Roho ya Paka Sehemu ya Kwanza
NEW AUDIO

Ep 01: Roho ya Paka

SIMULIZI Roho ya Paka
Roho ya Paka Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA


Simulizi : Roho Ya Paka

Sehemu Ya Kwanza (1)

ILIKUWA ghafla, kama pigo la kisu ambalo lilipenya mwilini na kuujeruhi moyo wa Inspekta Kombora. Kati ya yote aliyoyatarajia jioni ya leo, simu kama hiyo, ya maafa, haikuwamo kabisa akilini mwake. Kwa jumla, ilikuwa kama iliyopigwa muda huu kwa ajili ya kumsimanga au kumdhihaki.

Muda mfupi uliopita alikuwa akiitazama kwa furaha kubwa chati yake ya taarifa za wizi, ujambazi na mauaji nchini. Ingawa tabasamu ni kitu ambacho huutembelea uso wa Kombora kwa nadra sana, lakini leo liliutawala uso huo kwa muda mrefu wakati akiitazama chati hiyo. Furaha iliyotokana na jinsi idadi ya vitendo hivyo ilivyokuwa ikishuka kwa kasi. Ukiacha udokozi mdogomdogo, wizi wa kuaminiana na ule wa kalamu vinginevyo rekodi hiyo ilikuwa ikielekea kwenye sifuri. Wakati wowote Tanzania ingeweza kujitangaza duniani kama taifa pekee ambalo limeushinda kabisa ujambazi.

Kombora alikuwa mtu wa kwanza aliyestahili kuifurahia hali hiyo kwani alikuwa mstari wa mbele kati ya wale wachache ambao huumiza vichwa vyao na kukesha usiku na mchana pindi linapotokea tukio lolote ambalo hutishia usalama wa taifa hili. Hivyo, alichekelea huku akimpongeza kimoyomoyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema, ambaye alisimamia kwa dhati ulinzi wa sungusungu ambao uliwajumuisha raia wenyewe kujilinda usiku. Kombora aliamini kabisa kuwa hilo lilichangia sana kupunguza wizi, uvunjaji wa majumba na mauaji ambayo yalifikia kiwango cha kukatisha tamaa.

Hata hivyo, tabasamu la Kombora lilitoweka. Lile wazo lililokuwa likimpekecha ubongo mara kwa mara lilipomjia tena, wazo la kwamba, kama imefikia hatua ya raia wenyewe kukesha nje wakijilinda, vyombo ambavyo vina jukumu hilo vinafanya nini? Havitoshi? Haviwezi? Havifai? Haviaminiki? Na kama jibu limo katika moja ya maswali hayo kuna umuhimu gani wa kuwa na vyombo hivyo na kuvitengea mamilioni ya pesa kila mwaka?

Akiwa askari mwaminifu, anayeipenda na kuiamini kazi yake Kombora alijisikia haya. Angefurahi zaidi kama idadi hiyo ya matukio ya kijambazi ingekuwa inashuka kutokana na uwezo wa polisi au usalama. Angefurahi zaidi kama raia wote wangelala usingizi wao kwa amani kama ilivyokuwa miaka michache iliyopita. Pamoja na hayo, aliendelea kuifurahia hali ya usalama. Alijiona kama kwamba wanausalama wako mapumzikoni au chuoni wakiandaa mkakati ambao utawafanya warudipo kazini watimize jukumu lao kwa uhakika zaidi.

Ni wakati alipotoka mbele ya jedwali hilo na kuketi juu ya kiti chake pindi ilipolia simu hii na kuupasua moyo wake kwa habari za mauaji. “Unasema unaitwa nani vile?” Kombora aliuliza kwa ukali kidogo.

“Sajini Brashi, mzee. Wa kituo Kikuu… Ni kweli hunifahamu. Lakini mimi nakufahamu…”

Kombora alimkatiza tena, safari hii kwa ukali zaidi, “Kwa nini unipigie mimi? Huna mkuu wako wa kazi? Sikiliza, Sajini. Kama hadi leo hujafahamu taratibu za kazi yako nadhani njoo zako hapa tukupe barua ili urudi tena chuoni.”

“Sivyo, mzee,” upande wa pili ulijibu, kiasi sauti yake ikiwa na hofu. “Naufahamu wajibu wangu. Lakini kuna jambo katika mauaji haya, ambalo nadhani ungependa kuliona kabla ya mtu mwingine yeyote.”

“Jambo lipi hilo?”

“Labda nikuombe uje mara moja. Ni mwendo wa dakika tano tu, mzee…”

***​

PONGWE Hotel ni moja kati ya yale mamia ya hoteli za kitalii ambazo ziliibuka kama uyoga huku na huko nchini, mara baada ya kutangaza ule uhuru wa kiuchumi. Hii ipo katika Mtaa wa Livingstone, Kariakoo. Ina ghorofa sita, vyumba mia na ishirini vya kulala, vyote vikiwa vinajitegemea kwa bafu, choo na mashine ya kurekebisha hewa.

Kwa nje hoteli hii inaonekana kama hoteli nyingine nyingi za mji huu, kana kwamba wajenzi wake walikusudia kumfanya mpitanjia asivutiwe kabisa na majengo, rangi wala mandhari yake. Lakini ndani, hali ilikuwa tofauti kabisa. Utaalamu na utajiri vilijumuishwa kiasi cha kumfanya Kombora, ambaye hapati nafasi ya kutembelea hoteli mara kwa mara, atikise kichwa chake.

Zilimchukua dakika tisa, badala ya tano, kutoka ofisini kwake hadi hapa, hali ambayo ilisababishwa na msongamano wa magari na ubovu wa barabara. Alimkuta Brashi, kijana mwembamba, mrefu, mwenye nywele nyingi aliyevalia kiraia, akimsubiri mlangoni.

“Hadi sasa, zaidi ya mhudumu wa chumba hicho na meneja wa hoteli, hamna mtu mwingine anayejua kilichotokea,” Brashi alimweleza Inspekta akimwongoza ndani. “Ni katika ghorofa ya tano, chumba namba 108.”

Walipita mapokezi ambapo mhudumu wa kike alikuwa akiwakaribisha wageni wanne kwa maneno na tabasamu lililotosha kabisa kuwashawishi wakae hotelini hapo kwa miaka. Kutoka hapo waliingia chumba cha vinywaji. Huko nusu ya viti vyote tayari ilimezwa na wateja walioonekana wachangamfu zaidi kutokana na bia nyingi zilizokuwa wazi mbele yao. Wawili kati ya wateja hao waligeuza nyuso zao kuwatazama Brashi na Inspekta Kombora, waliokuwa katika mavazi yao ya kawaida. Watumiaji hao waliwapuuza mara moja kwa kuwachukulia kama wanywaji wenzao. Brashi alimwongoza Kombora kuifuata ngazi ya kupandia juu.

Mbele ya chumba walichokihitaji walimkuta meneja akinong’ona na mzee mmoja mwenye tumbo nene na uso wa mtoto mdogo ambaye, kwa kumtazama tu, Kombora alifahamu kuwa ni Mchaga. Nyuso zao zilijawa na wasiwasi.

“Karibu mzee,” Meneja aliwakaribisha. “Huyu hapa ni bwana Mmari, ndiye tajiri wa hoteli hii. Nilikuwa nikimfahamisha mkasa uliotukuta.”

Walishikana mikono. Kisha, wote wakaingia katika chumba hicho ambacho kwa mtazamo wa kawaida kilikuwa kama kawaida. Shuka zilitandikwa vizuri kitandani. Juu ya kitanda hicho alilala kifudifudi msichana mwembamba, mweupe, ambaye huhitaji kumtazama usoni ili ujue kuwa ni mzuri. Alivaa nguo zake zote; gauni jepesi, refu japo lilifunua paja moja na kuonekana kutokana na kulala vibaya. Mikono yake laini ilijaa bangili na pete ya dhahabu. Shingoni pia alikuwa na mkufu wa dhahabu ambao ulioana na nywele zake ambazo pia zilibeba rangi ya dhahabu. Kwa kila hali alikuwa msichana mzuri wa kileo.

Angeweza kuwa amelala… angeweza kuwa amejipumzisha. Kombora alimtazama Brashi kama anayetaka ufafanuzi wa hayo.

“Amekufa mzee,” Brashi alijibu swali hilo ambalo alilisoma katika macho ya kombora. “Amekufa kifo cha kikatili kupita kiasi.”

Kombora hakuelewa. Alimwonyesha hivyo Brashi katika macho yake.

“Labda nikuonyeshe, mzee,” alisema akimsogelea marehemu. “Nikuonyeshe jeraha mzee?” Kombora alipotikisa kichwa kukubali, Brashi alichukua kitambaa cha meza ndogo kando ya kitanda hicho na kukifunga katika mkono wake wa kushoto. Kisha, akautia mkono wake tumboni mwa marehemu na kumgeuza taratibu huku akiyafumba macho yake na kusema taratibu, “Jiandae kwa mshituko.”

Kwanza Kombora hakuelewa. Ilikuwa kama anaota ndoto ya ajabuajabu inayotisha kuliko vitisho vyote. Kisha, akadhani kuwa haoti, bali anatazama sinema ya kuogofya kupita kiasi. Alipotanabahi kuwa hayuko pichani wala ndotoni alihisi alishikwa na kichefuchefu. Hakuhitaji kutapika kwani bwana Mmari alikuwa akitapika badala yake huku akitokwa na sauti ya kilio cha ghafla.

Ilikuwa picha ya kutisha, picha isiyoelezeka wala kutazamika. Yeyote aliyefanya kitendo hiki hakuwa binadamu wa kawaida isipokuwa mnyama. Vinginevyo, hangewezaje kuthubutu? Angewezaje kufikiria hilo?

Bila kujua atendalo, Kombora alijikuta akimshika Sajini Brashi mkono kwa vidole vyake vikubwa na kumbana huku akimuuliza kwa sauti ndogo, “Mimi nahusika vipi na maiti hiyo Sajin? Kitu gani hapo ambacho uliona kitapendeza sana niskikiona?”

Brashi alijaribu kujitoa katika mkono wa kombora. Ilikuwa kama kujaribu kujikwatua toka katika pingu. Badala yake ndiyo kwanza vidole hivyo vilizidi kudidimia katika ngozi yake. Japo maumivu yalikuwa makali, lakini hayakumzuia kushangazwa na nguvu za mzee huyu. “Anakula nini?” alijiuliza akimtazama usoni.

“Kitu gani ulichodhani kitanipendeza hapa?” Kombora aliuliza tena.

“Unaniumiza Inspekta.”

Ndiyo kwanza Kombora akafahamu kuwa alikuwa amemshika Brashi mkono. Akamwachia na kuiona damu ambayo ilianza kutoka katika michubuko iliyosababishwa na vidole vyake. Angeweza kumwomba radhi, lakini hakufanya hivyo. Rohoni mwake, aliona adhabu hiyo ndogo inatosha kabisa kumfunza adabu sajini huyu kwa kosa lake la kuivuruga amani na starehe aliyokuwa nayo moyoni kwa siku chache zilizopita bila misukosuko ya kutisha.

Kumwita hili atazame maiti hii iliyokuwa katika taswira ya kutisha kupita kiasi, maiti ambayo haitamtoka akilini wala katika ndoto zake, kwa muda mrefu bila sababu ya maana, aliona ni ufedhuli wa hali ya juu. Alimkazia Brashi macho akifikiria adhabu ipi ya pili ambayo ingemfaa zaidi.

Brashi hawezi kuwa mbumbumbu kiasi hicho. Hawezi kuwa mtu pekee nchini na duniani ambaye hafahamu kuwa Kombora alikuwa akiongoza idara maalumu na pekee ambayo hushughulikia yale masuala mazito na yanayotishia usalama wa serikali na taifa, si masuala madogomadogo, ya kawaida ambayo yangeweza kushughulikiwa na polisi wa kawaida.

Kana kwamba anayasoma mawazo yake, Sajini Brashi alisema, “Samahani sana Inspekta, nilidhani wewe na Joram Kiango mna aina fulani ya uhusiano. Sijui namna yoyote ya kumpata Joram, ndipo nikaona nikuarifu wewe kabla ya kulipeleka suala hili kwa wakuu wangu ambako linaweza likatangazwa ovyo au kupuuzwa. Kama nimekosea, Inspekta, naomba radhi…”

“Sijakuelewa Joram anahusika vipi na huyu marehemu?” Kombora aliuliza, moyoni akitetemeka kidogo kwa jibu atakalopata.

“ Yawezekana huyu marehemu ni Nuru, yule mwenzi na mpenzi wake Joram Kiango. Kama ndiye…”

“Hukuona mzee?” Brashi alikatiza mawazo yake. “Hukuona? Basi nitalazimika kumfunua tena marehemu.”

“Kuona nini?”

Kombora alijaribu kumzuia, lakini alichelewa. Tayari alikwishamgeuza maiti chali. Kombora alilazimika kulitazama tena jeraha hilo.

Bado lilikuwa halitazamiki. Utalitazamaje jeraha ambalo lilikuwa zaidi ya jeraha? Pale ambapo palitakiwa kuwa na uso wa msichana huyo, toka sikio hadi sikio, na paji la uso hadi kidevu, badala yake palikuwa na shimo la kutisha lililokuwa limekula nyama zote na kuacha mifupa mitupu. Pale yalipostahili kuwepo macho, pua, midomo na ulimi sasa yalikuwa mashimo ambayo yaliacha wekundu wa nyama na damu uonekane kiasi cha kutisha zaidi ya fuvu lolote la binadamu.

Safari hii, akitazama kwa makini zaidi, Kombora aliweza kubuni kilichokula nyama hiyo. Kama si biological weapon ya kisasa zaidi ambayo inatoa wadudu wadogo na wengi sana ambao wanashambulia nyama ya binadamu kwa dakika kadhaa kabla ya kufa, basi ni aina kali sana ya asidi ambayo ilimchoma binti huyo uso mzima na kuacha mifupa mitupu.

“Unaona mzee?” Brashi alimzindua.

“Nini?”

“Tazama hapa,” alielekeza mkono wake pale ambapo palistahili kuwa kinywa, ambapo sasa palikuwa na meno yaliyotokeza kana kwamba yanalia au yanacheka. Kombora aliinama na kuchungulia. Ndipo alipoweza kukiona kipande cha karatasi kilichokuwa kimelazwa humo kinywani. Kilikuwa na maandishi. Kombora aliinama na kuyasoma.

“TUNAMTAKA JORAM KIANGO”

Kombora aliyasoma kwa mara ya pili kabla hajaupata ujumbe huo. Alipoupata aliingiza mkono wake mfukoni na kutoa kitambaa. Akakizungushia katika vidole vyake na kuvididimiza humo kinywani hadi alipofikia hicho kipande cha karatasi. Alikichukua na kukizungushia katika kitambaa hicho na kisha kukitia mfukoni mwake.

Baada ya hapo alimgeukia Brashi na kumwambia, “Sikia sajini, umefanya kazi nzuri. Wanamtaka Joram Kiango. Tutampa ujumbe wao.” Alimkazia macho kabla hajaendelea, “Sasa unaweza ukaendelea na taratibu zako zote, kama kawaida. Tafadhali nitaomba unipe taarifa kamili ya upelelezi wenu juu ya mauaji haya mara mtakapokuwa tayari. Sawa?”

Brashi alitikisa kichwa.

“Na unajua sajini? Sikio la mtu yeyote nje ya chumba hiki lisisikie kuwa mauaji haya ni salamu tu kwa Joram Kiango. Nataka iwe siri, tafadhali.”

“Bila shaka Inspekta.”

“Ngoja nikuonyeshe,” alisema akiinama tena kitandani na kumshika maiti.

***​

HADITHI ilikuwa fupi na nyepesi. Kwa jina aliitwa Sofia Ali, mzaliwa wa huko Dodoma, wilayani Mpwapwa. Alikuja Dar es Salaam kama ilivyowatokea wasichana wenzake wengi wa hirimu yake. Amemaliza shule darasa la saba hana kazi wala mchumba. Jirani, mke wa bwana fulani huko Dodoma mjini anatokea na kumshahuri wafuatane naye mjini kumtunzia nyumba. Mshahara? Mia tano kwa mwezi. Chakula bure, malazi bure, nguo alizochoka nazo mama mwajiri bure, Akatae? Kama wengi wengine Sofia alijikuta yuko mjini.

Maji ya bomba ya mara kwa mara, chai ya maziwa kila asubuhi, chakula chenye viungo vyote; pamoja na ile dokoadokoa ya vipodozi vya mama ilifichua kiumbe mrembo aliyejificha katika umbo lile lililochakaa la Sofia Ali.

Badala yake, miaka miwili baadaye, aliyesimama mbele ya mama mwajiri alikuwa Sofia mwingine kabisa, Sofia aliyewiva, Sofia aliyejaza, Sofia ambaye alimfadhaisha baba mwenyenyumba na kumtisha mama. Matokeo yake Jumapili moja alipewa tiketi ya kurudi Mpwapwa. Kufanya nini? Kazi basi.

Hakurudi Mpwapwa. Akafuate nini? Jembe na mpini wake? Amwachie nani starehe za sinema na muziki ambazo ndio kwanza alikuwa ameanza kuzionjaonja? Rafiki yake aliyekuwa akiishi Tambuka Reli, ambaye alikuwa ameanza kujitegemea baada ya kupitia mkondo huohuo, alimpokea.

Chumba chao chenye upana wa futi tano kilibeba kitanda chao cha futi tatu na majukumu yote ya jiko, ghala; na mengineyo. Ungewatembelea mchana wakati wa joto, huku moshi ukiwaadhibu, usingekosa kuwahurumia. Lakini waone jioni, wakati tayari wameoga, wamevaa na kujitengeneza usingekosa kujiuliza kwa nini hawajatokea wachumba wakawaoa.

Mwaka mmoja baadaye, Sofia alikuwa Sofia hasa. Hata shoga zake walianza kumchukia kwa wivu. Hakujali, kwani alikuwa na marafiki wengi wa kiume kuliko wa kike. Na ni hao ambao aliwahitaji. Wakati huo hata jina alianza kulibadili. Badala ya Sofia sasa alijiita Soffy. Na alipenda sana baba yake aitwe Ally badala ya Ali. Hata lugha yake ilianza kubadilika. Katika kila sentensi alijikuta akiweka walau neno moja la Kiingereza. Hakujua kilipotokea hicho Kiingereza chake Lakini alikuwa na hakika nacho.

Sofia alifanya kosa. Mimba iliingia bila taarifa wala hiyari. Bwana hakumjua wala hakuhitaji mtoto. Alimeza vidonge mimba ikafa. Miezi miwili baadaye mimba ya pili ilimkamata. Hii haikusikia vidonge. Miezi mitatu, minne, mitano! Kila mtu alianza kumshuku. Elfu tatu zilimaliza kazi. Daktari mmoja asiye na huruma, alifanya kazi hiyo na kutupa mtoto anakokujua. Sofia aliponea chupuchupu. Baada ya miezi mitatu ya maumivu, afya yake ilimrudia. Mji wa Dodoma akauona nuksi. Huyoo, akaingia Dar es Salaam.

Dar ilimlaki juujuu. Rafiki yake mmoja wa Kinondoni, akijua kuwa umbo la Sofia lingemwongezea riziki, alimkaribisha kwake na kumwonyesha mji. Madisko ya Lang’ata na Ushirika yaliwakoma. Madansi ya DDC na Friend’s Corner yaliwatambua. Mabaa ya Sky Way na Kilimanjaro, yaliwaheshimu. Mabwana walikuwa tele, wa kila kabila na kila rangi. Sofia hakujua kumkataa mtu. Ni yeye aliyeanzisha msemo wa “… Ni pochi yako tu.”

Jioni ya leo alikuwa katika Hoteli ya Sky Way, ndipo alipomwona yule kijana mrefu, mnene, ambaye alikuwa akinunua vinywaji kwa fujo kuliko mtu mwingine yeyote hotelini hapo. Na mifuko yake bado ilionekana kuwa imetuna. Wasichana wengi waliokuwa wakimzengeazengea walipewa bia na kufukuzwa toka mezani pake. Sofia hakuwa mtu wa kuomba bia. Yeye huitwa au kufuatwa. Alimtupia jicho moja tu kijana huyo na kuona tayari ameimeza ndoano yake. Hakukosea kwani dakika mbili baadaye alianza kuletewa bia, oda ya kijana huyo. Na dakika kumi baadaye tayari waliketi pamoja, na kuanza kushikanashikana.

“Unasemaje?

“Pochi yako tu, darling.”

“Kiasi gani?”

“Hata wewe? Nilidhani umesoma, brother.”

Maongezi yao yaliishia katika kimojawapo cha vyumba vya hotelini. Baada ya nusu saa ya vilio na vicheko vya uongo na kweli Sofia alipokea “pochi” yake. Wakati akijiandaa kuondoka kijana huyo alimshika mkono na kumwambia, “Unajua Soffy, ni tamaa tu iliyonifanya niamue kuanguka nawe. Kwa kweli, nina rafiki yangu mpenzi, mwenye kitita cha pesa, kuliko hiki changu ambaye amenituma hapa Sky Way kumtafutia mwanamke mzuri. Kweli, hata hizi pesa nilizokuwa nikizinywa ni zake, kama hujachoka nikupeleke.”

“Kuchoka!” Sofia alicheka. “Nani aliwahi kuchoka kupokea pochi? Kama una wivu, I can understand, kama huna nipeleke.”

Kisha, Sofia alishituka na kusita kidogo wazo jipya lilipomjia. “Huyo, rafiki yako, What is his name?” aliuliza.

“Jina simfahamu.”

“Why! Ni binadamu kweli?”

“Sema, maana mambo ya siku hizi you can’t understand. Mimi sijachoka kiasi cha kumvulia underware yangu mnyama.”

Kijana huyo alicheka. “Unadhani mimi ni crazy kiasi hicho? Huyo ni mtu mwenye hadhi na heshima zake. Naamini hujapata kukutana na mtu mzito kama huyo.”

Bado Sofia alisitasita kidogo. “Jina humjui. Wewe mwenyewe unaitwa nani, honey?”

“Niite Ram Shog.”

“Na huyo friend wako yuko wapi?”

Alipomalizia kuvaa, Ram alimshika mkono Sofia na kumwambia, “Twende nikupeleke. Amepata chumba katika Hoteli ya Pongwe.”

***​


Kiti cha Kombora kilikuwa kama chenye moto. Hakikukalika, mara aliinuka mara aliketi kana kwamba alikalia kaa ambalo lilikuwa likimchoma. Mkononi alikumbatia redio call yake kwa utulivu kama roho yake. Aliitazama na kuitingisha kama yai ambalo hakuwa na hakika kama ni zima au bovu.. Hata hivyo, alikuwa na kila hakika kuwa haikuwa mbovu. Ni ile ya upande wa pili ambayo alihitaji kuitilia shaka.

Muda mfupi tu uliopita alikuwa akiwasiliana na Koplo Shoka toka Lang’ata. Mara mawasiliano hayo yakakatika. Hakujua kama ilitokana na ubovu wa chombo hicho au Shoka alikata ghafla maongezi kuepuka mtu ambaye angeweza kuyasikia. Alichokuwa ameambulia ni “…Afande … tumempata…” na kisha “ amefika…” kisha chombo kikazimwa. Juhudi zote za Kombora kumpigia tena hazikuzaa matunda.

Wazo la kufanya uchunguzi kwa makini hapo Lang’ata lilimjia Kombora kutokana na uzoefu wake juu ya tabia za muuaji. Mara kwa mara katika kesi nyingi za mauaji hutokea muuaji akapenda kutembelea eneo na hata nyumba yalimotokea mauaji hayo.

Mara nyingine hutokea muuaji akadiriki hata kuhudhuria mazishi ya mtu aliyemuua. Kitu ambacho Kombora alikuwa haelewi ni sababu ipi ambayo hufanya wauaji hao wafanye hivyo. Hakujua kuwa walikuwa katika upelelezi wa kuelewa polisi wamefikia wapi katika uchunguzi wao, ama ni yaleyale waliyosema wahenga kuwa “damu nzito…” kwani mara kadhaa wauaji wengi wamepatikana kutokana na makosa hayo. Ni hilo tu ambalo lilimfanya amwamuru Shoka kuendelea na uchunguzi wake hapa Lang’ata ingawa siku mbili zilizopita hazikuwa na mafanikio.

Hivyo basi, redio yake ilipopata uhai na sauti ya Shoka ilipojitokeza na kusema “Tumempata” alijisikia kulia kwa furaha. Mara ukimya huu ukazuka. Dakika saba sasa zilikuwa zimepita. Aliendelea kuisubiri redio ya Shoka ipate uhai, aendelee kumwarifu alichogundua.

Dakika nane.

Dakika tisa.

Mara Kombora akaruka kama aliyeguswa na waya wa umeme. Akapiga ngumi kwa nguvu juu ya meza. Ameanza kuwa mzee? alijiuliza kwa hasira akiutia mkono katika fungati la meza yake na kuutoa ukiwa umeshikilia bastola yake kubwa ambayo aliitia mfukoni mwake.

Akatoka nje ya ofisi yake na kuchungulia ofisi ya msaidizi wake. Hakuwepo. Chumba cha pili alimpata askari mmoja ambaye alimtumia kuwakusanya askari wote waliokuwa ofisini wakati huo. Ukiwa usiku wa saa tano kasoro kituo kilikuwa na askari wanne tu. Wengine walikuwa katika shughuli nyinginezo au mapumzikoni. Kombora aliwachukua askari wawili na kumwamuru mmojawao aendeshe gari kasi iwezekanavyo kuelekea Lang’ata.

Gari lilikuwa likiruka, nusura lipae, lakini Kombora alizidi kumhimiza kijana huyo akanyage mafuta. Mara mbili askari mmoja alijaribu kumdadisi Kombora Lang’ata kulikoni lakini hakupata jibu lolote. Si kwamba Inspekta hakupenda kuzungumza, la! Isipokuwa hakuiamini sauti yake.

Hisia za hatari zilikuwa zikichemka akilini mwake na kumjaza hofu kila alipoyakumbuka maneno ya Shoka “…tumempata…” na kisha maongezi kukatika. Ni hili la mwisho lililomtisha zaidi. Amefika! Bila shaka ni Kakakuona. Amefika wapi? Alikuwa amefika katika ukumbi au alimfumania Shoka akiipiga redio hiyo? Kama ni hivyo kipi kinachofuata? Kombora alimwamini Shoka. Lakini pia aliamini kuwa Kakakuona yu kiumbe hatari zaidi ya simba aliyejeruhiwa. Ni hilo lililomtoa kasi ofisini.

Wakati wanafika mbele ya lango la ukumbi huo walisikia muziki ukikatika ghafla na kimya kikubwa kuzuka ndani ya ukumbi.Kombora aliruka nje ya gari na kumwambia askari mmoja alinde lango, asiingie wala kutoka mtu yeyote. Askari wa pili aliamriwa kufuatana naye.

“Kakakuona,” Kombora aliwanong’oneza. “Inawezekana yumo humu ndani. Picha zake mnazo. Mkimwona, kama hana silaha, msisite kumuua kwanza, maswali tutamuuliza baadaye. Okey?”

Ndani aliwakuta watu wakizungumza kwa sauti ya hofu na minong’ono. Umati mkubwa ulikuwa ukipambana kuingia choo cha wanaume ambako kila aliyetoka huko alikuwa kimya, aliyeduwaa kama aliyeona mzimu.

“Kuna nini?” Kombora alimuuliza mtu mmoja.

“Mtu amepigwa risasi.”

“A-me-kufa?” Kombora aliuliza akijaribu kuficha mshituko uliomkumba ghafla.

“Ataponaje? Unajua risasi mzee?” Kijana huyo alimjibu.

Ilimchukua Kombora na msaidizi wake dakika tatu nzima kuweza kupenya umati huo kuyafikia maiti. Hakuwa na haja ya kuyatazama kwa makini kabla ya kumtambua Shoka ambaye alilala kifudifudi kama anayechungulia kitu katika shimo la choo huku damu ikiendelea kutiririka na kufanya bwawa dogo jekundu liendelee kupanuka.

Kombora aliyasaga meno yake kwa hasira. Kisha alimwamuru mgambo ambaye alikuwa mbele ya mlango huo wa choo, akijaribu kuwazuia watu, kuufunga mlango wa choo hicho na kuulinda. Akarudi mlangoni ambako alitoa amri mpya. Watu wote watoke ukumbini humo, lakini si kabla ya kukaguliwa kila mmoja, tangu mifuko hadi vitambulisho.

Polisi wa Kituo cha Magomeni ambako tayari walikuwa wamepigiwa simu walipewa amri hiyo pia na kusaidiwa kuitekeleza. Wasichana, watoto na watu ambao hawakuwa na haja ya kushukiwa walitoka kwa urahisi. Watu wenye vitambulisho halali na shughuli zinazofahamika pia waliachiwa bila tabu. Lakini kuna wale ambao hata wao wenyewe hawazifahamu kazi zao, wale wenye zaidi ya kitambulisho kimoja, wao walitokwa jasho kwa maswali.

Baadhi yao walijikuta wakitupwa katika magari ya polisi na kupelekwa kituoni ambako waliendelea kuchunguzwa.

Muda wote huo Inspekta Kombora alikuwa nje ya ukumbi, kaegemea gari lake, mkono mfukoni ukiipapasapapasa bastola yake. Macho yake yalikuwa makini yakiuangalia kila uso na kila sura. Hakuiona dalili yoyote ya Kakakuona. Wala hakuwa na matumaini makubwa ya kuiona. Alivyomfahamu, kama mauaji hayo alikuwa kayatenda yeye, kwa vyovyote muda huo alikuwa maili kadhaa nje ya eneo hilo.

Hata hivyo, yawezekana akawa hakuyafanya yeye. Mtu aliyeyafanya anaweza akazubaa humo ukumbini, au akawa ameshirikiana na mtu ambaye atazubaa. Hilo ndilo lililomfanya asisitize uchunguzi wa makini kwa kila mtu.

Baada ya muda alimwita mgambo mwingine aliyekuwa akilinda magari na kumuuliza taratibu, “Ulikuwepo muda wote au ulitoka?”

“Nilikuwepo mzee.”

Unaweza kukumbuka ni magari mangapi yameondoka dakika kumi kabla ya tukio hili.”

“Kama sikosei, ni magari matano tu mzee.”

“Jaribu kukumbuka taratibu, unieleze magari hayo ni ya aina gani, yaliwachukua kina nani na yaliwapeleka wapi?”

Mgambo huyo alikuwa na kumbukumbu kali ambayo ilimfurahisha sana Kombora. Aliweza hata kukumbuka namba za magari matatu kati ya hayo, mawili ya kwanza yakiwa ya wenye disko hilohilo lililokuwa likipigwa hayakumvutia Kombora. Gari la tatu ambalo lililokuwa na wavulana wawili na wasichana wao pia halikumsisimua. Magari mawili ya mwisho ndiyo yalimfanya amtazame mgambo huyo kwa makini zaidi huku akitoa daftari lake dogo.

“Datsun nyekundu! Unasema ilikuwa na shombe wawili tu! Ambao walifika wakakaa dakika tano na kuondoka?”

“Ndiyo, mzee.”

“Namba yake…”

“TZA 42112”

Kombora aliinakili na kuuliza “Ilielekea wapi?”

“Sikumbuki vizuri nadhani ilielekea mjini.”

“Na hii nyingine unasema ni TZB 414, sio?”

“Ndiyo.”

“Toyota Corolla?”

“Ndiyo.”

“Ilikuwa na mtu mmoja tu! Ulimwangalia vizuri?”

“Sikupata nafasi ya kumwona vizuri. Lakini kwa harakaharaka nilimwona kama afisa hivi. Hata mavazi yake yalikuwa ya bei. Alitembea taratibu sana mkono mmoja mfukoni na kuingia katika gari lake. Nilitegemea atanipa walao asante kwa kumlindia gari lake, lakini hata kuniaga hakuniaga. Nadhani hiyo ndiyo sababu iliyonifanya niitazame gari yake na kuiweka namba akilini.”

Kombora alimsikiliza kwa makini na kunukuu hili na lile. Wakati akitaka kumtupia swali lingine, aliitwa mlangoni haraka. Mtu mmoja alikuwa amekamatwa na bastola. Alijaribu kuificha katika mapaja yake lakini mikono ya askari hao, ambayo imeelimika, ikaifikia.

Akapelekwa katika chumba cha ofisi ambamo aliendelea kuhojiwa huku Kombora akiifungua bastola hiyo na kuangalia risasi. Ilikuwa na risasi sita. Haikuwahi kufyatuliwa. Kibali cha kuwa na silaha? Hakuwa nacho. Kazi anayoifanya? Hakuijua. Kwa nini alikuja kwenye starehe na silaha? Hakujua. Kwa mtazamo wa harakaharaka, Kombora hakumwona kama mtu wake. Hivyo, aliamuru apelekwe kituoni pamoja na watuhumiwa wengine.

Hadi anahojiwa mtu wa mwisho ilikuwa yakaribia saa tisa alfajiri. Ndipo Kombora aliporudi ofisini baada ya kuhakikisha maiti yanapelekwa Muhimbili na familia yake kuarifiwa.

Ofisini Kombora aliinua simu na kumpigia Mkuu wa Usalama Barabarani, Mkoa wa Dar es Salaam. Bosi huyo, akiwa na usingizi mzito, alikoroma kwa hasira katika chombo cha simu “Nani?”

Lakini aliposikia jina na sauti ya Inspekta Kombora usingizi ulimtoka mara moja, akakiacha kitanda na kuuliza kwa upole, “Nikusaidie nini, mzee?”

“Samahani kwa kukusumbua,” Kombora alimwambia. “Ni suala ambalo haliwezi kulala. Naomba uwaambie vijana wako ambao wako zamu wanitafutie habari za magari haya mawili. TZB 414 na Datsun TZA 42112. Ikiwezekana waambie wayafuatilie kuona sasa hivi yako wapi. Waonye wasiwaulize wenyewe swali lolote ambalo linaweza kuwafanya washukiwe. Sawa?”

“Sawa.”

“Naweza kuyapata maelezo haya ofisini hapa kesho kabla ya saa moja asubuhi?”

“Tutajitahidi… nadhani tutapata.”

Kombora akaizima simu na kumtazama kijana wake mmoja ambaye alikuwa ameingia chumbani humo na kusimama kama aliyeitwa.

“Enhe?” Kombora akamtupia.

“Nimepokea simu kwa niaba yako mzee, baada ya kuona una simu nyingine. Imetokea Central ambako wanasema wamearifiwa na wavuvi juu ya maiti ya msichana mcheza disko ambayo wameiokota ufukweni. Wanasema amenajisiwa na kulawitiwa…”

“Kwa nini waniarifu mimi?” Kombora alimkatiza kwa ukali kidogo.

“Sura”

“Sura?”

“Wameniambia kwamba nikikwambia sura yake…”

“Inatosha!” Kombora alimwambia akiinua mkono wake kuuegemeza kwenye kichwa chake. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake alihisi uzee ukianza kumshinda nguvu.

AKIWA mgeni katika hoteli hiyo, Sofia alivutiwa mara tu baada ya kushuka toka katika teksi iliyowaleta. Ram akamwongoza hadi mapokezi ambako aliomba ufunguo wa chumba namba 108. Walipanda ngazi hadi ghorofani ambako walifungua na kuingia hadi chumbani.

“Itabidi umsubiri,” Ram alimwambia Sofia ambaye alikwishajitupa juu ya kitanda na kujilaza. Usingizi wa pombe ukamchukua.

Hakuamka tena hadi majuzi, meneja wa hoteli alipojaribu kumwamsha na, hatimaye, Sajini Brashi alipomgeuza na kukutana na uso ule ambao aliokutana nao.

GARI lilimteremsha Joram Kiango mtaa wa pili. Kama ilivyo Dar es Salaam nzima, pamoja na kwamba sasa ilikuwa usiku wa manane, bado mitaa yote ilikuwa na watu waliokuwa na shughuli zao. Wako walioketi kwa makundi wakinywa pombe mbele za nyumba mbalimbali ambazo zimetokea kuichukulia biashara hiyo kama kitegauchumi muhimu.

Wengine walikuwa wakiuza chipsi, chai, au kahawa katika magenge. Baadhi walikuwa wamekaa tu kuepuka joto na mbu waliokuwa wakiwasubiri vyumbani mwao. Hivyo, ilikuwa rahisi kwa Joram kujipenyeza hapa na pale hadi alipoupata uchochoro uliomfikisha nyuma ya nyumba yake.

Alisikiliza kwa makini hadi alipohakikisha kuwa nyumba ilikuwa tupu kama alivyoiacha kisha, kama mwizi alifungua mlango taratibu na kujipenyeza ndani. Kama mwizi, vilevile hakuthubutu kuwasha taa. Badala yake alitumia tochi yake ndogo kufanya uangalifu mkubwa kuepuka asiguse kiti kilichotegwa bomu. Alilifikia kochi. Akaketi na kuanza kusubiri.

Kusubiri, ikiwa kazi ngumu kuliko zote kwa Joram Kiango, kulianza kumkinaisha dakika tano tu baadaye. Hata hivyo, alijua hiyo ilikuwa silaha yake pekee ambayo ingemfanya akabiliane na adui ana kwa ana. Maadui hao wakiwa wanaamini kuwa wamemlazimisha kuketi juu ya kiti chenye bomu, alikuwa na hakika kuwa baada ya muda wangependa kujua matokeo ya kikao hicho. Hivyo, wangetuma watu au mtu kuangalia. Ni mtu huyo ambaye Joram alikusudia amfikishe mbele ya bosi wao na mbele ya Nuru ambaye wamemteka nyara, apende asipende.

Subira ilikuwa dawa pekee.


Nuru pia alikuwa akivuta subira. Walikuwa wametua mahali fulani katika pwani ya Zanzibar kitambo. Lakini yeye aliendelea kujifanya hana fahamu adui zake hao walipokuwa wakiufunga vizuri mtumbwi wao na kisha kujitenga kando ambapo walipanga mambo yao kwa sauti za mnong’ono. Baada ya muda walimrudia Nuru, mmojawao akimtikisa.

“Bado amezirai?” mwenzie alijiuliza kwa mshangao.

“Asidanganye huyu,” yule ambaye alikuwa amemshika mkono alisema.

“Dawa yake ndogo sana.”

Aliupeleka mkono wake mfukoni na kutoa kibiriti, akawasha njiti moja na kukichoma kidole cha Nuru. Maumivu yalikuwa makali kupita kiasi. Lakini Nuru alijikaza kisabuni, bila kutikisika wala kufumbua macho.

“Au amekufa?” mwenzie aliuliza tena. “Angalia usimtie jeraha. Bosi hatafurahi. Angependa sana kumpata akiwa kamili. Mpe Konyagi kidogo itamzindua.”

Kiberiti kikazimwa na Konyagi kutolewa kutoka katika mfuko wa koti la mmojawao. Nuru aliponyweshwa fundo la pili alijitia kupiga chafya huku akifumbua macho.

“Ni… ni…niko wapi?” alijitia kuuliza.

Adui zake wakaangua kicheko.

“Uko wapi?” Chongo alimdhihaki. “Uko kisiwani. Uko katika kisiwa cha karafuu. Uko likizo ndogo.” Kisha, akazungumza kwa sauti ya amri. “Ni hivi. Tuko Zanzibar kwa ajili ya mapumziko kidogo. Tunataka kukuburudisha kwa wiki moja hivi kabla ya kurejea Dar. Mimi na rafiki yangu hapa tumeafikiana kuwa wewe ni msichana mzuri.”

“Na mtamu,” mwenzie alidakia.

“Ndio, mtamu tosha,” aliendelea. “Hatuna shaka kuwa tutakuwa kama wewe. Tumeafikiana, itakuwa mmoja anaburudika mmoja anashuhudia, ni mchezo mzuri… tunaamini utapenda.”

Nuru alihisi akiingiwa na hofu kubwa zaidi. Atafanya nini na watu hawa wenye wazimu? Alijiuliza. Apige kelele? La! Ni aibu kwake. Vilevile, kabla sauti yake haijafika popote risasi zingekuwa tayari zimeifumua kichwa chake. Hawakuwa watu wenye hata chembe ya simile.

Alichohitaji ni subira. “Tunaye rafiki yetu mmoja anayeishi hapahapa,” yule mwenye chongo aliendelea kueleza. “Tutakufungua kamba za miguu na kukufunga za mikono kwa namna ambayo itakuruhusu kutembea kwa urahisi zaidi. Mimi nitakuwa nyuma yako, ndugu yangu. Lazima utembee kama kawaida kana kwamba tupo pamoja. Sawa?”

Nuru alitikisa kichwa.

“Sina mchezo! Sina mchezo kabisa!” Chongo aliendelea kubweka. “Unaiona hii?” aliitoa bastola yake na kumwonyesha Nuru. “Unaona kuwa ina kiwambo cha kupotezea sauti! Kwa taarifa yako, mara tu utakapojitia unaanza umalaya wako mimi nitabonyeza. Kwangu ni rahisi sana. Unaonaje?” alisema akilenga bastola hiyo kwenye uso wa ajabuajabu wa mwenzie na kuifyatua.

Nuru hakuyaamini macho yake. Alimtazama adui huyo anavyotapatapa na hatimaye kuanguka chini kama gunia, huku tundu kubwa lililojitokeza hapo usoni likivuja damu nyingi.

Nuru alipomtazama tena mwenye chongo alimwona akitabasamu. Kwa sauti inayotabasamu vilevile alimsikia akijigamba, “Unadhani ningekubali kuchangia mtoto mzuri kama wewe na dude hilo? Usiwe na shaka mpenzi, ni mimi na wewe tu.”

Baada ya maneno hayo alianza kufanya kazi harakaharaka. Alimzoa Nuru na kumbwaga chini. Kisha akamzoa mwenzie huyo ambaye alikuwa akipapatika na kumbwaga ndani ya mtumbwi. Akautia mkono wake mfukoni na kuutoa ukiwa na kititita cha pesa na kukididimiza mfukoni mwake. Kisha, akaufungua mtumbwi na kuuelekeza baharini. Akautega usukani vizuri na kuufunga kwa kamba halafu aliwasha mashine, mtumbwi huo uliondoka kasi kuelekea baharini. Akamrudia Nuru na kumfungua kamba za mikononi na miguuni.

‘Sasa!’ Nuru aliwaza na kujiandaa kupambana. Hata hivyo, alisita. Hakuona kama ulikuwa usiku wake, kwa jumla ulikuwa usiku wa adui yake. Wangeweza kufanya chochote walichotaka. Hata ukimya na uhaba wa anga lao, mvuvi mmoja katika pwani yote hiyo ilikuwa dalili ya ushindi wa maadui. Ni hilo lililomfanya Nuru asite, azidishe unyonge na ulegevu, pindi kamba zikifungwa upya ubavuni mwake.

“Twende zetu,” Chongo alisema baada ya kuhakikisha ubora wa kazi yake. “Kama nilivyosema, kumbuka hila ndogo tu ni mauti yako.”

Wakaondoka, Nuru mbele, Chongo nyuma. Ulikuwa sawasawa na msafara wa malaika wa shetani.


Saa kumi na mbili kamili ilimkuta Kombora akiwa tayari ofisini mwake. Alikuwa amejiiba kwa dakika arobaini tu kwenda nyumbani kwake ambako alioga na kubadili mavazi. Akajaribu kunywa kifungua kinywa ambacho kilikataa kushuka, akaishia kunywa kahawa kikombe kimoja na kuipooza kwa glasi ya maji ya kunywa.

Ofisini alikuta majalada kadhaa yakiwa juu ya meza yake. Moja ilikuwa taarifa ya magari aliyoyahitaji, ambalo lilifika nusu saa iliyopita. Nyingine ilikuwa taarifa ya uchunguzi mbalimbali la watu waliokuwa wamekamatwa pale Lang’ata. Jalada la tatu lilikuwa la taarifa ya kifo cha Doll.

Shingo upande, Kombora alianza na jalada hilo la mwisho, mara tu alipolifunua macho yake yalikutana na ile picha ya kusikitisha ambayo hakutaka hata kuiona. Picha ya marehemu, msichana mzuri, ambaye alilala juu ya mchanga, ufukoni, uchi kama alivyozaliwa, mavazi yake yakiwa yametupwa kando. Umbo lake lilikuwa zuri, la kuvutia toka miguuni hadi shingoni, usoni kulikuwa hakutazamiki. Sura yake ilikuwa imeharibiwa kinyama kama wale marehemu waliotangulia. Kombora alifunika huku akisaga meno yake kwa hasira kisha akayasoma maelezo yalioambatana na picha hiyo.

Ilikuwa kama ilivyotarajiwa maiti aliokotwa na wavuvi mnamo saa sita na robo usiku akiwa kama alivyo pichani. Taarifa ya madaktari ilithibitisha kuwa aliuawa kwa aina ileile ya sumu iliyowaua waliotangulia, sumu ambayo hadi sasa wanamaabara walikuwa hawajapata kuifahamu. Taarifa hiyo ilieleza jina la marehemu, wazazi wake, marafiki zake na kwamba jioni hiyo alionekana katika ukumbi wa Lang’ata muda mfupi kabla ya kifo chake.

Kombora aliliweka kando jalada hilo na kutwaa lile lenye maelezo ya watu walioshukiwa usiku huo. Alifunua harakaharaka akitafuta maelezo ambayo yangemfanya ayape uzito mkubwa zaidi. Kama alivyotarajia, hakuona kuwa kati ya hao kuna yeyote ambaye angeweza kuwa mtu wake.

Yule aliyekamatwa na bastola alitambulika baadaye kama jambazi mkubwa ambaye alikuwa akitafutwa muda mrefu kwa kosa la mauaji ya tajiri mmoja wa Kihindi huko Mwanza. Watu wawili waliokuwa na vitambulisho vya bandia walifahamika kama matapeli wenye tabia ya kughushi hundi za bandia. Mmoja hakuwa na akili timamu. Alikuwa kavaa vizuri anazungumza kama kawaida. Hata hivyo, iliwachukua polisi saa nzima kugundua kuwa wanazungumza na punguani.

Inspekta Kombora aliandika maelezo mafupi ya jalada hilo. Aliagiza wasio na hatia waachiwe mara moja. Kisha, akalitupa kando na kuvuta jalada la mwisho ambalo ndilo hasa alilolihitaji, taarifa ya mienendo ya magari mawili ambayo aliyatilia shaka. Maelezo yalikuwa mafupi, lakini yakiwa wazi kabisa.

Datsun TZA 42112 ni mali ya Swaleh Akbar, Mwarabu mwenye damu mchanganyiko, mama mswahili wa Rufiji, aliondoka nchini zaidi ya miaka kumi iliyopita na kuhamia Oman ambako amerudi juzi na malori matatu, basi kubwa la abiria na gari hilo dogo la kutembelea.

Akiwa na umri wa miaka ishirini na mitatu tu, Swaleh ni mtundu na mtumiaji kupita kiasi. Kila jioni gari lake huwa liko njiani, katika majumba ya starehe. Katika usiku mmoja gari lake linaweza kuonekana katika majumba kumi ya starehe. Si mnywaji sana, lakini anapenda sana kunywa katika makundi huku akinunua bia kama maji.

Baada ya kupokea amri ya kulisaka gari hilo askari wa barabarani walilipata mnamo saa kumi kasoro, likitokea Buguruni. Lilikuwa likielekea Kariakoo. Ghafla waliliona likibadili njia na kuelekea Keko. Sasa hivi gari hilo liko mbele ya nyumba moja mbovumbovu, hukohuko Keko. Askari mmoja wa Kombora ameichukua kazi hiyo toka mabegani mwa polisi wa Usalama Barabarani. Analitazama gari hilo toka mbali, akiisubiri amri ya Kombora.

Kombora aliwaza kwa muda, kisha, akaichukua kalamu yake na kuandika juu ya karatasi hiyo, “Watu wawili zaidi waende huko. Watumie njia yoyote kuingia humo ndani, kuona wanafanya nini na kama ni watu wetu waletwe mara moja.”

Taarifa ya pili ilikuwa fupi zaidi, lakini Kombora aliisoma kwa makini zaidi. Si kwa ajili ya hisia ambazo zilikuwa zikichemka katika roho yake tu, bali kwa kuwa aliona taarifa nyingine zote hazikumpa hali aliyotarajia.

Gari dogo aina ya Toyota Corolla TZB No. 414 lilionekana katika Barabara ya Ocean likitembea taratibu. Lilipofika mbele ya Hoteli ya New Africa, lilipaki na dereva wake kuingia hotelini ambamo alionekana kuchukua ufunguo mapokezi na kupanda lift hadi ndani ambako yaelekea amelala.

Gari hili ni mali ya kampuni moja ya ukodishaji magari iitwayo Shabir Safaris Limited ya Morogoro. Kwa mujibu wa mwenye kampuni hiyo, Shabir Datoo, gari hilo lilikodishwa wiki mbili zilizopita kwa Mmarekani mweusi mmoja na mkewe, hati ya usafiri namba… iliyotolewa mjini Miami miaka minne iliyopita chini ya jina la Morrice Juakali.

Huyu ni mtu wetu! Kombora aliwaza akiisoma tena taarifa hiyo. Alitafuna ncha ya kalamu yake kwa muda kabla hajainama na kuandika katika jalada hilo.

“Ongezeni ulinzi nyuma na mbele ya hoteli. Kila mmoja awe na silaha na awe na picha halisi ya mtu wetu akilini. Kila hadhari ichukuliwe kumfanya mtu huyu asishuku anachunguzwa. Na mara tu atakapoonekana akitoka nitaarifiwe mara moja.”

Baada ya hayo Kombora alijaribu kutulia kwa kuagiza aletewe kahawa huku akivuta jalada la Kakakuona na kuanza kulipekua tena. Japo alilisoma mara kadhaa swali lilelile lilikuwa wazi, bila majibu yoyote, rohoni na akilini mwake; Kakakuona anahitaji nini kwa Joram Kiango? Kwa mara nyingine aliamua kuliweka swali hilo kando na kuendelea kusubiri kukamatwa kwa Kakakuona.

Alipoikumbuka kahawa yake tayari ilikuwa imepoa tena.


‘Mchezo umeanza kuwa mtamu,’ Kakakuona aliwaza akichungulia dirishani katika tundu dogo aliloliunda kwa kutoboa pazia la dirisha. Akiwa mtu mwenye uwezo wa kumnusa polisi hata awe wapi, hakuwa kipofu wa kushindwa kuwatambua watu walioiinamia injini ya teksi aina ya BMW, iliyoegeshwa mbele ya hoteli hiyo, kando ya gari lake, kuwa ni polisi.

Mtu wa tatu alikuwa ameongezeka, polisi pia. Chumba chake kikiwa upande mzuri, ghorofa ya tano katika hoteli hii, alikuwa na nafasi nzuri sana ya kuwatazama.

Tangu usiku alipokuwa akirejea toka ufukoni, ambako alimshughulikia kikamilifu yule msichana na kumwacha maiti baada ya kuiharibu sura yake, Kakakuona alihisi kuwa anafuatwa. Hakuwa na hakika.

Hivyo, alifanya hila za kupita hapa na pale, kupinda kona hii na ile, kupunguza na kuongeza kasi n.k. Wakati alipoamini kuwa amelipoteza gari hilo aligeuza njia na kuja New Africa. Alipokuwa akivikusanyakusanya vifaa vyake na kuvitia katika briefcase ndipo alipoliona gari hili likizimika katikati ya barabara na watu wawili kushuka. Walilivuta hadi kando ya gari lake na kulifunua boneti. Kisha, wakafunga hiki na kufungua kile. Hawakuinua uso kumtazama, lakini Kakakuona alijua kabisa kuwa wako pale kwa ajili yake. Alitulia katika gari kwa dakika kadhaa akivuta sigara huku mkono wake ukiipapasa bastola yake, Alipoona hawamjii alifahamu kuwa askari hao hawakuwa na amri ya kumkamata. Hivyo, aliingia chumbani ambako, alioga akaweka vifaa vyake sawa na kisha akazima taa na kujilaza kitandani.

Nusu saa baadaye aliamka na kuwachungulia. Mtu mmoja alikuwa ndani ya gari wa pili akiendelea kuhangaika na injini ‘Watasubiri sana’ aliwaza akijilaza tena na kujaribu kuwaondoa akilini.

Hata hivyo, akili yake haikumruhusu kustarehe. Hisia za hofu, kitu ambacho kwa kawaida hakimo kabisa katika damu yake, zilikuwa zikimnyemelea. Alijihisi akijilaumu na kujutia uamuzi wake wa kwenda Lang’ata na kumfuata yule msichana ambaye aliamini kwa namna moja au nyingine amekuwa chanzo cha polisi kumnusa mapema namna hiyo.

Pamoja na ukweli kuwa hakuwa hata na chembe ya hofu ya kukamatwa na polisi hao, bado hakuona kama ilimstahili kushukiwa mapema hivyo, jambo ambalo lingemfanya aanze upya maisha ya kujifichaficha hata kabla ya kwenda kuyazoa yale mamilioni ambayo yanamsubiri pindi atakapomfikisha Joram Kiango au mzoga wake mbele ya wadhamini wake.

‘Hawana lolote la haja wanalofahamu juu yangu,’ aliwaza. ‘Wangekuwa nalo wangekuwa wamekwishanipigia hodi. Nitalala zangu kwa amani. Kesho mchana nitamshughulikia Joram na kisha kumfuata Chongo popote alipojichimbia.’

Sasa ilikuwa saa mbili asubuhi. Gari lile lilikuwa likiendelea kuchokonolewa. Mara liliwaka. Wale watu wawili wa mwanzo walitabasamu. Baadaye walionekana wakimlipa yule mtu wa tatu na kisha kuondoka zao. Yule mtu wa tatu alitazama huku na huko, kisha, akavuka barabara na kuanza kutembea taratibu kando ya Benki ya City Drive hadi alipotokomea, miongoni mwa watu wengine.

Kakakuona hakuwa mtu wa kuingia katika mtego mdogo kama huo. Alijua fika kuwa kuondoka kwa watu hao ni kubadili zamu tu. ‘Wako wengine sehemu nyingine, ambao wananichunguza kwa makini. Acha waendelee kupoteza muda wao,’ aliwaza akiingia bafuni ambako alioga, akabadili nguo na kisha kupakia vitu vyake vyote muhimu katika briefcase yake maalumu. Kisha, akawaita wahudumu wa vyumba na kuagiza kifungua kinywa na gazeti la Daily News. Alikunywa chai yake kwa utulivu huku akilipekuapekua gazeti hilo.

Mara macho yake yakavutwa habari fupi iliyopachikwa kando katika ukurasa wa nne. Ilieleza juu ya mtumbwi wa mashine ambao uliokotwa baharini na wavuvi wa Zanzibar, ukiwa na maiti ya mtu mwenye jeraha la risasi. Habari hiyo iliendelea kueleza kuwa marehemu huyo alikutwa na bastola mfukoni mwake, jambo ambalo lilifanya iaminike kuwa alijiua mwenyewe.

Maelezo juu ya umbile na mavazi ya hayati huyo, yalimfanya Kakakuona amtambue mara moja. ‘Chuchu’ alinong’ona. ‘Chongo amemuua. Sasa bado zamu yake.’

Alitazama saa yake, tatu kasoro. Akainuka, akauchukua mkoba wake na kutoka nje ya hoteli. Baadaye akamtupia macho msichana wa mapokezi ambaye alikuwa akimchekea kana kwamba yuko katika mashindano ya kutabasamu. Akalifuata gari lake na kuingia.

Alhaji Salum Banduka ni mmoja kati ya watu wanaojiheshimu na wanaoheshimika sana mjini Zanzibar. Tangu alipohamia hapa toka Bara, aliondokea kuwa mtu ambaye kila mtu alipenda kumtolea mfano.

Tazama aliingia hapa hana kitu zaidi ya mtaji wake wa shilingi elfu ishirini, kanzu moja, suruali ya pili na makubazi miguuni. Tripu nane za Bara na Pemba zilimfanya aache biashara ya chakula na kuanza kwenda zake Uarabuni. Leo hii tayari anayo maduka matatu, daladala nne na hoteli kubwa ya kitalii!

Tazama! Pamoja na utajiri wote huu hata sala moja haimpiti. Tayari amehiji Makka mara tatu na anatarajia kwenda tena mwaka huu. Wala hana kiburi. Kila siku huwa yupo katika magenge ya vijana na wazee akisimulia jinsi shilingi elfu ishirini zilizomfanya awe tajiri.

“Hawakukosea wazee waliposema, “Akili ni mali…” Banduka alipenda sana kuitumia methali hiyo mwisho wa maelezo yake, kwa sauti ya kicheko.”

Huyo alikuwa Banduka wanayemjua wao; mtu mfupi, mnene, mwenye tumbo la kutosha na kovu lililomeza nusu ya shavu lake la kushoto, mtu ambaye alitulia na wake zake wawili, mmoja akiwa na damu ya Kiarabu wa pili ya Kimvita.

Kama wangefahamu kuwa Banduka huyuhuyu ndiye yule aliyevuma sana huko Bara zaidi ya miaka kumi iliyopita kwa ushiriki wake katika wizi, ujambazi na mauaji, kamwe wasingempa hadhi msikitini wala heshima mtaani.

Kama wangejua kuwa kuja kwake visiwani ilikuwa ni kujificha baada ya kushiriki katika kazi nzito ambayo iliacha familia nzima ya Mhindi mmoja mahututi hali wao wakiondoka na milioni saba kamwe visiwa hivi vya amani na utulivu visingempokea.

Banduka alikuwa na bahati ya mtende. Siku hiyo kazi yake ilikuwa ndogo tu, kukaa chonjo, bastola mkononi, akilinda mtu yeyote ambaye angetokea kuitibua kazi yao katika nyumba hiyo. Kazi ilikwisha kwa amani. Yeye, ambaye hakujitokeza mbele ya uso wa Mhindi, akapewa jukumu la kulinda furushi hilo la fedha ili ikipoa wagawane.

Kama muujiza, usiku huohuo wenzake wote walikamatwa. Yeye akatoroka na jahazi la makasia hadi hapa ambapo alijichimbia. Kwa kuwa haukupatikana ushahidi wa kutosha wenzake walichukua miaka saba, saba. Hakuna aliyemtaja.

Ndipo alipolivua jina lake la Bandua na kujiita Banduka. Akauvua ujambazi pia katika fikra zake na kuapa kuwa kamwe asingejihusisha nao tena kwa namna yoyote.

Lakini kiapo chake hicho hakikudumu muda mrefu. Mara tu alipoanza kuipanua miradi yake alijitokeza askari kanzu mmoja ambaye jioni moja alijipenyeza hadi katika chumba chake cha sala. Banduka alishtukia mtu kasimama mbele yake akitabasamu kifedhuli.

“We’ nani?” alifoka.

“Usitake kunifahamu. Suala ni kwamba mimi nakufahamu wewe. Unaitwa Alhaji Banduka. Mimi najua kuwa wewe ni Bandua, mwizi, muuaji na tapeli mkubwa ambaye unasubiriwa Bara kwa hamu kubwa sana. Kataa…”

Banduka aliduwaa. Hakutarajia kuwa kisiwani hapa kulikuwa na binadamu yeyote anayehifahamu rekodi yake.

“Usishangae,” askari huyo alimzindua “Wewe una pesa, mimi ninayo siri yako. Leta pesa nikufichie siri. Vinginevyo, kesho hutakuwa huru.”

Baada ya ubishi mrefu, Banduka akijaribu kukanusha, aligundua kuwa kidudumtu huyo alikuwa na ushahidi tosha dhidi yake.

“Unataka kiasi gani?” alimuuliza.

“Milioni tatu tu.”

“Milioni tatu!” Banduka alifoka. “Una wazimu!”

“Labda. Lakini ni milioni tatu au roho yako. Mimi pia nimechoka kukesha usiku na mchana nikiwalinda wenye pesa zao. Nataka kupumzika kama wewe.”

Baada ya ubishi mwingine mfupi Banduka aliafiki. “Njoo kesho kuchukua.”

Kauli hiyo ilimfanya askari huyo aangue kicheko. “Nina akilia bwana Banduka. Mara tu nikiondoka utaanza kubuni mbinu za kuniangamiza. Pesa hizo nazitaka leo. Sasa hivi. Nimeingia humu kwa siri bila ya mtu yeyote kuniona ili tumalizane kabisa. Nikitoka kila mtu ajue lake.”

Kipande hicho cha habari kilimsaidia sana Banduka. Alikuwa amechoka kusumbuka. Alikuwa ameishiwa na hamu ya kufungwa na kuwakimbiakimbia polisi. Alivuta droo yake ndogo kama anayetaka kuchukua ufunguo. Alipoutoa mkono wake ulikuwa umeshikilia kisu chake kirefu ambacho dakika hiyohiyo kilipotelea katika kifua cha askari huyo, ambaye hakuwahi kupiga hata kelele. Alianguka hali katokwa macho kwa mshangao na maumivu.

Banduka aliifanya kazi ya kufuta damu na kumzika marehemu kwa siri sana. Kisha, akatulia kusikiliza kama kuna mtu yeyote ambaye angemuunganisha yeye na “kutoweka” kwa askari mgeni aliyetokea Bara. Wala.

Ikafuata miaka ya starehe, amani na utulivu. Banduka akaweka kiapo kingine cha kutojihusisha tena na aina yoyote ile ya ujambazi, kiapo ambacho leo hiihii alikikumbuka na kuanza kukitilia shaka kama kweli atatimiza.

Alfajiri hii aliamka mapema, kama ilivyokuwa kawaida yake ili aende zake msikitini. Alipoitazama saa yake aligundua kuwa alikuwa ameamka nusu saa kabla ya muda wa sala. Akiwa chumbani peke yake, baada ya mkewe mkubwa kwenda zake Bara, aliamua kuamka na kuoga. Akajaza maji baridi katika beseni la kuogea na kuyapoza kwa maji moto kidogo. Wakati akivua taulo alilojifunga kiunoni ili ajitumbukize alihisi mlango wa bafuni ukifunguka na umbo la mtu kujipenyeza.

“Nani?” alifoka kwa mshangao.

“Taratibu, aisee. Mie wako. Tuseme umenisahau?”

Banduka alimtazama mtu huyo aliyeingia kama kivuli. Roho ikamlipuka. Miaka zaidi ya kumi iliyowatenganisha katu isingemfanya amsahau Chongo, mmoja kati ya watu ambao Banduka hakupenda kabisa kuwatia machoni. Hisia za hatari zilimwingia. Aliduwaa kwa muda kabla hajauliza kwa sauti ya unyonge, japo ilijaa hasira, “Umeingiaje humu?”

“Nimeingiaje? Mimi na wewe! Usiniambie kuwa umekuwa bwege kiasi hicho Banduka. Jumba lako hili halina kufuli hata moja. Kila nilipokuwa nikija hapa Zanzibar kutumia, nilikuwa naitembelea nyumba yako kuichunguza. Nilishangaa unavyoishi kama ndege ukijifanya mswahilina. Nasikia hata Makka umekwenda. Si umekwenda tu kuutia nuksi mji ule takatifu? Wewe ni wa kwenda Maka!”

Hofu ilianza kumtoka Banduka. Akijua kila dakika anayokaa na mshenzi huyo ilikuwa ikihatarisha usalama wake, alimwambia kwa ukali kidogo, “Sijui umefuata nini hapa. Sina hamu ya kuisikiliza sauti yako mbovu wala kuitazama sura yako nzuri. Inatosha. Sasa ondoka niendelee na sala zangu.”

“Sala!” Chongo alicheka. “Sala! Ha! Ha! Wadanganye binadamu usimdanyanye Mungu. Sala zako hazitoki nje ya chumba hiki, Banduka,” alisema na kuongeza, “Unajua Banduka nakudai pesa nyingi, mamilioni. Nafahamu kuwa ulitusaliti ukituacha tuozee gerezani hali wewe unatumia pesa zetu. Lakini hakuna anayekulaumu. Hakuna mwenye shida kati yetu. Kwa upande wangu mimi sihitaji utajiri. Nahitaji pesa kidogo za kula. Lakini kwako sihitaji pesa. Nahitaji hifadhi kwa siku mbili tatu tu. Niko na mpenzi wangu.”

“Siwezi kukupa hifadhi. Katafute pengine.”

ITAENDELEA

Roho ya Paka Sehemu ya Pili

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment