Roho ya Paka Sehemu ya Nne
NEW AUDIO

Ep 04: Roho ya Paka

SIMULIZI Roho ya Paka
Roho ya Paka Sehemu ya Nne

IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA


Simulizi : Roho Ya Paka

Sehemu ya Nne (4)

Kombora alianza kupandwa na hasira juu ya watu hawa. Aliona wazi kuwa ama walikuwa punguani wa akili kama ilivyokuwa kwa baadhi ya viungo vyao, ama walikuwa wakimdhihaki. Akaamua kucheza mchezo waliotaka wao. Aliinuka akawashukuru na kutoka nje huku akihisi kila jicho linaloona, la kila mmoja kati yao, likiwa limemganda mgongoni huku linamcheka.

Alipanda gari na kuamuru liondoke. Baada ya kupinda kona moja alisimamisha gari na kumwamuru kachero mmoja arejee na kutafuta uwezekano wa kuilinda ofisi hiyo kwa makini bila ya yeye mwenyewe kuonekana.

11

Ilikaribia saa kumi na mbili Kombora aliporejea ofisini kwake kama mgonjwa aliyeruhusiwa kutoka hospitali baada ya kukata tamaa ya kuendelea kuishi. Alijibweteka juu ya kiti chake na kujiinamia kwa muda, mikono yake yote miwili ikiwa imekilea kichwa chake.

‘Msichana mzuri, asiye na hatia yuko mikononi mwa muuaji wa hatari, aliwaza kwa uchungu, mbele ya macho yangu mwenyewe jambazi huyohuyo ameua watu wawili wasio na hatia… Na ametoweka…mbele ya macho yangu mwenyewe. Mimi … ambaye najiita mkuu wa kikosi hiki…’ alishindwa kuendelea kufikiri. Hasira zilikuwa zimefura katika kichwa chake kiasi cha kufanya ubongo wake ukitishia kuchemka. ‘Lazima nitunze kichwa changu,’ alinong’ona kimoyomoyo huku akiiitoa mikono yake kichwani na kuipeleka mezani ambako ilirudi na faili ambalo hakulihitaji. Alilitupa mezani hapo na kuiingiza mikono mfukoni ambamo alitoka na kile kijitabu cha maelezo ya kampuni ya Kangaroo. Alikipekuapekua kwa dakika chache kabla hajainua simu na kumpigia mmoja wa wasaidizi wake, ambaye alifika mbele yake mara moja na kupiga saluti ambayo haikujibiwa.

“Fanya kila unaloweza nipate taarifa za kampuni hiyo kabla ya saa mbili,” alimwamuru akimwonyesha kijitabu hicho. “Nataka kujua imeanzishwa lini na wapi, hapa nchini imeingia lini, nani hasa mwenye kampuni hiyo, shughuli zake hasa ni zipi na kila unachoweza kupata. Zaidi, jitahidi nipate kila ambalo linaweza kupatikana juu ya wakurugenzi wake wawili walioko hapa, Paul Powel na Philip Benjamin. Tumia watu wote unaoweza kuwapata. Upo?

“Nipo afande.”

“Haya! Bado unasubiri nini zaidi?”

Amri ya pili ambayo Kombora aliitoa na kumtaka Sajin Kangura mwenyewe kuhakikisha inatekelezwa mara moja ni ile ya kupata ramani ya majengo ya Sunrise Modern Club na Kangaroo Enterprises katika muda wa saa mbili.

“Ni zaidi ya saa mbili sasa, afande. Ofisi ya Ardhi na jiji zitakuwa zimefungwa…”

“Zinaweza kufunguliwa. Kama wanaohusika hawapatikani mtafute waziri wao azifungue. Na kama hana funguo mwambie azivunje.”

“Ndiyo, afande.”

Kombora alipobaki peke yake alijaribu tena kukisoma kijitabu cha maelezo ya kampuni ya Kangaroo. Maelezo yalikuwa mengi, marefu yaliyowekwa katika mpangilio ambao ungemfanya msomaji yeyote ahisi kuwa kampuni hiyo ilikuwa moja ya makampuni makubwa sana duniani. Yalitaja matawi yake katikasehemu mbalimbali za dunia. Hata hivyo, ilimshangaza Kombora kuona kuwa anuani za matawi hayo hazikutajwa wala makao makuu, ambayo yalidaiwa kuwa yako New York, Marekani. Hali kadhalika, zaidi ya Powel na Philip, kijitabu hicho hakikuwa na jina jingine la Mkurugenzi yeyote.

Hayo yaliyoongeza mashaka ya Kombora juu ya kampuni hiyo, mashaka ambayo yalianza tangu alipowatia machoni wakurugenzi hao wawili, ambao pamoja na kutojiweza kwao hawakuonekana kuwa na lugha ya biashara hata chembe. Kwa ujumla, Kombora hakuwaona kama wafanyabiashara. ‘Kama wanafanya biashara, lazima biashara hizo zitakuwa haramu,’ aliwaza. ‘Si biashara walizoziorodhesha hapa.’

Kombora alijua ambacho angefanya kesho. Alijua kuwa angehitajika kuwataka msaada polisi wa kimataifa, Interpol, toka nchi zote ambazo Kangaroo ilizitaja kuwa ina matawi yake na kumwomba juu ya uhalali wa makampuni hayo, biashara halisi wanazozifanya na taarifa kamili za wakurugenzi wake.

Hilo lilikuwa la kesho. La leo ambalo lilikuwa likimsumbua Kombora na ambalo lisingesubiri kesho lilikuwa la kumtoa Nuru mikononi mwa Kakakuona, akiwa hai. Alitazama saa yake na kuona ikikaribia moja na nusu usiku; lakini hajapata bado jibu toka kwa watu aliowataarifu kupata taarifa za Kangaroo, jengo lao na lile la Sunrise. ‘Wako wapi hawa’ alinung’una akiinua uso wake kutazama mlangoni.

Juu ya meza yake Kombora alishukuru kuona kuwa mtu mmoja alimwekea chupa ya chai au kahawa na mayai matatu ya kuchemsha. Ndio kwanza akahisi kuwa alikuwa na njaa kali. Akavunja yai moja na kulitafuna. Yai la pili vilevile alilila kavukavu. La tatu ndilo aliloshusha kwa chai nzito ya maziwa toka katika chupa. Baadaye, aliinuka na kuukamilisha mlo wake kwa glasi mbili za maji toka katika friji yake ndogo ya ofisini. Wakati akirudi mezani simu ililia. Kombora aliinyakua na kuidaka masikioni mwake.

“Afande, Kabweka hapa.”

“Najua, uko wapi?”

“Napiga toka bandarini, nilikuwa katika kuhakikisha kama kweli hawa Kangaroo wanaingiza vitu toka nje.”

“Enhe!”

“Ni waingizaji maarufu wa vitu vya nje, Mzee, nimeona mizigo yao mingi ambayo haijatolewa. Nimeambiwa pia kuwa safari hii wamekodi meli mbili. Moja inatarajiwa kuanza kushusha mali zao wakati wowote. Ya pili haijapata nafasi ya kuingia bandarini, imetia nanga nje kidogo ya pwani.”

Hazikuwa habari nzuri sana kwa Kombora. “Ni hayo tu uliyoyapata?” Kombora aliuliza akitaka kuthibitisha kama hakukuwa na habari nzuri zaidi.

“Ndiyo mzee, lakini…”

“Lakini nini?”

“Kuna jambo moja ambalo limenitatanisha.”

“Lipi?”

“Hawa wakurugenzi wake. Idara yetu inayoshughulikia taarifa za wageni haina lolote kabisa juu ya Philip na Powel. Hakuna kinachofahamika zaidi ya kuwa ni raia wa Urusi ambao walikwenda Angola kuwasaidia wazalendo dhidi ya Wareno, wakati walipokuwa wakipigania uhuru wao. Taarifa hizo hazionyeshi maisha yao huko Urusi, waliondoka lini na walikuwa wakipigana kikosi kipi. Zinaonyesha kuwa MPLA tayari wameulizwa juu ya watu hawa na wakashindwa kutoa majibu. Wanasema kwa kuwa watu wengi vitani hupenda kutumia majina ya bandia huenda watu hao walishiriki. Urusi nako, kikosi chao cha KGBkimesema hakina majina hayo katika kumbukumbu zao.”

Kombora alimsikiliza kwa makini, “Kwa hiyo, unawafikiriaje watu hawa, Kabweka?” Kombora alimwambia.

“Nahisi kuna kitu wanaficha na kuna kitu zaidi wanafanya. Inawezekana hawa ni wanachama wa kikundi cha Mafia ambao wanajishughulisha na biashara haramu za dawa za kulevya au nyara za serikali,” alieleza na kuongeza kwa sauti ya kujiamini. “Inawezekana mzee, hawa ni maadui wa Joram Kiango.”

“Ahsante kwa mchango wako. Endelea na usikose kuniarifu kila utakapopata kitu kipya,” Kombora alisema akiitua simu chini.

Papo hapo ikaita tena. Safari hii aliyepiga alikuwa Sajin Kangura. Alikuwa akipiga toka Halmashauri ya jiji. Alimwarifu Kombora habari ambazo zilimsisimua zaidi. “Inashangaza, afande. Si wizara ya Ardhi wala jiji ambao wana nakala ya ramani ya majengo hayo yote mawili.”

“Kwanini?”

“Haieleweki. Jiji wanadai kuwa wana hakika walikuwa na nakala za majengo hayo lakini hawazioni. Hata hivyo, mmoja wa maafisa wa jiji ananieleza kuwa jengo la Sunrise lilikuwa dogo la ghorofa moja lakini liliibuka ghafla na kupanuliwa hata kabla ya kukamilisha taratibu za ujenzi. Kuwa waliingia katika mgogoro na mwenye jengo hilo ambapo baadae ulitatuliwa na akaruhusiwa kundelea.”

“Hamkuweza kumpata mwenye jengo hili awapeni ramani hiyo?” Kombora alimwuliza.

“Yeye pia yalimkuta makubwa,” Kombora aliambiwa “Inadaiwa kuwa huu mwaka wa tatu tangu alipotoweka”

“Katoweka!”

“Ndiyo, afande. Tumeambiwa kuwa bwana huyo, Fabian Kalila, ambaye alikuwa maarufu kwa ujenzi mara tu baada ya kukamilisha jengo hilo la Sunrise aliaga siku moja kuwa anakwenda Kigamboni kukagua uwanja mpya ambao ulihitajiwa kujengwa nyumba ya pili. Bwana huyo alifika hadi Ferry ambapo alionekana akizungumza na watu anaofahamiana naye.Watu waliomwona kwa mara ya mwisho walidai alipanda na kwenda ng’ambo. Lakini huko ng’ambo hakuna aliyemwona, yametolewa matangazo magazetini na maredioni lakini hazijafika taarifa zozote juu yake, wala maiti yake.”

“Naam, iko namna,” Kombora aliropoka kwa namna ya mtu anayezungumza peke yake.

Kangura alikuwa akiendelea, “pamoja na hayo, afande, tumefanya upekuzi mkubwa katika makabrasha yake yote, tumeweza kuona karibu nakala za majengo yote aliyowahi kushughulikia isipokuwa hili la Sunrise na Kangaroo. Hatukuweza kupata hata zile za majaribio.”

“Ni yeye aliyeshughulikia jengo lile pia?”

“Ndio, afande”

Kombora hakujua afanye nini zaidi. Alichanganyikiwa kupita kiasi. Kwa ujumla, hakujua kama anakwenda mbele au anarudi nyuma katika suala hilo. Alitua simu chini bila kusema neno lolote zaidi.


Mtu mwingine aliyekuwa jengo Fulani mtaa fulani, wa jijini hapo, baada ya kuyasikiliza maongezi hayo ya Kombora na wasaidizi wake aliitua simu yake chini taratibu. Kisha, akakichunguza chombo chake cha kunasia sauti kuona kama kilikuwa kinafanya kazi vizuri.

“Not so bad” alitamka, akitabasamu. Aliitoa kanda hiyo na kuitia mfukoni mwake. Akategesha upya chombo chake na kisha kuondoka zake toka chumbani humo, tabasamu likiwa bado usoni mwake.


Mtaa wa tatu toka hapa mtu mwingine alikuwa akitabasamu. Lakini hili lilikuwa tabasamu lake la kwanza kwa siku hiyo, na pengine kwa wiki hiyo. Mtu huyo aliitwa Joram Kiango.

Kama ungemtazama harakaharaka alivyoketi juu ya kochi, ndani ya chumba alichokodi katika hoteli hii ya Mawenzi usingemfikiria kabisa kuwa alikuwa na tatizo kubwa la kutisha ambalo lingetosha kabisa kumtia kichaa. Badala yake ungemwona kijana mtanashati, aliyevaa suti yake nyeusi iliyomkubali vilivyo; akiwa ameketi juu ya kochi pana glasi ya wiski ikiwa mbele yake, sigara mkono mmoja na simu mkono wa pili.

Hali hii ilimrejea joram baada ya kujiaminisha tena na tena kuwa alihitaji kutuliza kichwa chake ili kupambana kikamilifu na janga hilo. ‘wewe ni Joram Kiango’ nafsi yake ilimwambia, ‘Endelea kuwa Joram Kiango vinginevyo Nuru utampoteza na maisha yako yatapotea.’

Hakujali sana juu ya maisha yake lakini alipomkumbuka Nuru na ukatili wa watu wanaomshikilia, alituliza akili yake na kuwa Joram Kiango. Na kwa mshangao wake alikuta akili yake ikichemka kwa ukamilifu kama betri zilizochajiwa upya.

Aliwakumbuka marafiki zake wote, wa nje na ndani. Namba zao za simu teleksi na faksi ziliibuka kama chemichemi akilini mwake. Akiwa na pesa za kutosha haikumchukua muda kukifanya chumba hicho kidogo kigeuke ofisi kubwa ya mawasiliano ambayo yalitoka huku na huko.

Simu yake ya kwanza ilimwendea rafiki yake mmoja anayemiliki kampuni yake binafsi jijini. Huyu akiwa ni mtu ambaye kila kitu kwake ni biashara, alikuwa anafahamu kila mtu na kila kampuni jijini Dar es Salaam. Hivyo, Joram alipomwuliza anafahamu nini juu ya Kangaroo Enterprises rafiki yake aliangua kicheko.

“Vipi? Sioni kama jina hilo linachekesha,” Jorama alimsaliti.

“Sio jina braza, ni pesa” Sauti ilijibu toka upande wa pili.

“Pesa?”

“Pesa hazina macho,” alieleza na kuongeza “pesa, kwa kweli mara nyingine inapotea njia.”

“Sijakuelewa?” Joram alimkumbusha.

“Kwani hujawaona wakurugenzi wa kampuni hiyo?”

“Wakurugenzi gani?”

“Powel na Philip.”

“Wanakasoro gani?”

“Swali sio wana kasoro gani , ila kasoro gani hawana” kicheko “Wale mabwana ukiwaona utafikiri pacha. Wenyewe wanadai hawana undugu wowote. Ukiwaona utadhani ndio kwanza wanaibuka toka kaburini; utafikiri waliwekwa katika pipa wakachemshwa na kisha kutolewa kabla ya kukata roho. Mmoja ni nusu kipofu asiye na mkono wa pili, mwingine nadhani kiziwi na hana mkono mmoja. Kwakweli mabwana wale ni watu wa kuchekesha sana.”

“Sioni wamewezaje kupata pesa,” Joram alichochea.

Baada ya maswali mengi alibaini kuwa kampuni ya Kangaroo Enterprises ni mpya inayoongozwa na watu wasiojiweza, Paul powel na Philip Benjamin. Pamoja na kwamba kampuni hiyo ilidai inajishughulisha na mambo mengi, lakini taarifa alizozipata ni kuwa kazi kubwa ambayo kampuni hiyo imekwishafanya ni uingizaji wa pickup, bidhaa toka nje na kuzisambaza kwa wauzaji mbalimbali wa jumla jijini. Bidhaa yao kubwa, Joram aliarifiwa, ni vipodozi vya aina kwa aina, hasa kwa kina mama.

Alifahamishwa kuwa kampuni hiyo ilijenga maghara yake kando ya barabara ya Nelson Mandela katika eneo la Tabata.

Joram alimshukuru rafiki huyo na kumtaka amwarifu kila atakachokipata juu ya wakurugenzi hao wawili.

Rafiki yake mwingine alikuwa miongoni mwa vijana wa Inspekta Kombora. Kila alipopata wasaa aliwatoroka wenzake na kumdokeza Joram juu ya kila tukio. Alimfahamisha jinsi ambavyo Inspekta Kombora alikuwa taabani baada ya watu wawili wasio na hatia kuuawa mbele yake na Nuru kutoweka mbele ya macho yake. Aidha, alimfahamisha juu ya harakati zote ambazo zilifanyika kulikagua jengo hilo na majengo yote ya jirani bila mafanikio yoyote.

“Sasa hivi ukimwona mzee Kombora utadhani ana umri wa miaka mia moja, kwa jinsi alivyozeeka ghafla,” Rafiki huyo alidokeza katika maongezi hayo.

Baada ya Joram kuuliza kwa makini ukubwa wa jengo la Sunrise Modern Club, Kangaroo Enterprises zilivyojengwa ndani na nje, sehemu ambayo Kakakuona alimwua dereva wa taksi na alipomwua msichana wa mapokezi, na mengine mengi, alipatiwa majibu yote aliyoyahitaji kwa kiwango cha kuridhisha. Maelezo hayo yalifuatwa na onyo, “Joram kama unakusudia kufuata nyayo za Kakakuona, lazima ujihadhari sana. Huyu sio mtu wa kawaida. Mambo aliyoyafanya hapa ambayo nimeyaona kwa macho yangu sio mambo ya kawaida. Labda tunayoona katika filamu baada ya watu wa studio kuweka utaalamu wao. Huyu si binadamu ningekushauri ufikirie mara mbili.”

Ni hilo ambalo lilimfanya Joram atabasamu kwa mara ya kwanza siku hiyo. Yalimchekesha mengi. Moja likiwa lile la kujua kuwa nje ya maadui, ni yeye peke yake ambaye alifahamu kuwa Kakakuona hayuko duniani tena. Jingine alipoona rafiki yake huyo asivyomwelewa kikamilifu kwa kumtahadharisha kumfuata Kakakuona. Laiti angejua kuwa alikuwa tayari kumfata hadi kuzimu, na kuhakikisha akirejea na Nuru, akiwa hai au salama! Hata hivyo, Joram alimshukuru rafiki huyo na kumtaka aendelee kuwa macho.

Joram alipata msaada mkubwa zaidi toka kwa rafiki yake mmoja wa kampuni ya simu. Huyu, alimwezesha kupata moja kwa moja mawasiliano yote ya simu yaliyokuwa yakiendelea katika ofisi ya Kombora kwa kuiunganisha na laini moja ya hoteli ambayo Joram aliikodi kwa bei mbaya.

Mawasiliano hayo yalimpunguzia Joram kazi kwa kiasi kikubwa. Hakuhitaji tena kujishughulisha na uraia wa watu hao kwa wakati huo kutokana maongezi baina ya Kombora na msaidizi wake. Hakuwa na haja tena ya kutafuta ramani ya majengo hayo wala ujenzi wake kutokana na taarifa hizohizo. Hali kadhalika, asingepoteza muda wa kutafuta habari za kampuni hiyo huko nje kwani tayari ilionyesha kuwa taarifa zao sio za kweli. Zaidi, Joram hakuwa na wasiwasi juu ya Nuru kuhamishwa toka jengo hilo kwa kujua kuwa vijana wa Kombora walikuwa wakilinda doria na kumtaarifu juu ya kila tukio lililotendeka, taarifa ambazo yeye pia alikuwa akizipata.

Kitu ambacho kwa sasa kilisumbua sana akili ya Joram Kiango kilikuwa kushindwa kuoanisha maelezo juu ya maumbile ya wakurugenzi hao wa Kangaroo na mkasa huu mzima. Kama kweli ni watu wasiojiweza,wenye biashara zao halali, vipi wajihusishe na ujasusi huo wa kimachomacho? Watakuwa wanajiamini nini?

Kitendo chao cha kumteketeza Kakakuona hata kabla hajakamilisha jukumu alilopewa pia lilimtatiza. Kama wangemwua Kakakuona na kisha kumwachia Nuru angeweza kuelewa. Ingekuwa ishara ya kukubali kushindwa. Lakini kumwua Kakakuona, na kuendelea kumshikilia Nuru kwa vyovyote vile ni dalili ya kutangaza shari zaidi, shari ambayo kwa maumbile yao yalivyo, wasingeweza kuitekeleza bila msaada wa mtu mwingine mwenye uwezo na akili timamu zaidi ya Kakakuona.

Joram alihitaji kumfahamu mtu huyo kwa gharama yoyote ile kwani ni yeye tu aliyekuwa kipingamizi baina yake na Nuru. Vinginevyo, angeweza kwenda zake, mchana kweupe, na kumpokonya Nuru toka mikononi mwao.

Simu ililia. Akaipokea na kuisikiliza, kisha akaitua, haikuwa na kitu cha muhimu.

Teksi ikapata uhai. Taarifa ilitoka katika tawi moja wapo la NBC mjini hapo, ilimtajia namba ya akaunti ya Kangaroo Enterprises na kitita cha pesa kilichokuwemo. Kwa kampuni kama hiyo, bilioni moja na nusu si ela nyingi. Kilichomsisimua Joram ni habari kuwa pesa hizo ziliingia toka katika akaunti moja ya mjini New York, Marekani.

Joram aliitazama saa yake. Ilikuwa saa kumi kasoro. Aliandika ujumbe harakaharaka na kuutuma kwa faksi kwenda kwa rafiki yake mmoja mwenye kampuni ya upelelezi wa kujitegemea mjini humo, akimtaka kuichunguza akaunti hiyo kuona ina pesa kiasi gani na nani anamiliki. Ujumbe ulichukua nusu dakika kufika na baadaye kupata jibu ambalo lilimfahamisha kuwa anashughulikiwa.

Nusu saa baadaye alipata majibu ya maswali yake. Benki hiyo haikuwa na akaunti yoyote yenye jina la Kangaroo wala namba zilizotajwa si za benki hiyo.

‘Haya.’ Joram aliwaza baada ya kuisoma faksi hiyo, ambayo pia iliandikwa kwa mkono, kazi ndio kwanza inaanza! Hata hivyo, hilo alikumsumbua sana Joram. Kitendo cha kuficha ukweli wa pesa zao ni jambo la kawaida kwa wafanyabiashara kote duniani. Alipoitazama tena saa yake aligutuka kugundua kuwa imetimia saa tatu za usiku akiwa ameketi kwenye kochi hilohilo. Akiwa si mtu wa kuketi alifurahi kuona usiku umeingia. Kwake giza ni mali, giza ni uhai; hali ambayo alihitaji sana.

Akavuta kabati na kutoa vifaa vyake vyote muhimu alivyokuwa ameviandaa kwa safari yake ya Zanzibar; bastola moja, visu viwili, funguo zake Malaya, bomu moja la mkono alilolitengeneza mwenyewe na vikorokoro vingine vingi. Vyote alivifutika katika mifuko ya siri baada ya hapo alichukua kitita cha pesa na kukifutika mifukoni. Kabla ya kutoka alitegesha chombo cha kupokelea simu ambazo angepigiwa. Wakati akikamilisha kufanya hivyo, simu iliyomwunga na redio call ya Kombora ilipata uhai. Joram akainua chombo cha kusikilizia na kulitegesha sikio lake.

“Ni mimi afande koplo Shomari. Bado nilikuwa nikilinda ofisi ya Kangaroo ninamashaka kuna kitu wanafanya mzee…”

“Kitu gani?”

“Ni sanduku kubwa ambalo linatosha kupakia watu watatu wazima. Sioni kwanini mzigo huo usafirishwe saa hizi…”

“Nisubiri nakuja.” Sauti ya Kombora ilisikika. “Usiache mzigo huo ukupotee machoni. Kadhalika, usiruhusu wajue kuwa unawatazama.”

“Sawa, afande…”

Jibu hilo la mwisho halikumfikia Joram. Alikuwa tayari amekwisha funga mlango na kukimbia hadi nje ambako alimwomba dereva wa teksi bubu moja, aina ya Toyota Corolla, aliyekuwa amepaki nje ya hotel hiyo, amwazime gari. Ili mtu huyo asiwe na shaka Joram alimkabidhi laki tano. “Nikirudisha gari salama laki mbili zako, laki tatu utanirejeshea,” alimwambia baada ya kumwelekeza namba ya chumba chake na kumtajia jina lake la bandia.

Dakika tano baadaye gari hilo likawa limepaki jengo moja toka ilipo ofisi ya Kangaroo, boneti ikiwa imefunguliwa huku dereva wake akihangaika, mara achungulie ndani ya injini mara aingie ndani na kujaribu kuwasha, mara ajitie kulisukuma. Lakini wakati wote huo macho yake yalikuwa yakiangalia kwa umakini kila kinachoendelea katika ofisi hiyo.

Utulivu wake na jinsi alivyokuwa akiitazama saa yake mara kwa mara vilimfanya Joram aanze kuhisi kuwa chochote kilichomo ndani ya sanduku hilo hakikuwa na thamani yoyote kama alivyotarajia. Hakuamini kama Nuru alikuwa ndani ya sanduku hilo. Badala yake alihisi kuwa zilikuwa zinafanyika njama za kuwaita polisi nje ya eneo hilo ili aweze kuhamishwa kwa utulivu zaidi.

Wakati Joram alipokuwa akiwaza hayo, aliona gari ya Inspekta Kombora likifika katika eneo hilo. Lilikuwa Rangerover lenye namba za kiraia. Lilijipitisha katika eneo hilo kama ambalo halina shughuli yoyote na jengo hilo, kwa mwendo wa taratibu na kutokomea mitaani.

Kana kwamba dereva wa pickup yenye ‘mzigo’ alikuwa akisubiri ishara hiyo, aliingia ndani ya gari lake na kulitia moto. Alifuata barabara ya UWT na baadaye kuingia ya Morogoro. Dakika mbili baadaye Joram aliona gari ya Kombora, likiwa na watu wawili zaidi, waliovaa sare za polisi wakilifuata gari hilo.

Joram alisita kabla ya kuamua kulifuata gari hilo au la. Lakini, shingo upande alilifanya gari lake Lionekane kama limepona, akaliwasha na kuyafuata magari ambayo yalikuwa yakitokomea mbele yake.

Saa hizo, magari yakiwa yamepungua barabarani, haikumchukua muda kuyapata magari hayo. Aliacha magari mawili, moja likiwa daladala yamtenganishe na Kombora ambalo lilikuwa nyuma ya ile pickup. Waliipata kariakoo wakaivuka jangwani na kuingia magomeni ambapo pia waliinuka hadi Manzese.

Wakati wakikaribia kiwanda cha urafiki, Joram alimwona Inspekta Kombora akilipita gari hilo na kisha kulisimamisha kwa mkono. Liliposimama yeye na wenzake wawili, bastola zikiwa wazi mikononi, walishuka na kumfuata dereva wa pickup hiyo.

“Una nini ndani ya sanduku…? Joram alimsikia Kombora akiuliza alipokuwa akiwapita taratibu.

Asingeweza kusimama hapo. Hivyo, aliwapita kama hatua mia moja na kisha kulisimamisha gari lake kando ya barabara. Huku akijifanya anakagua matairi ya gari, macho yake yalikuwa makini yakitazama kinachoendelea baina ya Inspekta Kombora na dereva wa pick up. Alimwona dereva akishuka na kuzunguka nyuma ya gari. Alihangaika kama anayetaka kulifungua sanduku hilo. Kisha, jambo la ajabu lilitokea. Joram alimwona Inspekta Kombora akipaa angani na kisha kuanguka chini kama mzoga. Alipojaribu kuinuka alipokea kipigo kingine ambacho kilimfanya apepesuke na kurudi chini huku bastola yake ikifyatuka na askari wengine walikuwa wakigalagala chini, mmoja kashikilia mbavu zake, wa pili shingo ikiwa haifanyi kazi.

Tukio hili lilifanyika kwa muda mfupi sana kiasi kwamba ilimchukua Joram Kiango nusu dakika kuelewa kinachotokea. Baada ya hapo alikuwa ameliacha gari lake na kutimka mbio kuelekea eneo la tukio. Alikimbia kwa kunyata kama chui. Alimfikia dereva huyo ghafla na kuachia teke ambalo lilitua tumboni barabara. Dereva huyo alipepesuka na kutokwa na macho ya mshangao. Hata hivyo, Joram aliporusha teke la pili lilidakwa na mguu wake kuanza kupindwa. Alitumia mguu wake wa pili kuruka tiktak ambayo ilimpata barabara dereva huyo usoni na kumfanya aanguke na kumwachia Joram ambaye aliviringika! Waliinuka kwa pamoja na kuanza kunyatiana kwa mwendo wa chui walio mawindoni. Macho yao yalitazamana. Hayakuwa macho ya kawaida. Kila mmoja aliona kitu katika macho ya mwenzie, kitu kisichoelezeka, kinachoonyesha waziwazi wao ni nani katika dunia hiyo.

Joram alihisi kupata kuyaona mahali fulani macho hayo. Macho ambayo yana dalili zote za tamaa ya kuwa kiu ya mauaji. Wapi aliyaona macho haya? Alijiuliza wakati akinyata kutafuta fursa nzuri ya kummaliza adui yake, huku akijua fika adui huyo pia anatafuta nafasi ya kumwua.

Wakati huo kikundi cha wapita njia kilikwisha wazingira, kila mmoja akiwa mdomo wazi kwa mshangao na kutoelewa kinachotukia. Dereva huyo alitazama huko na huko kisha akatia mkono wake mfukoni na kuutoa ukiwa umeshikilia tufe ambalo alilipiga chini kwa nguvu. Papo hapo ulitokea moshi mzito unaowasha zaidi ya bomu la machozi. Joram alilazimika kufumba macho huku akiruka upesi kutoka eneo hilo, kitendo ambacho kilimwokoa na pigo la judo ambalo lingemmaliza. Akiwa ameyafumba macho yake yaliyojaa machozi, huku watu wengi wakilia na kukimbia ovyo, hakuwa na uwezo wa kufanya lolote kuizuia pick up hiyo kuondoka kwa mwendo wa kasi.

‘Ninja’ aliwaza kwa mshangao. ‘Ninja Tanzania!’

Fahamu zilipomrudia Kombora alijikuta kaketi juu ya sakafu hali kaegamia ukuta, wasaidizi wake wawili wamelala chali; kila mmoja akiwa amekilaza kichwa chake juu ya paja lake moja. Walilala kwa utulivu, kila mmoja akiwa amekiacha kinywa wazi na kutokwa na macho nje. Haikimchukua Kombora muda kuelewa kuwa wote wawili walikuwa maiti. Alipatwa na mshituko mkubwa na kukurupuka wima huku akitazama huko na huko.

Ndio kwanza akagundua kuwa alikuwa katika chumba kisichokuwa cha kawaida, chumba kipana chenye kuta za chuma kisicho na mlango wala dirisha. Hewa chumbani humo ilikuwa nzito iliyojaa harufu ya kifo au maiti. Kombora alitazama huko na huko, akitafuta uwezekano wa kutoka katika chumba hicho. Hakuuona. Kwa kila hali, kilionekana chumba madhubuti kilichojengwa chini ya ardhi maalumu kwa ajili ya kumfanyia binadamu unyama.

Akayarudisha macho yake kuwatazama wasaidizi wake ambao sasa walikuwa marehemu. Kila dalili ilionyesha kuwa walikufa baada ya mateso makubwa ya kinyama. Mmoja alikuwa kavunjika shingo, jambo ambalo lilimfanya alale kama mzoga wa mbuzi. Na wa pili alikuwa na jeraha kubwa kifuani, ambalo lilionyesha kitu kigumu kilipenya humo na kuzifumua figo zake.

Kombora aliitazama saa yake. Dakika arobaini tu zilikuwa zimepita toka alipotoka ofisini kwake kufuata wito wa Koplo Shomari, ambaye sasa ni marehemu, ikimwarifu juu ya sanduku lililokuwa likisafirishwa toka ofisi Ya Kangaroo. Tayari watu wawili ni marehemu hali yeye akiwa hai kwa fadhila au kebehi ya wauaji hawa. ‘Kwanini hawakumwua yeye pia? ’ kwa nini?’ alifoka kimoyomoyo akitembea huku na huko chumbani humo kwa uchungu. Hasira zilianza kumpanda zikamfanya asahau hofu aliyonayo juu ya maisha yake na kujikuta akijenga chuki kwa yeyote Yule aliyekuwa akimtendea haya. Alitamani ampate papo hapo, amchanechane kwa mikono yake na kuacha viungo vyake vikiliwa na fisi.

Hasira zilikuwa zikimcheka kichwani mwa Kombora, hasa zikisababishwa na unyama wa binadamu huyu ambaye hakuwa na shaka ni Kakakuona mwenyewe; bali jinsi alivyoufanya unyama wake mbele ya macho yake, hadharani, kana kwamba Kombora hakuwa lolote wala chochote mbele yake. Yeye, ambaye historia ya Tanzania na dunia kwa ujumla haitamsahau kwa mengi aliyoyatenda kuifanya serikali iendelee kuwepo na amani izidi kutawala nchini! Yeye ambaye jina lake tu lilikuwa sumu kali kwa yeyote aliyekuwa na ndoto za kuidhuru Tanzania!

Kamwe asingejisamehe kwa tukio hili la leo ambalo lilimfanya atoke ofisini bila kuaga, na kujikuta akisindikiza mzigo ambao hakujua ni wa nini. Asingejisamehe kuruhusu dereva wa pick up hiyo atoke nje na kuwazubaisha kwa maelezo marefu ya kebehi na mara ageuke kama chui ambaye alipaa angani na kuanza kuwachalaza kwa kong fu, judo na kareti kwa namna ambayo Kombora na umri wake wote katika ukachero hakupata kuiona.

Ilikuwa kama hadithi ambazo hutokea katika michezo ya sinema. Dakika moja walikuwa wima wakizungumza naye, dakika ya pili walikuwa wakigalagala chini kwa maumivu yasiyosemeka. Kwa mbali, kama ndoto, Kombora alihisi kumwona mtu mwingine akipambana kwa kiwango kama kilekile, kana kwamba hayati Bruce Lee amefufuka na anafanya vitu vyake. Lakini tukio au ndoto hiyo ilitoweka ghafla kwa mlio wa kutisha uliofuatwa na moshi mzito unaowasha, ambao ulimfanya Kombora aishiwe nguvu kabisa. Hakuwa na la kufanya wakati alipobebwana kutupiwa nyuma ya gari kama mzoga.

Wala hakuwa na neno alipohisi akinukishwa kitu fulani ambacho kilimfanya apoteze kabisa nusu ya fahamu alizobaki nazo. Na zilipomrudia ndipo alijikuta kaegemea ukutani. Maiti za vijana wake zikiwa zimelazwa juu ya mapaja yake kwa namna ya kumdhihaki.

‘Nitalipa kisasi’ kosa moja wamefanya kuniacha hai. Kwa vyovyote watalijutia.’

Wakati akiwaza hayo, alikuwa akitembea huko na huko kukikagua chumba hicho. Alikuwa na hakika kuwa kina mlango na dirisha, vinginevyo wao wasingeingizwa chumbani humu. Alikagua kwa makini kila sentimita ya chumba hicho. Haikumchukua muda kugundua sehemu aliyotaka. Nusu ya ukuta huo ulikuwa pande zito la chuma ambalo lilionekana kama mlango. Hata hivyo ilikuwa dhahiri kuwa lango hilo lilifunguliwa kwa umeme, toka nje ya chumba hicho.

‘Watafungua tu na watanikuta tayari nikiwasubiri.’ Kombora aliwaza akiupeleka mkono wake kuitafuta bastola kama alivyotegemea ilikuwa tayari imetoweka. ‘No problem, nitawasubiri na kupambana nao hata kwa meno.’

Mara taa ya umeme iliyokuwa inawaka chumbani humo ilizimwa, likafuata giza nene la kutisha. Kisha, ziliwashwa taa nyingi zaidi zenye Nuru kali kuliko giza lililokuwemo. Nuru hiyo ikafuatwa na joto kali ambalo dakika moja baadae lilimfanya Inspekta Kombora aanze kutapatapa huku tayari ameloa jasho.

“Karibu sana Inspekta Kombora’ sauti nzito ambayo haijulikani inapotokea, ilitamka ghafla kwa kiingereza. “Karibu kwetu. Karibu katika chumba cha mauti. Hajawahi binadamu yeyote kuingia humo akiwa hai na kutoka hai”

Sauti ikafuatiwa na kicheko ambacho binadamu yeyote asingekiita kicheko kwa jinsi kilivyokuwa hakina hisia zozote za binadamu.

Haikuwa sauti ngeni kwa Kombora. Wala Kombora hakuhitaji kufikiri sana ili kukumbuka alipata kuisikia wapi. Ilikuwa sauti ya mmoja kati ya wale wakurugenzi wawili wa Kangaroo, Paul na Philip.

“Nilijua kitambo kuwa mna kasoro fulani akilini mwenu” Kombora alifoka bila kujua kama anasikika au la. ‘Kama mlivyo na kasoro katika miili yenu.’ Alitamani kuongeza kwa hasira lakini hakufanya hivyo. Badala yake alisema “Kwahiyo mtindo wenu ndio huu, wa uoga na kujificha nyuma ya ukuta ndipo muweze kumkabili binadamu? Ni hili ambalo pia mmelifanya kwa msichana wa watu asiye na hatia.”

Kicheko kingine kibaya kilifuata. Kikafuatwa na sauti ileile ikisema, “Hatujifichi Inspekta, hatuna haraka ya kuonana nawe, kwa ujumla hatukuhitaji sana. Orodha yetu ilikuwa na watu wawili tu katika Tanzania. Wewe umejilazimisha na kuwa wa tatu. Hivyo, bado mmoja, Yule kijana mtukutu ambaye nyie mnamwita Joram Kiango. Baada ya muda mfupi tutakuwa naye hapa. Na hapo ndipo tutaanza kufanya vitu vyetu ambavyo mtavishuhudia kwa macho yenu wenyewe.”

“Mnataka kufanya nini?” Kombora hakustahimili kuuliza. Kicheko kingine cha kebehi kikafuata.

“Usiwe na haraka Inspekta. Uko hapa utajionea mwenyewe. Kwanza, lazima ujihesabu kama mtu mwenye bahati kuwa hai hadi sasa hivi. Ungeweza kuwa marehemu kama hao kuku wenzako waliolala hapo. Kwa bahati, bado tunakuhitaji. Tunahitaji uwe shahidi, uone kwa macho yako mwenyewe kile ambacho kitatokea nchi yako. Baada ya hapo utakufa kwa amani utapumzika kuzimu hali ukiwa na picha halisi akilini mwako, picha ya kupendeza ambayo kamwe haitafutika akilini mwako.”

Kombora hakuweza kumsikia vizuri. Joto kali lilimzidi kimo na kumfanya aanze kutapatapa kama samaki anayekaangwa akiwa hai. Aliruka huko na huko akiyavua magwanda yake, mishipa ya fahamu ikikaribia kupasuka, macho yake yalipoteza nuru na kizunguzungu kumshika ghafla. Polepole alijikuta akiteleza na kuanguka sakafuni, kando ya maiti ya vijana wale.


“Twende huku, ukamwone hawara yako mwingine aliyekuja kukusalimu,” Nuru aliamrishwa akiinuliwa toka sakafuni alipojibweteka na kusukumwa kama mzigo.

Mikono iliyomwinua toka sakafuni hapo ilikuwa mikakamavu yenye nguvu kama chuma. Hakuwa na hali ya kupingana nayo ingawa moyo wake ulimtaka sana kufanya hivyo. Mwili wake haukuwa na uwezo wala akili yake hakuiona kama ilifanya kazi kwa kiwango chake. Kwa ujumla alijiona kama kondoo au zezeta lililokuwa tayari kufuata amri yoyote ambayo alipewa na viumbe hawa wawili, amri yoyote ile; hata kama ingekuwa kujitumbukiza mwenyewe katika shimo ambalo lingempeleka moja kwa moja hadi kuzimu.

Kitu kimoja Nuru alikuwa na hakika nacho. Ukondoo au uzezeta haukumjia hivihivi kutokana na ukatili usioelezeka ambao aliushuhudia kwa macho yake mwenyewe ukifanywa na Kakakuona mbele yake, la hasha! Aliamini kabisa kuwa uzezeta huu ulitokana na sindano alizokuwa akichomwa mara kwa mara zilimfanya apoteze fahamu na zilipomrejea akajikuta mzembe akilini na mwilini kiasi cha hata kuwa mvivu na kukumbuka yote yaliyomtokea.

Kwa namna ya ndoto tu, alikumbuka yaliyomtukia kisiwani mara moja tu Joram alipoondoka. Alikumbuka jitihada zake ambazo zilisababisha vifo vya watu wawili kati ya wale waliokuja kumkamata, lakini waliobaki wakafanikiwa kumteka nyara. Alikumbuka alivyopelekwa Zanzibar na chongo kumwua mwenzie na kisha yeye mwenyewe kuuwawa. Alikumbuka pia kuwa mwenyenyumba Banduka, alivyouawa na kufichwa na Kakakuona ambaye alimrejesha Dar Es Salaam kwa mtutu wa bastola huku watu waliosafiri nao wakiwa hawana habari. Na alikumbuka alivyofika forodhani na kumwona Joram Kiango akiwa katika mavazi bandia yaliyomfanya asifahamike na yeyote zaidi yake.

Matukio ya kutisha zaidi, ambayo Nuru aliyakumbuka kama mabaya zaidi ni yale ya kuuawa kwa dereva wa teksi na msichana wa mapokezi, hadharani, mbele yake bila ya yeye kuwa na uwezo wa kufanya lolote. Mkono wake ambao aliutia haraka katikati ya miguu yake ili kuichukua bastola yake mbayo alikuwa ameificha mahali hapo, haukuweza kutoka na silaha hiyo kama alivyokusudia kwani ni wakati huohuo alipopigwa kitako cha bastola kilichomfanya azirai na kupokonywa bastola hiyo.

Na alipozinduka ndipo akajikuta katika chumba hiki, ambacho kwa kila hali, kilionekana kuwa kilichojengwa chini ya ardhi, maalum kwaajili ya kufanyia maasi au maovu. Na baada ya hapo ndipo alipoanza kudungwa sindano zilizomlewesha na kumpumbaza hata akawa hajiwezi, hajitambui. Kila dawa hizo zilipoisha nguvu alidungwa tena, jambo ambalo lilimfanya awe taabani daima.

Wakati akiwa taabani, kama ndoto vilevile, Nuru aliwaona watu wawili wenye maumbo ya ajabu wakimjia na kumtazama kwa muda mrefu. Mara mbili tatu watu hao walimvua nguo na kumchezea matiti na sehemu zake za siri kwa vidole vyao vikavu. Mara moja mmoja wao alijaribu kumnajisi, lakini Nuru alihisi kuwa alishindwa kwani hakuuhisi uume wake mwilini mwake. Hata hivyo waliendelea kumchezea wakifurahia kila kitendo chao.

Nuru alihisi kupata kuwaona watu hawa, lakini hakumbuki wapi. Watu wasiojiweza, wasio na viungo kamili, wanaoonekana kama walipata kutupwa katika tanuru la moto na kisha kutolewa kabla hawajateketea kabisa; aliwaona wapi? Mara kwa mara aliituma akili yake nzito kumfahamisha, lakini nayo haikuwa na jibu. Hivyo, alijikuta akiamua kuamini kuwa hakuna mahala popote ambapo aliwaona isipokuwa usingizini, katika moja ya zile ndoto zake mbaya ambazo humtokea binadamu mara chache katika maisha yake; ndoto za viumbe wa ajabuajabu wanaotisha ambao humwandama mtu usingizini na kumfanya aamke huku akitweta, jasho likiwa limemjaa mwilini tepetepe.

Kitu kikubwa kilichoisumbua zaidi akili iliyodumaa ya Nuru ni dawa hizo alizokuwa akilazimishwa kutumia. Baada ya kudungwa mara tatu alihisi mwili wake ukizitamani na kutaka apewe mara kwa mara. Ni jitihada kubwa sana zilizomfanya asitamke kwa sauti, kuomba tena au kuzidishiwa

Hili lilimtisha sana kwani alijua fika kuwa anachotumia ni kitu hatari kwa maisha ya binadamu. Kama haikuwa Cocaine basi ilikuwa Heroine au Mandrax. Hakuwa mtaalamu sana katika masuala ya madawa ya kulevya, lakini hicho kidogo alichofahamu kilimfanya aelewe kuwa alikuwa katika hatari kubwa wa kuwa teja wa dawa hizo, jambo ambalo lingemfanya apoteze akili, afya na hata uhai wake.

“Nimekwambia inuka, nenda kule ukamwone hawara yako mwingine,” sauti ilimwamrisha tena Nuru akizidi kusukumwa kwenda mbele. Msemaji alikuwa akizungumza kiingereza.

Macho ya Nuru yalikuwa mazito kufunguka. Lakini alitumia akili yake kufikiri sauti hiyo. Haikuwa sauti ya Kakakuona. Ilikuwa sauti ya mtu mwingine. Hata lafudhi yake haikuwa ya Kiafrika. Nuru alihisi kuwa msemaji alikuwa Mjapan au Mchina. Akajilazimisha kufungua macho yake. Kwa taabu, aliweza kumwona mtu huyo. Alikuwa mrefu mwenye kifua cha simba ingawa alitembea kwa kunyata kama chui aliye mawindoni.

Nuru hakujisumbua kuwaza uwezo wa kupambana naye. Hali haikumruhusu. Hivyo, aliruhusu kusagwa kikondoo hadi katika chumba kingine ambacho kilifunguka baada ya mtu huyo kubonyeza tufe la umeme na sehemu ya ukuta huo kumeguka. Alisukumwa chumbani humo na kujikuta ameangukia mwili wa mtu mnene, wa makamo ambaye Nuru alimtambua mara moja.

“Inspekta Kombora.’ Alinong’ona. Sauti haikutoka. Kando ya Inspekta huyo ambaye alilala nusu uchi, baada ya kuitupa suruali na shati yake huku na huko kupunguza joto kali ambalo lilimfanya azirai, Nuru aliona miili ya watu wawili ambao hakuhitaji kuambiwa kuwa wamekufa.

Hakushituka. Wala hakushangaa. Alikwisha vuka kiwango hicho.


Kwa Joram Kiango, ulikuwa usiku mfupi kuliko matarajio yake. Angependa sana uwe mrefu zaidi. Usimame, kama Biblia inavyodai jua lilisimama wakati Waisrael wakiwateketeza wapalestina ili waweze kushinda vita vile ambavyo viliwawezesha kuichukua nchi ya Ahadi. Lakini Joram hakuwa na bahati hiyo. Alipoitazama saa yake ilimwambia kuwa ilikwishatimia kumi na robo za usiku. Alihitaji saa sita zaidi ya kiza ili aweze kukamilisha awamu ya pili ya kazi yake.

Awamu ya kwanza alihisi kuwa ameitimiza. Ilikuwa kumtia adui jeraha la moyo ili naye apate uchungu na kuanza kutapatapa, kama ambavyo adui huyo aliamini Joram anatapatapa, kwa kuteketeza watu wasio na hatia, kumteka Nuru na hatimaye Inspekta Kombora.

“jeraha” ambalo litausononesha moyo wa adui huyo ni pale alipoamua kuteketeza maghala yake yote ambayo yalikuwa na mali ya mamilioni ya pesa za kigeni. Joram alihakikisha kila kitu kinateketea na kuwa jivu kwa moto aliouanzisha.

Hatua ya kutenda kitendo hicho, ambacho kilikuwa kinyume na desturi yake, Joram aliichukua ghafla mara baada ya tukio la saa chache zilizopita Barabara ya Morogoro.

Akiwa taabani kwa maumivu ya Moshi ule, ambao ulipenya hata kooni na kukwaruza, Joram alifanya haraka kukimbilia nyumba za jirani ambako aliomba maji na kunawa. Wakati akiondoka eneo hilo, alisikia kishindo cha watu waliozolewa na kutupwa katika pick up, na kisha kusikia ikiondoka kasi. Hakuwa na uwezo wa kufanya lolote.

Baada ya kunawa na macho yake kurudia hali ya kawaida alilirudia gari lake huku akipishana na watu waliokuwa wakitapatapa, baadhi yao wakipiga mayowe kwa maumivu na taharuki. Alilitia moto gari lake na kuifuata njia hiyohiyo ya Morogoro hadi alipofika ubungo ambako alipinda kushoto na kufuata barabara ya Mandela. Haikumchukua zaidi ya dakika kumi kabla hajaona kibao ambacho kiliashiria kuwa ameyafikia maghala ya kiwanda hicho.

Alisimamisha gari lake toka hatua kadhaa toka kibao hicho. Kisha, akavuka barabara kuyafuata majengo hayo ambayo toka hapo alipokuwa aliyaona kuwa yalikuwa makubwa kuliko alivyotegemea, alipoyafikia, kama alivyotegemea, alikutana na ukuta mkubwa uliyoyazunguka. Mbele ya ukuta huo kulikuwa na lango kubwa la chuma ambalo lililindwa na watu wawili waliovaa mavazi ya Jeshi la Mgambo. Joram alisita kwa muda akiwatazama.

Tangu alipoipata safari hii, hata kabla hajaamua kuifuata pick up ambayo iliwatorosha Kombora na wasaidizi wake, Joram alijua kuwa ingekuwa safari ya hatari. Alikuwa na kila hakika kuwa viumbe wale, kwa mujibu wa maelezo aliyoyapokea toka pande zote, hawakuwa watu wa kawaida na hivyo hawakuwa wakifanya biashara za kawaida. Hivyo, dhamiri yake kuu ilikuwa kuikagua biashara hiyo ili aelewe kabla ya kuwakabili viumbe wenyewe.

Hali kadhalika, alikuwa na mashaka kuwa mabohari hayo yalitumiwa kuficha maovu yao mengi, ambayo yaliwafanya wajiamini na kufanya maovu yao kwa dharau, bila hofu wala wasiwasi wowote. Kwa ujumla, licha ya biashara haramu kama dawa za kulevya au nyara za serikali, Joram alitegemea maghala hayo kuwa maficho ya kikosi cha mauaji ambayo yalikuwa yakiendelea nchini. Na alijiandaa kwa hilo.

Ambacho hakujiandaa nacho ni kukutana na ninja. Kamwe hakutarajia kuwa watu hao, ambao pamoja na ukatili wao walionekana wapuuzi, wangefikia hatua ya kumleta ninja nchini, ili waweze kufanikisha adhma yao.

Sio kwamba Joram alimwogopa ninja. Kinyume na watu wengi yeye alifahamu kuwa ninja ni binadamu kama binadamu wengine. Kilichowapa umaarufu, licha ya ukatili wao, ni upya wa taaluma yao machoni mwa watu kiasi cha watu kuondokea kudhani kuwa ninja ni zaidi ya kuwa binadamu wa kawaida.

Joram hakuwa ninja, lakini taaluma ya uninja iliiva kichwani mwake sawa na ninja yeyote yule. Alichokosa ni Master ambaye angeweza kumtangaza U-ninja kwa kumpa baraka ambazo angeambatana nazo maishani.

Lakini hilo halikumsumbua hata chembe. Kwa kiwango chake, baada ya visa na mikasa yote iliyomkumba wakati akiishi nchini Marekani, hakuhitaji mwalimu ambaye angemtangaza rasmi kwani hakuwa katika kikundi chochote wala ukoo wowote ambao ulihitaji kumkubali au kumkataa.

Joram aliipata taaluma ya u-ninja kwa gharama ya sehemu kubwa ya jasho na damu yake, nusura imgharimu roho yake. Alianza kwa kujiunga na vyuo vidogovidogo vya kareti na judo, ambavyo wakati huo vilienea sana nchini Marekani. Jitihada zake kubwa zilifanya apendwe na walimu wake ambao baada ya kumfundisha kila walichojua walipendekeza vyuo vingine hadi alipojikuta katika chuo kile ambacho kilikuwa kikifundishwa na hayati Bruce Lee mwenyewe.

Joram alikuwa mtoto mweusi pekee katika darasa hilo. Lakini jitihada zake na uwezo wake wa kuzingatia kila alichofundishwa kilimfanya awe kipenzi cha hayati huyo, jambo lililomfanya achukiwe na wanafunzi wenzake wote shuleni hapo.

Kifo cha kutatanisha cha hayati Bruce Lee kilipotokea, Joram alihisi kama aliyepotelewa na baba au kaka yake wa damu. Alikosa raha kwa siku kadhaa. Baada ya msiba alijaribu kutafuta chuo kingine ambacho kingemfaa, lakini alijikuta akipoteza muda wake bure kutokana na jinsi mbavyo alijiona amevuka kiwango cha mafunzo mengi yaliyotolewa kitaaluma na kivitendo. Hivyo, mafunzo mengi kwake ilikuwa kujikumbushia tu.

Hali hiyo ilimwongezea uadui hata miongoni mwa walimu. Wako walimu wa Kichina na Kijapan ambao waliamini kuwa taaluma hiyo ni maalumu kwa ajili yao tu. Hivyo, hawakuona haki ya mgeni kuifahamu kama wao au zaidi ya wao. Na wamarekani hawakuona haja ya mtu mweusi kutamba mbele yao. Hivyo, kila ilipotokea nafasi, Joram alijikuta akiingia katika ugomvi ambao hakuujua chanzo chake. Lakini aliibuka mshindi katika kila tukio. Baadaye walianza kumshambulia katika vikundi. Bado mara kwa mara Joram alivisambaratisha au kutoroka bila matarajio yao.

Lakini ilitokea jioni ya siku moja, akiwa katika viwanja vya mazoezi peke yake, Joram alijiwa na mtu aliyevaa mavazi meusi kiasi cha kufunika mwili mzima isipokuwa macho tu. Alikuwa akitembea harakaharaka lakini kwa kunyata kama kivuli. Joram hakuitaji kuambiwa kuwa alitembelewa na ninja. Alikwisha soma habari zao katika vitabu vingi, ingawa hakupata kukutana ana kwa ana.

“Joram Kiango?” mgeni huyo alimwuliza.

“Kama ndiye?” Joram alimjibu kwa swali jingine.

Mgeni huyo alimtazama toka miguuni hadi utosini. Akaonyesha kuridhika na alichokiona, “Nimekuwa nikizisikia sifa zako. Nimekuja nione kama ninachokisikia ni kweli. Uko tayari?”

Joram hakuwai kukataa kupambana na mtu yeyote, hasa anapoonyesha shahuku ya kumjaribu kama huyo. Alimkubalia na kujiandaa. Adui yake alimtazama kisha akaanza kunyata huku na huku, kabla hajapata fursa ya kuachia pigo ambalo lilikingwa na Joram kirahisi. Pigo hilo lilikuwa kama la kumzindua tu kwani wakati huohuo alifyatuliwa miguu kwa namna ambayo hakuitegemea na kujikuta akiviringika. Mara tu alipoinuka alifyatuliwa tena. Wakati huohuo akiwa amekwisha jiandaa alianguka hali akiachia teke ambalo lilimpata adui yake tumboni na kumfanya apepesuke. Aliviringika toka sakafuni hapo na kumfuata adui yake ambaye aliruka na kudaka miti ya mazoezi ambayo aliitumia kukimbia kwa mikono kama nyani. Wakati Joram akiwa ameduwaa kwa hilo adui huyo alichupa hewani kama chui na kutua juu ya kifua chake.

Kilichofuata ni kitu ambacho Joram hatokisahau hadi leo. Vipigo vilimnyeshea kama mvua. Hakupata fursa kujitetea kwani alipouinua mkono wake ulikuwa hauna kazi, hauna nguvu. Walimwokota hapo, dakika ishirini baadaye, walimpeleka hospitali moja kwa moja, ambako alipimwa na kugundulika kuwa alivunjika mkono, mbavu tatu na kuteguka mguu.

Alikaa hospitali mwezi mmoja. Aliporuhusiwa kutoka, hata kabla ya POP halijaondolewa alianza mazoezi. Na mara lilipoondolewa, wiki tatu baadaye, alikuwa safarini toka mjini Washington kuelekea mjini Carfornia ambako alisikia kuna mwalimu wa kichina aliyekuwa akitoa mafunzo ya U-ninja kwa “wateule” wachache aliodhani kuwa wanafaa. Joram aliondoka bila kuwaaga wazazi wake ambao walipinga hatua yake ya kujihusisha na mambo hayo.

Ilimchukua wiki nzima kugundua kilipojificha. Chuo hicho kilikuwa katika moja ya misitu mikubwa iliyokuwa haijaanza kutumika ya mtengenezaji mmoja mashuhuri wa filamu katika mji wa Hollywood. Chuo hicho kilikuwa kinaongozwa na mzee mmoja mfupi, mnene mwenye upara uliomeza robo tatu ya kichwa chake. Mzee huyo alimtazama Joram kwa macho yaliyojaa chuki na dharau dakika mbili nzima kabla ya kumjibu kwa swali, “alikuambia nani kuwa nafundisha taaluma hiyo? Na hata kama, nitamfundishaje panya mchezo wa paka?”

Joram alitumia hekima yake kubembeleza na kusihi hadi alipoona mwalimu huyo akianza kumsikiliza kwa makini “Unadhani unafahamu nini juu ya taaluma hii?” mwalimu huyo aliuliza.

“Sifahamu chochote”

“Kwa hiyo, unifahi, sifundishi watu mbumbumbu.”

Joram alipozidi kumbembeleza mzee huyo alipiga makofi. Mara miti iliyokuwa imeenea eneo hilo ikapata uhai. Zaidi ya vijana sita, ambao Joram hakujua kuwa walijificha juu ya matawi hayo wakimtazama, waliruka na kutua chini wakiwa wamemweka kati. Joram alimfahamu mmoja wao. Alikuwa Yule ambaye majuzi tu alimfanya alazwe hospitali kwa mara ya kwanza maishani mwake.

“Niondoleeni mbele yangu hii takataka” mwalimu huyo aliamrisha.

Mara vijana hao wakageuka mbogo. Kwa pamoja walimvamia joram na kuanza kumshambulia. Akijua kuwa huu ulikuwa mtihani mbele ya mkufunzi huyo Joram alichachamaa na kupigana kwa nguvu zake zote na moyo wake wote. Dakika mbili baadaye watatu kati ya hao walikuwa wakigaragara chini, hawajitambui. Joram mweyewe akiwa taabani, lakini hakukubali kushindwa. Muda si mrefu aliwatupa wawili wengine na kujikuta amebakiwa ana kwa ana na yule mkuu. Wote walitweta kama majogoo yanayoogopana baada ya Joram kuikwepa kila hila iliyofanywa na kijana huyo.

“Inatosha.” Mkufunzi huyo alisimamisha pambano, uso wake ukionyesha kufurahishwa sana na alichokiona “Pumzikeni, kesho tutaangalia ambacho tunaweza kufanya kwa mgeni wetu huyo machachari.”

Joram aliliona jicho la chuki likimtazama toka kwa kijana huyo.

Kesho yake, bila ya mwalimu huyo kujua chuki baina yao bado alimkabidhi Joram kwa kijana huyo ili ampe zoezi kabla hajaanza kumfundisha mwenyewe.

Kijana huyo ambaye baadaye Joram alifahamu kuwa anaitwa Adrian, mchina aliyechanganyika na Mmarekani, aliondokea kuwa mwalimu, hasa kwa Joram. Kutwa nzima ambayo alimchukua porini alimtesa kwa kumpa adhabu za kutisha, huku akitamba kwa kumwonyesha Joram ujuzi wake katika hila ambazo wengi hudhani ni mazingaombwe, mbinu za kuruka ambazo wengi hudhani ni miujiza, kuparamia miti ambako baadhi wanafikiri ni uwezo utokanao na mitishamba, kuzua moshi ambako hata Joram alidhani ni uchawi n.k.

Yote hayo Adrian aliyafanya kwa kujisifu, kwa nia ya kumwonyesha Joram kuwa hajui kitu. Lakini hakujua kiasi gani Joram alikuwa akiyafuatilia yote hayo na kuyachora katika ubongo wake.

Jioni moja Master alitangaza mwenyewe kuwa angeanza kumfundisha Joram. Usiku huohuo Adrian alimnong’oneza Joram, “Hii sio taaluma ya nyani weusi. Kesho alfajiri ondoka urudi kwenu. Ukiendelea kukaa hapa mpaka jioni nitakuua.”

Joram alimpuuza lakini kilichotokea mchana huo kilimfanya aamini kuwa Adrian hakuwa na mzaha. Mwalimu alikuwa amekwenda nje ya kambi na kuwataka waendelee na mazoezi. Adrian alimwita Joram na kumtaka amfuate ili amwonyeshe kitu ambacho hakupata kukiona huko nyuma. Walipofika katikati ya kichaka, Adrian ghafla aligeuka mbogo na kuanza kumshambulia Joram. Mapigo yake yote yaliashiria kuua. Kwa bahati mbaya hakujua Joram amejizatiti kiasi gani. Baada ya dakika arobaini za mapambano, Joram alikuwa amelowa jasho na damu, mkono wake mmoja ukiwa haujiwezi. Lakini Adrian alikuwa chini, chali, nusu maiti.

Joram alijikongoja na kumburuza hadi kambini ambako alikutana na macho makali ya Master akimsubiri kwa ukali.

“Wewe ni mnyama. Huyu ni mwanangu, mwanangu wa pekee. Tazama ulivyomfanya! Sasa nakuamuru uondoke mara moja katika kambi yangu. Ukiendelea kukaa, dakika moja zaidi nitakuua kwa mikono yangu mwenyewe.”

Joram hakuwa na hili wala lile zaidi ya kuondoka.


Naam, Joram hakuwa mgeni wa maninja. Hata hivyo, kitendo cha ninja huyo kumdhihaki na kuondoka na mtu mkubwa kamaa Inspekta Kombora mbele ya macho yake, kilimwongezea hasira na kumpa ari ya kuteketeza bidhaa hizo bila huruma.

Wale walinzi wawili waliovaa mavazi ya mgambo hawakumpa shida. Alichofanya ilikuwa ni kuwanyemelea hadi mita nne nyuma yao, kisha akachupa hewani na kutua huku wote wawili wakiwa chini yake. Kabla hawajafahamu kinachotokea alikwishawagonganisha vichwa mara kadhaa hata wakapoteza fahamu. Baada ya hapo aliwafunga kamba za mikono na miguu, akawatia matambara mdomoni ili watakapozinduka, wasiweze kupiga kelele na kisha akawavuta na kuwalaza katika kibanda chao cha ulinzi.

Kwa kutumia funguo zake malaya aliufungua mlango wa geti na kisha kushughulika na makufuli ya kuingilia ghalani. Ilimgharimu dakika kumi, ambazo Joram aliona kama miaka kumi hadi makufuli yalipokubali. Alipigwa na butwaa kwa wingi wa mali zilizokuwemo humo ndani. Jengo zima lilifurika kwa makatuni yaliyopangwa vizuri hadi kufikia kabati. Joram alishusha baadhi ya makatuni na kutazama majina yake, Glamorous Perfume, Glamorous Cream, Glamorous toilet soap, Glamorous powder, n.k.

Joram alikumbuka kuona matangazo ya bidhaa hizo katika magazeti na televisheni. Aidha, alipata kusikia yakitangazwa pia katika redio. Akiwa mtu ambaye hajishughulishi na vipodozi, hakuyatilia maanani matangazo hayo.

Hata hivyo, alikuwa na uhakika kuwa hazijaanza kuuzwa nchini kwakuwa tangazo moja lilikuwa likitangaza tarehe ambayo bidhaa hiyo ingeanza kusambazwa kote nchini. Hakutegemea kama bidhaa inayoingia nchini kwa majaribio, ambayo ilitajwa wazi kuwa ingeanza kutumika duniani kwa mara ya kwanza, ingeweza kuletwa kwa wingi kiasi hicho.

‘Bahati yao mbaya, itabidi walete mali mpya,’ aliwaza wakati akipanda juu ya masanduku hayo na kuchokonoa umeme. Kuanzisha moto ukiwa mchezo mdogo kwake, haikumchukua nusu saa kuona nyaya za umeme alizozitegesha zikianza kusafirisha moto ambao utakapokutana mlipuko usingekuwa wa kawaida.

Alifanya hivyo katika jengo la pili pia. Kisha, akatoka nje na kuwaburuza walinzi wale wawili hadi barabarani ambako aliwafungua kamba na kuwaacha wakiwa wameduwaa. Akapanda gari lake na kulitia moto, akilielekeza mjini.

Kabla hajafika popote mlipuko wa kwanza ulitokea. Ulifuatiwa na moto mkubwa ambao ulifanya usiku ugeuke mchana. Mlipuko wa pili ulimkuta keshafika mjini.

Ukubwa wa mlipuko na ukali wa moto toka katika maghala hayo ulimshitua karibu kila mtu katika maeneo ya Tabata, Buguruni, Ubungo na kwingineko. Watu wengi waliamka na kuutazama kwa hofu, huku vibaka wakifukuzana kwenda katika eneo hilo kwa matumaini ya kujipatia chochote. Hakuna kilichopatikana. Hata zima moto ambao walifika katika eneo hilo, nusu saa baadaye, waliduwaa wakiutolea macho moto huo jinsi ulivyokuwa unatafuna na kuteketeza kila kitu katika majengo hayo. Hakuna aliyethubutu kuusogelea.

Taarifa za kuungua kwa maghala ya Kangaroo iliwafikia wakurugenzi wa kampuni hiyo, Paul na Philip, dakika arobaini baadaye. Walikurupuka toka katika ofisi yao, ambayo kwa juu yalikuwa makazi yao na kujikongoja kulielekea gari lao.

“Number One!” mmoja aliita. Alipoita mara ya pili kile kilichoonekana kama kivuli, ambacho kilisimama katika kivuli cha mchongoma ulioizunguka ofisi hiyo, kilipata uhai na kuwaendea kwa mwendo wa kunyata.

“Tulikuajiri kwa kazi moja tu” Philip alisema kwa sauti yake ya mkwaruzo. “Kumpata Joram Kiango na kumleta kwetu akiwa hai, wewe umekaa hapa kivulini wakati yeye anatufanyia madhara ghalani. Twende tuone ni kiasi gani cha madhara alichotufanyia”

Number One hakuwajibu. Hakuwa mtu wa maneno mengi isipokuwa vitendo. Zaidi, alikuwa na mashaka kuwa waajiri wake hawa walikuwa na dosari katika vichwa vyao kama ilivyokuwa katika miili yao. Hakupata kuwaelewa hata mara moja. Hata hivyo, alilazimika kuwatii kwa kuwa tu alihitaji pesa zao ambazo aliziona kama za bure kwa wepesi wa kazi waliyomtajia.


ITAENDELEA

Roho ya Paka Sehemu ya Tano

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment