Dimbwi la Damu Sehemu ya Kwanza
MAISHA

Ep 01: Dimbwi la Damu

SIMULIZI Dimbwi la Damu
Dimbwi la Damu Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA: ERIC SHIGONGO

*********************************************************************************

Simulizi: Dimbwi La Damu

Sehemu ya Kwanza (1)

Ilikuwa ni siku ya jumapili mjini Arusha, mawingu yalitanda kila mahali angani na manyunyu yalikuwepo kiasi cha kuwafanya watu wavae makoti, ilikuwa si kawaida ya mji wa Arusha katika kipindi hicho cha mwaka kuwa na baridi.

Jioni ya siku hiyo kulikuwa na kila aina ya furaha nyumbani kwa Martin na mkewe Hoyce! Shangwe na vigelegele vilitawala, watoto wengi kutoka nyumba za jirani walialikwa! Ilikuwa ni sikukuu ya kuzaliwa kwa watoto wao wawili mapacha, Victoria au Vicky na Nicholaus au Nicky kama walivyoitwa na wazazi wao!

Walikuwa watoto wawili mapacha waliofanana kupita kiasi kama ungekuta wote wamevalishwa magauni usingesita kusema walikuwa ni watoto wa kike! Walikuwa ni watoto wazuri na wenye afya njema! Walimvutia karibu kila mtu aliyewaona.

Martin, alikuwa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite aliyemiliki kampuni kubwa ya uchimbaji wa madini iliyoitwa Tanzamine Limited ambayo makao yake makuu yalikuwa mjini Arusha. Ilikuwa ni kampuni kubwa kuliko zote Afrika ya Mashariki, katika umri wake umri wa miaka 26 Martin alitisha kwa utajiri wake! Alihesabika kuwa kijana tajiri kuliko wote nchini Tanzania na hata Afrika ya Mashariki

Ilikuwa si rahisi kukadiria kiasi cha fedha alichopata kutokana na biashara yake, aliuza madini yake katika nchi ya Bangladesh, Singapore, Ufaransa na Marekani, alikuwa ni mtu mwenye kazi nyingi kupita kiasi na alisafiri katika nchi 26 duniani kila mwezi akikaa na familia yake kwa muda wa siku nne tu katika mwezi.

Yeye na mke wake Hoyce walioana miaka mitatu kabla na walikutana kwa mara ya kwanza ndani ya ndege, Martin akisafiri kutoka Uingereza kibiashara na Hoyce akitoka masomoni Uingereza, walijikuta wamekaa kiti kimoja ndani ya ndege hiyo ya shirika la ndege la Uingereza, British Airways! Kabla ya kupanda ndege Martin alimwona Hoyce akikumbatiana na mvulana wa kizungu.

Baada ya kukutana moyo wa kila mmoja wao ulikwenda mbio na damu iliwatembea kwa kasi ya ajabu, pamoja na hali hiyo hakuna aliyetaka kumuonyesha mwenzake waziwazi hisia zilizokuwemo moyoni mwake, kila mmoja alijitahidi kuficha hisia zake lakini jambo hilo halikuwezekana kwa Martin kwani walipofika Muscat, Martin alilazimika kueleza ukweli wake.

“Yule mwanaume wa kizungu niliyekuona ukiongea nae uwanja wa ndege ni nani?”

“Ni boyfriend wangu!”

“Aisee! Anaitwa nani?”

“Anaitwa Richard Ford!”

“Ford? Ni mtoto wa yule tajiri au?”

“Hapana ni mjukuu wake!”

“Inaonekana unampenda au siyo?”

“Sana na tuna mpango wa kufunga ndoa!”

“Inamaana utarudi tena Uingereza?”

“Hapana ila yeye atakuja Tanzania mwezi Novemba na tutafunga ndoa nyumbani!” alisema msichana huyo bila kujua ni kwa kiasi gani aliuumiza moyo wa Martin! Katika maisha yake Martin alishaona wasichana wengi wazuri lakini hawakuwa kama msichana aliyekaa nae kiti kimoja ndani ya ndege hiyo, lilikuwa si jambo la ajabu kumfananisha na Malaika aliowaona katika michoro ya hadithi za Biblia.

“Unajidanganya! Utakuwa wangu tu utake usitake, huyo mzungu wako utaachana nae ili mradi nimekupenda!” alijisemea Martin moyoni mwake huku akimwangalia msichana huyo kupita kona ya kushoto ya jicho lake!

Kwa uwezo aliokuwa nao kifedha Martin alikuwa na uhakika wa kumteka tena msichana huyo na kumfanya wake! Hiyo kwake haikuwa kazi ngumu.

Martin alizaliwa Agosti 12,1969 hivyo nyota yake ilikuwa ni Simba, watu wa nyota hii inaaminika wana uwezo mkubwa wa kushawishi na ni wapendaji wazuri, wakimpenda mwanamke humpenda kikweli kweli na mwanamke huyo hujisikia Malkia, lakini kasoro yao ni wivu! Wana wivu kupindukia, wengi wanaume ambao hujinyonga au kuua sababu ya mapenzi ni waliozaliwa kati ya Julai 21 hadi Agosti 21.

Sifa zote za watu wenye nyota ya Simba alikuwa nazo Martin! Alikuwa si mtu wa kumwacha akiongea na mtu aliyegoma kufanya kitu fulani kwa hata dakika kumi asibadili msimamo wake! Sifa hiyo pamoja na pesa nyingi alizokuwa nazo tena katika umri mdogo zilimpa Martin kiburi cha kumchukua msichana yoyote yule aliyemtaka.

“Huyu nikimwingia kwa mkwara wa pesa sitampata, ni lazima nijifanye sina kitu lakini baadaye mambo yatakuwa sawa!”Aliwaza Martin.

“Ulikuja London kufanya nini?”

“Mimi?”

“Ndiyo!”

“Nilikuja kwa matembezi na hivi sasa narudi nyumbani!”

“Unafanya kazi gani Tanzania?”

“Ah! Ah! Sina kazi ila dada yangu anaishi hapa London na aliniita ili anitafutie kibarua lakini imeshindikana na ameamua kunirudisha nyumbani!” Martin alificha ukweli.

Mara nyingi alipowaambia wasichana ukweli juu ya utajiri aliokuwa nao hata wasiompenda walijifanya kumpenda ili wawe naye na kutumia utajiri wake.

“Pole sana.”

“Ahsante wewe je ulikuwa ukifanya nini London?” Martin aliuliza.

“Mimi nilikuwa nachukua Shahada ya Pili ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Oxford na sasa narudi nyumbani kwetu Tanzania!”

“Hongera! Kwa hiyo umemaliza masomo yako?”

‘Ndiyo!” aliitikia msichana huyo huku akitabasamu, ni tabasamu hilo ndilo lililozidi kuyapeleka kasi mapigo yake ya moyo wa Martin alishindwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa kinataka kumtokea katika maisha yake, lilikuwa ni penzi lililokuwa likija kwa kasi ya ajabu.

Hoyce alikuwa ni msichana mrefu, mwembamba na mwenye ngozi nyororo ya maji ya kunde, nywele zake zilikatwa na kuwa fupi, hali iliyomfanya aonekane kuwa na muonekano wa Kiafrika haswa.

“Unafanana sana na mwanamitindo Alek Wek.”

“Ndiyo na watu wengi sana husema hivyo lakini si kweli kwa sababu Alek ni mweusi zaidi halafu hana mwanya kama nilionao mimi!”

“Una mwanya?” Martin aliuliza kwa mshangao.

Hakuna kitu kilichomchanganya akili Martin ndani ya mwanamke kama nafasi iliyokuwepo kati ya meno mawili ya mbele! Wanaume wengi duniani walivutiwa na maumbile lakini kwa Martin ilikuwa tofauti kwani kila alipoona mwanya wa mwanamke alihisi umeme ukipita katikati ya mgongo wake.

Alipenda sana wanawake wenye mwanya kiasi cha kushindwa kutofautisha kati ya mwanamke mwenye mwanya na mwenye pengo, rafiki yake wa mwisho kimapenzi, Lightness waliyeachana nae baada ya kumfuma akifanya mapenzi na rafiki yake mpendwa hakuwa na mwanya hilo lilimfanya Martin alazimike kumpeleka kwa daktari bingwa wa meno na kuchonga mwanya wa bandia.

Taarifa kuwa msichana huyo alikuwa na mwanya zilizidi kumchanganya akili Martin, alitamani sana kumwambia akenue lakini aliona taabu kwa sababu hakumzoea, alijitahidi kumchekesha ili akenue na kuonyesha mwanya wake lakini msichana huyo alicheka kizungu bila kufungua mdomo! Roho ya Martin ilizidi kuumia.

“Ulisema unatiwa nini vile?”

“Naitwa Hoyce!”

“Aha! Na yule boyfriend wako anaitwa nani?”

”Richard!”

“Kwa hiyo siku hiyo itakuwa Richard to Hoyce au siyo?”

“Aaaa sanaa! Nitakupa kadi uhudhurie harusi yetu kama utaweza!” Aliongea Hoyce akionyesha furaha ya ajabu.

“Utamwacha tu!” aliwaza Martin kichwani mwake

Ndege British Airways kutoka London ilitua katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam saa kumi na moja jioni na abiria wote waliteremka na kuanza kutembea kuelekea nje ya uwanja ambako wenyeji wao waliwasubiri.

“Hoyce ulisema unaishi wapi kweli?”

“Naishi Masaki ambako kuna nyumba yetu ila wazazi wangu wanaishi Himo, Marangu Moshi!”

“Kwa hiyo kuna watu watakuja kukupokea siyo?”

‘Nafikiri hivyo kwa sababu wana taarifa za ujio wangu!”

“Sawa lakini kama ukitaka kuwasiliana na mimi utanipigia simu kwa namba zilizoandikwa kwenye kadi hii! Mungu akubariki sana Hoyce ahsante kwa kampani yako nzuri, nimefurahi sana kusafiri na wewe!”

Hoyce hakujibu kitu macho yake yalikuwa bado yapo juu ya kadi aliyopewa, alionekana kutoamini alichokisoma katika kadi hiyo! Alianza kurudia tena na tena kuisoma kadi hiyo Martin akiwa amesimama pembeni yake.

“Managing Director,

Martin Assets Limited! Martin Tours Limited, Martin Transporters Limited, Tanzamine Limited, Martin pipelines limited. Zote hizi ni kampuni zake?” Alisoma na kujiuliza Hoyce.

Aliponyanyua macho kumwangalia Martin alikuta vijana kama watano hivi wakinyanyua mabegi yake yote na mwingine akichukua koti lililokuwa mkononi mwa Martin, aliyekuja mwisho alikuja na mwavuli akaufungua na kumfunika Martin kwa juu ili asichomwe na jua! Yote haya yalimshangaza Hoyce, alishindwa kuamini kama mtu aliyekwenda Uingereza kutafutiwa kazi angeweza kupokelewa namna hiyo.

Alibaki mdomo wazi bila kupata jibu la maswali yaliyoendelea kichwani mwake! Aligundua waziwazi kuwa alikuwa amedanganywa na Martin! Baada ya fikra za muda wa dakika mbili alimkumbuka Martin, alishasikia habari akiwa nchini Uingereza, watu walimwongelea kama Mtanzania kijana aliyepata mafanikio.

Mara nyingi sana aliitembelea tovuti yake na kuona shughuli alizozifanya kijana huyo, kweli alikuwa ni kijana mdogo mwenye mafanikio makubwa! Lakini Hoyce hakuwahi hata siku moja kufikiri angeweza kukutana naye ana kwa ana na hata kuongea naye.

“Hivi kweli wewe ndiye Martin?” aliuliza Hoyce akionyesha kutoamini.

“Hapana Martin ni kaka yangu!” alificha.

“Siyo kweli ni wewe acha utani basi!” alisema Hoyce huku akionyesha msisitizo.

“Ok! Ni mimi!”

“Sasa kwanini ulinificha tangu tuondoke London?”

“Kwa sababu huwa sipendi sana kujulikana!”

“Mh!” Hoyce aliguna.

“Ahsante Hoyce kwa kusafiri na mimi tafadhali nipigie simu!” alisema Martin na baadaye kuanza kutembea kuelekea mahali gari lililokuja kumpokea lilipoegeshwa, mlango ulifunguliwa na kijana mwingine na Martin aliingia ndani bila kugusa mahali popote, Hoyce alibaki akishangaa! Alishindwa kuelewa Martin alikuwa kijana wa aina gani kwani kwa kijana wa kawaida lazima angetamba na kujisifu kwa mali alizonazo ili kumshawishi yeye amkubali kimapenzi.

Martin aliishi Arusha hivyo baada ya kupokelewa kwa gari lake mwenyewe alisafiri kwa muda wa masaa matano na kuingia mjini Arusha usiku, katika muda huo tayari alishapokea simu za Hoyce kumi na tano! Kwa vitendo hivyo tayari alishaelewa kuwa mtoto alishaanza kupagawa kama ilivyokuwa kawaida ya Martin kuwapagawisha watoto wa watu.

“Watoto wa kike bwana yaani tayari keshalewa penzi! Wakati aliniambia anampenda sana mpenzi wake wa Uingereza, hawa viumbe ni dhaifu sana, nafikiri mtoto mwenyewe hajatulia!” Aliwaza Martin akimsagia Hoyce.

Hivyo ndivyo walivyoanza na mawasiliano kati yao hayakukomea siku hiyo kwani baadaye yaligeuka kuwa penzi zito lililopelekea wao kufunga ndoa miezi sita tu baada ya kukutana na kuwa mke na mume! Richard Ford alipokuja nchini kumtembelea Hoyce alikuta tayari amekwishaolewa alilia machozi kwa uchungu na kuahidi kulipa kisasi.

“I will kill them in a bad accident let me go back home once I come back they will know my name!”(Nitawaua katika ajali mbaya sana, acha nirudi nyumbani nikirudi watalijua jina langu!) alisema Richard kwa hasira akiwa amedhamiria kuua.


Mwaka mmoja baada ya ndoa yao walijaliwa kupata watoto wawili mapacha wa kike aliitwa Victoria na wa kiume aliitwa Nicholaus! Walikuwa watoto wazuri sana waliowaunganisha Hoyce na Martin zaidi, waliishi maeneo ya Uzunguni mjini Arusha na biashara za Martin zilizidi kukua, safari zake za nje ya nchi ziliongezeka maradufu mpaka akalazimika kuwa na ofisi katika nchi za Uswiss, Ufaransa na Ubeligiji, ambako aliajiri Wazungu kumfanyia kazi kama wawakilishi waliopokea madini yake na kuyauza.


Sikukuu ya miaka 5 ya kuzaliwa Nicholaus na Victoria:

Siku hiyo ya jumapili Agosti 16, ilikuwa ni kati ya siku nne ambazo Martin alikuwa nchini Tanzania kupumzika na familia yake, akiwa nchini nchini ilikuwa ni lazima afanye tafrija yoyote na familia yake!Siku hiyo ilikuwa ni siku ya sikukuu ya kuzaliwa kwao! Watu wengi walifurika nyumbani kwao kusherehekea sikukuu hiyo.

“Mama wawili bado kitu gani au kila kitu kimekamilika?”

‘Kila kitu tayari ila bado keki tu!”

“Sasa tufanyaje?”

“Labda tuifuate pale best bites niliweka oda yangu na nikalipia nusu, wale ni mabigwa wa kutengeneza keki hapa Arusha!”

“Basi wewe baki mimi niende nikaichukue!”

“Hapana bwana twende wote!”

“Wewe baki tu!”

“Bwanae sitaki au una mipango yako nini?”

“Siyo hivyo nataka ubaki na watoto bwana!”

‘Sitaki bwana hebu twende wote na mimi nikalishe macho kila siku ndani!” Alizidi kung’ang’aniza Hoyce.

“Ok! Twende si umeng’ang’ania, tatizo lako mke wangu huniamni sijui kwanini?” Alisema Martin kwa utani.

“Siyo hivyo lakini kuna ubaya gani mtu akichunga mali zake?”

“Panda twende basi mpenzi!”

Wote walipanda garini lakini kabla gari halijaondoka Vicky alilikimbilia gari hilo!

“Mom!Mom! where are you going?”(Mama! Mama! Mnakwenda wapi?)

“To the best bites for your birthday cake!”(Tunakwenda best bite kufuata keki yenu ya siku ya kuzaliwa)

“Can I come with you mom?(Niwafuate mama?) Aliuliza Vicky.

“Ok! Get into the car!”(Haya panda basi garini) alisema Hoyce na Vicky alipanda bila kuchelewa Nicky hakutaka kuondoka aliendelea kucheza mpira na rafiki zake.

Hoyce alimwita Nicky kabla gari halijaondoka na mtoto aliondoka mbio.

“We are going downtown, take care of everything and make sure every friend of yours has a glass of juice Ok? We wont delay coming back!”(Tunakwenda mjini tafadhali angalia kila kitu nyumbani na hakikasha rafiki zako unawapa juisi ya kutosha sawa? Tutarudi sasa hivi!) Hoyce alimwambia Nicholaus akiwa na uhakika angerudi.

“Niiiicky!” Vicky alimwita kaka yake akatoa mkono wake wa kulia nje na kumpungia.

“Yoooo!” Nicholaus aliitika.

“See you later! I will sing happy birthday to you ok?”(Tutaonana baadaye nitakuimbia wimbo wa bethidei sawa?) Vicky alisema huku akicheka lakini Nicky hakujibu alikimbia kuelekea kwenye dirisha la dereva.

“Daddy!Daddy! Daddy! Buy me Ice cream when you come back ok?”(Baba!Baba!Baba! Ninunulie Ice cream mnaporudi sawa?) Nicholaus alimwambia baba yake.

Alikuwa kipenzi kikubwa cha baba yake, hawakuwa baba na mtoto tu bali mtu na rafiki yake, Martin alishindwa kuelewa bila mtoto wake Nicholaus kuwepo furaha yake ingekuwa wapi! Hoyce pia alifahamu kuwa Martin alimpenda sana Nicholaus na kwa sababu hiyo naye akajikuta akimpenda sana Victoria, mtoto mmoja akawa na mama na mwingine wa baba.

Hakuna mtu kati yao aliyejua wala kuhisi kuwa siku hiyo ingeishia kuwa machozi na majonzi makubwa katika familia yao, hakuna mtu aliyehisi kuwa wasingeonana tena, hakuna mtu aliyejua hawakuwa na masaa hata matatu mbele yao! hakuna mtu aliyejua walikuwa wakimwacha Nicky katika mateso makubwa.

Walipofika best bite waliichukua keki na kulipa pesa iliyobaki, Vicky alimkumbusha Martin kununua Ice cream, akafanya hivyo na wote wakaingia tena ndani ya gari tayari kwa kurudi nyumbani! Kabla gari halijaingia barabarani Vicky aliongea kwa sauti.

“Baba nataka maputo ya bethidei!”

“Tutayanunua wapi saa hizi mwanangu?”

“Labda twende supermarket ya Imalaseko!” Alishauri Hoyce.

Bila kutia neno kwa sababu Martin alitaka kumridhisha mtoto wake alikata kulia na kuanza kuliendesha gari lake aina ya Landcruiser kuelekea katikati ya mji lilikokuwa duka kubwa la Imalaseko ambalo liliuza kila aina ya bidhaa bora katika jiji la Arusha.

Gari ilitembea kwa kasi na wakati huo huo mawazo ya Martin kama ilivyowafanya biashara wengi duniani yalishahama ndani ya gari na kwenda sehemu nyingine akiziwazia biashara zake mbalimbali nje ya Tanzania.

“Mamaaaa weee! Martin! Baba wawili!” Hoyce alipiga kelele.

“Nini mke wangu?” Martin alishtka kama mtu aliyetoka usingizini

“Treni hilo hulioniii?”

Martin alipogeuza macho yake kuangalia upande wa pili alilia macho yake yalipokutana na kichwa cha treni kikija kwa kasi! Alipiga kelele lakini haikusaidia kitu, dereva wa treni hakusimama treni liliigonga gari yao na kupita juu yake! Ikawa kimya kabisa, treni halikusimama liliendelea na safari yake.

Nyumbani kwake sherehe iliendelea kama kawaida na Nicholaus aliendelea kuwamiminia rafiki zake juisi kama walivyoagizwa na mama yake, yeye hakunywa juisi kwa sababu alijua baba yake angemletea isicrimu kama alivyoagiza.

Martin ni kijana aliyefanikiwa sana katika maisha yake tena katika umri mdogo, anamuoa Hoyce msichana waliekutana nwaye katika ndege na Mungu anawajalia kupata watoto wawili mapacha, Nicholaus na Victoria! Ni familia yenye furaha ingawa Martin ni mtu wa kusafiri mara nyingi kwenye biashara zake.

Ilikuwa ni siku ya furaha akiwa nyumbani baada ya safari na kuwafanyia watoto wake skukuu ya kuzaliwa Wageni wamealikwa nyumbani kwa ajili ya sherehe hiyo, ni furaha tupu lakini fuaha hiyo inabadilika na kuwa kilio! Martin, Hoyce na mtoto wao Victoria wanapata ajali mbaya ya gari lao kugongwa na trewni la mizigo. Nyumbani hakuna mtu ambaye ana habari na tukio hilo sherehe bado inaendelea! Je, nini kitaendelea? Je, ajali hii ni ya kisasa? Endelea ……………

Nyumani sherehe iliendelea hadi saa mbili usiku bila Martin na mke wake pamoja na mtoto wao wa kike Vicky kurejea nyumbani, watu wengi waliokuwepo nyumbani walianza kuingiwa na wasiwasi mioyoni mwao, walishindwa kuelewa ni jambo gani lililotokea mpaka wakachelewa kiasi hicho! Pamoja na watu wote kuwa na wasiwasi bado Nicholaus aliendelea kucheza na watoto wenzake akijua wazazi wake wangerejea na kuendelea na sherehe kama kawaida.

“Kwanini baba na mama yako hawarudi?” Watoto wenzake waliuliza.

“Watarudi tu labda wamepita sehemu fulani!” Alijibu Nicholaus bila kujua kuwa baba, mama na Vicky walipata ajali mbaya ya kugongwa na treni.

“Njaa zinatuuma wangerudi tukala na kushiba kisha tuondoke!

Mpaka saa tatu na nusu za usiku walikuwa bado hawajarejea na wasiwasi ulizidi kuongezeka, hata Nicholaus na umri wake mdogo alianza kuhisi wazazi wake walikuwa wameptwa na tatizo fulani.

“Pigeni simu kwa baba mdogo namba ile pale labda watakuwa wamepita huko!” Alisema Nicholaus akionyesha namba ya simu iliyokuwa ukutani.

“kwani walikwenda wapi?” shangazi aliuliza

“Walikwenda kuchukua keki ya sikukuu ya Bathdei ya watoto wao!”

“Sikukuu yenyewe hamjatualika halafu mapiga simu kutuuliza, mnatujoki nini? Si wanajifanya matajiri wacha wamalize matatizo yao wenyewe wamezidisha sana maringo!” Alisema shangazi kwa ukali na kukata simu.

“Hawajaonekana!”Alisema mama huyo.

Baadaye saa nne usiku wageni waliokuwa kwenye tafrija hiyo walianza kuondoka kurejea majumbani kwao, uvumilivu ulianza kumshinda Nicholaus akaanza kulia, mtumishi wa ndani alianza kumbembeleza lakini hakunyamaza aliendelea kulia mpaka saa sita ya usiku.

“Usilie sana Nicky, watakuja tu!”

“Baba na mama wako wapi?”

“Watakuja tu!”

“Au wamepata ajali?”Nicholaus ajikuta akitamka maneno hayo bila kujua aliongea ukweli!

“Hapana hawezi kupata ajali,

baba huendesha gari vizuri!”

Relini:

Watu wengi walijaa eneo la ajali kushuhudia ajali ya treni kugonga gari, gari lilipondwapondwa na vipande vya miili ya watu vilisambaa kila mahali, ilikuwasi rahisi hata kidogo kuwatambua watu waliokuwa ndani ya gari hilo! Wasamaria wema walijaribu kulisoma gari hilo namba ili kujua ilikuwa gari la nani lakini hawakukiona kibao. Baadaye mtu mmoja aliokota kipande cha kioo alikisoma aliziona namba za gari hilo.

“Ni TZX 201745! Hili huwa la nani kweli?”

“Ni gari la Martin!”

“Yaani Martin ndiye amekufa?”

“Nina hakika ni yeye!”

Martin alikuwa ni maarufu mno mjini Arusha, kila mtu alimfahamu na hata gari lake aina ya Landcruiser lilifahamika na wengi, kila mtu aliyekuwepo eneo la ajali alisikitika kuona Martin alikufa kifo cha aina hiyo. Walipotazama vizuri kwenye gari waliona mkono wa mwanamke, kila mtu akajua alikufa pamoja na mkewe.

Wakati wakimsubiri trafiki wafike eneo hilo kupima ghafla kilisikika kilio cha mtoto, kutoka katika kichaka kilichokuwa jirani kabisa na eneo hilo!

Watu wote walishtuka, ilikuwa sauti ya mtoto akiomba msaada!

“Ba.. ba ni saa.. i..die.. nakufa!”

Watu wote walikimbia kwenda kwenye kichaka hicho cha miti ya michongoma, mtau mmoja aliingia hadi ndani bila woga na kilichofuata ni kelele za mtu huyo kutoka ndani ya kichaka.

“Jamani kuna mtoto humu ndani kaumia sana hebu njooni muone!”

“Mbebe utoke naye huku nje!”

Bila kupoteza muda mtu huyo alitoka na mtoto huyo hadi nje ya kichaka, uso wake ulijaa damu tupu na alikuwa na majeraha kila sehemu ya kichwa chake! Hakuwaona tena sababu ya kuendelea kuwasubiri trafiki, walimpakia mtoto huyo ndani ya gari la msamaria mwema na safari kwenda hospitali ya Mount Meru ilianza!

Mtoto huyo hakuongea kitu tena hadi walipofika hospitali ambako alipokelewa na kukimbizwa haraka chumba cha upasuaji ambako madaktari walifanya kila walichoweza kuokoa maisha yake, hakuna mtu hata mmoja aliyelifahamu jina la mtoto huyo na kwamba alikuwa mtoto wa nani!

Masaa matatu baada ya kuingizwa chumba cha upasuaji mtoto huyo alitolewa na kupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi ambako alilala bila kujitambua akivuta hewa kwa kutumia mashine ya oksijeni! Hakuna aliyekuwa na uhakika kuwa mtoto huyo angepona.

Pamoja na umri wake kuwa mdogo usiku wa siku hiyo Nicholaus hakupata hata lepe la usingizi, alilia mpaka sauti ikamkauka akiwalilia baba na mama yake pamoja na dada yake Vicky, hakubembelezeka hata kidogo! Masikio yake yalikua nje yakisikiliza kila kilichoendelea! Hata aliposikia paka au mbwa akipita alijua mama na baba yake pamoja na dada yake wanarudi, alinyanyuka na kukimbia hadi mlangoni lakini hakuna mtu aliyegonga mlango! Moyo wake ulizidi kuwa na wasiwasi zaidi alishindwa kuelewa wazazi wake walikuwa wapi na nini kiliwapata!

Leah, mfanyakazi wa ndani nyumbani kwao usiku mzima alimbeba mkononi mwake akizidi kumbembeleza lakini alizidi kulia kwa sababu Nicholaus alikuwa ni mtoto aliyependa sana kuangalia televeheni hasa vipindi vya wanyama, Leah alimamua kumuwashia luninga ili aangalie wanyama lakini badala ya kukuta kipindi cha wanyama alikuta ni taarifa ya habari na kuamua kuingalia ingawa hakupanga!

“Ajali mbaya ya treni!” Ndivyo alivyoanza msoma taarifa ya habari wa siku hiyo na baadaye kuendelea “Jana majira saa moja jioni gari aina ya Landecruiser lenye namba za usajili TZX 201745 Liligonga treni la mzigo lililokuwa safarini kutoka maeneo ya viwandani kurejea kituo cha reli cha Arusha, miili ya watu wawili ikiwa iimepondekapondeka imeokotwa eneo la ajali gari likiwa limeharibika vibaya na si rahisi kulitambua! Mtoto mdogo mwenye umri wa miaka kati ya mitano na sita ambaye inaaminika alikuwemo katika gari lililogongwa aliokotwa katika kichaka akiwa amejeruhiwa vibaya na sasa amelazwa katika hospitali ya Mount Meru, hali yake ikiwa mbaya.

Mpaka tunatangaza taarifa hii watu waliokufa na hata mtoto huyo bado hawajatambulika kwa majina! Uongozi wa hospitali ya Mount Meru unawaomba waliopotelewa na ndugu zao wafike hospitali ya Mount Meru kutambua miili ya marehemu na pia mtoto huyo ambaye hivi sasa amelezwa katika wodi ya wagonjwa mahututi!!!” alimaliza msomaji huyo.

Picha ya gari la Martin ilionekana likiwa limegongwa na kuharibiwa vibaya! Leah hatutaka Nicholaus aione picha hiyo, alimfunika usoni kwa kiganja ili asione lakini tayari Nicholaus alishaona na kuanza kulia.

“Dada! Baba na mama gongwa na treni?

“Hapana!”

“Si nimesikia na gari la baba nimeliona?”

Leah alikosa cha kumjibu, alichofanya ni kumbeba Nicholaus mgongoni na kutoka nje ya nyumba akafunga mlango na kumwomba mlinzi amsindikize kwenda hospitali ya Mount Meru, kabla hajatoka mlangoni alikutana na majirani wengi pamoja na marafiki wa Martin wakija nyumbani kwao baada ya kuiona taarifa ya habari katika luninga!

“Leah!”

“Naaam!”

“Umesikia taarifa ya habari?”

“Ndiyo!”

“Hivi kweli lile gari ni la baba yako?”

“Ni kweli kwani tangu waondoke jana kwenda kutafuta keki ya Bethidei ya watoto wao hawajarudi!”

“Hawakurudi?” Aliuliza mmoja wa majirani aliyekuwepo jana yake wakati wa tafrija!

“Ndiyo!”

“Basi ni lazima twende huko hospitali upesi kuhakikisha!”

Wote walitoka na kuingia ndani ya gari na safari ilianza haraka sana kuelekea hospitali ya Mount Meru, muda wote wa safari Nichoulaus aliwalilia wazazi wake.

Walipofika hospitali waliuliza mapokezi na kuelekezwa mahali alikolazwa mtoto aliyetangazwa redioni na kwenye television!

“Alipoletwa hapa hali yake ilikuwa mbaya sana haikuwa rahisi hata kulitambua jina lake, ila amelazwa chumba cha wagonjwa mahututi baada ya upasuaji twendeni niwapeleke alipo!” alisema muuguzi mmoja na kuondoka nao.

Walitembea na walipofikia jengo la wodi ya wagonjwa mahututi waliingia moja mwa moja hadi ndani na kuonyeshwa mtoto alipolala!

“Maskini Vicky!” Leah alishindwa kuvumilia baada ya kumuona Vicky katika hali aliyokuwa nayo alimwaga machozi na kutaka kuanguka juu ya kitanda na kumkumbatia lakini muuguzi alimshika kabla hajafanya hivyo, kilio cha Nicholaus aliyekuwa mgongoni mwa dada yake kilikuwa si rahisi kukielezea, alilia huku akiliita jina la dada yake na bado alitaka aonyeshwe mahali walipokuwa baba na mama yake.

“Wako wapi baba na mama wangu!” aliuliza Nicholaus huku akitokwa na machozi, alimtia huruma kila mtu aliyemwona, alionyesha wazi pamoja na umri wake kuwa mdogo ni kiasi gani aliumia moyoni mwake.

Kumwona Vicky kuliwafanya waamini na kuwa na uhakika kuwa hata waliokufa walikuwa ni Martin na Hoyce!! Kila mtu alilia machozi ya uchungu ilikuwa si rahisi kuamini kuwa mwisho

wa maisha yao ungekuwa ule! Walikuwa tayari kuamini baada ya kuiona miili yao!

Kutoka wodini huku wengi wao wakilia waliongozana moja kwa moja kuelekea chumba cha maiti ambako waliomba waonyeshwe miili ya ndugu zao, ilikuwa kazi ngumu sana kukubali

kuwa maiti walizoonyeshwa zilikuwa ni za Martini na Hoyce, kwani ziliharibiwa vibaya mno zilikuwa ni vipande vilivyokusanywa pamoja! Walilazimika kuamini hivyo sababu walikwashamuona Vicky wodini!

Majirani waliondoka chumba cha maiti kurudi nyumbani wakilia na kwenda nyumbani ambako walitangaza msiba! Leah na Nicholaus walibaki wodini pembeni mwa kitanda cha Vicky.

Mamia ya watu walikusanyika nyumbani kwa Martini kuomboleza kifo cha kijana aliyekuwa na umaarufu mkubwa mjini Arusha baada ya kupata utajiri katika umri mdogo! Lilikuwa ni jambo la kusikitisha sana na karibu kila mtu aliyekuwepo nyumbani pale alilia machozi ya uchugu

Wazazi wa marehemu Martini waliofariki miaka mitano kabla ya kifo chake na katika tumbo la mama yake walizaliwa watoto watatu yaani Mrtini , dada yake Christina na mdogo wake wa kiume Alphonce! Baada ya kufariki wazazi wao walioishi kijijini Bupandwamhela wilayani Sengerema mkoani Mwanza. Martini aliyeishi Arusha aliamua kuwahamisha ndugu zake kuwapeleka Arusha ambako aliwapa mitaji ya kufanyia biashara.

Walihama pamoja na familia zao, Christina aliyezaa watoto watatu kabla ya kuolewa alihama na watoto wake na Alphonce aliyekuwa na wake wawili na watoto wanne alihama nao kwenda Arusha, kwa wema wake Martin aliwanunulia kila mtu nyumba yake wakaishi maisha ya raha mustarehe.

Baada ya kufika Arusha Alphonce alianza biashara ya madini ya Tanzanite aliyofanya kaka yake lakini kwa sababu ya kuzidisha starehe na ulevi baada ya muda mfupi mtaji wake ulikwisha, akarudi tena kwa nduguye na kupewa shilingi milioni tatu lakini nazo pia alizimaliza katika ulevi na wanawake!

Christina naye baada ya kupewa Milioni tano na kaka yake alimpenda kijana mdogo wa Kimasai na kumkabidhi pesa zote kijana huyo alizitumia katika starehe zake mpaka zikaisha, alirudi tena kwa kaka yake na kupewa milioni mbili zaidi nazo zilipondwa na mpenzi wake.

Mara tano mfululizo Martin alitoa pesa kuwasaidia ndugu zake lakini alikata tamaa na kuamua kuwaacha kama walivyo, muda mfupi baadaye alimuoa Hoyce ndiyo chuki ikaongezeka kati yake na nduguze wakidai alichotwa akili na mwanamke wa Kichaga na kuwasahau ndugu zake.

Kwa huruma zake Martin ndugu zake walipopata shida nyingi aliamua kuwapa kazi katika machimbo yake huko Mererani na kuwalipa mishahara kama wafanyakazi wengine ili waendeshe maisha yao sababu hawakuwa na sehemu yoyote ya kwenda! Hiyo nayo haikutosha walifanya ukorofi kazini ikabidi awasimamishe kazi.

Wodini:

“Mama maputo yangu! Nipeni maputo yangu twende nyumbani kwenye pati yetu Nicky na watoto wengine wanatusubiri!” Hayo ndiyo maneno aliyoanza kusema Vick aliporudiwa na fahamu zake baada ya siku tano za kuzirai! Ilikuwa ni siku tatu baada ya baba na mama yake kuzikwa.

Pembeni mwa kitanda chake alikuwepo Leah na Nicholaus ambao walielewa ni kitu gani alichokuwa akikisema Vicky! Walilia machozi ya uchungu, kwa sababu Vicky alifungwa bendeji machoni hakuweza kugundua kuwa Nicholaus na Leah walikuwa pembeni mwa kitanda chake, aliendea kuwaita baba na mama yake!

“Mama! Baba! Njooni twende!” Aliendelea kusema Vicky kama mtu aliyekuwa usingizini, maneno hayo yalizidisha uchungu mioyoni mwa Nicholus na Leah na kuwafanya walie zaidi, walipiga magoti na kuanza kusali sala ya baba yetu ulie mbinguni wakimwombea Vicky! Waliona hawakuwa na kimbilio jingine zaidi ya kumuomba Mungu! Hawakutaka kupoteza kila kitu, walitaka angalau Vicky abaki hai na waendelee kuwa naye.

Wakiwa bado wamepiga magoti mlango ulifunguliwa na watu waliingia hadi ndani ya chumba hicho! Hawakuongea kitu mpaka Leah na mtoto Nicholaus waliponyanyuka na kuketi.

“Mnasali dhehebu gani?”

“Sisi?”

“Tunasali Lutherani”

“Ok! Hata mimi ni mlutheri pia”

“Sawa daktari!” Alijibu Leah huku akimpisha daktari amwangalie Vicky ambaye bado aliendelea kuongea maneno mengi.

“Kaanza saa ngapi kuongea hivyo mgonjwa!”

“Hana hata dakika kumi na hata sisi bado hatujaongea nae, tuliposikia anaongea ndipo tulipopiga magoti kumshukuru Mungu!”

“Kweli Mungu ni mwema, Vicky kapona!” Aliongea daktari kwa mshangao hata yeye kumbe hakuwa na matumaini.

“Kweli ataoiba?”

“Atapona ila kitu kimoja tu ………..”

“Macho yakeyameharikika kabisa! Hayafai kutumia tena inavyoonekana kuna vipande vidogo vidogo vya vioo vilimwingia katika macho yake siku ya ajali na kuyapasua kabisa! Hakuna uwezekanao mwingine kumsaidia zaidi ya kuyang’oa macho yake inasikitisha lakini inabdi iwe hivyo!”

“Mungu wangu! Kuyang’oa ina maana Vicky atakuwa kipofu?”

“Hivyo ndivyo itakavyokuwa lakini bi bora awe hai!” Daktari aliongea kwa huzuni.

“Daktari hakuna njia nyingine ya kumsaidia kweli?”

“Nasikitika hakuna !”

“Dada Leah!”

Naam!”

“Kumbe upo? Nicholaus yuko wapi? Baba na mama wako wapi?” aliuliza Vicky.

“Baba na mama waliku…………..!” alitaka kujibu Nicholaus lakini kabla hajamaliza sentensi yake Leah alimziba mdomo wake!

“Wapo nyumbani watakuja baadaye!” Leah alimficha.


“Nani kafunga?” Leah aliuliza baada ya kukuta kuna kufuli jipya kwenye mlango wa nyumba yao walipotoka hospitali. Kabla hajapata jibu mtu mmoja alitokea nyuma yake na kuuliza wao ni akina nani.

“Sisi?”

“Ndio!”

“Kwanini unatuuliza?”

“Mimi ni mlinzi mpya nimeletwa hapa na shangazi yenu Christina hamtakiwi kuingia katikanyumba hii!”

“Kwanini?””Nyumba hii imechukuliwa na yeye mnatakiwa mtafute mahali pengine pa kuishi!”

Leah alijifanya hakusikia maneno hayo na kuuparamia mlango na kuanza kulivuta kufuli lao, mlinzi alimkamata na kuanza kumzaba vibao vingi usoni.

“Unajifanya kiburi siyo?”

Roho ya Nicholaus iliumia kuona Leah akipigwa bila sababu, alirudi nyuma na kuokota kipande cha jiwe na kulirusha kwa nguvu zake zote likatua usoni kwa mlinzi huyo! Damu iliruka kama bomba kutoka sehemu lilipotua jiwe, mlinzi huyo alianguka chini na kutulia tuli!

Leah na Nicholaus hawakuwa na mahali pa kulala ilibidi wakae nje wakinyweshewa na mvua hadi usiku wa manane! Kifo cha Martin na Hoyce kilionekana kuwa mwisho wa kila kitu.

Mpaka majira ya saa nane hivi usiku Leah na Nicholaus walikuwa bado wako nje wakinyeshewa mvua na kupigwa na baridi! Mlinzi alikuwa bado amelala chini lakini ghafla walimwona akinyanyuka na kukaa kitako, kwa mkono wake wa kulia alijishika usoni na kupambana na kidonda pamoja na damu iliyoganda! Leah alishtuka akijua kama mlinzi angewaona ni lazima angewadhuru.

“Twende tukajifiche nyuma ya nyumba Nicky!” Leah alisema na kuanza kumvuta Nicholaus wote wawili wakazunguka nyuma ya nyumba na kuingia ndani ya shimo refu la takataka na kujificha! Wakiwa ndani ya shimo hilo walisikia vishindo vya mtu akitembea kuelekea mahali lilipokuwa shimo hilo, walijua lazima alikuwa amewaona na alikuwa akiwafuata lakini ghafla walisikia vishindo hivyo vikigeuza na kuelekea tena mbele ya nyumba.

“Nikiwakamata ni lazima niue mwenye kwa mkono wangu kabla hata huyo shangazi yao hajaja!” Alisikika akisema mlinzi huyo Leah alizidi kumkumbatia Nicholaus wakiwa ndani ya shimo la takataka lililoendelea kujaa maji ya mvua.

Hali ikawa shwari hawakusikia tena vishindo vya mlinzi lakini mvua ilizidi kunyesha na maji yalizidi kutiririka kuingia ndani ya shimo wasiwasi wa maji kujaa na kuwafunika ulizidi kumwingiea Leah! Nicholaus alitetemeka kwa baridi kiasi cha meno yake kugongana lakini kwa hali iliyokuwepo hakuthubutu kulia kwani hata yeye tayari alishaigundua hali ya hatari iliyokuwepo.

Maisha yao yalikuwa yameharibika ghafla hawakuwahi hata siku moja kufikiri wangekuja kupatwa na shida walizokuwa nazo usiku huo tena wakiwa nje ya nyumba iliyojengwa na baba yao!

Muda mfupi baadaye majira ya kama saa kumi hivi za usiku Leah alisikia lango likifunguliwa na baadaye sauti za watu wakiongea zilifuata, aliposikiliza vizuri aliitambua moja ya sauti hizo! Ilikuwa ni sauti ya shangazi yao ikimuuliza mlinzi ni wapi walikokuwa watoto.

“Walikuja nikawazuia wasiingie ndani ya nyumba lakini yule msichana akataka kuingia kwa nguvu ndipo nikalazimika kumpiga! Lakini kile kitoto kidogo kikanipiga na jiwe hapa puani sijui kilinipiga vipi hata mimi sielewi nikajikuta nimeanguka chini na kupoteza fahamu zangu kabisa! Nilipozinduka nilijaribu kuwatafuta humu ndani lakini sikuwaona!”

“Geti lilikuwa wazi ulipozinduka?”

“Hapana lilikuwa limefungwa kama mlivyolikuta!”

“Sasa wametoka vipi?Nina hakika bado wapo humuhumu ndani hebu watafute mimi nimekuja na hao vijana kuwamaliza kabisa ili hizi mali ziwe zangu moja kwa moja!” Alisema shangazi yao na Leah pamoja na Nicholaus waliyasikia maneno hayo na kuzidi kuogopa.

“Dada Leah,kwanini shangazi anataka kutuua?”

“Inavyoonekana anataka hizi mali zenu!”

Mlinzi alianza kuzunguka nyumba tena akiwatafuta shangazi akiwa nyuma yake mara kwa mara walilikaribia shimo walilojificha Leah na Nicholaus lakini hawakupata wazo na kuangalia ndani yake kwa jinsi mvua ilivyonyesha walikuwa na uhakika kulikuwa na maji hivyo walikata tamaa ya kuwatafuta.

Walikaa ndani ya shimo hilo maji yakiwa yamemfikia Leah kiunoni na Nicholaus shingoni hadi asubuhi bila kugundulika! Walikuwa wakitetemeka sana miili yao, Leah alijua ni lazima Nicholaus angeugua kichomi.

Majira ya kama saa moja hivi walisikia lango likifunguliwa na shangazi pamoja na vijana wanne aliongozana nao waliondoka na kumwacha mlinzi peke yake, Leah na Nicholaus waliendelea kukaa ndani ya shimo hilo hadi saa sita za mchana! walisikia geti likifunguliwa tena na kufungwa wakajua mlinzi alikuwa anatoka kwenda nje, Leah aliamua kuitumia nafasi hiyo kuokoa maisha yao.

“Nicholaus njoo twende!” Alisema Leah na kumpakata Nicholaus wakatoka shimoni na kuanza kutembea kuelekea getini ambako walitoka hadi nje kabla hawajafika mbali walimwona mlinzi akija mbio kuwafuata!

“Nyie mlikuwa wapi?”

“Tulikuwa ndani!”

“Haya twendeni nikawafungulie mlango muingie!” Mlinzi alidanganya lengo lake likiwa kuwarudisha ndani halafu ampigie simu shangazi ili aje na vijana wake kukamilisha mpango wao wa mauaji, kwa sababu walishasikia kila kitu usiku walikataa kurudi.

“Hapana tuna haraka tunakwenda hospitali kumwona mgonjwa!”

“Mtakuja tena jioni? Nimeambiwa na shangazi niwafungulie!”

“Sawa! Tutakuja!” Aliitikia Leah lakini ukweli hakuna mtu ambaye angerudi tena katika nyumba ile hadi mwisho wa maisha yake!


Martin na Hoyce waliishi na Leah kwa miaka mitano kabla ya kifo chao walimchukua binti huyo kutoka kwenye kituo cha kulelea watoto cha Msamaria mwema kilichopo katikati ya mji wa Arusha na kuamua kuishi naye baada ya kufikish umri wa miaka kumi na tatu uliokuwa mwisho kwa kituo hicho kulea mtoto Yatima.

Leah hakumjua baba wala mama yake alitupwa mtaani na mama yake baada tu ya kuzaliwa na mama huyo akaondoka kwenda kusikojulikana! Hivyo kwake Martin na Hoyce walikuwa ni kama baba na mama na aliwachukulia Nicky na Vicky kama wadogo zake na aliahidi kuwa na watoto hao hadi hatua ya mwisho!

Walinyoosha hadi hospitali na kwenda katika wodi aliyolazwa Vicky lakini hawakumkuta kwenye kitanda alicholazwa! Leah alishtuka lakini kabla hajafanya lolote au kumuuliza mtu ghafla alishtukia sauti ikimwita kutoka ofisini kwa wauguzi alipogeuka alikutana na sura muuguzi akimwita.

“Naam mama!”

“Hebu njoo hapa kidogo!”

Leah akiwa amemshika Nicky mkono walitembea hadi ofisini kwa wauguzi na kuwasalimia watu wote aliowakuta wodini.

“Wewe ni ndugu yake Victoria?”

“Ndiyo yupo wapi?”

“Walikusubiri sana asubuhi ili utie saini karatasi kabla hajapelekwa chumba cha upasuaji, hivi nyumbani kwenu hakuna watu wazima?”

“Watu wazima?”

“Ndiyo!”

“Wote wamefariki!”

“Wamefariki?”

“Ndiyo kwani wewe hukusikia dada watu waliogongwa na treni juzi?”

“Mh! Nyie ni watoto wa Martin?”

“Ndiyo!”

“Masikini poleeeni!”

“Ahsante!”

Nesi alimueleza Leah sababu ya Vicky kupelekwa chumba cha upasuaji, Leah alilia machozi.

“Vipi mbona unalia?”

“Nashindwa kuelewa nitaishije na hawa watoto!”

“Kwani vipi?”

“Sasa wakiyang’oa macho ya Vicky mimi nitamtunzaje?” Alisema huku akilia kwa sauti kubwa zaidi.

“Dada kwa hiyo Vicky hataona tena?” Nicholaus aliuliza.

“Hapana atakuwa anaona kwa kutumia mashine!”Leah alimdanganya Nicholaus kwa kuogopa kumkatisha tamaa.

Alipotolewa chumba cha upasuaji masaa manne baadaye uso wake wote ulifunikwa na bendeji, lakini alikuwa na fahamu kama kawaida! Leah alishangaa kwani matarajio yake yalikuwa tofauti yeye alitegemea Vicky angerudi akiwa katika mzito wa nusu kaputi.

“Hapana katika operesheni za aina hii huwa hatutoi nusu kaputi bali huwachoma wagonjwa sindano za ganzi katika macho yao!”

Masaa mawili baadaye Vicky alianza kulalamika maumivu katika macho yake ikabidi apewe dawa za kutuliza maumivu pamoja na usingizi.

“Mpeni sindano ya Pethedine 25mg itamsaidia!” alisema daktari na kweli Vicky alipochomwa sindano hiyo alilala usingizi kabisa na kuzinduka saa mbili ya usiku.

“Dada poleeee!” Nicholaus alisema.

“Ahsante!”

Victoria alikaa hospitali pamoja na Leah na kwa muda wa siku saba bila baba yao mdogo wala shangazi yao kufika kuwaona, waliishi maisha ya shida wakila chakula cha hospitali kama wagonjwa wengine, kilikuwa chakula kibaya kikilinganishwa na chakula walichozoea kula nyumbani wakati wa uhai wa wazazi wao mara nyingi Nicholaus alikataa kula na kujikuta akikonda.

Siku ya kumi na mbili waliruhusiwa kutoka wodini, Leah alishindwa kuelewa baada ya kutoka hospitalini angekwenda wapi na watoto hao kwani asingeweza kurudi tena kulikokuwa nyumbani kwao ambako alikuwa na uhakika Nicholaus na Victoria wangeuawa!

Kwa siku tatu mfululizo alilala mitaani mbele ya maduka ya wahindi pamoja na ombaomba wenye Ukoma, usiku mzima yeye na watoto waliwalia wazazi wao, aliwaonea huruma Nicky na Vicky kuliko alivyojionea huruma mwenyewe! Hakuwa na njia nyingine ya kupambana na maisha zaidi ya kuombaomba! Hiyo ndiyo ikawa njia pekee ya kumwezesha yeye na watoto kuishi mjini.

Aliwaeleza watoto ukweli juu ya yaliyotokea na kuwaomba wawe wavumilivu, walichofanya kila siku kikawa ni kupita mitaani katika maduka ya wahindi hasa siku ya ijumaa na kuomba, Victoria akiwa mbele na kopo!

“Hili ni fundisho ni lazima tuwe tunawaandalia watoto wetu mazingira mazuri!”

“Kwanini?”

“Wale watoto niliowapa pesa pale ni watoto wa Martin!”

“Mh! Kweli?”

“Ndiyo! Baada ya kufariki Martin baba yao mdogo na shangazi wamechukua mali zote hivi sasa watoto wanateseka mitaani wao wanatesa na mashati ya marehemu!”

“Masikiniii!” Mke wa bwana huyo alisema kwa huzuni, machozi yalimtoka kwa sababu alimfahamu Martin na utajiri aliokuwa nao ilibidi arudi mbio hadi waliposimama watoto na kuwaogezea noti nyingine ya shilingi elfu kumi!

“Poleni sana watoto Mungu atawasaidia!”

“Ahsante!” Aliitikia Vicky ingawa hakumwona mtu aliyewapa pesa.

Muda mfupi baadaye gari aina ya BMW open roof aliyoitumia Martin kuwapeleka watoto ufukweni kabla ya kifo chake ilipita na Nicholaus akaiona.

“Dada Leah gari ya baba hiyooo!” Nicholaus alisema.

“Sio yenyewe!” Leah alikataa ingawa alimwona hata aliyekuwa akiendesha, alikuwa baba yao mdogo! Hakutaka kuwaumiza watoto.


Kwa pesa walizopata katika omba omba kila siku Leah alipanga chumba kimoja maeneo ya Njiro kilikuwa ni chumba kidogo lakini kilitosha na alinunua pia vyombo vya kupikia, jiko na mikeka ya kulalia! Baada ya kupanga chumba alianza kazi ya kulea watoto nyumbani kwa mhindi mmoja mjini Arusha!

Alifanya kazi yake tangu asubuhi hadi saa mbili ya usiku aliporudi nyumbani na kuwapikia watoto chakula cha usiku huo na siku iliyofuata! Maisha yalikuwa magumu lakini alivumilia.

Miaka mitano baadaye:

Pamoja na kupenda shule Vicky na Nicky hawakupelekwa shule na baba mdogo na shangazi walizidi kuponda mali bila kujali kuwa watoto wa ndugu yao walikuwa wakiteseka, watoto wao wakisoma shule za kimataifa nchini Kenya na Uganda! Kila mara Nicholaus alilia shule lakini Leah hakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Baadaye Nicholaus akiwa na umri wa miaka kumi na mbili aliandikishwa darasa la kwanza, lakini kwa sababu ya kuanza shule akiwa na umri mkubwa alishindwa kumaliza darasa la saba na kukomea darasa la sita akaanza biashara za kuuza mafuta ya taa mitaani ili kusaidiana na Leah katika maisha yao ya kila siku.

Lakini biashara hiyo haikudumu sana mtaji aliopewa na Leah ulikwisha Nicholaus akajikuta akiwa kijiweni ni huko ndipo alikojifunza tabia chafu! Ni huko ndiko alikoharibika, mazingira yalimlazimisha kuharibika. Alikuwa na shida nyingi na hakuwa na mtu wa kumsaidia au kumsikiliza zaidi ya Leah.

Mara tatu mfululizo alishakwenda nyumbani kwa baba yake mdogo kuomba msaada lakini alifukuzwa kama mbwa! Roho ilimuuma sana ukizingatia mali waliyotumia ilikuwa ya baba yake, aliondoka akilia na kuahidi kutorudi tena.

“Ni bora niondoke hapa nchini vinginevyo nitamuua baba mdogo tena kwa mkono wangu mwenyewe!” Nicholaus alimwambia Leah.

Nicholaus alishajifunza habari za ulaya na Marekani kutoka kijiweni

ITAENDELEA

Dimbwi la Damu Sehemu ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment