa kwa namna tofauti tofauti kutegemea mtu na mtu. Kuna mtu anaweza kuitazama familia yake kama kitu kisichokuwa na thamani kubwa sana na hata kushindwa kuilinda pale inapobidi.
Ni watu wangapi huwa tayari kushurutisha watoto wao wahukumiwe kwenda gerezani, ama kushindwa kujitoa kwa ajili ya wenza wao?
Kwa mzee Pilipili lilikuwa jambo zito sana linapokuja suala la familia. Alikuwa mkali kweli na mwenye maamuzi ya kutisha anapokuwa kazini lakini sio mbele ya familia yake.
Sio kwamba alikuwa bwege, lakini alikuwa mwanaume mwenye mapenzi ya dhati.
Kitendo cha kushuhudia watu wawili wakiuwawa mbele yake kilimaanisha kuwa muuaji alikuwa anajua anachokifanya na alikuwa anamfahamu bwana Pilipili nje ndani.
Ile hali ya kutambua kuwa muuaji alikuwa akimfahamu kwa ukaribu ilimaanisha kuwa muuaji alikuwa akiijua vyema familia yake.
Hili lilimsisimua sana na upesi akalazimika kuchukua hatua.
Alielewa wazi kuwa si yeye mwenye maamuzi ya kuifuta kesi ile ama kuacha kuifuatilia. Na katu asingeeleweka kwa mkuu wake wa kazi iwapo angemshauri kuwa waache kufuatilia ile kesi kwa sababu tu adui yao anawajua vizuri.
Jeshi la polisi Tanzania katu lisingekubaliana na jambo lile.
Hivyo Sajenti Pilipili akaamua kuchukua maamuzi binafsi kwa ajili ya kuilinda familia yake, usiku mnene akawatorosha kwa umakini kabisa…….
Akawarudisha kijijini alipozaliwa mkewe.
Bada ya kuwatorosha akajifikireia yeye mwenyewe na usalama wake. Hakutaka kuendelea kuishi nyumbani kwake, na hata nyumba za kulala wageni alizijua vyema.
Kuna wafanyakazi wanapenda kuingilia yasiyowahusu, wakimuona pale wataanza kutanganza kama wameombwa vile!
Baada ya mafikirio ya muda mrefu mwisho akapata jawabu.
Mama Jose!
Ni huyu angeweza kumuamini kabisa kuwa hawezi kumchomea kwa wabaya!
Ikawa hivyo, akahamia kwa Mama Jose, kule alipokuwa amempangishia!
Alikuwa anaingia pale usiku mnene kwa tahadhari na kuondoka asubuhi sana kwa tahadhari pia.
Hofu ilikuwa ikiandamana naye kila mahali.
Lakini walau sasa familia yake aliiona ina asilimia kadhaa za kuwa salama wakati huu harakati za kumsaka Vonso zikiendelea.
Na vile alitambua wazi kuwa Geza ambaye anasadikika kutekwa na maadui hajawahi kupajua nyumbani kwa mama Jose hivyo na yeye alikuwa mahali salama.
Ikaanza siku moja, ikafuata ya pili na ya tatu hatimaye akaanza kuzoea ile hali.
Hatimaye yakawa majuma mawili!!
Ikaja ile siku aliyopokea simu asiyoijua huku akiwa usingizini, akajibu anavyojisikia kisha akakata simu.
Mama Jose alikuwa ameiacha simu yake jirani na kochi ambalo sajenti alikuwa analitumia kulala siku zote alizokuwa akiishi pale .
Sajenti wala hakujali alivyojibu kuwa yeye ni mume wa mama Jose, kwa sababu mume wake alikuwa hayati tayari.
Hakuwaza hata kidogo kuwa alimjibu muhusika moja kwa moja.
____
RAMA alikosa raha kabisa, kila mara alijaribu kukwepa fikra zilizokuwa zinamkabili.
Mara akumbuke ile siku aliyokuwa anatukanwa na nduguze zamu kwa zamu kwa sababu ya kufikia maamuzi ya kuoana na mama Jose. Ambaye wanatofauti ya kidini.
Akilizuia hili hapo linamvamia jingine, mara anajiona alivyokuwa anambembeleza mama Jose alipokataliwa nyumbani kwao katukatu asithubutu kukanyaga tena endapo ataoana na Rama.
Rama akakumbuka jinsi alivyokuwa akibembeleza hadi kufikia kutokwa na machozi ya hisia.
Mawazo haya yalifuatana na mengine mengi.
Rama akawakumbuka wasichana kedekede warembo kabisa waliokuwa upande wake kidini ama waliokuwa tayari hata kubadilisha dini ili awaoe lakini wote akawafungia vioo kwa sababu moyo wake ulitua juu ya mama Jose.
Haya yote yaliitesa nafsi ya Rama.
Ikafikia hatua Rama akajiuliza ni kwanini alifanya harakati za kutoka katika chimbo la mauti, ni kwanini basi hakuamua kubaki tu na kufia katika chimbo lile huku akiwa hajui kabisa kama mkewe wa ndoa amejiingiza katika penzi na mtu mwingine.
“Kila jambo huja kwa sababu zake, nadhani mimi hili limekuja hili nimyooshe mama Jose. Na nikishamchukua mwanangu atajuta kuzaliwa…. Yaani…” Rama alijisemea huku akitembea barabara nzima huku anapepesuka.
Baada ya mwendo mrefu kidogo akashtuka kuwa hajui hata anapoelekea, akabadili uelekeo akaenda dukani na kununua maji huku akitumia uteja ule kuuliza maswali mawili matatu.
Majibu yale yakamsaidia sana.
Akapata tiketi kwa njia zisizokuwa halali, akatengenezewa na kitambulisho.
Pesa za yule mwarabu zilimsaidia sana.
Baada ya siku tatu alikuwa ndani ya ndege. Akiwa mtulivu kabisa, akifanana na baadhi ya abiria.
Ilikuwa safari ya kurejea nchini Tanzania.
Si kwa ajili ya Vonso tena lakini kwa ajili ya mkewe msaliti.
Lakini kitendo cha Rama kumsahau Vonso hakikumaanisha kuwa nd’o mwisho wa jinamizi lile kulindima katika maisha yake.
Mambo yalikuwa yanazidi kutokota.
______
KIKAO CHA DHARULA
KWA MARA ya kwanza ndani ya miaka kumi kilikuwa kimehitishwa kikao kikubwa sana kwa mara ya kwanza!
Awali vikao vilikuwa vinafanyika kwa njia za mtandao tu wanapashana habari na kugawana mapato. Lakini hiki cha sasa washika dau wote walipanda ndege na kutua nchini Kenya katika mji wa Mombasa kwa ajili ya kujadiliana kwa kina.
Nyuso zao zilijawa hofu, kila mmoja akiwaza kwa niaba ya nafsi yake, itakuwaje iwapo mambo hayataenda sawa?!
Kikao hiki kilijaa maswali mengi zaidi kuliko majibu. Huyu akiuliza hili na yule naye anauliza hili kisha anakosekana wa kutoa majibu yanayoeleweka.
Wahusika katika kikao hiki walitoka katika mabara matatu, Afrika, Asia na Ulaya. Walikuwa ni watu waliotakatishwa na ubora wa maisha yao, marashi ya bei ghali yalitawala katika chumba hiki cha mikutano katika hoteli waliyoichagua.
Kati ya maswali ambayo yalikuwa yanakosa majibu ni pamoja na kitendo cha Rama kutoroka kule chimbo la umauti ni nani aliyempa ramani na kushiriki katika kumtorosha???, nini kilifanyika hadi Geza akatoroka pamoja na Zay B???.
Rama, Geza na Zay B wanapatikanaje?
Kisha maswali mengine yakamgeukia kiongozi ambaye alikuwa anategemewa sana katika upande wa bara la Afrika hususani Tanzania..
“Muheshimiwa lakini hawa watu wako si ulisema unawamudu na umewazuia kufuatilia jambo hili?” mmoja kati ya wajumbe akauliza.
Muheshimiwa akabaki kuumauma kalamu yake huku kichwani jina Pilipili likijirudiarudia hovyo.
Hakujibu!
Mjumbe mwingine kutoka bara la Asia akalalamika.
“Nchi yangu kenda nyonga mimi…. Habataki kabisa neno hii ya nyanyasaji kule… watanyonga mimi…”
Hakuna aliyemjali!

Baada ya maswali yanayojibika kujibiwa hatimaye maamuzi magumu yakapitishwa.
Ikaangushwa mezani orodha kuu ya watu ambao wanatakiwa wapotezwe katika ulimwengu ndani ya muda mfupi kabisa ili mtandao ule uendelee kuwa imara kama zamani ama la mmoja tu akibaki hai basi mtandao utachafuliwa na hatimaye kufa kimyakimya huku wahusika wa mtandao huu kila mmoja akijiweka katika wakati mgumu sana dhidi ya dunia.
Majina yale yalikuwa yanatisha kwa wingi, na ilishangaza wengi pale lilipoorodheshwa jina la mtoto wa kwanza wa IGP Sungura aliyeitwa Sungura pia kama alivyoitwa baba yake mzazi.
Akaligeuza jina lake moja na kujiita ‘Rabbit’ ikiwa na maana ile uile ya Sungura.
Wenzake wakazoea kumuita Rabbit wa Sungura!!
Akazoeleka hivyo.
Kila mmoja akabaki kuguna chinichini, inakuwaje jina la Rabbit linakuwa la kwanza katika orodha, lakini pale hapakuwa na muda wa kujibu maswali bali kukimbizana na wakati ili waweze kujiokoa kutoka katika dhahama inayonukia mbele yao.
Baada ya majina kutajwa, katibu mkuu katika ule mkutano wa siri alinyanyua simu akazungumza kwa sekunde chache, mlango ukafunguliwa na watu watatu wakaingia pale ndani.
Suti walizovaa zilikuwa zinafanana na hata maumbo yao hayakupishana sana.
Wajumbe katika mkutano ule walikuwa wanaziona sura zile kwa mara ya kwanza. Lakini walipotajiwa majina yao kila mmoja moyo wake ukatulia tuli. Waliwahi kuyasikia majina yale.
Walikuwa ni wauaji wa kulipwa ambao waliajiriwa katika mtandao ule kwa shughuli za kumnyamazisha yeyote ambaye atasogeza pua yake kunusa kinachoendelea.
“Ndugu zangu, sina cha kueleza sana kwa sababu nyote mnawafahamu watu hawa…. Na wao wanawafahamu ninyi…. Na kuhusu nini cha kufanya katibu atawaeleza. Ila nimewaita hapa mbele yenu ili kwa pamoja tusije kulaumiana… ninawapa jukumu la kuondoa uhai wa yeyote katika mkutano huu ambaye watahisi anatufanyia usaliti wa namna yoyote ile…” akasita mwenyekiti akameza mate na kuendelea, “tumeaminiana kwa miaka kumi lakini haina maana kuwa hakuna wasaliti…. Wapo,” akageuka na kuwatazama wale vijana watatu.
“Tunawategemea sana…. Mnaweza kwenda” akawaaga wakatoka.
Matumbo yalikuwa ya moto kwa kila mjumbe, ile kauli ya kwamba wale mabwana wakihisi usaliti waue ilitisha sana.
Kila mmoja akawa na hofu ya kuhisiwa!!
Mkakati uliendelea kupangwa na kuona ni jinsi gani zoezi litaendeshwa vyema, waliweka vyema kila hatua na kuona dalili ya ushindi hasahasa baada ya kupata watu wengi wa kuweza kuwanunua ili waweze kushirikiana nao.
Swali jipya kutoka kwa mjumbe mmoja lilizua jambo jipya.
Na hapo kila mmoja akajikuta kimoyomoyo akilitaja jina la Vonso.
Mwishowe mwenyekiti akatoa kauli thabiti kuwa iwe isiwe lazima Vonso apatikane…….
Ni miaka sita ilikuwa imepita tangu jina hili lilipotajwa mara ya mwisho. Sasa linatajwa tena na kuna baadhi hawakuwahi hata kuifahamu sura ya Vonso!
Huu ukaonekana kuwa mtihani mkubwa haswa
Je ni nani na nani katika hiyo orodha ya kuuwawa…
Ugomvi wa kuwania mke nao…..
Vonso anasakwa tena!!

Mvua ilikuwa inanyesha na kuleta kiubaridi cha aina yake, kibaridi hiki kilikuja wakati muafaka na kuwafanya wakazi kulisahau joto kwa muda.
Nyumba nyingi walikuwa wamejifungia ndani ili kukwepa balaa la kunyeshewa.
Ni kawaida ya mji huu, mvua kuwa kitu tishio kwa wakazi.
Mvua ile ilitumiwa vibaya na wakazi wengine waliyoigeuza baridi ile kuwa mtaji wa kuzama nyumba za kulala wageni na wanawake wasiokuwa wao ama waume za watu!
Wakati watu wakiwa wamejifungia ndani, kuna wengine walijihifadhi katika nguo zao za kuzuia baridi na kuendelea na hekaheka zao.
Wakazi wawili, mwanaume na mwanamke walikuwa wakiongozana katika mvua ile ya rasharasha, mwanaume akitangulia mbele huku mwanamke akimfuata kwa ukaribu zaidi.
Wote hawa walikuwa wameivika miili yao nguo za kukabiliana na ubaridi ule.
Walikuwa kimya hatua kwa hatua hadi walipoifikia nyumba fulani iliyokuwa imejitenga kiasi kutoka katika nyumba nyingine.
Mwanaume alitazama kushoto na kulia kisha akaruka juu na kupapasa juu ya mlango akatoka na funguo.
Upesi akafungua akaingia ndani, huku nyuma akifuata na mwanamke.
Mlango ukafungwa!
“Hapa ndo nyumbani kwa Geza Ulole…..” Mwanaume akamweleza mwanamke, kisha akaendelea kuzungumza.
“Hapa hakuna umeme… kuna majirani tulikuwa tunachangia nao kulipia LUKU walikuwa wananinyonya.. nikawaambia wakate umeme wao waone kama ntakufa….” Aliendelea kuzungumza huku akitoa lundo la nguo lililokuwa katika kochi, ili yule mwanamke aketi.
“Kwa hiyo wakakata…”
“Walikata na hadi sasa sijafa… najua wanaumia sana!” alijibu Geza, na hapo cheko dogo likatoka kutoka kwa yule mwanamke.
“Ulisema unaitwa Zainabu au nani vile…” sasa alikuwa anautafuta mshumaa.
“Zay B…” akajitambulisha yule binti.
“Hilo ndo jepesi… Zay B.!” akarejea Geza huku tayari akiwa ameuwasha mshumaa.
Alipoketi tu, Zay B akafungua mfuko fulani na kutoka na makaratasi kadha wa kadha, wakayasoma tena kwa mara ya pili.
Makaratasi haya japokuwa hayakuwa katika muunganiko mzuri sana lakini ni haya yaliyowafanya wawili hawa walipofanikiwa kutoroka katika nyumba ile ya siri wasijipeleke kwa akina Sajenti Pilipili na IGP Sungura.
Makaratasi haya waliyapata baada ya Geza kupambana na yule mtu aliyemtisha na kumsimamisha wakati anatoka akiwa amembeba mgongoni Zay B.
Mtu huyu aliyewasimamisha alikuwa ameagizwa kuyapeleka mahali makaratasi yale, lakini bahati ikawa mbaya upande wake. Geza alimfyatua vibaya mno na kuundoa uhai aliokuwa anaumiliki.
Kosa alilofanya ni kumkaribia Geza aliyekuwa amembeba Zay B
Akamuuliza yeye ni nani Geza akajitambulisha kuwa yeye ni Solo. Jina ambalo alilisikia na kulikariri alipokuwa amebanwa na wale watu wawili aliowaacha ndani wakiwa hawana uhai.
Kujitambulisha kama Solo kukalegeza mashaka ya yule mtu, akaendelea kuwasogelea.
Geza akamsihi Inspekta Zay B afanye kitu.
“Legeza mikono yako…” Inspekta akamnong’oneza GEza. Geza akatii……
Kisha likabaki suala la kungoja yule mtu awakaribie zaidi. Zay B akahesabu hatua kwa hatua hadi alipofika panapotakiwa, akatokwa na pigo la umauti, yaani pigo ambalo litamtupa mbali adui yake huku na yeye akitua chini asiweze kuamka tena.
Ikawa!
Zay B akajitupa vizuri,akautumia mguu wake uleule uliojeruhiwa na Geza akamwadhibu yule bwana bunduki ikamtoka huku akitokwa na yowe la hofu.
Kabla hajakaa sawa Geza alikuwa amefika tayari, akamruka Zay B na kutua juu ya yule bwana akamshindilia ngumi nzitonzito hadi akalainika.
Huyu naye wakamuhoji maswali mawili matatu, akagoma kujibu.
Geza akamuua!
Wakaondoka na begi lake dogo.
Katika begi hilo wakayakuta makaratasi yaliyokuwa na maeolezo mbalimbali.
Kilichowavuta na kuwafanya waishi kwa tahadhari kubwa zaidi ni kukuta barua ikiwa imeandikwa ikitumwa kwenda kwa mtu aliyeitwa, Rabbit Sungura!!
Wote wakamuwaza IGP Sungura Sungura!!
Kengele ya hatari ikakung’uta vichwa vyao.
Wakakubaliana kwa sauti moja kuwa hawataenda kujionyesha mbele ya IGP wala sajenti Pilipili na badala yake watalitazama hili jambo kwa jicho la tatu.
Hatua ya kwanza ilikuwa Inspekta kupata tiba, hili walilifanyia Mlandizi mkoani Pwani nje ya jiji la Dar es salaam, baada ya Inspekta Zay B kuwa sawa walirejea jijini Dar es salaam na sasa wapo nyumbani kwa Geza Ulole.
Wanayasoma upya yale makaratasi, wakarudia kuisoma barua iliyoandikwa kwenda kwa Rabbit Sungura…. Wakakutana pia na barua kwenda kwa mtu aliyeitwa Vonso Almeida.
Jina hili likamshtua sana Inspekta Zay B.
Barua ile iliambatana na vitisho kedekede kuelekea kwa mtu aliyeitwa Vonso Lmeida.
Barua ile ikaambatana na majigambo kuwa wanaoandika barua hiyo wanafahamu fika kuwa Vonso anapatikana Kitunda. Na kama asipotii matakwa yao watamuua……
Wakaenda mbali zaidi kimajigambo na kutimiza masharti ya mkwara wakamtajia hadi nyumba aliyokuwa anaishi!

Barua ile ilipatikana pia ikiwa imeandikwa kiingereza na kuna nyingine ilikuwa katika kiarabu.
Zote zikitumwa kwa Vonso Almeida wa Kitunda.
Geza kama kawaida yake hakutaka wauache usiku upite.
Japokuwa Inspekta Zay B aliona kama ni uamuzi wa hatari sana na inawezekana maadui wakawawahi lakini Geza alitoa jibu lisilotarajiwa.
“Hakuna kitu napendelea katika maisha yangu kama michezo ya hatari. Hawa wajinga kwanza ni waoga yaani wanamuandikia mtu barua ya kumtishia kumuua? Ukitaka kuua usiandike barua we ua tu…..” akasita kidogo kisha akaendelea, “Yaani mimi enzi zangu shuleni, ukitokea ugomvi sijui wanaanza kuchora mstari atakayeuvuka mbabe… mi kabla hawajamaliza kuuchora tayari nishamvaa adui yangu nampiga ngumi ya usoni halafu nakimbia…” Geza akamaliza akimuacha Zay B akipambana kuzibana mbavu zake asicheke kwa sababu Geza alikuwa anamkumbusha mbali sana enzi za utoto.
“Kumbe na wewe ulipitia hizo..” Zay B akatia neno.
“Na nd’o chanzo cha kuacha shule mapema…. Wakati nipo darasa la sita kuna siku nilichelewa shule, ile mwalimu anataka kunichapa nikawa najaribu kukwepa… akaniuliza kama nataka kupigana naye. Akatupa fimbo chini akakunja ngumi…. Doh! Sijui nilipatwa na wazimu gani hata ile anatupa fimbo nikamtandika ngumi nikakimbia moja kwa moja, baadaye nikasimuliwa kuwa aling’oka jino.”
Zay B akastaajabu, akataka kuuliza zaidi lakini Geza akasihi waondoke kwenda eneo la tukio.
Hawakujua kuwa wakati wa balaa ulikuwa umewadia
______
Barabara ilikuwa mbaya sana kutokana na mvua kunyesha jijini Dar es salaam, na njia waliyopita ilikuwa na madimbwi mengi sana ya maji.
Hadi wanafika Kitunda nguo zao zilikuwa zimelowana kwa matope na pia kunyeshewa mvua ambayo bado ilikuwa inanyesha.
Geza asiyekuwa na utaalamu sana katika mambo ya namba za nyumba aliongozwa na Inspekta nyumba kwa nyumba hadi wakaifikia nyumba iliyokuwa imeandikwa katika ile barua.
Hakuna aliyekuwa na uhakika ikiwa nyumba ile ni sahihi ama la lakini walihitaji kumjua Vonso.
Wakauendea mlango na kubisha hodi kama mara tatu, mlango ukafunguliwa na mtoto mdogo.
Alikuwa ametawaliwa na usingizi hata hakukumbuka kusalimia.
Inspekta akamuuliza nani yupo ndani, bila wasiwasi mtoto akajibu kuwa babu yake yupo ndani.
Babu? Wakashangaa…..
Mtoto akaelezea kuwa babu yake alikuwa amelala zamani sana na hakuwa na kawaida ya kuamka asubuhi hadi panapokucha.
Geza hakukubali akamlazimisha yule mtoto amwamshe babu yake kwa sababu kuna jambo la msingi sana wanahitaji kumpa taarifa.
Mtoto akatoweka, baada ya dakika tano alirejea akiwa amemshika mkono mzee wa makamo kiasi.
Geza akamsalimia, mzee akawauliza wao ni akina nani.
Badala ya kujibu Geza akamuuliza iwapo yeye ni Mzee Vonso.
“Hapana naitwa mzee Magea… David Magea ndo jina langu!” alijibu huku akionekana kutetemeka.
Inspekta akaigundua ile hali, akatambua kuwa mzee alikuwa anadanganya.
“Mtakuwa mmekosea nyumba wanangu!” aliwaeleza huku akiwa anataka kuondoka.
Geza akamdaka mkono.
Akaisoma namba ya nyumba katika ile barua na kumuuliza kama ni nambari ya nyumba yake, mzee akatikisa kichwa kukubali.
“Sikiliza mzee sisi hatuna nia mbaya tupo hapa kukusaidia, hatupo hapa kwa sababu mbaya kabisa, kuna watu wabaya wanakutafuta. Ikiwa utasimamia msimamo kuwa we ni mzee Magea sijui mzee David shauri zako tutaondoka na wao wakifika watakucharanga mapanga wewe na mjukuu wako….” Alikoroma inspekta.
Kisha akafanya mkwara wa kumshika mkono Geza kama anayemtaka waondoke.
“Sikiliza,, sikiliza kidogo lakini aaargh! Lakini… ndio naitwa Vonso nyie ni akina nani…..” alijibu kwa kujilazimisha na sijue jibu lile iwapo lina msaada kwake ama amenunua balaa.
“Hutakiwi kulala katika nyumba hii leo….” Geza alimjibu.
“Ni kweli hautalala hapa tutaondoka wote mzee.” Ikasikika sauti mpya katika kile chumba.
Balaa!
Geza akapoteza umakini akageuka na kujikuta akichapwa ngumi kali begani akaenda chini, Inspekta Zay akawa makini zaidi tena katika ule ubora wake wa juu hasahasa akiwa na ghadhabu.
Akaruka juu juu na kufyatuka teke kali lililompata yule bwana kichwani akaenda alipokuwa Geza.
“Mbuzi kafia kwa muuza supu…” akaropoka Geza huku akimdaka yule bwana na kumtia kabali ambayo labda ilikuwa mara ya kwanza kupigwa katika maisha yake.
Alirusha miguu mpaka nafsi ilipopatwa uchovu ikaamua kuondoka zake.
Akatulia tuli.
Vonso alibaki akiwa amekodoa macho yake huku mjukuu akiwa hajui hili wala lile alikuwa ameuchapa usingizi.
Zay b upesi akaruka na kumdaka yule mtoto kisha Geza naye akamshika mzee Vonso wakatoka nje.
Huku wakamkuta bwana mmoja akiwa anavuta sigara.
Alipowaona akashtuka, ni kama hakutarajia kama watatoka salama humo ndani badala yake alitarajia mwenzake ndiye atakayetoka.
“Bastard!” akaponyokwa na lile neno huku akizikunja ngumi zake.
Inspekta Zay B akataka kujipeleka apambane naye Geza akaingilia huku akizungumza.
“Huyu hachukui hata dakika moja… ikizidi dakika moja nastaafu kupigana…” akazungumza Geza huku akijiweka sawa kumkabili yule bwana aliyeonekana kuwa mjuzi haswa katika hicho alichokuwa anakifanya.
Kweli haikuchukua hata nusu dakika, ile yule bwana anajiandaa kufyatuka, Geza akaingiza mkono wake mfukoni, akaichomoa ile bunduki aliyoizoea.
Akamfyatua kimya kimya mguu.
Akatokwa na yowe akatua chini kama mzigo.
“Si nilikwambia…” akajitapa huku akimsogelea yule bwana aliyekuwa anaugulia pale chini.
Akampiga kibao kikali sana usoni na kumuuliza maswali kadhaa kwa Kiswahili.
Akawa anajibu kwa kiarabu!
Geza akamtandika kibao kingine, akaanza kujibu kiingereza.
Kisha akamzamishia bisu katika mkono wake, “Mamaaa” akatokwa mayowe na hapo akagundua kuwa kumbe hata Kiswahili alikuwa anakijua.
Akambana maswali akayajibu.
Akajieleza kila kitu kuanzia mkutano mkubwa uliofanyika Mombasa, mkutano uliotoa orodha ya wanaostahili kuuwawa.
Geza akapekenyua katika mifuko yake na kuitoa ile orodha.
Ebwana eeh! Kati ya watu kumi walio katika orodha wanne kati yao walikuwa wamepigiwa tiki za rangi nyekundu tayari!!

Hili jambo liliwavuruga akina Geza na kujiona wapo dakika kadhaa nyuma ya wapinzani wao. Lakini walau waliwahi kumdaka Vonso waliamini kuwa huyu lazima atawaonyesha njia zaidi.
Yule bwana ambaye Geza amemchapa risasi ya mguu kimyakimya alikuwa bado chini, Geza akamwendea na kumnyanyua kisha akampa kitisho kikali.
Sasa Geza alikuwa na ghadhabu isiyopimika na hii ni baada ya kuona kuwa ule mchezo ulikuwa umekolea tayari.
Wakaondoka na yule bwana wakitumia usafiri wa pikipiki kwa dhana kwamba yule ni mgonjwa wao wanamuwahisha hospitali na kila mara Geza alimkumbusha kuwa akileta masihara anamtandika risasi bila huruma.
Sasa alitakiwa kuongoza njia.
Geza alipanda pikipiki moja na yule bwana huku Inspekta Zay B akipepea na mzee Vonso na mjukuu wake.
Wakati wawili hawa wakiwa katika harakati hizi za ‘ukizubaa umezikwa’ kuna bwana mwingine naye alikuwa katika harakati hizi lakini yeye aliongozwa na hisia pamoja na hasira kali.
____
PIKIPIKI aliyokuwa amepanda ilimpeleka hadi alipokuwa anahitaji kufika. Aliamini kiuhakika kabisa kuwa alikuwa hajakosea hata kidogo njia.
Alishuka akamlipa dereva kisha akaenda mlangoni na kugonga mlango.
Hakuwa na saa mkononi lakini mara ya mwisho wakati anatazama saa yake ilikuwa yapata saa nane usiku na dakika nyingi.
Hakujali kuhusu muda alikuwa anaongozwa na hasira hivyo hakuna alilojali.alikuwa amesubiri vya kutosha na aliona kuwa siku hii ilikuwa muafaka kabisa kuuvunja ukimya, upelelezi wake wa kimyakimya ulikuwa umegonga mwamba akaamua kujionyesha wazi.
Alibisha hodi zaidi na zaidi, hatimaye alisikia sauti ikimuuliza yeye ni nani.
“Rama! Mimi ni Rama…. Baba Jose…” alijitambulisha kwa sauti iliyosikika vyema.
“Nani? We nani…” sauti ya kike ikahoji kisha akamsikia muulizaji akiondoka kwa kasi, “Baba Aneth… we baba Aneth amkaa…” aliisikia sauti.
Ukimya ukatanda baada ya muda akasikia akiulizwa tena yeye ni nani, akajitambulisha kiufasaha zaidi.
“Tafadhali naomba mfungue mlango nina jambo la msingi sana” alizungumza.
“Wewe ni Rama yupi. Maana Rama amekufa huko Oman….” Alihoji mzee Fidelis ambaye ni baba mzazi wa Aneth.
Rama akajieleza kwa ufupi juu ya kilichotokea, hakutaja kuhusu chimbo la umauti bali alidai kutekwa na sasa yupo huru.
Akawasisitiza kuwa hajafa!
Nani afungue mlango? Hilo likawa swali, mama Aneth akamsihi baba Aneth afungue… wote walikuwa waoga wakiamini kuwa ule huenda ni mzimu.
Baba Jose akaenda mbali zaidi na kuhisi ni mzuka wa baba Jose umekuja kulipa kisasi kwa kitendo chake cha kumchapa makofi mtoto wake mdogo.
“Baba na mama… tafadhali tafadhali sana, je kuna ambaye aliona maiti yangu… sijafa nawaomba mfungue tafadhali… nina jambo la muhimu..” alisihi sana.
Baba Aneth akaufungua hatimaye, lakini alikuwa mwenye hofu bado.
Rama akamsalimu lakini hakutaka kuingia ndani akayamalizia mazungumzo nje.
“Nimeenda nyumbani kwangu, sijakuta mtu… nina shida na mke wangu…. Sijui kama yupo hapa?” aliuliza Rama akionekana mwenye wasiwasi na asiyetaka kupoteza muda kabisa..
“Umejaribu kumpigia simu yake…” aliuliza mama huku akiwa nyuma ya mgongo wa mumewe.
“Nimejaribu lakini sijapata majibu mazuri, nahitaji tu kuonana naye….”
Baba Aneth akamtazama Rama usoni, lile tukio la kumpiga Jose kofi la haja shavuni likajirudia akajiona mwenye hatia kubwa sana.

Na kitendo cha mwanaye kuondoka akiwa amesusa kilikuwa kinamtesa sana.
Mzee Fidelis akaona hii ni fursa ya kuitafuta suluhu na mwanaye kupitia kurejea kwa mume wake.
Akachukua simu yake akaziandika nambari za Aneth na kupiga, simu iliita bila kupokelewa.
Anamaanisha alichoapa!! Aliwaza mzee Fidelis.
“Sasa mwanangu, naomba ulale hapa sebuleni kisha asubuhi nitakuelekeza alipohamia Aneth… sio mbali sana….nadhani sasa hivi si muda mzuri” Alitoa muafaka, Rama hakuafiki alihitaji kwenda usiku huohuo.
“Doh! Basi sawa nitakupeleka lakini asijue kama ni mimi nimekupeleka maana naona anaishi… aah anaishi na mwanaume fulani na ni kama hataki watu wajue anapoishi mimi nilimwona kibahati tu nikafuatilia hadi nikapajua anapoishi….” Mzee Fidelis alitoa majibu yaliyomtia ukakasi Rama, ni kweli alihisi kabisa mkewe amemsaliti tayari lakini kimoyomoyo alikuwa anaomba hisia zake zisiwe kweli hata kidogo.
Sasa baba mtu anapigilia msumari mwingine!
Eti ni kweli Aneth mkewe anaishi na mwanaume.
“Sawa baba sitamweleza! Na vipi kuhusu Jose mwanangu” alijibu kinyonge.
“Yupo, anaishi naye..”
Mzee Fidelis akaingia na kujiandaa kisha akamuaga mkewe na kuondoka.
“Rama mwanangu!” mama Aneth alimuita, Rama akageuka
“Usichukulie hasira… kila mtu alijua umekufa nakuomba sana mwanangu sawa…. Mkumbuke mmezaa mtoto….” Alisihi mama Aneth huku akijenga picha jinsi Rama atakavyomshambulia Aneth kwa makofi na mateke pindi atakapomfumania na mwanaume mwingine.
Roho ikamuuma!.
Maneno haya yakawa yanashindilia ngumi nyingi zaidi katika fundo la maumivu ya Rama.
Akazidi kuumia!
Walipanda pikipiki moja watu wawili. Wakaenda kwa mwendo wa dakika ishirini na tano wakawa wamefika mahali stahiki. Wakashukia umbali wa mita zipatazo mia mbili kutoka nyumba anayoishi Aneth.
“Huyo mwanaume unamfahamu baba? Au aliwahi kuja kujitambulisha kabla yangu nyumbani?” Rama alihoji huku akitetemeka midomo.
Sauti ya Rama ilimuumiza mzee Fidelis alijua wazi kijana huyu anapitia uchungu mkali wa mapenzi.
“Hapana namfahamu kwa wadhifa wake tu lakini si mengineyo…”
“Kwa hiyo mama Jose alifuata pesa kwa jamaa sio?!” alihoji Rama huku machozi yakimlengalenga.
“Looh! Rama mwanangu, hapa nitakudanganya mi sijui lolote, kuna muda niligombana naye kidogo ndo akaondoka na nikagundua anaishi na huyo mwanaume…ni askari tu!” alijibu huku akibinua mabega kujitoa katika hatia ya uchonganishi.
Kusikia kuwa mama Jose ameangukia kwa askari, Rama akashtuka na kuanza kumchimba zaidi mzee Fidelis juu ya muonekano wa huyo mwanaume.
“Mwanangu… huyo mwanaume wanasema tu yupo ila mimi sijawahi kumuona, wanasema anaingia usiku sana na kutoka asubuhi..”
“Sawa baba asante sana…. Nitakujuza kitakachojiri” alizungumza kinyonge Rama huku akimgongagonga mgongoni baba mkwe wake ambaye alipanda pikipiki ili aweze kuondoka zake kabla Rama hajafanya alilokusudia.
“Rama usiwaletee vurugu zozote, anaweeza kuwa na bunduki huyo bwana mkazua mengine… licha ya yote yaliyopita Rama mi nawapenda sana nyote wawili. Ninajua makosa yangu ya wakati wa nyuma na nimeyajutia.. sitaki kuwapoteza Rama” alizungumza kwa hekima sana mzee Fidelis, hii ikiwa ni mara yake ya kwanza kabisa kuzungumza hivi dhidi ya Rama.
Rama akatikisa kichwa kukubali, pikipiki ikaondoka.
Rama akawasindikiza kwa macho, akawa anamtazama mzee Fidelis na kukiri katika nafsi yake kuwa hakika mzee yule alikuwa amebadilika.
Ile anataka kugeuka ili aelekee katika nyumba ile kufanya alilokusudia mara ukasikika mlio wa risasi, tairi ya pikipiki ikafyetuliwa baba mkwe akarushwa kule na dereva naye akibaki hoi. Rama alikuwa ameshtukizwa sana, alibaki kuduwaa…
Lakini hakutukubali iwe namna yay eye kufikia mwisho kirahisi vile, akajirusha pembeni na kisha akajificha katika jumba lililokuwa linaendelea kujengwa. Akiwa anahema juu juu sana akawa anachungulia kule lilipotokea tukio la ghafla akajisahau kuwa ficho huwa ni la wote sio la mtu mmoja.
Ubaridi ukapenya katika shingo yake, na kisha ikawa amri tulivu kabisa.
“Ukipiga kelele ama kufanya jaribio lolote la kipuuzi nakuua!” sauti ilimtisha nyuma yake.
Alikuwa ametekwa!
Rama akasalimu amri kwa kunyoosha mikono juu.
Akavamiwa na kupigwa ‘mtama’ akatua chini, na hapo akajikuta akitazamana na mdomo wa bunduki.
“Nauliza mara moja kifuatacho kitendo….” Ilihoji ile sauti na kuendelea, “Rabbit Sungura yupo wapi? Sihitaji jibu la sijui ama la nasambaratisha kichwa chako…..” ilikoroma ile sauti isiyokuwa na punje ya masihara. Na hapo kwa macho yake Rama akakiona kidole cha yule bwana aliyeuziba uso wake kikianza kuvuta kiwambo cha kuruhusu risasi itoke.
Lakini ghafla ukasikika mshindo mkubwa, Rama aliyekuwa amefumba macho akafumbua. Hakuwa chini peke yake…
Alikuwa pamoja yule bwana lakini tayari alikuwa maiti.
“Take the gun!” aliisikia sauti ikimsihi, hakutaka kujua ni nani akaichukua bunduki kutoka pale chini, kisha akabiringita na kujiweka tayari kwa pambano lolote litakalokuja mbele yake.
Kwa mbali alimwona baba mkwe wake pamoja na dereva wakiwa bado wametulia tuli!!
Rama akiwa katika ficho lake, mara akamwona mwanamke akitoka katika ile nyumba, macho yake hayakumdanganya alikuwa amemuona mke wake wa ndoa akiwa amevaa nguo nyepesi kabisa ya kulalia iliyoyachora maungo yake.
Mara nyuma yake akatoka mtu aliyemfahamu fika.
Angeweza kuwa mwanaume mwingine asinge jali.
Lakini alikuwa ni sajenti Pilipili akiwa amevaa pensi pekee huku akiwa kifua wazi na bunduki yake mkononi.
“Simameni hapohapo mlipo wendawazimu wakubwa nyinyi!” Rama alitoka katika ficho lake akiwa ameielekeza bunduki kuwaelekea Aneth na Sajenti Pilipili.
Wote wakasimama wakijua ni adui.
“Sajenti umenitupa Oman niende kufa ili ufanye haya?” alilalamika.
Mara Aneth akiwa amembeba Jose mgongoni aligeuka.
“Mume…”
“Shhhh!!! Hakuna mume wako hapa… mbele yako ni mwanaume mwenye roho mbaya kupita kiasi….. ukipiga hatua mbele zaidi ninakuua malaya wewe, nawe muuaji tupa hiyo bunduki chini kabla sijaielekezea hii bastola katika korodani zako…”
Sajenti akaiachia bunduki yake huku akiwa amepigwa na butwaa kumuona Rama akiwa hai.
“Rama… ni nini hiki?” alihoji.
“Unaniuliza ni nini hiki…. Hiki ni kituko cha mwaka, mwanaume mmoja mwenye madaraka anaamua mwenzake afe ili amrithi mkewe… simple tu kama hivyo.” Alijibu Rama huku akilazimisha tabasamu.
Alikuwa mwenye hasira kali sana na alikuwa tayari kuua.
Macho yake yalikuwa yanawatazama watu wawili ambao kwa jinsi mavazi yao yalivyokuwa basi muda si mrefu walikuwa wametoka kuridhishana kimapenzi.
Akafumba macho huku akimjengea picha jinsi Aneth alivyokuwa akifanya jitihada ili kumfurahisha sajenti Pilipili kitandani.
Huenda Jose alikuwa bado hajalala, kwa hiyo mwanangu amemuona mama yake anafanya mapenzi na mwanaume mwingine!
Aliwaza Rama huku akiuma meno yake kwa ghadhabu kali…..
Nawaua! Aliapa…….
Kisha ghafla akafyatua risasi!!

Bunduki ilikuwa haipo katika kiwambo cha kuzuia sauti ilitoa mlio mkubwa sana baada ya Rama kufyatua. Alikuwa amefyatua hewani
Mama Jose akaanguka chini, akawa amemwangukia Jose. Jose akaanza kulia.
Kilio chake kikapenya katika masikio ya Rama…..
Akajikuta anaishiwa nguvu, akaishusha bunduki yake chini.
Akakimbilia alipokuwa mama Jose akamkwapua mama Jose huku akiwa makini kabisa kumtazama Sajenti asije kuzua balaa lolote.
“Rama… sajenti aliita, “ kisha akaendelea “sio muda huu Rama, sio muda huu hatuwezi kuzungumza lakini elewa kuwa hili ni pumbazo….” Alitaka kuendelea kuzungumza lakini ghafla akapokea pigo maridhawa kutoka kwa Rama. Lilikuwa pigo ambalo hakulitarajia, teke kali likatua katikati ya miguu yake.
Sajenti akatoa kilio kikubwa haswa cha uchungu.
“Nyamaza mwanangu!!” Rama alimbembeleza Jose aliyekuwa akitokwa na kilo kikubwa bado.
“Rama hebu nisikilize kidogo!” alisihi sajenti. Rama akamtazama lakini hakusema neno lolote.
“Rama unalodhani si sawa hata kidogo, tuondoke eneo hili si salama kwetu hata kidogo. Tazama Rama ningekuwa na nia mbaya nisingefyatua risasi na kumuua huyo bazazi aliyetaka kukumaliza, kwanini nisimwache akuue ili nifanye hayo unayowaza kuwa nilikuwa nafanya!! Rama kuwa mwanaume imara sina nifanyalo na mkeo, nimekuwa nikimlinda…” alizungumza kwa kufoka sajenti.
Rama akaanza kuingiwa na yale maneno, na palepale sajenti akatokwa na teke kali la haja likaipiga ile bunduki ikarushwa mbali.

Rama aliyekuwa amebeba mtoto akataka kuikimbili lakini tayari Sajenti alikuwa ameokota bunduki yake kisha akamwonya Rama asipige hatua zaidi.
“Kwa hiyo unataka kuniua ili umfaidia mke wangu sajenti…” alizungumza kinyonge.
“Niue lakini usimwache mwanangu hai.. tuue sote. Ubaki na mwanamke wako..” alimalizia Rama.
“Rama mimi ni mtu mzima, unajua kuhusu familia yangu Rama.. nimewahi kukueleza hapo kabla familia yangu ni kitu cha muhimu kupita kitu kingine duniani, Rama nipo hapa kwa sababu tu nimetakiwa kuwepo sijawahi na wala sina mpango wowote wa kushiriki dhambi hii unayonitamkia. Rama mtandao wa Vonso umechachamaa, ni hawa waliotaka kukuua dakika kadhaa nyuma, Rama hatupo sehemu salama. Simama kama mwanajeshi weka haya mambo kando!” akasita akameza mate kisha akatoa amri.
“Ninazungumza kama mkuu wako wa kazi sasa, mpatie mtoto mama Jose kisha pick up the gun tunaingia vitani!!”
Ilikuwa sauti ya amri haswa Rama akatii!
Lakini ni kama alichelewa sana kutii, walijikuta wamezungukwa na watu wanne wenye silaha nzito kabisa.
Hakuna ambaye alithubutu walau kufyatua risasi kutoka katika bunduki yake.
Wakatekwa na kufungwa vitambaa vyeusi usoni, wakapakiwa katika gari na watu wasiowajua.
Ndani ya gari sajenti alimlaumu Rama kwa kuendeshwa na hisia zaidi kuliko uhalisia
_____

MWAKA 1965, Visiwani Zanzibar.

ILIKUWA imepita miaka miwili bada ya mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanya kisiwa hiki kuwa huru kutoka katika utawala wa mwarabu.
Waarabu ni moja kati ya watu ambao hawakufurahia kabisa jambo hili kwa sababu walizoea kuishi katika kisiwa hicho. Lakini si waarabu pekee wapo waswahi wachache ambao pia hawakufurahia jambo hili.
Mmoja kati ya waswahili hao alikuwa ni Sameer bin Alafat ambaye baadaye alibadili jina lake na kujiita Vonso Almeida, jina alilotunukiwa na mtawala wake ambaye ni mwarabu.
Huyu alikuwa ananeemeka kutokana na uwepo wa waarabu, aliwafanyia kazi na kuwanyenyekea walivyotaka na kujikuta akiipata ridhiki yake kiulaini sana.
Kuna waswahili walikuwa wakimchukia lakini hakujali kwa sababu kila mmoja alikula kwa jasho lake.
Kitu cha msingi ni kwamba katu hakuwahi kuvujisha siri zozote alizojua kuhusu harakati za kuusaka uhuru.
Waarabu walimpenda kwa sababu ya unyenyekevu wake, na hata baada ya uhuru walimuuliza iwapo yupo tayari basi waende naye Oman.
Vonso akakubaliana nao.

Aliyazoea mazingira ya Oman upesi sana na ni huko alipujifunza mengi kuhusu waarabu, aligundua kuwa ni watu wasiopenda kufanya kazi za mikono, badala yake wanapenda kufanyiwa kila kitu.
Hizi kazi yeye aliziweza na aliamini kuwa wazanzibari wengi tu wanaziweza kwa sababu walizoea suluba za utumwa.
Akiwa ametimiza umri wa miaka thelathini mnamo mwaka 1975 akiwa sawa kabisa na waarabu wa Oman, Vonso alianza kuwatafutia neema wazanzibari wenzake. Kila akienda Zanzibar anaondona na wanaume watano na wasichana watano na kuwapeleka Oman kufanya kazi ambapo walikuwa wanapata malipo mazuri kabisa.
Waarabu wenginje waliposikia juu ya hili na wao wakaanza kumsumbua Vonso awatafutie wafanyakazi.
Hatimaye mwaka 1980 Vonso akafungua kampuni yake ya kusaidia watu kupata ajira akaiita Vonso Almeida!.
Kampuni hii ilimwingizia kipato, lakini pia ukawa mwanzo way eye kupumzika na kuwaacha watu wengine wasafiri kwenda Tanzania bara na visiwani kusaka wanaohitaji kufanya kazi nje ya Tanzania.
Kuna tetesi zilianza kuvuma miaka ya 1985 ambazo zilimtesa sana Vonso ambaye ni mcha Mungu!
Alisikia kuwa kuna baadhi ya vijana wake wanachukua rushwa ya ngono kwa wanawake kabla ya kuwafikisha Oman ambapo wanakuja kufanya kazi.
Alilikemea jambo hili lakini hakutajiwa muhusika, kampuni nayo ikazidi kuwa kubwa!
Mnamo mwaka 1990 kesi zikawa nyingi sana za unyanyasaji, sasa haikuwa kutoka kwa waswahili peke yao bali waarabu kwenda kwa waswahili.
Vonso alikuwa anawaheshimu sana waarabu kwa jinsi walivyomtunza kuanzia uvulana hadi anakimbilia uzee wake.
Kuliko kuzua mabishano nao, akaamua kung’atuka katika kiti chake cha ukurugenzi.
Akawaambia maneno yake machache sana, wenzake ambao wote walikuwa wanamzidi kisomo.
“Kama mnalofanya mnalijua ni dhambi na mnalificha huku mkiendelea kulifanya wallah! Nawaapia mwenyezi Mungu atawahukumu siku moja…!
Wasomi wakacheka wakampuuza!
Vonso akaondoka lakini hakuwakabidhi hati wala katiba ndogo ya kampuni yake.
Akarejea Tanzania bara badala ya Zanzibar, akaanza kufanya ujenzi na kisha akahamia nyumbani kwake maeneo ya Kitunda akatulia tuli akajisahaulisha kabisa kama aliwahi kuwa na kampuni kubwa kabisa iliyokuwa inamuingizia pesa.
Na ili asahau zaidi juu ya ile kampuni, alipotua pale Kitunda akajitambulisha kwa jina la David Magea!
Wakamzoea kwa jina la mzee Magea.
Maisha yakaendelea!
Miaka inakatika na sasa yupo mikononi mwa akina Geza usiku wa manane pakiwa na hekaheka juu ya kampuni yake inayojishughulisha na biashara ya utumwa wa kisasa.
Si kijana tena sasa ni mzee!
Maelezo ya Vonso yaliwagusa sana Inspekta na Geza, wakamuuliza maswali mawili matatu.
Akaelezea kila alichokuwa anakitambua.
Geza akamwagiza Inspekta waende kuwahifadhi mahali Vonso na mjukuu wake ili wao waingie kazini moja kwa moja.
Ikawa hivyo!

_______

MAKUTANO YA PUMBAZO

KIMYA kilikuwa kimetanda haswa, na giza lilikuwa limetawala. Baadaye taa ikawashwa…
Mateka kadhaa wakaonekana wakiwa na vitambaa vyeusi usoni.
Hakuna mateka aliyepewa nafasi ya kujitetea zaidi ya kuitwa jina lake na anapoitika anasogezwa mbele zaidi katika foleni.
Liliitwa jina la Ramadhani, akaitwa Sajenti Pilipili, akaitwa Mama Jose, akaitwa Jose yule mtoto akawekwa peke yake huku analia, hakuna aliyejali, akaitwa mzee Fidelis, akaitwa Rabitt Sungura, lakini hakuwa amepatikana bado.
Kisha kikafua kitendo cha bunduki kuandaliwa kwa ajili ya kuwaondoa katika uso ule wa dunia kwa kosa la aidha kugundua juu ya harakati za chimbo la mauti ama namna yoyote ile.
“Geza….. chukua wawili na mimi nachukua wawili wale wenye silaha…” alinong’ona inspekta Zay B kutokea katika kona waliyokuwa wamejificha wakiwa wameingia mapema zaidi kuliko kundi lile la watu wengi… alipomgeukia Geza aligundua kuwa Geza alikuwa akibubujikwa na machozi.
Ilikuwa mara yake ya kwanza kabisa kumuona Geza katika hali ile hakuweza kuhoji kwa sababu muda ulikuwa unazidi kwenda.
Inspekta akahesabu hadi tatu kisha akafyatua risasi akiwaangusha wale wawili lakini Geza alimfyatua mmoja tu na hakutumia risasi tena akatoka mbio kutoka katika lile ficho.
Inspekta akabaki kuduwaa ni nini kilikuwa kinamsibu Geza.
Geza akajirusha na kumkamata yule bwana aliyediriki kumshika yule mtoto na kumweka katika orodha ya wanaostahili kufa bila kujali kilio chake. Alikibamiza kichwa cha yule bwana chini mara kadhaa akaamka naye akajirusha naye chini.
Kwa kifupi Geza aliua kwa hasira kali zaidi kuliko mara zote alizowahi kuua.
Baada ya hapo alisimama akiwa amelowa damu.
“Sina mtoto lakini ole… ole kwa atakayediriki katika hii dunia kumnyanyasa mtoto mdogo mbele yangu..” alisema huku akimsogelea Jose, akamfungua kile kitambaa cheusi na kumkumbatia.
“Ba…. Ba….” Jose alisema kwa sauti ya kitoto toto….
Zay b akatokwa machozi.
Baada ya dakika kadhaa Zay B alikuwa anapiga saluti ya heshima mbele ya Sajini Pilipili.
Rama alikuwa amekumbatiana na mkewe huku wakihofia kumwomba Geza awapatie mtoto aliyeonekana kumzoea na kumpenda tayari.
Fahamu zilikuwa zimerejea kwa mzee Fidelisi na dereva wa bodaboda, wao walikuwa wakijiuliza kulikoni na hakuna aliyewajibu.
“Vonso ni mtu hatari sana..” Sajenti alisema, Geza akacheka kwa sauti…. Hii ilikuwa mara yake ya kwanza kutokwa na kicheko kikubwa vile.
Inspekta Zay B akaelezea kwa kifupi juu ya Vonso na hapo akampa pole Rama kwa yaliyomsibu.
“Mbona uliniacha nikatekwa Zay B” Rama alihoji.

“Nilipokupungia mkono nilikuwa nimetekwa tayari… tumshukuru Mungu kuwa tupo hai.” Alijibu kwa sauti tulivu yenye mahadhi ya Zanzibar.
Rama akatabasamu.
_____

Mwili wa Rabbit Sungura ulikutwa katika ufukwe wa bahari ya hindi jijini Dar es salaam ukiwa ulishapoteza uhai muda mrefu sana.
Nchi za Tanzania na Oman zilishirikiana kikamilifu kuwatia nguvuni wote waliohusika katika mkakati huu wa kiuaji.
Maafisa wa uhamiaji walikamatwa kwa fujo katika msako huo, huku wengine wakikutwa na hatia.
Wahusika katika mpango huu walifikishwa mbele ya sheria, wale wa Tanzania walihukumiwa maisha jela huku wale wa Oman wakihukumiwa kunyongwa.
Wakati haya yanatokea familia ya Rama pamoja na ile ya Aneth kwa pamoja walikuwa wanasheherekea upya harusi ya watoto wao hawa.
Watu baki kadhaa akiwamo Nasra walijumuika pia katika hili
Yaliyopita si ndwele ndo walivyosema!!

Geza kama kawaida yake, alipotea katika uso wa wanadamu na kuendelea na maisha yake mbali kabisa na jiji la Dar es salaam, hakuwepo hata katika ule mgao wa zawadi kubwa waliyotunukiwa wote walioshiriki katika kung’amua uozo huu wa miaka kumi.
Sajenti Pilipili na Inspekta Zainabu walipandishwa vyeo, huku IGP akirejeshwa kazini baada ya kupelelezwa na kuonekana hausiki na hakujua juu ya mwanaye kushiriki katika mkakati ule.
Umoja kati ya Oman na Tanzania ukazidi kukua maradufu huku ulinzi ukiimarishwa zaidi ili tukio kama hili lisiweze kutokea tena asilani.
Ile siku IGP anarejeshwa kazini alipokea ujumbe kutoka katika namba mpya.
“Ujue hadi leo sijalipia zile bia pale baa walipokunywawale mademu! Mtume Pilipili anapafahamu wanadai kama elfu sita mia tano hivi! Msalimie Zay B mwambie tutakutana tena”
Mtuma ujumbe hakuandika jina lake, lakini IGP alijikuta anatabasamu.
“Vipi mkuu!” alihoji sajenti akiwa pamoja na IGP.
“Geza kanitumia ujumbe….”
Wakajikuta wanacheka kwa pamoja, safari hii wote walikuwa wanamjua vizuri!

Na huu ndo mwisho wa riwaya hii ya Pumbazo.
Ni Tungo kutoka kwa mwandishi George Iron Mosenya, tungo hii ni haikuwa na nia yoyote mbaya kwa jamii yoyote ile.
Ikiwa kwa namna moja ama nyingine imevunja amani ya nafsi yako.
Ninakuomba radhi!

MWISHO

TOA MAONI YAKO, LEO USIPITE KIMYAKIMYA

ASANTENI!!!

Leave a Comment