Tufaa Jekundu Sehemu ya Tano
NEW AUDIO

Ep 05: Tufaa Jekundu

Tufaa Jekundu Sehemu ya Pili
Tufaa Jekundu Sehemu ya Tano

TUFAA JEKUNDU

SEHEMU YA 4

‘Aokotwa amekufa Mwanza, silaha ya kisasa yahusika’ habari hiyo ilibebwa na kichwa cha namna hiyo. Kamanda Amata akameza mate kwa shida na kukodoa macho akiisoma habari hiyo.

‘…Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza amethibitisha kuokotwa maiti hiyo jana alfajiri katika fukwe ya Ziwa Viktoria huku ikiaminiwa silaha ya kisasa aina ya TSA 1 kuhusika,’

“Gina! hivi hawa jamaa wako siriasi au leo ni tarehe moja ya mwezi wa nne?” akauliza huku akikitua kile kipande mezani na kulivuta gazeti la Mfanyakazi mbele ya uso wake.

“Mi siwezi kusema kitu, soma na hilo gazeti nalo uone,” Gina akamwambia. Kamanda Amata akapekua ukurasa wa pili na kukutana na habari nyingine.

‘Maiti ya mwanamke yaokotwa nje ya baa,’ maandishi yaliyopewa uzito wa kati yalisomeka namna hiyo. Gazeti lile liliendelea kutamba kuandika kuwa inaonekana muuaji anayetekeleza vifo hivyo bado ‘anakula bata’ mtaani huku polisi wakishindwa kumtia nguvuni.

‘…Jeshi la polisi limesema litahakikisha linamtia nguvuni muuaji huyo haraka iwezekanavyo ili kuondoa hofu kwa raia…’

Kipande hicho kiliimalizia ile habari. Kamanda Amata akaweka mezani lile gazeti na kuwasha kompyuta yake, akaperuzi mambo fulani fulani ya hapa na pale anayoyajua yeye alipojiridhisha na mitandao aliyokuwa akiipekua pekua akainua shingo na kumtazama Gina.

“Unaichukuliaje habari hiyo?” akamwuliza Gina.

“Naichukulia siriasi sana kuliko unavyofikiria. Hawa jamaa wanakutafuta kwa udi na uvumba,” Gina akaeleza.

“Sasa mi nataka kuijua hiyo silaha mpya …” akasema Amata huku akinyanyuka na kuliendea dirisha lake kubwa na kuangalia nje upande wa chini.

Hakukuwa na jipya, yaleyale tu ya siku zote yalikuwa yakiendelea upande huo, sekunde kadhaa zikampitia mahala hapo bila kujua hasa ni nini anachokiangalia, akarudi na kuketi tena juu ya kiti chake.

Gina alikuwa akimwangalia kwa muda wote bila kumsemesha lolote, akajua tu kwamba mtu huyo akitoka hapo atakuwa na uamuzi mmoja tu, mapambano.

“Wananiita,” akasema

“Watanipata kwani karibu nitaitika ikiwa tu mama yangu atataka nifanye hivyo,” akaongeza. Gina hakusema lolote akabaki kumtazama tu kijana huyo ambaye mara nyingi akishikwa na hali ya kufanya uamuzi basi liwazo lake ni karanga mbichi. Akainuka alikoketi na kuliendea kabati dogo lililokuwa na vitu mbalimbali ndani yake. Akatoa chupa moja ya plastiki na kuifungua pomo yake kisha akamimina karanga hizo katika kibakuli na kumwekea mezani. Amata akamtazama binti huyo kwa jicho upande kisha wote wawili wakaanza kucheka.

“Najua tu ndicho kinachofuata,” Gina akamwambia.

“Haya mpenzi umeshinda,” akamjibu. Gina akarudi kitini mwake na kuketi upya.

“Sikia kamanda, baada ya kusoma hiyo habari katika gazeti la leo, ilinipasa kuifuatilia katika magazeti yaliyopita, nilikwenda maktaba kuu na kuifanikisha kazi hiyo…”

“Ulifanya vizuri sana,” kamanda akamkatisha.

“Lakini wakati narudi nilikuwa nikifuatwa,” Gina akaongeza kusema huku akikaza macho kwa Amata.

“Kama ni hivyo, basi ulikuwa ukifuatwa tangu unaenda ila hukugundua, siku nyingine uwe makini tangu unapoondoka,” Amata akasisitiza.

“Sasa ulifanya nini baada ya hilo?”

Gina akamweleza Amata mchezo mzima ulivyokuwa pale mjini akiwa na Jasmine mpaka kufanikiwa kuwapoteza wale jamaa. Amata alibaki kutikisa kichwa huku akaiendelea kusoma sentensi zinzofuata kutoka katika kinywa cha Gina kabla ya yeye kuzitamka.

“Basi Gina, ina maana kuwa hawa watu wanafanya haya kwa kukusudia ili kuninasa, hakuna silaha inayoitwa TSA 1 inayomilikiwa na mtu mwingine zaidi ya serikali.

Wanataka nifanye kitu ndiyo maana wametega watu wao hapa jirani nasi ili ama kupata nyendo zangu au kunifanya niamshe hasira zangu wanipate kirahisi. Wanatumia mbinu za kizamanai sana, sasa wataona mlango ninaotokea”. Akasimama akavuta mtoto wa meza na kutoa bastola moja ndogo aina ya Beretta Pico na kuhakikisha ina risasi za kutosha, akachukua nyingine inayofanana na hiyo akaitazama, iko sawa akampa Gina.

“Tunatoka, tunakwenda ofisi ndogo,” akamwambia kisha yeye akatangulia na Gina akafuatia nyuma yake.

Chini ya jengo lile la ghorofa, JM MALL, shughuli za watu ziliendelea kama kawaida, hakuna mtu aliyekuwa na muda wa kuwatazama wawili hao waliokuwa wakitembea dimwe dimwe kana kwamba hawafahamiani. Moja kwa moja wakalifikia gari la Amata, akalegeza vitasa kwa kifaa maalumu mkononi mwake, kisha akaiinua saa yake na kuizungusha kwenye ile pete ya juu, ilipowaka mwanga wa kijani akamruhusu Gina kuingia upande wa pili. Na yeye akakaa nyuma ya usukani. Wakachukua Barabara ya Samora na kuelekea Picha ya Askari ambako walizunguka na kuendelea na barabara hiyo.

***

“We’ si tumeshaagana sasa inakuwaje unarudi tena hapa?” Madam S alimuuliza Amata huku akiketi tena juu ya kiti chake cha ofisini. Akawatazama kwa zamu Gina na Amata.

“Mshapeana ujauzito au?” kwa kauli hiyo wote watatu wakaangua kicheko. Kamanda Amata akachukua lile gazeti na vile vipande akampatia na kisha kumwacha bibi huyo asome kwa makini habari zilizopatikana katika vipande hivyo. Dakika tano baadaye, Madam S akainua uso wake na kumtazama Amata.

“Ndiyo kwanza naona, ina maana kuna mambo yanapita huko nje na idara haijui,” aliongea kwa sauti ya chini ambayo ni wao tu watatu walioweza kuisikia.

“Nilisikia juu ya haya mauaji lakini nikayaona ni kazi ya polisi tu, lakini sasa kuna kitu nataka kukijua hapa, nani anaendesha mtandao huu na kwa lengo gani?

Haya Kamanda Amata na Gina kazini sasa hivi, maelekezo mengine nitawapa waliobaki kadri ya matokeo utakayonipa,” Madam S aliongea huku akiwatazama wawili hao. Kamanda Amata akasimama na Gina akafuatia, wakatoa salute kwa Madam S.

“Nataka mkadodose tu na sio kupambana na mtu yeyote kisha tutaona cha kufanya kama kuingia kazini au la, ndiyo maana nawatuma ninyi peke yenu,” akamalizia.

Gina na Amata wakatoka ndani ya ofisi ile na kuingia garini kisha wakaondoka zao.

MWANZA

JUA LA MAGHARIBI lilianza kuchukua nafasi yake kuashiria kuwa saa nne zijazo utakuwa si mchana tena bali usiku. Vilio na nyimbo za maombolezo vilisikika kutoka katika eneo hilo la Mabatini. Ndani ya Jiji la Mwanza. Kila aliyekuwepo eneo hilo kama hakuwa katika sura ya huzuni basi alikuwa kazungukwa na maswali yasiyo na jibu.

Msafara wa magari ulikuwa ukiwasili katika makaburi ya Mabatini, watu waliokuwa katika shughuli hiyo walikuwa tayari kwa hilo, kuzika. Ulikuwa msiba wa mrembo, msichana ambaye kila mtu aliguswa kwa namna yake jinsi alivyokuwa mzuri, mcheshi na mkarimu katika uhai wake.

“Chema hakidumu!” alisikika kijana mmoja akisema kwa kauli ya kukata tamaa huku akivuta hatua kujipanga mstari tayari kupokea sanduku lenye mwili wa mrembo huyo. Shughuli ya mazishi iliendelea, ibada fupi ilichukua nafasi ikiongozwa na mchungaji kama ilivyo ada.

Wakiwa katikati ya ibada ndipo waliposhangazwa na jambo moja geni kidogo. Mwanamke mmoja aliyejaa mwili kwa nyama zake lakini alionekana kuwa ‘mtu wa kazi’ alipenya penya katikati ya watu ili kufika mbele kabisa ambako ibada ile ilikuwa ikiendelea. Watu hawakumwelewa lakini baadaye walimpisha wakijua labda ni mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye amechelewa kufika mazishini.

“Mpeni nafasi apite jamani,” alisikika mtu mwingine akiwaomba wenzake nao wakatekeleza hilo. Hakuwa mwingine, ni WP Melina, sajini wa jeshi la polisi ambaye mkuu wake wa kazi alimpa kushughulikia shauri hilo. Ni yeye aliyetoa kibali cha mwili ule kuzikwa baada ya kukamilisha uchunguzi na kujiridhisha. Akafika mbele kabisa mpaka kwa mchungaji aliyekuwa akiendelea na ile ibada. Akamnong’oneza jambo, kisha amchungaji akawaita wanandugu wa karibu akiwamo baba wa marehemu na kuongea jambo fulani.

“What’s going on?” (nini kinaendelea?) kijana mmoja akamuuliza mwenzake.

“Shiiit!” Yule mwenzake akang’aka, Melina, akajisemea moyoni mwake. Kisha akatoka mahali aliposimama na kuelekea kwenye ujia ambao Melina alikuwa akipita kurudi alikotoka.

“Melina! Melina!” akaita. Melina akasimama na kumtazama kijana huyo kama hamjui.

“Melina si nakuita wewe au?” Yule kijana akaendelea huku akimshika mkono kwa kumlazimisha.

“Shedi, niache, niko kazini,” Melina akajibu, huku akiutoa mkono wake kwenye himaya ya kijana huyo.

“Huu ni msiba wako? Mbona sikuelewi? …basi tuonane baadaye,” akamwambia huku akimwacha aende zake, “Nitakupigia…” akaongeza kisha akarudi kwa yule mwenzake.

“Ndugu, jamaa na marafiki, tunasikitika kuwaambia kuwa hatutaendelea na shughuli hii ya maazishi kwa sasa. Ni amri kutoka juu mwili huu urudishwe hospitalini kisha watatupatia tena. Basi tunawaomba tuwe wavumilivu na msiba utaendelea palepale nyumbani, asanteni,” tangazo la mwongoza shughuli lilisikika na minong’ono ikaanza kusikika kati ya waliopo hapo, maswali yasiyo na majibu nayo hayakucheza mbali.

***

“Mtusamehe sana kwa kuwakatisha shughuli yenu ya mazishi,” sauti ya Kamanda Amata ilipenya katika masikio ya ndugu wanne wa marehemu na askari polisi waliokuwa katika chumba hicho.

“Ni sababu za kiusalama zilizofanya tuamue hili, hapa tunapowaeleza tumetokea mbali kuja kufanya jambo hili, mtuvumilie ni saa moja tu kisha tutawapa mwili muendelee na shughuli hii nyeti,” aliongeza kusema huku akiinuka kitini baada ya kujitambulisha kwao kuwa yeye ni polisi kutoka makao makuu ya jeshi hilo huko Dar es Salaam.

Daktari Jasmine akiwa katika vazi lake maalum na vifaa vyake tayari kwa kazi alijifungia ndani ya chumba maalum katika hospitali hiyo ya Sekou Toure akiwa na watu wachache akiendelea kufanya uchunguzi upya kama alivyofanya akiwa Tanga. Ukimya ulikuwa umetawala, kazi iliendelea kwa takribani dakika arobaini na tano kisha akarudisha vifaa vyake na kufunga kila kitu akiacha wahudumu wakihifadhi upya ule mwili na kisha kuukabidhi rasmi kwa ndugu.

***

Katika chumba kidogo ndani ya jengo la kituo kikuu cha polisi jijini Mwanza walikuwa wameketi watu watano; Kamanda Amata, Gina, Daktari Jasmine, Melina na mkuu wa idara ya upelelezi wa wilaya SSP.

“Ipo hivi, marehemu hajafa kwa kupigwa risasi, kwani hana tundu la moja kwa moja kutoka kisogoni mpaka kinywani,” Jasmine alilieleza jopo. Mkuu wa upelelezi alionekana kushangaa wazi.

“Sasa hii ina maana gani?” akadakia kuuliza.

“Ina maana kwamba kuna watu wanaofanya mauaji haya na kuweka hiyo risasi ndani ya kinywa cha marehemu. Hii inasaidia kupoteza ushahidi wa kiini halisi cha kifo cha marehemu, lakini inaonekana wazi kuwa amepigwa na kitu kizito kilichopasua mfupa wa kichwa chake,” akamalizia.

“Na vipi kuhusu hiyo silaha inayosadikiwa kutumika, TSA 1?” Yule Mkuu wa upelelezi akauliza. Swali hili lilitaka kumfanya Amata kucheka lakini akajizuia.

ITAENDELEA…

Tufaa Jekundu Sehemu ya Sita

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment