Pasipoti Ya Gaidi Double Agent Sehemu ya Tano
NEW AUDIO

Ep 05: Pasipoti Ya Gaidi ‘Double Agent’

Pasipoti Ya Gaidi Double Agent Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE


Simulizi : Pasipoti Ya Gaidi ‘Double Agent’

Sehemu Ya Tano (5)

Alipouvuka tu akasimama na kutazama bafuni, ila hakuelekea kule, alisikiliza yale maji na kugundua kuwa yalikuwa yakimwagika tu sakafuni na si juu ya kitu, akilini akaelewa kwamba hapo kachezwa shere tu kwa kuwa alijua sauti ya maji kama yanamwagikia kitu fulani lakini hiyo ilimjuza kuwa maji hayo yalifika sakafuni moja kwa moja hivyo akiweka jibu kuwa bafuni hakuna mtu. Jicho lake likatua kitandani, shuka lilikuwa limevurugwavurugwa na kusongwa kando. Alikuwa amelala, akawaza, na sekunde hiyo akaondoa usalama wa bastola yake na kuiweka tayari, alijua kama nakuja au kuna mtu anayemtarajia? Akajiuliza. Jicho lake lilipotua tena juu ya meza ndogo liliona heleni moja ambayo nyingine yake alikuwa ameiokota kule Quity House, akmata akashusha bastola na kuipachika kiunoni kisha akiendea ile heleni pale mezani, alipoinama kuichukua. Teke kali likatua tumboni pake na kumrudisha wima.

Yule mwanamke alikuwa amejificha kwenye kona ya kabati jirani kabisa na ile meza, Amata alijishika tumbo kwa maumivu kwa kuwa hakutegemea kitendo hicho. Akajitokeza pale mafichoni na kuvurumisha mapigo mazito kwa kasi ya ajabu lakini Amata akaamua kumwonesha kuwa yeye ni nani, akayakinga mapigo yale kwa ustadi kisha alipopata nafasi, akampa pigo moja la karate lililotua kifuani. Yule mwanamama akayumba kidogo, Amata akaelewa kuwa lile pigo limefika mahali pake na alihisi kifua lazima kimbane kwa sekunde kadhaa. Pigo lingine likamweka sawa kisha akamshushia konde zito na yule mwanamke akatua kitandani kwa kishindo, Amata akamwahi palepale na kutua tumboni akamkalia na kumdaka mikono aliyokuwa akitaka kuitumia dhidi yake.

“Tulia mwanam….”

Kabla hajamalizia sentensi yake miguu ya yule mwanamke ikaikamata shingo ya Amata kutoka nyuma na kumvuta kwa nguvu, akaruka sarakasi na kutua sakafuni, yule mwanamke akajirusha kutoka pale alipo na kutua upande wa pili. Kamanda akaisoma ile mbinu, naye kwa wepesi akaruka na kutua eneo lilelile, na kuupiga mkono wa yule mwanamke na bastola aliyoiwahi ikamtoka mikononi na kuanguka chini. Akarusha ngumi lakini Amata akaidaka na kuunyonga mkono.

“Ooooohhh!” yule mwanamke akapiga kite kwa uchungu. Amata akaunyonga tena na kumpiga kichwa cha maana, yule mwanamke akajibwaga kitandani pasi na nguvu.

“Tulia,” akamwambia huku akiliendea dirisha na kuchungulia nje, kisha akamrudia.

“Unaitwa nani na unamfanyia kazi nani?” akamwuliza huku akimtazama kwa jicho kali. Yule mwanamke hakujibu kitu, akabaki akimtazama Amata.

“Niambie unaitwa nani, unamfanyia kazi nani, na kwa nini ulitekwa pale uwanja wa ndege?”

Maswali hayo yaliyokuja mfululizo yalimfanya yule mwanamke kujiinua na kuketi kitandani, akamtazama Amata.

“Unanifuata fuata sana, tangu Arusha mpaka huku, unanitakia nini?” akauliza.

“Tulia na wala usitake kujua,” akajipapasa kiunoni na kuchomoa pingu, akampachika mikononi na kumwacha kitandani, akaliendea kabati na kulifungua, hakukuwa na kitu.

“Unachotafuta nini hum…”

Amata aligeuka na kuchomoa bastola, akafyatua na risasi ikapita kati ya mapaja ya yule mwanamke na kutoboa godoro.

“Nitakuua ukileta kelele zako, paka we!” akamkaripia na yule mwanadada alikuwa hoi pale kitandani jasho la ghafla likawa likimwagika.

“Hauna nguo, hata mkoba, na pasipoti zako zote za uongo wamekunyang’anya,” akamwambia huku akiliacha lile kabati na kujishika kiuno akimwangalia. Akasonya na kuinua jaketi lililoonekana limevuliwa muda si mrefu, alimtupia jicho yule mwanamkle na kumwona jinsi alivyovimba kwa hasira, akalipekuwa hapa na pale ndani ya jaketi hilo aliigundua mifuko ya siri ambayo si rahisi kuigundua kama hauna taaluma hiyo. Katika moja ya mifuko hiyo alitoa kitambulisho, akalitupa lile jaketi pembeni. Akakigeuzageuza kile kitambulisho cha bluu nyeusi ambacho juu yake kilikuwa na nembo ya chuma ya dhahabu iliyoitambulisha idara ya usalama ya Namibia, NIS.

“NIS” akasema kwa sauti ndogo huku akimwangalia yule mwanamke pale kitandani. Akachomoa funguo ya ile pingu na kumrushia, yule mwanadada akaiokota na kujifungia ile pingu, akaitupia kando.

“Jebeleth Isaac, Namibia Inteligency Service,” akasoma yale maandishi yaliyomtambulisha mwanamke huyo, “Niambie misheni yako ni nini hapa Maputo, na ni ipi ilikuwa kule Arusha?” akaongeza swali mara hii aliketi kitandani akimtazama, akamrushia kitambulisho chake. Yule mwanamke hakujibu akabaki kimya akihema kwa nguvu kama mbwa aliyetoka kukimbizwa, kifua chake kipana kilichopendezeshwa na matiti ya duara kilikuwa kikipanda na kushuka mithili ya chura wa Kihansi.

“Usitake kujua!” akajibu kwa mkato.

“Sawa sipaswi kujua lakini kumbuka kwamba mara mbili nimekuokoa kwa mikono yangu ijapokuwa mara zote umenitoroka, nimetumwa kukukamata wewe…”

“What! Nani kakutuma?” akang’aka,

“Bwana ‘ako!” Amata akajibu. Amata akachomoa simu yake na kuibonya hapa na pale kisha akweka laudi spika na sauti kutoka ndani ya kifaa hicho ilimfikia Jebeleth vyema kabisa. Mazungumzo ya kuagizwa Amata amkamate mwanadada huyo yalisikika. Jebeleth akakosa la kujibu, akabaki macho kodo juu ya huyo kijana.

“Sikia, nina uwezo wa kukuua kwa kuwa nimelipwa tayari kwa kazi hiyo, na nina uwezo wa kukuchukua ukiwa hai nikupeleke kwa wateja wangu kwa kuwa nitalipwa zaidi ikiwa nitafanya hivyo, lakini sifanyi lolote kati ya hayo mawili kama utanambia upo hapa kwa ajili gani?” Amata akasisitiza huku akiweka sawa bastola yake na kukifunga vyema kiwambo cha sauti cha bastola hiyo.

Jebeleth akashusha pumzi, “Naitwa Jebeleth…”

“Endelea…”

“NIS, nipo kwenye misheni ya uchunguzi wa kifo cha Dr. Hamadou…”

“Enhe…!”

“Enhe nini? Si nimeshamaliza!”

“Usilete upumbavu mwanamke, nitakuumiza sicheki nukta hii hata kidogo,” Amata akawa mkali na kuigeuza sura yake. Jebeleth akajawa na hofu pamoja na ujasiri wote wa kipelelezi.

“Namtafuta muuaji…”

“Umempata?”

“Alikuwa Arusha lakini amekimbilia hapa,”

“Umejuaje? Na muuaji wako ni nani?”

“Anaitwa Ludovique, nilipata maelezo yote juu yake nilipokuwa Merarani pale Arusha kabla sijakamatwa na yule bwege, uliponikuta, name nikapata mwanya wa kutoroka,” akaeleza.

“Kwa hiyo ulipotoroka ndiyo ukapata kuja huku?”

“Hapana nilirudi kwanza Namibia kisha nikaja huku,” akajibu huki sura yake kaiinamishia chini. Jebeleth pamoja na ushujaa wake siku hiyo alijua wazi kuwa kapatikana, “Nimeshajieleza vya kutosha, nawe ni nani?” akauliza swali.

“Ha! Ha! Ha! Utanijua tu, kwanza natakiwa kuondoka na wewe kukupeleka kwa mteja wangu kwa maana almeniagiza kama ulivyosikia,” Amata akamwambia na Jebeleth akabaki kimya.

“Vaa Jaketi lako tuondoke,” akamwamuru, naye akafanya hivyo.

“Unanipeleka wapi?” akauliza.

“Hilo siyo swali la kuuliza, twende! Tangulia,” Amata akamwambia na kumtanguliza mbele kisha yeye kufuatia nyuma. Mkononi wake wa kulia aliufunika kwa jaketi lake jeusi lakini ndani yake kulikuwa na bastola ambayo ilikwishaondolewa usalama. Akamwongoza mpaka kwenye gari yake.

“Unataka niingie kwenye gari?” akuliza.

“Ndiyo, tena kaa kwenye usukani,” wakati mwanamke yule anainama kuingia garini, Amata alisikia mlio mwembaba wa bunduki ianayoandaliwa kupigwa, akamvuta yule mwanamke chini na sekunde iyo hiyo risasi ilitua kwenye kioo cha mlango wa gari, akamkumbatia na kuvingirika naye mpaka uvungu wa gari iliyofuata na kuinukia upande wa pili. Kutoka pale alipo alisikia mgurumo wa gari inayokuja kasi, lakini kabla hajafanya lolote, ile gari ilisimama kwa breki kali, akaruka na kutua juu ya boneti, bastola mkononi, alipoifytua shabaha yake ilikuwa sahihi. Mtyu mmoja aliyejitokeza mlangoni ili amnyakue yule mwanamke alipaishwa juu na risasi ile akajibwaga kwenye maua. Ile gari ikaburuza tairi na kupigwa norinda, ilipokuja kutulia tayari Jebeleth alivutiwa ndani nayo ikaondoka kwa kasi.

Amata alitoka haraka na kuingia kwenye gari yake, akawasha na kuizungusha kutoka maegeshoni kisha akaikamata barabara ile waliopita wale jamaa. Akakunja kona na kuikamata barabara kubwa inayopita kandokando ya bahari, umbali kama wa mita mia tano hivi aliiona ile gari ikipotelea kwenye mwinuko, akabadili gia na kuiweka O.D.

Injini ya Kilimanjaro ikaanza kufanya vitu vyake, huku mkono mmoja ukiwa nje na shotgun ambayo daima huwekwa ndani ya gari hiyo, aliweza kuiona vizuri ile gari, akainua bunduki yake na kumwaga njugu, kioo cha nyuma cha ile gari kikafumuka na kuacha wazi dirisha lile. Risasi kutoka kwenye gari ya adui, zilipiga tairi za gari ya Amata, ikapasuka na kuyumba barabarani, akaiweka sawa, risasi nyingine zikatua kwenye kioo cha mbele lakini hazikufanya lolote kwani kioo kile kilikuwa hakiruhusu risasi kupenya. Akaongeza mwendo na kuikaraibia kabisa, akajaribu kuipita lakini ile gari ikasogea kushoto na kuibana gari ya Amata, akakanyaga breki na ile gari ikapitiliza upande wa huo kisha akaachia breki na kukanyaga mafuta huku akijaa zaidi upande wa kulia. Alipokuwa sambamba za ile gari akashusha kioo cha upande wa kulia na kufyatua risasi kadhaa zilizokwenda na kuchakaza kabisa kioo cha ile gari, akaiyumbisha ya kwake na kuigonga kwa nguvu gari ya adui. Ikayumba na kuzunguka lakini dereva alikuwa stadi sana akairudisha barabarani.

Gari ya Amata ikiwa imesaga mpira wa tairi moja, bado aliiongoza kwa ufundi wa hali ya juu, hakutaka adui yake apotee huku rim ya gari yake ikiwa inasaga lami. Kitendo bila kutegemea, alihisi usukani ukimponyoka na gari yake ikavutwa kushoto, akaiongoza kuiweka barabarani sawasawa, akahiosi ikivutwa tena upande wa pili.

“Puuu!” akasikia mlio juu ya boneti, pande la mpira wa tairi limedondokea juu yake, mara sauti ya vyuma vinavyosugua lami vikasikika kwa nguvu.

“Shiiit!” akang’aka baada ya kupata taarifa kutoka kwenye dashboard ya gari kuwa tairi zake zimepasuka zote nne na kumtaka kusimama kwani ni hatari kwake. Hakuelewa nini kimetokea, gari ya adui yake tayari ilikuwa mbele, wakati akaihangaika kuweka mambo sawa ikampa taarifa kuwa imeshanusa kombora zito mbele yake, alipoinua uso alikuta jamaa akijiandaa kufyatua RPG alilolichomoza kwenye kioo cha nyuma.

Usiku huo barabar ilikuwa nyeupe kabisa, lakini kwa mbali nyuma yake kulikuwa na gari moja iliyokuwa ikija kasi sana nanyuma kabisa kulikuwa na gari za polisi nazo zikija kwa kasi ileile huku zikiwasha taa zake na kupiga kelele.

“ ’mamae! Dili ishaharibika!” akasema kwa sauti ndogo.

“…upende wa kushoto tafadhali!” sauti ya mwanadada ikamtahadharisha na kumpoa maelekezo ya kufanya, sekunde kumi zilikuwa nyingi, aliiyumbisha gari kushoto, ile gari ikanyanyuka tairi za upande huo na kutembelea tairi mbili, lile kombola likapita uvunguni. Kupitia kioo cha kuendeshe aliona ile gari ya nyuma ikayumba vibaya na kugonga taa za barabarani. Bado Amata alikuwa kolikoli na adui zake.

“…tafadhali waweza kutumia roof machine gun…” sauti hiyo ya kike ikampa maelekezo mengine. Katika dashboard ya gari kukatokea maadishi kuwa kama yuko tayari kutumia hiyo bunduki au la akaminya ‘YES’. Sehemu fulani ya juu ya ile gari ikafunguka na mitutu kama sita hivi ikajitokeza …

Kibonyezo kidogo kilichoandikwa ‘fire’ kilikuwa kikiwakawaka juu ya control box iliyopachikwa kulia mwa usukani wake, akaibofya na kuiruhusu mashine hiyo ifanye kazi. Risasi mfululizo zilimwagika na kuichjakaza ile gari ya mbele. Sekunde tano nyingi, ile gari iliacha njia na kujipiga kenye mti ulio kando ya barabara, kama haitoshi ikarudi barabarani na kubingirika vibaya kisha ikaanguka upande wa poili wa barabara. Amata akaegesha gari yake na kiuteremka haraka haraka, akaiwahi ile gari na kumtazama Jebeleth, akammwona akiwa katika hali mbaya, lakini wakati huo tayari ving’ora vya polisi vilikuwa vimefika kabisa eneo hilo, Amata akatoka kando na kupotelea kwenye msitu wa miti uliokuwa eneo hilo.

Wale polisi wakazunguka lile eneo, wakateremka na kutoa msaada katika ile gari iliyopata ajali, walimtoa Jebeleth na kumpakia kwenye kwenye gari ya wagonjwa kisha kumpeleka hospitali, wakawakusanya na wengine nao walikuwa katika hali mbaya wakawachukua na kuwawahisha hospitali.

SEHEMU YA 18


“Ahaaaaaaaaa! Huyo ndiyo kijana wangu Moya!” Bocca alijikuta akishangilia baada ya kuiona ile habari katika televisheni, lakini huyu mwanamke hajafa! Akawaza. Akavuta simu iliyokuwa mezani na kubofya tarakimu fulani fulani kisha akaiweka sikioni, ile simu ikaita na upande wa pili ukawa kimya mpaka ikakatika. Akarudia tena kuipiga ile namba na baadaye ikapokelewa.

“Hey Colonha!” akaita.

“Hell Bocca, vipi?” Colonha akaitika kutoka upande wa pili.

“Sasa kijana wangu keshawasogezea mzigo puani…”

“Sikuelewi!”

“Oh! Colonha, sikiliza, yule mwanamke aliyetoroka hapa, nilimtuma Moya amtafute kwa siri aniletee ili nimkabidhi kwa hao jamaa zetu, lakini bahati mbaya hakumpata naona, ila kuna ajali hapa nimeiona kwenye TV yule mwanamke anahusika na amejeruhiwa vibaya sana,” Bocca akaeleza.

“Waoh! Ok, ngoja tushughulike ikiwezekana tukammalizie ukohuko hospitali,” Colonha akaeleza.

“Fanya hivyo, lazima tufanye vizuri ili watu wetu wafurahi na biashara ziende,”

“Obrigado!”

Ile simu ikakatika, naye akaiweka juu ya kifarasi chake, na kujitupa kochini. Bocca alikuwa ni mtu asiyependa kulala usiku wala kuzurula mchana, muda wote alipenda kushinda katika nyumba yake hiyo iliyo hapo Quiety Corner, nyumba iliyozungukwa na Ulinzi wa kutosha. Alikuwa mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya na genge lake alikuwa pamoja na Colonha. Biashara yao ilisambaa katika mataifa mengi Afrika, wakihonga wanausalama na kuwalubuni wanasiasa wenye dhamanai nao kuingiza unga huo haramu bil akificho wala kubugudhiwa. Katika siku hizo walikuwa wamefungua soko kubwa huko Nduruta hivyo kuwa na ukaribu wa ajabu na Rais wa nchi hiyo Bwana Sebutunva, aliwasaidia wakamsaidia, walimsaidia akawasaidia na uswahiba ukakua.

8

Dar Es Salaam

Operesheni Kimbunga

Kikao cha Rais na waandishi wa habari kilichukua nafasi katika Ikulu ya Tanzania, siku hiyo iliyokuwa na hali ya mvua kiasi ilikuwa ni siku iliyosubiriwa kwa hamu sana. Hii ilitokana na vitendo vya ujambazi kwa kytumia silaha nzito za kiivita kutawala maeneo mbalimbali ya nchi, benki zilivamiwa, mabasi yakatekwa na mambo kadha wakadha ya udhalilishaji wa kibanaadamu yalitukia. Wananchi walilalamika, vyombo vya habari vikaandika na kilio kikafika mahali pake.

“Hata mimi nimechoka, na sisi kama taifa tunachukua maamuzi magumu,” kauli hii ya Rais ikapigiwa makofi, vimulimuli vya kamera vikammulika.

“Nasema hivi, idara ya Uhamiaji ishirikine na Jeshi la Wananchi pamoja na Jeshi la Polisi, kuwaondoa raia wote waishio nchini bila vibali hasa wale wa mipakani kwa kuwa hawa ndio huingiza silaha nzito kutoka nchi za ng’ambo na kupenyeza mamluki wanaotuletea shida kwenye vyombo vyetu vya dola. Waondolewe, narudia tena waondolewe. Operesheni hii haitawahusu wale wenye vibali halali, kwa maana tulishawaambia kuwa wanotaka kuwa raia wafuate utaratibu lakini wamekaidi, hivyo waondolewe…”

Hotuba hiyo ilishangiliwa kwa nguvu sana na kila aliyeisikia na operesheni ile ilianza mara moja. Katika ya raia wengi waliokuwa nchini, walikuwamo wale kutoka Nduruta na hili lilikuwa pigo kwa harakati za kijasusi. Vikosi ambavyo tayari zilikuwa huko mipakani vilitekeleza amri hiyo moja kwa moja.


NDURUTA

KAMA NI UGONJWA wa kichwa, basi Rais Sebutunva aliupata ghafla, mara tu baada ya kupata taarifa ya uamuzi wa serikali ya Tanzania alihisi ganzi katika ubongo wake. Huyu jamaa ataniua kwa presha, kwa nini kila upande anabana? Akajiuliza huku akitembeatembea katika korido ya jengo hilo ambako makazi yake ya kiofisi yalikuwapo.

Saa nane mchana wa siku hiyo, alikutana na watu wake wa usalama wa nchi, kikao kilikuwa cha siri sana, kila mmoja aliitwa kwa wakati na jinsi yake lakini ilipofika muda walikutana wote katika ofisi moja nyeti sana. Rais Sebutunva aliketia upande wa mbele na wengine waliketi katika meza ya mzunguko wakimsikiliza.

“Hawa jamaa bado wananipa wakati mgumu sana wa kutimiza azma ya kuimarisha ngome yangu…” akavua miwani na kuiweka mezani kisha akafikicha macho yake kwa kitambaa safi cheupe na kutuliza mikono yake mezani, “Kitendo cha kufukuza watu wanaoishi bila kibali ni taarifa mbaya kwa kuwa tulikuwa tunaingiza watu wetu kwa njia hiyo ndani ya nchi ile. Naomba make chini na mfikirie nini cha kufanya ili juhudi zetu zisife hivihivi kama kuku mwenye mdondo,” akawaambia.

“Mimi sina budi kuondoka usiku wa leo kuelekea Mozambique kwa kuwa kule kuna kazi kubwa, kama mnavyojua mtu wetu, kijana wetu, aliyetekeleza mauaji ya Hamadou yupo kule mafichoni. Lakini taarifa ninazozipata ni kuwa kuna mpelelezi hatari wa NIS ambaye alikuwa Arusha keishanusa harufu ya Benzilahagi na ametua huko Maputo, nilitoa maagizo auawe mara moja lakini amewatoroka…”

“Samahani Mheshimiwa, na yule wa Tanzania yule mkorofi sana vipi maana tusimwangalie mmoja tu,”

“Ni kweli, lakini mpaka sasa watu wetu waliopo kule ambao wananipa ripoti za moja kwa moja wanasema bado hawajaona wala kunusa dalili zake, lakini kinachoshangaza wale waliopo Tanzania wanasema mtu huyo haonekani kule wala wenzake yaani wote hawapo,” Sebutunva akaliambia jopo.

“Mkuu hiyo ni hatari, kama wote wamepotea na hawaonekani kwenye darubini zetu, hatujui wanaenda kuibukia wapi!” mjumbe mmoja alieleza.

“Nataka upelelezi wa nguvu ufanyike pale Dar na Tanzania nzima ili kujua hawa watu wapo wapi, kusema kweli yaani hii idara yao inaniumiza kichwa sana, sijui mafunzo wamepata wapi wale jamaa,” akaeleza shaka yake huku akitikisa kichwa.

“Sasa Mkuu unaenda Mozambique, na ziara yenyewe ni ya dharula, vipi kuhusu watu wetu kule watajipanga saa ngapi?”

“Usiwe na wasiwasi, nitaenda tu kupumzika, sitahitaji ulinzi mkubwa, ila lazima nirudi na vijana wangu, na lazima nihakikishe huyo NIS anauawa ili asiharibu kazi za wakubwa,”

“Sawa Mkuu wa Wakuu. Lakini vipi operesheni zetu za kule Mpumbutu? Maana nikiangalia sana naona kama kuchukuliwa lile eneo kumetuathiri hata kiuchumi!” mmoja wa wajumbe alizungumzia swala ambalo liliuchoma moyo wa Sebutunva moja kwa moja.

“Hilo niachie mwenyewe naju nini cha kufanya na Mpumbutu. Sasa naomba kila mtu akamilishe majukumu niliyompa mi kama nilivyowaambia naondoka na hii ni siri kwenue kama ilivyo siri nyingine, nawaaamini hivyo ikijulikana sipo basi mmoja wenu lazima auawe maana atakuwa kavujisha hilo, kwa herini!” akamaliza na kuwaaga watu hao walioonekana wapole lakini kumbe ni moto wa kuotea mbali.

“Saa nne baadae Rais huyo aliondoka nchini Nduruta kwa siri kuelekea Msumbiji kama alivyowaambia watu wake na majukumu yite kwa muda huo akayakasimu kwa Makamu wake.

HOSPITAL CENTRAL DE MAPUTO

MAJERUHI WA AJALI walifikishwa kwenye hoapitali hiyo kubwa na inayosifika kwa huduma bora katika jiji la Maputo. Jebeleth alihifadhiwa katika wodi maalum ya akinamama lakini chumba cha peke yake. Wale wengine walioumia walihifadhiwa wode tofauti kiloa mmoja alkadhalika miili ya marehemu ilipelekwa katika chumba chao maalu na kuhifadhiwa jokofuni.

“Sasa hawa tuwaeleweje? Majambazi au vipi?” polisi mmoja alimuuliza mwenzake mara baada ya kuhakikisha watu hao wamefika na wanaendelea kupatiwa matibabu.

“Unajua siku hizi mji wetu umechafuka sana na hasa hii biashara ya dawa za kulevya, we haiwezekani mtu kwenye gari ana silaha nzito namna hii, hii ni vita hii!” aling’aka mwingine huku akitoka nje ya jengo hilo.

“Kweli maana hata matukio yamefuatana sana, kule La Peruz imelipuliwa na leo hili, yaani Beira na Maputo ni shida kwa hii biashara. Hapa lazima wamedhulumiana tu,” akaongeza mwingine. Waandishi wa habari walikuwa wakihaha kupata hili na lile ili kupamba magazeti yao siku inayofuata, hivyo hospitali hiyo ilikuwa imetingwa na nyendo za huku na kule.

Kamanda Amata aliwasili dakika chache tu baada ya gari za wagonjwa kufika hospitalini hapo. Kwa nyendo za kinyonga aliweza kuona na kukariri wodi zote walizokuwa wamelazwa wale watu. Alipojiridhisha akaondoka lakini wakati huo hakuwa na gari yake maana alipoiacha pale eneo la ajali gari ile ilichukuliwa na polisi.


Katika kituo kikuu cha polisi jijini Maputo uchunguzi wa gari mbili ulikuwa ukiendelea.

“Asee mimi hii gari siielewi sasa mbona ipo hivi?” askari mmoja aliuliza.

“Ipoje?”

“Haifunguki milango, vioo vyake vigumu ka vya ndege du!” akalalama. Dakika chache baadae ile gari ikawa imezungukwa na wataalam mbalimbali wakiitazama jinsi ilivyoundwa.

“Aisee hii mpya! Ina maana hii gari imetembea kwa rim kilomita nne?” akauliza afisa mwingine.

“Itakuwa ya magaidi, hii gari si ya kawaida, na imekuwaje inatumika nchini hata serikali haijui,”

“Kwani gari yenyewe ya wapi? Japan, Korea, USA, Uingereza au?” mwingine aliuliza na hiyo ikawafanya kutafuta jina la gari ili kujua ni ya wapi haswa.

“Kilimanjaro!”

“Kilimanjaro?” akadakia kwa swali mmoja wa wakaguzi na kuzunguka nyuma kuitazama, “Lo! Ndio mara yangu ya kwanza kuona gari inaitwa jina hilo, msiniaminishe kabisa kuwa hiyo gari imetoka Tanzania, ni ndoto ya alinacha!” akalalama huku akifunga faili lake na kuwaacha vijana wake wakitazamana bila jibu.

***

“….Moja ya gari hizo iliyopatikana ajalini, imeshindikana kufanyiwa uchunguzi kutokana na milango yake kutokufunguka. Msemaji wa jeshi la polisi amenukuliwa akisema kuwa gari hiyo ni ya ajabu kwani iliweza kutembea bila mipira kwa kilomita nne kabla ya kukutwa katika eneo la ajali; jambo lingine lililowatatiza wakaguzi na wataalamu wa vyombo hivyo kutoka katika kampuni mbalimbali za magari ni aina ya gari na wapi imetengenezwa. Gari hiyo aina ya Kilimanjaro yenye shepu ya Sungura, bado inafanyiwa uchunguzi zaidi…”

Banginyana akazima TV kwa hasira baada ya kupata habari hiyo, akamtazama Benzilahagi kwa jicho jekundu.

“Vipi Comrade?” Benzilahagi akauliza.

“Huyu mwanamke lazima amaliziwe palepale!”

“Huu ni mwiba, lakini mpaka alipo kumpata ni rahisi, sasa hii gari mbona inaitia wasiwasi?” Benzilahagi akamwambia Banginyana huku akijiweka vyema kwenye lile kochi kubwa la vono.

“Kwa nini?”

“Hii gari si ya kawaida, gari kama ya James Bond! Haijawahi tokea Afrika na mbaya zaidi inaitwa Kilimanjaro, huoni kuwa Tanzania inaweza kuwa imetia miguu hapa?” akauliza kwa shaka.

“Hapo umenena, Benzi…! Kwanza huyu aliyekuwa na mwanamke yule ni nani hata kusababisha vifo vya watu wetu!” Banginyana akanyanyuka na kuiendea simu ya mezani akazungusha namba fulani na kuiweka sikioni. Upande wa pili ilipokelewa na Colonha.

“Hey Comrade! Niambie,”

“Sijaielewa hiyo ajali, nani alikuwa akimpigania mwanamke yule?” akauliza.

“Aaaa, eeee ipo hiv….”

“Ngrrrrrrrrrrrrrrrrrrrr! Ngrrrrrrrrrrrrr!” Simu nyingine ikaita.

“Subiri kidogo Colonha nitakupigia,” Banginyana akakata simu na kuipokea ile nyingine.

“Fika la Pertela Villa mara moja, uwe na Ludovique tafadhali, MM1” ile simu ikakatika. Bangnyana akamtazama Benzilahagi.

“Vipi?”

“Tunatakiwa Pertela Villa sasa hivi…!”

“Mh! Usiwe mtego tu!”

“Hapana, MM1,” Banginyana akamweleza swahiba wake.

“Nina wasiwasi sana, MM1 inapiga kutoka Maputo?”

Benzilahagi bado alikuwa na shaka.

“Ok, tufanye hivi, kila mtu aende kwa gari yake, ili kama kuna la kutokea basi tuwe tumewacheza shere.

“Mia!”

Punde si punde gari mbili ziliondoka kwa njia tofauti, moja ilitokea mlango mkubwa wa mbele na nyingine mlango mkubwa wa nyuma na kuelekea mjini.


Johnson Juvenali akashusha darubini yake na kumgonga bega swahiba wake.

“Vipi?”

“Ametoka!” akamwambia.

“Ok! Waambie vijana wamfuate kimya kimya, na sisi tusicheze mbali,” akamwambia na yule jamaa akainua koti lake upande mmoja akawapa taarifa watu wake waliokuwa wameizunguka ile nyumba kwa saa sabini na mbili bila Benzilahagi wala Banginyana kujua. Ufuatiliaji ulikuwa wa siri na kitaalamu zaidi kisi kwamba ilikuwa ni vigumu sana kama huna taaluma hiyo kujua kuwa kuna mtu anafuatiliwa.

Zile gari zikaonekana zikiingia ndani ya kasri moja kubwa sana lililozungukwa na miti mingi iliyofanya kitu kama msitu, na katika lango la kasri hilo kulikuwa na kibao kilichoandikwa ‘Villa De Pertela’. Lile lango likajifungua na zile gari zikaingia kisha likajifunga tena. Wale jamaa wakapita bila kusimama eneo hilo na kuuacha ule utulivu wa ukimya ukiwa kama ulivyokuwa.

“Tunafanyaje?” Johnson akauliza.

“Kuhusu…?”

“Tumdungue au tufanyeje?” Jonson akamuuliza swahiba wake ambaye hapo alionekana kama mkubwa wake.

“Hapana, tusimdungue, tufanye juu chini tumtie nguvuni, ili atueleze kinagaubaga.

“Hawa jamaa washafanya hili chaka la kujificha, lazima tuwasafishe, huyu tumtyie nguvuni kisha atatueleza sawasawa,” Johnson alisistiza. Wakatulia kwenye gari wakisubiri kujua nini hasa kinaendelea. Vijana waliojipanga vyema walikuwa kwenye kona mbalimbali kila mtu kwa jinsi yake bila kujulikana na mwingine.


VILLA DE PERTELA

RAIS SEBUTUNVA alijitokeza na kukutana na vijana wake, makamanda wale walisimama wima kiukakamavu kabisa. Sebutunva akaketi kwenye kiti na kuwapa ishara wale vijana kufanya kama hivyo.

“Mko salama?” akawauliza.

“Tupo sawa ijapokuwa kazi imekuwa ngumu sana,” Banginyana akajieleza.

“Kwa nini kazi imekuwa ngumu?” akauliza Mkuu wa wakuu.

“Unajua tumezungukwa, na hatujui adui yetu, huyu mwanamke wa NIS tunamwandama na karibu tutakamilisha kazi yetu, lakini inaonekana kuna mashirika mengine hapa, pia sina uhakika sana na Tanzania ila ile gari kwenye ajali ya jana yanitia shaka!” akaeleza kwa kirefu.

“Sikiliza Bensoir! Swala la Tanzania kuwa hapa au la, lisikusumbue kulifikiria, we jua kuwa mnayepambana naye hapa ni Mtanzania, na mbinu zote hizi mnazoona zinawapa shida kuzitegua ni wao. Nakuhakikishia majasusi wa Tanzania wapo hapa na wanafanya kazi kwa akili ya hali ya juu ambayo itawapa tabu sana kutimiza azma yenu,” Sebutunva akaeleza.

“Mh!” Benzilahagi akaguna, “Nipe ruhusa nijitokeze nifanye hii kazi vyema, na nafikiri tunaweza kuimaliza kama mimi na kanali hapa tutaingia moja kwa moja kwenye uwanja wa mapambano, wawili ni wawili, hii ya kupigana kwa rimoti hatutafanikiwa,” akaongeza kusema.

“Wazo zuri,” Banginyana akaunga mkono.

“Ok, kuanzia sasa hivi, nataka muingie wenyewe kazini ili tumalize haraka, utaratibu ni uleule shoot on the spot,” Sebutunva akawaeleza, “Nimepata habari kuwa huyo mwanamke yupo hospitalini baada ya ajali…”

“Ndiyo,” Banginyana akadakia.

“Nataka auawe palepale, na hiyo kazi nataka iwe leo,” akatoa maagizo, “Kisha mfanye juu chini mjue pango mzima dhidi yenu,” akaeleza zaidi.

Baada ya mazungumzo marefu kati yao waliagana na Sebutunva aliwaambia kuwa hatoondoka hapo mpaka kazi hiyo iwe imekamilika. Alikuwa banginyana wa kwanza kuondoka katika jumba hilo na kisha akafuatia Benzilahagi, kila mmoja akiwa katika gari yake. Wote wawili hawakuwa wakijua kuwa wanafuatiliwa na wafuatiliaji hawakuwa wakimjua Banginyana ila Benzilahagi peke yake au Ludovique wa bandia. Gari zole zilipotoka, wakajikuta wana wakati mgumu sana wa gari ipi hasa waipige tageti.


“Tunafanyaje sasa, tuingia kazini?” Johnson akamwuliza bosi wake.

“Subiri, endelea kumfuatili mpaka atakapoishia,”

“Lakini hapa hatujui tunayemtaka ni yupi,” Johnson aliendelea kulalamika.

“Fanya hivi, ifuatilie hii ya nyuma, mpaka itakapoishia kisha tuweke vijana wachunge nyendo, mimi nishushe hapa,”

akamwambia na ile gari ikawaka indiketa na kusimama kando. Johnson akashuka na kuiacha ikiondoka.

“Tax!!” akaita na gari moja ndogo ikakaribia, akafungua mlango na kuingia.

“Wapi boss?” dereva akauliza.

“We fuata hiyo nji ya kwenda mjini, kisha nitakuwa nakwambia wapi pa kukata,”

“Ok!” akajibu na kuingiza gari barabarani huku akifuata maelekezo yote ya bosi wake. Baada ya kona kadhaa waliwasili katika jengo moja kandokando ya bahari, Johnson akamwamuru dereva kusimama, akamlipa na kushuka, ile taksi ikaondoka. Kwa hatua ndogondogo akasogea karibu na lile jengo na kukiende kibanda cha mtu aliyekuwa akiuza biodhaa ndogondogo, akanunua sigara na kuiwasha kisha akaipachika kinywani mwake na kupiga pafu mbili.

Kupitia matundu madogo ya vidirisha vilivyokuwa katika wigo wa jumba hilo aliweza kumwona Banginyana akiteremka kwenye ile gari na kuingia ndani ya lile jumba.

“Aaaaaah! Sio huyu!” akajisemea kwa sauti ndogo, na kuamua kusimamaisha tksi nyingine ili aondoke, lakini ghafla aliiona ile gari ambayo alimwamuru Johnson aifuate aikifika eneo lile na kuingia ndani ya lango lilelile. Kupitia zile luva alimwona Benzilahagi (Ludovique) akiteremka na mara moja akaingia ndani ya lile jumba.

“Ok!” akasema na kutikisa kichwa juu chini, akavuka barabara mpaka upande wa pili, akainua upande mmoja wa koti lake na kusogeza karibu na kinywa chake.

“Johnson, ova!” akaita.

“Umesomeka, ova!” akajibu.

“Jamaa yupo huku, ova!”

“Nimeliona shimo la panya, ova!”

“Vizuri, usiku wa leo inabidi kutuma paka, ova!”

“Read and Clear, ova!” akamaliza na kukata ile simu ya upepo ambayo iliweza kuunganisha watu walio ndani ya mita mia moja hamsini za mraba.


HOSPITAL CENTRAL DE MAPUTO

UKIMYA ULITAWALA KATIKA katika chumba alicholazwa Jebeleth, muuguzi aliyekuwa akimtazama mwanamke huyo alipohakikisha amelala alitoka na kwenda kwenye chumba kingine cha wauguzi. Nje ya chumba hicho kulikuwa na askari wawili wakiweka Ulinzi maana waliambiwa wasiruhusu wagonjwa hao waonwe na mtu yeyote.

Jeep Cherokee moja ikaingia katika maegesho ya gari hiyo, kijana wa makamo, mwenye nguo za kawaida kabisa aliteremka, akaipachika miwani yake usoni na kuvuta hatua kuliendea jengo hilo la hospitali akiwa na begi dogo jeusi mkono wake wa kulia na mashine ya BP mkono wake wa kushoto. Aliwapita watu kadhaa na kufika katika jengo la hospitali, akafungua mmoja wa milango na kupotelea ndani.

Jebeleth pale kitandani, alishtuka na kufumbua macho baada ya kuhisi mlango ukafunguliwa na mtu mmoja aliyevaa kitabibu aliingia ndani na kuurudisha mlango nyuma yake.

“Unajisikiaje anti?” akauliza huku akivuta faili lililokuwa limebanwa kwenye upande mmoja wa kitanda hicho. Akalisoma harakaharaka kana kwamba anaelewa kilichoandikwa, na kuandika andika mambo fulani, akatikisa kichwa na kuliweka chini kwenye miguu ya Jebeleth, kisha akatoka katika wodi ile na kupita kwenye korido za hospitali mpaka chumba kingine akaingia.


Chiba aliendelea kukata kinywaji katika moja ya vioski vililivyojengwa katika hospitali hiyo. Jicho lake lilikua halibanduki zaidi ya sekunde tano kwenye mlango mkubwa wa kuingia ndani ya wodi alikolazwa Jebeleth.

Dakika chache baadae alimwona mtu anayemjua akishuka kwenye taksi na kutembea kwa miguu kuelekea lile jengo. Chiba alitoa simu yake na kutazama kwenye boksi la picha na kumwona yule aliyeingia kwanza, Kepteni Benzilahagi, akawaza. Akamtazama yule mtu mpaka alipopotelea kwenye lile jengo. Haikupita hata dakika tano akaona kwenye ule mlango ikitolewa machela ya kusukuma na wauguzi wawili walikuwa wakiisukuma kuipeleka mahali fulani. Chiba akateremka kutoka katika kiti alichokuwa ameketi, akagugumia kinywaji chake kilichobaki na kuondoka eneo lile, akili yake ilikuwa ikifanya kazi mara tano zaidi ya kawaida, akaingia ndani ya lile jengo na kutembea hatua kadhaa nyuma ya wale wauguzi. Akawaona wakiingia ndani ya chumba kingine ambacho mlangoni kiliandikwa ‘X-Ray’, akasita kidogo.

“Mh!” akaguna na kisha akaendelea na safari yake ya uongo, mita kadhaa akatoka mlango wa kuendea nje upande wa pilia wa jengo hilo. Alipokuwa huko akashuhudia gari moja ya wagonjwa ikiegeshwa usawa kabisa wa kile chumba cha X-ray. Kengele zake za hatari zikafanya kazi, akajificha kwenye nguzo na kusubiri ile gari ikae sawa, ilipokuwa tayari, akavuta hatua mpaka kwenye mlango wa dereva na kuufungua, bastola mkononi.

“Sogea upande wa pili, haraka!” akamwamuru na yule dereva akasogea.

“Inama chini, chini!” akamwamuru na yule kijana akainama chini. Chiba akavuta kioo cha kidirisha kilichokuwa nyuma yake na kuangalia nini kinaendelea, ile machela ikapakiwa ndani ya gari harakaharaka.

“Ludovique?” mmoja akauliza.

“Yeye atakuja kwa njia nyingine, kwa sababu ameamua tuondoke naye mzima akajibu maswali yetu,” mwingine akamjibu.

“Kwa hiyo wapi, chimbo au?”

“Hapana, Pertela hiyo,” mara yule jamaa akagonga bodi ya gari na Chiba akaiondoa pale na kuitafuta barabara kubwa.


Kamanda Amata aliingia chumba cha Jebeleth, hakuna mtu.

“Sheet!” akang’aka, alipotaka kuondoka, akakumbuka faili la mgonjwa akalivuta na kulisoma, “Come on!” akajikuta akipiga kelele, akatoka nje na kuwakuta wale askari wawili, kwa kuwa alikuwa naye amevaa kidaktari hawakuhofu lolote.

“Mgonjwa wa humu yuko wapi?” akawauliza kwa Kireno safi.

“Ameondolewa…” wakati wakijibu na muuguzi wa zamu akafika, Amata akamtupia swali lile lile.

“Kwani hayupo?” akauliza na kukimbilia ndani ya kile chumba, hamna mtu, kitanda tupu. Yule muuguzi akachukua faili na kusoma, akakunja sura.

“Vipi?”

“Inaonekana kapelekwa X-Ray, imeandikwa hapa na daktari,” akaeleza na mara akatoka nje, na kuwauliza askari wakamjibu kuwa kuna daktari alikuja na baadae mgonjwa akaondolewa; hawana kosa!

“Nesi, tangu lini mgonjwa akaenda X-Ray bila faili? Na huyo anayemfanyia hiyo picha atajua apige kiungo gani bila hili faili?” Amata alijikuta akiuliza swali ambalo ilipaswa ajiulize mwenyewe ili hesabu zake zikae sawa, moja na moja kumi na moja.

“Twende haraka, kuna kitu hakipo sawa hapa,” akamwamuru yule muuguzi na wote wawili wakatimua mbio huku wale askari na silaha zao wakifuata nyuma. Kutokana na kuchanganyikiwa muuguzi hakukumbuka hata kutazama kuwa Amata hana kitambulisho cha kazi kifuani mwake. Walifika na yule muuguzi alibofya namba za kufungulia mlango, walipoingia ndani walikutana na maiti mbili za wale wauguzi zikiwa na matundu ya risasi katika mapaji ya nyuso zao.

“Uwiiiiiiiii mamaaaaa!” yule muuguzi alipiga kelele na kupoteza nguvu, akaanguka sakafuni amelegea, Amata akavua lile koti na kuliweka kando.

“Tafuteni huku na huko labda muuaji yupo hapa ndani!” Amata akawaambia wale aakari. Wakati wametingwa na msako, yeye akatokea mlango mwingine na kuondoka zake akiwahi gari huko nje.

Akasimamisha taksi na kuondoka nje ya hospitali hiyo akiacha huko nyuma mtafutano wa nani kaua, mgonjwa yuko wapi.

Mara simu yake ikafurukuta mfukoni mwake, akaichomoa na kuitazama, ilikuwa ‘private number’.

“…Barabara ya Durban…” iliandika hivyo basi.

“Nipeleke barabar ya Durban,” akamwambia dereva naye akaondoka zake na kuifuata barabara hiyo kubwa iliyokuwa ikipita kando ya bahari kuelekea Afrika ya Kusini.

“Sehemu gani?”

“We twende tu!” akamwambia na yule dereva akabadili gia na kuongeza mwendo. Dakika ishirini baadae walikuwa nje ya mji wa Maputo, hakukuwa na makazi ya watu. Kwa mbali aliona kama gari imeegeshwa kulia mwa barabara. Akachomoa miwani yake na kuivaa, akazungusha vioo vya miwani hiyo na kugundua kuwa ile gari pale ni gari ya wagonjwa. Wakaipita.

“Simama hapo mbele!” akamwambia na yule dereva akasimama huku akionekana kuwa na hofu nyingi sana.

“Nisubiri!”

“Wapi?”

“Hapa!”

“Hapa?” yule dereva akauliza huku akikaa vizuri kitini. Amata akashuka na kuchomoa bastola yake, akakimbia kuielekea ile gari ya wagonjwa, alipoifikia akasikia mlio wa ile taksi ikiondoka kwa kasi na haikumsubiri. Hakujali akaiendea ile gari na kutembea kwa minyato mpaka mlango wa dereva, akachungulia ndani kwa dereva, akaona maiti moja, akaigeuza na kuitazama, hakuijua lakini kwa saa yake akaipiga picha. Akaipekua mifukoni hakuna kitu, akatoka na kuzunguka nyuma, akafungua mlango na kutazamisha ile bastola ndani ya boksi hilo, hamna aliye hai, maiti mbili za vijana, alipoangalia vizuri hakuzijua. Akazipekua kila moja hakuna cha maana, akachukua simu ya mmoja wao akaigeuza na kuitaza vyema, Android, akawaza. Akaipachua nyuma na kufungua betri, akalitupa ndani ya gari hiyo akaondoka na mashine tupu, hatua tatu akasimama.

Nyuma yake akasikia redio ya gari hiyo ikiita kuuliza dereva yuko wapi, akaiendea na kuiweka kinywani, akafyatua batani ya kuongelea na kuwatajia uelekeo wa gari ile ilipo, kisha akakata na kuondoka zake. Kichwani mwake alikuwa na mawazo mengi sana kwanza Jebeleth yuko wapi, pili nani alimtumia ujumbe na tatu kwani aitwe halafu akute maiti tu? Utata!

IKULU – DAR ES SALAAM

MADAM S ALIKETI KATIKA ofisi nyeti ya Rais kwa kikao cha siri. Kwa kuwa yeye aliwajibika moja kwa moja kwa Mkuu wa nchi hivyo ripoti na kazi zake asilimia kubwa zilikuwa lazima zipewe Baraka ya Mkuu huyo.

“Sellina!”

“Ndiyo Mheshimiwa,” akaitika na kuketi vyema.

“Nipe ripoti ya kazi,”

“Kazi inaenda vyema, vijana wawili nimewatuma pale na kila mmoja anafanya vizuri, kwa taarifa ambazo ninazo ni inawezekana wakampata muuaji ndani ya saa chache zijazo,” akaeleza.

“Sawa! Lakini unajua hii kazi inazunguka sana, nimesoma lile faili lako uliloniletea nimeona kuwa bado tuna kazi ngumu kwa kuwa hawa jamaa walikuwa wamjipanga kufanya mapinduzi na kuimarisha ngome yao, je tutaweza kuwamaliza?” akauliza kwa wasiwasi.

“Mheshimiwa, nimetuma vijana wangu kila panapohusika, kazi zinaenda vyema kabisa ijapokuwa kazi ngumu ipo Msumbiji, Benzilahagi yupo kule na sasa wanatafuta jinsi ya kumkamata, ningependa tumpate hai na kijana wangu anajaribu hilo. Lakini taarifa niliyoipata muda si mrefu ni kuwa Kanali Bensoir Banginyana…”

“Kiongozi wa waasi?” akauliza kwa kudakia.

“Ndiyo, naye yuko huko tena yuko na kikosi cha watu kama kumi au kumi na tano, wamekwenda kule kuharibu mipango, kumwokoa kijana wao,” akaeleza.

“Subiri Sellina, sijaelewa hapo yaani unasemaje?”

“Taarifa nilizozipata kutoka Maputo ni kuwa kuna Jasusi wa kike kutoka Namibia, huyu Jasusi anawindwa vikali na hawa jamaa inasemekana hata Arusha alikuwepo, sasa bado haijajulikana misheni yake ijapokuwa tuna wasiwasi ni katika kufanya uchunguzi wa kifo cha Hamadou. Sasa Banginyana ameonekana Maputo katika kumwinda mtu huyo ila jambo la kufurahisha ni kuwa hawajajua kama tupo pale…”

“Oooh! Good!” akapiga makofi, “Yule nani yule Amata si yupo kule!?” akauliza.

“Yeah, yupo na anafanya kazi ngumu sana anayaweka maisha yake rehani,” Madam S akampigia upatu.

“Kwa kweli yule kijana namkubali sana, yaani jina lake nikilisikia tu naamini kuwa kifo hakiletwi na mwanadamu bali Mungu, ha! Ha! Ha! Ha!Haaaaaa!” akacheka sana na kugonga mikono yao. “Mwaka huu watauona moto…” akamalizia.

“Ok! Sasa lipi zaidi?”

“Hapa napo hatujapaacha hivihivi, nimewapanga vijana na kazi inaenda, nitakupa taarifa punde wakikamilisha,” Madam akajibu.

Akiwa katika mazungumzo hayo, saa yake ya mkononi ikamfinya ikiahiria ujumbe unaotaka kuingia. Moja kwa moja alijuwa kuwa ni moja ya vijana wake watakuwa wanaleta taarifa ya kazi.

“Samahani kidogo Mkuu kuna taarifa nyeti hapa inataka kuingia,” akapmba samahani, akakubaliwa. Madam S akabofya moja ya kitufe pembeni mwa saa hiyo na kuiruhusu ujumbe ule kuingia, kijimkanda chembamba kikachomoza taratibu na yeye akawa anakivuta huku anausoma ujumbe huo.

“… Nimefanikiwa kumwokoa Jebeleth Isaac NIS kutoka katika mikono ya Banginyana, nimemweka mafichoni…. Kazi inaendelea, Amata anafanya vyema na daima nautazama mkia wake, fine! TSA 2”

Akatikisa kichwa na kuukata ule mkanda.

“Vipi?” Rais Robert akauliza.

“Maputo, wanaendelea vizuri. Mheshimiwa Rais naomba niwasilishe taarifa fupi tena kwa maandishi kama ilivyo kawaida na nirudi kwenye majukumua mengine,” Madam S akasimama na kumkabizi kabrasha hilo. Wakaagana na Sellina akaondoka katika jengo lile tukufu.


MAPUTO

KAMANDA AMATA alifika hotelini kwake na kujibwaga kitandani akiwa amechoka sana, akachukua ile simu na kuipachua line kisha akaiweka kwenye simu yake ya akiba, akaiweka pembeni kusubiri, lakini hakuna ujumbe wala simu iliyopigwa, akapekua majina kadhaa na jicho lake likakwama kwenye jina moja tu ambalo halikuweza kujificha ‘Bensoir’. Bensoir? Akajiuliza. Akapekua baadhi ya jumbe zilizomo na hiyo moja ilimvutia, iliandikwa kwa lugha ya Kifaransa ikiwataka vijana hao kufanya kazi yao kwa Umakini, kuhakikisha wanamuua au wanamchukua hai na kumfikisha Villa De Pertela.

Amata akiwa pale juu ya kitanda alipata jambo jipya ‘Villa De Pertela’, akaapa kuitafuta. Akajibwaga kitandani na kupitiwa na usingizi mzito wenye ndoto za ajabu ajabu.

“…Nimekuja kukuua, mwanaharamu wewe unayejifanya unajua kuharibu kazi ya watu…” sauti ya mtu iiliyokuwa ikiongea kana kwamba mtu huyo yuko ndani ya maji ilisikika kichwani mwa Amata. Mara jitu la kutisha lenye macho mekundu likaibuka majini, kono lake kubwa lenye ganja pana likainua jisu kubwa tayari kushindilia katika kifua cha Amata. Mahangaiko yake pale kitandani hayakuwa na mafanikio, kwani kila alipojaribu kujigeuza hakufanikiwa, akapiga kelele lakini kono la pili la mtu yule likatua kinywani na kumziba pumzi, Amata akachomoa bastola na kuiweka sawa akafyatua kulilipua lile jitu.

Wakati huo akashtuka na kuketi kitandani akihema kwa nguvu na jasho likimmwagika huku mkononi mwake akiwa na bastola na kioo cha TV kikiwa vipande vipande sakafuni. Ilikuwa ndoto ya kutisha iliyompitia katika usingizi huo mzito.

Kiupepo mwanana kikapita kutoka dirishani, pazia likatikisika, akainuka na bastola yake na kuliendea dirisha, aliposimama na kutazama chini kuna gari ilikuwa ikiegeshwa na watu wawili wakateremka, nywele zikamsimama, akaigundua hatari inayomkabili. Daima Amata aliheshimu hisia zake, hili ni moja ya funzo la juu kabisa alilopewa katika medani hiyo ya Kiintelijensia, kuheshisimu hisia ya sita ‘sixth Sense’. Ni binadamu wachache wenye uwezo huo na hiyo imechukuliwa kuwa ni sifa mojawapo ya kuwa katika kitengo kama hicho.

Akatoka pale dirishani na kuvuruga mashuka ya kitanda, akatengeneza kama mtu aliyelala na kumfunika shuka, pembeni karibu na kichwa akiweka simu kisha yeye akajificha nyuma ya mlango kiasi kwamba kama kuna mtu anayekuja akifungua basi hatoweza kumwona kirahisi. Hakuwa mbali na hisia zake, alihisi kitasa cha mlango kikifunguliwa na mara taratibu mlango ule ukafunguka, alichokishuhudia hakikuwa kingine ni shotgun iliyotema risasi mfululizo juu ya kitandakile na kuharibu godoro lote pale juu, kisha mlango ukafungwa na kusikia nyayo za mtu anayetembea harakaharaka. Akacheka kimoyomoyo na kuliendea dirisha lile lile, dakika tatu au nne hivi akaona watu wawili wakipanda kwenye ile gari na kuondoka kwa kasi.

Hapa hakuna usalama tena! Akawaza huku akiliacha lile dirisha, akainua mkono kutazama saa yake, tayari pambazuko lilikaribia. Akaichukua simu yake na kupekua hapa na pale, na wakati uohuo ikaita, alipotazama jina hakuwa mwingine, Bocca!

“Hello!”

“Hakikisha asubuhi saa nne unakuwa hapa, wale jamaa zangu watakuja ukutane nao ikiwezekana uwasaidie katika yao,”

“Sawa nitakuwa hapo! Lakini yule mwanamke ametekwa na watu wasiojulikana,”

“Najua, sasa mkakati ni jinsi ya kumpata kwa kuwa kuna wasiwasi mpya uliotuingia ambao hata wewe usipokuwa makini wanaweza kukufanya mbaya,” Bocca alimwambia Amata naye akakubali wito huo. Alipokata ile simu mawazo lukuki yakaja kichwani mwake.

Nani kamteka Jebeleth kutoka kwenye gari ile? Akajiuliza, ina maana wamegeukana?

Akakosa jibu. Maswali hayo hayakumpa jibu alilolitaka sanasana yalikuwa yakiongeza

maumivu ya kichwa, akaingia bafuni kujimwagia maji ili apate akili mpya.


Gari moja ya polisi iliwasili jirani kabisa ya jumba kubwa alilokuwa akiishi Benzilahagi, kama walivyokuwa wameelekezwa na Johnson, mwanausalama aliyekuwa akifuatilia nyendo za mtu huyo. Kitendo cha muuaji huyo kukimbilia katika ardhi ya nchi hiyo hakikuifurahisha serikali ya Msumbiji, hivyo iliamua kuingia kazini kimya kimya kuhakikisha inamtia mbaroni kwa kuwa ingeijengea sifa mbaya kama ingeendelea kuukumbatia uovu huo. Nchi zote za SADC ziliapa kumsaka ama yeye kama yeye au na wenzake.

Alfajiri hiyo baada ya kumfuatilia muuaji huyo walimuona akitoka na baadae akarudi. Waliamua kumtia nguvuni bila kuchelewa kwani walishang’amua kuwa muda wowote akijua anafuatiliwa basi angeweza kutoroka. Msumbiji ilitamani iitaarifu Tanzania kuwa mtu huyo yupo nchini hapo kwa kuwa ilimtambua kama mwanajeshi aliyetoroka jeshi huko Tanzania kwa kuwa majeshi yote yalikuwa na taarifa hiyo na mpaka wakati huo MI kutoka JW walikuwa wakimsaka kwa udi na uvumba.

“…Hatumkamati kama mwanajeshi wa Tanzania, bali kama muhalifu mwingienwa Kimataifa,” Johson alikumbuka kauli hiyo kutoka kwa mkuu wake wa kitengo wakati anapewa kazi hiyo ya siri, na sasa alikuwa amefika wakati wa kushirikisha watu wengine wanaoweza kumkamata mtu huyo.

“…Lakini kumbuka yule jamaa licha ya kuwa mhalifu pia ni mwanajeshi aliyepitia medani za vita, hivyo kumkata lazima tujiandae,” yeye alimjibu hivyo.

“…Mtandao huu umelelewa sana hapa nchini… tumpate hai, tumbane atutajie na kundi au waliomhifadhi hapa nao watiwe nguvuni…” akakumbuka kauli hiyo.

Bila shaka Mkuu! Akajibu mawazoni.

“…Maana naona Watanzania wamerest tu, hawajui mtu huyu ni hatari kwao kwani ana information za kiusalama kwa taifa hilo na anaweza kuziuza popote na nchi kuwa hatarini…” sentensi hii alipoikumbuka ikamfanya kidogo kuona hofu juu ya hatima ya taifa hilo rafiki, alikumbuka mwaka alipofuatwa na watu wa idara ya Usalama wa Taifa akiwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Alijiunga katika idara hiyo na kufanya mafunzo kadhaa nchini Tanzania kisha akarudi kwao kuendelea na majukumu mengine.

Sure! Akajibu kimoyomoyo.

Askari waliofika katika nyumba hiyo waliizunguka wakiwa na silaha kali, ukiwa ni mgawanyo sahihi Kadiri ya operesheni yao, ndani waliingia vijana watatu wa jeshi la Msumbiji wakiwa katika sare za kijeshi, MP mabegani mwao. Kwa kuwa walishasikia jinsi mwanajeshi huyo alivyotoroka pale Dar es salaam, wao walijipanga vyema. Walichopanga kufanya ni uvamizi, kwani baada ya kujipanga katika kona za jumba hilo, walivunja mlango na kuingia ndani ya jumba hilo.

Benzilahagi (Ludovique), alishtuka aliposikia kishindo hicho, alitoka chumbani akiwa na Sub Machine Gun mkononi mwake, akiwa ndiyo kwanza anajiandaa kulala. Lakini aliponusa tu nje ya mlango, alikutana na teke zito, lililompepesua. Akakosa stamina na kuanguka kando.

“Upo chini ya Ulinzi!” sauti ya askari mmoja ilisikika, alipoinua kichwa na kugeuka akajikuta akitazamana na mitutu miwili ya bunduki nzito.

“Simama juu, acha silaha yako chini,” akaamuriwa, naye akasimama.

“Weka mikono kichwani! Tulia hvivyo hivyo, ukileta ujinga tu nitaruhusu risasi hizi zikuishie,” yule askari akaamuru.

“Petros! Mtie pingu mikono na myororo miguuni!” akatoa amri kwa mtu mwingine. Benzilahagi alijikuta hana ujanja kila alipoiangalia ile mitutu na watu walioikamata hakuwa na la kufanya, kichwani mwake mawazo mengi yalimzunguka. Naweza kuyatoka haya mabomba mawili kweli? Alijiuliza. Wakati yule kijana akisogea tayari kumtia pingu, Benzilahagi alishusha mikono kwa nguvu na pigo lile likatua katyikati ya paji la uso, bila pingamizi askari yule alikwenda chini huku akitoa yowe la uchungu. Ludovique wa bandia alijirusha juu ya kochi kubwa, na risasi zikapiga na kuchimba ukuta.

“Anatarorokaaaa!” akapiga kelele askari mmoja.

“Ua!” yule kiongozi akatoa amri na risasi za kutosha zikatawala ile nyumba. Benzilahagi alichumpa na kutoka na kioo cha dirisha lakini alipotu tu kwenye bustani hakufanya lolote kwani vijana walio nje walimwahi na kumkamata kwa taabu kwani alitembeza kichapo cha maana lakini mwishowe alizidiwa na kutiwa pingu.

“Umepatikana!” yule kiongozi akamwambia. Benzilahagi au Ludovique wa bandia akajikuta hana ujanja katikati ya askari hao wenye silaha za kila aina, wakamtutusa na kutupia garini, kisha wakaondoka naye.

Johnson akatikisa kichwa kuonesha amekubaliana na kazi hiyo yadakika nne iliyofanywa na vijana wa jeshi na polisi. Akaiua simu yake na kubofya namba fulani kisha akaiweka sikioni.

“Kazi imekwisha!” akaongeza katika simu hiyo.

“Weldone boy!” sauti ya upande wa pili ikajibu na simu ikakatika.


“Wewe ni nani?” Jebeleth akamuuliza mtu anayemuona mbele yake ijapokuwa sauti yake ilitoka kwa taabu lakini ilieleweka. Kati ya wawili hao ni hakukuna kitu kingine zaidi ya vijichupa kadhaa vya dawa.

“Usijali kunijua, lakini upo kwenye mikono salama!” Chiba akajibu, “Una nguvu sasa, inuka, haujaumia kabisa ila ulipata mshtuko tu,” akaongeza kumwambia.

“We ni daktari?” Jebeleth akauliza.

“Hapana, mi ni Malaika Mlinzi,” akajibu huku akivuta begi lake na kulipachika mgongoni, “Unakumbuka nini cha mwisho?” akamwuliza.

Jebeleth akakaa kimya kwa nukta kadhaa, “Nilimwona muuaji, kisha sikumuona tena,” akajibu.

“Muuaji gani?”

“Ludovique, nilimuona Ludovique, lazima apatikane mshenzi yule,” akang’aka Jebeleth huku akisimama kwa kusaidiwa na Chiba. Kisha akamgeukia Chiba na kumtazama, “We siyo mmoja wao?” akamuuliza.

“Ningekuwa mmoja wao ningekuacha hai?” akamjibu kwa swali kama ilivyo tabia ya Watanzania wengi, “Tuondoke hapa, turudi mjini,” akamwambia na kisha wote wakaanza kutembea kwa miguu ijapokuwa Jebeleth alikuwa akijivuta kutokana na maumivu machache aliyokuwa akiyahisi mwilini mwake.


Kanali Bensoir Banginyana, aliipiga teke luninga iliyokuwa ikitangaza kukamatwa kwa Ludovique. Ilikuwa alfajiri mbaya kwake, kwani siku hiyo ndiyo walipanga kufaya kazi kwa nguvu zote ili wahakikishe wanamaliza misheni hiyo kama walivyopewa maagizo na Mkuu wa wakuu ambaye naye alikuwa ndani ya jiji hilo la Maputo kwa siri.

“Shiit!!” akang’aka na kusimama moyo ukimwenda kasi.

Bila kusubiri, akatoka ndani ya jumba lile alilokuwa akiishi na vijana wake wa kazi, akaingia kwenye gari na kuondoka kwa kasi. Moja kwa moja alifika katika lile kasri la ‘Villa De Pertela’ na kuegesha gari mahali pake. Kwa mwendo wa haraka, alaikwea ngazi na kutokea sebuleni ambako tayari alimkuta Sebutunva akiwa na kikao na watu wengine ambao hakuwatambua.

“Excuse pour ingérence…” ‘samahni kwa usumbufu’, alisema huku taratibu akipita pale sebuleni na kuelekea chumba fulani.

ndani, wakajifungia wawili tu.

“Monsieur, Benzilahagi amekamatwa mapema asubuhi ya leo!” akampa taarifa ambayo almanusura imwangushe Mkuu wa wakuu. Macho yalimtumbuka, alimtazama Banginyana bila kuongea kitu.

“Amekamatwa vipi?” akauliza.

“Kwa kweli Mkuu sijaelewa nimeona tu kwenye vyombo vya habari,” akaeleza huku mikono yake ikiwa kichwani. Sebutunva alibaki kabutwaika, alikwenda kona hii na ile bila jibu.

“Sikia Bensoir! Sasa naelewa wazi kuwa Tanzania ipo hapa, kwa vyovyote watakuwa wamepanga mpango wa kumkamata kwani wanajua kuwa yule ni mwanajeshi wao…”

“Ndiyo!”

“…kosa kubwa sana tumefanya hatujamaliza kuchukua zile information kwa Benzilahagi,” akajishika kiuno na kutikisa kichwa.

“Tunafanyaje?”

“Hilo sio swali kumbuka Benzilahagi alikuwa Double Agent, ana information kutoka za kijeshi za Tanzania na ana information za kimtandao za kwetu. Watanzania wamemuwahi, watambana mpaka atatoa siri, na sisi tungejua tungemaliza kukusanya information zote kutoka kwake,” akanyamaza, akaiondoa miwani usoni pake.

“Hatuwezi kumtorosha, tufanyeje sasa,” akaongeza kwa sauti ndogo huku akitembeatembea. Banginyana alihisi akili yake ikifa ganzi, “Mzee! Kutokana na cheo chako huwezi kuomba mabadilishano ya wafungwa? Si unajua kule Nduruta tuna wafungwa wa Kimozambique,” akatoa ushauri.

“Banginyana! Mbona unaonekana kupoteza ubora wa akili yako? Umesahau kuwa yule anahesabika kama Mtanzania? Lazima atapelekwa Tanzania tu na si kwingine…”

“Oooh Basi, Mkuu nimepata wazo, pindi wakifanya hivyo ndipo pa kumteka…”

“Safi, andaa vijana, tufanye uchunguzi wa kujua mpango mzima ukoje kisha tunafanya yetu,”

“Bingo!”


Ndani ya Hoteli ya Postana Rovuma, Chiba aliketi kitandani akimwacha Jebeleth akiingia bafuni japo kujimwagia maji. Mkoba uliokuwa kitandani ulikuwa na nguo mpya ambazo mwanadada huyo alikuwa kanunuliwa na Chiba wakiwa njiani kuja katika hoteli hiyo. Akawasha luninga iliyopachikwa ukutani ndani ya chumba hicho na ndipo alipopambana na taarifa ya habari ya saa kutoka BBC iliyokuwa ikirusha habari ya kukamatwa kwa Benzilahagi.

“…Mtu huyo alikamatwa ndani ya nyumba liyokuwa akiitumia kujifichwa baada ya kikosi kazi kilichojumuisha vijana wa jeshi na polisi kufanya uvamizi wa ghafla…”

Taarifa ile iliendele kudadavua mambo mbalimbali na kuionesha baadhi ya picha za mtu huyo akifikishwa gerezani kwa ajili ya kuhifadhiwa ili kusubiri taratibu nyingine za kidiplomasia.

“Jebeleth!” Chiba akaita, “Njoo haraka utazame hii…!”

Jebeleth alitoka na taulo kiunoni na kukodoa macho luningani, alijikuta anabaki kinywa wazi kwa habari hiyo, akageuza sura na kumtazama Chiba.

“Washaniwahi!” akasema.

“Sasa utafanyaje?”

“Basi, operersheni itaishia hapa ila serikali itajua ifanyeje maana mi nilitumwa kumtia nguvuni kama wao wenyewe walikuwa na mkakati huo na wamekamilisha tutajua tufanye nini,” alipomaliza kusema hayo akarudi bafuni kuendelea na shughulia zake na Chiba akajibwaga kitandani. Dakika chache baadae Jebeleth akawa kamaliza kujiandaa na wakati huo Chiba alikuwa kajiondoa pale kitandani kumpisha mwanamke huyo kubadili mavazi na mwonekano wake, yeye akaenda zake kwenye veranda ndogo na kujitokeza kwa nje akiangalia mapito huku na kule. Mkononi mwake alikuwa na simu yake pana aliyokuwa akitumia kusafirisha taarifa mbalimbali za kazi yake. Akapachika vifaa vyake vya masikioni na kutafuta uelekeo wa kaka yake TSA 1 ni wapi. Haikumchukua muda simu yake ikaunganaishwa na kifaa maalumu ambacho Amata aliwekwa mwilini mwake, kupitia kifaa hicho aliweza kuifungua simu ya Amatana kuiweka kwenye mic on kisha akasikiliza kila kinachozungumzwa. Aliyasikia mazungumzo yote ya Amata pamoja na Bocca na Colonha, alitulia kabisa huku akiruhusu simu yake kurekodi kila kitu.

Kazi ipo, naona Amata yuko jirani kabisa na domo la mamba, sasa itakuwaje kuhusu huyu mshenzi Benzilahagi, hastahili kuishi, lazima kitu kifanyike kabla hajatema chochote, hapa sina jinsi lazima nguvu iunganishwe tufunge kazi, akawaza huku akitikisa kichwa mwenyewe kama anayesikiliza muziki.


MWISHO

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment