Pasipoti ya Gaidi ‘The Return of Kamanda Amata’ Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
Simulizi : Pasipoti ya Gaidi ‘The Return of Kamanda Amata’
Sehemu Ya Tatu (3)
Amata alinyanyuka ghafla na kumpiga ngumi moja nzito yule jamaa, akayumba na kujigonga vibaya ukutani, akapoteza fahamu kwa mara ya pili. Kutoka pale kitandani, akajiinua na kusimama wima, mwili wake ukiwa umechoka nab ado damu zilikuwa zimemganda huku na kule, akajinyoosha viungo na kujiweka sawa. Kutoka nje ya chumba hicho alikuwa akisikia watu wakitembea kuja sehemu hiyo, akaufunga mlango kwa ndani. Mara ukimya ukatawala, kisha hodi ikafuatia kugongwa baada ya hodi hiyo kutokuwa na mafanikio, Amata akajua kinachofuata, akajificha nyuma ya mlango, kitasa kikanyongwa na ule mlango ukafunguliwa ghafla, wale jamaa waliingia kwa kasi na kukuta wenzao wakiwa chini.
“Katoroka! Toa taarifa!” mmoja akamwambia mwenzake. Kutoka kwenye kona ya mlango, Amata alijitokeza, konde moja lililotua nyuma ya shingo ya huyu aliyempa mgongo lilimfanya ampamie mwenzake na wote wakaenda chini. Mmoja aliyekuwa juu akajigeuza na kujiinua kiufundi kabisa, lakini aliposimama tu alikutana na pigo linguine baya zaidi la karate lililotu kwenye kifua na kuufanya moyo ushindwe kufanya kazi sawasawa, akajibwaga chini kama mzigo, huku akiwa kakodoa macho. Yule mwingine akasimama wima na kutaka kukimbia, lakini hakuweza kwani ngwala aliyopigwa ilimpaisha juu na uso wake ukatua katika mpango.
“Mh!” akaguna, akajigeuza chali na kujiinua, teke la pili la Amata likadakwa, Yule jamaa akauzungusha ule mguu kwa minajiri ya kuuvunja lakini alikose sana kwani TSA 1 alifanya vitu vywake kwa kujiinua na kujizungusha kisha mguu wa pili ukatua kwenye shavu la Yule bwega akamwachi Amata kisha naye akaenda chini, na alipoanguka aliikamata redio call.
“…Ame-to-roka! Msaada tafadh…” kabla hajamaliza kusema alijikuta amekanyagwa shingoni.
“Bismark …. Bismark ….!” Ile redio ilikuwa inaita, Amata akainyanyua na kusikiliza wanachoongea, “Andre… mateka ametoroka paleka msaada haraka,” ile sauti kwenye redio ikawa inatoa taarifa upande mwingine. Kwa haraka, akamvua suruali kijana mmoja aliyeonekana kushahabiana naye kimwili akaivaa na nguo ya juu nayo akaivaa, akachukua ile shotgun na kuikamata mkono huu na nyingine mkono ule, akatoka ndani ya kile chumba, alipoangaza jicho akakutana na kamera ya usalama ikimtazama, akaifumua kwa risasi kisha akapita eneo lile na kujibana kwenye ngazi za kuelekea chini, akawaona wale jamaa wamefika na wananyata kuingia kwenye kile chumba.
“Hayupo! Kuna wenzetu tu, aiyaaaaa wamekufa!” sauti moja ilisikika ikisema. Kamanda Amata akacheka kimoyomoyo, akatazama zile ngazi hakujua zinaelekea wapi. Akazifuata akajionee hukohuko.
Dakika thelathini kama alivyoambiwa, ile treni ilisimama katika stesheni ya Mannheim, Scoba akashuka na kuingia mtaa kama wan ne hivi huko huegeshwa magari, pikipiki au baiskeli ambazo watu wamechoka kuzitumia na hapo husubiri kuchukuliwa kwenda kuyeyushwa na kutengeneza bidhaa nyingine. Akapepesa macho huku na kule akakutana na pikipiki kubwa limeegeshwa mahali hapo, akaliendea akajaribu kuliwasha halikuwaka, huku na kule aliona kituo cha mafuta, akalikokota mpaka pale akajaza lita kumi na kuliwasha likakaubali, akatua juu yake na kuondoka kwa kasi huku kila mtu akimtazama mwafrika huyo.
Jumba la Jirack Peterson lilionekana kwa mbali, Scoba alipoitazama ile GPS yake pale mkononi limuonesha kuwa yuko jirani zaidi, kutokana na eneo hilo kuwa wazi bila makazi na jumba pekee lililoonekana na ni hilo akajua hana budi kulikabili. Akapita na kuegesha pikipiki yake kwenye vichaka vya mizabibu, akalifuata kwa miguu kupitia mashambani. Ukuta wa jumba hilo ulikuwa na nyaya za umeme juu yake ambazo hutumika kuzuia wezi, aliutazama na kuuona unawezekana kabisa kupandika au kuuruka kama mtu una mazoezi ya kutosha ya kuruka viunzi. Scoba alijua kwa vyovyote vile akijaribu tendo hilo hajui anapotua kuna nini, akaambaa na ukuta mpaka mbele ya jingo hilo kulikuwa na geti kubwa na kamera mbili huku na huku, nimekamatika, akawaza. Hatua tatu akalifikia lango kuu na kubofya kengele bila woga, mlango mdogo ukafunguka, kijana mmoja akajitokeza lakini Scoba tayari alikuwa na bastola mkononi na kuingia ndani, ule mlango ukajifunga nyuma.
“Mtu wangu yuko wapi?” akauliza. Yule jamaa hakujibu akabaki katumbua macho, Scoba alimuona Yule jamaa akirudi nyuma na mkono wake kubonyeza swichi moja nyekundu, akajua kuwa swichi hiyo ni swichi ya hatari, alipotaka kumvamia ili kumpa kichapo, Yule jamaa alikuwa tayari kabonyeza ile swichi. Scuba akamtandika ngumi tatu na kumwacha chini hoi, akachuku bastola. Alipojitokeza, nje akakutana na vijana wawili wakija getini, Scoba akachomoa visu viwali na kuvirusha kwa ustadi kabisa, kila kimoja kikakwama kwenye kolomeo la mmoja, wakaanguka chini na kugalagala, bastola yake ikawatungua wengine waliokuwa juu nao wakajiachia hadi chini. Scoba akapita na kuingia mlango mdogo waliotokea wale jamaa.
“Weka mikono kichwani!” akamwamuru kijana aliyekuwa mbele yake. “Nipeleke alipo rafiki yangu, haraka!” Yule kijana akaanza kuongoza njia huku Scoba akifuata nyuma yake kwa tahadhari, wakateremka ngazi na kufika eneo linguine upande huo wa chini. Mbele yao walitokea vijana wawili wenye silaha.
“Nimetekwaaaa!” Yule bwege akapiga kelele huku akiwakimbilia wale wenzake lakini kabla hajawafikia alikula risasi ya mgongo iliyompaisha na kuwaangukia wenzake, Scoba hakufikiri mara mbili alitawanya risasi na kuwamwaga wale jamaa sakafuni.
Kamanda Amata alisikia mlio ule wa bastola, Beretta! Akajisemea moyoni mwake na jinsi risasi zile zilivyopigwa akajua kuwa huyo ni Scoba kwa maana wao walikuwa na mtindo wao wa kufyatua risasi endapo unapiga zidi ya mbili ili kufahamaina kwa haraka. Ukimya ukatawala jumba hilo, maiti kama kumi natano hivi zilikuwa katika vibarabara vya hilo jumba, Amata akajitokeza kwa tahadhari katika moja ya zile korido, na upande wa pili akajitokeza Scoba na bastola mkononi.
“Upige!” Amata akpiga kelele, na Scoba akauma meno na kushusha ile bastola chini, akatikisa kichwa. Amata akaongeza hatua mpaka kwa Scoba, wakakumbatiana na kupeana pole.
“Ilikuwa ngumu kutoka kwa kuwa sijui hata watu hawa wako wangapi na wapi njia ya kutokea, ahsante braza umekuja!” Amata akamwambia Scoba.
“Usijali, nilipata shida sana kutambua ulipo mpaka nilipopata signal ya smoke star, ndio nikaanza kukutafuta, nilikuwa Berlin,” Scoba akamwambia huku akianza kuondoka na Amata akimfuata.
Walipofika karibu na mlango wan je waliona geti likifunguka lenyewe na gari tatu nyeusi zikaingia, wakajificha mmoja upande huu na mwingine ule wa mlango.
Zile gari zikasimama, Peter Jirack akateremka, sura yake haikuwa ya furaha hata kidogo, na katika gari zingine walishuka vijana tofauti walikuwa na silaha nzito mikononi mwao wakalizunguka lile jumba huku watatu kati yao wakiongozana na Jirack kuingia ndani. Wakapita palepale pasi na kuwaona Amata na SCoba kutokana na haraka zao za kwenda kule kwenye chumba walichomfunga Amata. Huku nyuma wawili hawa wakatoka na kulivuka geti mpaka nje.
“Una usafiri?” Amata akauliza.
“Kuna pikpiki moja kuleee!” akamwonesha huku akielekea upande huo.
“Piga namba hizi tafadhali,” Amata alimwambia Scoba naye akazibonyeza zile namba kadiri alivyotajia kwenye ile simu yake pale mkononi.
“Hizi namba za nini?” akauliza.
“We ukimaliza bonyeza ok, hizo ni namba za mpenzi wangu,” Amata akajibu huku akikaa nyuma ya pikipiki lile na mbele akiwa Scoba tayari kukamatia usukani. Kwa mbali waliona gari mojawapo ikitoka pale getini. Scoba akabonyeza ok kwenye ile simu yake. Ni sekunde ileile mlipuko mkubwa ukatokea, lile jumba la Jirack likalipuka vibaya, ardhi ya eneo lile ikatetemeka kwa nukata kadhaa. Scoba akamtazama Amata.
“Ulitega bomu saa ngapi?”
“Usijali, hilo bomu lilikuwa kwenye viatu, tuondoke!”
Scoba akaliwasha lile pikipiki na kuondoka kwa kasi, alipopita mbele ya lile jumba lililokuwa likiendelea kuwaka moto, gari moja ilijitokeza kwenye ujia uliokuwa pembezoni na kuanza kuwafukuza.
“Scoba, tuna marafiki huku nyuma!”
“Wataisoma namba!” Scoba akajibu wakati akibadili gia na kuongeza mwendo wa pikipiki hilo kubwa linalotumia propeller shaft badala ya mnyororo. Akiwa barabarani alikuwa anayapita magari kwa mitindo ya ajabu huku ile gari nayo ikifuatia vivo hivyo. Risasi kutoka katika ile gari zilikuwa zikiwaandama lakini Scoba alihakikisha anawasumbua wale jamaa.
“Hauna silaha?” Amata akauliza kwa sauti kali kutokana na upepo uliokuwa ukiwasumbua.
“Kwe nye koti,” Aakajibu Scoba huku akililaza lile pikipiki na kuzipita gari kama tatu hivi kwa wakati mmoja na kusababisha ajali za hapa na pale. Amata akachomoa bastla kwenye koti la Scoba.
“Niletete niwamalize, wapumbavu hawa!” Amata aling’aka huku akijiweka sawia. Scoba alipofika mbele kabisa hakukuwa na magari mengi, ile ya wale wapumbavu ilikuwa inakaribia kabisa kuwafikia, akasopgeza pikipiki karibu na ukuta wa kutenganisha barabara, akaishtua ikanyanyuka na kupita juu ya kile kiukuta. Amata akageuka nyuma na kuiona ile gari ikifunga breki, akainua bastola yake na kufyatua risasi mfululizo, vioo vya gari hiyo vikatawanyika na moja ya risasi ikapata mdomo wa tanki ya mafuta. Moto ukalipuka, kile Kigali kikapaishwa juu na kutua chini huku kikisababisha ajali kubwa kwa magari mengine.
Scoba alitua barabara ya upande wa pili na lile pikipiki, walikuwa tayari kwenye daraja kubwa sana, na chini yake kulikuwa na mto mkubwa unapita.
“Scoba, acha pikipiki!” Kamanda akamwambia na Scoba akasimamisha hiyo pikipiki pembeni huku ving’ora vya polisi vikiwa vimewakaribia, wakakimbia na kupanda kingo za daraja kisha wakajirusha kuelekea majini. Polisi walikuja kasi na bunduki zao lakini walishuhudia tu maji yakitawanyika huku na huko.
IKULU – DAR ES SALAAM
NDANI YA JENGO HILO tukufu, jingo jeupe, Chiba alikuwa ameketi katika chumba maalum chenye luninga nyingi zinazopiga picha kila pembe ya nje na ndani ya jingo. Alijaribu kurudisha nyuma matukio ili aone nini hasa ilitukia siku hiyo, usiku wa manane. Picha zile zilimchanganya kidogo, zilikuwa zikionesha hali ya utulivu kabisa muda wote lakini ilipofika saa nane kama na dakika arobaini na tano hivi, kamera zote zikazimika na zile luninga zilionesha chenga chenga na dakika moja tu baadae ikarudi ile picha ya awali. Hakukuwa na wa kumuuliza kwani aliyekuwa zamu huko aliuawa usiku huo baada ya kiujaribu kuilinda kazi yake. Siku hii alikuwa na vijana wengine kabisa. Alirudiarudia ile picha ili kuitazama vizuri kisha akaipeleka mbele mpaka ilipoanza kufanya kazi sawasawa, akarudisha tena nyuma na kutazama pale ilipokuwa inasoma saa nane na dakika arobaini na tano. Aliangalia kamera moja baada ya nyingine, katika kamera ya upande wa baharini ndipo alipoona kitu kigeni kidogo. Palionekana bomba refu la maji taka lililoingia huko baharini, kisha akaona lile bomba linakuwa jeusi kutoka kule mwanzoni yaani ndani ya maji mpaka lilipoishia ambapo barabara ya lami alkatiza kabla ya kuufikia ukuta, akatikisa kichwa na kurudiosha tena picha hiyo, akaitazama kwa makini, hakika kwa mtu wa kawaida hasingeweza kugundua tofauti hiyo.
Akachukua kijitabu chake na kuandika vitu Fulani.
“Umegundua nini? Maana mi naona maruweruwe tu!” Gina akamwuliza Chiba
“Nitakupa tathmini baadae, lakini kwa sasa subiri kwanza,” Chiba akajibu kisha akahamia luninga nyingine na nyingine. Ilimchukua kama saa tatu hivi kukaa kwenye chumba hicho, akarekodi matukio yote ya siku hiyo aliyoyaona kwenye zile runinga na kuyahifadhi kwenye hard disc yake akaitia mkobani.
“Sasa twende nje ya uzio kuna kitu nataka kukiangalia,” akamwambia Gina, wakatoka pamoja na kuagana na Yule kijana aliyekuwa ndani ya ofisi ile. Nje ya uzio, upande wa baharini, usawa wa lile bomba, Chiba akasimama na kuutazama ule ukuta. Kutokana na weupe wa ule ukuta aligundua alama za kiatu zilizo hafifu. Mpandaji alikanyaga pale, akafikiri kisha akavuta hatua na kuuendea ule ukuta, akachukua kamera yake ndogo akapiga picha na kuhifadhi alama ile ya soli ya kiatu kisha wakarudi ndani.
Kwa upande wa ndani katika eneo sawa na lile ambalo ameona ile alama ya soli ya kiatu alikuta mchimbiko wa mtuo wa miguu ya mwanadamu, walitua hapa! Akawaza na kustikisa kichwa. Kutoka pale aliposimama Chiba aliinua uso juu na kuangalia kushoto na kulia na kuiona ile kamera ya jirani kabisa, akaomba msaada na kupanda pale juu kuitazama kwa makini.
“Gina!” akaita kutoka pale juu ya ule ukuta.
“Sema!” Gina akabetua kichwa chake na kutazama juu alipo Chiba ambaye alikuwa akiioneshea ile kamera kwa kidole chake, akatoa taarifa chumba cha mawasiliano kuwa anaizima kamera hiyo na kuiondoa kwa muda. Chiba alilifanya zoezi hilo na baadae akaweka kamera nyingine yeye akabaki na ile aliyoing’oa pale juu. Wakatoka na Gina mpaka chumba cha watu wa Usalama wa Taifa, pale akakutana na maofisa mbalimbali, wengi walikuwa wamemzidi umri, akaawamki na kuvuta siti moja kati yanyingi zilizokuwa hapo, Gina naye akafanya vilevile.
“Tunakusikiliza kijana maana tunajua utatupa lolote juu ya shida ‘etu,” mmoja wazee wale alivunja ukimya huo ghafla.
“Bado sina jibu la kuwapa, uchunguzi unaendelea, samahani nahitaji kuona maeneo yote yenye milango ya siri ya kutokea ndani ya jingo hili,” Chiba akaomba.
“Wewe umeambiwa, kila tafutishi yako utujulishe ofisi hii sasa unasemaje kuwa ‘uchunguzi unaendelea’?” mmoja aliyeonekana mzee kuliko wote lakini alikuwa na tambo kubwa hivi, alimkoromea Chiba.
“Naomba npatiwe msaada ninaoutaka na siyo kelele!” Chiba naye akawa mkali, wakati huo wote Gina alikuwa ametulia akiwasikiliza.
“Kijana nashindwa kujua ilikuwaje ukaajiriwa na kupewa kazi nyeti kama hii, maana kila unapoelekezwa huelekezeki, ningekuwa bosi wako ningekufaya auti,” Yule mzee aliongea huku amesimama na kuruhusu kuonekana ukubwa wa mwili wake.
“Ndiyo maana hukuwa bosi wangu, mbona wenzio wote wametulia na kuelewa kwa nini wewe usielewe?” Chiba akauliza, “Mtu yeyote anayehitaji na kung’ang’ania jibu la swali ujue jibu hilo analijua sasa anataka kuoanisha na la kwako. Nimekuweka alama we mzee,” Chiba akamaliza na kutoka huku Gina akimfuata.
“First Lady alichukuliwa kutokea chumbani mwake usiku huo, vitendo vyote vilifanyika kimya kimya kwa kuwa hatuna hata sauti iliyorekodiwa na mitambo yetu. Kwenye mitambo utasikia tu vitu vidogovidogo lakini si watu wakiongea,” Othman alikuwa akiwaeleza Chiba na Gina, baada ya maelezo marefu waliliridhika na kuondoka zao ndani ya jengo hilo jeupe.
OFISI NDOGO
NDANI YA ofisi ndogo ya Madam S, jopo la TSA lilikutana kujadili kile walichokiita uchunguzi wa awali. Madam S, Chiba, Jasmine na Gina walijifungia na kupanga awamu ya pili ya kazi yao.
“Hawa jamaa kwanza walikuwa na mavazi meusi, na waliivamia Ikulu kupitia upande wa baharini kwa kutambaa juu ya bomba la maji machafu ili kuhadaa wanausalama walio kazini. Kwenye ukuta wa upande huo nimekuta kitu hiki,” akawaonesha zile picha za ile soli ya kiatu.
“Chiba!” Madam S akaita kwa mshtuko.
“Nini Madam?”
“Endelea nitakwambia kitu,” akamruhusu.
“Sasa hawa wavamizi, naomba niwaite magaidi, walianza kazi yao kwa kuichokonoa hii kamera ya CCTV, waliilubuni hii kamera kitaalam kiasi kwamba ikazisimamisha kamera zote za upande huu kusafirisha still picture ya saa 8:45 usiku wa manane”.
“Sasa Chiba, hiyo kamera wameilubuni vipi, hapo umenichanganya asee ijapokuwa tulikuwa wote!” Gina aliuliza na wengine wakatikisa vichwa.
“Hizi ni tekniko za kiufundi jamani, sio kila kitu muelewe, kwa kifupi, aina hii ya CCTV tunayotumia pale Ikulu zinatumia kadi maalum kwa ajilki ya usafirishaji wa picha zake kwenda kwenye monitor, sasa hawa jamaa ina maana wanazijua hivyo wakabadilisha kadi, na kadi hiyo siyo rahisi kwa fundi wa kawaida kugundua. Hivyo ni vitu ambavyo sisi tunajifunza kwa sababu maalum,” Chiba akaeleza na wakati huo huo simu ya mezani kwa Madam S ikaunguruma, akawap ishara ya kunyamaza kisha akinyanyua na kuiweka sikioni.
“Hello!”
“…TSA1 online…”
“Copy! Endelea…” Madam S alijibu kwa furaha.
“…mwanaume bado anapumua, niko njiani kuja nyumbani, uno trabajo!” ile simu ikakatika.
“Kamanda Amata yuko njiani…!” akaliambia jopo na wote wakalipuka kwa furaha kushangilia taarifa hii.
“Kazi imekwisha, nilikuwa nawaza mimi, maana Madam ulinipa kazi nzito sana,” Gina akasema huku akienda kwenye jokofu na kuchukua mvinyo mlipuko, akaifungua na kuwapatia kila mmoja kwenye bilauri yake.
MAKAO MAKUU YA NCHI YA NDURUTA
KANALI BENSOIR BANGINYANA alikuwa katika kikao kifupi na rais wa nchi ya Nduruta au Mkuu wa wakuu kama alivyopenda kumwita. Kikao hiki kilifanyika mara tu baada ya kutoka Uwanja wa Ndege na kabla hajaenda Mpumbutu.
“Mkuu, kijana wangu ameuawa huko Ujerumani kama nilivyokutumia taarifa, na mtu aliyemuua ni huyu,” akampa picha ya Amata, Yule rais akaiangaliaa na kusonya.
“Huyu ni nani?”
“Anaitwa Amata Ric au kamanda Amata,” Bensoir akajibu. Yule Rais akafinya macho na kuibana pua yake kisha akaiweka miwani yake ya duara vizuri katika macho yake na kumtazama Banginyana huku akiichana ile picha na kuitumbukiza kwenye pango la kukokea moto.
“Nimeshamjua, huyu bwana ndiye tulimpendekeza kumaliza lile swala la kule Afrika Kusini, ndiye aliyemuua Sir Robinson Quebec,” akasimama na kulielekea dirisha.
Baada ya dakika kama tatu hivi alaimgeukia banginyana, “Sikiliza Banginyana, hii nchi ya Tanzania isijifanye ndiyo yenye nguvu katika ukanda wa Maziwa Makuu, tupo wenye nguvu na tutazidhihirisha muda si mrefu. Nasema hivi, huyu ajenti wao namuua…”
“Mkuu, mbona yupo mikononi mwa Jirack…”
“Eeeeeee, ishia hapo hapo!” akamsogelea, “Ametoroka, na lile jumba kule Manheim amelilipua lote, na sasa hajulikani alipo,” Rais Kadanse Sebutunva alimwambia Banginyana ambaye alionekana kushtuka maan hakujua kilichoendelea.
“Kanipigia simu Jirack na amesema yuko tayari kufadhili kila aina ya ufadhili ili huyo anayejiita Amata afutiliwe mbali katika uso wa dunia. Huko Ujerumani haonekani alipo na wanamsaka kila kona,” rais akaeleza, “Tuyaache hayo, silaha zitashushwa kesho Mpumbutu, uwe pale, hakikisha ndani ya siku nne umesafisha hicho kijeshi chao, hii operesheni nyingine niachie mimi nitakwambia mambo yanaendeleaje,” akamaliza na kuondoka kwenda zake ofisini kwake.
Kichwa kilimzunguka hakujua nini anatakiwa kufanya, huyu rais wa Tanzania hanijui mimi, sasa namtangazia vita, naamsha watu wangu wote niliowapachika waanze kumhujumu, kuanzia kwenye idara yake ya usalama mpaka Jeshi analolitegemea laity angejua kuwa kuna watu wangu asingeleta nyodo, sasa nammaliza, akawaza na kupiga ngumi mezani. Akainua simu na kuitisha kikao cha dharula cha vibaraka wake kutoka nchi jirani, na ni siku hiyohiyo usiku wa manane. Na wao kutokana na kutawaliwa bila wao kujijua walikutana usiku huo huo katika mji mkuu wa Nduruta na kufanya kikao hicho cha siri.
Akawasimulia kila jambo lililotukia huko ughaibuni na jinsi alivyokasirika na mipango aliyoamua.
“Huyu sio mwenzetu kabisa, unajua wao wana linchi likubwa lakini uchumi wao umedorola kila siku, mi nataka ile nchi iwe chini yangu,” akaeleza hisia zake.
“Iwe chini yako kivipi? Utaingiaje pale?” swahiba wake ambaye hupenda kuvaa pama mara nyingi aliuliza huku akigusagusa mustachi wake pale chini ya tundu za pua.
“Sikia sasa tutampa pigo la kwanza la kisaikolojia, hili ni pigo la kiuchumi, unajua nchi yangu, Ngoko na nyingine kama ile kule Lamawi zote tunategemea bandari kwake nah ii inamnufaisha sana…”
“Sasa unataka kufanyaje?” mjumbe aliyekuwa kimya muda wote akauliza.
“Nataka tujenge reli itakayotokea nchini kwako, ipite kwa huyu bwana ije mpaka hapa Nduruta kisha mizigo yetu yote itapita kwenye bandari yako hiyohiyo na kusafirishwa kwa reli mpaka hapa, kwisha habari…”
“Mi nilifikiri unataka tumvamie kijeshi,” Yule mwenye pama akasema.
“Hata kama ni kijeshi, hana kitu Yule, unajua mipango yake yote ya kiusalama ninayo hapa, silaha zake zote za kijeshi ninazo hapa, kila wanachofikiria juu yetu ninakijua kwa hiyo wala hanibabasihi, najua mpaka leo saa ngapi ataenda kuoga, sasa kazi inaanza, sikilizeni redio,” akamaliza akiwa anatokwa na jasho la pua.
“Mi nafikiri ili tuwe vizuri, kwanza ni kuanzisha umoja wa nchi hizi nne halafu yeye mwenyewe atajiona anatengwa mpaka hapo tayari atajua kuana jambo,” Yule mjumbe mkimya akatoa wazo lake na wote wakaliafiki, wakapanga kukutana baada ya wiki moja na vyombo vya habari vitangaze mkutano huo.
MSITU WA MPUMBUTU
JESHI LA TANZANIA lililokuwa chini ya mwamvuli wa UN lilisonga mbele ndani yam situ huo, walishangaa hakukuwa na upinzani wowote katika harakati hizo mpaka wamekaribia kabisa eneo wanalolihitaji, kwa mbaaaaali chini ya milima waliona kambi ya waasi iliyokjengwa kwa mahema mengi sana. George Kolongo, mtaalamu wa kusoma ramani wa jeshi hilo, aliigua karatasi yake kubwa na kuitazama akishirikiana na wenzake watatau.
“Hii ndiyo kambi kuu ya waasi, ndiyo ile paleeeee chini ya milima, ahalafu huku nyuma yam lima Busese ndipo kwenye machimbo ya almasi hadimu ya Mpumbutu inayosababisha haya yote” Kolongo aliwaambia wenzake.
“Sasa hawa tuwavamie kwa mtindo wa ‘mtu kati’, tuwazunguke kisha tukiteremka tunawamaliza,” Kapteni Ngauya alitoa wazo huku akionesha maeneo ya kuingilia kwa kutumia vidole vyake juu ya hiyo karatasi.
“Mshapata mbinu ya jinsi ya kuwavamia?” akauliza kiongozi wa vikosi vyote aliyekuwa mstari wa mbele ambaye kwa amri yake wangefanya vile alivyosema.
“Tayari, hapa ni kupiga ring attack kama mnavyojua ni mbinu yetu ambayo tumeitumia sana kwa hawa watu na tumeona matunda yake, tukishakuwa tayari tuna kamilisha kazi,” Yule kiongozi aliyekuwa na cheo kikubwa begani mwake aliwaambia vijana wake, kisha kwa kutumia kifaa chake cha mawasiliano alivipanga vikosi vyote kuzunguka ile himaya na wakati huo akiwatuma nyoka wake wateremke chini na kuingia kambini ili kupata habari mbili tatu kabla hawajaangusha timbwili ambalo wao waliliita ‘parapanda’.
“Kumbukeni tunaenda kusafisha waasi, naomba vikosi vyote tasa vipite kushoto na vile vya shufwa vipite kulia, wadunguaji pia mtatawanyika kwa mtindo huo huo lakini ninyi hamtashuka, bali mtabaki juu mita 500 ili kuua nguvu za waasi,” kisha akateua vikosi vitano vilivyoshiba na kuvipanga kudhibiti machimbo ya almasi kwani walishakubaliana kuwa baada ya kuiteka kambi ya waasi watoa taarifa ili majeshi zaidi yaje kukalia eneo hilo.
“Tunawachapa kwanza kuwatia adabu kisha ndiyo tunawaita hao wengine waje kudhibiti eneo,” akawaelekeaza na kila mmoja akachukua kona yake tayari kwa kazi. Mbinu ya kusogea eneo husika ilikuwa ni ileile ya kujificha na kutembea, mbinu hii iliwafanya wasionekane kabisa.
“Kila mtu awe na hasira na ndugu zetu watano waliokufa na wengine waliojeruhiwa ambao hatujui kama watapona au la,” Yule kiongozai aliwapa mori vijana wake na kuwaondoa woga kwa kutumia misemo mbalimbali ya kijeshi ambayo daima huwapa hamasa wapiganaji kufanya kazi yao.
Wapiganaji wale waliitikia wito wa kiongozi wao, wakaanza kuizunguka ile ngome kama walivyoelekezwa, ndani ya saa moja tayari walifanikisha zoezi hilo la kuizunguka ile ngome, wadunguaji walijiweka vizuri kwenye engo walizoona zinawafaa huku wakitupia macho yao katika lenzi zilizokuwa zikiwaonesha kwa ukaribu kabisa kila kitu kinachoendelea. Kila mdunguaji alikuwa na msaidizi mwenye darubini kubwa yenye nguvu ambaye alitoa maelekezo muda na nani wa kupiga. Nyoka waliopewa kazi ya kuingia kambini nao tayari kwa mwendo usio na papara kama ule wa nyoka waliteremka vilima hivyo huku wakipewa maelekezo wa pi pa kuingilia.
HOTEL NEW AFRIKA
JUA LA MAGAHARIBI lilikuwa likipotelea katika katika kona zake za jiji la Dar es salaam. Rangi nzuri ya dhahabu ilikuwa ikilipendezesha jiji hilo wakati gari moja land Cruizer nyeusi iliposimama mbele ya mlango mkubwa wa hoteli hiyo.
Hakuwa mzee aliyeshuka ndaniye bali kijana wa makamo tu, kadirio la miaka 35 hivi, ana mwili wa wastani na sura iliyoonekana haina usawa kwani ilikuwa na aina Fulani ya mabonde ya tabu na matataizo. Hakuwa mweusi wala hakuwa mweupe, huyu alikuwa wa rangi ya udongo lakini udongo uliopigishwa jua kwa nguvu na nyuma ya rangi hiyo basi kulikiuwa na rangi halisi ya mtu huyu mfupi ila aliyeonekana ana mazoezi ya mara kwa mara. Mashavu yake yalijaa kana kwamba anatafuna kitu lakini sivyo bali misuli ya mashavu yake ilikuwa ngangari.
Anaitwa Kubra Kaleb, aliufunga mlango nyuma yake na ile gari ikaondoka kisha yeye kwa hatua fupifupi lakini za haraka haraka akapotelea ndani ya hoteli hiyo, moja kwa moja mpaka kwenye lifti na kupanda mpaka ghorofa ya nane, akaingia kwenye chumba namba 806 na kumkuta mwenyeji wake, mtu mzima, Briston Kalangila.
“Kwema?” akauliza.
“Kwema kidogo, kuna sampuli inabidi kuondolewa sokoni haraka sana, mimi nina moja na Mkuu wa wakuu ana nyingine,” Briston Kalangila akamwambia huku akiketi chini na kufungua pombe kali ya Captain Morgan na kujimiminia kwenye bilauri kisha akaipunga hewani na kuinywa.
Kubra Kaleb naye akavuta kiti na kuketi juu yake, akachukua Coca cola na kuchanganya na Konyagi ya kiroba akainusa na kupiga funda moja.
“Malkia yupo salama?” Briston akauliza.
“Yupo salama anakula na kulala,” Kaleb akajibu.
“Good! Jamaa atasalenda tu, maana kwa sasa namwona yuko kimya sana,”
“Huyu ni jeuri sana, lakini hata wafanye nini hawawezi kugundua chochote, tulivyoingia wala tulivyotoka,” Kaleb akaeleza huku ile bilauri ikiwa bado mkononi mwake.
“Najua, najua kazi yenu, na hapa lazima wapate tabu,” Briston akaongeza.
“Mmemweka kulekule kilindini?”
“Ndiyo! Hakuna sehemu salama na isiyoweza kugundulika kirahisi kama ile”.
“Ah! Ah! Ah! Ah! Safi sana, Kubra Kaleb, Mkuu wa wakuu hakupoteza pesa yake,” Briston akacheka na kusifia.
“Sasa sikiliza, una vijana wangapi mafichoni?”
“Sita, na wote ni komandoo watoro”.
“Safi sana, tazama hii picha…” Briston akamwambia na kumwonesha picha mbili.
“Unamwona huyu?”
“Ndiyo!” kaleb akajibu.
“Huyu kijana leo asubuhi alikuwa anafanya uchunguzi wa kamera za usalama pale Ikulu, anaonekana mkorofi sana, mimi nataka ashughulikiwe mara moja,” Bristona akamwambia kisha akajikohoza wakati Kaleb akiinua ile picha na kutabasamu, “Na nyingine ni hii hapa,” akampa picha nyingine, “Hii imetumwa kwa email na Mkuu leo mchana, sikiliza kwa makini, huyu kijana na ni mtu hatari sana ni Mtanzania alikuwa Ujerumani akichunguza ni akina nani wanaoleta silaha kwa waasi…”
“Amefanikiwa…?”
“Ndiyo amefanikiwa, na amefanya uharibifu mkubwa kwenye ngome ya Yule tajiri, ameua mfuasi wa Banginyana katika ile casino kubwa pale Berlin, wanasema ana weledi mkubwa sana wa kupigana na kuwakwepa maadui. Ametoroka ndani ya ngome ile ngumu ya Jirack, huyu si wa kawaida. Mkuu anaitaka roho yake kabla hajaleta madhara kwani ni mwiba, anasema huyu akifika hapa anaweza kuharibu mpango wote,” Briston akamwambia Kaleb.
“Sawa! Kazi hiyo itafanyika leo hii, cha muhimu ni kumtafuta kujua yuko wapi,” Khaleb alieleza huku zile picha akizitia katika mfuko wake wa shati.
“Bado yuko Ujerumani, ila muda wowote atatua hapa Dar,” Briston akaleza huku akiendelea kupiga funda lingine na lingine kisha akaitua ile bilauri mezani.
“Kikao chetu kitakuwa hapahapa kila mara,” Briston akamaliza na kuagana na Khaleb.
“Sawa hakuna tabu, ila sasa lazima niweke watu pale uwanja wa ndege wa Dar ili akitua tu amalizwe, hafai kuishi. Unajua Briston kuna watu hawatakiwi kuishi duniani; wambea, wachawi, wezi, wanga na watu kama hawa, nakuhakikishia hatoikanyaga ardhi ya nchi yake akiwa hai, lazima wapokee mwiliwa marehemu,” akaitoa ile picha na kuichana vipande viwili kisha akaichoma kwa kiberiti chake cha gesi, na kuufungua mlango tayari kwa kuondoka.
“Khaleb! Be careful” Briston akamwambia kisha wakaagana kwa macho.
Khaleb akaiacha hoteli hiyo ya New Africa na kuingia katika gari hiyo, ndani ya gari aliifungua kompyuta yake na kuwasiliana na watu anaowajua yeye kuwa wanaweza kumsaidia kazi yake, akapekua hapa na pale na kumpata kijana mmoja anayemwamini sana ambaye kishawahi kumfanyia kazi ngumu na za haraka na akafanikiwa pasi na kushtukiwa na mtu yeyote au mamlaka husika. Baada ya kumpata mtu huyo, akawasiliana na vijana wengine wa huko Ujerumani kuhakikisha Amata ni ndege ya shirika gani anaondoka nayo, akawapa maagizo wasimdhuru bali wahakikishe usalama wake mpaka atakapoingia ndegeni.
HEIDELBERG – UJERUMANI
KAMANDA AMATA akiwa na Scoba waliwasili kwenye moja ya hoteli ndogo za jijini Heidelberg, mjia ambao haukuwa mbali kutoka Mannheim. Walifika katika jiji hilo baada ya hapa nap le kupanda katika magari ya wakulima watokao mashambani na kuwasili alfajiri ya siku iliyofuata.
“Sasa hapa tusipoteze muda, inabidi turudi Berlin ili nikachukue vifaa vyangu,” kamanda akamwambia Scoba wakati wakitembea kwa miguu na kukatiza viunga vya jiji hilo. Bado watu walikuwa hawajaamka lakini baadhi ya magari tayari yalikuwa barabarani kuelekea huku na kule, baridi ilikuwa kali miezi hiyo ya mwisho wa mwaka lakini Amata na Scoba waliivumilia huku wakijikunyata hapa na pale.
“Nafikir hapa patatufaa kwa dakika chache kabla hatujaliacha jiji hili maana lazima ubadilike Kamanda,” Scoba akamwambia huku akikata barabara moja kuelekea kwenye hoteli ndogo iliyo upande huo.
“Ndiyo Scoba, na inabidi tuanze kutafuta usafiri sasa wa kuondoka Berlin haraka,” kamanda akaisistiza.
“Usijali, niko hapa kwa ajili yako, lakini Berlini hapakufai kwa sasa maana hujui adui yako anakusubiri wapi,” Scoba akamwambia.
“Usijali wakati mwingine huna budi kujionesha kwa adui ili upate dondoo za kuendelea mbele,” akiwa katika kuzungumza hilo, tayari waliwasili katika moja ya hoteli ndogo za hapo Heidelberg, Hoteli Kohler. Moja kwa moja wakaingia na kufikia mapokezi ambapo walipokelewa na kuchukua vyumba viwili kwa kujibadili kidogo kimavazi. Scoba akauliza kama anaweza kupata huduma za manunuzi ya nguo na vitu kadhaa, wakampatia kitabu maalumu akajaza na kuingiaza namba za kadi zake za benki kisha Yule mwanadada akachukua ile kadini na kuichanja kwenye kimashine Fulani kisha akamrudishia na kumpa funguo ya chumba.
Scoba na Amata wakapanda ghorofa ya pili na kila mmoja akaingia katika chumba chake. Ndani ya chumba cha kila mmoja kulikuwa na kila kitu, vinywaji mashati ya kubadilisha. Amata alivuta hatua mpaka kwenye kabati na kufungu akakutana na suti pea nne za kisasa na za gharama, akachagua ile yenye namba inayomtosha na baada ya kujiswafi maliwato akaivaa nguo hiyo iliyomsitiri vizuri na kuonesha ushababi wake wazi wazi.
Nusu saa iliwatosha watu hao kujibadili kabisa na kuonekana wengine kutokana na utanashati wa mavazi hayo, wakatoka na kusaini kwenye vitabu kisha wakaondoka zao majira kama ya saa tatu asubuhi. Tax waliyokodi ikawafikisha katika stesheni ya treni iendayo kasi, wakakata tiketi ya kuelekea Berlini na dakika tano zilizofuatia walikua njiani kulikabili jiji hilo.
“Tutafika kwanza hotelini kwangu, na wewe ndiye utakwenda kunichukulia vitu vyote,” Kamanda alimwambia Scoba.
“Kamanda Amata, kila kitu nilishakihamisha, sasa hivi ni kufika na kunyanyua begi lilipo na kuondoka,” Scoba akajibu.
“Waoh, ulishafanya hilo?”
“Muda mrefu sana, nilipoona tu signal yako imepotea name nikafanya hilo,”
“Ulikuta nini chumbani kwangu?”
“Kwani we uliacha nini zaidi ya kukuru kakara zako tu?” Scoba akauliza.
“Nilimwacha msichana mrembo kalala kitandani,” Amata akajibu huku akiendelea kunywa kahawa katika chumba hicho walichoketi wao wawili tu huku wakiangalia madhali ya ya miji waipitayo kasi kuelekea Berlin. Wakiwa katikati ya maongezi, mlango wao ukagongwa na kisha kufunguliwa, vijana wawili waliovalia mavazi ya kiaskari lakini hawakuwa askari walijitokeza, hawakuongea chochote, waliwatazama tu kisha wakafunga ule mlango na kuondoka. Scoba na Amata wakatazamana kisha wakacheka bila kutoa sauti.
“Sikumkuta huyo mrembo,” Scoba alianzisha tena mazungumzo. Hapo Amata akili yake ikakimbia kwa kasi na kugundua kuwa Precious Nancy yuko hai, ndiyo maana Scoba hakumkuta chumbani alikomwacha amezimia.
“Vipi kaka mbona hivyo? Maana we nakujua damu ikishaanza kukuchemka unakuwaje…”
“Ni kweli Scoba, nilimwacha mrembo mmoja akiwa amezimia kitandani kabla mi sijatekwa na hawa majahili. Kama hujamkuta ina maana yuko hai na anaweza kuwa tatizo kwangu.”
Asubuhi ya saa tano waliwasili Berlini, wakajiweka sawa kwa kuteremka kwenye treni ile.
“Uko tayari?” Amata akauliza.
“Ndiyo!” Scoba akajibu kisha wakatoka ndani ya kile chumba. Amata akatazama huku na huku kisha akakunja kushoto na kuufuata mlango uliokuwa tayari umefunguka automatiki ukisubiri watu kushuka. Alitangulia Amata kukanyaga ardhi ya jiji hilo kwa mlango wa upande mmoja na Scoba akashuka kwa mlango wa upande wa pili. Kamanda Amata akaitazama saa yake na kurudihsa mkono chini, alipoinua kichwa kutazama upande wa pili wa treni hiyo ambapo aliweza kuona japo kwa nusu kutokana na ukubwa wa vioo, moyo wake ulipiga chogochemba kwani hakuamni kama anayemwona ni Precious. Kajuaje kama nitakuwa hapa sasa? Akajiuliza huku akihakikisha mwanamke huyo hapotei machoni pake. Akiwa katika mshangao huo akahisi kitu kikimpiga mgongoni.
“This way!” kikafuatiwa na sauti hiyo, alipogeuka akamwona Scoba kishapita hatua mbili tatu mbele, aliporudisha macho hakumuona Precious. Amata akamfuata Scoba mp[aka kwenye maegesho, hapo Scoba akaikuta ile gari imetulia kama alivyoiacha jana yake. Akaminya saa yake, ikawaka mwanga wa kijani tu.
“Usalama upo?” Kamanda akauliza.
“Upo!” wakaingia na kuketi kisha akawasha na kuliondoa eneo hilo.
UWANJA WA NDEGE WA TEGEL – BERLIN, UJERUMANI
SCOBA ALIEGESHA gari panapohusika, akateremka na kufungua buti, kila kitu kilikuwa salama wakateremsha mizigo tayari kwa kuondoka. Mbele yao ikapita gari moja BMW kwa kasi sana kisha ikasimama umbali wa kama mita ishirini na kurudi nyuma mpaka pale walipoa Scoba na Amata ikasimama, kioo kikataremka na uso mrembo wa Precious ukajitokeza, akamtazama Amata kisha akasonya.
“Wasalimie kuzimu!” akamwambia huku kioo kikipanda na ile gari ikiondoka. Scoba na Amata wakatazamana tena, kisha wakavuta mabegi yao kuelekea ndani ya uwanja huo.
Kubra Khaleb alivivutavuta vindevu vyake vichache huku akiiweka simu masikioni mwake tayari kuongea na mtu wa upande wa pili.
“Yes, anaondoka na ndege ya shirika la Qatar, atapitia Doha, hakikisha unapata usafiri na kumaliza kazi. Huyo mtu hatakiwi kuteremka akiwa hai bali mwili wake tu ili uzikwe na wengine,” akamaliza na kukata simu. Kisha akarudi na kuingia katika gari.
“Sikilizeni, baada ya saa saba, wewe na wewe mtakuja hapa uwanja wa ndege muhakikishe huyu mtu ameshuka akiwa marehemu na si vinginevyo,” akawaambia vijana wake huku ile gari ikiondolewa…
“Na vilevile kijana wetu atakuwa kava shati la maua maua mumpokee na kumleta hoteli ya New Africa,” akaongeza kusema wakati ile gari ikichanganya mwendo. Ukimya uliotawala ndani ya gari hiyo ulikatishwa na kelele ya simu ya Kubra, akainyakuwa na kuiweka sikioni.
“… sawa! Sawa kabisa, basi nategemea kazi itakuwa sawa,” akakata simu na kuwageukia watu wake, “Amepata…”
UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA
DOHA – QATAR
RAJAN KADAH aliwasili uwanja wandege wa Doha dakika arobaini na tano kabla ndege ile haijafika, akakamilisha taratibu zote za safari ikiwamo ukaguzi wa tiketi na hati yake ya kusafiria. Alipohakikisha kila kitu kipo sawa alisubiri safari hiyo huku moyo wake akiwa keishaupanga kwa kazi moja tu. Muda ulipofika ndege ile iliwasili Doha na abiri walitakiwa kubadili ndege baada ya nusu saa kwa safari za Dar es salaam na miji mingine mikubwa ya ulimwenguni. Kamanda Amata na Scoba waliteremka lakini kila mmoja alikuwa na hamsini zake kiasi kwamba ilikuwa ngumu kujua kuwa watu hao wako pamoja, kila mmoja kati yao alikuwa na simu mkononi na kupachika vifaa vya kusikilizia masikioni. Lakini kwa vifaa hivyo waliweza kuwasiliana kwa siri juu ya kile ambacho walikuwa wakikitilia shaka.
Kama kawaida ya Amata, nusu saa ya kusubiri kwake ni kubwa sana, akajipenyeza na kuibukia kwenye duka la vinywaji vikali ndani ya uwanja huo, akaagiza kile anachohitaji kutumia na kuketi katika moja ya viti vilivyopo hapo. Scoba aliendelea kuketi palepale kwenye viti na abriria wengine huku akiendelea kusikiliza muziki lakini pia jukumu la usalama lilikuwa palepale.
Scoba aligongana macho na kijana huyo wa Kihabeshi katika harakati zake za kutazama huku na kule, kutokana na utaalamu wake kama kachero wa kumsoma na kumtambua mhalifu, akili ya Scoba ilitua kwa kijana huyo umakini wake ukayasoma macho. TSA 4 akauona wazi uhalifu wa kijana huyo ndani ya mboni za macho yake mawili. Akampa ishara Amata ambaye bado alikuwa akipombeka pale kwenye kile kiduka. Amata alipopata taarifa hiyo ya kumhofia huyo kijana alihitaji kujiridhisha kama anaweza kuwa na madhara. Amevaa shati la dhambarau, akawaza huku akiteremka kutoka pale kitini maana tangazo tayari liliwataka kuingia ndegeni.
Rajan Kadah alikuwa akimwangalia Scoba kwa wizi, kisha mara kwa mara alikuwa akiangalia picha ndogo aliyonayao na kuona haifanani na mtu huyo, lakini kila alipopepesa macho kwa abiria wengine hakuona mtu ambaye haswa anamtaka. Akanyanyuka kutoka pale alipokuwapo, na kujiunga katika foleni ya kuingia katika mlango maalum ambao ungemfikisha katika ndege hiyo. Rajan akasubiri Scoba aende kwenye foleni hiyo na Scoba alilijua hilo, bila kufikiri akaenda zake na Yule kijana akaja nyuma yake. Muda huohuo, Amata aliwasili kwenye foleni na kusimama nyuma ya Rajan. Katika harakati za kuingia ndegeni kijana huyo akageuka nyuma na kukutana macho na Amata, mshtuko wa wazi uliyashika macho yake, Amata hakutetereka alimkazia macho yake na kisha wakaendelea kwenda.
Ndani ya ndege hiyo waliketi viti tofauti huku Rajan akiwa kiti cha nyuma ya Amata, Scoba yeye alikuwa kiti kama cha tatu lakini katika safu ya upande mwingine, hivyo aliweza kuwaona wote yaani Amata na Rajan. Ndege ilipokuwa angani, Rajan alionekana wazi kukosa utulivu, mara ajishike hapa mara pale ilimradi tu alikuwa hajui anapaswa kufanya nini. Dakika moja mbele Kamanda Amata aliinuka na kufuata ujia uliokuwa ukielekea nyuma ambako kulikuwa na huduma ya maliwato. Nyuma yake na Rajan aliinuka na kuelekea upande uleule, alipofika kwenye mlango wa choo kile akakuta kitasa kimejiandika ‘vacant’ ikimaanisha kuwa mlango huo haujafungwa au ndani yake hakuna mtu anayetumia choo hicho, akatulia kama sekunde tano hivi kisha akakamata kile kitasa na kukinyonga taratibu, alipohakikisha kuwa kimeshafayatuka akauvuta mlango na kuingia ghafla lakini hakukuwa na mtu, akabaki kapigwa na butwaa. Kaenda wapi mshenzi huyu? Akajiuliza huku akitazama juu na chini ndani ya kijichumba hicho, akasonya na kugeuka tayari kwa kutoka. Hamad, alipofika mlangoni alikutana uso kwa uso na yule anayemtafuta, Rajan alihisi ganzi mwili mzima, akamtazama Amata aliyesimama bila kuonesha hata tabasamu. Amata alivuta hatua kuingia ndani na kijana huyo alirudisha hatu kurudi ndani kisha Amata akaufunga mlango.
“Kwa nini unanifuata fuata?” akamwuliza.
“Wewe unajua kwa nini nakufuata, au unataka kujua aliyenituma?” Rajani akarudisha jibu ksha akapiga swali.
“Sina haja ya kumjua mpumbavu yeyote aliyekutuma kwa kuwa kama uliona anakutuma basi ujue amekuua,” Amata akamwambia kwa sauti ndogo.
“Never!, huwezi kunikua wewe mbwa mweusi. Inelekea hujawahi kukutana na Rajan Kadah! basi leo utabaki histori,” Rajan akamkazia macho Amata ambaye naye alikuwa amesimama bila kupepesa macho hata kidogo, “Kwanza utaniuaje?” Rajana akauliza.
“Kwanza nitakuvunja mfupa Clavicle, kisha nitakuuliza maswali mawili tu yenye vipengele na mwisho nitakuvunja shingo,” Amata akamwambia. Rajan akacheka sana aliposikia maneno hayo. Kamanda Amata alimtazama kijana huyo anayejigamba kuwa hawezi kuuawa na mbwa mweusi. Kwa kasi ya umeme, Kamanda Amata akapiga pigo moja kali la karate likatua begani karibu kidogo na shingo akavunja clavicle kisha kwa kichwa chake alimpiga Rajan naye akajibamiza ukutani na kuanguka chini akigugumia maumivu. Kamanda akamkanyaga shingoni kwa nguvu na kutazamana naye.
“Nani unamfanyia kazi?” akamwuliza lakini Rajan hakuweza kujibu, maumivu ya lile pigo kwa namna Fulani yalimpa wakati mgumu. Rajani kutoka pale alipo, aliinuka ghafla na mkono wake ukakamata korodani za Amata. Kwa pigo moja la nguvu Amata aliivunja shingo ya kijana huyo, naye akaanguka chini bila ubishi.
“Vipi?” Scoba aliuliza kutokea nyuma.
“Kwisha kazi!” Amata akajibu, huku akimpekua hapa na pale na kutoa vitu mbalimbali mfukoni mwa yule jamaa, miongoni mwa vitu hivyo kulikuwa na kadi za benki, hata ya kusafiria yaani pasipoti, simu na pesa tasilim. Kamanda hakuchukua pesa hizo alimwachia marehemunna yeye akachukua vinavyomhusu.
“Sasa hapa itakuwaje, si watagundua!” Scoba akamwambia Amata.
“Shauri zao!” akatoka na kuufunga mlango kisha akakwanyua kitasa na kukivunja ili iwe ngumu kwa mtu kutoka nje kuingia kisha akarudi katika kiti chake na kuketi.
Gina aliegesha gari uwanja wa ndege majira ya saa kumi na mbili jioni hivi, hakuteremka bali alifyatua kiti chake na kujilaza akiruhusu sauti ya muziki laini kuyapenya masikio yake, akiwa katika starehe hiyo akapitiwa na usingizi.
Nyuma yake ilikuja Land Cruiser moja na kuegeshwa katika mstari uleule lakini kati ya gari hiyo na ile ya Gina kulikuwa na nyingine kama nne hivi. Hisia za Gina akiwa usingizini zilifanya kazi, akafumbua macho taratibu na kuinuka huku akikiacha kiti bado kipo katika mtindo uleule wa kulala. Alipogeuka huku na huku akawaona wale jamaa wawili walioshiba wakiwa wanelekea kule uwanjani, akili yake ikamsihi atie umakini juu ya watu hao, naye akatii. Akateremka na kuifunga gari kisha akawafuata kwa nyuma huku akihakikisha kuwa silaha yake aliyo nayo iko tayari kwa kazi endapo italazimu.
Wale jamaa wakatafuta nafasi ambayo iliwawezesha kuona vyema kule ile ndege itakaposimama na kutoka hapoi wangeweza kuona kila anayeshuka, mikononi mwao walikuwa na picha ya Amata kuwa endapo akishuka hai basi wamfungie kazi.
Saa kumi na mbili kamili jioni, ile ndege ikawasili pale JNIA na kuchukua eneo lake la kuegesha, kisha ngazi kubwa kabisa ikasogezwa na kupachikwa mlangoni, dakika moja iliyofuata watu wakateremka na kuteremka lakini hakuoneka Yule mwenzao wala hawakumwona Amata. Wakati wale jamaa wakihamaki kutomwona mwenzao na Gina alihamaki kutomwona Amata wala Scoba.
Wale jamaa wakapiga simu kwa Khaleb na kumweleza hali halisi.
“Ina maana hakuwamo katika ndege?” wakaulizwa.
“Hatujui kwa sababu abiria ndiyo wameshaisha nay eye hatumwoni, wala huyu mjinga uliyetupa picha yake naye haonekani,” kiongozi wa operesheni hiyo akajibu.
“Fanyeni kila mnachoweza mhakikishe mnapata habari zote juu ya jambo hilo kabla hamjauacha huo uwanja, mgawane, mwingine apeleleze kujua kama Rajan alikuwamo na mwingine apeleleze kujua huyo Amata sijui Amanda yuko wapi kisha mnipe taarifa moja kwa moja, nasubiri”. Ile simu ikakatwa na wale jamaa wakabaki kutazamana wakiwa hawajui la kufanya.
***
“Scoba kwa vyovyote vile kuna watu wanaosubiri ujio wetu huko nje, sasa ili kuwaonesha kuwa huwa hatukamatwi kama jongoo tupitie huku…” akaonesha kwa mkono, “… ili tuwapumbaze,” Amata akamaliza kusema huku akiondoka na Scoba akimfuata. Wakapita mpaka vyumba vya nyuma kabisa ambako huko huwepo wale wahudumu wa ndege husika. Kamanda Amata alipita hapa na pale na kufika sehemu ambayo chini kulikuwa na kitu kama mfuniko, ulikaa vizuri kabisa lakini kulikuwa na mshikio ambao ungeweza kushika na kuufunua mfuniko huo. Akafanya hivyo na kuiona ngazi ndogo ikiwa imeelekea huko akateremka na kufuatiwa na Scoba kisha wakaufunga tena ule mfuniko.
Mara hiyo walijikuta wapo katika chumba kikubwa cha mizigo ambcho tayari kilikuwa wazi na zile gari maalum za mizigo zinazovuta vibehewa vingi viliwasili tayari kwa kazi hiyo. Mizigo ilikuwa imefungwa kwenye makasha maalum ili kurahisisha upakiaji na upakuaji, Amata akaingia kwenye oja ya makasha hayo alikadhalika na Chiba akafanya vivyo hivyo. Nusu dakika tu yale makasha yakaanza kuondolewa na na kupaliwa kwenye vile vitrela. Wakasubiri zile gari zifike mahala pazuri, walipohakikisha kufika eneo linalowafaa kila mmoja aliruka na kujificha nyuma ya mapipa ya lami yaliyokuwa yamepangwa eneo hilo kisha wote wakatulia kwanza kuangalia upepo unaendaje. Walipohakikisha usalama upo, wakajipeyeza na kuifikia seng’enge. Hakukuwa na watu eneo hilo, wakakwea kwenye nguzo na kutua nje kisha wakaambaa na uzio huo mpaka kwenye ukuta wa jengo. Moja kwa moja wakaelekea kwenye maegesho kulikokuwako magari kadhaa. TSA walikuwa na maeneo yao waliyoyateua kuegesha gari mara nyingi, Amata na Scoba walipofika eneo la kwanza, hawakuona gari yao lakini lile pili waliiona na moja kwa moja wakingia na kuketi ndani.
Gina aliingia ndani kabisa ya jingo la uwanja wa ndege, mahali ambapo abiria huchukua mizigo yao, hakumwona Amata wala Scoba, akilini mwake alijuwa tu kuwa vijana hao kwa vyovyote watakuwa wameshateremka isipokuwa wamepita njia nyingine. Alilielewa hilo, akatoka nje na kuwatazama walea jamaa aliokuwa akiwahisi vibaya tangu mwanzo, hakuwaona.
ITAENDELEA
Pasipoti ya Gaidi ‘The Return of Kamanda Amata’ Sehemu ya Nne
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;