Jiue Mwenyewe Sehemu ya Kwanza
KIJASUSI

Ep 01: Jiue Mwenyewe

Jiue Mwenyewe Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE


Simulizi : Jiue Mwenyewe

Sehemu Ya Kwanza (1)

UTANGULIZI….

TRACEY TASHA Muuaji hatari mwanamke kutoka nchi ya Marekani, anafanikiwa kumuua tajiri mkubwa wa Afrika Kusini, The Great Khumalo…

Ni mara tano na zaisdi ameshindwa kumuua tajiri huyo, lakini sasa anafanikiwa baada ya kubadili mbinu.

Zaidi ya huyo anafanya mauaji mengine katika miji tofauti ya ulimwengu, na hii inamfanya awekwe kwenye orodha ya watu hatari duniani ambao labda hawakutakiwa kuzaliwa.

Mashirika ya kipelelezi na Kijasusi ulimwenguni yanamsaka mwanamke huyu na kushindwa kumkamata.

siku chache baadae anapata kazi nyingine ya kufanya mauaji katika Afrika Mashariki, Tanzania…

Je ni nani huyo anayetakiwa kuuawa? Fuatilia kisa hiki mpaka mwisho….

CHAPISHO LA 01

1

DURBAN – AFRIKA KUSINI-Saa 3:21 asubuhi

NDANI ya jengo refu kuliko yote, Monte Blanc, lililopo katika jiji la Durban, jimbo la KwaZulu Natal, Afrika ya Kusini, ni mtu mmoja aliyekuwa akiwindwa kwa udi na uvumba. Ni mara sita kama si tano mtu huyo kakoswakoswa na muuaji hatari wa kike kutoka Marekani, Tracey Tasha. Mara hii kamfuata hukohuko katika ardhi ya nchi yake, Afrika ya Kusini.

Lamborghini Veneno, gari ya gharama kabisa duniani iliegeshwa taratibu katika maegesho Monte Blanc, nyuma yake ikasimama gari nyingine, BMW nyeusi, vijana wane wakakamavu waliovalia suti nyeusi zilizotanguliwa na mashati meupe na shingoni mwao kila mmoja alining’iniza tai ndefu nyeusi. Walikuwa kikazi zaidi; macho yao yakitazama kila upande kwa umakini wa hali ya juu, mmoja wao aliiendea ile gari, Lamborghini, akaufungua mlango na kuukinga upande wa juu kwa kiganja cha mkono wake wa kushoto ili atokaye ndani asijigonge. Kwa mtindo huu ilionekana atokaye ndani ya gari hiyo ni Mheshimiwa sana, delicate person.

The Great Khumalo kama alivyojiita, alitoka nje ya gari ile, akajiweka vizuri suti yake ya gharama, huku mkono wake wa kulia ukiwa kwenye kifundo cha tai ili kuirekebisha alianza kuvuta hatua ndogo ndogo na mwamvuli ukiwa umeshikiliwa juu yake ili manyunyu ya mvua yaliyokuwa yakinyurunyuta mudaasubuhi hiyo yasimletee tabu. Viajana wake walifuata nyuma wawili na mbele wawili, yeye alikuwa katikati. Ilikuwa ni ngumu kumgusa mtu huyu, tajiri sana katika jiji la Durban; nani asiyemjua Khumalo? Hakuna shule ambayo hajawahi kuifadhili katika jiji hilo, alijulikana, alipendwa, alitazamwa kama almasi. Anaitwa Gervas Khumalo aliyezaliwa na kukulia katika kitongoji cha Berea, alizaliwa katika familia yenye maisha ya kati, lakini iliyoweza kumlipia masomo yake ndani na nje ya nchi mpaka akawa mtu mkubwa.

Hatua zake zilimfikisha katika mlango mkubwa wa jengo hilo, ukafunguliwa kwani yeye hakutakiwa kushika sehemu yoyote, kila mtu alimhusudu, lakini hakukuwa na nafasi ya kumpa hata mkono kwani alikuwa akilindwa vilivyo, moja kwa moja wakaingia katika lifti ili kupanda juu katika ofisi Fulani ya jengo hilo. Monte Blanc, jengo lenye urefu wa mita 133, sakafu (ghorofa) 40, lililojengwa hapo tangu mwaka 1985. Ndani ya lifti hiyo alizungukwa pande zote na vijana wake waliosheheni silaha ndani ya makoti yao.

23, mmoja wao alibofya kitufe kilicho katika kuta ya dude hilo na mara tu likaanza kupanda juu. Lilipofika mahala lilipoamrishwa likasimama kitu kama kengele kikagonga kwa pigo moja laini, mlango ukafunguka, wakateremka na kutembea kuelekea mahala Fulani, wakaipita milango kadhaa. Kila mtu alipisha tajiri huyo apite. KwaZULU Beauty and Massage, wakasimama hapo, mlango wa kioo ukafunguka wawili wakaingia na tajiri wao na wawili wakabaki mlangoni kuhakikisha ulinzi. Khumalo moja kwa moja alienda katika kochi kubwa na kulikalia mara baada ya vijana wake kulihakikisha kuwa lina usalama wa kutosha. Muda huo huo mwanamke mrembo mweupe wa Kiafrika alijitokeza kwenye mapazia yaliyokuwa na nakshi za kumetameta. Ndani ya ofisi hiyo pana na nzuri kulikuwa na wasichana wane waliokuwa katika kazi zao za kila siku, mwingine mapokezi, mwingine kupokea pesa na kutoa risiti, mwingine usafi na mwingine kuongoza wageni kule wanakotakiwa kwenda.

“You are welcome Sir,” (karibu sana mheshimiwa) yule mwanamke akamsalimu. Ukimwangalia alivyo, utasema ni Malaika kashushwa kutoka Mbinguni lakini alikuwa ni Binadamu kama wengine.

“Thank you so much,” (asante sana) The Great Kumhalo akaitikia karibisho hilo, yule Mwanamke akampa ishara ya kumfuata naye akafanya hivyo.

Haikuwa mara ya kwanza kwa tajiri huyo na matajiri wengine wengi kufika sehemu hiyo, wote walifika hapa kwa minajiri ya kupata huduma ya kukandwa mwili, ili kuirudisha miili yao katika hali nzuri ya kiafya. Bwana Khumalo alikwishazoea mara nyingi kuja mahala hapo kwa ajili ya huduma hiyo, alikuwa amejipangia ratiba kabisa ya tendo hilo.

Akainuka na kumfuata yule mwanamke huku walinzi wake nao wakiwa nyuma yake, wakaingia katika mlango ule wa mapazia na kufuata korido ndefu, waliipita milango mingi ya vioo ambayo ndani yake kulikuwa na wanawake waliokuwa wakifanyiwa urembo wa mwili na nywele, vyumba vingine vilikuwa ni vya mazoezi ya viungo, kulikuwa na mabafu maalum kwa ajili ya wanaotaka kuusafisha mwili kwa mvuke.

Walifika kwenye moja ya milango ambayo daima huingia hapo, wale walinzi wakasimama nje ya mlango na bosi wao akaingia ndani pamoja na yule mwanamke kwa ajili ya kumpa huduma hiyo. Juu ya mlango ule kuliandikwa V.I.P.

SAA I6 ZILIZOPITA

UWANJA WA NDEGE WA LOUIS BOTHA

Ndege aina ya Boeing 747 ya shirika la ndege la Amaerica (American Airlines) ilikanyaga barabara za uwanja huo na kwa mwendo wa maringo iliegeshwa kandokando ya jengo kubwa na zuri. Ngazi zilisogezwa na abiria wakashuka mmoja baada ya mwingine. Katikati ya wasafiri hao alikuwa mwanamke mmoja wa kizungu, aliyezifunga nywele zake kwa mpira nyuma ya kichwa chake, miwani myeusi ya kumkinga jua ilitulia sawia usoni mwake ijapokuwa jua halikuwa kali sana kwani ilikuwa jioni tayari. Kwa hatua za hesabu na mwendo wa maringo aliiacha ngazi hiyo na kutembea kwa haraka kidogo kuingia ndani ya jengo kubwa la kupokelea wasafiri. Hakuwa na mizigo zaidi ya kibegi kidogo kilichotulia mgongoni mwake, akafanya itifaki za uhamiaji kisha akatoka nje ya jengo hilo. Moja kwa moja akaziendea tax zilizosimama nje hapo, akafungua mlango na kuingia.

“Hard Rock Café,” akamwambia dereva tax, naye hakuuliza mara mbili aliwasha gari na kuifuata barabara kuu, akakaza mguu mpaka katikati ya mji mbele ya mgahawa huo maarufu kabisa katika miji mingi mikubwa duniani.

Tracey Tasha, akamlipa dereva tax na kumuomba kadi yake ya kibiashara, bila kinyongo yule dereva akampatia. Tracey akazikwea ngazi na kuingia kwenye mgahawa huo uliosheheni Wazungu, hakuona mtu mweusi zaidi ya wafabyakazi wachache waliokuwa hapo, alipotupa macho upande wa pili aliona kumejaa watu weusi wengi sana wakw kwa waume pamoja na familia zao. Ubaguzi hauwezi kwisha nchi hii, alijiwazia huku akitoa noti ya Randi 50 na kuagiza kinywaji cha matunda. Kwa jinsi alivyokaa jioni hiyo katika mgahawa huo, alikuwa akitazama upande wa barabara, na ng’ambo ya barabara hiyo kulikuwa na jengo kubwa la takribani ghorofa kumi hivi, likipambwa na maandishi makubwa meusi yaliyobandikwa kwenye ukuta wa njano, KHUMALO TOWER, yalisomeka namna hiyo.

…Saa 2:00 usiku milango yote hujifunga kwa mitambo maalum ya kiusalama, ukisogele mita kumi na tano tu taarifa hupelekwa panapohusika…

Aliikumbuka sauti ya mteja wake bwana Robinson kutoka Canada alipokuwa akimpa maagizo akimwelekeza eneo ambalo atampata mbaya wake. Tracey, alishajaribu sana kumuua Khumalo kwa kulipwa kitita cha pesa lakini ni mara tano au zaidi alimkosa, alipompiga kwa risasi pale Uingereza miaka miwili iliyopita, alikuwa amevaa vazi lizilopitisha risasi, hakumpata, akajilaumu kwa hilo, mteje wake hakukata tama. Miezi kumi na moja baadae alimvizia tena katika hoteli kubwa huko Ethiopia akamtilia sumu kwenye chai, lakini kabla ya kunywa kulikuwa na mtu maalumu wa kuonja chakula au kinywaji chake, yule mtu akadhurika na kufa lakini bwana Khumalo akabaki hai. Kwa mara nyingine Tracey alimkosa mtu huyo. Tracey hakuwa mtu wa kufanya makosa, alipokabidhiwa kazi kama hiyo ni saa kumi tu angekwishakutoa uhai lakini kwa Bwana Khumalo ilikuwa ngumu, alitumia mbnu zote lakini alishindwa. Haiwezekani, alijisemea na kupiga ngumi meza.

Safari hii alimhakikishia mteja wake, kuwa ahesabu kazi imekamilika kwani hakuna njia nyingine zaidi ya kutumia mikono yake.

…Utaweza?…

Swali lililompa utata sana ambalo Mteja wake alimuuliza, nitaweza tu, kama nilivyoweza kwa wengine, akajibu mwenye ndani ya moyo wako. Punde si punde giza likaikabili Durban, Tracey akainua macho yake na kuona taa za barabarani zimeupendezesha mji huo, akanyanyuka taratibu na kutoka nje, akavuka barabara kubwa na kufika upande ule wenye lile jengo alilolikusudia, watu walikuwa wakitoka ndani yake kwani muda wa kazi ulikuwa umekwisha, Tracey alifika mlangoni na kuingia ndani akipishana na wafanyakazi wa maofisi mbalimbali ambao walitakiwa kuliacha jengo hilo kabla ya saa mbili kamili usiku.

“Fanya haraka uwahi kutoka bado dakika arobaini tu,” sauti ya mlinzi ilimwambia Tracey ambaye tayari alikuwa ameifikia lifti ya jengo hilo na kuingia, akabonya kitufe namba kumi, lakini lengo lake lilikuwa ni kufika ghorofa ya saba ambapo ndipo zilipo ofisi za tajiri, mmiliki wa jengo hilo The Great Khumalo. Akili yake ilicheza haraka sana, alijua wazio akibofya kitufe namba saba walinzi wangemshtukia kwa kuwa ghorofa hiyo mtu huenda kwa miadi maalum, hivyo akaenda gholofa ya kumi kisha akashika ngazi kuruidi ghorofa ya saba, akakutana na mlango wa kioo uliofungwa, akajaribu kuugusa na kuutikisa, haukutikisika, kitasa chake kilifungwa kwa ndani, akashusha besi lake chini akafungua na kutoa kifaa kinachojulikana kama Circular Glass Cutter chenye ncha ya almasi katika mwisho wake, akakibandika upande mmoja katika ule mlango na ile ncha akaizungusha vizuri kabisa alipotoa kile kifaa chake akatoka na kipande cha kioo katika mtindo wa duara, kikaacha pale tundu, akapenyeza mkono na kufungua kile kitasa kisha akaingia ndani kwa mwendo wa polepole akiangalia kila upande, mpaka alipoufikia mlango wa ofisi iliyoandikwa kwa maansidhi ya dhahabu M.D Khumalo, akachukua funguo yake katika mikoni iliyovikwa soksi maalumu za mikono ili kutoacha alama mahala popote, akaufungua taratibu nao wala haukumpa shida. Akaingia na moja kwa moja aliielekea meza kubwa iliyo tanguliwa na kiti kikubwa cha kuzunguka. Hakika ilikuwa ofisi ya kisasa mithili ya ile ya Rais.

Akatupa jicho mezani na kuona kile alichotaka, kitabu kikubwa cha kumbukumbu, akakipekua mpaka tarehe ya siku hiyo, akatazama tazama na kuona vyote viliandikwa kwa lugha ya kwao ki-zulu, katika tarehe inayofuata, akaona alichofikiri kingemfaa.

‘KwaZulu Natal Beauty and Massage, saa 3:30 asubuhi’, ilikuwa ni miadi ya kila mwezi, Tracey akatikisa kichwa kwa mtindo wa juu chini, akafunga kitabu hicho na kutoka ndani ya ofisi ile, akafunga ule mlango wa kioo na kukirudisha kile kipande cha kioo kwa gundi kali sana ambayo huwezi kugundua kirahisi kama palikatwa. Akatoka na kukwea ngazi mpaka ghorofa ya kumi akaingia kwenye lifti na kuteremka chini.

§§§§§

Mwanamke aliyekuwa ameandaliwa kwa ajili ya kazi ya kumfanyia massage alikuwa akisubiri mteje wake kama alivyoelkekezwa na bosi wake, na daima ni yeye tu aliyekuwa akimfanyia kazi hiyo kwa maana baada ya kumaliza zoezi hilo basi ndani ya vyumba hivyo Khumalo alipeana mapenzi mazito na mwanamke huyo.

Kabla tajiri huyo hajaingia katika chumba hicho walinzi wake walikikagua na kuhakikisha usalama, ndani kulikuwa na mwanamke mmoja tu kwa ajili ya kazi hiyo, wakatoka ili kumruhusu bosi wao aendelee na starehe zake. The Great Khumalo akaingia ndani ya kile chumba na kuingia tena katika kijichumba kingine kwa ajili ya kutoa nguo zake na kuvaa taulo.

Khumalo alitoka na kulala kifudifudi kwenye kile kitanda cha kufanyiwa massage, yule mwanadada akasogea na kibweta cha mafuta na kuanza kumpaka mgongoni.

“Yesss Beibi, fanya kama siku zote, mmmmmmhhh!” Khumalo alianza kuguna kwa ule mtomaso laini wa yule mwanadada, aliazna kumpigapiga vijingumi kwenye sehemu zake za mbavu, mgongo akipanda mpaka karibu na mabega na kushuka mpaka katikati ya mgongo.

Tracey Tasha alikuwa kimya kabisa kajificha katika bafu la chumba hicho, alipoona dakika kumi zimepita akajua sasa ndio wakati wa kutekeleza azma yake, kutekeleza kazi yake, leo nimekupata, akajisemea, akatoka taratibu kutoka katika lile bafu na kusigea mpaka pale kitandani nyuma ya yule mwanadada aliyekuwa akiebndelea na kazi yake. Akamsogelea na kusimama pembeni yake, yule mwanamke akamuona Tracey, alipopigwa na bumbuazi, Tracey alimuoneshea ishara ya ‘kimya’ kwa kuweka kidole chake cha shahada juu ya midomo yake. Kabla yule mwana dada hajaondoa mkono wake pale mgongoni mwa Khumalo Tracey alikuwa ameweka wa kwake, kisha akamsogeza nyuma yule mwanamke.

“Ooh Baby, vipi mbona umesita?” Khumalo akauliza.

“Hapana nipo naendelea na kazi we tulia tu,” Tracey alijibu.

The great Khumalo alishtuka kwa sauti ile ngeni akataka kugeuka kuona ni nani huyo, akachelewa, Tracey kwa nguvu zote za mkono wake wa kulia alipiga finger kwenye uti wa mgongo (lumber vertebrae),kwa vidole vyake viwili cha gumba na cha kati, alikamata uti wa mgongo na kuuvuta juu, akatengenisha pingili zake. Khumalo, alikuwa kama kapigwa shoti ya umeme, aliganda macho yamemtoka na kinywa kimeachama. Tracey alipohakikisha mtu huyo hana uhai, na zile pingili zilizoachana zimetokeza juu lakini bado ziko ndani ya ngozi, akapiga kapigo ka wastani kwa kutumia kiganja cha mkono zikarudi kama zilivyokuwa. Khumalo akalala kimya, Tracey alikuwa amevunja pingili za uti wake wa mgongo na kukata kabisa spinal cord upande wa juu kama unakuja shingozi, ganzi kali ikampanfda Khumalo, uhai wake ukaondoka ndani ya sekunde kumi tu za shambulizi hilo.

Tracey akageuka na kumuona yule mwanamke akiwa amechanganyikiwa hajui afanye nini, akamchukua na kumfungia kwenye chumba cha kubadilishia nguo, akamfungia kwa nje, akatoka na kuufungua mlango, akawakuta wale askari wawili pale nje, akajua akiondoka tu itakuwa soo, akawaita ndani akawaambia kuna shida, wakaingia, aliwakamata na kuwagonganisha vichwa kwa nguvu wakaanguka chini hawana fahamu, akatoka mlangoni na kuufunga kwa nje, taratibu akatoka mpaka mapokezi na mwisho nje wa jengo lile, ile tax ilikuwa imefika, akapanda na moja kwa moja akaelekea Uwanja wa ndege, amemaliza kazi.

“Boss, nimemaliza kazi kwa mkono wangu bila vurugu kabisa,” alimwambia Bwana Robinson kwa simu.

“Oh, hongera sana mwanamke, fika haraka Ontario, nakusubiri,” Robinson akamjibu.

Saa nne na nusu ndege ya shirika la ndege la Amerika iliiacha ardhi ya Durban na kuondoka zake.

§§§§§

PARIS – UFARANSA

Kilikuwa kikao cha watu wanne tu walioonekana kuwa na pesa sana mifukoni mwao na hata katika mabenki mbalimbali duniani.

Danford Touzony, mtu mwenye pesa za dhuluma, mwenye siri nzito kifuani mwake, siri isiyotakiwa kujulikana na mtu mwingine yoyote, alikuwa na rafiki zake hao wakiongea mawili matatu juu ya biashara zao na maisha kwa ujumla, hakuwa na hili wala lile kama hapo alipo kuna mtu aliyekuwa akimwinda mchana huo.

Walikuwa katika hoteli kubwa ya kisasa iliyojengwa katika mnara mkubwa wa Eiffel mjini Paris, nchini Ufaransa.

Bwana Danford Touzony alipata pesa nyingi sana na kuanzisha mabiashara makubwa baada ya kutoa siri nzito za kijasusi ambazo zilikusanywa na mtandao wa KGB na kuhifadhiwa katika makao makuu ya taasisi hiyo kule Lubyanka, Moscow nchini Urusi.

Alikuwa mwenye cheo cha kawaida sana katika shirika hilo miaka kadhaa nyuma, ushawishi alioupata na watu asiyowajua waliokuwa wakitaka kupata baadhi ya habari za kijasusi kutoka ndani ya shirika hilo walimwinda Danford mpaka walipohakikisha wamemtia mkononi na kumuahidi maisha mapya ya kila fahari aliyokuwa akihitaji.

Baada ya kukamilisha zoezi hilo hatari kabisa na kukabidhi siri hizo kwa watu waliozihitaji; alilipwa pesa nyingi sana na akapewa hifadhi katika nchi hiyo ya Ufaransa kwa kuwa swahiba zake wa KGB walikuwa wanamsaka kwa udi na uvumba. Baada ya ugumu mkubwa ulioonekana katika kumpata mtu huyo ilibidi wataalamu hao wa KGB kukutana na kujadili jinsi ya kummaliza mtu huyo hata kama amehifadhiwa vipi.

Likaja wazo la wao kutumia mtu binafsi kwa kazi hiyo, mtu ambaye hatodhaniwa kama ana kazi maalum kwa kuwa wao mara nyingi walikuwa wakijulikana kila wanapojaribu kufanya lolote dhidi ya mtu yeyote.

Walizihitaji siri zilizoibwa, na waliyahitaji maisha ya Touzony ili wengine wasije kufanya hivyo huko mbeleni. Iliwashtua sana kwa kuwa Touzony mwenye asili mbili zinazojenga ile isiyojulikana. Alizaliwa na mama Mrusi na baba Mfaransa akakua na kusoma Urusi, alikadhalika hata kazi alifanya Urusi, alipojiunga na idara hii ya KGB aliaminika sana katika kitengo cha TEHAMA, alikuwa mtaalamu asiyefananishwa na mwingine katika kucheza na kompyuta, siri zote za idara hiyo zilipita mikononi mwake kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa Mtawala katika mfumo huo wa kompyuta. Kulikuwa na siri nzito iliyofichwa kwa miaka mingi sana, miongo mingi sana. Siri ya mambo mazito ya Patriotic War of 1812 au kule Ufaransa wao waliita siri hiyo kwa jina la French Invasion of Russia.

Serikali ya Ufaransa ilifanya mbinu mbalimbali za kuinasa siri hiyo, mwishowe wakapata kumfahamu kijana huyu na kumfanyia hila, akwa mgumu sana lakini wakammezesha utaifa, uzalendo, uasili; akalainika, ikapenyezwa lupia, kijana hakuwa na chaguo, elimu ya ziada aliyopewa na wazee wa mikakati kutoka katika serikali ya Ufaransa, Danford alifanya alichoambiwa kwa umakini wa hali ya juu na kuitoa siri hiyo kwa wanaoitaka. Akagundulika; naye akatoroka, hakupatikana kwa miakaa mingi. Alisakwa na kusakwa, KGB walifanya kazi kubwa kumsaka kila kona sayari hii mpaka miisho ya dunia, hawakumwona wala kusikia tetesi zake. Lakini baada ya kipindi kirefu walipata tetesi kuwa mtu huyo yupo Paris, hapo ndipo ari ya kumtia mkononi iliporudi, walishajua kumpata akiwa hai ni ngumu basi japo afe. Ndipo walipokutana kuliangalia kwa mapana na marefu.

§§§§§

“Nani anaweza kazi hiyo?” waliulizana.

“Hatuna budi kuwa wapole hapa,” mwingine alijibu, “Kwa sababu inatubidi tupitie orodha ya wauaji makini duniani na wengi ni wale ambao hata sisi tunawasaka kwa tukio Fulani au lingine, lakini sasa hatuna budi kufanya nao urafiki kwanza, je watatuamini?” utata ulianzia hapo.

Hayo yote yalijadiliwa wiki mbili kabla ya Bwana Touzony kukutana hapo katika mnara wa Eiffel na marafaiki zake hao.

Iliwashwa kompyuta yenye makabrasha ya siri, jina lililowadondokea wote ni la huyu mwanamke Tracey Tasha aliyeonekana kwenye picha akiwa mrembo aliyevaa bikini na kujilaza juu ya mchanga.

Walipochambua rekodi yake waliona mauaji mbalimbali aliyowahi kuyafanya, ya kitaalamu zaidi, kati ya yote ni asilimia arobaini tu ya mauaji hayo alitumia bunduki lakini yaliyobaki alitumia mikono, sumu, kemikali na siraha ndogo ndogo, ndipo walipoona mauaji ya mwisho aliyoyafanya kule Durban miezi miwili iliyopita, wakamhusudu. Wazo likaja la kumtumia mwanamke huyo, kwa kuwa ni mwanamke basi labda ingekuwa rahisi kumnasa mbaya wao. Majadiliano yakaendelea kwa muda wakakubaliana la kufanya, Tracey atafutwe apewe kazi.

“Usimwambie kama umetumwa na hii idara, we mpe picha mwambie cha kufanya,” sauti nzito ya mkuu wa taasisi hiyo ya kijasusi ya KGB ilimpa maagizo kijana mmoja shababi ambaye ilibidi aonane na Tracey uso kwa uso.

ALKANSAS-U.S.A

Simu ya mezani ikaita katika nyumba iliyojengwa shambani kabisa na kuzungukwa na mahindi mengi yenye urefu wa ajabu. Mwanamke aliyekuwa kitandani na mwanaume wakipeana raha za dunia, aliinuka na kuiacha shuka akatembea kwa madaha kama mlimbwende akiwa uchi kama alivyotoka tumboni mwa mama yake, akaiendea simu na kuinyakuwa akaiweka sikioni.

“Hellow!” aliita kwa sauti ya mahaba kiasi kwamba mtu wa upande wa pili alichelewa kujibu labda kwa ganzi iliyopenya mwilini mwake.

“Yeah, unaongea na Laurent kutoka Ujerumani,” sauti ilisema.

“Biashara au mapenzi?” Tracey aliuliza.

“Biashara,” akajibiwa.

“Wapi?” akauliza

“Paris, Ufaransa,”

“Tuonane baada ya saa tano kutoka sasa, nitakuwa kwenye Metro naelekea Paris unipe maelekezo, usisahau hundi ya Paundi za Kiingereza Milioni tano,” akakata simu.

SAA MBILI BAADAE

Treni ya kutumia umeme ilikuwa ikitoka Ujerumani kuelekea Ufaransa kwa kasi ya ajabu, treni hiyo ambayo wao huiita Metro iliondoka mapema kabisa kutoka Berlin kuelekea Paris, Laurent akiwa ndani yake. Katika meza aliyoketi alikuwa peke yake, kiti cha mbele yake ambacho alitegemea kuketi na Tracey na hivyo aliuhusudu urembo wake, hakikuwa na mtu. Akaitazama saa yake akajaribu kufananisha. Atoke Marekani afike Berlin tuonane kwenye Metro ndani ya masaa matano… alijiwazia huku akiendelea kunywa kinywaji chake taratibu. Akiwa katika mawazo huku akitazama kwenye dirisha akajikuta hayuko peke yake tena, akageuka na kukutana uso kwa uso na mtu asiyemjua, mwanaume mwenye sura ya kitoto. Mtu huyo hakuwa na maongezi marefu.

“Nipe mzigo,” akamwambia Laurenti, akapigwa na butwaa akiwa hajui nini cha kufanya, Huyu ndo Tracey? Akajiuliza. Hakupata jibu.

“Muda unakwenda, nipe mzigo,” yule kijana akakazia kauli yake. Laurent akampa bahasha, yu;le kijana akaifungua na kutoa picha tano tofauti za Bwana Touzony, kisha hundi ya Paundi za Kiingereza Milioni tano.

“Ok, anapatikana wapi?” akauliza.

“Paris Ufaransa,” Laurent akamjibu. Yule kijana akasimama na kuondoka kuelekea behewa la nyuma.

Laurent akaingiwa na wasiwasi, vipi kama huyu si Tracey?, akajiuliza, akainuka kumfuata, akamuona akiishia katika mlango wa behewa la nyuma yake, akamuwahi lakini alipofika kwenye lile behewa, hakuomuona yule mtu, kapotea. Lauretnt akajua kama sio jinni basi shetani, akarudi kitini kwake na kuketi.

Alijaribu kuyatauliza mawazo yake dhidi ya mtu huyo lakini haikuwezekana, alifikiria itakuwaje kama atakuwa kampa mtu mwingine pesa na picha ya mlengwa, ubongo wake ulisawajika kwa mawazo mapya. Aliamua kumsaka mtu huyo kabloa treni ile haijasimama. Alizunguka kiula behewa kuangalia lakini hakumuona hata wa kufanana naye. Laurent hakujua la kufanya aliinua simu yake na kupiga kwenda namba anayoijua yeye, simu ikapokelewa, ilikuwa ni ya mmoja wa watu waliompa kazi na alitakiwa atoe taarifa mara tu akionana na Tracey. Alijuwa kwa vyovyote atapata shida kueleweka kwa uzembe alioufanya. Lakini alishangaa alipoambiwa ‘well done’ na kisha simu kakatwa.

§§§§§

Akiwa ndani ya suti nyeusi iliyobeba umbo lake la kike lililovutia wanaume waliokuwa wakimwangalia wakati akishuka katika gari iliyomleta. Kila mtu alimwangalia mwanamke huyu wa kizungu lakini ngozi yake ilikuwa imepoa kwa rangi, ilikuwa kama aliyekaa juani muda mrefu, miwani nyeusi iliyaficha macho yake ya buluu, macho ya paka, viatu virefu vyeusi vilimbeba na kumfanya atembee kwa mwendo wa madaha. Alizivuta hatua za wastani kuelekea pale kwenye ule mnara mkubwa kabisa na maarufu duniani, mnara wa Eiffel uliopo Champ de Paris, mnara mkongwe uliojenga kati ya miaka ya 1887 na 1889, mnara uliojengwa kwa vyuma tupu, uliosanifiwa kitaalamu na Stephen Suvestre, wenye sakafu tatu na lifti tisa za kukupandisha juu na kukushusha chini.

Tracey, aliingia kwenye moja ya lifti hizo na kunyanyuliwa kuelekea juu kwenye sakafu ya tatu ambako ndiko liliko windo lake, alifika na kutoka ndani ya lifti hiyo. Ulikuwa mgahawa mkubwa uliokusanya watu mbalimbali wenye pesa, wakila na kunywa wanachotaka, pesa zilikuwa zikiteketea na kujaza matumbo yao yasiyoridhika.

Danford Touzony, pamoja na rafiki zake walikuwa wakiendelea kuburuka pasi na hili wala lile, walikunywa wakacheka, waliongea na kufurahi. Mwanadada mmoja mhudumu wa mgahawa huo, alikuja mpaka kwenye meza ya watu hao, meza aliyoketi Danford akamnong’oneza mmoja wa watu waliokuwa na Danford kwa kuwa haikuwa rahisi kumfikia mlengwa, ukimya ukachukua nafasi.

“Kuna simu ya mheshimiwa,” yule mwanadada alimwambia huyo kijana.

“Ok, nakuja kuisikiliza,” akajibu yule mtu.

“Hapana, simu imesisitiza kuongea moja kwa moja na Mr. Danford,” yule mwanadada alijibu. Kauli hiyo ilimfanya yule bwana kufungua macho ya akili yake, jukumu alilopewa ni kuhakikisha usalama wa mtu huyo, mtu aliyeitwa ‘muhimu’ na serikali ya Ufaransa. Danford Touzony alisimama na kuelekea kwenye kile chumba cha simu, na kama kawaida nyuma yake alifuatwa na yule bwana kwa ajili ya ulinzi.

Tracey Tasha, alikuwa katulia katika meza moja iliyojazwa vinywaji akinywa polepole huku jicho lake lililokuwa nyuma ya miwani yake lilikuwa likimwangalia Danford, mkononi mwake alikuwa amekamata kidubwasha kidogo kama rimoti ndogo kabisa ukubwa wa kidole gumba. Alikitumia kidubwasha hicho kutafuta namba ya simu ya moja ya vijichumba vya simu katika mgahawa huo, akapata, kwa kuunganisha na kipini kilichobanwa sawia katika pua yake chenye uwezo wa kunasa sauti na heleni iliyoweza kumfikishia ujumbe, alichanganyikiwa kidogo kuona badala ya mlengwa wake tu kuinuka aliinuka na mtu mwingine.

“Shiit!” aling’aka kwa sauti ya chini, akaibana vyema ile rimoti mkononi mwake kisha akasubiri kidogo. Alimtazama Touzony, aliyeukaribia mlango wa kile chumba na kisha akampa ishara yule bwana aliyekwenda naye, asubiri hapo nje ya mlango wakati yeye anapokea simu hiyo, lakini kabla hajaingia, yule bwana alitangulia kwanza akatazama ndani ya chumba kile, hakuna jipya, akampa ishara bwna Touzony ya kuendelea kuongea na simu yake, akaingia na kuuchukua mkono wa simu uliokuwa umeegeshwa juu ya kijimeza kidogo.

Tracey alimtazama kwa chati kwa mtindo wa kugeuka kiufundi, alikuwa akisubiri ainue mkono wa simu auweke kichwani, ili afanye yake.

Danford Touzony, aliingia ndani ya kile chumba na kuinua ule mkono wa simu, akauweka katika sikio na ile sehemu ya kuongea akaiweka kinywani.

“Oui,” alianza kwa kuitikia kana kwamba kuna kitu alikuwa ameambiwa. Akajisiki kama anapaliwa na kitu, akakohoa kusafisha koo, lakini bado, akakohoa na kukohoa, akaanza kuishiwa nguvu, akaanguka ndani ya chumba kile, akajishika shingoni huku akikohoa kwa nguvu. Mlango nulisukumwa na yule aliyekuwa nje akaingia na kumkuta Danford akigalagala chini, akaomba msaada na wengine wakaja, wakamsaidia kumbeba Danford, haraka haraka akawekwa kwenye machela, hekaheka zilikuwa kubwa, watu wa huduma ya kwanza walifika, na kumsaidia kwa hili na lile. Kwa ujumla hali ilikuwa tete katika mgahawa huo. Danford alipakiwa kwenye helikopta ya red cross na kuondole kutoka hapo kukimbizwa hospitali huku akiendelea na matibabu akiwa angani.

Tracey Tasha, alirudisha rimoti yake katika mfuko wa suruali huku akitikisa kichwa kukubaliana na lililotukia, aliinuka kutoka pale alipoketi na kumalizia kinywaji chake kisha akateremka chini kwa kutumia lifti. Huko nje waandishi wa habari walijaa wakimbana maswali polisi mmoja aliyeonekana kuwa ndiyo msemaji wa polisi hao. Tracey alipita taratibu na kutokea nyuma ya kundi lile, huku akiacha polisi wakipanda kule kwenye ule mgahawa wakiwa na uhakika wa kupata lolote.

Danford Touzony alifikishwa katika hospitali ya Taifa mjini Paris, harakaharaka huku akiwa amewekewa vifaa maalum vya kumsaidia kupumua huku chupa za maji zikifanya kazi yake ya kumuongezea maji mwilini hata kama hayakupungua. Machela iliyombeba ilikuwa ikisukumwa na vijana nane waliokuwa wakikimbia nayo kupita kwenye korido ya hospitali hiyo kuelekea chumba maalumcha uchunguzi. Akiwa juu ya ile machela, Danford Touzony alikuwa amelala kimya, hakuongea lolote, na macho yake akiwa ameyafumba.

Sekunde ishirini zilitosha umfikisha katika chumba kilicholusudiwa, aliteremshwa na kuwekwa kitandani kisha waganga wenye vifaa vya kisasa walimzunguka, kila mmoja akiwa na kazi yake, kila mmoja akichukua kipimo anachokihitaji; mpishano wa humo ndani hakika ulionesha ni jinsi gani hospitali za wenzetu walivyo makini na kazi yao na jinsi walivyojali uhai wa mwanadamu.

Tracy Tasha alisimama katika mlango wa chumba hicho alicholazwa Danford Touzony, hakuna aliyeruhusiwa kuingia, vidirisha viwili vidogo vilivyotengenezwa katika mlango na kuwekwa kioo kinene vilimruhusu Tracy kutazama ndani na kumuona Danford aliyekuwa kimya kitandani akizungukwa na mitambo tiba pamoja na wauguzi wachache ambao walikuwa wametingwa na kutafsiri michoro na tarakimu mbalimbali zionekanazo katoka mitambo tiba hiyo. Alitaka kuhakikisha Danford amekufa kwani sumu mbaya aina ya Cyanide ilikuwa imefanya kazi yake.

Mara ghafla, moja ya mtambo tiba ilianza kutoa majibu ya ajabu kidogo, wale wauguzi walionekana kuchanganyikiwa, walishika hiki wakashika kile, mmoja akabofya kitufe Fulani kilicho karibu na kichwa cha mgonjwa. Tracy aliona madaktari wengine kama wane wakikimbia kwenye korido kuja pale kwenye kile chumba, akawapisha wakaingia na kuanza kushika hapa na pale, mmoja wao alionekana kujisjika kichwani ilhali wengine walichukua vifaa maalum vya kutumia umeme na kujaribu kumwamsha Danford; walijaribu na kujaribu lakini haikuwezekana, kisha wote wakatazamana kwa huzuni, kifaa kimoja baada ya kingine kikaanza kuondolewa mwilini mwa mgonjwa na shuka jeupe likavutwa mpaka, hakukuwa na jambo jipya, Danford Touzony alifariki dunia.

Watu watano wa makamo waliovalia suti nadhifu nyeusi waliingia kwenye kile chumba wakiongozwa na daktari mmojawapo, walimpita Tracy aliyekuwa ameketi kwenye viti vilivyojipanga kando ya ukuta wa korido hiyo pana, alimtambua mmoja wa wale watu, alikuwa ni ofisa katia maofisa wa juu wa idara ya usalama wa Taifa ya Ufaransa. Waliingia ndani ya kile chumba, hawakuwa na la kufanya zaidi ya kuondoa shuka juu ya ule mwili na kuutazama kwa masikitiko huku wote wakiwa wameshika mikono yao kwa mbele. Baada ya dakika kumi hivi walitoka. Pale koridoni, mmoja wao alimuona Tasha akiwa ameketi kakunja nne akisoma gazeti kana kwamba kuna mtu anayemsubiri.

Alipohakikisha watu wale wameondoka kabisa na kile chumba hakina mtu isipokuwa mwili wa marehemu tu, aliinuka taratibu na kwa kutumia funguo yake inayoweza kufungua vitasa asilimia 90 vya milango duniani, alifanikiwa kuingia ndani ya kile chumba, kwanza akasimama mlangoni pembeni kidogo, akatazama kwa umakini kisha akajivuta na kuuendea ule mwili, akakamata kidani alichovaa marehemu akakata na kukitia mfukoni. Mara akasikia watu wakiongea nje ya mlango, akainama na kujificha chini ya kile kitanda, walipokuwa wakifungua mlango, akajivuta na kujificha pembezoni mwa kabati, akaiziba kwa mapazia marefu ya dirisha. Wale watu wakafika na kitanda kingine, wakamtoa marehemu na kumweka kwenye kitanda kingine kisha wakatoka nae nje ya chumba hicho. Dakika moja baadae, Tracy akatoka na kuufunga mlango kisha akatokomea anakokujua yeye.

§§§§

TRACY Tasha, binti Yatima wa miaka ishirini na nane aliondokea kuwa muuaji mwenye uwezo mkubwa wa kuitekeleza kazi yake katyika mazingira yoyote yale na jinsi yoyote ile. Alipata mafunzo yake ya kutumia mikono katika mapambano katika moja ya vyuo mahiri huko U.S.A, kutokana na juhudi zake hizo akapata mkanda mweusi akawa mpiganaji mzuri sana katika chuo chake. Miaka kadhaa mbele alikwenda huko Uchina, akaingia tena kwenye mafunzo ya sanaa ya mapigano na kuendelea kupata tuzo mbalimbali; alipohakikisha kuwa yuko vizuri katika sanaa hiyo hakuishia hapo, kwa ufadhili wa tajiri mmoja wa huko Ontario, Canada, Tracy alipelekwa Japan kujifunza Karate, nako alifanya vizuri sana kabla ya kurudi Marekani na kujifunza matumizi ya silaha za aina aina.

Alikuwa mkimya sana asiyependa kuongea, wazazi wake waliouawa miaka kadhaa nyuma katika tukio la ujambazi lililotokea ndani ya nyumba yao huku yeye mwenyewe akishuhudia, lilimfanya awe sugu wa kutoogopa nkuua. Alitoroka akihofia kuuawa, akajiingiza kwenye makundi ya kihuni ya vijana wasiona adabu, akavuta sigara, akavuta bangi, ndiiko huko akajifunza ukorofi, kupigana na vijana wa kiume, kupora, kuuza dawa za kulevya na mengine mengi.

Siku moja alipokuwa akipeleka mzigo wa dawa za kulevya gram 500 kwa tajiri mmoja wa Canada, aligoma kumkabidi mzigo huo kutokana na tajiri huyo kutaka kuuchukua kwa nguvu bila malipo ndipo Tracey alipokuwa mbogo, yule tajiri akatuma vijana wake wawili wamshughulikie, lakini sivyo alivyotarajia, vijana wake walipata kichapo ambacho hawakutegemea kutoka kwa binti huyo. Yule tajiri akampenda Tracey, akamchukua kama bidhaa ya bei ghali, akampeleka katika vyuo mbalimbali vya mapigano na matumizi ya silaha. Tracey akaondokea kuwa mahili katika taaluma hiyo, taaluma ya uuaji. Alitumwa akaue, akaenda na akaua iwe kwa bunduki au mikono yake, au kwa sumu ya aina yoyote ile, aliijua kazi yake vizuri. Makachero wa FBI walihangaika sana kumsaka muuaji huyo, amabye kila walipofika katika tukio walizikuta nyayo zake tu, kama marehemu hakupigwa risasi ya kichwa, basi alivunjwa shingo, kama sivyo; basi alifyatuliwa pingili za mgongo; kama la, basi alipewa sumu ya Cyadine, walioanisha tu risasi inayotumika, aina ya sumu, aina ya pigo na kadhalika, lakini waliwiwa na utata, kitendawili kama muuaji alikuwa ni mtu mmoja au watu tofauti, uchunguzi unaendelea.

2

Dar es salaam – Tanzania.

MADAM S aliipokea fax iliyoingia punde tu kutoka katika mashine yake iliyopo mezani hapo, ilipomaliza kuandika, aliivuta ile karatasi na kuichana, akaiweka mezani, kabla ya kuisoma akainuka na kuiendea meza ndogo iliyo pembezoni kabisa mwa ofisi hiyo, akawesha birika la umeme na kujitengenezea kahawa, akarudi tena mezani kwake na kikombe mkononi, akaketi na kunywa taratibu. Alikwishahau kama kuna fax iliyoingia muda huo, uzee sasa ulimkabiri. Aliwasha televisheni yake ya ofisini na kuendelea kutazama habari ya kimataifa iliyokuwa ikirushwa na kituo cha Al-Jazeera.

Habari hii ilimvutia sana Madam S, ilikuwa ni juu ya mauaji ya Danford Touzony, mtangazaji aliipamba ikapambika. Lakini bado habari haikuelezwa kinagaubaga juu ya tukio hilo.

Madam S akainua simu yake, akabofya namba Fulani na kuweka sikioni.

“Yeah! Kamanda Amata,” akaita.

“Niambie Madam…” akajibu.

“Washenzi wameshafanikiwa, hebu fungua Aljazeera ujionee,” Madam S alimwambia.

§§§§§

Akiwa juu ya kiti chake cha kuzunguka, ndani ya ofisi ya AGI International, Kamanda Amata alibadilisha stesheni na kuweka ile aliyoambiwa na Madam. Alilakiwa na picha za Danford Touzony, zilizomuonesha enzi za uhai wake. Aliifuatilia kwa makini, na muda kidogo alimwita Gina wakaungana kutazama habari hiyo, ilitokea huko Paris dakika chache zilizopita.

“Lazima muuaji ni mtaalam anayeijua kazi yake,” Amata alimwambia Gina.

“Kwa nini?” Gina akauliza.

“Kwa kuwa Touzony alikuwa anapewa ulinzi mkali sana, haikuwa rahisi kumpata, wamejaribu kila mbinu ya kumuua lakini wameshindwa, ila sasa mbinu waliyoitumia inanitia wazimu,” Kamanda Amata alieleza.

“Kwa nini wasema hivyo, unafikiri atakuwa ameuawa?” Gina alidadisi.

“Bila shaka ameuwa, kwa maelezo ya daktari pale waliposoma taarifa yake ameuawa kwa sumy ya Cynadine iliyowekwa kitaalamu kwenye mkono wa simu, muuaji lazima awe mtaalamu sana,” Kamanda alimweleza Gina.

“Sasa, kama simu iliwekwa sumu si wangekufa wengi Kamanda!” Gina alionesha kutoelewa katika kifo hicho.

“Usijali Gina, utajua tu wanavyofanya, yaani hapa muuaji anakusoma mwenendo wa maisha yako ili ajue wapi atakupata kirahisi, hainiingii akilini kuwa hawajamkamata muuaji au hata kumshuku, lazima alikuwa hapo hapo, tabia ya wauaji kama hawa hupenda kufuatilia kujua kama mtu wao amekufa au la, hivyo huyu kwa vyovyote alikuwa pale pale sema tu kawazidi ujanja kwa namna moja au nyingine,” Kamanda alieleza. Gina alisikiliza kwa makini sana na akatingisha kichwa kuaonesha ameelewa.

Kelele ya simu ya mezani iliwakatisha mazungumzo yao, Gina akainyakuwa na kuiweka sikioni.

“Ufike hapa na Kamanda Amata mara moja,” ilikuwa ni sauti ya Madam S. Gina akarudisha simu mahala pake na kumpa ujumbe Kamanda Amata, mara moja wakanyanyuka na kuteremka chini kutoka katika ghorofa iliyobeba ofisi yao.

Dakika kumi baadae walikuwa katika ofisi ya Madam S, pamoja nao alikuwepo Chiba, Scoba na Dr. Jasmine.

“TSA 1 na wenzako, kuna hii fax hapa imefika, hebu muipitie kwanza kabla hatujaanza mazungumzo,” Madam S akamwambia Kamanda Amata. Akaichukua na kuipitishia macho, ilikuwa ni kurasa moja tu iliyoandikwa kwa mashine.

Ilikuwa ikieleza juu ya tukio la kifo cha Touzony, taarifa hiyo iliyotoka katika shirika la kijasusi la ndani ya Ufaransa ilikuwa ni kuomba msaada wa kupatikana muuaji huyo kutoka katika mashirika mengine makubwa duniani, kwa mara ya kwanza taarifa hizi zilifika katika shirika la kijasusi la Tanzania, TSA. Kulikuwa na picha kama kumi zilizoambatana na taarifa hiyo zikionesha yule anayesadikiwa ni muuaji, picha hizo ziligawanywa makundi matatu, na zilikuwa za watu watatu tofauti, ambao kwa maelezo ya taarifa hiyo ni kwamba watu hao waliingia katika chumba hicho na kutumia simu hiyo kwa tofauti ya dakika ishirini kwa wastani, kati yao mmoja alikuwa mwanamke.

Kamanda Amata alijikohoza na kumpa Chiba ile karatasi pamoja na picha zile. Akamtazama Madam S aliyekuwa bado anaangalia luninga yake iliyokuwa ikipeperusha habari za Mashariki ya kati. Aliposikia kikohozi cha uongo na kweli cha Amata aligeuka.

“Utatuambukiza bwana!” akamtania, “ Enhe sema,” akaongeza.

“Ina maana shirika lao la kipelelezi limeshindwa kumkamata mtu huyo mpaka waombe nje ya nchi haraka hivi?” kauliza.

“Sikia Kamanda, hawa wanaamini kabisa kuwa muuaji kama hayupo kati ya wale watatu basi tayari anaelea angani akitoroka nchi, ndiyo maana wameomba msaada huu,” Madam alitoa jibu.

“Ok, kazi yetu ni nini?” akauliza tena.

“Kuweka ulinzi na kubaini kama mtu huyu au mmoja wa hawa ataonekana hapa nchini tuwape taarifa,” Madam S akamwambia Amata huku akimwangaliza usoni.

“Kwa hiyo tukiwapa taarifa watakuja kumkamata?”

“Ndiyo maana yake,”

“Kama walishindwa kumkata pale pale wataweza huku? Ok, basi mi nafikiri hii kazi iko chini yetu, sio kiwango chetu, watawanyie hiyo taarifa idara ya usalama wa Taifa wa ndani ili waweke mitege yao uwanja wa ndege, bandarini, vituo vya mabasi na sehemu zozote zinazotumika kuingia au kutokea watu nje ya nchi,” Kamanda akajibu na kutroa maelekezo.

“Niliwaza hivyo,” Madam akaunga mkono. Baada ya hapo akatoa maelekezo mafupi kwa vijana wake kisha akafanya lile walilokubaliana.

MWAKA MMOJA BAADAE

KIKAO CHA SIRI

NDANI ya chumba maalumu ambacho hakuna aliyekuwa akikijua zaidi ya watu hawa watatu, kulikuwa na kikao kizito kikiendelea, kikao cha siri kwa mambo ya siri. Walikuwa wakijadiliana swala zito kidogo lililoonesha kuwachanganya akili ghafla. Walikuwa watatu tu walioketi kwa kutazamana lakini ukiwaangalia hawakuwa kutoka sehemu moja, mmoja alionekana mzungu kabisa, mwingine alikuwa mweusi kabisa na wa mwisho alikuwa yupo yupo tu, Mwarabu si Mwarabu, Mchina si Mchina ilimradi alizaliwa na anaishi basi.

Yule Mzungu aliyeonekana kama kuchanganyikiwa, aliwatazama wenzi wake hao wawili waliongia hapo muda si mrefu.

“Tusipoangalia tutaingia mkenge,” aliwaambia wenzake hata bila ya salamu.

“Na mi nilijua tu, nilijua huyu jamaa si wa kumwamini sana, ni ndumilakuwili,” akadakia yule asiye na uraia wa maana.

“Anakiuka, utaratibu, kama mnavyojua tulikubaliana kugawana migodi, Mwadui, Buzwagi na Bulyanhulu ili tumfanikishie yeye mambo yake, sasa tumemuwezesha mabillion ya dola tumetumia, leo hii anataka kuwapa mali watu wengine, huyu ana akili kweli huyu?” yule Mzungu aliyeonekana kama Mwenyekiti wa kikao aliongea kwa hasira na uchungu, mara kwa mara alikuwa akfuta kamasi jembamba lililokuwa likitoka katika tunda za pua yake.

“Haina haja ya kupoteza muda, tuonane nae haraka atueleze kama inawezekana au la, baada ya hapo tutajua la kufanya, sisi sio watoto, tunajua tufanyalo,” alisema yule Mwafrika. Baada ya mazungumzo marefu kati yao waliamua kumtafuta mtu huyo ili wajue nini kinaendelea kati ya mikataba yao.

“Tukutane tena hapa hapa baada ya masaa matatu, najua tayari tutakuwa na jibu kamili, kazi hii nakupa Namba Tatu uonane na ndugu yetu, utuletee mustakabali, ili leo hii tuiache ardhi hii tukiwa na jibu,” yule Mzungu aliyejulikana kama Kinara kutokana na cheo chake katika jopo hilo alimaliza na kufunga kikao. Kila mmoja alipita kwenye mlango wake alioutumia kuingilia, hakuna aliyejua mwenzake kaenda wapi na anafanya nini.

SAA TATU BAADAE

ILIKUWA katika chumba kilekile, kama walivyokubaliana, walikutana tena, sasa wakiwa na shauku ya kusikia habari za huyo waliyemtuma, Namba Tatu (kama wanavyomwita).

“Tuambie!” Kinara alifungua kikao kwa neno hilo.

“Nimeonana naye mwenyewe,” yule aliyetumwa akaeleza.

“Amesemaje, maana muda unazidi kwenda,” akadakia yule asiye na uraia wa maana.

“Nimeongea naye kwa muda wa dakika ishirini na tano, ana kwa ana, anasema ‘yeye kwa kuwa tumemsaidia hana budi kulipa fadhila, na katika kulipa fadhila ana mlolongo wa watu ambao wote wanahitaji malipo hayo tukiwamo sisi, hivyo amepanga mambo haya kwa awamu…”

“Kwa awamu!” alishtuka yule Kinara.

“Ndiyo kwa awamu, na sisi ametuweka kundi la mwisho,” akamalizia kusema.

“Anatuchezea, anatutania, hajui tulilokubaliana au amesahau yale aliyotuahidi tulipukuwa pale East Java? Sina muda wa kusubiri, kilichobaki ni kutekeleza kurasa ya mwisho ya makubaliano yetu, basi,” alimaliza yule Kinara.

“Samahani Kinara, kabla ya kurasa ya mwisho kuna kurasa ya mkakati tuliyoifunga kwa pini za dhahabu,” yule mwenye uraina bubu alidakia pia.

“Oooh Shiit! Nilipitiwa, sasa tutamkumbusha baadae kadiri ya makubaliano na kisha tutaona la kufanya kama ni kutekeleza kurasa ya mwisho au tufungue kurasa za siri,” Kinara akaongeza.

“Ok, nafikiri tutekeleze mkataba, tumkumbushe, lakini kurasa yetu ya mwisho iwe ya mwisho, nikiwa na maana kuwa tufungue kurasa ya siri kisha tumalizie kurasa ya mwisho kwa kuwa hii ya siri ipo katikati ya mkataba wetu,” akamalizia yule Namba Tatu.

Kikao kikafungwa na utekelezaji wa hayo ambao ni wa siri zaidi ukasubiriwa. Walichotakiwa wao kufanya ni kutoa taarifa wasipopajua juu ya kile kinachoendelea.

Wakatawanyika.

MIEZI MIWILI BAADAE

§§§§§

Msafara wa Mkuu wa nchi ulikuwa ukipita kwa kasi katika barabara itokayo Bagamoyo kuja Dar es salaama mjini. Gari zipatazo sita zilizokuwa zikienda kwa kasi ya ajabu zikitanguliwa na pikipiki kubwa ya polisi iliyokuwa ikiendeshwa kwa madaha na kijana aliyekuwa juu yake. Baada ya pikipiki hiyo nyuma yake kulifuata gari ndogo ya polisi aina ya 506 Peugaot iliyokuwa ikiwasha vimulimuli juu yake, baada ya hiyo kulikuwa na Land Rover Defender ambayo juu kulikuwa na polisi wa kikosi cha FFU wakiwa na bunduki zao tayari zikitazama kule wanakoelekea. Nyuma yao ilifuata Land Cruiser moja nyeusi modeli ya V8, iliyokuwa sambamba na gari mbili aina ya BMW nyuma yake kabla ya kumalizia ile ya mwisho ambayo hubeba watu wa Usalama wa taifa. Ndani ya Toyota Land Cruiser alikuwamo Mkuu wa nchi, ametuna katika kiti cha nyuma hapa pembeni yake ameketi mkewe ‘First Lady’. Ilikuwa ni safari ya kutoka shambani kwao kupumzuka na sasa alikuwa akirejea kazini kwa ajili ya kuendelea na shughuli za kulijenga Taifa.

Kila mmoja alikuwa ametulia kwenye gari akifikiri hili na lile, mwendo kasi wa gari hizo ulifanya barabara yote kuachwa wazi na kuruhusu hizo tu kupita kwa mwendo wautakao. Walikuwa wakimaliza kitongoji cha Bunju, wakalielekea daraja kubwa lililojengwa mtoni, hapo ndipo kila mmoja alipopagawa kwa tukio la ghafla. Walinzi wa gari ya nyuma waliishuhudia ile Land Cruiser ya Mkuu wa nchi ikiyumba na kuacha njia, kisha ikagonga mwamba wa daraja. Dereva alikuwa akijitahidi kuiweka tena barabarani lakini ilikuwa ni ngumu. Ilijipiga tena na kunyanyuliwa juu kabla haijajibwaga chini nje ya barabara. Kitendo cha haraka, wale FFU walikwisharuka chini na wale wa usalama wa Taifa walikwishateremka na kukimbilia eneo la tukio, ulinzi mkali ukawekwa ili wananchi wasivamie eneo. Haraka sana makachero waliokuwa katika gari za nyuma walishuka hai hai na kuvunja mlango wa ile V8, wakamto Mkuu wa nchi salama lakini alikuwa akivuja damu nyingi mwilini, mkewe alikuwa amezimia. Dereva wa gari alifia pale pale.

Lilikuwa ni tukio lililovuta hisia za walio wengi, haikuwahi kutokea.

“Mkuu upo salama usijali, sasa hivi tunaelekea Hospitali,” kiongozi wa Usalama wa Taifa mwenye jukumu la mwisho la kumwambia Mkuu ‘Twende’ au ‘Tusiende’ alimwakikishia usalama Mkuu wa nchi.

“Mke wangu yuko wapi?” akauliza.

“Yuko salama Mkuu usijali,” akajibiwa.

Walihaha, walikimbia huku na huku, na muda huohuo helikopta ya serikali ilifika na kutua katikati ya barabara hiyo. Mkuu wa nchi aliondolewa haraka na kuwekwa katika Helkopta hiyo pamoja na mkewe ambaye alikuwa hana fahamu kabisa; wakaondolewa mahala pale.

§§§§§

Idara ya Usalama wa Taifa ilikutana kwa dharula katika ofisi zao za makao makuu huko kandokando ya barabara ya Bagamoyo kujadili hali iliyotokea saa moja iliyopita katika barabara ya Bagamoyo eneo la Bunju Darajani.

“Haiwezekani, gari zote zilikuwa ziekaguliwa ipasavyo, mipira mipya na bora kabisa kutoka General Tyre, iweje mtuambie gari ya Rais inapasuka mpira?” aliuliza afisa mmoja wa Usalama wa Taifa.

“Hii bwana ni hujuma, baada ya ukaguzi wa kina tumegundua smpasuko wa tairi haukuwa wa kawaida ila ni kitu chenye ncha kali kilichosababisha hayo yote,” alijibu mtu aliyepewa kazi ya uchunguzi.

“Ok, Comrade, hebu tuambie nini mlikiona barabarani wakati mnapita eneo hilo?” akauliza yule afisa.

Akiwa na bandeji yake katika mkono wa kulia, akajibu kwa taabu kidogo, “Kwa kweli hata mimi nashangaa, maana Rider alipita bila tabu, na ile gari ya polisi ilipita eneo lilelile pamoja na ile ya F.F.U, lakini gari ya Mheshimiwa ikapata tatizo, tulishuka na kukagua eneo kwa haraka ikiwa ni pamoja na kuangalia katika nyumba za jirani na maduka kama kuna lolote la kutusaidia kupata jibu, hakukuwa na chochote, barabarani hakukuwa hata na chupa au kipande cha chupa,” akaeleza kinagaubaga.

Wakati kikao hicho kikiendelea mara mlango ukafunguliwa na faili moja dogo likaletwa mezani, msichana aliyelileta akamkabidhi yule afisa na kisha yeye kutoka nje. Yule afisa akalitazama na kulifungua ndani lilikuwa na kurasa mbili tu zilizoandikwa kwa mkono, ilionekana mwandishi alikuwa akiandika kwa taabu sana.

…Tumedunguliwa, nikiwa katika mwendo kasi wa kilomita 150 kwa saa mbele yangu upande wa kushoto, umbali wa takribani mita 110 palikuwa na mtu mmoja aliyejipenyeza kandoni mwa penyo za ukuta ghafla na kuinua kituka bunduki, sikuweza kujua haraka aina hiyo ya silaha, kabla sijafanya lolote nilihisi gari ikinivuta kushoto, tairi ilikuwa imechanika na yule mtu akatoweka.

Nilijaribu kadiri ya uwezo wangu kumuokoa Mheshimiwa kwa adha ile kwa kuigongesha gari kwenye mwamba wa daraja ili kuizuia isilete madhara zaidi, nikafanikiwa (…)

Haikuwa ajali ya kawaida, tumedunguliwa, hakika ni hujuma…

Zaidi ya hapo kulikuwa na maelezo kadhaa ya liyoijaza taarifa hiyo ya dereva wa gari ya Rais. Kila mtu alibaki mdomo wazi, hakuna aliyeamini kinachosomwa hapo.

“Mtu kabisa kudungua gari ya Rais, anajitaka au la?” mmoja aling’aka huku akisimama.

“Lazima apatikane,” mwingine alidakia.

“Sasa hivi naomba kikosi cha watu wane kitumwe eno lile kufanya uchunguzi wa siri, wengine waende hospitali kumhoji zaidi dereva ili atumbie zaidi, maana hapa kaandika kwa shida, wengine hakikisheni chumba alicholazwa Rais na Mkewe kinakuwa na usalama wa hali ya juu. Nitahitaji taarifa zote kila baada ya saa moja kwa redio zetu za siri,” yule afisa akafunga kikao na wajumbe wakatawanyika kila mmoja akiwa na jukumu la kufanya siku hiyo.

§§§§§

BUNJU Darajani, eneo lenye wakazi wengi na shughuli mbalimbali za kujitafutia maisha, maduka, magenge, mabaa, vilabu vya pombe za kienyeji vyote hapo palikuwa ni mahali pake. Siku hiyo ya tukio kila mmoja alikuwa kachanganyikiwa kwa namna yake, hawakuwahi kuona tukio kama lile katika maisha yao, hata kulisikia tu katika historia ya Taifa lao lililojawa na wingi wa amani, likisifiwa kwa weredi wa hali ya juu wa usalama na upelelezi. Baada ya hali kuwa shwari kabisa; kila kitu kuondolewa mahala pale ikiwamo gari iliyombeba Rais, watu walirudi katika shughuli zao lakini mazungumzo katika vikundi yaliendelea kubaki, vilabuni na hata katika magenge ya bangi.

“Ile mi niliiona tangu inavyoanza kutokea, lakini yule dereva mi namsifu aisee, unajua angekuwa kama madereva wetu hawa, sasa hivi tunashusha bendera nusu mlingoti. Lakini jamaa alicheza nayo mpaka ikagonga ukuta wa daraja, lo,” kijana mmoja alisikika akipiga soga na wenzake wakimsikiliza kwa makini sana, huku wakionekana kushabikia yale anayowasimulia.

“Yaani ilikuwa kama muvi, kaka zile gari zinakimbia ni balaa, dakika moja tu hapa walitanda njagu wa kutosha, wote hatukusogea pale tulikodoa macho kwa mbali tu,” mwingine alieleza.

Wakati mazungumzo hayo marefu yakiendelea, kijana mmoja aliyekuwa kwenye kazi maalum alikuwa ameketi jirani na eneo hilo lakini aliweza kusikia yote kwa umakini kabisa huku akiyameza kuyakumbuka baadae, alivaa ki-kawaida kabisa, jezi ya Taifa Stars na suruali ya jeans, hakuna ambaye angemzania kuwa ni mtu mwenye jukumu zito hapo alipo, waliendelea kuleta stori.

Upande mwingine wa eneo hilo kulikuwa na wazee waliokuwa wameketi wakinywa kahawa na wengine wakicheza bao, mchezo uliopendwa na Mwl. Nyerere, huku wakitaniana na kuongea na hili na lile. Wakiwa katika hali ile, alipita mzee mwingine wa makamo aliyevalia kanzu ya kawaida kabisa na baraghashia kichwani alisimama mahala pale na kuomba acheze kidogo bao kwa kuwa naye aliupenda mchezo huo. Watanzania hawana hiana siku zote, walimpa nafasi naye akawapa kikombe cha kahawa kila mmoja akafurahi, maisha yakaendelea. Mazungumzo ya wazee yakaendelea na kubwa lilikuwa lile lile la ajali ya msafara wa Rais, yule mzee mgeni alikuwa akiskiliza na kuwapa maneno ya hamasa ili waongee zaidi.

“Ile ajali bwana, hivi wewe kwa jinsi nchi hii ilivyokuwa na wana usalama wenye weredi wa juu kabisa unafikiri mtu anaweza kuhujumu msafara ule! Hata siku moja, kabla hawajapita hapa panakaguliwa pote, mnavyokaa kuwakodolea macho wengine mko nao hapo ni Usalama wa Taifa,” mzee mmoja alikuwa akiongea kwa sauti ya juu huku akiendelea kucheza bao.

“Wewe mzee umesema, hii nchi kwa upelelezi hata F.B.I wanaiogopa, we ni wewe!” mzee mwingine akadakia.

“Lakini watu nao wajanja siku hizi wameendelea, unaweza kukuta mtu kaja hapahapa ili kuhujumu msafara, siku hizi kuna Boko Haram, Al-Qaeda, I.S sijui na nani hawa wa Somalia… eee Al- Shabab,” aliongeza kusema yule mzee mgeni akiwa na haja ya kuwachokonoa wabwabwaje zaidi.

“Yaani mzee mwenzangu umesema, na hawa wageni wageni wanaokuja kujifana Watalii sijui vidudu gani wengine wana mambo yao hawa, sasa we mzee Shomari yule mgeni aliyekuja juzi hapa yule mwanamke akapanga chumba pale Kibilisa Gesti hausi, hivi kweli we mzungu unaweza kupanga pale chumba, Gesti chafu, inanuka maana ni uzinzi kila kukicha,” akadakia mzee mwingine.

Kwa habari hiyo yule mzee akatega masikio akijifanya yuko bize na bao kumbe alishtuka kidogo, kisha akadakia kusema, “Sasa we unashangaa yeye kukaa gesti kama hiyo wale hata juu ya miti wanakaa, wenzetu sio kama sisi wanajichanganya popote,” alisema.

“Wenzetu sio kama sisi mzee mwenzangu, yule mdada sijui mzungu zlivyo pale au chotara, amekaa siku tatu hapa, yuko pale gesti ya Kibilisa,” mazungumzo yakapamba moto.

Baada ya muda huyu mzee mgeni akaaga akaahidi kurudi kesho yake kwani kapenda kile kijiwe, akawanunulia kahawa.

KIBILISA GESTI HAUSI

VIJANA wawili wa idara ya usalama walifika eneo la nyumba hiyo ya wageni majira ya saa nne usiku baada ya kuipeleleza na kuhakikisha hakuna mtu aliyetoka wala kuingia mwenye muonekano tofauti na Watanzania. Walipojiridhisha ndipo wakaijongelea gesti hiyo na kuingia mapokezi, walimkuta mwanadada mmoja aliyekuwa akifumua nywele kwa chanuo la mti.

“Habari dada!” wakamsabahi.

“Salama, niwasaidie nini? Kama vyumba vimejaa,” akawajibu huku akiendelea na kazi yake.

“Tunaomba kitabu chako cha wageni,” mmoja wao akamwambia.

“Cha nini? Kwani ninyi ni nani?” akauliza huku akisimama kutoka pale alipoketi kwenye kochi kuukuu. Wakamwonesha vitambulisho vya idara ya Uhamiaji. Bila kusita alitoa kile kitabu kwa maana alishazoea kutembelewa na watu hao mara kwa mara kukagua wahamiaji haramu lakini kilichomshangaza leo ni kuwa sura zilizokuja zilikuwa ni ngeni tupu. Wakachukua daftari na kuanza kulikagua, kila chumba kilichokuwa na shaka kikatiliwa alama.

“Mgeni wa chumba namba 23 yupo?” wakauliza.

“Hapana ametoka tangu asubuhi hajarudi mpaka sasa,” akajibu.

“Ni Mtanzania?” wakauliza.

“Hapana, kwa maana hajui hata Kiswahili vizuri zaidi ya kile cha kuombea maji,” akajibu yule mfanyakazi.

“Kwa nini hapa hukujaza namba ya passport yake?” wakatupa swali linguine.

Yule dada akabaki amebung’aa macho, hakuwahi kufikiri swali kama lile lingemjia.

“Tueleze kwa kina, alikuwa peke yake? Anajishughulisha na nini?”

“Yukon peke yake, ni mwanamke msichana tu, mwanafunzi wa chuo huko kwao Jamaica kwa jinsi alivyoniambia, kila siku alitoka na kurudi usiku, ila leo bado hajarudi,” yule dada akaeleza. Mara hiyo kengele za hatari zikalia kwa makachero wale.

“Tunaomba kukagua chumba chake,” wakasema. Hatua zikachukuliwa, mjumbe akafika na mlango wa chumba hicho ukafunguliwa kwa funguo ya akiba, wakaingia ndani ya chumba hicho, wakabaki wametumbua macho, hakukuwa na kitu wala mtu, walipekua hapa na pale mpaka juu ya dari lakini hakuna kilichoonekana, wakakifunga chumba hicho na kuongeza kufuli nyingine ili kisiguswe na mtu kisha wakamchukua yule mfanyakazi kwa mahojiano zaidi wakaondoka naye.

Mtaalamu wa kuchora picha aliketi mbele ya yule dada katika kituo cha polisi cha Tegeta, akijaribu kueleza jinsi alivyokua akimuona yule mgeni katika sura tofauti, mara akivaa kofia, mara akitoka na kilemba na kadhalika. Mtaalamu yule wa uchoraji, aliendelea kuchora picha na baada ya maelezo hayo, alizinakshi kwa muonekano mzuri, akapata picha zipatazo kumi na tano tofauti tofauti, akamwonesha yule mfanyakazi wa gesti, hakika, alishtuka sana.

“Ni yeye, yaani kama umempiga picha vile,” akasema. Zile picha zikawekwa katika bahasha na kukabidhiwa afisa wa Usalama wa Taifa kwa muendelezo wa msako dhidi ya mtu huyo.

Picha za mtu huyo zilisambazwa kila kona ambayo ina uwezekano wa kupita kutoka nje ya nchi; Viwanja vya ndege vyote nchini, Bandari, Vituo vikuu vya mabasi, Vituo vya reli. Zaidi ya hapo mahoteli makubwa ya Dar es salaam nayo yalikuwa kwenye taabu siku hizo, kukaguliwa na kupekuliwa kila dakika, kila nanyeingia na kutoka alitathminiwa kikamilifu. Picha zilisambaa na siku chache baadae zilitoka magazetini. Kila mmoja aliziona, kila mwananchi alizitia machoni

Q

§§§§§

MADAM S alishusha gazeti alilokuwa akisoma, ‘Mfanyakazi’ akaliweka mezani kabla ya kushusha pumzi ndefu. Juu ya gazeti hilo kulipambwa na picha ya huyo anayetafutwa ikiongozwa na maneno ‘ANATAFUTWA’ na maelezo mafupi yaliyoeleza hasa juu ya wajihi wake yalifuatia.

Watampata tu waongeze juhudi, alijiwazia huku akiendelea kutazama televisheni yake ya ofisini. Mara ghafla mlango ukafunguliwa, Kamanda Amata akaingia katika ofisi hiyo bila hodi, akaketi katika kiti akitazamana na Madam S.

“Vipi, mbona unakuja kwa shari?” Madam akamtupia swali.

“Hapana, ila kuna kitu kimenifurahisha leo,” akajibu.

“Kitu gani?” Madam akapenda kujua.

“Mdunguaji, anayefikiriwa, ninayo picha ya mchoro wa jana, na nikiitazama inafanana sana na ile tuliyoletewa miezi ya nyuma kutoka Ufaransa” akajibu.

“Come on Kamanda, sikuwahi kufikiri hilo, hebu lete hapa,” akasema huku akionesha ishara ya mkono kuwa apewe picha zile.

Madam S akazitazama zilizochorwa Tanzania na zile zilizopigwa kwa CCTV kule Ufaransa, kweli alikuwa ni yuleyule jinsi alivyoonekana kwa umbo na sura yake.

“Kamanda, unataka kunambia yupo hapa?” madama akauliza kwa shauku japo alinong’ona.

“Sijui, labda ni pacha wake,” akajibu huku akijiweka sawa kitini mwake. Madam S, akamtazama kijana huyu shababi, kisha akatikisa kichwa.

“Hivi unajua idara nzima ya Usalama wa Taifa itapanguliwa punde tu!” akamwambia Kamanda ambaye kwa hilo alikuwa hajui lolote.

“Uzembe?” Kamanda akajibu.

“Sikia Kamanda, sio uzembe, bali tulizidiwa kete, unajua hii hali ya kujiamini kuwa nchi yetu ina amani inatubwetesha sana,” Madam S alieleza kwa kukata tama, “kuna wageni wengi sana nchi hii, hata hawajulikani kazi zao, wengine wanajifanya Watalii, Wengine sijui misaada ya kibinadamu, wanaitana tu wanajazana, ndivyo tunavyokaribisha Magaidi na wauaji wa Kimataifa kama hawa Kamanda, lazima vyombo vyetu vya usalama vibadilike sasa, hali ya kuaminiana imekwisha, huu ulimwengu mwingine huu, watu wako kazini, shauri yenu,” akavua miwani yake na kuiweka mezani.

“Madam, usemayo ni kweli kabisa, tunafanya mambo kwa mazoea lakini madhara yake ndiyo haya sasa, tusemeje, alitaka kumuua Rais akasindwa akapasua mpira wa gari?” Kamanda akauliza.

“Hapana,” akajibu Madam

“Kwa hiyo alidhamiri kufanya hivyo, hakukusudia kuua, unajua maana yake ni nini? Tunaamshwa usingizini Madam,” Kamanda akaongeza huku mara hii akiwa kaiegemea meza ya Madam S, baada ya nukta chache za kutazamana, akaendelea, “Wao ndio walioshindwa, lakini maadam kafanya haya ndani ya ardhi ya Tanganyika nakuapia, atapatikana tu awe hai au mfu,” Amata alijibu kwa kujigamba.

Msako ulifanyika kila kona ya mkoa wa Dar es salaam, lakini ilikuwa ngumu kupatikana mtu anayefanana na picha ile. Siku tano zilipita hakuna jibu la matumaini zaidi ya kukamatwa tu wanawake wanaofanana kidogo na huyo lakini walipowahoji wwliwaacha tu baada ya kugundua hata kushika manati hawawezi.

Ilipokamilika wiki moja baadae, idara ya Usalama wa Taifa ikapanguliwa na kufumwa upya, wengine wakiwajibishwa kwa kutokuwa makini na kazi yao, Rais alibadilisha walinzi wake wa karibu na kuteua wengine, hapa na pale paligeuzwa hivi na vile ilimradi tu kujaribu kuweka mambo sawa. Wale waliokuwa Ikulu walibadilishwa na kupewa idara nyingine ikiwemo kuwapeleka mikoani na wapya kabisa walipewa kazi ya ulinzi wa karibu wa Rais.

§§§§§

ULIKUWA mwezi umepita tangu msafara wa Rais ulipokoswakoswa, siku hii Mkuu huyu wan chi alikuwa ofisini kwake kama ilivyo kawaida, ilikuwa ni Jumatatu na maana ya neno Jumatatu ni ‘bize’.

Mlango wa ofisi yake uligongwa mara mbili haraka haraka na kisha mara moja, akamruhusu mtu aliyekuwa akiingia.

“Karibu sana,” alimkaribisha bwana huyo aliyevalia suti nadhifu kabisa, alikuwa mkuu wa Usalama ambaye ni yeye tu aliweza kumruhusu Rais kufanya jambo Fulani kila anaporidhishwa na hali ya usalama wa eneo husika.

“Wageni wako tayari wanakusubiri, waweza kwenda,” akazungumza. Mheshimiwa akanyanyuka na kutoka nje ya chumba cha ofisi na kuelekea ukumbi wa wageni. Alipofika walisalimiana na kuketi kwa mazungumzo mafupi, ulikuwa ni mkutano wa dakika ishirini tu lakini uliojitosheleza. Hazikuwa sura ngeni kwake, alizijua kwa maana alikutana nazo huku na kule duniani wakati akiwa Waziri wa wizara nyeti ilikuwa ikijenga mahusiano na nchi nyingine. Mazungumzo yalikuwa mafupi sana kisha wakamkabidhi bahasha ndogo nyeupe. Ulikuwa ni ujumbe uliotumwa kwake na mtu ambaye hakuweza kufika katika kikao hicho. Akaichana ile bahasha na kuisoma…

…Umetugeuka?

Kwa nini unashindwa kutekeleza upande wa pili wa makubaliano yetu? Sisi tumetekeleza yetu lakini wewe unashindwa kutekeleza yako.

Tunajua kuwa huwezi kuamua peke yako lakini kumbuka nguvu na amri ya dola unayo wewe, ukisema iwe na itakuwa tu.

Sina maneno mengi ila kumbuka kabrasha la makubaliano yetu lina kurasa thelathini na tano tu na sasa nenda ukasome uone tupo kurasa ya ngapi na nini kinafuata baada ya hapa.

Hatufanyi utani katika hili tupo makini …

Ilimaliza barua ile iliyoandikwa kwa wino wa dhahabu. Alikunja sura, akaikunjua akabasilisha mkao, kijoto kilichochanganyika na kiubaridi kwa mbali kilimpitia kutoka utosini mpaka unyayoni. Baada ya hapo walipeana mikono wakaagana. Wale wageni wakondoka zao na kuliacha jengo la Ikulu. Mkuu wan chi au tumwite Rais aliikunja ile bahasha na kuitia mfukoni mwake, hakumpa yule mtu anayemshikia makabrasha yake, la hii aliiweka mwenyewe. Akarudi ofisini lakini dakika chache alihitaji kupumzika kwani kichwa chake kili-stuck kabisa.

MIAKA MITATU NYUMA

WASHINGTON DC

“Sisi tutamiza ombi lako, kukufanya wewe ukae madarakani ndio kazi yetu, ukitazama kila kona ya Afrika tumeweka watu, jukumu letu ni kuwawezesha ninyi wenye sisa za mlengo wa pekee madarakani lakini baada ya utawala wako miaka miwili na nusu huna budi sasa kutuwezesha na sisi kadiri ya makubaliano yetu yaliyomo humu, je unakubali? Kama unakubali basi we saini, maana kwa kusaini tu tayari umekuwa Rais na ukikiuka…” akafungua kurasa ya tano kutoka mwisho iliyoandikwa ‘JIUE MWENYEWE’

Mheshimiwa huyu alishusha pumzi na kusoma tena na tena kurasa hizo thelethini na tano zilizoandikwa kwa wino wa dhahabu, yalikuwa ni makubalino mepesi sana kutekeleza, hata ungekuwa wewe ni mepesi tu, hayakuhitaji damu ya mtu wala kiungo chake bali yalihitaji wewe kufanya watakalo wao.

“Na nikishindwa je?” akauliza yule Mheshimiwa.

“Huwezi kushindwa, sisi ndio tunaweka watu madarakani, uchaguzi wa Rais mwaka kesho ambao wewe unataka kugombea utaigharimu dola ngapi serikali yenu masikini ya Tanzania?” akaulizwa naye akajibu kwa ufasaha kabisa.

“Ok, sisi tutawafadhili pesa za kampeni na mambo yote, alkadhalika tutawatengenezea karatasi maalum, peni za kupigia kura na masanduku ya kupigia kura ambayo tunatumia teknolojia mpya inayoendana na karatasi hizo, karatsi ukiziona ni za kawaida kabisa, lakini tunavyowapa kama ni karatasi milioni thelethini basi ujue kura zako za NDIYO ni milioni ishirini na moja bila kuharibika,” akaambiwa, akafarijika.

“Hapo nimekuelewa Comrade,” akajibu Mheshimiwa.

“Basi ni hayo tu, lakini kumbuka, utatawala miaka miwili na nusu kwa manufaa yako na serikali yako, miaka miwili nanusu inayobaki ni kwa manufaa yetu, tutakuja kwa njia nzuri tu kama tulivyokwambia, uwekezaji,” yule Bwana akamweleza Mheshimiwa.

Kila Mheshimiwa alipojaribu kumtazama yule bwana aliyempachika jina la Comrade alishindwa kumuona sawasawa kwani kwa jinsi alivyoketi hakuonekana sawasawa sura yake, hivyo mpaka anamaliza kuongea naye hakumjua ni nani.

§§§§§

Kama alivyoahidiwa, aliukwaa uongozi wa Nchi bila tabu kwa asilimia za kutosha, kura zilihesabiwa mara kadhaa kwa kushuku kuwa wamefanya utapeli lakini jibu lilikuwa ni lilelile. Ilikuwa miaka miwili na nusu ya neema kama ndoto aliyoiota Yusuph, alijitahidi kutimiza ahadi zake kwa wananchi kwa nguvu kubwa. Hakuna aliyegusa wala kumwuliza juu ya kubaliano lile, wafadhili wake walikuwa wakiangalia kutoka mbali kila linaloendela. Waliendelea kusubiri tu wakati wao ufike, nao waneemeke kwa kuitwaa migodi ya madini inayotoa madini kwa fujo bila kuchoka, walijuwa wazi kuwa ndani ya miaka miwili na nusu waliyokubaliana wangeweza kupata faida maradufu ya pesa waliyofadhili kwa Kiongozi huyo.

Ulikuwa ni mkataba wa kitoto, kuwapati mgodi au migodi kwa majina tofauti na kila mgodi serikali itapata 10% na wao watabeba zilizobaki. Mkataba wa kitoto, utakaowaumiza Wananchi, wao walicheka sana wakijikuna matumbo yao.

Walijijenga, walikuwa na nguvu ya ushawishi, waliweza kufanya lolote bkatika dunia hii, walikuwa na uwezo wa kuleta migogoro isiyokwisha ninyi mkipigana wao wakibeba madini na rasilimali zenu kwa kuwapa bunduki na makombora ya kisasa ili muendelee kuuana, wakiwapa condom na dawa za majira ili msiendelee kuzaana, wakiwapa chanjo mbalimbali ambazo ni wao tu wanaojua kazi yake katika miili yenu, leo hii tunashuhudia dada zetu kati ya kumi wawili watazaa salama na wengine mimba zitaaribika au kunusurika kwa msaada wa madaktari wenye utu ambao ni wachache sana hasa kwa wewe usie na ‘njuruku’. Ukitazama kila kinachokuja kutoka ughaibuni kwetu ni ufahari kukinunua, kuwa nacho, lakini wenzetu ndio wanaojua nini walichokiweka ndani yake, wametusahaulisha kila kitu, tukiuza ng’ombe wetu mamia kwa mamia, tukifanya kazi kuchwa kutwa na kupata mshahara tunakimbilia dukani kununua simu kubwa na kurudi kwetu tukipiga miayo.

3

Miezi mitatu baadae

MGODI WA ALMASI MWADUI

NDEGE ya serikali aina ya Foker Friendship ilitua katika kiwanja kidogo cha ndege katika Mgodi huo mkoani Shinyanga. Walioshuka hawakuwa wageni sura zao, alikuwa ni Waziri wa madini na nishati, alishuka akifuatana na watu wengine kama wanne hivi, wakaliendea geti kuu la mgodi huo. Hakuna aliyewazuia, walifunguliwa lango na kuingia ndani yake, moja kwa moja wakasindikizwa kwa ulinzi mkali wa mbwa mpaka ndani ya jengo lenye ofisi za utawala, wakapokelewa na mwanadada mrembo, Makivango, aliyekuwa katibu muhtasi wa ofisi hiyo.

Akawakaribisha kwa heshima zote na kuwaruhusu kuonana na meneja wa Mgodi huo, wakapita ndani wakamkuta.

Dr. Justine McLean, alitulia akivuta mtemba wake, akawakaribisha na kuwapa sehemu za kuketi. Aalikuwa akiusubiri ugeni huo tangu asubuhi ya siku hiyo hivyo hakutoka kabisa ofisini kwake.

“Kama unavyotuona, hatuna muda wa kupoteza, tumekuja kama taarifa zilivyo lakini kuna mabadiliko kidogo, ni dharula na ni lazima itekelezwe, tunahitaji almasi makasha yasiyopungua matano sasa hivi, ni amri ya serikali,” yule Waziri akamwambia Dr. McLean. Mshtuko dhahir ukaonekana katika uso wa Meneja huyo. Yeye alitegemea ugeni wa kuja kutembelea Mgodi sasa anakutana na habari nyingine.

“Kuna utaratibu Mheshimiwa wa kufuata hata kama Mgodi ni wa serikali,” akajibu.

“Na mimi ndio Waziri mwenye dhamana, na nina kibali cha Ikulu,” akasema huku akitoa karatasi zake na kumpatia. Ilikuwa barua kutoka Ikulu iliyosainiwa na Rais mwenyewe na kugongwa mhuri wa wa Ikulu. Dr. McLean akarudisha karatasi ile kwa Waziri huyo.

“Hapana, hii baki nayo wewe kwa faili lako kama utaletewa shida yoyote,” yule Waziri akamkabidhi naye akaipokea na kumwita Makivango.

”Makivango, nenda kwa mkuu wa bohari mwambie atoe kasha tano kubwa za almasi ampatie mheshimiwa Waziri, serikali inazihitaji kwa shughuli za haraka,” Makivango hakuwa na lingine alitoka na kuiendea ofisi kama ya tatu hivi, akatoa maagizo aliyopewa na michakato ikafanyika. Wakiwa ofisini walipewa vinywaji huku mazungumzo ya kikazi yakiendelea. Wale waliofuatana na Waziri ambao waliipendezwa kwa mavazi ya kipolisi walikuwa wakisimamia zoezi la kupakia katika ile ndege.

Baada ya kama dakika kumi tu, Makivango alirudi na kumpa taarifa kuwa zoezi limekamilika kisha yeye akatoka na kuacha wakiagana wakuu hao.

Wakati wafanyakazi na walinzi wa mgodi huo walikuwa nje wakiitazama ndege ile ikipotelea mawinguni, Makivango alikuwa hana hili wala lile, aliendelea kuchapa kazi.

Zilipita dakika thelethini Makivango akiendelea na kazi zake, alipoitazama saa yake ilikuwa saa saba za mchana akagundua kuwa amechelewa kupeleka kahawa kwa boss wake ambaye kila saa saba kamili lazima anywe kahawa. Harakaharaka akandaa katika birika la umeme, alipokamilisha na kuweka katika chano vikombe viwili vya kahawa kwa boss wake Muingereza na mgeni wake, akauendea mlango wa Dr. McLean, akaususukuma kwa mgongo na kugeuka na chano yake kuingia ndani, akasimama ghafla, ile chano ikamtoka mikononi mwake na kuanguka chini, vikombe vikatawanyika, hakuamini anachotazama mbele yake.

Dr. McLean alikuwa amelalia meza na damu nyeusi ikimtoka na kusambaa mezani, mgeni wake hakuwepo ofisini. Makivango alipiga kelele za msaada hakuna aliyesikia ndipo alipokumbuka nobu ya hatari iliyopo chini ya meza yake, akaikimbilia huku mwili wake ukiwa umejaa hofu, akaibonyeza na dakika hizohizo walinzi waliingia kwa fujo na kumkuta Makivango akiwaonesha ishara ya mkono kuwa waelekee ofisini kwa Dr. McLean. Wote wakapigwa na bumb uwazi, walishangaa kumkuta meneja wao katika hali hiyo.

Ilikuwa ni hali ya kuogofya sana, Makivaango hakuweza kuielezea alibaki kimya muda wote. Nusu saa baadae polisi walifika na kufanya utaratibu wao ikiwamo na kuchukua maelezo kwa watu wawili watatu kuchukua alama za vidole kila ilipobidi na kuchukua picha za mwili wa marehemu kisha kuuondoa mwili wake.

“Mnafikiri nani atakuwa kafanya hivi?” wakauliza, lakini wafanyakazi wakabaki kutazamana, “Mbona mnanitazama, haya nahitaji wafanyakazi wote hapa, haraka,” yule polisi mwenye cheo cha Inspekta akatoa amri na baada ya dakika tano wafanyakazi wote wakafika, lakini walipotazamana mmoja hakuwepo.

“Hapa Boharia hayupo,” akasema Fomeni wa mgodi.

“Yuko wapi? Na kwa nini hayupo? Naanza kumtilia mashaka, kamwangalieni ofisini mwake, mumlete hapa haraka, tunataka tufanye kazi,” akatoa amri. Lakini mtu aliyetumwa alirudi na jibu tata. Boharia naye alikutwa amekufa. Utata.

MADAM S alibaki kinywa wazi, hakuelewa mambo yuanavyoenda, likitoka hili linakuja lile na yote yamejawa utata, aliitua simu taratibu kutoka katika sikio lake na kuipachika katika kikalio chake kwa jinsi hiyohiyo. Akaurejesha mkono wake mezani lakini hakugundua kuwa hata ukope wa jicho lake haukuwa ukifumba, hakutabasamu wala hakukasirika alibaki yupoyupo tu.

Simu ilitoka Ikulu, ikimpa taarifa juu ya tukio la Mwadui.

“Haiwezekani, Waziri!

Waziri kabisa anaweza kufanya hivyo?” alijiuliza kwa sauti ya chini ambayo mtu wa pili hakuweza kusikia. Akainuka na kuiacha meza yake, kisha akakiendea kioo kikubwa kilicho pembeni ya ofisi yake, akajitazama na kujiona jinsi umri unavyomuacha, yanipasa kupumzika na kazi hizi zinazonipa msongo wa mawazo kilan kukicha, alijiwazia. Akairudia meza yake, akainua simu na kubonyeza tarakimu kadhaa, akaitega sikioni.

“Uje sasa hivi, acha lolote unalofanya,” akakata simu mara tu alipomaliza kusema hilo. Akajibwaga kitini na kupitisha mkono wake kwenye mvi za kichwa chake zinazoongezeka kila kukicha.

Mlango ulifunguliwa kwa pupa na kijana aliyemtarajia aliingia, Amata Ric au Kamanda Amata alisimama akimtazama mama huyu aliyeonekana kuchanganyikiwa kiasi Fulani.

“Madam!” akaita.

Madam badala ya kujib u akamuonesha ishara ya kuketi kitini, naye akafanya hivyo.

“Kuna mambo yanayotokea kila kukicha katika serikali yetu, mi yananipa mashaka, kuanzi lile la msafara wa Rais miezi mitatu iliyopita kuna vitu sijui tuite vituko au tuiteje, vinanitia wasiwasi Kamanda,” Madam alieleza huku akionekana wazi kuchoshwa na kazi.

“Ndio Madam, lipi tena limetokea hata unite kwa haraka na ghafla namna hii?” kamanda akauliza.

“Kamanda!” akaita huku akisimama wima na kumatazama kijana huyo usoni. Kamanda Amata akajua wazi kuwa sasa kuna jambo lisilo la kawaida, maana alikwishazoea Madam S akikwambia jambo huku amesimama mkitazamana basi ujue hilo jambo ni siriasi kuliko maelezo na ulifanyie kazi kwa nguvu zote, lazima ujue kuwa anakutuma, hivyo Kamanda akatulia kwa heshima ya kikazi kumsikiliza bosi wake.

“Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, wiki hii yupo katika ziara ya kutembelea migodi yote inayoendeshwa na serikali, lakini jambo la kushangaza na kusikitisha limetokea, amefika katika mgodi wa almasi pale Mwadui dakika sabini na tano zilizopita na kuchukua makasha matano ya almasi na kuondoka nayo akisema kuwa katumwa kutoka Ikulu na ameonesha barua ya Ikulu iliyosainiwa na Rais na kugongwa mhuri wa Ikulu, Kamanda Amata naoma sasa hivi tunavyoongea uanze uchunguzi wa kina wa kadhia hii na unipe majibu kila baada ya dakika sitini za uchunguzi wako. Sawa?”

“Yes, Sir” kamanda akajibu kwa utani kama kawaida akikutana na Madam S.

“Ukihitajiu msaada wowote unajua la kufanya, haya ondoa mkia wako hapa!”

Kamanda Amata akatoka na kuchukua gari yake, kwanza alionelea ni lazima afike nyumbani kwake, Kinondoni ilikuchukua zana zake za kazi zitakazomfaa kwa siku hiyo. Kichwani mwake aliona wazi kuwa pa kuanzi auchunguzi wa tukio hilo ni Mwadui palepale. Aliinua simu yake na kumpigia Gina aliyemwacha ofisini kwake akiendelea na majukumu mengine ya uongo na kweli.

“Naomba nitafutie chata ya kukodi, nina safari ya haraka kuelekea Mwadui mchana huu,” alipomaliza tu akakata simu, hakuwa na muda wa kuendelea kuzungumza. Aliingia ndani na kuufunga mlango nyuma yake.

Moja kwa moja akaelekea chumbani kwake, hakukuwa na jipya akajiandaa na kujitoma maliwato, akajiswafi na kurejea tena chumbani, akachagua silaha za kumfaa, akazipachika katika mkoba wake maalumu ambayo hata ukipekuwa vipi huwezi kuziona, akazipanga, zikapangika. Bastola mbili zilizojaa sawasawa zikawekwa kiunoni mwake, suti nadhifu ikafuata juu yake. Kamanda Amata akasimama mbele ya kioo akajitazama, waoh akaonekana mithili ya mfanyabiashara maarufu duniani, kamwe hawatanijua kama ni jasusi mtata katika historia ya nchi, akajiwazia. Kisha akachukua kofia yake aina ya pama na kujitupia kichwani. Akainua mkoba wake na kutoka taratibu mpaka mlango mkubwa, akaminya nobu zake za siri na kuwasha mtambo wa usalama unaoruhisi kamera za siri kunasa picha zote ndani ya nyumba yake, kamera hizo ni yeye peke yake anayezijua hata Gina ambaye mara nyingi hulala katika nyumb a hiyo bado hakujua juu ya kamera hizo.

“Kamari wapi?” Scoba akamtupia swali Kamanda Amata wakati akiingia garini tayari kwa safari ya uwanja wa ndege.

“Mwadui Cassino, Shinyanga,” kwa jibu hilo wote wakacheka na kugonganisha viganja vya mikono yao, kisha ile gari ikaondolewa na kushika barabara ya Kinondoni makaburini kuelekea Ubalozi kabla ya kuikamata ile ya Ally Hassan Mwinyi mpaka Bibi Titi na kumalizia ya Pugu kupitia Mkurumah mpaka Uwanja wa ndege.

ITAENDELEA

Jiue Mwenyewe Sehemu ya Pili

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment