SIMULIZI

Ep 02: Geza Anasakwa Auwawe

SIMULIZI Geza Anasakwa Auwawe – Ep 02
SIMULIZI Geza Anasakwa Auwawe – Ep 02

RIWAYA: GEZA ANASAKWA AUWAWE
NA: George Iron Mosenya


SEHEMU YA NNE
Jua lilikuwa linazama majira ya saa kumi na mbili jioni, mitaa ya Changanyikeni pembeni ya jiji hekaheka za hapa na pale zilikuwa zinaendelea kama ilivyokuwa kawaida kwa siku zote.
Wauza chipsi wengine hiyo ndo ilikuwa mida yao ya kufungua mabanda huku wauza nguo wakiyafunga maduka yao.
Bwana mmoja aliyejihifadhi katika suti iliyomkaa vyema kabisa katika mwili wake na miwani nyeusi iliyoyaweka nyuma macho yake, alikuwa anakunywa taratibu kabisa glasi yake ya bia. Alikuwa anatikisa kichwa kufuatisha midundo ya muziki kutoka katika redio iliyokuwa katika eneo lile, kuna nyakati alijaribu kufuatisha mashairi kidogo japokuwa yalimshinda akaishia njiani.
Majira ya saa mbili usiku bado alikuwa pale na akili yake ilikuwa sawa kabisa, hakuwa amelewa. Macho yake yalipatiliza hadi katika geti kubwa jeusi, alikuwa haachi kutazama kule. Kuna jambo alikuwa akilitarajia litokee humo.
Alisubiri kwa hadi wakati huo, na hapo akawaona viumbe wawili wakitoka katika geti lile dogo, mwanaume akiwa amemshika mkobno mwanamke.
Moyo ukapiga kwa nguvu sana!
“Mshenzi amemfanyia umafia au?” alijiuliza huku akiendelea kumalizia bia katika glasi yake, hadi walipompita.
Kituo cha daladala hakikuwa mbali sana kutoka pale alipokuwa ameketi na hata walipojadiliana kuhusu kutumia bajaji badala ya daladala aliwasikia vizuri.
Lakini kabla hawajapitisha maamuzi hayo, mara daladala ilifika, kondakta na mpiga debe wakahimizana kuwaeleza watu kuwa ile ni gari ya mwisho.
Mwanadada akaruka ndani kisha yule kidume akapunga mkono kumuaga, daladala ilipotaka kuondoka. Bwana mwenye suti akapiga mluzi kumuhimiza kondakta asimamishe gari.
Kondakta akagonga bodi gari ikawekwa kando,.
Bwana mwenye suti akatimua mbio hadi akaifikia gari akaingia na kwenda kuketi nyuma kabisa.
Kituo kimoja baadaye, mtu aliyekuwa ameketi na yule dada akashuka, bwana mwenye suti akahamia ile siti.
Akatulia tuli, hadi kondakta alipofika kuchukua pesa ya nauli.
Akatoa noti moja kisha akafanya alama ya vidole viwili akimaanisha analipia watu wawili.
Kondakta akamrudishia baki yake.
Yule dada akatoa noti nyingine na kutaka kumpatia kondakta.
“Nimekulipia tayari!” alizungumza kwa mara ya kwanza.
Mungu wangu!
Vinyweleo vikamsimama yule binti, hakuamini sauti aliyoisikia.
Hofu ikatanda!!


MAPENZI ni kitu kimoja cha ajabu sana, huonekana cha kawaida yakiwa katika mapenzi ya ulaghai lakini yakiwa katika ule usemi wa mapenzi ya dhati basi hapo ndipo uajabu wake huonekana.
Yalianza kama masihara pale ambapo mwanaume kutoka pasipojulikana alipoingilia ugomvi usiomuhusu na kuufanya wake, alipambana dhidi ya watu kadhaa waliounga mkono binti mmoja kudhalilishwa na konda kisa tu kudai haki yake.
Yeye akasimama upande wa binti na kuwabadilisha wote waliokuwa wakimuunga mkono kondakta.
Waliposhuka binti akiwa ametaharuki hakukumbuka hata kutoa shukrani. Lakini lipangwalo lipo mwanadamu kulizuia hawezi.
Ikatokea siku waliyokutana tena, ilikuwa ni ufukweni, binti akiwa na familia yake wameenda kuogelea na kubalizi upepo wa bahari.
Mwanaume akiwa hana hili wala lile akashangaa kupungiwa mkono.
Hakujibu!
Mara akaona binti anakuja upande wake.
Hakujali!
Na hakuamini kama anakuja kwake.
Ikawa hivyo, alikuwa anakuja kwake.
“Kaka mambo?” alimsabahi huku akitabasamu.
“Safi” alijibu kwa kifupi sana.
“Naitwa Edina…. Sijui unanikumbuka?” alihoji.
“Siwezi kusahau kirahisi…” alijibu kama asiyejali kishaakamalizia.
“Kwenye daladala.”
“Unakumbukumbu nzuri sana, asante sana kwa kunitetea, asante kwa kuniamini…. Sijawahi kuibia mtu mimi… wale ni wezi na waliniibia simu yangu sikuwa naongopa.” Alianza kujieleza huku akionekana kuumizwa na simulizi ile.
“Yaliisha!” alijibu mwanaume.
“Mbona unanijibu kamahujapenda kuniona tena?” kwa karaha alihoji yule dada.
“Sikujua kama nitakuja kukuona tena.”
“Kwanini?”
“Kwa sababu nilikutetea ili uwe huru na sio kwa misingi ya kukuona tena.” Alijibu huku akisimama. Kisha akampa mkono yule binti.
“Naitwa Geza….. ulimi wako ukiwa imara zaidi unaweza kuniita Geza Ulole… umesema unaitwa Edina, na nikikuita Dina sidhani kama nitaharibu maana.”
Wakashikana mikono yao, mioyo ikazungumza na huo ukawa mwanzo wao wa kufahamiana.
Dina akapafahamu nyumbani kwa Geza maeneo ya Msongola na Geza akamfahamu mzee Michael baba yake Dina. Baba ambaye tayari anafahamu kuwa binti yake ana mchumba aitwaye Lameck.
Wakaivana na kuwa marafiki, Geza akamnyoosha Dina na kumfunza jinsi ya kuishi katika jamii, na kubwa zaidi akambadilisha na kuwa na moyo mgumu.
Moyo unaoweza kutunza siri na kuvumilia magumu.
Baada ya kuhakikisha kuwa Dina amenyooka, Geza akamtangazia rasmi kuwa anataka kumpiku bwana Lameck katika mbio za kuwania kumtolea mahari na kumuoa.
Dina alidhani masihara lakini Geza alikuwa anamaanisha.
Alitarajia kuwa uchomaji wa mkaa aliokuwa anaufanya katika pori la Kidole kwa Jongo utalipa na hapo atapata mahari ya kumshawishi mzee Michael kumwachia Dina awe mkewe wa ndoa.
Wakati akiwaza haya dudumizi linaingia katikati Geza hayupo huru na zimesalia siku kadhaa kabla Lameck hajamtolea mahari Dina.
Geza akampigia simu Dina na kumweleza juu ya uhitaji wake kipesa.
Dina akaumiza kichwa na hatimaye akamuingia Lameck.
Lameck akamweleza kuwa aende nyumbani kwake kisirisiri kuzichukua, makubaliano yalikuwa anafika na kuondoka lakini ajabu amekaa huko masaa mengi.
Yupo garini hasira zikiwa zinamfukuta anatokea mwanaume na kumlipia nauli katika daladala.
Kabla hajahoji mwanaume anazungumza.
“Geza!” akashangaa Dina.
“Tazama mbele usinitazame…. Halafu hilo jina limeze katika kifua chako.” Alinong’ona Geza akiwa katika vazi lile la suti.
Ikiwa mara yake ya kwanza kabisa mbele ya Dina kuonekana akiwa amevalia suti pamoja na kofia nzuri katika mtindo wa pama.
“Umependeza.” Alisema Dina.
“Kioo hakikuniongopea.” Alimalizia Geza.
“Umekaa sana alikuwa anafanya nini?” alimuhoji kwa sauti tulivu. Lakini bado wivu ulidandia na kuchomoza.
“Alinilazimisha nimekataa kabisa.”
“Amekupa ngapi?”
“Zote”
“Ziko wapi?”
Dina akamsogezea bahasha Geza.
“Unaondoka nazo zote?” Dina akahoji.
“Niliomba kiasi hiki, lakini kama umepiga chako cha juu nitakutumia kwenye simu yako. Na ikiwa inapungua hata kidogo itabidio tu uangalie namna ya kujazilizia.” Geza alijibu huku akitabasamu na na bahasha akiiweka katika mfuko wa ndani ya koti la suti. Ni kama aliyekuja kuichota pesa yake aliyokuwa anaidai kwa siku nyingi.
“Amesema kesho atakuja nyumbani.” Dina alinong’ona.
“Hatakuja!” alisema Geza kisha akafyatuka ghafla na kushuka gari liliposimama.
Dina akabaki mdomo wazi. Geza alimfuatilia vipi hadi kumpata namna ile.
Hakupata majibu yenye kumpa mwanga lakini alichojua katika nafsi yake ni kwamba Geza alikuwa makini sana.
Nafsi yake ilikuwa na amani tele, kumsikia Geza na kumwona pembeni yake ilikuwa ni faraja tosha.
Lakini alihisi kuwa Geza amezidiwa na tatizo hilo na anachanganyikiwa.
Ile kauli ya kusemakuwa Lameck hatokwenda nyumbani kwao siku ifuatayo ilikuwa na ukakasi wa hali ya juu.
Geza hajui analosema!!
Dina aliwaza. Hakujiruhusu kuendelea kuwaza hasi juu ya Geza.
Akajinusa katika bega lake, harufu ya Geza wake kwa mbali ikampa tumaini.
Harufu tu!


SAFARI ya kutoka Moshi hadi Mbezi mwisho jijini Dar es salaam aliifanya maksudi kwa kuchelewa ili aingie usiku jijini Dar Es salaam. Mpango wake ulienda sawa kabisa.
Alipofika hakuchukua chumba cha kulala popote pale, alijua jinsi gani jiji la Dar es salaam vijana wamekuwa watumwa wa mitandao na wanaopenda kujadili habari mlipuko kana kwamba zinawaletea kula katika maisha yao.
Geza alijua wazi kuwa anajadiliwa sana mitandaoni, hivyo sura yake itakuwa na umaarufu fulani.
Akiwa na kofia yake kichwani, Geza aliingia katika choo cha kulipia, akaoga na kubadilisha nguo.
Akajihifadhi katika suti aliyoinunua mjini Arusha.
Akajiona amekuwa mpya haswa, hapo ndipo alipoenda kuchukua chumba.
Aliamini kuwa hawezi kufahamika.
Karata yake ilikuwa sahihi.
Siku iliyofuata alitega nyumbani kwa akina Dina akifuatilia nyendo za hapa na pale hadi alipomuona Dina akiwa katika mavazi yanayoonyesha kuwa anaenda mbali kidogo.
Kwa sababu Geza alikuwa anapajua nyumbani kwa Lameck, alipomuona Dina anapanda daladala akafahamu nia yake.
Yeye akamtangulia kwa kutumia pikipiki.
Karata zikaendelea kujichanga vyema.
Dina akaingia, naye akamsubiri mpaka alivyotoka. Wakaipanda daladala moja na kuketi kiti kimoja.
Ndani ya dakika kadhaa anatoweka bila kuaga.
Shilingi milioni moja kibindoni.
Geza ni kama alikuwepo halafu ghafla akageuka kuwa ndoto.


Geza hakugeuka nyuma baada ya kushuka katika ile gari, akapanda pikipiki na kurejea hadi nyumbani kwa Lameck. Akabisha mlango na kufunguliwa geti.
Kwa jinsi alivyopendezea katika lile vazi la suti, mlinzi hakuona shida kumkaribisha ndani. Akamuuliza shida yake akasema ye ni ndugu yake Dina.
“Mwambie kaka yake Dina, ataelewa…” alimuelewesha mlinzi huku anaiweka sawa suti yake, akanyanyua simu na kumpigia bosi wake.
Alipotambulisha kama Geza alivyotaka aliliona tabasamu la mlinzi liking’ara, naye akajibu kwa tabasamu hafifu.
Punde alikuwa sebuleni kwa Lameck, akauona ufahari usivyojificha kwa kuitazama tu sebule yake.
Geza alikuwa bado na kofia kichwani, baada ya kujiridhisha kuwa pale nyumbani hapakuwa na mtu mwingine zaidi ya Lameck. Akaitoa kofia na miwani yake.
“Shemeji, Umewahi kuniona mahali labda..” alimuuliza huku akitabasamu.
Lameck akataka kupiga kelele kwa hofu, ni muda mchache tu uliopita alitoka kuiona sura ya Geza katika runinga ikitajwa kama muuaji anayesakwa.
Na sasa ilisemekana kuwa yupo kanda ya kaskazini. Hii ni kwa taarifa ya waliomuona katika ile nyumba ya kulala wageni aliyokuwa amepanga.
Kabla Lameck hajapiga kelele Geza alijirusha na kulikaba koo lake vyema.
Lameck alijaribu kufurukuta lakini hakuweza.
“Naitwa Geza… nipo hapa kwa ajili yako. Na tunaondoka wote kwa utulivu kabisa, nina kitu hapa kiunoni kwangu nina bunduki. Tangu nianze kuitumia sijawahi kumlenga mtu halafu asife, achana labda na upuuzi unaoitwa kukosa, mimi huwa sikosi mtu. Nakujua Lameck una dada una mdogo wako na una mtoto mdogo wa nje anakutegemea yeye na yule mama yake kisilani… siamini kama utafanya upuuzi ufe kishamba. Eti umeonywa halafu ukajifanya mjanja. Anyway nisiongee sana… kwa kifupi nitakuua ukileta ushamba.” Alimalizia Geza akijionya kutoongea sana angali tayari amezungumza sana.
Akamwacha Lameck asimame huru, alikuwa makini kabisa kumtazama asije kupepesa macho na kufanya maamuzi mengineyo.
Lameck alikuwa anatetemeka sana.
“Keti!” Geza akamweleza kisha akaendelea,
“Kuna mgeni yeyote unamtarajia labda….”
Lameck akatikisa kichwa kuashiria anakataa hana mgeni.
“Ona hili nalo, sasa ukiongea kwani unaona nitafaidi. Mpaka unijibu kwa kichwa” Geza akalalamika.
“Sitarajii mgeni yoyote mkuu!” Kwa nidhamu tele akabwata.
Geza akasimama na kuuendea mlango, akaufunga vyema na funguo.
Wakati anaufunga mlango alijikuta anatabasamu mwenyewe kwa sababu tayari alizisikia hatua za Lameck zikimnyemelea.
Upesi akageuka akatokwa na teke moja kali sana la haja. Mguu wa kuume ukatua juu kidogo ya tumbo la Lameck.
Kilio!
“Ona sasa suruali yangu imechanika?” alilalamika Geza wakati huo Lameck anagalagala chini kwa maumivu.
“Nimetokwa na shilingi elfu tisini, Moshi hiyo wale wachaga hawana huruma hawaangali huyu ni msukuma tumpunguzie bei. Wanapiga tu!….” Aliendelea kuzungumza Geza kama vile hakuna kilichotokea.
Lameck akawa anamshangaa tu. Yaani badala ya kumuhoji juu ya kwanini alijaribu kumkabili anaanza kumpa mkasa wa Moshi.
“Jah! Una sindano ya mkono humu ndani aisee!”
“Hapana kaka!” Lameck alijibu kwa uoga.
“Hamna dogo hapo nje tumtume fastafasta, maana jau kweli nikitembea hivi imechanika. Si unajua tena wachunguliaji wengi mno, kuna watu hapa tauni hawana mitikasi wao ni kuchungulia tu nani kava nini, nani nguo imechanika.”
Lameck alishindwa kutoa ushirikiano, akili yake na mwili vilikuwa havipo sambamba. Alikuwepo tu kama gogo.
Geza akamnyanyua pale chini wakaelekea hadi kilipo chumba cha Lameck.
Kila alichokuwa akikiona Geza alikuwa anaulizia bei yake, hadi nyembe za kunyolea aliuliza bei na Lameck alitakiwa kujibu kiufasaha kabisa. Kuna vingine alihitaji kuelekezwa wapi aliponunulia, na jina la aliyemuuzia.
Geza alidai kuwa atakwenda kununua siku za usoni.
Hadi inatimu saa nane usiku alikuwa amemtoa jasho haswa.
Hapo sasa alimwongoza wakatoka nje.
Lameck akiwa mateka wake rasmi. Walipofika nje akamrudisha tena ndani.
“Hivi wewe babu yako ni mchawi?” Geza alihoji, Lameck kiuoga akatikisa kichwa kukataa. Mara akakumbuka kuwa Geza hapendi kujibiwa kwa alama akajibu kwa kinywa.
“Sasa mbona nakuchelewesha hivi?” akamuhoji huku akimtazama, halafu akaendelea kuzungumza, “Nadhani sifa zangu umezisikia kwenye vyombo vya habari… naua tena naua kweli sina masihara. Umewahi kusikia malaika moja anaitwa Israeli?” akamtupia swali.
“Ndio kaka… nimewahi.”
“Shughuli zake unazijua? Yule ni malaika mtoa roho, sasa nakuibia siri.. Israeli na mimi ni baba mmoja mama mmoja. Israel kaniachia titi mimi. Yaani kama ulishawahi kusikia kitu kinaitwa ‘kwa mbinde’ basi nd’o bro Israel aliniachia titi kwa mbinde. Maza nd’o alinisimulia lakini.” alimalizia kuzungumza Geza kisha akacheka peke yake, akiifurahia simulizi aliyokuwa amemaliza kuitoa.
“Mbona hucheki?,” mara akamgeukia ghafla,
“Yaani inamaanisha sichekeshi au?” akampandishia swali jingine.
Lameck akajilazimisha kucheka, akawa kama analia.
Geza akacheka zaidi!
“Sikuui leo Lameck, ila ntakuua siku utakayonyanyua mguu wako na kwenda nyumbani kwa akina Dina, ama siku utakayonyanyua huo mdomo wako kwenda wapi sijui kushtaki.”
“Nitakuona kila hatua ambayo utakuwa unapitia, huruma yangu usiitumie vibaya Lameck. Na nimekuhifadhi kwa sababu nyumbani kwetu wa kwanza anaitwa Israel, wa pili mimi Geza wa tatu anaitwa Lameck… umechangia jina na mdogo wangu. Tii masharti bila shurti, uishi kwa amani.” Alimaliza Geza kisha akaondoka bila kuaga.
Kwa ule mkwara, Lameck alinyooka.


ITAENDELEA

Leave a Comment