Risasi Nne Sehemu ya Kwanza
KIJASUSI

Ep 01: Risasi Nne

SIMULIZI Risasi Nne
Risasi Nne Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA: RICHARD MWAMBE

*********************************************************************************

Simulizi: Risasi Nne

Sehemu ya Kwanza (1)

MWAKA 1978 -79 Tanzania iliingia katika vita na taifa jirani la Uganda, hii ilitokana na ujeuri wa Rais aliyekuwa akiiongoza nchi hiyo kwa mabavu, Idd Amin kudai kuwa sehemu fulani ya Kagera ni Ardhi ya Uganda.

Unyayasaji, mauaji na matukio mengi kinyume na haki za binadamu yaliyokuwa yakiendelea katika nchi ya Uganda kipindi hicho yaliichukiza dunia ikiwemo Tanzania. Mwl Nyerere, aliyekuwa ndiyo Rais wa Tanzania aliamua kuingia vitani kumpiga nduli huyo, ilikuwa ni vita ya ukombozi isiyosahaulika kati ya nchi hizi vizazi na vizazi.

Kama unavyojua, vita haikosi makandokando. RISASI 4 ni riwaya fupi ya kubuni inayomuelezea kijana Joseph Rutashobya aliyeathirika na mazingira hayo baada ya kupoteza wazazi wake wote wawili akishuhudia kwa macho jinsi walivyokuwa wkiuawa na vibaraka wa nduli huyo. Ni nini kilichomo katikakisahiki? fuatana na mtunzi wako asiye na mpinzani Tanzania ujue nini kilijiri…… Riwaya yetu ya kihistoria inaanzia Mtukula….

KAMBI YA JESHI MTUKULA

August 1998

“Mguu pande! Mwiliiiiiiii legeza!” ilikuwa ni sautinya amri kutoka kwa kiongozi wa gwaride maalumu la vijana wa JW lililokuwa likifanyika katika kambi ya Mtukula, karibu kabisa na mpaka wa Tanzania na Uganda. Askari wote waliweka mguu pande na kulegeza miili yao huku wakitazama mbele.

Jua kali lilikuwa likiwaka katika uwanja huo, vumbi lilikuwa likitimuliwa na kaupepo hafifu.

Wakiwa katika mistari minne yenye askari kumi na mbili kila mmoja, James Rutashobya alikuwa na mawazo lukuki, kijasho chepesi kikitiririka kutoka katika katika kofia lake la chuma na kuishia kidevuni…..

Upepo tulivu ulikuwa ukiendelea kuvuma, kila mtu alikuwa ametulia katika uwanja ule. Ndugu jamaa na marafiki walikuwa wakitazama vijana wao wakakamavu wakiwa uwanjani.

Joseph Rutashobya ‘Joru’ kama walivyokuwa akiitwa na kuruta wenzake wa kombania moja lakini service man wake alipenda kumwita ‘Nyoka wa kijani’, alikuwa kijana mpole asiye na maneno mengi lakini aliyejawa na vitendo zaidi, alijiamini, aliamini uamuzi wowote uinaokuja kichwani mwake, tangu aanze mafunzo ya kijeshi katika kambi hiyo miezi sita iliyopita wanaomjua wanadai alikuwa haongei maneno zaidi ya hamsini kwa siku. Hakuna aliyekuwa akijua kwa nini kijana huyu yuko hivyo, daima alipenda kukaa peke yake kila apatapo nafasi akyaruhusu mawazo yake kupita hapa na pale, kujenga hili na lile. Daima alirudishwa mbali kifikra na hali hii.

Akiwa mguu pande, aliinama kichwa chake na kuangalia bunduki lake aliloliinamisha kwa mbele, likimtazama kwa huruma, likitanguliwa na singe linalong’aa kwa jua la saa nne asubuhi huku kitako cha mti usiooza kikiwa kwenye vumbi la ardhi hiyo kavu. Aliitazama kwa uchungu na kukumbuka aina hiyo ya bunduki ilipomuacha katika hali duni akiwa mtoto wa miaka kumi tu, likambakisha yatima, bila msaada wowote na kumsukuma katika maisha magumu ambayo hakuyategemea wala hakuwahi kuyafikiri, maisha ya shida na taabu, maisha ya kutokuwa na baba wala mama. Aliendelea kutazama singe lile ambalo nyuma yake kulikuwa na tundu dogo lenye kutoa risasi pindi tu liamurishwapo. Alilitazama tena na tena bila kuchoka moyoni akliambia

‘Ni wewe nakukumbuka sana kwa sura yako, mdomo wako mdogo ulipiga kelele za kutisha nikamshuhudia mama yangu akianguka chini huku akilia kwa uchungu, ni wewe ambaye baadae ulifanya vilevile na kumuacha baba yangu akiwa hana uhai, sasa naelewa tukio ulilofanya miaka ile, usihofu, hukuwa wewe ila umefanana naye,’

Joru alijikuta ndani ya kumbukumbu nzito, akiongea moyoni kwa uchungu huku akiitazama ile ‘rifle’ bunduki aliyoishika mkononi mwake.

Alilolitarajia likatokea, uchungu ukatawala hisia zake, hasira zikapanda kama moshi wa tanuru, Joru akarudishwa kihisia katika kumbukumbu mbaya iliyomrudisha miaka 21 nyuma, chozi likatoka katika jicho lake na kuning’inia chini ya kidevu chake, likajiachia na kudondoka ardhini, kishindo kikubwa kilisikika moyoni mwa Joru, vumbi lisilo la kawaida lilitimka na kumfanya mapigo yake ya Moyo kuongeza kasi, damu kwenda mbio, pumzi kutoka kwa nguvu.

‘Kesho na keshokutwa utakua kijana mwanangu, hakikisha unalipa kisasi kwa damu hii inayomwagika, damu ya familia yako, damu ya wazazi wako,’

Sauti ya baba yake ilijirudia kwa mwangwi wa ajabu kichwani mwake ikitanguliwa na kile kishindo cha lile chozi kufika ardhini, yote hayo hakuna aliyeyahisi wala kuyasikia isipokuwa Joru peke yake.

“Gwarideeeeee!!!!” ilikuwa amri nyingine iliyomgutusha kutoka katika ulimwengu wa mbali, aliinua kichwa akatazama mbele.

“Silaha beganiii

iii weka!” amri iliendelea kutoka kwa kiongozi wa gwaride. Kishindo kimoja kikasikika, bunduki zile zikishikwa kwa ukakamavu wa mikono ya wale wana wa jeshi, wanaomaliza mafunzo, zikapandishwa begani na miguu kuwekwa sawa kisha ukimya ukatawala. Muziki maalumu wa tarumbeta ulisikika ukitoka katika kikundi cha bendi ya jeshi kilichokuwa kikisindikiza vijana hao, muziki huo uliashiria kuwa mgeni wa siku hiyo alikuwa akiwasili.

Baada ya dakika chache mgeni yule alipanda katika kibanda maalumu, alikuwa ni amiri jeshi mkuu, mkuu wa nchi, juu ya kibanda kile maalum alisimama akiwatazama wale vijana waliokuwa ndani ya mavazi adhimu ya kijeshi yaliokuwa na mabaka, yaliyowapamba wakapambika, walikuwa ni vijana kutoka kambi zote za mafunzo za kanda ya ziwa wakihitimisha mafunzo yao kwa pamoja, hakika ilikuwa sherehe kubwa. Wakati wengine wakifikiria kukutana na ndugu na jamaa zao baada ya gwaride hili, wakiwapongeza kwa kuhitimisha mafunzo hayo magumu, haikuwa hivyo kwa Joseph Rutashobya, hakuwa na mtu wa kuja kumlaki wala kumwambia hongera katika shughuli hiyo, hali hii ilimpa uchungu sana lakini hakuweza kupingana na ukweli halisi uliopo, hana ndugu, hata wale waliopo hawajui kama siku hiyo anamaliza mafunzo yake ya jeshi kwa maana ni miaka mingi imepita hata hawakujua kijana huyo yuko wapi, walilia wakanyamaza, wakajua kama hajafa basi amepotea kimazingara.

Kiongozi wa gwaride akatoa amri nyingine, sasa ilikuwa ya kutoa heshima kwa Amiri jeshi mkuu; kama kawaida, zile bunduki zikatolewa mabegani na kushikwa mikononi kwa umahiri mkubwa.

Wimbo wa Taifa kombozi la Tanzania ulirindima, wapigaji walipiga kwa umahiri mkubwa, wimbo wa Taifa la Tanzania ambao kutokana na maneno yenye ujumbe mzito na melodi ya kupendeza mataifa kama Zambia na Afrika ya kusini yaliufanya kuwa wimbo wao wa Taifa vilevile, na ingependeza kama Africa nzima ingekuwa na wimbo huu mmoja kwa kila Taifa wenye maneno matamu ‘Mungu ibariki Afrika, wabariki viongozi wake na watoto wake pia’. Joru alitulia kwa ukakamavu hisia zake zikatekwa tena na wimbo huo ambao alijifunza alipokuwa shule ya vidudu na ile ya msingi madarasa mawili tu aliyoyasoma, chozi lingine likadondoka ardhini na kufanya kishindo kilekile moyoni mwake, mara sauti ya kilio kikali ikapita mawazoni mwake…

‘Aaaaaaaaaagggggghhhhh, kimbia Jose kimbia, usitazame nyuma,’

Aliikumbuka sauti hii ya mama yake kipenzi ikimjia katika hisia kali na nzito, Joru alijikuta akilia kwa kumbukumbu hizo. Alimtazama mgeni rasmi, mkuu wa nchi aliyetulia juu ya kibanda kile akiwa ndani ya suti safi ya kimaghalibi, hakuwa mbali kutoka katika kibanda kile.

Joru alikuwa katika gadi ya pili ambayo kwa mpangilio wao ilikuwa mbele kushoto ilikuwa gadi ya kwanza na kulia ilikuwa gadi ya tatu, katika gwaride hilo kulikuwa na gadi kumi na tano.

Joru alimtazama kwa makini mgeni rasmi moyoni akmwambia,

‘…Hujaubeba Uafrika, kama ungeubeba basi ungevaa vazi nadhifu la kitenge ama cha Sunguratex, Kilitex, au Mwatex.’

Wimbo wa Taifa bado ulikuwa ukiendelea, ‘Heshima umoja na amani, hizi ni ngao zetu, Africa na watu wake,’ maneno haya yalimpa uchungu Joru, akaitazama Africa kwa mapana yake,

‘Afrika bara zuri, bara aliloishi mwanadamu wa kale, lilokuwa na umoja mkubwa,

Afrika, kwa nini tunapigana Afrka?

Kwa nini tunakosa upendo Afrika?

Kwanini tumepoteza thamani ya maisha hadimu ya kiafrika yenye tunu zisizo kifani? Umoja, mshikamano, upendo na ujamaa, unapotea kati ya Waafrika? Chuki, ubabe, ubinafsi vimeiteka Afrika, vimeingia mioyoni mwa Waafrika na viongozi wake. Watu wa kale waliita bara hili bara la giza lakini sasa tunastahili kuliita bara jekundu kutokana na damu inayomwagika siku hadi siku.’

Wimbo ule mtukufu ulipotelea katika mawingu, mawingu ya anga la Mtukula, mawingu safi meupe yaliyopendezesha anga hilo, ndege aina ya mbayuwayu waliokuwa wakiruka hapa na pale walifanya nyimbo nyingine tamu mara tu baada ya kuisha ule wimbo hadhimu. Joru alikuwa bado katika hali ya ukakamavu mpaka amri nyingine ilipotolewa.

Mgeni rasmi alishuka kutoka katika kibanda chake na kuongozwa na askari maalum alieandaliwa kwa shughuli hiyo ya ukaguzi wa gwaride. Pamoja nae mkuu wa majeshi mkoa wa Kagera aliomsindikiza, brigedia Shibagenda. Walipita mbele ya mistari ya vikosi hivyo kwa mwendo wa madaa wakiongozwa na wimbo maarufu wa enzi zile.

‘Tanzania Tanzania, nakupenda kwa moyo wote, Tanzania Tanzania jina lako ni tamu sana…’

Joru alitulia bila hata ya kutikisika, akisikiliza muziki ule wa uliokuwa ukipigwa na bendi ileile huku hisia zake zikiimba pamoja na melodi hiyo.

‘Nilalapo na kuota wewe, niamkapo ni heri mama we…’

Ni siku hii Joru alipogundua umaana na uzito wa wimbo huo, picha za mauaji ya wazazi wake zilimrudia na kumsumbua kichwa. Machozi yalimtoka kijana huyu mkakamavu mwenye tambo la mtu anayenyanyua vyuma au kufanya mazoezi ya vitu vizito.

Mgeni rasmi alipomfikia alisimama na kumtazama Joru ambaye alisimama kiukakamavu; ukiacha machozi yaliyokuwa yakitoka machoni pake na kumwagika kwa fujo huku kelele nyingi za vilio zikimrudia, akiwaona askari wa Uganda chini ya kiongozi wao Mali ya Mungu wakitesa na kuua wanakijiji ndani ya mpaka wa Tanzania na Uganda, kipande cha ardhi ambacho Uganda ilidai kuwa ni chao, ubabe na utemi vilitawala.

MASAKA – UGANDA, 1976 February 20, saa 5 as.

LAND ROVER 109 ziliingia katika uwanja wa shule ya sekondari Masaka kwa fujo za aina yake, vumbi jekundu ‘ngunja’ lilitimka huku na kule, kelele za wana Uganda waliojazana katika uwanja huo zilisikika zikishangilia tukio hilo huku akina mama wakipepeza matawi ya miti kunogesha tukio. Vikundi vya ngoma vilianza kurindimisha midundo ya Kiganda na vijana wa kike na kiume wakionesha umahiri wao katika kusakata mirindimo hiyo. Yote hayo yakiendelea, zile gari zikasimama na wanajeshi wenye bunduki wakateremka kuweka ulinzi eneo hilo wakishirikiana na wale waliowakuta pale.

Ndani ya benzi moja nyeusi ya kijerumani iliyokuwa ikipepea bendera ya Uganda aliteremka binadamu mwenye tambo kubwa, mweusi ti; aliyependezeshwa kwa mavazi ya jeshi la Uganda yaliyochafuka tepe na vyeo anuai, hakuwa mwingine, bali ni yule ambaye wewe ulimdhani kuwa ni katili, asiyecheka na mtu, la, huyu alikuwa mcheshi aliyesalimiana na watu wa kila rika, aligusika na kila mmoja, japo alikuwa akitawala nchi kwa mabavu baada ya kumtoa Rais aliye madarakani mwaka ’62, Milton Obote. Huyu alijulikana kwa majina mengi ya kibabe ndani na nje ya Uganda, huwezi kuamini, aliwapenda watu wake na kila alilofanya alilifanya kwa manufaa ya watu wake ijapokuwa katika macho ya wengine ilikuwa ni ukatili, uonevu, udikteta na mengineyo, alikuwa Idd Amin Dada, aka The butcher of Africa, aka The Conqueror of England Empire, aka The Lord of all beasts, alikuwa na majina mengi na huku kwetu tulimwita ‘Nduli’…

“Uganda oyeeeeeeee” alianza namna hiyo pale tu alipopanda katika jukwaa lililoandaliwa.

“Oyeeeeeeeeeee” aliitiliwa kwa nderemo na vifijo.

“Habari…!” aliwasalimu watu wake kwa lugha ya kiswahili, akaendelea; “Leo nipo hapa Masaka nimekuja kuwasalimu ninyi watu wangu, najua kila mtu anapenda Uganda sio? ‘Ndiyooooooo’, Basi na kama ni hivyo lazima tuilinde nchi yetu, tuipende na kuipigania, serikali yenu inawapenda japokuwa mataifa mengine hayatupendi lakini ni kwa sababu ya wivu, wanatuonea wivu kwa maendeleo yetu, msihofu hakuna wa kutupiga bali tutawapiga, na katika hili nitataka wote muungane nami atakayebisha, atakayesaliti juhudi mnajua nitakachomfanya. Sasa tuna mpango wa kwenda kukomboa kipande chetu cha ardhi huko Tanzania, kwa maana ni mali yetu pale Mtukula, ni mali yetu mto wa Kagera, tuogope nn? Tuogope nn? Uganda oyeeeeeeeee!!!!!!”

Ilikuwa hotuba fupi ambayo ilishangiliwa kwa hamasa kubwa, ngoma zikaanza kurindima tena, sasa ilipigwa ngoma ya kwao, alikozaliwa, Idd Amin, akashuka na kuungana na wanachi kucheza ngoma hiyo kwa ustadi mkubwa sana, watu walimsahangilia huku wakimrushia maua kuonesha wamemkubali kiongozi wao.

Sura ya kutisha kiumbe huyu haikusahaulika kwa wengi waliodhurumiwa roho za ndugu au marafiki zao, walimtazama na walitamani wamle nyama lakini haikuwezekana, ilikuwa ukizungumza vibaya juu yake unaamka hauna kichwa au umepambwa kwa matundu ya risasi, hali ilikuwa mbaya, mtu huyu aliogopwa na kila mtu lakini amini usimini alikuwa na marafiki wakubwa waliompenda na kumpa misaada mingi kwa ajili ya watu wake. Baada ya shughuli hiyo hapa Masaka akaendelea na kazi zingine za kujenga taifa lake.

§§§§§

Mgeni rasmi wa gwaride lile alifika pale aliposimama Joru, aliyashuhudia machozi yaliyokuwa yakimtiririka usoni, alionekana wazi ana uchungu na kitu, akasimama mbele ya kuruta huyu, akamtazama tena na tena, mkuu wa majeshi aliyekuwa pamoja na mgeni rasmi ndiyo kwanza alimtambua kijana huyo Joseph Rutashobya ‘Joru’, mkuu wa majeshi alibaki katumbua macho hakutegemea kabisa kama angemuona kijana huyo, akakumbuka miaka mitatu nyuma, jinsi alivyokutana na kijana mtukutu, Joru, katika mazingira ya kutatanisha.

MIAKA MITATU ILIOPITA

MISITU YA BIHARAMURO

TAARIFA ya duru za usalama ilisema kuwa idadi ya vitendo vya ujambazi imekuwa kubwa, kila uchwao, mabasi yanatekwa, watu wanaporwa, wengine kuuawa na kubakwa, polisi walifanya kazi kubwa ya kupambana na majambazi hayo lakini walijikuta wakizidiwa kwani majambazi yalikuwa na silaha kubwa za kivita walizozipata kutoka nchi jirani, wakifanya ujambazi na baadhi ya wanajeshi wa nchi hizo sio tu kuteka mabasi bali hata kuvamia maduka na kupora.

Siku moja kulifanyika uhalifu mkubwa, mabasi sita na malori ya mizigo yaliyokuwa yakienda Kagera na Ngala yalitekwa na majambazi hao walipora mali nyingi za thamani, wakawavua nguo abiria na kuwaacha uchi kisha kuwaamuru waimbe wimbo

‘Mtaji wa masikini ni nguvu zake’

Ilikuwa ni aibu ma fedheha kwa watu hao.

Joru akiwa kajificha msituni, juu ya mti, aliyashuhusia hayo yote yaliyokuwa yakitukia, aliumia sana lakini hakuwa na msaada. Alitazama kwa uchungu na alijua wazi kuwa akileta tabu lazima watamuua, alijibana palepale na kuendelea kutazama.

Wale majambazi wakamaliza kazi yao wakakusanya kila kitu, wakikung’uta nguo walizowavua wale abiria na kuchukua kila kilicho katika mifuko kisha wakatokomea msituni.

Joru alitulia kulekule juu ya mti akihofia kushuka akijua kwa vyovyote watafikiri kuwa yeye ni mmoja wao. Baada kama ya nusu saa tangu wale majambazi waondoke, polisi walifika na landrover zao aina ya 110, kwa ajili ya kuwalinda raia hao. Waliwahoji juu ya tukio zima jinsi lilivyokuwa, wakasimulia. Baada ya kila kitu kuwa sawa, yale mabasi na malori yaliondolewa eneo lile.

§§§§§

Usiku wa siku ile ya tukio, polisi wakishirikiana na JW, waliuvamia msitu na kufanya msako wa haja, walipekua kila kichaka na vichaka kusaka mali na majambazi hao.

Wimbi la utekaji mabasi lilikuwa kubwa katika mkoa wa Kagera, askari wa jeshi wa nchi jirani walikuwa wakishirikiana na majambazi katika uporaji huo. Wasafiri na wananchi waliilalamikia serikali kwa hali hiyo. Wahusika walisikiliza kilio hicho, wakakaa kikao na kuamua kulivalia njuga swala la ujambazi katika mkoa huo.

Joru alikuwa ndani ya kichaka usiku huo akiwa kajipumzisha, mara akasikia kelele za mbwa na watu wanaoongea, hakufanikiwa kuchomoka kwani mbwa wa polisi walifika katika kichaka hicho, alipojaribu kujiokoa alichelewa, kwa amri moja walimvamia na amri nyingine walimwacha akiwa hoi, wale polisi na wanajeshi wakamtia pingu kijana huyo kisha msako ukaendelea.

Usiku huo walifanikiwa kuwakamata watu 12 akiwemo Joru, wakawakusanya na kuwatembeza kwa miguu kuelekea barabarani walikoacha magari. Kati ya hao 12 kuna walioleta ujeuri njiani, walipigwa risasi na kuuawa kisha kutelekezwa msituni, ilikuwa ni hali ya kuogofya sana kwa Joru, hakutamani kuangalia nyuma.

Mwendo kama wa nusu saa hivi wakafika barabarani na kuwakuta askari wengine, wakawapokea kwa kichapo cha haja kisha wakawaamuru wote kuchuchumaa chini. Kiongozi wa operesheni hiyo akasogea na kumtazama mmoja mmoja kwa sura akimmulika kwa kurunzi yenye mwanga mkali, akafika kwa Joru, akasimama na kumwangalia sana kijana huyu kwa makini.

“Yaani hata wewe ni jambazi?” akamuuliza Joru.

“Hapana afande,” Joru akajibu.

“Sasa unafanya nini huku?” yule kiongozi wa msako alimuuliza Joru,

“Ni stori ndefu sana mzee,” yule kiongozi wa operesheni ambaye alikuwa ni mtu wa makamo alimtazama tena Joru.

“Unaitwa nani?” akamuuliza

“Joseph Rutashobya,” akajibu.

“Haya nambie kwa nini umekuja huku msituni? Ukinambia ukweli nakuachia ukinidanganya nakufunga jela,” yule askari alimkaripia. Joru alitulia kimya kisha akaanza kulia.

“Unalia nini?” Yule askari akauliza kwa ukali.

“Afande ni stori ndefu nay a kusikitisha sana, huwa siipendi kuikumbuka kwa maana inanitia uchungu” Joru alisema huku bado akilia kwa vikwifukwifu. Yule askari akamtazama Joru kwa jicho la huruma sana, moyo wake ukaingia ganzi akashindwa kuvumilia, chozi likamdondoka hata kabla Joru hajaweza kuongea chochote katika hilo.

Baada ya kujifikiria mara kadhaa, Joru aliinua kichwa na kumtazama Yule askari jeshi, Shibagenda, kisha Joru akajaribu kukumb uka lile tukio la kutisha katika maisha yake akamueleza kisa na mksa way eye kuwa msituni siku hiyo.

1977

Kijiji Fulani huko Mtukula

“Hatuwezi kukubali kunyang’anywa ardhi hivi hivi, ye nani? Kama ninyi mnamuogopa basi mimi simuogopi,” ilikuwa sauti ya mzee Rutashobya katika mkutano wa kijiji uliotishwa siku moja na mwenyekiti wa kijiji hicho.

Suala la Idd Amin kuvamia Tanzania na kudai maeneo Fulani ni ya Uganda huko pande za Kagera lilichukua kasi, ilikuwa haipiti wiki wanakijiji hawa walisikia sehemu Fulani Amin amevamia na kuteka kijiji Fulani, ilikuwa hali ya kuogofya sana iliyokuwa ikifanywa na hao vibaraka wake ambao wakati mwingine walivamia sit u kwa madai hayo bali kupora mali za wanakijiji na hata kufanya unyanyasaji wa kijinsia kama kubaka na kuwapa wananchi mateso makali mwishoe kuwaua. Mzee Rutashobya, hakuipenda sana hali hiyo, alikuwa akiumia sana kila aliposikia taarifa hizo hasa kupitia redio idhaa ya taifa. Alitamani siku moja apambane na watu hao awaoneshe kama kweli yeye alikuwa ni mmoja wa askari wa KR, jeshi la mkoloni, aliyepigana vita ya pili ya dunia kwa upande wa Ujerumani.

“Mzee Rutashobya unasema tu wewe, wakija hapa sijui hata kama utaweza kukimbia,” mzee mwingine alimpinga Rutashobya.

“Sikia wewe mimi si muoga kama kuku, niko tayari kufa, kama kufa nimeshaona wengi waliokufa siwezi kuogopa kufa, nitajisikia furaha kufa kwa ajili ya nchi yangu na si kwa lingine,” alibisha. Mkutano ulikuwa mrefu sana katika kijiji hicho, hoja ikiwa ni jinsi gani ya kukilinda kijiji chao dhidi ya askari wa nduli Amin ambao waliteka na kunyang’anya ardhi ya wananchi kila kukicha.

Si kwamba viongozi wa chama na serikali kwa ujumla walikuwa hawalijui hilo lakini bado roho ya subira ilikuwa ikitawala roho za viongozi hao waliokuwa wakisikiliza kila agizo kutoka kwa Mwl J.K Nyerere, ambaye ndiye alikuwa Rais na Amiri jeshi mkuu mwaka huo. Baada ya mkutano huo kwisha na kila mtu kurudi katika kaya yake iliadhimiwa kuanzisha ulinzi wa kulinda kijiji chao.

Usiku wa siku hiyo, mzee Rutashobya na familia yake ya mtoto mmoja, Joseph, walikuwa wameketi nje, mkekani, wakiangaziwa na taa ya kandili iliyokuwa kati yao. Mkewe alikuwa akiendelea kuchambua buni alizokuwa amezivuna kutoka shambani wakati Mzee Rutashobya aliketi kwenye kiti chake cha uzee, macho yake yakiangaza huku na huko katika migomba iliyozunguka eneo hilo lote, pembeni yake alikuwa amelaza bunduki kubwa aina ya gobole na risasi kadhaa zikiwa kwenye mfuko wa suruali yake aliyokuwa amevaa, mdomoni mwake alikuwa akivuta kiko huku akimsimulia hadithi mbalimbali za kale na kumfundisha stadi za maisha mwanae pekee Joseph.

“Na wewe siku moja utakuwa mkubwa,” alimwambia mwanawe.

“Na mi nikiwa mkubwa nitakuwa kama wewe?” Joseph aliuliza.

“Ndiyo, tena itabidi uwe mkakamavu sana, uwe mwanaume asiyeogpa kitu kama mimi baba yako, sikiliza mwanangu, mimi baba yako tangu nikiwa mdogo wakati wa ukoloni, nilikuwa najifunza kila kitu kutoka kwa baba yangu, kuwinda, kulima na kila kitu.” Akavuta kiko chake na kupuliza moshi kwenda angani kisha akaendelea kumueleza mwanae, “Na wewe ujifunze kutoka kwangu, usikubali mtu akuonee hata siku moja, uwe Mtanzania imara, mwana TANU thabiti, hakikisha unaitetea nchi yako katika lolote lile ikiwa hata kufa, kufa, huo ndio uzalendo mwanangu,” Mzee Ruta alikuwa akimwambia mwanane ambaye alikuwa ameduwaa kwa maneno hayo makali.

“Baba, mi mbona naogopa kufa?” aliuliza.

“Kwa sasa utaogopa kwa sababu hujui, lakini ipo siku hautaogopa kufa, mazingira yatakufanya usiogope kufa hata kidogo, lazima uwe mwanaume kweli kweli, hata mi nikikuachia mji huu basi uweze kuutunza na kuulinda maana ndio utakuwa wajibu wako, wewe huna dada huna kaka, upo peke yako kwa hiyo uwe mkakamavu katika kila kitu, usijione mdogo” Mzee Ruta aliongea huku akimpigapiga mgongoni mwanawe huyo, hata baadaye aligundua kuwa tayari amekwishalala muda mrefu, na maneno yale yalikuwa yakiingia katika ubongo wake kama ndoto ya kutisha sana yenye matukio ya ajabu ambayo Joseph hakuwahi kuyaona maishani mwake.

§§§§§

Joseph Rutashobya, mtoto pekee wa mzee Rutashobya alikuwa na umri wa miaka tisa wakati alipokuwa akiambiwa hayo yote na baba yake ambaye tayari umri ulikuwa umekwenda, lakini pamoja na umri wake mkubwa alikuwa ni mkorofi na hakuna mwanakijiji aliyekuwa hamjui mzee huyo. Joseph hata shuleni ilikuwa ni vigumu kupewa adhabu kutokana na ukorofi wa baba yake, ijapokuwa yeye alikuwa ni mpole sana asiyependa kuongea na watu, wengi walisema ni tabia ya mama yake, shuleni hakuwa akichangamana na marafiki, daima alikuwa akiambatana na mtoto wa shangazi yake tu, Kemilembe. Daima utawakuta pamoja hata kama si muda wa masomo, ilikuwa ni vigumu wawili hawa kuwatenganisha kiasi kwamba walionekana kama mapacha wanapoambatana. Si Joseph wala Kemilembe aliyewahi kufikiri kuwa siku moja watakuja kutengana au kutenganishwa, daima katika maongezi yao ya kitoto waliweka ahadi za kuwa wakiwa wakubwa wataishi kama wazazi wao wanavyoishi, kuishi nyumba moja, kulala pamoja, wao kwao ilikuwa ni kama sehemu ya maisha ya ukubwa ambayo walijua wazi kuwa siku moja watayafikia.

Hata wakati Kemilembe alipoanza kuota matiti, alimwambia Joseph kuwa kifua chake kinavimba huku na huku, Joseph alitazama uvimbe huo na kubonyezabonyeza lakini alikutana na vitu vigumu, kwa kuwa Kemilembe aliamini kuwa Joseph anajua mengi kwa kuwa ni mwanaume, alifurahi sana alipoambiwa na Joseph kuwa “Sasa utakuwa kama mama, utakuwa na maziwa makubwa, tukiwa na motto atanyonyamo.”

Joseph mara nyingi alikuwa akimsikia baba yake anavyosikitika hasa asikilizapo redio yake ndogo ya mbao aina ya Phillips iliyokuwa ikimpa habari kila saa nne, saba na kumi ya kila siku. Mzee Rutashobya alichukizwa wazi na yale anayaoyasikia kutoka kwenye chombo hicho kidogo ambacho Joseph aliaamini kabisa kuwa kuna watu ndani wanaoongea.

“Baba kila ukisikiliza humu unakasirika, kwa nini?” Joseph alimuuliza baba yake.

“Mwanangu, dunia hii sijui tunakwenda wapi, kila siku watu wankufa lakini wenye nguvu wanafumba macho,” akamjibu kana kwamba anamjibu mtu mzima mwenye uelewa mpana. Joseph akamkazia macho baba yake akimaanisha hajamuelewa alichomwambia.

“Umeshawahi kumsikia Idd Amin?” Rutashobya akamuuliza mwanawe.

“Ndio, mwalimu ametuambia kuwa ni mtu mbaya sana, anaua watu,” Joseph akajibu huku akionesha huzuni ya wazi usoni mwake. “Sasa kwa nini polisi wasimkamate?” akauliza.

“Aaah Jose, polisi wote wako chini yake, wanamsikiliza yeye,” Rutashobya akajibu.

“Mi ningekuwa polisi ningempiga bastola,” Jose akajibu akiwa hajui anachokiongea.

Siku iliyofuata….

“…Idd Amin akifa, mimi siwezi kulia, nitamtupa Kagera awe chakula cha Mamba…” zilikuwa sauti za watu wakiimba kutoka mbali sana. Joseph akiwa na Kemilembe walikuwa njiani kuelekea shuleni alfajiri ya siku hiyo, mikononi mwao walikuwa na fagio pamoja na vidumu vya kuchotea maji kwa ajili ya kumwagili bustani zao za mbogamboga.

“Kemi, unasikia hao wanaoimba?” Jose alimuuliza Kemilembe.

“Ndiyo, kwani ni akina nani?” Kemilembe aliuliza. Joseph akatulia kwanza bila kujibu akisikiliza zile sauti za ule wimbo ulioonekana kumpa faraja kubwa masikioni mwake.

“Unataka kuwajua?” Joseph aliuliza.

“Ndiyo,” Kemi akajibu. Joseph akamshika mkono Kemilembe na kumvutia kwenye majani, wakajificha huku zile sauti zikikaribia pale walipo. Punde si punde kundi kubwa la watu waliogawanyika katika makundi makubwa manne walipita wakikimbia mchaka mchaka. Walikuwa wanajeshi wengi wenye silaha mikononi, wakiwa wamevaa magwanda yao yenye mabaka mabaka yaliyowafanya waonekane kama wadudu, kofia za chuma zilikuwa zimezungushiwa majani mengi na kufanya kama wamebeba vichaka, walikuwa wakiimba kwa jazba na wakipiga mbinja nyingi. Walipokwisha pita, Joseph na Kemilembe wakajitokeza kutoka kwenye lile chaka walilojificha.

“Wanaenda wapi?” Kemilembe akauliza.

“Watakuwa wanakwenda kumkamata Idd Amin,” Joseph alijibu kwa kujiamini kisha wakavuka barabara na kuelekea shuleni.

Watu wa eneo hilo ilikuwa ni kawaida kwao kuona wanajeshi wakipita na kuimba au wakiwa wamejificha machakani wakiwa katika mazoezi ya kivita kutokana na hali halisi iliyopo. Walikuwa katika hali ya utayari muda wote hasa wale wa mpakani, Mtukula.

Mashuleni nako kulikuwa na ulinzi mkali, tahadhari kabla ya hatari.

Mchana wa siku hiyo, masomo yalipokwisha, Joseph na Kemilembe waliwahi kurudi nyumbani tofauti na siku nyingine. Siku hiyo Joseph alifika nyumbani na kumkuta mama yake akiwa ndio kwanza ametoka shambani lakini hakumkuta baba yake. Alimuuliza mama yake kuwa baba yake amekwenda wapi akajibiwa tu amekwenda kijiji jirani hatochelewa kurudi. Joseph alipitiwa na usingizi baada ya shibe ya mchana, akajilaza kwenye kijitanda kidogo kilicokuwapo sebuleni.

Alishtuliwa na sauti ya baba yake aliyekuwa akimsimulia mama yake habari mbaya na ya kutisha kuwa wameokota maiti za watu katika mto Kagera. Mzee Rutashobya alikuwa akiongea kwa huzuni sana na uchungu juu ya hali hiyo. Joseph aliyekuwa amelala kisungura alikuwa akisikiliza yote. Baadae alipoamka hakusita kumueleza baba yake kuwa amekutana na wanajeshi wakienda kumkamata Idd Amin ili wmtupe Kagera aliwe na Mamba. Joseph akamuuliza baba yake kama katika hizo maiti ilikuwepo ya Idd Amin. Baba yake akamtazama kwa mshangao lakini akajua kuwa ni akili za kitoto tu.

Usiku wa siku hiyo wazee wa kijiji kile walikutana pamoja kujadiliana juu ya hali halisi ilivyo kwa usalama wao kwa mara nyingine, ikiwa pia kuweka zamu ya kulinda. Siku hiyo mzee Rutashobya na wengine tisa walikuwa zamu ya kuweka ulinzi. Mzee Rutashobya kutokana na uzoefu wake wa medani za kivita alipokuwa huko ughaibuni katika vita ya pili ya dunia.

“Mnajua tukiwa wazi watatuona kirahisi, hapa ni kujificha kwenye migomba na wengine kwenye mibuni,” alitoa maelekezo kwa wengine, yakaeleweka. Kila mtu akajificha kama alivyoambiwa, hakuna aliyekuwa hamuamini mzee huyo kwa mipango bahati mbaya tu hakuwa kiongozi katika kijiji hicho.

Usiku wa manane…

Kutoka pale alipojificha mzee Rutashobya, alisikia mlio wa gari lililokuwa likielekea kule kijijini kwao, likishuka mlima wa karibu. Alijitokeza kwa hadhari kubwa na gobole lake mkononi akiwa keshaliweka tayari kwa mashambulizi endapo anayekuja ni adui. Akawapa alama wenzake ishara ya mruzi kama mlio wa ndege akiwaweka tayari kwa lolote.

Yalikuwa malori mawili makubwa, moja lilikuwa na askari na linguine lilikuwa tupu, wakatelemka kuanza kuvamia mazizi ya mifugo, wakaanza kuswaga ng’ombe na mbuzi kupakia katika lori lililo tupu, huku wengine wakianza kuvunja milango ya nyumba. Askari mmoja aliyekuwa akivunja mlango kwa teke alichomwa mshale wa mgongo na kupiga yowe la nguvu, hapo waligundua kuwa kuna watu nje wenye silaha, wale wavamizi wakavamia machaka ya migomba kuanza kusaka huku wakipiga risasi kila wanayemkamata. Mzee Rutashobya alimlenga mmoja aliyeonekana kimbelembele kwa kutoa amri hizo, akamlega na gobole lake akafyatua shabaha safi, ikapasua kichwa cha Yule mtu, kisha akahama kile kichaka na kwenda kichaka kingine ikiwa ni moja ya kuwapoteza wale wavamizi. Mara risasi kama mvua zikakata na kutengeneza uwanja katika lile eneo ambalo risasi ya Rutashobya ilitokea.

“Atakuwa ameshakufa huyo!” mmoja wa askari akasema, lakini kabla hajatoka eneo lile, gobole la Rutashobya lilifanya kazi nyingine likamtungua Yule aliyekuwa akisema hayo, akajibwaga akiwa kifua chote hakitamaniki. Hali ikawa mbaya, kiongozi wa wavamizi aliyejulikana kama Mali ya Mungu ambaye muda wote huo alikuwa ndani ya lori akivuta bangi alimua kuteremka na kumsaka huyo anayejifanya mdunguaji. Mpaka yeye aliposhuka tayari vijana wake wanne walikuwa chini bila uhai, wakiwa wamelazwana gobole la Rutashobya. Mali ya Mungu akajua wazi kuwa wanapambana na mtu anayejua anachokifanya.

Kelele za akina mama na watoto ziligubika anga la kijiji hicho, ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia vilitendwa hadharani kwenye mbalamwezi nyeupe. Mzee Rutashobya bado alikuwa akiwaumiza vichwa wale wavamizi huku akiangalia kila linaloendelea, ijapokuwa roho ilimuuma sana, lakini haikuwezekana yeye kujificha muda wote huku akiwasumbua wale wavamizi, risasi zilimwishia akabaki na gobole tu. Wakiwa bado wanamsaka kwenye migomba, mzee Rutashobya sasa alikuwa amejificha kwenye kichuguu. Mmoja wa wavamizi alikuwa akija huku akifuatiwa na wenzake kuelekea nyumba ya Rutashobya, walipofika walivunja mlango na kumtoa mke wa Rutashobya, Joseph naye alishtuka usingizini, akatoka nje kasi ili kumsaidia mama yake lakini teke kali lilimtupa upande wa pili, kitendo hicho kilimfanya Rutashobya kutoka mwenyewe kwa kasi kumkabili Yule askari aliyefanya hivyo, wakakutana ana kwa ana, Yule mvamizi alimuona Rutashobya akija kasi wakati akijipanga na bunduki yake kumlipua alichelewa kwani kitako cha gobole kilitua shavuni na kuvunja taya la jamaa huyo, Rutashobya akavamiwa na askari kama watano na kuanza kupigwa vibaya, wakati huo kiongozi wao Mali ya Mungu akija taratibu kumuona mtu huyo aliyekuwa akiwanyanyasa na tayari alikuwa ameua askari wane kwa risasi zake nne.

“Muacheni!” sauti ya Mali ya Mungu iliwafanya vijana hao wenye hasira kumuacha Rutashobya akiwa hoi kwa kipigo, wakati huo mkewe akilia kwa kwikwi na Jose ndio hatamaniki.

Mali ya Mungu akamsogelea Rutashobya, akamtazama kwa tuo, “Wewe ndio unajifanya kujua siyo?”alimwuliza huku akimzunguka, kisha akasimama na kugeuka upande mwingine, “Mleteni mkewe hapa, lazima niwaue wote wawili kwa mkono wangu huu uliolaaniwa,” alizungumza kwa sauti yake mbaya huku akiupunga hewani mkono wake wa kuume.

“Aaaaaaaaiiiigghhh!!!!” ilikuwa sauti ya mke wa Rutashobya alipokuwa akiburuzwa kuja kwa mumewe. Joseph alikuwa akitazama huku machozi yakimtoka, alitamani kuwaokoa wazazi wake lakini haikuwezekana hakuwa na nguvu za kufanya hivyo, alibaki kajikunyata na kutazama ukatili huo wanaotendewa wazazi wake. Askari mmoja alimuona Joseph pale alipojikunyata akatoka kwenda kumfuata.

“Kimbia Joseph, usirudi nyuma!” mama yake alimgutusha na Joseph alinyanyuka na kukimbia bila kutazama nyuma akipita katika machaka ya migomba, akilini mwake alihisi kuna mtu anayemfuata nyuma kumbe ulikuwa ni mwangwi wa nyayo zake kila zinapotua ardhini, alipogeuka nyuma kuangali huku akiwa kwenye mbio hizo alijibamiza kwenye mti na kuanguka vibaya, damu zilikuwa zikitiririka kwenye jeraha lililotokea pembeni mwa paji la uso wake, akadondoka chini na kupoteza fahamu.

Giza nene lilimchukua Joseph kusikojulikana, alikuwa akisikia sauti za watu ambao walikuwa hawaeleweki wanachokiongea, hakuweza kuona kitu isipokuwa giza lililomzunguka, giza nene kuliko unavyofikiria, mara akaona watu wa kutisha wenye mapembe na ndimi zinazowaka moto kila waachamapo vinywa vyao, zile kelele zikanyamaza, kukawa na kimya kikuu, sasa Joseph alikuwa akisikia sauti ndogo ya tone la maji lililokuwa likianguka kutoka juu na kutua katika dimbwi kubwa la maji, sauti ile ilijirudia rudia, akahisi kiu kikali kimeshika, akainuka kutoka pale alipolala, mbele yake alisimama mtu mwanaume ambaye mkono wake wa kuume alimshika mwanamke, wote wawili walikuwa wakionekana kwa tabu kutokana na giza lile. Mara mwanga mwembamba ukawamulika, walikuwa wamevaa maguo meupe yaliyokuwa yamewafunika hata nyuso zao zisionekane. Yule mwanaume alijifunua uso wake, alikuwa ni binadamu asiye na sura, sura yote ilikuwa imeliwa kama si wadudu basi sijui ni kitu gani.

“Joseph, hivi ndivyo tulivyofanywa wazazi wako,” ilikuwa sauti ile ile ya baba yke ikimwambia maneno hayo, kisha ikaendelea, “Sasa unabaki kwenye ulimwengu wa peke yako, utateseka sana mwanangu lakini roho za babu zako hazitakuacha, lipa kisasi cha damu hii, damu ya mzimu wa Rutashobya haiendi bila malipo”. Mara tone la maji baridi sana likamdondokea Joseph, akakurupuka kutoka katika mzimio huo, na kujikuta peke yake porini. Ilikuwa ndoto kama ndoto ya kutisha ndoto ya kuogofya sana, Joseph alikuwa akibubujikwa na machozi, kijua kitamu cha asubuhi kilikuwa kikimchoma akiwa juu ya umande wa asubuhi, akajinyanyua na kutazama huku na huko, hakuna alichokishuhudia, ni moshi mkubwa uliotapakaa angani, Joseph akashikwa na uchungu akaanza kutimua mbio kurudi kijijini kwao. Baada ya mwendo wa dakika kumi na tano hivi bila kusimama alitoke upande wa nyuma wa kijiji hicho, akakutana na kibao kikubwa kilichoandikwa, “ENEO HILI LIKO CHINI YA SERIKALI YA UGANDA, USIKATISHE.”

Joseph akasimama ghafla akatazama na kusoma kibao hicho lakini hakuelelwa sawasawa kilichoandikwa, alitembea taratibu ndani ya machaka ya migomba, akitazama nyumba zilizokuwa zikifuka moshi kwa kuchomwa moto, miili ya watu bado ilikuwa imelala chini na wengine hawakujulikana walipo, aliendelea kuvuta hatua ndogondogo akitazama vizuri, akafika usawa wa ilipokuwa nyumba yao, moto ulikuwa ukimalizia kuangusha mti wa mwisho uliokuwa umeshikilia nyumba hiyo, yote ikalala chini, jivu. Joseph akajitokeza na kuvunja sheria asiyoijua, akasimama mbele ya nyumba hiyo, alipogeuka, mara akasikia kama mtu akikohoa, akageuka huku moyo wake ukifanya paaaaa! Alikuwa ni mtu aliyelala chini kwenye vumbi na jivu, Joseph akamwendea kwa uoga na kumfikia, aliitambua nguo ya mtu huyo, alikuwa baba yake, aliyekuwa na majeraha na damu kila kona ya mwili wake, sura yake ilikuwa imechafuka na kugandwa na damu nzito ambayo ilificha kabisa sura yake.

“Baba!” Joseph aliita. Mzee Rutashobya aliisikia sauti ya mwanane lakini hakuwa na uwezo wa kumuona kwani alikuwa ametobolewa macho, kabla ya kupigwa risasi mbaya ya kifuani, alikuwa akihangaika kupigania roho yake iliyokuwa ikimuacha taratibu.

“Jose! Hauna wazazi, utabaki Yatima, nilikuwa napigania nchi yangu, lakini haikuwa hivyo, utakuwa mtu mzima, tafadhali damu ya Rutashobya isipotee bila malipo, malipo yanayoistahili,” alipokuwa akisema hayo alikuwa akimwagikwa damu nyingi, akijaribu kuinua mkono wake kuonesha kitu Fulani lakini hakuweza.

“Nini baba?” Joseph aliuliza huku akilia kwa uchungu, “Nyuma ya shimo la ch….o….. chiiiooooo,” Mzee Rutashobya, akarudi ardhini, Roho ikamuacha akatulia tuli, kwa utulivu mkubwa. Upepo mkali ukaanza kuvuma katika eneo lile, vumbi la moto na jivu likasambaa kila mahali.

“Joseeeeeee kimbiaaaaaaa!!!!!!!!!!” alihisi sauti ya mama yake ikimwambia kwa kelele kubwa, Joseph akatimua mbio na kukimbilia kusikojulikana.

§§§§§

Vijana wa Jeshi la Wananchi kutoka Mtukula walifika eneo hilo kwa kuchelewa, walikuta tayari mauaji mabaya yameshafanyika na kijiji kizima kipo chini kwa moto, hakuna hata jiwe lililosalia juu ya jiwe. Kiongozi wa vijana hao Kepteni Tibaijuka, hakuwa na la kufanya, alitazama maafa hayo akabaki kimya, hakuna aliyeongea na mwingine, kila mmoja alitoa kofia yake kichwani kuonesha ishara ya majonzi.

Taarifa ya uvamizi huo mbaya kuliko iliyowahi kutokea katika eneo hilo ilifika makao makuu kwenye kitengo chake. Amiri jeshi mkuu alishikwa na masikitiko makubwa juu ya hali hiyo. Alijishika mikono shavuni akiegemeza viwiko vya mikono hiyo mezani huku kifimbo chake akiwa kakibana kwapani, alionekana wazi kuchoshwa na taarifa hizo za kila siku, aliyafunika macho yake kwa viganja vyake kisha akayafikicha kiasi na kutoa ile mikono na sasa akaiweka mezani na kuwatazama wale walioketi mbele yake. Mkuu wa majeshi, Musuguli na wasaidizi wake, wote walibaki kimya hakuna aliyeongea katika mkutano huo wa dharula.

“Mzee, sisi tulishakwambia kabisa kabisa huyu si mtu wa kumwacha hivi, tazama sasa anavyonyanyasa watu wetu!” Yule mkuu wa jeshi akamwambia Mwalimu.

“Nimekuelewa kijana, hata mimi hapa nafikiri nini cha kufanya, maana hii inatisha, anatudharau huyu, anaingia mpaka ndani kwetu akidai ardhi ni yake, anavunja mikataba ya kimataifa juu ya mipaka ya nchi,” Mwalimu alijibu kwa uchungu, akakiweka kifimbo chake mezani na kujiegemeza kwenye kiti chake cha enzi, kiti kilichoibeba nembo ya taifa, akatafakari jamabo, jamabo la kuamua juu ya usalama wa raia wake.

Wakati Mwalimu akivuta muda kwa busara zake huku akitumia mazungumzo kumsihi Nduli huyo aache anachokifanya, wananchi walikuwa tayari wamechoshwa na hali hiyo, kila mmoja alitamanai kumkamata mtu huyo na kumtafuna nyama lakini wote walikuwa wakisubiri amri ya mkuu wan chi, majeshi yalikwishajipanga kwa vita, yalikuwa yakisubiri amri ili yaanze kazi ambayo kwayo ndio maana wamekuwa wanajeshi

§§§§§

ITAENDELEA

Risasi Nne Sehemu ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment