Mauaji ya Kasisi Sehemu ya Nne
KIJASUSI

Ep 04: Mauaji ya Kasisi

SIMULIZI Mauaji ya Kasisi
Mauaji ya Kasisi Sehemu ya Nne

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE


Simulizi : Mauaji Ya Kasisi

Sehemu ya Nne (4)

Ndani ya Dagoreti corner super pub, Kamanda Amata aliketi karibu kabisa na kaunta wakati Ndege alibana kule kunako mlango wa kuiingilia wateja wote. Mbinu hiyo ilitegwa mahsus kuwakamata wale waliomuua Rose Kahaba, Amata na Ndege walijiua wazi kuwa katika sakata hilo nguvu ya watu wawili ingetosha ilimradi tua mnajipanga kitaalamu. Kamanda Amata alitembea taratibu kuelekea mbele kabisa ya pub ile, akavuta kiti na kuketi. Mhudumu alipokuja alimkuita Amata amekwishaketi.

“Nikusaidiwe nini kaka?” Mhudumu huyu mwenye lafudhi ya Kimombasa alimuuliza Kamnada Amata pale alipoketi.

“Nipe Tusker light,” Amata alijibu, alipokwisha letewa alimsubiri yule aliyemhitaji katika pub hiyo. Melchior Ndege aliketi meza ya mlangoni kabidsa akisubiri aone kile kitakachoendelea kwa kamanda na hao wageni wake.

Ndege aliiona Toyota Spacio moja ikiegeshwa mbele tu ya pub hiyo , akaikazia macho sana na kuwaangalia watu wanaoshuka kuingia ndani ya pub hiyo. Vijana wawili mashababi, wakateremka na kuongeza mambo machache kasha wakaingia ndani na kuelekea moja kwa moja sehemu walioelekezwa, Kamanda Amata akawapa ishara aliyowaambia, wakamfuata na kuketi pembeni yake. Mhudumu wa puba hiyo akaja, vikaagizwa vinywaji na nyama choma za kufa mtu.

“Niambieni kazi ilikuwaje?” Amata alianzisha mazungumzo

“Ah boss, kazi ilikuwa easy tu, tulimkuta anaoga tukammalizia huko huko!” mmoja alijjibu

“Hamkupata upinzani wowote?” kamanda aliendelea

“Hatukupata boss, ila boss mwanamke mzuri kama Yule kwa nini ulitutuma tukatishe maisha yake kinyama vile?” mwingine aliuliza swali lisilo na tija. Kamanda Amata alimtazama kwa jicho kali.

“We unaijua kazi yako?” alamwuliza. “Ndiyo,” naye akajibu

“Yule mwanamke mzuri kwa sura lakini si mzuri kwa roho, kama mlimuua bila kumbaka basi mmekosa utamu alionao,” Amata aliposema hayo wote wakacheka.

“Ilo muhimu boss,” Yule wa kwanza akasema. “Dah! Aisee nyi mna dhambi kweli yaani mmembaka hivihivi halafu ndo mkamuua, au kwa sababu alikuwa anaoga mkamtamani?” kamanda Amata alizidi kuwafurahisha wale vijana.

“Sasa Boss, si hatutaki kukaa sana si unajua Nairobi imechafuka sasa hivi,” jamaa alimwambia Amata.

“Usijali, nataka mnipeleke mlipomfukia Yule Malaya, malipo yenu nayafanya sasa hivi kama ifuatavyo,” Kamanda Amata akavuta briefcase yake ndogo na kuifungua, akavuta bulungutu moja la pesa na kumpa kila mmoja la kwake, “Sina haja ya kuhesabu kwani najua kazi mloifanya ni kubwa,” aliwaambia. Vinywaji vilizidi kuteketea kati yao, na walipomaliza.

Walijipanga kuondoka. Melchior Ndege, alikuwa kwenye meza moja karibu kabisa na mlango wa kutokea nje, alimuona Kamanda Amata akinyanyuka na wale vijana, alijua wapi wanaelekeakea kwani mazungumzo yao yote alikuwa akiyasikia kupitia earphone zake ndogo alizopachika sikioni zikiongozwa na kinasa sauti ambacho Kamanda Amata alikipachika kama moja ya kifungo cha shati, haikuwa rahisi kwa mtu wa kawaida kugundua hilo mara moja. Akawatazama walipokuwa wakija taratibu huku wakiongea akawaruhusu wapiti pale alipoketi na kuilekea ile Toyota Spacio.

Mara simu ya mmoja wapo ikaita, akaitoa mfukoni na kuitazama kiooni, private number, akaipokea na kuongeza na mtu wa upande wa pili.

“Yeah, nimewapa kazi mbona hamnijulishi kinachoendelea?” sauti ya mtu wa upande wa pili iliuliza.

“We ni nani, na kazi gani ulitupatia?” Yule kijana akauliza. Kamanda Amata alishajua nini kinaendelea katika majibizano hayo, akajiandaa kwa litakalofuata, huku Ndege akiwa bado ameketi kataika kiti kilekile alikuwa akiangalia nini kitaendelea.

Baada ya kuongeza na ile simu, akashusha mkono wake na kumgeukia Amata, akiwa mekunja sura kama mtu aliekula pilipili pa si kutarajia, alifyatua ngumi kumuelekea Amata, lakini akamkosa kwa kuwa Amata aliepa kwa ustadi sana.

“Nini kijana mbona unarusha ngumi bila taarifa?” Amata aliuliza.

“Bastard! Unajifanya wewe ndo ulotupa kazi kumbe sio?” alilalama Yule jambazi.

“Kama si mimi kwa nini nimewalipa? Basi twendeni kwa huyo anayesema yeye ndo kawapa kazi, mtakuja kukamatwa na polisi bure,” Amata aliwaambia, wale jamaa wakabaki wamrchanganyikiwa hawajui lipi la kufanya, nani boss nani tajiri, wakatazamana, “Samahani Boss” mwingine aliyekuiwa kasimama pembeni akajibu. Kisha wakaingia kwenye gari pamoja na Amata, safari ikaanza.

Baada ya kukata mitaa kadhaa wakaliacha jiji la Nairobi na kuchukua barabara ya kuelekea Kisumu mpaka njia panda ya Kinangop, wakapita Soko mjinga na kusonga mbele kama kilomita tano hivi, wakachepuka na kuingia kushoto barabara ya vumbi mwendo mfupi wakasimama, “Aisee, mmemzika mbali hivi?” Amata aliuliza, “Ah boss, umesahau kama ulituagiza tumlete huku,” akajibu mmoja wao.

“Ah, nshasahau aisee,!” Amata alijibu baada ya kujigundua kuwa amejisahau. Wakafika eneo lile walilomfukia Rose, Amata alinyamaza kimya mara wakasikia majani yakitaikisika na mtu mmoja akaibuka kama ninja.

“Hapo hapo mlipo, mikono juu,” Yule mtu aliamuru. Hawakuwa na ujanja walikubaliana na hilo wote wakaweka mikono yao juu.

“Tunawatafuita sana wauaji kama ninyi, fukua hapo!” aliamuru Yule mtu, kamanda Amata akiwa mikono yake iko hewani alijua wazi kila kinachoendelea, akatulia kimya, wale vijana wakaonekana jinsi wanavyotetemeka. Mara taa za gari zikamulika upande ule zikimaanisha kuna gari ambayo ilikuwa inakuja pale walipo. Polisi watatu waliteremka wakiwa na pingu mkononi mwao, wakawafunga wote pamoja na Kamanda Amata, kasha wakawapakia katika Land cruiser yao wakawapakia, Yule aliyewakamata kwanza akavua soksi aliyoivaa kichwani na kuruhusu sura yake kuonekana, Melchior Ndege alikuwa kasimama mbele yao.

“Fukua hapa,” Ndege akawaamuru vijana waliokuja na gari ya polisi, wakafanya hivyo na kuukuta mwili wa mwanamke kwenye mfuko mkubwa wa plastiki, ‘Ukatili gani huu,’ Ndege alijiuliza kichwani mwake.

§§§§§

Wambugu, alibaki kujiuliza maswali mengi, vijana aliowapa kazi walikuwa hawajarudi kumpa taarifa, alipowapigia akagundua wazi kuwa hakuna uelewano kati yao. Aliendelea kuketi pale kitandani akijiuliza la kufanya, tayari alikwishajua kuwa kuna mchezo umechezwa kati yake na vijana wake. Akinuka na kulisogelea dirisha, moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, aliona siku zinavyozidi kwenda ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya, alihaha, sasa alibaini wazi kuwa Bill alikuwa msaliti mbaya kuliko msaliti wa kawaida. Akachukua rimoti na kuwasha tv, habari ya saa mbili usiku ilikuwa ipo katikati lakini alibaki mdomo wazi kwa habari aliyokuwa anaiona mbele yake, habari ya kukamatwa kwa jamabazi sugu la kike lililowasumbua polisi kwa miaka mingi, Mellina.

Wambugu hakuamini anachokiona mbele yake, ‘Mellina katika mkono wa dola’ alijiwazia akiwa kasimama huku kajishika kiuno, ‘bass hapa usalama hakuna tena usalama,’ akazidi kugubikwa na mawazo. Wambugu akaamua kutoroka maana alijuwa wazi kuwa endapo Mellina atabanwa vya kutosha lazima atataja, alifunga kibegi chake harakaharaka akaweka kila anachoona kinafaa katika kibegi chake akakiweka mgongoni, bastola yake akaipachika kiunoni na ikafunikwa kwa jacket alilokuwa amelivaa, akauacha mlango na kutoka nje ya gesti hiyo a,liyopanga na kutokomea mtaani.

Gari moja nyeupe ilisimama kando mwa gest hiyo, kijana mmoja shababi, akashuka na kuiendea kaunta ya nyumba hiyo, “Mwenyeji wangu yuko chumba namba saba,” alimwambia Yule mhudumu pale kaunta.

“Chumba namba saba leo hakina mtu, tayari ame-check out,” Yule dada alijibu.

“Amecheck out? Lini?” Kamanda Amata akauliza.

“Yaani hata masaa mawili hayajaisha,” Yule dada akamueleza, Amata alipita kwenye korido mpaka katika kile chumba na kumkuta mtu wa usafi akifanya kazi yake. Akarudi kaunta, hana la kusema, akarudi kwenye gari. “Vipi?” Ndege akamuuliza.

“Jamaa kaondoka, hayupo hapa, tena wanasema kuwa ni kama masaa mawili yaliyopita” Amata na Ndege walikuwa hawana la kufanya.

“Ningempata huyu mshenzi leo, ndo angenipa uelekeo wa Bill yuko wapi!” Kamanda Amata alimwambia Ndege.

“Usikate tamaa braza, tutampata ndani ya masaa ishirini na nne, mimi ndiyo ninayoijua Nairobi na Kenya yangu,” Ndege alijibu huku akigeuza gari na kutrudi mjini.

“MADAM S, Kamanda Amata yupo Nairobi, kwa habari tulizozipata kutoka kwa watu wetu huko,” Chiba alimwambia Madam. Madam S alitikisa kichwa kutokana na kujua hilo kwa kuwa tangu muda mrefu alihisi kwa vyovyote atakuwa huko.

“Vizuri sana Chiba, sasa mpelekee taarifa mwambie namhitaji haraka sana ofisini.” Madam S alitoa amri.

Ilikuwa ni usiku ambao Madam S alibanwa na kazi nyingi, akikumbuka kikao chake cha machana na watu wengine wa idara ya usalama wa taifa alihisi jambo jipya hasa kutokana na kutoroka kwa Amata hospitali na kwenda kusikojulikana. Walimtuhumu kuwa ni mtovu wa nidhamu, asiyejali yale anayoambiwa na wakubwa wake, wote kwa sauti moja wakaona Kamanda Amata anyang’anywe cheo chake hasa kutokana na uzembe anaouonesha kwenye kazi za maana kama hizo. Ijapokuwa mvutano ulikuwa mkubwa sana kati ya wana kikao, lakini mtu mmoja alionekana kushikia bango sana kamanda ashushwe cheo, kwa kuwa hafai tena, lakini kabl;a ya yote atafutwe, arudishwe kasha apewe barua ya kushushwa cheo na abadilishiwe idara.

Kichwa kilizunguka, Madam S alibaki njia panda, hoja imepitishwa lakini bado moyoni mwake anamhitaji sana maana alijua wazi kuwa hakuna mtu anayeweza kushika nafasi hiyo ngumu. Atafanyaje, lazima afuate maamuzi ya kikao, Madam S alianza kuwaza kustahafu kazi endapo Kamanda Amata atashushwa cheo, amtetee vipi? Aliumiza kichwa kwa hilo. Alipoona hapati jibu kwa hilo, aliamua kuachana nalo, ataona wakati ukifika, alijipanga kwa safari ya Nairobi ili akakutane na Kamanda, waongee wamalizane hukohuko, aliamua kufanya safari hiyo kwa siri sana, asijue mtu yeyote.

Akafunga ofisi na kuondoka zake kujipumzisha nyumbani kwake Masaki. Hakuwa na muda wa kupoteza, alipotoka tu ofisini aliwasiliana na watu wa uwanja wa ndege akapata ndege yashirika la Swiss ambayo ilikuwa iondoke saa nne usiku huo kuelekea Zurich, kwa kuna watu waliokuwa wapandie Nairobi, kwa heshima yake alipatiwa siti moja kwa bei ya kawaida yenye punguzo la asilimia 25. Aliweka kibegi chake cha mgongoni tayari, nguo chache na vitu muhimu, bila kusahau kikoba cha vipodozi. Bastola zake mbili aliziandaa tayari kwa safari hiyo, alipohakikisha yuko poa alijiswafi kidogo kisha akajitupia jeans moja kali na fulana nyeuzi kichwani nakavaa kapelo nyekundu iliyomrudisha katika ujana kwa kila atakayekutana naye.

Saa nne kasoro robo ilimkuta uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, akaegesha gari yake mahala pa usalama ndani ya uzio wa uwanja huo kwa kibali maalumu kisha akingia ndani katika eneo la kuondokea wasafiri. Akatoa hati zake na kumkabidhi mwanadada aliyekuwa hapo kwa kazi hiyo.

“Ooh, karibu sana, tulikuwa tunakusubiri wewe tu, watu wote wako tayari kwenye ndege,” alizungumza Yule mwanadada aliyevalia nadhifu kabisa alimkaribisha Madam S na kuingia nae ndani moja kwa moja kwenye ndege hiyo ya kisasa kabisa, alimuonesha siti yake na Madam akaketi tayari kwa safari, baada tu ya yeye kuwa ameingia, ndege ile ilijitoa katika vizuiz vyake ikisukumwa na gari kubwa kuipeleka barabarni.

§§§§§

NDEGE na Kamanda Amata walikuwa wameegesha gari yao pembezoni mwa jengo la Posta katika mji wa Nairobi, wakijadiliana hili na lile jinsi ya kumnasa Wambugu. Kamanda Amata alichukua simu ya Wambugu, simu ya kisasa kabisa akaigeuzageuza na kumtazama Wambugu, “Unamjua Wambugu kwa sura?” akamuuliza.

“Hapana, sijawahi hata kumuona, hata hilo jina ni geni sana kwangu,” Ndege alijibu. Kamanda Amata akaichukua namba ya Wambugu na kuiingiza katika simu hiyo, akaiunga kwenye mtandao wa internet, kisha akaingiza nambari Fulani Fulani na kufungu mtandao wa usalama wa Tanzania, akaingiza ile namba pamoja na jina Wambugu katika na kujaribu kufananisha vitu hivyo. Haikumchukua muda mrefu simu hiyo ilimpa majibu, namba, jina na picha vyote vitatu vilionekana kwa wakati mmoja na maelezo mengine kedekede.

“Ndege!” Amata aliita na kumpa ile simu, “Unahisi huyu anaweza kuwa ndiye?” akamuuliza, Nege akaitazama ile picha kwa makini sana akatikisa kichwa.

“Naijua sura hii vizuri, ni moja kati ya wahalifu wanaoisumbua serikali,” Ndege alijibu huku akiirudhisha ile simu kwa Kamanda, kamanda Amata akaihifadhi ile picha katika sehemu maalumu kwa kazi hiyo ndani ya simu ile. Kisha akafunga ule mtandao na kurudisha simu katika hali ya kawaida, hakuishia hapo, “Ndege, piga simu kwa jamaa yako wa kampuni ya simu, atuambie simu tatu za mwisho za Wambugu zinasemaje tunaweza kupata majibu ya shaka letu.” Ndege akaichukua ile simu na kufanya hivyo kisha wakasubiri jibu watakaloletewa. Haikuchukua muda ukatumwa ujumbe wa sauti katika simu hiyo, Ndege akaufungua na kusikiliza, hawakukosea, ilikuwa sauti ya Bill ikimtaka Wambugu aende Iryamurahi akajifiche huko.

“… najua kuwa una mahangaiko makuu, najua kuwa Mellina amekamatwa, sasa sikiliza, na husijibu simu hii bali tekeleza unaloambiwa, ondoka haraka Nairobi kwa njia za siri unazozijua wewe, njoo Iryamurahi utanikuta hapa, kisha tupange mpango kabambe wa kuondoka katika nchi hii, nakusubiri, ukifika hapa mjini nitakupigia…”

Ilikuwa ni mwisho wa ujumbe ule wa sauti.

“Ina maana Bill yupo Iryamurahi?” Ndge aliuliza kwa mashaka, huku akiwasha gari na kuliingiza barabarani kuchukua barabar ya kueleka Embu.

“Ndege, Bill ni jasusi la kimataifa, hawezi kukaa nchini kwako wakati kazi aliyopewa imekwisha,” Amata alimjibu Ndege, akaichukua tena simu ya Ndege nakuanza kufanya utundu mwingine wa kupata uelekeo ambao Wambugu atakuwepo kwa wakati huo.

“Unafanya nini?” Ndege akauliza.

“Natafuta uelekeo wa Wambugu atakuwa wapi, kama katoka Nairobi au bado hajatoka tusije tukapoteza muda,” Kamanda Amata alijibu.

“Hiyo kazi ndogo Kamanda, piga simu kwa huyo jamaa atatuambia point gani alipigia simu mara ya mwisho na sasa atakuwa maeneo gani kadiri ya signal inavoonesha,” Ndege alimuelekeza Kamanda.

“Ndege acha kutumia njia za kianalogia hizo, sasa hivi namtafuta kwa GPS na nitakwambia alipo,” Kamanda Amata akaiweka simu katika program ya GPS akajaribu kuingiza namba za Wambugu na kuitafuta simu anayoitumia, jibu likaja, ikatumwa namba ya IMEI ya simu ambayo kwa wakati ule ilikuwa imebeba sim card ile, akaendelea na utundu wake mpaka akaweza kuunganisha mtandao huo, taraytibu ramani ya Nairobi na vitongoji vyake ikaonekana katika kioo cha simu hiyo, kidoti chekundu kikatua katika maeneo ya Juja. Kamanda Amata alicheka kwa ushindi huo.

“Wambugu hayupo mbali sana,” Amata alimwambia Ndege, akamtajia na vpimo vya ardhini kabla hajamaliza Ndege akamwambia hilo ni eneo gani.

Gari ikaongeza moto kuelekea barabar ya Embu kumuwahi Wambugu, “Tusifanye lolote, twende nae mpaka Iryamurai tukaone kuna nini,” Kamanda Amata alimwambia Ndege aliyekuwa katika usukani akiendesha gari hiyo kwa kasi ya ajabu.

“Kamanda, kimpata Bill utamfanyan nini?” Ndge aliuliza swali la kizushi.

“Sijui, ila shetani anajua maana nina hasira nae, na nitamfuata popote alipo katika dunia hii, mpaka nimtie mkononi,” Amata alijibu. Wakati huo walipita maeneo ya Kasarani na kuendelea kuikanyaga lami kusonga mbele.

§§§§§

Saa sita usiku, ndege ya Swiss ilikanyaga ardhi ya Nairobi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta. Madam S alikuwa ni mtu pekee aliyeshuka katika ndege hiyo, aliwashukuru wafanyakazi kwa ukarimu wao na kuzishuka ngazi hizo kwa fujo. Alipomaliza itifaki zote, alitoka nje lutafuta usafiri wa kwenda mjini.

“Karibu Madam, karibu sana Nairobi,” ilikuwa ni sauti ya kiume iliyotokea kwa nyuma yake, madam alisita kwa kuwa hakutegemea kupata ukaribisho wa aina yoyote hapo Nairobi, mkono mmoja ukiwa ndani ya jacket aliloliva muda mfupi uliopita katika kukabiliana na baridi ya Nairobi, aligeuka nyuma na kumuona kijana huyo mwembamba mrefu, sura yake haikuwa ngeni sana machoni, alimtazama tena na tena kisha akamkubuka, “Mashaka?” alimuuliza.

“Ndiyo, Mashaka, kutoka ubalozi wa Tanzania,” alijibu Yule kijana ambaye jina lake ni Mashaka, alietumwa miaka kadhaa nyuma kufanya kazi za idara ya usalama katika ofisi za ubalozi wa Tanzania huko Kenya.

“Kwangu?” Madam aliuliza.

“Ndiyo,” Yule kijana akajibu, kisha madam akaondoka eneo lile na kuelekea kunakoegeshwa tax, akaingia na kuketi ndani, Yule kijana akarudi na kuingia kwenye gari binafsi nyingine. Dereva wa tax hiyo akageuka nyuma na kumtazama Madam S, kabla hajaongea chochote Madam S alimwambia, “Safari Park Hotel,” kisha akampa noti tatu za shilingi elfu moja moja za Kenya, safari ikaanza.

Kwa kuwa ni usiku haikuwa tabu na wala haikuchukua muda kwao kufika katika hotel hiyo. Akiwa ameketi katika gari hiyo mara alihisi mfinyo katika mkono wake wa kushoto, akauinua na kuitazama saa yake kisha akabofya kitufe Fulani, mara mkanda mwembamba ukatoka kwa chini ukiwa na maadishi Fulani, akausoma na kuukata kisha akautia kwenye mfuko wa suruali.

‘…Kamanda Amata yupo Nairobi, kwa sasa yupo barabara iendayo Embu akielekea upande wa kaskazini, nimemnasa pindi alipotumia mtandao wetu wa usalama kwa kupitia nywila yako. Chiba…’

Ulikuwa ni ujumbe uliokuwa katika kijimkanda hicho. Madam S alikunja sura, ‘mshenzi kabisa Amata, kaipata wapi password yangu?’ alijiuliza.

Ilimbidi Kamanda Amata kutumia password ya Madam S baada ya kugundua kuwa ile yak wake ilikuwa imefungwa hivyo hakuweza kuingia kwenye mtandao wa usalama wa Tanzania, alijaribu kuibuni password ya Madam S mara mbili, mara mbili ya tatu akaipata na kuingia kwa kutumia jina hilo, baada ya kumaliza kazi hiyo ndipo Chiba alipojua kuwa kamanda Amata yupo Nairobi kwa jinsi alivyokuwa akichukua data ambazo zinaendana na kazi aliyotumwa tangu mwanzo huko Nairobi.

Ubalozi wa Tanzania huko Kenya kupitia mtaalamu wa mawasiliano aliyepelekwa kwa ajili ya kublock password zilizoibwa na Bill, Frank Masai aligundua kuwa muingiliano huo uliotokea Nairobi kwa vyovyote madam S alikuwapo hapo, alipowapa taarifa hiyo wengine wakafanya uchunguzi wa haraka na kugundua kuwa Madam S yupo njiani kuja hapo Nairobi, hivyo wakamtuma Mashaka kumuwekea ulinzi kutokana na hali halisi ilivyo katika jiji hilo.

Madam S aliweka kambi katika hotel ya Safari park, alihakikisha kila kitu kipo salama, na kupanga jinsi ya kumsaka Kamanda Amata kwa udi na uvumba. Aliifungua laptop yake ndogo na kuingia kwenye mtandao wa idara ya usalama, kwanza akaangalia ni nini Kamanda Amata alikuwa akifanya katika mtandao huo, akasoma maelezo ya Wambugu na kuitazama picha yake, akaangalia na maelekezo mengine mengi, akaichukua namba ya simu iliyojitokeza hapo ambayo Amata aliitumia kuchukua maelezo hayo, akatabasamu na kumsifu Amata kimoyomoyo kwa jinsi alivyokuwa mtundu wa kufikiri pindi anapohitaji maelezo Fulani. Alikumbuka jinsi anavyoweza kuiga sauti na saini za watu pindi anapohitaji kufanya hivyo, hakushangaa kusikia kuwa ameweza kupenya mtandaoni kwa kutumia password yake.

Alijiuliza mwenyewe, nani anaweza kukaa katika cheo cha Kamanda Amata na akatosha katika kila idara, mapambano ya mikono, utumiaji wa silaha za aina na aina, lugha za kutumia, utundu wa kuendesha vyombo vya ardhini, majini na angani, utundu wa kuiga sauti za watu, saini za watu, vyote hivi nani angeweza, kama isingehitajika watu wawili au zidi kufanya kazi ya mtu mmoja. Jambo moja tu lililomuuzi ni wanawake, Kamanda Amata alikuwa mdhaifu sana mbele ya mwanamke, na adui zake wengi walimuweza kwa hilo tu, walimkamata kwa hilo tu. Lakini bado walipokuja kuona jinsi na njia aliyotumia kutoroka walibaki hoi. ‘Kamanda atabaki kuwa Kamanda tu,’ Madam S alijisemea huku akiifunga laptop ile ndogo na kuirudisha mahala pake.

EMBU – KENYA

EMBU, mji uliopo kilomita takribani 120 kutoka Nairobi, upande wa Kaskazini mashariki kuelekea mlima Kenya. Ukifika miezi ya kumi na kumi na moja utafurahi kuona barabara na viunga vyake vilivyopambwa kwa maua ya rangi ya zambarau kutoka katika miti ya Jacaranda.

SAA 4:15 USIKU

MAINA HIGHWAY HOTEL

KWA KUTUMIA mwendo wa miguu, Wambugu alivuta hatu kuelekea katika hoteli hiyo iliyopo katikati ya mji katika mtaa ya Haille Selasie, moyoni mwake alikuwa na amani sana kuwa sasa kafanikiwa kulitoka jiji la Nairobi. Akitegemea kukutana na mtu wake, Bill siku inayofuata huko Iryamurai, kabla hajaifikia kaunta ya hotel hiyo simu yake ikatikisika mfukoni mwake, akaitoa na kuitazama, private call, ilijiandika, hakuipokea akaenda kaunta na kuchukua chumba.

Akiwa ndani ya chumba chake Wambugu aliiona tena simu yake ikiita, akainyakua na kupoke,

“Wambugu, nikipiga simu upokee mara moja, unafuatwa, hapo mahali si salama, ondoka mara moja, nenda utafute sehemu salama,”

Ile simu ikakatika, Wambugu akabaki ameduwaa, hajui la kuamua, ‘Nani ananifuata?’ alijiuliza, ‘Bill amejuaje?’, ulikuwa ni wakati mgumu sana kwa Wambugu kufanya uamuzi, kwa kuwa alikuwa akijiandaa kuoga, ilibidi aahirishe zoezi hilo na kujipanga kutoka katika hoteli hiyo, alirudi kaunta akiwa kaweka mkono wake mfukoni, kashikilia bastola tayari kwa lolote ambalo litatokea. Alikabidha funguo na kuaga kuwa atarudi muda si mrefu. Alitoka na kuzishuka ngazi kadhaa za mlango huo na kupotelea kwenye kichochoro Fulani ambacho kilimleta katika maduka na mchanganyiko wa watu, ‘niende wapi?’ akajiuliza, hakupata jibu, usiku ulizidi kuwa mnene, kichwa kikimuuma, mawazo yake yakivurugika, mipango ikigoma kupangika, ulikuwa wakati mgumu.

Wambugu alivuta hatua ndogo ndogo kuelekea kituo cha tax, pale alizikuta tax chache zinazongoja abiria wa usiku, akiwa kutahamaki hivyo mara gari moja aina ya Jeep Cherokee ilisimama ghafla miguuni mwake, mlango ukafunguliwa kwa haraka na Kamanda Amata akatoka bastola mkononi, Wambugu akajua hapo kazi nzito, alipiga risasi moja kwenye kioo cha dereva, wakati Kamanda Amata anazunguka gari kiufundi ili kumfiikia Wambugu, kumbe mwenzake alishaliona hilo, akalala chini na kupita uvungu wa gari akatokea upande wa pili kisha risasi mbili zilifumua matairi nay a tatu ikalenga tank la mafuta. Kamanda Amata alipogeuka nyuma alishuhudia ile gari ikipaishwa juu kwa mlipuko huo, akajishika kichwa kwa sekunde kadhaa kisha akaikimbilia ile gari na bila kujali, alifungua kwa taabu mlango wa dereva, na kumtoa Ndege ambaye alipigwa risasi begani na Wambugu, akamvuta na kumtoa nje, hali ya Ndege haikuwa nzuri kwani jeraha la risasi na ule moto almanusura vimmalize. Haikuwa na aja ya kumtafuta Wambugu aliomba msaada wa wananchi na kumkimbiza hospitali ya Agha Khan.

Wambugu baada ya kuona kafanikisha hilo, alikimbilia kwenye viunga vya mji na kutokomea mbali kidogo na mji. Alitembea polepole na kutafuta mahali pa kujihifadhi usiku huo maana aliona sasa hakuna sehemu yanye usalama kwake.

Polisi wa Embu, walifika katika hospitali hiyo na kukutana na Kamanda Amata aliyekuwa pembeni mwa kitanda cha Ndege wakati mwenyewe akiwa katika chumba cha upasuaji.

“Tunataka tujue ni nani jambazi na nina mwanausalama?” askari mmoja alieonekana kuwa ndio mwenye sauti aliuliza. Kamanda Amata alimtazama kwa tuo askari huyu aliyeonekana anajua sana kuongea. Akamuonesha kitambulisho chake, lo, Yule askari alilowa ghafla na kutoa salamu ya kiaskari kwa ukakamavu wa hali ya juu.

“Sasa sikia, kuna jambazi hili hapa,” akachukua simu ya Ndege na kumuonesha ile picha, Yule polisi akashtuka kidogo na kushangaa akiwa kakunja ndita si kitoto, “Huyu, kafika hapa, ni mtu hatari sana tunamtafuta nchi nzima mpaka nje ya mipaka, ok sasa kama unaruhusu nianze doria usiku huu,” Yule polisi alimueleza Kamanda Amata, baada ya kufikiri kidogo, akaona hiyo ni njia nzuri ya kujua ni wapi huyo mtu anaweza kuwapo. “Ok, hakikisheni mnampata akiwa hai maana kuna maelezo nayataka kutoka kwake,” Yule askari alipopokea hiyo amri, akapiga saluti na kuondoka.

Usiku huo mchakamchaka ulianza, kila kona kila mtaa ni gari za polisi kumsaka Wambugu. Kila nyumba ya wageni ilipekuliwa usiku huo na akila aliyefanana alibebwa na kupekwa kituoni.

Melchior Ndege alirudishwa wodini baada ya lisaa limoja kwa oparesheni iliyofanikiwa sana ya kuitoa risasi iliyokwama katika mifupa ya bega lake la kulia, majeraha ya moto hayakuwa mabaya sana, aliweza kuongea kama kawaida japo chupa ya damu ilikuwa ikiendelea kuingia mwilini mwake.

“Kamanda! Siwezi tena,” alimwambia kamanda Amata kwa sauti ya chini kidogo, wakati huo Kamanda Amata alikuwa ameketi kwenye kiti jirani kabisa ya kitanda kile,

“Kwa nini kaka? Tupo pamoja usijali,” Amata alijibu.

“Sikia, nina hasira sana na Wambugu kama wewe ulivyo na hasira na Bill, nenda kamsake popote alipo, nitapona tu nikisikia kuwa umempata na umemtoa roho, nenda Kamanda kamalize kazi kabla hawajajua kuwa tuko pamoja,” Ndege alimueleza maneno hayo Amata. Wakapeana mikono, Kamanda Amata akatoka pale hospitali na mlangoni wakakutana na Yule polisi, “Vipi?” alimuuliza, lakini Yule polisi hakujibu kitu, nyuma yake kulikuwa na polisi wengine watatu, “Kamanda Amata, upo chini ya ulinzi kwa kuwa unaifanya kazi hii kinyume cha sheria,” Yule polisi mkubwa akasema hayo, “Nani aliyekwambia?” Kamanda Amata akauliza, “Tumepata taarifa kutoka makao makuu ya polisi Nairobi kwa uthibitisho kutoka katika ofisi yako huko Tanzania, twende kituoni,” Yule askari alimuamuru Kamanda. Kamanda Amata hakuwa na ubishi, alitii sheria bila shuruti, akapakiwa katika gari na kuondolea hospitalini hapo.

Wambugu alipoona hali si nzuri, polisi kila upande alijua kuwa sasa mambo yameharibika, alichomoka kutoka maficho yake na kutega barabara kuu kuona kama kuna gari litakalotokea. Mara akaona pikipiki ikija upande wa kulia kwake akaokota jiwe na kumpiga nalo Yule mwendesha pikipiki, kisha akajitokeza barabarani na kuokota ile pikipiki, akakaa juu yake na kuitia moto, akaondoka kwa kasi kubwa.

Gari iliyokuwa imemchukua Kamanda Amata ilikuwa ikipita barabara hiyo na mara wakaiona ile pikipiki ikija kwa kasi sana, dereva akapunguza mwendo kuona ni nani huyo, “Msimamishe tafadhali,” Yule mkuu akamwambia polisi mwingine, ambaye kwa haraka aliruka chini na kutua barabarni kisha akasimama katikati ya barabar kumsimamisha jamaa huyo, lakini akiwa katika hali hiyo, mlio wa risasi ukasikika na mara Yule polisi akawa chali barabarani, Kamanda Amata akatzama huku na huku akishuhudia Yule dereva akishuka kumsaidia mwenzake, akaruka upande wa mbele kwa dereva na kuigeuza gari kwa fujo kuifuata ile pikipiki, mwendo uliokuwa ikiendeshwa hiyo land cruiser haikuwa ya kitoto, Kamanda Amata alikanyaga mafuta kwa ustadi wa hali ya juu, akaiona ile pikipiki ikikata kushoto na kuingia barabara nyingine nae alipofika pale vivyo hivyo akakunja kuelekea kushoto akiendelea kuifuata ile pikipiki.

§§§§§

Usiku wa manane, Madam S alipata taarifa ya kukamatwa kwa Kamanda Amata, taarifa zilitoka katika ofisi za ubalozi usiku huo, likaandaliwa gari kwa ajili ya kwenda Embu kutoka ubalozini kwa minajiri ya kumchukua Kamanda na kumrudisha Tanzania. Aliamka kwa kusuasua, na kujiandaa, alipokuwa tayari aliteremka kwa lifti mpaka chini ambako aliikuta gari hiyo ikimsubiri, akaketi kiti cha mbele na kuanza safari na watu wengine wawiliyaani dereva na Mashaka, Yule kijana waliekutana pale uwanja wa ndege.

Upande mwingine bwana Shikuku alishtushwa na taarifa za kijana wake Ndege kupigwa risasi na Wambugu pia kupata ajali ya moto uliosababishwa na mtu huyo huyo, moyo ulimchafuka na usiku huo akapanga safari yake ya kwenda Embu kujua nini kinaendelea. Akiwa njiani alikuwa akijaribu kuwasiliana na watu wa usalama upande huo kujua hali kwa ujumla ikoje, na kama ni chuki basi hakuna mtu aliyemchukia wakati huo kama Wambugu, aliapa moyoni lazima amtie nguvuni na atumikie kifungo chake kwa mateso makali.

Kwa ujumla usiku huo kila mtu alikuwa akiwaza yake juu ya Wambugu. Madam S alikuwa ametulia kitini haongei chochote, aliwaacha dereva na Mashaka waongee.

Haikuwachukua muda mrefu usiku huo, masaa mawili na nusu tu tayari walikuwa Embu na moja kwa moja walienda katika kituo kikuu cha polisi na kukutana na mkuu wa polisi wa kituo hicho. Madam S alijitambulisha kwao na kuonesha kitambulisho chake.

“Tunasikitika kuwa kijana wako ametoroka,” ilikuwa kauli ya mkuu Yule. Mashaka akamtazama Madam S ambaye alikuwa ameketi bila kuongea neno lolote, “Na isitoshe ametoroka na gari ya polisi,” akaongeza tena Yule mkuu wa polisi. Madam S alikuwa akitikisa kichwa tu kuashiria kuwa ameelewa anachoambiwa.

“Atarudi tu, msiwe na shaka,” madam S akajibu kwa kifupi, kisha akanyanyuka na kumuamuru dereva waelekee hospitali ya Agha Khan ili akamuone bwana Ndege aliyejeruhiwa katika sakata hilo. Alipofika tu pale hospitali alikutana na Bwana Shikuku, kila mmoja alimkumbuka mwenzie, waksalimiana kwa bashasha kwa kuwa ni miaka mingi hawajaonana. Baada ya hapo wote wawili wakaelekea ndani ya hospitali hiyo kumuona Ndege aliyekuwa amelala usingizi.

“Kwa nini usimrudishe Nairobi kwa matibabu?” Madam S akauliza.

“Amesema hatotoka hapa mpaka amuone Kamanda Amata,” Shikuku alijibu.

“Ok, wameivana hawa. Ulikuwa unajua kama AmaTa yuko hapa?” madam S aliuliza tena.

“Ndio kwanza nafahamu sasa kuwa yuko hapa siku nzote sikuwa najua,” Shikuku alidanganya, wakati Ndege alishamwambia kuwa kamanda Amata yupo Nairobi kwa shughuli hiyo ila si kiofisi.

Madam S alitulia kimya akitafakari jambo Fulani, alionekana wazi kukosa raha usiku huo, aliitazama saa yake ilikuwa tayari ni saa kumi alfajiri.

§§§§§

Kamanda Amata alikunja kona kali kuingia ile barabara ambayo ile pikipiki iliingia, alipoenda kama mwendo wa mita mia hivi hakuiona ile pikipiki wala dalili zake, akajua kwa vyovyote huyu jamaa atakuwa mitaa, akasimamisha gari na kushuka bastola yake mkononi, akawa anashangaa akitafuta huku na kule akizungukazunguka kwa hadhari kubwa sana, alipokuwa tayari kukata tama alisikia mnguruno wa pikipiki kwenye vichaka, akawahi na kuiona ikitokomea porini, akainu bastola yake na kufyatua risasi ya kwanza haikua na shabaha ila ya pili alipiga tairi na kulitoa upepo, ile pikipiki ikaanguka, na Wambugu akawa chini, Kamanda Amata akafika eneo lile na kumkuta Wambugu amekwishasimama na amejiandaa kwa mapigano, Kamanda Amata alitaka kufyatua risasi lakini akakuta zimemuishia, aliirusha ile bastola kumpiga nayo Wambugu, Wambugu aliruka hewani kama ninja na kuipiga tik tak ile bastola ikapotelea kwenye vichaka, wakati huo tayari Amata alifika pale kabla hajajiweka sawa, mguu wa nguvu ulimshukia Amata begani, akayumba upande na Wambugu akasimama kwa mguu mmoja kisha akaushusha ule mwingine taratibu kwa madaha,

“Siku zote mnajua kuwa kila mtu ni bwege, kama ulikuwa hujui basi mimi ni Sempai,” Wambugu alijisifu huku akisimama katika pozi la kungfu, Kamanda Amata akaona hapo ndo penyewe, “Huwa sijibishani na wahalifu kabla sijawafundisha adabu,” Kamanda Amata alizungumza kwa gadhabu, akaruka hewani kiufundi na kuimshia mapigo makali Wambugu, lakini mapigo yote aliyapangua vizuri sana, kisha akaanza yeye kupeleka mashambulizi ya mikono kwa Kamanda Amata, ambaye naye alikuwa akiyapangua kiufundi sana mpaka Wambugu akamaliza mapigo yote, Kamanda Amata alipomuona sasa hana ujanja mwingine ndipo alipombadilishia staili kutoka kungfu kwenda kick boxing.

Teke la kwanza lilitua mbavuni kabla hajakaa sawa lapili likatu shingoni kisha zikafuata ngumi mfululiozo kama ishirini na tano zilizomuacha Wambugu hoi akigalagala, “Nyanyuka juu Sempai, upambane na mwanaume wa shoka, hayo mapigo niliyokupa niliagizwa na Melchior Ndege sasa naanza ya kwangu,” Kamanda Amata alipomaliza maneno hayo, alijivuta kwa hatua ndefu amgfikie Wambugu, lo, Wambugu akamzidi ujanja, alijirusha kutoka pale alipolala akasimama kisha akajibinua na miguu yake yote miwili ikatua tumboni mwa Amata na kumfanya ateme damu, hasira za Amata zikawaka ghafla, aligeuka nyuma kwa kasi na kumchota ngwala Wambugu lakini jamaa akaruka na ule mguu ukapita chini kisha Wambugu akashusha pigo moja la karate lililotua sawia kwenya shingo ya Amata na kumpeleka chini mzima mzima. Kamanda Amata alitambaa kama motto, damu zikimvuja puani na mdomoni, akaona wazi asipofanya makeke anaweza akazimishwa na watu wasiione maiti yake.

“Ha ha ha ha Tanzania Secret Agency namba 1 ndio wewe!!? Unatambaa kama motto, nyanyuka upambane na jabali la chuma linalotisha kama kifo, Kenya yote wananijua na hapa kila goti linapigwa,” Wambugu akasema hayo kwa kujitamba akijipigapiga kifuani. Maneno hayo yalimuuma sana Amata, akanyanyuka kwa kasi na kugeuka akitazamana na Wambugu ambaye mkononi mwake alikuwa ameokota gongo, akaliinu na kumpiga nalo Kamanda lakini Kamanda akalidaka kwa mkono mmoja, akatazamana na macho mabaya ya Wambugu.

Taswira za mauaji ya kikatili ya kahaba Rose ikamjia na kumtia hasira, taswira ya Ndege akiungua moto ikamjia na kumuongezea hasira, kauli ya kushushwa cheo ikamaliza kila kitu akilini mwake.

Kamanda Amata akiwa kalishika lile gongo kwa mkono mmoja alinyanyua mguu wake na kulikanyaga kwa juu akalivunja kwa mtindo huo kisha akabaki na kipande, kwa hasira na visasi akamchoma nacho Wambugu tumboni, yowe la uchungu lilimtoka akaanguka chini, Amata akamuendea palepale alipo na kumvua kibegi chake kisha akakivaa yeye mgongoni, akamnyang’anya simu yake na kuitia mfukoni kisha akamkamata ukosi wa jacket lake na kumburuza mpaka kwenye kibarabara, akampigiza sura yake chini kwa nguvu, “Bill yuko wapi?” akamuuliza kabla hajajibu akampigiza tena kwa nguvu na kuvunja mfupa wa pua. “Sasa ukiniua ndio ntasema?” Wambugu alijibu kwa uchungu. “Nambie haraka, Bill yuko wapi?” Kamanda aliuliza kwa kelele maana hasira ilikuwa bado imetawala kichwa chake. Wambugu alinyanyua uso wake na kutema mabonge ya damu,

“Kuna binadamu ambao hamtakiwi kuzaliwa kabisa, kama wewe na Bill, nakuuliza mara ya mwisho kabla sijakutenganisha na roho yako, Bill yuko wapi?” Kamanda aliendelea kuhoji,

“Mi si si si sssjui,” Wambugu alijibu kwa tabu sana. Kamanda Amata akamburuza mpaka aliposimamisha gari na kumuinua akamsimamisha wima akimuegemezea katika bodi la gari. “Wambugu! Nakuua,” Amata alimwambia,

“Niue braza, kwa maana ukiniacha hai nitateseka sana na mkono wa sheria,” Wambugu akajibu.

“Niambie Bill yuko wapi?” akauliza tena,

“Braza utanitesa utaniua lakini mimi sijui Bill yuko wapi alishatoroka hapa muda mrefu,” kamanda Amata alishikwa na hasira akampiga kichwa kimoja maridadi na kumuachia akianguka chini kama mzigo.

Mara taa za gari mbili zikawamulika kutoka barabara kuu, na zile gari zikaja mpaka pale, walikuwa ni polisi, wakateremka haraka na kumuweka Kamanda Amata chini ya ulinzi. Kamanda Amata akanyosha mikono juu, wale polisi wakaja na kumtia pingu, nyuma yao akaja mtu mnene kiasi aliyeonekana kuwa na sura ya kikatili isiyo na chembe ya huruma, akamuendea Kamanda Amata, akamtazama usoni, juu mpaka chini,

“Hey, askari!” akaita,

“Mfungue pingu Kamanda, mpe na begi lake,” wale askari wakafanya hivyo, kamanda Amata akapokea lile begin a kulitupia mgongoni.

“Mzima au amekufa?” Yule bwana akamuuliza Kamanda. “Mzima huyo hawezi kufa kirahisi,” Amata akajibu. Yule bwana akatoa amri ya kupakiwa Wambugu garini kisha yeye na Kamanda Amata wakaingia katika gari ndogo ya polisi na kurudi mjini.

“Kamanda Amata, umetusaidia kazi moja ngumu sana ambayo jeshi la polisi la Kenya na vyombo vingine vya usalama imetusumbua kwa miaka takribani kumi kumpata huyu mtu, asante sana kijana” akamshukuru Kamanda na safari ikaendelea mpaka kituo cha polisi cha Embu.

Madam S na Mashaka walikuwa hapo kituoni pia wakimsubiri Kamanda Amata, walimuona alipokuwa akishuka katika ile gari na waziwazi alikuwa ameumia sana kwa jinsi alivyokuwa akitembea, wakakutana uso kwa uso na Amata, wakatazamana. “Madam, kijana wako huyo wapo, sisi hatuna deni nae!” alisema Yule bwana mwenye mwili mnene, kisha akapita kwenda ndani ya kituo hicho, ijapokuwa ilikuwa alfajiri lakini watu walijazana kutaka kuhakikisha kama kweli jambazi sugu Wambugu limekamatwa, jambazi lililowanyima usingizi Wakenya wengi kwa miaka mingi.

Kamanda Amata, Madam S na Mashaka waliingia kwenye gari yao na kuondopka eneo lile, moja kwa moja mpaka hospitali ya Agha Khan ili kwanza apate huduma ya kwanza. Ndani ya nusu saa alikuwa tayari amefanyiwa check up ya nguvu na kutibiwa palipohusika, Mashaka akamuendea Amata katika chumba alichokuwapo kisha akamkabidhi begi jeusi mpano wa briefcase, alkipofungua ndani akakuta suti mpya, saa ya kisasa kwa kazi yake na bastola ndogo.

“Umerudi katika hali yako Kamanda,” Madam S alimwambia walipokutana mara tu Kamanda alipotoka kule ndani, “Yeah, lakini bado kitu kimoja,” kamanda alisema, “Nini?”

“Nataka kumuona Ndege,” akajibu. Wote watatu wakaingia wodini alikolazwa Ndege na kumkuta tayari amewekwa katika kitanda cha magurudumu, amefungwa mikanda sawia na chupa ya majiiliyowekwa baada ya ile ya damu ikiendelea kwenda, “Melchior Ndege,” Kamanda alimwita huku akwa amemuinamia pale kitandani, “Amekufa au amekimbia?” Ndege aliuliza kwa shauku, “Hali yake ilivyo hawezi kuiona jioni, yuko katika mikono ya polisi,” Amata alimwambia Ndege ambaye alionekana wazi kuifurahia habari hiyo. “Asante Kamanda,” Ndege alishukuru, “Asante na wewe” Kamanda akamalizia.

§§§§§

Kama kuna habari iliyomfurahisha Sargeant Maria, basi ni hii ya kupatikana kwa Wambugu, kwa sababu baada ya kumbana sana Mellina kwa kipigo na mateso makali alitaja washirika wote akiwamo Wambugu. Sargeant Maria na wenzake waliishiwa nguvu kusikia kuwa Wambugu anahusika na mauaji ya Kasisi, swali lilikuwa, tutampataje? Lakini ghafla alfajiri hiyo wanaambiwa kuwa Wambugu kapatikana huko Embu karibu na msitu wa Njukiri baada ya vyombo vya usalama kupambana nae vilivyo, baada ya kutaka kujua zaidi ndipo Sargeant Maria aliposikia juu ya Kamanda Amata ambaye yeye siku zote alijua ni mtu wa kwenye riwaya tu, hakujua kuwa ni burudani ya waandishi kuandika visa vyake kila amalizapo kimoja na kuanza kingine. Ulikuwa ni ushindi mkubwa, mkubwa sana, Maria alijiuliza, Mellina tumemkamata, Cheetah, kauawa, Wambui kauawa, Wambugu ndio huyu hapa, sasa ile Mostrance ambayo ndicho chanzi cha kazi nzima haijapatikana, bado kuna kazi mbele.

8

SIKU MOJA BAADAE – DAR ES SALAAM

KAMANDA AMATA na Madam S walikuwa wakitembea kwenye korido ya jengo la ukumbi wa jiji, wakiwa wanatoka kupata kahawa katika kamgahawa kadogo ndani ya ukumbi huo, walikuwa wakizungumza mawili matatu, wakibadilishana mawazo ya hili na lile.

“Sasa Kamanda, kama uliovyoambiwa, umeshuswa cheo na umebadilishiwa idara, idara gani mi na wewe hatujui, lakini nataka uniambie jambo moja tu, baada ya kumkamata Wambugu, umepata chochote juu ya jasusi Bill Van Getgand?” Madam S akauliza. Wakasimama na kugeukiana, “Yeah, Bill yupo German, alishaondoka kitambo sana, na habari hizi nimezifanyia uchunguzi wa kina sana kutoka katika tafutishi zangu kupitia simu na maelezo ya Wambugu,” Kamanda Amata akajibu.

“Ok, Una akili sana Kamanda, siwezi kupata mtu kama wewe tena katika ofisi yangu. Sikiliza, baadae nitakupigia simu tuonane.” Baada ya mazungumzo machache kati yao waliagana na kuondoka kila mtu na hamsini zake.

Ndani ya ofisi za AGI Int’, Gina alikuwa ameandaa bonge la keki na mvinyo wa kutosha kusherehekea kurudi salama kwa boss wake Kamanda Amata. Walipongezana wakiwa wawili tu, wakikata keki na kunywa mvinyo kwa fujo kiasi. Wakiwa katika hali hiyo ndipo simu ya Kamanda iliita kwa fujo, “Aaaaaaa nani tena huyo?” Gina aliuliza kwa sauti ya kilevi. “Madam S” Kamanda Amata akajibu na kuiweka ile simu sikioni.

“Unikute hapa katika ofisini kwangu mara moja,” na ile simu ikakatika, Kamanda Amata akashusha ile simu na kuitia mfukoni, mara Gina akamvamia na kumkubatia kwa nguvu, “Kamanda, sikjawahi kukwambia jamani, mi nakupenda, unioe, uwe mume wangu,” Gina alilalama akiwa kalewa chakari, chezea Dompo wewe! “Hebu toa ulevi wako Gina,” Amata aling’aka lakini Gina bado alikuwa kamng’ang’ania sasa akitaka kumpa ulimi, Amata akamuweka kwenye kiti.

“Wewe, uwe na akili, umelewa wewe, mi naenda kwa Madam S kaniita,” Amata alimwambia Gina, “Tunaenda wote,” Gina nae akaliunga. Dakika chache tu ziliwachukua kuwasili katika ofisi ya Madam S iliyopo mkabala na jengo la hazina, akaingia getini na kuegesha gari panapotakiwa, aliteremka na kumuacha Gina akiwa anakoroma garini, tayari alibebwa na usingizi mzito. Akajiweka tai yake vizuri kisha akajitupia koti lake na kuziendea ngazi zinazoingia katika ofisi hiyo, akiwa mlango wa kwanza alikutana na mtua mmoja ambaye alimjua vilivyo ni mwenzake wa idara ya usalama wa taifa lakini vitengo tofauti akiwa kakunja sura hata hakumsalimu, Kamanda aliponyosha mkono kumsalimi hakupokelewa, akaona isiwe shida alimpita na kuingia ofisini kwa Madam S.

“Karibu Kamanda,” Madam S alimkaribisha huku amesimama badala ya kukaa.

“Asante Madam kwa kunikaribisha katika ofisi yako tukufu ambayo sikutegemea kuiona tena,” Kamanda Amata alizungumza akiwa siriasi kabisa.

“Kamanda Amata, kutokana na mchango wako mkubwa katika kuliokoa Taifa, na kutatua migogoro mizito na mikubwa ambayo ama ingelipoteza Taifa au maisha ya wananchi, maamuzi ya kikao cha watu wa idara ya usalama kimeamua kikushushe cheo kutokana na kutoitilia umakini nafasi uliyopewa na kudharau amri au maamuzi ya wakubwa wako, hivyo umeshushwa cheo na kubadilishiwa kitengo, kutokana na hilo kuanzia sasa ofisi yako ya kazi itakuwa Ikulu, kuratibu na kuhakikisha usalama wa msafar wa Mheshimiwa Rais pindi awapo nje ya jengo la Ikulu.” Madam S alimtazama Kamanda Amata usoni hakuona dalili ya tabasamu wala chuki kutoka kwa mpiganaji huyo. Kwa kuwa yeye kupata nafasi hiyo alikuwa ametokea katika jeshi la polisi kitengo cha CID alitoa heshima ya kijeshi kwa Madam S ya kuonesha amekubaliana na uamuzi huo bila ubishi.

Madam S akamkabidhi barua maalu yenye mhuri wa serikali kuthibitisha hilo pamoja na muhtasari wa kikao, akavipokea na kuvibana kati mkono wake wa kulia. Madam S akamtazama tena Amata, “ Kamanda Amata, kutokana na kuwa idara ya usalama imekosa mtu wa kuishika nafasi yako mithili ileile ya jinsi ulivyokuwa ukifanya kazi kwa makini na akili nyingi, ukiwa tayari kufa kwa ajili ya Taifa lako au kwa ajili ya wanyonge, imeonelewa tukurudishie cheo chako cha Tanzania Secret Agency namba 1 kwa muda usiojulikana mpaka itakavyoamriwa vinginevyo,” Madam S alimtazama tena Kamanda usoni akakutana na sura ileile ya ukakamavu. Akachukua beji maalum ya utambulisho kwa watu wote wa usalama wa Taifa na kuipachika katika upande wa kushoto wa ukosi wa koti lake, beji ambayo ilichukuliwa wakatia alipofikishwa hospitali Muhimbili akitokea Kenya. Madam S akamkabidhi kikasha kimoja kilichofungwa kwa utepe mwekundu.

Akakipokea akaukata utepe na kukifungua ndani, bastola aina ya Walther PPK (PPK ni Polizei Pistole Kriminal-The Criminal Police Pistol), pembeni ya bastola hiyo kulikuwa na kiwambo chake cha sauti. Chini ya hicho kikasha kulikuwa na bahasha ndogo, akaichana na kuifungua, ilikuwa tiketi ya ndege kwenda Ujerumani, alipochambua vizuri akakutana na picha ya Bill Van Getgand, juu yake imeandikwa ‘WANTED’ yaani ‘ANATAFUTWA’ halafu chini yake wameorodhesha mashirika mbalimbali ya kijasusi ambayo yanamtafuta jasusi mwenzao aliyehasi huko KGB na kuingia kwenye mikono ya uhalifu wa kimataifa.

“Kamanda Amata, sasa unaenda kufanya kazi ngumu ambayo shirika la letu la ujasusi japo halitambuliki hivyo kimataifa linakutuma, Safari njema.” Madam S alimaliza na kuketi tena katika kiti chake. Akili ya Kamanda Amata ilianza kufanya kazi ndani ya muda mdogo akiikabili kazi hiyo ngumu na ya hatari ambayo hakujua wapi itaishia. Alimtazama madam S kwa tuo. “Keti chini kamanda,” Madam S alimwambia Kamanda Amata wakati mlango ukifunguliwa na jamaa mmoja akiingia na sanduku moja dogo la chuma, akakaribishwa na kuketi katika kiti kingine pembeni ya kamanda Amata. Kamanda Amata alielewa kinachotakiwa kufanyika, walihitaji kuiridisha ile microchip ya GPS ambayo huweza kumfanya aonekane popote alipo.

Yule daktari akatoa mashine Fulani na kumfanyia vipimo vichache ikiwamo presha ya damu na vitu vingine, kisha akachukua kitu kama sindano iliyounganishwa na bomba kabisa ambapo ndani yake kuna hiyo microchip, akamdunga sehemu Fulani ya msuli wake wa mkono juu ya kiwiko na chini ya bega akasukuma kama anavyosukuma dawa katika sindano ya kawaida, ile microchip ikasafiri katik ule msuli na kujikita ndani kabisa, baada ya hapo akafungwa bandeji na kupewa dawa Fulani za vidonge za kutumia.

Wakati huohuo mlango ukafunguliwa na Chiba akaingia ndani akiwa na begi lake ambalo daima hupenda kutembea nalo, akatoa kompyuta yake ndogo lakini yenye kazi nyingi za kijasusi, akaiweka mezani na kuiwasha kisha akaanza kuingiza namba Fulani Fulani, waya mmoja akaupachika katika sehemu ile aliyohisi ile chip imetuama, ikashikiwa kwa ile bandeji na waya mwingine wenye kitu kama kibanio mwishoni ukabanwa katika kidole gumba cha mkono mwingine, kisha Chiba akawa akifanya kazi katika kompyuta yake.

“Ok, kila kitu tayari,” akasema huku akimtoa zile nyaya zote. Kisha akaingiza mkono katika upande mwingine wa lile begi lake, “Hii hapa saa ya kutumia Kamanda, saa hii ina uwezo wa kukata chuma cha aina yoyite kwa kutumia nishati ya infrared ambayo imekwishawekwa ndani yake, ina uwezo wa kutuma fax fupi na pia inatambua hatari ya mlipuko mahala popote ambapo umetegwa. Uwe mwangalifu kijana,” Chiba alimaliza maneno yake huku akimpigapiga mgongoni.

“Kamanda!” Madam S aliita, “Nimekupigania sana mwanangu, nenda kafanye kazi, nakuomba usichezecheze na wasichana hawa huko, ujue kwamba Bill ni jasusi, si ajabu akawa anajua safari yako yote hata sasa, nimemaliza kwa heri,” Madam S alimaliza na kuagana na Kamanda Amata akabaki na Chiba ofisini.

Kamanda Amata akashuka ngazi na kuiendea gari yake ambako alimkuta Gina bado kalala akikoroma. Akaingia na kuwasha gari akaondoka zake mpaka nyumbani kwake Kinondoni, hakuwa na muda wa kutosha alipanga vitu vyake vichache, akakusanya silaha zake zote za siri na kuzificha panapostahili katika kijibegi chake cha mgongoni ambacho ni yeye tu aliweza kujua kipi kiko wapi na wapi kiko kipi, wakati lile sanduku lilikuwa na nguo na zana ndogondogo. Alijiangalia kwenye kioo cha chumbani mwake na kujiuliza aingie vipi Ujerumani, mkimbizi? Mfanyabiashara, mtalii, muandishi wa habari au vipi, akapata jibu, akafungua kabati na kuchukua bunduki yake ya kisasa kabisa, iliyotengenezwa kwa mfano wa camera kubwa ya picha mnato lakini ndani yake ilikuwa na uwezo wa kubeba risasi ishirini na nane za bastola aina ya Smith and Wesson.

Alipohakikisha kila kitu kipo sawa, akatulia juu ya kitanda huku mawazo yote yakiwa juu ya Bill, kila akikumbuka kitendo alichofanyiwa na Bill alijikuta hasira zikimpanda maradufu, aliamua kumfungia kazi kikweli, ‘ulimwengu utatambua kuwa Bill kauawa na mkono wa Amata, sitaiacha roho yake ipotelee jela wala kwenye mikono ya nani, mi sijui nitakapomuona tu uso kwa uso ama zake ama zangu’ yalikuwa ni mawazo yaliyopita katika kichwa cha Kamanda Amata muda huo. Usingizi ulimpitia na ndoto mbaya zikamuandama, mara anakabwa mara anakimbizwa mara anatumbukia kwenye shimo, basi shida tu.

Kengele ya saa ya mezani ilimuamsha ilikuwa yapata saa nne usiku, alikurupuka na kuingia bafuni akaoga harakaharaka na kujiandaa, alipoenda mutazama Gina, alimkuta bado yuko hoi kwa usingizi akamuandikia ujumbe na kuufutika mahali alipolala kisha ye akachukua gari yake na kuondoka zake kuelekea JNIA tayari kwa safari.

Majira ya saa saba usiku, ndege kubwa ya sirika la Qatar Airways au kama wanavyoliita dege lenye hadhi ya nyota tano liliiacha ardhi ya Dar es salaam na kukata anga kuelekea Doha ambako abiria wangebadilisha ndege ili kuendelea na safari zao. Kamanda Amata alitulia kitini katika behewa hiyo ya VIP akiwa kanyoosha miguu kwa raha zote akipata raha kwa kuwatazama warembo wa Qatar waliokuwa wakijipitisha pitisha na kuumuuliza hili au lile. Akili na mawazo yake tayari yalikuwa yamejipanga kimchezo huo wa hatari ambao unamkabili mbele yake ambao alipenda aufanye kwa siri na kwa muda mfupi.

ACHEN – UJERUMANI

ANDREAS Schurmann alimtazama Bill Van Getgand, hakummaliza, mtu huyo mnene, mwili jumba lakini mwepesi kwenye mapambano alikuwa ameketi mbele ya tajiri huyo, tajiri anayejulikana sana katika mji wa Achen na pembezoni. Ilkuwa ni siku moja tu baada ya Bill kuwasili katika jumba hilo la kifahari lililojengwa katika eneo la Mausbach. Jumba la bei mbaya ambalo hakuna asiyelijua katika mji huo.

“Nini kilikuwa kinakushinda siku zote kupata kitu kidogo kama hiki Bill?” Don Andreas alimuuliza Bill huku akimmiminia bia aina ya Pilsner, bia bora Ujerumani.

“Hata huko nilikoipata usifikiri kazi ilikuwa rahisi, imebidi kumwaga damu,” Bill alijibu huku akiinua glass yake na kuiweka mdomoni kabla hajamiminia kinywaji kilichomo ndani yake, akabeu kidogo, “Imebidi tumwage damu, hakukuwa na jinsi,” alimalizia kusema. “Usijali, maadam tumepata tunachotaka basi,” Don Andreas akamtia nguvu kwa maneno hayo.

“Hii mali yetu kaka, aliwekeza baba wa babu yetu, alikuwa na makusudi mazima juu yake,” Andreas aliendelea kuongea huku akiigeuzageuza ile monstrance mikononi mwake, “Pure Gold!” alitamka maneno hayo huku akiibusu. Akairudisha katika begi lake na kuketi tena kochini. “Ndio Bwana Bill, kazi yangu mi na wewe imekwisha, au kuna linguine la kuniambia? Maana malipo yako tayari yapo benki haijapungua hata senti moja nyekundu,” Andreas alimwambia Bill. Tabasamu pana likamjia Bill usoni, likachanua kama ua la yugiyugi, akainua glass yake na kugonga cheers na Andreas, wakati glass hizo zikagongana simu ya Bill ikaita kwa fujo katika mfuko wake wa shati, akaitoa na kukutana na ujumbe mfupi wa maandishi,

“…Wambugu amekufa mikononi mwa polisi, kazi ya Kamanda Amata,”

Meseji hiyo ilimshtua sana Bill. “Vipi? Mbona unashtuka?” Andreas akauliza. Bill akashusha glass yake na kuiweka mezani. “Mmoja wa vijana wangu ambaye nilimpanga wa mwisho kufa, ameuawa,” Bill alijibu.

“Sasa wewe kinakushtua nyingi, si ndio amekufa!” Andreas akamwambia.

“Tatizo sio kufa, ila nani kamuua” Bill akamwambia Andreas.

Andreas akatikisa kichwa kuashiria kuwa amemuelewa Bill, “Ok, nani amemuua?” akauliza.

“Amekufa mikononi mwa polisi, na ni kazi ya Kamanda Amata, Jasusi la kiafrika kutoka Tanzania, TSA,” Bill akajibu.

“Unasema! Africa kuna majasusi? Tangu lini? Tena Tanzania?” Andreas alionekana kushangazwa na taarifa hiyo.

“Don Andreas, hata kama ASfrica hakuna majasusi, lakini huyu Amata ni zaidi ya Jasusi,” Bill alieleza huku mikono yake ikiwa kiunoni.

“Acha uwoga wewe, wao wapo Africa wewe upo Ulaya, waache wauane tu, hiyo ndiyo sera yetu mataifa makubwa, tunawachonganisha wanauana sisi tunakula maisha,” Andreas akajibu huku akijimiminia kinywaji chake kama kawaida lakini Bill hali haikuwa sawa kama mwanzo, Lijitupa kochini na kuweka mikono yake huku na huko kisha akashusha pumzi ya kina.

“Andreas, ili tuwe na amani katika hili lazima Amata auawe kwa njia yoyote ile,” Bill aliongea kwa jazba.

“Kama wewe umesema kuwa ni mtu hatari basi fanya kazi ili asiharibu mambo yetu, nakuaminia wewe ni jasusi wa KGB hata kama uliwasaliti na kuwakimbia,” Andreas alimwambia Bill huku akimpigapiga mgongoni.

Bill Van Getgand aliingiwa ganzi mwili mzima baada ya kusikia Wambugu kafia katika mikono ya polisi na ni kazi ya Kamanda Amata, hiyo ilikuwa ni salamu tu ambayo alijikuta anashindwa kuijibu. Alikumbuka sumu kali aliyompatia akijua kwa vyovyote asingeamka kwa muda mfupi kama ule, japokuwa hakusikia habari za kifo chake redioni, bado Bill aliamini kabisa kuwa Kamanda Amata mpaka dakika hiyo ni marehemu. Ukimya uliendelea akitafakari jinsi gani swahiba wake Wambugu atakuwa ametoa siri za mpango wao na labda hatari kubwa itakuwa ikiwanyemelea.

Bia iligoma kupita kooni, akili yake bado ilikuwa inazunguka huku na huko akifikiri la kuifanya, alipopata jibu akainua glass yake na kujitupia kinywaji kama kawaida, huku laptop yake ndogo ikiwa mezani tayari kwa kazi Fulani. Aliifungua na kutaka kuingia mtandaoni, Bill nalikuwa na uwezo wa kuingia mtandao wowote anaoutaka kwa kutumia nywila za bandia ambazo huzibuni kiufundi sana yeye mwenyewe na kufungua faili au mtandao wowote anaoutaka ili kujipatia taarifa kwa ajili ya mambo yake ya kijasusi, aliingiza nyila zake ili kuifungua kompyuta hiyo, ilipofunguka kioo chote kilikuwa cha blue, “Shiit!!!” akang’aka, akajaribu tena, hali ilikuwa ileile, akabaki mdomo wazi, kijasho chembamba kikamtiririka kutoka kwapani mpaka maeneo ya kiuno, Bill alihangaika kutumia njia zake zote lakini hakufanikiwa.

Ilikuwa ni kazi ya kijana Frank Masai aliyekuwa akishirikiana na Chiba katika kuunda kirusi kibaya kabisa maalumu kwa kuiua kompyuta ya Bill kusudi asiweze kuingia katika mtandao wa siri za usalama wa Taifa la Tanzania, walifanikiwa, Bill Van Getgand alibaki teee, hana la kufanya, “Wameniweza,” akajisemea kwa sauti ya chini. Bill alikurupuka kitini na kumuaga Andreas kuwa atarudi jioni ya siku ya hiyo, alitoka nje ya hekalu hilo la kifahari na kuingia kwenye gari yake aina ya Jaguar na kuondoka zake. Akiwa na mawazo mengi kichwani alielekea moja kwa moja katika hotel aliyofikia ili akajaribu mbinu nyingine kupata taarifa za watu mbalimbali na mienendo yao kwa siku hiyo.

BERLIN-SCHONEFELD AIRPORT

Saa 10:30 jioni

QATAR AIRWAYS ilikanyaga ardhi ya Ujerumani jioni hiyo ikiwa tayari imemaliza safari yake iliyoanzia Doha na kupita miji kadhaa kabla ya kufika Berlin. Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Schonefeld, watu walikuwa wengi wakija kuwapokea na kuwalaki ndugu zao waliokuwa wakitoka pande mbalimbali za dunia kuja ama kusalimia jamaa au ndio wanarudi nyumbani, ilimradi tu maisha ya binadamu ni ya kuhamahama. Miongoni mwa waliokuja kupokea ndugu zao alionekana mtu mmoja mwenye ndevu nyingi, aliyevaa vazi la kikasisi lililomkaa sawia, kanzu ndefu nyeusi na kofia kubwa ya rangi hiyo hiyo, alisimama karibu na nguzo Fulani akiwa hana papara ya lolote, alionekana kumfahamu vyema Yule anayekuja kumpokea na si vinginevyo.

Baada ya Kamanda Amata kukamilisha itifaki za uhamiaji ambapo aliingia Ujerumani kama mwandishi wa habari, aliiweka kamera yake vizuri kifuani mwake, kizibao cha khaki kilichomkaa vyema na jeans yake nyeusi, vilimuonesha wazi kuwa ni mwanahabari halisi, usoni mwake aliipachika miwani safi nyeusi, miwani ambayo inaweza kuvuta vitu vya mbele pindi unapojitikisa kichwa kichwa chako, miwani hiyo ina uwezo wa kukuonesha vitu vya nyuma yako kwa kutumia vioo vidogo vilivyowekwa kwenye miimo yake, ina uwezo wa kurekodi picha mjongeo na sauti kwa wakati mmoja. Mkononi mwake alivaa saa kubwa ya kisasa ‘Casio’ yenye uwezo wa kutuma na kupokea fax fupi, inayoweza kukata chuma chenye ugumu wowote kwa kutumia miali mikali ya laser CO2 iliyowekwa ndani yake, kiatu chake cha mpira kisichoathirika kwa mafuta yoyote wala kuungua kwa moto kirahisi kilikuwa mguuni mwake.

Taratibu alitoka katika mlango wa kutokea wasafiri, akiangaza huku na huko na kwa kufanya hivyo miwani yake iliweza kumsogezea watu wote karibu na kuweza kuwachambua kwa harakaharaka, kwa mbali alimuona Yule kasisi aliyekuwa kwenye kiti cha chuma akiwa anasubiri mgeni wake, Kamanda Amata akasita kidogo, mara mkono wake ukafinywa na kitu kama sindano ndogo sana, akainua saa yake na kuiangalia, ilikuwa ikiwaka taa ndogo sana nykundu katikati ya mishale yake, akabofya kitu Fulani na ikaonesha maandishi katika kioo, ‘A priest’ yaani ikimaanisha Kasisi. Hakusita alimuendea kasisi huyo na wakakutana uso kwa uso kila mmoja akimwangalia mwenzake kwa umakini wa hali ya juu.

“Karibu Berlin,” Yule Kasisi alimkaribisha Kamanda wakakumbatiana kusalimiana kisha lile sanduku lake likachukuliwa na Yule Kasisi nay eye akafuata kwa nyuma, muda wote alikuwa akitembea huku akitazama kila amuonaye kuona kama kuna hatari yoyote. Moja kwa moja wakaiendea gari moja ya kisasa sana VolksWagen (VW) modeli mpya wakaingia na kuketi ndani yake.

“Naitwa Fr Frank, raia wa Austria, nafanya kazi katika kanisa kuu la Achen,” alijitambulisha Yule Kasisi, Kamanda Amata akatikisa kichwa kuashiri kuwa ameelewa alichoambiwa.

“Yeah, kamanda Amata,” kisha wakacheka pamoja na kugonganisha viganja vya mikono yao. Kwa jinsi walivyokuwa wakipanga waliona haitakuwa vyema Kamanda asishukie moja kwa moja Aachen, ila ashukie Berlin kisha aende Aachen kwa usafiri wa gari, hii ilikuwa ni mbinu ya kuwapoteza malengo kama wapo wanaomsubiri. Mazungumzo yaliendelea kati ya wawili hao huku wakijaribu kupanga mkakati wa kumaliza kazi yao.

“Kilichonileta Fr Frank, sio Bill tu, ila nahitaji kuipata ile Monstrance pia,” Kamanda Amata alimwambia yule Kasisi.

“Unajua, Bill baada ya kumchunguza sana, nimegundua kuwa anafanya kazi na tajiri mmoja anaitwa Andreas Schurmann au ‘Don’ kama wengi walivyozoea kumwita, na mimi tangu nimekuja hapa najua kwa vyovyote vile monstrance ile ipo kwake,” Fr Frank alimueleza Kamanda Amata, “Andreas anafanya nini zaidi?” Kamanda kauliza.

“Yeye ni mfanyabiashara mkubwa, ana viwanda na mahoteli makubwa, nyumba tu anayoishi inaizidi ikulu ya Ujerumani,” Fr Frank alimjibu Kamanda.

“Safi nahitaji kuiona nyumba yake na ikiwezekana pia kujua baadhi ya makampuni yake ili nijue nafanya nini,” kamanda Amata alieleza. “Ila ni kibarua kigumu sana Kamanda, “Yule jamaa ana ulinzi kama Rais wa nchi” Fr Frank aliendelea kumueleza Kamanda hali halisi ya kitu alichokuja kukifuata. Kamanda Amata alijaribu kuangalia uzito na kubwa wa kazi yenyewe.

Masaa matano yaliwatosha kufika mji wa Achen ulio kilomita 538.8 kutoka Berlin, kamanda Amata alitulia tuli kama maji ya mtungini, akiwa amechoka na safari kwa namna moja au nyingine. Saa tatu usiku, walifika katika kanisa kuu la Aachen ‘Aachener Dom’ kama linavyoitwa. “Utakaa hapa na sisi, pana usalama zaidi kuliko hotelini, katika mahotel, huku kwenye nchi zetu, huwa wanatoa siri za wageni wanaofika kwa watu wa usalama na wengine kwa wenye nia mbaya. Usijali Kamanda, hapa pako sawa na hii oda tumepewa kutoka kwa watu wako wa ubalozi,” Fr Frank akiwa katika kusema hayo alikuwa tayari akiegesha gari katika maegesho ya ndani ya jengo kubwa kabisa lililojengwa kiustadi nyuma ya kanisa hilo. Hakuwa na la kusema, zaidi ya kufuata kila anachoambiwa.

Mhudumu aliyepokea mizigo ya Amata alimkaribisha katika chumba maalum kilichokuwa ghorofa ya tatu upande wa kaskazini wa kanisa hilo kubwa. Alikikagua kwa jinsi anavyojua yeye lakini hakuona chochote kilichowekwa kwa nia mbaya kwa ajili yake, aliliendea dirisha dogo lililokuwa hapo, akavuta pazia na kuangalia nje huku akiwa amezima taa ya ndani, hakuna kitu alichokiona zaidi ya jengo kubwa umbali kama wa kilomita moja hivi, likipendezeshwa kwa taa nyingi na nzuri. Akiwa bado akiliangalia jengo hilo mlango ukafunguliwa na Fr Frank akaingia, sasa akiwa katika mavazi ya kawaida kabisa, lakini cha kushangaza hakuwa na ndevu tena, “Kamanda Amata, hilo jengo unaloliangalia ndio jumba la Don Andreas,” Fr Frank alimwambia Kamanda Amata, “Nimekupa chumba hiki kwa makusudi mazima ili uweze kuliona jumba hilo, sasa sisi tunakuacha ratiba zako utapanga wewe, kama utahitaji msaada kutoka kwetu basi usisite kunijulisha,” Fr Frank akondoka zake.

Kamanda Amata alifunga vifaa vyake ikiwemo camera kubwa moja na darubini yenye nguvu kabisa ambayo inaweza kuona umbali wa kilomita kadhaa pia yenye madini ya kukuwezesha kukuonesha gizani, akaiweka pale dirishani pamoja na kamera ndogo ambayo ingeweza kupata picha nzuri za mnato na mjongeo kupitia darubini hiyo. Alipohakikisha vyote viko sawa, alijaribu kuangalia kwa kupitia darubini ile, aliweza kuona walinzi waliokuwa wakizunguka huku na kule wakiwa na mambwa mwakubwa ya kutisha, ndani ya jumba hilo hakukuwa na chochote kinachoendelea, inaonekana ama watu walikuwa wamelala au walikuwa mahali pengine, lakini yeye alikuwa akifanya majaribio tu, hivyo hakujali kama wapo au la.

§§§§§

BILL VAN GETGAND alikuwa mezani akijaribu kuangalia mtandao huu na ule, alipitia mitandao yote ya mashirika ya ndege zinazoingia na zilizoingia siku tatu nyuma lakini hakuona dalili ya mtu anayemuhisi kufika au kuja. Akafanya mawasiliano na watu wake katika mahoteli lakini haikuonekana kabisa kama kuna mtu kutoka upande anaoufikiria. Bill hata kama alihakikishiwa usalama kuwa hakuna anayemdhania kuwepo nchini humo, bado moyo wake ulihangaika maana alijua wazi kuwa Kamanda Amat anweza kuharibu mambo yote na anaweza kuingia Ujerumani hata kwa kuogelea endapo anabaini kuwa anawindwa.

Usingizi haukua na nafasi kwake siku hiyo, alijaribu kuwapanga vijana wake jinsi anavyoweza ili kuhakikisha anapata habari juu ya ujio anaoutarajia. Bill bila kujua kinachoendelea alifumbua macho na kukuta jua tamu linalopenya katika dirisha lake likimmulika usoni, akajiziba macho kwa kiganja chake cha mkono, hakuelewa saa ngapi alilala ila alijua tu muda ailoamka. Aliketi kitandani alipokumbuka juu ya Kamanda Amata moyo wake ulianza kumuenda mbio na akakosa raha.

Katika maisha ya Bill, maisha yake ya kazi yake ya kijasusi tangu akiwa KGB kule Urusi hakuna siku aliishi kwa hofu kama siku hii ambayo alimuhofia sana Kamanda Amata. Japokuwa alishapambana na majabari katika kazi yake, majitu yenye mbinu na uafanisi mkubwa katika mauaji ya kila aina lakini kwa Kamanda Amata alikuwa anajikuta hana kitu, hasa akifikiria jinsi alivyomuwekea sumu na amepona, kwake aliona Amata anatisha zaidi ya kifo. Alijaribu kutuliza mawazo na alipoona yuko sawa, alitoka katika nyumba yake na kuliendea gari lake aina ya Mercedes Benz na kutokomea mjini. Huku akiwa amejiimarisha kwa kila hali siku hiyo maana alijua lolote linaweza kutokea kwa kuwa alama zake za hatari zilikwishamuonesha hilo. Safari hiyo ilikuwa ni katika moja ya makampuni ya Adreas kama walivyopatana jana yake.

AKIWA ndani ya kanzu nyeusi ya kikasisi huku kichwani akiwa na kofia yake nyeusi aina ya barret, Kamanda Amata alikuwa akitembea tembea katika uwanja wa kanisa hilo kubwa kabisa katika mji huo wa Aachen. Kila aliyemuona alimsalimi kwa lugha ya Kijerumani ambayo alikuwa akiifahamu vema. Alipohakikisha ameyachoka mazingira hayo, akaliendea gari moja jeusi lililokuwa limeegeshwa hapo pembeni kwenye maegesho ya magari.

Akaingia na kuketi nyuma ya usukani, ilikuwa ni Land Rover County short Chassis, aliiwasha na kuitoa taratibu katika maegesho yake, kishs akaliendea geti kubwa na kufuata ujia mrefu uliokuwa ukiiendea barabara kubwa ya kuelekea katikati ya mji, Kamanda Amata aliendesha gari hiyo kwa mwendo wa wastani akielekea njia ile ambayo ilikuwa ikipita katika jumba la bwana Andreas. Njiani gari nyingi zilimpita nay eye akazipita zingine ilimradi kufanya barabara ipendeze. Baada ya mwendo kama wa dakika kumi hivi aliichepuka na kukunja kushoto kisha akaingia kama shimoni na kupita uvunguni mwa hiyo barabara akatoke upande wa pili. ‘AACHEN COMMONWEALTH GRAVE YARD’ (Uwanja wa makaburi ya jumuia ya madola ya Aachen), lilikuwa ni bango kubwa la kijani lililoandikwa kwa maandishi meupe likionesha mshale kuelekea upande wa kushoto, Kamanda Amata akawasha indiketa kueleka upande huo, akapinda na kulielekea geti kubwa upande huo, ambalo lilifunguka lenyewe bila kufunguliwa na mtu.

Akaingiza gari na kushuka, mkononi akiwa na ua moja zuri na kitabu kidogo cha sala. Moja kwa moja akaliendea moja ya makaburi lililokuwa nyuma ya yote, kaburi hilo lilionekana kuwa ni la siku hizi tu kwa uwanja ule ulikuwa umeungana na uwanja wa kuzikia mapadre, akaenda na kulifikia lile kaburi akasimama na kuinua uso wake, mbele yake aliliona jumba kubwa la Don Andreas likiwa limetulia kabisa. Akainama na kuweka lile ua juu ya kaburi hilo, akatulia kimya akiwa amezama katika sala lakini muda wote akiwa analiangalia lile jumba, kwa kutumia miwani yake aliweza kupiga picha kadhaa lile jumba huku akingalia jinsi ulinzi mkali ulivyo, askari waliokaa juu kaabisa ya jengo walionekana kwa uzuri wakiwa na bunduki zao za kawaida tu wakiimarisha doria. Alipohakikisha ameridhika na utafiti wake, aliinuka na kulielekea gari lake, mara akasimama ghafla, baada ya kukuta watu wawili waliosimama katika gari yake mmoja upande huu na mwingine upande ule. Kamanda Amata aliwatazama harakaharaka watu wale waliovaalia suti nyeusi wakiwa na vipara vichwani mwao, kila mmoja alionekana kutafuna jojo ikiwa ni moja ya kupambana na baridi ya mji huo.

Kamanda Amata akaendelea kuifuata gari yake, hakutaka wajue kama ameshtuka kuwaona pale, akafika na kuwasalimu, lakini hakuna aliyejibu, akauendea mlango wa gari yake na kutaka kuufungua, Yule jamaa akamshika mkono kumzuia asiufungue ule mlango, kamanda Amata aligeuka na kumtazama, “Mnataka nini?” aliwauliza kwa lugha ya Kijerumani isiyo na kovu lolote, “Tunakutaka wewe!” mmoja alijibu, wakati huo Yule mwingine alikuwa akizunguka kuja upande ule, alipomfikia Amata akamshika ukosi wa kanzu yake na kumvutia upande ule wa pili alikokuwa wakati huo Yule mwingine alikuwa ameingia katika usukani akisubiri mateka wao apandishwe garini. Kamanda Amata alikuwa mpole kupita maelezo, alipofikisha kwenye mlango wa upande wa pili ndipo alipowaonesha kuwa yeye ni nani, liwiko kilichotua katika kidevu cha yule jamaa kiliangusha jino moja, kabla hajakaa sawa alimpa konde la kwanza na la pili ambayo yalimpeleka chini.

Yule wa ndani akaona mwenzake anazidiwa, akachomoa bastola aanze mashsmbulizi, akachelewa, Kamanda Amata hakuwepo mahali pale, alikuwa ametoweka kama mzuka, akiwa katika kushangaa hilo aliguswa mgongoni na Kamanda ambaye alikuwa nyuma yake upande ambao hakutarajia, alipogeuka alikutana na konde moja lililoshiba kisawasawa ambalo lilimpotezea mtandao kwa sekunde kadhaa, alivutwa chini na Amata na kupewa kichapo cha mbwa mwizi ambacho kilimuacha hoi, akamshika mkono wake huku akimshikisha bastola ileile akamgeukia yule mwingine aliyekuwa akijivutavua pale chini, kwa kupitia uvungu wa gari, alivyatua risasi moja ilifumua vyema goti lake kisha akamgeuzia huyu aliyekuwa naye na kumfanya kitu kilekile. “Mpeni ujumbe Bill, mwambieni kifo chake kimekuja mlangoni mwake,” Kamanda Amata aliwaambia kwa lugha ya Kijerumani na kuingia kwenya gari yake na kutokomea. Yule mwenye bastola akaona asipoteze nafasi, akacheza na bastola yake kulenga tairi la gari ya Amata lakini alishangaa vyuma vikigongana tu, alipotazama ile bastola haiukua na magazine, alibaki kuduwaa maana hakujua ni wakati gani imeondolewa.

Kamanda Amata aliendesha gari kwa kasi sana mara hii kuelekea misheni alikofikia, aliingia getini na kukuta misa ya maazishi ikiendelea, akaegesha gari na kuteremka harakaharaka, akauendea mlango mkubwa na kupanda kuelekea katika chumba chake, akafika na kujifungia chumbani, akaenda katika ule mtambo wake alioufunga pale dirishani na kuanza kuchunguza nyumba ile, hakujua ni jinsi gani wamejua kama yupo katika mji huo au wameotea kwa kuwa yeye ni mweusi. ‘Mara hii sipotezi nafasi,’ alijiwazia, akchungulia vyema kupitia ile darubini yake, akaangalia vizuri jumba lile tena kwa dirisha moja baada ya jingine, alipofika dirisha la ghorofa ya pili ndipo aliweka tuo kuangalia kinachoendelea. Hakuweza kusikia lakini aliweza kuona matendo ya watu wawili waliokuwa wakibishana kitu, alijaribu kuziangalia sura zao lakini hakufanikiwa kuzipata, akageuza darubini yake na kuangalia upande mwingine wa jengo lile.

Gari moja nyeusi aina ya BMW ya kisasa kabisa ilikuwa ikiegeshwa polepole kabisa mbele ya jumba lile huku ikifuatwa na gari nyingine mbili za mtindo ule. Mtu mmoja mnene, aliyevalia nadhifu kabisa alishuka ngazi akifuatwa na wanadada wawili na vijana wengine wawili waliokuwa kwenye suti nadhifu. Kamanda Amata aliendelea kuwachunguza na kuwaona wakiwa kamili na vyombo vya mawasiliano masikioni mwao, wote wakaingia katika magari na kisha ule msafara ukaondoka, na kuchukua barabara kuu kuelkea upande wa pili wa mji. Kamanda Amata akashusha pumzi, lengo lake yeye ajue kama Bill huwa anapatikana katika jumba lile au la. Alichomoa memorycard kutoka katika ile darubini akaipachika katika kompyuta yake kisha akatuma zile picha kwa Chiba Tanzania, acheki kama zina lolote. ‘Nimuueje Bill?’ alijiuliza, ‘Uso kwa uso au nimdungue kwa mbali?’ bado alikuwa akishindana na nafsi yake katika kuamua juu ya hilo, ‘Kumdungua ni kumuogopa, nitapambana nae,’ alikata shauri.

§§§§§

BILL hakuamini anchosikia kutoka kwa mmoja wafuasi wake, kuwa Kamanda Amata yupo Aachen na tayari ameshawajeruhi vibaya walinzi wa nje wa Andreas waliokuwa wakimfuatilia kule makaburini. “Nani aliwaambia yule mtu anafuatwa namna hiyo mliyofanya nyie?” Bill aliwauliza wale vibaraka wake. Baada ya kumaliza mazungumzo yake na watu wake, hakuna kilichokuja akilini mwake zaidi ya kukimbia mji huo na kujificha sehemu nyingine, ‘Lakini nitaonekana nimemuogopa, nitapambana nae hapahapa. Bill alitoka mchana huo na kuelekea mjini ambako baada ya pitapita zake akaingia katika kanisa kuu la mji huo, akiwa sasa medhamiria na ameamua kumsaka Amata kwa njia yoyote ile.

Alikuta watoto wakicheza cheza katika ngazi za kanisa hilo, mara mbele yake gari oja ilikuwa ikija pale aliposimama, Bill akaisimamisha, alikuwa ni Fr Frank, akitoka kwenda mjini kutafuta mahitaji, Bill aliiendea ile gari na kufungua mlango akaingia na kuketi kiti cha pembeni bastola mkononi, “Unahifadhi wanausalama sio?” alimuuliza Fr Frank ambaye alionekana kutetemeka mwili mzima. “Hapana, hapana,” akamjibu. “Huyo kasisi wenu mweusi ni nani? Si Kamanda Amata?” swali lingine lilitua sikioni mwa Fr Frank. Kisha Bill akamuamuru Fr Frank kuendesha gari mpaka maeneo anayoyajua yeye. Lilikuwa ni shamba kubwa ambalo lilikuwa na aina mbalimbali ya miti na mazao, Bill alimshusha Fr Frank na kumuongoza katika banda Fulani, akaingia, alichokifanya ni kumfunga kamba kisha kuanza kumpa mateso makali ili amueleze kama ni kweli wamemficha Kamanda Amata ndani ya nyumba yao, Fr Frank hakujibu kabisa swala hilo. “Unajifanya jeuri siyo, basi yatakupata yaliyompata Fr Gichuru kule Nairobi,” Bill alimwambia Fr Frank huku akimpa kipigo kikali kwa kutumia mkanda wa kijeshi.

Kisha akamuacha ndani ya banda hilo nay eye akaondoka kurudi mjini. Breki yake ilikuwa moja kwa moja ofisini kwa Andreas, kumpa habari hiyo nyeti. Andreas hakuonekana kuumiza kichwa kwa swala hilo. “Bill, nimeshakwambia fanya nunaloweza umuue bas, sitaki habari nyingine,” Andreas alisisitiza. Kabla hajajibu kitu, Andreas akamwambia Bill, “Ila leo jioni tukutane pale nyumbani kuna tafrija fupi kwa ajili ya kijupongeza kwa kukamilisha hili swala, na Fr Gustav atakuwepo maana tayari yuko njiani.” Bill aliupokea mualiko huo na akawa tayari kujumuika na wageni watakaokuwepo siku hiyo.

Fr Frank alibaki kule bandani peke yake, mwili wake ukiwa hoi kwa maumivu makali ya kipigo alichokipata kwa Bill, kwa kutumia ujanja alionao alijua jinsi ya kujinasua katika kifungio hicho, akafanya makeke yake na baada ya dakika kumi na tano alikuwa huru, sasa kilichomsumbua ni kupata funguo ya kutokea nje. Fr Frank alitafuta mahali pazuri kwa kujificha ndani ya banda lile akapapata, akajificha na kutulia tuli akisubiri yeyote atakayekuja aelewane nae.

Fr Frank hakuwa mjinga katika mapigano iwe ya mikono au ya silaha, alikumbuka sana alipokuwa jeshini mara baada ya kuhitimu masomo yake huko Austria, alipokuwa akijifunza karate na kungfu akiwa seminari, alimstahi Bill kwa kuwa alihisi labda kuna kitu atakachokigundua mahali hapo. Fr Frank aliajiriwa na FBI kisirisiri na alikuwa hapoa Aachen kwa kazi moja tu ya kumnasa Bill na kupeleka taarifa zote huko Marekani ili wajue jinsi ya kumnasa na kumuweka chini ya ulinzi. Hakutaka kujionesha juu ya hilo hivo alikuwa makini sana katika kulifanya. Ni miezi mitatu sasa tangu ahamishiwe katika kanisa hilo kuendelea na uchunguzi wake, na alikuwa akiju kila ktu kilichotokea kule Nairobi. Akiwa katika mawazo kule katika maficho yake alisikia mlio wa gari ikija maeneo yale akatulia na kusubiria watu hao ambao walikuwa wakizungumza wao kwa wao, harakaharaka alielewa kuwa watu hao wa[po watatu.

ITAENDELEA

Mauaji ya Kasisi Sehemu ya Tano

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment