Kitanzi cha Mwisho Sehemu ya Kwanza
KIJASUSI

Ep 01: Kitanzi cha Mwisho

SIMULIZI Kitanzi cha Mwisho
Kitanzi cha Mwisho Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE

*********************************************************************************

Sehemu ya Kwanza (1)

Maisha yanayotuzunguka yana mambo mengi sana, chuki, wivu, furaha, inda na mengi yanayofanana na hayo. wakati wewe unafanya kilicho halali wenzako wanafanya kilicho haramu, wewe ukinunua wenzako wanaiba ilimradi tu dunia ni kama tambala bovu.

wapo wasiopenda uishi kwa raha na wapo wanaokuombea maisha mema.

Binadamu tuna mambo mengi… kutana na msichana Yaumi uone shida alizopata kutokana na furaha ya watu wengine, Yaumi anaingia kwenye mzozo na watu asiowajua wala kujua… anataka kulipa kisasi kwa nini? twende pamoja….

TRAILER…

KELELE za watu waliokuwa wakikimbizana wakipanda ngazi za jengo moja zilisikika. Alikuwa ni mwanamke mmoja aliyevalia gauni tepe, refu lakini alilishika kwa mikono yake na kuifanya miguu yake kuwa huru, alionekana ni mwanadada aliyepitia kama si JKT basi MGAMBo maana alipanda ngazi kwa kukimbia huku nyuna yake akifuatiwa na kijana akiyeevalia suti nadhifu ya kijivu akiwa na bastola mkononi. Mbio zile ziliendendelea huku yule mwanaume akisikika akisema

“Simama, au la nakulipua,”

lakini yule mwanamke hakusimama aliendelea kupanda ngazi kwa kasi ileile, lakini mbio za sakafuni huishia ukingoni. Ilikuwa ni juu kabisa ya ghorofa ambako mwanamke yule alisimama akijiandaa kujirusha chini.

“Tulia hivyohivyo!” yule kijana alimnyooshea bastola yule mwanamke, akiwa anahema kama mbwa, yule mwanamke aligeuka upande ule wa yule kijana.

“Nimechoka, nimechoka kuandamwa nanyi kila wakati, sioni haja ya kuishi, nimehukumiwa kifo lakini mnanitesa tu, bora nijiue mwenyewe” alifoka yule mwanamke.

Akiwa bado kamnyooshea bastola yule mwanamke, Kamanda Amata alishusha pumzi na kutulia,

“Sikia mrembo, hapa upo kwenye mikono salama, sitaki kukudhuru, na kitendo cha kile kitanzi kukatika ni mimi niliyefanya hivyo, nakuhitaji wewe kwa shughuli za kiusalama, hakuna atakayekugusa, naitwa Kamanda Amata kutoka idara ya usalama wa Taifa kitengo kisicho na mipaka”

Yule mwanamke akashusha punzi na kuliachia lile gauni lake limfunike sehemu kubwa ya chini iliyokuwa wazi. Kamanda Amata alirekebisha tai yake na kuirudisha bastola yake katika kikoba maalum ndani ya koti lake. Akamsogelea yule mwanamke

“Unaitwa nani?” alimwuliza

“Yaumi” yule mwanamke alijibu kwa utulivu sana, hamu yake ya kujiua ilipotea ghafla na hamu ya kutimiza azma yake ilipata matumaini, kamanda Amata alimshika mkono na kuteremka nae ngazi za upande wa nje kwa maana alisikia kuna watu walipandisha juu kwa mgazi za ndani wakibishana kuwa mwanamke huyo yupo huku juu, polisi.

Waliteremka mpaka chini, Land Cruiser V8 yenye vyoo vyeusi ilisimama mbele yao, kamanda Amata almsukumia ndani Yaumi na yeye kufuatia, kisha ile gari ikaondoka kwa kasi.


YAUMI aliketi katika kiti cha mbao mikono yake miwili akiishikamanisha na kuiweka juu ya meza mbele yake na kuinamisha uso wake juu yake, nywele zake ndefu ziliuficha uso wake. Mawazo yalimtawala, hasira ilimshika, kisasi kikiujaza moyo wake, kwa nini Yaumi?

MAHAKAMA KUU

JAJI Ramson alitulia tuli juu ya kiti chake maalum, pembeni yake mezani kukiwa na kijinyundo kidogo, alitulia akisikiliza hati ya mashitaka iliyokuwa ikisomwa na mwendesha mashitaka wa serikali, mwanzo mpaka mwisho, ushahidi uliwasilishwa na Yaumi alkutikana na hatia ya mauaji dhidi ya mumewe bwana Kajiba A. Kajiba,

baada ya kuahirishwa mara nyingi kwa kesi hiyo hatimaye siku ya hukumu ilifika na jaji Ramson akasoma hukumu kwa lisasa limoja nanusu, Yaumi alihukumiwa kunyongwa hadi kufa, kwa kosa la kumuua mumewe na watu wengine watatu zaidi.

Jaji Ramson alimtazama Yaumi kwa huruma lakini sheria ilishachukua mkondo wake.

Askari polisi wa kike alimuongoza Yaumi kwenye landrova ya magereza na kuchukuliwa mpaka gereza la Segerea akisubiri kunyongwa kwake. Yaumi aliketi sakafuni kwenye chumba kidogo sana, pembeni yake kukiwa na kijindoo kwa ajili ya haja zake. Moyo wake uliuma sana, hasira ilimshika kwa nguvu, ‘wangeniacha nimalizie kazi yangu, kwani alibaki mmoja tu’ alijiwazia.


YAUMI, alikuwa akiishi na mumewe huko Tabata Kimanga, ndani ya nyumba yao walibaki wawili tu kwani watoto wao wawili wote walikuwa masomoni nje ya nchi. Yaumi na mumewe Kajiba walipndana sana daima walipenda kutoka wote kwenda outing, mara baharini au kwenye hoteli kubwakubwa, maisha ya upendo kati yao yalikuwa ndiyo nguzo imara.

“Mke wangu Yaumi, tumeishi kwa muda mrefu sasa maisha matamu ya ndoa, lakini kuna kitu sikuwahi kukushirikisha” Kajiba aliongea taratibu huku akinywa juice yake taratibu, akaendelea, “Sasa hv mimi mumeo naishi na roho mkononi, kuna watu wanataka kuitoa roho yangu, watu wangu wa karibu tu,” Kajiba akashusha pumzi na alionekana wazi kutetemeka tangu moyoni.

“Oh mume wangu, mbona wanitisha honey?” Yaumi aliuliza kwa hofu yenye mashaka

“Siku zote, unayekula nae na kunywa nae hutokea kuwa adui mkubwa na mbaya sana” Kajiba alisema.

“Ah! Sitakubaliana na hilo, kuna nini sweetie?” Yaumi alizidi kuhoji.

“Nitakwambia kila kitu, lakini kabla ya yote, nataka nikwambie kitu kingine cha msingi,” walitazamana kwa majonzi, Kajiba akainuka kitini na kumsshika mkono mkewe, wakatoka katika eneo lile na kutembea taratibu huku wakiwa wameshikana mikono,

“Nitakapokufa, utunze watoto wetu vizuri kabisa, hakikisha wanasoma mpaka mwisho, unajua tuna pesa nyingi sana kwenye benki za nje, hilo la kwanza, la pili nitakupa funguo, ya posta endapo nitakufa uende ukachukue kilichopo kwenye box hilo ujumbe wote utaupata humo,” wakiwa waktika ma zungumzo, mara ghafla

Toyota Prado nyeusi ilisimama jirani kabisa ya miguu yao, Kajiba akamvuta mkewe ypande wapili na kuwa nya wote waanguke chini kutokana na ule msukumo.

Kioo cha upande wa dereva kiliteremka taratibu wakati gari ile ilikuwa imesimama huku ikiunguruma, mtu mmoja aliyevaa miwani myeusi aligeuka kulia na kuwatazana Kajiba na Yaumi waliokuwa pale chini, hakuongea kitu ila alisonya na kupandisha kioo juu kabla ya kutimua mbiyo na gari hiyo. Kajiba na mkewe waliinuka kutoka vumbini na kujikung’uta vumbi.

“Nani yule?” Yaumi aliuliza.

“Ah! Wadau mke wangu” alijibu Kajiba.

“Lakini mume wangu, mi nahisi kuna kitu katikati yake huniambii” Yaumi alilalama.

“Wanaitafuta Roho yangu” Kajiba alijibu kifupi kama kawaida yake. Alisimama kidogo na kushusha pumzi huku mikono akiwa kaiweka kiunoni, akatikisa kichwa kisha akamshika mkono mkewe na kuendelea kutembea.

Walipofika mbele ya geti la nyumba yao Kajiba alisimama akamgeukia mkewe,

“Mke wangu, nenda dukani ukanunue ile wine unayoipenda, wakati tunakunywa nukueleze mambo yote,” alitoa wallet yake na kuchomoa noti kadhaa nyekundu kisha yeye akaingia ndani kumsubiri Mkewe ambaye alikuwa amekwenda dukani.


SARGEANT Magreth alibaki katega masikio akiwa amezungukwa na polisi wenzake pale kituo cha Tabata Jalil, mbele yao kulikuwa na simu ya kizamani kidogo iliyochakaa hapa na pale ilitoa sauti ya mtu anayelia na kutaabika.

“Mke wangu, mke wangu tafadhali, w….ananiua,”

mara ukasikika mlio wa risasi na kufuatiwa na kilio chenye maumivu, simu ile ikakatwa, ukimya ukatawala.

Land cruiser ya polisi ilifunga breki mbele ya nyumba ya mzee Kajiba na polisi wanne wakiwa na sargeant Magreth walikimbia na kuingia getini.

“Msishike geti!” Magreth aliwatahadharisha, wakaingia ndani na kukuta na mlango wazi, moja kwa moja macho yao yalitua kwa Yaumi ailiyekuwa ameshika kisu mkono mmoja na mwingine bastola akilia kwa kutetemeka huku mwili wa mume wake ukiwa umelala chini katika dimbwi kubwa la damu, jeraha la kisu kifuani mwake na tundu la risasi kichwani katika paji la uso.

Sargeant Magreth alimtazama Yaumi aliyekaa karibu na mwili wa mumewe akilia kwa kwikwi, Magreth alimuamuru askari mwingine kuchukua kile kisu na ile bastola kwa ajili ya uchunguzi. Baada ya itifaki za kiusalama kumalizika mwili wa marehemu ulichukuliwa.

” jamani mume wangu mimi wamemuua!” alili Yaumi huku akivalishwa pingu na Magreth,

“Nimekosa nn mimi?” aliendelea kulia Yaumi huku akipakiwa garini, watu mtaa mzima walisimama kwa huzuni wakiangali mwili wa Kajiba ukitolewa hali umefunikwa kwa shuka jeupe.


“Haya sasa! Hii ndiyo nyumba yako mpaka ukipata amri nyingine” ilikuwa ni sauti ya sargeant Magreth ikimuamuru Yaumi huku akimsukumia ndani ya chumba hicho na kumfungia kwa kufuli nyuma yake.

Yaumi aliendelea kulia na kumuomboleza mumewe, kilichomuuma zaidi ni ile hali ya kusubiri kuambiwa siri ile na mumewe, lakini likatokea la kutokea. Yaumi alijitazama jinsi alivyolowa damu katika dela lake alilovaa, aliuona mwisho wake, Yaumi akasimama akauegemea ukuta na taratibu akausotea kukaa chini.

‘Lazima nilipe kisasi, haiwezekani kama kufungwa ntafungwa tu lakini lazima nimsake muuaji’ mawazo hayo yalipita moyoni mwa Yaumi kwa kasi ya ajabu.

  • * *

SIKU YA KESI

“YAUMI Masharubu, umri miaka 36, kabila Mzaramo. Mnamo tarehe 26 mwezi wa 8 mwaka 1996 siku ya alhamis, saa moja na dakika 25 jioni katika nyumba yenu ya Tabata Kimanga, ulifanya mauaji na kumuua mumeo bwana Kajiba kwa kutumia kisu na bastola aina ya Magnum, ulikutwa ukiwa umeshikilia vitu hivyo huku mwili wako ukiwa umetapakaa damu za marehemu” ilikuwa ni sauti ya muendesha mashitaka PP Kibona.

Yaumi hakutakiwa kujibu kesi hiyo kwani mwenye haki ya kuifanyia maamuzi ni jaji pekee. Yaumi alipakiwa garini tayari kurudishwa Segerea kusubiri siku ya kesi itakapotajwa mara ya pili. Yaumi alitulia kwenye karandinga akiwa na mawazo tele, akipanga na kupangua juu ya hatima yake.

Yaumi alirudishwa lumande kusubiri siku nyingine ambapo kesi ile itasomwa tena. Usiku wa mng’amung’amu ulimpa tabu sana, ndoto za jinamizi na makorokoro mengine viliujaza usiku huo.


KICHWA cha Yaumi kilikuwa na mengi ya kuwaza na kuwazua, kupanga na kupangua, jinsi gani ya kumpata muuaji na kwa nini alimuua mumewe, ijapokuwa kwake alijua wazi kuwa kesi hiyo hana budi kuhukumiwa kifo, lakini asingependa kufa bila kuhakikisha kuwa kisasi dhidi ya muuaji wa mume wake kumalizika.

Akiwa ameketi katia kijitanda chake, Yaumi alikuwa akifikiri jinsi ya kuupata uhuru wake ili azma yake itimizwe. Alipojiridhisha na mipango yote kichwani alitulia na kupata usigiizi.

Asubuhi ya siku ilofuata ilimkuta Yaumi akiwa kakaa na kauegemea ukuta huku kichwa xhake kikiwa kimeegemea magoti yake.

“we!” sauti ya kiume ilisikika na kumgutusha, alimtazama kijana huyo polisi aliyesimama mbele ya mlango huo wa chuma.

“We ndio Yaumi?” aliuliza

“Ndiyo”

“Ok,” akaingiza mkono mfukoni na kutoa funguo kisha akafungua lile geti na kumpa ishara ya kumfuata naye akafanya hivyo. Hatua chache ziliwafikisha katika chumba fulani kikubwa tu chenye vitu vichache, meza moja na viti kadhaa, kila kiti alionekana kuketi mtu mmoja isipokuwa kimoja tu, Yaumi alijua kuwa kiti hicho bila shaka ni chake, alikiendea akaketi juu yake, mbele yake kulikuwa na kijana mmoja polisi aliyevaa kiraia ila muonekano wake wa nwele ulimtambulisha kuwa huyo ni polisi, walitazamana kidogo na Yaumi, kisha yule polisi akajikooza.

“Sasa Yaumi, nipo hapa kwa kazi moja tu, tunapenda utueleze ukweli kabisa juu ya mauaji ya mumeo ili tuone jinsi ya kuiweka kesi hii na we urudi uraiani, haya nambie kwa nini ulimuua mumeo bwana Kajiba?”

Yaumi alitumbua macho kwa swali hilo,

“Nani amekwambia kuwa mimi nimemuua mume wangu?”

“Faili lako linaonesha hivo, na umekutwa ukiwa umeshika kisu na bastola, bila shaka kwa macho ya kibinaadamu hapo wewe utatuhumiwa kuwa muuaji”

“Ni kweli afande lakini mimi si muuaji, na wala sijamuua mume wangu, na nina hamu ya kumjua aliyefanya hivi”

“Yaumi usituzungushe sana, tuambie umeua au la?”

“La” Yaumi alijibu huku machozi yakimtoka na mwili kuanza kutetemeka.

“Utanyongwa Yaumi kama hutosema ukweli” yule polisi aliendelea kumchokonoa.

“Acha tu waninyonge, kwanza sioni faida ya kuishi bila mume wangu” akajibu.

Kila alichoeleza Yaumi kilikuwa ni ngumu kukubalika na watu hawa.

Baada ya hapo Yaumi akarudishwa lumande na kuwaacha wale jamaa pale.

“Anaonekana hajui kitu” aliongea mtu mmoja mwenye ndevu nyingi.

“Umeona ee! Basi hili limekwisha, tuangalia mengine” akasema yule polisi. Ilionekana wazi kuna kama mchezo unaochezwa lakini kwa nini? Hakuna ajuae.


Nyumba ya Kajiba ilikuwa imefungwa, hakuna mtu aliyeishi kila kitu kiliachwa kama kilivyo, mchana huo mtu mmoja alikuwa ndani ya nyumba hiyo ambayo ilikuwa chini ya uchunguzi wa polisi kwa kufungwa utepe maalum wa njano, lakini huyu ni nani hata aingie ndani humo na asionekane na watu. Alizunguka chumba hiki na kile akafungua hapa na pale, ilionekana akitafuta kitu fulani ambacho hajui wapi kimewekwa, aliendelea bila mafanikio, meisho akaamua kurejea alikotoka bila kupata tafutishi yake.

Uchunguzi uliendelea lakini katika kila walilolifanya bado ilikuwa ngumu kujua chanzo cha mauaji hayo.

“Nyie mnasumbuka bure, hata ile simu aliyopita marehemu, kama mnakumbuka alikuwa akimtaja mke wake kuwa anamuua, sasa nyie hapo mnafanyaje? Huyu ndiye muuaji”

wote walitazamana na kuonekana kuafiki.

Yaumi alikuwa kasimama katika mlango wa selo mara tu yule askari alivoondoka, akagundua kitu kuwa lile kufuri halikubanwa sawasawa, akalishika na kulitikisa, he! Kumbe halikufungwa sawasawa, aalilizungusha taratibu na kulitoa pale kwenye komeo kisha akafungua mlango mdogo na kuikanyaga sakafu ya coridor ndefu inayoelekea huku na kule, akatazama kushoto kisha kulia na kutoka kwa minyato kuelekea kushoto, mwisho wa ridor ile kulikuwa na kijimlango kidogo ambacho alikitumia kutoka nje na kuukabili uwanja uliokuwa hapo, lakini mataa makali yalikuwa yakimulika eneo hilo, akafikiri mara mbilimbili atapita vipi, hakupata jibu. Kutoka pale alipo akambaaambaa na ule ukuta mpaka katika ukingo wa jengo hilo kisha akakatulia kuongalia kama kuna anyekuja upande huo, mara kivuli kikubwa kikawa eneo hilo, kumbe ile taa iliyo katika kibanda cha mlinzi huwa inageuka huku na kule, Yaumi aliona hiyo ni bahati ya mtende, alikimbia kwa hatu ndogondogo na kukatisha kale kauwanja mpaka chini ya banda mlinzi na kujificha chini yake akitazama huo ukuta mrefu ulimuwekea pingamizi, machozi yalimtoka hakujua afanye nini kutimiza lengo lake, hakukata tanaa, kwa njia ya kificho aliendelea kutembea huku akiiangalia ile taa kama inamgeuki ili ajifiche, akiwa katikati ya ule ukuta, Yaumi alihisi ile taa inammulika na tayari wakati huo alibakisha kipande kidgo afike upande wa nyuma wa gereza hilo….

YAUMI alijificha karibu na nguzo iliyoushika ukuta ule wakati ile taa kubwa ilipokuwa inamulika upande huo, mwanga mkali ulimulika pale alipo kwa sekunde kadhaa, Yaumi alishikwa na woga mkuu akajua kuwa sasa atakamatika, mara ule mwanga ukageukia upande mwingine.

TARATIBU aliambaa na ukuta ule, Mungu si Athumani mbele yake alikuta matofali yaliyopangwa tayari kwa ujenzi, kwa hadhari kubwa akakwea yale matofali na na muda kidogo akajikuta juu ya ukuta ule na upande wa pili kulikuwa mti wa muarobaini, ‘Aliyepanda mti huu, abarikiwe na Bwana’ alijiwazia wakati akishika moja ya tawi la mti huo na kuteremkia kwa nje.

  • * *

Ulikuwa ni usiku wa mbala mwezi pevu, Yaumi aliiona nyumba yake kwa mbali akiwa katika tax.

“Simama hapa dukani,” alimuamuru dereva, “Nakuja sasa hv usiondoke” aliongeza, kisha akavuta hatua na kupita kati ya kichochoro kimoja kilichotenganisha nyumba mbili, upande wa pili alitoke nyuma ya nyumba yake aliyokuwa akiishi na marehemu mumewe, hakukuwa na dalili ya watu eneo hilo kwani msiba ulihamishiwa kwa dada wa marehemu. Moja kwa moja alikwenda katika sehemu yao ya siri na alipohakikisha usalama alichimba kishimo pembezoni mwa ukuta na kuchomoa kijaruba cha ngozi kisha akafuata ule ukuta na kufikia mlango mdogo uliopo pembeni mwa ukuta huo, Yaumi aliutomasa kwa moja ya zile funguo nao ukafunguka, akaingia ndani ya ua mkubwa sana, pale alikuta gari zake tatu zikiwa salama kabisa, akausogelea mlango wa kuingilia ndani na kutulia kidogo, alipohakikisha ukimya akaufungua mlango huo na kuingia ndani kisha akavuta hatua fupifupi na kupanda ngazi kuelekea chumbani kwake na kuingia, moja kwa moja aliliendea kabati na kwa kutumia kitambaa maalumu alichojifunga kiganjani aliivuta droo ya kabati hilo,

‘Ewaaaaa’ alijitamkia moyoni alipohakikisha kile anachokitaka kipo, akatoa basola moja na risasi kumi na nne kwenye kikasha chake, kisha akachukua kisu na documents fulanifulani, droo ya pembeni alitoa kijibriefcase kidogo na kuvitia vitu hivyo, aliendea droo ya kitanda na kutoa kadi za benki na burungutu la pesa lililowekwa hapo, Yaumi alitazama chumba chake vizuri, aligundua wazi kuwa kuna vitu havijakaa sawa, wasiwasi ulimjaa, akashuka ngazi mpaka sebuleni akiwa na peni na karatasi, mwendo wake uliishia kwenye dimbwi la damu ambayo sasa ilishaganda na kutoa harufu nzito, aliitazama ile damu ya mumewe na kupiga magoti kisha akaandika vitu fulani kwenye ile karatasi yake huku akitazama sehemu ile iliyo na damu.

+256-16841-5576 pos, Yale maandishi yaliyojalizwa kwa namba nyingi yaliishia hapo, Yaumi alifikiria sana juu ya namba zile hakujua maana yake nini na hakujua kwa nini mumewe aliandika namba hiyo kwa kutumia damu yake kabla ya kukata roho. Alikikunja kile kikaratasi na kukifutika katika nguo yake ya ndani. Alipokuwa katika harakati za kutoka alisikia mngurumo wa gari ikisimama huko nje na watu waliokuwa wakiongeaongea walisikika wakiuendea mlango mkubwa wa nyumba hiyo.

Yaumi, alijificha nyuma ya kabati la jikoni ambapo alihakikisha anaweza kuona watakapoingia, mara mlango ukafunguliwa watu wanne wakaingia ndani ya sebule hiyo, wakasimama katikati ya sebule kwa mshangao, wakikodolea macho pale palipokuwa na damu iloganda ambayo sasa haikuwepo kama mwanzo ilikuwa imesafishwa yote lakini iliachwa kwa maandishi ‘REVANGE’ kisha mbele yake kukiwa na risasi moja.

Kutoka pale alipojificha, Yaumi aliwaona wale jamaa jinsi walivyochanganyikiwa.

“Mh!” mmoja aliguna huku akiivua kofia yake aina ya pama.

“Ina maana kuna mtu aliingia humu ndani?” aliuliza mmoja wao

“Kitendawili hicho” mwingine alijibu.

“Naanza kuwa na wasiwasi, nani huyu? Vijana, tumsake tummalize atatuletea shida huyu kabla hatujaanza msako wetu. Ila hakikisheni leo lile faili tunalipata” kiongozi wao alieleza.

“Faili lipi boss?”

“Kuna faili tumehifadhi mambo yetu nyeti ambalo huyu Kajiba analo, kwa maana nina uhakika na hilo, kile kibegi kule nyumbani ni cha kwake, so ina maana yeye kachukua cha kwetu baada ya ile ajali pale Magomeni, hebu chunguzeni”


YAUMI alitetemeka pale alipo, sasa picha ilianza kumjia juu ya kifo cha mumewe, alikumbuka siku ambayo mumewe alirudi usiku sana akamwambia kuwa walipata ajali magomeni hivyo katika pilikapilika za huku na huko alichelewa kurudi nyumbani, alifika na kutupia mezani briefcase ndogo nyekundu na yeye kwenda kuoga huku akimuachia mkewe kazi ya kuweka sawa makabrasha yao ya biashara ambayo yapo ndani ya briefcase ile. Kilichotokea ni kuwa Yaumi alishindwa kuifungua kwa zile namba alizozizoea akampa taarifa mumewe naye alipojaribu alishindwa, akahisi kuchanganyikiwa, akamruhusu kuvunja ile briefcase, Yaumi akafanya hivyo, ile briefacase ikavunjika na macho ya Yaumi yalikutana na faili moja jekundu, alipigwa na butwaa akamtazama mumewe.

“Vipi mbona unashangaa?” Kajiba alimuuliza mkewe huku akiivuta ile briefcase upande wake.

“Hili faili humu ndani mbona siyo nililolizoea mpenzi?” Yaumi aliuliza.

Kajiba alilitazama lile faili akaliinua kutoka pale lilipokuwepo na kulifungua kuona vilivyomo.

Kajiba alibaki kaduwaa juu ya hilo faili, kurasa ya kwanza, ya pili na ya tatu zilimuwacha mdomo wazi. Hakujua nini kimetokea, alilichukua lile faili na kuliweka juu ya kitanda kisha akaenda zake kuoga akimwacha Yaumi akiwa pale chumbani.

Baada ya kuoga alirejea kitandani kuungana na mkewe lakini kabla alilipitia tena lile faili na kushtushwa na yaliyoandikwa, akalifunga na kulihifadhi vizuri kabatini kisha akajilaza lakini kichwani mwake kulikuwa na mawazo mengi sana.


YAUMI aliendelea kuwaangalia na kuwasikiliza wale watu waliokuwa bado pale sebuleni.

“hebu kafanyeni upekuzi huku na huko tuondoke” huyu mmoja aliwaamuru wenzake, nao wakatii amri na kufanya upekuzi katika nyumba ile. Baada ya dakika kadhaa wote walirudi pale sebuleni,

“Hamna kitu boss!” mmoja alitoa taarifa.

“Dah! Huyu jamaa katuweza aisee, sasa hapa tudili na mkewe lazima anajua kitu” yule boss alisema

“Sasa mkewe yuko lumande tutampataje?” mwingine aliuliza

“Aaa hilo lisiwaumize kichwa, uko huko lumande ataeleza kila kitu. Boss anataka jibu haraka iwezekanavyo” aliongea huku kasimama na kuuelekea mlango wa kutokea nje akifuatiwa na wale wenzake kisha wakaufunga mlango.

Yaumi alisikia mngurumo wa gari alitamani hata japo ajue namba zake lakini haikuwa hivyo. Aliitazama ile briefcase yake pale chini na zana alizozichukua kule chumbani, akaiangalia saa ya ukutani, ilikuwa yapata saa saba za usiku.

‘Yanipasa kurudi’ alijisemea kisha taratibu akatokea mlango wa nyuma ule ule alioingili na kuficha funguo mahali pale pale. Akiwa ndani ya baibui hakuna aliyeweza kumtambua alipokuwa akipita mbele ya nyumba yake na kuiona ikiwa bado imefungwa ile mikanda ya plastiki ‘police line’.

Akavuta hatua za haraka haraka na kusimama barabarani, kidogo tu ilipita tax akaisimamisha.

“Tabata tafadhali” alimwambia dreva tax. Haikuchukua muda aliwasili na kumlipa dreva tax kisha yeye kutokomea gizani.

Mwendo wake uliishia mbele ya nyumba ya wageni Bondeni Lodge akapanga chumba kimoja kidogo cha thamani ndogo. Akaweka kibegi chake cha nguo na ile briefcase akaificha juu ya dari ili wafagizi wakija wasiione, akafanikiwa.

Aliketi kitandani na kuichukua simu ya mumewe, marehemu Kajiba na kuiwasha kisha akatulia kusubiria kitakachotokea katika simu hiyo.

‘Usipotupatia lazima tukupoteze’

Ilikuwa ni meseji iliyotumwa saa 24 kabla ya kifo cha mumewe, akapekua tena na tena.

‘Endelea kujifanya jeuri, lakini utaiona faida yake’

Ilikuwa meseji nyingine.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

‘Tunajua kuwa umechukua briefcase yetu kama sisi tulivyoichukua ya kwako, tuko tayari kukupa ya kwako, utupatie ya kwetu pia’

Ilikuwa meseji ya nyuma zaidi.

Yaumi aliishiwa nguvu, ‘kwa nini siku zote hakuniambia’ alijiuliza huku macho yake yakijawa na machozi.

Aliichukua ile simu na kujaribu kuangalia namba iliyotuma meseji zile; private namba, akaishiwa nguvu lakini alijipa moyo. ‘Lazima nilipe kisasi kwa ajili ya mume wangu mpendwa’, aliizima ile simu na kuipandisha darini kisha akatoka na kuufunga mlango.

“Dada natoka naenda kazini mara moja nitarudi kwa kuchelewa sana, usishangae kutokuniona si unajua kazi zetu za usiku sisi warembo” alisema huku akimkabidhi funguo na noti ya shilingi elfu kumi.

“Hii utakunywa japo soda” kisha akaondoka zake na kupotelea gizani.

Kwa mtindo uleule Yaumi aliuzunguka kwa tahadhari ukuta wa gereza la Segerea mpaka upande wa nyuma kulikokuwa na nyumba chakavu akavua lile baibui lake na kulisweka ramboni kisha kuuficha ule mfuko kwenye kijichaka na yeye kuufuata ule mti wa Muarobaini na kuukwea ili kuingia ndani, alipofika juu alitulia kuangalia usalama na alipoona pana ukimya akashukia ndani kupitia yale matofali, huku akiukwepa ule mwanga wa ile taa kubwa alifanikiwa kurudi mahali pake na kujifungia kwa ndani, mara alisikia nyayo za watu zikielekea upande ule

“Una uhakika lakini?” mmoja alimuuliza mwenzake

“Aaa sana nimekwenda mpaka pale hakuna dalili mi naona yale ni mashuka tu, katoroka huyu” mwingine alisema. Yaumi aligundua kuwa kuna uwezekano kuwa walikuja kumtazama na wakamkosa, alijifunika shuka lake la jela na kutulia kitandani, uzuri ni kwamba lumande ya wanawake huwa haijai kwa hiyo wanalala kwa raha tu.

“Itakuwa aibu sana kutorokwa na maabusu, sijui tutaeleza nn sisi?” sauti zile zililizidi kukaribi na mara wadada wawili wakatoke pale mlangoni na kutazama ndani ya chumba kile.

“Ha! Si yule pale au macho yangu?” alisema mmoja wao

“Mh, hii miujiza, mi nimefika mpaka pale hakukuwa na mtu” alisisitiza yule wa kwanza.

“Tutamhoji kesho vizuri muache alale”


MAWAZO yalikijaza kichwa cha Yaumi, mambo mengi yalipita kama mkanda wa filamu, wakati yeye akiwa amejikalia juu ya kijitanda kidogo mwili wa mumewe ulikuwa bado mochwari ukigandishwa kwa barafu mapaka mamlaka husika itakapoamua uzikwe.

Kila mtu aliyemjua bwana Kajiba alisikitishwa na kifo hicho, japokuwa watu wengi walisikia kuwa Kajiba kauawa na mkewe, wengine wengi hawakuliamini hilo.

“Hata kama ni mahakamani nitamtetea” alisikika mzee mmoja wa kipemba akisema hayo.

+256 Iilikua ni namba inayokuja na kutoka kichwani mwa Yaumi, hakujua kuwa ile namba yote ni ya simu au ni ya kitu gani, kama ni ya simu simu hiyo ina maana gani, ulikuwa ni mtihani mgumu kwake.

‘Leo nikifanikiwa kutoka nitapiga hii namba’, lakini atamueleza nini mtu atakayepokea? lilikuwa ni swali lingine ambalo halikupata jibu. Alikirudisha kile kikaratasi kweny chupi yake tena baada ya kusikia kuwa kuna watu wanakuja upande ule.

Askari wawili wa kike walikuja na kusimama mlangoni, mmoja alikuwa na chupa ya chai na mkate,

“Chukua unywe! muuaji wewe” aliongea kwa ukali, maneno hayo yalimchoma sana moyoni Yaumi, alitamani amrukie amafanye lolote lakini haikuwezekana. Alisogea hadi mlangoni na kuchukua vile vitu.

“Kwanza jana usiku ulienda wapi?” yule askari alimuuza Yaumi.

“Nitaenda wapi wakati mi mmenifungia humu?”

“We mwanamke usijifanye mkorofi, jana usiku nimekuja hapa sijakukuta”

“Basi hujaja!”

Sonyo refu lilimtoka yule askari, kisha akampa ile chai na kuondoka zake. Yaumi alirudi na kuketi katika kile kitanda akinywa chai taratibu huku bado mawazo yakiwa mengi kichwani, hakuelewa kama alionekana wakati anatoroka au huyu askari kaamua tu kusema hivyo, hofu ilimuingia na akajihisi kutetemeka kwa woga.

Alimaliza kunywa ile chai na kusogeza vile vyombo jirani na mlango kisha akarudi na kuketi palepale na kuendelea na fikra zake, alijaribu kuvuta hisia kurudi nyuma kukumbuka matukio ya mumewe kabla ya mauaji yale labda angepata picha. Kama kuna kitu kilimjia kichwani ni zile meseji alizosoma kwenye simu ya mumewe usiku ule ‘…uliichukua katika ajali pale Magomeni…’ hii ilimvuta zaidi, ajali ya Magomeni, akakumbuka siku ambayo mume wake alirudi na ile briefcase alimsimulia kwa kifupi tu kuwa kulitokea ajali, hakuwa na shaka kwa kuwa briefcase ile ilikuwa vilevile kama ya mumewe cha kushangaza tu iligoma kufunguka kwa namba zilizozoeleka.

TUKIO LA AJALI MAGOMENI…

ILIKUWA usiku wa saa mbili katika makutano ya barabara ya Morogoro na ile ya Kawawa, mvua ya rasharasha ilikuwa ikinyesha, Toyota Coaster moja iliyokuwa na abiria ilikuwa ikitokea Ubungo kwenda Kariakoo kwa kasi ya hatari, ilikuwa ikifanya ovateki za ghafla mpaka kila abiria alikuwa akilalamikia uaendeshaji huo.

“Utatuua bwana watu tuna familia nyumbani!” alisikika mama mmoja.Kiti cha tatu nyuma ya dereva alikuwa ameketi bwana Kajiba mikononi ameikumbatia briefcase yake yenye makabrasha yake ya biashara , vitabu viwili vya hawala za fedha na kitita cha milioni nne, alikuwa akirejea nyumbani kutoka katika makusanyo ya biashara zake. katika mtindo uohuo kiti cha nyuma kabisa kulikuwa na watu wawili walioketi hapa na hapa, mmoja wao alikuwa na briefcase ndogo inayoshahabiana kabisa na ile ya Kajiba kwa kila kitu.

Ile Coaster ilishafika katika taa za makutano ya barabara, haja ya dereva ilikuwa awahi kuvuka na taa zile za kijani lakini la, alipokaribia tu taa ya nyekundu ikawaka bila kutanguliwa na ile ya njano, kuangalia kushoto barabara inayotoka Kigogo tayari kuna semi Trailler ilikuwa imeshaingia kwani ni zamu yake kupita. Dereva akakanyaga breki kwa nguvu zake zote breki zikafeli na ile coaster ikaendelea kutiririka sasa kwa kasi zaidi na kuingia ubavuni mwa ile Trailer, lo! vilio vilisikika kila kona ile gari haikutamananika hata kidogo. Katika harakati za kutaka kujiokoa kila mtu alikuwa akifikiri njia yake, Kajiba alisimama kutoka katika kiti alichokaa baada ya kujitutumua kwa nguvu zote kwani alilaliwa na watu kutoka viti vya nyuma, alipofanikiwa aligundua kuwa ile briefcase yake haipo mkononi, akatazama huku na huko akaiona kwa mbali ikiwa kwenye sakafu ya gari hiyo, akaiwahi na kuicvhikua kisha akatoka nje ya gari na kuitazama ajali hiyo jinsi ilivyokuwa mbaya, alipogundua kuwa hajaumia popote aliamua kuondoka eneo hilo na kurudi nyumbani….

UBONGO wa Yaumi ulivuta kumbukumbu nyingi juu ya matukio ya nyuma. Alilisogelea geti lililokuwa limetenganisha yeye na wengine walio upande wa pili. Katika geti la mbele yake ambalo lilitazamana na lake na kutenganishwa na ujia wenye upana wa kupita suzuki kulikuwa na mwanamke mwingine aliyevaa juba lililomfunika mwili mzima.

Alizishika nondo za geti lile kwa mikono yote miwili na kichwa chake kukiegemeza kwenye nondo hizo kwa kugusisha paji la uso.

Mara akasikia mtu akipiga kofi moja hafifu, Yaumi aliinua uso wake na kutazama ilipotokea sauti ile. Macho ya wanawake hawa yaligongana, Yaumi alimtama mwanamke yule kwa tuo, zaidi ya macho yake aliyoweza kuyaona ni juba kubwa la kijani, zito, lililomfunika sawia. Mtazamano ulichukua sekunde kadhaa,

“Hey!” Yaumi aliita kwa sauti ya kunong’ona, lakini alishangaa yule mwanamke alikuwa akimtazama tu huku akigeuzageuza kichwa chake, Yaumi alimtazama akiwa amekunja uso, yule mwanamke akapiga tena kofi lamtindo uleule na kutoa ishara fulani kwa kutumia miko yake akimuonesha Yaumi kuwa yeye alikuwa hasikii, kiziwi.

Bahati iliyoje kwa Yaumi, kukutana na mtu wa mtindo huo. Yaumi alitikisa kichwa kuashiria ameshukuru kwa hilo, alimkumbuka baba yake mwalimu Juma Saanane aliyekuwa akifundisha shule maalum kwa watu hao, alikumbuka siku moja baba yake alimwambia,

“… Mwanangu Yaumi, jifunze lugha ya alama, siku moja utajikuta kwenye matatizo na wa kukupa msaada anajua lugha hiyo tu…”

Yaumi aliangusha machozi kumkumbuka marehemu baba yake, akamshukuru moyoni kwa unabii wake, alijifuta machozi na kuanza kuongea kwa ishara. Walipojikuta wanaelewana vizuri, urafiki mkubwa ukajengeka kati yao. Yaumi alijua kuwa yule dada ni Msomali aliyekamatwa kwa kuuza mirungi na bangi katika maeneo ya Buguruni, hayo yote alimueleza kwa lugha hiyo ya alama. Yaumi aliona kuwa ni jambo zuri kufahamiana hasa kwa lugha ambayo hakuna mwingine anaijua, kwa kutumia lugha hiyo, Yaumi alimueleza juu ya namba ile +256 na nini maana yake, bial kusita yule dada alimueleza juu ya maana ya namba hiyo kuwa ni international code ya Uganda, Yaumi alishtuka kidogo ‘Uganda’ akajiwazia. Baada ya kujua kuwa huyo dada Msomali anaishi Buguruni kwa Mwinyi Amani au kwa Mnyamani kama inavyotamkwa na namba ya nyumba, Yaumi alifurahi sana, aliona kuwa huyu anaweza kuwa msaada pekee kwake.


“Wewe jana usiku ulienda wapi?” sargeant Marina alimuuliza Yaumi huku wakiwa wanatzamana ndani na nje ya geti la chumba kile.

“Mi nilikuwapo, nililala uvunguni” Yaumi alijibu, jibu lilimkera sana yule askari magereza Sargeant Marina.

“Acha upumbavu we mwanamke,”

“Sio upumbavu, mi nitatokaje huku na kumefungwa, we askari mbona hutumii akili?!”

“Hivi wewe unajiamini nn? Kwa taarifa yako sasa, hukwepi kifo, jana ulitoroka na taarifa zako tunazo, usirudie tena, muuaji mkubwa wewe”

Kama kuna kitu kilikuwa kinamuudhi Yaumi ni kuitwa muuaji, alimtazama kwa jicho kali yule askari kisha akamsonya sonyo la haja lililomtia hasira yule askari.

“Kwa nini we mwanamke unanifuatafuata sana? Nimeshakumaki sura, ntadeal na wewe, najua kuwa unafahamu mengi juu ya ishu hii,” Yaumi alizungumza hayo kisha akavigongesha vidole vyake, aliiona wazi hasira iliyomshika yule askari mwanzo mwisho. Sargeant Marina alimtazama kwa tuo Yaumi.

“Najua nitakachokifanya kwako subiri” Marina alimjibu kisha akaondoka zake eneo lile.

Yaumi alishusha pumzi ndefu na kujikaliza kitandani huku akipambana na mbu wa mchana, alimtazama yule swahiba wake upande wa pili hakumuona, muda ulikwenda masaa yakakatika hakumuona kurudi, hata wenzake waliporudi kutoka mahakamani yeye hakurudi, hii ilimtia hofu Yaumi, moyoni mwake alijiwekea tu kuwa swahiba wake ametoka kwa dhamana, kwa hiyo lazima amtafute labda atapata msaada kutoka kwake.

Yaumi aliendelea kutulia, alijua wazi kuwa baada ya siku tatu ni kesi yake itasomwa mara ya pili, alijuwa wazi kuwa mchezo mchafu unasukwa juu yake, bila kipingamizi alijua wazi kitanzi kilikuwa kinasukwa ili kummaliza,

‘Kabla sijanyongwa, lazima nilipize kisasi kwa lifo cha mume wangu’

alijiwazia Yaumi huku akipigapiga ngumi kile kijitanda chake kisha akainamisha kichwa chake na kulia kwa kwikwi.

‘Mume wangu, niongoze nijue siri ya kifo chako, nilipize kisasi kabla sijaja kuungana nawe huko kuzimu, wewe wajua kila kitu mimi sielewi chochote…’

Yaumi alifuta machozi, na kuketi kwenye kona moja ya kijichumba hicho akisukwasukwa na njaa kali maana mchana huo hakuwa nachochote cha kula, hata chai ya asubuhi hiyo hakujua ni nani aliileta. Alijaribu kufikiri kama ni busara kutoroka usiku huo ili kuweza kumuona yule Msomali japokuwa hakujua kuwa kafungwa au yuko nje kwa dhamana.

»»»

YAUMI alijilaza sakafuni njaa ilikuwa ikimnyanyasa kuliko unavyofikiria, akiwa bado katika hali ile mara alihisi muanguko wa kitu kando ya miguu yake, alipofumbua macho yake japokuwa kwa shida kidogo aliweza kuona mfuko wa plastic uliofungwa vizuri ndani yake kukiwa na mkate, pemeni yake kuna chupa ya maji aina ya Ndanda, aliviangali vitu vile lakini hakuona nani aliyevirusha humo ndani.

“Nyanyuka ule mrembo muuaji,” sauti ya sergeant Marina iliingia kwa mara nyingine masikioni mwa Yaumi, sauti asiyoipenda hata kidogo. Aliinua zaidi uso wake na kukutana na sergeant Marin aliyekuwa katika nguo zake za kazi, shati jeupe na sketi yake ya rangi ya ugolo.

YAUMI alivichukua vile vitu na kuvitazama kwa makini, kisha akamtazama tena Marina ambaye bado alikuwa amesimama palepale kwenye lile geti.

“Ulizoea kukaa kwenye meza kubwa ukila mapochopocho ya kila aina, sasa unalo hilo, kula mkate huo shushia na maji, maana usiku wa leo una wageni” Marina aliendelea na maneno yake ya unyanyasaji yaliyokuwa yakimtesa sawia Yaumi. Kma alitarajia kuwa Yaumi angekula ile mikate basi haikuwa hivyo, Yaumi alisonya na kuirushia uvungu wa kitanda, kisha akajilaza pale chini na kufunga hisia za masikio na macho yake. Sergeant Marina alikasirishwa kwa kitendo cha Yaumi, hakusema neno zaidi ya kumtazama kwa dharau na nyodo, ndipo akafuangua mdomo wake,

“Utakula tu, na njaa inavyonyanyasa, haya nitarudi baadae” akaondoka kutoka pale aliposimama. Yaumi akatazama na kumtomuona askari yule aliyekuwa mwiba mchungu kwa maneno yake.

‘Kwa nini ananifuatafuata hivi? Lazima kuna kitu’, Yaumi aliwaza akawazua; ‘Labda nisitoke humu ndani, nitakula nae sahani moja’ Yaumi alijiapia kwa hilo.

Baada ya kama masaa mawili jioni ilipoanza kuingia, Yaumi alisikia jina lake likitajwa na mmoja wa askari waliokuwa eneo hilo, mara yule askari msichana mdogo ambaye hata maziwa yake bado hayajaanguka alikuja na kumpatia chai pamoja sambusa nne, alivipokea, kutokana na njaa aliyokuwa nayo hakuuliza hata vimetokea wapi na vimeletwa na nani, alianza kuvishambulia kwa fujo, alipochukua sambusa ya pili aligundua kitu tofauti, kitu kama karatasi ndogo kilichoviringwa kwa ustadi katikati ya chembe za vitunguu ndani yake, Yaumi akakitazama kisha akakifungua na kukuta unga mweupe sana mithili ya vumbi kwa udogo wake, kwa kuwa hakujua ni nini alikikunja tena kwa mtindo uleule na kukirudisha ndani ya sambusa ile kisha akaiweka pembeni na kula ile ilobakia.

Giza lilianza kutawala nuru ya nje na mataa nayo yakaanza kuwaka kila kona, kelele za ndege katika mapori ya Segerea na Kinyerezi yalianza kupotea na ukimya kuchukua nafasi yake, ‘lazima nitoke, liwalo na liwe’ alijiwazia wakati mwili wake ukikusanya nguvu kutokana na chai ile aliyoipata jioni ile.

“Yaumi!” sauti iliita, alitazama na kumuona yule askari msichana akiwa amesimama pale katika mlango wa nondo uliokidhibiti kijichumba kile, akamuoneshea ishara ya kumuita kwa kidole kimoja, nae akaitii akaenda mpaka pale, watazamana kwa muda, yule askari akamuoneshea ishara ya kutaka kitu, Yaumi akachezesha akili yake kwa haraka, hakutambua mara moja askari yule alitaka nini.

“Unasemaje?” alimuuliza yule askari msichana

“Sambusa” alijibu. Yaumi mara moja akenda na kuitoa ile sambusa ambayo aliyokuwa ameimega kipande akamletea yule askari, akaipokea na kuchomoa kile kikaratasi kilichoviringwa na kuondoka nacho si kuelekea nje bali ndani zaidi ya lile gereza la mahabusu la Segerea. Yaumi hakuelewa kinachoendelea, alirudi na kuketi akisubiri muda wa tarumbeta ya kulala ufike ili afanye yake.

˜˜˜˜

“Sijawaelewa mnachokisema, ina maana kuna shetani lilikuja na kuingia ndani ya nyumba hiyo? Ilhali tumeifunga na ipo chini ya ulinzi kwa uchunguzi.” Sauti nzito ilisikika ikiwauliza swali hilo vijana watatu na kiongozi mwingine mmoja ambaye alionekana kuwa ndiye wa kujibu maswali hayo.

“Kwa kweli hatujaelewa katika hilo, ila hali halisi ndiyo hiyo tuliyokueleza boss” alijibu.

“REVENGE! Alitamka neno hilo kwa mara nyingine kwa utulivu wa hali ya juu, ok niachieni mimi nitajua nani na nini kimetokea, kaeni tayari kupata amri nyingine kutoka kwangu muda wowote” aliyeitwa Boss mwenye ile sauti nzito aliwaeleza kisha wote wakaondoka….

GABRIEL Matinya alivujwa na kijasho cha kwapa kwa habari aliyopewa na vijana wengi, alijaribu kuunga matukio hayakuungika, REVENGE, neno lililoandikwa kwa kutumia damu ya marehemu liliashiria hatari, lakini ni nani aliyeandika? Wakati gani? Anataka nini? Yalikuwa ni maswali machache kati ya mengi yanayotaka majibu, lakini la.

Kiti hakikutosha kutokana na hali hiyo, amani ilitoweka moyoni, afanye nini bwanyenye wa watu? Akainua mkono wa simu na kuzungusha namba fulani, kisha akasubiri sauti ya upande wa pili iitikie simu hiyo, ilipoitikia aliongea maneno machache na kutoa maagizo kadhaa ya kufanyiwa kazi..

“Hello!” sauti kakamavu ya kijana ilisikika.

“Hivi kwenye nyumba ya tukio mliweka ulinzi wa kutosha pale?” Kambale aliuliza.

“Ndiyo mkuu” akajibiwa

“Ok, naomba vijana watatu leo jioni twende pamoja nami tukahakikishe usalama”

“Sawa mkuu,” ile simu ikakatika.

Baada ya dakika chache, jioni hiyo OCD Kambale alifika kituoni hapo na kukuta tayari vijana wamejiandaa, bila kuchelewa waliingia garini na kuelekea eneo la tukio.

“Sasa tukutane pale pale ili tuhakikishe tunalitia mkononi faili hilo au kujua chochote juu ya wapi lilipo” Kambale alitoa maagizo kupitia simu yake.

Haikuchukua muda kufika katika nyumba ya marehemu Kajiba, askari wawili walikuwa pale kuweka ulinzi na wale wengine nao walijiunga pamoja, OCD Kambale akifuatana na vijana watatu ambao walifika jana yake usiku na kukuta hali ya kutatanisha walizama ndani ya nyumba hiyo na kuanza kupitia kitu kimoja baada ya kingine wakipekua huku mikono yao ikiwa ndani ya gloves maalumu kuhakikisha hawaachi alama yoyote ya vidole vyao. Ijapokuwa upekuzi ulikuwa wa makini sana lakini hakuna walichokiambulia zaidi ya REVENGE iliyokuwa pale pale kwenye dimbwi la damu.

Baada ya kumaliza kazi yao wakaondoka na kurudi kituoni lakini OCD Kambale aliachana nao na kwenda kuonana na bwana G. Matinya.

Wakiwa katika sebula kubwa ya kifahari na vinywaji vikali vikiteketea katuika matumbo ya wawili hao mazungumzo yaliendelea.

“Kambale, nina hofu sana hii nyaraka ikaingia kwenye mikono isiyo salama halafu wote tukawa matatani,” Matinya alimueleza Kambale

“Yeah, ni kweli mzee, lakini nina wasiwasi mmoja, ile nyumba walikuwa wakiishi wawili tu, Kjiba na mkewe, sasa baada tu ya tukio mkewe tukamsweka rumande na nyumba tukaifunga, sasa nani anayeweza kuingia katika ndani na asionekane na askari wanaolinda! Labda shetani.” Kmabale alijibu hoja ya Matinya

“Kusema mkewe, hilo ondoa, haiwezekani, labda kama kuna mtu anayepata taarifa kutoka kwa mkewe” Matinya alieleza. Kambale alitulia akiwaza jambo, akainua bilauli yake iliyojaa pombe na kuigigida yote kinywani mwake kabla haijaenda kutulia tumboni na kuishusha mezani.

“Mzee, kuna mtu anazunguka katika hili,” Kambale aliongea kwa utulivu huku akigonga konzi kioo cha meza hiyo.

“Mmh! Unasemaje kijana?” Matinya alishtuka kidogo kama aliyekurupuliwa kutoka usingizini.

“Nasema, kuna mtu hapa anazunguka, na asipojulikana ataharibu kila kitu” kambale aliongea kwa msisitizo.

“Kambale, fanya unachoweza, mtie mkononi anayejihusisha, lakini kitu kikubwa kuliko vyote inabidi tumpate yule mwanamke ikiwezekana na tumbane atueleze juu ya hiyo nyaraka.” Matinya alikandamizia.

“Aaa mzee, yule mwanamke atafia kitanzini usiwe na shaka, sanasana hapa ni kuona tunafanyaje kumbana bila kumteka au kumtorosha pale lumande” Kambale aliongea.

“Kambale fanya hivyo nakuaminia, ile ni nyaraka nyeti sana ya serikali, jeshi litakupa zawadi kijana”.

Baada ya mazungumzo hayo waliagana na kila mtu kuendelea na hamsini zake. Matinya alinyanyuka kitini na kuuelekea mlango wa chumbani kwake kisha akaingia zake chumbani na kufunga mlango nyuma yake.

“Mh beibi kwa maongezi, hayaishi, mi mwenzio nasubiri mpaka mwili unapoa jamani, njoo unishikeshike beibi” sauti ya kike ilitokea pale kitandani ambapo Matinya alijitupa juu yake na kutokana na ukubwa wa mwili wa mzee huyo kitanda kililalamika, alipotulia alijiinamia na kuonekana mwenye mawazo sana.

“Marina!” aliita

“Be!” Marina aliitika

“Kazi niliyokupa mpenzi uliifanya?”

“Niliifanya beibi, vipi kwani?”

“Habari ninazozipata zinanipa shida moyoni, kama yule Malaya itashindikana kufa kwa kitanzi basi kitanzi cha mwisho kitanimaliza mimi” akashusha pumzi ndefu, na kuendelea, “Sikia, wewe ni sergeant wa jeshi la Magereza umejifunza medani za uchunguzi, unalionaje hili swala, nani anaweza kuingia kwenye ile nyumba ilhali imefungwa ba iko chini ya ulinzi?” Marina aliinuka na kuketi kitandani,

“Beibi, yule mwanamke ni Ninja, mi nina uhakika ni yeye aliyafanya hayo yote, lakini bado kuna utata, atatokaje katoka ulinzi madhubuti wa Magereza, labda kama ni njama za mtu mwingine nitakubali. Sasa kwa upande wa Magereza kule niachie mimi, usiku huu nitapita kuona kama yupo au hayupo, kisha utakuwa ndiyo mwisho wake, si unajua kesi yake inasomwa kesho kutwa kwa mara ya pili na ushahidi wote utakuwepo, hivyo yuko mbioni kufungwa au kunyongwa, tukichelewa tumekwisha,”

SARGEANT Marina alijitupa kitandani na bwana Matinya, mapenzi motomoto yakachukua nfasi kati ya wawili hawa, yaliyowafanya kusahau hata kama duniani kuna kufa, utundu na ufundi wote wa kuweza kumtuliza mume wa mtu yalifanyika. Baada ya zoezi zito kausingizi ka rasharasha kaliwapitia wote wawili, kengele ya saa ndiyo ilimgutusha Marina, muda wa kwenda kazini ulifika. Alikurupuka na kukimbilia maliwato kujiswafi kisha akaagana na buzi lake na kujiandaa kutoka kuliacha jumba hilo kubwa alilojengewa na bwana Gabriel Matinya, mume wa mtu aliyesahau familia na kujiweka katika hekalu hili pamoja na kimada, askari wa jeshi la magereza, sergeant Marina, mh! Duniani kuna mambo, ukishangaa ya Musa utayaona ya Firauni.

Askari wa zamu waliingia na kubadilishana na wale waliokuwapo tangu saa nne asubuhi, makabidhiano ya lindo lao yalikuwa salama kabisa, askari wanaume walikabidhiana upande wa wanaume na wale wa kike nao walikabidhiana upande wa kike. Marina aliwasili mbele ya gereza hilo na kuegesha gari lake aina ya Suzuki Swift aliyohongwa na bwana Matinya, alishuka akiwa kakunja sura kanakwamba kagombana na mtu lakini sivyo.

“Mh keshafika huyo ‘mama gereza’,” mmoja wa askari aliwaambia wenzake huku akitoka eneo lile.

“Enhe, vipi hapa kila kitu shwari?” Marina aliuliza na akajibiwa, “Shwari afande” huku wakiwa wamebana mikono yao vizuri na kwa ukakamavu mkubwa kuonesha nidhamu ya kijeshi.

Marina alipitiliza moja kwa moja na kuingia ndani kwenye ‘cell’ selo walizohifadhiwa mahabusu wale wa kike, huku akipitisha fimbo yake katika nondo za ile milango na kusababisha kelele zisizo na mpango. Alipofika kwa Yaumi akasimama na kumtazama, Yaumi alikuwa amejilaza kwa kujikunyata kwenye kona ya chumba hicho, Marina alimtazama na kuita, lakini Yaumi hakuitika, akaita mara ya pili lakini hali ikawa ileile, Marina akatulia kidogo na kuuliza mlango wa pili yake, akaambiwa tangu mchana alikuwa katika hali hiyohiyo, Marina alipatwa na hofu akawaita askari wenzake wakafungua mlango na kuingia ndani walipomtazama, walikuta amejitapikia sana, wakawafungulia mahabusu wawili wamsaidie mwenzao kasha wakamkimbiza zahanati ya magereza apo hapo katika kambi ya Segerea na kulazwa.

“Shoga vipi?” dokta Omongwe alimjulia hali Yaumi pale kitandani.

“Nataka kutimiza azma yangu,” yaumi alijibu

“Azma? Azma ya nini?” dokta alisaili kwa tuo

“Azma ya kuwasaka waliomuua mume wangu, kulipiza kisasi” Yaumi aliongea.

“Mbona wewe ndiye uliyeua shoga?” dokta Omongwe aliuliza

“Shoga, mbivu na mbichi utazijua, fsnys tulivyoongea”

“haina shida shoga, wewe nakuaminia hata tulivyokuwa jeshini mambo yako niliyajua, ulivyokuwa ukimtoroka afande Yombayomba, ila shoga tafadhali usichelewe maana utaniharibia hapa, namba yangu unayo, haya mzigo wako huu hapa”. Omongwe alimkabidhi Yaumi mfuko wa Rambo na kuuficha chini ya godoro na kujilaza kimya.

Usiku wa saa sita, dokta Omongwe almuamsha Yaumi. Yaumi alielekea chooni na kuvalia baibui lake kisha tax ilikuja mpaka pale, tax iliyozoelewa kumchukua Omongwe mara kwa mara na kumpakia Yaumi kisha kuondoka nae, walitoka pale gerezani mpaka stendi ya daladala ya segerea.

“Niache hapa kaka,” alimwambia dereva

“Sista kasema nikuache home” dreva alileta ubishi kidogo

“Mi mwanamke bwana nina mambo yangu bwana, niache hapa ntakucheki baadae”

Yaumi akashuka na kusubiri yule dereva aondoke eneo lile, alipohakikisha kila kitu kipo sawa alichukua bodaboda.

“Kaniache Tabata Liwiti” alimwambia jamaa wa bodaboda na safari ikaanza mpaka Kimanga, pale alitembea kwa mguu na kukatiza vichochoro viwili na kufika Bondeni Lodge, akingia mapokezi na kuomba funguo ya chumba chake akapewa na kuingia, jambo la kwanza ni kuangalia ile mali yake aliyoificha juu ya dari akaikuta kama ilivyo, jambo la pili akavalia jeans yake iliyomkaa vizuri kabisa na kuibana ile bastola iliyoshibishwa risasi nane na za akiba katika mfuko wa suruali, pesa kidogo mfukoni, tshirt nyeusi na kakoti ka ngozi juu, kofia ya cape ilimfunika sawia kichwa chake, kiatu cha raba ‘saucony’ kikauhifadhi mguu wake, Yaumi alikuwa tayari, akatoka na kuaga pale mapokezi.

“Dada hupumziki? Kufika na kuondoka na jana hivyohivyo” alihoji muhudumu wa mapokezi.

“Kazi mdogo wangu lazima niwe hivyo” alimjibu huku moyoni akimwambia ‘acha umbea mtoto wa kike’, yaumi akaingia mtaani, safari ya kwanza ikiwa nyumbani kwake Kimanga kuona kama mtego wake umenasa lolote, hicho tu.

Alifika na kupita mbele ya nyumba ile, alishangaa kuona ule utepe wa polisi haupo tena na hakuna ulinzi wowote, alizunguka nyuma na alipohakikisha hakuna anayemuona aliuchukua ufunguo pale anapouweka na kufungua mlango wa uani kisha wandani, na kwa tahadhari kubwa alitembea kwenye kikorido kwa nuru hafifu inayoto nyumba jirani na kuingia kupitia dirisha kubwa la mbele, moja kwa moja alifika kwenye pazia la kutengenisha sebule na korido akatulia na kusikiliza kama kuna lolote, kimya, akaingia sebuleni huku bastola yake ikiwa mkononi maana alihisi nywele kumsisimka, kisha akaliendea kabati kubwa na kusukuma kioo na kuchukua kitu Fulani alichokihifadhi hapo, alipokuwa anageuka kutoka eneo lile, alisikia stuli ikisogezwa,

“Tulia apo hapo, nilikuwa nakusubiri wewe mwana haramu unayeharibu mipango ya watu, kumbe mwanamke!” aliyasema hayo kijana mmoja mkakamavu aliyekuwa amekaa katika stuli iliyokuwa kwenye kona moja ya nyumba, Yaumi alijua hapa habari imekwisha, kama umeme aligeuka akiwa tayari bastola yake imeshaondolewa usalama, kidole kwenye trigger, bila kuangalia sawasawa aliona tu kivuli cha mtu, moja kwa moja akalenga alipoona yeye ni sahihi na kufyatua, Colt 45 ikafunguka na kupiga pigo moja la karibu, risasi iliyotua sawia katikati ya uso wa mlengwa, na kupaishwa kabla ya kujibamiza ukutani na kuanguka kama mzigo juu ya meza ndogo iliyopambwa kwa ua la kichina, bila kutoa sauti, roho ikaacha mwili. Yaumi akasonya na kuirudisha bastola yake vizuri kasha kitendo cha haraka, akausogelea ule mwili na kuingiza mikono mfukoni akatoa kila kilichopo, hakujali damu inayomwagika kwenye kichwa kilichofumuliwa vibaya cha mtu huyo ambaye hata sura yake hakuitambua kama ni mjomba wake au la, alipohakikisha kila kitu anacho akatoka pale sebuleni haraka haraka, akasimama, akakumbuka kitu, akarudi na kuwasha kitochi chake akatazama huku na huku apale chini na kuokota ganda la ile risasi na kulitia mfukoni kisha akatokea mlango alioingilia, safari hii hata funguo hakuona haja kuiacha, akatokomea zake mpaka barabarani, akachukua bodaboda mpaka Tabata Liwiti kasha Bondeni Lodge.

“Dada, mi sikai tena nimepata safari ya dharula” akalipia chumba na kuchukua vitu vyake na kutokomea kusikojulikana.

˜˜˜˜

GABRIEL Matinya alikuwa amejilaza kitandani usiku huo akisubiri habari yoyote imfikie lakini kimya kilitawala hadi saa tisa usiku, mawazo yalimchukua akili yake, akaivuta simu yake na kutazama, hakuna ujumbe wala nini, akabofya namba ya mmoja wa vijana wake, Scogon, lakini namba iliita na haikupokelewa, ‘Hawa jamaa vipi, mbona siwaelewielewi’, Matinya alionekana kuchanganyikiwa, alinyanyuka pale kitandani na kuliendea kabati la nguo aliposimama mbele yake akajicheka maana hakujua hata anaenda kufanya nini au kuchuku nini, akarudi kitandani na kuchukua tena simu yake kwa mara nyingine, sasa lipokuwa anabonyeza tu na simu nyingine ikaingia kwa fujo, alipotazama kioo ‘Opereshen 01’, Matinya akatabasamu na kuipokea kwa madaha,

“Nipe habari haraka”, ukimya ukatawala, kilichosikika ni mihemo ya mtu kama anakimbizwa, “We nini, sema basi mbona unanihemea tu kama unavyomuhemea mwanamke wako kitandani,” aliwaka Matinya.

“Kiongozi,” akatulia kidogo, “Sema,” Matinya akaamuru, “Man down,” akajibu na kutulia, “What, very good vijana, mmemmaliza ee? Nakuja sasa hivi” aliingea kwa shangwe Matinya

“No, no, Kiongozi,” yule mtu aliikatisha furaha ya Matinya, “Sasa nini?” aliliza kwa mshangao wa taharuki,

“Tumepambana na adui, Mdumi ameuawa na adui katoroka” Scogon alitoa taarifa ya uongo ili tu isionekane kama yeye na mwenzake walitoka na shughuli zao zingine. Matinya alijikuta akikaa chini na kushusha pumzi ndefu, akabaki machokodo…

“Adui umemuonaje? Mwanamke au mwanaume?” Matinya aliuliza. Scogon aliona swali hilo kuwa ni la mtego, alitulia kidogo kisha akafungua kinywa chake, “ Aaa, alikuwa amevaa suruali na tshirt na pia eneo la mapambano lilikuwa na giza, hivyo sikung’amua kama ni mwanamke au mwanaume”

“Ok, rudini na muuache huo mwili huko nitaongea na mhusika aushughulikie” Matinya alimueleza Scogon kisha amri ikatekelezwa.

Scogon, na Simbila walionoka eneo lile na kurudi maskani.

Wakijipanga njiani ni lipi la kusema pindi wakikutana na boss Matinya.


YAUMI alichukua boda boda na kuomba apelekwe moja kwa moja eneo la Ukonga njia panda Segerea, alishuka na kumlipa mtu wa bodaboda kisha alipohakikisha ametoweka eneo lile akatafuta mahali pa kujihifadhi. Mshangano Guest House, Majumba sita, ilikuwa ni gesti sahihi kwake aliijongelea na kuuliza kama vyumba vipom jibu halikuwa lingine zaidi ya vipo.

Akiwa ndani ya chumba alijitupa kitandani na kujilaza, mara usingizi ukataka kumchukua akaamka ghafla na kutizama saa yake ilikuwa saa tisa kasoro, akaifikiria nafsi yake akajiuliza maswali mengi, hakujua nini cha kufanya, ameua, jambo ambalo hakuweza kuliamini moyoni mwake. Aliichukua simu ya mumewe na kuiwasha kisha akaiweka mezani kwa dakika kadhaa ili aweze kupata ujumbe wowotw kama utaingia, lakini haikuwa hivo. Yaumi alirudia kusoma zile meseji za vitisho alizotumiwa mumewe na kulaumu kwa nini mtumaji aliificha namba yake, kwa maana kama asingeificha basi ingekuwa kazi ndogo kumpata, lakini kwa kuificha namba ile kazi kwa Yaumi ilikuwa ni ngumu lakini alijiapia kuwa lazima ampate, kwa udi na uvumba. Simu ya Yaumi iliita alipotazama kioo alikuwa ni dokta Omongwe.

“Oya muda, fanya fasta wanoko washaanza pitapita” Omongwe alimaliza na kukata simu. Yaumi alifunga vizuri vitu vyake na kama kawaida alivipandisha darini, alikuwa na bahati kila chumba anachopanga ndicho chenye tundu la kuingilia juu a dari. Alitoka mpaka mapokezi na kumwambia yule mhudumu kuwa anatoka anaingia kazini atarudi jioni inyofuata. Kisha kama kawaida akachukua bodaboda mpaka Segerea na kuikuta tax ikimsubiri, ileile aliyokuja nayo.

“Ah, mi nilifikiri ndiyo umeondoka vile!” aliuliza dereva tax

“Aaaa, hapana mi nilienda kwa shemeji yako tu sasa narudi kwa sista ili alfajiri tuondoke wote.

Ile tax ilisimama mbele ya zahanati ile na dokta Omongwe akaja na kutazama uku na huku alipoona hakuna shida yoyote alimshusha Yaumi na kumwambia aende chooni moja kwa moja.

˜˜˜˜

Sergeant Marina, alikuwa ameketi katika kitanda cha Yaumi pale zahanati, aliingia pale muda mfupi tu kabla ya Yaumi kurudi. Mara Yaumi aliletwa chumbani na dokta Omongwe akisaidiwa na nesi mmoja, yaumi alikuwa na drip iliyochomwa mkononi mwake, huku yule nesi akiwa ameishikilia kwenye kile kining’inizio chake, Yaumi alikuwa akitembea taratibu kwa maumivu makali mpaka kitandani, Marina alimpisha na kusaidia kumlaza kitandani.

“Jikaze mwanamke, hujui kesho unasimama kizimbani?” Marina alianza maneno yake ya uchokozi. Yaumi alimtazama na moyoni alipata uchungu sana, ‘Ipo siku yako’ alijisemea moyoni mwake na kujilaza kitandani. Marina alinyanyuka na kumuaga dokta Omongwe kisha akarudi gerezani kuendelea na kazi zingine. Omongwe alimwangalia mpaka anapoishia akatikisa kichwa na kuendelea kujipumzisha pale alipoketi. Yaumi alitoa lile shuka usoni na kutulia akiwa mwenye mawazo mengi, Omongwe alikuja kumtazma,

“Vipi maendeleo yako?” alimuuliza

“Naendelea vyema,” Yaumi alijibu

“Umeanza kupata nafuu dhidi ya ugonjwa uliokuleta huku?” Omongwe alihoji,

“Ndiyo, kidogo afadhali naanza kuona mwanga wa matumaini, mwanga ambao bado una giza jembamba” Yaumi alimjibu Omongwe huku akimkabidhi kitu mkononi mwake, Omongwe alikipokea bila kujua ni kitu gain kisha akakitazama, ganda la risasi colt 45 lilikuwa mkononi mwake, “Vipi tayari?” alihoji.

“Ndiyo, one down! Kasikilize redio na TV utasikia”alipomaliza kusema hayo akajilaza tena na kujifunika kisha akaanza kulia kumuomboleza mumewe, mr Kajiba.

˜˜˜˜

HARD ROCK CAFÉ – Dar es salaam

“Sasa, mheshimiwa ni nimekuita hapa kwa swala dogo sana, wewe unanijua mimi ni nani na mimi nakujua wewe ni nani, kama sijakosea wewe ndiyo umeshika ile kesi ya mauzji ya yule dada Yaumi, sivyo?” aliuliza bwana Gabrieli Matinya huku akimtupia macho makali aliyekuwa mbele yake, jaji Ramson Semindu.

“Aaa, yeah, ni mimi nimepewa ile kesi, na kesho itasomwa tena pale mahakama kuu ya Kisutu” alijibu Ramson.

“Oooh! Good, nafikiri ushahidi wote wa kesi ile umekamilika bila shaka” Matinya aliongea kwa sauti ya upole.

“Aaa mzee, sasa tusiendeshe mahakama hapa, sio mahali pake, tusubiri kesho tuone ushahidi umekamilika kiasi gani.

Gabriel Matinya alimtazama jaji huyu kijana aliyeonekana mkakamavu wa mawazo na maamuzi, Ramson alipatwa na maswali, kwanza kwa nini huyu mernyrji wake anakuwa na maswali ya mtindo huo. Akiwa katika kutafafakari, alishtushwa na kishindo juu ya meza, alipogeuka alikutana na kitita cha pesa kilichotulia juu ya meza hiyo iliyopambwa kwa glass mbili za juisi. Jaji Ramson alitahamaki, alizitazama zile pesa na kisha kumtazama yule bwana mkubwa,

“Unataka kunipa rushwa?” Ramson aliuliza kwa mshangao

“Hapana hii si rushwa hii ni hongera kwa kazi unayotakiwa kuifanya, kijana usiwe mjinga watu tupo kazini pokea kisha usikilize maagizo nitakayokupa” Matinya alizungumza kwa sauti kavu.

“We nambie tu unachotaka nifanye lakini si kwa kunipa rushwa, tena mtu mkubwa kama wewe, hapana, sema unachotaka nami nitakusikiliza na kukusaidia,” Jaji Ramson alisema..

“Ok, ipo hivi, yule mtuhumiwa ni binamu yangu, najua sheria lazima ichukue mkondo wake kadiri ya kesi itakavyokwenda, ninachotaka mimi yule mtuhumiwa umpe dhamana kesho ili arudi uraiani kwani kukaa kule anateseka ukizingatia watoto wake karibu wanakuja likizo,” Matinya alimueleza Jaji Ramson.

“Hilo lisikupe homa mkuu, haina haja ya kupoteza pesa zote hizo wakati dhamana ni haki ya mtuhumiwa.”

Siku ilofuata… Mahakamani Kisutu

Watu walijaa mahakamani siku hiyo tangu saa 2 za asubuhi, waandishi waliokuja kujua nini kitajiri juu ya kesi ya Yaumi walijana wenye canera za mnato na mjongeo wote walikuwa hapo, achana na wale wanaoitwa waandishi wa kujitegemea nao walikuwepo kujua kitachojiri. Polisi walikuwa na kazi ngumu ya kutawanya watu na kuwapanga vizuri. Ndugu wa Yaumi walifika nao kusikiliza shauri la ndugu yao, lakini hakuna hata ndugu mmoja wa bwana Kajiba aliyefika kwani wote walimtuhumu Yaumi kumuua ndugu yao, hivyo walijenga chuki juu yake.

Mara king’ora cha land cruiser ya magereza kilisikika kikitokea barabara ya Bibi Titi kueleka hapo Kisutu, ikiwa imewasha taa zake gari ile ikunja kona kushoto na kuingia katika lango kuu la mahakama hiyo kwa mbwembwe huku askari sita walikokuwa na silaha walikuwa wakiweka ulinzi wa kina katika gari hilo.

Sekunde chche baadae, Toyota vitz nyeusi iliingia taratibu na kusimama katika maegesho ya mahakama hiyo. Hakuna aliyeshuka na wala hakuna aliyekuwa na muda wa kuliangalia gari hilo. Kutoka kwenye ile gari ya Magereza watuhumiwa kama watano hivi walishuka wakiwa na pingu mikononi mwao, Yaumi alikuwa na pingu mikononi na minyororo iliyofunga miguu yake, alisindikizwa na askari Magereza wa kike mpaka kwenye benchi maalumu ndani ya mahakama hiyo na kuketishwa.

Haikupita muda, mahakama ilianza, Jaji Ramson aliketi katika kiti chake huku upande wa chini kukiwa na muendesha mashitaka, karani wa mahakama pamoja na wakili wa serikali, wote wakiwa tayari kuendesaha kesi hiyo iliyovuta wengi. Kama ilivyo ada, muendesha mashitaka alisoma hati ya mashitaka kwa mtuhumiwa kama alivyofanya siku ya kwanza, baada ya kumaliza alimuachia jaji shauri hilo, naye jaji alimuuliza swali moja tu mtuhumiwa kama ni kweli au si kweli yale aliyosomewa, Yaumi alikana mashitaka na kwa kuwa upelelezi ulikamilika kadiri ya upande wa serikali, ushahidi uliletwa na kutolewa maelezo.

Kutoka katika kitengo maalum cha polisi cha utambuzi wa alama za vidole au nyinginezo kilichojulikana kama identification beureau ambacho kwa sasa kinajulikana kama foresinc beureau walisema kuwa alama za vidole zilizopatikana katika, mpini wa kisu na bastola ambazo alikutwa nazo Yaumi pembeni ya mwili wa marehemu zilikuwa ni zake bila kificho, alama za mtu wa mwisho kumshika marehemu zilikuwa pia ni za Yaumi, ushahidi wa WP Magreth ulithibitisha kuwa simu iliyopigwa marehemu alilalamika kuwa ‘Mke wangu w…ananiua’, kwa ushahidi huo, Yauimi alijikuta akitetemeka mwili mzima, lakini bado alishika msimamo wake kuwa yeye hajaua. Baada ya mambo ya ushaidi kukamilika, jaji Ramson alitoa nafasi ya dhaman kwa mtuhumiwa, ndipo alipojitokeza kijana mmoja mtanashati na kumuwekea dhamana ya shilingi za kitanzania milioni thelathini, na Yaumi akaachiwa huru kwa dhamana, kesi ikaaihirishwa mpaka baada ya mwezi mmoja uchunguzi bado ukiendelea.

Baada ya yule kijana kukamilisha mambo yote ya dhamana, Yaumi alifunguliwa pingu na ule mnyororo akaachiwa huru akitakiwa kufika tena siku ya kesi, yule kijana alimchukua Yaumi na kuingia nae katika ile Toyota Vitz.

Ile gari ilitoka maegeshoni taratibu na kuuacha uwanja wa mahakama hiyo huku ikisindikizwa na picha za waandishi wa habari.

Ndani ya Gari hiyo kulikuwa na watu wawili tu, yule kijana na dereva tu, walichukua barabara ya Bibi Titi mpaka makutano ya Ohio, na Ally Hassan Mwinyi kisha wakachukua uelekeo wa kwenda Morocco.

“Mwanamke!” yule mdhamini wake aligeuka nyuma na kuitoa miwani aliyoivaa na kumtazama Yaumi, “Uko sahihi kukana mashitaka, kwani wewe hujaua, ila kabla ya hukumu yako kuna kazi unatakiwa utukamilishie ndiyo mahakama iendelee na utaratibu wake,” maneno hayo Yaumi aliyaelewa sawia bila hata msaada wa mfasiri, aligundua kuwa ametekwa!

“Inabidi ufike kwa boss, ukatoe ushirikiano wa kutosha, tuipate briefcase yetu kisha utaachiwa huru ili usubiri hukumu yako” yule kijana alimueleza Yaumi huku aakimtumbulia macho. Yaumi akiwa kiti cha nyuma alimtemea mate yule kijana, kabla hajajiweka sawa akiwa anajifuta yale mate usoni alstukia kofi moja kali la macho, dereva aliposikia hayo ikabidi atoe gari pembeni kwa usalama. Mdumi akiwa katika kupambana na Yaumi, yule dereva alikuja kuingilia na kumshika Yaumi kwa nyuma, Mdumi kwa hasira alimpiga ngumi nzito tumboni mpaka Yaumi akajitoa yoe la uchungu.

MDUMI alimtazama Yaumi aliyekuwa kajikunja kuinamia tumbo alipoachiwa na yule dereva, akasonya na kujiweka vyema kitini huku yule dereva akijiweka tena vizuri nyuma ya usukani, Yaumi aliiona bastola iliyopachikwa vyema katika mkanda wa suruali ya Mdumi, hakufanya ajizi, kwa wepesi wa ajabu alimrukia Mdumi na kuichomoa ile bastola kisha kuimiliki mikononi mwake, kama Mdumi alifikiri mwanamke huyo hajui kutumia chombo hicho alikosea sana kwani alishuhudia ikiondolewa usalama kwa ustadi wa hali ya juu, kabla hajafanya lolote, Mdumi alifungua mlango na kutoka nje akiwa haamini kinachoendelea, mlango ukiwa umebaki wazi, Yaumi akimshuhudia mwanaume huyo akiduwaa bila kujua la kufanya, akIsogea karibu na mlango na kuufunga kisha akamuamuru dereva kuliondoa lile gari haraka,

“Tunaelekea wapi?” aliuliza yule dereva

“Nyoosha tu mpaka nikikuamuru vingine” Yaumi alimjibu.

Ile Vitz ilirudi barabarani na kuvuka mataa ya Morocco ikaelekea Mwenge, hakuna aliyeongea ndani ya gari ile, dereva hakutaka hata kutikisika zaidi ya kuloa jasho ambalo halikuwapo kabla. Baada ya mwendo mrefu sana walipita Lugalo barracks na kufika maeneo ya njia panda ya Kunduchi, yaumia akamuamuru dereva kukunja kushoto na kuelekea Salasala mpaka eneo moja linaloitwa machimbo.

“Simama hapa!” Yaumi aliamuru, yule dereva akaweka gari pembeni, eneo lote lilikuwa ni mikorosho na miembe tu, hakukuwa na nyumba za watu maana zote waliziacha nyuma.

“Nataka unieleze kwa tuo, kila nitakalokuuliza, ukileta ujeuri sintosita kukufumua kichwa chako,” akameza mate na kugusisha domo la ile bastola kwenye kisogo cha yule dereva,

“Dada samahani hiyo kitu haina masikhara hata kidogo, itoe tafadhali” yule dereva alioangea kwa woga akitetemeka.

“Hilo mi silijui, haya nieleze ni nyie mliomuua mume wangu mpendwa sivyo?” alianza kwa swali la mwisho badala ya la kwanza.

“Aaah, mi sijui kwa kweli, mi naagizwa kuendesha gari tu” alijibu. Yaumi hakuisjiwa na maswali, akaendelea, “Ok, na gari lako huwa unaendesha kuanzia wapi, nataka nijue”

“Inategemeana dada angu” akakatishwa na sauti ya hasira ya Yaumi, “We bwege mi sio dada yako, na wala usinipotezee muda, sema haraka kabla sijakumaliza kama yule hayawani mwenzenu aliyevamia nyumba yangu usiku wa majuzi,” kwa maneno yale yule dereva alishtuka na kugeuka nyuma akiwa kakunja ndita usoni mwake, na kuuliza,

“Kwa hiyo we ndiyo ulimuua Jamal?”

Hapo yaumi akagundua kuwa yule maraehemu alikuwa anaitwa Jamal, akaendelea kumtazama yule dereva ambaye sasa hakuonesha uwoga tena wa ile bastola, wakati Yaumi akishangaa alistukia mkono wake ukipigwa kwa nguvu na ile bastola kumtoka mkononi, kabla hajakaa sawa ngumi nzito ilitua usawa wa shavu lake na kumfanya kudondokea upande wa pili huku kisogo chake kikijipiga kwenye kioo cha dirisha, mguno hafifu ulisikika huku akiona kama taji la nyota likizunguka mbela yake, yule dereva akajitahidi kupita kati ya zile siti mbili za mbele ili kuja upande wa nyuma, akiwa katika kupenya ili amshambulie vema Yaumi alijikuta akicharazwa kofi moja kali lililochana shavu lake na damu zikaanza kutiririka, pete ya uchumba ya Yaumi aliyovalishwa na bwana Kajiba ilikuwa imejizungusha upande wa pili wa kidole chake cha shahada ikikingwa na ile ya ndoa ili isitoke, sehemu ya lile jiwe la yaspi lilimchana vibaya yule dereva, Yaumi hakulitegemea hilo aliitazama ile pete na kuibusu, yule dereva akajishika shavuni na kukutana na damu nyingi, mara kila mmoja akakumbuka bastola na wote kwa pamoja mikono yao ikakutana kwenye sakafu ya gari hiyo wakigombea bastola, kikiri kakala, huku na kule, mikono yote iliishika bastola amabayo tayari ilikuwa imeondolewa usalama, hamad! Kidole kimoja kikafyatua trigger na risasi moja ikafyatuka na kuchimba kwenye ile sakaru ya gari, bila kipingamizi ilipenya na kulifikia tank la mafuta, petrol, bila mzaa yale mafuta yakakutana na risasi ya moto.

Lipppppp!!! Mlipuko wa ghafla ulitokea ile Toyota Vitz ilinyanyuliwa na kurushwa upande wa pili kutokana na ile nguvu ya mlipuko. Ndani ya gari hiyo kulikuwa mshikemshike, sasa sio ule wa kugombania bastola bali ule wa kutafuta pa kutokea, Yaumi alifanikiwa kutoka katika kioo cha nyuma ambaco kilikuwa kimesambaratika huku akimuacha yule dereva ambaye kwanza alitafuta jinsi ya kujinasua kati ya vile viti viwili ndipo apate nafasi ya kutoka lakini haikuwa hivyo, moto ulizidi na moshi mzito kumfanya akose nguvu na kuishia humo.

˜˜˜˜

Tumbo kubwa la bwana Gabriel Matinya lilikuwa likikisaidia kifua kupanda na kushuka kwa hasira huku macho na masikio yake yakiwa bado yameelekeza nguvu zote kwa Mdumi aliyeketi mbele yake na chupa kubwa ya maji akikata kiu.

“Unajua mi haingii akilini kabisa kama huyu mwanamke anaweza kufanya yote haya,” aliongea kwa hofu na kushusha pumzi, kisha akaendelea, “Na bila shaka yeye ndiye aliyetekeleza mauji ya Jamal,” ijapokuwa alisema hayo, Matinya bado alikuwa na utata ndani ya kichwa chake, ‘Itawezekanaje kutoka chini ya ulinzi wa askari makini wa magereza?’ jibu lilikuwa gumu.

Mara mlango ulisukumwa na wanaume wawili wakaingia, Scogon na Simbila walikuwa pale wakimtazama Mdumi aliyekuwa ameketi akiwa hana swaga. Kisha wote wakachukua nafasi zao na kuketi.

“Najua tulipanga tukutane sasa ili tumshughulikie yule mwanamke, lakini mpango wetu hauko vile” Matinya alizungumza huku akijifuta jasho kwa kitambaa chake, yule mwanamke katoroka na Sergie na hatujui huko waliko nini kinaendelea, simu ya Sergie haipatikani, ilikuwaje muulizeni Mdumi” Matinya alimaliza na kujiegemeza katika kochi lile kubwa. Mdumi alichukua nafasi hiyo kuwasimulia kilichojiri na kila mtu alishangaa.

Scogon alimuangalia Mdumi na kujiweka vizuri kitini, akasema, “Mzee, nafikiri hapa tunapambana na mtu makini, na mwenye roho mbaya ya revenge,”

“Ni kweli, sasa sikiliza Scogon, panga kikosi chako kamili ingia kazini, nataka mniletee yule mwanamke akiwa hai kwa gharama yoyote ile na pia mjue hatima ya Sergie, kwa shida yoyote nipigieni,” Matinya alitoa amri na vijana wakaingia kazini.

˜˜˜˜

ITAENDELEA

Kitanzi cha Mwisho Sehemu ya Pili

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment