Balaa Sehemu ya Kwanza
KIJASUSI

Ep 01: Balaa

SIMULIZI Balaa
Balaa Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA: HALFANI SUDY

*********************************************************************************

Simulizi: Balaa

Sehemu ya Kwanza (1)

KILWA KIVINJE, mwaka 1989.

Ilikuwa tarehe kumi na tano, mwezi wa nne, mwaka elfu moja mia tisa themanini na tisa. Ilikuwa usiku wa manane, usiku wenye kiza kinene, usiku ulioandamana na mvua kubwa sana, na radi iliyotoa sauti kali na za kutisha sana pamoja na miale yenye mwanga wa kuogopesha.
Usiku huo ulikuwa ni usiku muhimu sana, kwa Don Genge pamoja na kundi lake hatari sana. Usiku huo wa tarehe 15 mwezi wa 4 mwaka 1989 katika chumba cha kuhifadhia maiti, katika hospitali ya wilaya ya Kilwa, maarufu kama Kinyonga, iliyopo katika mji wa Kilwa Kivinje, mkoa wa Lindi, kulikuwa na mkutano wa siri.
Don Genge akishirikiana na madaktari mahiri wa hospitali ya Kinyonga, pamoja na manesi wenye roho nyeusi, roho mbaya kabisa, roho zisizokuwa na chembe ya huruma hata kidogo, roho zinazojari pesa na kusahau utu, walikuwa wanaendelea na kikao chao cha Siri, kilichofanyika katika chumba cha siri, kikiwahusisha watu wanaojua kutunza siri.

Katika kikao hiko cha Siri. alikuwepo Don Genge mwenyewe ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao, Dokta Zaidi Kilumba, mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dokta Sharifa Juma, daktari bingwa wa upasuaji wilayani Kilwa, Dokta Tamaa Karimu, daktari aliyekuwa ndiye mkuu wa chumba hiko cha kuhifadhia maiti, kulikuwepo pia na watu sita, walinzi wa Don Genge, walikuwa walinzi mahiri, walinzi makini, wenye kujua kupigana aina zote za mapigano. Walinzi waliopitia vyuo mbali mbali duniani, waliojifunza aina mbali mbali za kuuwa na kufuzu kwa kiwango cha juu sana, waliopitia mateso makubwa sana katika mafunzo hayo, mateso ambayo si rahisi kuvumilika kwa binadamu wa kawaida, ndio, walipitia mateso katika mafunzo, mateso ambayo yamewafanya wawe imara sana leo hii, kutokana na mateso hayo sasa wana uwezo mkubwa sana wa kutesa, kumtesa mtu yeyote yule na kusema chochote watakachomuuliza, hata kama aliapa kiapo cha damu kutosema, vijana hao sita walikuwa wanajulikana kama SIX KILLERS, na majina yao walipewa kwa namba, kulikuwa na one, two mpaka six, namba zilizotolewa kutokana na ubora wao katika mapigano, ubora wao katika kujua mambo.
Katika kikao hiko cha siri walikuwepo pia manesi watano, manesi ambao walikuwa na umuhimu mkubwa sana katika mpango huu wa siri, manesi walioapa kuzitunza siri, kuzitunza siri vifuani mwao zikatulia tuli katika mioyo yao mibaya.

Ulikuwa mkutano muhimu sana kwao, labda ungeweza kufanyika sehemu nyingine tofauti na chumba hiki cha kuhifadhia maiti. Lakini sehemu zingine zote waliona siyo sahihi kwao, wakihofia siri zao kuwa hadharani. Waliamua kufanya kikao chao hiki katika chumba hiki, wakiamini ni sehemu salama sana, chumba ambacho kingekuwa ndio ofisi yao ya muda katika kutekeleza mambo yao hayo ya kinyama, mambo ya siri sana, yaliyohitaji sehemu ya siri na kuhusisha watu wenye kujua kutunza siri kama hawa.

“Naamini wote tumekula kiapo hapa, kile kiapo kinaitwa kiapo cha moto, kiapo kisichofutika hata mmoja wetu atakapokufa. Kiapo kile tulichokula inamaana tutaitumikia kazi hii katika siku zote za maisha yetu, na hata tukifa. Kazi tulionayo ni nyepesi, na kwa kuwa nyinyi ni watu makini naamini itakuwa nyepesi zaidi. Kazi yetu ni kuhakikisha hakuna maiti inayoenda kuzikwa kaburini kutoka katika hospitali hii ikiwa na moyo, lazima tuhakikishe kila maiti inayotoka katika chumba hiki, cha kuhifadhia maiti haina moyo.
Kwa siku tuna mkataba wa kupeleka mioyo ya watu kumi na mbili. Najua ni idadi ndogo sana hiyo, kwa hospitali kubwa kama hii, hospitali inayohudumia wilaya nzima.
Wote tunajua maiti zote za hospitali hii zinapitia humu, na ndio maana Dr Tamaa Karimu ukajumuishwa katika mpango huu” Mwenyekiti Don Genge aliacha kuongea, alitulia ili Kuhakikisha kila neno aliloongea linapenya na kunasa vizuri katika vichwa vya watu wale. Mle ndani kulikuwa kimya, kulikuwa na utulivu mkubwa sana, baada ya kimya cha kama dakika moja Don Genge aliendelea.
“Lakini inawezekana ikatokea siku hawajafariki watu kumi na mbili, na hivyo tukashindwa kupata idadi ya mioyo tunayoihitaji, Dr Zaidi Kilumba ndio maana ukajumuishwa katika jopo hili, wewe ni mganga mkuu katika hospitali hii, lakini kazi yako hapa itakuwa ni Kuhakikisha mioyo tunayoihitaji inapatikana kila siku, na ikiwezekana izidi, kazi yako kama mganga mkuu ni Kuhakikisha watu kumi na mbili au zaidi ya kumi na mbili wanakufa kila siku katika hospitali yako, isipofikia idadi hiyo itabidi uhakikishe unawauwa wewe, hapa sitaki kukufundisha utawauwa vipi, wewe ni daktari, kwa kuwa unajua kuwatibu, bila shaka na kuuwa unajua pia” Alipofika hapo Don Genge alitulia tena. Ili maneno hayo yazame na kujikita vizuri katika bongo za watu wale.
Baada ya muda mfupi aliendelea tena.
“Najua kazi hii inahitaji kufanya upasuaji, kuzipasua maiti ili kutoa hiyo mioyo inayohitajika, Dr Sharifa Juma ndio maana upo hapa, kazi yako ni Kuhakikisha unazipasua maiti kumi na tano kila siku na kuzitoa mioyo. Najua kazi yako ni ngumu na inahitaji wasaidizi, ndio maana kuna hawa madada watano, watakusaidia kila utakapohitaji msaada.” Don alitulia tena, Akafungua chupa yake ya maji na kunywa funda tatu kwa pupa, bila kujari kama alikuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti. Kuingia tu katika chumba kile kulihitaji ujasiri mkubwa, hili la kunywa maji lilihitaji uwe kichaa kidogo. Chumba cha maiti chenye harufu ya ajabu ya dawa zilizopuliziwa maiti ili zisiharibike halafu unywe maji, ama hakika zilihitaji ukichaa, ukichaa kama wa Don.
“Kanuni za kazi hii ni mbili tu, kutunza siri na ushirikiano. Kila mmoja wetu lazima atunze siri, huu ni mpango hatari kwa hiyo unahitaji usiri mkubwa mno, pia lazima tushirikiane ili kuweza kufanikisha Mpango huu, ushirikiano uwe ndio nguzo yetu kuu. Bila ushirikiano hakuna litakalofanyika. Mwisho kabisa, tutahakikisha akaunti ya kila mmoja wenu inajazwa pesa nyingi sana kila siku mtakapotukabidhi mzigo wetu. Pesa ambazo hamjawahi hata kuwaza kuwa nazo, hapo sisemi sana, mtajionea wenyewe…”

Alipofika hapo Don Genge alitulia, alitembeza macho yake taratibu kwa kila mtu mle ndani. Wote walikuwa kimya, Don Genge alivua miwani yake, akaanza kuipangusa vumbi kwa kutumia shati, ingawa haikuwa na vumbi hata kidogo. Wanajopo wote walimwangalia Don Genge, sasa ilikuwa zamu yake kuangaliwa.
“Nadhani tumeelewana” Don alisema huku akiendelea kuifuta miwani yake.
“Ndio” Wanajopo wote waliitikia. Kila mmoja kwa sauti yenye hisia tofauti. Wengine hisia za uwoga na wasiwasi, wengine hisia za majonzi, wengine hawakuwa na hisia yoyote, wao waliona wanaenda kufanya jambo la kawaida tu.
“Good, napenda sana watu majasiri kama ninyi, hii nchi imeshaoza, kila mmoja anakula kutokana na urefu wa kamba yake. Acha viongozi wafisadi kwa kupitia mikataba wanayosaini, mikataba ya kijinga kama ya chifu Mangungo. Nasi lazima tufisadi kwa nafasi yetu. Nchi haina mwenyewe hii, kila mmoja anakula anapopata nafasi ya kula” Don aliongea maneno hayo ili kuhalalisha wanachotaka kufanya. Wote mle ndani walisahau kwamba, ubaya haulipwi kwa ubaya, njia bora ya kulipa ubaya ni kumfanyia wema kwa aliyekufanyia ubaya, ili nafsi imsute, ili ajifunze.
Kikao kilifungwa saa tisa alfajiri. Kila mmoja alitoka katika kikao kile na dhamira moja tu, Kuhakikisha mioyo kumi na tano inapatikana kila siku, kwa njia yoyote ile.


Yusuph Shaweji, alikuwa ni daktari kijana sana katika kituo cha afya Kilwa Masoko. Marafiki zake walizoea kumwita Dr Yusha, wakichukua herufi ya kwanza ya jina lake, na herufi ya kwanza ya jina la baba yake.
Dr Yusha alikuwa daktari mwadilifu sana, mwadilifu kwa madaktari wenzake, mwadilifu kwa wagonjwa. Alikuwa ni daktari mwenye weledi na kazi yake. Daktari mwenye kuheshinu miiko na maadili ya kazi yake.

Usiku ule wa tarehe 15/ 4/ 1989, wakati Don Genge, madaktari pamoja na manesi wa hospitali ya wilaya ya Kilwa Kivinje, wakipanga mpango wao ule hatari, Dr Yusha alikuwa katika ukumbi wa Sillent in, katika sherehe ya ndoa yake, baada ya kufunga ndoa mchana wa siku ile. Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa Dr Yusha kutimiza ndoto ile adhimu katika maisha yake, ndoto iliyodumu katika moyo wake kwa muda mrefu sana. Kuoa ilikuwa ni ndoto yake, kumuoa Nasra, Ilikuwa ni ndoto yake kubwa sana.

Wakiwa katikati ya sherehe, katikati ya furaha, wakati Mc wa sherehe ile akitangaza kuwa ulikuwa wakati wa kulishana keki maharusi, ndipo Dr Yusha akipoisikia simu yake ikiita kwa mbali katika mfuko wa koti lake.

Katikati ya sherehe ya ndoa yake Dr Yusha aliitoa simu yake.

“Haloo Dr, mwanangu anaumwa sana, nahitaji msaada wako sana” Bila salamu sauti ilianza kuongea, Ilikuwa ni kama sauti ya kizee ama sauti ya mtu aliyechoka kutokana na madhila makubwa. Sauti ikiyotoka kwa hisia kali, ikiomba msaada.
Pamoja na kelele za muziki pale ukumbini, pamoja na kelele za watu pale ukumbini, lakini sauti ile iliyochoka ilipenya japo kwa shida katika spika ya simu ya Dr Yusha, na kutua kwa shida vilevile katika sikio lake la kushoto la Dr Yusha.

“Upo wapi?” Dr Yusha aliuliza kwa sauti kubwa kidogo.
“Hospitali Kivinje”
“Ngoja nimpigie Dr Kilumba, tuone atawasaidiaje?”
“Dr Kilumba na Dr Tamaa wote tumejaribu kuwapigia, hawapatikani kwenye simu zao kaka yangu” Ulikuwa mtihani mkubwa sana kwa Dr Yusha. Pamoja ya kuwa hospitali ya Kivinje hakikuwa kituo chake cha kazi, lakini alijiona ana dhima ya kusaidia wagonjwa popote pale. Sasa alikuwa anawaza, aendelee na sherehe ya ndoa yake au aende Kivinje kumsaidia mgonjwa.
“Nakuja baada ya nusu saa” aliijibu ile simu.
Mtihani mwengine ukafata, atatokaje katika ukumbi ule ilhali yeye ndiye bwana harusi. Upande mwengine wa shilingi maadili ya kazi na kiapo cha udaktari vilikuwa vinamsulubu kwa zamu.
Dr Yusha aliamua kwenda kumsaidia mgonjwa kwa njia yoyote ile.
Aliangaza mle ukumbini, alipigwa na butwaa, ukumbi mzima ulikuwa unamwangalia yeye. Ukumbi ukimshangaa. Dr Yusha akatulia kwa sekunde kadhaa, ndipo aliposikia, kumbe mshereshaji wa sherehe alikuwa amemwambia akakate keki iliyokuwa mbele ili akamlishe mkewe, Nasra, wakati yeye alikuwa busy na simu.

“Ndugu bwana harusi tunaomba uje ukate keki na kwenda kumlisha mkeo mpendwa ” Mshereshaji alikuwa anayarudia kwa mara ya tano maneno hayo. Wakati Dr Yusha akiwa mbali kwa mawazo, ya kumfikiria mgonjwa. Dr Yusha alikuwa anawaza, akakate keki ama aende Kivinje kumsaidia mgonjwa.
Alikuwa anafikiria kwa kina, kumlisha mkewe mpendwa Nasra ile keki tamu aende kuokoa uhai wa mgonjwa.
Nasra, mwanamke aliyekuwa anampenda kuliko kitu chochote hapa duniani alikuwa analia. Hakuelewa kabisa mumewe kakumbwa na nini.
Dr Yusha alinyanyua mguu wake wa kulia taratibu na kuelekea kwenye meza iliyowekwa keki, ghafla simu yake iliita tena….BALAA.
Dr Yusha alisita sasa, akakosa msimamo thabiti, akaanza kuitoa simu yake kwenye koti….

Akaiangalia simu yake. Ilikuwa namba ileile iliyompigia mwanzo, Dokta Yusha alijishauri kidogo, aipokee ama asiipokee….simu iliita mpaka ikakata. Akaitia tena mfukoni. Ukumbi mzima ulikuwa kimyaa, watu wote wakiwa hawaelewi kinatokea nini. Dr Yusha alipiga hatua nyingine ya kivivu kwa mguu wa kushoto kuifuata meza ya keki. Hatua ilivyotua chini, na simu iliita kotini.
Dr Yusha aliitoa kwa haraka.
Akaipokea.
“Uhai wa Mtoto wetu unakutegemea wewe, tunaomba uje kutusaidia baba” Ile sauti ya mwanzo sasa ilikuwa inalia. Sauti ile iliyosikika katika hali ya huruma ilipenya hadi katika moyo wa Dokta Yusha. Badala ya kuelekea kwenye keki, alielekea katika mlango wa ukumbi ule. Aliitafuta gari yake harakaharaka, akakumbuka funguo hakuwa nayo yeye. Alitafuta pikipiki ya kulipia (bodaboda).
“Kivinje faster” Alisema huku akiipanda.
Mwenye ile pikipiki hakuwa na cha kuuliza, aling’oa ile pikipiki kwa kasi, akaishika barabara inayoelekea Kilwa Kivinje. Jamaa alikuwa ‘ faster’ kweli.
Dokta Yusha aliacha taharuki kubwa sana kule ukumbini. Watu wote walibaki midomo wazi, wengi wakiamini Dokta Yusha amechanganyikiwa. Kwa bahati mbaya hakutokea mtu hata mmoja aliyepata wazo la kumzuia Dokta Yusha. Ilikuwa ni kama ukumbi mzima wamepigwa na ganzi.

Nasra, mke wake kipenzi Dokta Yusha alikuwa hakamatiki, alikuwa hashikiki. Analia kwa sauti na kugaragara chini. Ama hakika kilimuumiza sana kitendo kile. Aliona amepata aibu, aibu mbele ya wazazi wake, aibu mbele ya rafiki zake, aibu aibu aibu. Kwa mara ya kwanza alimchukia Dokta Yusha, kwa moyo wake wote alimchukia mwanaume yule wa maisha yake.
Wazazi wa Dokta Yusha nao walikuwa katika hali ya huzuni na masononeko makubwa. Hakika mtoto wao aliwaaibisha sana, tena katika sherehe ya ndoa yake, mbele ya umati mkubwa. Sherehe ile ya ndoa, iliyotangazwa sana, iliyogharimu pesa nyingi sana, ilikomea kati, kwa bwana harusi kutokomea na pikipiki, kusikojulikana, balaa !

Dakika kumi zilitosha pikipiki aliyopanda Dokta Yusha kufika hospitali, Kilwa Kivinje. Dokta Yusha aliruka kabla ya ile pikipiki haijasimama na kukimbilia kuingia ndani ya hospitali ile. Akiacha yule dereva wa pikipiki hajamlipa. Sasa ule mshangao wa watu wa kule ukumbini, ulihamia kwa mwendesha pikipiki. Dokta Yusha alifika hadi wodini, alikuta hali ya wodi shwari, hakuna mgonjwa yeyote aliyekuwa mahututi. Alienda mapokezi, hakukuwa na mtu yeyote usiku ule, alijaribu kuipiga ile namba, ilikuwa haipatikani, Balaa!
Sasa ule mshangao aliowaachia watu kule ukumbini, mshangao alioondoka nao na kumletea mwendesha bodaboda, sasa ulimvaa mwenyewe kwa kasi. Hakumwona kabisa mmiliki wa ile sauti iliyompigia simu, pale hospitali.

TANO, ni miongoni mwa walinzi wa Don Genge. Yeye ndio alipewa kazi ya kusafisha njia, ili mpango wao uendelee kama ulivyopangwa. Kusafisha njia ilikuwa inamaanisha kung’oa magugu yote, ambayo yangeweza kuwa kikwazo kwa mpango wao. Mmoja wa gugu ambalo walipanga kuling’oa ni daktari huyu kijana.
Walipanga kumuuwa Dokta Yusha !
Ni Tano ndiye aliyepiga simu ile, lengo ni kumleta Kivinje ili amuue. Bila kujua Dokta Yusha aliingia katika mtego huo hatari. Tangu Dokta Yusha alivyowasiri kwa pupa na pikipiki, mpaka sasa, Tano alikuwa makini nae kila anapokwenda. Lengo ni kupata sehemu sahihi ya kuweza kumuuwa Dokta Yusha.

Baada ya Dokta Yusha kutomuona mgonjwa aliyeitiwa, na simu ya mtu aliyempigia kuzimwa. Alikaa chini na kutafakari kilichotokea. Kila kitu kilijirudia katika kichwa chake kama filamu, sasa akaona ukubwa wa kosa alilolifanya. La kukimbia katikati ya sherehe ya harusi yake. Ukubwa wa kosa uliongezeka zaidi kwa kuwa hakukuwa na mgonjwa kweli pale hospitali…

Dokta Yusha sasa alikumbuka hali atakayokuwa nayo mke wake kipenzi Nasra kwa tukio lile baya alilolifanya. Alikumbuka pia huzuni atakayokuwa kawaachia wazazi wake wapendwa kule ukumbini baada ya kuondoka bila kuaga. Alijiona kafanya kosa kubwa sana.
Ghafla, majimaji mepesi yalitiririka katika mashavu yake, Dokta Yusha alikuwa analia. Kwa kosa kubwa alilolifanya usiku ule.

Wakati Dokta Yusha akiwaza yale, na chozi la uchungu kumdondoka pale hospitali. Muuaji namba tano alikuwa hatua chache sana na pale alipokaa Dokta Yusha, akifikiria jinsi ya kumuua. Aliona kumuua kwa risasi itazua tafrani kubwa pale hosptali, alipanga kumuuwa Dokta Yusha kwa mikono yake ama kwa kisu. Alihisi njia hizo ni salama zaidi. Sasa alikuwa anasubiri Dokta Yusha afanye kosa lolote lile.

Kule Kilwa Masoko, hali ile ya taharuki na huzuni iliendelea mle ukumbini.
Baada ya saa moja watu wote waliamua kurudi majumbani kwao. Huku kila mmoja akiliongelea kwa aina yake tukio la kukimbia kwa bwana harusi katikati ya sherehe. Wapo waliolifanya kama hadithi nzuri ya kufurahisha, wapo waliolifanya kama hadithi mbaya ya kusikitisha na kuhuzunisha.
Watu wa mwisho kurudi nyumbani katika usiku ule wa sherehe ya harusi ni familia mbili zilizokumbwa na kisanga kile cha kuajabisha, familia ya Dokta Yusha na familia ya Nasra. Waliweka kikao kidogo mlemle ukumbini kulizungumzia tukio lile. Kikao kilichoisha bila maelewano yoyote. Walijaribu kumpigia Dokta Yusha, simu iliita tu bila kupokelewa. Sasa familia zile mbili wakiwa na Bi harusi walikuwa wanarudi nyumbani, katika gari mbili tofauti, wakiwa na huzuni na simanzi tele. Huku wanawake wachache ndani ya familia zile walikuwa wanalia, wakiongozwa vizuri na Bi harusi, Nasra.

Katika gari aliyopanda Nasra, kulikuwa na watu watano, Kulikuwemo na dereva, baba yake Nasra, mzee Mpaukha, mama yake Nasra, mama Mpaukha, na mpambe wa Bi harusi, rafiki yake kipenzi Nasra, Hasina Omary.
Dereva wa gari ile, alikuwa anaitwa Musa. Dereva wa siku nyingi sana wa familia ya mzee Mpaukha.
Musa alikuwa amelewa sana pombe, pombe ambayo aliinywa vilivyo na marafiki zake mle ukumbini. Pombe ilimfanya apoteze umakini pale katika sukani na kuleta balaa kubwa sana.
Walitoka vizuri pale ukumbini, lakini gari lilivyokamata lami mwendo ulibadirika. Musa akawa anaendesha gari bila umakini wowote, siku zote pombe haziongopi.
Hakukuwa na mtu aliyekuwa makini na mwendo ule, wakati Musa alikuwa amelewa pombe, watu wengine wote waliobaki walikuwa wamelewa na kitendo alichokifanya Dokta Yusha kule ukumbini. Gari zima walilewa kwa aina mbili tofauti. Kila mmoja alikuwa amekaa mkao wa kuchoka katika siti yake.
Gari wakati inakata kona ya kuelekea nyumbani kwa mzee Mpaukha, dereva ilimshinda. Ilikuwa kona kali sana, iliyomshinda kabisa Musa, gari liliacha njia na kujisweka kwenye kapori kadogo….ilikuwa balaa !
Gari ilijipiga kwa nguvu sana katika mti mkubwa kule kwenye kapori. Kishindo kikuu kilisikika.

TANO, baada ya kushindwa mpango wake wa kumuua Dokta Yusha usiku ule. Alirudi mafichoni kwa wenzake kujipanga upya. Usiku wa siku uliofuata kundi lile hatari la SIX KILLERS walikuwa na kazi kuu mbili.
Kwanza Kuhakikisha utoaji wa mioyo kwa maiti zilizokuwepo katika chumba cha kuhifadhia maiti unafanyika bila wasiwasi wowote.

Pia kuhakisha Dokta kijana anayejifanya ana morali ya kazi, Dokta Yusha anauwawa.
Kwa kushirikiana na wale madokta wasiokuwa na maadili ya kazi waliamini watafanikiwa katika malengo yao hayo mawili.

Jioni ya siku ile familia ya Dokta Yusha, ilikwenda hospitali kuwaangaalia wenzao. Yalikuwa majonzi makubwa sana baada ya kusikia mama Mpaukha alikuwa amefariki. Na ndugu wengine wa Mzee Mpaukha nao waliwasiri, na waliamua kuuchukua mwili wa mpendwa wao usiku wa siku ile ili kwenda kufanya maandalizi ya mazishi.

Hadi muda huo, madaktari wakuu katika hospitali hiyo walikuwa hawajulikani walipo. Nia yao ilikuwa ni kukaa mafichoni muda mrefu ili idadi ya watu watakaofariki waongezeke, ili mradi wao wa kupata mioyo kumi na tano kila siku ukamilike. Walijua wasipokuwa kazini wao, wagonjwa wengi watakufa.

Saa nne kamili usiku, mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya ya Kilwa, ndugu Zaidi Kilumba, Daktari Mkuu wa upasuaji Dokta Sharifa Juma, Mkuu wa chumba cha upasuaji, Dokta Tamaa Karimu, wale manesi watano, na kundi zima la SIX KILLER waliwasiri katika eneo la hospitali ile, kwa magari aina mbili tofauti. Madokta na manesi walipanda gari yao na lile kundi hatari walipanda gari yao. Walitofautiana kufika eneo la hospitali kwa dakika kumi tu, wakitangulia wale madaktari. Walikuwa wamekuja kufanya kazi ya kutoa mioyo ya maiti, wakifuatiwa na gari la kundi la hatari la Six Killers waliokuja kulinda hali ya usalama pale hospitali, na kumuua daktari aliyeonekana kizuizi kwa kazi yao, Dokta Yusha.

Wale madaktari waliposhuka tu pale hospitali, walilakiwa kwa furaha na bashasha kubwa sana toka kwa Dokta Yusha. Lakini wao hawakuonesha kabisa sura za furaha, haikuwa kama ilivyo kawaida yao kila walipokuwa wanakutana hapo kabla. Madaktari wale walionesha sura zilizoonesha dharau na kiburi.
Madaktari wote watatu walikataa kushikana mkono na Dokta Yusha wakati wa kusalimiana ! Waliuacha mkono wa Dokta Yusha ukielea hewani.

“Hivi wewe hiki ni kituo chako cha kazi, au unataka kutuaminisha kwamba wanaopanga vituo hawana akili?” Dokta Sharifa alimuuliza swali kwa dharau Dokta Yusha.
Dokta Yusha hakujibu swali lile, alitumbua macho kuonesha mshangao wake. Aliwaangalia kwa zamu madaktari wale. Wote walionesha kutojari kabisa mshangao wake.
“Au unahamu…..?” Dokta Kilumba nae aliuliza swali lililoelea hewani, bila kutanabaisha Dokta Yusha alikuwa na hamu ya nini.
“Mbona siwaelewi ndugu zangu” Dokta Yusha aliongea kwa sauti ndogo iliyokuwa ikiashiria kutoelewa kinachoendelea.
“Naitwa Tamaa Karimu, unaitwa Yusuph Shaweji, sina undugu na wewe na wala sijawahi kuwa na undugu Na wewe, labda hawa wenzangu ndio ndugu zako”
“Nani, mimi nitakuwa na ndugu kama huyo?” Dokta Sharifa alirukia kwa mtindo wa swali.
“Lazima niwe makini, kuna kitu kinaendelea” Dokta Yusha alijionya mwenyewe kimoyomoyo.

Wakati wanaongea na Dokta Yusha, lile kundi la wauaji walikuwa wamejipanga vizuri kule katika chumba cha kuhifadhia maiti. Tayari kwa kulinda usalama ili wale madaktari waje kufanya mchezo wao hatari. Mchezo wa kutoa mioyo ya maiti ! Pale walikuwa wanamchanganya tu Dokta Yusha ili kupoteza umakini wake, na kuwapa nafasi kundi la Six killers wajipange vizuri kule katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Na walifanikiwa !

Lile anguko la Mwanasheria lilimpeleka moja kwa moja kule kwenye kibonde kidogo lilipoingia gari la Mzee Mpaukha, na kujikuta ameulalia mwili wa mpambe wa Bi harusi,
Hasina Omary.
“Mamaaaaaa”
Mwanasheria alipiga kelele kali sana. Akiwa amemlalia Hasina, macho yake mbele yake alikutana na picha mbaya sana. Picha ya kutisha.

“Ni nini hii, inamaana tumekufa wote” Mwanasheria alijiuliza mwenyewe. Pombe haziongopi kabisa, Mwanasheria alijiona kama na yeye alikuwemo katika ile gari iliyopata ajari, na sasa watu wote wamekufa, akiwemo na yeye. Yalikuwa mambo ya ajabu sana.
Alijiinua taratibu toka katika mwili uliojeruhiwa vibaya sana, mwili wa Hasina, akasimama wima, huku akiwa anayumbayumba, Mwanasheria aliangalia vizuri eneo lote lile la ajari. Japo kwa shida kutokana na giza na kwa macho ya ulevi, lakini alitambua vizuri madhara makubwa yaliyotokea mahali pale.

“Ni nini hii?” Alijiuliza mwenyewe Mwanasheria. Mara akili zake za kilevi zilimtuma kufanya kitu. Alitoa simu yake mkononi na kupiga simu, alipiga simu kwa Robert, alikuwa ni rafiki yake kipenz.

“Hallo Robert” Aliongea kwa sauti ya kilevi.
“Nambie Mwanasheria, mbona usiku sana” Robert aliongea kwa sauti iliyoonesha alikuwa anatoka usingizini.
“Tumepata ajari rafiki yangu”
“Ajari ?”
“Ndio wenzangu wote wamekufa nimebaki mimi peke yangu”
“Ulikuwa na kina nani”
“Siwajui”
Pombe zilimfanya Mwanasheria ajione kama naye alikuwemo katika ile ajari.
“Sehemu gani imetokea hiyo ajari?”
“Mtaroni”
“Come on Mwanasheria be serious”
“Kweli my friend”
“Ulikuwa unatoka wapi mwanasheria?”
“Kilabuni”
Robert alitoa msonyo mrefu na kukata simu. Akihisi Mwanasheria alikuwa katika maruweruwe yake baada ya kunywa pombe za kutosha.

Upande wa Mwanasheria, ulibaki na mshangao, kwanini rafiki yake kipenz Robert kamkatia simu wakati yeye anamueleza jambo muhimu na zito sana.
Mwanasheria alianza kupiga kelele, na maneno ajari na balaa yakisikika mara kwa mara katika kelele zake.
Majirani na lile eneo walisikia walisikia vizuri sana kilio kile cha Mwanasheria, lakini nani katika mji ule alikuwa hamjui Mwanasheria, nani angekithamini kilio cha mlevi yule, kila mtu alipuuzia kilio cha mlevi, Mwanasheria. Lakini Mwanasheria hakupuuza, alizidi kupiga kelele…

Kule hospitali Kivinje hali ya mviziano iliendelea. Baada ya Dokta Yusha kukaa pale kwa muda mrefu, bila simu yake kupigwa, bila kumuona aliyempigia simu, aliamua kuondoka. Huku kichwani alikuwa anawaza, atamwambia nini Nasra na kumuelewa, atawaambia nini wazazi wake. Alitoka nje na kumkuta dereva wa ile pikipiki amesinzia, alimuasha na kupanda.
Wakaondoka.
Wakati wanaondoka walipishana na gari moja lililoingia kwa kasi sana mle hospitali, almanusra liwagonge.
Walipofika Singino, simu ya Dokta Yusha iliita, kuangalia namba ni ya ile sauti ya kizee iliyompigia mwanzo…

Sasa, akawa anajishauri, apokee ama asipokee ile simu.
“Hebu simamisha pikipiki kidogo” Dokta Yusha alimwambia dereva wa pikipiki ile kwa sauti kubwa. Pikipiki ikasimamishwa.
Dr Yusha aliipokea simu ile na kuisikia sauti ileile ikimsisitiza aende Kivinje kumsaidia mgonjwa wake.
“Mbona nimetoka hapo hospitali muda huu?” Dokta Yusha aliuliza kwa sauti yenye kukereka.
“Tupo huku nyuma, karibu na jengo la kuhifadhia maiti”
“Sasa mbona nilipofika niliipiga hii simu ilikuwa haipatikani”
“Simu iliisha chaji, yaani hapa nimeilazimisha tu kuiwash…”
Simu ikakatika.
Dokta Yusha aliamini kweli, simu ya yule jamaa haikuwa na chaji, maana ndomana hata sasa ilizimika kutokana na tatizo hilo.
“Turudi hospitali” Alimuamuru yule dereva pikipiki. Yule kijana aligeuza pikipiki haraka, yeye alikuwa kazini, na aliamini ujira wake unaongezeka kila inavyoongezeka safari.

Kule Kivinje, Tano alikuwa hajafanikiwa Mpango wake, hadi Dokta Yusha anapanda pikipiki na kuondoka, hakuiona nafasi sahihi ya kumuua daktari yule kijana. Wakati Dokta Yusha anaondoka Tano alijishauri, amfate Dokta Yusha na kumuua njiani ama afanyaje. Mwishowe aliamua kumrudisha tena Dokta Yusha kwa kutumia ile simu. Na alifanikiwa, Dokta Yusha alikuwa njiani anarudi.
Tano alijificha nyuma ya jengo la kuhifadhia maiti la Hospitali ile, na kisu chake mkononi. Akisubiri kwa hamu ujio wa Dokta Yusha. Daktari wakiyeamini angekuwa kikwazo katika Mpango wao walioupanga usiku wa siku ile.

Muda mfupi baadae, Pikipiki aliyopanda Dokta Yusha iliwasiri pale Hospitali. Dokta Yusha alishuka kwenye ile pikipiki. Siyo kwa haraka sana kama mwanzo. Akawa anaelekea upande wa kushoto kilipo chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ile.

Dokta Yusha alikaribia kabisa kile chumba cha kuhifadhia maiti.
Ghafla, alisikia kelele kali sana zikitoka kule mapokezi.
“Uwiiiiiiii, jamani tusaidieni, tumeamua vibaya saaaaana, tusaidieni, madaktariiiiii, tunakufaaaa….” Zilikuwa kelele kali sana. Kelele ambazo zilisababisha Dokta Yusha abadiri uelekeo. Toka kwenye kifo kurudi katika uhai. Dokta Yusha alitimka mbio kurudi kule mapokezi, alikosikia makelele ya mtu akiomba msaada. Alipofika pale alimtambua vizuri sana mpiga kelele, alikuwa Mwanasheria, mlevi maarufu sana Kilwa Masoko. Taratibu alianza kupunguza mwendo akijua Mwanasheria yupo katika makelele yake ya kawaida ya pombe. Lakini kadri ya alivyokuwa anamsogelea Mwanasheria, umakini wake uliongezeka.
Mwanasheria alitapakaa damu mwili mzima, huku kundi dogo la watu likiwa limemzunguka. Dokta Yusha alijitahidi kupenya kundi la watu wale na kumfikia mlevi yule.

“Vipi Mwanasheria?” Baada ya kumkaribia Dokta Yusha lilimtoka swali.
Mwanasheria alimwangalia Dokta Yusha na kumtambua.
“Tumepata ajari Dokta, sote tumekufa” Mwanasheria alitoa kauli iliyomchekesha kila mtu.
“Come down Mwanasheria, wewe hujafa”
“Nimekufa Dokta, nimekufaaaaaa” Alisema kwa sauti kubwa sana.
Dokta Yusha aliona pale hawawezi kuelewana.
“Hao wenzako wako wapi?”
“Wapo humo Dokta” Mwanasheria alisema huku akionesha kwa kidole chumba kulichokuwa karibu na pale walipokaa.
Kwa mwendo wa taratibu Dokta Yusha alielekea kule chumbani. Alikutaba na balaa.
Mwili wa kwanza kuuona ni wa rafiki yake kipenzi, mke wake kipenzi, Nasra. Alienda mbele ya mwili ule uliolazwa vibaya sakafuni na kuuinamia. Dokta Yusha aliona ufa mkubwa sana katika kichwa cha mpenzi wake , pale alipojigonga na jiwe baada ya ile ajari ya kizembe kutokea. Aligusa upande wa kushoto wa kifua cha Nasra, mapigo ya moyo yalikuwa yanapiga kwa mbali sana. Akajua kosa lolote litasababisha ampoteze mke wake.
Alinyanyuka taratibu, huku chozi likimdondoka na kuufata mwili wa pili, alikuwa ni mkwewe, mama Mpaukha. Hakuhitaji kumgusa sehemu yeyote kutambua kama mkwewe kipenz alikuwa amefariki. Aliusogelea mwili wa tatu, mwili wa Alex. Dereva wa Mzee Mpaukha. Alimuona na damu nyingi sana, huku mabaki ya vioo yakiwa yamebaki katika mwili ule. Ilikuwa ni picha mbaya sana kuiangalia. Akausogelea mwili wa nne, wa Hasina, mpambe wa bibi harusi. Aliona mbonyeo mkubwa katika upande wa kulia wa kichwa kile. Pale alipojigonga na kioo Wakati Musa alipojaribu kukata kona ile kali. Mwisho aliusogelea mwili wa Mzee Mpaukha, mwili ambao haukuwa na tofauti sana na mwili wa dereva Musa. Nao mahali ya vioo yalikuwepo katika mwili ule.
“Balaa” Dokta Yusha alijisemea mwenyewe.

“Jamani tunakufaaa” sasa ndio alizisikia kelele za Mwanasheria kule mapokezi.
Dokta Yusha alitoka nje kumwangalia Mwanasheria alikuwa ameumia sehemu gani. Alimfikia Mwanasheria na kumkagua mwili mzima. Mwanasheria hakuwa na jeraha lolote zaidi ya zile damu zilizompakaa. Dokta Yusha akawaza labda Mwanasheria kaumia ndani kwa ndani. Wakati akimwangalia Mwanasheria ndipo alipomuona Fred kwa mbali, rafiki yake wa siku nyingi. Na ndiye alikuwa mpambe wake wa harusi siku ile.

“Vipi Fred”
“Ebana wameumia vibaya sana, afadhali nimekuona, nimewafata madaktari mpaka nyumbani kwao, hawapo, sijui wameenda wapi?”
“Kwani kilitokea nini Fred?” Dokta Yusha aliuliza kwa sauti yake yenye kwikwi.
“Mimi kanipigia simu huyo jamaa anayelia, muda mfupi tu nilipofika nyumbani kutoka kwenye sherehe, sijui hata namba yangu aliitoa wapi, yeye alikuwa analia tu, huku akisema wote wamekufa. Alinielekeza mahali ilipotokea ajari. Nilienda haraka kwa gari, na kukuta familia ya Nasra wamepata ajari mbaya sana ya gari aisee, majeruhi wako ndani huko” Fred alisema bila kujua kama Dokta Yusha kashaingia mle ndani na kujionea mwenyewe athari za ajari ile.

Kule nyuma ya chumba cha kuhifadhia maiti, Tano alikuwa anasubiri ujio wa Dokta Yusha. Alikuwa amejiandaa vema kumuua Dokta Yusha pindi atakapotokea tu. Alijibanza konani na kisu chake mkononi. Hakujua kabisa kuwa kwa wakati ule Dokta Yusha alikuwa amesahau kabisa habari ya simu ya mtu yule.
Tano alisubiri na kusubiri.
Alfajiri, mji wa Kilwa Masoko, waliamka na habari kuu mbili.
Habari ya kwanza ilikuwa ni kutokea kwa ajari katika kona inayoelekea mtaa wa Lumumba. Vijiwe vyote vinavyojadiri habari ngumu waliijadiri sana habari hiyo. Habari iliyohusisha ajari mbaya waliyoipata familia ya Mzee Mpaukha.

Habari ya pili ni kukimbia kwa bwana harusi katikati ya sherehe. Habari iliyopambwa na kusimuliwa vizuri sana na mafundi wa kusimulia. Tena wengine hawakuwepo hata katika ile sherehe yenyewe lakini ndio walikuwa wasimuliaji wakubwa. Vijiwe vyote vya waambea waliipa sana ‘airtime ‘ habari hii ya bwana harusi kukimbia katikati ya sherehe kuliko habari ile ya ajari.

Kule Kilwa Kivinje majeruhi wote sasa walikuwa wodini. Dokta Yusha alifanya kazi kubwa sana usiku ule. Yeye mwenyewe alifanya kila kitu kuhakikisha majeruhi wote wanapata huduma. Na ile maiti ya mama Nasra ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na kusubiri taratibu zingine za mazishi ziendelee.

Hadi Asubuhi, Dokta Mkuu wa hospitali ya Kinyonga, Zaidi Kilumba, Dokta Mkuu wa upasuaji Sharifa Juma, na Dokta anayesimamia chumba cha kuhifadhia maiti, Dokta tamaa Karimu walikuwa hawajawasiri kazini, na wala simu zao zilikuwa hazipatikani.
Hospitalini walikuwa wanafanya kazi manesi, wakishirikiana kwa ukaribu mkubwa na Dokta Yusha.

Hadi saa sita mchana, majeruhi wale wanne walikuwa hawajapata fahamu. Hali ilikuwa tete. Dokta Yusha alifanya kazi kama punda, huku akimshukuru Mungu kwa kuwa alikuwa na likizo kwa ajili ya mapumziko ya ndoa yake.
Madaktari wengine katika hospitali ile, hawakuwa na ari kabisa ya kufanya kazi.

Saa kumi na mbili jioni, kazi ya Dokta Yusha ilianza kuleta mafanikio. Mzee Mpaukha alirudiwa na fahamu. Alifumbua macho taratibu akiwa mbele ya nesi aliyekuwa karibu na kitanda chake.

“Niko wapi hapa?”
“Tulia baba, uko sehemu salama”

Nesi alimjibu huku akiweka vizuri dripu ya maji ilikuwa inaingia mwilini kwa Mzee Mpaukha.
Mzee Mpaukha, alifumba macho na kutafakari. Matukio yote yaliyotokea usiku uliopita yalijirudia mithili ya sinema. Tangu wakiwa ukumbini hadi gari lao lilivyoacha njia.

“Tunakufaaaaaaa!”

Mzee Mpaukha alitoa ukelele mkubwa akiwa pale kitandani. Ukelele huo uliokuwa na faida ndani yake. Ukelele ule alifika moja kwa moja katika masikio ya Musa, na kumuamsha Musa, dereva wake, toka katika usingizi mzito aliolala kuja duniani. Musa naye aliunga kumsaidia Mzee Mpaukha

“…..kufaaaaaaa”
Nesi sasa akakimbia kwa kasi kwenda katika kitanda cha Musa. Huku akimshukuru Mungu kwa kuweza kuwaamsha wagonjwa wawili kwa mpigo, tena katika njia ya ajabu.

Nusu saa baadae, Dokta Yusha aliwasiri, alipatwa na furaha isiyo na kifani kukuta wagonjwa wake wawili wamerejewa na fahamu. Ilikuwa faraja kubwa sana kwake. Asilimia hamsini ya kazi alikuwa amefanikiwa. Walipoteza fahamu wagonjwa wanne, wawili walikuwa wamerejewa na fahamu zao na kubaki wawili…

TANO, baada ya kushindwa mpango wake wa kumuua Dokta Yusha usiku ule. Alirudi mafichoni kwa wenzake kujipanga upya. Usiku wa siku uliofuata kundi lile hatari la SIX KILLERS walikuwa na kazi kuu mbili.

Kwanza Kuhakikisha utoaji wa mioyo kwa maiti zilizokuwepo katika chumba cha kuhifadhia maiti unafanyika bila wasiwasi wowote.

Pia kuhakisha Dokta kijana anayejifanya ana morali ya kazi, Dokta Yusha anauwawa.
Kwa kushirikiana na wale madokta wasiokuwa na maadili ya kazi waliamini watafanikiwa katika malengo yao hayo mawili.

Jioni ya siku ile familia ya Dokta Yusha, ilikwenda hospitali kuwaangaalia wenzao. Yalikuwa majonzi makubwa sana baada ya kusikia mama Mpaukha alikuwa amefariki. Na ndugu wengine wa Mzee Mpaukha nao waliwasiri, na waliamua kuuchukua mwili wa mpendwa wao usiku wa siku ile ili kwenda kufanya maandalizi ya mazishi.

Hadi muda huo, madaktari wakuu katika hospitali hiyo walikuwa hawajulikani walipo. Nia yao ilikuwa ni kukaa mafichoni muda mrefu ili idadi ya watu watakaofariki waongezeke, ili mradi wao wa kupata mioyo kumi na tano kila siku ukamilike. Walijua wasipokuwa kazini wao, wagonjwa wengi watakufa.

Saa nne kamili usiku, mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya ya Kilwa, ndugu Zaidi Kilumba, Daktari Mkuu wa upasuaji Dokta Sharifa Juma, Mkuu wa chumba cha upasuaji, Dokta Tamaa Karimu, wale manesi watano, na kundi zima la SIX KILLER waliwasiri katika eneo la hospitali ile, kwa magari aina mbili tofauti. Madokta na manesi walipanda gari yao na lile kundi hatari walipanda gari yao. Walitofautiana kufika eneo la hospitali kwa dakika kumi tu, wakitangulia wale madaktari. Walikuwa wamekuja kufanya kazi ya kutoa mioyo ya maiti, wakifuatiwa na gari la kundi la hatari la Six Killers waliokuja kulinda hali ya usalama pale hospitali, na kumuua daktari aliyeonekana kizuizi kwa kazi yao, Dokta Yusha.
Wale madaktari waliposhuka tu pale hospitali, walilakiwa kwa furaha na bashasha kubwa sana toka kwa Dokta Yusha. Lakini wao hawakuonesha kabisa sura za furaha, haikuwa kama ilivyo kawaida yao kila walipokuwa wanakutana hapo kabla. Madaktari wale walionesha sura zilizoonesha dharau na kiburi.
Madaktari wote watatu walikataa kushikana mkono na Dokta Yusha wakati wa kusalimiana ! Waliuacha mkono wa Dokta Yusha ukielea hewani.

“Hivi wewe hiki ni kituo chako cha kazi, au unataka kutuaminisha kwamba wanaopanga vituo hawana akili?” Dokta Sharifa alimuuliza swali kwa dharau Dokta Yusha.
Dokta Yusha hakujibu swali lile, alitumbua macho kuonesha mshangao wake. Aliwaangalia kwa zamu madaktari wale. Wote walionesha kutojari kabisa mshangao wake.
“Au unahamu…..?” Dokta Kilumba nae aliuliza swali lililoelea hewani, bila kutanabaisha Dokta Yusha alikuwa na hamu ya nini.
“Mbona siwaelewi ndugu zangu” Dokta Yusha aliongea kwa sauti ndogo iliyokuwa ikiashiria kutoelewa kinachoendelea.
“Naitwa Tamaa Karimu, unaitwa Yusuph Shaweji, sina undugu na wewe na wala sijawahi kuwa na undugu Na wewe, labda hawa wenzangu ndio ndugu zako”
“Nani, mimi nitakuwa na ndugu kama huyo?” Dokta Sharifa alirukia kwa mtindo wa swali.
“Lazima niwe makini, kuna kitu kinaendelea” Dokta Yusha alijionya mwenyewe kimoyomoyo.

Wakati wanaongea na Dokta Yusha, lile kundi la wauaji walikuwa wamejipanga vizuri kule katika chumba cha kuhifadhia maiti. Tayari kwa kulinda usalama ili wale madaktari waje kufanya mchezo wao hatari. Mchezo wa kutoa mioyo ya maiti ! Pale walikuwa wanamchanganya tu Dokta Yusha ili kupoteza umakini wake, na kuwapa nafasi kundi la Six killers wajipange vizuri kule katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Na walifanikiwa !

Usiku uleule wa saa nne, familia ya Mzee Mpaukha walijipanga kwenda kuchukua mwili wa mpendwa wao kule chumba cha kuhifadhia maiti. Walikuwa wanamsubiri Dokta Yusha tu ili waende kuchukua mwili wa marehemu. Walikuwa wameshaongea na Mkuu msaidizi wa mhifadhi wa chumba cha maiti. Bila kujua Mpango hasi uliokuwemo katika chumba kile…..Balaa !

Alivyotoka kuongea na madaktari wale waliombadirikia, Dokta Yusha moja kwa moja alienda wodini. Hali aliyoiacha wodini ndiyo aliyoikuta. Hadi muda ule. Ni Mussa na Mzee Mpaukha tu ndio waliorejewa na fahamu. Dokta Yusha alisogea hadi kitanda alicholazwa mke wake kipenz, Nasra, alikaa pembeni ya kitanda kile. Huku akimwangalia mkewe aliyekuwa amefumba macho. Akiwa amehama kabisa katika Dunia hii. Mwanamke aliyekuwa nusu mfu kwa sasa. Aliangalia jinsi dripu ikivyotiririka taratibu katika mishipa laini ya Nasra.

Wakati Dokta Yusha akiwa pale na mkewe, Dokta Kilumba aliingia mle wodini. Alisogea taratibu hadi pale kitandani alipokuwa amekaa Dokta Yusha. Taratibu Dokta Yusha aliacha kuiangalia ile dripu na kumwangalia Dokta Kilumba. Dokta waliyetoka kugombana naye punde tu kule nje.
Dokta Kilumba alipofika pale naye hakuongea. Alikaa pale kitandani, karibu kabisa na Dokta Yusha, kiasi kwamba magoti yao yaligusana. Hali ya ukimya iliendelea kama dakika tatu, ndipo Dokta Yusha alikiharibu kimya hiko.

“Vipi Dokta, mbona umekuja kimya kimya halafu hauongei ?”
“Tusamehe Dokta, haikuwa dhamira yetu hali ile itokee”
“Msijari mambo ya kawaida tu kupishana kauli”

Baadae walielewana. Na kuanza kuongea mambo mbalimbali.
Dokta Kilumba alikuja kuongea na Dokta Yusha kwa dhamira maalum. Dhamira mbaya kabisa. Ni kuchelewasha muda kwa Dokta Yusha kwenda kule chumba cha kuhifadhia maiti kuchukua maiti ya mama Mpaukha. Kwa kuwa na maiti ya mama Mpaukha ilikuwa katika orodha ya maiti zilozotakiwa kutolewa moyo siku ile !

Kule nje familia ya Mzee Mpaukha walikuwa wanamsubiri Dr Yusha atoke wodini kuangalia hali za wagonjwa, ili waende naye kwenda kuchukua maiti yao kule katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Bila kujua lengo la Dokta Kilumba, Dokta Yusha aliendelea kuongea nae. Alifurahi sana kuelewana na daktari yule Mkuu, alijua itakuwa rahisi sana kuwasimamia wagonjwa wake kwa kuelewana na Dokta yule.

Kule katika chumba cha maiti hali ilikuwa ya kutisha. Ilihitaji mtu jasiri kuangalia kilichokuwa kinaendelea. Mioyo kumi na nne toka katika maiti kumi na nne ilikuwa imeshapatikana tayari, na kuhifadhiwa katika deli moja kubwa jekundu!
Sasa ilikuwa zamu ya kutolewa moyo wa kumi na tano, ili kukamilisha idadi yao ya siku ile. Kisha baada ya hapo wakachungulie katika akaunti zao kitaongezeka nini. Waliikumbuka sana ahadi ya Don Genge.

Hali ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti ilikuwa ya utulivu sana. Kila mtu akifanya kazi yake kwa umakini mkubwa. Utafikiri walikuwa katika operesheni moja muhimu sana ya kuokoa maisha ya mtu. Kumbe walikuwa wanafanya vitendo vya kinyama sana!

Dokta Sharifa alikuwa ameshika kisu maalum kwa ajili ya upasuaji, mbele yake kulikuwa na kitanda kidogo kikichotumika kulaza zile maiti wakizozitoa mioyo!

Dokta Sharifa alikuwa anapasua maiti na kutoa moyo kisha kuishona tena miili ya marehemu. Wale manesi walikuwa wanafanya kazi ya kubeba maiti na kuzileta pale kitandani, kisha kuzirejesha katika sehemu zao baada ya kufanyiwa upasuaji na kushonwa na Dokta Sharifa. Dokta wa kike katili !
Dokta Tamaa yeye alikuwa anasimamia kazi kama inaenda vizuri, ndiye alikuwa Mkuu kwa muda ule, wakati Dokta Kilumba hakuwepo.

Nje kulikuwa na ulinzi imara. Walinzi wote sita wakiwa na bunduki, walikuwa wamekizunguka chumba cha kuhifadhia maiti , tayari kwa kupiga mtu au kitu chochote kitakachosogelea chumba kile. Walikuwa makini, Kuhakikisha hawafanyi kosa lolote la kiufundi.

Manesi wawili walienda kufungua kabati moja la kuhifadhia maiti. Walivuta droo taratibu. Sura ya maiti yule ilikuwa inaonekana vizuri. Sura tulivu kabisa, sura ya kipole, sura isiyokuwa na hatia yoyote, sura ya mama Mpaukha. Wale manesi wawili waliitoa maiti ile na kuilaza vizuri kwenye machela. Waliisukuma machela ile kuelekea pale alipokuwa Dokta Sharifa, ili Dokta afanye kazi ile ya kikatili !
Kazi ya kuutoa moyo mwili ule, mwili wa mkwe wa Dokta Yusha.

Mwili wa mama Mpaukha ukawekwa katika kile kitanda maalum kwa kazi hii ya kikatili!
Dokta Sharifa alinyanyua mkono wake wa kulia ulioshika kisu juu, akakielekeza kile kisu katika upande wa kushoto katika kifua laini cha marehemu mama Mpaukha, akichana taratibu.

Kilikuwa ni kitendo cha kikatili sana, lakini daktari yule wa kike alikuwa anakifanya bila wasiwasi wowote. Alikizungusha kile kile kisu kwa mtindo wa duara, kisu maalum kilichokuwa kimezama vizuri katika nyama za kifua cha mama yule. Alipoona imetosha aliingiza mkono wake wa kulia, aliokuwa amevaa gloves, alichezesha mkono wake kama dakika moja katika shimo baya alilolijenga pale kifuani, na kutoka na moyo uliozungukwa na damu!
Aliuweka pembeni kwenye sahani ya chuma moyo ule, na kuanza kuushona mwili ule, mwili usiokuwa na moyo kwa sasa.

Kule wodini ‘story’ zilinoga kati ya Dokta Yusha na Dokta Kilumba. Walikuwa wanasimuliana mambo mbalimbali kuhusu fani yao ya utabibu. Bila kujua mambo ya siri yaliyokuwa wanaendelea katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Mara, mjomba wake Nasra aliingia wodini.
“Samahani Dokta, inabidi tukautoe mwili wa marehemu ili tukaufanyie maandalizi”
“Sawa, ngoja tumpigie mtu wa chumba cha kuhifadhia maiti” Dokta Kilumba alidakia ilihal hakuambiwa yeye.
Alimpigia Dokta Tamaa, na Dokta Tamaa alimjibu kwamba mambo yako vizuri wakauchukue tu mwili mpendwa wao.

Dokta Yusha akiongozana na ndugu mwengine walienda kuuchukua mwili ule usiokuwa na moyo kwa sasa na kwenda nao Kilwa Masoko kwa ajili ya maandilizi ili wauzike.

Siku ile ya kwanza kundi la Don Genge kwa kishirikiana na madaktari wale wenye roho mbaya kabisa walifanikisha Mpango wao ule wa kinyama!

Siku ya pili Asubuhi, ndio ilikuwa siku ya kuuosha mwili ule tayari kwa kwenda kuuzika. Mshono waliukuta katika kifua cha mama Mpaukha ulimshangaza kila mtu aliyekuwa mle chumbani wakati wanauosha mwili ule…

Wakati mwili unaoshwa, kizaaza kikaibuka!
Mwili wa mama Mpaukha ulikuwa na mshono mkubwa sana ambao ulikuwa haujapona bado.
Mshono uliowaacha midomo wazi waoshaji. Pamoja na mshangao wao lakini waoshaji wale walihisi labda jeraha lile ni mojawapo ya madhara aliyoyapata mama yule katika ajari ile mbaya!
Wakina mama wale Waliamua kukaa kimya na kuendelea na kazi yao ya uoshaji kama kawaida.
Mwili wa mama Mpaukha ulioshwa na kwenda kuzikwa katika makaburi ya Sanga bila uwepo wa mwanae mpendwa, Nasra, bila uwepo wa mumewe kipenzi, Mzee Mpaukha .

Mama Kindumba, alikuwa mlevi maarufu wa kike katika mji wa Kilwa Masoko. Kutokana na kupenda sana kunywa pombe za kienyeji alikuwa na marafiki wengi sana walevi, miongoni mwa marafiki ni Mwanasheria.

Mama kindumba alikuwa anakaa jirani sana na familia ya Mzee Mpaukha. Ujirani huo ndio uliosababisha na yeye apate fursa ya kwenda kuuosha mwili wa mama Mpaukha. Na Mama kindumba ni miongoni mwa watu waliostushwa sana na ule mshono wa mama Mpaukha ulikuwepo pale kifuani.

Baada ya kumzika mama Mpaukha, jioni ya siku ile mama kindumba ilimkuta kilabuni akipata pombe za kienyeji kama kawaida yake. Kikao kilikuwa kimependeza ingawa mwenyekiti wa kikao hiko alikuwa hajawasiri bado.
Baada ya muda mfupi Mwenyekiti aliwasiri huku akiimba wimbo wa bendi ya msondo ngoma. Alikuwa Mwanasheria.

“Eeeeeeh nilikuwa nakusubiri kwa hamu Mwana” mama kindumba aliongea kwa nguvu baada ya kumuona Mwanasheria.
“Kuna nini tena mama kindumba maana nawe huishiwi michapo”
“Ni kuhusu ile ajari yenu” mama kindumba alisema huku anacheka.
“Umeanza kuharibu sasa” sauti ya Mwanasheria ilipoa kidogo.
“Kumbe yule maza alipata bonge la jeraha kifuani. Alichomwa na chuma nini pale”
“Mama gani tena?” Mwanasheria alihoji.
“Si jirani yangu tuliomzika leo kule Sanga”
“Acha zako mama, ushalewa nini, yule mama hakuumia sehemu yoyote. Alikufa bila jeraha”
“We si ulilewa Mwanasheria utakuwa na kumbukumbu kweli, maza alikuwa na jeraha kubwa sana kifuani”
“Hamna kitu kama hicho mama”
Ulizuka mbishano mkubwa sana kati ya mama Kindumba na Mwanasheria. Walevi wengine walibaki kuwa wasikilizaji tu.

“Tusiandikie mate, ngoja nimpigie Dokta Yusha tumuulize, halafu naweka sauti ya nje kabisa” Baada ya mzozo mkubwa Mwanasheria alishauri.

“Simu itakayozua kizaazaa kipya” tusubiri hiyo kesho tuone!”

Mwanasheria akatoa simu yake. Akabofyabofya muda mfupi kuitafuta namba ya Dokta Yusha, aliiona na kuipiga.

Wakati simu ile inapigwa, Dokta Yusha alikuwa wodini. Akiwahudumia wagonjwa mbalimbali, wakiwemo mkewe Nasra na na rafiki wa Nasra, Hasina. Mzee Mpaukha na Musa hali zao sasa zilikuwa vizuri sana.

Akiwa amekaa pembeni ya kitanda cha mkewe simu yake iliita. Kuangalia kioo cha simu yake kilisomeka Mwanasheria, alitabasamu. Alitoka nje na tabasamu lake, alikumbuka vizuri sana vituko vya Mwanasheria. Alitoka nje ya geti ili akaongee na Mwanasheria.

“Hallo”
“Dokta tuna ubishi hapa” Mwanasheria alianza kuongea bila hata salamu.
“Ubishi gani tena?”
“Eti katika ile ajari marehemu alikuwa na jeraha lolote?”
“Hapana, alifariki kwa mstuko tu”
“Aliumia kifuani doktaaaa” sauti ya mama kindumba ilisikika katika ile simu kwa sauti kubwa.
“Hapana, hakuumia!”
“Tafuta mtu yeyote aliyekuwepo wakati wa kuosha maiti atakwambia” Mama kindumba alisema.
Na simu ili katika. Bila shaka kwa kuisha salio ama chaji.
Dokta Yusha alichanganyikiwa sana.

Ingawa taarifa ile ilitoka kwa walevi lakini Dokta Yusha aliipa uzito unaostahili. Alipanga kuufatilia ukweli wa taarifa ile na kuujua ukweli wa taarifa hiyo ya kushangaza.

Tano wa kundi la Six killers bado alikuwa anafatilia nyendo za Dokta Yusha. Na nia yao ya kutaka kumuuwa Dokta Yusha bado ilikuwa palepale. Tano alikuwa anapata ugumu sana kwa kuwa Dokta Yusha alikuwa anakaa wodini muda wote. Wodi yenye wagonjwa muda wote, na kufanya kazi ya kumuua iwe ngumu sana.

Wakati Dokta Yusha akiongea na simu ile, Tano alikuwa hatua chache nyuma yake. Alisikia kila kitu alichoongea Dokta Yusha na Mwanasheria….alilishika kichwani jina la Mwanasheria.

“Mwanasheria anahitaji kuuwawa!” Alilipitisha katika kichwa chake.

Kule kilabuni ubishi bado uliendelea. Huku Mwanasheria akiwa amepata nguvu na kuelekea kushinda. Ubishi sasa ulipata washiriki zaidi, walevi walianza kuchangia mada, huku walevi wengi wakimuunga mkono Mwanasheria.

Tano aliona mambo yao sasa yameanza kuingiwa na vijidudu vibaya. Na jukumu lake lilikuwa ni kuviondosha vijidudu vyote. Sasa naye Mwanasheria akaingia katika orodha ya kifo!

Baada ya kuongea na simu ile toka kwa Mwanasheria, Dokta Yusha alikuwa na mawazo mengi sana. Kwa uyakinifu mkubwa aliipima ile taarifa ya Mwanasheria. Akajua kuna kitu. Alikaa pale kitandani huku akiingalia bandeji kubwa aliyefungwa mkewe kichwani. Kichwa cha Nasra kiliathirika sana. Huku kukiwa na wasiwasi kama Nasra akiamka atarejewa na kumbukumbu zake.

Dokta Yusha alichukua simu yake na kuitafuta namba ya Shangazi yake Nasra. Alijua kwa vyovyote lazima alikuwepo wakati maiti ya mama Mpaukha inaoshwa. Aliiona namba na kuipiga huku akiwa anatoka nje ya wodi.
“Hallo Shangazi”
“Habari Dokta?”
“Safi kwema Shangazi”
“Tupo tu hivyohivyo”
“Kuna kitu nataka nikuulize Dokta”
“Kitu gani hiko Dokta”
“Ulikuwepo kati ya watu waliomuosha marehemu leo?”
“Ndio nilikuwepo”
“Eti marehemu alikuwa na jeraha lolote?”
“Tena kubwa sana kifuani, aisee bila shaka ndio litakuwa limesababisha kifo chake lile”
“Sehemu gani lilikuwepo”
“Juu ya kifua, sehemu unapokaa moyo!”

Mwili wa Dokta Yusha ulipigwa ganzi. Ni yeye ndiye aliyepima mapigo ya moyo ya mama Mpaukha, mara tu walipoingia katika chumba cha matibabu kabla ya mwili ule kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Alikumbuka aliweka kifaa cha kupima mapigo ya moyo sehemu ileile unapokaa moyo. Hapakuwa hata na mchubuko. Iweje leo aambiwe kuna jeraha kubwa sana?

“Halo Dokta….Halloo…unanisikia?”
Shangazi wa Nasra alikuwa anaongea peke yake simuni. Ingawa Dokta Yusha aliweka simu sikioni lakini alikuwa mbali sana kimawazo, alikuwa hasikii chochote.

Usiku uleule Tano alienda Kilwa Masoko. Kummaliza Mwanasheria. Alijua kumuacha hai Mwanasheria basi habari juu ya kidonda kilichoibuka ghafla katika kifua cha mama Mpaukha itaendelea kusambaa. Ilikuwa ni lazima kumuuwa Mwanasheria ili kumziba mdomo milele !

Usiku wa saa nne usiku ulimkuta Mwanasheria akinywa bia katika baa ya Tiga Tisa. Alikunywa bia nyingi sana. Tangu saa kumi na mbili jioni alikuwa hapo akipata ulabu.

Meza ya tatu toka pale alipokaa Mwanasheria kulikuwa na mgeni. Mgeni aliyewasiri pale majira ya saa tatu usiku. Mgeni huyo alikuwa makini kwa kila alichokuwa anakifanya Mwanasheria. Mgeni huyo hakuwa mwengine ila ni Tano wa Six Killers. Alikuwa anamsubiri mwanasheria anyanyuke ili akamfanye alichotaka kwenda kumfanya.

Saa tano usiku Mwanasheria alinyanyuka pale kwenye kiti. Tayari kuelekea nyumbani kwake. Alisogea taratibu kwenye gari yake, alipanda na kuliwasha. Safari kwenda nyumbani kwake ilianza. Tano naye alitoka pale Tiga Tisa. Alichukua pikipiki yake na kulifuata gari la Mwanasheria kwa nyuma.
Mwanasheria alikuwa amelewa hasa. Alipoteza kabisa umakini na hakutambua kabisa kama alikuwa anafuatwa. Alifika nyumbani kwake na kuingia ndani. Kutokana na ulevi Mwanasheria alijikuta amelala katika sofa pale sebuleni.

Tano alipaki pikipiki yake kwa nje. Alifika hadi mlangoni katika nyumba ile ya Mwanasheria. Kwa bahati mbaya nyumba ile haikuwa na fensi.
Kwa kutumia funguo malaya alifungua mlango wa sebule wa Mwanasheria. Ilikuwa ni kazi ndogo sana, kazi iliyodumu kwa dakika tatu. Alifungua mlango na kumkuta Mwanasheria amelala pale sebuleni kama mzoga. Alichomoa kisu chake mkononi. Kwa mwendo wa kunyata akawa anamsogelea pale sofani.
Akamtikisa kidogo, Mwanasheria hakuamka, alikuwa amelewa sana pombe. Alimtikisa tena. Nia ya Tano ni kumuamsha Mwanasheria ili kumjua mtu wa pili aliyedakia ile simu wakati yeye anaongea na Dokta Yusha. Lakini Mwanasheria hakuamka.
Tano aliamua kuua tu, akijipa moyo atamjua tu huyo mtu. Alirudisha nyuma ule mkono uliishika kisu, kwa nguvu aliungiza katika tumbo la Mwanasheria, akatoa akaingiza tena. Alirudia mara nne.Mwanasheria akakata roho akiwa amelewa.

Tano alitoka nje huku akiwa na furaha tele. Bila kujua kama alimuua mtu asiye sahihi. Yeye alimuua Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, Ndugu Juma Ngozi. Wakati Mwanasheria aliyeongea na Dokta Yusha, Mwanasheria mlevi alikuwa kilabuni wakati ule, akinywa pombe na kupigizana kelele na kina mama Kindumba…

ITAENDELEA

Balaa Sehemu ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment