Mikononi Mwa Nunda Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA
*********************************************************************************
Sehemu Ya Nne (4)
SURA TA TANO
“KHA! Msichana sijui yukoje yule?” Neema alisema walipobaki wawili.
“Yukoje?” Joram alimwuliza.
“Sijui yu koje. Naona yu mzuri lakini uzuri wake una kasoro. Kakaa kama mchawi hivi.”
Joram akaangua kicheko. “Nilijua utasema hivyo, Neema. Mtoto wa watu hana kasoro yoyote. Aliumbwa akaumbika. Tatizo lako ni lilelile ambalo humsumbua kila mwanamke, wivu. Unamwonea wivu kwaajili ya sura yake…”
“Sivyo,” Neema akamkatiza. “Sijamwonea wivu wala kuitamani sura yake.Ukweli ni kwamba sikumpenda tangu alipoingia hapa. Mtu akaribishwe vizuri, lakini atoke kama alivyoingia, bila angalau tabasamu dogo la shukrani.”
“Kama ni hilo lisikusumbue mpenzi,” Joram alimjibu baada ya kurejesha kicheko chake hadi kuwa tabasamu. “Kama ni hilo lisikusumbue hata kidogo,” akarudia. “Binti yule hana uwezo wa kucheka hata kidogo. Ana tatizo kubwa sana. Nunda anamnyemelea.”
“Nunda!” Neema akafoka kwa hofu. “Ana balaa basi! Nunda ametamani nini kwake?” akasita na kumkazia Joram macho makali. “Nawe umeahidi kumsaidia? Angalia sana Joram. Nunda sio mtu wa mchezo. Jiji zima hili limo mikononi mwake. Juhudi za polisi na wapelelezi wote, kwa Nunda hazifui dafu. Nakuonya Joram, usijiingize katika janga zito kama hilo. Uliyoyafanya kumsaidia yanatosha sana. Umeona mwenyewe jinsi Nunda alivyojificha kama kunguni na kuliendesha jiji zima apendavyo. Joram…”
“Neema,” Joram alimkatiza. “Nani aliyekufunza kusema maneno mengi kiasi hicho? Usijisumbue kupiga kelele zisizo na msingi. Nunda na ununda wake wote nitamtia mikononi. Ana bahati mbaya kuwa sasa nimepata mteja anitakaye kufanya kazi hiyo. Siwezi kumwambia mteja wangu, msichana mdogo na mzuri kama yule, ati nimeshindwa kukuokoa. Nimeshindwa kumpata Nunda! Wewe unanifahamu vizuri sana, Neema. Unafahamu wazi kuwa jambo kama hilo halijamtokea kamwe Joram Bin Kiango. Au sio?”
Ilikuwa sauti ya kikazi, sauti ya wazi, isiyo na mzaha. Lile tabasamu pia lilikuwa tayari limemezwa na sura nyingine kabisa, sura yenye macho maangavu yatoayo nuru kali yenye ari na nia. Neema, akiyaona hayo na zaidi, katika macho na sauti ya Joram, hakusema mengine zaidi ya “mh!”
Baada ya shughuli za hapo ofisini Joram alirejea nyumbani ambako alipumzika kidogo akijisomea. Kisha alilitia gari yake moto hadi West Bar ambako alichukua meza ya mbali na kaunta. Hakuwa mgeni sana katika baa hii. Safari zake kadhaa zilizomfikisha hapa, pamoja na ubora wa mavazi na umbo lake viliwafanya watumishi wote wa baa hii wamweke akilini. Hivyo, mara alipoketi tu mhudumu mmoja, mwenye mimba au kitambi cha pombe alimkimbilia na kuketi mbele yake. “Tukusaidie nini leo? Pombe au una maswali yaleyale yasiyo na mbele wala nyuma?” aliulizwa.
Kama kawaida yake, Joram alimzawadia mhudumu huyo moja ya tabasamu lake mwanana, tabasamu ambalo lilitimiza wajibu wake. Likamlainisha mwanamke huyo hadi akasahau haraka zake na kujikuta akiangua kicheko.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Leo ninahitaji chupa moja ya bia na jibu la swali moja lenye mikondo mingi,” Joram alimjibu. “Tuanze na pombe. Lete chupa mbili, moja kwa ajili yako.”
Pombe ikaletwa. Wakati wakiinywa Joram alianza kuhoji, “Katika moja ya safari zangu hapa niliwahi kumkuta msichana mmoja mzuri sana kwa sura na umbile. Yuko wapi siku hizi? Sijamtia machoni kwa muda mrefu au amepata bwana aliyeamua kumwachisha kazi?”
“Yupo… Yule Suzana! Kwa nini wanaume wote mnamtaka? Kwani mwanamke peke yake? Tumechoka na…”
“Aliitwa Suzana, sio?” Joram alimkatiza.
“Ndiyo,” akameza funda moja la pombe na kuendelea, “Yule sidhani kama amepata bwana. Kwa kweli, sijaona msichana kama yule. Hata siku moja sikupata kumwona akishughulika na mwanaume yeyote. Wengi sana walimpenda, lakini alikataa yote waliyopendekeza. Tena angefaidi sana. Ule uzuri wake na ujana wake! Ni kweli, kwenye miti hakuna wajenzi. Mimi ningeupata uzuri kama ule, angalau nusu yake tu, ningehakikisha napata nyumba na gari.”
“Tunamzungumzia Suzana, sio wewe,” Joram alisema akicheka. “Unaweza kuwafahamu jamaa zake au angalao alikokua akiishi?”
“Nadhani niliwahi kukwambia kitambo kuwa hatumfahamu vyema. Kwanza, hakukaa hapa zaidi ya miezi mitatu. Wala hakuwa mwenye tabia ya kupenda uhusiano na wenzake. Tulikua tukikutania hapa na kuachana hapahapa.” Akameza fundo jingine la pombe kabla hajasema tena. “Alikuwa msichana wa ajabuajabu, mtu asiyeeleweka… Hapana sio wa ajabu. Nasikia wako wataalamu wanaodai kuwa wazimu una aina nyingi, kwamba wazimu mwingine humfanya mtu apende dini kupita kiasi, mwingine ukimlazimisha kupenda masomo au mambo mengine. Kama kuna ukweli katika madai hayo basi naamini hata binti yule alikuwa na wazimu. Lakini wake ulikuwa wazimu usioelezeka. Mtu asipende dini, asipende wanaume wala pesa zao, ni nini lingine alilopenda duniani?”
Badala ya kujibu Joram alitabasamu huku akitikisa kichwa. Yakafuata maongezi mengine. Yalipoanza kuadimika Joram aliinuka na kuaga kwa kumshukuru mama huyo. “Umenisaidia sana, kwa kweli.”
“Mwongo mkubwa wewe,” mama huyo alijibu. Kama ungekuwa mtu mwenye shukrani si ungeshukuru kwa kunilaza loji angalao kwa siku moja? Niupime huo ujanja wako kama umo mwilini kweli au umeishia mdomoni tu.”
“Alaa! Ni hilo tu? Mbona hukusema zamani? Basi subiri kidogo. Iko siku…” alisema akienda zake.
“Mwongo,” Sauti ilimfikia pindi akitoka nje ya lango.
Kutoka hapo alisafiri hadi Kariakoo ambako aliliegesha gari lake mbele ya Mzalendo Lodge. Wakati huo ilikuwa kama saa mbili za usiku. Aliingia kwa hila bila kumruhusu mtu yeyote kumtia maanani, macho yake yakisoma namba za vyumba. Alipoufikia mlango wa chumba alichoelekezwa na Adela Mtambala, aliukuta ukiwa wazi. Aliugonga mara moja na kusikia sauti ya kike ikimjibu. “Ingia tu”
Joram akaingia. Macho yake yakavutwa moja kwa moja na umbo zuri la Adela ambalo lililala kama kujipumzisha chali juu ya kitanda. Umbo hilo laini lilikuwa limehifadhiwa na vazi jepesi la kulalia, vazi ambalo halikuhifadhi kikamilifu yote yaliyokusudiwa kutengwa na macho ya Joram. Naam, lilikuwa umbo jema linalovutia na kulazimisha ingawa kwa Joram lilipoteza ukamilifu kwa kutokuwa na mwenzi ambaye angekamilisha jozi.
Alitamani awe mmoja wa jozi hiyo, aguse na kuhisi joto na ulaini katika umbo hilo. Lakini hakufanya hivyo. Hakukiendea kitanda hicho kama ulivyomshawishi moyo wake. Bali aliifuata stuli iliyokaa kando ya kitanda hicho na kujiketisha.
“Za jioni?” alisalimu.
“Nzuri tu,” alijibiwa.
Macho ya Adela yalimtazama Joram ana kwa ana, yakiliona waziwazi tabasamu lililochanua katika uso na macho yake; tabasamu ambalo humfanya kila msichana alainike mwili na roho kila linapoelekezwa kwake. Kwa Adela halikufanya hivyo. Dalili yoyote ya kubabaishwa nalo haikujitokeza katika macho hayo. Badala yake yaliendelea kukazwa usoni mwa Joram. Akiwa anafahamu uwezo wa tabasamu lake hilo kwa wasichana Joram alihisi kitu kama hasira kuona halina athari zozote katika fikra wala sura ya msichana huyu.
“Samahani kwa kuichafua starehe na utulivu wako,” alimwambia. “Haja ya ugeni wangu ilikuwa ni kukichunguza chumba hiki ili nione usalama wako. Nadhani hakina kasoro. Hata hivyo, ningekushauri ujihadhari na kujitambulisha kwa jina lako halisi. Vilevile haitakuwa vyema iwapo utawakaribisha wanaume wengi usiowafahamu…”
“Simkaribishi hata mmoja,” Adela alimkatiza. “Siwapendi wanaume. Wala silaghaiki tena kwa ulaghai wao wenye ahadi tamu na matokeo machungu. La, sio mimi kamwe.” Sauti yake ilikuwa kali iliyodhamiria. Ikamfanya Joram kusahau hasira yake na kutabasamu.
“Inaelekea unawachukia sana wanaume,” alisema.
Adela aliukunja uso wake kidogo alipomjibu, “Ndio, siwapendi kwa kweli, sijui kama nitatukia kuwapenda. Kinachoudhi kwao ni tabia yao ya kuwa wanafiki na wanaopenda kunufaika binafsi. Wamewageuza wanawake kuwa vyombo vya kuwastarehesha badala ya kuwaona kama watu walioumbwa na kuumbika kama wao.”
“Sidhani kama ni kweli,” Joram alimjibu. “Kwa maoni yangu mimi naona jamii nzima imepotoka. Wanawake wanautumia uzuri wao na unyonge wao kwa haja ya kuwakamua wanaume. Ni wao wanaojitembeza na kujiuza ndipo wanaume huwatwaa na kuwatumia kwa manufaa yao.”
“Sio kweli,” Adela alifoka. “Hujui tu wenzako tunavyoadhirika. Tunalazimika kucheka ili tuwafurahishe wanaume, hali ndani ya mioyo tunayo majeraha makubwa; tunawaimbia nyimbo tamutamu ilihali rohoni tuna vilio vya miaka; tunacheza nao hali fikirani tuna maombolezo. Hujui tu, kaka yangu. Wala huwezi kuelewa kwa kuwa wewe hu mwanaume, kama wao.”
“Labda, lakini nina tofauti moja. Ninapenda sana kuelewa matatizo ya watu wengine. Maelezo yako yameninufaisha sana. Nimekuelewa na kukupenda sana kwa tabia hiyo ya kujieleza kinaganaga.” Akacheka kidogo kabla ya kuongeza, “Maadamu tunaelewana nadhani mimi ndio mwanaume pekee nikufaaye. Siku yoyote utapojisikia kumpenda mwanaume mkumbuke Joram Kiango. Au sio dada Adela?”
“Pengine, tutaona.”
Bado halikuwa jibu alilolihitaji Joram. Walao tabasamu dogo japo kwa kukosea!
“Ngoja niende,” alisema akiinuka. “Nadhani yote hayo yatafuata baada ya kumaliza kazi uliyonituma, yaani mara baada ya kukuletea huyo ajiitaye Nunda ili umfanye upendavyo.”
Maneno hayo yakamfanya Adela akurupuke kitandani na kuketi vizuri. “Joram, kweli nilikua nimesahau. Umefikia wapi katika uchunguzi wako?” sauti yake haikuwa kali kama awali. Ilikuwa yenye kitu kama hofu.
“Niko mahala pa kuridhisha sana. Usiwe na shaka mpenzi. Nitamtia mikononi mwako hivi karibuni…”
“Kweli! Una hakika Joram! Utafanya nini?”
“Atapatikana tu. Hilo hakuna shaka. Mhalifu yeyote, kwa hali yoyote, hupatikana. Hata awe mwerevu kiasi gani.” Akasita na kumkazia macho kabla hajaongeza, “Hukuwahi kusikia ile habari ya mwuaji ambaye alifanikiwa kuwaua watu zaidi ya hamsini kule Amerika? Mbinu zake zilikuwa za ajabu. Juhudi za polisi na raia wote hazikufua dafu angalao kumfahamu tu. Lakini ilitokea siku ambayo mwenyewe aliwapigia simu polisi akisema, “Njooni mnikamate kabla sijaua mtu mwingine zaidi… niko mahali fulani.” Polisi walidhani ni mzaha wa chizi mmoja. Hata hivyo, walikwenda mahala hapo ambapo walimkamata mtu huyo.”
Macho ya Joram yalikuwa juu ya uso wa Adela. Yalishuhudia na kuiona hofu iliyojikusanyha katika uso huo, hofu ambayo baadaye ilimezwa na kitu mfano wa tabasamu aliposema, “Pengine. Lakini nadhani hiyo ni hadithi tu kama zile za sungura na mizabibu.”
“Unadhani hivyo? Utaamini hapo nitakapokuletea huyo Nunda basi,” alisema akitoka na kuyaacha macho ya Adela yakimfuata.
***
Siku zilizofuata Joram alikuwa akipita katika majumba ya marehemu waliouawa na Nunda na kuuliza hili na lile. Sana alitembelea nyumba ya Ukeke Maulana, pamoja na ofisi yake. Huko alihoji mengi, akajibiwa mengi, mengi ambayo yalimfurahisha sana, ingawa waliomjibu hawakuona vipi majibu yao yangemsaidia.
Saa za jioni alikuwa akimtembelea Adela hotelini kwake. Alijaribu kumhoji mengi juu ya maisha yake, lakini ikamdhihirikia kuwa Adela hakufurahia hata kidogo kuzungumza chochote juu ya maisha yake ya nyuma wala ya baadaye. Badala yake wakawa wanazungumza mambo mengine kabisa, mambo kama anasa, starehe na tafrija mbalimbali. Siku zote walikuwa tofauti kimawazo katika kuzungumzia fani hizo. Joram alizisifia hali Adela akizilaani mara kwa mara.
“Kuwepo kwa starehe ndio chanzo cha maovu yote duniani,” siku moja aliwahi kusema. “Kila mtu anahitaji starehe, lakini si kila mtu mwenye uwezo wa kustarehe. Fedha huwa kipingamizi. Hilo humtuma mtu kufanya unyama kama wizi, unyang’anyi, rushwa, magendo na hata mauaji ili azipate – astarehe.”
“Sio kweli,” Joram alimjibu. “Unyama wautendao watu ni adui mkubwa wa starehe. Ni kinyume chake. Mtu anamwaga damu ya mtu ili astarehe yeye, itaisha hiyo starehe? Ni dhambi na upotovu tu kiasi cha kuifanya dunia kuwa chaka la maovu linalotegemea msaada wa polisi kuendelea kudumu.”
Mikutano hiyo ya mara kwa mara, Joram akija na kwenda zake, kuliwafanya wazoeane tosha. Adela akawa anazungumza kwa uhuru zaidi, huku macho yake yakianza kuonyesha dalili za kuhitaji kile ambacho hapo awali hakukihitaji, mwenzi, mwanaume. Naye hakuwa zaidi ya Joram. Ndiyo, Joram aliyaona hayo katika macho ya Adela kila alipofika na pindi akiondoka. Alipokuwa akifika macho hayo yalianza kupata nuru na kuchangamka, na alipoondoka msiba ulikuwa ukiyateka macho hayo.
Ikatukia siku ambayo Joram aliona kitu kama machozi yakimlengalenga Adela mara alipoinuka kutaka kuaga. Akamwendea na kuuweka mkono wake juu ya bega la Adela na kumnong’oneza, “Usijali mpenzi. Nipo na nitaendelea kuwepo tu. Kesho…” lakini Adela alimkatiza kwa kuuvuta mkono huo na kuukumbatia kwa nguvu huku akiufutika uso wake mzuri katika mto.
“Joram, sijui ni kitu gani kinachonisumbua juu yako. Labda ndicho hiki wanachoita mapenzi. Labda nakupenda Joram. Kwa kweli, nimevutiwa sana kwa tabia yako ya ukosefu wa tamaa kama walivyo wanaume wengine. Siku zote ambazo tumekuwa tukikaa chumbani humu, ungekuwa mtu mwingine ungekwishaniparamia kwa nguvu. Wewe una tofauti Joram. Unaujua na kuuheshimu utu wa kila mtu,” alisema kwa sauti ndogo, mfano wa mtu aliyekuwa akiomboleza.
“Labda ni kwa ajili ya kukupenda Adela. Hujui, lakini ni ukweli kuwa nimeondokea kukupenda mno. Wala si ajabu kukupenda kwangu. U kiumbe chema cha kike, kinachopendeza na kutamanika kuliko vyote nilivyowahi kukutana navyo maishani,” alisema, maneno yake yakifuatwa na lile tabasamu lake la asili.
Kwa mara ya kwanza tabasamu lilitimiza wajibu wake katika nafsi ya Adela. Akajikuta hajifai, hajiwezi. Bila fahamu akainuka na kumkumbatia Joram kwa nguvu. Joram alimpokea kwa kumvuta kwake na kumbusu mdomoni, busu ambalo Adela alilipokea kwa furaha kuu.
“Joram… Joram,” alinong’ona. “Unaonaje ukinioa? Siwezi kustahimili tena kutengana nawe. Naona wewe u mwanaume pekee ambaye uliumbwa kwa ajili yangu. Nioe, tafadhali. Nitakuwa kwako kama dada mwema mwenye njaa ya kukuhudumia kwa yote utakayo,” akasita alipouinua uso wake uliolowa machozi toka katika kifua cha Joram na kumtazama usoni.
“Unasemaje Joram?” aliuliza.
“Nina urithi mnono. Tutaishi vyema maisha yote. Sema tafadhali. Sema nikusikie.”
Joram alimsogeza kistaarabu hadi kitandani ambako alimlaza pole pole. Alipojaribu kuinuka Adela alimshika mkono. Hivyo, akajilaza kando yake na kumbusu tena.
“Nipe jibu lako mpenzi,” Adela alisisitiza.
Walikuwa wakitazamana ana kwa ana, wakiwa wamekumbatiana. Joram alilitazama umbo hilo zuri lenye sura njema. Kichwani mwake alihisi akitazama moja ya maua mema ambayo moyo wa mwanadamu hufarijika kuyatazama, ua ambalo kuwa nalo katika bustani yako kungekufanya uonewe wivu na jirani zako wote; kila mmoja akitamani kuwa nalo, liwe lake. Lake peke yake. Joram, kama wanaume wengine wote alijisikia hivyo. Alitamani amvute Adela mara moja na kumwambia, “Ndiyo kesho,” alitamani afoke kwa nguvu ili nchi nzima isikie, kila mtu asikie, asije akatokea yeyote wa kuingilia kati na kumnyang’anya zawadi hiyo. Lakini hakufanya hivyo. Hakumpa Adela jibu alilohitaji. Badala yake alisema, “Mpenzi, naijua thamani ya jibu langu kwako. Kadhalika, naifahamu thamani yako kwangu. Najua kabisa kuwa mimi ni kijana mwenye bahati sana kupendwa na msichana kama wewe. Si kwa ajili ya utajiri wako, la. Bali hasa kwa ajili ya umbo lako. Kwa kweli, simjui mwingine aliyekamilika kama wewe. Hata hivyo, sidhani kama ninayo haki ya kukuahidi ndoa wakati huu. Niliahidi kuwa nitamkabidhi Nunda mikononi mwako umfanye upendavyo. Nimezoea kutimiza ahadi zangu. Kwa hiyo, siwezi kukubali ombi lako kabla ya kutimiza nadhiri hiyo.”
Furaha iliyokuwemo katika uso wa Adela ilimezwa ghafla kwa tamko la Joram alipomtaja Nunda. Zilikuwa zimepita siku nyingi bila ya jina hilo kutajwa baina yao. Kumtaja Nunda kulikuwa kama kuliirejesha hofu iliyoanza kutoweka, hofu ya kifo. Kwa hofu hiyo Adela akamkazia Joram macho yenye dalili zote za huzuni kwa muda wa nusu dakika hivi. Nusu nyingine iliyofuata alikuwa amebadilika kiasi cha kuwa mkali mfano wa chui aliyejeruhiwa. Joram aliyakazia macho mabadiliko yote hayo katika uso wa Adela. Kisha akamwona Adela akitabasamu kwa namna ya uchungu mkubwa na kusema, “Mpendwa Joram naomba radhi sana kwa hali iliyonikumba. Kwa kweli, umenirejesha katika milki ya hofu na huzuni kwa kule kunikumbusha mkasa ulioko mbele yangu, mkasa wa Nunda. Kwa kweli, nilikuwa nimeanza kusahau yote tangu nilipohisi kukupenda. Niambie tafadhali. Niambie wapi umefikia katika kumjua Nunda. Ni nani?”
Joram alimwendea na kuutua mkono wake juu ya bega lake. Kwa sauti yenye tabasamu akamwambia, “Usijali mpenzi, nitalitimiza jukumu ulilonipa hivi karibuni. Ninachohitaji ni msaada wako tu, kwa jambo dogo. Nataka leo tutoke wote twende zetu pale West Bar, Buguruni, ili nikamilishe uchunguzi wangu.”
“La, siendi huko. Kwa nini niende?” Adela alikana mara moja. Sauti yake haikuwa na mzaha.
Tabasamu la Joram liligeuka kicheko aliposikia jibu hilo. “Tulitazame swali lako hilohilo kwa upande mwingine. Kwa nini usiende?” alimwuliza.
Adela aliduwaa akiwa hana jibu lolote. Badala yake aliyakaza macho yake kumtazama Joram usoni.
“Sijui kwa nini hutaki kwenda hapo. Ungekuwa umetoa mchango wako katika kumtia Nunda mbaroni,” Joram alisema akiutia mkono wake mfukoni na kutoa kitu. “Hata hivyo, bado kuna jambo jingine ambalo unaweza kunisaidia. Hiyo ni picha,” alimpa kitu hicho alichokitoa mfukoni. “Itazame uniambie kama unamfahamu mtu huyo.”
Ilikuwa picha ya marehemu Ukeke Maulana, ilionyesha kikamilifu sura yake. Joram aliiazima toka nyumbani kwake ili aitumie katika shughuli zake.
Adela aliitazama mara moja tu na kisha kumrudishia Joram huku akikunja uso ghafla. “Simjui mtu huyu. Sijapata kumwona tangu nilipozaliwa,” alisema.
“Alaa!” alinong’ona. “Basi umenisaidia sana mpenzi.”
Kikafuata kimya kifupi. Adela akiwa ameduwaa hali Joram akipambana na tabasamu lililohitaji kuumeza uso wake, pambano ambalo liliifanya midomo yake iwe ikichezacheza. Adela alikitibua kimya hicho kwa kuuliza swali lililomshtua Joram, “Unaupenda uzuri Joram?”
“Ndiyo, wa kila kitu, hasa wa mwanamke ambaye kila jicho humtamani.”
“Joram, unaupenda utajiri?”
“Sana. Ili niweze kuishi nipendavyo nikitimiza matakwa yangu yote.”
“Unaupenda uhai, Joram?”
“Naam. Endapo uhai huo utanipa uhuru wa kukamilisha matakwa yangu.”
“Yote hayo utayapata, mpenzi Joram” sauti ilikuwa yenye huba, macho yakiwa yamepoa kumtazama Joram ambaye alitulia kumsikiliza kwa makini. “Utayapata yote iwapo tu utaniahidi jambo moja tu. Kwamba utaacha leo na sasa kujishughulisha na upelelezi wako juu ya Nunda. Hapana. Usijibu harakaharaka, tafadhali. Ngoja nikueleze,” akapumua kwa nguvu na kisha kuendelea, “Hujui kwanini nakuonya ujihadhari naye. Kuna sababu nyingi. Mojawapo ni mapenzi niliyonayo kwako. Nimeondokea kukupenda kupindukia. Pengine hujui, au labda hutaamini. Lakini ni kweli kuwa wewe u kijana wa kwanza ambaye nimeondokea kumpenda duniani. Wa kwanza na wa mwisho. Nitakuwa radhi kufa kuliko kustahimili kukukosa, Joram. Madhara na ukatili wa Nunda mimi na wewe tunaujua. Kila mtu anaujua. Kwa hiyo, nakuonya tena ujiepushe naye tangu leo. Sawa?”
Joram alitaka kusema kitu, lakini Adela alimkatiza. “Ngoja nimalizie. Nimesema uzuri utaupata? Sio mzaha. Nadhani uliwahi kuniambia kuwa mimi ni mzuri. Sio wewe tu. Kila mtu aliyewahi kuniona huamini hivyo. Wengine wamekuwa tayari kutoa chochote ili waupate uzuri huu. Sikuwa tayari kuwapa. Lakini kwako mpenzi, kwako wewe ambaye u afya na heri yangu najikabidhi kwako. Nakupa kila kilicho changu ukifanye upendavyo. Tangu sasa…” akapumua kwa nguvu na kuendelea tena, “Ndio, ni pamoja na utajiri wote nilionao, niliorithi. Yote tangu leo ni yako. Yatatustarehesha hadi kufa bila haja ya kufanya kazi yoyote. Unasemaje, Joram?”
Joram alimsikiliza kwa makini. Kila neno lilimfanya atabasamu hadi, hatimaye, akajikuta akicheka. Lakini hakikuwa kicheko cha furaha ya kupata bahati hiyo kama alivyotaka Adela. Ilikuwa kinyume chake. “Waweza kuwa unanipenda sana dada yangu. Lakini nadhani hujanielewa vizuri. Nimesema mara nyingi na sasa narudia kwa mara ya mwisho. Mimi si mtu ambaye naweza kuacha mambo kijuujuu. Siwezi kununuliwa kwa bei yoyote ile kiasi cha kuhairisha matakwa na malengo yangu. Niliahidi kukuletea Nunda. Ni lazima nikuletee. Kama kweli unanipenda acha kwanza nitimize ahadi hiyo, ndipo mengine yatafuata baadaye. Nadhani leo iwe mwisho wa kuonana nawe hadi hapo nitakapomleta Nunda mikononi mwako, umfanye upendavyo…”
“Joram!” ilikuwa sauti yenye majonzi, ya Adela. “Sikia Joram…”
“Sina la kusikiliza zaidi. Ni hilo tu,” Joram alisema akitoka zake nje.
“Joram…” sauti ya Adela ilimfuata nje kama kilio. Hakugeuka wala kusita kumsikiliza.
*****SURA YA SITA****
Siku mbili baadaye, Joram alikuwa mtulivu katika ofisini yake, akijisherehesha kwa moshi wa sigara zilizokuwa zikiteketea moja baada ya nyingine. Mbele yake kulikuwa na barua kadhaa ambazo ndio kwanza zilikuwa zimeletwa toka posta. Alipomaliza moja ya sigara zake, alizitwaa barua hizo na kuzitazama kwa makini kama ilivyo kawaida yake. Hupenda kufahamu kila barua imfikiayo itokako, aliyeiandika na hata kushuku kilichoandikwa kabla ya kufungua.
Moja ya barua hizo ilimvutia. Si kwa kuwa ilikuwa imepostiwa siku hiyohiyo tu, bali hasa kilichomvuta ni aina ya mwandiko uliotumiwa juu ya bahasha. Ulikuwa mwandiko uliokorogwa kwa namna ambayo ingemdhihirishia kila msomaji kuwa ilikusudiwa kupotezwa mwandiko halisi wa mwandishi. Aliifungua barua hiyo mara moja na kutoa kipande cha karatasi kilichopigwa chapa kwa wino mwekundu. Alipoanza kuisoma tu alijikuta akitabasamu. Na alipomaliza tabasamu lake tayari lilikuwa kicheko. Kicheko chake kikamfanya Neema, ambaye alikuwa akishughulika na yake, akiache kiti chake na kumjia Joram. “Kuna nini?” alimwuliza.
“Soma hii,” Joram alisema akimsogezea barua hiyo.
Neema aliisoma harakaharaka. Alipomaliza tayari alikuwa akitweta na kutetemeka. “Joram, hili kweli ni jambo la kuchekesha? Huoni kama uko katika wakati mbaya kuliko nyakati zote zilizowahi kukupitia?… Joram!… ilikuwa sauti isiyoelezeka kwa jinsi ilivyochanganyika na hofu, huzuni na mshangao. Macho yake yalimtazama Joram kwa namna ya kutoamini.
“Usijali Neema!” Joram alimjibu kwa kumtoa hofu. “Sina budi kufurahi kwani Nunda ametangaza vita ana kwa ana baina yangu na yeye. Amenipa uhuru wa haki ya kumtia mikononi mwa sheria kama nilivyokusudia. Atakipata anachohitaji. Vitisho vyake kamwe haviwezi kuwa kipingamizi cha kuninyima ruhusa ya kumkamata. Ole wake kwa hatua hii ya mwisho.”
“Joram! Unamataja Nunda kama mtu wa kawaida! Unasahau ukatili na unyama wake ambao unaitaabisha nchi nzima? Hukumbuki kuwa polisi wote wa jiji wameshindwa kumnasa na walao kumjua tu? Angalia sana Joram.”
Badala ya kujibu Joram alitabasamu tu, tabasamu ambalo kwa Neema lilimdhihirishia kuwa yote aliyosema yalikuwa yakipitia sikio moja na kutokea katika sikio la pili. Kwa huzuni na moyo uliokata tamaa, aliyaondoa macho yake toka katika uso wa Joram hadi juu ya ile barua ya Nunda aliyokuwa bado kashikilia mkononi, iliyoandikwa;
Ndugu Joram Kiango
Waraka huu kwako si ombi bali ni amri. Tangu sasa komesha ndoto zako za kumpeleleza Nunda. Ukionekana ama kusikika kuwa unaendelea, kichwa na roho yako vitakuwa halali yangu. Umo mikononi mwangu.
Wakumbuke wote ambao nimewafanya marehemu, utagundua kuwa sifanyi makosa ninapokusudia kuua.
Ndimi,
NUNDA MLA WATU.
“Barua hiyo imenifurahisha kwa jambo moja,” Joram alitamka ghafla, macho yake yakimtazama Neema. “Imenionyesha uoga wa huyo juha anayejiita Nunda. Hana hali, anatetemeka, tangu aliposikia Joram Kiango ameamua kumsaka. Hilo linathibitishwa na barua hiyo. Ilikuwa kawaida yake kudai fedha kwa watu. Kwangu hadai chochote ila ombi ili niache kumsaka. Dalili ya hofu, anafahamu kuwa hatua niliyofikia katika uchunguzi wangu ni hatari sana kwake.”
“Kwa hiyo, ameona huna budi kufa,” Neema akaingiza.
“Na kwa bahati mbaya hawezi,” Joram alimjibu. “Joram si mtu wa kufa kwa mkono wala hila za juha kama huyo.”
“Joram…”
Upinzani wa Neema haukuzaa matunda. Alichoambulia ni kushuhudia furaha ikizidi kuneemeka katika uso wa Joram. Mara akamuaga na kudai kuwa anakwenda zake nyumbani kujiandaa kupambana na Nunda.
***
Alikuwa ameliegesha gari lake kwa dakika tatu tu toka ofisini pake alipolazimika kusimama baada ya kuombwa na mtu aliyesimama kando ya barabara. Karibu ya mtu huyo ulilala mwili wa mtu ukiwa umeloa damu miguuni. Hali ya mtu huyo aliyelala chini ndiyo iliyomfanya Joram kusimamisha gari kando yao na kuwaendea.
“Tusaidie ndugu yetu. Mwenzangu kagongwa na gari. Gari iliyomgonga imekimbia kabla hata sijanukuuu namba. Magari mengine yote yamekataa kutusaidia…” yule mtu aliyemsimamisha alisema.
Halikuwa jambo geni katika jiji la Dar es Salaam. Madereva wengi hutoroka mara baada ya ajali. Pengine wanastahili lawama, pengine hawastahili. Inategemea msimamo wa watu waliyoishuhudia ajali hiyo. Watu wengi usahau kumshughulikia majeruhi na badala yake kumvamia dereva na gari lake kwa mawe na marungu, jambo ambalo huatarisha maisha ya watu wawili badala ya mmoja. Akijua hayo Joram hakuona kama aliwajibika kumlaumu dereva wa ajali hiyo au la.
“Imetokea saa ngapi ajali hii?” aliuliza akimkazia macho msemaji baada ya kuyaondoa juu ya majeruhi.
“Kama nusu saa iliyopita.”
“Kwa nini hukupiga simu hospitali?”
“Kweli! Kwanini sikupiga hospitali?” mtu huyo alijiuliza kwa sauti. “Pengine nilichanganyikiwa kwani ajali hii nusura itukumbe wote. Tulikuwa tukitembea bega kwa bega. Mara…”
“Usijali. Nitakusaidia,” Joram alimkatiza. “Tumpeleke wapi? Muhimbili au hospitali yoyote iliyo karibu?”
“Nadhani popote. Yuko mahututi sana.”
Wakashirikiana kumwinua na kumwingiza garini, mlango wa nyuma. Wakamlaza juu ya kiti kwa uangalifu. Kisha Joram na yule mtu wa pili wakapanda mbele na kuondoka.
Wakati Joram akijitayarisha kukanyaga mafuta kikamilifu, kama inavyomstahili dereva yeyote ampelekaye mgonjwa hospitali, alilazimika kusita mara alipoguswa na kitu baridi kisogoni. “Huna haja ya kwenda hospitali yoyote. Siumwi…” ilifuata sauti nzito ya mtu yule ambaye hapo nyuma kidogo alikuwa akikoroma kwa maumivu. Joram alipogeuka kumtazama alikutana na domo la bastola kubwa ikimwangalia. Aliyeishikilia ni yule aliyekuwa mgonjwa. Alikuwa akimtazama Joram kwa dhihaka ingawa uso wake ulikuwa mkavu uliokunjamana. Tabasamu la kuchukiza likautokea uso huo na kuruhusu meno machafu kutokeza hadharani. “Tumekupata au sio? Leo huna hila Joram,” ilifuata sauti ya mtu huyo.
Kabla Joram hajajua afanye nini alihisi kutekenywa ubavuni. Alipogeuka alikutana na mtutu mwingine wa bastola ukimkuna, bastola ambayo ilishikiliwa na yule mtu wa pili ambaye kitambo tu alikuwa akibembeleza kwa sauti ya huruma. Kama mwenzake, huyu pia alikuwa akichekelea. Tofauti ndogo ni kwamba tabasamu la huyo halikuwa la kuchukiza kama mwenzake. Lilikuwa la kawaida. Na meno yake yalikuwa meupe. “Ndiyo, Joram Kiango, mpelelezi mashuhuri. Umo mikononi mwa Nunda. Umeingia kirahisi kuliko nilivyokutegemea. U wapi ule ushujaa ambao inasemekana unao? Labda nitauona pindi ukipambana na risasi. Nitapenda nikuue mwenyewe,” akacheka kabla hajaongeza, “Kwa sasa endelea kuendesha gari hadi nitakapokuelekeza wapi uende, wapi usiende. Sitapenda ubishi kwani nina ruhusa ya kukulipua wakati wowote.”
Joram alikubali kwa tabasamu jembamba.
***
Neema Iddi alibaki ofisini akijaribu kufanya hili na lile. Lolote alilolifanya aliliacha kabla ya kumaliza na kuanza jingine. Hilo pia aliliacha, akajaribu la pili. Hatimaye, alijikuta kaacha yote na kuduwaa kimya katikati ya chumba. Kilichokuwa kikimsumbua ulikuwa wasiwasi juu ya waraka alioupokea Joram toka kwa Nunda… umo mikononi mwangu… ulisema waraka huo. Lakini ilimshangaza kuona Joram akiuchukulia kama mzaha. Vipi?
Ni kweli kuwa hakuwa mgeni kwa Joram. Alimjua fika, sifa na vitendo vyake. Kadhalika, alikuwa na historia kamili juu ya vitendo vyake visivyoshindikana. Vitendo ambavyo siku zote viliwaacha polisi midomo wazi. Hata hivyo, hakuona kama suala la Nunda lingechukuliwa kimzaha kiasi hicho. Nunda ambaye amewababaisha polisi wote… Nunda ambaye anaua kama mchezo… Nunda ambaye amefichika kama chembe ya mchanga katika pishi ya mchele na hali yu kiumbe wa hatari zaidi ya kifaru aliyejeruhiwa… la, Joram hastahili kufanya mchezo naye. Akiyawaza hayo alijishtukia machozi yakimponyoka na kudondokea sakafuni. Machozi hayo yakamrejesha katika kipindi kingine cha mshangao, kipindi ambacho humtukia kila mara anapokuwa mbali na Joram. Hujihisi maradhi yasioelezeka na msiba usio na sababu, maradhi ambayo humfanya atamani kuondoka; hata kama ni usiku wa manane; akiache kitanda na kumfuata Joram kokote aliko; amnong’oneze neno. Neno lipi? Hakulifahamu kikamilifu. Labda, kwamba anampenda? Kwake hilo halikuwa swali. Ulikuwa ukweli ambao ulimwumiza kila alipojiuliza kama Joram naye alikuwa akimpenda. Hakujua. Ni kweli kuwa Joram alikuwa akimtazama kwa macho ambayo alihisi yameficha mapenzi. Lakini si kweli kuwa Joram alitumia tazama hiyohiyo kwa kila mwanamke? Kutokana na jibu la swali hilo hakukumzuwia kuacha kumlilia Joram rohoni. Aliendelea, moyo ukisononeka na nafsi kutaabika. Naam, kwa ajili ya Joram, ambaye anaifurahia nafasi ya kufa kama ya kuzaliwa upya!
Hofu ikazidi kuongezeka moyoni mwake kila alipoona dakika baada ya dakika zikipita pasi ya ujumbe wowote toka kwake. Mara kwa mara aliitazama saa yake kisha akautazama mlango kama ambaye alimtegemea kurudi ghafla. Hakurudi. Saa za kufunga ofisi ziliwadia bila ya kumwona. Kabla ya kufunga alikumbuka kupiga simu nyumbani kwa Joram. Haikujibiwa. Akafunga na kwenda zake nyumbani. Saa kumi na mbili aliiacha nyumba yake na kufuata kibanda cha simu ambako alizungusha namba za Joram tena. Bado haikujibiwa. Saa mbili, kadhalika. Tatu… sasa machozi yalikuwa yakimiminika machoni mwake bila kipingamizi, machozi mengi kiasi cha kumfanya ashindwe kuwaona watu wengi waliokuwa wakimtazama kwa mashangao; magari ambayo yalimkosakosa na chochote kingine. Alianza kuona alipowasili nyumbani kwa Joram. Alikuta nyumba imefungwa. Jirani hawakuwa na la kumwambia. Akaiacha nyumba hiyo na kuelekea kituo cha polisi cha Msimbazi.
“Joram ametoweka,” alimweleza askari wa zamu mara tu alipowasili.
“Nini?”
“Ametoweka. Naamini Nunda amempata. Mtafuteni haraka.”
“Shangazi embu jieleze kiutu uzima ili tuweze kukuhudumia,” askari alimweleza. “Vinginevyo tutashindwa kuelewa wapi unatoka, wapi unaelekea.”
Ndipo Neema alipojikaza kisabuni na kulieleza suala zima tangu alfa hadi omega, jinsi Joram alivyopata waraka toka kwa Nunda; jinsi alivyoupokea waraka huo kwa furaha kama mwaliko wa karamu; jinsi alivyoondoka ghafla; na yote mengine. Polisi walimsikiliza kwa makini, kisha wakamshauri kurejea nyumbani ili akapumzike.
“Kijana huyu mpumbavu sana,” Inspekta Mkwaju Kombora alinguruma mara tu baada ya kupewa taarifa hiyo. “Nilimwonya kwa ukali na upole ajiepushe na mkasa huu, hakunisikia. Siku zote yeye hujidhania mjanja zaidi ya polisi, mpelelezi mzuri zaidi na kwamba anaweza kupambana na chochote kama polisi au zaidi yao. Haya, tayari yamempata aliyoyataka…” kisha alisita ghafla baada ya kugundua kuwa alikuwa anazungumza mambo ambayo, yeye kama askari, na hasa kama mkuu wao, hakustahili kuzungumza mbele yao. Wajibu wake ulikuwa ni kulipokea suala hilo kama inavyostahili, na kulishughulikia kikamilifu.
Ndivyo alivyofanya dakika chache baadaye. Alisambaza habari huko na huko katika vituo vyote vya polisi. Jina la Joram, umbile lake na gari lake vikafafanuliwa kikamilifu. Yeyote aliyeona dalili yake alishauriwa kuripoti kwa Kombora mara moja.
Wakati akisubiri matokeo ya uchunguzi huo, akiwa nyuma ya meza yake, alivuta sigara mfululizo kufukuza usingizi ambao ulijaribu kumtongoza. Sigara hazikufanya chochote. Kilichopoteza usingizi huo ni mawazo mazito juu ya tatizo la Nunda, tatizo ambalo siku mbili tatu zilizopita lilikuwa kimya hata akadhani limekwisha, kwamba Nunda tayari alikuwa amechuma na kuridhika. Wazo hilo ingawa halikumfurahisha lakini lilimfariji. Kwa kweli, alihitaji sana kumtia mbaroni Nunda. Lakini alihitaji zaidi amani na usalama. Kwa hiyo, utulivu uliopita ulimpa faraja. Kumbe ilikuwa faraja batili! Nunda alikuwa bado hai na mkatili. Bado alikuwa na kiu ya damu. Joram amepatikana. Nani atakayefuata? Swali hilo ndilo lililomeza usingizi wote.
Ripoti mbalimbali zilimfikia hapo ofisini. Zote alizipokea kwa shahuku. Lakini zilimvunja moyo mara aliposikia kuwa hakukuwa na chochote kipya. Hadi mapambazuko hakukuwa na fununu yoyote ya Joram.
Wakati mchana ukikaribia kuteka milki ya giza ndipo ilipowasili ripoti ya kwanza yenye matumaini. Hata hivyo, yalikuwa matumaini yaliyotisha na kukatisha tama; kwamba gari la Joram, likiwa tupu na michuruziko ya damu, lilionekana likiwa limeachwa ovyo kando ya barabara ya Lumumba.
Habari hiyo ilizidi kumfanya akune kichwa. Hakujua kama huo ulikuwa mwanzo au mwisho wa matumaini ya kumpata Joram akiwa hai au angalau maiti yake. Wala hakujua aelekee upande upi kumtafuta, toka hapo lilipoachwa gari.
Akiwa katika hali hiyo ya mshangao na kukata tama, simu iliyokuwa mbele yake ikaanza kulia. Aliinua na kusikiliza. Sauti ya upande wa pili ilimfikia wazi na kumdhihirishia kuwa msemaji alikuwa katika hali ya utulivu na kujiamini sana. Alisema… “Inspekta Kombora? Njoo mtaa wa Zanaki, nyumba namba mia moja ishirini, mbele yake kuna mnazi; utakuta zawadi niliyokuandalia ambayo naamini itakupendeza.”
“Zawadi! Zawadi gani?”
“Inahusiana na Nunda.”
“Nini? Nunda! Ebu ngoja. U nani wewe? Na…”
Maswali ya Kombora hayakujibiwa wala kusikilizwa kwani simu ilikatwa ghafla.
***
Tabasamu lilikuwa bado limenawiri katika uso wa Joram wakati alipoanza kupewa amri badala ya kuombwa kama ilivyokuwa kipindi kilichopita. “Ifuate njia hii hadi njia panda… pinda kulia… kushoto… haya simama.” Yote aliyatii na kuyatekeleza kwa utulivu ambao, hatimaye ulianza kuwajaza hofu watekaji wake. “Haikusaidii kitu kujitia ushujaa, Bwana Joram. Kwa taarifa yako hutarudi kwa miguu yako. Unaelekea kuzimu…” mmoja wao alifoka.
Kama alikusudia kumtia hofu, Joram, basi hakufanikiwa. Ndio kwanza tabasamu lake likageuka kicheko. Kicheko ambacho kilifuatawa na sauti yake tulivu ikisema, “Mnajidanganya. Hakuna lolote litakalonitokea. Tangu mlipoanza mbinu zenu hafifu za kujisingizia ajali niliwang’amua. Sikuwachukulia hatua yoyote kwa kuwa nilijua ninyi ni watumishi tu, mliotumwa kunikamata, ili mnipeleke kwa bosi wenu. Ninamtaka bosi huyo, sio nyie.”
Yule aliyekuwa nyuma, ambaye alijisingizia kugongwa na gari aliguna kivivuvivu kisha akasema, “Ulijua sio, basi fahamu kuwa umefanya kosa kubwa kuliko yote uliyowahi kufanya. Laiti ungekimbia. Sasa huna maarifa. Kesho maiti yako itaokotwa barabarani.”
Joram hakumjibu. Akaendelea kupokea amri. “Hama gari hii,” aliambiwa walipofika barabara ya Lumumba. Ingia katika teksi ile pale. Ukijaribu kutoroka hatutasita kukuripua hapahapa.”
Teksi hiyo ilikuwa na dereva ambaye Joram hakusita kumtambua kama mmoja wao, kwani mara tu alipoingia na wale wenye bastola ambazo zilifutikwa mifukoni zilimwelekeza kuketi, gari lilichomoka kama mshale likielekezwa walikotokea. Likaiacha barabara ya Lumumba na kuingia Kisutu hadi lilipotokea barabara ya Morogoro, likaifuata barabara hiyo kidogo na kisha kuiacha, likifuata mtaa wa UWT hadi ule wa Maktaba. Hapo lilijipenyeza vichochoroni na kutokea mbele ya nyumba ambayo Joram alisoma namba zake. Nyumba ilikuwa tupu. Wakaifungua na kumwongoza Joram ndani, katika kimojawapo cha vyumba kadhaa.
“Mfunge kamba,” yule aliyekuwa na Joram mbele alishauri. Mwenyewe aliketi mbele na kuielekeza bastola yake tumboni mwa Joram.
“Nahitaji kumwona mkubwa wenu. Nunda. Yuko wapi? Joram alidai.
Badala ya jibu alikwatuliwa ngwala ambayo ilimtia mweleka. Zikafuata kamba ambazo zilifungwa miguuni na mikononi kwa nyuma. Kisha mikono mikavu ikapita huko na huko katika mavazi ya Joram ikatafuta chochote cha muhimu. Kilichopatikana ni noti chache za miamia, moja ya ishirini na makaratasi ambayo waliyatazama kidogo na kuyatupa sakafuni.
“Sijui inakuaje mzembe kama huyu aogopwe ati yu mtu hatari zaidi ya polisi. Hajui kujihadhari. Hana hata silaha,” yule aliyemkagua alisema. “Unaonaje Tom? Tumwache domo wazi? Alivyo mwendawazimu anaweza kupiga kelele.”
“Kweli Brown. Nilisahau. Mtie chochote mdomoni kisha tulifunge domo lake kwa tambara.”
Chochote kilichopatikana kilitukia kuwa soksi kuukuu chafu kupindukia. Ikadidimizwa kinywani mwa Joram. Tambara bovu pia likafungwa kuuzunguka mdomo wake. Harufu mbaya ya vitu hivyo ilimfanya apumue kwa shida. Akautumia ulimi wake kurekebisha soksi hiyo, kitendo ambacho kiliwachekesha adui zake.
“Bora kifo sio?” yule aliyeitwa Tom aliuliza. “Usijali tutafanya kazi hiyo baadaye. Kwa sasa kwaheri.” Wakatoka na kuufunga mlango nyuma yao.
ITAENDELEA