LIFESTYLE

Mambo 11 wasiyopenda wanaume

Mambo 11 wasiyopenda wanaume
Mambo 11 wasiyopenda wanaume

Bila kuwachosha niende moja kwa moja kwenye mada ya wiki hii ambayo inahusu mambo 12 wasiyoyapenda wanaume kwa wapenzi au wake zao.

1. Kujipamba kupitiliza
Mwanamke kama mwanamke ni mapambo na ili awe mwanamke anao ulazima wa kuhakikisha anaonekana smati kwa kujipamba lakini si kama wafanyavyo wanawake wa siku hizi.

Wanaume wengi wamejikuta wanachukizwa na hali ya mwanamke kujipamba kupitiliza.

Yaani unakuta mwanamke anajipamba utadhani siku hiyo ni siku yake ya kufunga ndoa, hilo ni tatizo na husababisha hata mwanaume kuogopa kuongozana naye.

Sasa je, kama unatoka na mume au mpenzi wako, unajipamba hivyo kumfurahisha nani hasa? Mbona ukiwa nyumbani unakuwa wa kawaida tu?

2. Matumizi makubwa ya fedha
Mwanamke mwenye matumizi makubwa ya fedha ambaye hafikirii kesho itakuwaje ni adui mkubwa wa mwanaume.

Hata kama atakuwa anakupenda kiasi gani, atakuvumilia siku za mwanzo lakini kadiri mnavyokwenda atajitoa kwako taratibu. Hii ni kwa sababu mwanaume atahisi siku akija kuwa hana kitu anaweza kuibiwa na wenye fedha.

3. Muongeaji sana
Mwanamke muongeaji sana asiyekuwa na staha, mwanamke ambaye hawezi kumvumilia mwanaume pale anapokuwa akimsema kwa jambo f’lani kwa nia ya kutaka maelewano ni tatizo.

Namzungumzia yule ambaye muda wote anataka kushindana na mume/ mpenzi wake katika kuongea, yaani kuonesha kuwa hajakosea, anaonewa au na yeye yumo kwenye kuongea, huyu hawezi kumshika mtu wake.

Mwanamke anayeijenga ndoa yake anatakiwa kuwa chini pale mwanaume anapokuwa anapaza sauti, akishapoa na wote mmepoa. kama una dukuduku lako ongea naye taratibu.

Haiwezekani mume na mke kuwa juu hasa mnapokuwa kwenye mgogoro, inatakiwa mwanamke kumsoma mume wake au mpenzi wake kwa wakati huo.

4. Mwanamke kiguu na njia
Sifa ya mwanamke ni utulivu, kama wewe mwanamke una tabia za kupenda kwenda kila unaposikia ngoma au sherehe, wanaume wengi huwa hawapendezwi na tabia hii. Basi kuwe na sababu ya wewe kutoka si kila shughuli ikuhusu wewe.

Wapo ambao hukatazwa na waume zao na kulazimisha kwenda ilimradi tu aonekane naye hajapitwa na sherehe huku akiwa amevaa sare. Kama una tabia hiyo jiangalie.

5. Wivu wa kupindukia
Mwanamke mwenye wivu wa kupindukia humfanya mwanaume kukosa amani kwani hata awapo kazini kwake mwanamke atataka kumfuatilia na kumnyima uhuru.

Hawa wenye tatizo hili huachwa na wanaume wao haraka kwani wengi hawapendi kuonewa wivu wa hivyo, wengine huuita wivu wa kijinga.

Isikupite Hii: Tabia za Mwanaume Ambaye Hakutaki

6. Mashoga wengi
Wanaume si waumini wa wanawake wanaopenda kuwa na mashoga lukuki au vikundi. Huwachukulia wanawake hao kama wambeya wanaopenda makuu.
Utakuta mwanaume anampenda mwanamke f’lani akimchunguza na kuona ni mwanamke anayependa makundi au ana mashosti kibao huamua kumuacha.

7. Kumsifia aliyepita
Wanawake wengi wakiudhiwa na wanaume wao wawapo kwenye malumbano hupendelea kukumbushia penzi la zamani kwa kusema: ‘Nilipotoka sikuwahi kufanyiwa kama hivi unavyonifanyia sasa.’

8. Kumpanda mume kichwani
Wapo baadhi ya wanawake ambao mara nyingi wanapenda waonekane ndiyo wenye sauti ya mwisho ndani ya nyumba. Kwamba akisema kitu mume asihoji, akitaka kufanya lake asizuiwe.

Hili ni tatizo na kwa wasiojua ni kwamba wanaume wengi hawapendi wanawake wenye hulka hii.

9. Kujifanya ‘expensive’
Mwanamke anaweza kuwa kaolewa au yuko kwenye uhusiano na mwanaume wa kawaida ambaye hana pesa kivile na hata akizipata, hana makuzi. Katika mazingira hayo mwanamke anatakiwa kuwa makini sana, akijifanya anapenda makuu anaweza kujikuta anamkwaza mwenza wake.

10. Kumganda wakati wote
Mwanaume anapenda kuwa na mwanamke ambaye atajali pia ‘interest’ zake kwa maana ya kumpa muda wa kufanya mambo yake.

Kuna wanawake wengine wanapenda kuwaganda wanaume wao wakati wote, yaani kwa sababu anampenda basi anataka awe naye wakati wote, hata akitaka kutoka kwenda kwa marafiki zake kubadilishana mawazo na yeye anataka kuwa naye. Huyu atakuwa hajitaki!

Soma: Maneno 6 ya kumfurahisha mpenzi wako

11. Visingizio kila mara
Wanaume huwa hawapendi mwanamke mwenye visingizio vya mara kwa mara. Hapa naongelea suala la faragha, utakuta mume ana hamu na mke lakini kila akimtajia jambo hilo mara amechoka, mara anaumwa.

Ni kweli una haki ya kueleza unavyojisikia lakini sasa ikiwa ni kila siku visingizio, utasalitiwa kama siyo kuachwa kabisa.

Leave a Comment