Kitisho Sehemu ya Pili
KIJASUSI

Ep 02: Kitisho

Kitisho Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE


Simulizi : Kitisho

Sehemu ya Pili (2)

HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI- SAA 6:47 USIKU

KAMANDA Amata akifuatana na Gina waliingia moja kwa moja chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo, wakamkuta Daktari akiendelea na uchunguzi. Wakiwa wanaongozwa na muuguzi waliingia ndani ya chumba hicho. Walipofika wakaonesha vitambulisho vyao kwa Yule daktari, hivyo hakuwatilia shaka.

“Karibuni sana!” akawakaribisha.

“Asante!” Gina akawa wa kwanza kujibu.

“Sijui niwasaidie nini? Maana nimechoshwa na maswali yenu yanayofanana,” Yule daktari akauliza huku akiwa amesitisha kuendelea kufanya uchunguzi.

“Nataka kujua maraehemu amekufaje?” Kamanda akauliza.

“Amepigwa risasi,” akajibu daktari.

“Ngapi?” Gina akawahi.

“Mbili za kifuani,” akajibu.

Kamanda Amata akasogea jirani na kutazama yale majeraha yalivyojipanga, moyo wake ukapiga chogo chemba, yalikuwa mithiri ya yale ya Frederick Masawe na Petit kule Uswizz, akatazama kwenye paji la uso la marehemu akaona alama ndogo ya risasi nyembamba iliyopenye bila uharibifu.

“Daktari, nah ii je?” akauliza. Yule Daktari akasogea na kwa kutumia kurunzi yake maalumu akagundua tundu hilo, wakamgeuza marehemu na kisogozi wakakuta matone machache ya damu.

“Amepigwa risasi tatu,” Kamanda akaeleza, “Asante Daktari, tulitaka kujua hilo tu,” wakamwacha na kuondoka zao.

“Kamanda hii kazi nyingine sasa,” Gina akamwambia Amata.

“Usijali Gina, hii kazi lazima imalizike usiku huu, kimya kimya mpaka kitaeleweka, leo nataka tufanye kazi hii ngumu mi na wewe tu, jua likichomoza tujue nini tumefanya na dunia ya pili isijue nini kimefanyika, usiogope, Art Of War iliyoandikwa na Sun Tzu inasema ‘Nenda taratibu kama upepo na muwe karibu kama miti. Shambulia kama moto na uwe imara kama Mlima’” Kamanda akamwambia Gina huku wakitoka nje ya chumba hicho.

“Twende nyumbani kwanza tukachukue dhana za kutosha kisha tuingie rasmi kwenye mpambano, tufanye haraka kabla watu wetu hawajapata madhara zaidi, Gina, piga simu Polisi Mabatini waambie kuna mwili wa marehemu kule Gongo la Mboto ili waende kutazama, na kama adui alitegemea kutunasa huko atapambana na vijana wa khaki,” Kamanda alimwambia Gina na mara baada ya Gina kufanya hivyo, wakaingia kwenye Tax.

“Kinondoni makaburini tafadhali!” Kamanda akamwambia dereva tax, kisha wakaondoka eneo hilo. Baada ya kuuacha Mtaa wa Mindu na kuchukua barabara ya Umoja wa Mataifa ndipo kamanda alipogundua kuwa kuna gari ikiwafuata, akamtazama dereva ambaye alionekana hajui chochote, walipopita shule ya Sekondari Tambaza ile gari ikawapita kwa kasi na kuwazuia kwa mbele.

Watu watatu walishuka kwa kasi kwenye ile gari, mikononi wakiwa na Shot Gun, waliishambulia ile tax kwa risasi na kuichakaza vibaya.

Kamanda Amata alimvuta dereva na kumsweka chini, mtawanyiko wa vyoo uliwafanya kushindwa kufanaya lolote, Gina alishuhudia lile begi likinyakuliwa na alipotaka kulitetea alipigwa na kitako cha bunduki akarudi chini, wale jamaa wakaondoka kwa kasi na gari yao wakapotelea katika mitaa ya Upanga.

Kamanda Amata akajinyanyua na kutoka nje, akamtoa Gina kisha Yule dereva ambaye alikuwa katika hali mbaya, hakuguswa na risasi lakini hofu ya milio ya zile mashine ilimfanya kuachia mkojo bila kujijua.

Kamanda Amata akachomoa kadi moja ya kibiashara na kumpatia Yule kijana, “Kesho jioni unitafute!” kisha yeye na Gina wakapotea eneo lile kabla Polisi hawajafika.

Walipokuwa wakikimbia, Gina alikuwa akiishiwa nguvu kila muda ukienda.

“Kamanda, Kamanda! Nakufa!” alilalamika.

“Jikaze Gina!” akamhimiza lakini hali haikuwa nzuri, Gina akaanguka chini. Kamanda akamtazama vizuri akaona mchaniko mkubwa a kichwani na damu zikimvuja eneo moja la mgongo karibu na nyonga, ilikuwa ni risasi iliyompata barabara katika eneo hilo.

“Shiiitttt!”

Akatazama huku na kule, akaona gari ikija kwa mbali, akamweka Gina chini na kuizuia kwa kuingia barabarani, hakuuliza, alimbeba Gina haraka na kumwingiza kwenye gari.

“Nifikishe Mtaa wa Upanga Seaview haraka!” akaamuru.

“Aliyekwambia hii tax ni nani?” Yule deeva akajibu kijeuri huku akizima gari na kuchomoa ufunguo. Kamanda Amata hakuwa na muda wa kupoteza, alfungua mlango akazunguka upande wa dereva, akafyatu lock na kumvuta nje, akamtupia barabarani kisha akakaa kwenye usukani, akachomoa kadi yake ya benki na kuivunja katikati, akaislaidi, katikati yake pakatokea ufunguo mdogo wenye meno mawili akaupachika kwenye swichi ya gari n kuiwasha kisha akaingia barabarani na kumwacha Yule mmiliki wa gari akipiga kelele.

§§§§§

SAA saba na nusu usiku ilimkuta Kamanda Amata katika jumba kubwa lililojengwa kandokando ya bahari ya Hindi huko Upanga, akaegesha gari mahala pake kisha akamtoa Gina ambaye tayari alikuwa amekwishapoteza fahamu.

“Usife Gina, usife tafadhali, subiri kidogo Gina!” kamanda alikuwa akiongea kama aliyechanganyikiwa huku kambeba Gina katika mikono yake akielekea ndani ya jumba hilo.

Dr. Khadrai alikuwa mlangoni akimwangalia kijana huyo ambaye wamekutana mara chache sana katika harakati za maisha yao.

“Karibu Amata, pole sana!” akamkaribisha na kumwongoza moja kwa moja mpaka kwenye chumba maalum ambacho kilishehenu kila aina ya kifaa tiba unachokijua, akamwonesha kitanda pa kumlaza Gina. Dr. Khadrai akamtazama Gina harakaharaka kisha akamtazama kamanda Amata. Akavuta mashine yake kubwa na kuchukua trei iliyojaa vikorokoro kisha akaanza kazi yake ya kitabibu, kwa kumsafisha Gina majeraha na kumtoa risasi iliyokuwa imenasa ndani. Kamanda Amata hakuwa na muda wa kusubiri.

“Daktari, maadam yuko mikononi mwako, naomba niende, kama kuna shida yoyote naomba unitaarifu kwa namba hizi,” akampa namba za Gina, kisha yeye akachukua simu mbili za Gina, akachukua saa na kumwachia simu moja ndogo ambayo si rahisi kwa mtu mwingine kuitumia kwa jinsi ilivyo.

“Amata usiwe na wasiwasi, huyu hajadhurika sana, akiamka tu nitakwambia,” kisha akaendelea na kazi yake.

KEREGE – saa 7:35 usiku.

PANCHO Panchilio alishusha siga alilokuwa amelipachika kinywani mwake na kulibana kwenye kibompoli maalumu cha kuzimia dubwasha hilo. Akainua macho yake na kutega masikio akisikiliza michakacho ya miguu ya mtu aliyekuwa akitembea sebuleni. Kwa jinsi alivyoijenga nyumba yake hiyo, yeye aliweza kumwona kila mtu lakini wale watu hawakuweza kumwona yeye nah ii iliwafanya kusikia sauti daima na kutokuona sura ya bosi wao.

“Karibu sana!” sauti yake ikaijaza sebule yote.

“Mkuu tumefanikiwa kuipata kompyuta uliyotuagiza Mkuu!,” Yule mtu akasema.

“Vizuri sana, sikufanya kosa kabisa kuwachagua ninyi watu makini katka kazi hii, je wale hayawani wawili mmewapata?” akauliza.

“Hapana hatujawapata lakini bila shaka wamefia kwenye gari waliyokuwa wakiitumia kwani tumeishambulia kwa risasi za kutosha,” akajibu, mara hakusikia kitu zaidi ya ukimya uliofuwatiwa na sonyo refu.

“Fanculato!” akatukana, “Kwa nini msihakikishe kama amekufa? Yule bwana ni hatari sana, hakikisheni mnapata habari zake usiku huu, naitaka roho yake kabla hakujapambazuka, potea!” akamukuza.

Pancho Panchilio alikuwa amekodi vikosi viatatu kwa nyakati tofauti na vyote kuvipa kazi moja tu ya kukisambaratisha kikosi cha TSA kuanzia Madam S mpaka wa mwisho. Mipango ya kazi hiyo ilipangwa kitaalamu sana na ilitumia mbinu za hali ya juu, mpaka dakika hiyo alikuwa tayari amefanikisha kwa asilimia sitini ya kile alichokidhamiria, nab ado muda wake bado ulikuwa unaruhusu kumalizia asilimia zilizobaki. Alihakikisha vikosi vyake hivyo havijuani na wala havikutani lakini vyote alikuwa amevipa kazi ileile kwa saa zilezile za kutekeleza lakini muda tofauti wa kufanya kazi.

Hakuona hasara sana kwa kupoteza vijana watatu usiku ule yeye aliishupalia dhamira yake tu ndio maana alikodi watu hao.

Kikosi cha kwanza kiliongozwa na Kibosho, Kanali wa jeshi aliyehasi na kupotea pasikojulikana, sasa alirudi baada ya kuitwa na Mhinidi huyo kwa kufanya kazi kama hizo. Kikosi cha pili kiliongozwa na mtu mmoja hatari kutoka nchi jirani aiyejulikana kama Kaburu na kikosi cha tatu kiliongozwa na mpiganaji aliyebobea kwenye taaluma ya kuua bila kukusidia huyu alikuwa ni mtaalmu wa kucheza na kifo mbele ya binadamu yeyote Yule, ni jambazi la kimataifa kutoka Kigoma, alijulikana kama Naima.

Hawa wote walipewa kazi kwa nyakati tofauti na wenyewe hawakujuana kama wana kazi moja kwa maana kila mtu hiyo ilikuwa ni siri kwake. Walipewa saa kumi na mbili za usiku tu kukamilisha kazi hiyo ngumu. Nao waliwasaka wabaya wao kwa hali na mali kuhakikisha wanamfurahisha bosi wao, malipo waliyopewa ni makubwa na yaliwapa jeuri ya kufanya hivyo.

Usiku huo kwao, ulikuwa usiku wa kazi.

3

KAMANDA Amata alikuwa kachanganyikiwa akili kwa namna moja au nyingine, alikuwa akiona kama ndoto inayotokea mbele yake, hakuamini kama wamewahiwa namna hiyo na kwa kasi ya ajabu, alijiuliza kila wakati ni nani mwenye uwezo wa kuwanasa namna hiyo, hakupata jibu zaidi ya hapo aligundua kuwa kwa vyovyote ni watu hatari wanaojua nini wanafanya na kwa wakati pia alielewa watu hao wamepewa kazi kwa muda maalumu hivyo nay eye kama ilimpasa kuwa saidia wenzake alitakiwa ajipe muda maalum na muda wa kazi yake uwe mdogo kuiko muda wa adui zake pia ucheze ndani ya muda wa adui zake. Alitikisa kichwa kana kwamba kuna mdudu akimtembea kwenye ubongo wake, akaitazama saa yake, saa zinayoyoma kwelikweli.

Ilikuwa inakaribia saa nane usiku alipokuwa akifungua geti la nyumbani kwake, akaingia na kulifunga nyuma yake, kisha akasimama kidogo kuangalia nini kinaendelea huku na kule, kwa macho yake makali aliweza kuona ua moja kubwa likitikisika kidogo, akaelewa wazi kuwa mtikiso huo lazima kuna kitu na si wa upepo kwani hali yah ewe ilikuwa imetulia sana na haikuwa na upepo. Damu ikamtembe haraka mwilini, hakufanya lolote, akauendea mlango wa nyumba kubwa na alipoufikia alikuta karatasi iliyoning’inizwa mlangoni, kisu chembamba chenye makali kuwili kilitumika kuishikia hiyo karatasi pale mlango.

Mwisho wa zama zenu umekwisha, mtaongea na Ngurumo.

Ulikuwa ujumbe uliosomeka katika karatasi hiyo pale juu. Akakikamata kile kisu na kukichomoa kwa nguvu, akakibusu, akaiokota ile karatasi na kuishika mkononi kisha akaingia ndani na kuuacha mlango wa nyumba yake bila kuufunga makusudi tu. Moja kwa moja akakiendea chumba chake na kufungua kabati kubwa lililokuwa mbele yake. Akavuta fulana yake nyeusi kaba shingo ya mikono mirefu akaivaa ikitanguliwa na vesti nyeusi pia. Kizibao cheusi chenye mifuko mingi ya kuwekea zana mbalimbali kikafuata juu yake, na zana zake zikapachikwa, bastola nne zilizosheheni risasi zikakaa mahala pake, visu vidogodogo vikawekwa mahala pake, paketi za risasi zikawekwa mahala pake, Shotgun mbili zikabanwa mahala pake nazo zikiwa zimetimia. Akakusanya vikolokolo vya kutosha kwa pambano hilo ambalo hakujua ni nani haswa anakwenda kupambana naye.

Akiwa kasimama kwenye kioo, anajiweka sawa, akahisi vinyweleo vyake vikisimama, mwili ukamsisimka, akajua kuna jambo, akalisubiri huku akijifanya hajui lolote.

Palepale kwenye kioo alimuona mtu akiingia kwa minyato kumfuata, Kamanda alitamani kucheka kwa sababu hata kama alikuwa akinyata wakati yeye alikuwa akimuona kwenye kioo ni kazi bure. Akamsubiri amkaribie ili ajue nini cha kumfanya. Yule mtu akajiandaa kwa waya aliokuwa kaufunga kutoka mkono hu mpaka ule mwingine.

Anataka kunikaba, Kamanda akawaza. Kisha kwa kasi ya ajabu akageuka na guu lake lenye nguvu likatua kichwani mwa Yule mtu, akajibwaga na kujibamiza kwenye mwamba wa kitanda, yowe la maumivu likamtoka, kabla hajafanya lolote akamnyanyua na kumpa kichapo kikali, alipohakikisha kuwa hali aliyokuwa nayo hawezi fanya lolote akamkalisha chini na kumwegemeza ukutani, akamtikisa na kumtazama usoni.

“Nani bosi wako?” akamwuliza.

“Si-si-simjui!” akajibu kwa tabu.

“Unaniletea utani siyo?” akamwuliza kwa ukali.

“Kweli simjui, mi natumwa tu na kulipwa ujira mkubwa wa kunitosha, kwa hali ya nchi yetu nakubali kufanya kazi yoyote kwa malipo yoyote,” akajieleza.

“Nafikiri hunijui sawa sawa sasa utanijua!” Kamanda akamwambia kisha akamkamata korodani zake na kuziminya kwa nguvu.

“Aaaaaiiiiggggghhhh…. Niache, niache nitasema,” akalia kwa uchungu.

“Sema, nani bosi wako, nani aliyekutuma kuja hapa?” kamanda akauliza sasa kwa ukali zaidi.

“Kweli kaka sim-ju-jui…” akajibu huku akijigeuza geuza.

Kabla Kamanda hajauliza linguine, akashuhudia povu jeupe likitoka kinywani mwa Yule mtu.

“Shiiit! Limejiua,” akang’aka kwa sauti, akaanza kumpekua.

Katika moja ya mfuko wa suruali yake akatoa simu ya mkononi, zaidi ya hapo hakuona chochote cha maana. Akaitazama ile simu, akaenda kwenye kitabu cha majina akakuta majina matano tu, la kwanza kabisa likamvutia, lilikuwa limeandikwa kwa jina moja tu ‘Naima’, kisha akaliangalia la pili na la tatu. Akaamua kuanza kampeni na jina hilo la kwanza.

Akaperuzi upande wa ujumbe mfupi, akakutana na ujumbe kutoka kwa Naima uliotumwa ndani ya dakika kumi zilizopita lakini ulionekana kutojibiwa.

‘…Akifika nijulishe nije nimalize kazi…’

ujumbe ulisema hivyo.

Lilifikiri litaniweza, sasa naanza na Naima, kawaza na kuamua kuujibu ule ujumbe.

Kamanda Amata akaujibu ule ujumbe, kisha akaburuza mwili wa Yule mtu na kuubwaga katika mlango wan je kisha yeye akalitoa pikipiki lake na kuliegesha nje kabisa, akisubiri kuona kinachoendelea.

Akiwa nje ya nyumba yake, juu yapikipiki lake kubwa akasubiri kimya nje kabisa ya nyumba yake.

Dakika tano hazikupita, mwanga wa taa za gari ukaonekana ukijitokeza katika kona ya barabara na kuelekea mtaa huo ilipo nyumba ya Kamanda Amata. Ilikuwa Ford Ranger nyeusi, haikuwa na namba za usajili, ikasoge polepole na kuegeshwa karibu kabisa na lango la nyumba hiyo, watu watatu wakashuka, mmoaj kati yao alikuwa mwanamke, alionekana ndiye akiongoza wengine, aliwapanga, mmoja alimwamuru abaki langoni, yeye na mwingine aliyeonekana pande la jitu waliingia ndani.

§§§§§

Naima na lile jitu moja kwa moja waliingia getini na kutembea kwa mainyato huku silaha zikiwa mikononi mwao. Wakiwa wanajigawa kiufundi zaidi kuuelekea mlango, walishangazwa na ukimya uliotawala, lakini hawakujali. Lilikuwa ni lile pande la mtu lililotangulia kuuendea mlango, kabla halijafika likajikwaa kwenye kitu kama gogo.

“Aah!” likajivuta na kujibwaga mbele. Lilipogeuka nyuma likaona mwili wa binadamu, “Shiit! Amemuua,” akasema kwa sauti.

“Nani amemuua?” Naima akauliza, kisha akashusha silaha yake na kusogea pale ulipo ule mwili, akaugeuza, na kuchomoa kijikaratasi kilichopachikwa kinywani mwa marehemu.

…Naanza na wewe…

Naima akageuka huku na kule asione mtu, anaanza na mimi! Hata kama Naima alikuwa ni muuaji mzuri kitaaluma lakini alijikuta akishikwa na ubaridi wa ghafla. Wakaingia ndani wakatafuta huku na kule hawakuona mtu zaidi ya redio kubwa iliyokuwa ikipiga muziki laini wa ‘Killing me softly’ akasonya na kutoka nje. Wakabeba mwili wa mwenzao na kutoka nao. Wakaubwaga katika nyuma ya pikap yao na kufungia. Kisha nao wakaingia garini na kuondoka.

§§§§§§

Kamanda Amata akawasha pikipiki lake, bila kuwasha taa, akaingia barabarani na kuwafuata taratibu, wakaikamata barabara ya Kinondoni na kuvuka daraja la Salenda kisha wakaelekea mjini, moja kwa moja mpaka Mbowe Club, wakaegesha gari na kuteremka kisha wakapotelea ndani.

Kamanda Amata akaingia baada yao na kuhakikisha hawapotezi katika himaya ya macho yake, akaketi katika moja ya viti vya kaunta na kuagiza glass moja ya Whisky akachanganya na sprite baridi kisha akawa anakunywa taratibu.

Wale jamaa wakaketi mahala Fulani wakijadiliana jambo lakini wakionekana kuwa na wasiwasi, kila mara Naima alionekana kuisoma ile karatasi na kuiweka tena mfukoni. Mara lile jitu la miraba mine likanyanyuka na kutoka mahala pale likamwacha Naima na mwingine mmoja. Kamanda Amata alipogeuka hakuliona lile jitu limeingilia kona gani, akili yake ikazunguka mara mbili, akateremka katika kile kiti na kujichanganya katikati ya watu waliokuwa wakiburudika na uziki katika ukumbi huo. Dakika kadhaa baadae akaliona lile jitu pale kaunta likinga’aang’aa macho, likabeba vinywaji na kuelekea kule lilikokaa tangu mwanzo, yote hayo Kamanda Amata alikuwa akiyatazama kutoka katika kundi la watu wale. Alipoona kuwa hakuna aliye na yeye alirudi tena kaunta na kuagiza kinywaji, lakini hakuweza kukimaliza baada ya kumwona Naima akinyanyuka kitini na kuelekea nje, Kamanda Amata naye akatoka na kumfuatilia mwanadada huyo.

Naima alisimama kati ya magari na kuweka simu yake sikioni kisha akaendelea kuongea na aliyekuwa upande wa pili.

Naima akiwa anaendelea kuongea na simu alihisi ubaridi ukimgusa maeneo ya shingoni, akashtuka akataka kugeuka.

“Tulia!” sauti nzito ya Kamanda Amata ikapenya sikioni mwake. Naima akatulia kama alivyoamuriwa, “Nilikwambia nitaanza na wewe, na ndiyo sasa naanza,” akaongeza.

“Weweni nani?” Naima akauliza kwa sauti yake nyororo inayoweza kumnyong’onyesha mwanaume yeyote Yule rijali.

“Mimi ni Yule mnayenitafuta, Kamanda Amata, na nataka unambie watu wangu wako wapi?” Kamanda akaongeza swali kisha akatulia. Naima naye alitulia bila kujibu, akitafakari la kufanya. Baada ya sekunde kadhaa, uamuzi aliofuanya haukuwa mzuri hata kidogo. Aligeuka na pigo kali kwa Kamanda Amata, lakini Kamanda aliliepa kiufundi huku bastola yake ikimtoka mikononi. Naima aliruka sarakasi kwa minajiri ya kuiwahi le bastola lakini kabla hajafika alijikuta akipokea teka la nguvu mbavuni na kutupwa upande wa pili, akajiinua haraka na kusimama wima kumkabili Amata. Amata alijiweka sawa mwili wake na kumwendea kama mbogo, Naima alijiweka sawa na kuvamiana na Amata, kama Kamanda alifikiri mwanamke huyo anapigika kirahisi alikosea, mapigo matatu ya haraka yalimwingia Kamanda akajikuta anapoteza netweki, akajaribu kujitutumua lakini akajikuta amedhibitiwa ka mikono imara ya mwanamama huyo.

Naima alijirusha hewani kama jani la mkorosho na kuachia dabo kiki za maana zilizotua sawia kifuani mwake na kumpeleka chini.

Kisha Naima akatua chini kwa miguu miwilia akimtazama Kamanda Amata akigalagala chini.

“Ha ha ha ha niliambiwa kuwa Amata ni mwanamume wa chuma kaa mbali naye! Chuma kiko wapi hapa? Na sasa nakuua kwa mkono wangu kwani nimeahidiwa pesa nyingi sana kama roho yako nikiipeleka kwa bosi wangu,” Naima aliongea kwa kujiamini huku akiiweka sawa mikono yake tayari kumshushia pigo la mwisho kijana huyo. Alipomjia kumvamia alimshuhudia Kamanda Amata akijirusha kutoka chini kwa mtindo wa ajabu na guu lake la kulia likatua chini ya kidevu cha Naima, akanyanyuliwa na kubwagwa upande wa pili meno kadhaa yakimtoka.

“Mpo chini ya ulinzi!” sauti kali ikasikika upande mwingine. Kamanda alipotupa jicho akaona polisi eneo hilo, akaruka sarakasi na kutua upande wa pili wa gari, akajibana sehemu ambayo kutokana na nguo zake hakuweza kuonekana, akitazama linaloendelea.

Amata alishuhudia wale polisi wawili wakichezea kichapo cha maana kutoka kwa Naima, wakishindwa kujitetea hata kwa ngumi moja kwani kipigo kilikuwa cha sekunde kadhaa lakini kikali.

Huyu mwanamke ni balaa! Akajisemea, upo muda wake nitamtia mkononi tu, akajisemeana kusonya.

KEREGE – saa 8 usiku.

KIKAO cha dharula kiliitishwa ndani ya kasri la Pancho Panchilio, watu watatu walingia ndani ya jumba hilo kupitia milango tofauti kiasi kwamba hata walinzi tu hawakuweza kuwaona wageni hao. Walijikuta ndani wakiwa waneketi katika mtindo wa duara na Yule kinara wao akiwa mbele pa si na kuonekana. Wote waliketi kimya kabisa wakisubiri mkuu wao aongee.

Akajikohoza kidogo kutengeneza koo lake, kisha akafungua kikao hicho kisicho rasmi.

“Wajumbe mtashangaa nimewaita ghafla usiku huu, lakini lengo ni kuwapa taarifa ya kile kinachoendelea mpaka sasa,” Pancho alianza.

“Ndio tunakusikiliza,” mjumbe mmoja akaitikia.

“Vikundi vyetu vimefanya kazi kubwa sana na vimefanikiwa kuwakamata watu watatu, yaani namba moja, namba tatu na namba nne, na hali zao ni kifo muda wowote,” akaendelea.

“Ndiyo hata mimi nilikwishasema kuwa, hawa wakikamatwa ni kuwaua tu na maiti zao tunateketeza kwa moto ili kupoteza ushahidi,” Mjumbe mwingine akaongeza.

“Lakini sasa kuna kikwazo kimoja,” Pancho akatulia hapo.

“Kikwazo gani tena?” akauliza mjumbe.

“Namba moja wao ndiyo anyelete shida na kati ya watu wetu tuliowapa kazi kumbukeni ni vikosi vitatu mashuhuri, watu wane wameshapoteza maisha kwa mkono wake,” akawapa ujumbe uliowashtua kidogo.

“Unasema!” Mjumbe mmoja akaonekana kuanza kuchanganyikiwa.

“Habari ndiyo hiyo! Hivi sasa vijana wapo mtaani wanamsaka mshenzi huyo, mmoja kati ya hao tumemuua yupo katika machaka ya Gongo la Mboto ambako huko pia tumemkosakosa Amata ijapokuwa vijana wetu walilishambulia vikali gari lake lakini alitoweka.”

“Huyo siyo binadamu ni shetani, kwanza mi siku zote sijawahi kumwona japo nimefanya juu chini nimwone japo kwa sekunde moja, namsoma tu vitabuni,” mjumbe ambaye ni mzee kuliko wote aliongeza na wote wakacheka.

“Sasa tunafanyaje?”

“Vikosi vyetu vipo kazini, bado vinasakana na huyo Amata, hwa tulio nao nafikiri ni kuwamaliza kuwaweka hapa ni hatari kwani wakipata nguvu madhara yake ni makubwa,” Pancho akashusha pumzi, “Ila hapa kuna habari njema,” aliposema hayo wote wakakaa sawa.

“Tumeipata kompyuta mama, ile ambayo anatumia boss wao Yule bibi,” akawaambia.

“Eewaaaa hilo nalo neon asee!”

“Sasa ina neno fungushi ndiyo tatizo (password), maana humu ndimo kuna siri zote za hawa jamaa, nilikuwa nawasubiri kwa pamoja tuamue la kufanya,” akaeleza.

“Ni kutumia nguvu tu kupata hiyo password, wenyewe wanaijua, sasa wape kazi vijana watumie nguvu ili kupata hiyo password tujue kilichomo, hawawezi kutupanda kichwani,” Mjumbe mzee akatoa wazo.

§§§§§

Taarifa za kupatikana kwa mwili wa Scoba zilimfikia Kamanda Amata, nguvu zilimwishia kabisa hakuwa hata na la kufanya. Aliitazama saa yake mkononi ilikuwa saa nane na uchafu wake, muda unayoyoma, hakujali aliliwasha pikipiki lake na kuelekea hospitali ya jeshi Ukonga ambako aiambiwa mwili huo umehfadhiwa kwenye chumba maalum.

Hakuamini alipomkuta Scoba kalala kimya huku madaktari wakijaribu kupigania uhai wake wa mwisho. Kamanda Amata alisimama mlangoni na kisha akarudi nje, akajinaamia kwenye ukuta machozi yakimtoka.

Akachomoa mfukoni simu yake na kuiweka sikioni, akamsubiri mtu wa upande wa pili ajibu.

“Ndiyo konokono vipi?” sauti ile ikauliza.

“Konokono anahitaji miguu ya kutembea!” kamanda akaeleza kwa lugha waliyoelewa wenyewe.

“Mwambie aje kuchukua!” akajibiwa na simu ikakatika.

Kamanda Amata akapiga namba nyingine na kuisikiliza.

“Hello!” sauti ikaita.

“TSA namba moja anaongea!” akajibu lile itikio.

“Unasema nani a-a-naonge-a” kigugumizi kilimshika mtu wa upande wa pili.

“TSA namba moja ninaongea, Mkuu naomba tuonane ofisini kwako usiku huu, haraka sana,” Kamanda akatoa amri.

“Kuna nini Namba moja?” akauliza Mkuu wa Usalama wa Taifa Bwana Hosea.

“We naomba tuonane tutajua hapohapo kuna nini…”

“Ok! Copy and paste,” Hosea akajibu huku akikiacha kitanda na kumbusu mkewe Techla aliyekuwa kazama usingizini, kalala fofofo.

USALAMA WA TAIFA – saa 8:40 usiku.

MKUU wa kitengo cha Usalama wa Taifa, Bwana Hosea aliwasili katika jengo hilo na kupokelewa na walinzi, kila mmoja alishangaa kumwona mtu huyo usiku mnene kama huo, kuja kwake halikuwa tatizo, tatizo ni kuja ghafa na bila taarifa. Hakuongea na mtu, alipita moja kwamoja katia sebule kubwa ya kupokelea wageni.

“Mkuu mbona hivyo vipi?” Avanti alimtupia swali walipokutana koridoni.

“Salama tu, upo nani ofisini?” akamuuliza.

“Nipo na Muba,” akajibu.

“Ok, kuna lolote la ajabu mliloliona? Au taarifa mliyoipata?” akamwuliza.

“Ni ajlia iliyotokea Salenda, lakini tumeishaianyia kazi, na mauaji ya Mheshimiwa Mbunge wa Miroroso,” Avant akamweleza.

“Ok, nitawaona baadae kama nitawahitaji,” akamwambia huku akiiendea ofisi yake.

Dakika moja tu baada ya yeye kuingia katika jingo hilo, pikipiki kubwa la Kamanda Amata lilifika getini.

“Jitambulishe!” ilikuwa sauti ya mlinzi.

Kamanda Amata, akataja namba yake ya siri inayomtambulisha kikazi badala ya kitambulisho. Ukimya ukachukua nafasi kisha geti likafunguliwa naye akaingia. Akaegesha pikipiki lake na kuuendea mlango mkubwa, moja kwa moja ofisini kwa Hosea. Akamkuta Mkuu huyo akiwa ametulia kitini na bastola yake kaiweka uchi mezani.

“Karibu Namba moja!” akamkaribisha kwa hofu sana.

“Asante Mkuu! Samahani kwa kukusumbua maana imebidi umwache shemeji,” akamtania.

“Usijali, ndiyo kazi zetu hata yeye anajua, niambie Namba moja, vipi usiku huu, maana hujawahi fika ofini kwangu zaidi ya mwaka mmoja sasa,” akaanza kumhoji.

“Mkuu hali ni mbaya! Ni Kitisho!” kamanda akaanza namna hiyo.

“Unasema?” akauliza.

“Nasema idara ina hali mbaya!” akakazia.

“Kamanda Amata, TSA 1, nini tatizo?” Hosea akauliza.

“Mkuu, Madam S hajulikani alipo, Chiba, Dr. Jasmine wote hawajulikani walipo, Gina yuko mahututi kwa Dr. Khadrai, Scoba naye habari yoyote inaweza kutokea,” Kamanda akaeleza na kuangusha chozi.

“Kamanda Amata…!” Hosea akanyanyuka kitini na kuliendea dirisha kubwa la ofisi yake, alionekana wazi kuchanganyikiwa na taarifa hiyo, akajishika kiuno, akatikisa kichwa, akajipigapiga kichwani mara kadhaa kana kwamba analazimisha kukumbuka kitu, akasonya na kugeuka alipo Kamanda Amata.

“Eti unasemeje? Ina maana wametekwa au wameuawa?” akauliza tena kama hakusikia aliloambiwa.

“Siwezi kujua kama wametekwa au wameuawa! Ila wametoweka, na hapa unaponiona ninatafutwa kwa ubani na uvumba,” Kamanda akaeleza.

Mara hodi katika mlango wa ofisi hiyo ikabishwa.

“Ingia!” Hosea akaitikia, “Vipi, usiku huu sasa!”

“Samahani Mkuu, kuna taarifa hapa ambayo ungeikuta asubuhi lakini maadam upo ni muhimu kuiona tena haraka iwekanavyo,” Mubah akakabidhi karatasi ndogo kwa Hosea kisha yeye akaondoka. Hosea akaitazama kwa makini, akairudiarudia kuisoma kama haielewi.

“Japokuwa si kazi yako lakini tazama hii taarifa,” akampa Kamanda Amata, akaipokea na kuisoma, moyo ukamlipuka, akaanza kuhema kwa nguvu.

…Moja ya gari zenu imepata ajali leo wakato wa mvua kubwa katika daraja la Salenda, ndani ya gari hajapatikana majeruhi wala maiti, tunaomba ushirikiano wenu…

Ilikuwa ni sehemu ya taarifa hiyo, Kamanda Amata akashusha ile karatasi na kuiweka mezani.

“Naomba niwe na haraka!” akamwambia Hosea.

“Bila shaka kamanda!” akamjibu. Amata akachukua simu ya ofisini kwa Hosea na kuzungusha tarakimu kadhaa kisha akaweka sikioni.

Akaongea na mtu aliyemtaka kisha akaishusha simu na kuiweka mahala pake.

“Kamanda, njoo huku!” Hosea akamwambia kisha wakatoka na kuelekea chumba cha mawasiliano.

Wakaingia katika chumba kipana ambacho kilikuwa na kila aina ya mawasiliano ikiwe zile kamera za mabarabarani na sehemu nyeti Dar es salaam.

“Nyie, hii ajali imetokea saa ngapi?” Hosea akauliza.

“Saa moja kama na nusu hivi Mkuu!” Mubah akajibu.

“Sasa, saa moja mpaka sasa nane, na mnajua gari iliyopata ajali ni ya kwetu, eh! Mubah, Avant mlikuwa mnafanya nini humu ndani…?” Hosea aliongea kwa hasira, Mubah na Avant wakabaki kimya huku Mubah akimtazama Avant kwa chini.

“Hebu rudisha nyuma nione hiyo picha kwanza!” Kamanada akaomba. Avant akafanya hivyo na ile picha ikafika mahala pake, Kamanda Amata akashuhudia ile gari ikiacha njia na kupanda tuta la katikati kisha ikajipiga mwambani na kupinduka vibaya kabla ya kutumbukia kwenye mikoko chini ya daraja. Akairudiarudia kama mara tano hivi, kisha akamgeukia Hosea.

“Vipi?”

“Hii ni gari pekee ya Madam S japo siioni vizuri kutokana na mvua lakini bila shaka, tazama hapa, hapa, hii ni BMW umeona ee?” akamwonesha vizuri Hosea.

“Nyie vijana muwe makini nyie! Siku nyingine nitawafaya, sasa unajua kwa kuchelewa kupata hii taarifa meshaliweka pabaya Taifa na ninyi kazi yenu ni kuangalia usalama wa Taifa, nipigieni simu wakati wowote ule nitakuja kazini,” Hosea alilalama.

“Samahani boss, siku niliyopiga simu mkeo Techla alinitukana eti mi ni hawara wako,” Avant alilalamika.

“Avant haya ni mambo ya kazi achana na mke wangu! Sawa?” akafoka na kutoka ofisini. Wakasimama kwenye korido yeye na Kamanda Amata wakijadilia jambo.

“Sasa Mkuu, yaani hapa muda hautoshi, lazima kwanza niione hiyo gari kisha nijue la kufanya, na mimi nahusisha matukio haya na lile la mauaji ya Mbunge,” Kamanda akaeleza.

“Hapo umenichanganya kidogo!” Hosea akamwambia Kamanda.

“Nilikwenda kukagua maiti ya Mheshimiwa, mauaji yake yamefanana kabisa nay a wale waliouawa Uswizz, mlenga shabaha alifanya vile vile, kumbuka huyu Mbunge ni Yule mwenye kelele za kuibua mambo bungeni hasa sakata hili la kutorosha mapesa nje ya nchi,” kamanda akaeleza kwa undani mambo mbalimbai anayoyatilia mashaka.

Hosea, Mkuu wa idara ya Usalama wa Taifa wa nchi akabaki kinywa wazi, akajishika kidevuni hasijue la kufanya.

“Ok Kamanda, sasa ulikuwa unasemaje?” Hosea akarudisha mazungumzo nyuma.

“Mkuu kwanza nilikuwa nakupa hiyo taarifa na unajua taarifa zetu huwa ni salama kwa kuziongea ana kwa ana,” akamweleza.

“Ok Kamanda, sasa ulikuwa unasemaje?” Hosea akarudisha mazungumzo nyuma.

“Mkuu kwanza nilikuwa nakupa hiyo taarifa na unajua taarifa zetu huwa ni salama kwa kuziongea ana kwa ana,” akamweleza.

“Idara, imepata taarifa kama ulivyoileta, sasa wewe endelea na harakati zako, na mi hapa nawaita vijana wangu usiku huu, ili kuanza uchunguzi wa kina nitakutaarifu muda wowote nikipata lolote, nawe unitaarifu muda wowote ukipata lolote, kama kuna mahala utahitaji nguvu nafikiri una kibali cha kuomba jeshi la polisi muda wowote sivyo?” Hosea akunguruma.

“Ndivyo!” Kamanda akajibu.

“All the best!”

KITUO CHA POLISI SALENDA – saa 9:11 usiku

GARI ya Madam S haikutazamika mara mbili, kwa ujumla ukiitazama ni kama imegeuzwa nje ndani; ndani nje, vyoo vyote hakuna, injini iko nje na mengine mengi. Kamanda Amata akaitazama kwa kina, akaikagua hapa na pale kwa utaratibu maalum sio kama ule wa polisi wa haraka haraka, yeye aliangalia kimoja kwa kingine. Akakagua magurudumu na kisha akatulia kimya.

Akiwa katika kuangalia ndani ya gari hiyo ndipo alipoona kitu cha pekee kabisa, heleni, heleni ambayo yeye anaifahamu sana, akaiokota akaitia mfukoni mwake. Kisha akamgeukia polisi aliyekuwa naye mahala hapo.

“Twende eneo la tukio!” akamwamuru.

Yule WP aliyekuwa zamu akajiweka tayari kwa safari fupi ya usiku huo, wakapiga hatu mbili.kamanda akamsimamaisha.

“We WP! Tunakoenda huko unafikiri kupo salama? Hata kama hamruhusiwi kubeba silaha, mimi nakwambia kachukue silaha,” akamwambia kwa ukali.

Dakika mbili baadae Yule WP alikuwa na SMJ iliyoshiba vyema, wote wakakaa juu ya pikipiki kubwa aina ya BMW wakaelekea darajani.

Mikoko mingi ilikuwa imekatika huku na kule, kwa ujumla palisambaratika.

“Mlikuja wangapi?” Kamanda akamwuliza.

“Tulikuja watatu,” Yule WP akajibu.

“Hamkukuta mtu hapa, majeruhi wala maiti?” akauliza.

“Hatukukuta,” akajibu.

“Njoo hapa!” Kamanda akamwita, kisha akamwonesha alama za miburuzo.

“Unaona hii, huyu ni mtu kaburuzwa kutoka hapa ilipoangukia gari mpaka kule juu labda, na hizi ni alama za viatu vya huyo aliyemburuza,” akamweleza. “Tazama hiki kioo cha mbele, hii ni risasi, kioo cha ajali hakiwezi kupasuka namna hii, kwa hiyo ajalia hii kabla haijatokea dereva alipigwa risasi,” akaendelea kumjuza.

Baada ya kuridhika na hapo wakarudi kituoni.

“Wote mlilikuwepo ajalini?” akauliza tena.

“Hapana walikuwapo watatu tu,” akajibiwa.

“Naomba wote waliokuwepo wafike hapa haraka!” akaamuru. Sekunde tu. Askari watatu wakasimama mbele ya Kamanda Amata akiwemo Yule WP.

“Vueni viatu!” akawaamuru. Nao wakavua na kuviweka pembeni.

Akavichukua kimoja kimoja na kuvigeuza chini kuangali soli za viatu hivyo, akawarudishia. Kisha akawashukuru na kuondoka kituoni hapo, alipovuka tu daraja la Salenda, mbele ya ubalozi wa Ufaransa akasimamisha pikipiki lake, akaichukua ile heleni na kuipachua katikati kisha akaipachika sikioni kama earphone.

Kwanza akasikia miruzi mikali, kisha utulivu ukafuata na sauti ya Madam S ikasikika kwa mabli kidogo.

…Nataka wote tukutane ofisini, Shamba, Chiba na mimi tumepata ujumbe wa kitisho, hili sio la kupuuzia, (ukimya ukatawala) nimetoka nyumbani, naelekea shamba, ofisi za Ubalozi, Daraja la Salenda…

Kisha ikasikika sauti ya maumivu, na kelele ya kishindo kikubwa kilichojirudia mara kadhaa.

…Angalieni kwa chini, ndani ya gari, fanyeni haraka. Atakuwa amekufa huyu! Sawa tu, mchukueni hivyo hivyo…

Akasikia sauti ya kitu kama kijiwe kikianguka kisha ukimya ukatawala. Kamanda Amata akashusha pumzi ndefu, akaitoa ile earphone na kuiweka tena kama heleni kisha akaiweka mfukoni, pepo wa hasira akampanda, akapiga kiki moja na pikipiki lile likakubali sheria, akaingiza barabarani na kuchukua barabara ya Kinodoni, kisha akakunja ile ya Kawawa akaambaa nayo mpaka Kigogo akatobolea Tabata akasonga mbele.

GEREZA LA UKONGA- saa 10:01 alfajiri.

MBELE ya Kamanda Amata kulikuwa askari Magereza mmoja aliyekuwa zamu usiku huo, baada ya kuwasiliana na Mkuu wa gereza na kuwasili pale, wote kwa pamoja wakakaa ndani ya chumba kidogo kwa mazungumzo ya kikazi.

“Ndio bwana!” Yule Mkuu wa gereza akaanzisha mazungumzo.

“Asee Mkuu, nahitaji kuona rekodi ya wageni wanaomtembelea Kanayo O. Kanayo na Mahmoud Zebaki, hilo tu!” Kamanda akatoa ombi lake.

Punde si punde ikaletwa rekodi karibu ya mwezi mzima, kila mtu alitembelewa mara nyingi na mkewe isipokuwa tu kwa Mahmoud Zebaki, huyu zaidi ya mkewe alikuwa akitembelewa na mtu mwingine aliyejiandikisha kwa jina la Ravi Kumar, Amata akatikisa kichwa. Akatazama juu huku na kule.

“Mna kamera za usalama hapa gerezani?” akauliza.

“Ndiyo zipo,” Mkuu wa gereza akajibu.

“Naomba nione rekodi yake ya tarehe 21 May mwaka huu,” wakanyanyuka wote na kupita kwenye ujia mrefu mpaka ofisi nyingine ndogo ambako walimkuta kijana mmoja mwenye cheo cha koplo, akafanya hivyo walivyoomba.

Tarehe ile mwezi ule saa ile, akaonekana mtu mwenye asili ya Kihindi akiingia katika chumba cha kuongelea, kisha Mahmoud Zebaki akaja pale wakafanya mazungumzo mafupi kama dakika tano tu. Kamanda Amata alikuwa akiangalia midomo yao na matendo yao, walipokuwa wakiagana. Mahmoud aliiweka mikono yake juu ya mbao iliyokaa kama meza katikati yao ijapokuwa walitenganisha na nondo, na Yule Mhindi akaweka juu yake na kuiondoa. Kamanda Amata akatazama sana kitu hicho na kukirudisha nyuma mara kadhaa akagundua kuwa kabla ya Ravi kuweka mikono juu ya mikono ya Mahmoud kuna kitu alikuwa akikisoma au kukiangalia kwa makini. Kisha akaondoka na kumwacha Mahmoud akiwa na tabasamu pana.

Walipoangalia tukio la siku nyingine walimuona Ravi akifuatana na mke wa Mahmoud na mazungumzo yao yalikuwa yalionekana wazi hayakuwa ya Kiswahili bali lugha Fulani kama si Kihindi basi ni Kibangla.

“Asante Mkuu!” Kamanda akashukuru.

“Umeridhika? Ni wajibu wetu kulinda Taifa, mimi na wewe,” Yule Mkuu wa gereza akamweleza Kamanda Amata.

“Ni kweli, nikiwa na shida yoyote juu ya haya nitakutaarifu,” akamjibu.

“Bila shaka, muda wowote karibu sana,” wakaagana na Kamanda Amata akaondoka. Kamanda Amata akashika njia na pikipiki lake kuelekea mitaa ya Msasani ambako nyumba ya Mahmoud Zebaki ndiko iliko na familia yake yote iko huko, akiwa njiani akapiga simu kwa kutumia simu ileile ya Gina kwa Inspekta Simbeye, akaomba askari watatu wenye kibali cha upekuzi na gari haraka sana, akapatiwa.

Saa kumi na moja alfajiri alikuwa tayari amewasili Msasani Peninsula na ile gari ilikuwa tayari iko pale.

“Mko kamili?” akawauliza.

“Ndio afande!” wakajibu.

Wakagonga na kuingia ndani ya jumba hilo, walinzi hawakuwa na tatizo baada ya kuona serikali imefika hapo. Wakagonga mlango mkubwa na mfanyakazi wa ndani akatoka.

Walipouliza kuhusu mama mwenye nyumba wakajibiwa hayupo lakini kwa kuwa walikuwa na kibali cha upekuzi na walipita kwa Mjumbe wa shina ambaye alifuatana nao upekuzi ukaanza, nusu saa iliwachukua polisi wale kupekuwa nyumba huku wote waliobaki wakiwa wameanyang’anywa simu zao za mikononi, hakuna kibaya walichokipata isipokuwa kitabu cha kumbukumbu kilichoonesha kuwa Yule mama amekwenda Zanzibar likizo yeye na watoto wake. Ndani ya kijitabu hicho pia baada ya kupekuwa sana wakakuta namba za simu za watu mbalimbali ikiwemo Ravi Kumar, na namba hiyo iliandikwa tarehe 21 May. Kamanda Amata aaliendea likitabu likubwa la TTCL linaloitwa Yellow Page na kutafuta jina hilo mpaka akalipata, na kugundua mtu huyo anakoishi, Mtaa wa India kitalu namba 453RF, wakaagana na Mjumbe wa shina na kuondoka zao mpaka mtaa huo, haikuwa tabu kufika ghorofa ya tatu na kumkuta bwana huyo akiwa hoi kwa usingizi.

“Nyie taka nni kwagu, usiku hii bana!” Ravi alalamika. Kamanda Amata hakuwa na shaka naye kwani picha aliyoiona ni ilele iliyosimama mbele yake.

“Mchukueni huyo, tuondoke naye,” Kamanda akaamuru.

“Jamani mmi nafanya nini nyinyi? Manonea sana raia nyie bana, acheni mimi tawapa pesa jingi sana mfungue maduka!” akalalama.

“Kelele!” Kamanda akamkoromea kisha wakampakia kwenye gari ya polisi mpaka kituo cha kati. Wakamwifadhi chumba maalum.

§§§§§

ITAENDELEA

Kitisho Sehemu ya Tatu

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment