Najisikia Kuua Tena Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA
Simulizi : Najisikia Kuua Tena
Sehemu ya Nne (4)
SAUTI hiyo ilimzindua Joram. Akamwacha muuaji huyo aliyelala kama mzoga na kumsogelea mtu huyo aliyekuwa akijaribu kuinuka ili ainue tena jisu na kummaliza adui yake. Joram hakuwa na haja ya kuambiwa kuwa mtu huyo ni Dismas Komba!
“Asante kwa kuokoa maisha yangu Bwana Dismas,” alimweleza haraka haraka. “Unadhani kwa nini walitaka kukuua?” aliuliza.
“Wamekwishaniua…Nakufa…” Komba aliendelea kulalamika.
“Wewe sio mmojawao?”
“Mimi ni adui yao mkubwa.”
“Wewe ni nani?”
“Huwezi kunifahamu. Kwa jina ni Joram Kiango.”
“Joram! Nakujua sana…” Komba alisema kwa juhudi kubwa. “Joram! Walinitesa sana…Laiti wangeniua…nilikuwa sina hali siku zote. Nikienda huku nakutana nao. Nikikaa hapa usiku wanafika na kuniadhibu kwa vitisho na mateso. Wameniua…” akaanza tena kulalamika.
Ingawa nuru ilikuwa hafifu, ikitoka katika mshumaa uliowekwa kwenye kona moja ya chumba, lakini ilitosha Joram kuona katika macho yake Dismas Komba kuwa uhai ulikuwa ukimtoka harakaharaka. Hakuwa na muda wa kuishi zaidi.
“Sema haraka,” Joram alimhimiza. “Dismas kwa nini walitaka kukuua?”
“Wameniua tayari… nakufa…”
“Kitu gani wanadai kutoka kwako?”
“Wa…wame…wa…” Komba akaishiwa na uwezo wa kuzungumza. Alichofanya ni kuinua mkono kwa udhaifu akiuelekeza katika pembe moja ya chumba. Joram aliufuata mkono huo na kuona unaelekea debe lililokuwa hapo. Akaliendea na kuchungulia.
Alilakiwa na harufu kali ya kinyesi cha haja kubwa na ndogo ambacho kilikuwepo ndani ya debe hilo. Akarudisha macho ya kutoelewa kwa Komba. Akaona kakazana kuelekeza kidole papohapo, akajitahidi kutamka neno ambalo halikutamkika. Joram akahisi kuwa lazima kama kuna chochote alikuwa kaficha haikuwepo nafasi ambayo isingeweza kufikiriwa zaidi ya hapo. Hivyo akazidi kupekuapekua kando ya debe.
Akaliinua. Chini yake akakuta bahasha iliyofurika karatasi. Akaitwaa na kumgeukia Komba. Alimwona akitabasamu kisha kuanguka kwa nyuma. Mara akaanza kutapatapa kwa maumivu pindi roho ikimtoka. Joram alikimbia na kujaribu kumshika, haikusaidia. Tayari, Komba alilala kwa utulivu katika usingizi usio na mwisho.
Joram hakuona lipi zaidi angeweza kulifanya kuokoa maisha ya mtu huyo. Akaiendea swichi ya taa ya umeme na kuiwasha, haikuwaka. Hivyo akaichomoa tochi yake yenye ukubwa wa kalamu na kuiwasha. Nuru ilitoka kumwezesha kusoma neno moja tu ambalo liliandikwa juu ya bahasha hiyo USIFUNGUE.
Joram hakumtii yeyote aliyeandika neno hilo, akaifungua na kutoa karatasi ndefu ambayo iliandikwa kwa mashine ya aina yake kwa lugha ya Kiingereza, maneno ambayo tafsiri yake ilisema:
…NI DHAHIRI KUWA NJAMA ZETU ZA KUCHANGIA HALI NGUMU YA KIUCHUMIAMBAYO ILIKUWA IKIIKABILI NCHI HII HAZIKULETA MATUNDA TULIYOYAHITAJI, YAANI KUWAFANYA WANANCHI WAENDE KINYUME NA UTARATIBU WAO NA KULETA GHASIA AMBAYO TUNGEINGILIA KATI NA KULETA UTAWALA WETU. NI WAZI KABISA KUWA WAMEWAELEWA VIONGOZI WAO NA WAKO NAO BEGA KWA BEGA KUJENGA UPYA UCHUMI WAO. BAADA YA MUDA MFUPI, NJAMA ZETU ZA KUCHANGIA HALI HII NGUMU ZITAJULIKANA.
NA HAPO WANANCHI WATAKAPOAMKA NA KUPATA MOYO MPYA AMBAO SI KWAMBA UTAWAFANYA WASHINDE VITA VYA KIUCHUMI TU BALI WATAENDELEA KUIAMINI NA KUITEGEMEA KABISA SIASA YA UJAMAA NA KUJITEGEMEA. HAPO NDOTO ZETU ZA KUUWEKA UTAWALA MIKONONI MWETU KATIKA NCHI HII ZITAKUWA ZIMEKWISHA.
NAAMINI INAFAHAMIKA WAZI KUWA, NCHI HII NI KAMA NURU AMBAYO AFRIKA NZIMA INAIFUATA. UKOMBOZI WA NCHI ZOTE ZA KUSINI AMBAZO ZILIKUWA HAZIJAPATA UHURU WAKE NA ZINAZOENDELEA KUUPATA UMETOKANA NA MSIMAMO WA NCHI HII.
BAYA ZAIDI NI UHURU WA KIUCHUMI AMBAO NCHI HII INAONGOZA MAPAMBANO. MARA ITAKAPOJIIMARISHA KIUCHUMI NCHI YA SIASA YA UJAMAA, NCHI ZOTE ZITAONA NURU NA KUIFUATA HILO LITALETA MUUNGANO WA AFRIKA. HATUTAKI MAMBO HAYO YATOKEE LEO WALA KESHO. INASIKITISHA KUWA PAMOJA NA HALI KUWA NGUMU YANAELEKEA KUTOKEA.
KWA HIYO UAMUZI ULIOFIKIWA NA TWAA, WADHAMINI WETU NI KUUCHUKUA UTAWALA HUU KIMABAVU. YATAFANYIKA MAPINDUZI YA SILAHA. HATUJALI KUMWAGIKA DAMU WALA MAAFA, MAADAMU TUMESHINDA. WATU TULIOWAANDAA HUKO JESHINI, KATIKA BARAZA LA MAWAZIRI, NDANI YA CHAMA, KATIKA MASHIRIKA YA UMMA NA VYUO VIKUU WATASAIDIA KUULAGHAI UMMA ILI UTUUNGE MKONO. VILEVILE WANANCHI WATAPAKWA MAFUTA KWA MGONGO WA CHUPA KWA KULETEWA VITU ADIMU KAMA SUKARI, SABUNI, MAFUTA, NGUO NA KADHALIKA. WATAAMBIWA KUWA HAYO NI MATUNDA YA UTAWALA MPYA.
WATAFURAHI. BAADA YA HAPO MAMBO YATABADILIKA. UBEPARI UTARUDI MTINDO MMOJA. HATAKUWEPO YEYOTE MWENYE AMRI YA KUUPINGA UTAWALA WETU.
MPAKA SASA MASHARTI BADO NI YALEYALE ; KUWAPA WADHAMINI KISIWA KIMOJA ILI WAFANYE KAMA KITUO CHAO CHA UTAFITI WA SILAHA. WANANCHI WOTE WATAHAMISHIWA HADI KISIWA KINGINE ILI KUWARUHUSU KUANZA BIASHARA ZOZOTE ZA KIUCHUMI BILA MASHARTI, KUWASHUKURU KUTEUA AU KUPENDEKEZA VIONGOZI WANAOWATAKA NA MENGINE YATAKAYOJITOKEZA.
KWA SASA BADO VIONGOZI NI WALEWALE AMBAO WALITAJWA KATIKA KIKAO KILICHOPITA;
TOP KOLOTO – RAIS WA NCHI
MOTO MATATA – MAKAMU WA RAIS
BOMBO MTORO – WAZIRI WA MAMBO YA NCHI ZA NJE
CHEMA CHITIME – WAZIRI WA HABARI
JOE KILEO – WAZIRI WA ULINZI.
WALIOSALIA WATATEULIWA KUTOKA KATIKA ORODHA YA WANACHAMA WETU WALIOKO KATIKA NAFASI KUBWA SERIKALINI.
Taarifa hii ni ya mwisho itakayofanyika kwa siri kubwa kiasi hiki. Wakati wowote katika wiki mbili zijazo mambo yatapamba moto. Watu wetu wataarifiwa kwa dharura ili kuanza mambo. Ndipo maji yatakatwa kwa siku kadhaa kuwalegeza wananchi, vyombo vya habari vitatoa habari za ajabuajabu zenye nia ya kuwachukiza wananchi dhidi ya Serikali yao, kisha siku hiyo umeme utakatika ghafla na mapambano kuanza. Itakuwa rahisi sana. Wachache watatiwa pingu, wachache watauawa na kutakapopambazuka utawala utakuwa mpya.
Joram alimaliza kuisoma karatasi hiyo huku akitetemeka kidogo. Haikuwa na mzaha hata chembe ingawa aliamini kuwa iliandikwa na watu wenye wazimu na tamaa ya madaraka ya uroho wa utajiri wa haraka haraka. Kama alivyokuwa amehisi kitambo, zilikuwepo njama kubwa zaidi ya ile iliyofikiriwa na polisi ya mwandishi aliyechanganyikiwa –Bazile – kupata kichaa na kuanza kuua ovyo. Mauaji hayo yalipangwa tu, yakitumia jina la Bazile ili yaendelee kufanyika kwa siri bila wahusika kuhisi lolote. Na kiini cha mauaji pengine kilikuwa hiki cha kuficha siri hii ambayo kwa namna moja au nyingine iliondokea kuifikia mikono ya watu wasiohusika.
Mara Joram akagutuka na kumsogelea yule adui aliyekuwa akipambana naye muda mfupi uliopita. Alikuwa amekumbuka kuwa sura yake haikuwa ngeni machoni mwake. Akainama na kummulika usoni kwa kurunzi lake. Naam, sura ilikuwa ile ile ambayo si yeye tu bali karibu kila mtu aliifahamu na kuiogopa. Sura ya mtu yuleyule ambaye alikuwa akihitajiwa sana na polisi. Yule mtunzi wa vitabu vya mauaji na ambaye aliondoka kuwa muuaji mkubwa; Bazile Ramadhani.
Ugunduzi huu ungeweza kuwafurahisha polisi, kwani mtu hatari sana alikuwa amenaswa. Lakini kwa Joram Kiango, kunaswa kwa Bazile hakungeweza kumpa furaha hata chembe: Taarifa ya njama za mapinduzi ilikuwa mfukoni ikimkodolea macho. Hakuona vipi Bazile aliweza kuingia katika kikundi hicho na vile aliondokea kuwa hodari kwa mauaji.
Kwa kweli alikuwa haamini kuwa muuaji ni Bazile. Na kama alikuwa huyo, kulingana na madai au ushahidi wa polisi hasa kwa kifo cha Kitenge yule mtoaji vitabu, basi Joram aliamini ni kifo hicho tu ambacho angeweza kukifanya. Vifo vingine alihisi kuwa ziko njama za mtu au watu wengine. Lakini leo kashuhudia mwenyewe, na anaye mkononi Bazile huyohuyo, muuaji, anaweza vipi kuendelea kukanusha? Akazidi kumtazama vizuri.
Akaingiza mikono yake mifukoni na kutoa silaha za kijasusi ambazo hutumiwa na majasusi wa hali ya juu sana. Vitu kama vikopo vyenye sumu za kulevya, vidonge viwezavyo kuua kwa muda mfupi sana, bastola ndogo, kitambulisho na kadhalika. Vyote hivyo Joram alivitia mfukoni mwake. Kisha akarudisha macho yake juu ya uso wa Bazile kwa mshangao.
Macho yake yalikuwa wazi yakimtazama kwa ujeuri na kutokujali. Hayakuwa macho ambayo Joram alimtegemea mwandishi huyo kuwa nayo. Akaupeleka mkono wake kuupapasa uso huo. Mara Joram akaangua kicheko. Alipoutoa tena mkono wake ulikuwa umeshikilia ngozi ya uso wa Bazile ambao uling’oka kwa taabu. Uliobaki badala ya uso huo ulikuwa uso mweupe wa mtu mwenye sura mbaya. Uso wa jasusi lenye moyo wa mnyama ambalo bila
shaka lilikuwa limekodiwa kufanya mauaji hayo.
“Kill me” lilimwamuru Joram jitu hilo.
“Who are you?” Joram alimuuliza.
“Just kill me.”
Joram akaokota tambara chafu na kulididimiza katika domo la jitu hilo ili lisiendelee kusema. Kisha akahakikisha kamba alizotumia kulifunga jitu hilo zilitosha. Akaongeza nyingine na kutoa kila kifaa mwilini mwa jitu hilo. Aliporidhika, alitoka chumbani na kuufunga mlango vizuri akiwa na hakika kuwa jasusi huyo asingepata mwanya wowote wa kutoroka.
Saa yake ilidai ni zaidi ya saa nane za usiku. Bado alikuwa na saa nne ili aendelee na harakati zake za kumaliza upelelezi huo.
Akaamua kusubiri papohapo akimlinda mateka wake. Alitumia funguo zake ‘malaya’ kuingia chumba cha pili ambako alikuta kitanda kizuri kikimsubiri. Akajilaza. Usingizi haukumjia. Akijua kwamba chumba cha pili kina muuaji hatari na maiti ya mtu, mawazo hayakuweza kutulia.
Zaidi, alishindwa kulala kwa jinsi fikara zilivyokuwa zikimpita kichwani juu ya barua hiyo ya siri aliyokuwa nayo. Alifahamu kagundua siri kubwa. Lakini bado alifahamu kuwa hajagundua lolote dhidi ya watu hao wanaokusudia kuichukua nchi. Ilikuwa wazo kuwa majina hayo yalikuwa bandia tu. Hakuwa na muda wa kujisumbua kumtesa mateka wake mzungu ili amwambie.
Kwani, kwa kadri anavyowafahamu majasusi hao, hawawezi kutamka lolote. Hata hivyo, Joram alijua lipo ambalo angefanya kesho ili kuweza kupata walao njia ambayo ingemwezesha kuwafahamu watu hao waliochoshwa na amani. Kiasi pia alijiuliza juu ya Bazile. Kama muuaji alikuwa akiutumia uso wake, yeye mwenyewe yuko wapi? Pengine naye kauawa na kuzikwa kwa siri?
Mapambazuko! Joram aliyasubiri kwa hamu kubwa mapambazuko ili apate majibu ya maswali hayo na mengi mengine.
KULIPOPAMBAZUKA, Joram aliwachungulia maiti na mateka na kuona wako katika hali ile ile ya usiku. Akawafungia tena na kuamua kuwaacha katika hali hiyo. “Maadam nyumba inaogopwa kuwa ina mkosi au majini, wanaweza kuendelea kukaa humu walau kwa saa sita bila kuonekana,” alijisemea akihifadhi vizuri vifaa vyake vyote alivyopata katika nyumba hiyo. Akakiendea kivuko ambako alikuwa miongoni kwa abiria wa kwanza. Upande wa pili alitembea kwa mguu hadi kituoni ambako alipanda basi lililompeleka uwanja wa ndege.
Wafanyakazi walikuwa ndio bado wanawasili na mabasi yao. Joram alitazama hadi alipomwona yule binti aliyempa orodha ya wasafiri wa ndege aliyoihitaji jana. Binti huyo alimtazama kwa macho ya kufahamiana na tabasamu.
“Mbona mapema hivyo?” alihoji.
“Kuna kitu nilisahau kuuliza jana,” Joram alihoji na kuongeza,
“Tafadhali jaribu kukumbuka kama uliona tukio lolote la ajabu au ambalo halikuwa na kawaida siku ile?”
“Ipi?”
“Ile waliposafiri watu hawa,” akamwonyesha orodha ya majina yao.
Msichana huyo alijaribu kuwaza sana. mara akakumbuka jambo.
“Nakumbuka yuko mzee mmoja kati yao ambaye alitujia katoa macho pima na kudai kuwa begi lake limeibwa, mikononi alikuwa na begi lingine aina ileile ya suitcase. Tulipomuuliza hiyo kapata wapi alisema ameikuta badala yake. Tukamwelekeza kwenda chumba ambacho begi hilo lingeweza kufunguliwa ili ijulikane nani mwenyewe. Alienda huko. Aliporudi huko alikuwa akicheka na kutuambia kuwa begi lilikuwa lake isipokuwa lilikwaruzwa kidogo ndipo akalisahau.”
“Unamfahamu mtu huyo?”
“Sana. huwa anasafiri mara kwa mara. Jina lake ni Kwame. Nasikia ana kampuni yake binafsi.”
Joram hakuweza kujizuia kuonyesha furaha aliyoipata baada ya kusikia hayo. Tayari alikuwa na shilingi mia mbili mfukoni akimpa binti huyo huku akisema, “Umenisaidia sana mpenzi.”
“Sioni nimekusaidia vipi.”
“Utaona baadaye,” Joram alisema akiondoka kuendea teksi zilizosimama kando yao zikiwasubiri abiria.
Hisia zake za awali juu ya kuhusika kwa Kwame kwa njia fulani katika njama hizi sasa zilikuwa zimethibitika. Kupotelewa na mfuko, Joram alifahamu ni jambo lililotokea. Pengine marehemu Komba aliuchukua mfuko huo kwa kukosea, pengine alikusudia. Kwame bada ya kugundua hayo, akijua kuwa kuna siri kubwa ambayo hakupenda ijulikane, alichanganyikiwa na kuwapigia kelele wahudumu.
Lakini baada ya kufikiri zaidi ndipo alibuni uongo kwa kudai kuwa mfuko ni wake kwa matumaini ya kumfahamu mwenye mfuko huo kwa kusoma hati ambazo zingekuwepo ndani ya mfuko huo.
Ni njia hiyo iliyomwezesha kumpata marehemu Komba. Pengine, hata kuchelewa kumuua kulitokana na hofu yao ya kutojua iliko barua ile ya siri. Naye Komba yaelekea alikuwa mgumu wa kuitoa kwa kufahamu kuwa mara waipatapo, wasingesita kummaliza.
Wakati wakiwaza hayo, Joram alikuwa ndani ya gari akielekea mjini. Teksi ilimfikisha nyumbani kwake ambako alioga vizuri, akavaa mavazi yaliyomstahili na kuweka mifukoni vitu alivyovihitaji, kisha alitoka kwenda ofisini.
Neema alimlaki na maswali mengi. Joram alijibu machache tu akimwahidi kuwa baada ya saa chache atajibu yote. Kisha, aliandika kadi moja ya ‘express’ na kumwomba Neema aipeleke Posta. Aliporudi, Joram alimpa maelekezo mengine ambayo yalimfanya Neema atoe macho kwa shauku na tamaa akijua kuwa mambo yameanza.
Joram aliitazama saa yake, kisha akajistarehesha juu ya meza akisoma gazeti la Daily News ambalo lilikuwa na habari za kuchekesha chini ya kichwa cha habari: BAZILE MUUAJI HATARI YU HAI BADO
Joram aliisoma habari iliyofuata kama hadithi kisha akalitupa juu ya meza na kuendelea kusubiri, sigara zikiungua mdomoni mwake moja baada ya nyingine.
Kwame, kwa mara ya kwanza tangu alipoanza harakati zake alijikuta katika hali ya wasiwasi na mashaka makubwa. Kwa mbali, moyoni mwake, hofu ilikuwa iitishia kuutawala hasa kwa hisia zilizokuwa zikimnong’oneza kuwa mambo yameanza kumwendea mrama. Rohoni alipata wazo lililomshawishi kutoroka nchini mara moja, aende kokote duniani ambapo angeishi kwa starehe akitumia utajiri wake mkubwa. Wazo hilo alilipinga kwa kujikumbusha mara kadhaa kuwa hiyo dalili ya uoga wa kike.
Mashaka hayo yalikuwa yamemnyima usingizi usiku kucha tangu alipoarifiwa kuwa Joram Kiango alikuwa ametoweka baada ya kumshambulia mmoja kati ya watu aliowaamini waliokabidhiwa jukumu la kumlinda. Ingawa alikuwa na uhakikia kuwa Joram bado alikuwa hajui lolote la haja, lakini alimshakia sana hasa kwa kujua kuwa, iwapo angefika Kigamboni na kumsikia Komba angeweza kugundua mengi ya hatari. Kwa hofu hiyo, baada ya Joram kutoweka, ndipo akaamua Komba auawe mara moja bila kujali tena kupatikana kwa zile nyaraka za siri ambazo Komba alizipata kwa ajali na kuzing’ang’ania kama roho yake.
Mtu aliyetumwa kuua, Kaburu Vosgan Bon alikuwa mtu mwenye hakika na kazi yake. Kwame hakuwa na shaka naye, hasa kwa kukumbuka alivyokwisha fanya mauaji yote kwa ukamilifu chini ya kivuli cha yule kijana mtunzi, Bazile Ramadhani, kiasi cha polisi na taifa zimakuendelea kuamini kuwa muuaji si mwingine zaidi ya kijana huyo.
Hata hivyo, hofu ilianza kumshika baada ya kuona mapambazuko yakifika kabla ya kupewa taarifa juu ya kazi hiyo.Pengine alifanya makosa kuondoa makachero wote waliokuwa wakimlinda Kombaili Bon afanye kazi yake vyema? Yawezekana Bon amekwama kwa njia moja au nyingine? Hata hivyo, alifarijik kidogo baada ya kukumbuka kuwa pantone hufungwa saa fulani za usiku hadi alfajiri ya siku ya pili, hivyo yangewezekana baada ya kuua, Bon ameshin dwa kuvuka na angetokea kama kawaida kesho yake. Yawezekana? Bon ni mtu wa kushindwa kupata ngalawa au hata kuogelea hata alale mahala penye hatari kiasi hicho?
Ni hayo yalimtia Kwame mashaka, ingawa alipotoka asubuhi na kwenda kzini kwake alikuwa katika hali ya kawaida. Aliwasalimu wafanyakazi wengine na kumpita katibu wake mahsusi hadi ofisini mwake ambamo aliketi juu ya kiti akijiuliza lipi afanye katika hali kama hiyo. Kabla hajajua la kufanya katibu wake alimjia akiwa na barua mkononi yenye bahasha iliyobandikwa kijikaratasi cha ‘express’ yaani haraka. Aliipokea kwa mashaka na kuitazama kwa makini kabla hajagundua kuwa bahasha hiyo ni ile ile ambayo ilikuwa imehifadhi nyaraka za siri alizokuwa akizitafuta sana kutoka kwa Komba.
“Umeipata wapi hii?” alihoji hafla alipoikumbuka bahasha hiyo.
“Imeletwa na mtu wa posta asubuhi hii hii.”
“Vizuri unaweza kwenda.”
Binti huyo malipoondoka Kwame aliifungua haraka haraka na kutoa kadi ambayo iliyavuta macho yake kwa hofu kubwa .ilikuwa imeandikwa:
Bwana Kwame, nadhani bado una ndoto za kuendelea na mipango yako michafu ya kuleta maafa katika nchi hii. Kama bado unayo, nakushauri uiache tangu dakika hii. Nimekwisha kufahamu wewe pamoja na wenzako wote. Ninachokushauri ni nyie wenyewe kujitoa serikalini na kuomba radhi. Iwapo itafika saa sita kabla hamjafanya hivyo nitachukua hatua mabzo zitakuonyesha kuwa sina mzaha hata chembe.
Kwame alisoma mara kadhaa kabla hajayaamini macho.Alipojikuta akiwajibika kuyaamini, alijisikia akitetemeka ghafla. Hakuwa na uwezo wa kueendelea kukanusha kuwa tayari siri imemfikia mtu hatari kama Joram. Hakujua ilitokea vipi hadi siri hiyo akaipata. Wala hakuwa na nafasi ya kujua hayo kwa sasa. Alichotaka sasa ni kupata ufumbuzi kabla ya saa sita, awe amemfanya Joram marehemu, siri irudi katika milki ya siri na harakati ziendelee kama zilivyopangwa.
Hilo halikuwa jukumu rahisi.
Hivyo aliinua simu na kuwapigia washirika wake ili kuwatane hapo ofisini haraka iwezekanavyo. Simu ya pili iliwaamuru wasaidizi wake wa idara ya mauaji wahakikishe kabla ya saa sita za mchanawawe wamempata Joram Kiango na kumuua. Alisistiza kuwa kazi hiyo lazima ifanyike haraka, mahala popote na kwa njia yoyote.
Baada ya simu hizo, alitulia kwa muda akiwaza wa uchungu uwezekeano wa kufa kwa Jorm bila ya kuwepo kwa muuaji aliyekubuhu-Bon, ambaye hadi sasa hakujulikana aliko. Yaweza kuwa amekamatwa na kuuawa na Joram? Alijiuliza. Pengine…
Mlango wake wa siri sakafuni ukatoa alama ya kudai kufunguliwa. Akabonyeza kidude ambacho kiliufungua. Mtu mmoja akapanda ngazi na kuingia chumbani. Wakasalimiana kimya kimya. Baada ya muda walifuata watu wengine kwa njia hiyo hiyo. Nyuso zao zilionyesha wasiwasi, hivyo walisalimiana bila uchangamfu wowote, huku kila mmoja akiketi juu ya kimojawapo ya viti vilivyomzunguka Kwame. Walipokamilika Kwame alimtahadharisha katibu wake kuwa asingependa kusumbuliwa na mtu yeyote. Kisha akawatazama wageni wake kwa macho yaliyoonyesha kuchanganyikiwa, hajui wapi aanzie kueleza.
“Nadhani tulikubaliana kuwa tusikutane tena katika hali kama hii hadi mambo yatakapoonyesha kuwa nchi iko mikononi mwetu,” mmoja kati ya wageni hao alisema alipoona Kwame ameduwaa. Kwa hali hiyo nadhani Bwana Kwame angetueleza haraka kisa cha mwito huu ili tuondoke hapa.”
Wenzake wakatikisa vichwa kumuunga mkono.
“Ni juu ya waraka huu,” Kwame alisema akiwapa ile kadi. Waliisoma na kisha kutazamana kwa hofu kubwa.
“Nilisema zamani kuwa singewezekana…” mmoja alisema ghafla.
“Hata mimi,” alidakia mwingine.
“Kwa hiyo?” mwingine akaropoka.
“Tusubiri kitanzi,” jibu lilitolewa.
Yakafuata mengi. Kila mmoja akisema hili na lile. Hawa wakifokeana, huyu akilalamika, yule akjilaumu na kadhalika. Kisha Kwame alifanikiwa kuwanyamazisha kwa kusema, “Jamani, tusiwe kama watoto. Nimekuiteni ili tupate jawabu la pamoja. Joram ni mtu mmoja tu, kijana mdogo sana, ambaye hwei kushinda kundi hili pamoja na jeshi letu la siri lililojengeka. Kisha kafanya ujinga wa kutuarifu kwanza na kutupa muda wa kutosha. Bado tuna saa mbili. Zinatosha kabisa kumpata Joram na kumweka kaburini.
“Labda humfahamu Joram, bwana Kwame,” alidakia mwingine..
“Mimi namjua vizuri sana. ni kijana mdogo lakini anajua anachokifanya. Tusijidanganye…”
Kwame akamkatiza kwa hasira. “Uoga siyo dawa,” aliongeza,” sisi ni wanaume. Tunajua kabisa tusingeweza kutegemea utajiri mkubwa na vyeo vinono bila kutaabika kidogo. Bsuala la Joram ni tatizo dogo tu kati ya mengi yawezayo kutokea. Nilichotaka kupendekeza ni kuharakisha mambo yetu. Leo hii tukamilishe mipango, usiku mapinduzi yatokee, kesho sisi tulio hapa tuwe baraza lipya la mawaziri. Mnasemaje?”
“Joram jee?” alihoji mtu.
“Suala lake niachieni mimi. Hadi saa sita atakuwa safarini akielekea walikohamia babu zake. La muhimu ni sisi wenyewe. Tukubaliane moja. Tukitoka hapa kila mmoja akafanye jukumu lake haraka. Mnasemaje jamani? Angalieni hii ni nafasi yetu ya pekee ya kula nchi.”
Kabla hajajibiwa simu kutoka kwa katibu wake ilimfikia Kwame. Alii9nua chombo cha kusikilizia na kuunguruma ndani yake, “Nimesem sitaki usumbufu. Una nini kichwani wewe msichana?”
“Kumradhi mzee. Kuna mtu mwenye haja kubwa kukuona. Anasema jina lake ni Von.”
“Nani? Von! Mwambie aingie mara moja.”
Macho yake yalielekea mlangoni kumsubiri mgeni huyo. Aliingia taratibu bila haraka yoyote mikono mifukoni, macho yake yakimtazma kila mgeni kabla hayajamrudia Kwame ambaye kama wenzake wote alikuwa katika hali ya mshangao na mashaka mashaka. Mashaka ambayo yalitokana hasa na mgeni huyo kuwa katika sura ya Bazile Ramadhani, mtu ambaye alisadikiwa kuwa yu muuaji na aliyekuwa akitafutwa sana na kila mtu.
“Bon!” Kwame alifoka kwa Kiingereza. “Unawezaje kutebea hadharani mchana huu katika sura hiyo?”
“Usijali, siyo rahisi kujulikana.”
Sauti yake ilizidi kumtia Kwame mashaka. “Bon?” aliuliza tena.
“Ni wewe Bon! Ulikuwa wapi muda wote huu?”
Akajibiwa kwa tabasamu. Mikono ikatolewa mfukoni na kuelekea mdomoni ikiwa na sigara. Ilikuwa mikono ya mtu mweusi.
“Wewe sio Bon!” Kwame alifoka ghafla.
“Ndiyo.”
“Wewe ni nani?”
“Unataka kujua mimi ni nani? Ni rafiki yako mpenzi.
“Labda nitoe dude hili usoni unione vizuri.” Dude lilipotolewa kiufundi uso uliotulia mbele yao ukitabasamu ulikuwa wa Joram Kiango.
“Joram!” wote waliropoka kwa hofu na mshangao.
“Ndiye,” aliwajibu kwa dhihaka.
“Joram,” Kwame alifoka tena. Very well. Umejileta mwenyewe. Hutatoka humu ukiwa hai.”
Joram hakuonyesha kushtushwa na vitisho vya Kwame. Aliendelea kuivuta sigara yake, huku akiwatazama kwa makini. Nadhani tufahamiane vizuri ndugu zangu. Sipendi sana tabia ya kutumia majina ya bandia. Nani kati yenu anayejiita Top Koloto?” aliwahoji.
Alimuona mmoja akigutuka na wawili kumtazama mwezi wao jambo ambalo lilimfanya Joram amfahamu mara moja.
“Na Moto Matata?”
Wakazidi kugutuka. Joram akaangua kicheko. “Sikieni waheshimiwa,” akasema. “Hasa mheshimiwa Joe Kileo ambaye naamini u kiongozi wa kikundi hiki,” alikuwa akimtazama Kwame.
“Najua hii ni jumuia ya watu wenye njaa kali ya utajiri na kiu kubwa ya vyeo. Najua nyote hamtosheki na mlichonacho na kamwe hamtatosheka na lolote mtakalopata. Wengi wenu mmebahatika kuwemo katika madaraka makubwa, lakini hii ndiyo zwadi ya kwanza toka kwenu kwa nchi na wananchi; kupanga njama ambazo zimedhamiria kuleta umwagaji wa damu na kisha nchi iangukie mikononi mwenu. Iwe kama shamba lenu, wananchi wote wakiwa watumwa badala ya watu huru katika nchi huru. Waheshimiwa,” alipunguza hasira kutoka katika hali ya hasira na na kuwa ya huruma zaidi.
“Hamwoni aibu kwa uchafu wa vitendo vyenu?”
Hutuba yake ilikuwa imewafanya wote waduwae.walipopata nafasi ya kujikumbuka baada ya kuulizwa swali hilo, walitazamana kwa kutojua la kujibu. Kisha Kwame akafoka ghafla.
“Tusibabaishwe. Tusibabaishwe na kijana huyu mwenye hila kama knyonga.” Akainuka na kusogea mbele hatua moja akiendelea kusema, “Dakika chache kabla hajaingia hapa tulikuwa tukijadili kifo chake. Hatujabadili utaratibu huo. Atakuwa marehemu muda mfupi ujao.” Akageuza sauti kuwa amri. “Haya wote nendeni mkaendelee na mopango, huyu niachieni mimi.”
Umati ukaanza kuinuka. Joram akagutuka kidogo. Kama kawaida yake kujileta kwake haikuwa moja kati ya njia zake za kuwadhihaki adui zake tu. La hasha, nia ilikuwa ni kupata hakika juu ya kuhusika kwa Kwame ktika mpango ule wa mapinduzi – jambo ambalo tayari alikuwa amelipata – pamoja na kutaka kuwafahamu wote wengine ambao walikuwemo katika njama hizo. Kwani baada ya kutuma warakaule aliamini Kwame asingesita kuita wenzi wakeili wajadiliane kabla haujawadia muda aliotishia. Na ndipo akaingia ofisini huko mapema zaidi ili awafumanie kama alivyowafumania. Hakuwa amekuja mikono mitupu. Silaha zake muhimu zote zilikuwa tayari katika sehemu zake za siri. Zaidi kamera yake ndogo ya siri ilikuwa ikiendelea kupiga picha za umati huo hali kinasa sauti kkiendelea kunasa yote yaliyokuwa yakisemwa. Hivyo, ushujaa wa Kwame kiasi ulimtisha. Alihitaji muda zaidi ilia pate ushahidi zaidi kisha aondoke na kupata msaada wa polisi kuwanasa. Maadamu hakuwa tayri kwa hilo, aliona heri abadili mbinu na kuwaambia.
“Bado. Msiondoke kabla. Hamjafahamu kwa nini niko hapa na nije peke yangu badala ya kuongozana na polisi ambao wangewatieni pingu kesho muwe vizimbani na kesho kutwa mahabusu mkisubiri kitanzi.”
“Hatuna muda wa kukusikia…” Kwame alizidi kufoka. “Umejileta mbele ya mauti na hutatoka kwa miguu yako mwenyewe. Haya wote ondokeni mkaendelee na mipango yetu. Fanyeni haraka.”
“Msiondoke,” Joram akaamuru. “Angalieni, huyu anataka kuwaponza. Nilikuwa na nia njema kwenu nyote, nikizingatia kuwa nyote mna hadhi serikalini kiasi kuwa endapo mambo haya yatajulikana itakuwa aibu mno kwenu.” Alipoona wametulia kumsikiliza, aliongeza, “Kwa hali hiyo, nia ya kuja kwangu ilikuwa kuwashaurini kwa amani muache ndoto hizo. Na endapo mmedhamiria, mimi nipeni chochote ili nikae kimya. Milioni moja zinanitosha. Najua mnazo, au siyo Kwame?
Kwame alianza kubadilika, uso ukichukiza na macho kutisha, “Una wazimu,” alinguruma. “Huna utakachopata zaidi ya zawadi ya kifo. Nazifahamu sana hila zako za kitoto. Kwangu umekwama bwana mdogo.”
Joram akatabasamu, “Kwa hiyo uko tayari niipeleke siri polisi? Yuko mtu ambaye nimempa jukumu la kupeleka mambo haya polizi na kumtaka awaambie waje hapa mara moja endapo dakika kumi zaidi zitapita kabla sijamfikia hapo anaponisubiri.”
Kwa mshangao, Joram alimwona Kwame akiangua kicheko. “Polisi? Watafanya nini? Najua huo ni uongo lakini hata wakija hawatagundu lolote. Watakachofanya ni kuizoa maiti yako. Pindi watakaposubiri kesho kupata ushahidi, nchi itakuwa mikononi mwetu.” Kwame akawageukia wenzake. “Hamjaondoka tu? Tafadhalini ondokeni na mkatimize wajibu wenu bila hofu.”
Hayo Joram hakuyategemea. Lakini hakuduwaa kuwaza. “Hakuna atakayeondoka,” alifoka ghafla. Walipomtazama walijikuta wakitazamana na bastola yake ambayo aliishika kishujaa, “Wote mtaketi chini na kuwasubiri polisi.”
Wenzi wa Kwame waliduwaa, hata hivyo walipata moyo walipotazama na kuona naye kashika bastola iliyokuwa ikimwelekea Joram huku akicheka na kusema, “Kinda anapoamua kucheza na chatu asitegemee fadhila. Haya nendeni mmoja mmoja, huyu niachieni mimi.”
“Atakayethubutu kuondoka, risasi yangu halali yake,” Joram alionya.
“Msiogope vitisho vyake,” Kwame aliongeza. “Kama mnavyomfahamu, yeye ni mtundu tu, lakini yu mwoga mno wa kuua. Nendeni.”
“Aondoke mtu…” Joram alifoka tena. Lakini sauti yake ilikatizwa na king’ora chenye sauti kali ambacho kililia ghafla mezani mwa Kwame. Kikafuatwa na sauti ya watu waliokuwa wakisema haraka.
“Inspekta Kombora hapa. Kikosi cha kumi na mbili…”
… “Kombora? Sikieni, kuna mauaji yanafanyika katika ofisi ya Snow Fund. Nendeni haraka mtawapata wauaji.”
“Wapi? Snow… haya… tunaondoka mara moja…”
Wote wakazidi kuchanganyikiwa. Joram aliwatazama kwa kebehi. Lakini, alipomgeukia Kwame, aliambulia kuona akibonyeza kidude fulani na chumba kumezwa na giza Ghafla. Mlio wa bastola ukasikika. Joram alijtupa sakafuni na kutambaa kutoka alipokuwa. Mra akasikia harufu ya aina fulani ya marashi ikimfikia ghafla. Papo hapo usingizi mzito ukammeza na kumteka. Kama ndoto, alisikia ubishi mkali ukiendelea kwa sauti za wasiwasi, huyu akisema hili na huyu lile.
“Tumuue.”
“Nasema hapana. Mwacheni alale. Anajitia kujua. Hivyo atafurahi sana atakapoamka baada ya saa ishirini nan ne na kuona bendera mpya ikipepea.”
“Tumuue…”
“Nasema hapana.”
Kisha alisikia hodi kwa mbali. “Hodi… fungua…” huku mikono inayotetemeka ikijatribu kumbeba na kushindwa. “Polisi… funguia…” ikaendelea kusikika. Joram hakusikia lolote zaidi.
Bazile Ramadhani aliibuka kutoka katika kitu kama ndoto au usingizi mzito ambao ulikuwa umemmeza kwa muda mrefu ambao hakuweza kukadiria. Usingizi ambao ulikuwa umemwanza kwa namna isiyoelezeka tangu usiku wa siku ile ambayo alimwendea Kitenge ofisini kwake kumpa maneno ya hasira kwa ajili ya muswada wake alioupenda kuliko yote. Kumpa yale maneno makali ambayo hata hakumbuki wapi alipata uwezo wa kuyaropoka.
Alipofika nyumbani aliendelea na shughuli zake kama kawaida. Usiku alipanda kitandani na kujilaza. Usingizi uliomchukua ulikuwa na tofauti kubwa na ule aliouzoea. Ulikuwa mzito mno. Ndoto zake zikiwa kama jinamizi. Mara, alihisi kubebwa na kupakiwa kama gunia. Mara, alihisi akilazwa juu ya meza kubwa huku uso wake ukipimwa na jitu lenye madevu. Mara, alihisi kusikia watu wakipanga au kujadili kifo na mazishi yake na mengi mengine ya kutisha.
Hakuwa na uwezop wa kuamka wala kufumbua macho isipokuwa leo baada ya kuhisi na kisha kuona mtu akimdunga sindano. Alijikuta akiwa katika chumba ambacho hakupata kukiona maishani.
“Ni.. nini? Niko wapi?” alihoji kidhaifu.
Mtu aliyekuwa akimhudumia alimtazama kwa macho makali na kumwamuru ainuke, “Pita hapa uende huko,” aliambiwa.
“Wapi?” Bazile alihoji kwa udhaifu huku akijikongoja kuinuka.
“Fanya haraka!” alifokewa.
“Kama kondoo aliinuka na kufuata mlango alikoelekezwa. Baada ya kupita milango na vyumba kadhaa, aliamriwa kusimama.
“Geuka huku.”
Alipogeuka alikutana na risasi ya bastola isiyo na mlio ambayo ilimfanya ausahau udhaifu wake na kupaa juu. Alipotua chini tena alikuwa chali, damu nzito zikimvuja huku akiwa tena kamezwa na na aina nyingine ya usingizi ambao haukuwa na ndoto wala hisia.
“Fungua,” Kombora alifoka tena. “Polisi hapa,” aliongeza akiitazama saa yake. Dakika tatu zilikuwa zimepita tangu alipowasili hapo na kuwakuta askari wa doria wakiendelea kuugonga mlango wa ofisi ya Kwame
“Mnadhani kuna nini kinachofanyika humo ndani?” aliwahijo.
“Hatujui mzee. Hatusikii chochote.”
“Msichana anayekaa hapa mmemkuta?”
“Hatukumkuta.”
“Okay, tutavunja mlango. Nitaita kwa mara ya mwisho… FUNGUA!” akafoka.
“Mara mlango ukafunguka polepole. Kwame alitokeza akitetemeka mwili mzima isipokuwa macho yake tu. Kombora hakuyaona kuwa na dalili yoyote ya hofu. Aliwatazama kwa mshangao na shukrani.
“Karibu,” aliwaambia akiwapisha mlangoni.
Walipoingia macho yao yalidakwa na mizoga ya binadamu wawili waliolala juu ya sakafu. Mmoja akiwa kalala chali bastola mkononi. Wa pili ambaye ilikuwa dhahiri alikuwa marehemu alikuwa chali, sura yake ikitazama angani. Kombora na wasaidizi wake sita walimtazama marehemu huyo mara moja na kisha kutazamana.
ITAENDELEA
Najisikia Kuua Tena Sehemu ya Tano
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;