Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden Sehemu ya Pili
IMEANDIKWA NA THE BOLD
************************************************************************
Simulizi: Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden
Sehemu ya Pili (2)
Baada ya ‘mahojiano ya kina’ yaliyochukua siku 48 kwa kutumia ‘mbinu zilizoboreshwa’ hatimae al-Qahtani akafunguka na kueleza ukweli.
Kwanza akakiri kuwa jina lake ni Mohammed al-Qahtani na ni raia wa Saudi Arabia.
Pia akakiri kuwa ni yeye ndiye aliyekataliwa kuingia nchini Marekani siku ya Tarehe 3, Agosti 2001 na akaeleza kuwa alipewa maagizo na mtu anayeitwa Khalid Sheikh Mohammed ili aje marekani kwaajili ya kazi maalumu. Pia alieleza kuwa aliwahi kupatiwa mafunzo maalumu ya utendaji wa kishushushu na mawasiliano ya usiri (Operational training in Covert Communications) na aliyempatia mafunzo hayo alijulikana kama Abu Ahmed al-Kuwait.
Baada ya kupewa maelezo haya ilikuwa ni hatua kubwa kiasi kwa CIA lakini bado kulikuwa na mambo kadhaa hayakuwa sawia.
Kwa upande Khalid Sheikh Mohammed (KSM) mtu ambaye kijana huyu alimtaja kuwa ndiye alyemuagiza aje Marekani, mtu huyu alikuwa anafahamika vizuri na CIA. Walimfahamu kuwa ndiye moja wa Lutenati wa ngazi za juu wa kikundi cha Al Qaeda na ndiye ‘mchora ramani’ wa mashambulizi ya septemba 11, 2001.
Lakini mtu wa pili (Abu Ahmed al-Kuwait) aliyetajwa na huyu kijana kuwa ndiye aliyempatia mafunzo kijana juu ya ushushushu na mawasiliano ya siri, mtu huyu CIA walikuwa hawamfahamu. Ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kulisikia jina hilo.
Hivyo basi kipaumbele kikawekwa kwamba kijana huyu ‘ahojiwe’ zaidi ili atoe taarifa zitakazofanikisha kumpata KSM (Khalid Sheikh Mohammed) ‘mchora ramani’ wa mashambulizi ya Septemba 11. Mahojiano kwa kutumia mbinu zilizobordshwa yakaendelea.
Kwa msaada wa maelezo waliyoyapata kutoka kwa kijana al-Qahtani maafisa wa CIA kwa kushirikiana na maafisa wa ISI (Inter-Service Intelligence – Idara kuu ya masuala ya usalama na ushushushu nchini Pakistani) walifanya oparesheni maalumu ya kumkamata KSM (Khalid Sheikh Mohammed) baada ya kumuwinda kwa muda mrefu sana na hatimae siku ya Machi 1, 2003 walifanikiwa kumkamata KSM akiwa hai katika katika jimbo la Ralwapindi nchini Pakistani.
Baada ya kukamatwa tu na taarifa hiyo kufika makao makuu ya CIA Langley, Mkurugenzi mkuu Bw. Panetta akaamuru KSM awekwe ‘mahali salama’ mara moja. Na pasipo kupoteza muda siku hiyo hiyo CIA wakampandisha ndege KSM na kumpeleka gereza la Guantanamo. Na baada ya KSM kupokelewa Guantanamo alipewa selo kwenye jengo mojawapo la Guantanamo linaloitwa Camp Echo na akatambulika kama mfungwa namba ISN 10024.
Kesho yake ‘mahojiano ya kina’ yakaanza kwa kutumia ‘mbinu zilizoboreshwa’.
Haikuchukua siku nyingi za ‘mahojiano’ KSM akaanza kufunguka na kusema ukweli. Kwanza akakiri kuwa yeye ndiye ‘mchora ramani’ wa shambulizi la Septemba 11, na ni moja ya malutenati wanaotegemewa na Al Qaeda katika kueneza propaganda za kikundi hicho. Akakiri kuhusika kutafuta vijana watakaotekeleza shambulizi hilo, akakiri kusaidia baadhi yao kupata mafunzo ya urubani na akakiri kusaidia kuwaingiza marekani vijana hao.
Maafisa wa jeshi na CIA walimbana zaidi KSM aeleze ni namna gani wanaweza kuwapata viongozi wa ngazi za juu wa Al-Qaeda na hasa hasa kiongozi mkuu lakini jibu la KSM liliwashangaza kila mtu. KSM akawaeleza kuwa hata yeye afahamu kiongozi mkuu yuko wapi au anapatikanaje.
Mwanzoni walihisi anawadanganya lakini baada ya ‘kumbana’ zaidi wakagundua kuwa anamaanisha kuwa hajui ‘kiongozi mkuu’ yuko wapi wala namna ya kumpata.
KSM akawaeleza kuwa kiongozi mkuu, Osama Bin Laden aliacha kutumia simu toka mwaka 1998 maada ya mawasiliano yake ya simu ya satelaiti kudukuliwa na CIA na kuponea chupu chupu kuuwawa na wanajeshi wa kimarekani.
Akawaeleza kuwa tangu hapo aliacha kutumia na mawasiliano ya simu na mawasiliano yote mengine ya kisasa na kwa upande wa mawasiliano akawa muumini wa falsafa ambayo imekuja kutumiwa na karibia maafisa wote wa ngazi za juu wa vikundi vya wapiganaji katika mashariki ya kati, kwamba; “If you live like you are in the ‘past’, the ‘future’ will never find you”! (Ukiishi kama upo kwenye nyakati za zamani, usasa hautakukamata kamwe).
Kwa hiyo mawasiliano yote yalikuwa yanafanyika kwa mdomo kutoka kwa mtu kwenda kwa mtu au kwa barua za kuandika kwa mkono.
CIA wakambana zaidi aeleze je yeye alikuwa anapataje maagizo kutoka kwa kiongozi mkuu na akawajibu kulikuwa na mtu mmoja tu ambaye alikuwa anaaminika kwa asilimia mia moja na kingozi mkuu na ndiye aliyekuwa ‘mpambe’ wa karibu wa Bin Laden na kwamba kwa miaka kadhaa wapiganaji wa Al-Qaeda wala malutenati wa ngazi za juu walikuwa hawajawahi kumuona Bin Laden wala hawajui alipo na maagizo yote waliyapata kwa mdomo kutoka kwa mtu mmoja pekee aliyeitwa Abu Ahmed al-Kuwait.
Maafisa wote wa jeshi na CIA waliduwaa. Hii ilikuwa ni mara ya pili wanasikia jina hili. Mara ya kwanza walilisikia kutoka kwa kijana al-Qahtani kuwa alipatiwa mafunzo ya ushushushu na Abuu Ahmed al-Qahtani na sasa wanaelezwa na KSM ambaye ni lutenati wa ngazi za juu kabisa wa Al Qaeda kuwa hajawahi kumuona kiongozi mkuu kwa miaka kadhaa na maagizo yote yalikuwa yanaletwa kwake na mtu anayeitwa Abu Ahmed al-Kuwait.
Kitu kilichowasahangza zaidi CIA ni kwamba walikuwa wanawafahamu viongozi na malutenati wote wa ngazi za juu wa Al Qaeda lakini jina hili lilikuwa jipya kwao. Hawakuwahi kumsikia Abu Ahmed al-Kuwait.
Wakiwa bado wapo kwenye mshangao wapigani wa kikurdi kutoka nchini Iraq wakawasiliana na serikali ya marekani kuwaeleza kuwa wamemkamata Hasaan Ghul moja ya mawakala wa Al Qaeda anayetegemewa nchini Iraq.
CIA wakampakia Hassan Ghul kwenye ndege na kumpeleka kwenye jela za siri nchini Romania.
Baada ya ‘kumuhoji’ kwa siku kadhaa Hassan Ghul akawaeleza kuwa maagizo yote kuhusu mashambulizi na mipango mingine anayapata kutoka kwa kiongozi mkuu Osama Bin Laden kupitia kwa mtu anayemfahamu kwa jina la Abu Ahmed al-Kuwait.
Mshangao wa CIA ukageuka kuwa kitendawili. Huyu Abu Ahmed al-Kuwait ni nani na wanawezaje kumpata?
Mkurugenzi Mkuu wa CIA akaamuru kuwa kumtambua na kumkamata Abu Ahmed al-Kuwait kiwe kipaumbele namba moja..
Baada ya mchakato wa muda mrefu hatimae mwaka 2007 CIA walifanikiwa kumtambua Abu Ahmed al-Kuwait ni nani! Wakafanikiwa kupata jina lake halisi (Ibrahim Saeed Ahmed) na kwamba mwanzoni alikuwa ni mwanafunzi wa KSM kabla hajapanda ngazi kuwa mpambe wa Bin Laden.
Baada ya kumfahamu kwa kiasi CIA wakaanzisha mpango maalum wa kumchunguza ili wapate taarifa zaidi juu yake. Ili waweze kumpata kirahisi CIA wakafanya zoezi maalum la kuwatambua ndugu zake mbali mbali waliokuwa wanaishi kwenye nchi tofauti tofauti za kiarabu.
Baada ya kuwatambua ndugu hao CIA wakafanya kazi ya kudukua mawasiliano ya simu ya ndugu zake na katika kitu kimojawapo ambacho walikigundua ni kwamba ndugu zake hao walikuwa na desturi ya kuwasiliana na namba za simu tofauti tofauti lakini zote zikiwa ni za Pakistan. Hii ilipelekea CIA kuhisi kwamba namba hizi ni za al-Kuwait lakini alikuwa anazibadilisha mara kwa mara ili kuepuka kugundulika.
Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden Sehemu ya Tatu
Also, read other stories from SIMULIZI;
- Plata O Plomo – Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja (Pablo Escobar) Sehemu ya Kwanza
- Plata O Plomo – Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja (Pablo Escobar) Sehemu ya Pili
- Plata O Plomo – Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja (Pablo Escobar) Sehemu ya Tatu
- Plata O Plomo – Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja (Pablo Escobar) Sehemu ya Nne
- Plata O Plomo – Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja (Pablo Escobar) Sehemu ya Tano