Mama’ke Mama Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA: GEORGE IRON MOSENYA
********************************************************************************
Simulizi: Mama’ke Mama
Sehemu ya Tatu (3)
Nilipiga hatua fupifupi hadi nikafika eneo lile ambalo mama alikuwa amezungukwa na wanakijiji.
“Ngomeni…” niliisikia sauti ya mama ikiniita na hapo babu akanishika mkono na kunipitisha nikafika mbele za mama… sasa alikuwa ameketi kitako na alikuwa anatabasamu tu!! Japo lilikuwa tabasamu la kujilazimisha.
Haikujalisha kitu kwangu, mama yangu alikuwa yu hai. Ilitosha.
“Ngomeni, sasa najisikia vizuri usiwe na mashaka sawa eeh!” alizungumza huku akimpatia babu mkono, babu akamnyanyua.
Mama aliweza kusimama peke yake, akawashukuru wote waliomuhangaikia hadi hapo alipokuwa alisema anaweza kutembea vizuri kabisa.
Mimi nilikuwa mdogo na hali hiyo ilinifanya niogope kusema kitu ambacho nilikisikia wakati ule nilipokuwa katika kusali kama yule mtaalamu alivyokuwa amenielekeza nilijua hata nikisema nilichokisikia hakuna atakayeniamini.
Nikalazimika kuwa kimya huku nikitegea muda nitakaobaki na mama pekee ndipo nitamueleza kuhusu zile sauti za wanawake na pia juu ya kupokelewa pale nyumbani kwa babu na yule mwanamke ambaye alikuwa shuleni kama mwalimu akanichapa kiboko kilichoniletea kizaazaa.
Mwanamke yuleyule ambaye mama yangu alimshutumu kuwa alimuua baba yangu.
Tulitembea hadi nyumbani kwa babu tukisindikizwa na baadhi ya wanakijiji huku wakiizungumzia hali iliyomkuta mama kuwa si yeye wa kwanza kutokewa na hali ile jambo la msingi wakamsihi sana kuwa ajitahidi ajilinde, sikuelewa ni kitu gani wanamaanisha hadi ukubwa huu ndo naelewa nini maana yake.
Mama alizungumza na babu kwa kirefu baada ya kufika kisha akaniita na mimi na kuniomba nimuelezee babu kila kitu kama nilivyomueleza yeye hapo awali. Nikajieleza kwa babu kila nilichokuwa nakumbuka. Safari hii sasa hata zile sauti zilizonijia masikioni wakati mama anapigania uhai wake nilisimulia.
Babu alikuwa mtulivu sana katika kutusikiliza, na ni kama aliyeonekana kujua mambo mengi sana ama la! Basi lile halikuwa jambo geni sana kwake.
Babu alitusihi sana tusilale hapo kijijini bali tumwachie yeye kazi ya kutazama hilo tatizo linasababishwa na nini. Alimwambia mama kuwa tatizo lililopo lazima litakuwa kubwa na anayelileta tatizo hilo amejipanga vyema katika mashambulizi.
Mama alitii alichoshauri babu, tukaondoka kurejea nyumbani.
Tulifika tukiwa tumeanza kuyasahau mambo kadha wa kadha yaliyotutokea tukiwa kule kijijini.
Tukala chakula na kisha kila mmoja akiwa amechoka kwa kiwngo chake, akaingia kupumzika.
Ni mimi ndiye niliamka kama nilivyokuwa siku iliyopita lakini mama aliamka ule mguu wake sasa ukiwa umevimba maradufu, ulikuwa umekuwa wa kijani huku misuli ikiwa inaonekana kusisimka sana yaani alitisha kumtazama.
Hiki nini? Tulijiuliza mimi na ndugu zangu. Mama aliyelala akiwa salama kabisa, anaamka akiwa katika namna hii ya kutisha.
Mama alikuwa hawezi kuongea bali alikuwa akitokwa na povu tu mdomoni, tulilia sana familia nzima hadi majirani wakajaa pale na kufanikiwa kumpeleka mama hospitali.
Hospitali walijaribu kupambana mguu ule uweze kutulia lakini ule uvimbe na ukijani ukazidi kutambaa kuelekea juu ya goti.
Ushauri wa haraka ukatolewa, ili kunusuru maisha ya mama basi mguu ule unatakiwa ukatwe.
Akaagizwa mtoto mmoja aweze kuzungumza na mama juu ya jambo hili. Weakati wengine wakijiuliza ni nani aende.
Nikajichagua mimi na kwenda moja kwa moja katika chumba alichokuwa amelazwa mama. Sindano ya kupunguza maumivu aliyokuwa amedungwa ilikuwa imesaidia sana. Aliweza kuongea japokuwa kwa tabu.
Nilimweleza mama juu ya shauri la daktari. Akanishika mkono wangu huku akiwa ananitazama.
“Ngomeni!” aliniita na kisha kuzungumza kwqa kabila letu, kabla hajaanza kuzungumza kiswahili.
Uso wake ukiwa na kitu kinachofanania na tabasamu.
“Jana uliona nilivyokuwa natembea?”
“Nilikuona mama.” Nilimjibu nisijue anataka kusema nini zaidi.
“Utanisaidia kuwasimulia wajukuu zangu kuwa mama aliwahi kuwa na miguu yake yote miwili. Alikubeba wewe mgongoni pamoja na wadogo zako, aliwatafutia chakula na aliwapenda sana.” Mama alizungumza huku ule mfano wa tabasamu bado ukiwa usoni pake.
“Nguvu za giza kamwe hazijawahi kupata ushindi wa kudumu katika vita yoyote ile. Ushindi wao siku zote ni batili. Nikikatwa huu mguu na nisiamke tena, tambua kuwa mimi ni mshindi. Nawe uwe mshindi siku zote, najua hawataishia kwangu tu. Watakuja tena kwako… hakikisha unawashinda kwa ajili yangu. Usiwaache wakushinde kwa sababu hawajawahi kuwa washindi. Kamwambie kaka yako atie saini wanikate tu huu mguu, napatwa na maumivu makali sana!” mama alimaliza kuzungumza, akauachia mkono wangu.
Niliondoka pale nikiwa tayari na picha ya kuwa baada ya masaa kadhaa mama yangu atakuwa hana mguu mmoja.
Niliumia sana lakini sikuwa na lolote ambalo ningeweza kufanya juu ya lililojiri.
Naam! Mama akahamishiwa chumba cha upasuaji.
Ilichukua masaa mawili kabla kaka yangu ambaye awali aliweka sahihi yake juu ya upasuaji huo kuitwa katika chumba cha daktari.
Yeye hakuchukua muda mrefu sana kabla hajarejea na taarifa ya msiba!
Mama alipoteza maisha katika chumba cha upasuaji. Ni maajabu tupu yaliyojiri huko lakini yote yaligota katika hitimisho la mama kupoteza maisha.
Mimi niliyeyashuhudia mengi nilibaki na chuki kubwa sana juu ya wanadamu.
Ndani ya kipindi kifupi sana tukageuka kuwa yatima.
Lakini hiyo bado ilikuwa haitoshi.
Ni kama mambo yale yaliisha, tukabaki kutangatanga na dunia, leo kwa mjomba kesho kwa ma’mkubwa.
Mwaka mmoja ukazaa mwingine, msoto ukazoeleka.
Ikawa miaka, na mabalaa yakamaliza likizo yao na kurejea tena kuweka kambi.
Sasa ikawa ni vita yangu!
Tafadhali nakusihi unisikilize kwa umakini neno kwa neno huenda haya yaliyonikuta mimi na wewe yanakutokea bila kujua.
_________________
Nilipofikisha umri wa miaka kumi na tisa nikiwa kijana ambaye sikupata elimu kubwa zaidi ya kuishia kidato cha nne na kuanza kujishughulisha mwenyewe nilikutana na msichana ambaye nilisoma naye shule moja hadi kidato cha nne. Wakati tupo shuleni dada huyu aliyeitwa Jasmin alikuwa kama dada yangu kwani alinizidi umri na umbo vilevile, lakini baada ya miaka kuwa imepita nikiwa nimekutana na suluba mtaani katika utafutaji wa maisha nikiwa kiokote nilikutana naye. Sasa mwili wangu haukuwa mdogo tena bali kipande cha mtu.
Siku ya kwanza tulikumbushiana mambo mengi sana ya kishuleshule….. ikawa hivyo mara kadhaa za kukutana.
Lakini ukaribu ule ulivyozidi kama ilivyo ada! Tukajikuta tukiangukia penzini.
Jasmine alikuwa akifanya kazi kwa muda katika ofisi moja ya kupokea na kusafirisha mizigo, huku mimi nikiwa ni mtu wa kushika lolote linalokuja mbele yangu likiwa halali. Ilimradi kuingiza chochote mfukoni.
Nilikuwa si maskini wa kutupwa na hii ni kutokana na utafutaji wangu katika juhudi kubwa.
Nilikuwa nimepanga chumba kimoja huku nikiwa namsomesha mdogo wangu!!
Alikuwa yu kidato cha sita wakati huo!!
Mapenzi yetu yalianza kama utani, mara anitanie kuwa mimi ni mdogo wake, mara siku nyingine ananilazimisha nimsalimie.
Ilianza hivyo, hadi siku tuliyojikuta tukishindwa kuzizuia nafsi zetu kuutangaza ukweli uliokuwa ukijifichaficha!!
Haya yalikuwa mahusiano yangu ya kwanza kabisa katika maisha yangu ambayo nilijikuta nikiyapa uzito mkubwa kabisa.
Kabla ya kukutana faragha yoyote na Jasmin tuliendelea kuonana sehemu za wazi nikamweleza Jasmini juu ya maisha kiujumla na ugumu wake, nikamsihi afanye kazi kwa bidii sana ili hatimaye aje kuwa na maisha bora hata kama hatakuwa katika mahusianio na mimi.
Zaidi ya mwezi mzima ulipita pasi kukutana na Jasmini faragha. Sikuwahi kujali juu ya hilo.
Hadi ilipofika siku aliyoomba sana aje nyumbani kwangu kunisaidia kufua nguo, hapo nilikuwa nimelalamika kuwa nina nguo nyingi sana za kufua na sijisikii vizuri kiafya.
Ile siku ya kwanza kumkaribisha Jasmin nyumbani kwangu ndipo nilikuwa nimelikaribisha balaa kubwa kupita lile balaa ambalo nilikuwa nimelisahau miaka kadhaa nyuma wakati nikiwa mdogo.
Ni hapa nilipokiri kuwa hakika wanadamu tunafanana nyuso lakini mioyo yetu imebeba fumbo zito kubwa sana.
ILE SIKU ilianza vizuri kabisa, asubuhi majira ya saa tano hivi tayari Jasmin alikuwa nyumbani kwangu, ilikuwa ni chumba kimoja nilichoishi lakini kwa sababu kilikuwa kikubwa kwa kiasi cha kutosha nilikigawanya kwa kutumia pazia hivyo kuwa kama chumba na sebule.
Kujituma kwangu kulizaa matunda yaliyokuwa yakionekana wazi…. nilikuwa nina samani za kukidhi haja za kile chumba.
Jasmine alipoingia alinisifia sana, kisha moja kwa moja akaingia kufanya kile kilichokuwa kimemleta pale nyumbani, akatoa kanga katika mkoba wake akavua nguo alizokuja amevaa akajivika kanga na kuingia katika zoezi la kufua.
Alianza na nguo nyeupe akazifua wakati huo akinisihi mimi niende sokoni kuhemea mahitaji ili aweze kunipikia pindi atakapomaliza kufua.
Nilisuasua sana kuondoka nikawa naingiza mada nyingine lakini baada ya mada niliyoizalisha kumalizika alinisihi tena kuwa niende sokoni kwanza.
Hatimaye nikaondoka, nilianzia buchani kisha nikaingia sokoni nikahemea mahitaji yote ya msingi.
Uzuri ni kwamba japokuwa sikuwa na utaratibu wa kupika pale nyumbani lakini nilikuwa nina vyombo vyote vya ndani.
Wakati narejea mapigo yangu ya moyo yalikuwa yanaenda kasi sana kana kwamba kuna kitu kimenitokea. Nilijishangaa kwa muda kisha nikatabasamu. Nikapuuzia mabadiliko yale katika mwili wangu.
Nilitembea hadi katika kona moja hivi ambayo baada ya hapo unakuwa umefika katika kibanda changu ninachoishi. Nikasikia kama sauti ikiita jina langu, ilikuwa sauti ya kike.
Unaweza ukaniuliza ni kwa nini nilihisi ni mimi ninayeitwa wakati kuna uwezekano wa kufanana majina.
Kilichoniweka katika hali ile ni kwamba jina Ngomeni lilikuwa jina langu peke yangu pale mtaani. Lilikuwa ni jina la ukoo, na yeyote ambaye angeitwa jina lile basi alikuwa na nasaba na mimi.
Niligeuka na kutazama nyuma lakini sikuona mtu yeyote akijishughulisha na mimi. Nikaamini kuwa niliwaza tu, haukuwa uhalisia.
Nikaendelea mbele kidogo, mara ikanikumba hali fulani hivi ambayo iliwahi kunikumba enzi za utoto wangu. Mwili wangu ulikumbwa na joto kali. Joto lililodumu kwa sekunde chache tu.
Yaani ni kama niliyepishana na jiko linalowaka moto.
Nakumbuka enzi hizo nilipokumbwa na hali hii mama yangu aliniuliza kisha likatokea jambo ba yasana mama akachomwa na mwiba uliosababisha purukushani ya aina yake na hadi anakata roho alidai kuwa alikufa ile siku alipochomwa na ule mwiba wa ajabu.
Na hapo hapo nikakikumbuka kitabu cha simulizi kiitwacho mama yangu anakula nyama za watu kilichoandikwa na mtunzi Irene Ndauka. katika kitabu hiki kuna ukurasa mmoja unazungumzia juu ya hii hali ya kukumbwa na joto ghafla. Sasa nilikuwa mimi katika kuhakiki.
Ndugu msikilizaji ukijikuta katika hali hii basi yumkini kuna mchawi ambaye ametanua miguu yake na kupita juu yako hii ikiwa ni dalili mbaya kabisa ya kukuzulia tatizo. Hivyo kama imewahi kukutokea hali hii basi ulikuwa unapita chini ya miguu ya mchawi.
Hii hutokea pia kitandani, ukihisi joto la ghafla basi haujalala peke yako!
Kama una imani thabiti, inuka fanya dua.
Mungu wetu kamwe huwa halali.
Nilipounganisha matukio hayo nikapatwa na hofu na hapa sasa nikatambua kuwa moyo wangu ulikuwa unapiga kwa kasi sana kwa sababu ya hali ile.
Niliongeza mwendo hadi nikaikaribia nyumba niliyokuwa naishi, kwa mbali kabisa nilitazama pale alipokuwa Jasmini akifua nguo, hakuwepo lakini vyombo vya kufulia vyote vilikuwepo.
“Au ameenda kuanika nguo huyu?” nilijiuliza huku miguu yangu ikiwa mizito sana kutembea. Hofu ya kukutana na mchawi ilikuwa imetanda.
Nilipiga hatua mbili zaidi kisha nikaliita jina la binti yule mara mbili, kimyaa!!
Hakuna alichojibu.
Nikakitua kile kikapu chini, nikajivuta hatua nyingine sasa nikaufikia mlango nikawa kama ninayechungulia ndani, nikamuita tena Jasmini.
Safari hii aliitika kutokea ule upande wa pili wa chumba changu niliotenganisha kwa pazia.
Uuuh! Moyo ukapata nafuu, Jasmin alikuwepo.
“Una nini mbona upo ndani?” nilimuuliza hapo nikiwa nimepiga hatua nyingine mbele. Nikijilazimisha kuwa katika hali ya kawaida.
“Tumboooo… Tumbo linaniuma” niliisikia sauti yake ikijibu kwa tabu sana.
Alipolalamika vile nilisahau kuhusu ule uoga nikaingia ndani. Nikafunua upande wa pili na kuingia, alikuwa Jasmin amelalia tumbo.
Nikafika na kumgusa taratibu huku nikimsihi kuwa niende kumnunulia dawa!
Hakunijibu badala yake alikuwa anakema tu!!
“We Jasmin.. nikakununulie dawa ipi.. au sio tumbo la kawaida?” nilizidi kumuhoji huku nikimtikisa kwa utaratibu.
Mara ghafla Jasmin aligeuka kwa nguvu sana, ile naushangaa ule mgeuko wake mara ghafla nikashtukia nikiwa nimenaswa kibao kikali sana.
Lahaula! Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nilikuwa nakutana na mauzauza ya waziwazi huku macho yangu yakishuhudia mchana kweupe.
Hakuwa Jasmini bali ni kibibi kizee katika mavazi ya Jasmini.
Sura yake ilikuwa imefanya makunyanzi yaliyokuwa yanadhihirisha kuwa alikuwa amekula chumvi nyingi.
Alipozungumza neno la kwanza nikakiona kinywa kisichokuwa na jino hata moja ndani yake.
“Unataka nife mara ngapi ndio uje?” aliniuliza kwa sauti imara kabisa tofauti na sura yake.
Swali lake sikulielewa kabisa….. akabaki kunitazama huku akihema juu juu.
“Nakuuliza wewe kiumbe!!” alikoroma sasa allipiga hatua kunisogelea.
Nilitetemeka sana huku nikilia kama mtoto na kamwe sauti isitoke.
“Nisamehe…nisamehe” nilijikuta naomba msamaha usiokuwepo. Yaani niliomba msamaha bila kujua hata ni kosa gani nilikuwa nimefanya lililostahili mimi kuomba huo msamaha.
Kiumbe yule wa ajabu hakunijibu lolote alinifikia na kisha akainama akanipa mkono wake, nilisita kuushika.
Kwa kufanya vile akanizaba kofi kali sana usoni!! Na wakati naugulia maumivu akanisimamisha wima.
Alikuwa na nguvu jama!
“Naondoka nikirejea tena ni aidha tunaenda kwa lazima… ama la nitakufanya kitu kibaya ambacho hujawahi kufanyiwa maishani.
Alipomaliza kusema vile akanipuliza, nikausikia mwili wangu ukiwa unaishiwa nguvu nilijaribu kujizuia lakini haikuwezekana nikajikuta natua chini kama mzigo, ile naugua pale chini nikasikia kama upepo mdogo ukivuma na kisha kutoweka.
Nilibaki kujivutavuta pale chini, sikuwa na cha kufanya nilikuwa natokwa jasho.
Nikiwa vilevile nilisikia sauti ya Jasmini ikiiniita nje. Iliita kama mara tatu mimi nikiwa kimya tu, hakuna kitu kingine nilichokuwa nawaza zaidi ya yale maluweluwe yaliyonitokea.
Baada ya kama sekunde kumi hivi, mara mlango ukafunguliwa. Mawazo yangu yakiwa bado hayajafikiria kitu kinachoitwa maamuzi, yuel aliyeufungua akapiga hatua moja mbele, nikaiona ile nguo ya Jasmine ambayo baadaye niliiona ikiwa imevaliwa na kiumbe yule wa ajabu kabisa.
Aliyeufungua akapiga hatua ya pili, mimi bado nilikuwa pale pale chini. Mkojo ukiwa umejiamria wenyewe kutoka na kulowanisha nguo yangu.
Nilikuwa naogopa mno! Haya mambo hadithiwa tu kama hivi. Ni mazito
“Ngomeni wewe… umerudi saa ngapi…. hee! Mbona umelala hapo chini sasa? We ngomeni mbona jasho linakutoka hivyo!!” ilikuwa ni sauti ya Jasmini na sura ya Jasmini ikinihoji vile.
Alipojaribu kunisogelea mimi nilirudi nyuma kwa kutambaa huku nikimsihi anisamehe, yaani sikuamini kabisa kuwa yule ni Jasmini.
Nilimuogopa kupita kawaida.
“We Ngome wewe una nini lakini? Alizidi kushangaa..
“Ulienda wapi?” nilimuuliza.
“Nilienda kuanika nguo kule uliponielekeza vipi kwani?”
“Aliyeingia humu ndani unamjua??” nilimuuliza huku nikiwa pale chini hofu ikiwa imetawala.
“Ngomeni yaani hizo dakika mbili za kuanika nguo usitake kunambia eti tumevamiwa?” alinijibu kwa mshangao mkubwa sana.
“Jasmini… we Jasmini unanipenda kweli!” nilimuuliza, kwa kuropoka. Sikujua hata mantiki ya swali langu.
Hapo sasa akanisogelea huku akipiga goti, nikajisogeza nyuma zaidi hadi nikafikia kitanda, hapo sasa sikuweza kurudi nyuma zaidi.
“Nimekukosea nini Jasmini eeh! Nimekukosea nini nisamehe kama kuna baya nimekufanyia, Jasmini mimi sina baba wala mama, nina mdogo wangu namsomesha naomba uniache kama kuna lolote nimekukosea nisamehe… baba yangu na mama yangu si wametosha au?” nilimuuliza huku natetemeka.
Wakati nazungumza haya nikakumbuka kuwa chini ya uvungu wangu kuna panga huwa nalihifadhi hapo kwa sababu za kiusalama.
Nilichowaza kwa kipindi kile ni kupambana na kiumbe huyu aliyepo mbele yangu, kama mama alivyonieleza kabla hajafariki kuwa jisaidie na Mungu atakusaidia.
Nikapapasa na hatimaywe nikalishika vyema lile panga.
Wakati nimelishika vizuri Jasmini naye akazidi kunisogelea huku akitembea kwa kutumia magoti yake.
Kitendo cha kutembea kwa kutumia magoti kikanifanya nizidi kumuogopa na hapo nikakusudia kumfyeka.
Liwalo na liwe!!!
BONASI: Kama kawaida kwa wasomaji wenye ari shirikishi… LIKE, COMMENT bila kusahau muhimu kabisa SHARE simulizi hii. Nami nitakutembelea inbox na sehemu inayofuata ya simulizi hii.
Fisi yule akaondoka kwa utulivu kabisa akamfukuza fisi aliyekuwa amemdhibiti yule kijana, na mara akamrukia na ndani ya nukta moja yule kijana alikuwa anatokwa na kilio kikubwa sana huku fisi akitafuna sikio lake la mkono wa kuume.
Ilitisha sana kutazama!!
Niliusikia mkojo ulipokuwa unanitoka lakini sikuweza kuuzuia hata kidogo.
Nilijua kuwa baada ya kijana yule kupewa onyo kwa kukatwa sikio na kisha sikio kutafunwa na fisi ilikuwa inafuata zamu yangu!
Mkojo ulimwagika hadi ukamalizika lakini haukusaidia kuipunguza hofu iliyokuwa inanikabili.
“Ngomeni tunaenda ama nikuache na huyu fisi?” aliniuliza kikongwe yule huku akiyaacha mapengo yake yaonekane waziwazi. Na hakurudia swali lake bali alinikazia macho yake makali, ni kama macho yap aka mwenye hasira.
Nilijiuliza kidogo tu kuwa yule mwenzangu amekwanguliwa sikio lake na nimeshuhudia kwa macho yangu fisi akilitafuna na kulimeza, kile kilio chake cha uchungu hata nisingekisia bado ningeweza kuukadiria uchungu mkubwa aliopitia.
Mimi je?
Nikakubali upesiupesi kuwa nipo tayari kwenda bila kujua ni wapi ambapo ninapelekwa.
Yule bibi alicheka sana kwa sauti ya juu, kinywa chake kisichokuwa na meno kikiendelea kufanya dhihaka. Na mara nikazisikia ngurumo mithiri ya dalili ya mvua.
Kisha zikatoweka na yeye akaacha kucheka halafu akaniuliza.
“Unataka uende kwa usafiri gani, huu hapa ama unahitaji usafiri mwingine. Nikuagizie” aliniuliza akimaanisha kupanda katika mojawapo ya fisi kama yeye alivyokuwa amepanda.
Nilikataa kata kata kuwa siwezi kupanda juu ya fisi, akasikitika kisha akaniambia kuwa nisijali jambo lolote nitaenda kwa usafiri mwingine.
Ndugu msikilizaji tega sikio lako kwa makini zaidi katika kulisikiliza hili kisha umshike Mungu wako kwa nguvu zote.
Tambua kuwa hakuna mchawi mwenye nguvu kuzipita zile nguvu za mwenyezi Mungu lakini hii huja panapo imani, ukiwa na imani dhaifu kama niliyokuwanayo mimi basi bila shaka lolote lile huwezi kuwazuia wala kuwatetemesha viumbe hawa. Wachawi hawa wana uwezo wa kutikisa nyumba za viongozi wa kiroho na kuwatoa jasho.
Siwezi kusema wao wana imani kali sana. Lakini abadani! Imani za wengi ni dhaifu zaidi.
Baada ya kuwa ameniambia kuwa nitaenda kwa usafiri wowote ninaouhitaji zile ngurumo zikarejea tena, sasa anga ilibadilika na kuwa kiza kinene, fisi walitoweka kwa kasi wakatuacha tukiwa peke yetu yaani mimi pamoja na kile kikongwe, kikongwe kisichokuwa na meno kinywani.
Mara ikawa mvua, kadri mvua ilivyokuwa inanyesha ndipo nikagundua kuwa maji yaliyokuwa yanamwagika, kwanza hayakuwa maji ya kawaida na pili yalikuwa maji yaliyokuwa na rangi mithiri ya damu na yalipomwagika hayakuzama ardhini bali yalijaa kuja juu. Ni kama kwa muda ule ardhi ilikuwa imetiwa saruji. Wakati haya yote yanatokea kikongwe yule alikuwa anacheka tu na kunifanya nione kero kubwa sana. Sauti yake ilikuwa inakwaruza kama mtu ambaye baada ya dakika kadhaa hataweza kusema tena.
Lakini huyu aliendelea kucheka.
ITAENDELEA
Mama’ke Mama Sehemu ya Nne
Also, read other stories from SIMULIZI;