Zawadi ya Ushindi Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA BEN R. MTOBWA
************************************************************************
Simulizi: Zawadi Ya Ushindi
Sehemu ya Nne (4)
mabaya mengine kadha wa kadha. Watu wengi walisema mengi. Wengine walilitukana, wengine wakililaumu. Baadhi hata walihama nchi na kwenda nje kwa kulichukia ama kuliogopa. Na ndipo lilipogundua kuwa dunia si mbaya bali wanadamu. Na kwamba taabu yangu haikuletwa na kuishi ila watu tunaoishi nao. Kama si hivyo kwa nini waichukie hata sera ambayo ina nia ya kumtengenezea mwanadamu maisha? Kwa nini waitukane siasa yenye lengo la kuleta uhuru halisi na haki? Kumbe starehe yao ni kutuona tukitembea matako nje na kulala njaa? Waache waseme wapendavyo, waache waame nchi. Mimi binafsi nilimwona Nyerere na wote waliofanikisha mpango huo kama nguzo pekee ambayo mnyonge anaweza kuitegemea. Nikaiacha pombe, nikaacha gofu na kichochoro nilichokuwa nikiishi na kwenda zangu kijijini ambako nilijipatia ardhi na kulima na kiwanja cha kujenga nyumba. Nilifanya kazi kwa bidii ambayo ililetwa na matumaini hadi shamba langu likawa kubwa lenye mavuno bora. Nyumba nyangu pia imepata bati na saruji…”
Alisita ghafla na kumkazia Sikamona jicho kali, jicho ambalo lilimtisha Sikamona nusura kumfanya ainuke na kukimbia. Alistahimili kwa kujikaza tu huku akiusikiliza moyo wake unavyotetemeka ndani ya kifua chake.
“Vipi tumwache mtu ambaye anavamia nchi kwa nia ya kupotosha yote hayo anirejeshe tena katika kundi la ombaomba? Kwamba anataka kuitoa nchi itokane na ujamaa! Tuishi wapi?
Wala si kupotosha maendeleo yetu, bali pamoja na kufanya matumaini ya nchi nzima yawe ndoto. Aharibu maisha, aharibu matumaini ya wenetu. Twawezaje kumwacha? Anastahili adhabu. Anahitaji kipigo. Tena kipigo halali kabisa. Tusipofanya hivyo tutakuwa wasichana badala ya wavulana. Tutakuwa kichekesho kwa dunia nzima. Tuna kazi moja tu, kumpiga.” Akasita tena ghafla kama alivyoanza. Ilikuwa sauti ndogo lakini inayofoka, sauti ambayo ilimfanya Sikamona si amwogope tu bali pamoja na kumwona kama mtu mpya katika macho yake.
“Kwa hiyo ndugu yangu,” sasa alikuwa mpole tena, mpole kama kawaida yake, sauti yake ya kuelimisha na kuonya, “Tuna kila haki na wajibu wa kupigana. Tunao uhalali wa kuua. Tusipoua si kwamba tutauawa sisi tu, bali pamoja na matumaini yetu, matumaini ya taifa zima. Lazima hilo uliweke kichwani.”
Kikafuata kimya kirefu.
Ndani ya kimya hicho, Sikamona alihisi hatia. Mdoe alikuwa ameuweka uchi moyo wake. Amezifichua siri za maisha yake, siri za imani yake, siri za matumaini yake, siri ambazo hakuwai kuzitoa kwa mtu yeyote wala hakutarajia kamwe kufanya hivyo. Alikuwa amempa yeye. Kwa sababu gani? Urafiki? La.
Yalianza siku nne zilizopita, tangu baada ya lile pambano lake la kwanza, nafasi yao ya kwanza kuwa katikati ya mizoga ya binadamu, kutazama damu inavyomwagika na kushuhudia
mwanamume anavyotahabika anapokata roho. Hali hiyo ilimtia simanzi kuu. Ikamnyima usingizi kwani kila alipolala alizisikia sauti za wafu wakilalamika kwa uchungu wa risasi. Alishindwa hata kula. Alipojaribu kula nyama alijihisi anakula nyama ya mtu mmoja baina ya maiti kadhaa alizosaidia kuzika. Ndipo akawa mnyonge, mgonjwa si mgonjwa, mzima si mzima. Alijitahidi kuwaepuka watu na kukaa peke yake, akiwaza. Juhudi za akina Mdoe na wenzake kumshawishi ale hazikufua dafu.
Lakini si sasa, baada ya Mdoe kumfunulia undani wake wote, maongezi ambayo hadi yanafika mwisho yalimfanya Sikamona ajisikie analo la kumwambia. Akapanua mdomo kulitamka. Lakini… neno lenyewe liliyeyuka kinywani mwake kama barafu na kutoweka. Badala yake aliduwaa akimtazama kwa macho yasiyomwona.
Kabla hajajua lipi lingefuata ishara ya vita ilisikika ghafla. Mdoe akashangaa kumwona Sikamona akiwa wa kwanza kuinyakua bunduki yake na kuondoka mbio.
Akamfuata.
ALIDUWAA mbele ya mahema. Hawakujua walipaswa kwenda wapi. Kadhalika, hawakumwona hata mtu mmoja. Yaelekea lilikuwa shambulio
la ghafla. Badala ya kwenda kokote walitazama huko na huko na kisha kutazamana kwa macho yanayoulizana swali lilelile, “Ni upande gani?” ngurumo za bunduki na mivumo ya risasi ndio iliyowapa jibu. Ilikuwa imezuka ghafla toka mbele ya kambi yao. Sikamona akaanza tena kukimbia kuelekea huko, Mdoe akimfuata.
“Sika!”
Akageuka kumtazama. Mdoe alikuwa hamtazami. Alikuwa ametoa macho kutazama wanakotoka, nyuma ya mahema yao. Mdomo wake ulikuwa wazi na uso kaukunja kwa makini kama aliyekuwa akiona kitu. Sikamona alitulia kumtazama na kutazama huko na huko bila
ya kuona chochote. “Twende zetu…” alijaribu kumweleza mwenzake, lakini mkono wa Mdoe ambao ulipunga hewani kumnyamazisha ulimfanya si anyamaze tu bali pamoja na kutulia kabisa. Hakujua alichokuwa akikiona Mdoe. Alijaribu kufikiria hicho anachokitazama mwenziwe bila mafaniko. Mawazo yake yalikoma pale Mdoe aliponong’ona bila ya kumtazama. “Adui.”
Akatoa jicho na kulikaza kadiri ya uwezo wake kutazama huko alikokuwa akitazama Mdoe. Bado hakuona wala kusikia chochote. Sauti pekee katika masikio yake ilikuwa ule uvumi wa risasi nyuma yao. “Yu wapi adui?” alinong’ona.
“Nifuate,” Mdoe alitoa amri huku akianza safari ya kurudi walipotoka.
Sikamona alisita kwa muda kabla ya kumfuata. Walitembea kwa kunyata polepole, kisha Mdoe akamwashiria Sikamona kuinama. Baada ya muda Mdoe alimwashiria kulala chini. Wakaenda wakijivuta kifudifudi mfanowa nyoka. Wakayaacha mahema yao na kutokea kwa nyuma. Wakaendelea kujiburuta hadi walipokifikia kichaka ambacho kwa kila hali kilistahili kuwa maficho. Hapo Mdoe alimwashiria mwenziwe kutulia. Wakalala bega kwa bega. Bunduki zao zilikuwa zimeelekea mbele ambako Mdoe alikutazama kwa makini hali Sikamona haoni wala kusikia chochote. “Anaona nini?… Uoga? Kichaa? Au damu ya watu inamdhuru kama ilivyo…” alijiuliza kimoyomoyo.
Mdoe alimkatiza mawazo yake kwa kuelekeza
kidole chake mbele huku akimnong’oneza, “Tazama.” Ndipo alipoweza kuviona vichwa viwili vya askari vikiwa vimeinuliwa toka manyasini. Vikitazama upande waliko. Kofia zao zilionyesha dhahiri kuwa walikuwa adui. Sikamona aliinua bunduki yake na kulenga kimoja cha vichwa hivyo tayari kuifyatua. Lakini Mdoe alimzuia akisema, “Hapana, ngoja.”
“Kwa nini?” alifoka kwa mnong’ono, “Unajua wale ni maofisa? Wanajadili mbinu za kutuhujumu.”
“Ndio, lakini subiri.”
Wakatulia wakiwatazama. Vichwa hivyo vilipotazama tena ndipo Mdoe alipomgeukia mwenzake na kumnong’oneza. “Sikia Sika, mbinu zilizotumiwa na hawa jamaa ni za hatari. Hivyo vita vinavyopiganwa huko si vita kamili. Hiyo ni mbinu tu. Wamewatuma hao wenzao, pengine kikosi kidogo ili wakati tukikiangamiza wao watuzingire na kutuangamiza pamoja na kuyateketeza makambi yetu. Hivyo, inatupasa kuangalia sana.” Akasita akifikiri kwa makini. “Sika,” baadaye alisema. “Tuna jukumu kubwa mbele yetu. Kuangamia au kunusurika kwa kikosi chetu kinategemea akili na juhudi zetu. Hivyo bwana, nakuomba unisikie, nenda upesi kwenye mapambano. Mwambie Kamanda hali halisi ilivyo. Mimi nitakuwa nao. Endapo wataanza mashambulio nitakuwa tayari kuwajibu. Sitaruhusu hata kibanda kimoja kiungue. Nenda.”
Sikamona akamshanagaa.
“Unaweza kupambana peke yako na maelfu ya watu? La. Tutakuwa wote. Na kama ni kwenda huko twende wote,” alisema.
“Sika, nasema nenda.”
Kulikuwa na kitu katika sauti ya Mdoe, kitu ambacho kilimfanya Sikamona ainue uso. Ndio kitu hichohicho kilikuwa katika macho yake. Kiliyafanya macho hayo kutoa nuru kali ambayo katika nafsi ya Sikamona ilikuwa amri isiyopingika. Bila kutamka neno jingine alianza kutambaa upesiupesi kurudi alipotoka.
Alikuwa hajafika mbali kabla hajasikia mlipuko wa risasi nyuma yake. Aligeuka na kuanza kurudi. Kisha alijishauri na kuamua kwenda. Amri na maarifa ya kijeshi yote yalimtoka akilini. Badala yake alijikuta akiinuka na kuanza kukimbia akisukumwa na mshindo wa buduki nyuma yake na kuvutwa na uvumi wa risasi mbele yake.
“Simama,” Sauti kali toka kichakani ilimfokea.
Akasimama akitweta. Sauti za risasi zilimdhihirishia kuwa alikuwa karibu ya kuingia katika uwanja wa mapambano aliokuwa akiukimbilia. Kisha, akageuka kutazama ilikotoka sauti hiyo. Aligongana na bastola ambayo ilikuwa imeshikiliwa na MP mwenye cheo cha Koplo.
“Mikono juu,” Koplo huyo alitoa amri nyingine.
Badala ya kutii Sikamona alifoka. “Afande unapoteza muda bure. Adui wako nyuma yetu wametuzingira. Nilikuwa nikienda kumpa
habari mkuu wetu. Kwa hiyo, mwambie hivyo. Tumezingirwa.”
“Muongo wee! Hutoroki mapambano wewe? Hutoki ulipokuwa umejificha na sasa unakwenda huko baada ya kuona adui amejitoa?” Koplo alifoka akimsogelea Sikamona. “Sema ukweli. Ni ujinga kunidanganga kwani…”
“Afande,” Sikamona alinguruma. “Utakuwa na haki ya kubeba hatia iwapo adui atafaulu katika mbinu yake. Nakuomba tena, nenda kampe mkuu wa Kombania habari upesi sana. Mwambie kuna adui nyuma yetu.” Baada ya kusema hayo aligeuka tena, hima kama alivyokuja na kuanza kukimbia.
“Wee! Simama!”
Sikamona hakujishughulisha wala kugeuka nyuma.
Alimkuta Mdoe kalala hatua chache toka pale alipomwacha, bunduki yake ikiwa imeishiwa risasi na sasa anapambana na adui kwa kuwatupia mabomu ya mkono. Damu zilikuwa zikimvuja shingoni, tumboni na usoni. Hali yake ilidhihirisha wazi kuwa alikuwa katika dakika za mwisho za maisha yake.
“Mdoe, unakufa!” Sikamona aliropoka baada ya kumtazama.
Ndio kwanza Mdoe akageuka na kumwona. “Uko hapa bado?” akauliza akifoka. “Hujaenda kupeleka habari? Nenda Sika, nenda haraka.”
Tayari nimeenda na kurudi” alimjibu akitweta. “Unajua Mdoe, unahitaji kumwona daktari upesi.”
“Usijali, bado wakati.”
“Haiwezekani. Lazima…” Kitu cha moto kilipenya katika paja la Sikamona na kuukomesha ubishi wake. Hima, akajilaza kikamilifu na kuiwasha bunduki yake kujibu risasi za adui ambazo zilikuwa zikidondoka huko na huko kama mvua. Iliwachukua dakika kama tano katika shughuli hiyo. Halafu, risasi za adui zikakoma ghafla. Sikamona akafahamu kuwa tayari jeshi lao limewasili. Akainuka na kuwaona adui wakianza kutawanyika mbio kama kundi la kondoo lililovamiwa na nyuki. “Barabara,” alinong’ona.
“Ndio. Tumefanya kazi njema.” Sauti ikamzindua Sikamona. Ndipo alipomkumbuka tena Mdoea. Akainama na kumtazama. Nuru ileile iliyokuwemo katika macho yake. Kisha alikuwa akicheka. “Ilikuwa kazi njema. Wako wapi? Tazama wanavyokimbia. Wengi wao sasa ni maiti, roho zao ziko ahera. Walidhani wangetuweza kwa hila ya kike kama ile?”
Sikamona hakuweza kumsikia. Alikuwa ametishwa tena na hali ya Mdoe. Damu. Damu kila mahali. Damu usoni, damu kinywani, damu mwilini. La, hakuwa mtu wa kupona. “Mdoe twende kambini,” Sika alimwambia akiinama kumwinua.
“Ya nini? Hapa nilipo pananifaa. Najiona niko nyumbani.”
“Usiseme hivyo Mdoe.”
“Ndio, niko nyumbani. Nina furaha kamili. Nitakuwa hapa hadi kiyama, nione kama watainuka hawa waliokusudia kutuhujumu.”
“Hapana Mdoe…” alisema huku akijitahidi tena kumnyanyua. Maumivu katika paja lake yalikuwa makali, hivyo alijikuta akichechemea kwa taabu kubwa na mtu mzito kama Mdoe mgongoni. “Jikaze kidogo basi,” alimwambia.
“Ya nini, Sika?… Usi… Usisumbuke. Niache tu, niko nyumbani.” Sasa hata sauti yake ilikuwa imebadilika, alitamka kila neno kwa kujilazimisha. Sikamona hakumsikiliza bali alizidi kujivuta.
Walipenya msitu na kuacha kelele za vilio na ngurumo za silaha kali nyuma yao. Wakawa wakiikaribia kambi.
“Sika… nitue…” Hakumsikiliza.
“Nitue Sika… Nitue…” alifoka kidhaifu. Bado Sikamona hakumkubalia.
“Haya… najua unajisumbua bure. Mimi niko nyumbani… umekuwa mwisho mzuri… mwisho wa kiume… mwisho unaomstahili mwanaume. Au siyo Sika?… Wako wapi? Wako wapi? Na wajitokeze kama wana ndevu…”
Kikafuata kimya kirefu. Sikamona aliona uzito ukizidi. “Mdoe,” akaita. “Mdoe!”
Hakujibiwa. Akagutuka na kumtua chini. Mdoe
alikuwa ametulia kimya, bila dalili yoyote ya maisha. Jambo lililomshangaza Sikamona ni lile tabasamu ambalo lilikuwa bado katika uso wake, tabasamu refu lenye dalili zote za faraja.
Ndipo naye alipohisi upya yale maumivu katika mguu wake wa kushoto, maumivu makali mfano wa moto unaowaka mwilini. Akafahamu kuwa alikuwa na madini ya shaba mwilini mwake. Jasho likaanza kumtoka. Juhudi zake zote za kushindana na maumivu hazikumsaidia. Akajikuta akianguka polepole na kulala kwa utulivu kando ya Mdoe.
11
LIWASHANGAZA askari wote walioshuhudia tukio hilo, kuona maiti mbili, nje kabisa ya uwanja wa mapambano, zikiwa zimekumbatiana. Kila mmoja aliyefika
katika eneo hilo aliduwaa na kutekwa na huzuni, damu ikiyashurutisha macho yake kuendelea kutazama. Baada ya muda umati mkubwa ulikwisha zizingira maiti hizo.
Kisha, jambo la ajabu zaidi likatokea. Mmoja kati ya maiti hao alionekana akifunua macho. Si hilo tu, bali ilikuwa pamoja na juhudi za maiti huyo kujiinua. Aliposhindwa, alijilaza tena, lakini macho yakiwa wazi. Halafu alionekana kukumbuka jambo. Akajikongoja kuinua mikono yake na kuanza kumsukasuka maiti mwenzake.
“Mdoe, Mdoe…” aliita kwa nguvu. “La, huwezi kufa, Mdoe,” alilalamika kwa sauti ya majonzi. “Mdoe, la…” sasa kilikuwa kilo.
Ndipo watazamaji wakafahamu kilichokuwa kikitokea. Mmoja alikuwa maiti, mwingine mahututi. Wakawainua mmojammoja na kumpeleka Sikamona kwa daktari. Maiti ya Mdoe, kama mashujaa wengine waliopoteza maisha siku hiyo, ilihifadhiwa kwa heshima kusubiri safari ya kurejeshwa nyumbani.
***
Sasa alipigana kishujaa, kwa moyo na nia moja.
Ilikuwa baada ya kupona lile jeraha lililomfanya kulazwa kwa siku kadhaa.
Ari hiyo mpya haikutokana na ile sifa ya ushujaa ambayo alipewa, pamoja na Mdoe, kwa ajili ya kitendo chao ambacho kiliyaokoa maisha ya kikosi kizima na kulifanya taifa lijipatie ushindi mwingine mkubwa. Ingawa walikuwa wamevunja amri zote za kijeshi kwa kitendo chao hicho, lakini bado walisifiwa na majina yao kuingia katika orodha ya mashujaa kati ya mashujaa. Na ni kweli kuwa kila askari ambaye alipishana naye hakukosa kumtupia lile jicho lenye tabasamu inayowakilisha hadhi yake mpya. Lakini bado hiyo haikuwa sababu. Haikuwa sababu kwa kuwa alifahamu kuwa kitendo hicho ndicho kilichomleta katika uwanja wa mapambano. Hakikuwa zaidi ya wajibu ambao aliapa kuutimiza.
Wala haikuwa kwa ajili ya kumuwaza Rusia na kujiambia jinsi ambavyo angemshangilia baada ya kurudi na sifa hizo. Ndio, angelakiwa kwa tabasamu halisi lenye husuda na hongera,
ambalo lingefuatwa na sauti nzuri ikisema, “Mpenzi umefanya jambo kubwa… ipokee zawadi yako…” hilo lilikuwa likimfanya ajiulize swali ambalo limetamba kichwani mwake kwa muda mrefu. Zawadi gani ambayo angepewa? Ingawa hakuifahamu aliendelea kuisubiri kwa hamu kubwa. Lakini bado hiyo haikuwa sababu ya ari yake mpya.
Hasa, ari hii ilikuwa imezuka katika nafsi yake kutokana na kifo cha Mdoe. Kumshuhudia Mdoe peke yake akiunyima umati wa adui njia ya kuingia katika kambi yao, na hatimaye kukata roho mgongoni mwake, kulimfanya azaliwe upya, upya kabisa! Alijihisi mwanamume kamili mwenye ujana kamili, mwili na rohoni timamu. Akili yake ikapambazukiwa na jambo moja tu: kupigana. Usipopigana utakufa. Kila mara alihisi maiti ya Mdoe mgongoni mwake, ikimkumbusha kifo, pamoja na kusikia tena ile sauti yake ya mwisho yenye furaha na majivuno ikisema, “Umekuwa mwisho mzuri, mwisho wa kiume…” Hayo yakaifukuza hofu ya kifo rohoni mwake, yakaiondoa huruma ya kike rohoni mwake, pamoja na kuzitokomeza zile ndoto za jinamizi na uoga wa damu katika moyo wake. Akajitupa katika kila pambano lililofuata kwa hasira na nia halisi, sauti ya maiti ya Mdoe ikimsukuma na kumpa ari zaidi. Alihakikisha mateka ambao walianguka katika miguu yake wanajuta kuzaliwa kabla hawajapelekwa kunakowastahili.
Leo walikuwa wamewateka askari chungu
nzima wa Amini. Kati yao kulikuwa na Waarabu kadha wa kadha. Sikamona alimsogelea Mwarabu mmoja na kumchangamsha kwa teke la tumboni. “Utasema kilichokutoa kwenu na kuja kufanya uharibifu huku.” Akamwambia akiongeza teke la pili. Mwarabu hakusikia Kiswahili. Badala ya kujibu, alilia kwa maumivu. “Sema kilichokuleta huku” Sikamona alimwuliza tena kwa kiingereza huku akimtia ngumi ya kifua. Bado Mwarabu huyo hakumsikia. Lakini alipozidiwa na kipigo aliangua kilio kwa nguvu akitamka neno lililosikika kama “Gadaffi, Gadaffi.”
Akamwacha huyo na kumwendea Mganda ambaye alionekana jeuri kuliko mateka wengine. Alikuwa na macho mekundu, sura ya kikatili na umbo la kinyama. Kila kiungo katika mtu huyo kilidhihirisha kuathiriwa na bangi. Alidhoofishwa na gongo pamoja na kutaabishwa kwa kila kitu ambacho ni hatari kwa maisha ya mwanadamu. Sikamona hakumchelewesha. Alimpiga kichwa ambacho kiliyafanya macho yake mekundu yazidi kuwa mekundu. Akamwinua na kumpiga ngumi ya pua. Kisha akamwuliza kilichomtoa kwao na kumleta Tanzania kufanya unyama. Mganda huyo alicheka, jambo ambalo lilimzididhia Sikamona hasira kali. Akamtia vibao vya mfululizo huku akisema, “Utajuta kuja Tanzania.”
“Sijuti,” Mganda alimjibu. “Labda nijute kuzaliwa.”
“Kwa nini?” Sikamona alisita kumpiga na kumwuliza kwa mshangao.
“Nahitaji kura, nahitaji kuishi. Nisingesaliwa nisingehitaji fyote hifyo. Kwa kuwa nilisaliwa lazima niishi. Maisha ni kasi. Mimi nimekosa kila kasi isipokuwa uashikari. Uashikari ni kama imbwa. Niko tayari siku sote kufanya bwana wangu asemafyo. Anasema kamata, nakamata. Ua, naua…”
“Bwana wako nani?” “Idd Amini.”
Sikamona akazidi kushangaa. “Yaani uko tayari kuua kwa kuwa umetumwa kuua? Huna haya wala utu ili uogope kuangamiza kiumbe asiye na hatia?”
Sasa walizungumza kama marafiki.
“Utu utanisaidia nini mbere ya maisha? Haya itanipa chakura? Watu wanafanya kila kasi iri ware. Wengine wanadeki fyoo fya wensao. Wengine wanafua nguo za wensao. Mimi naua. Nahitaji mshahara. Nire.”
“Unaua kwa ajili ya mshahara?” “Askari ni mbwa bwana”
Sikamona hakulisikia jibu lake. Alikuwa hamwulizi Mganda huyo tena, bali akijiuliza mwenyewe. Yawezekana ni kweli mtu kuua kwa ajili ya mshahara? Ni ipi thamani ya maisha basi? Labda ni kweli askari ni kama mbwa? Kama ni hivyo, wakulima na wafanyakazi maelfu kwa maelfu ambao wanataabika katika nchi kadha wa kadha ni wanyama gani? Punda?
Akaacha kumpiga Mganda huyo na kwenda zake huku kainamisha kichwa kwa wingi na uzito wa maswali kadha wa kadha ambayo yalikiteka upya kichwa chake.
Askari ni mbwa!
Wengine wanafagia vyoo, mimi naua ili nile.
***
Halafu ikatokea. Ujumbe wa siri uliijia kambi yao usiku ukiwa na ombi la wananchi wa Uganda kwa Jeshi la Wanachi wa Tanzania, kwamba ukatili na unyama wa Idd Amini ulikuwa umewachosha, wanaomba msaada wa kusaidiwa kuikomboa nchi yao ili watokane na makucha yake, na kuuepuka utawala wake.
Machozi ya furaha yalimtoka Sikamona kwa kule tu kufahamu jambo hilo, kwamba Waganda wameamua. Mdoe angesemaje iwapo angekuwa hai na kuisikia habari hiyo? Alijiuliza.
MBI lilikuwa limekubaliwa.
Hivyo, waliingia Uganda mchanamchana, wakifuata barabara na kupenya misitu. Ilimshangaza
Sikamona alipoona raia wa huko wakiwalaki kwa shangwe na vigelegele huku wakiwatupia maua na kuwaita “Wakombozi.” Haikuwa kuwalaki tu, bali pamoja na kuwaongoza katika maficho yote ya askari wa Amini pamoja na vijana kadha wa kadha kujiunga katika “Jeshi la Ukombozi.”
Kilichomshangaza zaidi ni ile furaha waliyokuwa nayo wazee wa huko kila walipokutana na askari wa Tanzania. Walionyesha kuridhika kwa kila kiasi kwamba iliwabidi kutamka mshangao wao kwa maneno.
“Wana adabu, wana heshima…”
“Ndio, na upendo pia. Uliona walivyombeba
mzee Mukasa alipojeruhiwa na bomu walilotega askari wa Nduli?”
“Si hilo tu, ona wanavyotusalimu kwa adabu. Ona wananvyotoa shikamoo kwa raia… uliwahi kuona askari wetu akifanya hivyo?”
Shukrani na moyo huo wa Waganda ukazidisha ari na upendo katika mioyo ya Watanzania. Wakajikuta wakipigana bila ya kujiuliza wanampigania nani. Kazi ikawa rahisi kuliko ambavyo ingestahili kuwa, kwani ilikuwa kama kusafishasafisha askari ambao sio kwamba walikuwa na imani kwa Idd Amini bali walitegemea hongo aliyokuwa akiwapa kwa kuiita mshahara.
Baada ya miezi kadhaa wakawa wameitapakaa Uganda nzima kama nyuki walioingia katika mzinga usiowatosha. Amini akasikika akilalamika, mara atakuja Tanzania kuomba radhi, mara Umoja wa Taifa uingilie kati, lakini ilikuwa kazi bure.
Kama ambavyo alikuwa akichekelea ukatili wake dhidi ya Waganda, ndivyo dunia ilivyotulia ikimcheka.
***
“Kazi mliyotutuma tumeimaliza,” Sikamona alijisikia hivyo. Alikuwa ameegemea mti mkubwa, mbele ya nyumba ya Idd Amini katika kijiji cha Gulu, kijijini kwao baada ya kusafisha nchi nzima. Baada ya kuikomboa Uganda dhidi ya utawala haramu wa kinyama ambao uliathiri maisha na uchumi kwa muda wa miaka minane kazi ilikuwa
ITAENDELEA
Zawadi ya Ushindi Sehemu ya Tano
Also, read other stories from SIMULIZI;