Pasipoti ya Gaidi ‘The Return of Kamanda Amata’ Sehemu ya Pili
IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
Simulizi : Pasipoti ya Gaidi ‘The Return of Kamanda Amata’
Sehemu Ya Pili (2)
UJERUMANI
KANALI BENSOIR BANGINYANA alipokelewa uwanja wa ndege wa Berlini na kuchukuliwa moja kwa moja mpaka nje ya jiji hilo na huko akapakiwa kwenye helikopta iliyompeleka mbali zaidi karibu na mpaka wa Ujerumani na Luxembourg. Akiwa na watu wawili katika msafara wake waliwasili kwa mwenyeji wao jioni ya siku hiyo na kikao cha biashara kilichoambatana na kula na kunywa kati yao na Jirack Paterson kilichukua nafasi.
“Safari hii naona umeleta mzigo mkubwa zaidi!” Jirack akamwambia Banginyana
“Unajua kule sshamba tuna tatizo jipya, si unakumbuka tuliyatoa yale majeshi ya SADC, sasa kuna jeshi la Tanzania limewekwa kule kwa ajili ya kukomesha waasi. Kiukweli bwana Jirack lile jeshi ni mwiba mkali tena wa sumu, siku tano zilizopoita almanusura waniondoe, kama si mbinu zangu za kikomandoo kuondoka eneo lile, aaaaaaaa, redio na televisheni za ughaibuni zingeingiza hela kwa habari hiyo,” Banginyana akaeleza.
“Pole sana, hao inabidi washughulikiwe kama wale waliojifanya wajanja kule Sierra Leone, tuliwasafisha kabisa. Sisi tunataka madini na ili tuyapate tunaweka mbinu nyingi sasa we ni nani utuzuie wakati viongozi wenzako wote wanakula hapohapo,” Jirack akaonesha kuhuzunishwa na hali hiyo.
“Sasa nimekuja na mzigo mkubwa kama mlivyoongea na Mkuu wa wakuu, tunahitaji silaha nzito za kuwashughulikia wale manyang’au, wanaojiita Jeshi la Tanzania…”
“Jeshi la Tanzania, linajiita jeshi wakati hata vita waliyopigana ya maana hatuioni!” Jirack akamwita mwanadada mmoja aliyekuwa hapo, akamnong’oneza kitu kisha akatulia kitini na yule mwanadada akaelekea kwenye kijichumba Fulani na baada ya kama dakika moja hivi akatoka na simu kubwa mkononi, akamkabizi Jirack. Kwa kidole chake cha kati akabofya tarakimu fulani fulani kisha akaiweka sikioni. Ilipopokelewa akaongea kama dakika ishirini hivi kwa lugha ambayo Banginyana hakuielewa kabisa, alipomaliza akakata ile simu na kumtazama kanali huyo usoni.
“Umepata! Wadau wamesema silaha zipo tena za kisasa ambazo hakuna jeshi la nchi yoyote Afrika inalozimiliki,” Jirack akamwambia Banginyana huku akiinua bilauri yake ya pombe kali na kuipunga hewani kisha akapiga funda mbili nayo ikakauka.
“Nashukuru yaani unipe hata ‘kifaru’ ikibidi ….”
“Oh! No! No! Banginyana kifaru huwa tunatoa kwa majeshi ya serikali ambayo yana mkataba nasi tu, kwa makundi yenu ninyi hatuwapi vifaru kwa sababu kifaru bwana ni ishara ya vita, nyie yale yenu ni mapigano tu. Tutawapa bunduki za kisasa, mabomu ya kisasa, badala ya kifaru tutawapa LPG za kisasa kabisa. Mwenyewe utaziona na tutazileta kwa njia yetu ileile, we usijali, kutoka sasa ni saa ishirini na nne zitakuwa pale,” Jirack alimkatisha na kumwambia maneno hayo.
“Sawa, nashukuru sana!” Banginyana akamalizia.
“Sasa bwana Bensoir, mimi katika biashara yangu hii huwa sina ubinaadamu kabisa nafikiri hata wewe pia. Nilimuua mke wangu kwa sababu alikuwa anatoa siri zangu nje mpaka nikaingi matatizoni na watu Fulani, sikuona haja ya kumuacha awe tatizo kwangu, nikatuma vijana wakamuondoa. Sasa lazima ujue kuwa mtu yeyote anayetoa au kuniharibi biashara zangu kwangu hana haki ya kuwa na maisha au ya kuishi hapa duniani. Mimi nina jeshi kama ilivyo serikali nyingine, timu yetu tupo nane, tuna pesa kama matundu ya neti, pesa kwetu ni kila kitu na si uhai wa mtu.” Aliposema hayo akamwita yule mwanadada na kumnong’oneza kitu kisha yule mwanadada akaondoka.
Muda mfupi baadae yule mwanadada alirudi na nyuma yake alifuatiwa na bintiu mrembo sana mwenye nywele ndefu zenye rangi ya dhahabu.
“Ni binti yako?” Banginyana akauliza huku akijilamba ulimi kwa jinsi binti yule alivyokuwa mzuri wa sura na umbo.
“Yeah, ni binti yangu anaitwa Butterfly!” Jirack akajibu. Na mara hiyo yule binti akaketi kitini pamoja na watu hao wane waliokuwa wakila na kunywa. Baada ya kusabahiana na waliopo, Jirack akamtazama binti yake kwa jicho kali sana.
“Butterfly, ulichokifanya juzi sicho, kinaniuma mpaka kwenye uvungu wa moyo wangu,” akamweleza.
“Kitu gani baba?” yule binti akuliza kwa woga.
Jirack akawatazama Banginyana na vijana wake, “Kanali Bensoir Banginyana, tusipotumia akili ya ziada tutapata pigo. Kuna mtu anaitwa Mr. Spark, mmewahi kumsikia?” akauliza na wao wakajibu kwa vichwa kuwa hawamjui.
“Huyu bwana amekuja hapa kufanya biashara ya madini tena ya almasi, alikuja na sampuli mbili, moja ya Bagon na nyingine ya Mpumbutu!” akawaeleza.
“Ya Mpumbutu?” banginyana akashtuka na vijana wake nao wakabaki kukodoa macho.
“Ndiyo, ya Mpumbutu. Alielekezwa kwangu na Mc Donald. Nmeshtushwa sana ameipata wapi ile sampuli ilhali ni ninyi wenye ule mgodi? Ina maana kuna mtu kaingia ndani yenu na ninyi hamna habari, ulinzi wenu uko wapi?” Jirack akaeleza kwa uchungu, “baada ya kumchunguza huyu bwana kwa kuingia kwenye mitandao ya watu hatari tukampata kuwa si mfanya biashara ni spy kutoka Tanzania anaitwa Amata Ric au amezoeleka kwa jina la Kamanda Amata, Tanzania Secret Agent namba moja alikuwa ameketi hapa na mimi,” akaongeza.
Taarifa hiyo, ilimfanya Bensoir na vijana wake kutazamana huku kijasho chembamba kikiwatiririka kwa zamu, Banginyana alihisi ganzi mwili wote.
“Simjui mtu huyo,” Banginyana akaeleza.
“Ni mtu mmoja matata sana, huwa hashindwi kitu akiamua kukivuruga, mi mwenyewe sikumjua kabla lakini file lake nililolipata mtandaoni, ni mtu hatari, akili yake ni 3D…”
“Yuko wapi sasa tumshughulikie asije kuwa tatizo kwetu,” Banginyana akang’aka na sura yake ikabadilika na kuwa ya kiumbe kibaya kabisa. Yule binti pale jirani yake ailikuwa akitetemeka muda wote.
“Nilikuwa nimemweka vizuri iuli nimchunguze, na nikamjua lakini unamwona huyu binti, huyu binti yangu, sasa amemchezea samba sharubu. Juzi amkwenda kwa Spark, akamwambia habari zote kuwa tumemgundua, na sasa yule bwana haonekani kwa sababu huyu Butterfly alimwabia kuwa tunataka kumuua hivyo aondoke, na yule bwana ametoweka lakini najua yuko hapa Ujerumani kwani watu wangu kwenye kona zote za kutokea nje ya nchi hawajamwona mtu huyo iwe ka sura wala kwa jina, lakini nimefanya msako kila mahali sijagundua alipo, tazama mtu huyu alivyo hatari, katoweka mbele ya macho yangu ambayo si rahisi binadamu mwenye nyama kuyatoroka,” Jirack akaeleza kwa uchungu, “Lakini yote hayo ni huyu binti Malaya,” akamtazama binti yake, “rudi chumbani kwako nisikuone hapa, ala!” akamwambia yule binti naye akanyanyuka haraka huku akilia. Jirack akachomoa bahasha chini ya meza yake na kumpa Banginyana, ndani yake kulikuwa na picha za Kamanda Amata wakati anazungumza na Jirack. Banginyana akazitazama zile picha kwa makini sana na kuwapa vijana wake nao wakazikodolea macho kwa zamu.
“Kabla sijaondoka hapa, roho yake naihitaji,” Banginyana akamwambia Jirack.
“All the best, Bensoir!” tuwasiliane saa tatu kabla hujaondoka hapa Ujerumani, kwa lolote katika msako wako wasiliana na kijana wangu. Lakini uwe makini sana na huyu kiumbe maana hapa nilipo nashindwa kujua wapi yupo, ila nikijua tu alipo nitakujulisha ili umshughulikie,” Jirack akamaliza na kuagana na Banginyana na timu yake.
Katika viunga vya mji wa Mannheim, kilomita kadhaa kutoka mpaka wa Ujerumani na nchi ndogo ya Luxembourg ndiko kulikokuwako kasri kubwa sana la tajiri Jirack Peterson ukiacha lile jumba lake la kule Potsdam ambako Kamanda Amata ndiko alilokutana na tajiri huyu, bado alikuwa na majumba mengi sana ya kifahari ambapo kila jumba alikuwa na watu anaokutana nao na kuna wengine hata balikuwa hakutani nao ndani ya Ujerumani.
Kamanda Amata aliishusha darubini kutoka machoni pake alipokuwa akiiangalia ile helikopta ikitua taratibu ndani ya jumba hilo katika mji wa Potsdam. Akiwa ndani ya mavasi ya kizee, nywele nyeupe alizozigeuza haraka haraka na ngozi yake ya kihindi iliyopchoka, aliiweka ile darubini kwenye koba lake wakati ile helkopta imepotelea ndani ya wigo mkubwa wa lile jumba lililo peke yake pembezoni mwa jiji la Berlin. Akaanza kujivuta taratibu kwa mwendo wa kizee mpaka mbele ya jumba lile ambapo alishuhudia gari mbili zikitoka kasi kuelekea mjini. Kamanda Amata akavuta hatua nyingine za kutosha na kufika katika jengo fulani, akaingia na ndani yake kulikua na vyoo vingi. ndani ya choo kimojawapo akabadili baadhi ya mavazi, akaonekana si mzee tena bali ni mtu wa makamo, sharubu za kubandika alizozisokota vyema zilimpendeza kabisa, akatokea mlango wa pili na kuingia kwenye gari alilokuwa ameegesha huko nje pamoja na gari nyingine nyingi ambazo huwekwa kwa ajili ya kuharibiwa kwani zimepita muda wake.
Akaitekenya na kuiingiza barabarani kisha akakamata barabara kubwa ya kuelekea Berlin. Baada ya kukamata barabara ya mwendo kasi kabisa ilimchukua dakika kumi na tano tu kuzikuta zile gari mbili, alizipita kwa kuwa zenyewe zilikuwa katika barabara ya mwendo wa kawaida. Kilometa tano mbele kulikuwa na makutano makubwa ya barabara, Kamanda Amata alihama kutoka ile barabara na kuchukua nyingine kisha akatoka nje kabisa na kuegesha gari katikakituo kikubwa cha mafuta. Dakika kumi baadae zile gari zikapita naye akaingia tena barabarani na kuchukua njia ileile, sasa alikuwa akiwaona muda wote.
HOTEL LOUISA – BERLIN
ZILE GARI MBILI ziliwasili kwenye hoteli hii iliyowekwa kwenye majengo ya kizamani sana, Maghalibi mwa jiji la Berlin karibu kabisa na Wilmesdorf. Banginyana na vijana wake wakateremka na mizigo yao ikaingizwa ndani na wahudumu. Yote haya Kamanda Amata alikuwa akiyatazama kutoka kwenye gari yake aliyoiegesha pembezoni mwa hoteli hiyo. Dakika hiyo hiyo ile gari moja ikaondoka na kubaki moja. Biashara nzuri sana, kumbe, sasa nimepata jibu la kazi niliyopewa, Amata aliwaza huku akitikisa kichwa na kuandika kwenye kijitabu chake huku tayari akiwa na picha kadhaa alizozipiga kupitia katika darubini yake. Taratibu akaiondoa gari yake kuiweka maegeshoni kisha akashuka na kuchukua tax akarudi hotelini kwake. Hakupoteza muda aliingia maliwato na kuurudisha ule mwili wake uliozoeleka siku zote, alipomaliza akarudi chumbani na kujiweka mbele ya kioo akichonga vindevu vyake kwa namna ya kupendeza. Akiwa ametingwa na kioo mlango wake ukabishwa hodi ya fujo, akachukua bastola yake na kuiweka tayari, akauendea mlango na kuufuangua kwa ghafla akamshika mkono huyo aliyemwona na kumrusha kitandani, kisha akaufunga mlngo kwa mguu wake huku bastola ikielekea pale kitandani.
“Usiniue, usniue Mr Spark!” ilikuwa sauti ya Butterfly, sauti nyembaba nzuri ambapo akiongea utafikiri anaimba.
“Kwa nini unakuja bila taarifa nyakati mbaya kama hizi?” Amata akauliza.
“Ukiona hivi ujue kuna sababu, Spark kwa nini hujaondoka? Watakuua, hakika watakuua, na sasa wamejua kuwa bado upo ijapokuwa uliwatoroka.” Yule binti akasimama na kumwendea Amata, “Sikiliza, mi nakupenda sana japo nimekuona leo mara ya tatu tu, nyumbani kwetu huwa wanakuja watu wengi sana kufanya biashara na mzee, biashara za kidhalimu zinazogharimu maisha ya watu wengi sana huko katika nchi za dunia ya tatu. Sikuona hilo juu yako, nilijua una nia ya biashara lakini wao wangekuzunguka. Upo hatarini, ondoka Spark, kama huwezi mi nitakutorosha kwa njia yoyote ile,” Butterfly alimwambia Amata.
Akairudisha bastola yake mahala pake na kumkumbatia yule binti, kisha nyuso zao zikakutana, “Kwa nini unitoroshe? Kwa nini usinihifadhi?” akamwuliza huku akimtomasatomasa mbavuni, Butterfly alijitahidi kujitoa kwenye mikono ya Amata lakini alijikuta hawezi, taratibu akaanza kulegea.
“Nitakuhifadhi wapi?” akauliza, “mimi ninaweza kukutorosha tu bila kujulikana,” akaongeza.
“Nihifadhi moyoni mwako…”
“Oooh please Spark,” yule binti alijikuta akipewa mabusu kutoka kwa Amata, alilalamika lakini alishindwa kuchomoka kwenye ile himaya. Kamanda Amata akakutanisha ulimi wake na wa yule binti mrembo mtoto wa tajiri, kisha wakaangukia kitandani nacho kikawapokea bila kinyongo.
Zilikuwa saa mbili za shughuli nzito juu ya kitanda hicho, Butterfly alikutana na jogoo la kiafrika lililompa raha za ajabu, alilalamika kimahaba, akashughulika vya kutosha, alihakikisha anakwanguliwa mpaka tone la mwisho. Simu ya Amata ikakatisha raha walizokuwa wakipena bila kuchoka, kila Amata alipotaka kutoka, yule binti alihitaji tena na tena. Amata akainyakua ile simu kwa taabu sana na kuiangalia kwenye kioo, ‘private call’, akaifyatua na kuweka sikioni.
“…Mr. Spark… naona sasa biashara yetu imechukua sura mpya. Baada ya kunionesha sampuli za almasi sasa naona unanionesha sampuli nyingine ya utaalamu wako wa kufanya mapenzi na binti yangu, umenitukana, sasa nimeamua kukufungisha ndoa na huyo Butterfly, muishi pamoja mpaka kifo kiwatenganishe…” ile simu ikakatika. Kamanda Amata akakurupuka na kusimama pembeni akiwa kama alivyo, akavuta taulo na kujifunga haraka haraka, akaliendea dirisha na kutazama nje, akarudi ndani na kufungua mlango, akaangaza huku na huko ndani ya kile chumba.
“Mr. Spark! Kuna nini mbona unahangaika…” binti akauliza.
“Wewe ndiyo Butterfly?”
“Ndiyo mimi, unasemaje Spark?”
“Chukua nguo zako uende, hapa tayari pameharibika!”
“Kitu gani Spark?”
“Fanya hivyo haraka!” akamwambia huku yeye akiingia bafuni, dakika moja tu zilimtosha kukamilisha shughuli yake akatoka kurudi chumbani.
“We Butterfly, mbona hivyo, nimekwambia uondoke hapa hapafai ndiyo kwanza umelala!” akabwata, “Butterfly! Butterfly! Butterfly!” akaita mara tatu lakini yile binti alitulia vilevile, akamwendea na kutaka kumtikisa lakini alipomkaribia alisimama ghafla.
“Shiiit!” akang’aka kwa hasira. Butterfly alikuwa amelala kimya, uchi wa mnyama juu ya shuka jeupe, macho yake yalikuwa yakitazama bila kupoteza uzuri wake, katikati ya paji la uso palikuwa na tundu dogo lililotiririka damu kidogo tu, alikuwa ameuawa. Amata akainua macho kueleka dirishani akakuta tundu la zaizi ileile limetoboa kioo na kuacha nyufa kadhaa pembeni mwake.
Mbisho wa hodi ukamstua kutoka katika wimbi la mawazo, huku mkono wake ukiwa umeshika kifua cha Butterfly pale kitandani, chozi la uchungu likamdondoka huku ile hodi ikiwa inamletea makelele kichwani mwake. Kwa hasira zilizojawa uchungu akashusha ngumi nzito juu ya meza ya kioo na kuitawanya vipande vipande huku ile hodi ikizidi kupigwa kwa fujo. Akainuka na bastola mkononi taulo kiunoni, akauendea mlango na kuufungua kwa ghafla …..
“Oooh Mr Spark!” sauti ya Preciuos Nancy ikapenya kwenye masikio huku ye mwenyewe akijipenyeza ndani ya chumba hicho, “Samahani kumbe ulikuwa na mwanamwali humu ndani, nimekuharibia starehe, mwanaume gani wewe kila siku kubadilisha wanawake kama nguo za ndani…” akaongeza nkukiendea kitanda, akakamata shuka ambalo Amata alimfunika Butterfly.
“Noooo!” Amata lipiga kelele lakini alichelewa, Precious alikuwa tayari kaondoa shuka lote na kumwacha marehemu kama alivyo, ukimya ukapasua anga la chumba hicho. Kamanda Amata akasogea na kuufunika tena ule mwili, yule mwanamke akageuka na kumtazama Amata. Kama Amata alitarajia sura ya gadhabu kutoka kwa Precious Nancy basi haikuwa hivyo, sura ya tabasamu ilimpokea, Precious akamkubatia Amata.
“Wonderfull, Mr Spark. Kweli unanipenda, umemuua hasimu wangu wa mapenzi, usijali nitakusaidia kuzika huu mwili,” maneno ya Precious Nancy yaliuchanachana moyo wa Amata. Hakusema kitu, alimwangalia tu kisha akamsukumia pembeni na kuchukua pochi ya Butterfly akaikagua ndani na kukuta vipodozi na bastola moja ndogo, akaichukua na kuikamata mkononi mwake, kisha akaziendea nguo zake na kuzipekua huku na kule, hakukuta kipya zaidi ya hela tu kwenye baadhi ya mifuko ya siri, mfuko mmoja. Akasogea kando na kuvaa suruali yake, shati huku macho yake yakiwa kiooni yakimwangalia Precious Nancy, akikikagua kiatu cha Butterfly, akakivuta kisigino na kukirudisha tena. Kisha akakiweka pale chini.
“Unachukua simu ya nini?” Precous akamwuliza Amata.
“Nawataarifu polisi juu ya hili…”
“Ooh! No! no! no! usifanye hilo, utaingia matatizoni sasa hivi mya dear Spark. Subiri jioni ifike, nimekwambia nitakusaidia kuuzika huu mwili na mtu yeyote asijue kilichotokea, tuondoke,” akamwambia. Amata akaitazama saa yake ilikuwa saa kumi na moja jioni. Akachukua vitu vichache pamoja na ile bastola ya marehemu akavitia kwenye begi lake. Bastola yake moja aina ya PPK akaipachika kiunoni na kuondoka na Precious.
“Unanipeleka wapi leo?” Amata akamwuliza Preciuos wakati akiondoa gari yake pale hotelini.
“Usijali nakupeleka sehemu nzuri sana ambayo utainjoi na kumsahau huyo marehemu wako, tukacheze muziki, kamali, tule tunywe kisha tuje tufanye ila kazi yetu,” akajibu yyule mwanamke huku akibadili gia ya gari lake kuongeza mwendo.
SPIELBANK POTSDAMER PLATZ
Berlin Casino
PRECIUOS NANCY aliegesha gari yake nje ya jengo hilo kubwa lililozungukwa na vioo kila upande na kufanya mandali ya kuvutia kutokana na kuakisi kwa mianga ya taa mbalimbali zinazowaka barabarani. Giza lililkuwa likianza kulifunika jiji hilo. Magari mazuri ya kifahari yalikuwa yakiegeshwa huku na huko na watu walioonekana wenye pesa walikuwa wakiingia ndani ya jumba hili la kuvutia.
“Berlin Casino, hii ndiyo casino bora yenye chat Ujerumani, karibu sana Spark; leo hapa kuna kamali zawadi ya kwanza ni Range Rover ya kisasa mpya kabisa brand new, ukitaka kuwaona matajiri wa Berlin leo hii,” Preciuos alimwambia Amata.
“Sawa!” Amata akajibu kwa mkato kisha wote wakateremka na kuongoza kwenye jengo hilo. Kila alipokuwa akivuta hatua moja na nyingine Amata alihisi uzito miubwa na nywele zikimsisimka. Ndani ya jengo hilo kulikuwa na casino kubwa tatu, moja wapo ilikuwa ya wacheza kamali, hapop kulikuwa na michezo kama Poker, blackjack na mingine kama hiyo na pembeni yake kwa juu kulikuwa na sehemu ya mazungumzo kulikuwa na meza zenye viti viwili, vitatu, vine na kuendelea, kulikuwa na kaunta kubwa ya pombe za kila aina kali, tamu kwa chungu. Muziki laini uliokuwa ukipigwa na Tori Amos alikuwa akifanya eneo hilo kuwa la kipekee sana.
Ghorofa ya pili kulikuwa na casino nyingine huko kulijaa mashine za bahati (slots machine) nyingi kupita maelezo na ghorofa ya tatu huko kulikuwa na disko zito, vijana wengi walijaa huko.
“Unapenda kuangalia Poker? Au Blackjack?” akauliza Precious.
“Napenda kunywa pombe, twende tukaketi kule juu,” wakapita na kupanda ngazi chache, wakakaa kwenye moja ya meza ambazo zilikuwa na viti viwili tu, vinywaji vikaletwa na burudani zikaendelea.
Wakiwa wamezama kwenye mazungumzo ya hapa na pale huku pombe ikizidi kuwachukua, simu ya Precious ikaita, akanyanyuka na kwenda kuipokea pembeni ambako Amata hakumwona sawasawa, akainua bilauri yake iliyojaa pombe ile aina ya Couvosier, akaimiminia kinyani na alipoitua akakuta hayupo peke yake. Kiti kile alichoketi Precious kulikuwa na mtu mwingine mweusi kama yeye, aliyevaa suruali nyeusi, shati jeupe lenye tai ya kipepeo ya rangi ya buluu na kujifunika kwa koti jeusi, mkononi mwake alikuwa na bastola Magnum 22 iliyofungwa kizuia sauti ikimtazama. Sura ya mtu huyu haikuonesha hata kama alikuwa na masihara au vipi, ilitulia na katika paji lake la uso kulifanya mawimbi machache ya kunyanzi la ngozi, ndita. Hakutabasamu wala hakununa alikuwa katikati lakini mkono wake uliokakamaa na kushika ile bastola ambayo tayari ilikuwa haina usalama, ulipambwa kwa kovu moja kubwa lililoanzia kwenye kiwiko na kuzunguka mpaka karibu na kiganja upande wa juu.
Kamanda Amata akataka kuchukua ile chupa ili ajimiminie kinywaji.
“Usilete ujanja! Tulia kama ulivyo na ufuate amri yangu,” yule bwana aliongea kisawahili safi kisicho na hila.
“Sawa! Unataka nini?”
“Nataka kujua almasi uliyoileta kuiuza, sampuli kutoka Mpumbutu umeipata wapi?”
“Unataka nikuuzie au? Maana biashara hiyo haikuhusu sasa wewe unaiulizia ya nini?” Amata akajibu kijeuri.
“Kamanda Amata!” yule jamaa akaita, “Ujue mkononi nina bastola iliyojaa risasi, ukijifanya jeuri sintosita kuitumia na kuyakatisha maisha yako,” akaongeza.
“Nimeipata Mpumbutu,” akajibu.
“Nimepewa kama zawadi,”
“Na nani?”
“Unataka umjue?” akauliza na yule bwana akajibu kwa kubetua kichwa.
“Nimepewa na bosi wako, Kanali Banginyana,” alipojibu hilo akajiegemeza kwenye kiti na mara akahisi kitu baridi kikigusa kisogo chake.
“Usigeuke, inuka hivyohivyo,” sauti ilimuamuru, akainuka, “Ongoza njia hiyo moja kwa moja”. Hakuwa na ujanja akafuata na kutii hiyo amri, wale jamaa wakamwongoza mpaka kwenye eneo la vyoo, wakamwamuru aingie ndani ya jengo hilo la vyoo vya VIP. Ndani ya eneo hilo hakukuwa na mtu, ni ukimya tu ulitawala kila mahali.
“Geukia ukutani!” akaamuriwa naye akatii.
“Weka mikono kisogoni”. Akatii. Kamanda Amata alikuwa kawapa mgongo wale jamaa wote wawili wakiwa na bastola zao, mmoja akiwa kasimama karibu na mlango na mwingine karibu na Amata.
“Piga magoti!”
Anafasi hiyo ndiyo hasa aliyokuwa akiisubiri, alikwenda chini kana kwamba anapiga magoti, akajibiringisha kwa sarakasi ya kitoto miguu yake ikafika ukutani akajiinua kwa nguvu na yule jamaa akaachia risasi iliyopita milimita kama mbili hivi kwenye ngozi ya began a kuchimba ukutani. Amata alijisukuma kwanguvu kwa miguu yake na kuja kutua kwenye kifua cha huyo bwege, kabla hajakaa sawa akapamiana na mwenzie aliyemwacha mlangoni. Amata akaanguka chini na kujiviringa huku mguu mmoja kimchota ngwala yule jamaa na kumbwaga chini kama mzigo, alipojaribu kujinyanyua alikutana na ngumi nzito iliyo,rudisha chini, yule mwenzake alianza kuweweseka, akiiweka bastola yake vizuri, Amata tayari aliikamata bastola yake ya PPK mkononi na kuifyatua, ikabanja na kumvunja mguu yule wa pili, akaenda chini huku akitoa yowe la uchungu. Kabla hajajiweka vizuri, Amata akajikuta akipigwa teke la maana nyuma ya kisogo kutoka kwa yule jamaa aliyeanguka pale chini, akagumia kwa uchungu maana netweki ilipotea kidogo, akamgeukia na kumshushia kichwa kisha akamdaka kabali ya maana. Yule jamaa naye alikuwa mzuri si haba, akajikunja na kujigeuza akamnasa Amata kwa miguu yake shingoni na kuvuata kwa nguvu, mikono ya Amata ikaachia shingo na kudaka miguu ya yule bwege wote wakaenda sakafuni.
Yule jamaa wa pili hakuwa na uwezo wa kufanya lolote, alijivuta na kutambaa kuilekea bastola yake. Wakati mapigano ya wawili hao yakiendelea yule jamaa akaikamata bastola yake, hisia za Amata zikamshtua, akamwona jamaa kwa jicho upande akiiweka ile bastola sawia. Akatumia nguvu zake zote na kubingilika mara kadhaa na risasi zile zikawakosakosa. Amata kwa mikono yake yenye nguvu aliitanua miguu ya yule jamaa akafanikiwa kuitoa, akajigeuza na kumtwanga ngumi ya kwenye korodani, wakati anagalagala, Amata aliinuka na kusimama wima.
“Weka mikono yako juu!” yule jamaa aliyevunjika mguu akamwabia Amata huku akiwa kamwelekezea bastola, hakuweza kusimama kutokana na mguu wake. Mara mlango wa chooni ukaanza kugongwa kwa nguvu, yule jamaa akageuka kuangalia mlangoni akajikuta akipigwa teke la nguvu kifuani akaenda chini, Amata kwa bastola yake akamshindilia risasi mbili za kifua na kumkata ngebe. Sekunde hiyo hiyo mlango ulipigwa kikumbo ukafunguka, Amata akajirusha na kujibanza nyuma yake, vijana watatau waliovalia sare za kiaskarai, moja kwa moja Amata alijua walikuwa walinzi wa casino hiyo waliingia na nyuma yao walifuatiwa na Precious Nancy.
Precious Nancy alikuwa na bastola ndogo mkononi, Amata akaitazama ile bastola, ilifanana kabisa na ile ya marehemu Butterfly, akili yake ikagonga, alipoona wale jamaa watastuka alipo akapiga risasi tatu juu na zile kelele za bastola wote wakalala chini, akatoka ndani ya kile choo na kufunga mlango kwa nje kisha akavunja kitasa ili mtu wan je asiweze kufungua kiurahisi. Akaondoka eneo hilo na kujichanganya na watu wengine mpka nje kabisa, akaondoka zake.
Tax aliyochukua ilimfikisha Hoteli Louisa, akalipa na kuingia kwenye gari yake aliyoiacha hapo tangu mchana ule, akaketi kwa utulivu na kuangalia kinachoendelea. Gari moja nyeusi ikaingia pale kwa kasi na kuegeshwa, akashuka yule jamaa aliyepambana naye kule casino, mkononi mwake alikuwa amesika kitambaa na kuibana pua yake, aliingia ndani na ile gari ikabaki imesimama pale nje. Kijana mwingine wa kizungu akatoka kawney ile gari na kusimama nje, Amata akachukua darubini yake na kumtazama vyema alikuwa yule mwenye nywele ndefu aliyempokea kule hotelini na kumpeleka kwa Jirack. Timu moja! Akawaza. Dakika mbili baadae, watu wawili wakatoka mle hotelini, yule wa kwanza aliyepambana naye na mwingine aliyevalia suti nadhifu, walionekana kuwa na harakaharaka. Matukio yote hayo alikuwa akiyanasa kwa kutumia darubini yake ndogo ikiyrekodi kwa picha mjongeo, ila gari ikaondoka nay eye akasubiri sekunde thelathini akaondoka zake.
Amata aliwasili kwenye hoteli aliyofikia, akafungua mlango na kuusukuma taratibu huku jicho lake likitua kitandani alipouacha mwili wa Butterfly, haupo. Aliuacha mlango na kuingia ndani bastola mkononi. Kitanda kilitandikwa safi kabisa tena kwa shuka zenye chapa ya hoteli ile ile. Akanyata na kufungua mlango wa bafuni, hakuna mtu! Kila kona hakukuwa na mtu, alichoshangaa zaidi hadi kioo kilikuwa kimebadilishwa tayari, akafungua kabati na kukuta sanduku lake lipo vilevile, mkoba wa Butterfly haukuwepo, lakini ile bastola alikuwa ameiweka kwenye mkoba wake ilikuwepo. Amata akahisi kama akili yake inapata ganzi, akatoa na kuangalia namba ya mlango wa chumba, ileile. Aliporudi ndani akahisi mlango unafunguliwa nyuma yake, alipogeuka akamwona Preciousy Nancy. Kofi moja kali lilimpepesua Precious mpaka kitandani.
“Unanifanya mi bwege siyo? Unalala na mimi kumbe unanizunguka sivyo? Leo utaniambia nani unayemfanyia kazi,” Amata alilalama na kumtia kofi linguine na linguine.
“Spark, unathubutu kunipiga mimi? Sijawahi kupigwa tangu kuzaliwa kwangu, nguruwe mweusi we,” Precious naye akachacharuka, lakini kabla hajatulia alipokea konde moja zito toka kwa Amata, akarudi kitandani huku damu zikichuruzika puani. Amata akamkamata vizuri.
“Nani alikutuma kwangu, nani unamfanyia kazi?”
“Hakuna ninayemfanyia kazi, mimi nipo kwa biashara zangu mwenyewe za kuuza mwili,” alijibu huku akipambana na damu iliyokuwa inavuja puani kwa kasi.
“Najua, kifo cha Butterfly wewe unahusika!”
“Hapana Spark! Hapana!”
“Kwa nini umekifurahia kifo chake, kwa nini ulisema utanisaida kuuzika mwili wake na sasa sijaukuta? Utanieleza leo,” makofi mengine ya nguvu yalipita kwenye mashavu laini ya Precious.
“Unanionea Spark!”
“Nakuonea ee!” Amata akaingiza mkono kwenye paja la Precious na kuchomoa bastola ndogo iliyojaa kignjani kwake.
“Hii bastola ya nani?”
“Ya kwangu hiyo,” Amata akamwacha na kuingiza mkono wa pili mkobani kwake na kutoa bastola ya Butterfly.
“Na hii je? Kwa nini inafanana nay a kwako kwa kila kitu? Usiponambia nakuua,” Kamanda Amata alifyatua risasi iliyochimba kwenye godolo sentimeta chache kutoka kwenye paja la Preciuos.
“Nasema, nasema! Nafanya ka-ka-zi kwa ba-ba wa Butterfly”
“Kazi gani?”
“Inategemeana ninayopangiwa, kwa sa-sa nilita-ta-kiwa kuhaki-kisha nyendo za-ko zote zinajulikana” alijibu kwa kitetemeshi. Hasira za Amata zikawaka juu ya mwanadada huyo, akamzabua konde moja zito lilitua usawa wa sikio lake, Precious akaenda chini kaitandani na kupoteza fahamu. Haraka haraka alichukua mkoba wake na kufunga begi lake, akaondoka mpaka mapokezi.
“Nacheck out, nimepata dharula kuwa nyumbani kuna wagonjwa,” akamwambia yule mwanadada wa mapokezi.
“Ulikuwa umeomba kwa wiki mbili na sasa ni moja tu,”
“Usijali!”
Kamanda Amata akatoka ndani ya hoteli ile, akiwa katika ngazi za hoteli ile akaangaza macho na kuiona gari yake ikiwa kando, palepale alipoiacha imeegeshwa, kwa hatyua zisizo na shaka akaindea na kuufungua mlango kwa kifaa maalumu cha kielektroniki, akatupia begi lake katika siti ya nyuma nay eye akaketi nyuma ya usukani tayari kwa safari, akapachika ufunguo na kuwasha gari, haikuwaka, akajaribu tena, kimya. Kila lipozungusha funguo funguo ilizunguka tu lakini hakukuwa na jibu lolote, kwenye dashboard ya gari hiyo nako hakukuwa na dalili yoyote ya uhai.
Akateremka na kuelekea upande wa boneti la gari hiyo, akafungua na kuangalia ndani yake.
“Shiiiiit!” akang’aka kwa hasira baada ya kuona hakuna betri, nani kaondoa betri hapa? Akajiuliza pasi na jibu, akalibamiza lile funiko la boneti kwa hasira, wakati huohuo akahisi kupigwa na kitu kizito kisogoni, akakosa nguvu na kujibamiza garini akaanguka chini chali. Watu watatu waliovalia suti nyeusi walisimama, aliwatazama kwa maluweluwe na kuwaona zaidi ya kumi na tano, wamekuja wengi kweli, akawaza, aaa wameniua hawa sina ujanja, akalalama nafsini mwake. Amata akaanza kupoteza nuru taratibu, zile taa zilizokuwa ziking’aa akaziona kuwa nyekundu sana, masikio yake yakagubikwa na kelele nyingi sana, akainua mikono yake akajiziba masikio, giza likamtawala na ukimya mkuu. Alihisi anatumbukizwa kwenye shimo refu sana lisilo na mwisho.
4
MSITU WA MPUMBUTU
JESHI LA UMOJA WA MATAIFA lilikuwa katika operesheni yake iliyokuwa ikiongozwa na vikosi kutoka Tanzania. Ndani ya Msitu wa Mpumbutu, vijana hao hodari na wapiganaji waliotumainiwa walikuwa kwenye maficho yao ya kila siku. Wanakiji walipita kwenda poleni kutafuta kuni na mahitaji mengine lakini hawakuweza kabisa kugundua maficho ya askari hao, walikuwa wakitembea kwa nyakati maalum kusingambele kuelekea kambi kuu ya waasi wale. Wakati yote hayo yakiendelea hakuan hata mmoja wao aliyejua kuwa kiongozi wa waasi hayupo msituni hapo kwa zaidi ya saa arobaini na nane. Iyalikuwa mapambano ya kimyakimya, hii iliwapa waasi wakati mgumu sana wa kulidhibiti jeshi hilo kwa kuwa daima walishindwa kujua ni wapi wamejificha, walichomaua kufanya ili kuwachokoza walitoa askari watatu wapiti msituni kama chambo ili wakiuawa basi watajua ni ueleo gain wapeleke mashambulizi yao.
Kikosi namba moja kikiwa kimya kabisa msituni kiliwaona vijana wale waliovalia sare za kijeshi na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) wakirandaranda msituni. Wadunguaji kama kawaida yao waliashaanza kuwamezea mate vijana hao.
“Msifanye lolote, huo ni mtego!” sauti ya kiongozi wa mapambano mstari wa mbele iliyoa angalisho na wale askari wakatulia tuli kusubiri amri nyingine. Mmoja wa wale askari waasi akainua redio koli na kuibofya kinobu Fulani kisha akaongeza kidogo.
“Zone namba moja iko shwari, tunasonga mbele, ova!” ukafuata mlio Fulani kama wa kukoroma hivi.
“Songa mbele ova!”
“Roja! roja!” akaitua ile redio na kuitumbukiza mfukoni, wakaondoka mahala pale na kuendelea mbele bila kujua kuwa nyuma yao wanawaacha wanajeshi wa kutosha waliojificha kimya kwenye nyasi na mawe na mapango yaliyozunguka eneo hilo. Dakika moja baada ya wale askari kuondoka na kusonga mbele lilifuata kundi kubwa la waasi waliokuwa na silaha nzitonzito miilini mwao, mabomu ya kurusha kwa mkono na mabunduki makubwa yalikuwa miongozi mwa silaha hizo, wengine walikuwa bado ni vijana wadogo umri wa kwenda shule. Wakapita eneo lile kwa mstari mmoja.
Kepteni Chwaka aliyekuwa kikosi namba moja cha jeshi la UN aliwahesabu vijana wale walikuwa kama kumi na nane hivi.
“Waaceni wapiti!” akawaambia wengine. Dakika mbili baadae walipita wengine na wengine. Ulikuwa ni msafara uliokuwa ukielekea mahali Fulani ambako hawa wanajeshi hawakukujua. Dakika tani baadae hakuna waasi waliopita zaidi ya wale waliotangulia.
“Operesheni yetu si kulinda amani ni kusafisha waasi, sasa kikosi namba tano kiwashambulie kutoka nyuma wengine tulieni kama mlivyo,” amri ikatoka kwa Kepeteni Chwaka.
Kikosi namba tano kikatoka mafichoni na kuwavamia waasi hao kwa nyuma, milio ya risasi ilipoanza kusikika katika msitu huo wale waasi nao walitawanyika kwa jinsi ya kupendeza na kuanza kurushiana risasi na askari hao. Kutokana na utaalamu wa majeshi ya Tanzania yaliyokuwa huko msituni chini ya UN waliweza kuwaua waasi wengi, huku wao wakipata majeraha madogomadogo kwa maana walikuwa wakirusha risasi na kujikinga kwenye mawe makubwa na wengine kwenye miti huku wakijitokeza na kulindana kwa ufundi kabisa.
Wale waasi walipoona wanazidiwa nguvu na jeshi hilo waliamua kutoa taarifa kambini kwao. Na mara hiyo chopa moja yenye rangi nyeusi ikawasili na kuangusha mabomu na risasi nyingi kutoka kwenye Heavy Machine Gun iliyofungwa kwenye lango la chopa hiyo. Hili lilikuwa pigo zito sana kwa majeshi ya UN, iliwawia vigumu jinsi ya kujificha katika eneo hilo kwani wale waasi walio kwenye chopa walikuwa wanajua kulitumia mashine hilo vizuri kabisa. Mmoja wa vijana mahiri wa vikosi vya UN aliyekuwa na jukumu la kutumia RPG hakuaona haja ya kupoteza muda, aliiweka sawa bunduki hiyo kubwa ambayo hutumika badala ya ‘kifaru’, alipohakikisha ipo sawa akaipachika begani na kusimama nyuma ya jiwe ambako haikuwa rahisi kuonekana.
Wenzake wa jirani naye wakapisha pembeni kuepa mlipuko unaotoka wakati wa kufyatua grenade hiyo ambayo ilikuwa na kasi ya mita 294 kwa sekunde. Akaipachika dole lake la shahada kasha akabana jicho kutafuta shabaha ya kulidungua chopa hilo. Huku akitoa matusoi ya nguoni kwa sauti ndogo, alikuwa akifuatisha mwendo ule wa ile chopa alipoona yuko sawa, bila kusita, akavuta nyuma dole lake, lile kombora likafyatuka na sekunde mbili tu mlipuko mkubwa ulitokea hewani, ile chopa ikakatika vipandevipande na kuanguka porini.
“Retreat retreat retreat!” sauti ya amri hiyo ikawafikia wanajeshi wote na wale waliokuwa kwenye uwanja wa mapambano wakarudi mafichoni mwao huku kikosi kingine kikijitokeza na kumalizia waasi waliokuwa bado wako hai, hii ililetwa na hasira baada ya kuona miili ya wenzao ikiwa chini. Dakika moja baadae msitu ulikuwa kimya na mioshi ya baruti ilitapakaa huku na kule. Wapiganaji watano wa jeshi la UN wakawa chini bila uhai.
Kepteani Chwaka na wengine wakajitokeza kusaidia majeruhi na kuhifadhi zile maiti. Ilikuwa ni huzuni kubwa kwa wapiganaji wote hawa, wakavua kofia zao, wakainamisha chini bunduki zao kuonesha ishara ya huzuni kwa tukio hilo.
Chonjo aliweka redio lake chini na kubofya hapa na pale kutafuta mawasiliano na kambi yao iliyokuwa mpakani mwa Tanzania na Ngoko katika upande huo wa kusini.
Alipopata mawasiliano nao, akawapa taarifa hiyo na kuomba msaada wa haraka. Nusu saa baadae chopa la kijeshi lenye nembo ya UN uvunguni likawasili eneo hilo na kutafuta mahali penye uwezekano wa kutua likafanya hivyo, ile miili ya wanajeshi watano ikapakiwa na wale majeruhi kadhaa nao wakapakiwa kwenye chopa nyingine iliyokuwa na alama zaidi ya Msalaba Mwekundu zikaondoka eneo hilo na kuwaacha wale wengine wakiwa bado kule msituni.
Kepteni Chwaka akawatazama vijana wake, “Tumepungukiwa, kikosi namba tano kimepungukiwa wapiganaji watano, nina uchungu sana. Sasa tuhakikishe tunafika katika kambi yao huko machimboni na tusibakishe hata salio, sasa ni jino kwa jino, aluta continua,” akawaambia vijana wake na kuamuru wasonge mbele nao wakafanya hivyo.
IKULU – DAR ES SALAAM
RAIS ROBERT SEKAWA alisikitishwa na taarifa ya vifo vya wapiganaji wake wa mstari wa mbele vilivyotokea huko Ngoko. Yeye kama maafisa wengine wa usalama walishikwa na wingu zito la sintofahamu ijapokuwa walikuwa wameridhishwa na taarifa ya kuwa waasi wote eneo lile waliuawa na chopa lao kudunguliwa bado vifo hivyo vilisumbua nyoyo za viongozi hao.
“Mpumbutu imekuwa kaburi la vijana wetu?” alimuuliza Mkuu wa Majeshi aliyekuwa amefika Ikulu kutoa taarifa hiyo.
“Hapana, mapambano bado yanaendelea, na tutahakikisha tunafutilia mbali hao waasi wa X65 bila huruma,” yule Mkuu wa Majeshi aliyechafuka vyeo mabegani kifuani aliongea kwa kujiamini. Wakiwa katika mazungumzo hayo, mmoja wa wale walinsi wake anaombatana nao daima ambaye huwa na nguo za kijeshi muda wote yaani ‘Aide de Camp’ (ADC) alimjia na kumnong’oneza kitu mara baada ya kutoa saluti ya utii, akamjibu kwa kumnong’oneza na yule jamaa akaondoka. Baada ya dakika tu akaja na bahasha na kumkabidhi, rais akaifungua na kuisoma. Ilikuwa nukushi iliyotumwa mchana huo.
…Tunarudia tena, ondoa majeshi yako katika msitu wa Mpumbutu ama la tutakalolifanya sio dogo kwa jeshi lako mnalolitumia kama jeshi la UN. Kumbuka hao waliokushauri kulituma jeshi lako huko wamekuingiza kwenye domo la mamba. Waliokufa leo ni patgazeti tu film inakuja, tutafanya kitu kibaya, tega sikio….
Baada ya kuisoma, akatulia kidogo na kutikisa kichwa, “Naomba yule kijana wako wa MI afike hapa mara moja!” akatoa oda na wakati huohuo taarifa ikafika makao makuu ya jeshi.
“Ninavyoona hii vita ni kubwa na imetuzunguka,” rais akaendelea kuongea.
“Ni kweli hatuna budi kuhusisha vikundi vingine vya kiintelijensia kutoka majeshi mengine kama polisi au Usalama wa Taifa ili sote tuweze kuchunguza kila mtu kwa nafasi yake, najua tutafanikiwa,” akashauriwa. Kikao kile kikaendelea kwa dakika kadhaa huku rais akiomba ile miili ya wanajeshi ifanyiwe utaratibu wa kurudi nyumbani kwa ajili ya kuzikwa kijeshi na kishujaa.
SIKU HIYOHIYO – SAA 8 MCHANA – IKULU
BMW NYEUSI ilifunguliwa geti na kuingia moja kwa moja mpaka kwenye maegesho ya wageni. Mvua ya rasharasha ilikuwa ikinyesha, milango yake haikufunguliwa na gari hiyo iliku imetulia palepale bila kwenda popote huku ikiunguruma. Dakika tano baadae, mlango wa upande wa dereva ukafunguliwa. Mwanamama mtu mzima, nywele zake zilizachakaa kwa mvi, alikuwa ndani ya miwani na suti safi ya kijivu, alikuwa na mwili wenye afya, kutoka mbali utamjua kuwa alikua akitembea kwa umakini wa hali ya juu. Akazikwea ngazi za jingo hilo na kupokelewa na wasaidizi wa Ikulu, moja kwa moja akaongozwa katika mlango mmojawapo ambapo alikuatana na Othman, mwana usalama namba moja wa Rais, akampokea na kuingia naye ndani ya ule mlango. Ndani yake wakateremka na lifti mpaka chini kama mita tatu hivi.
Kilimanjaro Square, maandishi yalisomeka mlangoni, yule mwanausalama akabofya tarakimu Fulani na ule mlango ukafunguka.
“Karibu ndani, karibu sana” akamkaribisa kasha yeye akarudi mahala pake pa kazi.
Madam S, mkuu wa kitengo cha TSA, idara nyeti ya Usalama wa Taifa inayofanya kazi moja kwamoja chini ya rais aliwasili ndani ya ofisi hiyo nyeti ambayo siyo rahisi kwa mtu wa kawaida kufika. Wakapeana mikono na Mheshimiwa kasha wakaketi katika mtindo wa kutazamana.
“Pole mheshimiwa kwa kupoteza wapiganaji watano huko Ngoko,” Madam S alivunja ukimya.
“Asante lakini hali ni mbaya sana, na wewe unajua bila shaka, Selina tunahitaji kuimaliza hali hii, bila kuyumbisha chochote nahitaji idara yako ichukue nafasi ya uchunguzi wa uvamizi wa Ikulu na watakaobainika wafanyiwe kazi bila huruma,” rais akamwambia Madam S aliyetulia kimya akisikiliza maagizo ya kazi hiyo mpya, “najua unavijana makini, wenye weledi wa hali ya juu na wanaweza kufanya kazi hii kwa muda mfupi sana,” akamaliza na kujiegemeza kwa nguvu kwenye kiti chake.
“Bila shaka mkuu tutaifanya kwa kuwa ni kazi yetu, na kiapo chetu ni kukilinda kiti cha rais, nakuhakikishia kazi hii itamalizika haraka,” akamjibu.
“Patakapohitajika msaada wowote usisite kuwasiliana na mimi moja kwa moja kwa ile namba ya Alpha,” akamwambia. Madam S akasimama nakuanza kuuelekea mlango.
“Oooh Sellina, hakikisha katika kazi hii Yule kijana wako machachari Yule nani anaitwa Yule…”
“Amata Ric au Kamanda Amata…” Madam akasaidia kujibu.
“Enheee huyohuyo asikose kwenye hiyo operesheni,” akaagiza.
“Oh, mheshimiwa Kamanda Amata yuko Ujerumani,”
“Kuna nini Ujerumani?” akauliza kwa wahka.
“Anafanya uchunguzi kujua ni wapi waasi wa Ngoko wanapata silaha, hii kazi tuliombwa kuifanya na Umoja wa Afrika,” akamweleza kwa usahihi.
“Oh ok, sasa hilo tuliache, huyo kijana arudi hapa mara moja na kazi yake naomba idara impe mtu mwingine akaanzie yeye atakapoishia, right?” Mheshimiwa rais aliongea huku kijasho kikimtiririka na kutoa maagizo hayo kuwa Kamanda arudi nchini.
“Right Sir!”
“Ok!”
Madam S akatoka ndani y ofisi hiyo huku kichwa kikianza kumzunguka kama kawaida yake, jambo la kwanza alilolifanya ni kutuma taarifa kwa njia yao ileile.
…fika nyumbani haraka, mama ni mgonjwa sana. Tena sana aisee…
Ujumbe huo uliwafikia kila mtu kwa muda uleule na mara nyingi walijua wazi wakiapewa taarifa hiyo basi nyumbani ni wapi na mama ni nani.
Akiwa amegubikwa na usingizi wenye ndoto nzitonzito Gina aligutushwa na kijimuziki kilichokuwa kikisikika kutoka ndani ya pochi yake, akainua mkono na kuivuta, akaifungua na ndani ya pochi hiyo ndogo kulikuwa na kijitaa chekundu kikiwaka waka, akakibonyeza na kusikiliza.
‘…fika nyumbani haraka, mama ni mgonjwa sana, tena sana aisee…’
“Ujumbe umefika na unafanyiwa kazi!” akajibu kasha akaifunga ile pochi na kukurupuka kutoka kitandani. Jicho lake likatua kwenye saa ya ukutani, saa tisa za alasiri, akaingia maliwatoni na kujiweka sawa, akachukua bastola yake na kuijaza risasi, akaibana mahala pake ndani ya nguo alizovaa, akainua pingu yake na kuipachika kiunoni katika suruali yake. Gina alipenda kutembea na pingu kutokana na mazoea ya kazi yake ya awali kabla Amata na Madam S hawajafanya longolongo kumhamishia TSA. Akajitazama kwenye kioo na kuinua rangi ya midomo akajipakaa vyema na kuibanabana midomo hiyo, alipohakikisha ana kila itu tayari, akatoka na kuufunga mlango kasha akajitupa ndani ya gari yake Peugeot 405, akaingia barabarani na kuondoka.
Ndani ya mgahawa wa Steers, Daktari Jasmine alikuwa ameandamwa na kijana mmoja shababy aliyekuwa akimtaka kimapenzi. Ijapokuwa Jasmine alionesha kukataa muda mrefu lakini kijana huyo hakukata tama.
“Hivi nikwambie mara ngapi ili unielewe kuwa sikutaki?”
“Aaaa dokta, unaniumiza moyo, hebu tazama ni muda mrefu kiasi gani nakufuatilia lakini unanikataa, au kwa sababu sina hela, lo jamani masikini sisi tutakosa vingi vitamu,” Yule kijana alikuwa akilalamika huku macho yake yakitoka machozi. Sekunde hiyohiyo wakati Jasmine akiendelea kunywa juice yake alihisi kitu kama pini kikimchoma kwenye kidole chake cha shahada, alipoiangalia pete yake aliona lile jiwe likibadilika rangi, akajua kuna ujumbe nyeti umefika. Akainuka haraka na kutoka kwenye ile meza.
“Wapi tena sweetie?”
“Unikome…!” akajibu huku akiteremka ngazi chache kisha akavuka barabara na kuifikia gari yake ndipo alipogundua uwa kuna mtu nyuma yake, akageuka kumtazama ni Yule kijana.
“Hivi wewe unanielewa, najua kuwa unanipenda, lakini kwa sasa sina muda huo, nitafute siku nyingine,” Jasmine akamwambia huku kamkazia macho. Akafungua mlango wa gari na kuingia kasha akajifungia. Akainua mkono wake na kukifunua kile kifuniko cha pete ambacho juu yake kuna lile jiwe la urembo akasogeza sikioni na kuupata ule ujumbe sawia kabisa.
“Ujumbe umefika na unafanyiwa kazi,” akajibu huku akiwasha gari na kuondoka eneo lile akimwacha Yule jamaa kazubaa pale. Mijitu mingine bwana yaani inawaza mapenzi na ngono muda wote mpaka inasahau kazi, akajisemea moyoni na kusindikiza kwa sonyo refu, akaingia barabara ya Samora na kukunja kushoto akapotelea mitaani.
SHAMBA
NI WATU WANNE tu walikuwa wamekutana kwenye meza yao ya umbo la yai ambalo daima hukutana na kupanga mambo mazito yanayolikabili taifa. Wawili hawakuwepo, Kamanda Amata na Scoba hawa walikuwa kwenye misheni maalum za kiofisi kila mmoja na jukumu lake.
“Scoba nampata kwenye signal, lakini kamanda Amata haonekani kabisa,” Chiba alimweleza Madam S huku akiendelea kubofyabofya kompyuta kompyuta yake.
“Signal hamna kabisa kabisa yaani?” Madam S aliuliza huku kwa mbali akianza kupatwa na hofu.
“Oh, kamanda!” akajikuta akijisemea kwa sauti ya chini.
“Mpigie Scoba, anaweza kujua nini kinaendelea?” Madam akamwambia Chiba, naye kwa kutumia kifaa kilekile akabonya sehemu fulani kasha akabonya kinobu chenye namba 3 akainua mkonga wa simu uliopachikwa pembeni tu kompyuta hilo na kuuweka sikioni. Sekunde kama thelathini hivi zilipita.
“…TSA 2 nakupata!” Sauti ya Scoba ikasikika kupitia simu ile ya satellite ambayo Chiba alikuwa ameifunga ili isiweze kudakwa na watu na kusikiliza mazungumzo yao.
“TSA 3 nashindwa kumpata TSA 1 nipe ripoti…” akabonyeza kitufe Fulani na kusubiri kidogo kama sekunde tano hivi.
“TSA 1 yuko shimoni, najaribu kuwatafuta panya waliompeleka shimoni lakini naona wako undercover siwapati kabisa, nimefika pangoni mwake nimekuta mzimio wa mwanamke. Sasa nipo katikati ya jiji la Berlin najaribu kutafuta njia ya kujua liliko shimo hilo, roja!”
“Nimekupata, nitakuja kwako tena,” Chiba akamaliza na kukata ile simu.
Gina akashusha pumzi ndefu na kujiweka sawa kitini, macho yake yalianza kuonesha huzuni ya wazi, yakaanza kutona kwa machozi ya mbali. Madam S akamkazia macho makali, Gina akaelewa nini maana yake akatoa kitambaa mfukoni na na kujifuta.
“Hii kazi wewe, unatakiwa kuwa mwanamke wa chuma sio kitu kidogo kulialia tu” Madam S akamwambia Gina.
“Samahani,” akanyamaza na kuruhusu kikao kuendelea.
“Nimewaiteni hapa, najua wazi mnafahamu kilichotokea siku tano zilizopita pale Ikulu,”
“Ndiyo!” wote wakaitikia.
“Sasa basi tumepewa kazi ya kuingia kazini, kutafuta na kujua nani ni nani na First Lady apatikane ndani saa chache,” Madam S akaunguruma kikazi.
“Bila Amata?” Gina akalopoka.
“Kama amekufa je? Hujui kwamba wewe ndiyo upo katika kitengo chake? Tulikupeleka mafunzo miezi mitatu ulifikiri nini, safari hii we ndiyo unaanzia pale mpaka Kamanda atakapopatikana. Nimepanga hivi, Gina utakuwa mstari wa mbele kwa mapambano ya ana kwa ana itakapobidi, Chiba utabaki nafasi yako ileile ya uchunguzi wa kimtandao lakini nakuongezea utauchunga mkia wa Gina mara zote, Dr. Jasmine utabaki katika utabibu pale watu wanapopata majeraha lakini safari hii utachukua nafasi ya Scoba pia kwa uokoaji, usafiri na kadhalika. Mimi nashughulika na swalka la huko Ujerumani kwani kuna kazi nyeti ambayo Amata alienda kuifanya,” akamaliza.
Ukimya ukawa dhahiri shahiri kati ya watu hao, kila mmoja alitafakari kazi yake na jukumu alilopewa.
“Chiba uwe masterplan wa mchezo mzima, na tunaanza sasa kila mtu aingie kitengoni, na Mungu awatangulie. Gina mtu tunayemtaka akiwa na uhai wake ni Mke wa Rais tu hao wengine usiwape nafasi, shoot on the spot, uno trabajo!” akamaliza na kuondoka ndani ya chumba hicho kuelekea ofisini kwake huku akionekana wazi sura yake jinsi ilivyosawajika kwa habari ya Kamanda Amata. Gina alimkumbatia Jasmine wakaangusha machozi ya maana.
Kufanya kazi na wanawake shida tupu, sijui tutafanikiwa maana niko peke yangu, Chiba aliwaza huku akiwaangalia wale wananwake wanavyojililia kama wana msiba.
“Jasmine, naomba unipeleke Ikulu kazi yote lazima ianzie pale, kuna mambo ya kuchunguza tukiyamaliza pale ndipo tutapata jambo la pili,” Chiba alimwambia Jasmine. Wakaachana na Gina kila mmoja akajiweka sawa kwa kuchukua kifaa hiki na kile na kuvijaribu kama vinafanya kazi.
“Point of reference namba moja?” Jasmine akauliza.
“Chiba wa Chiba, kama kawaida,” Gina akajibu.
“Point of reference namba mbili,” akauliza tena
“Dr. Jasmine kwani muda mwingi utakuwa garini,” Gina akajibu.
Kutoka kwenye lile kabati lao la chuma, walipakua vifaa vya mawasiliano vya aina mbili wakimaanisha kuwa mawasiliano nya kwanza yatakuwa yakipitia kwa Chiba ndiyo ‘point of reference namba moja’ hayo yakishindwa kwa njia yoyote ile basi watatumia laini ya pili ambayo mtambio wake mdogo atakuwa nao Jasmine. Walipohakikisha sasa wako tayari wakapeana mikono na kukumbatiana kwa pamoja.
“Mama ni mgonjwa lazima asaidiwe, sisi ndiyo tiba haswa ya mama huyu, tutakieni mkono wa heri katika kazi,” Chiba aliwaambia kasha wakapeana mikono na kila mmoja akamalizia mambo yake machache.
5
MANNHEIM – UJERUMANI
KATIKA JUMBA MOJA KUBWA lililojulikana kama jumba la shetani kwa kuwa halionekani mtu kuingia wala kutoka, tukio hilo kwenye jumba hilo huwa ni kama kupatwa kwa jua. Ndani ya chumba kimoja kikubwa kilichooneka hakikumaliziwa kujengwa kwani chini hakikusakafiwa bali kilikuwa kimemwagiwa sementi iliyochanganyika na mawe, kuta zake nazo hazikuwa na rangi bali ni plasta iliyoachwa hivyo na makolokolo mengine mengi yalikuwa yamelundikana pembezoni mwa kuta hizo.
“Na utasema ni nani aliyekutuma kuja kuchunguza kazi za watu!” sauti nzito nene ya kikatili ilisikika ikiwa na mwangwi wa kutosha. Amata Ric akiwa juu ya kiti cha chuma kilichokuwa na tundu katikati. Alivuliwa nguo zote na kukalishwa hapo huku mikono yake ikiwa imefungwa kwa nyuma kwenye vyuma vya kiti hicho na miguu imefungwa kwa nyuma ya miguu ya mbele ya kiti kilekile. Damu zilikuwa zikimvuja maeneo mbalimbali ya mwili.
“Hautaki kujibu siyo? Kweli wewe jasusi sasa nakukata korodani zako ili ujue kwamba kufanya mapenzi na motto wangu lilikuwa kosa kubwa sana,” Jirack Paterson, alifungua kitu kama bakuli kubwa la chuma ndani yake kulikuwa na vifaa mbalimbali vya kutesea, kulikuwa na vifaa vya kukata ulimi, kubana korodani, pini za umeme na vingine vingi. Akachukua kifaa kama mkasi ambacho kwa mbele kilikuwa na meno yaliyokaa nusu duara kila upande, nyuma ya kifaa hicho kulikuwa na kijichuma kido kilichotokeza ambacho ukikibana yale meno kule mbele nayo yanabana na kupasua korodani.
“Aaaaa aaaa aa please, please!” Amata alilalamika alipokuwa akiletewa kile kifaa.
“Ah! Ah! Ah! Kumbe na wewe unalia, Ah! Ah! Ah!” Jirack akacheka sana kasha akamgeukia Bensoir.
“Nampasua korodani kisha, nakuachia kazi yako,” Jirack akamwambia Bensoir aliyeonekana kujawa na hasira kali. Kwa kasi akakipiga kiti kikaanguka chini kwa nguvu.
“Aaaaaaaiiighhh! Aaaaaaaah! Mnaniua jamani, mnajua mkiniua mimi mtapata tabu sana,” kamanda alipiga kelele huku akiwa chini na kiti kile. Jirack akakamata kile kifaa na kukiendea kile kiti kilichoanguka na Kurusu korodani za Amata kuwa huru upande huu wa chini ya kile kiti.
“Noooooooooooo! Nasema nasema nasema, aaaaaiiigh nasema!” Amata alilia baada ya kilekifaa kuanza kubana zile korodani.
“Sema haraka, nani bosi wako, serikali au kundi gani limekutuma?” Bensoir akabwata.
“Mimi sio jasusi, aaaaaaiiigghh! Koh! koh! koh!” akaeleza huku akilia.
“Sasa kwa nini umemuua kijana wangu?” Bensoir akahoji.
“Yule nimemuua kwa sababu aliniuzia almasi kutoka Mpumbutu, nika-nika- aaaaaaiiighhh, mnaniumiza…”
“Sema uka- ukanini?”
“Nikamhurumia dhidi ya mkono wako, ndiyo maana huyu nikamwacha, mi sio jasusi mi mfanyabiashara,” akjitetea.
“Kadanganye mbwa wewe sio mimi! We ni TSA namba 1 wa serikali ya Tanzania nani asiyejua, ninyi mmepeleka majeshi kule Ngoko dhidi ya waasi kukomesha biashara za wakubwa, na tunajua umekuja huku kujua mambo mengine mengi. Basi kabla hujayajua utakuwa umeshafika kuzimu, pumbavu wewe, waliokutuma wamekusaliti na wanajeshi wenu watano jana wameshauawa na sasa tunapeleka silaha mpya za kisasa na kuwafutilia mbali hilo jeshi la UN wakati ni la Tanzania…” Bensoir aliunguruma huku macho yamemtoka, akampiga Amata teke kali la kwenye korodani.
“Ah!” Amata alitoa ukulele huo mmoja na kunyamaza ghafla, akafinya macho yake na kasha akayalegeza, akawa kama anayetaka kuinama lakini alishindwa kutokana na kamba alizofungwa, akanyamaza kimya.
Kijana wa Bensoir akamwende pale chini na vijana wengine waliokuwa na silaha mabegani mwao, wakamgeuza na kufungua macho.
“Vipi?” Jirack akauliza.
“Naona amezimia huyu! Lile pigo lilikuwa kali sana. Mkuu tummalizie kwa risasi ya kichwa,” mmoja wa wale vijana wa kizungu alimwambi Jirack.
“Hapana, huyo bado, kuna siri nyingi sana anazo lazima azitaje zote kwa faida yetu na wenzetu, mtoeni hapo mwekeni kwenye kile chumba cha pili, mumlinde mpaka atakapoamka. Akiamka tu mniite kuna watu wengine wanakuja kuonana naye,” Jirack akawaambia wale vijana kasha yeye na Bensoir pamoja na Yule kijana wa Bensoir wakaondoka zao.
“Sasa huyu kijana wako mwingine tunafanyaje? Maana familia yake lazima itahitaji kumzika,” Jirack akamwambia Bensoir.
“Hana familia, Yule kisa cha kuingia jeshini ni kisasi familia yake ilichomwa moto ikiwa ndani usikuu wamelala, kwa hiyo tusubiri mambo haya yatakapotulia tutatuma watu kuja kuchukua mwili,” akajibu.
Saa mbili baadae Kanali Bensoir Banginyana, alikuwa uwanja wa ndege tayari kwa safari ya kurudi huku akiwa na hasira za kumpoteza kijana wake.
“Hakikisha Yule mshenzi anakufa,” alimwambia mmoja wa vijana wa Jirack kasha yeye akaondoka zake.
“Count on me!” yule jamaa akajibu.
Katika lile jumba ambamo Amata alilazwa kwenye kitanda cha chuma kisicho na godoro uchi wa mnyama huku akiwa kafungwa kwa pingu mikono kila mmoja upande wake na miguu vivyo hivyo, kulikuwamoi na vijana watatu wenye silaha, wawili mlangoni kwa nje na mwingine alikuwa ndani. Wote watatu walikuwa na shotgun zilizojaa risasi. Yule jamaa wa ndani akaangaza angaza na kuvuta nguo za Amata zilizokuwa juu ya meza shaghalabaghala. Hawa jamaa huwa wana vitu vya ajabu sana, ngoja nipekuwe nijipatie changu, akajisemea huku akipekua mifuko ya suruali ya Amata. Katika mmoja wa mfuko akatoa kitu kama saa lakini kisicho na mikanda, akakitazama na kukigeuza geuza, mh! Nini hiki? Akajiuliza. Katikati ya kidubwasha kile kulikuwa na kinobu chekundu, Yule bwege akakiangalia na kusogeza dole gumba lake tayari kwa kukibonyeza, mh! Kama bomu je! Akajiwazia. Haiwezi kuwa bomu hii ni saa hii, akabonyeza …..
na kushikilia kwa muda kuona nini kinatokea, hakuna kitu, akabaki kaduwaa. Sasa hiki kitu gani? Akajuliza, akakigeuzageuza tena huku na huku, na kukiweka juu ya meza ndogo.
‘Piiiip! Piiiip! Piiip!’ kile kidubwasha kilianza kutoa sauti kali iliyokuwa ikiumiza masikio, Yule mjinga mle ndani alijiziba masikio na kuanza kuhangaika, ile sauti kali ya kile kidubwasha ilikuwa ikimsumbua sana masikio, akaanza kugonga mlango. Wale vijana waliokuwa nje wakasikia kelele za ule mlango, wakafungua na kuingia wakamkuta mwenzao kajiziba masikio huku kakunja sura. Wale jamaa nao wakaanza kutaabika na ule mlio mkali sana lakini mlio ule ulikuwa haufiki mbali zaidi ya kile chumba. Kamanda Amata kutoka katika usingizi mzito alianza kuusikia ule mlio, akili yake ikarudi taratibu, akajitikisa mkono umefungwa, akatikisa miguu imefungwa, kwa mbali akaona wale jamaa wanavyohangaika. Mmoja wao akakinyanyua kile kidubwasha, na kujaribu kukizima, alipobonyeza katikati kikalipuka, moshi mzito wa kahawia ukatoka kwenye kile kidude na kuwafanya wale jamaa wasionane. Vikohozi vya dharula vilitokea huku na huko. Amata alihisi kitu kinamwangukia jirani yake, ukimya wa vikoozi ukatawala na ule moshi taratibu ukaanza kupungua. Pumbavu wakubwa nyie!
Akawatukana kimoyomoyo lakini bado alikuwa hawezi kujitoa pale kitandani, kutokana na alivyofungwa Amata alijinyanyua na kuketi huku akihisi kizunguzungu kwani ule moshi kama hujaujua sawasawa lazima usimie ila kama unaujua unachotakiwa ni kutompumua kwa nguvu na kutumia muda mwingi kubana pumzi. Akatazama wale jamaa wamelala pale chini huyu mmoja alikuwa jirani kabisa na yeye, akajipinda kwa tabu na kuung’ata mkanda wa bunduki kasha akaivuta taratabu kwa kutumia kinywa na meno yake akaukamata kwa mkono akausogeza kwa vidole, mpaka akaikamata ile shotgun, alipohakikisha ameishika vyema akajaribu kutafuta shabaha ya zile pingu za miguuni, lakini ilimuwia ngumu kutokana na nguvu ya mkono uliofungwa, alipohakikisha hapo yuko sawa bila kuhofia lolote, akafyatu na ile risasi haikufanya mzaha. Pingu ya mguu wa kulia ikatawanyika na kuuwacha mguu huo huru. Katika harakati zile mmoja wa wale jamaa akatikisika, akapiga chafya na kufumbua macho, alipoona hali aliyokuwa nayo akakurupuka na kusimama huku akiiweka sawa bunduki yake. Lakini kabla hajakaa sawa, Amata akiwa na ile bunduki mkononi kwa vidole vyake vitano akaikamata sawasawa.
“Tulia hivyo hivyo!” sauti hafifu isiyo na nguvu ya Amata ilimwamuru kijana huyo, naye akatulia, “Tupa bunduki yako kabla sijakumaliza,” akatupa. “Haya nifungue nitoke,” akamwamuru.
“Nikikufungua boss ataniua,”
“Atakuua vipi wakati ushatoroka, fungua!” akaongea kwa nguvu kidogo, Yule jamaa kwa kutetemeka akatoa funguo na kufungu pingu moja ya mkono wa pili kisha akafungua ya mguu uliobaki, Amata akanyosha mkono ule uliofunguliwa na kuchukua ile shotgun kutoka mkono wa pili, yule kijana akaufungua ule wa pili huku akitetemeka.
Simu ya Scoba aliyokuwa kaivaa mkononi na kuifunika na mkono wa suti yake ilitoa ukulele mdogo, haraka, akavuta ule mkono wa koti nyuma na kuitazama, juu ya kioo ilionesha tarakimu nyinginyingi kama kumi hivi, alipozisoma akaelewa kuwa hiyo ni namba ya kumtambulisha TSA 1 kwa njia ya satellite. Akabofya hapa na pale na kuiomba impe uelekeo, kwenye kile kioo ikatokea tufe la dunia likajizungusha na kuleta bara la Ulaya, ikajisogeza karibu na kulieta ramani ya Ujerumani, mji wa Mannheim, ikamwonesha na nmba Fulani za eneo lakini haikuonesha kama mtu huyo yupo hapo au alikuwa hapo. Kutokana na umbali wa hapo alipo mpaka huko Mannheim ilimpasa kama ni gari kuendesha kwa saa zizizopungua nne.
Shittt! Akang’aka huku akiondoa gari haraka pale alipo na kuelekea stesheni ya treni iendayo kasi. Dakika mbili tu alikuwa tayari stesheni na bahati akaikuta ndiyo inaingia, akaegesha gari haraka na kuteremka huku akifunga mlango nyuma yake. Bastola zake mbili zilikuwa tayari kwenye makwapa yake na visu vidoko kama kumi na tano alikuwa kavipanga kwenye ubavu huu na huu, akaiwahi ile treni na kuondoka.
“Unaelekea wapi?” mtu mmoja aliyevalia sare nadhifu alimwuliza, moja kwa moja Scoba akajua kuwa huyo ni mfanyakazi wa treni hiyo.
“Mannheim! Ni muda gani tutachukua?” akauliza.
“Dakika thelethini tu,” akajibiwa. Scuba akaketi huku akiitazama ile sa yake na wakati huo bado ilikuwa inaonesha kitu kilekile.
ITAENDELEA
Pasipoti ya Gaidi ‘The Return of Kamanda Amata’ Sehemu ya Tatu
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;