Kitisho Sehemu ya Kwanza
IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
Simulizi : Kitisho
Sehemu Ya Kwanza (1)
Mbowe club saa 1:23 usiku
RADI kali ilipasua anga na kufanya mchoro wa kutisha, mwanga wake ulilipoteza giza kwa sekunde kadhaa, kila kilichojificha kilionekana wazi.
Hakuna mtu hata mmoja aliyekuwa nje muda huo. Ni mvua kubwa na ngurumo za kutisha zilitawala kila kona, ilikuwa ni hali ya kuogofya sana. Mifereji na mito ya dhalura ilianzishwa na maji ya mvua hiyo.
Kama ilivyo ada katika jiji la Dar es salaam, barabara zote zilikuwa zimejaa maji, kama ukiwa dereva mgeni basi hutoweza kujua ni wapi barabara ilipo. Sehemu kubwa ya mji hasa katikati ya jiji gari nyingi ziliegeshwa kando ya barabara kusubiri mvua iishe lakini haikuwa hivyo kwani mvua ilikazana zaidi ya saa nne.
Wakati hayo yote yakiendelea, ndani ya ukumbi mkubwa wa starehe unaojulikana kama ‘Mbowe Club’ watu hawakuwa wakijua kama nje kuna mvua, disco liliendelea kwa nguvu zote, watu walicheza, wakanywa na kuburudika. Katika kaunta kubwa ya ukumbi huo kulikuwapo walevi kadhaa ambao tayari walikwishabadilisha lugha ya mawasiliano kutoka Kiswahili na kuwa Kiingereza.
Gina binti Komba Zingazinga alikuwa ni miongozi mwa watu wachache waliokuiwa wamesaliwa na akili zao na utashi pia, alikuwa akinywa kinywaji chake taratibu huku jamaa mmoja akijitahidi kumzengea zengea lakini asifanikiwe. Kila wakati alionekana kuitazama saa yake aliyoivaa mkononi na aliposhusha mkono aliinua ule uliokamata ile bilauri yenye kiuno iliyojaa mvinyo kutoka Dodoma. Baada ya kupiga funda moja kasha la pili aliiteremsha taratibu na kuiweka juu ya mbao mwororo iliyoifunika na kuipendezesha kaunta ya ukumbi huo. Macho yake yalikuwa yakizunguka huku na kule yakitazama au kutafuta kitu ambacho hata yenyewe hayakukijua.
Upande wa pili wa ukumbi huo, kwenye sakafu iliyojengwa juu kidogo na ili uifikie itakulazimu kuzikwea ngazi kadhaa, kulikuwako watu watatu, wawili wanaume na mmoja mwanamke. Mwanaume mmoja alikuwa na tambo kubwa lililojaa kimazoezi, enzi za utoto wetu tungeweza kumwita Pawa, lakini enzi hizi wanamwita Baunsa, yote hayo ni mabadiliko ya nyakati. Watu wale watatu walikuwa wakiongea jambo Fulani na meza yao ilikuwa imechakazwa kwa pombe kalikali na sahani za nyama zilizokuwa zikipishana, vyote hivyo vilimiminwa katika matumbo hayo matatu. Ilikuwa ni vigumu kusikia nini wanachokiongea kutokana na muziki mkubwa uliokuwa ukipigwa ndani humo. Kati ya kaunta alipokuwapo Gina na ule upande kulitenganishwa na kundi la vijana waliokuwa wacheza muziki huo kwa mitindo mbalimbali. Gina alihakikisha hapotezi macho yake upande ule kwani mwili wake ulikuwa ukisisimka mara kwa mara na hiyo kwake ilikuwa ni ishara ya hatari.
Dakika chache baadae alimuona Yule mwanamke akiinuka na kutoka katika vile viti, akitembea kwa mwendo wa ki-levi levi. Akamtazama na kujua mara moja kuwa alikuwa anaelekea chooni, Gina akajikuta akishuka kutoka kwenye kiti kirefu alichokuwa amekalia, akaigugumia pombe yake yote kinywani mwake, kasha akavuta hatua fupifupi akikumbana na walevi na wacheza muziki akaelekea kule alikokwenda Yule mwanamke.
Halafu nitamwuliza nini? Akajiuliza pa si na kupata jibu. Lakini aliendelea kuvuta hatua kuelekea kule chooni, akapinda kona ya kwanza na kuingia kwenye milango Fulani iliyokuwa ikielekea huko atakako, mbele kidogo alimuona Yule mwanamke akiingia katika moja milango ya vyoo vile. Gina; mkono wa kulia ukiwa nyuma ya suruali yake ndani kidogo ya jaketi lake, sikwambii alishika kitu gani, aliuendea ule mlango, mara ghafla akaanza kuhisi kitu kikimfinya mkononi mwake, ilikuwa ni saa kubwa ya mkononi, saa yenye uwezo wa kupokea nukushi, kupiga picha za mjongeo na mnato, yenye uwezo wa kurekodi sauti na pia unaweza kuitumia kama simu. Akainua mkono na kubofya kitufe Fulani kasha akasubiri kidogo. Wakati akisubiri kijimkanda hicho chembamba kikitoka kwenye saa yake, Yule mwanamake bado alikuwa chooni.
Mama yuko mahututi Shamba, Tena Saan Aisee! Uikuwa ni ujumbe uliosomeaka hivyo katika kile kijimkanda. Akakikata na kukitia mfukoni mwake kisha akaanza safari ya kutoka ndani ya Klabu ile, akili yake ilikwisha sahau juu ya Yule mwanamke, akapita mlangoni na kukumbana kikumbo na Yule mwanaume mwenye tambo kubwa, akielekea kule choo cha wanawake, Gina akasukumwa pembeni; na Yule bwana akapita.
Nje ya Klabu hiyo ndipo alipokutana na mvua ya kutisha, akapachua kikofia katika ukosi wa jaketi lake na kukivaa kisha akaliendea gari lake, mita kadhaa kabla hajalifikia akapiga breki na kuacha kinywa wazi, hakuamini anachokiona. Vioo vyote vya gari yake vilikuwa vimevunjwa, tairi hazina upepo na ndani kulijaa maji ya mvua. Wameiba? Akajiuliza, kisha kwa mwendo wa tahadhari akasogea kwenye lile gari, juu ya kiti cha dereva kulikuwa na bahasha ngumu ya khaki, akatazama huku na kule, alipojihakikishia usalama akaingiza mkono kwa minajiri ya kuichukua ile bahasha ijapokuwa ilionekana kulowana.
Daraja la sarenda saa 1:55 usiku.
BMW nyeusi iliyokuwa iking’azwa kwa mwanga wa radi, ilshuka katika barabar hiyo ya Kenyata kwa kasi sana ikitokea maeneo ya Masaki. Ilipofika katika makutano ya barabar hiyo na ile ya Ally Hassan Mwinyi mkabala na Ubalozi wa Ufaransa iliingia barabara kubwa bila kungalia usalama huku ikirusha maji juu kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha usiku huo.
Madam S alikuwa katulia kwenye usukani akiiongoza gari hiyo ya Mwingereza kwa umahiri mkubwa. Akakunja ushoto na kukanyaga mafuta kueleka mjini. Ilikuwa ni tabu kuona mbele kutokana na wingi wa mvua, barabara imejaa maji, umeme umekatika, ilikuwa ni shida juu ya shida. Madam S hakujali alilikanyaga daraja la Salenda na kuendelea mbele, lakini kabla hajalimaliza, hamad, kulikuwa a mwili wa mwanadamu uliolala barabarani huku mikono yake ikiwa imefungwa nyuma. Akaiyumbisha gari kuukwepa mwili huo, gari ikasota na kukosa muelekeo, akarudisha usukani kulia kuukwepa mwamba wa daraja, akaknyaga krachi na kuachia mafuta kasha akatoa gia ya tano na kushusha ya nne, kutahamaki gari yake ilikuwa ikihamia barabara ya pili, akakanyaga breki lakini ikashindwa kusimama, akaknyaga tena breki bado gari ilikuwa ikiendelea, ikapanda tuta lakutenga barabara, ikajipigia na kutua barabara ya pili, akili ikamrudia, akavuta breki ya mkono na ile BMW ikaserereka na kujizungusha.
Kishindo kikubwa kikasikika, BMW iligongana na Land Rover Defender, ikaangushwa pembeni. Madam S akajikuta kwenye pori la mikoko chini ya daraja la Salenda, akafyatua mkanda, akapiga kioo cha mbele kwa kukikanyaga kwa mguu, akatoka, akajipapasa na kukuta bastola zake zipo salama.
Damu zilizikuwa zikitiririka semu ya paji la uso juu kidogo ya jicho la kulia, wakati akijitahidi kusimama, radi kali ilipiga na kufanya mwanga mkubwa uliong’aza vichaka vyote, Madam S akaona mbele yake kama kivuli cha mtu aliyesimama nyuma yake. Akajua ni mawenge ya ajali tu, akageuka nyuma na mara ghafla akakutana na pigo la kitu kizito kilichotua katikati ya paji la uso, akayumba vibaya lakini mikono yake tayari ilikuwa imekwishachomoa bastola zake, kabla hajafyatua akafunikwa na gza nene lililomfanya ashindwe kuona chchote, akaanguka kama mzigo na bastola zikimtoka mikononi mwake.
Ofisi ya usalama wa taifa saa 2:00 usiku.
MAAFISA wa Idara ya Usalama wa Taifa walikuwa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida usiku huo. Katika moja ya ofisi za jengo hilo, vijana wawili na msichana mmoja walikuwa bize kutazama luninga nyingi zilizowazunguka zinazoonesha maeneo mbalimbali muhimu ya Jiji la Dar es salaam. Kupitia luninga hizo waliweza kuona moja kwa moja kile kinachotokea kwenye maeneo hayo kama Uwanja wa ndege, Bandarini, Stesheni ya Treni, Uwanja wa Sabasaba, Makao makuu ya Rais na maeneo mengine mengi ambayo yamepewa umuhimu wa pekee kwa sababu hii au ile.
Avant, msichana mbichi wa miaka takribani thelathini hivi alikuwa katingwa kuangalia tukio la ajali iliyotokea daraja la Salenda, bado alikuwa anapata shida kujua hasa nini kinaendelea kutokana na ile picha kufichwa na mvua ilikua ikinyesha eneo hilo lakini kila ilipokuwa radi ikipiga ndipo alipoweza kuona kitu, baada ya dakika kadhaa alipuuza na kuendelea kutazama maeneo mengine.
Mubah akajikohoza kidogo na kumgutusha Avanti kutoka pale alipokuwa akitazama.
“Si ukapime, au Mama yako anajua?” Avanti akamtania Mubah.
“Unanianza we mrembo, mi nasubiri time hapa niingie viwanja!” Mubah akajibu, huku akitoka kwenye kiti chake na kukiendea kile alichoketi Avant, akasimama nyuma yake, machoye akiwa kayakaza kwenye ile luninga.
“Shiit! Avant, nini hicho?” akauliza huku akisogea jirani zaidi.
“Ajali, imetokea kama dakika kumi hivi,” Avant akajibu.
“Kwa nini usipige simu polisi wawahi kama kuna chochote cha kuokoa?” Mubah akahoji.
“Sasa Mubah, Salenda pale kituo kipo jirani wataenda tu,” akaeleza huku akimtazama Mubah usoni.
“Yaani wewe! Kitendo cha kuitega kamera pale hatukufanya kwa makosa, lile ni eneo nyeti sana, kama ni ajali lazima polisi wafike mapema ili kuondoa kilichopo, pale vipngozi asilimia 99 wanapita, ikiwa hujuma utalaumiwa wewe kwani ndio eneo lako la kutazama leo!” Mubah akalalamika huku akiliendea kabati dogo lililo hapo jirani.
Avant akainua simu na kubofya tarakimu Fulani Fulani kasha akatoa taarifa hiyo kituo cha polisi cha Salenda. Haikupita dakika tano tayari kupitia luninga yake aliweza kuona gari na nyendo za polisi eneo hilo bila kujali mvua iliyopo. Avant aliendelea kutazama huku akigonga gonga karamu yake.
§§§§§
Gina alivuta hatua na kuingia katika lango kuu la Ofisi Nyeti, Shamba, akabofya namba zake za siri, kasha akaweka kiganja chake juu ya kioo Fulani kilichopo mlangoni na baada ya hapo akafanya kama anachungulia, kijimwanga chekunfu kikapita kati ya macho yake na kitasa cha ule mlango kikafyatuka, akaufungua na kuingia ndani. Moja kwa moja akaingia chumba Fulani na kuvua jaketi alilovaa, akabadilisha nguo na kurudi katika hali ya ukavu, akatoka na kutembea mwendo mfupi kabla hajagonga mlango Fulani kwa mtindo wa pekee na mlango ule ukafunguliwa.
“Karibu Gina!” Dkt Jasmine akamkaribisha na nukta chache baadae akampatia kikombe cha kahawa.
“Hawajafika?” Gina akauliza.
“Hapana, we ndiye wa kwanza, leo sijui kuna nini, labda kwa sababu ya mvua,” Dkt. Jasmin akaeleza.
Gina akashusha pumzi ndefu, mazungumzo mengine yakaendelea huku wakiwasubiri wengine, kila mara walikuwa wakitazama saa zao, hakuna simu wa taarifa yoyote iliyokuwa ikifika katika nyumba hiyo, Gina na Jasmine wakaanza kupata wasiwasi. Jasmine akainua uso na kuitazama saa kubwa ya ukutani, ikamwonesha kuwa ni saa 3:15 usiku.
“Hapana Gina, hii sio kawaida, tuanze kuwatafuta mmoja baada ya mwingine,” Dkt. Jasmin akamweleza Gina, kasha wote wawili wakaenda kwenye chumba maalumu cha mawasiliano, ndani ya chumba hicho ambamo ndiyo ofisi ya kudumu ya Chiba wa Chiba kulijawa na makompyuta na luninga nyingi huku na kule, simu za upepo, za kawaida na zile za satellite zilikuwepo. Kila kitu kilikuwa kinafanya kazi kwani haikuruhusiwa kuzima chochote labda tu kama kuna matengenezo, kila mmoja akaketi katika kiti chake na kuanza kucheza na simu zao za siri zilizounganishwa moja kwa moja.
Hakuna simu ya mkononi iliyokuwa ikipatikana si ya Madam S wala ya nani, walipigwa na butwaa na kubwa simu za nyumbani zote zilikuwa zikiita bila kukoma hazikupokelewa. Gina akamgeukia Dkt. Jasmine.
“Oya Shost, hapa ni mguu kwa mguu nyumba moja baada ya nyingine tukapate kujua kilichojiri,” Gina akamwambia Jasmine kasha wote wakaingia vyumbani na walipotoka walikuwa katika mavazi ya kazi, kila moja alibeba silaha anazoamini zingemfaa usiku huo kwani hawakujua hatari itakayowakabili. Wakiwa katika harakati hizo ndipo Gina alipokumbuka ile bahasha.
“Nisubiri Jasmine!” akarudi kwenye kile chumba akaichukua ile bahasha, bado ilikuwa imelowa akaichana taratibu na kuitoa karatasi ya ndani kwa uangalifu.
“Nini Gina?” Jasmine akauliza.
“Hii bahasha niliiokota kwenye ari yangu lakini sikuwahi kuifungua ndani,” akamjibu.
Gina alibaki kakodoa macho baada ya kukutana na kichwa cha habari kikubwa kilichosomeka ‘KITISHO!’ kisha chini yake kuliandikwa sentensi moja tu
Mwisho wa zama zenu umefika, mtaongea na Mzee Ngurumo.
Maneno hayo yalizigonga kwa nguvu nyoyo za wadada hawa, wakabaki wakitazamana, wkageuza macho yao wakaitazama tena ile karatasi.
“Gina!” Jasmine akaita.
“Jasmine!” naye akaitikia na wote wakatoka na kuingia kwenye gari ya Jasmine na kuondoka eneo hilo.
§§§§§§
Kerege – bagamoyo saa 4:07 usiku
TOYOTA Hilux Double Cabins, iliingia taratibu getini na kuegeshwa karibu na bustani ya maua iliyotengenezwa ndani ya ngome kubwa iliyobeba jengo la kifahari kuliko fahari yenyewe. Walinzi kadhaa walionekana kwenye kona zake, hawakushughulika kabisa na gari hiyo bali kila mmoja alishika lindo lake.
Dereva akashuka na watu wengine kama watatu hivi wakashuka, wakazunguka nyuma na kufungua funiko kubwa la alluminium lililotengenezwa ili kufunika mzigo uliopo ndani yake.
“Washushe hao, kisha wapeleke Kuzimu,” mmoja wa wale vijana aliyekuwa ameketi mbele akawaagiza wenzake kasha yeye akazikwea ngazi kulielekea jengo hilo lililoendezeshwa kwa taa zenye marembo mbalimbali.
Sauti za viatu vyenye kisigino kigumu zilisikika zikitembea lakini aliyevaa hakuonekana, Bwana Mpaya alibaki kusimama na kutazama kule sauti ile ilikokuwa ikitokea na asione mtu zaidi ya giza lililomlaki isipokuwa aliposimama yeye mwanga ulikuwapo na kufaya nuru ya kupendeza. Kasha ukimya ukatawala na sauti nzito ikalipenya lile giza.
“Ndio Bwana Mpaya, karibu sana, natumaini umekamilisha nililokutuma, sivyo?” alikuwa ni Pancho Panchilio aliyeyafikia masikio ya Mpaya aliyekuwa amesimama katikati ya sebule pana lakini asimwone anayeongea naye, isipokuwa sauti tu.
“Ndiyo Boss, tumewaleta lakini hali zao ni mbaya sana,” akaeleza.
“Vizuri sana, nani na nani mmempata?” akauliza tena.
“Tumempata Boss wao na Mtaalamu wao wa kompyuta,” akajibu.
“Ha! ha! ha! ha! ha!” akacheka cheko la pesa.
“Ok, wape vijana posho yao kama nilivyokwambia kisha unitafutie kichwa cha Kamanda Amata, huyu hasa ndiye mwiba kwangu, nataka apotee kwenye uso wa nchi ili binadamu tule vizuri, kuna pesa ndefu sana nimeiandaa mkilikamilisha hili,” Pancho akiwa mafichoni mwake akakohoa kidogo wakati Mpaya alikuwa akitoka, “Sikia Mpaya, hakikisha ukimuua Kamanda Amata, mkate kichwa, kisha kiwiliwili mkichome moto na kichwa mniletee, mbwa wangu hawajala nyama siku nyingi sana, maana Yule ni shetani anaweza kujiunganisha tena halafu akaangusha balaa, kwa heri!”
Alipomaliza kusema hayo na taa ndani ya jengo lile zikazimika.
2
KAMANDA Amata akaitazama gari yake aia ya Subaru Forester jinsi ilivyochakazwa kwa risasi, akashusha pumzi ndefu.
Wadude hawa wangeniua! Akajisemea moyoni huku akijaribu kuiwasha nayo ikawaka, akairudisha barabarani na kushika njia ya kwenda mjini, alijipapasa mifukoni hakuiona simu yake, wala saa yake mkononi haikuwepo. Any way! Akajipa moyo. Huku akiendelea kuutafuta mji wa Dar es salaam, saa ya ndani katika gari yake ilimwonesha kuwa ni saa tano za usiku.
Gina sijui kama atanielewa, maana tulikubaliana saa moja na robo, labda nitamkuta! Akaendelea kuongea na nafsi yake, huku akiiacha Gongo la Mboto na kuitafuta Uwanja wa Ndege. Katikati ya safari yake akafungua redio ndani ya gari na kusikiliza kinachoendelea. Ilikuwa ni kituo kimoja cha redio binafsi kikirusha habari hiyo ya dharula iliyoyanasa masikio ya Amata usiku huo.
…Mwili wa Mheshimiwa huyo umekutwa sakafuni bila uhai na kitu kama matundu ya risasi yakionekana kifuani mwake. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wake ili kuwakama waliohusika na mauaji hayo…
Amata akakanyaga breki kali na kuitoa gari barabarani kwani taarifa hiyo haikujitosheleza kwake, akaegesha gari pembeni na kutazama huku na kule hakuona mtu kupita eneo hilo, pembeni yake kulikuwa na bar iliyokuwa ikiendelea kuburudisha watu kwa vinywaji na vilaji, akashuka na kuiendea, alipofika tu akakutana na mwanadada mrembo aliyevalia nguo nyeupe juu na sketi nyeusi chini.
“Karibu kaka, karibu kiti,” Yule dada akamkaribisha Amata huku akifuta meza iliyokuwa hapo. Ijapokua haikuwa nia ya Kamanda kuketi, akajikuta amefanya hivyo, “Pole!” neon hilo likaupasua moyo wa Amata akamtazama Yule dada Mhudumu wa bar.
“Pole ya nini?” akauliza
“Una damu kichwani,” akamwambia.
“Shiit!” akang’aka na kujigusa, kweli akahisi maumivu na kitu kama jeraha.
“Asante sana!” akamjibu, “Unaweza kunisaidia simu yako?” akamwuliza.
“Haina salio lakini, halafu ni kisimu cha tochi,” akajibu kwa aibu.
“Naomba hivyo hivyo.”
Yule mwanadada akachomoa simu yake akampatia Amata. Ilikuwa ni simu iliyochakaa, iliyoonekana kupita katika mikono mingi ya watu mpaka kuifikia mikono hii ya huyu Mhudumu wa baa. Ilifungwa kwa mipira ya manati, betri lake lilishikiliwa na kipande cha mpira wa manati. Hakujali, aliitazama vyema kasha akaanza kubofya hapa na pale.
“Haina vocha hiyo!” Yule Mhudumu akaeleza tena.
“Usijali, kaniletee Bia baridi sana bila glass tafadhali,” Kamanda akamwagiza Yule dada lakini alilotaka yeye haikuwa bia ila zile dakika mbili za kubaki peke yake. Vidole vyake vikaanza kutomasa tarakimu Fulani Fulani na alipomaliza, akapumzika, wakati huo bia yake ilikuwa imefika, akaigusa, akamwonesha Yule Mhudumu alama ya dole gumba, kisha akabaki na hamsini zake.
Meseji iliyofuata katika simu hiyo ilikuwa ni kutoka katika kampuni moja ya simu nchini, Kamanda Amata alikuwa amechukua muda wa hewani kwa namna yao ya siri na sasa simu ile Kimeo ilipata uhai.
Akaanza kupiga namba za maswahiba wake wa kazi, Chiba; simu haikuita kabisa, Madam S vivyo hivyo, akaduwaa wa sekunde kadhaa, haikuwa kawaida kwa watu hao kuwakosa kwenye simu, akili ya Kamanda ikiruka chogo chemba. Mbele yake kulikuwa na luninga kubwa iliyokuwa ikionesha matukio mbalimbali ya Kitaifa na lile lililomvutia ni ajali ya Salenda, alisahau kupiga simu na kutazama tukio lile. Kamanda Amata alikaza jicho kutazama picha hizo lakini hakuzitilia maanani kwani wakati wa mvua ajali kama hizo ni za kawaida sana.
“Kaka hadi bia imepoa!” Yule Mhudumu alipita tena kwenye ile mea aliyokaa Amata.
“Oh, sorry,” akamjibu kasha akainua chupa na kujijiminia mafunda kadhaa, alipoishusha ilikuwa nusu tu.
Akaitazama tena ile simu akabofya tarakimu nyingine, akaweka sikioni, simu ikaita na kuita haikupokelewa kama ilivyokuwa kwa simu za nyumbani za Chiba na Madam S, akashusha pumzi. Nini kinaendelea? Akajiuliza. Akarudia kuipiga namba ya mwisho, akaweka simu sikioni, baada ya dakika moja ile simu ikakwapuliwa na sauti nyororo ya kike ikasikika tofauti na alivyotegemea.
“…Polisi Kituo cha Kati, nikusaidie nini?” ile sauti ikauliza.
“Mwenye Ofisi, Inspekta Simbeye yupo?” Kamanda akauliza.
“…Inspekta leo alitoka kama mida ya saa tisa alasiri, hajarudi bado…” Yule mwanadada akajibu.
“Alisema kuwa atarudi au aliacha maagizo yoyote?” Kamanda akauliza.
“…alisema tu kuwa angerudi kabla ya saa kumi na ni kawaida yake kutoka saa tisa na kurudi saa kumi kila siku, lakini leo mpaka sasa hajarudi…” sauti ile iliendelea kueleza.
“We umeingia kazini saa ngapi?” akamwuliza.
“…nimeingia saa nane nitatoka saa nne usiku… samahani lakini naogea na nani?” Yule mwanadada alipouliza hivyo simu ikakatika.
Ndipo Kamanda alipojikuta hayuko peke yake mezani, mbele yake kulikuwa na mwanamke mmoja aliyevaa vazi refu jeusi, hijab na kujificha uso wote isipokuwa macho. Kamanda Amata akamtazama mtu huyo kwa tuo, akainua chupa yake na kupiga funda la mwisho, alipoishusha ilikuwa haina kitu ndani.
“Kwa nini unapenda kudhalilisha dini ya watu? Unaingia baa na vazi kama hilo?” Kamanda akaanza uchokozi, lakini Yule mtu hakujibu kitu, alikuwa akimwangalia tu. Jinni au! Akajiwazia, kabaridi ka haja kakapita kutoka utosini mpaka unyayoni.
§§§§§§
GINA aliegesha gari mita mia mbili hivi kutoka katika lango la kuingilia nyumba ya Madam S kule Masaki, akateremka na Jasmine akafanya vivyo hivyo, kisha wote wawili wakarudi taratibu wakiachina nafasi ya mita kadhaa katikati.
Lango la mbele lilikuwa limefungwa, Gina alitazama huku na huko hakuona hata dalili ya binadamu kupita myaa ule, isipokuwa manyunyu tu ya mvua yalikuwa yakimnyurunyuta mwilini mwake. Akajipapasa katika kiuno cha suruali yake na kufatua kijipini chenye ncha mbili zilizojikunja kwa mtindo wa pekee, kishapo akachukua kipini kingne kutoka kwenye kibanio cha nywele zake, akatanguliza kile chenye ncha mbili katika tundu la funguo ya lango hilo, akachukua kile cha tatu na kukitumbukiza kati, akafanya manuva kidogo tu, kitasa kutoka Uingereza kikafyatuka na kuuruhusu lango lile kuwa wazi.
Skunde mbili zikapita, ya tatu na ya nne bila Gina kuingia ndani ya wigo ule mkubwa, akatazama tena usalama, bado barabara ilikuwa tupu, hakumuona Jasmine, moja kwa moja akajua kuwa kwa vyovyote keshajiweka katika kona maalum ya kumlinda swahiba wake. Akaingia ndani ya wigo huku bastola yake aina ya Winchester ikiwa mkononi. Akatembea kwa hadhari kubwa huku na huko akitazama hakuona mtu. Hatua tatu kuelekea mlango wa nyumba hiyo, ndipo alipoona kitu kilichomshtua sana, akasimama mapigo ya moyo yakimwendea kasi kifuai mwake.
Mbele yake kulikuwa na mwili wa Binadamu uliolala chali ukiitupa mikono yake huku na huko, hakuwa na uhai. Gina akajiweka tayari kwani aliona huo unaweza kuwa mtego kwake, akatazama jumba la Madam S, taa za ndani zilikuwa zikiwaka kwa mwanga wa kupendeza, ina akajikuta anaishiwa nguvu, akainua mkono wake na kuizungusha saa yake kwa namna ya pekee kasha akaisogeza karibu na kinywa chake.
“…Jasmine …” akaita, hakupata jibu, akazidi kuingiwa na wasiwasi. Dina akatulia pembeni ya ule mwili, akahisi kama kuna mtu anayekuja nyuma yake, akakamata bastola yake barabara, liwalo na liwe, akageuka ghafla tayari kwa shambulizi, hakuna mtu.
Shiit! Akajisemea. Akauruka ule mwili na kuufikia mlango wa nyumba ile kubwa, akatoa gloves mfukoni na kuivaa, kisha akashika kitasa kwa mkono wa kushoto uliokuwa na gloves akaingia ndani ya sebule pana, iliyomlaki bila hiana. Kila kitu kilikuwa katika utulivu wa hali ya juu sana, hakukuonekana kama kulikuwa na purukushani yoyote ndani ya nyumba hiyo, akajivuta kuelekea chumba cha Madam S, akaufikia mlango na kuujaribu, ulikuwa umefungwa. Akatumia hila ileile na kuufungua. Hata chumbani kulikuwa tulivu kabisa, hakukuwa na ishara yoyote iliyoonesha kama kulikuwa na pambano la kufa na kupona.
Akaenda pembeni mwa kitanda upande wa kichwani, akachuchumaa na kubonya vijinamba Fulani vya kificho ambavyo kwa mtu wa kawaida huwezi kuvigungua mpaka mmiliki akuoneshe. Droo moja ikafunguka na ndani yake ikajifunua kompyuta kubwa ika simama mbele yake, Gina akatikisa kichwa juu chini, kwani alijua kama hiyo kompyuta haipo mahala pake basi hali ya Taifa iko hatarini. Alikumbuka maneno ya Madam S siku alipomkaribisha nyumbani kwake kwa mara ya kwanza.
….heri mimi nife lakini hii kompyuta ibaki. Nikifa au nikipotea kabla hamjatangaza kifo change hakikisheni mnang’oa kompyuta hii na kuikimbiza Shamba kisha mtangaze matanga. Siri yote ya Taifa hili ipo hapa, mipango yote mibaya na mizuri ipo humu, watu wote wabaya na wazuri wapo humu…
Gina alijikuta analia machozi peke yake, nifanyeje, niondoke nayo? Akajiuliza, nitaifikisha Shamba salama? Akajiuliza bila majibu. Gina alijikuta kachanganyikiwa, hajui la kufanya, aichukue au aiache, kichwani mwake alielewa kuichukua kompyuta hiyo ina maana kuwa Madam S kafa au katoweka, na je kama kuna wanaotaka na wameshindwa kuipata hatoweza kuwa kawarahisishia kazi?
Ulikuwa ni mgongano mkubwa wa mawazo kati ya roho, moyo na ubongo wake, akaamua kuiacha. Akabofya tena zile tarakimu na ile kompyuta ikajirudisha ndani taratibu na kujigia mahala pake. Gina akashusha pumzi ndefu, akaitazama bastola yake na kunyayuka taratibu, akaufuata mlango na kutoka akiufunga nyuma yake.
KAWE – saa 4:02 usiku
LAND CRUISER ya polisi ilikuwa nje ya lango kubwa la nyumba ya Mheshimiwa Mbunge wa jimbo la Miroroso, wananchi wasio na dogo nao walijumuika nje ya nyumba hiyo wakikodoa kodoa macho kushangaa tukio hilo lisilo la kawaida. Hakuna aliyejali mvua ya rasharasha iliyokuwa ikiendelea kunyesha, watu walijikusanya kwa kujikunyata kutazama.
Ndani ya jumba hilo kulikuwa na Polisi waliovaa kiraia wenye bunduki kubwa kubwa wakiwa wanatembea hapa na pale, mwili wa marehemu Mbunge ulikuwa ndani ya chumba chake cha kulala. Polisi waliokuwa huko chumbani wakifanya taratibu zao za uchunguzi walikuwa wamekamilisha kazi yao, walitoka sebuleni na kuwapisha vijana wachache kutoka idara ya dharula ya kampuni binafsi ambayo husambaza gari za wagonjwa mitaani kwa minajiri ya kusaidia hali za dharula kama hizo.
Waliufunga sawia mwili wa Mheshimiwa katika mfuko maalumu na kuupakia kwenye machela yenye magurudumu, kasha wakaisukuma kuelekea kwenye gari yao iliyokuwa imeegeshwa pembeni tu mwa jumba hilo. Vilio vilisikika, wananchi wakalia na kuomboleza, walimpenda Mheshimiwa, ijapokuwa alipojenga jumba lake haikuwa jimboni mwake lakini bado alitoa misaada ya hali na mali kwa waliomzunguka.
“Alikuwa shujaa, kwa vyovyote wametumwa kumuua,” mwombolezaji mmoja alisikika akisema huku akifuta machozi yake.
Baada ya zoezi hilo ndipo Wananchi waliruhusiwa kuingia ndani na kuanza msiba huo. Hakuna aliyeamini kabisa juu ya lililotokea.
Lakini ilibaki hivyo kuwa Mbunge wa jimbo la Miroroso aliuawa na watu wasiojulikana.
§§§§§§
Kamanda Amata aliwekwa kati ya watu wawili huku mmoja na huku mwingine, mbele yake kulikuwa na mwingine tena ukiacha dereva aliyekuwa akiongoza gari hiyo. Wote walivaa maguo yaliyowaficha miili na sura zao. Hakuna aliyeongea; ile gari ilipita daraja la Salenda na kufuata uelekeo wa kwenda Mwenge, baada tu ya kupita daraja hilo, ikakunja kulia na kufuata ile Kenyata Drive, ilipomaliza maofisi ya Mabalozi iliiacha ile ya kwenda Coco Beach na kukunja kushoto, nyumba ya nne mbele ikasimama.
“Usilete makeke yako ya kipumbavu, tunataka kompyuta anayotumia boss wako basi,” akaambiwa na kuteremshwa chini, wakauendea mlango mkubwa na kuufungua, Kamanda Amata akatangulia mbele na wale jamaa wakamfuata nyuma, wote watatu walkuwa na Shot Gun mikononi mwao.
Wakatembea taratibu na kuipita ile maiti pale nje, moja kwa moja wakaingia ndani ya sebule, mmoja wao akasimama nje ya mlango wa sebule kuweka usalama, mwingine akabaki sebuleni na wa mwisho akaenda na Amata mpaka chumba cha Madam S.
“Usilete ujanja wako, tunajua kuwa ni wewe tu unayeweza kuitoa hiyo kompyuta hapo, haya fanya hivyo,” akamwambia huku akiwa kasimama umbali wa mita kama mbili hivi. Kamanda Amata akaiendea ile droo na kuingza mkono wake mahala Fulani, akapapasa anavyojua yeye, mara ile droo ikajivuta mbele na kufunguka, hakuna kompyuta! Yule mjinga akabaki katoa macho, akashangaa mahala pale hakuna kompyuta waliyokuwa wanaitaka ilhali wao walikuwa na uhakika kuwa ipo hapo baada ya kufanya uchunguzi wa kina.
“Haipo?” akauliza.
“Si unaona mwenyewe haipo!” Kamanda akajibu.
“Imeenda wapi?” akarusha swali la kijinga.
“Mimi na wewe tumeingia pamoja sasa nitajuaje ilipokwenda?” Kamanda akajibu kwa swali. Kama kuna kosa alilolifanya Yule mtekaji na atalijutia kuzimu ni ktendo cha kwenda kuhakikisha kwa macho kuwa Kompyuta ile haipo pale. Kamanda Amata kama umeme, kutoka pale alipokuwa amechuchumaa kuitoa ile Kompyuta, alijikunjua na kutawanya miguu yake sentimeta mbili kutoka usawa wa sakafu, Yule mjinga alipigwa ngwala kutoka upande wa nyuma na kujibwaga akitanguliza kisogo, yowe na kishindo vilimshtua Yule wa sebuleni akaja kwa kasi. Kamanda Amata alijirusha upande wa pili wa chumba na risasi zilizotoka katika bunduki ya Yule mtu wa pili zikachimba sakafu.
Kabla Yule bwana hajajiweka sawa, mwendo wa sekunde moja tu aliyoitumia kufanya shabaha ya pili dhidi ya Kamanda Amata, alijikuta akipaishwa juu na kujibwaga kama mzigo sakafuni tayari damu ilikuwa ikimtoka kama bomba. Amata alishuhudia hilo kwa haraka sana hakuelewa nini kinatokea.
Wamegeukana? Akajiuliza.
“Upo salama Kamanda Jitokeze!” sauti ya Gina ilimrudishia matuamaini. Kamanda Amata akajitokeza mzima mzima, lo! Domo la shot gun lilikuwa likimtazama umbali wa mita tatu tu kutoka pale alipo.
“Umeharibu utaratibu, nilikwambia usifanye makeke yoyote sasa wewe umekiuka kanuni, namuua huyu Malaya wako kasha naondoka na wewe,” sauti ya mtekaji ilisikika. Kamanda Amata akaona sasa mchezo usio rasmi unaanza kwani hakuwa na taarifa yoyote juu ya hii hatari.
“Umeshasema Malaya, we muue tu, hana thamani kwangu!” Kamanda akajibu.
“Leo hana thamani kwako wakati kila siku unamlala nyumbani kwako!” Yule mtekaji akaendele kuropoka, maneno ambayo yalimtia hasira Gina, akajaribu kukukuruka lakini hakuweza kutoka kwani kono la mtekaji lilimbana koo na akajihisi kukosa pumzi. Kamanda Amata alaimtazama Gina anavyoteseka, akawasiliana naye kwa macho, gina alielewa kitendo alichokifanya Kamanda.
Gina aliachia mkono wake kutoka kwenye ule wa Mtekaji lakini bado alikuwa kabanwa kwa kabala, akajizungusha na kukamata uume wa mtekaji huyo, akaubana kwa nguvu na kuuzungusha ghafla. Yule mtekaji akapiga kelele za maumivu, akamwachia Gina akabaki katoa macho ya kutisha, Gina akaendelea kuuzungusha huku amezikamata na korodani zake, Yule mtekaji akaanguka chini, Gina hakumwachia mpaka alipohakikisha kamtoa roho.
“Asante Gina!” Kamanda akamshukuru wakakumbatiana.
“Kompyuta Gina,” Kamanda akamwambia.
“Usiwe na shaka, nimekwishaitoa muda mrefu, wakati naondoka ndipo nilipoona hiyo gari inakuja, nikajibana hapo kwenye kochi kubwa upande wa nyuma hamkuniona. Niliposikia kile kishindo huko chumbani mlipo, nikajua kumekucha, nikamwona huyu wa sebuleni akija kwa kasi huko ndani, name nikajitokeza kumwahi kabla hajaleta madhara, ndipo nikamfumua bichwa lake, lakini sikujua kama kuna mwingine huku nje ndo huyu mpumbavu akanibana kabala. Pole sana Kamanda, nafurahi kukuona, Idara imetikiswa!” Gina alieleza kinachojiri.
“Gina haina haja ya kukaa hapa, twende tukajipange juu ya hili,” Kamanda akamwambia huku wakitoka. Walipofika karibu na geti, Gina akauchukua begi kubwa alilokuwa amelificha hapo wakatoka nje.
“We ulikujaje hapa?” kamanda akamwuliza.
“Shiiit!” Gina aling’aka baada ya kugeuka na kutoiona gari aliyokuja nayo. Akageuka kwa Kamanda na kumtazama usoni.
“Dr. Jasmine!” akamwambia huku chozi likimtoka. Amata akamtazama na kisha akaliendea lile gari walilokuja nalo na wale watekaji, akaingia, bahati nzuri halikuhitaji ufunguo, lilikuwa ni la kubonya tu nalo likawaka, wakaingia barabarani kuondoka.
KUZIMU – shimo la mauti
Kilikuwa chumba kikubwa chenye vijichumba vingi vidogo kwa vikubwa, kwa ujumla kilitisha kwani mafuvu ya vichwa vya binadamu yalipambwa ukutani kama mapambo ya kawaida, taa nyekundu kwa buluu ndizo zilizong’aza eneo hilo la kutisha, kulikuwa na friji kubwa mithiri ya chumba cha kuhifadhia maiti. Sehemu nyingine kulikuwa na stoo iliyohifadhi kila aina ya vikorokoro vya kutisha maalumu kwa ajili ya kutesea, kunyongea, na hata kuulia kabisa.
Chumba hiki kilijengwa chini kabisa ya jumba la kifahari la Mhindi Pancho Panchilio eneo la Kerege njia ya kwenda Bagamoyo, hakuna aiyejua kinachoendelea. Kwa nje lilikuwa ni jumba linalovutia kuliangalia, asilimia kubwa ya wananchi wa eneo hilo hawakuwahi kumjua wala kumwona mmiliki wa kasri hilo, ni watoto tu waliopenda kusemajumba lile ni la wanyonya damu kutokana na mambo kadhaa waliyokuwa wakiyaona, mara watu wameletwa huku nyuso zao zimefungwa vitambaa vyeusi na mambo kadha wa kadha kiasi kwamba ilipelekea watoto wa kitongoji hicho kukaa mbali na jumba hilo.
Lakini tofauti na watu wazima, wao waliwachapa fimbo watoto wao waliokuwa wakisema maneno hayo kutokana na kwamba kutoka ndani ya jumba hilo waliweza kupelekewa maji safi kwa mabomba maalum yaliyounganishwa na pampu kubwa na yenye nguvu, hivyo waliondokana na kero ya maji ya kunywa.
Mwili wa Madam S ulibwagwa chini kama roba la chumvi, haukuwa na uzima wowote.
Kibosho, akaangalia hali ya chumba kizima walichouhifadhi mwili huo, aliporidhika nacho akatikisa kichwa juu chini na kuwageukia watu wake.
“Ulinzi wa nguvu zaidi ya ule wa Ikulu, sawa?” akaagiza.
“Sawa Mkuu!” wakajibu. Akawaacha na kutoka, akaelekea chumba kingine, akakuta vijana wakimsulubu vikali Chiba wa Chiba huku akiwa ananing’inia kwenye minyororo, mwili wote ulitota damu, hakutamanika, hakuangalika. Kibosho alisimama mlangoni.
“Karibu sana kuzimu!” akamwambia Chiba aliyekuwa hawezi hata kuinua uso, “Wewe ndiye kinara wa kuvuruga mitandao ya watu sivyo, sasa utakuwa binadamu wa kwanza kushuhudia kifo chako mwenyewe baada ya kuwaona wenzako wote wako hapa, mbuzi nyie, nani aliwadanganya kuwa mna uwezo wa Kijasusi wa kuitisha Dunia? Sasa leo mtapambana na Shetani nah ii ndiyo himaya yake,” akaongeza kusema kisha akageuka kando akawatazama vijana wake walioonekana wana uchu wa kuua.
“Na Yule bibi, mfungeni kama huyu, lakini msimtese mpaka azinduke kama bado hajafa ili mateso yote ayashuhudie kwa akili na ufahamu wake, nimekuja hapa kwa kazi moja tu,” akamgeukia Chiba “Kuua!” akamaliza na kutoka huku akifuatiwa na vijana watatu wenye misuli ya ajabu. Chiba akiwa katika ile minyororo hakufanya lolote zaidi ya kutulia tu na kusubiri kuona nini kinaendelea.
§§§§§
Kamanda Amata waliitelekeza ile gari eneo la Hoteli ya Sheratoni na kisha wao kutembea kwa miguu mpaka ilipo ofisi ya Madam S. ilikuwa tayari imepita saa tano usiku, walinzi wakawapokea na kuwaruhusu kupita kwani walishazoea kuwa muda wowote watu hao huwa wanaingia ofisini. Moja kwa moja jicho la Kamanda Amata likaenda kwenye maegesho na hakuliona gari la Madam S, wakaingia ofisini na kuketi katika viti vyao kwa namba zao, kwani katika ofisi hiyo kila moja alikuwa na kiti chake kadiri ya namba zao za kikazi. Ukimya ulichukua nafasi kati yao, hakuna aliyeongea kwa sababu wakiwa hapo ni Madam S huwa anasema alichowaitia.
Kamanda Amata akamgeukia Gina.
“Gina, hili eneo si salama kwa sasa!” akamwambia.
“Yaani mi sina amani na eneo lolote, hata kitanda change nakiogopa, natamani kutoroka,” akajibu.
“Kutoroka! Sio suluhisho,” Kamanda akamwambia huku akinyanyuka na kufungua jokofu lililowekwa vinywaji vya kila aina, akatoa Konyagi ndogo na kuketi kitini, akachanganya na Sprite kisha akanywa taratibu. Gina alionekana kuwa mwenye mawazo mengi sana. Wakiwa katka ukimya huo mara simu ya mezani ikaita kwa fujo. Kila mmoja aliitazama hakuna aliyeipokea, baada ya kukerwa na kelele ya chombo hicho Kamanda Amata akaiinua na kuiweka sikioni bila kuongea.
“Kamanda Amata”, kisha cheko zito na la dharau likafuata, “…leo mtaishi kama digidigi, na nitawafuata popote mlipo mpaka nihakikishe nawamaliza, kwa taarifa yako, kibibi chako ninacho hapa nusu mfu, na wengine wawili, mmoja tayari ni marehemu kama unataka kumwona nenda kwenye vichaka vya Gongo la Mboto njia panda ya kwenda kwenye makaburi ya Wachina… tuachane na hilo, naihitaji hiyo kompyuta usiku huu… nipe kompyuta nikupe marehemu wako ukazike…”
Hasira ya Kamanda Amata ikawaka juu ya huyo asiyemwona,
“…kama unaitaka hii kompyuta njoo uichukue!” akamjibu.
“…Nataka uniletee wewe mwenyewe kwa mkono wako au huyo Malaya wako ambaye pamoja nawe mmeshanipotezea watu wangu watatu, kama hamtaki basi nitaichukua mwenyewe…” ile sauti ikaendelea.
“Acha uoga wewe! Kama unajiamini jitokeze tupambane, atakayeshinda atachukua kompyuta!” Kamanda akaongea kwa jazba, tayari konyagi ilishaanza kufanya kazi ichwani.
Yule mtu wa upande wa pili akacheka sana kisha akaendelea
“…sifanyi hiyo michezo ya kitoto, lakini nakuhakikishia kuwa nitaipata hiyo kompyuta, na nitazichukua roho zenu wote sita kabla ya jua kuchomoza,” akapiga mkwara.
“Na mimi nakuhakikishia kuwa nitakuwa nimekwisha kutoa roho yako na vibaraka wako kabla ya jua kuchomoza, shetani wewe!” alipomaliza kusema hayo, akainuka kitini.
“Unaenda wapi Kamanda?” Gina akauliza.
“Huyu mshenzi keshanitia wazimu, nitahakikisha namjua usiku huu huu na namng’oa koromeo lake, hawezi kufanya dharau na kitengo nyeti kama hiki, huyu hafai kuishi,” Amata aliongea kwa hasira.
Gina naye akasimama wima na lile begi lenye kompyuta mkononi, “Na hii je? Maana inaonekana wana uchu nayo,” akamwambia Amata.
“Tia kwenye sefu salama hapo hata uje na kifaru huwezi kuitoa,” akamweleza.
“Sijui namba za kufungulia,”
“Oh, sorry!” Kamanda akaichukua ile kompyuta na kuingia kwenye kijichumba kidogo kisha akaiweka mahala salama na kutoka na lile begi, akafungua kabati linguine na kutoa kompyuta iliyofanana na ile lakini ilikuwa mbovu siku nyingi, akaipachua hard disk na kulichukua lile ganda tupu akalitia kwenye begi, kisha wakatoka na kuchukua gari mojawapo iliyo kwenye maegesho.
“Gina, upo vizuri? Akili ipo sawa?” Kamanda akamwuliza. Gina hakujibu, alionekana kujawa na hofu kuu, Kamanda akamwangalia na kumwuliza tena.
“Gina, unakumbuka The Art f War?” akamwuliza.
“Hapana Kamanda!” akajibu. Kamanda Amata akatikisa kichwa baada ya jibu hilo.
“Gina wewe ni mwana usalama na haya mambo umejifunza chuoni hutakiwi kusahau mama, sawa?”
“Sawa!”
“Sikiliza Sun Tzu aliandika ‘Jifanye mchovu unapokuwa na nguvu na jifanye una nguvu unapokuwa mchovu’, hata mimi Gina ninaogopa maana simjui adui yangu kasimama wapi, lakini lazima na mimi nimtishe hiyo ndiyo Art Of War,” Kamanda alimtoa hofu Gina.
“Nimekuelewa Kamanda, sasa tunapambana vipi na huyu hayawani?” Gina akauliza. Kamanda akabaki kimya kwa muda, kisha akamgeukia Gina.
“Gina, naomba nisikujibu, na wala usinambie unachofikiria, unajua kwa nini?” akamuuliza.
“Hapana!” akajibu.
“Art of War inasema ‘Ifanye mipango yako iwe siri, isipenyeke kama giza la usiku, na unapojitokeza jitokeze kwa nguvu kama radi’ sio maneno yangu nia Sun Tzu na daima huwa napenda kufuata maneno yake ndiyo maana unaona hapa nilipo,” alipotaka kupachika ufunguo kwenye switchi ya gari Gina akamdaka mkono.
“Kamanda! Hayo uliyosema si ajabu hata adui anayajua,” akafungua mlango na kumvuta Kamanda nje, kisha wakaelekea getini na kutoka nje mpaka barabarani.
“Naona sasa umeanza kujua unalotakiwa kufanya, vizuri sana Gina!” Kamanda akampongeza kisha wakaingia kwenye tax na kutokomea.
Breki ya kwanza ilikuwa mje ya ukumbi wa Jiji mkabala na bandari ya boti za Zanzibar, wakalipa na kisha wakapotelea gizani.
Katika kaunta ya kituo cha Polisi cha Kati, kulikuwa na PC wawili na WP mmoja, Kamanda Amata na Gina walikwea ngazi na kusimama mbele yao. Wale Polisi mara moja walimtambua Gina na kusimama imara kwa kumpa heshima yake ya kijeshi.
“Inspekta Simbeye, ameonakana tena huku?” Gina akauliza.
“Yupo afande, amekuja muda si mrefu,” Yule WP akajibu.
“Naomba tumwone!” Gina akasema hayo huku tayari ameshaanza safari ya kuifuata ofisi hiyo.
Inspekta Simbeye alionekana kuzeeka ghafla kwani mashavu yake yalikuwa yameshuka kiasi kwamba Kamanda Amata alitamani kucheka.
“Shikamoo mzee!” Amata alianza kwa kuamkia kama kawaida akikutana na Inspekta huyo.
“Sina haja ya shikamoo yako, nakupigia simu Amata hupatikani kwa nini?” akauliza kwa hasira.
“Inspekta, kama ulivyowakosa wengine wote na mimi pia usingeshangaa, hata mimi sina mji wa kupokea, hali ni mbaya, nilikutafuta ulikuwa umetoka,” kamanda akajibu.
“Kamanda Amata! Ni nani huyu anayetufanya sisi wapumbavu kiasi hiki, Mheshimiwa Mbunge wa Miroroso ameuawa usiku wa leo, ni masaa mawili tu yalopita,” kabla hajaendelea Kamanda akamkatisha.
“Na hilo hasa ndilo limenileta kwako, nilitaka kujua ni nani aliyeuawa maana nimesikia tua lakini sikujua ni nani aliyeuawa!”
“Ni Mbunge wa Miroroso,” Simbeye akajibu.
“Ok, nimeelewa Inspekta, sasa picha inaanza kujijenga taratibu na itakamilika tu,” Kamanda akajibu.
“Huu umekuwa usiku mbaya sana, siwezi kulala kwa kuwa kifo cha huyu Mbunge kimekuja wakati mambo haya ya vita vya Ufisadi mliyopambana nayo huko Uswizz bado hayajapoa, na huyu Mbunge ndiye alikuwa mstari wa mbele kabisa katika kuyafichua, je huu si mnyororo mmoja?” Inspekta akaonesha wazi hofu yake.
“Nimekupata Inspekta, naomba niondoke kisha tuwasiliane dakika arobaini na tano zijazo,” Kamanda akajibu kisha akaondoka na kufuatiwa na Gina.
ITAENDELEA
Kitisho Sehemu ya Pili
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;