Najisikia Kuua Tena Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA
Simulizi : Najisikia Kuua Tena
Sehemu ya Tatu (3)
BAADA ya kuyafahamu hayo, yeye kama Joram Kiango angekuwa tayari kufuata njia zake ambazo zingemfikisha hadi kisogoni au usoni pa muuaji huyo. Joram, angependa zaidi kukutana naye uso kwa uso, aupime na kuushuhudia kwa macho yake ujabali wa mtu huyo aliyeondokea kuwa jitu kwa muda mfupi tu.
Akiwa na uhakika na mbinu zake, pamoja na matumaini juu ya njia atakazopitia ambazo ni kinyume na zile za polisi, alijisikia furaha kana kwamba tayari kamtia adui huyo mikononi mwa sheria. Akaitupa sigara yake katika kasha la taka na kutoka nje akipiga mluzi.
BAADA ya kuwaona tena rafiki zake ambao humuuzia habari za siri kutoka polisi na kupata anuani za marehemu wato, alirudisha gari lake nyumbani kwake Ilala na kuanza kutumia ‘Dala Dala’ kwenda hapa na pale.
Safari yake ya kwanza iliishia Mapipa ambako alionana na mama aliyekuwa amempangisha marehemu Kitenge. Alizungumza naye mengi ambayo alidhani au kuamini kuwa polisi wasingekumbuka au kujishughulisha kuuliza. “mwenendo wa marehemu siku chache kabla ya kifo…” “Wageni au rafiki zake wa karibuni.” “Tabia na maongezi yao….’ Na kadhalika. Pia, alihoji sana juu ya Yule mwanamke ambaye alidai au kutishia kumuua marehemu. Majibu aliyoyapata aliona kama hayakuwa na msaada mkubwa. Bibi huyu alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa sana baada ya kuwa na kila hakika kuwa aliyemuua Kitenge ni Yule ‘malaya’ kisha vifo vya aina na vya kutisha mno vikaendelea kutokea.
“Yawezekana kuwa muuaji wa kitenge ni Yule mama. Huyu mwingine pengine anaitumia nafasi hiyo ili kutimiza dhamira yake tu,” Joram alimshauri.
“Yawezekana baba. Haya mambo kwa kweli yanatisha, yaweza hata kunitia wazimu kwa jinsi ninavyoyafikiria na kuwajibika kujibu maswali magumu kutwa kucha. Nadhani utaniwia radhi nipumzike baba.”
“Bila shaka bibi,” aliitikia Joram akiinuka na kumshukuru mama huyo. Kutoka hapo alienda mtaa wa india ambako alikutana na mke wa marehemu Wamangi. Jorah alimkuta mjane kajiinamia huku mkononi kashika gazeti ambalo baada ya Joram kulitupia macho alifahamu kuwa lilikuwa na habari za mauaji hayo. Baada ya kumsalimu na kumpa pole mama huyo, Joram aliwataka radhi jirani wawili ambao waliketi kando ya mama huyo, wakimfariji kwa kuwepo kwao pale. Watu hao wakaondoka na kumwacha Joram na mama huyo ambaye alianza kutokwa na machozi.
“Usilie mama,” Joram alimfariji, macho yake yakilikagua umbo la mama huyo na kuona kuwa umri wake wa kati ya miaka thelathini na arobaini ulikuwa haujauathiri sana uzuri ambao ni dhahiri uliwahi kuwepo katika umbo hilo nene lenye ngozi laini nyekundu.
Macho ya mama huyo yalikuwa malegevu, pengine yaliashiria ulegevu wa moyo, pengine ulegevu wa mapenzi. Joram akiwa mzoefu wa mitazamo hiyo hakubabaika bali alianza kumtupia maswali kwa sauti yake nzuri.
“Nadhani polisi wamekuuliza mara nyingi swali hili mama, lakini naomba si majibu bali maoni yako juu ya mtu ambaye anaweza kuwa kamuua mumeo. Yaani kufuatana na taarifa juu ya kifo hiki inaonyesha muuaji ni mtu ambaye ama anaifahamu sana nyumba hii, ama alidhamiria kwa hali na mali kumuua mumeo. Vinginevyo, asingepanda ngazi zote hizi na kuthubutu kuua hali na wewe umo kitandani. Unadhani ni nani mama?”
“Muuaji? Na huyu hapa aliyetajwa gazetini? Baba unauliza swali gani hilo? Kama unahaja ya msaada ni kumsaka huyu mtu ili apatikane haraka,” mama huyo alijibu kwa udhaifu.
“Nina maana,” Joram alitamka baada ya kumpa mama huyo moja ya tabasamu zake ambazo humsaidia mbele ya wanawake kupata akitakacho, “….nilikuwa na maana kuwa mtu huyo Bazile anaweza kuwa anafahamiana na mumeo au kuifahamu nyumba hii kiasi cha kufanya yote yale bila vikwazo? Yaani, kama nia yake ni kuua tu, kwa nini asivizie walevi huko manzese na buguruni? Kwa nini afanye kila njia kumuua mumeo?”
“Hata mimi nashangaa,” mjane alijibu. “Nadhani hiyo ndiyo kazi yenu kama wapelelezi.”
“Ni kweli,” Joram alijibu akitabasamu tena, “Lakini tunahitaji msaada wako pia mama. Kwa mfano, juu ya kifo kilichotokea, wewe na mumeo mlilala kitandani kama kawaida siyo?”
“Ndiyo.”
“Ulipoamka ukajikuta bafuni, ukiwa umefungwa kamba mikononi na miguuni, mumeo akiwa kachinjwa…” Joram alilazimika kusita mama lipoangua kilio. “Unadhani yawezekana katika usingizi wako wa kawaida mtu akufunge kamba na kukubeba hadi bafuni hali hujaamka tu?”
“Nimesema mara nyingi kwa polisi kuwa mtu huyo alitumia uchawi. Nashangaa walivyonicheka. Haijawahi kunitokea kamwe nikalala usingizi wa aina hiyo. Wala sifahamu mangapi mtu huyo alinitendea baada na kabla ya hapo.” Akaangua kilio tena kwa sauti ndogo.
“Una hakika kuwa haukuwa usingizi wa kawaida?”
“Kila hakika. Unajua mume wangu alikuwa ndiyo bado karejea toka Zanzibar ambako aliishi huko kwa miezi miwili na zaidi kwa shughuli za kikazi. Sidhani kama nina hakika ya kusema haya, lakini sina budi kukuambia kuwa kila arejeapo toka safari za mbali tulikuwa tukirejewa na ujana wetu. Tulilala na kukesha huku tumekumbatiana , kila mmoja kiwa hataki kumwacha mwenziwe.
Fikiria basi, katika hali kama hiyo, nani mwenye uwezo wa kututenganisha bila uwezo wa mazingaombwe? Zaidi nashangaa kwa nini hamtaki kuamini kuwa uchawi ulitumika. Wangapi wameibiwa kwa njia hiyo?”
Joram aliendelea kuhoji madhumuni ya safari hiyo ya Zanzibar ilikuwa lini , hali ya mume baada ya kutoka huko na mengi mengine. Majibu akiyopata yalikuwa ya kawaida kiasi cha kumfanya ashindwe kuona kama alikuwa akiendelea mbele au nyuma katika upelelezi wake. Hata hivyo alinukuu mengi katika daftari lake kisha akamshukuru mama huyo na kuaga.
Baada ya hapo Joram alipanda basi ambalo lilimfikisha katika kituo cha mabasi cha Mkwajuni, Kinondoni. Akasoma namba ya mtaa na nyumba ya marehemu Jugeni Kawamba. Joram hakuwa na matumaini mengi ya kumkuta mtu katika nyumba hiyo, hasa baada ya kuarifiwa kuwa marehemu alikuwa akiishi peke yake. Lakini alifurahi kukuta watu watatu jamii ya marehemu,wakiwa wamehamia hapo kulinda nyumba.
Walimkaribisha kwa huzuni huku macho yao yakimuuliza ni nani na anahitaji nini. Kama kawaida yake alijieleza kwa hila kisha kuanza kuwatupia maswali ambayo walibabaika kuyajibu.
Alipoona msaada wao ni mdogo kwa jinsi ambavyo hawakuwa wakiishi na marehemu, aliinuka na kuaga. Kabla hajainua mguu kuondoka macho yake yalidakwa na ganda la tiketi ya ndege ya ATC iliyokuwa imeanguka chini ya meza. Akainama kuiokota.
Alipoisoma ilimsisimua zaidi. Ilikuwa ya kutoka Zanzibar, ikiwa na tarehe ileile aliyoitaja mjane wa marehemu Wamangi mume wake alipotoka Zanzibar.
“Kumradhi marehemu alikwenda kufanya nini Zanzibar?” aliwahoji akimtazama mmojawao , mwanamume mwenye ndevu nyingi kinyume cha wenzake japo walionekana wana umri mkubwa zaidi yake.
“Alikuwa wapi? Zanzibar? Kijana huyo alimhoji Joram badala ya kumjibu.
“Kufanya nini?” mwingine aliongeza.
Joram akagundua kuwa hakukuwa na habari zozote za karibuni kuhusu marehemu ndugu yao. Akaondoka zake polepole baada ya kuwashukuru kwa mara nyingine. Nje ya nyumba alilihifadhi ganda hilo mfukoni huku akiingia katika teksi iliyosimama mbele yake ghafla.
“Airport,” alisema bila kumtazama dereva. Alikuwa akitazama saa yake ambayo ilidai ni saa tisa kasoro dakika kadhaa. “Tafadhali tupitie hapo Mapipa Mtaa wa Kiyungi,” aliongeza.
“Bila tafadhali,” dereva alisema huku akiigeuza gari yake kiufundi na kutia mwendo kufuata Barabara ya Morocco. Walipowasili nyumbani kwa marehemu Kitenge ,Joram alifanya haraka kuingia ndani ambako alipokewa na bi kizee kwa mshangao.
“Kumradhi mama, nimerudi tena baada ya kupata swali moja la muhimu. Nilitaka kufahamu kama marehemu aliwahi kufanya safari yoyote ya Zanzibar hivi karibuni. Kwa ndege au meli.”
“Siwezi kufahamu baba. Watu hapa mjini wanaweza kufanya lolote bila mtu wa chumba cha pili kufahamu. Na kama ni safari ya ndege si anaweza kwenda na kurudi bila watu kujua? Nasikia ni safari ya dakika kumi tu. Pengine …”
“Ahsante mama,” Joram alimshukuru akiondoka harakaharaka.
“Tafadhali endesha gari kama mwanamume,”alimweleza dereva. “Kama hujiamini acha niendeshe mwenyewe.”
Dereva alitabasamu na kumwambia, “ Utachoka mwenyewe.”
Naam, Joram alikubali kuwa wapo vijana wanaojua kukimbiza gari.
Baada ya dakika chache tu gari ilikuwa tayari imewasili uwanja wa ndege wa Dar es Salaam.
“Nisubiri, tafadhari “ alisema akimpa mqalipo yake. Kisha akaenda katika chumba cha kuhudumia wasafiri ambako alikuta watu wengi wakihudumiwa. Akaingia upande wa watumishi na kujieleza vizuri kwa mhudumu mmoja wa kike ambaye alionekana kuvutiwa na tabasamu la Joram pamoja na sura yake zaidi ya maombi yake. Hata hivyo baada ya muda mfupi tayari alikuwa kamkabidhi Joram orodha kamili ya abiria wote waliosafiri katika ndege aliyoitaka Joram, siku hiyohiyo tarehe 17 Machi 1984 saa ya kuondoka Zanzibar ikiwa kumi na moja kamili za jioni .”Niliwahudumia mimi,” alisema kwa furaha.
Safari hiyo ilikuwa imefanyika katika ndege ndogo aina ya Twin Otter. Abiria walikuwa watano: majina ya wasafiri yalikuwa kama ifuatavyo:
J. Kawamba-S.L.P 71701 Dar es Salaam
B. Kwame-S.L.P 6142 Dar es Salaam
F. Wamangi-S.L.P 4700 Dar es Salaam
D. Kombo-S.L.P 41421Dar es Salaam
K.Key- S.L.P 1600010 Dar es Salaam
Joram Kiango aliyanukuu majina hayo na kumshukuru msichana huyo. Baada ya kumtupia maneno mawili matatu ya ahadi za kukutana katika madisko ambazo alijua zisingetekelezwa na upande wowote, aliondoka harakaharaka.
Kichwani alikuwa na mawazo mengi. Hakuwa na uhakika kama anachofanya ni kitu cha maana chenye manufaa katika upelelezi wake. Hata hivyo damu ilikuwa ikimsisimka kwa kushuku jambo katika safari au orodha hiyo. Tangu alipogundua majina ya marehemu wawili waliokufa usiku mmoja yakiwa katika orodha ya safari moja, alijikuta akihisi kuwa lipo jambo fulani katika safari ambalo laweza kuwa kisa au mkasa wa vifo vyao.
Lakini alikuwa akirudiwa na mashaka kwa kuona majina mawili tu. Jina la Bazile ambaye alikuwa mshukiwa wa kwanza katika mauaji yaliyokuwa yakiendelea lilikuwa halimo. Pia jina la Kitenge – marehemu wa kwanza – lilikuwa halimo. Yawezekana kuwa alikuwa anaupoteza bure muda wake? Alijiuliza alipokuwa akijikumbusha msorokoto uliokuwa katika kesi au mauaji hayo: Kwanza yule mwanamke anayedai kwamba alimuua Kitenge, pili, Bazile Ramadhani anayeaminika kuwa muuaji na anaendelea kupigia simu polisi kuwa ataua tena. Aidha, yote hayo yalishangaza. Yakoje mambo haya?
Joram akaamua kutosumbua kichwa chake hadi atakapopata nafasi ya kufahamu na ikiwezekana kujadiliana na abiria waliosalia ambao angeweza kuwapata.
Nje ya jengo la huduma za wasafiri, Joram aliingia katika kibanda cha simu na kujipatia kitabu cha orodha za masanduku ya posta.
Akakipekua haraka haraka kutafuta anuani za abiria wale watatu ambao alikuwa hawafahamu. Anuani ya K. Key haikumsumbua sana. Mara moja aligundua kuwa haikuwepo katika orodha ya namba za masanduku. Ilikuwa imekosewa au imebuniwa. Kwa nini? Hakuwa na muda wa kujibu. Akaamua kutafuta anuani nyingine. Ya D. Kombo ilikuwa ya kazini kwake Kamata, na B. Kwame ilisemwa Snow Fund.
Mara moja Kiango akalikumbuka jina pamoja na kukumbuka ilipo ofisi yake. Akatoka kibandani hima na kukimbilia kituo cha teksi.
Gari lililomleta kwanza lilikuwa limeondoka kitambo. Akavamia jingine na akamwamuru dereva aichukue mbio iwezekanavyo kumfikisha mjini. Dereva hakuwa mbaya, ingawa Joram hakuridhika naye.
Saa kumi na moja kamili walikuwa mbele ya kituo cha mabasi ya Kamata. Joram akamtaka radhi dereva, akateremka na kuingia ofisini. Karani mwanamume akamtazama kwa makini.
“Tafadhali, nataka kumwona ndugu D. Komba,” Joram alisema.
“Komba? Dismas Komba?” alihoji kijana huyo. “Leo siku ya ngapi sijui hajafika kazini. Watu wengi mno wanamtafuta. Hatujui kwa nini haonekani. Pengine kapata kazi nyingine, pengine amerusha mali za watu huko mitaani na kutoweka.”
“Yaani hamna taarifa yoyote juu yake,” Joram alifoka kwa mshangao na hofu ambayo ilianza kumpanda.
“Hatuna taarifa…”
“Mnajua wapi anakoishi?”
“Hakuna anayejua…”
“Hakuna! Ofisi hii nzima hakuna anayejua?” Joram alifoka ghafla.
Sauti yake ilikuwa kali yenye amri ikamfanya kijana huyo kuinua uso kutoka katika majalada yaliyokuwa mbele na kumtazama Joram kwa makini zaidi. Ndiyo kwanza akayaona macho yake yalivyodhamiria na paji la uso lilivyokunjamana. Kwa muda kijana huyo aliduwaa. Joram, alipoona hivyo akamtia moyo kwa kucheka kidogo, kisha akaongeza kwa sauti laini kiasi.
“Sikia kaka, tuna shida kubwa ya kumpata haraka. Huwezi kufahamu mtu yeyote anayeweza kutuelekeza kwake?”
“Wewe ni CID?” alihoji kijana huyo.
“La, ni mgeni wake tu.”
Kijana huyo alionekana kutokuliamini jibu la Joram. Hata hivyo, alitoka ili kuwaona wenzake ambao wangeweza kumpa habari hizo. Aliporejea alikuwa na kipande cha karatasi chenye anuani ya Komba ambayo alidai anaishi Kigamboni hatua kadhaa kutoka Kivukoni. Joram alimshukuru na kutoka akiitazama saa yake ambayo ilisema dakika chache mbele ya saa kumi na moja.
“Kigamboni,” alimweleza dereva wake.
Walipita Barabara ya Nkurumah na kuifuata hadi mnara wa saa ambapo walifuata Mtaa wa Railway hadi Sokoine Drive. Msongamano wa magari ulivyokuwa mkubwa ilibidi gari liende polepole, kwa mwendo ambao ulimchukiza sana Joram Kiango.
Lakini baada ya muda alitabasamu alipoona ofisi ya makao makuu ya Snow Fund ikiwa wazi mbele yake. Mara moja akamwamuru dereva kusimamisha gari kando, akateremka na kufuata mlango wa ofisi hiyo.
“Kumradhi kwa kuchelewa kwangu,” alimwambia askari mgambo aliyesimama mlkangoni tayari kumzuia. “Nina miadi ya kuonana na bwana Kwame.”
“Saa hizi?” alihoji mgambo huyo. “Tulikuwa tukifunga. Tumechelewa kidogo…”
“Unazidi kuchelewesha. Atakufukuza kazi kwa kuniweka hapa muda mrefu,” Joram alitishia.
Mgambo huyo akatabasamu kidogo kuficha hofu iliyomwingia,
“Pita hapa,” akaelekeza. “Uende moja kwa moja hadi mlango ule utamwona katibu wake umweleze shida yako. Sijui kama atakuruhusu. Wafanyakazi wote wamekwishatoka.”
Joram alimwacha akiendelea kusema. Alipofika chumba hicho aligonga na kufungua mlango. Macho ya msichana mwenye dalili zote za uanamji yakampokea kwa mshangao. “Unataka nini saa hizi?” aliuliza alipomwona Joram akijiweka vizuri kitini.
“Samahani mpenzi,” alisema akiachia moja ya zile tabasamu zake. “Nina ahadi ya kuonana na Bwana Kwame.”
“Hana miadi ya kuonana na mtu yeyote leo. Isitoshe saa zimekwisha,” msichana alimjibu.
“Ni kweli dada yangu. Lakini mwambie kuwa kuna mgeni wake anayetaka kuzungumza naye jambo muhimu.”
“Jambo gani?”
“Mwambie ni juu ya safari yake ya Zanzibar majuzi.”
“Imefanya nini?”
Joram akachoka na upuuzi wa katibu huyo. “Sikia sister, kama huwezi kumwambia leta simu nizungumze naye mwenyewe,” alisema huku tayari amevamia mkono wa simu. Binti huyo akaupokonya mkono na kubonyeza kidude kilichomuunga na bosi wake.
“Jina lako nani?” akamuuliza Joram.
“Wananiita Kalulu bin Kalulumanga.”
“Nani?”
Joram akarudia jina hilo la bandia. Baada ya maswali mengi kiasi aliruhusiwa kwenda. Ikamshangaza Joram kuona ilivyokuwa safari ndefu kumfikia ‘bosi’ huyo. Ilimlazimu kupita vyumba vidogovidogo zaidi ya vitatu ambavyo havikuwa na chochote zaidi ya taa za umeme ambazo zilitoa nuru kali sana. Mjenzi wa aina gani huyu asiye na wazo lolote la kiuchumi kiasi cha kujenga hivi?” alijiuliza Joram. Alipofikia mlango wa Kwame aliukuta ukiwa wazi.
Macho makali yaliyofunikwa na miwani mieusi yalimlaki. Macho ya Kwame ambaye alikuwa kaketi nyuma ya meza pana iliyozingirwa na viti kadha wa kadha, mfano wa chumba cha mikutano.
Kwame alikuwa kavaa suti ya kijivu ambayo ilimkubali vyema na kuoana na umbo lake refu, nene lenye nguvu. Ofisi nzima ilikuwa katika hali ya kuvutia, mapambo ya aina mbalimbali, vinyago vya aina aina na vitu vingine ambavyo Joram hakuweza kuvifahamu vikiwa vimepangwa vyema kabisa, macho ya Joram yalitambaa kwa muda juu ya vitu hivyo kama ambaye hakusikia Kwame akiuliza kwa mara ya pili;
“Unataka nini kijana?”
“Ofisi hii nzuri sana bwana Kwame,” lilikuwa jibu la Joram.
“Nadhani hukuja hapa kuisifu ofisi yangu. Sema unachotaka kisha uende zako. Nina shida za muhimu ambazo zimeniweka hapa hadi saa hizi.”
“Usijali. Mimi pia sina muda wa kuchezea,” Joram alimjibu.
“Nimekuja kwa nia njema kwako. Nadhani unafahamu mauaji ambayo yanaendelea kutokea?”
Mauaji gani? Haya ya huyu mtu mwehu ambaye anaendelea kuua ovyo? Hiyo ni kazi ya polisi. Wewe ni nani hadi unifuate kuyajadili? Nami nahusika vipi?”
Jorah hakujishughulisha na kuyajibu maswali ya Kwame. Badala yake aliongeza swali lingine, “Unamfahamu kijana huyo muuaji mzee?”
“Kumfahamu vipi?” Kwame alihoji akimchunguza Joram kwa makini zaidi. “Namfahamu kupitia magazetini, toka alipojitokeza kuwa muuaji,” akaongeza.
“Hujamwona ana kwa ana kabla ya hapo? Huku Zanzibar…”
“Sijamwona kabisa. Wala sitaki kumwona,” alidakia. “Suala la Zanzibar linahusika vipi na mjadala huu?”
“Ndiyo. Umegusa dhamira kubwa Kwame. Nimekuja hapa kukutahadharisha maisha yako yapo mashakani. Muuaji huyu anaua watu wote mliosafiri katika ndege moja tarehe 17 Machi kutoka Zanzibar. Wawili wameshakufa. Bado wewe na wenzako wawili.”
“Upuuzi ulioje? Nani aliyekwambia hayo?”
“Nani aniambie? Nimefanya uchunguzi na kuona. Dakika yoyote muuaji anaweza kukufikia wewe au yeyote kati yenu. Ushirikiano wako ni muhimu mno bwana Kwame. Ni…”
“We ni nani?” Kwame alikatiza tena.
“Kwa jina ni Kalulu, kama nilivyokwambia. Swali lako halina maana kwa sasa tunachotaka ni maelezo yoyote uliyonayo juu ya safari hiyo, yepi yaliyotokea ambayo yangeweza kuleta kitu kama hiki. Vilevile naomba uniambie yukoje msafiri mwenzenu aliyejiita K. Key.”
Joram aliona tahayari katika macho ya Kwame mara alipolitaja jina hilo. Hapana alikosea. Lilikuwepo tabasamu usoni mwake! Tabasamu la dharau au kebehi! Nyuma ya tabasamu hilo macho ya nafsi ya Joram yalisoma kitu kingine kabisa. Kitu ambacho ni kinyume na tabasamu.
“Sikia kijana,” alisema Kwame baadaye. “Sina muda wa kupoteza hapa. Wala sina jibu lolote la kumpa C.I.D au wewe, kwani nikiwa safarini sijishughulishi na jambo lolote la mtu yeyote zaidi ya shughuli zangu. Zaidi, siamini kama una lolote la ukweli katika maongezi yako. Yaelekea wewe kama si punguani wa akili u mhuni mwenye nia nyingine nje ya madai yako. Kwa hiyo. Kabla sijakuitia polisi, inuka uondoke zako haraka. Na angalia usirudi hapa tena.”
“Joram akacheka, “Yaelekea unajua mengi bwana Kwame,” akamwambia. “Shukrani kwa kunionyesha hali hiyo. Nakwenda na nitarudi nikiwa na jambo ambalo litakusisimua zaidi.” Akainuka.
“Na kama madai yako ni ya kweli, huoni kuwa unakitafuta kifo kwa miguu yako mwenyewe? Ungali kijana sana bwana mdogo. Kifo chako hakiwezi kunifurahisha hata kidogo.”
Lilikuwa kama onyo la kidugu. Lakini masikioni mwa Joram akiyatazama macho ya Kwame ambayo yalikuwa na udugu, lilikuwa tishio kali ambalo lilikusudiwa kumfanya aache harakati zake zote. Jambo ambalo lilimfanya Joram atabasamu tena kwa namna ya kumweleza Kwame: “Nimekuelewa,” lakini hakusema hilo.
“Nakushukuru tena ndugu Kwame, tutaonana…” akageuka na kuvuta hatua kuelekea mlangoni.”
“So this is Joram Kiango” Kwame alinon’gona akitazama picha tatu ambazo zilifotolewa na mashine yake maalumu pindi Joram alipoondoka. Ilikuwa baada ya kulinganisha picha hizo na zile kadhaa za Joram ambazo hutokea gazetini, zilizohifadhiwa katika mafaili yenye habari zake na watu wengine ambao Kwame aliona haja ya kuhifadhi harakati zao.
Alizitazama picha hizo kwa makini, akihusudu uangavu wa macho ya Joram ambao ulidhihirisha busara na ubishi. Kadhalika alivutiwa na umbo lake refu lililokaa kiriadha, Joram Kiango! Akanong’ona tena akizidi kutabasamu. “Well…” akasita akiukunja ghafla uso wake.
ALIKUWA amelikumbuka lile pendekezo la mmoja wa wanakamati wenzake ambaye alitaka Joram auawe au kufanyiwa njama za kumfungisha jela kwa muda pindi harakati zao zikiendelea.
Kwamba angeweza kuingilia kati na kuharibu mipango yao yote kwa ukatili zaidi ya polisi. Lakini yeye Kwame alilidharau pendekezo hilo kwani kwa kadri alivyomfahamu Joram alimwona kama kijana mtundu tu, play boy, ambaye huingilia harakati za kitoto na kufanikiwa kuziharibu; si hizi ambazo zilikuwa zikifanywa na wasomi waliokubuhu katika fani ya ujasusi huku hatua zote na za ziada zikiwa zimechukuliwa kuweka siri.
“Hivyo, ilimshangaza sana kuona Joram amemfikia na kuuliza maswali ambayo yalimdhihirishia kuwa alikuwa hajapata picha yoyote dhidi ya mipango yao. Kuja kwake hadi mbele yake ilikuwa kubahatisha tu kama wasemavyo Waingereza ‘a shoot in the dark’.
Hata hivyo, Joram hakuwa mtu wa kuruhusiwa zake vivi hivi. Aweza kuwa hajui lolote lakini pengine ameona kitu katikka mambo nya Kwame. Hastahili kupewa mwanya wa kufikiri lolote. Akainua mkono wake na kubonyeza kidude fulani kilichowekwa kwa siri nyuma ya meza yake. Mara sauti ikasikika ikitokea katika kijisanduku kilichokuwa mezani kikisema:
“Number two here. On duty sir,”
‘Vizuri,” Kwame alimjibu. “Umemwona mtu aliyetoka humu ndani sasa hivi?”
“Nimemwona mzee.”
“Ni mtu hatari. Nataka afuatwe na kuangaliwa kila anachokusudia kufanya. Asiruhusiwe kuongea na watu hatari ambao orodha yao unayo. Sawa?”
“Bila shaka mzee.”
“Huenda nikayahitaji maisha yake wakati wowote baada ya uchunguzi wangu. Nitapenda kazi ifanyike vizuri sana. Afe kwa ajali ya gari, kizunguzungu au maradhi yoyote ambayo hayatamshangaza yeyote. Sawa?”
“Bila shaka, mzee.”
“Well.”
NJE ya nyumba hiyo, Joram alisita mlangoni akijaribu kuyaunga maandishi yote aliyoyasoma katika sura ya Kwame ili aupate kikamilifu ujumbe uliokuwemo. Haikuwa rahisi.
Mambo yote yalikuwa nusu nusu kiasi cha kutokupata ujumbe kamili. Alichoweza kufanya ni kupata hisia tu. Hisia ambazo zilimfanya amshuku Kwame kwa jambo moja au lingine.
Alimshuku hasa kwa hotuba zake ambazo zilidhamiria kumtisha., Kwa nini atishwe? Na ilikuwa vipi hata maongezi yake na Kwame yawe kwa maana ya uadui badala ya urafiki? Lazima lilikuwepo jambo. Na lazima afahamu ni lipi jambo hilo.
Wazo au mawazo hayo yakamtia shauku hata akajikuta kajawa na hamu kubwa ya kuendelea na upelelezi wake. Kwa hatua ndefu ndefu akaliacha eneo la ofisi hiyo na kuliendea gari aliloacha likimsubiri. Rohoni akihisi kama anayetoka makaburini au kuzimu na kurejea katika dunia hai.
“Twende zetu brother,” Joram alimweleza dereva ambaye alikuwa kainamia usukani akifikiri au kusinzia.
“Kwa nini? Tunaenda Kigamboni?”
“Kweli! Nilikuwa naanza kusahau,” alijibu akitia gari moto kuiondoa polepole. Msongamano wa magari uliwafanya wapoteze dakika kadhaa kabla ya kupata mwanya wa kurejea barabarani.
Walipoupata na kuanza kuifuata Sokoine Drive, Joram bila kujua kisa cha hofu yake, alijikuta akitazama kila pande kuhakikisha kama halikuwepo gari lolote linalowafuata. Baada ya kusoma kitu kile kisichoelezeka katika macho ya Kwame hakutaka ifahamike na yeyote wapi anakoelekea. Hakuona kama ilikuwepo gari yoyote inayowafuata katika msafara uliokuwa nyuma yao.
Hata hivyo, alimshauri dereva kuiacha Sokoine Drive na kuifuata Samora Avenue akipitia Barabara ya Makunganya. Ni hapo alipoona gari moja iliyokuwa mbele yao ikisita kidogo. Kisha iliendelea na safari. Ilikuwa Datsun yenye namba ambazo Joram hakuweza kuzisoma kikamilifu.
Akiwa katika barabara hiyo ya Samora mbele ya jengo la Kitega Uchumi, Joram aliona gari ile ya Datsun ikitokea mbele yao kasi na kuwapita baada ya dereva kumtupia Joram jicho la haraka haraka. Ndipo Joram alipopatwa na hakika ya kufuatwa huko.
Akamwamuru dereva kusimama, akamlipa na kumtaka aondoke.
“Kwa nini ndugu? Si tunaenda Kigamboni?” alihoji dereva huyo kwa mshangao.
“Nimebadili mawazo. Nitaenda siku nyingine.”
“Pamoja na hayo ndugu, itakuaje nikuache ovyo namna hii? Si bora nikufikishe nyumbani kabisa.”
“Usijali.”
Baada ya kufanikiwa kumwondoa dereva huyo, Joram aliingia katika jengo hilo na kupanda kwa lifti hadi ghorofa ya tano ambapo aliacha lifti na kusimama kando ya dirisha akichungulia chini. Haikumchukua muda kabla hajaiona ile Datsun ileile ikirudi polepole na dereva wake kutoka nje na kutazama huku na huko.
Ilikuwa dhahiri kuwa alimwona Joram alipoachana na ile teksi. Ilikuwa dhahiri pia kuwa mtu au watu hao walimhitaji Joram binafsi, si dereva wa gari ile.
Baada ya kupata hakika hiyo, Joram aliteremka chini na kutoka njeya jumba hilo kwa mwendo wa kawaida, kama ambaye hakujua kuwa kuna mtu anayemsubiri. Joram alipita kando ya gari hiyo bila kuitazama na kuanza kurudi katikati ya jiji. Mara tu alipoipita, Dutsun ilitiwa moto na kuendelea na safari kama gari yoyote isio na shughuli na Joram. Lakini jambo hilo halikumpumbaza Joram hata kidogo. Badala yake ilikuwa ushahidi mwingine ambao ulimtia hakika kuwa anapambana na timu kubwa inayojua wajibu wao. Kwani kuondoka kwa dereva huyo kulimaanisha kuwa huko aendako Joram alikuweko mtu au watu ambao wangeendelea na jukumu la kumfuata.
Hayo yalimfanya Joram acheke rohoni. Kadhalika damu ilimchemka na akili yake kuchangamka. Alihisi kuwa tayari ameingia katika mapambano. Ingawa alikuwa hajawafahamu adui zake, bado alifarijika kwa kuona adui hao tayari wameujua uwezo wake ndipo wakachukua hatua hizo za kumfuatafuata wajue lipi anafanya. Lipi zaidi angehitaji zaidi ya hilo kupata hakika kuwa alikuwa amegundua jambo fulani katika upelelezi wake dhidi ya vifo vya kina Kitenge? Sasa alichohitaji Joram kilikuwa kitu kimoja tu; kumjua adui huyo. Baada ya kumfahamu, isingemchukua muda kufahamu kiini cha mauaji hayo yote.
Kwa Joram Kiango kumjua mtu anayemfuata halikuwa tatizo. Alichofanya ni kuendelea kutembea polepole huku akiwa na hakika kuwa anafuatwa. Alipofikia sanamu ya askari, alipanda kufuata Barabara ya Maktaba.
Alisita kidogo mbele ya maktaba ya Wafaransa akitazama picha zilizowekwa ukutani, kisha aliendelea. Akapinda kona kuifuata Barabara ya Jamhuri. Baada ya kuifuata kidogo, aliacha barabara na kufuata uchocho mdogo wenye giza.
Hapo alijificha akichungulia barabarani. Haikuchukua muda kabla hajamwona mtu mrefu mwenye dalili zote za tabia ya kutumia nguvu akifika hapo na kutazamatazama. Mtu huyo alisita, kisha akajitoma kuufuata uchochoro huo. Alitembea kwa tahadhari na uangalifu.
“Unanitafuta mimi ndugu?” Sauti ya Joram ilimgutusha mtu huyo. Kabla hajajua afanye nini alipokea pigo la judo ambalo lilimtua vyema shingoni. Akalalamika na kuanza kuanguka. Lakini Joram alimdaka na kumweka chini kistaarabu huku akimzindua kwa ngumi ya uso. Mtu huyo alijaribu kujitetea lakini pigo lingine la Joramu usoni mwake lilimlegeza kabisa. Akakoroma kwa maumivu huku akiruhusu damu kumtoka kinywani na puani.
“Hiyo ni kukufahamisha kuwa sipendi kufuatwafuatwa,” Joram alimweleza kwa kebehi. “Sasa nataka uniambie mara moja nani amekutumeni kunifuata?” jitu hilo liliguna tu. Joram akalizawadia pigo lingine ambalo lilifanya lilalamike na kusema kwa udhaifu.
“Utaniua bure. Mimi simjui mkubwa wangu. Napewa amri na mtu mmoja anayeitwa Kauzibe bin Kaubandike. Nasikia naye pia si mkubwa wala hatumjui mkubwa wetu.”
“Mnapewa amri gani?” Joram alizidi kusaili.
“Amri ya kufanya lolote, hata kuua ikibidi. Tunachojali ni pesa ambazo ni nyingi.”
“Leo pia kawapeni amri ya kunifuata?”
“Ndiyo.”
“Saa ngapi?”
“Muda mfupi uliopita. Ilikuwa amri ya haraka sana.”
“Ilisemaje amri hiyo?”
“Tulipewa picha zako. Tukaambiwa usivuke kwenda Kigamboni.ukilazimisha kufanya hivyo tukuue. Hivyo endapo ungelazimisha ukiwa ndani ya gari ile ajali ingetukia. Na ingekuwa muujiza kama ungepona.”
“Mko wangapi?”
“Tuko wengi sana, lakini hatufahamiani. Sasa hivi watafika hapa endapo nitachelewa.’
Joram alijua huo ni ukweli ambao pia ulikusudiwa kuwa tishio kwake. Akaikagua mifuko ya mateka wake na kupata bastola ambayo aliipachika mfukoni mwake na vitambulisho vya uongo ambavyo alivichana.
“Unasikia wewe,” alifoka baadaye. “Mwambie yeyote huyo unayemwita bosi wako kuwa sipendi mzaha wa kufuatwa. Ningeweza kumwonyesha kuwa sipendi tabia hiyo kwa kukufanya wewe maiti, aiokote kesho, maadamu wewe mtumwa nimekusamehe. Mwambie akithubutu tena kufanya hivyo atapata salamu za Joram Kiango.”
Jina hilo lilimfanya yule mtu agutuke na kutoa macho ya mshangao na kutokuamini. “Nani… Joram…” Joram hakumjibu, aliondoka zake polepole lakini kwa hadhari zaidi.
Dakika kadhaa baadaye, hakuwa Joram Kiango yuleyule tena. Alikuwa mtu mwingine aliyebadilika kimavazi kiasi cha kuweza kumchanganya mtu yeyote. Sasa alivaa suti yake nyeusi, tai nyeusi, shati jeusi na kofia nyeusi. Kitu pekee cheupe mwilini mwake kilikuwa ni kitambaa cheupe alichofunga shingoni.
Kitambaa ambacho kukiondoa hapo kungemfanya aonekane kivuli au sehemu ya kiza ambacho kilitanda kwa silaha zake ambazo ni pamoja na bastola, visu, nyembe, tochi yenye ukubwa wa kalamu na dawa ambazo humsaidia katika shughuli zake.
Akiwa karidhika na hali yake, aliyaacha makazi yake, sehemu za Ilala na kukiendea kituo cha basi ambapo alijiunga na watu waliokuwa wakisubiri usafiri wa kwenda mjini kufunga siku kwa starehe za dansi, sinema na vinywaji.
Hayo yalikuwa yakitokea dakika arobaini na tano tu baada ya Joram kumwacha mahututi yule jambazi aliyekuwa akimnyemelea katika vichochoro vya Mtaa wa Jamhuri. Alikuwa amesafiri harakaharaka, akisaidiwa na usiku ambao ulianza kutawala na kumficha asionwe na gaidi mwingine na kuweza kusumbuliwa pindi akienda kwake.
Alipofika nyumbani alipiga simu ya haraka kwa katibu wake kumjulisha hali ilivyo, kisha hima akaanza kubadili mavazi na baadaye kujitokeza mitaani akiwa kama alivyo. Sura ikionyesha utulivu, mavazi yakitangaza starehe hali rohoni kabeba furushi la mashaka na taharuki kwa kufikiria jukumu lililokuwa mbele yake.
Hofu yake haikuwa juu ya maisha yake, ingawa kwa mujibu wa taarifa ya yule jambazi aliyepambana naye dakika chache zilizopita, alifahamu kuwa anaelekea eneo la hatari sana. Hasa, hofu yake ilikuwa juu ya maisha au usalama wa mtu aliyekuwa akimfuata; Dismas Komba. Aliamini kwamba yupo mashakani. Moyo ulimshawishi kufanya haraka sana ili kujaribu kumtoa katika hatari hiyo.
Lilitokea basi lielekealo Posta, Joram alikuwa mtu wa kwanza kulidandia. Na lilipowasili aliwatangulia wote kuteremka. Akafanya haraka kuchukua teksi ambayo ilimfikisha Ferry ambako alijiunga na wavuvi pamoja na watu wengine waliokuwa wakinunua samaki. Alijitia mteja wa kawaida lakini macho yake yalikuwa kazini yakisoma sura za watu kuangalia kama alikuwepo yeyote kati ya maadui ambao walipewa jukumu la kutokumruhusu kufika Kigamboni. Aliporidhika na nyuso hizo alimshawishi mvuvi mmoja, kijana ambaye alikubali kumvusha hadi upande wa pili kwa shilingi hamsini akitumia ngalawa yake.
Joram alimsaidia kijana huyo kwa kupiga kasia kwa namna ambayo ilimchekesha sana kijana huyo kwa jinsi asivyofahamu kazi hiyo. “Acha tu mzee,” alisema kijana huyo. Kisha alibadili sauti katika kicheko chake na kukifanya kiwe cha kitu kama dharau ama mshangao. Kicheko hicho kilifuatwa na swali lililodai, “Yaonyesha u tajiri sana mzee?”
“Kwa nini? Alihoji Joram.
“Watu wenye fedha ndogo kama mimi si rahisi kukodi mtumbwi. Pantoni iko pale na inachukua watu bure kwa haraka na usalama zaidi.”
Ikawa zamu ya Joram kucheka. Kijana huyu hakujua kuwa alikuwa ameepuka pantoni hiyo kwa hadhari akijua kuwa kama kuna ulinzi wowote dhidi yake, haikuwepo sehemu nzuri zaidi ya hapo kivukoni. Hivyo, alikuwa akiepuka kuonekana na jicho ambalo halikustahili kumwona hasa kwa wakati huo. Lakini alimjibu kijana huyo kwa kumlaghai, “Siku nyingi mno sijasafiri katika chombo kidogo kama hiki. Hizo shilingi hamsini nilizokupa ni kati ya mia nilizozipata katika bahati nasibu. Hazikuwa katika bajeti.”
“Kwa nini basi usingekuja mchana? Saa mbili u nusu za usiku! Utafaidi nini?”
“Safari ya usiku naipenda zaidi.”
Walipowasili upande wa pili nje kabisa na kituo cha kawaida, Joram alimshukuru kijana huyu na kisha kuanza safari ya kuingia Kigamboni. Akiyafuata maelekezo ya yule mtumishi wa Kamata alifikia nyumba ambayo alidhani ingekuwa ya Komba. Lakini mara baada ya kuuliza kwa mtoto aliyeketi nje ya nyumba hiyo aligundua kwamba aliikosea.
“Ni ile pale. Si yule Komba wa Kamata?”
“Ndiye.”
“Ile pale.”
Joram alipoanza kuondoka ili aiendee, mtoto huyo alimzuia kwa kusema, “Unakwenda pale mzee? Hapafikiki siku hizi. Hasa usiku kama huu!”
“Kwa nini?”
“Pana miujiza sana. Mambo ya ajabu yanatokea katika nyumba ile. Nadhani kuna jinsi au majini.”
“Kwani vipi bwana mdogo?”
“Mengi yanatukia pale. Wapangaji wote wamehama. Amebaki Dismas peke yake. Inasemekana kwamba anajifungi achumbani usiku na mchana. Bila shaka kati ya kesho na keshokutwa atakuwa chizi.”
Joram akajikuta akizidiwa na hamu ya kuyaelewa maongezi hayo. “Kijana, nieleze vizuri nikuelewe. Unataka kusema kwamba kuna mambo ya ajabu ajabu yanatokea katika nyumba ile? Kama yapi? Nieleze hatua kwa hatua.”
“Ni habari ngumu kueleweka. Watu wanadai kuwa kabeba jini kutoka Unguja alikokwenda hivi karibuni. Tangu alipotoka huko mambo yake hayaeleweki. Siku ya kwanza aliporudi, alikuwa katika hali ya kawaida. Usiku huo alisikika akilia na kunyamaza ghafla. Jirani aliyeamka na kumwendea alirudi mbio akilia ati kapigwa kama jiwe tumboni na mtu asiyeonekana. Asubuhi waliomwona Dismas walidai kuwa alikuwa kachubuka usoni na damu ikiwa imekaukia puani. Yasemekana alitoka ili aende mjini, akaingia katika pantoni na kuvuka ng’ambo, lakini aliporudi alirudi nalo huku akitetemeka.
“Ni hapo alipoanza tabia ya kujifungia ndani. Yasemekana pia kuwa wapangaji hao waliohama walikuwa wamelala ndani lakini walipoamka alfajiri walijikuta wamelala nje, uchi wa mnyama, hali vitu vyao humo ndani vikiwa vimetapanywa ovyo ovyo. Hata sisi watoto ambao tumekuwa tukicheza mbele ya nyumba hiyo tumeacha baada ya mwenzetu mmoja usiku wa juzi kutoweka ghafla na kuokotwa baada ya muda mrefu kalala ufukoni. Alipoulizwa kilichomfanya alale huko na vipi alienda huko hakuwa na jibu zaidi ya kushangaa tu.”
“Ni hadithi nzuri,” Joram alimjibu akitabasamu.
“Siyo hadithi. Yametokea na yanaendelea kutokea…”
Joram hakuwa na nafasi ya kumsikiliza zaidi. Mawazo yake tayari yalikuwa kazini yakiifikiria taarifa hiyo. Macho yake pia yalikuwa yakipambana na kiza kujaribu kutazama eneo la nyumba hiyo ambayo kiasi ilijitenga na nyumba nyingine kutokana na utaratibu usioridhisha wa mjenzi au mpimaji. Nyumba hiyo ilizungukwa na kichaka kikubwa cha miti au maua yasiyo katika utaratibu mzuri.
Kwa mtu kama Joram ilikuwa ni rahisi kuhisi kichaka hicho kingeweza kuwa hifadhi nzuri ya mtu au watu waliodhamiria kumtendea Dismas Komba jambo fulani, si kama walivyodhani watu wengine kuwa ni majini yaliyofanya yote hayo. Joram alimshuku pia kuwa kile kitendo cha watoto na majirani kilidhamiriwa kuwaweka watu wote mbali ya eneo hilo ili wapate nafasi nzuri ya kuendelea na harakati zao. Harakati ambazo zilikusudiwa kupoteza maisha ya Komba. Kwa nini?
Hakuwa na nafasi ya kujijibu maswali hayo. Damu ilikuwa ikimchemka na moyo kumwenda mbio huku nafsi ikimshawishi kufanya haraka kabla halijatukia lolote baya zaidi kwa Komba.
Hata hivyo, baada ya kumshukuru mtoto huyo kwa sauti ambayo haikuonyesha kuwa kaamini lolote kati ya hayo, aliondoka zake polepole akielekea upande mwingine. Mikono yake ilikuwa shingoni kuondoa kile kitambaa cheupe. Mara akawa kama kivuli. Ili kupima kama alikuwa katika hali ya kuridhisha alipiga hatua mbili nje ya barabara na kusimama.
Watu wengi walipita bila ya kumwona. Mara alitokea mzee, kafutana na binti mwenye umri wa mjukuu wake. Walikuwa wakizungumza mambo ambayo yalimshangaza Joram kupita kiasi. Walipomkaribia zaidi walisimama na kuendelea na maongezi yao.
Nusura atokwe na kicheko kwa kusikiliza utongozaji huo wa kizamani mno. Lakini alijikuta akishindwa kustahimili kuondoka pindi maongezi hayo yalipopamba moto na kubadilika kuwa mahaba kwa mtindo ambao Joram hakutarajia kuwa binti mdogo kama huyo angediriki kumtendea babu wa kiasi hicho.
Aliondoka kwa kunyata akiifuata nyumba ya Dismas Komba. Alipoikaribia alitafuta nafasi nzuri katika kichaka cha maua na kuketi chini akisubiri.
Alisubiri sana. Kusubiri ikiwa miongoni mwa shughuli zake hakukinai kuketi hapo, akivumilia mirija ya mbu huku macho yake ambayo yalikwishazoea giza yakiwa wazi kutazama lolote. Nia yake ilikuwa ifike saa saba au nane ya usiku ndipo aendelee na safari yake hadi katika nyumba ambamo alikusudia kuonana na Komba. Kwenda papara baada ya kusikia ‘hadithi’ ya yule kijana juu ya nyumba hiyo isingetofautiana na nondo aendavyo katika moto kwa tamaa ya mwanga.
Joram alipoitazama tena saa yake na kuona ikikaribia saa sita za usiku, alianza kujiandaa kuisogelea nyumba hiyo. Nia yake ikiwa ashughulikie dirisha moja au mlango na kuingia ndani ambako angehitaji kupata hakika kama sehemu ya kiza ikichezacheza hatua kadhaa mbele yake. Baada ya kutazama kwa makini aliona dalili za kiumbe hai, kikitembea polepole kuiendea nyumba hiyohiyo. Alikuwa mtu! Kavaa mavazi mieusi kama yake. Macho ya Joram yaliongeza juhudi kutazama kama mtu huyo alikuwa peke yake. Hakuona dalili ya mtu mwingine. Ndipo Joram alipouinua mguu mmoja baada ya mwingine kwa hadhari na utulivu kama kivuli akimfuata.
Mtu huyo alipoufikia mlango hakuchelewa sana kuushughulikia, ukafunguka polepole naye akaingia huku akiufunga. Joram alimpa dakika mbili, tatu kisha akausogelea mlango na kuujaribu. Haukuwa umefungwa. Akaufungua na kunyata ndani huku masikio yake yakiwa wazi, mkono wake ukiipapasa bastola yake.
Humo ndani kulikuwa na kiza ambacho kilitisha mno. Nuru hafifu sana ilionekana kwa shida kutoka chumba kimoja. Joram alikifuata chumba hicho na kutega sikio lake katika tundu la ufunguo akisikiliza. Haikuwepo haja ya kusikiliza kwa makini kiasi hicho.
Sauti ya mtu au watu wanaogombana kidhaifu ilimfikia kwa urahisi. Mmoja alikuwa akisema, “Wapi? Usiposema nitakuua…” Mwingine alilalamika tu.
“Nitakuua kweli,” ilidai tena sauti hiyo nzito zaidi. Ikafuatwa na malalamiko ya maumivu makali.
Joram hakustahimili zaidi. Akaufungua mlango kimyakimya kwa haraka zaidi na kujitoma ndani. Aliingia wakati mzuri sana wa kuwa shahidi aliyeshuhudia jisu kali na refu likiingia katika kifua cha mtu aliyelala juu ya sakafu.
Pigo la pili Joram alilizuia kwa kumpiga muuaji huyo judo ya shingo. Hakuwa amelipiga vizuri pigo hilo, kwani badala ya mtu huyo kuzirai kama alivyotarajia Joram, alishangaa kumwona akiinuka na kumtazama Joram kwa macho makali yenye mshangao. Joram akaachia pigo jingine. Hili lilimwingia mtu huyo, lakini halikumtosheleza. Alichofanya ni kupepesuka kidogo tu na kuinuka tena akimjia Joram huku kajiandaa tayari. Joram akaona kuwa alikuwa kakukutana na mtu hatari kwa judo.
Akajiandaa vyema zaidi. Mt huyo alimjia Joram, mikono yake iliyotapakaa damu ikiwa imetangulia. Joram alimwepuka nsa kurusha kung fu ambayo ilikwepwa na kufuatwa na karate ambayo ilimkubali Joram ubavuni. Kabla hajakaa vyema pigo la pili lilimtua shingoni.
Joram alitamani kuuzamisha mkono wake mfukoni ili apate bastola yake, lakini alihisi hiyo ni dalili ya woga na bado alifurahia nafasi hiyo ya kuupima uwezo wake kijudo. Hata hivyo alijutia uamuzi wake huo baada ya dakika kadhaa za mapambano na kujikuta katupwa chali, mikono ya jitu hilo ikitambaa kooni ili kumkaba. Joram alijitahidi kurusha mateke na mikono, haikusaidia.
Mikono ya mtu huyo ilikwishapata koromeo lake na sasa ilianza kumkaba kwa nguvu kana kwamba ni vidole vya chuma. Macho yakaanza kumtoka Joram kwa hofu. Lakini macho hayo yalibadilika na kutazama kwa faraja pindi alipoona yule mtu aliye sakafuni akijikongoja kuinuka na kuchomoa jisu kutoka kifuani mwake na kukididimiza mgongoni mwa adui aliyemkalia kifuani.
Lilikuwa pigo dhifu mno lakini lilimfanya mtu huyo kumsahau Joram na kugeuka nyuma. Joram aliitumia nafasi hiyo kuachia pigo zito la mwisho. Pigo ambalo lilitimiza wajibu wake. Muuaji akaanguka sakafuni. Joram akamwahi kwa kumtia kamba za miguuni na mikononi haraka haraka. Kisha akamwinamia na kumtazama vizuri.
“Mama.”
Sauti hiyo ilimzindua Joram. Akamwacha muuaji huyo aliyelala kama mzoga na kumsogelea mtu huyo aliyekuwa akijaribu kuinuka ili ainue tena jisu na kummaliza adui yake. Joram hakuwa na haja ya kuambiwa kuwa mtu huyo ni Dismas Komba!
“Asante kwa kuokoa maisha yangu Bwana Dismas,” alimweleza haraka haraka. “Unadhani kwa nini walitaka kukuua?” aliuliza.
“Wamekwishaniua…Nakufa…” Komba aliendelea kulalamika.
“Wewe sio mmojawao?”
“Mimi ni adui yao mkubwa.”
“Wewe ni nani?”
“Huwezi kunifahamu. Kwa jina ni Joram Kiango.”
“Joram! Nakujua sana…” Komba alisema kwa juhudi kubwa. “Joram! Walinitesa sana…Laiti wangeniua…nilikuwa sina hali siku zote. Nikienda huku nakutana nao. Nikikaa hapa usiku wanafika na kuniadhibu kwa vitisho na mateso. Wameniua…” akaanza tena kulalamika.
Ingawa nuru ilikuwa hafifu, ikitoka katika mshumaa uliowekwa kwenye kona moja ya chumba, lakini ilitosha Joram kuona katika macho yake Dismas Komba kuwa uhai ulikuwa ukimtoka harakaharaka. Hakuwa na muda wa kuishi zaidi.
*JORAM ANAKUMBANA NA KASHKASH KUBWA KATIKA HARAKATI ZAKE. HAPA KAKUTANA NA DISMAS KOMBA, LAKINI ANAMWONA KUWA HANA MUDA MREFU WA KUISHI. JE, NI KIPI KITAFUATA? FUATILIA RIWAYA HII KALI I
ITAENDELEA
Najisikia Kuua Tena Sehemu ya Nne
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;