Julai Saba Sehemu ya Pili
KIJASUSI

Ep 02: Julai Saba

SIMULIZI Julai Saba
Julai Saba Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA: RICHARD MWAMBE

*********************************************************************************

Simulizi: Julai Saba

Sehemu ya Pili (2)

Gari aina ya Toyota V8 yenye vioo vya giza iliinga katika geti kubwa la jingo Fulani huko maeneo ya Mabibo. Vioo vyake vya tinted havikuruhusu mtu wa nje kuona kilichopo ndani ya gari hiyo, kwa mwendo wa taratibu iliegeshwa na milango yake ikafunguliwa vijana wawili na mtu mwingine wa makamo wakateremka na kuufungua mlango wa nyuma, mwanadada mmoja akateremshwa na kupelekwa ndani ya ghorofa iliyopo ndani ya wigo huo.

“Ni mwanamke mjinga sana wewe!” ilikuwa sauti ya yule mtu wa makamo aliyetambulika kwa jina la Shailan aliyekuja kuchukua nafasi ya Betram, “ Tumekulipa pesa nyingi, tumekupa mafunzo ya kujitoa mhanga, sasa umefanya nini? Unazidi kutuingiza matatizoni, kaa hapo na leo hii tunakuchinja kwa sababau wewe tayari umeshakufa” alimalizia luongea kwa jazba kubwa.

Yule msichana alisukumiwa ndani ya chumba fulani chenye giza na kufungiwa. Kisha akaketi na wenzi wake pale mezani.

“Bora mmempata, maana wangempata wao, sijui tungemwambia nini Beishal, na ameshaamuru huyu msichana auawe mara moja, kwa hiyo baadae hiyo kazi ifanyike na mwili wake mtajua mtautupa wapi”

“Lakini kwa nini tusimuache kwanza tumbane atueleze kama kuna chochote alichoongea na hawa watu, ili tujue labda tuna la kufanya” aliongea kijana mwingine.

“Lakini pia ni wazo zuri, tumbane kwanza tukishapata tunachokitaka ndiyo tummalize” aliongezea Shailan, akanyanyuka katika kiti kile alichokalia na kuelekea katika chumba kile walichomfungia yule msichana, wakaufungua mlango na kuwasha taa,

“We mwanake mjinga, uliyeahirisha kifo ulichokiuza mwenyewe sasa utakipata kwa maumivu makali” Shailan alimueleza huku akilifuta jambia lake lililokuwa liking’aa huku na huku kutoka katika ala yake.

Yule msichana alikuwa ameketi kinyonge katika kona ya chumba hicho akiwatazama wanaume wale kwa huzuni.

??????

kuhusu

FARJAH

Farjah, msichana yatima kutoka Mombasa aliyekuwa akiishi katika mazingira magumu huko Mombasa, baada ya mama na baba yake kufa katika ajali mbaya ya gari, msichana huyu alibaki bila msaada huku akiwa ameachiwa wadogo zake wane wa kuwalea bila msaada wowote, akiwa katika harakati hizo alijikuta akiingia katika biashara haramu ya ukahaba ili kujipatia chochote kwa minajiri ya kusomesha na kusaidia wadogo zake kimaisha.

Siku moja usiku wa manane akiwa kwenye moja ya miahngaiko yake ndani ya club maarufu ya usiku ya ‘Mombasa by Night’ ndipo alipokutana na Shakrum Shakran ambaye alimtongoza mrembo huyo na kwenda kulala nae katika hoteli moja kubwa ambayo alifikia. Huko ndiko alikosuka mpango huo na kumshawishi Farjah kukubali mpango huo kwa malipo ya pesa nyingi sana ambazo zingeweza kusomesha wadogo zake na kuwaweka katika mazingira mazuri kwa miaka ishirini mpaka watakapoweza kujitegemea wenyewe, aliposaini pesa hiyo wadogo zake walijengewa nyumba kubwa na kuwekewa kila kitu na kulipiwa ada ya masomo yao, kisha Farjah alimuomba shangazi yake awalee wadogo zake hao wakati yeye anaenda nje ya nchi kwa muda mrefu, shangazi yake alikubali na Farjah alisafirishwa kwenda Somalia kupata mafunzo maalum ya kujitoa mhanga, mafunzo ya kutoogopa kifo, mafunzo ya kutumia bunduki za aina mbalimbali, na tayari akiwa huko alishatekeleza mashambulizi mbalimbali Somalia na Sudani, sasa alipewa kazi yake ya mwisho kuja kuifanya Tanzania maana mkataba wake ulikuwa mwishoni.

Masaa machache nyuma

Farjah alitafakari sana alipokuwa njiani kutoka Somalia kuja Tanzania, alifanya mashambulizi mengi sana ya mauaji lakini yalikuwa tofauti sana na haya anayotakiwa kufanya Tanzania.

Akiwa ameketi kwenye kochi kubwa la kisasa alionekana kuwa na mawazo mengi sana, kiasi kwamba iliwatia shaka mabosi wake.

“Farjah, mzima au?” aliuliza Shailan.

“Hapana, nipo vizuri tu” alijibu huku akiwa ameangalia chini, akitafakari kifo chake kinachofuata baada ya masaa machache.

“Farjah najua wazi kuwa una mawazo lakini wewe tayari hitima yako tumekwishaifanya, haupo duniani kama mkataba wetu ulivyo, tunakushukuru kwa kazi yote uliyotufanyia, na sasa unakwenda kumalizia na roho yako itapumzika mahali pema huko peponi” Shailan alikuwa akimwambia Farjah ambaye alionekana wazi kuvujwa jasho japo kiyoyozi cha LG kilikuwa kikitengeneza baridi kali ndani ya chumba hicho, Farjah alishusha pumzi ndefu na kujitupa kwenye kiegemeo cha sofa hilo. Mbele yake aliletewa ramani kubwa ya jengo la JM MALL.

“Ok, tazama hapa Farjah, jengo tunalolitaka ni hili, hapa ni floor ya saba, unapotoka tu katika lifti, kunja kushoto kuna milango kadhaa, utazipita ofisi zingine na wewe unatakiwa ufanye mlipuko wako ndani ya ofisi hii, pale utamkuta kijana mmoja matata sana na binti ambaye ni katibu wake, hakikisha unanionana na huyu kijana na mlipuko huu ufanyike ukiwa na huyo kijana, jihadhari huyu kijana ni mjanja sana na IQ ya hali ya hali ya juu, usipoteze muda. Mwisho wako ndiyo huo. Ole wako ulete ujinga na uzembe,” Shailan alimaliza kumuelekeza Farjah kisha akanyanyuka na kuelekea chumba fulani, Farjah akiwa katika kutafakari hili na lile mlango mwingine ulifunguliwa na kijana jalali akaingia akiwa na begi jeusi mkononi, Farjah alishtuka kumuona kijana huyu, alimfahamu, alinyanyuka na kumkumbatia kwa bashaha, Shakrum Shakran hakuwa na muda wa kukumbatia msichana, aliitazama saa yake na kuushusha ule mkono.

“Tunachelewa, vua hilo baibui lako,” ilikuwa sauti tulivu ya Shakrum, Farjah alipoisikia sauti hiyo aliikumbuka jinsi ilivyokuwa ikimbembeleza katika chumba kimoja cha hoteli huko Mombasa ikimwambia ‘vua mpenzi nataka nione umbo lako zuri, jeupe, lenye mvuto,’ lakini leo iliongea kwa mkato tu.

Farjah hakuwa na lakusema alivua lile baibui lake na kiblauzi kidogo ndani yake, chuchu zilizosimama zilikuwa zikimtazama Shakrum, kwa shida kidogo alimeza mate lakini haikuwa kazi iliyokusudiwa. Begi jeusi likafunguliwa na kitu kama mkanda kikatolewa na mbele yake kulikuwa na kitu kilichotunatuna, Shakrum akakizungusha kile kitu tumboni mwa Farjah na kuzunguka mgongoni mwake akakikutanisha na kufunga sawia kwa kutumi namba za siri (code number) ambazo ni yeye tu alikuwa akizijua. Akarudi upande wa mbele wa msichana huyu, akafungua kifuniko Fulani kidogo na kubonyeza vitufe kadhaa, mara kukawaka vinamba vilivyojiandika sifuri sifuri kama sita hivi na kutengenishwa na nukta mbili zilizobebana kila baada ya siruri mbili (colon), kisha akaseti vijinamba fulani, na alipoachia vikaanza kujihesabu, bomu la saa!

Shakrum alimwangalia usoni Farjah aliyekuwa amelowa jasho mwili mzima akitetemeka kwa hofu, akamshika kwa viganja vyake vya mikono mashavuni na kumbusu kwa kumnonya ulimi, usaliti!

“Farjah, fanya unalotakiwa kufanya na si vinginevyo” Shakrum alisema hayo na kuchukua ile baibui na kumvesha, kisha akamchukua hadi chini kulikokuwa na Prado nyeupe ikiwasubiri, wote wakaingia ndani na kuondoka eneo hilo.

˜ ˜ ˜

Katika kijibarabara cha watembea kwa miguu eneo la Buguruni Chama kuelekea Y2K bar, msichana mmoja alikuwa akitembea kwa hatua za haraka haraka huku akiangalia nyuma mara kwa mara, na kukibana kipochi chake kwa mbele, sketi fupi aliyoivaa ilimnyima uhuru wa kuongeza kasi, jioni hiyo watu wengi walikuwa katika harakati za kurudi majumbani, hivyo kijibarabara hiko kilikuwa na kazi ngumu ya kukanyagwa na ymati huo. Alipokaribia katika lango la kuingia kati ile bar, aliitoa simu yake katika pochi na kubofya namba fulani kisha akaiweka sikioni na kuonekana akiongea na mtu fulani huku akiwa hana amani kabisa, mara akairudisha simu ile na kuingia ndani ya ile bar, alipokelewa na mhudumu wa bar hiyo aliyevalia nadhifu kabisa, akamuongoza mpaka meza Fulani iliyokuwa na mtu mmoja tu, mwanaume aliyevalia kaunda suti kuukuu na kichwani akiwa na kofia aina ya pama, mezani kwake kulikuwa na safari bia iliyokua nusu na nyingine ikiwa katika bilauri. Yule msichana aliketi kwa woga akimwangalia mtu yule ambaye alihisi hajapata kumuona kabla, yule mtu akatoa kadi ya kibiashara nyingine na kumuwekea mezani, yule msichana alipoisoma jina akalikumbuka lakini mbona hafanani ndiyo swali alilojiuliza.

“Stephen Amalutwa!” alitamka kwa upole huku akiisukuma juu ile kofia yake, “Nilipata simu yako ndo maana nikakwambia tuonane hapa, ningependa kukujua kwanza kwa jina, kisha ndiyo unambie shida yako”

“Naitwa Mwada, mwadawa, naishi Magomeni Makuti nyumba namba 12C, mi nimekutafuta nikuulize kitu, ulipokuja ofisini na ulipoondoka bosi wangu kanikaripia sana kwa kukukaribisha, kisha kanipa likizo ya muda, hii hapa barua na kanilipa cheki ya millioni mbili, mi nimeshindwa kuelewa nini kimejificha” alijieleza Mwadawa

“Nafikiri mimi ningepaswa kukuuliza swali hilo, sivyo? Kama bosi wako kaupa likizo kwa kitendo cha mimi kuja kuandika habari kutoka ofsini kwenu, nini kimejificha hapo?” kamanda Amata, Stephen Amalutwa wa bandia aliligeuza lile swali, Mwadawa alitulia tuli akitafakari anachoulizwa,

“Mi kaka sijui, ninachoshangaa ni boss hatua aliyoichukua,” alijibu, Amata alimwangalia kwa jicho la chini,

“Ina maana wewe kama secretary wa ofisi hujagundua kitu tofauti siku hizi ofisini kwenu au nyendo tofauti na zile za kawaida za boss wako?” Amata alirusha swali, na ukimya ulitawala kati yao.

“Hapana zaidi ya wageni wengi wanaokuja siku hizi, ambao tunatambulishwa kuwa ni ndugu zake”

“Wageni wa namna gani?” kamanda aliuliza

“Ni hao ndugu zake, huja na kukaa hapa wiki au mwezi, wakibadilishana na kuwa na vikao visivyokwisha” alijibu Mwadawa.

Baada ya mazungumzo marefu na kamanda Amata kuridhika kiasi na majibu ya dada huyo waliagana.

“Kwa sababau umechelewa sana basi ngoja nikufikishe nyumbani” Amata alimwambia

“Oh, no acha tu bwana nitafika mwenyewe”

“Ok, take care!” Amata alimuaga Mwadawa, akabaki kasimama akimwangalia mwanadada huyo anavyopotelea nje ya bar hiyo maarufu hapo Buguruni ambayo daima huzungukwa na akina dadapoa wengi wanaofanya kuwavuta watu kufika hapo kila jua lilalapo.

Kamanda Amata, alimalizia kinywaji chake na kutoka katika bar hiyo, moja kwa moja aliiendea gari yake aina ya LandRover 110 TDI na kuingia ndani yake kisha kuelekea mitaa ya kati ya jiji la Dar es salaam, aliifuata barabara ya Uhuru mpaka katika mataa ya Karume na kukunja kushoto kuelekea Magomeni kupitia barabara ya Kawawa, pale Magomeni alinyoosha moja kwa moja na breki ilikuwa katika bar nyingine maarufu Kinondoni kwa Manyanya. Mara tu baada ya kusimamisha gari yake binti mmoja aliisogelea na kuzunguka upande wa kushoto kisha kuingia kiti cha mbele.

“Mungu anakupenda mrembo” Amata alianzisha mazungumzo

“Kwa nini wasema hivyo honey?” ilikuwa sauti tamu ya Gina, sauti inayoweza kumtoa nyoka pangoni, sauti yenye mtetemo wa kutatanisha inayoweza kukufanya kijana kupoteza network ya kichwa chako hata ukiambiwa uandike cheki ya milioni kadhaa utatii tu maana uatakosa la kufanya.

“Kwani sakata la leo hulijui? Yaani hapa nyaraka zote zimelowa huko ofisini,” Amata alieleza kisha akatulia kwa muda na kumtazama Gina, “Ungekuwa saa hii unalia mpaka unazimia maana tayari ningekuwa hata sura haijulikani, hawa jamaa ni hatari sana lazima nihakikisha nawafutilia mbali katika uso wa dunia kwa mkono wangu huu”. Ilionekana wazi hasira ya Amata ilikuwa moyoni mwake, kijana mcheshi anayependa kucheka muda wote hata na asiyemjua.

Gina alimtazama Amata usoni kisha akauweka mkono wake begani mwa kijana huyo,

“Pole!” alimtuliza.

“Ok, nipe tafutishi zetu” Amata alimwambia Gina.

Gina akatoa bahasha ndogo na kuchambua karatasi fulani Fulani na kumpatia, Amata alizichukua na kuzisoma kwa makini akatikisa kichwa kukubaliana na kilichoandikwa ndani yake.

“Shakrum!” Amata alitamka hilo jina, “Asante sana mpenzi, umefanya kazi kubwa,”

Alizikunja zile karatasi na kuziweka katika droo ya dashboard na kuwasha gari na kuondoka na binti huyo.

“Wapi Amata jamani?” Gina aliuliza huku akiuvuta mkanda wa usalama na kuufunga vizuri.

“Hapo tu mbele unisindikize, kwa chakula cha jioni”

˜ ˜ ˜

Addis in Dar, jioni hiyo watu wengi walikuwa wakiingia katika hoteli hiyo kwa mlo wa jioni, wengi walionekana na wapenzi wao wakishikana kimahaba kuingia ndani ya hotel hiyo nzuri yenye vyakula vya kuvutia vya tamaduni tofauti hasa vile vya Ethiopia. Amata alishuka garini akiongozana na Gina mpaka ghorofani na kuketi katika meza moja iliyopo katika kona ya ukumbi huo nadhifu, waliagiza vinywaji na vyakula kadhaa na kuwa wakila huku wakibadilishana mawazo.

“Gina, nisubiri hapa nakuja muda si mrefu!” alimwambia Gina

“Wapi tena Amata?” kuna rafiki yangu nina miadi naye nakuja, nipe lisaa limoja tafadhali” akanyanyuka na kumpa funguo za gari na kumuacha hela za kulipia chakula kisha yeye akateremka chini na kuondoka. Kwa hatua za harakaharaka aliifuata barabara ya Ursino kuelekea upande wa barabara ya Bagamoyo, aliikatisha na kupita mbele ya Kanisa la Kristo kisha akakunja kulia na kusimama karibu na mti wa mnazi ambaye ulilingana naye kimo, alitazama huku na huko hakuona dalili ya mtu, tayari ilitimu saa tano usiku, alitembea tena haraka haraka na kulipita geti lililosomeka FK Security na kuzunguka upande wa nyuma wa ukuta wa uzio, aliangali kama kuna usalama wowote akaona hamna shida, kwa kutumia mti wa mwarobaini ulioota upande huo aliukwea na kufika juu ya ukuta huo mrefu kisha kujirusha ndani na kutua kwa utulivu kwenye ardhi tifutifu, kishindo hafifiu kilimfanya mlinzi wa upande huo kusogea, Amata alitulia kwa mtindo uleule na kumsubiri, alipomkaribia kwa haraka aliruka na kumpiga karate moja ya nyuma ya shingo kisha kumdaka na kumshusha chini taratibu na kumvutia karibu na pipa la takataka, akamuhifadhi hapo na kuvuta hatua kwenda upande wa pili, pale alikuta magari kadhaa yamewekwa na mojawapo likiwa gari kubwa la zimamoto ndani yake kulikuwa na watu sita waliojilaza, akanyata taratibu akatoa mfukoni kichupa chake kidogo chenye dawa kali ya usingizi iliyochanganywa na dawa ya Halcion na kupuliza kwa kupitia dirishani, haikupita sekunde kumi wote walikuwa hoi kwa usingizi, Amata akauendea mlango mmoja ulio pembeni mwa jingo hilo na kutia funguo yake maalum mlango ule ulikubali na kufunguka, akaingia ndani na kuurudishia nyuma yake, kisha akaiendea korido ndefu kidogo yenye milango michache lakni yeye aliuchagua ule uliondika Director na kuutomasa kidogo kwa funguo zake ukafunguka akaingia ndani.

Aliiangalia ile ofisi nadhifu ambayo mchana wake tu alikuwa pale, kwa tahadhali aliizunguka na kuketi juu ya kiti kile cha bwana Scolleti, akaanza kuvuta droo moja baada ya nyingine huku akisaidiwa na tochi yake ndogo mfano wa peni yenye mwanga unaomulika pale tu upatakapo. Alipofungua kabati alikaribishwa na mafaili mengi sana ila alivutiwa na moja tu, akalishusha na kuliweka mezani kisha kuchambua nyaraka moja baada ya nyingine na hii ilimvutia, kadi za gari, sasa uongo ulijulikana. Kamanda Amata aligundua wazi kuwa lile lori la zimamoto lililotumika kumuokoa yule binti lilikuwa ni lao, walichokifanya ni kuibadilisha namba ya usajili, alipoendelea kuichunguza ile namba ya usajili akagundua kuwa ni namba ya Toyota Premio, Amata akatikisa kichwa kuashiria kuwa ameridhika kwa hilo, alitoa mashine yake ndogo yenye uwezo mkubwa wa kutoa photocopy, mashine ambayo huweza hata kuiweka katika mfuko wa shati na usiijue, akatoa vivuli vya kadi zile na kuzihifadhi vyema kisha akarudisha lile kabrasha mahala pake. Akavuta hatua kuliendea kabati lingine na kutoa faili lililoandikwa ‘ Wageni’ ndani yake kulikuwa na faili moja tu lililolazwa kana kwamba limesahaulika mle ndani, alilivuta na kuliweka mezani, akalifungua, kopi za hati za kusafiria zilikuwa humo za watu ambao labda atawahitaji wakati Fulani, nazo alifanya vilevile. Akavuta hatua za tahadhari kuuelekea mlango lakini kitu kilimvutia, kabla hajatoka, katika chano moja iliyoandikwa IN kulikuwa na kijimemo kidogo, akakirudia na kukinyanyua, ilikuwa ni miadi tu ‘Tuonane saa tisa alasiri kesho, White Sand hotel’ kisha kufuatiwa na namba Fulani ya simu. Amata aliirudisha ile kadi mahali pake na kuuendea mlango kisha kutoka na kuufunga nyuma yake.

Alitoka nje taratibu kwa kufuata njia ileile, alipofika kwenye ule mlango wa kutokea kwenye ule uwanja alisikia mngurumo wa gari kubwa na watu wakiwa wanazungumza, akawasikiliza kwa makini.

“Wamesema kulekule Kunduchi” sauti moja ilisema.

“Kunduchi ni mbali kwa nini isiwe jirani tu, si kesho wataokota” sauti nyingine ilijibu, kisha ule mlango ukafunguliwa, Amata akajibanza kwa nyuma yake, vijana wawili wenye sare ya kisecurity wakashuka na kuchukua kitu kama mfuko wa saruji na kutoka wakisaidiana huku na huku.

“Aaa hapo safi, kesho mtainjoy jioni,” ilisema sauti ingine ikifuatiwa na sauti ya lile gari iliyoonesha wazi kuwa dereva alikuwa amekanyaga pedeli ya mafuta, kutoka pale alipo, kwa kasi alaijitupa chini na kujiviringa mpaka uvungu wa lile lori, ijapokuwa kulikuwa na walinzi eneo lile kwa muda huo lakini hakuwa aliyemuhisi, sembuse kumuona. Amata alijishikia vizuri sana kwenye chuma imara cha chessis huku akiwa mbali kidogo na lile propeller Shaft lililokuwa likizunguka kwa kasi. Ile lori ikatoka getini na kuiendea barabara ya New Bagamoyo, wakati likijiandaa kuingia barabara kubwa Amata alitoka na kuliacha liende peke yake.

Akajinyanyua pale alipojitupia na kujikung’uta vumbi na nyasi kavu zilizonasa mwilini.

˜ ˜ ˜

3

Asubuhi ilofuata

Kikombe cha chai kilishindikana kufikishwa kinywani mwa Madam S wakati macho yalipogongana na habari ya kipolisi kuwa mwili wa mwanamke mmoja mwenye asili ya Kihabesh umeokotwa kwenye ufukwe wa bahari ya Hindi huko maeneo ya Kunduchi. Kisha picha kadhaa zilipitishwa kwenye luninga, na wakaomba kama kuna mtu aliyepotelewa na ndugu yake basi akautambue mwili huo katika chumba cha maiti pale Muhimbili.

Madam S, aliendelea kunywa chai huku akisikiliza watu wanaohojiwa juu ya tukio hilo, kwake yeye halikuwa na uzito sana kwani mara nyingi imetokea matukia kama hayo kusikika, labda tu watu wameuana kwa wivu wa mapenzi, hivyo hakufuatilia lolote. ‘Kazi za kipolisi’, alijiwazia.

Aliinuka kitini na kukusanya vifaa vyake kisha kuondoka kuelekea kazini, kama kawaida alikuwa kwenye foleni ndefu ya magari ya kuingia barabara ya Ally Hassan Mwinyi ili aelekee upande wa Posta, alifungua redio na kusikia tena habari ile ile aliyoiacha kwenye televishen, lakini katika redio hii kitu fulani kilimvutia, habari iliyosema kuwa marehemu ametupwa usiku uliotangulia na watu wasiojulikana. Alijaribu kuchanganya kichwa kama kuna lolote muhimu kwake lakini hakuona hilo, aliendelea na safari yake.

Mwananyamala hospitali

“YEAH, huu ni mwili wa mwanamke anayekadiriwa kuwa na miaka 25 hadi 30, ameuawa kwa kuvunjwa shingo,” Dr Semeni alikuwa akimueleza Amata aliyekuja kujua kilichojiri juu ya mwili ule uliookotwa kule Kunduchi Beach siku hiyo asubuhi. Aliufunua ile shuka iliyofunikwa mwili mzima na kuruhusu uso kuwa wazi, akatingisha kichwa kuashiria ameelewa kitu.

“Vipi?” Dr Semeni aliuliza.

“Hapana, nimekubaliana na uchunguzi wako” Amata alijibu. Amata aliugundua mwili ule, mwili wa msichana aliyekuja na bomu jana yake pale katika jengo la JM MALL kwa minajiri ya kujilipua, tena ofisini kwa Amata. ‘Inaonekana wamemuua baada ya kushindwa kutekeleza lile jaribio,’ alijiwazia Amata, huku akiandika andika katika kitabu chake cha kumbukumbu.

˜ ˜ ˜

“Mheshimiwa Rais ametuachia hilo jukumu sisi, kama tunaona ni vyema kumuachia huyu jamaa au la!” waziri wa ulinzi aliongea huku akiwaangalia mjumbe mmoja mmoja katika kikao hicho waliokaa kwa mtindo wa nusu duara, wakiwa katika majadiliano hayo na utayari wa kuandaa remove order, mara mlango ulifunguliwa na Amata akawa amesimama nyuma ya wale wajumbe wengine akitazamana na waziri uso kwa uso, wajumbe wote waligeuka nyuma kumtazama kijana huyu aliyeingia hapo bila kualikwa. Madam S alimtazama kijana wake kwa macho makali sana.

“Amata! Unafanya nini hapa, kikao hakikuhusu,” madam S aliongea huku akiinuka kitini kumkabili Amata.

“Mnisamehe kwa kuingia ghafla lakini imebidi nifanye hivyo kwani ningechelewa kidogo tu mngefanya kile nisichokitaka” Amata alizungumza kwa kujiamini.

“Kipi hicho?” waziri aliuliza.

“Swala la kumuachia huru Jegran Grashan, siliungi mkono hata kidogo, najua mna nia nzuri, lakini mimi naona mkifanya hivyo mtakuwa mmeharibu sana na watu watawashangaa kwa hatua hiyo, mimi suing mkono hata kama sina uwezo wa kuwazuia kufanya maamuzi yenu” Amata aliongea kwa hasira iliyomfanya kila mtu kutulia, “Wenyewe mnajua nilivyompata kwa shida hata kuhatarisha maisha yangu, halafu aachiwe kirahisi namna hiyo! Haiwezekani, kumuacha yule tutakuwa tumeonesha udhaifu mkubwa sana wa kiutendaji katika ngazi ya kiusalama. Sitakubaliani na hilo, yule akae ndani kama ilivyo sasa na hawa washirika wake ndiyo tutawapata kiurahisi, kitendo cha kumuachia ni kuwaweka mbali maadui zetu, sikubaliani na mnalotaka kufanya,” Amata alimaliza na kutoka ofisini mle kisha kuufunga mlango nyuma yake. Aliingia katika gari yake na kuketi nyuma ya usukani akionekana wazi kupoteza network kiasi Fulani.

Mara kioo cha dirisha la upande wake kikagongwa, alipogeuka akagongana macho kwa macho na madam S, walitazamana kwa nukta kadhaa kisha Amata akashusha kioo.

“Nione Ofisini,” Madam S akaongea kwa kifupi na kuielekea gari yake. Amata akawasha gari yake na kuondoka eneo lile.

Baada ya dakika kadhaa alikuwa tayari ofisini mwa madam S akiwa ameketi kwa mtindo wa kutazamana na mwanamama huyu, mkuu wake wa kazi.

“Umefanya nini Amata?” madam S aliuliza, “Unadiriki kuingia katika kikao kama kile bila idhini yoyote! Amata,”

“Ilibidi iwe hivyo kwani nilijua mnalolizungumzia mimi nalipinga kadiri ya mwenendo wa kazi hii” Amata alimjibu.

“Hukutakiwa kufanya vile, kwa nini hukusubiri kikao kiishe, kisha utoe rufani yako?”

“Isingewezekana ukizingatia nyote mliokuwa pale tayari mlikuwa na adhma moja tu, kumuacha huru Jegran, mimi hilo siwezi kulivumilia, nilimpata kwa tabu sana yule mtu, kumbuka mwenyewe madam jinsi ile kazi ilivyokuwa ngumu…”

Miaka minne iliyopita …

“HATA kama nimejeruhiwa, hakika siwezi kumuachia hayawani huyu aondoke aende akadhuru watu wengine, sambaza picha yake mipakani na mijini labda tutapata fununu juu yake,” Amata alizungumza kwa uchungu huku machozi yakimtiririka, mkono wake wa kushoto ulikuwa ukivuja damu baada ya kujeruhiwa na risasi na kusababisha jeraha katia nyama zake za juu ya kiwiko, lakini uzuri ni kuwa hakuna mfupa uliovunjika.

“Pole kamanda” Madam S alimpa pole huku akimwangalia kwa huzuni pale kitandani alipokuwa akipata tiba.

Baada ya kila kitu kukamilika, kamanda Amata na madam S walitoka hospitalini hapo na kurudi mjini, jua lilikuwa tayari likiuacha mji wa Dar es salaam na kupotelea Maghalibi kama ilivyo desturi mji ulianza kuchangamka wengine wakirudi nyumbani ilhali wengine wakiingia mjini kuanza kazi zao haramu na halali.

“Kumpata huyu jamaa ipo kazi kamanda” madam S alizungumza.

“Yeah, ni kazi ngumu sana lakini lazima tumpate, na atapatikana tu” alijibu kamanda Amata.

“Unafikiri tufanye nini ili tumtie mkononi?”

“Kwanza kabisa mpaka sasa sitegemei kama yupo Dar, kwa vyovyote atakuwa ameshatoka mji huu ili kutaka kukimbia”

“Ni ngumu, makachero wengi tumewasambaza katika sehemu muhimu ili kumnasa ama yeye au aliyefanana naye”

“Tutumaini, jamaa alitaka kufanya kitu kibaya sana pale uwanja wa ndege, tumshukuru Mungu niliwahi kuokoa lakini sasa hivi tungeongea mengine.” Amata alisema

“Ah, kwa kweli unastahili pongezi” madama S alimpongeza Amata

“Aah, tuwapongeze wale waliotufahamisha kuhusu Jegan kuwa pale, maana alijua wazi kuwa tumebana kila kona hivyo atumie njia ya kawaida kuondoka, ka kujibadili sura yake kiasi fulani”

Masaa machache yaliyopita

Uwanja wa ndege wa kimataifa Dar es salaam, DIA

JASMINE aliinua kichwa chake kumtazama mtu aliyekuwa mbele yake, alipata shaka na hati yake ya kusafiria, alimtazama kwa makini usoni kisha akarudisha macho katika hati ile, mashaka.

Aliichukua ile hati na kumkabidhi mwenzake aliaitazame upya.

“Samahani subiri pale kwenye kiti,” alimwambia mtu yule aliyekuwa na mandevu mengi kidevuni mwake. Yule mtu aliketi kitini na kuuweka mfuko wake wa plastiki pembeni yake, akisubiri kuona kinachojiri.

“Mh! Hii hati mbona yanitia mashaka?” mtumishi mwingine wa idara ya Uhamiaji alimuuliza Jasmine.

“Ndiyo maana nikakupa” Jasmine alijibu. Yule bwana akaiweka kwenye mtambo maalum na kuifanyia scan kisha akamrudishia le Hati Jasmine.

“Samahani kwa kukuchelewesha, tulikuwa tunaikagua kidogo hati yako, wakati mwingine unapoingia nchini kumbuka kupata kibali (visa) cha muda mrefu, maana hapa inaonekana kibali chako kimeisha tangu juzi,” Jasmine alimueleza yule bwana mwenye mandevu kisha akampa hati yake na kumruhusu kuendelea na utaratibu mwingine baada ya kumgongea mihuri kadhaa, kilichomshangaza juu ya huyu Bwana alikuwa haongei wala hajibu chochote isipokuwa kukutazama tu kwa macho yake mekundu.

Baada ya kuiscan ile hati, aliichukua kielektroniki ile picha ya mtu huyo na kuingiza kwenye mtandao maalum wa usalama wa taifa unaoweza kuitambua sura yoyote ya mtu na kukupa taarifa zake. Chiba akiwa nyuma ya kompyuta yake maalum kwa kazi hiyo, safari hii akiwa ndani ya sare za ofisa uhamiaji pale uwanja wa ndege alitulia tuli, akisubiri ule mtandao ufanye kazi huku akimtazama yule mtu asipotee machoni mwake.

Mlio fulani ulisikika kwenye kompyuta yake na alipoitazama, kwenye kioo kulikuwa na picha mbili, ile aliyoiscan na pembeni yake kulikuwa na nyingine iliyoletwa kwa msaada wa mtandao na maelezo kadhaa chini yake.

Jegan Grashan, mzaliwa wa Yemen; kisha zikafuatili tarehe za kuzaliwa na maelezo mengine mengi, lakini katika ile hati kulikuwa na maelezo tofauti kabisa. Jasmine aliitilia shaka kutokana na mihuri ya kibali chake cha kuwapo nchini ilifanana sana na ile ya idara ya uhamiaji isipokuwa kitu kimoja kidogo sana ambacho kwa raia wa kawaida huwezi kukitambua hakikuonekana katika mihuri ile.

Chiba alibofya vitufe Fulani kwenye hiyo kompyuta yake kisha akaandika ujumbe na kuutuma mahali. Alinyanyuka kutoka alipoketi na kuiweka tayari bastola yake kicha kuipachika katika mkanda wake wa suruali na kujitupia koti lake la buluu liliofunika vyema bastola ile.

˜ ˜ ˜

Akiwa kitandani na msichana mrembo, Kumbuka, kamanda Amata alikuwa akiendelea na shughuli hiyo nyeti ambayo haistahili kusimuliwa mbele ya watoto, alikuwa akitoa miguno iliyochnganyika na sauti nyembamba ya mahaba yaliyosindikizwa na raha kutoka kwa msichana huyu aliyeonekana wazi kuipagawisha roho ya Amata mchana huo wa jua kali katika hoteli fulani hapo Dar.

Kumbuka alimsukumia upande wa pili Amata na kujinasua katika mikono ya dume hilo lililokuwa bado likiendeleza libeneke wakati mwenzake alikuwa amekwishamaliza mizunguko yake. Kamanda Amata alitulia kitandani akimwangalia Kumbuka alipokuwa akikimbilia bafuni huku nyama zake za nyuma zikitisika kwa mpangilio hadimu ambao huwezi kuuona kirahisi kama hukumpembua mavazi binti huyu wa kihehe. Akiwa katika butwaa hilo mara saa yake ilimfinya kwa meno maalum yaliyo chini ya mfuniko. Akabofya kitu fulani na kutulia, mara mkanda mdogo ukatoka katika ile saa, Amata aliusoma ujumbe uliokuwamo katika kijimkanda hicho.

‘Mzigo wetu upo hapa Airport, njoo haraka, Tena Sana Aisee’

Amata, alikurupuka kitandani na kukimbilia bafuni, alijiswafi haraka haraka na kuvaa nguo zake.

“We vipi mbona hueleweki?” ilikuwa ni sauti ya Kumbuka, akimuuliza Amata wakati akiwa kwenye harakati hizo.

“Nitakutafuta baadae kuna dharula hospitalini” alimdanganya. Alipomaliza kujiweka tayri alitoka na kumuachia noti zenye thamani ya elfu hamsini kisha yeye kuliendea gari lake na kupotelea.

Madam S nae alikuwa njiani kuelekea hapo sambamba na kamanda Amata. Dakika chache Amata aliingia uwanja wa ndege na kuiwiweka maegeshoni gari yake, ulinzi tayari uliimarishwa na askari waliovaa kiraia, madam S naye aliteremka na kuongoza moja kwa moja katika mlango wa kuingilia wasafiri wenye kibao kilichoandikwa ‘Departure’.

“Geti namba 38” sauti ya Chiba ilifika masikioni mwa madam S aliyeonekana kuwa kikazi zaidi, tayari alikwishavuka huo mlango na kusimama mahali Fulani akipepesa macho yake huku na kule, kwa mbali alimuona Amata naye akiwa amebana kwenye kona Fulani.

“Chiba! Nenda pale alipoketi mwambie kuwa hati yake ya kusafiria ina mashaka kisha akikufuata tumtie nguvuni” Amata alimwambia Chiba kwa kutumia saa yake maalum inayoweza kusafirisha ujumbe wa sauti.

“Amata, nipe mpango wako!” Madam S alipeleka ujumbe wa sauti ka Amata.

“Chiba atakwenda kumueleza kuwa hati yake ina shida hivyo amfuate ofisini, kisha tutambana huko, najua lolote linaweza kutokea madam, watu wameshakaa kila kona kwa tahadhari” Amata alimjibu madam S.

“Ok, kamanda nakuaminia, hakikisha hasitoroke mshenzi huyo” madam S alimaliza kuongea kwa kutumia ile saa yake na kujiweka tayari. Amata akiwa kona ya upande wa pili aliweza kuona kila kinachoendelea.

Jegan Grashan alikuwa ameketi huku akisoma gazeti la Daily News, alionekana kutokuwa na utulivu maana kila wakati alikuwa akiiangalia saa yake. Chiba alivuta hatua ndogondogo mpaka pale alipoketi Jegan na kusimama mbele yake.

“Mheshimiwa!” Chiba aliita, na Jegan aliinua uso wake kumuangalia, “Samahani kwa usumbufu kuna tatizo dogo kwenye hati yako ya kusafiria, naomba unifuate ili tukairekebishe.” Jegan alimtazama Chiba kwa tuo,

“Mimi?” alimuuliza

“Ee ndiyo wewe bwana Hassanail Hussein” Chiba aliongeza na kumtaja kwa jina alilotumia katika hati yake. Jegan, gaidi la kimataifa, lilianza kuhisi harufu mbaya ya hatari, alitazama huku na huku na kwa mbali alimuona Amata amejibanza kwenye kona Fulani, akamtambua akaona hatari na janja inayotumika. Jegan alimkazia macho Chiba na Chiba akafanya vivyo hivyo huku akizisoma hisia za gaidi huyo, Chiba aliona wazi kuwa sasa kazi imeamka kazi ambayo hakuitarajia alitamanai Kamanda Amata awe jirani. Amata aliona kila kitu na akamtupia signal madam S, taarifa zikafika kwa wanausalama wa nje ya uwanja kujiweka tayari kwa lolote muda wowote.

“Ok twende,” Jegan alijibu, kisha akanyanyuka na kuongoza, hatua chache alimuona Amata akitoka kwenye ile kona aliyosimama. Jegan akasimama na kujifanya anafunga kamba ya kiatu, teke moja la nyuma lilimtoka na kumpepesua Chiba ambaye alienda chini bila pingamizi, kelele za wasafiri zikaamsha vurugu kwenye chumba cha kusubiria safari, Chiba alinyanyuka na kuchomoa bastola yake.

“Freeze!!!” alipiga kelele, lakini Jegan alijirusha kwa ustadi na kutua juu ya ngazi za umeme zilizokuwa zikielekea chini.

“Watu wote lala chini !” sauti ya Amata ilisikika na kila aliye ndani ya ukumbi ule alijitupa sakafuni. Polisi mmoja alimjia mbele Jegan, kosa. Jegan aliruka sarakasi na kutua miguu yake kifuani mwa polisi huyo na kumpeleka chini huku bunduki yake aina ya SMG ikimtoka kiurahisi mikononi na kudondokea pembeni, alipotaka kunyanyuka teke moja kali lilitua shavuni na kumvunja taya, Jegana sasa alikuwa na ile bunduki mikononi mwake, akaiondoa usalama tayari kwa mashambulizi.

‘Mambo yashaharibika’ Amata alijisemea akiwa anaelekea kule kwenye mapigano. Jegan alifyatua risasi kadhaa hewani na watu wote walitulia chini, alipoona Amata anamkaribia alimuinua mama mmoja wa Kihindi na kumuweka ngao.

“Ukiniletea shida namuua huyu mama” Jegan alimueleza Amata aliyekuwa kasimama mbele yake tayari na bastola mkononi. Jegan aliididimiza mtutu wa ile bunduki kwenye shingo ya yule mama, “weka silaha yako chini” alimuamuru Amata, Amata akaiweka chini bastola yake, “Vizuri, sasa isukumie kwangu kwa kutumia mguu wako” alitoa amri nyingine, Amata akatii na kuipiga kwa teke ile bastola nayo ikaseleleka kumuelekea Jegan, Jegan alimsukuma yule mama na kuiwahi ile bastola baada ya kufyatua magazine ya SMG na kutengeanisha na ile bunduki, alipogeuka kwenda uapande wa pili, alikutana na ngumi nzito toka kwa Chiba, kabla hajakaa sawa Chiba aliruka double kick na kumfanya ayumbe, wakati huo tayari Amata alikuwa jirani, Jegan alipanda ngazi haraka kuelekea upande wa juu akageuka na kufyatua risasi moja iliyotawanya vyoo kila upande,

“Kamanda…!!!!” ilikuwa sauti ya madam S, Amata aligeuka upande ule na kumuona madam S akimrushia bastola, Amata akaidaka kwa ustadi na kugeuka upande alipo Jegan hakumuona, kwa hatua za kunyata alipanda ngazi kuelekea juu na kufika tena pale kwenye sehemu ya kusubiria wasafiri, alisimama kwa utulivu akitazama huku na huku, ‘Uko wapi hayawani?’ alijiuliza mwenyewe huku akitembeza bastola yake huku na kule. Amata alijikuta akipigwa karate moja kali kutoka nyuma yake, akajirusha sarakasi na kutua mbele kama hatua tatu hivi kisha kugeuka kumkabili adui, aliruka juu na kuichanua miguu yake kwa mtindo wa kujizungusha na kumpata sawia Jegan ambaye hakutetereka bali alisimama kidete akamsubiri Amata kutua sakafuni, kama alivyotarajia, Amata alitua kwa mguu mmoja lakini kabla hajakaa sawa, Jegan alipiga teke kali na kuufyatua ule mguu, sasa Amata alianguka vibaya sakafuni lakini alipotua tu naye alipiga teke moja sehemu ya nyuma ya magoti na kumfanya Jegan apige magoti, teke la pili lilitua usoni na kumfanya aanguke chali. Amata alijinyanyua na kumuendea huku Chiba na madam S nao wakija kwa kasi, Jegan alinyanyuka na kumpiga dafrao Amata kisha kwa kasi ya ajabu alikimbi na kujirusha kwenye kioo kikubwa na kutoka nje huku milio na risasi vikimfuati kwa kasi lakini havikufanikiwa, Jegan alikuwa tayari nje ya jingo chini kabisa na kukimbia kuelekea pande za Kipawa, walinzi wa nje walipata wakati mgumu kumkamata haikuwezekana.

Amata alibaki kasimama huku kajishika kiuno pembeni yake madam S akionekana wazi kukasirika kwa kumkosa hayawani huyo. Amata alisonya na kuelekea pale kwenye lile tundu kubwa la kioo alipopitia Jegan.

“Amkeni, poleni kwa usumbufu” madam S aliwaambia abiria. Kisha akifuatana na kamanda Amata na Chiba waliteremka ngazi mpaka nje ya jengo hilo ambapo walikuta polisi wakiwa kwenye kibarua kizito cha kumsaka Jegan wakiwa na mbwa maalum kwa kazi hiyo.

Katikati ya vichaka vya eneo hilo ambalo wakazi wake walikwishahamishwa ili kupisha upanuzi wa uwanja huo mbwa wote waliishia kwenye kiatu kilichokuwa hapo, hawakuendelea zaidi, Jegan hayupo….

Rejea ofisini kwa Madam S

“Sasa mtu kama huyo kweli, ee! Madam, tumuachie? Watanzania takriban saba wamepoteza maisha pale ubalozini mwaka ule, na Wakenya zaidi ya mia mbili, hapana mkimuachia mi namuua, naapa!” Amata alimwambia madam S, akasimama na kutaka kuondoka.

“Kamanda hebu rudi kwanza hapa!” madam S alimuita, Anata akarudi na kusimama akimtazama boss wake, kisha madam S akaendelea, “Unalosema ni sahihi, lakini we unafikiri tufanyeje? Kwa maana hata mheshimiwa amelibariki hilo.”

“Sikatai, lakini si kwamba tumeshindwa kuliangamiza hili genge?” Amata aliuliza

“Hilo niachie mimi, nitaongea na wadau tuone njia mbadala,” Madam alimpoza jazba Amata. Amata akatoka nje na kuiacha ofisi ya madam S akiwa mwenye mawazo mengi sana.

˜ ˜ ˜

Aliingia kwenye gari yake na moja kwa moja alielekea ofisini kwake pale kwenye jingo la JM MALL, aliegesha gari na kuteremka, huku na huku aliangalia usalama na kuufunga mlango kisha kuingia ndani kupitia mlango mkubwa wa mbele, mlango wenye watu wengi wanaoingia na kutoka kwa kuwa ndani yake kulikuwa na supermarket kubwa ya Shoprite, alipiga hatua chache na kutulia kusubiri lift ya kumpeleka ghorofa ingine ambamo ofisi yake ilikuwamo, alifika na kubonyeza kengele kwa mtindo ule waliowekeana na Gina, mlango ulifunguliwa na akaingia moja kwa moja akaenda kujitupa katika kiti chake akiwa mwenye mawazo lukuki, Gina kama kawaida yake, aliandaa kahawa ya kiitaliano inayojulikana kama ‘Capucino’ na kumpelekea pale mezani,

“Karibu kamanda” alimkaribisha huku akitoa tabasamu pana lililomrudishia nguvu Amata,

“Asante mrembo, ndiyo maana nilikuajiri ofisini kwangu” alimsifia huku akijiweka sawa kitini, na kumkaribisha Gina kiti cha pili yake, kisha akatoa camera yake ndogo na kuiwasha sehemu ya kuangalia picha zilizokwishapigwa ambazo zimehifadhiwa humo, akachagua akachukua na waya wake wa USB na kuuchomeka kutoka kwenye camera mpaka kwenye kompyuta yake, sekunde chache zile picha zikaanza kuonekana pale katika kioo cha kompyuta.

“Gina, unamjua huyu?” Amata alimuuliza Gina, Gina alikodoa macho kuangalia ile picha, picha ya mtu asiye na uhai, mwana dada mweupe mwenye nywele ndefu zilizoijaza machela ya chuma ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Mwananyamala.

“Hapana, simfahamu” Gina alijibu

“Huyu ndiye aliyekuja hapa kufanya ule mlipuko, lilikuwa bomu hai,”

“Umempataje hadi kumuua?” Gina alisaili

“Hapana, sijamuua, wamemuua wenyewe, unajua hii ni mikataba, unapokwenda kujitoa mhanga maana yake wameshakulipa na wameshakuwekea matanga kwamba wewe nai marehemu hivyo uende ukaue na wewe ufe ukohuko, sasa huyu inaonekana kafeli hivyo wamemuua, wamemnyonga shingo” Amata aliposema hayo alimuona Gina akisisimka mwili.

“Watu wabaya!” Gina aliongea

“Sio kidogo!” Amata akaongeza, aliinua kikombe chake na kunywa ile kahawa kisha akakishusha n kujiweka vyema kitini.

“Nipe mrejesho, maana tangu juzi ile hatujakaa kuongea, nilikupa kazi, unakumbuka?” Amata aliuliza.

“Nakumbuka sana, nitakuwa sekretari gani kama nasahau kazi ninazopewa na boss?!” aliuliza kwa kejeli

“Na utakuwa mke gani kama utakuwa unasahau majukumu unayopewa na mumeo?” kisha wote wakacheka. Gina akanyanyuka na kuiendea meza yake na kuivuta saraka, akatoa kabrasha moja na kuja nalo pale mezani, akalifungua na kumpa karatasi moja Amata, aliipokea na kuisoma kwa makini.

“Ok! Gina nakupa kazi ingine, nenda ofisi ya Idara ya uhamiaji pale makao makuu waulizie jina hili Shakrum Shakran, yuko nchini kwa shughuli gani na wakupe anuani ya wapi kafikia,” Gina alitikisa kichwa kuwa amekubali, lakini kabla hajaondoka, “Gina, tafadhali usitumie simu, sawa?”

“Sawa Bro,” alijibu kisha akarudi katika meza yake na kufungafunga, akahakikisha anakariri lile jina kichwani kisha akaaga na kuondoka, Amata akaendelea kufanya kazi zilizopo kwa wakati huo ikiwa ni kupanga mipango mabalimbali ya kuhakikisha anamaliza mchakato huo mapema ili ikiwezeka akamsaidie Chiba huko China kwenye sakata lile la Watanzania waliokamatwa na madawa ya kulevya na kuchafua jina la nchi hii tukufu yenye unono wa maziwa na asali.

WHITE SAND HOTEL

KIJUA cha alasiri kilikuwa kinaendelea kuchoma ardhi katika mchanga wa pwani ya White Sand, kila mtu alikuwa na hamsini zake, wengine wakiogelea, wengine wakipata vinywaji, wengine wakicheza mpira wa mikono kwenye mchanga ilimradi tu kwamba kila mtu alikuwa na shughuli ya kufanya.

Mawimbi makali yalikuwa yakipiga huku na huko, hali ile watoto wa Kihindi waliifuarahia sana na iliwafanya hata wengine kutoka katika madimbwi ya kuogelea na kukimbilia huko baharini wakiwa na furaha ya ajabu.

Kamanda Amata, aliibuka kutoka katikati ya mawimbi makali akiwa ni mmoja na wale waogeleao kwa furaha, kwa hatua za kujivuta kidogo alijaribu kupingana na maji ya bahari huku akielekea pwani akiwa ndani ya bukta ya kuogelea, mwili wake ulioonekana wazi sehemu kubwa uliwavuta watoto wengi kumshangaa jinsi alivyojaza misuli kimazoezi na kujijenga mwili mithili ya ‘Daniel Craig’, alitoka mpaka pwani akasimama kidogo na kuangalia huku na huku kisha akakatiza katika ule mchanga kuiendea meza moja iliyo chini ya msonge maridadi, pale palikuwa na msichana mmoja wa kihindi ameketi akijisomea kitabu cha riwaya ‘ISABEL’ kilichoonekana kumkuna kwelikweli, Amata hakumuacha msichana huyu hapo, lakini alishangaa kumkuta ameketi pale bila wasiwasi wowote, Amata alichukua taulo lake na lilitengenezwa kwa mfano wa koti na kulivaa,

“Waoh!” yule msichana alitoa mshangao.

“Vipi mbona unashangaa?” Amata alimuuliza

“Aaaa, mmmm! Umejazia mbaba mpaka napata..”

“Unapata nini?” Amata alimkatisha, yule msichana wa kihindi akaita mhudumu na kuagiza juice mbili, mara zikaja, akachukua glass moja na kumpa nyingine Amata, Amata alitupa jicho la wizi kwa msichana huyu hasa kiuno chake kilichojengeka vyema na makalio ya kubinuka kidogo, ‘Huyu Mhindi au Mbantu?’ alijiuliza,

“Cheers!” alitamka yule msichana huku akigonga glass yake na ile ya Amata zikalia nge! Yule mdada akapiga funda, Amata alipokaribia mdomoni mara alimuona Gina kafika na kusimama katikati yao, Gina akaichukua ile glass na kuirudisha mezani, kisha akamgeukia yule msichana wa Kihindi na kumsonya,

“Mxiuuuuu! Acha waume za watu,” kisha akamvuta mkono Amata na kuongozana nae upande wa malocker maalum ya kuhifadhi nguo na vifaa vingine kabla hujaenda kuogelea, akamgeuza Amata mbele yake na kumuoneshea ishara ya kimya yaani kidole chake cha shahada akakiweka kukatisha midomo yake, “Shhhhhhhh!!!!!!, ile juice ina sumu Amata, ungekunywa tu umekwisha” Gina alimwambia.

“Asante sana, Malaika wangu mlinzi, umefikaje hapa na umejuaje niko hapa?” Amata aliuliza.

“Usichezee mtoto wa kike wewe!” nilijua wazi huku kunaweza kuwa na hatari ndiyo maana nikaja kukuchunga. Gina alimuachia Amata, wakatazamana, “Nipo ghorofa ya juu kwenye ukumbi wa chakula, nenda kaendelee na mpenzi wako” Gina alipokwishakusema hayo akageuka kuondoka, Amata akamdaka mkono kabla hajafika mbali,

“Gina, njoo, upo na nani?”

“Nipo mwenyewe tu, usijali swahiba nakulinda,” akafungua pochi yake kumuonesha ndani mlikuwa na bastola mbili zilijoaa vizuri na magazine nyingine tatu za akiba, “Hapa kitanuka Amata, utaniona mi nani leo, lete ujinga na huyo Malaya wako.” Gina akaondoka akamuachia Amata kifaa maalum cha kunasa sauti kati yao wawili.

Dakika tano zilikuwa nyingi, kamanda Amata akawa ndani ya suti nadhifu ya kijivu iliyotanguliwa na shati la buluu bahari safari hii hakuweka tai aliuruhusu upepo wa pwani upite kwenye shingo yake na kuingia mpaka kifuani. Kwa hatua za kibrotherman alitembea kuielekea tena meza ileile akiwa na shauku ya kujua ni nani yule mrembo na alikuwa akitaka nini kwake, aliifikia ile meza, peupe! Hakuna mtu, mezani kulibaki na juice glass moja na ile nyingine ipo nusu, kitabu cha riwaya ‘ISABEL’ alichokuwa akisoma yule dada kilikuwa kimefunguliwa kurasa Fulani na kulaziwa kisu juu yake, kwenye ile kurasa kulikuwa na tone moja la damu na sentensi Fulani ilipigiwa mstari kwa wino mwekundu, akaisoma harakaharaka iliandikwa

…“Kamwe hamtoweza kufisha juhudi za kimataifa, mpango huu umesukwa na kusukika”…

…“Mimi ni mwanamapinduzi halisi, nipo hapa kwa kazi moja tu ya kuondoka na roho yako”…

Kamanda Amata akatoa kifaa chake cha mawasiliano na kupachika earphone sikioni mwake,

“Umewahiwa kijana” sauti ya Gina ilimnong’oneza

“Kaelekea wapi?” Amata aliuliza lakini kwa kuwa alikuwa akipigwa na upepo mkali wa bahari alijisika sikio ili asikilizane vizuri na anayeongea naye,

“Amata!, toa mkono sikioni haraka” sauti ya Gina ilimkaripia, Amata akashusha mkono wake na kubaki hajui afanye nini.

hiyo Gina binti Komba Zingazinga, akiwa ghorofa ya juu katika ukumbi wa chakula wa hoteli aliweza kuona matukio mengi yanayoendelea pale chini akiwa kavaa miwani yake maalu yenye auto focus ambayo si yo rahisi mtu mwingine kujua, pindi unapotua jicho kwenye kitu Fulani na kutulia miwani ile iliweza kukisogeza karibu uweze kukiona kwa usahihi zaidi. Gina aliiba miwani hii ofisini mwa Amata pindi tu aliporudi na kutomkuta ofisini alijua wazi kuwa atakuwa ameelekea White Sand kwani alimpa habari hiyo tangu usiku uliopita kuwa atafanya hivyo ili akajue nini na nani wanakutana, Gina alishaona hali hiyo ya hatari, hivyo alimua kufuatilia kwa mbali ili kumsaidia boss wake inapowezekana, alifika pale hotelini na moja kwa moja akapanda ghorofa ya juu na kutega mambo yake huko.

“Geuka nyuma uketi kiti cha upande huo!” Gina akamueleza, Amata akatii akageuka na kuketi, alipotazama mbele akamuona Scolleti akiwa amekaa kitini peke yake akijisomea gazeti, Amata aliitazama saa yake, ilikuwa imetimu saa tisa kasoro dakika kumi, aliishusha na kujituliza, alimwita mhudumu na kumuagiza soda baridi lakini kabla akamuomba aondoe vile vitu pale mezani.

Soda ilipokuja akawa anakunywa taratibu, mara kutoka lango kuu akaona gari moja aina ya Toyota V8 nyeupe ikiingia na kusimama jirani kabisa na banda lile aliloketi Scolleti watu wawili wakashuka. Mara hiyo muuza magazeti alipita jirani na Amata, akamwita na kununua gazeti Mwananchi na kuliafungua kisha kuanza kusoma lakini bado aliweza kuona kinachoendelea. Watu wawili walioteremka katika ile prado waliielekea ile meza ya Scolleti na kusalimiana kabla ya kuketi. Shakran Shakrum alikuwa amefuatana pamoja na Shailan boss wake. Amata alikuwa akiwatazama tu na kuhakikisha wasije kumtoroka, mara kwa mbali alimuona binti yule wa Kihindi akitokea kwenye bwawa la kuogelea akiwa na nguo za kuogelea, Amata alimtaza kwa shauku na kusahau kilichomleta, msichana yule alitembea kwa madaha akipita mchangani mpaka pale alipoketi Amata, akageuka na kumpa mgongo Amata, “Mmmm, magnificent view” Amata alitamka, yule msichana akageuka na kutoa tabasamu la wizi na kuchukua taulo lake kama lile la Amata na kulivaa, kisha akageuka na kutoka eneo lile,

“Shiiiit!” sauti ya Gina ilimgutua Amata alipotazama pale mezani hakuona mtu, wameondoka.

“Gina, wameelekea wapi?”

“Sijui, mi nilikuwa nakuangali wewe na huyo Malaya wako nageuza macho siwaoni” Gina akajibu.

“Ok, shuka twende, hapa si salama tena” Amata akiwa katika kuongea hilo, Nissan cedric ya kijivu ilipita mbele yake na kufunga breki kali kama mita ishirini hivi, watu wawili wenye sox zilizoficha nyuso zao wakachomoza kama umeme na kumdaka yule dada wa kihindi na kumvutia ndani ya gari kisha ile Nissan ikatoka kwa kasi na kusugua ile barabara kwa nguvu, Amata aliichomoa bastora yake na kujaribu shabaha, risasi ya kwanza ilivunja kioo cha nyuma, ya pili ikalikosa tairi, lo tayari ilikwishachukua barabara ya kuelekea barabara kubwa ya Bagamoyo, Amata alikimbilia pale alipoegesha gari yake na kuingia ndani akafunga mkanda, na kuitia moto kabla ya kuiweka barabarani, na kuondoka kwa kasi,

“Amataaaaaaaaaaa!!!!!!!!!!!!!!!” Gina aliita kwa sauti kali, Amata alifunga breki kali na Gina aliingia kwa kupitia dirishani kisha gari ilitolewa kasi huku watu wakishuhudia miguu ya Gina ikimalizikia kuingia ndani ya gari ile. Wakiwa karibu na barabara kubwa ya kuelekea Bagamoyo, aliiona ile Nissan ikisaga lami kuelekea upande wa Bagamoyo, Amata naey akaingia barabarani na kuzifanya daladala kupiga honi ovyo, akakunja kulia na kuifukuza kwa kasi, barabara ilikuwa nyembamba kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kuwafikia, Gina alikuwa ameketi nyuma akiwa ametulia tuli kwa woga akiangalia jinsi kamanda anavyofanya ovateki za hatari huku akiacha ajali nyingi nyuma yake.

“Kamanda polepole” Gina alipiga kelele

Kamanda Amata kama hakumsikia, bastola mkono wa kulia, usukani mkono wa kushoto, ngoma ipo 110 Km/h, baada ya dakika kadhaa alikipita kiwanda cha saruji cha Wazo na kuipita Tegeta, sasa walibaki wawili tu barabarani mwendo mkali wakielekea Boko. Ile Nissan ilikuwa ikienda kasi sana kiasi kwamba Amata aliona wazi hatoweza kuipata, akamtazama Gina kwenye kioo cha ndani akamuona kajikunyata kama kifaranga cha kuku.

“Gina! Njoo uendeshe hapa nimalizie kazi!” alimwita

“No! kamanda mi siwezi,” Gina alijibu kwa kelele

“Come on, Gina, njoo haraka” Amata alipiga kelele huku akipigapiga usukani wa gari ile. Gina alipita katikati ya viti huku gari ikiwa kasi sana, Amata alhamia kiti cha abiria huku mkono mmoja wa kulia sasa ukiwa umeshika usukani, Gina alipenya chini ya mkono wa Amata na kuketi nyuma ya usukani na kuikamata gari ile barabara kabisa.

“Uuuuuuuuuuuuiiiiiiiiiiiiiii Kamandaaaaaa!!!!!!” Gina alipiga kelele baada ya Amata kumuachia usukani alijikuta akishindwa kuimudu na gari ile ikayumba vibaya kisha akairudisha barabarani. Amata akavuta saraka katika dashboard ya gari yake na kutoa sortgun aina ya Double Barrel na kuivunja katikati, ndivyo inavyowekwa risasi hivyo jamani, akatumbukiza risasi mbili, kwa maana aina hii ya short gun inabomba mbili na lazima uweke risasi mbili na unapopiga hutoka zote mbili. Kamanda Amata alipohakikisha ameiweka vizuri akarukiti cha nyuma na kutokeza dirisha la kulia nyuma akitanguliza ule mtutu, kichwa nje alibana jicho moja sawia na kulitafuta tairi la ile Nissan, alipohakikisha lipo kwenye shabaha, alipotaka kufyatua trigger tayari kupiga, alihisi gari yao ikiyumba nakisha ikazunguka mchoro wa S, barabara yote ikitoa harufu ya mipira na kusimama ikiangalia ilikotoka, katikati ya barabara. Kamanda Amata aliangukia kwenye kiti cha nyuma na kukaa, damu zilikuwa zikimtoka pembeni kidogo ya pua yake, shortgun yake ikiwa mapajani.

“Gina umefanya nini sasa? Tumepoteza nafasi nzuri sana ya kutegua kitendewili chetu” Amata alimueleza Gina amabaye alikuwa anatetemeka kama mgonjwa mwenye homa kali, “Gina, Gina!” Amata aliita na alipojinyanyua kuangalia kule kwa Gina, “Shiiiiiiit!!!!”….

Nyoka mkubwa aina ya black mamba alikuwa akitoka chini ya kiti cha dereva na taratibu akawaakijizungusha karibu na mguu wa Gina, Kamanda Amata alimtazama huku akiuma meno, aliichomoa bastola yake na kumlenga sawia na kukifumua kichwa chake, risasi ile ilisambarataisha kichwa cha nyoka yule. Gina alishusha pumzi na kufungua mlango, akatoka nje akiwa hajiamini. Kamanda Aamata alitoka na kwa kutumia mtutu wa ile shotgun kamtoa nje yule nyoka, alikua nyoka mkubwa sana, kisha akavaa miwani yake na kuchungulia chini ya kiti kimoja baada ya kingine na kuhakikisha hakuna hatari yoyote.

“Washenzi sana, saa ngapi walituwekea huyu nyoka?” alijisemea huku akiizunguka gari yake na kutoa sonyo refu kisha akamuendea Gina aliyekuwa bado kasimama hajielewi, akamshika mkono na kumvutia upande wa pili, “Pole mrembo, panda twende,” alimsihi na kisha kumfungulia mlango, naye akaingia upande wa dereva kisha akageuza gari na kurudi mjini.

˜ ˜ ˜

“Siku ya nne sasa inaisha, deni letu kwa serikali linabakia siku tatu, mnafikiri watatekeleza ombi letu?” Shailan aliwaeleza wenzake.

“Hata kama siku zimebaki tatu, tena tuseme mbili kwa sababu hii ya nne inaisha, bado tuendelee kuwasubiri kwa maana hatujui wana lengo gani.” Shakrum akajibu.

“Hata hivyo, lazima tuanze kuandaa mazingira ya shambulizi la mwisho, shambulizi baya kuliko yote ambalo dunia lazima itetemeke kwa hofu na Afrika iishi kwa wasiwasi, wakati Tanzania itajutia uamuzi wake,” Shailan alimjibu Shakrum.

Scollet muda wote alikuwa akiwasikiliza, alikuwa kimya kabisa kama mtu ambaye hayupo pale, kisha kama aliyegutushwa kutoka usingizini, “Sasa mnataka kufanya nini?” aliuliza.

“Hilo kwa sasa hatuwezi kuzungumzia kwa sababu kuna mawili, maana hili jukumu inabidi limalizwe Julai 7 na mtu wetu awe mikononi kwa njia yoyote ile, lakini kama watakuwa na shingo ngumu kama ya Firauni basi watajua sisi ni nani, kesho watapata ujume wao wa mwisho,” Shailan alimalizia kauli yake, alikuwa akiongea kwa jazba sana wakiwa wamesimama pwani karibu kabisa na bahari ya mti kwenye mchanga mweupe wa White Sand Hotel baada ya kuhama pale walipokuwa wameketi kwanza baada ya kupewa taarifa ya kujihami na walinzi wao waliokuwa eneo lile.

“Itabidi tuombe silaha mbili za kutumia kwa mara nyingine, silaha hai,” Shakram alimwambia Shailan.

“Yeah, huo ndiyo mpango!”

Mazungumzo ya watatu hawa yaliendelea kwa takriban nusu saa kisha wakiwa kulekule pwani, boti moja ndogo ilikuja na kusimama umbali kama wa mita hamsini, wote wakaingia majini na kuingia kwenye hiyo boti kisha wakaondoka zao eneo lile. Walifanya hivyo kadiri ya maelekezo ya walinzi wao waliowaweka pale tangu mapema kuangali kama kuna lolote baya juu yao, hivyo wakawashauri waondoke kutumia usafiri wa maji kwani hakuna usalama barabarani kwa wakati ule, hivyo waliliacha gari lao pale kwa minajiri ya kuja watu maalumu kwa kazi hiyo na kuliondoa eneo lile.

Shakrum, alichukua simu yake ya upepo na kubofya kitufe Fulani, “Vipi mzigo umefika salama?”

“Yeah, umefika salama japokuwa tulipata msindikizaji njiani” alijibiwa.

“Msindikizaji?! Mliweza kumng’amua hakuwaletea shida?” Shakrum aliuliza

“Yeah, na kama si mbinu aliyotumia Staina saa hizi tungeongea mengine,”

“Atakuwa nani huyo?”

“Nafikiri ni kachero wa serikali”

Shakrum alishusha simu yake na kupumua kwa nguvu, Shailan alimtazama na kumtupia swali, “Vipi?”

“Jamaa wanasema walipata msindikizaji njiani,” Shailan alishtuka kidogo kwa jibu hilo. Mpaka dakika hiyo hawakugundua uwepo wa Amata eneo lile hivyo wao walizitazama hatari nyingine tu.

˜ ˜ ˜

Geti kubwa lilifunguliwa na gari ndogo aina ya Subaru iliingia taratibu ndani ya yadi hii kubwa iliyosheheni malori ya mafuta yasiyopungua mia moja, gari ile iliegeshwa pembeni na milango yake kufunguliwa, vijana wane walishuka na msichana yule wa Kihindi,

“Huku tafadhali,” mmoja aliwaongoza, na wengine wakafuatia wakiwa wamemshika yule mwanamke uku na huku ijapokuwa walimfunga kamba za katani mikono yake. Walitembea nae mpaka kwenye jengo lingine lililoonekana kutumiwa kama ofisi, wakaingia na kumtupia yule dada wa Kihindi na kumfunsia ndani ya kijichumba fulani.

“Aaah, Mungu mkubwa, sikutegemea kama tutafika salama,” mmoja wao aliyekuwa ndiye dereva aliwaambia wenzake, aliliendea jokofu kubwa lililokuwa katika ofisi hiyo ndogo na kuchukua konyagi ndogo kisha akaifungua na kupiga funda moja na kuirudisha jokofuni.

4

KAMANDA Amata alijitupa kwenye kochi kubwa na kuvuta chupa ya maji iliyokuwa mezani na kuigugumia yote kama mtu aliyetoka jangwani na kuteseka kwa jua na vumbi.

“Gina, unaendeleaje?” alimuuliza Gina aliyekuwa hoi katika kochi lingine upande wa pili.

“Sijiamini kama nimefika hapa salama, Amata naogopa sana nyoka, leo sijui kama ntaweza kulala nyumbani peke yangu” alijibu.

“Usijali utalala hapa kwangu kama shida ni uoga, angalau hata jiko langu leo liwashwe” kisha wote wakacheka.

“Gina, asante kwa kuniokoa, hivi yule mwanamke wa Kihindi ni nani?”

Gina badala ya kujibu akacheka kwanza na kumtazama Amata usoni.

“Amata, siku yako ya kufa utakuwa umelala na mwanamke kitandani, maana ndiyo udhaifu wako huo. Ile juice haikuwa na sumu ni mimi tu nilitaka uwe makini na lililokupeleka na siyo kufuatilia wanawake wa watu,” Gina alijibu. Amata akasonya na kujiweka vizuri, “Na we ulikujaje kule?”

“Ha, mi si ni secretary wako, lazima nijue uendako na nikuandalie kila kinachotakiwa ikiwamo usalama. We mwenyewe ulinambia kuwa utaenda kule kwa sababu hizi, lakini sikuweza kutulia kwa kuwa naona wivu, wanawake wengine wakafaidi na mi nipo hapa nakula kwa macho. Nikatangulia, nikachukua tax na kuja kisha nikaketi juu ghorofani nikiangalia mazingira, tangu unaingia nilikuona na kila ulichofanya, ulipokwenda kuogelea ndipo yule mwanamke wa Kihindi alikuja pale ulipoketi kwanza, ulipoacha taulo lako naye akaketi. Kiukweli sijui alikuja wakati gain na ni nani lakini nilimuona pindi tu alipokuja pale ulipoketi. Mwanzoni nilijua wamekuwekea mtego ndiyo ulikuwa wasiwasi wangu lakini nimeshangaa kwa nini wale jamaa wamemteka tena, ina maana si mwenzao?” Gina alieleza na kuuliza.

“Mi sijui, maana nimeona wakiondoka nae, ndiyo maana niliwafukuza ili niujue ukweli,” Amata alijibu na kubaki kimya kwa muda.

Mara pale kwenye kochi simu ya Amata ikaanza kuita kwa fujo, akaangalia namba haijui, akatulia na kuiacha, baada ya muda meseji ikaingia, akaichukua nakuisoma

‘…Natafutwa, nafuatiliwa na watu nisiowajua, naomba msaada… Mwad…”

Kamanda Amata akashusha pumzi na kuisoma tena ile meseji, kisha akampa simu Gina naye akasoma.

“Nani huyo?” akauliza Gina

Amata akamsimulia Gina kisa chote cha msichana Mwadawa, tangu walipokutana pale ofisini na kisha kuachishwa kazi.

“Mh! Itakuwa wanamuwinda sana” Gina alijibu.

Kamanda Amata alijaribu kuipigia ile namba lakini mara ya kwanza haikupatikana, alipojaribu mara kadhaa aliipata na kuongea naye. Mwadawa alikuwa akiongea kwa sauti ya chini.

“Bwana Stephen, nipo matatizoni unisaidie tafadhali” sauti ya Mwadawa ilisema

“Uko wapi sasa?” Amata (Stephen wa bandia) aliuliza.

“Nimejificha huku Kariakoo shimoni” alijibu

“Ok, subiri hapo nakuja” alimueleza, “ Gina twende,”

“Aah we nenda mwenyewe, saa hizi muda wa kazi umeisha” Gina aliongea na kucheka.

Kamanda Amata alijiweka tayari bastola zake mbili kiunoni, akaenda stoo na kuchukua pikipiki lake kubwa kisha kutokomea mjini.


MTAA wa Tandamti ulikuwa na shughuli nyingi kama kawaida yake, watu wengi wakubwa kwa wadogo walionekana wakitafuta hiki na kile, magari ya lioegeshwa bila mpangilio yalisababisha msongamano na kufanya mtaa ule kuwa vigumu kupita, achilia mbali wale walioweka bidhaa zao chini nao walileta tabu kwa watumia njia hiyo.

Kamanda Amata aliiacha barabara ya Msimbazi na kuchukua ile ya Swahili kuelekea soko kuu la Kariakoo, kwa mwendo wa wastani alipita huku akingalia huku na kule, watu walilishangaa sana pikipiki lile na jinsi lilivompendeza muendeshaji wake, punde kidogo alisimama mbela ya posta ndogo karibu na kituo cha daladala za Mwenge, akatulia kidogo akijaribu kupanga na kupangua ili ajue aanzie wapi. Aliitazama saa yake, muda ulikuwa unamtupa mkono, akaondoa pikipiki lake na kuzunguka upande wa pili wa soko hilo kubwa mpaka pale kwenye foleni ya malori yanayosubiri kuingia shimoni ili kushusha mazao yaliyobeba kutoka mikoani na sehemu mbalimbali za nchi, akachukua simu yake na kubonya namba Fulani Fulani kisha akaiweka sikioni,

“…yeah, niko hapa kwenye lango la kuingilia magari, njoo utanikuta…” kisha akatega sikio kusikia sauti ya upande wa pili,

“…naogopa kutoka wananifuata…” alijibiwa

“…njoo nakusubiri hapa hakuna lolote litakalotokea…” alimhakikishia usalama kisha akasubiri pale nje bila kushuka kwenye lile pikipiki lake.

Mwadawa Said alitokeza taratibu kwenye lile lango na kuanza kupandisha kuelekea huko yalikopaki yale malori. Kamanda Amata alitulia pembeni mwa lori mojawapo akiwa bado kavalia ile kofia ngumu na mikono ikiwa mfukoni akiangalia wote watokao na waingiao, kwa mbali alimuona yule binti akiwa anakuja kwa mwendo wa uwoga uwoga,

Julai Saba Sehemu ya Tatu

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment