Tufaa Jekundu Sehemu ya Nne
TUFAA JEKUNDU
SEHEMU YA 4
Siku hiyo ilimwishia Melina akiwa anapita kituo cha polisi hiki na kile ili kupata kama kuna taarifa yoyote ya mtu kupotea lakini hakufanikiwa kabisa. Alipotazama saa yake ilikuwa saa mbili usiku tumbo likimchachafya bila huruma, ndipo alipokumbuka kuwa hajala siku nzima zaidi kunywa sharubati tu.
Baa ya Millenium iliyojengwa kandokando mwa Ziwa Viktoria ilimkaribisha mwanadada huyu mwenye uchovu wa siku ndefu ya kazi, akazikwea ngazi kwa mwendo wa madaha huku akipita meza hii na ile na kujichagulia ile ya peke yake.
“Karibu dada, kuna mchemsho wa kuku, ng’ombe, mbuzi na supu kibao bila kukosa chips nzito,” maneno ya kijana anayefanya kazi jikoni yalimfanya Melina kualichia lile tabasamu lake hadimu kwa wanaume ambalo hulitafuta kwa kila hali na lisipatikane.
“Nipatie mchemsho wa kuku, weka na pilipili bila kusahau limao,” akaagiza. Wakati kijana yule akiondoka ndipo alipogundua kuwa hayuko peke yake, mtu mwingine aliongezeka mezani pale. Alikuwa ni kijana mmoja aliyeshiba kimwili, aliyevalia mavazi ya vijana, fulana iliyoandikwa kwa maandishi makubwa ya kubandika ‘Kiss me’ yaliyotulia juu ya kifua chake, kofia yenye nembo ya mwanamapinduzi Che Guevara ilikifunika kichwa chake, na suruali ya jinzi ya bei mbaya haikucheza mbali.
Akazitua simu zake kubwa kubwa na kuziweka mezani huku akimtazama Melina ambaye alikwishaondoa lile tabasamu na kuweka ‘uso wa mbuzi’.
“Nimeona si vibaya kama nitaungana nawe hapa,” yule kijana akasema huku mikono yake akiiegemeza juu ya meza.
“Aliyekwambia meza ya baa ina mwenyewe nani? karibu,” Melina akamjibu huku akiendelea kucheza na simu yake.
“Tuletee bia tafadhali” yule kijana aliagiza, “Mrembo sijui unatumia bia gani?” akamwuliza Melina.
“Asante, mimi sinywi bia, labda maji tu,” Melina akajibu.
Dakika tano baadaye wote walikuwa na kinywaji na mazungumzo yakaanza polepole.
“Naitwa Shedi, sijui mwenzangu ni nani kama hutojali”.
“Melina” akajibu.
“Wa wapi labda?” Yule kijana akauliza.
“Aa mi mgeni tu hapa, nimefika leo hii” Melina akajibu akiendelea na mchemsho wake uliokuja muda si mrefu.
“Mgeni, mbona kama nakuonaga sana maeneo ya Pasiansi?”
“Umenifananisha, sio mimi, mi nimekuja leo, nimekuja msibani,” Melina akajibu kwa ufasaha.
“Msiba! msiba wa nani?” Shedi hakuchoka maswali, huku akiagiza bia nyingine.
“Mdogo wangu,” Melina akajibu.
“Oh! pole sana mrembo, alikuwa anaumwa?”
“Hapana ameokotwa amekufa leo asubuhi huko ziwani,” Melina akaeleza huku macho yake yakiwa yamejaa machozi. Shedi akatulia kidogo, moyo wake ukapiga kite baada ya kusikia juu ya kifo hicho.
“Binadamu wabaya sana!” Mara hii akaongea kwa sauti yenye uzito tofauti na ya mwanzo.
“Bila shaka umekisikia kifo hicho!” Melina akaongeza. Shedi akatikisa kichwa huku akijilazimisha kunywa bia iliyomo kwenye bilauri iliyoonekana wazi kupita shingoni kwa tabu.
“Pole sana mrembo,” akarudia kauli yake huku akiiweka mezani ile bia, macho yake hayakubanduka kwa Melina. Melina alifikicha macho yake na kujifuta kwa kitambaa.
“Sasa msiba upo wapi?” Shedi akauliza.
“Hatuwezi kuweka msiba hapa, nimekuja kuhakikisha kama ni yeye kisha nitafanya mpango wa kuupeleka kwetu Tabora,” Melina akamwambia Shedi huku akiinuka taratibu.
“Unaelekea wapi, nitakupeleka popote utakapo, usiku huu na jiji hili la Mwanza limeshaingiwa hofu,” Shedi alimbembeleza.
“Usijali, niko vizuri. Nipe namba yako ya simu nitakutafuta kabla sijaondoka,” Melina akamwambia na Shedi bila hiana akatoa namba yake kwa mwanadada huyo, kisha akamsindikiza kwa macho wakati akitoka ndani ya baa hiyo.
Mtikisiko wa mwili WP huyo ulimfanya Shedi kupata shida moyoni. akasonya na kurudi kitini. Melina alipotoka tu katika baa hile hakwenda mbali, alivuka barabara na kuingia katika baa nyingine iliyokuwa ikitazamana na ile ya Millenium, akaketi katika kiti cha pembeni ambacho kilimruhusu kuona mazingira ya baa ile ya Millenium, aliketi akiitazama ile baa muda wote huku akiendelea kupata kinywaji chake.
DAR ES SALAAM – siku iliyofuata
KATIKA MOJA YA MAJENGO MAREFU YA KUPENDEZA, hili lilijulikana kwa jina la JM MALL. Ndani ya jengo hili kulikuwa na maduka, migahawa, maofisi na mengine mengi.
Katika ghorofa ya sita kati ya milango mingi iliyojipanga vyema kulikuwa na mlango uliowekwa kibao kilichoandikwa‘AGI Investment’ kwa mwandiko wa kuremba na kujipindapinda kama nyoka. Ndani ya ofisi hiyo inayofanya kazi za kupokea na kusafirisha mizigo kulikuwako na msichana mmoja mrembo, mweusi, si mrefu si mfupi. Kwa jinsi tu alivyokaa kitini akitazamana na kompyuta yake utajua wazi kuwa akinyanyuka basi lazima ana umbo namba nane.
Nywele zake alizozisokota kwa mtindo wa dread zilimpa picha tofauti na utakavyomfikiria. Alikuwa mrembo kama Cleopatra, tabasamu lake halikumtofautisha na ndege aina ya Tausi. Alikuwa amezama kwenye habari aliyokuwa akiisoma katika gazeti alilolinunua asubuhi hiyo, aliendelea kulisoma taratibu huku akionekana wazi kutekwa na habari hiyo. Alipomaliza akalitua na kushusha pumzi, kisha akainua simu yake na kubonyeza tarakimu kadhaa kisha akaiweka sikioni.
“…Hello,” sauti ikaita.
“…uko wapi dear?” akauliza.
“…nipo ofisi ndogo kwa bibi,” akajibiwa.
Kimya cha sekunde kikapita, mwanadada yule hakutabasamu, bali aliliweka vizuri lile gazeti.
“Umesoma gazeti la leo?”
“Gazeti gani?”
“Gazeti la Heko. Litafute usome haraka sana ukurasa wa pili,” kisha akakata simu.
Gina akatulia huku akijaribu kuyapishanisha mawazo yake yaliyokuwa yakifanya fujo ndani ya kichwa chake. Zanzibar, Mwanza, na Tanga, aliwaza juu ya habari hiyo aliyoisoma ambayo ilimsukuma kutafuta magazeti ya siku kama nne nyuma ili apate habari hiyo kwa kushiba.
Alifunga ofisi na kuteremka chini, moja kwa moja akakodi teksi na kuelekea Maktaba Kuu ya Taifa ambako huko aliweza kuyapata magazeti yale aliyoyahitaji na kunukuu vile alivyovitaka kisha kurudi tena ofisini lakini mara hii aliamua kutembea kwa miguu. Hatua zake zilikuwa za harakaharaka lakini kutokana na macho yake ya kikachero aliwaona watu wawili ambao walikuwa wakiifuata njia yake hiyo.
Alipita ofisi za Culpa Motors na kuifuata barabara ileile ya maktaba bila kukunja popote huku bado akiwatazama kwa chati vijana wale. Alipohisi kuwa walikuwa wakimfuata akasimama kwenye moja ya meza za wang’arisha viatu na kuketi kwenye fomu.
“Karibu dada!” Yule kijana alimkaribisha.
“Asante, napumzika kidogo,” Gina akajibu huku akiichomoa simu yake na kuiweka sikioni.
“…Nina wasindikizaji…” akaongea kwenye ile simu kwa lugha ambayo hata yule kijana wa kung’arisha viatu hakuielewa.
“Barabara ya Maktaba mkabala na Posta Mpya,” akatoa maelekezo.
Wale vijana walipoona Gina ameketi pale wakaachana mmoja akavuka ile barabara kubwa na kusimama katika kituo cha daladala ziendazo Kivukoni na zile zinazorudi Mwenge, Ubungo mpaka Kimara huku yule mwingine akisimama kwa madereva teksi jirani kabisa na alipoketi Gina.
Kwa jinsi walivyosimama hakuna mtu ambaye angegundua kama wana shughuli nyingine zaidi ya kusubiri usafiri au kitu fulani. Dakika kumi hazikupita, BMW nyeusi ilisimama jirani kabisa na alipokuwa Gina, akanyanyuka na kuingia kiti cha nyuma cha ile gari ikatoka eneo lile, ikakunja kulia na kuchukua barabara inayopita mbele ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kunyoosha mpaka Barabara ya Ohio, wakakunja kulia na kurudi mjini.
Wale jamaa walipokuja kushtuka waliiona ile gari ikiishia kwenye kona. Wakawasiliana kwa simu zao ndogo zilizounganishwa kwa saa za mkononi, wakachukua teksi pale kituoni na kuifuatilia ile gari. Walipofika barabara ya Ohio hawakuiona.
“Tushushe hapa!” wakamwambia dereva na kumlipa kisha wakaanza kutembea kwa miguu wakiangalia huku na kule kuona kama wataipata ile gari. Hatua mia moja mbele mmoja alimgusa bega mwenzake na kumwonyesha ile gari ikiwa imeegeshwa mbele ya jengo moja refu lililoonekana kama ofisi ya shirika fulani hivi.
“Una uhakika kama ndiyo hiyo?” mmoja akauliza.
“Ndiyo yenyewe, hawako mbali lazima wako mitaa hii,” akamjibu mwenzake.
“Sawa, uwe tayari maana lolote linaweza kutokea,”
“Kumbuka tunamtaka akiwa hai,” mwenzake akasisitiza kisha wote wawili wakatawanyika kila mmoja upande wake.
***
Daktari Jasmine alimvuta Gina nyuma yake na kusimama kando tu ya mlango wa ofisi mojawapo ndani ya jengo hilo.
“Akina nani wale?” Jasmine akauliza.
“Hata sijui shoga, lakini nahisi walikuwa wananifuata,” Gina alijibu huku akijitoa taratibu katika mgongo wa Jasmine na kuusogelea mlango ili kutazama nje.
“Shiit!” akang’aka.
“Vipi?”
“Wapo nje,”
Jasmine akajitokeza nje ya mlango huku mkono wake ukiwa ndani ya kijikoti chake kutazama ni akina nani watu hao. Walikuwa vijana wawili weusi tii, waliovalia suruali za gharama za dukani na makoti ya suti ambayo hayakuendana na rangi ya suruali zao. Jasmine akashuka ngazi na kuiweka miwani yake vizuri usoni akaiendea gari yake na kuingia kisha akaketi nyuma ya usukani. Akajipa subira ya sekunde kadhaa kabla hajawasha gari hiyo, hakuna kitu! wale jamaa hakuwaona katika eneo lile.
Akainua simu yake na kuongea na mtu mwingine kisha akatoa gari na kuondoka, hakwenda mbali bali alizunguka upande wa pili wa lile jengo na kuiegesha kwenye maegesho ya juu kisha kwa kupitia mlango wa nyuma akarudi ndani ya jengo lile mpaka pale alipomwacha Gina.
“Nifuate!” akamwambia, wakatoka na kuzunguka kule nyuma, wakaingia ndani ya gari na kuondoka taratibu.
“Tumeshawapoteza!” Jasmine alijisifu.
“Unajifanya na we Amata? Haya twende, nirudishe ofisini mimi,” Gina akasema huku wakiliacha lile jengo na kuondoka zao.
AGI INVESTMENT
KAMANDA AMATA aliufikia mlango wa ofisi yake na kushika kitasa ili kuufungua, umefungwa, akachukua funguo zake za akiba na kuufungua kisha akatulia kidogo kutazama ndani japo kwa mbali, alipoona pako sawa akaingia na kuipita meza ya Gina kisha akaiendea ile ya kwake akaketi juu ya kiti chake kikubwa. Haikupita dakika tano akasikia mlango ukifunguliwa kwa nguvu na haraka, akaichomoa bastola yake na kuiweka tayari, alipoona mguu wa Gina umetangulia akaishusha na kutabasamu.
“Karibu,”
“Asante”.
Gina, moja kwa moja akaenda kwenye meza yake na kuchukua gazeti pamoja na karatasi nyingine mbili ambazo alitoka nazo Maktaba Kuu ya Taifa, akavibwaga juu ya meza ya Amata.
“Umeona huu ugunduzi wa bunduki mpya?” akauliza huku akimsogezea. Amata akajibu kwa kichwa kuwa hajui hilo, akavuta zile karatasi na kusoma karatasi ya kwanza ambayo ilikuwa ni kivuli cha kipande cha gazeti.
‘Maiti yakutwa hotelini Zanzibar’ kilikuwa ni kichwa cha habari kilichobeba kipande hicho, akakidolea macho kukisoma.
‘…aidha katika uchunguzi huo imeonekana mwanamke huyo kauawa kwa bunduki aina ya TSA 1 ambayo hata polisi wamekiri kutoijua aina hiyo ya silaha’. Kipande fulani cha habari kikasema hivyo. Amata akamtazama Gina huku sura yake ikiwa imebadilika ghafla. Akaiweka pembeni ile karatasi na kuivuta nyingine.
ITAENDELEA…
Tufaa Jekundu Sehemu ya Tano
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;