Mwanamke Mwenye Juba Jeusi Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE
*********************************************************************************
Simulizi : Mwanamke Mwenye Juba Jeusi
Sehemu ya Nne (4)
“Hawezi kutufanyia ujinga kama huu!” BIG aliwaeleza vijana wake kwa ukali, baada ya kugundua kuwa CD walioichukua kwa mama Chakwima ilikuwa ni ya vibonzo vya Tingatinga.
“Sasa, juu chini, CD ipatikane, Chakwima aletwe hapa au auawe, hayo ni maagizo ya wakuu” vijana walisikiliza na kuanza operesheni hiyo mara moja.
“Hii kazi ishafikia pagumu sasa, mambo mengi yamejiingiza kwa wakati mmoja” BIG alimueleza McField huku akimmiminia kinywaji katiak bilauri yake.
“Itakamilika tu” McField alimjibu huku akiteremsha kinywaji kile tumboni taratibu.
“Hata kama Max tumemuondoa lakini sasa kuna serikali, sijui tutafanyaje” BIG aliyaongea hayo huku akivuta akiti kuketi
“Usihofu, hapa kuna mtu mmoja tu tukishammaliza basi” McField alijibu huku akijiweka vizuri kitini
“Nani?” BIG aliuliza
“Kamanda Amata” McField alijibu, akakohoa kidogo na kuendelea “yule jamaa ni mpiganaji mzuri sana, usije ukatuma hivi vinyangarika vyako, atavivunjavunja vyote” McField alimaliza
“Tulimpata Amata tukamuweka hapa” McField alishtuka kwa sentensi hiyo
“Sasa ikawaje?” akauliza
“Yule mchawi, tumempa kibano hapa mara kwenye koti lake kukaanza kutoa moshi mwingi ukawachanganya vijana, akatutoroka” BIG alizungumza kwa masikitiko
“Hamumuwezi yule, nimekuja kwa kazi hiyo, kuhakikisha roho yake naondoka nayo, ili mambo yetu yaende sawa” Mc Field akacheka cheko la dharau, na kutoa bastola yake kisha akaifutafuta vumbi kwa kitambaa chake kidogo na kuibusu
“Nataka roho ya Amata” Aliiambia bastola hiyo na kuirudisha kiunoni.
“Nataka roho ya Amata” Aliiambia bastola hiyo na kuirudisha kiunoni. Kama bastola ile ingekuwa inajua kusema basi ingemwambia ‘huipati’.
George McField, muuaji hatari wa kimataifa, anayekodiwa kwa kazi mbalimbali za kuua, alitekeleza mauaji kwa yeyote aliyetumwa kakwe na kwa staili yeyote atakayoona inafaa. Mara hii alikodishwa kutekeleza mauaji ya Max Petito, tajiri wa Kiitaliano aliewekeza maisha yake katika nchi ya Tanzania huku akitanua wigo wake wa biashara haramu ya dawa za kulevya, akiwahonga viongozi wahusika mamilioni ya pesa na yeye kupitisha dawa hizo kiulaini sana katika viwanja vya ndege mbalimbali nchini, hakuna aliyesema mabaya juu ya tajiri huyu asiye na maneno mengi.
Max Petito alikimbilia Tanzania miaka takribani kumi nyuma akijiengua katika kundi la matajiri wenzake lililojikita katika udhalimu wa kulaghai viongozi wa nchi changa kwa pesa na mali na vijimisaada vidogodogo huku wakikomba rasilimali zao za kunenepesha matumbo yao.
Uwepo wake katika nchi ya Tanzania ulikuwa kikwazo kikubwa kwa waliokuwa washirika wake, hivyo wakati kampeni ya kuwekeza katika nchi hii ilipofika jambo la kwanza ilikuwa ni kumuondoa duniani tajiri huyu. Nani angeweza kuitimiza kazi hiyo kwa usiri na ufundi wa hali ya juu, hakuwa mwingine zaidi ya George Mc Field, raia wa Ureno aliyewahi kufanya kazi na shirika la kijasusi la KGB na kutekeleza maelfu ya mauaji sehemu mbalimbali duniani, japokuwa alikuwa mzembe sana katika utendaji wake lakini kamwe hakufanya ajizi katika swala la kuua. Safari hii alitua katika ardhi ya Tanzania kwa jambo moja la ‘kuua’, lakini kichwani mwake alitengeneza jambo lingine la binafsi ‘pesa’ .
Mwaka mmoja nyuma
VIENNA-ITALIA
Ndani ya jengo la kale, lililopambwa kwa sanamu nyingi zilizochongwa na mchonzi maarufu wa miaka ya nyuma ‘Michelangelo’, George Mc Field alisimama huku mikono yake minene kaikunja kifuani mwake na kumuonesha jinsi alivyo na misuli mipana, mawani yake myeusi ilitulia machoni pake na kufanya mtu yeyote amtazame kwa makini
“Mamy, guarda… Anold Schwazneeger” (‘guarda’ maana yake ni ‘tazama’)watoto wa Kiitaliano walisikika wakiwaambia wazazi wao. Mc Field alichekea tumboni hasa kwa kuwa alifananishwa na mtu huyo maarufu sana duniani.
Aliitazama saa yake na kuona kuwa bado dakika chache mwenyeji wake afike eneo hilo.
Mtu mmoja alisimama pembeni yake na kuangalia upande uleule aliokuwa akiangalia Mc Field,
“Unafikiri sanamu ile ni ya kitu gani? Au imekuvutia nini?” alimtupia swali Mc Field. Mc Field aliingiza mkono mfukoni na kutoa kipande cha noti ya Lira, na mtu huyo nae akafanya vivyo hivyo walipoviunganisha vipande hivyo vilikamilisha noti ya Lira 100. Kijana yule aliondoka bila kuaga na baada ya sekunde kadhaa Mc Fiels nae aliondoka eneo hilo kuelekea nje na moja kwa moja aliingia kwenye gari ya kifahari Ferrali iliyokuwa imeegeshwa nje ya jengo lile.
Max Petito alikuwa akicheza na mbwa wake katika bustani kubwa iliyopo nyuma ya nyumba yake katika eneo la ………………. pembezoni mwa mji wa Firenze. Alipomuona mgeni wake huyo aliachana na mbwa huyo na kumkaribisha kiti safi kilichopo hapo, huku wakitazama baharini waliongea machache tu.
“Time is tissue” Mc Field alimwambia Max Petito.
“Kazi, nataka CD ya mpango wa the Sixs” Max Petito alimwambia Mc Field
“Umepata” Mc Field alijibu
“Najua bado wapo kwenye mchakato” Max aliendelea
“Wamemaliza, imebaki utekelezaji” Mc Field alijibu na baada ya kumeza mate aliendelea “Malipo!” alitamka huku akiuweka mkono wake kama mtu anayeomba kitu fulani.
“5 Millions Euro” Max alimjibu.
Max Petito aliihitaji CD ile kwa gharama yoyote, kwa kuwa alijua wazi kuwa jamaa wa the Sixs kama wakiweza kutekeleza adhma yao ya kugeuza Tanzania, watamuharibia dili zake zote, alishawaweka vigogo wengi mkononi, na hii ilimfanya kuanziaha uhasama wa makusudi na washirika wenzake na yeye kujitoa katika kundi hilo, na kujikita katika biashara hiyo haramu ya kuzungusha madawa hayo duniani, alikuwa tajiri mwenye hati za kusafiria za nchi mbalimbali duniani. Alimtafuta Mc Field mapema ili kumpa kazi hiyo na alichohitaji ni CD ile original kwa kuwa alijua siku zote mbinu zao cafu zilihifadhiwa vipi.
Max Petito, baada ya kumaliza mazungumzo na mgeni wake huyo waliagana na kuahidiana kukutana baada ya mwaka mmoja kazi hiyo ikiwa imekamilika.
ÑÐ
Madam S alishusha pumzi ndefu na huku roho yake ikiwa inaenda kasi, alinyanyua bilauri yake iliyojaa kinywaji na kujimiminia chote kinywani mwake. Aliishusha bilauri ile kwa nguvu mezani, akionesha wazi kashikwa na gadhabu juu ya CD hiyo aliooneshwa na Amata.
“Shenzi sana, kumbe kelele zote majukwaani mambo yenyewe ndiyo haya!” alitikisa kichwa “Siasa zetu Afrika kama Mwanamke mwenye juba jeusi, ukimtazama mwanamke lakini unaona tu juba jeusi, hujui ndani yake kuna nini” alimaliza maneno hayo na kunyanyuka kuelekea dirishani, alikaza macho kuangaklia kinachoendelea
“Yaani watu wachache watununue kirahisi hivi?” alijikuta anauliza swali ambalo hamna wa kumjibu.
“Waafrika angalieni sana viongozi wenu, na wale wanaojiita wapinzani, hamna kitu, ni wizi na tama ya mali, ndiyo maana hatuishi kupigana wenyewe kwa wenyewe kila uchwao” Madam S aliongea kwa hasira na uchungu. Aliondoka pale dirishani na kuelekea kwenye kichumba chake kidogo ambacho amekifanya kama ofisi yake ya nyumbani. Amata alinyanyuka kitini aliitoa CD ile katika chombo kile na kuirudisha kashani kisha akamfuata Madam S ofisini, alimkuta kanyanyua simu yake ya mezani akisubiri upande wa pili uongee, Amata kwa haraka alibonyeza kitufe Fulani na kuikata simu ile.
“Hata kama unampigia mama yako huu si wakati wake” Kamanda Amata alimnyang’anya simu Madam S.
“Amata, amuru sasa hivi Punde Kishime akamatwe” Madam S alitoa amri.
“Hata kama wewe ni boss wangu, sasa nakufundisha kazi, hili swala lazima tulifuatilie taratibu, safari zote anazotoka mheshimiwa nje ya nchi au nje ya mkoa tumpe kampani ya siri ili tujue kwanza kama yumo mtandaoni basi yumo na nani, ili tutapoamua kumkamata basi tujue nani pia anahusika” Amata alimaliza kumueleza Madam S.
“Asante Amata, bibi yako nimezeeka sasa, kila nikimuomba Mheshimiwa Rais nistahafu hataki” Madam S alimalizia mazungumzo yao. Na wote wakajiandaa kuondoka kutoka katika kajumba hilo la Madam S.
“George McField, kwa nini unakuwa mzembe katika kazi tuliyokupa, time is beating George” Sir James Washington alitupia swali hilo kwa njia ya simu
“No. Sir”
“No Sir! Wiki mbili sasa, nini kinakushinda? Tumekupa pesa nyingi sana za kuua watu wawili tu ili sisi tupate njia na usisahau kuipata master cd yetu”
“Yes Sir”
“Fanya unaloweza, Chakwima umtoe uhai hara nakupa order, maana yeye anajua mengi juu yetu na kwa kuwa amekataa kuwa upande wetu basi hakikisha haamki na kuliona jua litalofuata” Sir J. Washington alikata simu na kurudisha mazungumzo kwa wageni wake waliokuwa wakimsubiri mezani pale.
“Tupe ripoti Sir” Mahmoud al-Bashir aliuliza kwa shauku.
“Oooh McField” Sir J. Washington alinung’unika na kujiweka vizuri kitini kisha akaendelea “Sijui kwa nini McField anafanya uzembe kama huu, swala ni kumuua tu Chakwima kabla hajabwabwaja chochote, halafu sisi tuelekeze nguvu zetu kwa Kishime ili tumfanikishie kama si kidemokrasia, basi kama kawaida yetu ni kufanya mpango hasi tu”
“Tusimlaumu sana McField” Bi Cedella aliwakatisha wajumbe wenzake “Tanzania, si nchi ya kuidharau, ina security ya hali ya juu sana, McField lazima awe muangalifu, la, tutampoteza”
Wajumbe walikuna vichwa vyao n akuendelea na mikakati yao mingine katika kufanikisha adhma waliyoikusudia. Mpango ulikuwa ni kujipenyeza katika nchi ya Tanzania na kuingiza sera zao chafu za kutumia viongozi wa kisiasa kwa mikataba laghai. Walimpata kiulaini sana Mheshimiwa Punde Kishime na kumfanya aasi chama chake na kuhamia kingine ili kutoka kule waweze kumtengeneza mbele ya macho ya wananchi wanaotaka kuona mabadiliko katika maisha yao ili nyuma yake wao wafaidike, lakini waligonga ukuta kwa mheshimiwa Chiwawa Chakwima, hata kama alipata jina na sifa kubwa niongoni mwa Watanzani lakini hakuwa tayari kuiuza nchi yake kwa mabepari hao wanaojiita The Sixs, aliipenda nchi yake na aliwapenda makabwela wenzake. The Sixs walipoona kuwa ushawishi wao kwa Mheshimiwa Chakwima umegonga ukuta na tayari walishampa siri kubwa ya matarajio yao waliona wazi kuwa ataweza kuwaharibia hivyo wakatafuta mbinu za kumuua hata kabla hajaiacha ardhi ya Abu Dhabi kwa majaribio mawili lakini haikuwa hivyo, sasa walihitaji kummaliza kabla hajaonana na watu wa usalama au wakubwa wake wa kazi huko Tanzania lakini bado kazi ilikuwa ngumu.
Siku zote muwinda huwindwa, kwa kuwa wao walikuwa wakiwinda basi kumbe nao walikuwa wakiwindwa pa si wao kujua.
Kikao kilimalizika na muafaka wa kukutana tena jijini Dar es salaam wiki inayofuata ili kukamilisha mipango yao na kibaraka wao Punde Kishime.
ÑÐ
George McField, alisimama katika kiambaza cha ukuta akiwa katika mavazi yake meusi ambayo hayakuruhusu kuonekana hata chembe ya ngozi yake, guo kubwa lililokuwa likining’inia mgongoni mwake lilimfanya aonekane kama mdudu au mnyama Fulani wa kutisha. Alitulia kimya akiangalia nyendo chache za walinzi katika hospitali ya Muhimbili ambako alikuja kwa ajili ya kazi moja tu ya kuondoa roho ya Chakwima. Alivuta hatua taratibu na kuliendea bomba kubwa la maji taka lililounganishwa kutoka chini mpaka ghorofa ya juu ya wodi hiyo, alikwea kupitia bomba hilo kwa kasi ya ajabu mpaka ghorofa ya pili na kwa kupitia dirisha la chooni alijipenyeza na kutua taratibu katika kijichumba hicho kidogo, akaichomoa bastola yake na kuifunga kiwambo cha kuzuia sauti, kisha taratibu aliufungua mlango wa choo hicho na kuruhusu jicho lake kuangaza katika wodi ile iliyoonekana tulivu sana, alishangaa kidogo kwa hali hiyo maana alijua wazi kuwa kitanda cha Chakwima unaweza kukiona moja kwa moja kupitia mlango wa chooni, alitupa jicho kwa umakini lakini jicho lake halikumdanganya, kitanda kilikuwa tupu, akajitokeza mwili wote na kuangalia chumba cha wauguzi ambako alimuona muuguzi mmoja tu akiwa amesinzia katika kiti chake huku ameegemea meza yake, kwa hatua za kipaka, alikijongea kitanda kile na mara miguu yake ilikufa ganzi, sasa aliamini kuwa macho yake hayakumdanganya, Chakwima hakuwepo kitandani, ‘amekufa? Sio rahisi! Yupo wapi?’, hakuwa anajua. George McField, alipigwa na butwaa, akili yake ilisimama kwa maana alijua sasa kazi inaanza, kazi ya mtafutano wa kufa na kupona.
Mr BIG aliketi akitazamana na McField, wote walitoleana macho na hawakujua nini cha kufanya walipigwa bumbuawazi juu ya kutokuwepo Chakwima kule hospitali. Mr BIG alimtazama jasusi huyu wa kireno aliyekuwa kajiinamia akitafakari jambo ambalo kwalo hakuwa na jibu, aliisogeza bastola yake na kuiweka sawa pale mezani, tayari kutekeleza lile aliloagizwa na swahiba zake kutoka Afrika ya Kusini. George McField alihisi kitu kibaya kutokea aliinua shingo yake taratibu na sura yake ikatazamana na domo la bastola iliyo mkononi mwa Mr Big.
“Hauna kazi na sisi” alimwambia McField ambaye alionekana kuwa na sura iliyojaa wekundu kwa hasira.
“Unataka kufanya nini? Kuniua?” alimuuliza BIG
“Ndiyo maagizo yaliyokuja”
“Nani aliyekupa maagizo hayo ya kijinga?”
“Mama yako” wakati BIG akizungumza hayo alijikuta akipata maumivu makali katika sehemu zake za siri kwa teke lililopigwa kwa ustadi sana kupitia uvungu wa meza hiyo ndogo, Mc Field aliinyanyua ile meza na kuitupa pembeni na kubaki uso kwa uso na BIG.
“Umechelewa!” McField alimueleza. Kwa wepesi wa ajabu alijirusha na miguu yake miwili ilitua kifuani kwa BIG ambaye alikwenda chini bila kipingamizi na ule mwili wake mkubwa, wakati McField akijiandaa kumkabili BIG pale chini alihisi eneo hilo hakuwa peke yake, hakukosea! Amata ga Imba alikuwa ameshafika katika himaya hiyo na vijana kadhaa kwa ajili ya kuiweka chini ya ulinzi.
“Freeze!” sauti ya Kamanda Amata ilitua masikioni mwa McField, ambaye bila kuchelewa alijirusha kiufundi na kutoka eneo hilo na kumuacha BIG akiwa bado pale chini akijizoazoa, Kamanda Amata aliona kama kivuli kikiondoka eneo lile alifyatua risasi kadhaa lakini shabaha ilikuwa siyo, risasi zilichimba ukuta eneo hilo na kushuhudia McField akipotelea katika uwazi mdogo ndani ya kiza kinene kilichofanywa kuwa hivyo na miti mirefu katika eneo hilo. Amata alimuacha BIG pale chini na kupita katika ujia uleule aliopitia McField, ulikuwa ujia mrefu unaopita katikati ya ukuta wa wigo na godown lililopo hapo, hamad! Kamanda Amata alihisi kitu kama popo kikitua hatua chache nyuma yake, alipogeuka alikutana na pigo moja takatifu ambalo lilimpotezea muelekeo, Amata alijiweka sawa na kukabiliana na kiumbe huyo, McField alipeleka mapigo kadhaa ya kung-fu lakini yote yalipita hewani na kupotea, Amata alikuwa akiyaepa na kuyakinga kwa ufundi wa hali ya juu, alipopata nafasi alijigeuza na kupiga teke la kuzunguka kwa nyuma na kuifikia shingo ya kiumbe huyo ambaye kwa ustadi mkubwa aliuepa na kuudaka mguu ule, Kamanda Amata alijinyanyua kwa haraka na kutumia mguu wa pili alipiga teke maridadi lilitua kwenye upande wa sikio la kiumbe huyo na kumfanya amuachie, kiumbe huyu alipepesuka wakati Amata akitua sakafuni kwa miguu yake miwili na kuanza kuvurumisha mateke ya mfululizo yaliyomchanganya yule kiumbe na kati ya yote hakuna lililomkosa kwani kasi ya mateke yale ilimfanya ashindwe kuyakinga na kujikuta akichezea kichapo kikali. Amata alitulia akiwa kasimama akihema akimtazama kiumbe huyu aliyevaa guo kubwa jeusi ambaye hakufanikiwa hata kumuona sura yake.
“George McField” aliongea Kamanda Amata, huku kwa hatua za taratibu akimfuata McField pale alipo. McField hakuwa mjinga kusubiri Amata amfikie pale alipo, akiwa kajiinamia alinyanyuka ghafla na kumpiga karate kadhaa Amata ambaye hakutegemea hilo kutokea, kabla hajakaa sawa Amata alichezea ngumi za uso zilizomfanya ajipange upya kumkabili Mcfield lakini haikuwa hivyo McField alijirusha na kutua nje ya ukuta, milio kadhaa ya risasi ilisikika upande wanje lakini tayari McField alikwishatoweka kizani.
ÑÐ
Madam S alikuwa akitazamana na Mheshimiwa Chiwawa Chakwima aliyekuwa ameketi mbele yake katika kiti cha magurudumu, alionekana mwenye mawazo mengi sana kichwani mwake.
“Usihofu Mheshimiwa, kila kitu kitapatikana” Madam S alivunja ukimya
“Nitashukuru, maana wale ni magaidi, wanayataka maisha yangu” Chakwima aliongea huku machozi yakimtoka.
“Hapa upo mahali salama sana, usiogope”
“Niko wapi?”
“Utapajua tu mambo haya yakiwa yamekamilika”
“Hebu niambie kuhusu Mh Punde Kishime na siasa zake za kuzuka” Madam S alimuomba Chakwima
“Kwa vyoyote, amenunuliwa na The Sixs” Chakwima alijibu
“The Sixs?!” Madam S aliuliza kwa mshangao, “Sijawahi kusikia”.
“Ni mtandao mkubwa unaoongozwa na watu sita tu wenye pesa za ajabu kutoka sehemu tofauti za dunia, wanajihusisha na kununua viongozi wa serikali za nchi zinazoendelea hasa zile ambazo zinaonekana kuwa na rasilimali nyingi kama hii ya kwetu. Wameshanunua nchi nyingi za Afrika nab ado wanaendelea…” Chakwima alimueleza Madam S habari nyingi za kundi hilo na kumfafanulia juu ya mipango na mikakati yao waliyojiwekea kwa Tanzania.
waliyojiwekea kwa Tanzania.
“Sasa nini wanakitaka zaidi kutoka kwako?”
“Wanajua wazi kuwa mimi nimeshajua hila zao, hivyo basi hawataki niseme chochote, wanataka kuniua, lakini kinachowachelewesha ni kuwa kuna cd ya huo mpango wote ambayo mimi nilipewa nikiwa katika ndege, cd hiyo sijawahi kuiona kabla, na ndiyo hasa inayowachanganya kwani ndani yake kuna mpango mzima na mikataba yote ya kishetani” Chakwima alijibu.
“Mh! Cd yenyewe iko wapi?” Madam S alizidi kudadisi wakati akijua wazi kuwa cd ile tayari wameshaipata.
“Nafikiri imeshafika mikononi mwenu, maana kijana wako nilimpa maelekezo yote. Nilimtuma motto wangu mdogo wa kike ambaye huwa anapenda sana katuni, kuwa akifika nyumbani achukue ndani ya koti cd na aiweke ndani ya kasha la Tom and Jerry na ile ya Tom and Jerry aiweke ndani ya kasha lile na kuirudisha kotini maana nitaihitaji nikisafiri tena. Na akafanya kama nilivyomuelekeza. Kisha nikamtuma mke wangu akaniletee cd iliyo ndani ya koti, wale magaidi walikuwa wakifuatili nyendo zote hivyo walijua kuwa nimemtuma kitu mama watoto, alipokuwa akitoka nyumbani, alipofika mataa ya Mwenge ndipo walipomvamia na kumpora cd ile kisha wakatokomea, mke wangu alifika hapa na kulia sana maana nilimsisitizia kuwa cd ile ni muhimu sana ahakikishe anaifikisha salama mikononi mwangu. Baada ya hapo nikampa maelekezo kijana wako na nina uhakika atakuwa ameipata na kuifikisha kwenu, namuamini sana yule kijana” Chakwima alimaliza kutoa maelezo hayo wakati huo Madam S alikuwa akiandika vitu Fulani kwenye kompyuta yake.
“Ok!” Madam S alishusha pumzi na kujiegemeza kwenye kiti chake cha kuzunguka akimwangalia Chiwawa Chakwima, “Punde Kishime” alijisemea kwa sauti ndogo ambayo ilimfikia sawia Chakwima.
“Punde Kishime, atakuwa amepewa pesa nyingi sana na kukubaliana na hila za wale jamaa…” Chakwima aliongezea “Inabidi mumwangalie sana na siasa zake” akamalizia.
“Yeah, tuna mpango maalum wa kujua kila kitu ndani ya siku hizi chache” Madam S alimpa matumaini.
Wiki tatu nyuma
Punde Kishime alibebwa na watu wawili walioficha sura zao kwa soksi maalum na kumpakia katika gari ya takataka akiwa hana fahamu, dakika chache baadaye walikuwa kwenye dampo kubwa maeneo ya Tabata na kulipaki lori hilo la manispaa ya Kinondoni, wakaketi kusubiri. Mara Noah Nyeusi ilisimama karibu yao na kuwasha taa za mbele mara tatu, vijana wale wakambeba tena Kishime mpaka kwenye Noah ile na kulaza ndani yake kisha wakaondoka zao. Muda kidogo wakawa mbele ya nyumba ndogo eneo la Keko Chang’ombe kwa Dr kazumari, daktari bingwa wa hospitali ya Temeke, alimuandaa Mheshimiwa kama mgonjwa anayesafirishwa nje ya nchi na kuweka documents zote sawasawa kisha wakampaki kwenye gari ya wagonjwa ya kisasa na safari kuelekea JNIA terminal 1 ikaanza.
Ndege ndogo ya kifahari aina ya Challenger 604 private jet, iliyokodiwa kwa kazi maalumu ilikuwa tayari imeshawasha engine zake, watu kadhaa walikuwa wameketi tayari kwa safari kitanda cha Mheshimiwa Kishime kilipandishwa na gari maalum na kuwekwa ndani ya ndege hiyo, na safari ikaanza.
Masaa kadhaa tu ndege hiyo ilikuwa katka ardhi ya Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh.
Asia Pacific Hotel, iliyopo katikati ya mji wa Dhaka ilikuwa ni hotel aliyowekwa Mheshimiwa Kishime kwa mapumziko mafupi.
Alizinduka kutoka usingizini na kujikuta mbele ya msichana mmoja mrembo, mweupe, mrefu wa wastani mwenye umbo la kimiss, mavazi yake yalionesha wazi kuwa ni kama ametoka maliwato au anataka kujipumzisha kitandani. Punde Kishime alimtupia jicho la uchovu, hakuelewa ni nani mwanamke huyo, kaingiaje hapo, akilizilipokuja sawa sawia alitambua kuwa mahali hapo hajawahi kupaona kabla, alijinyanyua na kuketi, ndipo alipogundua kuwa hakuwa na nguo isipokuwa ile ya ndani tu.
“Karibu Dhaka, Asia pacific Hotel” msichana yule alimkaribisha Punde Kishime kwa sauti ya kitetemeshi iliyomfanya Kishime kubaki hoi ukizaingatia ni mzee anayependa watoto wabichi, ghafla alijikuta anasahau hata kuuliza ni nini anafanya huko Dhaka baada ya kuona alichokifanya yule msichana. Kutokana na vazi alilovaa aliufungua mkanda maalum uliolikutanisha vazi lile mbele ya tumbo lake na vavi lile lilitii na kuanguka chini kuuacha mwili laini wa binti yule wa Kibangladesh kama alivyozaliwa, kwa hatua fupifupi na miondoko ya ki-paka alikijongea kitanda cha Kishime.
“Hey beibi, nilikuwa nasubiri uamke nikufanyie masaji” alimueleza Kishime huku akipanda kitandani na kuanza kumminyaminya sehemu mbalimbali za mwili wake. Kishime alitulia tuli bila kujitikisa akisikilizia mwili wake jinsi unavyosisimka kwa zoezi hilo.
“We ni nani kwanza?” kishime alizinduka na kumtupia swali yule msichana mwenye matiti machanga ambayo yalikuwa yakimchomachoma Kishime mgongoni.
“Mmmmmhhh! Usijali utanifahamu tu, jambo la kwanza natakiwa kukuondolea uchovu kama boss alivyoniagiza”
‘Boss’ Kishime alijiwazia, “Boss wako nani?” aliendelea kumsaili
“Utamuona tu, baadae kidogo”
Kishime alitulia, mwili wake ulikuwa aukishughulikiwa vyema na binti yule aliyepewa mafunzo maalumu kwa kazi hiyo, alilazwa kitandani naye bila kipingamizi alijitupa kwenye godoro hilo ambalo liliwapokea wawili hao bila hiyana na kuvumilia shida zote na mikikimikiki ya wapenzi hao wa ghafla.
Sir James Washington alikuwa ameketi katika meza yake kubwa ya kioo chenye nakshi nyingi, ndani ya ofisi kubwa iliyojalizwa na kila aina yap ambo unalolijua wewe. Akiwa na mtemba wake mdomoni alipekua hiki na kile kana kwamba kuna kitu alichokuwa akikitafuta na asikipate. Mara simu yake iliita na akaacha kila kitu akanyanyua mkono wa simu hiyo na kuuweka sikioni.
“Yes!” aliitikia
“Waruhusu haraka wapite” aliijibu sauti ya upande wa pili. Sekunde chache Sir James Washington alikuwa akitazana na Punde Kishime. Kikao hicho kilikuwa na watu watatu tu na si zaidi.
“Naitwa Sir James Washington, na huyu unayemuona ni Madam Hellen Sterling” alitoa utambulisho wa ufupi. Punde Kishime bado alikuwa haelewi kinachoendelea ndani hapo, sura kwake zilikuwa ngeni, hoteli aliyokaa ngeni, binti aliyefanya nae mapenzi kule hotelini mgeni, staili alizopewa ngeni, na hapo alipo anajikuta mgeni, mh! Basi ilikuwa shida juu ya shida.
“Sir James Washington, hivi unajua kosa unalolifanya?” Kishime aliuliza
“Kosa, kosa gani?”
“Kwanza umeniteka, pili unaitesa familia yangu, tatu umeleta usumbufu kazini kwangu…”
“Punde Kishime, sisi sio watoto au wajinga kama unavyofikiria. Kila kilichokutokea kilishapangwa” Sir james alimkatisha Kishime
“ ‘Sisi’ wangapi? Au wewe na nani?” Kishime aliuliza huku akionesha kuwa hana mzaha hata kidogo
“Kishime hebu tulia kwanza, aliyetujuza juu yako ni rafiki yako mpendwa Chiwawa Chakwima ambaye hata yeye kwa sasa yuko mikononi mwetu”
Kishime alionesha kuchanganyikiwa kwa jibu hilo.
“Hivi hamjui kuwa Chakwima yupo Uarabuni kwa shughuli ya kiserikali, halafu ninyi mtamuwekaje katika himaya yenu. Hivi mnajua mnachezea moto msiyoweza kuuzima, endapo ofisi yangu ya ubalozi itang’amua niko hapa, mpo matatani, mimi nui mtu mkubwa serikalini” Kishime alilalama huku mishipa ya shingo ikimtoka.
“Kishime, hebu tuliza munkari kwanza, huo mkutano wa wawekezaj huko Saudia sisi ndiyo tuliyouandaa kwa taarifa yako, na tunajua A mpaka Z kuliko wewe unavyofahamu. Sasa sikiliza, hapa tumekuleta kwa mpango maalum, mpango wa kutawala nchi” sera zao hazikuwa tofauti na zile alizopewa King Khalfan King ambazo zilivutia hata muandishi maarufu hayati Ben R. Mtobwa enzi za uhai wake aliandika kama riwaya iliyoitwa Nyuma ya mapazia au zile alizopewa Dr. Masurfu ambazo pia zilimvutia muandishi kijana Hussein Wamaywa kuifanya riwaya aliyoipa jina Harakati za kuelekea Ikulu.
Punde Kishime alitulia bila ubishi na kusikiliza Sir Washington akiongea mambo mengi na kumuonesha cd maalum iliyokuwa na mpango wote na mkakati mzima.
“Unasemaje? Kama upo tayari tuanze kazi mara moja” Sir Washington alitulia akimtazama Kishime aliyebaki katumbua macho kama mjusi aliyebanwa na mlango, moyo wake ulikuwa ukishindana na maamuzi yake kwa nguvu zote, ufisadi ukiivamia nafsi na uzalendo ukifukuziwa mbali.
“Tutakupa pesa za kutosha kufanikisha zoezi hili, sisi kwetu pesa si kitu cha kufikiri, na tutakupa msaada wowote utakaohitajika kwa ajili ya shughuli hii. Tunaamini kwa jinsi unavyopendwa na wananchi, sifa ulizojizolea tunaamini utafanya mapinduzi.” Sir James Washington alimaliza kauli yake, akavuta briefcase yake na kuipandisha mezani, kisha akaifungua, manoti yaliyojipanga humo ndani yalitaka kumfanya Punde Kishime awe kichaa, alijikuta anapigwa na butwaa, chezea pesa wewe!
“Hamna shida, nimekubali na nitafanya mpaka nihakikishe tumeingia madarakani” Kishime alilainika
“Ok, sasa mi na wewe tumemaliza, ila nipe akaunti namba zako za benki zinazotumia visa au master card hata kama una maestro ni sawa ili hela hii tukuingizie”
Punde Kishime aliorodhesha akaunti zake kadhaa ambazo zinamruhusu kutoa pesa popote duniani.
“Hizi hapa” alimsogezea Sir James kikadi chenye orodha hiyo.
“Sawa, la pili, chama utakachojiunga kikishakukubali nacho tutakipa nguvu za kiuchumi ili muweze kuiteka Tanzania na watu wake, chini kwa chini na sisi tutafanya kazi yetu kuhakikisha yanatimia. Rafiki yako Chakwima amekataa mipango yetu lakini ameshajua mambo mengi juu ya mpango huu kwa hiyo tunategemea kumuondoa duniani maana atavuruga mpango huu” Sir James Washington alimueleza Kishime waziwazi juu ya Chiwawa Chakwima, Kishime alijaribu kumshawishi bwana Washington kupunguza munkari, ajaribu kuongea na kumshawishi ili wafanye kazi hiyo pamoja.
“Sawa, sasa mi na wewe tumemaliza, jioni utakutana na mtu mwingine naye ni mmoja wetu na ana sera za kukwambia ili kuweka mambo sawa.
Wakapeana mikono na kila mtu akarudi alikotoka.
Wingu zito liliufunika mji wa Dhaka, lakini watu walionekana kuwa katika mambo yao kama kawaida, wingu hili liliashiria kuwa muda wowote mvua kubwa ingeshuka eneo hilo la katikati ya mji.
Punde Kishime alitulia tuli akiwa namawazo mengi kichwani mwake, kila alipojaribu kupiga simu nyumbani aligundua kuwa simu iliyopo chumbani kwake haikuruhusu simu za kimataifa ila za ndani tu ya eneo lile, hakuna jinsi ambayo angeweza kupata mawasiliano na familia au rafiki zake, aligundua hila hizi lakini hakujua ni jinsi gani zimefanywa na muda gani umechukua kuziandaa, alibaki kapigwa na butwaa, hajui la kufanya, alijitupa kitandani na kujilaza huku mawazo mengi yakimsonga, mawazo ya utajiri na yale ya kuwa mtu mkubwa serikalini, kiongoza wa dola mojawapo iliyopo Afrika ya Mashariki. ‘Nitaibadili historia ya Tanzania’ alijiwazia huku akijichekea mwenyewe kama juha. Mara mlango uligongwa na mtu mmoja aliingia ndani bila kukaribishwa. Punde Kishime aliinuka kutoka alipolala na kusimama wima.
“Gari ipo tayari, kwa safari mheshimiwa” yule kijana alimueleza Punde Kishime. Bila kipingamizi lakini akipigwa na butwaa alimfuata kijana yule, wakaingia kwenye lift na kuteremka chini ambako waliikuta BMW yenye rangi nyeusi ya kung’aa sana, mlango wa nyuma ulifunguliwa kutoka ndani na Punde Kishime akajitoma ndani, hakuamini anayemuona, mwanadada yule aliyekuwa akimpa burudani kule chumbani sasa alikuwa katika BMW hii, tena akiwa amevaa nadhifu, suti ya gharama kweli kweli, Kishime alibaki mdomo wazi, hakuamini kama huyu ndiye yule aliyekuwa akimkatia viuno kule chumbani. Gari ile iliondoshwa kwa mwendo wa wastani, ikiendeshwa na kijana nadhifu alionekana wazi akiijua kazi yake barabara. Ukimya ulitawala ndani ya gari hilo isipokuwa tu mziki wa soul uliokuwa ukisikika katika gari hiyo, muziki uliopigwa na mwanamama Aretha Franklin uliokwenda kwa jina la Chain of fools, akiwa amezama katika dimbwi la mawazo, alishtuka alipotakiwa kuteremka, safari mefika tamati.
Jengo refu lilikuwa mbele yao, nje yake kukiwa na bendera nyingi za nchi mbalimbali, Punde Kishime alishuka na kushangaa kidogo eneo hilo zuri lililozungukwa na vilima vya wastani vilivyopambwa na maua mazuri, hakika palipendeza, maji yalikuwa yakiruka kwa staili ya kuvutia ilimradi tu kukufanya wewe mgeni kujisikia uko peponi. RADISSOU BLU WATER GARDEN HOTEL maandishi mazuri yalisomeka juu kidogo ya mlango mkubwa wa kuingilia ndani, rangi zake zilikuwa zikikaribisha kila aliyefika eneo hilo. Punde Kishime akiwa pamoja na yule mwanadada ambaye mpaka hapo hakumjua hata jina lake waliingia moja kwa moja na pembeni kidogo ya mapokezi mwanadada yule alibonyeza vitufe Fulani kisha milango Fulani ikafunguka na wote wawili wakaingia ndani na milango ile ikajifunga, taratibu walijihisi wakishuka chini.
“Utakavyoviona huku, visikuogopeshe sawa?” yule mwanadada alimueleza Punde Kishime ambaye muda wote alikuwa kimya. Kutokana na kauli ile Punde Kishime alijikuta anaingiwa na woga na miguu ikimuisha nguvu. Sekunde chache walikuwa kwenye ukumbi mkubwa wenye watu wengi, kila mmoja lionekana na shughuli yake, asilimia kub wa walikuwa wamevaa suti nzuri nyeusi, wengine wakicheza karata, kamali na mbele kabisa akinadada waliocheza muziki wakiwa uchi wa nyama ili mradi dhambi zote zilikuwa humo. Walipita meza kadhaa mara moyo wa Kishime ulipiga paaa! Nusura adondoke, katika meza ya mbele yake kulikuwa na viumbe watatu, binadamu waliokuwa kama wafu, mifupa na nyama zinazowaning’inia ndivyo walivyoonekana, mara Kishime alipokaribia pale mmoja wa viumbe wale ambao walikuwa kana kwamba wanacheza karata aligeuka kumwangalia Kishime na macho yake yalitoa mwanga Fulani mwekundu na hii ndiyo ilimpa mshtuko Kishime. Zilikuwa ni camera za usalama zilizofungwa katika mtindo huo karibu kila eneo ndani ya casino hiyo. Waliliacha eneo hilo na kupanda ngazi mpaka ghorofa ya juu kidogo lakini bado wakiwa underground. Vijana wawili walimkagua Punde Kishime kisha wakamruhusu kuingia ndani ya chumba Fulani.
“Punde Kishime, lulu yetu, karibu sana, karibu kiti” mtu mmoja mwenye macho ya kibuluu alimkaribisha Kishime kitini, mvinyo na pombe kali zikaletwa mezani na kisha kila mtu aliondoka ndani ya chumba kile.
“Naitwa Fracesco Gonzalenz, nafurahi kukutana nawe leo” alijitambulisha kwa Kishime na baada ya kumeza fundamoja la pombe ile iliyosomeka katika chupa yake PUSHKIN, alimkazia macho Kishime na kuendelea “Hatuna muda wa kupoteza, baada ya kusini mkataba ule wa kwanza na Sir James Washington, sasa kuna mkataba wa pili utakaosaini na mimi, huu ndiyo utakaoanzisha safari yetu ya kuiendea Ikulu ya Magogoni”. Bado Punde Kishime alikuwa aking’aang’aa macho, hakuelewa anachotakiwa kusaini tena ni nini.
“Bwana Kishime, hata wanadamu wa ulimwengu huu walipotaka kukombolewa, Mungu alitoa sadaka ya mwanae wa pekee msalabani, si ndiyo?” swali lilitupwa ka Kishime.
“Ndiyo nakupata” alijibu
“Sasa sisi pamoja na wewe tunataka tuwakomboe Watanzania kutoka katika janga la umasikini la kutupwa. Tangu Mwalimu JK Nyerere, akaja Ali Hassan Mwinyi, tena akaja Benjamini Mkapa, na sasa yupo Jakaya Kikwete bado Watanzania wamelalia umasikini, sera yetu ni kufanya mageuzi na ni wewe tu unayeweza hili, achana na Chakwima amepoteza nafasi nzuri ambayo hatopata hata muda wa kuijutia” Gonzalenz aliongea huku akiendelea kubugia pombe yake. Alinyanyuka na kuliendea shelf kubwa lililopo hapo ndani na kubofya vitufe Fulani na droo yake ikajivuta nje, akavhuku faili moja kubwa lililofungwa kwa tepe ya dhahabu, akalifungua pale mezani, juu ya lile faili kulikuwa na picha ya fuvu la binadamu lililochorwa kwa wino wa dhahabu, Punde Kishime alibaki katyoa macho kuliangali faili lile huku moyo ukimuenda mbio kama saa ya ukutani…
Punde Kishime alibaki katyoa macho kuliangali faili lile huku moyo ukimuenda mbio kama saa ya ukutani.
“Hiki ni nini?” alimtupia swali Gonzalenz
“Si nimekwambia ni mkataba wa mwisho ili tuanze kazi, au umeshasahau?”
“Hapana sijasahau ila jinsi hili faili lilivyo linanitisha kidogo”
“Usijali huo ni urembo tu, fungua ndani usome”
Punde Kishime, alilifungua faili lile na kuanza kusoma kipengele kimoja baada ya kingine, kijasho chembamba kilikuwa kikimtiririka na alipofikia mwisho shati lote lilikuwa limelowa jasho wakati chumba hicho kilijazwa kwa baridi kali ya airconditioner,
“Mh!” aliguna na kulifunga faili lile kisha akalirudisha kwa Gonzalenz
“Nini, mbona waguna?”
“No, Hapana, haiwezekani”
“Mpaka umefika hapa maana yake ni kwamba ‘Inawezekana’”
“No, kama utaratibu ndiyo huu mimi hapana siwezi”
Punde Kishime alikuwa kitanzini, alipousoma mkataba ule alichanganyikiwa maradufu.
“Punde Kishime, urais si jambo la kitoto, tazama akina Mobutu, akina Paul Biya, akina Ravalo Manana, akina Kabila, akina Kagame na wengine wengi, wote ni wetu na wamesaini huu mkataba wakapata urais, si wale wanakula maisha, sasa wewe cha ajabu ni nini?”
“Ni bora nikagombee kiuhalali kuliko kwa njia hii”
“Nani aliyekudanganya kuwa urais wa Afrika aunapatika kidemokrasia? Acha ndoto za alinacha, hii ndiyo dunia, bila kukubaliana na matakwa ya wenye pesa huwezi fanya chochote, utakufa masikini. Haya ni mambo madogo sana.” Gonzalenz alimwangalia machoni Punde Kishime na kumuona jinsi alivyotaabika nafsi juu ya kiti kile, “Sisi tumeinunua Afrika kwa nini tushindwe kukununua na wewe?” Gonzalenz aliinuka na kuchukua cd Fulani na kumuonesha Punde Kishime juu ya mradi wao wote katika nchi mbalimbali za Africa na kumuelekeza kwa kina mpaka Kishime akalainika.
“Umeona? Hata mgogoro wenu wa Ziwa Nyasa ni kazi yetu, ule ni mkataba tuliosainiana na rais wa Malawi na lazima atekeleze. Sasa wewe unaogopa kutoa damu ya mtu mmoja katika kila mkutano wenu wa hadhara! Kwanza si ndugu zako shida nini, je tutakapohitaji roho yako mwenyewe itakuwaje. Kuna mambo hapo utayatekeleza ukishakuwa Rais, kama ndoa za jinsia moja, nchi zote zilizo na sisi lazima ziruhusu ndoa za jinsia moja hii ni N.W.O ‘New World Order’ na vyote vingine”
Punde Kishime alishusha pumzi na kuona wazi kuwa sasa anasaini mkataba na shetani, alimwangalia Gonzalena na mara alimuona kama ana mapembe, mara ana sura ya kutisha ata alipoongea alisikia sauti nyingi za watu zikitamka maneno yaleyale, hofu iliikaba roho yake, Kishime hakujua la kufanya alikuwa na maweweseko yaliyomfanya kujisikia hivyo. Aliinua glass ya mvinyo na kupiga funda moja kubwa.
“Gonzalenz, siwezi kusaini mkataba huu” Kishime alimezwa na jinamizi la uzalendo, alitazamana macho na Gonzalenz
“Kufikia hapa ulipofika ni sawa na kumuona Mungu uso kwa uso, na maandiko yanasema yeyote atakayemuona Mungu uso kwa uso lazima afe, kamwe hawezi kuishi. Musa alipopanda mlimani hakurudi. Sasa na wewe hutorudi”
Kishime hakuwa na la kufanya alilivuta faili lile na kuchomoa peni iliyowekwa katika kijuba maalumu akasaini mkataba ule na kumkabidi Gonzalenz, kisha yeye naye akapewa nakala moja ya mkataba ule ule kama ilivyokuwa kwa bwana Washington.
“Sasa waweza kwenda, lakini kama unataka kufurahia maisha hapa casino usijali, karibu na uione dunia mpya inavyofanana miaka kadhaa ijayo”
Mlango ulifunguliwa na yule mwanadada aliingia mle ndani akasimama kama mita tatu kutoka ile meza.
“Shaylati, mchukue bwana Kishime umpeleke popote anapotaka ndani ya jingo hili, muoneshe kila kona na mwisho umrudishe alikotoka” baada ya kusema hayo Gonzalenz alimpa mkono Punde Kishime na kuagana “Kumbuka taarifa zote za kinachoendelea tutazihitaji na msaada wowote utakaotaka utapata, sisi tunajua kazi yetu jinsi tunavyoifanya”
Akiwa na mwanadada yule Punde Kishime aliteremka ngazi na kushuhudia sasa pale jukwaani kwa wacheza uchi yakifanyika mambo ya ajabu, michezo iliyokosa maadili ilikuwa ikifanyika, alipitishwa eneo lingine ambalo alishuhudia watu wakifanya ngono bila kuogopa wengine ni wa jinsia moja. Punde Kishime aliketishwa katika meza moja ya mviringo na juu ya meza hiyo kulikuwa na kila aina ya vinywaji lakini kilichomtisha ni wale aliokaa nao, si watu bali ni mabaki ya watu ambayo yalionekana kama watu wakicheza karata.
“Kunywa unachokiona, leo ni siku yako hutoiona tena maishani” sauti ya yule mwanadada ilipenya masikio ya Kishime. Punde Kishime alilivuta lile faili alilopewa na Gonzalenz akalifungua na kulipiotia tena haraka haraka, kasheshe!
(…) Mheshimiwa hongera kwa kazi yako nzuri, kila mtu hachoki kulitamka jina lako, na mi pia nafanya vivyo hivyo. Kwa kazi yako nzuri hautaliona jua la kesho lakini uhai wako hautapotea bure endapo ukikubali kuja nilipo na kuzungumza, ukichelewa vijana watakuja kuchukua mzigo (…).
Maneno ya barua aliyoletewa ofisini yalijrudia kichwani mwake, sasa ndiyo akili ilimfunguka kujua nini siri ya barua ile, ‘Wajinga ndiyo waliwao’alijiwazi na kujipa faraja, akiwa kama kichaa alikunywa haraka haraka ile pombe.
“Vipi mbona unakunywa kwa fujo?” yule mwanadada aliuliza
“Nataka nimalize haraka tukafanye mapenzi na wewe, kama jana”.
Tayari pombe zilianza kumpeleka puta, Kishime hakuwa na ujanja, macho yalimuia maito alijaribu kuyakodoa lakini aliona duble duble, akajitahidi lakini wapi, akainama kichwa na usingizi mzito ukayajaza macho yake.
ÑÐ
“Balazuri mkubwa!” Amata aling’aka, alishasahau kama chini kuna mtu aliyekuwa amelala kwa kupigwa na Mc Field, aliitia bastola yake kiunoni na alipotaka kugeuka aliona kitu kama gongo kikimfuata usoni, kitendo cha haraka aliyumba kidogo na kufanikiwa kudaka gongo lile, alimtazama BIG kwa sekunde kadhaa hakujua amfanye nini, katika kuzubaa kule BIG aliachia lile gongo na kutaka kuwahi kuokaota bastola yake, teke moja la mbavu lilimuacha chale sakafuni. Amata aliwa na bastola yake mkononi,
“Simama,” BIG akatii alichoambiwa bila shuruti, “Niambie ninyi ni nani?”
BIG alibaki kimya mikono yake ikiwa juu
“Sifanyi utani ntakuumiza sasa hivi!” Amata alizungumza kwa hasira. BIG alisonya na kushusha mikono chini, kosa! Bastola ya Amata ilikoho na kupiga sawia katika kanyagio la mguu wa BIG
“Aaaaaaaaa!!!” sauti ya maumivu makali ilisikika, kabla hajajibu mlio wa risasi ulisikika na Kamanda Amata aliushuhudia mwili wa BIG ukianguka kama mzigo. Inspekta Simbeye alikuwa amesimama na bastola yake aina ya revolver ikiwa tayari kucheua tena.
“Umemuua?” Amata aliuliza
“Hapana sijamuu, nimemjeruhi tu, ili awe mpole”
Inspekta Simbeye alipiga mbinja fupi na vijana wanne wenye SMG waliingia eneo lile “Tia pingu huyu, mpakie kwenye gari”
“Mpelekeni Muhimbili, apate matibabu nina mazungumzo naye nyeti.” Amata alimueleza Simbeye huku akiiweka bastola yake vizuri
“Nyie nendeni mimi kuna mtu namsubiri hapa” Amata alimnong’oneza Simbeye.
Gari ya polisi iliondoka eneo lile bila kuacha ulinzi wowote. Amata alijificha kwenye ua kubwa akisubiri mtu asiyejua kama atakuja au la…
Gari ya polisi iliondoka eneo lile bila kuacha ulinzi wowote. Amata alijificha kwenye ua kubwa akisubiri mtu asiyejua kama atakuja au la.
Nyuma ya ua lile Amata alikuwa akipambana na na kiza kilichobeba mwanga hafifu wa taa iliyokuwa ikiwaka sebuleni kwenye kigorofa cha juu, mbu wakali walikuwa wakifaidi damu iliyojaa chumvi ya kiumbe huyo.
Baada ya muda kile alichokisubiri kilitokea, kwanza alisikia mlio wa gari kwa nje ya jingo hilo, mara mlango ukafunguliwa, mtu mmoja, mnene mwenye kitambi cha nyama choma na bia aliingia akifuatana na wengine kama watatu hivi. Kutoka pale, kamanda Amata aliweza kuwaona watu hao kwa uzuri, ijapokuwa si alichokisubiri lakini alifurahi kwa kupata ndege wawili kwa jiwe moja. Punde Kishime alitangulia na hao watatu walimfuata nyuma, Amata alijikuta moyo wake ukienda mbio alitulia na kuangalia kinachoendelea, walisimama pale upenuni na kuangaza angaza huku na huko.
“Mbona hakuna dalili ya mtu hapa!” Kishime alishangaa
“Ah, kimya kingi pia au wapo ndani?!” yule mwingine alidakiza, lakini hawakupata jibu. Punde Kishime alitoa simu yake na kubofya namba fulanifulani
“Hallo! Eee mbona hampo hapa?” aliuliza “Enhe, … ok … sawa, basi fanya hivyo tuonane”. Amata alibaki njia panda kwa kuwa hakujua upande wa pili wa simu ile kimeongelewa nini na nani. Punde Kishime na wale watu watatu wakapanda kijingazi kuelekea kule juu, kamanda Amata akautumia mwanya huo kuchomoka nakutoka nje kuliendea gari walilokuja nalo.
‘Ewaaaaa’ alijisemea moyoni baada ya kuiona ile GX 150 pale nje ambayo hata namba ilikuwa bado kupata. Kwa kutumia funguo zake za siri alifungua buti na kujitoma ndani kisha akalirudisha taratibu na kuacha sehemu ambayo angepata hewa.
Punde tu, alisikia watu wakizungumza na mara milango ya gari ile ilifunguliwa na kufungwa kwa sekunde tofauti, aliihesabu na kugundua kuwa wote watakuwa wameshapanda, aliweka tayari vifaa vyake vya kunasa sauti ndani ya buti lile ili kunasa mazungumzo yoyote. Safari ilianza taratibu na mazungumzo ya hapa na pale yaliendelea.
“Ilibidi tukutane hapa, lakini nashangaa dharula gani imewakumba hawa vijana” Sauti ya Kishime ilisikika vyema na Amata hakupata tabu kuigundua.
“Anyway ngoja tukutane nae huko Shemshi bar alikosema” sauti nyingine ilijibu.
“Na sisi tuliwaacha hapa ili kutimiza ile kazi yako uliyotuambia, wakasema tutawakuta apahapa. Nafikiri labda kutakuwa na shida iliyotokea”. Ndani ya gari ile kulikuwa na mazungumzo mengi sana ambayo kamanda Amata aliyafurahia. Aliinua simu yake na kubonyeza kitufe Fulani upande wa kushoto, mara kijitaa chekundu kikawa kikiwakawaka, kisha kwa kunong’ona akazungumza maneno Fulani kisha akazima kile kijitaa kwa kubofya palepale.
Saa ya Madam S ikamfinya kwa chini, alipoingalia ilkuwa akiwaka kijitaa chekundu, akabofya upande wa kushoto wa saa ile na mara mkanda mwembamba wa kiplastiki ukaanza kutoka upande wa kulia wa saa ile.
“Andaa kiti, Shemsh and sons, Gongo la mboto, mara moja, haraka Tena Sana Aisee 1”
Ulimaliza ujumbe ule, Madam S alinyanyuka kitini na kuelekea simu ya mezani akiwa kamuacha Chiwawa Chakwima pale,
“Chiba… uko wapi?” aliuliza kwenye simu
“Magogoni bibi”
“Haraka sana nenda Shemshi and sons, katege sikio pale, kamanda yuko njiani” madam akakata simu na kurudi mezani alipokuwa ameketi na mheshimiwa Chakwima wakiendelea na mahojiano.
Shemshi and Sons
Kama kawaida, wakazi wa Gongo la Mboto na wengine wa maeneo jirani walikuja hapo usiku huo kwa ajili ya kupata vinywaji, nyama choma, wengine kupumzika na wenzi wao au wake za watu, ilimradi tu shetani alikuwa akitawala.
Chiba aliegesha pikipiki yake nje kidogo ya bar hiyo na kuiweka helmet yake katika kioo cha pikipiki hiyo, akashuka na kuitazama saa yake, muda ulikuwa umekwenda kwelikweli. Simu yake ilitikisika mfukoni na alipoitoa alikuta meseji imeingia ‘Toyota GX 150 namba za injini’, aliposhusha mkono wake na kuitia simu ile mfukoni aliiona gari ndogo nyeupe ikiingia katika maegesho, akatuli kama mtu ambaye anasybiri mteja wa bodaboda, alishuhudia wakishuka watu wanne, aliwatazama kwa chati wakiwa wanajadiliana jambo, Chiba alivuta hatua kuulekea mlango wa kuingia ndani ya wigo wa bar hiyo, alisimama kidogo lakini wale watu hawakupita mlangoni
“Samahani napita!” aliwaeleza wale watu huku akimshika mmoja kwenye bega lake la kulia na kujitoma ndani. Walimwangalia Chiba lakini yeye aliendelea na safari yake mpaka kaunta ambako alivuta stuli moja ndefu na kuketi.
“Savanna mbili tafadhali” alimuagiza mtu wa kaunta wakati akitoa mfukoni kitu kama simu na kuunganisha chombo cha kusikilizia na kutia sikioni kisha akabofya vitufe fulanifulani na kukirudisha mfukoni.
Chiba kutoka pale alipo aliweza kuyadaka mazungumzo yote ya wale jamaa na kuyarekodi kwa chombo chake hicho ambacho ukikitazama kwa haraka utafikiri ni simu kumbe la!
Mlango wa buti la gari, ulisukumwa kwa nje taratibu na kwa utulivu wa hali ya juu Amata alitoka nje kisha akarudishia mlango huo na kuubana, aliangaza huku na huku akagundua hakuna aliyemuona kwa kitendo hicho, alivuta hatua taratibu na kuielekea ATM ya Barclays iliyopo pembezoni tu mwa bar hiyo, lakini kabla hajaifikia alisimama na kujiegemeza kwenye mnazi akiangalia matukio yote jinsi yanavyoendelea. Kutoka pale alimuona mheshimiwa Kishime na wale watatu wakiingia ndani ya bar ile na kupanda ngazi kuelekea kighorofa cha juu, Amata aliendelea kubaki palepale akingoja, anamngoja nani mimi na wewe hatujui. Mbele yake tu, gari moja aina ya Noah ilisimama na mtu mmoja mwanaume, kibonge wa wastani na anayeonekena amejazia kimazoezi, akiwa ndani ya jeans na t-shirt iliyofunikwa kwa kikoti cheusi cha ngozi kichwani akiwa na kofia kubwa ya ki-jah. Amata alimuona mtu huyo na kumtazama kwa makini ‘Mc Field’ , hakuwa na papara, alimuacha aingie ndani ya bar ile na moja kwa moja aliingia kwenye bar ile.
Amata alimuona Chiba akiwa kaunta akajua hakuna noma kazi itakamilika, akabaki pale kaegemea mnazi akisubiri matokeo.
Baada ya kama ya saa moja kupita, watu wale waliinuka vitini na kuondoka, safari hii waliingia katika magari kwa idadi sawa, wawili kwenye ile Noah na wengine kwenye GX 150 na safari ya mjini ikawiva.
Chiba aliteremka kutoka katika stuli ndefu na kuuendea mlango wa kutoka nje, moja kwa moja akliendea pikipiki lake akachukua kofia ngumu na kuitupia kichwani kisha akaketi juu ya pikipiki hilo tayari kuondoka, ndipo alipogundua kuwa nyuma alikuwa kapakia mtu mwingine.
“TSA” sauti ya mtu huyo ilipenya masikioni mwa Chiba, akawasha pikipiki na kuanza kuufuatilia msafara ule, ijapokuwa ulikuwa umefika mbali kiasi Fulani lakini haikuchukua muda kuiona ile Noah ikiwa inakaribia njia panda Segerea, Chiba hakucheza mbali nayo.
“Ifuate hiyo Noah tuone itakapoishia” Amata alimwambia Chiba nae akavuta mafuta kwa mkono wa ke kulia na kuzipita gari kadhaa kisha kuwa nyuma ya ile Noah akitenganishwa na gari moja kati yao.
Safari iliendelea mpaka kwenye mataa ya Chang’ombe, ile Noah ikapinda kulia na kuelekea upande wa Temeke, mwendo kidogo tu ilifika mitaa ya Keko na kuiacha lami kuelekea upande wa kushoto, barabara iliyojaa makorongo na madimbwi ya maji. Chiba aliendelea kuifuata kwa mbali mpaka alipoiona ikiingia kwenye jengo moja kubwa lenye geti jeusi na kupotelea ndani kabla ya geti lile kujifunga taratibu.
Amata aliteremka kwenye ile pikipiki na kuliangalia kwa makini jengo lile, akatikisa kichwa juu chini kuashiria kuwa kuna kitu amekinoti.
Chamwino – Dodoma
Uwanja wa shule ya msingi Chamwino ulijaa watu wa rika zote, wa kike kwa wa kiume, watu wenye uchungu na mabadiliko ya siasa ya nchi yao, machozi yaliwatiririka kwa uchungu jinsi walivyosikiliza hotuba kali nay a kuumiza mioyo iliyotoka kinywani mwa Punde Kishime aliyekuwa akiruka huku na huko jukwaani bila kujali nini kinaweza kutokea. Makofi na vigelele vilivosindikizwa na mbinja za vijana zilisikika kila baada ya maneno kadhaa ya mheshimiwa huyo aliyeonekana kuwa ni mkombozi wa wanyonge.
Noah nyeusi yenye vioo vya tinted ilikuwa inaingia taratibu katika uwanja huo, kutokana na wingi wa magari eneo hilo hakuna aliyeweza kuhisi chochote katika gari hiyo iliyokuwa ikienda kuegeshwa karibu kabisa na gari zingine.
Watu waliokuwa ndani ya gari hiyo, hakuna aliyeshuka hata mmoja, ilibaki ikinguruma palepale ilipoegeshwa.
“Sasa!” mmoja wao aliuliza
“Fanya kazi” mwingine alijibu. Ukavutwa mkoba mdogo mweusi, juu ya mkoba huo kulikuwa na picha ya fuvu, ukafunguliwa kwa mikono iliyofichwa ndani ya gloves nyeusi, kidubwasha Fulani ukubwa wa redio ndogo chenye vitufe kadhaa kikawa mikononi, antenna ya chuma ikavutwa nje ya kidubwasha hiyo, kitufe kimoja kikabonyezwa, taa ndogo nyekundu ikawaka, sekunde kadhaa zikapita kitufe kingine kikabonyezwa ….
kitufe kimoja kikabonyezwa, taa ndogo nyekundu ikawaka, sekunde kadhaa zikapita kitufe kingine kikabonyezwa.
Mlipuko mkubwa ukatokea eneo lile pembeni kidogo ya mnara wa kipaza sauti, watu walivurugana, walikanyagana, wakaumizana. Punde Kishime alivutwa pembeni na vijana wake na kuondolewa eneo lile la hatari, vilio bado vilitawala uku na kule hakuna aliyejua ni nini kimetokea zaidi ya kuona tu mlipuko huo.
“Shit, hii ni nini?” Punde Kishime aliwauliza vijana wake huku akijifuta vumbi usoni kwa kitambaa chake baada ya tukio lile, alitwenda kama mbwa aliyekimbizwa, akachukua maji aliyoletewa na mfuasi wake wa karibu na kunywa kupoza kiu.
“Mzee tuondoke hapa! Jamaa wanakuwinda wewe” mmoja wa walinzi alimwambia Kishime
“No, si ubinadamu, tusiondoke, tuone mwisho,” Kishime aliwaeleza vijana wake na wote wakabaki wakiangalia tafrani ile. Polisi walifanya kazi ya ziada kuhudumia majeruhi na wengine kuangalia aina ya mlipuko huo. Watu walijeruhiwa vibaya na wengine kupoteza maisha, damu ilitapakaa kila mahali.
Chiba, alishusha miwani yake myeusi na kuyaruhusu macho yake maangavu kuangalia eneo lile jinsi lilivyovurugika kwa tukio hilo, akipepesa kope zake kwa umakini wa hali ya juu macho yake yalitua katika gari aina ya Noah yenye rangi nyeusi, alishuhudia kioo chake kimoja kikipanda taratibu na kutoruhusu mtu kuona kilichomo ndani, kisha gari hiyo ikatoka taratibu katika eneo lile. Chiba akaingia katika gari yake aina ya Toyota Harrier na kuitoa taratibu kuifuatia ile Noah inakoelekea.
Hali ya eneo lile ilitulia, majeruhi walikimbizwa hospitali na waliopoteza maisha walipata hifadhi yao ya muda katika hospitali ya wilaya ya Chamwino. Polisi na askari wa JWTZ walikuwa kazini kuchunguza aina ya mlipuko au bomu lililotumika ili kutoa majibu sahihi kwa waliowatuma, hakuna aliyeshukiwa na kitendo hicho wala kukamatwa. Mabaki ya bomu lililotumika yalikusanywa na kuhifadhiwa kati chombo maalumu, lakini swali lilibaki, ni nani aliefanya kazi hiyo na kupoteza maisha ya Watanzania wenye uchungu wan chi yao wenye kudai mabadiliko ya kiuchumi na kiutawala, waliochoshwa na utawala wa chama mzee, lakini maisha yao yalibaki rehani katika hilo.
ASP Seba Sebanja alifikicha macho yake na alipoondoa mikono yake taswira ya Punde Kishime aliyeketi mbele yake ilijitengeneza taratibu, akajikohoza kidogo na kujiweka vizuri kitini.
“Mheshimiwa Punde Kishime!” Seba akatulia kidogo, Punde Kishime akainua uso wake na kumwangalia usoni askari yule, “nafikiri unajua lililotokea katika mkutano wenu leo alasiri,” alimjuza.
“Ndiyo kijana, nafahamu vema” Kishime alijibu.
“Unaweza kutuambia au unachohisi juu ya hili?”
“Kwa kweli, sisi tulikuwa tunaendelea na mkutanao na mara ghafla ule mlipuko ulkatokea, lakini kusema nani tunamhisi tutaudanganya umma” Kishime alijibu, “Nnachoweza kusema ni kuwa labda wale wasiopenda maendeleo ya chama chetu, jinsi kinavyokusanya wafuasi nchi nzima, lakini kusema Fulani, hapana!” alimalizia jibu lake.
“Kwa maelezo ya wataalamu, mlipuko uliwekwa katika mlingoti wa kipaza sauti, je huwezi kuwahisi mafundi waliofunga vipaza sauti?” Seba Sebanja ASP alitupa swali, Punde Kishime alibaki kimya kidogo, kisha akafungua kinywa chake,
“Siwezi kusema ndiyo au hapana katika hilo, kwa kuwa wakati wanafunga hivyo vyombo mi sikuwepo isipokuwa wale wanaohusika tu”
“Sawa Mheshimiwa, wakati mwingine mhakikishe usalama kabla ya kuanza shughuli za mikusanyiko, nikikuhitaji tena usisite kuonana nami au ukipata tetesi yoyote unipe taarifa, nijukumu la polisi kuhakikisha usalama wa raia na mali zao” alimaliza ASP Seba na kuagana na Punde Kishime. Kijasho chembamba kilimtiririka Punde Kishime, mishipa ya hasira ilionekana wazi usoni mwake, alitoka katika kituo cha polisi cha wilaya ya Chamwino na kuingia katika VX yake na kujitupa kwenye kiti cha mbele.
“Dodoma Hotel haraka!” alimuamuru dereva wake na mara moja wakaondoka eneo lile.
Chiba aliendelea kuifuata ile gari, sasa walikuwa maeneo ya jirani na Kisasa wakielekea mjini, kati yao kulikuwa na gari tatu tu, Chiba alihakikisha haipotezi gari hiyo ili ajue ni wapi ilielekea. Moja kwa moja walizunguka mzunguko wa kwanza (keep left) na kuendelea kuelekea mjini, baada ya mwendo wa dakika kadhaa gari ile iliishia kwenye maegesho ya Dodoma Hotel, Chiba alisimamisha gari yake karibu kabisa na hoteli hiyo na kushusha kidogo kioo cha kushoto kwake na kuangalia nyendo zinazoendelea, vijana watatu walishuka katika gari ile na kuelekea hotelini, ile gari ailgeuza na kuyaacha maegesho yale, Chiba aliona kuwa hiyo ni nafasi yake aliendelealea kuifuata kule inakoelekea, walitoka eneo la hoteli ile na kuingia katikati ya mji wa Dodoma na kuelekea pande za uwanja wa ndege, hakukose ile gari ilikunja kona na kuingia uwanjani hapo, harakaharaka alishuka mtu aliyekuwa na mkoba mmoja mdogo na kuielekea ndege iliyokuwa hapo, ilionekana ikimsubiri yeye tu, kwani baada tu ya kuingi ndegeni mlango ulifungwa na injini za ndege hiyo zilianza kuvuma kuashiria kuwa sasa safari inaanza.
ÑÐ
“Siku hiyo kwa kumbukumbu zetu inaonekena kulikuwa na ndege moja ya kukodi nayo haikutoka hapa, ni mali ya mtu binafsi ilikuja kuchukua mgonjwa kumpeleka nje kwa matibabu, watu wana pesa bwana!” mama mtu mzima, aliyekuwa zamu katika uapndewa custom katika uwanja wa ndege wa zamano au terminal one kama ujulikanavyo alikuwa akimpa ripoti kamanda Amata aliyekuwa ameketi mbele yake akimsikiliza kwa makini.
“Ok, unaweza kujua kuwa huyo mgonjwa alikuwa anatoka hospitali gani?”
“Katika makabrasha yetu, mgonjwa alitoka katika hospitali binafsi, hospitali ya Dr Kazumari.” Amata alitikisa kichwa kwa kusikia hilo na kuandika kwenye kijitabu chake, alipojiridhisha na majibu aliyopewa aliaga na kuondoka, lakini kichwani mwake alitawaliwa na jina moja tu ‘Dr Kazumari’, akiwa ndani ya Freelander yake aliondoka kwa kasi na kuuacha uwanja huo kuelekea ‘shamba’.
“Umefanya kazi nzuri sana, sasa leo hakikisha unalala hapo Dodoma Hoteli ili kiwezekana antenna yetu ipate habari” Amata alimueleza Chiba kwa njia ya simu.
“Sawa kamanda, hiyo kazi ndogo” alijibu Chiba.
Athuman Chiba, askari kanzu katika idara ya usalama wa Taifa, yeye alikuwa amebobea kati mambo ya kunasa mawasiliano ya watu kwa njia yoyote ile ‘telecom’, mafunzo yake haya aliyanyia nchi mbalimbali alipokuwa sambamba katika kazi za polisi wa interpool na aliondokea kuwa ‘mkali’ katika nyanja hiyo, alporudi nchini moja kwa moja aliwekwa katika kitengo hicho maalum kutafuta mawasiliano yoyote yale yanayoitajika iwe kielektroniki au njia yoyote nyingine, wakati mwingine hata kuhatarisha maisha yake, alikuwa na laptop yake kubwa ukiiangalia ni kama briefcase lakini kazi yake ilikuwa kubwa katika kunasa mawasiliano na kurekodi sauti yoyote aitakayo.
Amata alishuka ngazi za jingo hilo kuukuu na kuingia kupitia kijilango kidogo kabla ya kutokea kwenye ujia mrefu uliompeleka mpaka stoo ya jengo hilo. Kutokea stoo hiyo aliingia jikoni na kuibukia sebuleni ambako alimkuta Madam S akiwa anaangalia TV kubwa iliyo hapo akipata habari za kitaifa na kimataifa.
“Tumefanikiwa” Madam S alimtupia swali Amata
“Yeah, asilimia sabini na tano”
“Chiba vipi?” Madam S aliuliza tena
“Yuko poa, anafanya kazi nzuri sana. Nafikiri sakata hili litapata usumbufu sasa hivi, muda si mrefu” Amata alijibu huku akiliendea jokofu lililopo sebuleni hapo na kutoa chupa ya grants akajimiminia kwenye bilauri pamoja na vijibarafu vichache na kupiga funda moja.
“Baadaye leo nahitaji kuongea na lile bonge, na likinipa majibu ya msingi basi tunafunga hii kazi kwa ushindi mkubwa, ila mpaka sasa kazi ni mbichi” Amata aliongeza kusema mara alipoitua bilauri yake mezani
“Kivipi kamanda?” Madam S aliuliza huku akimmiminia kinywaji Amata.
Ajali ya Chakwima bado sijaiweka vizuri, nataka kumjua zaidi Max petito na undani wa kifo chake, kisha nijue undani wa siasa za Kishime, kumbuka tayari watu wane wampoteza maisha na wengine kujeruhiwa leo huko Chamwino, sasa hapa tuwe makini” Amata alimwambia madam S
“Nakubali Kamanda, yote hayo ufumbuzi wake haujakamilika ila uko mbioni kufichuka ulikojificha”
“Na kazi ya mwisho naitaka roho ya yule sijui ni kiumbe gani yule, mwanamke mwenye juba jeusi” Amata alimalizia na kupiga ngumi mezani. Akiwa katika maongezi hayo mara saa yake ilianza kumfinya ikiashiria kuna ujumbe unaotaka kuingia.
“Mkutano mkubwa wa kimataifa utafanyika hapa Tanzania, wajumbe ni sita tu na ukimalizika hapa utahamia Malawi…Inaonekana tukio la Chamwino ni moja ya mkakati wa mafanikio”
Ujumbe ule uliishia hapo, Amata alitikisa kichwa, akakivuta kijikanda kile na kukikata kisha akampa Madam S ambaye naye baada ya kukisoma akataharuki.
“Nilikwambia Amata, hizi siasa zetu zina mambo nyuma yake, umeona?” Madam S alimueleza Amata ambaye alibaki kashika tama akili ikifanya kazi kichwani mwake. Kama aliyeshtuliwa, Amata alinyanyuka kitini ghafla na kusimama wima
“Vipi?” Madam s aliuliza
“Nahitaji kuongea na bonge la mtu ili nijue twafanya nini, leo hii” Amata aliichomeka bastola yake sawia upande wa nyuma wa suruali yake na kuondoka katika jumba hilo…
“Jamani, ninyi wenzangu mnajua kilichotokea?” Punde Kishime aliwauliza viongozi wa chama na wadau wachache waliokuwepo katika mkutano huo usio rasmi. Hakuna aliyejibu bali wote walimtazama yeye.
“Hili swala, litaharibu sifa ya chama chetu tusipoangalia, katika historia ya nchi yetu haijawahi kutokea Kishime” kiongozi mmoja aliongea kwa msisitizo huku akigonga meza kwa ngumi na wengine wote waliafiki.
“Kwa kweli, mi sielewi ni nini kilitokea pale, nikirejea mkutano tulioufanya Jangwani ambao ulikuwa ni wa kumkaribisha bwana Kishime msongamano wa watu labda ulisababisha vifo hiyo haina shida lakini mara hii tunawekewa milipuko mikutanoni, nina wasiwasi, huenda wakawa wapinzani wetu baada ya kuona nguvu yetu ilivyo kwa sasa” kiongozi mwingine aliongezea.
“Lazima tutawindwa kila kona sasa hivi lazima tuwe makini,” mjumbe mwingine alizungumza.
Kikao cha tathimini kilikuwa kirefu, na baada ya kumaliza kikao hicho waliagana na kila mjumbe kurudi hotelini kwake.
Wakati mkutano ule ukiendelea Chiba aliketi ndani ya gari yake akiwa amefungua ile laptop yake kubwa maalum kwa kunasa mawasiliano akisikiliza kila kilichozungumzwa na kukirekodi, haikuwa kazi ndogo bali ilihitaji umakini wa hali ya juu sana.
Punde Kishime aliingia kuoga, dakika kama kumi hivi akatoka na kurejea chumbani hapo akiwa ndani ya pyjama, alishtuka kidogo maana aliona kitu ambacho kilimfanya mapigo ya moyo wake yaende mbio, juu ya kimeza kidogo kulikuwa na bahasha ndogo nyeusi ambayo juu yake ilikuwa na nembo ya fuvu lililochorwa kwa rangi ya dhahabu, aliisogelea meza ile, huku mikono ikiwa inamtetemeka aliichukua bahasha ile na kuifungua taratibu na kutoa kijikaratasi kidogo kilichoandikwa kwa wino wa dhahabu.
Aliisoma karatasi ile kisha akairudisha ndani ya bahasha yake aligeuka huku na huku hakuona mtu, ‘nani ameiweka?’ lilikuwa swali lililoanza kumtia hofu. Alisahau mkataba aliousaini kule Dhaka mbele ya bwana Gonzalenz
“Bwana Kishime, hata wanadamu wa ulimwengu huu walipotaka kukombolewa, Mungu alitoa sadaka ya mwanae wa pekee msalabani, si ndiyo?”
Maneno hayo ya bwana Gonzalenz yalimrudia kichwani mwake akakumbuka saini aliyoweka juu ya faili lile lililokuwa na urembo huohuo wa kutisha, Kishime alishusha pumzi lakini hakuwa na la kufanya ‘Mkataba wa Dhaka, mkataba wa kishetani’, raha yote ilimuishia alijitupa kwenye kochi na kupitiwa na usingizi.
Sir James Washington akiwa na wenzi wake kwenye kikao cha dharula, walijadiliana mambo kadhaa hasa ya mafanikio, katika kikao hiki maalumu kilichohudhuriwa na wajumbe watano kulikuwa na hoja za kupanga na zingine kupangua, hatua za utekelezaji ziilikuwa zikijadiliwa, hatua za kuwatia umasikini Watanzania ndiyo yalikuwa mafanikio yenyewe, hatua za kufanikisha tamaa za weusi wachache wanaosahau uzalendo wao na kukubali damu ya Wananchi imwagwe kama tambiko ilikuwa ndiyo utangulizi wa yote.
Katika kikao hicho kizito pia lawama zilitawala hasa juu ya McField kushindwa kutekeleza kazi yake sawasawa na ilijadiliwa kuwa aamuriwe kurudi mara moja na kulipa pesa zote alizolipwa, hivyo basi mkutano utakaofanyika huko dar es salaam utakapoisha McField atatakiwa kulipa gharama zote walizopoteza, na kazi hiyo alipewa Francesco Gonzalenz kuitekeleza. Mkutano mzima ulipigwa mshangao kwa taarifa waliyopewa kuwa Chiwawa Chakwima ametoweka hospitalini, hii iliwaogopesha maana walijua wazi kuwa huko alikopotelea kama ni katika mikono ya serikali basi mpango wao unaelekea kutofanikiwa, walipowasiliana na Punde Kishime bado jibu lilikuwa lilelile.
“Tusisitishe juhudi na kuliogopa taifa changa kama lile, tukishindwa mbinu hii tutatumia hata mtutu lakini azma yetu itimie” J. Washigton aliwapa moyo wenzake.
“Kama tuliiweza Libya, nini Tanzania?!” aliongeza bwana Mahmoud al-Bashir, tajiri wa kiarabu aliyebobea kwenye biashara ya mafuta.
Mijadala mingi ilijadiliwa na hatima ikafikiwa kwa wageni hawa kutembelea Tanzania na kufanya mkutano na viongozi wa chama cha bwana Kishime ili kukiongezea nguvu zaidi lakini ikiwa ni fursa pia kuweza kujionea utajiri wa nchi hii unaozagaa ovyo kila kona. Kadiri ya majukumu yao walijipanga kila mtu kuondoka kwa mtindo anaoujua yeye na tarehe ilipangwa ya kukutana Dar es salaam, hawakutakiwa kuonana kabisa kabla ya siku hiyo.
Waenyeji waliopata taarifa ya ujio huo waliteuliwa wachache tu kuhudhuria mkutano huo na waliambiwa wasishughulike na lolote bali wasubiri tu kuambiwa ni wapi pa kuonana na saa ngapi, baadhi ya watu wachache kutoka mataifa Fulani ya Afrika pia walijumuishwa katika mkutano huo lakini nao walitakiwa kuingia nchini katika mtindo huohuo.
George Mc Field, hakuwa na la kufanya, kosa alilolifanya safari hii alijua wazi kuwa litamgharimu maisha yake mbele ya ujumbe huo unaokuja, hakuna nafasi ya kutupa karata ya mwisho, kama ni albastini basi alipata galasha ambalo halina kazi kwa muda huo na kama ni last card basi alilala na joker.
Aliiwaza pata potea aliyoifanya kwa tamaa ya pesa za Max Petito na asizipate, cd aliyopewa ili kumshawishi zaidi Chiwawa Chakwima naye kuchukua original ili ampatie Max Petito kwa donge nono, akijua atatekeleza aliloambiwa na James Washington, alifanya hila na kuchukua cd original akitazamia kuwa Chakwima akishamaliza kuitaza yeye angeipata kutoka kwake kwa njia yoyote ile, na hii ndiyo iliyomfanya achelewe kuitoa roho ya Chakwima na siku alipodhamiria kabisa kumuondoa Chakwima duniani ili liwalo na liwe, hakumkuta, ametoweka hospitalini. George McField aliitoa taarifa hiyo kwa aibu kubwa sana mbele ya boss wake, mara hii alijiona jinsi alivyo mpumbavu na alijua wazi kuwa ni nini kitakachofuata kwake.
Hakuna jinsi kwa kuwa alijua kuwa ujumbe ule utaingia Tanzania muda si mrefu sana na yeye ndiye anayetakiwa kuweka mazingira yote katika hali ya usalama, alidhamiria kutoweka mara tu mkutano huo utakapokaribia ukingoni.
‘Nani amemuua Max Petito? Kwa nini?’ ni swali ambalo alijiuliza daima kwa maana mtu huyo amempotezea dili la pesa za kutosha kutoka kwa tajiri huyo wa kiitaliano aliyewekeza nchini na nyuma yake akifanya biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Majibu aliyoyapata kamanda Amata kutoka kwa BIG yalimpa njia ya wapi pa kuanzia katika kukamilisha sakata hili, alirudiarudia kusikiliza ile recorder yake na kufanya upembuzi yakinifu juu ya hilo. Akiwa katika umakini wa hali ya juu kusikiliza majibu yake kutoka kwenye ile mashine aliyokuwa akimrekodi BIG aligutushwa na mkono uliomgusa mgongoni.
“Unashtuka nini?” madam S aliuliza
“Aah sikutegemea kama mtu anaweza kuwa eneo hili kwa sasa” alijibu
“Ok! Nipe mrejesho wa tafutishi zako tyoka kwa BIG,”
“Ah BIG tumempa kibano cha kutosha na ametuambia mengi sana ya kutusaidia, hata nikikwambia mengine hutoamini kabisa” akashusha pumzi na kukizima kile kimashine na kuendelea, “Unajua hata Max Petito anahusika na kundi hilo?”
“Kundi gani?” madam S aliuliza
“The Sixs”
“What?” madam S aliuliza kwa mshangao
“Habari ndo hiyo” akajikohoza, “Max Petito ni mmoja wao, lakini miaka kadhaa byuma alijitoa kutokana na kutoelewana katika mgao wao baada ya mapinduzi waliyoyafanya kule Zaire kwa kumtoa Mobutu na kumuingiza Kabila. Kutokana na hilo aliamua kuachana na The Sixs na kuja huku kujifanya mtu mwema kumbe nyuma yake alikuwa na agenda tofauti ‘kwa sauti ya kunong’ona’ Max Petito alikuwa ni muuza madawa ya kulevya mzuri tu hapa nchini mpaka nje ya mipaka”
“Amata, stop! Huyu Max marehemu, aliyejenga mashule na mahospitali, aliyejaza madawa katika hospitali vijijini?” madam S aliuliza huku akiwa na sintoamini
“Yeah, uyo huyo, alikuwa mwema kwa mbele lakini ka ndani ameua vijana wetu wengi sana kwa kuwabebesha madawa haya hatari matumboni mwao, akiwaonga pesa nyingi wahusika ili kupitisha mizigo hiyo bila tabu. Tha Sixs walivyopanga mpango wao wa kufanya haya mapinduzi hapa kwetu kwa kumtumia Mheshimiwa Kishime waliona kwanza ni kumuua Petito ili asiharibu mipango yao kwa maana mpango huu alikuwa anaujua na alitaka awaibie siri yao. The Sixs wakakodi muuaji kutoka Afrika ya kusini ambako wana ofisi yao ndogo, na ndiko huyu BIG anatokea. Lakini bado kuna vitu vinanitatanisha madam…” alimalizia Amata
“Kitu gani?”
“Nimejua mpango wa kumuua Petito umetoka wapi, lakini kwa nini Max Petito alikuwa anataka kumuua McField? Hapa kuna siri ndani ya siri, na lazima nipate jibu” Amata alimueleza madam S.
“Vizuri, hatua nzuri, sasa na Punde Kishime inabidi ahojiwe kwa kina ili tujue kama matukio haya yana uhusiano au la!” madam S alizungumza.
“Lakini yeye si alishahojiwa?!”
“Mimi siafiki kabisa majibu yake, lazima tukitaarifu kikosi kifanye kazi hiyo mara moja, kama alivyotoweka na atoweke tena ili tupate tunachokihitaji”
Amata akashusha pumzi, alimuelewa sawia boss wake anachokimaanisha, aliinama kimya kwa muda kidogo kisha akaunyanyua uso wake na kumtazama madam S.
“Madam! Sio mapema sana, maana tukilifanya hilo wananchi watashtuka sana, na inaweza ikatuharibia kazi yetu”
“Hapana, haitaathiri kazi yetu kwa kuwa nayo ni moja ya kazi yetu, kwa hiyo basi atakapomaliza ziara yake huko Dodoma wakati anarudi, utekelezaji utafanyika kwa masaa kumi tu, nimemaliza Amata nasubiri majibu” madam S aliongea kwa msisitizo huku akinyanyuka na kuelekea kwenye meza ndogo iliyokuwa na kompyuta juu yake na kuketi akiendelea kufanya kazi zake. Amata alibaki kimya, hakuwa na la kusema baada ya boss wake kutoa oda hiyo iliyohitaji utekelezaji tu. Mara simu yake iljitikisa mfukoni, Amata akaitoa na kuangalia kwenye kioo chake na kuona jina la Chiba, akaifungua kijibahasha kile kilichojichora pale juu.
“Anaongea peke yake…” ujumbe ulisomeka namna hiyo, haikuchukua muda kuelewa maana ya maneno hayo, kwa haraka aliujibu “Usipoteze nafasi,” kisha akautuma.
9
George McField, akiwa ndani ya vazi lake jeusi hakuna mtu aliyemjua kuwa kiumbe kilichopo ndani ya vazi hilo ni mwanaume, alijivika juba, kininja kama wanawake wa kiislam, aliketi katika ukimya mkubwa sana hakuongea na mtu yeyote miongoni mwa wale walio jirani nae.
Dr. Kazumari aliiona hali tofauti ya kijana huyu muuaji wa kimataifa ambaye kwake alitambulishwa kama mwanadiplomasia katika hiyo safari ya Kishime, alimtazama bila ya kummaliza.
“Vipi kijana?” alimtupia swali la haraka haraka
“Hapana, niko sawa, najaribu tu kuangalia mazingira na ugumu wa kazi” alijbu kwa kiingereza fasaha kabisa. Alinyanyuka kutoka pale alipoketi na kuiendea simu ya mezani, kwa ishara ya mkono akamuita kijana mmoja kati ya wale walioketi pale.
“Sikia, tunafanya kama siku ile, nakupa namba unapiga halafu unaongea kwa kifupi maneno haya kwenye karatasi,” McField alimueleza yule kijana. Simu ikapigwa kwa namba zile alizopewa na mara akasikia muito wa simu ile upande wa pili.
“…kwa kuwa umeshindwa kutekeleza kile tulichokwambia kupitia barua yetu, sasa hutoliona jua la kesho…” simu ile ikakatwa. McField akashusha pumzi.
“Sikia Dr, Amata na kundi lake wameshafika mbali sana kutuchunguza, kitu ambacho mimi sikukitegemea kama kingewezekana kwa nchi kama hii, kila tulikofanya kazi ka hii mafanikio yamekuwa ni makubwa sana, na serikali haikupata nafasi ya kututambua, lakini hapa naona wazi mambo ni magumu” McField alimwambia Dr Kazumari ambaye alikuwa amesimama mbele yake akimuangalia.
“Kwa hiyo unasemaje?” Dr kazumari aliuliza
“Amata inabidi apotezwe haraka iwezekanavyo.”
“Ok, sasa sikia, kumpata Amata si kazi ngumu, naujua udhaifu wake toka nikutoke,” McField alionekana kuvutiwa na hili, “Niambie!” aliongea huku akisimama vizuri
“Kamanda Amata ni mbovu sana kwa wanawake, tukimtega hapo tu tumempata” Dr Kazumari alitoa kile anachokijua juu ya Amata.
“Ok, kama ni hivyo hiyo ni kazi ndogo sana,” Mc Field alitabasamu japo hakuna aliyeliona tabasamu lile kutokana na juba alilolivaa mpaka usoni.
ITAENDELEA
Mwanamke Mwenye Juba Jeusi Sehemu ya Tano
DOWNLOAD: Kontawa Ft Maua Sama – Sikuachi
Also, read other stories from SIMULIZI;