Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA THE BOLD
************************************************************************
Simulizi: Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden
Sehemu ya Tatu (3)
Kwahiyo walichofanya CIA ni kusubiri siku ambayo ndugu yoyote wa al-Kuwait akipiga simu yoyote kwenda nchi ya Pakistan basi wataifuatilia namba hiyo ili wafahamu ni nani aliyekuwa anaongea naye.
Siku hiyo haikukawia sana kwani mwaka 2010 ndugu mmoja wapo alipiga simu kwenda Pakistan katika mji wa Pashwar. Kwa kutumia Wapalestina waliokuwa wanafanya kazi kwaajili ya CIA waliifuatilia simu hiyo mjini Pashwar na kuthibitisha kuwa aliyekuwa anaongea na simu hiyo alikuwa ni Abu Ahmed al-Kuwait. Baada ya al-Kuwait kumaliza kuongea na simu aliingia ndani ya gari na kuondoka na wapelelezi hao wakamfutilia kwa makini wajue anakoelea.
Pasipo kujua kuwa anafuatiliwa al-Kuwait aliendeshe gari mpaka mji wa Abbottabad. Na alipofika Abbottabad akaingia kwenye Jumba moja la kifahari. Jumba hili lilikuwa na muonekano na ulinzi uliotia shaka. Na hii ikapelekea CIA kuamini kuwa ndani ya jumba hilo hakuwa al-Kuwait pekee anayeishi bali kuna uwezekano mtu wa hadhi ya juu zaidi alikuwa anaishi humo ndani. Pengine labda kiongozi mkuu wa Al Qaeda, Osama bin Laden labda alikuwa ni mkazi humo ndani.
Waziristan Haveli
Baada ya CIA kugundua nyumba hii na kuitilia mashaka kuwa kuna uwezekano inamuhifadhi kiongozi wa hadhi ya juu wa Al Qaeda pengine labda Osama bin laden mwenyewe, hivyo wakaingiza wapelelezi katika mji wa Abbottabad ambao walinunua nyumba mjini hapo kama raia mwingine wa kawaida. Baada ya wapelelezi hao kufanikiwa kufanya mkazi mjini Abbottabad wakaanza kazi ya kukusanya taarifa juu ya jumba hilo na wakazi wake.
Wapelelezi hao ambao walikuwa ni raia wa Pakistan wanaofanya kazi kwa niaba ya CIA wakaanza kuwadodosa majirani na wakafanikiwa kupata taarifa za kutosha kiasi.
Kwanza majirani waliwaeleza kuwa jumba hilo linamilikiwa na mtu wanayemfahamu kama Arshad Khan (Abu Ahmed al-Kuwait) ambaye anaishi na kaka yake pamoja na familia zao. Majirani wakaeleza kuwa Arshad amewaeleza kuwa kuwa yeye ni msimamizi wa biashara za Hoteli za familia yao zilizopo Dubai. Pia majirani walimueleza kuwa Arshad (al-Kuwait) alikuwa ni ‘mtu wa watu’ na alikuwa anahudhuria karibia kila msiba mtaani kwao.
Pia walielezwa kuwa licha ya kuwa na uwezo wa kifedha huwa anapenda kufanya manunuzi ya mahitaji yake ya nyumbani hapo hapo mtaani na mara kwa mara hutoka na watoto wake kwenda kuwanunulia mikate kwenye duka la uokaji (bakery) mtaani hapo.
Pia majirani waliwaeleza kuwa wamezoea kuliita jumba hilo Waziristan Haveli (Waziristan Mansion (Kasri la Waziristan)) kwani waliamini kuwa wakazi wa jumba hilo wanatokea Waziristan.
Baada ya CIA kupata taarifa hizi kutoka kwa wapelelezi waliojipenyeza mtaani hapo wakaamua wapanue wigo zaidi kwa kuwahusisha kitengo Maalumu cha Taifa la Marekani chini ya wizara ya ulinzi (DOD) kinachohusika na kukusanya taarifa na Ushushushu wa kijiografia (National Geospatial-Inttelligence Agency – NGA) ili wafahamu nukta baada ya nukta ya jumba hilo.
Kwa kutumia picha za satelaiti na kukusanya picha kwa kutumia ndege inayojiendesha yenyewe (drone) NGA walipata taarifa zote muhimu kuhusu jumba hilo kuziwasilisha CIA.
Taarifa yao ilieleza kuwa jumba hilo lililoitwa Waziristan Haveli lipo umbali wa takribani kilomita moja na nusu kutoka kituo cha mafunzo ya kijeshi cha Abbottabad cha jeshi la Pakistan. Mtaani ambao jumba hili lilikuwepo ulikuwa na makazi ya wastaafu wengi wa jeshi la Pakistan.
Jumba hili lilichukua eneo kubwa zaidi kuliko nyumba nyingene za jirani kwani jumba lilijengwa kwenye eneo la ardhi lenye ukubwa la takribani mita za mraba 3,500.
Jumba hili lilizungukwa na ukuta wenye urefu wa futi 12 lakini ndani yake ukiingia unakutana na eneo la wazi tupu alafu anakuta ukuta mwingine wenye urefu wa futi 18. Kuta zoto hizi juu yake zilikuwa na waya za miba miba na umeme.
Pia jumba hili lilikuwa na ghorofa tatu na katika balkoni ya gorofa ya tatu ilikuwa na ukuta wake wa kuikinga wenye urefu wa futi 7. Pia kulikuwa na kamera za ulinzi katika kila kona ya jumba hili.
Pamoja na hayo pia NGA waligundua kuwa ndani ya jumba hilo kulikuwa na bustani kubwa iliyopandwa mboga mboga, pia kulikuwa na kuku zaidi ya 100, sungura pamoja na ng’ombe mmoja.
Pia jumba hili lilikuwa na mdirisha madogo na machache kiasi kwamba ukiliangalia haraka haraka unaweza kudhani halina madirisha kabisa.
Pia idara ya ushushushu wa kijiografia ya Marekani NGA ilifanikiwa kukusanya taarifa za wakazi wa jumba hilo ambapo walifanikiwa kung’amua kuwa Kasri hilo lilikuwa na wakazi wapata 22 wanaoishi ndani yake wengi wao wakiwa ni watoto. Pa waling’amua kuwa kulikuwa na takribani wakazi watani ambao kamwe walikuwa hawatoki nje ya jumba hilo.
Baada ya NGA kuwasilisha taarifa yao kwa CIA kuhusu vile walivyovibaini kuhusu jumba hili, Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Leon Panetta alizidi kushawishika kuwa Kasri hili lilikuwa linamuhifadhi kiongozi wa hadhi ya juu wa Al Qaeda na pengine ni Bin Laden mwenyewe anaishi humo.
Hivyo basi akaamuru ufanyike uthibitisho wa mwisho kuhakiki kama ni kweli kile anachokihisi.
CHANJO FEKI
Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Pattena alitaka kwanza kuhakiki kama hisia zao ni za kweli kuwa Bin Laden anaishi kwenye Kasri hilo. Hivyo basi maafisa wa CIA wakaja na mpango kuwa wafanye uhakiki wa uwepo wa familia yake na kama familia yake ipo kwenye jumba hilo basi hapana shaka Bin Laden atakuwepo ndani ya hilo Kasri.
Kwahiyo maafisa hao wakaemweleza mkurugenzi wao wanachotakiwa ni kupata sampuli za vinasaba (DNA) za watoto wanaoishi ndani ya jumba hilo.
Kwahiyo mkakati ukawekwa kwamba ifanyike chanjo feki ili wapate fursa ya kuingia kwenye jumba hilo kuwahudumia watoto na wakifanikiwa kuingia watatumia mbinu kadhaa kuchukua sampuli za vinasaba za watoto eidha kwa kubakiza damu kiduchu za hao watoto kwenye sindano ya kutolea chanjo au mbinu nyinginezo.
Ili kufanikisha azma hii CIA walimuendea Daktari Bingwa aliyeitwa Shakil Alfridi ambaye alikuwa ndiye daktari mkuu katika maeneo ya Khyber mpakani na Afghanistan.
CIA wakafanikiwa kumshawishi daktari Hugo ashiriki kwenye mpango huo wa kutoa chanjo hiyo feki.
Oparesheni Ya Kukamatwa Osama Bin Laden Sehemu ya Nne
Also, read other stories from SIMULIZI;
- Plata O Plomo – Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja (Pablo Escobar) Sehemu ya Kwanza
- Plata O Plomo – Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja (Pablo Escobar) Sehemu ya Pili
- Plata O Plomo – Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja (Pablo Escobar) Sehemu ya Tatu
- Plata O Plomo – Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja (Pablo Escobar) Sehemu ya Nne
- Plata O Plomo – Ulimwengu Wa Siri Kiganjani Kwa Binadamu Mmoja (Pablo Escobar) Sehemu ya Tano