Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden Sehemu ya Tano
KIJASUSI

Ep 05: Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden

SIMULIZI Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden
Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA THE BOLD

************************************************************************

Simulizi: Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden 

Sehemu ya Tano (5)

Obama akawapa idhini ya mwisho kuwa amewaruhusu kufanya oparesheni hiyo siku itakayofuata yaani tarehe 30 April.

Kesho yake Obama akataarifiwa kuwa oparesheni imehairishwa kwa muda wa siku moja kutokana na hali ya hewa kutokuwa rafiki na badala yake itafanyika kesho yake tarehe 1.

Jioni ya siku hiyo Obama akampigia simu tena McRaven kumtakia kilala kheri yeye na makomando wake wa SEALs na akwashukuru kwa kujitoa kwao kwa ajili ya Taifa lao.

Siku ya tarehe 1 May ilipowadia wajumbe wa kamati ya usalama wa taifa walikusanyika katika chumba maalumu cha ikulu ya marekani (situation room) kufuatilia oparesheni hiyo kupitia kwenye runinga iliyokuwa inaonyesha picha za moja kwa moja zilizokuwa zinachukuliwa ndege ya kujiendesha (drone) iliyokuwa inafuatilia tukio zima la oparesheni hiyo.

Usiku wa manane Makomando wa SEALs wapatao 79 waliruka na helikopta za kijeshi kutokea kambi ya kijeshi ya Bagram mpaka eneo la mpakani Jalalabad. Walipofika hapo wakagawana. Makomando wapatao 24 pamoja na mbwa aina ya Belgia Malinois aliyeitwa Cairo waliingia kwenye helikopta mbili aina ya Black Hawk ambazo zimeboreshwa kuzuia kuonekana na Rada ya adui na kutotoa sauti.

Makomando waliosalia waliingia kwenye chopa kubwa za kijeshi aina ya Chinook.

Makomando ambao walipanda kwenye chopa za kivita aina ya Black Hawk hawa ndio walipewa jukumu la kuvamia makazi ya Bin Laden. Makomando wengine ambao walipanda kwenye chopa kubwa za kivita aina ya Chinook hawa watakaa maili kadhaa kutoka eneo la tukio kama tahadhali ikitokea wenzao wakahitaji msaada zaidi.

Baada ya kujigawanya hivi safari ya kuelekea kwenye makazi ya siri ya Bin Laden ikaanza.

Baada ya kuyafikia makazi ya Bin Laden Chopa moja ilitua eneo la mbele ya jengo na nyingine ilitua nyuma kwa juu na makomando wakashuka kwa spidi ya haraka kwa kutumia kamba.

Chopa ambayo ilitua mbele ya jengo, rubani aliiweka chini kwa makosa kidogo na kusababisha mkia wa helikopta kugonga uzio wa ukuta wa nyumba na almanusuura ipinduke chini juu lakini kwa ustadi akaiweka sawa na makomando wakashuka salama ingawa helikopta tayari ilikuwa imeharibika.

Baada ya makomando wote kufanikiwa kuingia ndani ya uzio wakaanza kuisogelea mlango mkubwa wa nyumba. Pembeni ya nyumba kubwa kulikuwa na vyumba vichache vimejengwa kwa ajili ya wageni na ndani yake walitokea wanaume wawili waliokuwa na bunduki aina ya AK-47 na kuwafyatulia risasi makomando wa SEALs.

Kabla watu hao hawajaleta madhara yoyote makonmando wa SEALs waliwadondosha chini kwa risasi mbili kila mmoja. Watu hawa wawili walikuja kutambulika baadae kuwa ni Abu Ahmed al-Kuwait pamoja na kaka yake aliyeitwa Abrar.

Kisha makomando wakaingia ndani ya nyumba. Na baada ya kuingia ndani kuna kijana akaonekana akikimbia kupandisha ngazi kwenda ghorofa ya juu. Naye akadondoshwa chini kwa risasi. Kijana huyu naye alikuja kutambulika kama mtoto mkubwa wa kiume wa Osama Bin Laden.

Baada ya kijana huyo kupigwa risasi mlango wa chumba kilichopo ghorofa ya juu ulionekana kufunguliwa na mtu akachungulia. Pia naye akafyatuliwa risasi kadhaa zikamkosa lakini moja ikampata ubavuni. Mtu huyo aligeuka haraka na kurudi ndani chumbani lakini kabla hajaufunga mlango wa chumba vizuri komando wa SEALs alifanikiwa kuruka na kubiringika mpaka ndani ya chumba hicho.

Katika kujitahidi kujificha mtu huyo (Bin Laden) alimnyakua mwanamke mmoja aliyekuwepo humo chumbani (mkewe Mdogo) na kumsukumia kwa komando wa SEALs lakini komando alifanikiwa kumkwepa mwanamke huyo na akafanikiwa kufyatua risasi iliyompata Osama kwenye paji la uso.

Papo hapo komando mwingine naye alikuwa ameshaingia chumbani naye akafyatua risasi iliyompata Osama kifuani. Bin laden akadondoka chini na komando mmoja akamfyatulia risasi nyingine kifuani akiwa hapo hapo chini. Pale pale roho ya Osama Bin Laden ikaach mwili.

Komando mmoja akatoa simu ya mawimbi ya kijeshi na kuwasiliana na kamanda McRaven aliyekuwa amebaki kwenye kambi ya Bagram. Baada ya kupokea tu simu komando akamueleza kamanda wake kwa kifupi tu “Geranimo”.

Kamanda wake nae akaitafsiri taarifa hii kwa watu waliopo Ikulu marekani pamoja na Rais Obama wakifuatilia Kupitia Satelaiti, kamanda McRaven akawaeleza “For God and for the country, Geranimo Geranimo Geranimo” kisha akamalizia “Geranimo EKIA” (EKIA – Enemy Killed In Action (Aduai ameuawa kwenye mapambano)). Geranimo ndio lilikuwa jina la fumbo (code name) la kumtambua Osama Bin Laden katika oparesheni hii.

Seneta Hillary Clinton kipindi akiwa kama waziri wa mambo ya nje wa Marekani naye siku alikuwepo Ikulu ndani ya situation room anaeleza kuwa mara baada ya Rais Obama kusikia taarifa hii kwa msisimko na hisia kubwa akaongea maneno machache tu, “we got him” (“tumempata/tumemmaliza”).

Baada ya kutoa taarifa hiyo kuwa wamefanikiwa kumuua Bin Laden, makomndo wa SEALs wakawakusanya wanawake na watoto wote waliowakuta ndani ya nyumba hiyo na eakawafunga kwa pingu za plastiki na kuwaacha hapo hapo. Kisha wakaubeba mwili wa Bin Laden na kuupakia kwenye Chopa.

Lakini kabla ya kuondoka wakailipua ile chopa iliyopata itilafu kwani isingeweza kuruka tena na hawakutaka watu wajue teknolojia yao ya siri inayotumika kwenye chopa hizo.

Zoezi lote hili lilipangwa kutumia dakika 40, lakini kutoka na umahiri wa hali ya juu wa makomando wa SEALs liliisha ndani ya dakika 30 pekee. Risasi 16 tu ndizo zilifyatuliwa na watu 5 waliuwawa (Osama, mtoto wake wa kiume, Abu Ahmed al-Kuwait, Abrar (kaka wa al-kuwait), na mke wa Abrar).

Baadaya ya hapo wakaruka mpaka kambi ya Bagram kisha mwili wa Bin laden ukapakiwa tena kwenye chopa na kupelekwa kwenye manowari ya kivita ya NAVY iliyoko baharini. Huko sampuli za DNA zikachukuliwa na mwili ukapigwa picha. Baada ya hapo mwili ukavilingishwa shuka jeupe alafu ukatumbukizwa kwenye mfuko mkubwa na imara, vikawekwa na vyuma vizito ndani yake, mfuko ukafungwa, ukatumbukizwa baharini. Huo ukawa mwisho wa Bin laden Duniani.

HOTUBA YA UTHIBITISHO

Jioni ya siku hiyo Rais wa marekani Barack Obama alitoa hotuba ambayo itakumbukwa kwa vizazi vingi vijavyo. Alisema;

“Habari za jioni, usiku huu napenda kuwataarifu Wamarekani na Ulimwengu wote kuwa Marekani imeendesha oparesheni iliyofanikiwa kumuua Osama Bin Laden kiongozi wa Al Qaeda na Gaidi anayehusika na vifo vya maelfu ya wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia……”

Ulimwengu ulisimama kwa sekunde kadhaa na wengine hawakuamini masikio yao na mpaka sasa wapo wasio amini na kumeibuka nadharia nyingi mno. Lakini hiki nilichokisimulia ndicho wanachoamini CIA na serikali ya Marekani, kuwa siku ya Tarehe 1 mwezi May mwaka 2011; “Geranimo E.K.I.A….. Adui aliuwawa katika mapambano.

Mwisho.

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment