Ulimwengu Mzima Kiganjani Mwa CIA Sehemu ya Kwanza
MEANDIKWA NA: THE BOLD
*********************************************************************************
Simulizi: Ulimwengu Mzima Kiganjani Mwa CIA
Sehemu ya Kwanza (1)
BAY OF PIGS Vs COLD WAR: MAREKANI, CUBA NA USSR, ULIMWENGU KIGANJANI MWA CIA, CRF NA KGB; NA AIBU YA DUNIA KWENYE ULINGO WA KIJASUSI.
Kwenye jengo la Pentagon ghorofa ya pili upande wa kushoto yani left wing kuna chumba namba 273, chumba ambacho ndio ofisi ya mshauri mkuu wa jeshi na wizara ya ulinzi ya Marekani yani “Chiefs of Staff counselor” , asubuhi ya Tarehe 13 mwezi wa 9 mwaka 1960, Kamati Maalumu ya Viongozi wa Juu Kijeshi nchini Marekani (Joint Chiefs of Staff Committee) chini ya Bw. L.M. Lemnitzer, iliidhinisha Operesheni iliyopewa jina la “Northwoods”, kwa lengo la kutafuta sababu ya kuivamia kijeshi nchi ya Cuba (pretext for military invasion of Cuba), Chini ya operesheni hiyo, kamati ilipendekeza mfululizo mashambulizi yenye taswira ya kigaidi ndani ya miji ya Miami, Washington, D.C na kwingineko, meli za mizigo na abiria za nchi ya Marekani zingelipuliwa au kuzamishwa, ndege kutekwa, mauaji ya raia kutekelezwa makusudi, utoaji wa orodha ‘feki’ za wahanga wa mashambulizi ili kuufanya umma wa Wamarekani kuingia taharuki na kuipigia kelele za hasira serikali kulipiza kisasi kwa kuivamia Cuba. Kwa mujibu wa mpango huo, kila shambulizi lilipangwa kuhusishwa na nchi ya Cuba.
Kuidhinishwa kwa operation hii kulifatia baada ya mapinduzi ya Cuba yaliyofanyika mwaka 1959, mapinduzi hayo hayakuungwa mkono na mataifa mengi, hasa Ulaya na Marekani kwa sababu moja kubwa kuwa utawala wa Castro ulikuwa unaweka hatari masrahi ya Marekani nchini Cuba, sababu hiyo ni kuwa uongozi wa kijeshi ulioondolewa madarakani nchini humo chini ya dikteta Fulgencio Batista ulijaa vibaraka, walioweka mbele matumbo yao kwa kuigeuza Cuba kama mali ya mabepari, hasa Marekani, hivyo Castro na wanamapinduzi wenzake muda mfupi baada ya mapinduzi hayo, waliwatimua Wamarekani, kwa kuhodhi makampuni yote ya biashara, migodi, kilimo na Njia zote za uchumi.
Kitendo cha utawala wa Castro kutaifisha makampuni ya Marekani kiliisababishia Marekani hasara kubwa kibiashara, huo ndio ukawa mwanzo wa uadui baina yao, Mipango ya kuipindua serikali ya Fidel Castro ikaanza kwa nguvu sana, na kwa namna tofauti, ntaeleza hili kwa undani kabisa huko mbeleni, serekali ya Marekani litaka kuirudisha madarakani serikali itakayo waunga mkoni huko Cuba ili waendelee kulinyonya taifa hilo, jambo ambalo Castro na wenzake hawakutaka litokee.
Jambo la kujiuliza hapa ni kwanini Marekani iliiamua kuweka uadui na Cuba, swali la kujiuliza zaidi ni kwanini Marekani ilifamya maamuzi ya kutaka kuivamia Cuba! Maswali haya na mengine kibao kuhusu masrahi ya Marekani nchini Cuba yanairudisha nyuma historia ya Marekani na Cuba miaka 70 kabla ya tukio la kuivamia Cuba asubuhi ile ya mwaka 1961 kwenye ghuba ya mapigano ya Playa Girón ambayo hufahamika kama bay of pigs.
Hivyo basi…
Historia ya nchi hizi mbili inaanzia karne ya 18, kipindi ambacho Cuba ilikuwa “shamba la Bibi” kwa himaya ya kikoloni ya Kihispania, Katika karne ya 19 mwishoni, wazalendo wanamapinduzi wa Cuba walianza kuasi dhidi ya wakaloni wa Hispania na kutaka kuitawala nchi yao wakiongozwa na Jose Mart, hivyo kupelekea kupiganwa kwa vita tatu vya kuasi utawala wa Kihispania, Vita hivyo ni vita vilivyojulikana kama vita vya miaka kumi (1868–1878), nyingine ni ile vita iliyojulikana kama vita ndogo (1879–1880) na nyingine ni vita ya kupigania Uhuru wa Cuba (1895–1898), vita ambavyo Cuba ilijitangazia Uhuru wake, na Jose Mart kuwa rais wa kwanza wa Cuba guru, huyu José Mart nchini Cuba hutazamwa kama Baba wa taifa, mwasisi na mwanamapinduzi mkuu nchini humo, falsafa yake ya “Siri, Vamia, shambulia, gawanya na miliki” ndio ilikuwa kanuni kuu ya mapigamo kwa Castro, tutaliona hilo kwenye uvamizi wa Playa Girón au Bay of Pigs huko mbeleni.
Lakini serikali ya Marekani ilianzisha vita na himaya ya utawala wa Hispania nchini Cuba, ikumbukwe kuwa Hispania bado ilikuwa inataka kuendelea kuikalia Cuba na hivyo kupelekea vita ya Hispania na Marekani mwaka 1898, vita ambayo Marekani ilitaka kuikalia Cuba, hivyo mara kwa mara Marekani ilivamia kisiwa cha Cuba na kuyafurusha majeshi ya Hispania nje ya kisiwa cha Cuba, Katika mpango maalum uliopewa jina operation Habana, Marekani walipanga kuingiza askari 375 ndani ya visiwa vya Cuba katika mapigano ya Tayacoba katika vita kati ya Hispania na Marekani, ambapo Tarehe 20 May 1902, Marekani iliishinda Uhispania na serikali mpya ilijitangaza na kuunda Jamhuri ya Cuba chini ya usimamizi wa Marekani huku gavana wa kijeshi wa Marekani Leonard Woodhanding akimuongoza Rais Tomás Estrada Palma, Mcuba mzaliwa wa Cuba mwenye uraia wa Marekani.
Ni katika vita hivyo ndio Marekani ililikalia eneo la Guantanamo bay kama sehemu ya miliki ya Marekani kama malipo ya vita dhidi ya Hispania, Taratibu idadi kubwa ya walowezi na wafanyabiashara wa Kimarekani walikuwa wanawasili Cuba na hadi kufikia mwaka 1905 asilimia 60 ya bidhaa za mashambani zilikuwa zinamilikiwa na wananchi wasio Wacuba kutoka Marekani ya Kaskazini na kati ya mwaka 1906 na 1909, wanajeshi wanamaji wapatao 5,000 wa Kimarekani waliweka kambi katika kisiwa chote cha Cuba, na walirudi tena mwaka 1912, 1917 na 1921 na kuweza kuingilia mambo ya ndani ya Cuba, wakati mwingine bila hata ridhaa ya Wacuba wenyewe, hivyo hatimae Cuba ikawa sehemu ya nje ya Marekani.
Baada ya kuona namna Marekani ilivyoingia nchini Cuba toka mwaka 1898 kwa kuwafurusha Wahispania Sasa tuendele mbele ili kupata kiini halisi cha undani wa mapinduzi yenyewe ya mwaka 1959 nchini Cuba, lakini pia kwa nini tena Wacuba waliokuwa wakiishi uhamishoni, hususan wale ambao waliokuwa wakiishi jijini Miami katika jimbo la Florida walitaka kuuangusha utawala wa Castro nchini Cuba, pia nini hasa taifa la Marekani liliamua kuwekeza fedha nyingi ili kufanikisha kuudondosha utawala wa Castro, jambo ambalo tutaona baadae ni namna gani Marekani ilivyo injini uvamizi wa Bay of Pigs.
Mwezi Machi mwaka1952, Jenerali wa Cuba na mwanasiasa, Fulgencio Batista, alitwaa madaraka katika kisiwa hicho, na kujitangaza yeye binafsi kama Rais baada ya kumpindua Rais aliyekuwa madarakani, Carlos PrÃo Socarrás wa chama cha Partido Auténtico.
Batista alifuta uchaguzi wa Rais uliotarajiwa kufanyika, awali Batista alipata kiasi fulani cha uungwaji mkono, lakini kwa Wacuba wengi waliona hiyo ni aina ya utawala wa kidikteta wa mtu mmoja ambao Batista anajaribu kuuanzisha, Wengi wa wapinzani wa utawala wake waliamua kuasi na kuchukua njia ya mapambano ya silaha kumpinga na kujaribu kuuondoa utawala wake, hiyo ilichochea mapinduzi ya Cuba, Mojawapo ya makundi haya lilikuwa ni kundi la The National Revolutionary Movement (Movimiento Nacional Revolucionario – MNR), kundi la muungano wa kijeshi lililojumuisha watu wengi wanachama wa daraja la kati lililoanzishwa na Profesa wa Philosofia, Rafael GarcÃa Bárcena. Kundi jingine lilikuwa The Directorio Revolucionario Estudantil (DRE), ambalo lilianzishwa na muungano wa wanafunzi wa vyuo vikuu, The Federation of University Students (FEU) chini ya Rais wake José Antonio EchevarrÃa (1932–1957).
Hata hivyo, miongoni mwa makundi yote hayo, kundi bora kabisa katika hayo yote yaliyokuwa yakimpinga Batista lilikuwa la “26th of July Movement” (MR-26-7), lililoanzishwa na Mwanasheria aliyeitwa Fidel Castro, Castro kama kiongozi mkuu wa MR-26-7, aliligawanya kundi lake katika mfumo wa vikundi vya watu kumi kumi, huku kila kikundi kikiwa hakijui uwepo wa kikundi kingine na kujua shuguli wanazozifanya kikundi kingine.
Kuanzia Desemba mwaka1956 mpaka mwaka1959, Castro aliongoza jeshi la msituni kupambana dhidi ya majeshi ya Batista kutoka katika ngome ya kambi yake kwenye milima ya Sierra Maestra, Kusambaa kwa vuguvugu la mapinduzi kulimfanya Batista kumpunguzia umaarufu, na kufikia mwaka 1958 majeshi yake yalikuwa katika uwezekano mkubwa wa kusalimu amri, hatimae Tarehe 31 Desemba mwaka 1958, Batista alijiuzuru na kukimbilia uhamishoni, huku akiondoka na kiasi kikubwa cha pesa zaidi ya dola za Kimarekani 300,000,000. Baada ya Batista kukimbia, Urais ukaangukia kwa Mwanasheria Manuel Urrutia Lleó, aliyechaguliwa na Castro, huku wanachama wa MR-26-7 wakidhibiti idadi kubwa ya nafasi katika baraza la mawaziri.
Ilipofika Tarehe 16 Februari mwaka 1959, Castro akachukua Madaraka ya kuwa Waziri Mkuu, akaondoa uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi, kwa siku za mwanzoni, Castro alidai kuwa utawala mpya ni mfano wa demokrasia ya moja kwa moja ambayo umma wa wacuba unaweza kujikusanya kwa pamoja na kufanya maandamano na kuelezea hisia za demokrasia wanayoitaka moja kwa moja kwake yeye binafsi, Hata hivyo wapo waliolaumu utawala mpya wakisema si utawala wa kidemokrasia, moja ya makundi walio laumu ni walowezi wa kimalekani ambao asilimia kuwa walikuwa ndio wanao miliki 95% ya uchumi wa Cuba.
Hatua hiyo ilianza kutengeneza kudorola kwa uhusiano wa Marekani na Cuba, jambo ambalo viongozi kadhaa Washington waliitazama Cuba kama adui mpya, kufatia hatua hiyo serikali ya Cuba ilitoa amri kwa makampuni ya mafuta ya Esso na Standard Oil yaliyokuwa chini ya makampuni kutoka Marekani na kampuni ya Anglo-Dutch Shell ya Kiholanzi kuanza kusafisha mafuta yaliyonunuliwa kutoka katika nchi za Umoja wa Kisoviet badala ya Marekani lakini kutokana na shinikizo kutoka serikali ya Marekani makampuni hayo yalikataa.
Castro alijibu kwa kuyazuia kusafisha mafuta kisha akayataifisha makampuni yote na kuwa chini ya usimamizi wa serikali ya Cuba, katika kujibu mapigo, nayo serikali ya Marekani ikaacha kuagiza sukari kutoka Cuba hivyo kupelekea Castro kutaifisha raslimali nyingi zaidi zilizokuwa zinamilikiwa na Marekani, ikiwemo mabenki na viwanda vya sukari.
Uhusiano zaidi wa Cuba na Marekani ukaanza kuzorota kufuatia kulipuka kwa meli ya Kifaransa iliyoitwa “Le Coubre” na kupelekea kuzama katika bandari ya Havana mnamo mwezi Machi, mwaka 1960, Chanzo cha mlipuko hakikujulikana lakini Castro aliitaja hadharani serikali ya Marekani kuwa ndiyo iliyohusika na hujuma hiyo, lakini jambo ambalo wengi awajui ni kuwa tulio hilo la kuilipua meri hiyo ya “Le Coubre” serikali ya Marekani ilihusika, ntalieleza hili kwa upana hapo mbeleni.
Asubuhi ya tarehe 13 Oktoba, mwaka1960, serikali ya Marekani ilizuia kwa sehemu kubwa bidhaa kadhaa kusafirishwa kwenda Cuba kasoro bidhaa za madawa na baadhi ya vyakula, ikiashiria kuanza rasmi kwa vikwazo vya kiuchumi, Cuba nayo katika kujibu mapigo kamati ya Taifa ya Mabadiliko iliamua kuchukua usimamizi wa biashara binafsi 383 zilizokuwa zinaendeshwa na Marekani, na siku ya tarehe 1 Oktoba na tarehe 25 Oktoba zaidi ya makampuni 166 ya Marekani ambayo yalikuwa yakifanya shughuli nchini Cuba, majengo yao yalichukuliwa na kutaifishwa ikiwemo Coca-Cola na na kampuni ya Sear Roebuck.
Tarehe 16 Desemba, Marekani tena ikaacha kuagiza robo yote ya sukari iliyokuwa ikiagiza kutoka Cuba, Serikali ya Marekani ikazidisha kuipinga serikali ya kimapinduzi ya Castro.
Hatimae Mwezi Agosti,1960 katika mkutano wa umoja wa nchi za Amerika, yaani Organization of American State (OAS) uliokuwa unafanyika Costa Rica, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Christian Herter, hadharani alidai kwamba utawala wa Castro “kwa uaminifu mkubwa unafuata misingi ya njia za Bolshevik” kwa kukazia mfumo wa chama kimoja cha siasa kwa serikali yake kuweka vyama vya wafanyakazi chini yake, kubana uhuru wa raia na kuondoa uhuru wa kuongea na uhuru wa vyombo vya habari na akaenda mbali zaidi kwa kusema kuwa nchi za kijamaa zinaitumia Cuba kama ngome yake ya kusambaza mapinduzi katika nchi za ncha ya Kaskazini na akatoa wito kwa wanachama wengine wa umoja huo wa OAS kuilaani Cuba kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.
Cuba nayo ikajibu mapigo, Castro alielezea namna jamii ya watu weusi inavyonyanyaswa na tofauti kubwa ya matabaka ya wafanyakazi aliyoishuhudia wakati akiwa New York, na kupiga kijembe na kudhihaki kuwa huo ndiyo “uhuru wa hali ya juu, demokrasia ya hali ya juu, utu wa hali ya juu, na kustaarabika kwa hali ya juu kwa jiji hilo.” Akadai kuwa masikini wa Marekani wanaishi katika “bakuli la mabepari wanyonyaji”, pia Castro aliushambulia mtiririko wa vyombo vya habari vya Marekani na kuulaumu kuwa unaendeshwa na wafanya biashara wakubwa.
Kwa namna nyingine Marekani ilikuwa inajaribu kuimarisha uhusiano wake na Cuba, Majadiliano mengi kati ya wawakilishi kutoka Cuba na Marekani yalifanyika katika kipindi hiki, Kurekebisha uhusiano wa fedha wa kimataifa ndiyo ilikuwa dira kuu ya majadiliano hayo, Mahusiano ya kisiasa ilikuwa ajenda nyingine kubwa ya mikutano hiyo, Marekani ilieleza kuwa haitaingilia aina ya serikali ya Cuba inayoitaka au mambo yake ya ndani hata hivyo Marekani ikaiaumu Cuba kufuta siasa za Umoja wa Kisovieti, walimshawishi Castro kuacha siasa za kisoviet kwa kumuhaidi miassada kibao ya kuendesha nchi, lakini Castro aligoma, hapa ndipo Marekani ikaamua kubadilisha muelekeo dhidi ya Cuba, hapa Sasa Marekani wakaingia kazini ili kuiadabisha Cuba.
Mwezi Augosti, mwaka 1960, CIA waliwasiliana na kundi la Cosa Nostra lilokuwa na makao yake jijini Chicago ili kuandaa mipango mbalimbali ya kuwaua Fidel Castro, Raúl Castro na Che Guevara, katika mpango huo Marekani ilikubaliana na kikundi hicho kuwa baada ya kupachika serikali ambayo inawaunga mkono nchini Cuba, watakubaliana kati ya CIA na kundi hilo la Mafia kupata umiliki wa michezo ya bahati nasibu, biashara ya umalaya na madawa ya kulevya ndani Cuba, hivyo mipango hiyo ikapangwa kuanza rasmi mwaka 1960, lakini mpango huo ulitakiwa lazima upate idhini ya rais wa Marekani.
Hivyo mkurugenzi mkuu wa CIA Allen Dulles, akaamdaa kikao maalumu ili kujadili namna ya kumshawishi raisi Dwight D. Eisenhower mpango wa kuivamia Cuba na kumuua Castro, Dulles akiwa na Rolando Cubela, afisa mipango wa CIA mwenyeji wa Frolida ambae alikuwa anaifahamu vizuri Cuba, akapewa kazi ya kuinjinia ramani mpango wa namna ya kuivamia Cuba, ikumbukwe kwamba Shirika la Ujasusi la Marekani yaani Central Intelligence Agency (CIA), ni shirika la kijasusi ambalo liliundwa na serikali ya Marekani mwaka 1960 kupitia sheria iliopitishwa na bunge la Congress mwaka 1947, kupitia sheria iliyoitwa “National Security Act” azimio namba 90551, CIA “ilikuwa ni zao la Vita Baridi”, shirika hili lilibuniwa ili kuzikabili njama za shirika la ujasusi la Umoja wa Kisoviet la KGB.
Sasa basi…
ITAENDELEA
Ulimwengu Mzima Kiganjani Mwa CIA Sehemu ya Pili
Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;