Dimbwi la Damu Sehemu ya Pili
MAISHA

Ep 02: Dimbwi la Damu

SIMULIZI Dimbwi la Damu
Dimbwi la Damu Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA: ERIC SHIGONGO

*********************************************************************************

Simulizi: Dimbwi La Damu

Sehemu ya Pili (2)

Roho mkononi Tehran:

Katika nchi zilizopiga vita madawa ya kulevya kwa nguvu zote ilikuwa ni nchi ya Kiislam ya Iran! Ndani ya nchi hiyo adhabu kwa mtu aliyekamatwa na madawa ya kulevya ilikuwa ni kifo kwa kupiga risasi mbele ya halaiki ya watu ili kuwa fundisho kwa wengine.

AbdulAziz Akem raia wa Iran na Samweli Mazengo raia wa Tanzania waliifanyabiashara hii kwa nguvu zao zote, walikuwa safari kuelekea Iran lakini wamekwama nchini Tanzania wakitokea India! Safari hiyo ilikuwa ni kama safari ya kifo hakuna mtu hata mmoja kati yao aliyekuwa na uhakika wangerudi salama kwani wakiwa Dar es Salaam walisikia na kushuhudia kupitia katika luninga watu wakipigwa risasi hadharani na kufa baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya aina ya heroine!

“Tutafanyaje sasa rafiki yangu!” Samweli alimuuliza AbdulAziz.

“Kwa kweli sijui, ila naogopa sana kuendelea na safari hii!”

“Na tajiri utamwambia nini”

“Siwezi kwenda kufa mimi!”

Waliendelea kuongea wakiwa wamekaa mbele ya hoteli maarufu Mjini Arusha iliyoitwa Bin One, hali zao hazikuwa nzuri madawa kwani waliyoyameza tumboni mwao yalionekana kutishia sana uhai wao.

“Cha kufanya tuyatoe tumboni na kuyaweka kwenye sanduku kisha tutafute mtu yeyote hapa Tanzania tujifanye tunamsaidia kwenda Ulaya na tumkabidhi sanduku hilo na tusafiri naye hadiTehran akikamatwa shauri yake sisi tunaingia mitini!”


Jioni ya siku hiyo baada ya kufanya kazi zake za kuosha magari mitaani Nicky alikuwa amechoka aliamua kupitia maeneo ya mjini akiwa njiani kuelekea nyumbani kwao Njiro! Alikuta magari mengi sana mbele ya hoteli ya Bin one akaamua kuingia ndani kutafuta kibarua cha kuosha magari hayo, alisikia sauti ikimwita upande wake wa kulia alipogeuka kuangalia aliwaona vijana wawili wamekaa kwenye viti pembeni mwa bwawa la kuogelea!

Mmoja wa vijana hao alikuwa Mwarabu na mwingine alikuwa Mweusi, alitembea na kuwasogelea hadi akawafikia walipokaa na kuwaamkia.

“Wewe kijana unaishi wapi?”

“Naishi Njiro!”

“Unaitwa nani?”

“Ninaitwa Nicholaus!”

“Aisee unaishi na nani nyumbani”

“Na dada zangu wawili!”

“Wanafanya kazi?”

“Hapana!”

Walimuuliza maswali mengi sana na kujifanya wamemwonea huruma sana walimwomba akae kitini wakamnunulia chakula! Katika maisha yake tangu wazazi wake wafariki hakuwahi kutegemea kula katika hoteli ya kifahari namna hiyo, alipomaliza kula alishukuru na wakampa noti ya shilingi elfu kumi kumsaidia nyumbani.

“Ahsante Mungu hii pesa yote nitamsaidia dada Leah kununua chakula cha mwezi mzima!” Alisema Nicholaus aliondoka akiwa ameahidi kukutana na watu hao kesho yake saa tatu asubuhi baada ya kuahidi kumsaidia zaidi.

Alipofika nyumbani aliwasimulia Leah na dada yake Vicky juu ya watu aliokutana nao hata wao walifurahi na walizidi kumshawishi siku iliyofuata arudi tena, usiku wa siku hiyo hakulala na siku iliyofuata asubuhi alidamka na kwenda hotelini.

Mapokezi mhudumu alipiga simu chumbani na wote Samwel na mwenzake waliteremka hadi chini na kumkuta Nicholaus akiwasubiri aliwasabahi na kuwaeleza hali ya nyumbani kwao.

“Dada zangu walifurahi sana kwa msaada wenu na wana hamu ya kuwaona!” Alisema Nicholaus bila kufahamu watu aliokuwa akiongea nao hawakuwa na mpango mzuri wa maisha yake.

“Ahsante lakini samahani kidogo hivi sasa tunatoka kwenda madukani, unaweza kurudi saa tisa na nusu jioni!”

“Sawa tu braza!” Nicholaus alimjibu Samwel

“Chukua pesa hii utaitumia kama nauli!” Samwel alimkabidhi Nicky shilingi elfu kumi.

Aliporudi saa tisa na nusu kama alivyoahidiana nao walimkaribisha chumbani ambako alipewa kikombe cha chai lakini alikataa kunywa akihofia kunywesha madawa ya kulevya.

“Labda kama kuna soda!”

Samwel alifungua friji na kutoa chupa ya soda na kumpatia Nicholaus akaanza kunywa alipomaliza maongezi yao yalianza.

“Kijana sisi ni Raia wa Iran! Tulikuja hapa nchini kutafuta biashara lakini kesho au kesho kutwa tutarudi nyumbani kwetu!”

“Kweli?”

“Ndiyo!”

“Sasa mbona mimi nimewazoea?”

“Unaweza kuongozana na sisi kama utapenda!”

“Kwenda Iran?”

“Ndiyo hakuna shida hata kidogo!”

“Kweli?”

“Ndiyo kwani huamini?”

“Nauli je?”

“Tutakusafarisha usiwe na shaka!”

“Oh! Ahsante Mungu, asante Mungu!” Nicholaus alipiga kelele akishangilia.


Alikwenda nyumbani na kuwasimulia Leah na Vicky walilia machozi! Vicky alilia zaidi akimbembeleza kaka yake asimwache lakini Nicholaus hakusikiliza.

“Sikiliza Vicky sitakusahau maishani nakwenda kutafuta maisha ili siku moja na sisi tuwe matajiri kama alivyokuwa baba yetu! Nataka nitajirike nijenge ghorofa katikati ya mji wa Arusha mimi na nyinyi tuishi pamoja kwa raha mustarehe” Alisema Nicholaus.

“Sio vizuri uondoke uniache mimi pacha wako tena nikiwa kipofu Nicholaus!” Alisema Vicky huku akilia.

“ Vicky unajua ninakupenda kiasi gani tafadhali niruhusu nikatafute maisha ili nije kukusaidia!” Aliendelea kumbembeleza Nicholaus.

Alimbembeleza dada yake hadi saa sita ya usiku ndipo Vicky alipokubali ombi hilo kwa shingo upande na hata Leah, ilibidi akubali wote watatu walikumbatiana na kusali pamoja wakilia, ilionekana kama hiyo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kuonana! Roho ilimuma sana Nicholaus kuona dada zake wakilia.

“Nyamazeni mimi nikirudi machozi yenu yote yatakauka dada zangu! Niombeeni tu kwa Mungu na mambo yakiwa safi mapema ninaweza kurudi kuja kuwachukua!”

“Sawa ahsante!” Aliitikia Victoria

Nicholaus aliingiza mkono mfukoni na kuchukua noti ya shilingi mia mbili akaichana katikati na kumkabidhi dada yake kipande kimoja.

“Victoria!” Aliita

“Naam!”

“Hicho ni nini?”

“Kipande cha karatasi!”

“Hicho ni kipande cha noti ya shilingi mia mbili je unaweza kununua kitu chochote na kipande hicho?”

“Hapana kaka yangu mpaka vipande vyote viwili!”

“Basi vivyo hivyo na mimi bila wewe ni kipande cha pesa siwezi kufanya lolote, nitakukumbuka sana Victoria na sipendi kutenganishwa na wewe ila imelazimu!” Alisema Nicholaus na wakakumbatiana wote huku wakilia machozi.

“Kitunze sana kipande hicho mpaka tutakapokutana tena usikitupe dada yangu huu ndio ukumbusho wangu kwako!”

“Sawa nitafanya hivyo Nicholaus!”

Wote walikuwa wakilia wakati Nicholaus akitoka ndani ya chumba chao tayari kwenda hotelini kwa safari, alipofika mbelealiangalia nyuma na kuwaona Leah na Vicky wamesimama mlangoni roho yake ikauma na kumfanya alie! Ulikuwa ni kama mwisho wa kuonana kwa upande mwingine wa moyo wake ulimwambia asiondoke lakini alipingana nao.


Alipofika hotelini alikuta AbdulAziz na Samwel wapo tayari, walimkabidhi karatasi zote za safari na kumkabidhi pia begi kubwa.

“Hilo begi lina nguo zako zote tumekununulia mdogo wetu, lakini kuna jambo moja la muhimu sana katika safari hii usitake watu wajue sisi na wewe tupo safari moja hutakiwi kutusemesha wala kutukaribia.

“Sawa tu ili mradi ninayo tiketi yangu tutakutana hukohuko Tehran wala msiwe na wasiwasi nawashukuru sana kwa msaada wenu!” Alisema Nicholaus bila kujua kuwa ndani ya begi lake kulikuwa na kitu ambacho kingeweza kuchukua uhai wake.


Wote watatu Samwel, Nicholaus na AbdulAziz waliondoka hotelini wakiwa ndani ya gari aina ya benzi lililomilikiwa na hoteli ya Bin One lilikodishwa kwa wageni mbalimbali waliopanga ndani ya hoteli hiyo!

Nicholaus alivaa suti nyeusi pamoja na viatu vyeusi vilivyong’aa kwa hakika alipendeza! Ilikuwa ni mara ya kwanza kwake tangu wazazi wake wafariki kuvaa nguo za thamani kiasi kile! Kila mara alijiangalia ilikuwa ni kama ndoto.

Njia nzima Nicholaus alimfikiria dada yake na roho ilimuuma sana kumwachaVicky, ukizingatia dada yake alikuwa kipofu! Hakuwa na la kufanya ilikuwa ni lazima aondoke kwenda kutafuta maisha, hakutaka kuiachia bahati aliyoamini ameipata.

Ndani ya nafsi yake aliamini baada ya muda mfupi tu angerudi tena Tanzania akiwa tajiri na kujenga jumba kubwa pia kununua magari ya kifahari na maisha yangekuwa ya raha mustarehe baada ya hapo!

“Nyie mnakaa mjini Tehran kabisa au?”

“Ndiyo!”

“Lakini mimi nataka kwenda Marekani, nchi yenu ina vita sana na mimi sipendi vita, watu wanakufa mno, sitaki kufa bila kumwona tena dada yangu!”

“Haina shida ili mradi sisi tumeamua kukusaidia tukishafika Iran tutakutafutia tiketi nyingine ya ndege ili uondoke kwenda huko Marekani au ulitaka kwenda Uingereza na Canada?” Samweli alimuuliza.

“Hapana mimi nataka Marekani tu!”

“Basi hakuna shida!”

Muda wa kuripoti uwanja wa ndege kwa abiria wote ilikuwa saa sita mchana masaa mawili kabla ya ndege ya shirika la Gulf Air kuruka. Gari lao liliwasili uwanjani saa moja kabla ya muda wa kuruka kutimia, ilikuwa ni mara ya pili kwa Nicholaus kufika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro!Mara ya mwisho ilikuwa miaka miwili kabla ya wazazi wake hawajafariki! Siku yeye na mama yake walipomsindikiza baba yao aliyekuwa akisafiri kwenda Ubeligiji kibiashara!

Uwanja wa ndege wa KIA ulimkumbusha mengi kuhusu wazazi wake na kumtia huzuni zaidi, aliwakumbuka baba na mama yake kwa kila kitu na aliamini kama wasingekufa asingekuwa safarini kwenda katika nchi asiyoifahamu siku hiyo.

“Baba na mama walikuwa na kila kitu lakini leo hii tunateseka, mali zote wanatumia baba mdogo na shangazi pamoja na watoto wao! Lakini hili ni kosa la baba sababu ya kutokuacha wosia mzuri nafikiri ni sababu ya kifo chake kilikuwa cha ghafla mno!” Aliwaza Nicholaus baada ya kuteremka katika gari.

“Nicholaus tangulia hukuelewa tulivyokueleza, hatutaki kuongozana na wewe au hutaki kwenda safari nini?”

“Nataka!”

“Haya basi tangulia!”

Huku akitabasamu na kuchukulia mkwara aliopigwa kama utani Nicholaus alianza kutembea taratibu kuelekea kwenye lango la kuingilia uwanjani tiketi yake ikiwa mkononi!

“Nicholaus!!!” Alisikia sauti ikimwita kabla hajaingia uwanjani alipogeuka alishangaa kumwona Leah akiwa amemshika mkono Victoria! Badala ya kuingia alikimbia kuwafuata walipokuwa wamesimama na kuwakumbatia.

“Vipi mbona mpo hapa mmekuja na nini?”

“Tumekodisha teksi!”

“Kwanini mnatumia pesa vibaya hivyo si tulishaagana lakini?”

“Hapana Nicky mimi sitaki uondoke, moyo wangu umeshtuka nahisi kuna kitu kibaya kinakwenda kukupata na hautarudi tena! Nahisi wanakweda kukuua!” Alisema Victoria huku akilia mwili wake ulishahisi kitu kibaya.

Kwa dakika kama mbili Nicholaus hakujibu kitu chochote alikaa kimya akitafakari alichoambiwa, alipomwona dada yake akilia naye alianza kulia, Leah nae alishindwa kujizuia wote watatu walianza kulia na waliendelea kwa kama saa nzima!

Nicholaus alikuwa njia panda na alitakiwa kufanya uamuzi mgumu kupita maamuzi yote aliyowahi kufanya katika maisha yake, upande mmoja wa akili yake ulimweleza asiondoke lakini upande mwingine ulizidi kusisitiza aondoke kwenda kutafuta maisha bora kwa ajili yake, dada yake na Leah.

“Kaka usiondoke! Tafadhali nakuomba Nicholaus kama kufa na umasikini wetu acha tufe!” Aliendelea kusisitiza Vicky huku akisaidiwa na Leah!

“Abiria wote wanaosafiri kwa ndege ya shirika la ndege la Gulf Air mnaombwa kupanda ndani ya ndege kwani ndege itaruka baada ya dakika kumi na tano, ahsanteni!” Ilikuwa ni sauti nzuri nyororo iliyotoka katika kipaza sauti kilichokuwepo uwanjani hapo!

Mwili wa Nicholaus ulishituka kufuatia sauti hiyo na alipoangalia kwenye lango aliwaona Samweli na AbdulAziz wakimwita kwa ishara! Alitaka awaeleze kuwa asingeondoka tena lakini alishindwa kufanya hivyo.

“Vicky!” Alimwita dada yake.

“Naam kaka!”

“Siwezi!”

“Huwezi nini?”

“Siwezi kuacha kuondoka, niombee tu kwa Mungu tutaonana Mungu akipenda na nitaendelea kukupenda siku zote za maisha yangu!” Alisema Nicholaus na baada ya maneno hayo alinyanyua sanduku lake na kuanza kukimbia mbio kwenda ndani ya uwanja akiwaacha dada yake na Leah wakilia.

“Nicholaus usiondoke tafadhali rudi!” Alisema Vicky huku akilia machozi mwili wake ulishahisi kaka yake alikuwa akienda kufa!


Kwa haraka na mbio alizokuwa nazo sanduku wa Nicholaus halikukaguliwa kabisa, aligonga tiketi yake mhuri na kukimbia mbio hadi ndani ya ndege bila kusimamishwa mahali popote na alikuwa mtu wa mwisho kuingia ndani ya ndege.

AbdulAziz na Samwel ambao hawakuwa na uhakika kama Nicholaus angekivuka kizingiti cha uwanja wa ndege wa Arusha walipomuona walinyanyuka vitini na kushangilia, Nicholaus alishangaa na hakuelewa ni kwanini walifurahi kiasi hicho alijikuta akiamini kuwa kweli walimpenda na waliamua kumsaidia!

Dakika kumi tu baada ya kukaa kitini na kufungiwa mkanda ndege ilianza kuiacha ardhi ya Tanzania! Akiwa juu aliingalia Arusha na roho ilimuuma sana, picha ya mwisho aliyoagana na dada yake pamoja na Leah uwanjani ilimuumiza kupita kiasi alishindwa kuelewa ni kwanini Vicky alisisitiza kuwa safari yake ingekuwa na matatizo.

“Wasichana bwana anataka tukae tu kuangaliana wakati umasikini unatutesa! Litakalokuwepo mbele acha liwepo Mungu anajua!” Alisema Nicholaus huku ndege ikiondoka

Safari kutoka Tanzania kwenda Iran kupitia Nairobi,Misri, Uturuki na Iraq iliwachukua masaa 16! Wakati Nicholaus anapanda ndege kwenye uwanja wa Kia moyo wake ulijaa furaha kwa sababu ilikuwa ni mara ya kwanza lakini kadri masaa yalivyozidi kwenda alizidi kuchoka na kuichukia safari hiyo.

Ndege ilipotua katika uwanja wa ndege wa Tehran majira ya saa kumi na moja alfariji na abiria wote walianza kushuka kwa kutumia ngazi! Wakati Nicholaus anachukua Sanduku lake alishutkia anaguswa begani, aligeuza uso wake na macho yake yalikutana na sura ya AbdulAziz! Alifurahi kumwona kwa sababu tangu Tanzania hawakuongea kitu chochote walipishana kama wasiofahamiana.

“Tumefika Nicholaus sasa sikiliza, sisi tunatoka na tutakusubiri nje ya uwanja wa ndani ya gari la aina ya BMW jeusi, lililokuja kutupokea sawa si unaifahamu BMW?”

“Ndiyo nilikuwa naziosha sana Arusha, si kama ile ya Frank Mshanga wa Arusha?”

‘Huyo mtu hatumjui ila wewe utatukuta nje mbele ya lango la kutoka sawa?”

“Sawa?”

“Beba vizuri hilo Sanduku lako lisiibiwe!”Alimaliza AbdulAziz na kuondoka.

Kazi yao ilikuwa karibu kufikia mwisho kipingamizi pekee kilichokuwa mbele yao ni uwanja wa ndege wa Tehran! Walijua kitendo cha kukamatwa kwa wauza madawa wengine saba wiki moja tu kabla ya kupigwa risasi kilikuwa kimefanya ulinzi katika uwanja wa ndege uimarishwe zaidi.

“Tukivuka hapa tayari tumetajirika!” Alisema Samwel.

“Lakini kwa ninavyoiona hali siyo rahisi kuvuka!” Walibadilishana mawazo Samwel na AbdulAziz wakati wakitoka nje ya uwanja!

Upekuzi waliofanyiwa siku hiyo haukuwa wa kawaida kulikuwa na mbwa kama kumi walionusa kila abiria aliyepita langoni kutoka nje na walifanya hivyo pia kwa kila mzigo uliotolewa uwanjani.


Askari waligundua madawa katika Sanduku la Nicholaus kabla halijateremshwa lakini hawakutaka kulichukua waliiacha lipelekwe sehemu ya kupokelea mizigo ili wamwone mwenye sanduku alikuwa nani!

Masanduku na mabegi yalizidi kupita katika sehemu iliyozungukwa na kila abiria alichukua begi au sanduku lake lilipopita mbele yake, makachero wa kitengo cha kupambana na madawa ya kulevya nchini Iran walimwagwa sehemu hiyo kushuhudia ni nani angelichukua sanduku lenye madawa.

Nicholaus alizidi kuangalia wakati mabegi na masunduku yakizidi kuzunguka mbele yake, kwa muda kama dakika tano hakuliona sanduku lake na kuanza kuingiwa hofu lakini ghafla aliliona na kufurahi kwani alikuwa na hamu kubwa ya kutoka nje ya uwanja alione jiji la Tehran lilivyokuwa!

Kwake kuingia katika nchi tofauti na Tanzania akiwa na umri mdogo kama wake yalikuwa mafanikio makubwa mno katika maisha. Lilipomfikia sanduku lake alilichukua na kuanza kutembea kwa haraka kuelekea nje ya uwanja! Kabla hajatoka alishtukia kundi la mbwa kama saba hivi likimvamia na kumwangusha chini na kuanza kumuuma kila mahali.

Nicholaus alilia kwa maumivu aliyoyapata, polisi walikuja na kumkamata wakaanza kumpiga na virungu kichwani huku wakimvuta kumpeleka sehemu asiyoijua.

“Samweeeel! AbdulAziz njooni mnisaidie!” Alipiga kelele Nicholaus lakini hakuna aliyemjali alizidi kuvutwa, waliposikia majina yao yakiitwa Samwel na AbdulAziz walimwamuru dereva wao aondoe gari kwa kasi.

“Jamani mbona mnanipiga? Nina makosa gani mie?” Aliuliza Nicholaus kwa kiswahili lakini hakuna mtu aliyemwelewa, alivutwa na kupelekwa katika chumba kilichokuwa pembeni kabisa mwa uwanja na kuketishwa chini na kuendelea kupigwa bila kulielewa kosa lake.

Nicholaus alilia kwa maumivu akiwaomba askari wamweleze kosa lililowafanya wampige hakuna mtu aliyemwelewa walionekana kutoelewa kiswahili! Muda mfupi baadaye aliingia msichana mmoja mrefu wa Kiafrika na kuchuchumaa mbele ya Nicholaus aliyekuwa amelala chini akilia.

“Ninaitwa Joan Leon wewe mtoto unaitwa nani?” Aliuliza dada huyo katika kiswahili.

Nicholaus alishtuka na kusikia mtu akiongea kiswahili tena Mwafrika kama yeye, aliona amepata mkombozi! Aliruka na kumng’ang’ania msichana huyo miguuni.

“Nisaidie dada wanataka kuniua bila kosa wamenipiga mno bila kosa lolote tafadhali nisaidie dada nimefurahi kukuona mswahili mwenzangu,nisaidie dada wataniua!” Aliongea Nicholaus huku akilia machozi.

“Wewe ni nani?”

“Naitwa Nicholaus!”

“Nicholaus nani?”

“Martin!”

“Tanzania unaishi wapi?”

“Naishi Arusha!”

“Mimi ni Mtanzania naishi hapa Tehran nafanya kazi katika ubalozi wetu hapa, sasa naomba unieleze ni kwanini unafanya biashara ya madawa ya kulevya wakati unajua kabisa katika nchi hii adhabu yake ni kifo cha kupigwa risasi hadharani?”

“Madawa? Madawa gani dada yangu?”

“Haya yaliyomo ndani ya sanduku lako!”

“Ndani ya sanduku kuna madawa?Madawa gani?”

“Ya kulevya!” Alijibu dada huyo na kulifungua sanduku la Nicholaus na kumwonyesha paketi za madawa zilizokuwemo ndani, Nicholaus alitetemeka.

Nicholaus alielewa alikuwa ameingizwa katika mtego bila kujua! Alielewa ni kwa sababu gani Samwel na AbdulAziz hawakutaka kuongea naye tangu Arusha! Kumbe walimtumia kusafarisha madawa yao! Alilia kwa uchungu na aliyakumbuka maneno ya dada yake uwanja wa ndege!

Alipomkumbuka Vicky alilia zaidi alijua sasa alikuwa anakufa tena kwa kupigwa risasi mbele ya halaiki ya watu! Alipofikiria jinsi risasi zingepenya mwilini mwake alizidi kuchanganyikiwa zaidi! Hofu ilimtanda mwili mzima, aliumia kufa na kumwacha dada yake kipofu peke yake duniani, alijua ni shida kubwa kiasi gani iliyokuwa ikimsubiri Vicky mbele yake.

“Kifo changu kitamsikitisha sana Vicky na sijui atajuaje kama nimekufa, masikini yeye ataendelea kujua nipo hai!” Aliwaza Nicholaus huku akilia.


Mbele ya halaiki

Siku iliyofuata mamia kwa maelfu ya wakazi wa jiji la Tehran walifurika katika uwanja wa Al-akri, uliotumika kuulia wahalifu ili kushuhudia kifo kingine cha muuza madawa ya kulevya biashara iliyochukiwa na kila mtu nchini humo!

Hakuna aliyemsikitikia muuza madawa alipopigwa risasi ilikuwa furaha kubwa kwa watu wa Iran! Nicholaus alifungwa kwenye mti mkubwa kwa kamba nene na nzito huku akiwa amefungwa na kitambaa cheusi usoni! Askari kumi wakiwa na bunduki zilizojazwa risasi kikamilifu walisimama mbele yake wakiwa wamemlenga wakisubiri amri kutoka kwa mkuu wa kitengo cha kuuza madawa!

Nicholaus aliendelea kulia machozi akijieleza ni kiasi gani hakuwa na hatia! Lakini hakuna aliyejali watu wote kiwanjani walionekana kufurahia kifo chake. Mawazo yake yote yalikuwa kwa Vicky, aliumia kufa kumwacha dada yake peke yake duniani aliamini alikuwa akiwafuata baba na mama yake ahera.

“Kama ningemsikiliza dada yangu Vicky haya yote yasingenikuta!” Aliwaza Nicholaus akisubiri risasi ziupenye mwili wake, alihisi ganzi mwili mzima na hakujua jinsi ya kujiokoa.

“Nahesabu moja na nikifikisha tatu wote mtafyatua bunduki zenu mpaka risasi zote ziishe nataka huyu mtoto asambae kabisa! Hatutaki madawa ya kulevya katika nchi yetu au siyo wananchi?” Alisema mkuu na watu wote walishangilia.

Nicholaus alishindwa kuelewa ni kwanini watu wa Iran hawakuwa na huruma kiasi hicho!Aliendelea kumwomba Mungu afanye muujiza ili kumuokoa katika kifo hicho.

“Haya moja….mbili….!” Alihesabu mkuu.


Kwa wiki nzima Vicky alishinda na kukesha akilia machozi, alimlilia kaka yake Nicholaus waliyezaliwa naye mapacha! Leah alijitahidi kwa uwezo wake wote kumfariji lakini haikusaidia Vicky aliendelea kulia. Kwa siku tatu mfululizo alikaa bila kula wala kunywa kitu chochote, Leah alikwenda kazini asubuhi na aliporudi jioni alikuta chakula alichokiacha kipo vilevile, Vicky alikonda na kukondeana kiasi kwamba Leah aliogopa na kufikiri Vicky angekufa kwa njaa!

“Sikiliza Vicky maisha yetu unayajua Mungu hata kama ukilia miaka miwili haisaidii kitu kama Mungu amepanga Nicky asafari na kurudi salama atarudi tu! Wala usiwe na wasiwasi kula tu mdogo wangu yote mwachie Mungu kwani yeye ndiye anayeyafahamu maisha yetu, usiache kula utaharibu afya yako bure mdogo wangu!” Kila siku Leah alimbembeleza Vicky ikabidi hata kazini aombe ruhusa na siku ya nne Vicky alikubali kula tena lakini aliendelea kumlilia kaka yake.

****

Kwa Vicky maisha hayakuwa kamili bila kaka yake Nicholaus! Kila siku baada ya kwake ilijaa mawazo na simanzi!Kila mara alilia akimlilia kaka yake! Leah alijitahidi kufanya kila kilichowezekana kumsahaulisha fikra juu ya kaka yake lakini haikuwezekana, Vicky alizidi kupoteza uzito wa mwili wake!

Kipande cha noti alichoachiwa na kaka yake ndicho kilichomhuzunisha zaidi, hakuwa na uwezo wa kufanya nacho jambo lolote, asingeweza kukitumia kununua kitu chochote mpaka kipande cha pili kipatikane, kipande alichoondoka nacho Nicholaus.

“Mpaka Nicholaus arudi ndio pesa hii itatumika tena!”

Alishinda nacho na kulala nacho mkononi mwake, kwake kipande hicho kilikuwa ni kaka yake mara kwa mara alikibusu na kukisemesha kama anaongea na binadamu! Vicky alikuwa tayari kupoteza kitu kingine chochote katika maisha yake lakini si kipande hicho cha noti!

Kila jumapili siku ambayo Leah hakwenda kazini, alijitahidi kumchukua Vicky na kwenda nae mjini kutembea ili kumsahaulisha machungu aliyokuwa nayo lakini haikusaidia bado Vicky aliendelea kumlilia kaka yake kadri siku zilivyokwenda.

“Hakuna kilichobaki kwangu! Sina baba, sina mama na sina hata kaka mtu pekee niliyenaye ni wewe Leah na ninakushukuru sana bila wewe sijui maisha yangu yangekuwaje!” Alisema Vicky.

“Watu wote tunaweza kukuacha Vicky lakini rafiki mmoja tu hawezi kukuacha, unajua rafiki huyo ni nani?”

“Ni wewe!”

“Siyo mimi Vicky ni Yesu Kristo!”

“Ha! Leah ina maana na wewe ipo siku utaniacha?”

“Hakuna kinachoweza kunitenganisha na wewe ninakupenda mno Vicky!”

Tangu siku hiyo Vicky alijifunza kumtegemea Mungu katika kila kitu alichofanya, kila siku ya jumapili Leah alimchukua na kumpeleka kanisa ambako alimwomba Mungu amlinde kaka yake popote alipokuwa ili siku moja awakutanishe tena! Alishindwa kuelewa siku ya kukutana na Nicholaus angekuwa na furaha kiasi gani.

Hakuna hata siku moja aliyotembea bila kukichukua kipande chake cha noti, alikwenda nacho kanisani alikwenda nacho chooni na kwa kufanya hivyo aliamini alitembea na kaka yake na kufurahisha moyo wake, kila kumbukumbu za maisha yake ya zamani akiwa na wazazi wake, akiwa na macho yake mawili na jinsi ajali ilivyotokea zilipomwijia alishindwa kuvumilia na kulia machozi!

Maisha yake yalikuwa yamebadilika mno, kupoteza familia na ndugu lilimuumiza sana na kutoka katika familia yenye maisha ya kifahari hadi kuishi katika chumba kimoja ambacho yeye na Leah wakitandika na kulala kwenye jamvi kulikuwa ni kushuka kwa hali ya juu!

Leah alilifahamu jambo hilo lakini siku zote hakuwa tayari kuliongelea kwa sababu kwa kufanya hivyo alijua angemuumiza sana moyo Vicky! Siku zote alikaa kimya na kujifanya maisha yalikuwa yakienda kama kawaida.

“Usijali Vicky ipo siku maisha yetu yatakuwa kama zamani hasa Nicholaus akirudi!”

“Kweli dada?”

“Ndiyo!”

Kwa Vicky, Leah hakuwa hausigeli tena bali baba, mama na kila kitu alichohitaji.


Siku, wiki, miezi ilizidi kupita hatimaye mwaka ukapita Leah akiendelea kufanya kazi nyumbani kwa tajiri yake wa Kihindi aliyeitwa Shabir Hussein, alikuwa Mhindi tajiri na mwenye roho nzuri sana, alisaidia Leah kwa kila kitu alimiliki mali nyingi sana mjini Arusha, mashamba ya Mkonge mkoani Tanga ilisemekana pia alimiliki viwanda nchini Canada na Uingereza.

Siku ya kwanza aliyofika nyumbani walipoishi Leah na Vicky, Shabir alilia hakuamini Leah aliishi sehemu chafu kiasi kile, alimwonea huruma sana hasa alipomwona mtoto wa kike kipofu Vicky aliyeishi naye.

“Tangu sasa nitakusaidia Leah wala usiwe na wasiwasi wowote!”

“Nashukuru sana baba!” Hivyo ndivyo Leah alivyomwita mzee Shabir siku zote, alikuwa ni mzee mwenye umri wa miaka kati ya hamsini na sitini.

Wiki mbili baadaye Leah na Vicky walihama katika chumba kimoja walichoishi kwenda maeneo ya Sanawari ambako Shabir Hussein alimnunulia Leah nyumba ya vyumba vitatu iliyokuwa na uzio kabisa! Ilikuwa ni nyumba nzuri ya kifahari yenye kila kitu ndani mpaka seti ya televisheni, aliwawekea pia mfanyakazi wa ndani aliyepewa kazi ya kumtunza Vicky!

Kwa Leah hiyo ilikuwa ni bahati kubwa ambayo hakutegemea kuipata, siku ya kwanza aliyoingia katika nyumba hiyo na kulala kwenye kitanda na godoro kubwa wala hakuamini! Alifikiri ilikuwa ni ndoto! Kwa upande wa Vicky pamoja na kuwa kipofu bado alielewa kuwa nyumba waliyoishi ndani yake wakati huo ilikuwa ya kifahari, sauti za televisheni na redio zilimkumbusha maisha yake na wazazi wake kabla ya kifo chao kilichochukua kila kitu kutoka kwake na kumwacha masikini.

“Hivi ni kwanini Shabir ameamua kutusaidia kiasi chote hiki?” Hilo ndilo swali ambalo Leah alimuuliza Vicky mara kwa mara.

“Katuonea huruma!” Ndilo lilikuwa jibu la Vicky

“Kweli?”

“Ndiyo dada inaonekana ana roho nzuri sana!”

“Lakini nina wasiwasi kidogo!”

“Kwanini?”

“Basi tu!”


Tangu tajiri Shabir atoe msaada wake kwa Leah tabia yake nyumbani ilibadilika kiasi kikubwa, kila mara alimsifia Leah kwa nguo alizovaa na alimzuia kufanya kazi chafuchafu kama kuosha vyombo na kupiga deki chooni! Muda mfupi baadaye alileta wasichana wengine wawili kutoka Sengerema kufanya kazi za ndani Leah akawa anashinda bila kazi yoyote.

Kwa sababu hiyo Shabir aliamua kumhamishia kwenye moja ya maduka yake katikati ya mji wa Arusha akawa anamsaidia kuuza mali mbalimbali!

Miezi michache hali hiyo ilimfanya mke wa Shabir ahisi kulikuwa na kitu fulani kati ya mume wake na Leah, ilitokea hali ya kutoelewana kati yao nyumba ikawa haina amani Leah akilalamikiwa kuingilia ndoa yao jambo ambalo halikuwa na ukweli wowote.

Baadaye mke wa Shabir, Sandra alimshinikiza mumewe ili amfukuze kazi Leah au yeye aondoke kurejea kwao Bombay! Shabir hakukubaliana na hilo mkewe akaondoka kurejea kwao India! Hofu ilimsumbua Leah kuwa angeweza kudhurika lakini Shabir alimwondolea wasiwasi huo na maisha yaliendelea kama kawaida.

Shabir na mkewe waliishi katika ndoa kwa miaka ishirini bila kupata mtoto, hivyo alipoondoka kurudi India mkewe aliondoka na mabegi peke yake.

Kuondoka kwa mkewe kulimfanya Shabir awe mpweke katika maisha yake na ni kipindi hicho ndicho alianza kumwangalia Leah kwa jicho tofauti! Alianza kugundua alikuwa msichana mzuri, kwa mara ya kwanza aligundua alikuwa na mahipsi na alikuwa na chuchu zilizosimama.

Hakuwahi kugundua kuwa Leah alikuwa na mwanya na alipocheka aliyaacha vishimo katika mashavu vyake! Aliyagundua yote hayo kuanza kuchanganyikiwa kimapenzi taratibu, hakuvumilia kwa muda mrefu sana na kujikuta akitoboa kila kitu kwa Leah siku moja usiku wakifunga duka.

“Mimi penda veve Leah, wewe iko taka nini?Taka jumba? Au taka gari? Wewe sema mimi iko pesa bana, mimi taka veve zalia mimi toto juri sawa?”

“Hapana mzee Shabir haiwezekani mimi nakuheshimu sana siwezi kufanya hivyo!” Alikataa Leah tena akinyanyuka.

“Oho! Veve pana taka mimi siyo? Basi veve toka dani ya jumba yangu keso!” Mzee Shabir alipiga mkwara

Jibu la mzee Shabir lilimshtua Leah kwa maisha aliyokwishazoea isingekuwa rahisi kuyaacha tena! Alipofikiria kuondoka katika nyumba kubwa aliyopewa alishindwa, hakutaka kurejea katika maisha yake ya zamani.

Pamoja na kuwa umri wake ulikuwa mdogo mno alipoyafikiria hayo alijikuta akilegea mzee Shabir alipomkamata na kumtupa juu ya meza! Aliyoyafanya mzee Shabir kwa binti mdogo kama Leah siku hiyo yalikuwa ni unyama usioelezeka kwa kalamu wala karatasi.

Baada ya ukatili wa kumbaka alimbeba Leah hadi ndani ya gari lake kumrudisha nyumbani usiku huo huo, siku iliyofuata Leah alishindwa kunyanyuka kitandani na kwa siku nyingine tano zilizofuata alibaki ndani amelala chali! Vicky alipouliza juu ya kilichompata hakuwa tayari kusema ukweli, ilikuwa siri yake tena siri ya kufa nayo moyoni mwake.

Katika siku zote hizo tano Shabir alilala nyumbani kwa Leah akimuuguza kama mtu na mke wake na huo ndio ukawa mwanzo wa penzi lao zito! Miezi mitano baadaye Leah alijikuta mjamzito jambo lililomfurahisha sana mzee Shabir. Hicho ndicho kitu alichokitaka siku zote kutoka kwa mwanamke.

Mapenzi yake kwa Leah yalizidi ingawa wahindi wenzake walimtenga kwa sababu ya kuoa mwanamke wa Kiafrika bado hakujali alichotaka ni mtoto wa kurithi mali zake nyingi na tayari alikuwa amempata.

Leah akawa si mfanyakazi wa Shabir tena bali mpenzi wake na watu wote mjini Arusha walilielewa jambo hilo, haikuwa siri tena kuwa Shabir alimuoa mfanyakazi wake Leah! Mimba ilizidi kukua na hatimaye miezi tisa ilipotimia Leah alijifungua mtoto wa kiume mwenye sura sawasawa na baba yake waliyemwita Lanjit.

Maisha yao yaliendelea vizuri katika familia yao kitu pekee kilichomsumbua Vicky akilini mwake kilikuwa ni fikra juu ya kaka yake Nicholaus, alikuwa bado hajamsahau na bado alikitunza kipande cha noti alichoachiwa na kila siku alimkumbuka katika maombi yake ili Mungu ampe uzima.

“Leah mimi sasa taka chukua wewe moja kwa moja! Taka veve kuwa mke yangu ili tufunge doa yetu lakini lazima veve badili dini yako kuwa Muislam sawa?”

“Sawa tu haina shida! Naweza kubadili!”

“Kweli veve naweza?”

“Ndiyo naweza sababu Mungu ni mmoja!”

Wiki moja iliyofuata tayari Leah alishabadili dini yake na kuingia katika dini ya Uislamu jina lake likabadilika kuwa Fatma Shabir! Mpango wa kubadili dini ulifanywa kwa siri ili Vicky asielewe, lakini hicho hakikuwezekana kwani siku mbili tu baadaye Shabir alirudi nyumbani na kumwita Leah kwa jina la Fatma! Ilibidi Vicky aulize juu ya jambo hilo na kuelezwa wazi kuwa Leah alibadili dini!

Vicky alilia sana baada ya kusikia habari hiyo alihisi kusalitiwa na Leah, alijaribu kumuuliza ni kwanini alifikia uamuzi huo.

“Ninampenda Shabir na pia mwanangu Lanjit!” Hilo ndilo lilikuwa jibu lake.

Baada ya ndoa yao tabia ya Leah ilianza kubadilika, Vicky aliligundua hilo mapema! Mapenzi yake yalihamia kwa mtoto wake na mume wake zaidi kuliko ilivyokuwa siku za nyuma. Kila siku ya Ijumaa Leah alikwenda msikitini na siku za kawaida aliswali sala tano kama ilivyo taratibu katika Uislamu akawa ni mama wa Kiislamu haswa!


Shabir alimpiga marufuku mkewe Leah kukanyaga kanisani hilo lilimfanya ashindwe kumpeleka Vicky kanisani kusali kila jumapili, akawa anashinda nyumbani kwa sababu asingeweza kutembea peke yake akiwa kipofu!

Roho ilimuuma sana Vicky na kumfanya awe anasali chumbani kwake kila Jumapili kitu ambacho hakutaka kukifanya, zilipopita wiki mbili mfululizo bila Vicky kuonekana kanisani waumini waliamua kufuatilia, aliwasimulia kila kilichotokea walisikitika na siku iliyofuata ulipangwa utaratibu wa mtu kuwa anakwenda nyumbani kwao kumchukua na kumrudisha nyumbani baada ya ibada.

Jambo hilo lilimkera sana Shabir na hata Leah ambaye tayari alishaanza kumgeuka Vicky kwa sababu ya mume wake! Wao walitaka familia yao yote iwe ya Kiislamu lakini Vicky akakataa kufanya hivyo, jambo ambalo Shabir alilichukulia kama dharau na chuki yake dhidi Vicky iliongezeka maradufu hata salamu yake akawa hapokei.

Vicky alihisi tatizo lilikuwa likija mbele yake, kumbukumbu juu ya kaka yake ziliongezeka lakini alimwomba Mungu amuepushe na mabaya! Mara nyingi alimlilia Nicholaus lakini wakati huo hapakuwa na mtu aliyemjali wala kumbembeleza tena kama alivyofanya Leah kabla hajabadilika! Hali hiyo ilimzidishia Vicky machungu.


Mabadiliko ya mfumo wa ukusanyaji wa kodi na kuanzishwa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) nchini Tanzania kuliwaogopesha wafanyabiashara wakwepa kodi! Wengi walidai kodi ya Tanzania ilikuwa hailipiki.

Miongoni mwa wafanyabiashara hao alikuwemo Shabir, hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuamua kuhamia Canada nchi ambayo wafanyabiashara wengi wa Kiasia walikimbilia! Ilidaiwa Shabir alikuwa na nyumba aliyonunua miaka ya themanini, aliuza kila alichokuwa nacho na kuzituma pesa zote nchini Canada.

“Mke wangu nataka hamia Canada lakini iko kitu moja nataka veve saidia mimi! Mimi hapana jua kama veve itakubali”

“Kitu gani mume wangu?”

“Veve najua kuwa mimi hapana taka Vicky siyo!”

“Ndiyo!”

“Mimi na veve hamia Canada lakini mimi hapana taka ondoka na hiyo kipofu!”

Leah alishindwa kujibu swali hilo na kukaa kimya kwa muda akifikiria jinsi ya kufanya uamuzi! Picha ya wazazi wa Vicky na Nicky zilimwinjia kichwani mwake ghafla, aliukumbuka wema ambao walimfanyia, kwake bila wao asingefika alipokuwa! Roho ilimuuma sana alishindwa aamue nini kwani kumwacha Vicky peke yake nchini Tanzania akiwa kipofu ilikuwa ni sawa na kumtupa jalalani!

“Sikia?” Shabir alimuuliza tena.

“Ndiyo nimesikia mume wangu!”

“Sasa veve sema nini maana mimi tayari kwisha uza kila kitu kwa Karimjee na pesa imetangulia Canada, si ajabu tukaondoka wiki ijayo!”

Kabla hajajibu swali hilo mlango wa chumbani kwa Vicky ulifunguliwa akatembea peke yake huku akipapasa ukuta kuelekea sebuleni, alijikwaa na kuanguka mguuni kwa Leah! Alikuwa ameyasikia maongezi yao.

“Dada Leah, tafadhali kataa, usiniache peke yangu, nakupenda dada ni wewe pekee niliyekubakiza duniani usiniache tafadhali!” Aliongea Vicky huku akilia.

“Weee hebu nyamaza pesi hapana piga kelele, kama wewe taka mimi ondoka na wewe lazima ubadili dini vinginevyo utabaki hapahapa! Mpumbavu wewe tabadili au no?”

“Mimi! Mimi! Mimi!……!” Vicky hakumaliza sentensi yake kwikwi ikamshika akamwaga machozi

“Shabir hebu mwache mimi nitaongea naye!” Alisema Leah alipomwangalia Victoria na kushikwa na huruma ! Aligundua kitu walichokuwa wakikifanya yeye na mume wake hakikuwa sahihi ukizingatia wema ambao wazazi wa Victoria walimfanyia yeye.

“Jamani msiniache nitaishije mimi?”

Leah alimnyanyua Victoria kutoka chini alipokuwa amekaa akamsimamisha wima na kumshika mkono kisha kuanza kutembea nae kuelekea nje ya nyumba ambako wote walikaa chini kwenye msingi wa nyumba!

“Victoria!”

‘Naam dada!”

“Si Mungu ni mmoja au? Na ni nini kitatufikisha mbinguni je madhehebu yetu au matendo yetu?”

“Matendo yetu dada!”

“Unafikiri Uislamu au Ukristo wetu ndio utatufikisha mbinguni?”

“Hapana dada!”

“Sasa kuna ubaya gani wewe ukiingia katika Uislamu na ukaendelea kumwabudu Mungu wako na matendo yako yakaendelea kuwa mema mbele za Mungu?”

Victoria aliinamisha kichwa chake kwa kama dakika kama tano hivi akiwaza bila kumjibu Leah kitu chochote! Kwa harakaharaka kichwani mwake alizichambua dini moja baada ya nyingine na kuona zote zilimwambudu Mungu! Aligundua mtu anaweza kuwa Mkristo lakini bado akawa na dhambi nyingi na kuishia jehanamu na mtu mwingine anaweza kuwa Mwislam lakini akawa na matendo yasiyofaa akaenda jehanamu vilevile! Kwake tofauti ya madhehebu au dini ilionekana kukosa maana!

“Cha muhimu ni matendo yangu, dhehebu langu halitanifikisha mbinguni! Dada nimekubali kubadili dini tena kwa hiari yangu kwani Mungu ni mmoja!”

Leah alimkumbatia Victoria na baadaye wote walisimama wima na kuanza kutembea kurudi tena ndani ambako walimkuta Shabir amekaa kitini akiwasubiri, Leah alimpa taarifa hizo mumewe nae hakuamini alichokisikia alinyanyuka na kumbusu Victoria usoni.

“Victoria umekubali sababu ya kukulazimisha au?”

“Hapana shemeji maneno aliyonieleza dada kule nje yamenifanya nigundue hakuna tofauti yoyote, sote tunamwabudu Mungu mmoja na yatakayotufikisha mbinguni ni matendo yetu wala si madhehebu!”

Mzee Shabir alishangazwa sana na maneno ya Victoria aligundua kumbe haikuwepo sababu ya kutumia nguvu kumghasi alimshukuru mkewe kwa diplomasia aliyoitumia.

Siku tatu baadaye taratibu za dini ya Kiislam zilifanyika Victoria akawa amebadilisha dini na jina lake tangu siku hiyo likawa Fatma! Hali ilibadilika sana ndani ya nyumba yao hapakuwa tena na chuki kila mtu alionekana kuwa na furaha.

Siku kumi na sita baadaye mipango ya safari ilikuwa imekamilika ingawa ilifanyika kwa siri kubwa mzee Shabir hakutaka watu wafahamu alikuwa akiihama Tanzania sababu kubwa ya kufanya jambo hilo ilikuwa ni kukimbia na pesa nyingi alizokuwa akidaiwa kama kodi.

“Nitafikiria kitu cha kufanya ili kuudanganya ulimwengu kuwa tumekufa!” Alimwambia mkewe wakiwa wamelala na siku mbili baadaye alikuwa na mpango kamili kichwani mwake.

“Nitatega shoti hapa ndani siku ya kuondoka ambayo itasababisha moto utakaoichoma na kuiteketeza kabisa nyumba yetu kila mtu ataamini sote tumeteketea ndani ya moto! Sitaki kutafutwa sababu nitatoroka na pesa za serikali!” Aliendelea kusema mzee Shabir na wote walikubaliana juu ya jambo hilo bila Victoria kufahamu!


Ulikuwa ni usiku wa manane gari lilikuwa nje ya nyumba yao likiwa limejazwa mafuta tayari kwa safari, Vicky alivalishwa nguo nzuri na safi na hata Man`0jit mtoto wao naye alipendeza.

Ilikuwa ni safari ya kuiacha Tanzania nchi aliyozaliwa na kwenda ugenini ambako Victoria hakumfahamu mtu yeyote, woga ulimwingia moyoni lakini hakuwa na chaguo jingine zaidi ya kukubali kusafiri! Kila kitu alichokuwa nacho alikuwa anakiacha, mdoli aliyenunuliwa na mama yake akiwa mdogo na kumtunza mpaka wakati huo alikuwa anamwacha pia.

Alikuwa tayari kuacha vitu vyote lakini si kipande cha noti alichoachiwa na kaka yake Nicholaus, hicho alikuwa nacho mkononi! Aliamini ndio kitu pekee kilichomkumbusha juu ya pacha wake kwake kilikuwa ni sawa na Nicholaus mwenyewe.

Leah akiwa amembeba Manjit alimshika mkono Victoria na kumuongoza hadi nje ya nyumba ambako walipanda ndani ya gari, walimwacha Mzee Shabir ndani ya nyumba akikamilisha kazi yake maalum na dakika kama kumi hivi baadaye alitoka na kuungana nao ndani ya gari.

“Tayari!” Alimwambia mke wake aliyekuwa amembeba Manjit mkononi aliyekuwa akilia sababu ya baridi kali iliyokuwepo mjini Arusha siku hiyo.

“Kwa hiyo?”Leah aliuliza.

“Itawaka baada ya saa nzima hivi!” Alijibu kwa sauti ya chini chini mzee Shabir na kuanza kuliondoa gari lake kwa kasi.

Alichofahamu Victoria ni kuwa kutoka Tanzania kwenda Canada ilikuwa ni lazima kutumia usafiri wa ndege lakini alishangaa kuona wanaondoka kwa gari, alitamani kuuliza lakini moyo wake ulisita na kuamua kuvuta subira.

Safari ilikuwa ndefu na gari lilikimbia kwa kasi, kulipokucha walikuwa jijini Nairobi ambako mzee Shabir alishughulikia mipango ya usafiri na kuikamilisha. Walikuwa na uhakika hakuna mtu aliyefahamu walikuwa nchini Kenya kwa wakati huo, waliamini watu wote mjini Arusha walijua Shabir na familia yake waliteketea kwa moto.

“Au inawezekana moto haukuwaka?”

“Kwani hukutega vizuri shoti?”

“Niliitega vizuri sana na kama haitawaka basi nina uhakika watanitafuta na nitarudishwa tena Tanzania kushtakiwa kwa kukwepa kodi!”

“Siyo rahisi!” Alisema Leah huku akimpigapiga mzee Shabir begani.

Walifanya maongezi yao taratibu wakihakikisha Victoria hasikii kitu lakini muda mfupi baadaye Leah alionyesha mshtuko alipotupa macho kwenye luninga iliyokuwepo ndani ya hoteli waliyokuwa wakila chakula kabla ya kwenda uwanja wa ndege.

“Baba Manjit hebu ona kule kwenye luninga, ona! Ona! Ona!” Alizidi kumpigapiga mumewe begani ili aangalie.

Shabir alipogeuka kuangalia alikuta ni taarifa ya habari ya shirika la CNN! Nyumba ilikuwa ikiteketea kwa moto, kwa hakika ilikuwa nyumba yao! Watu wengi walionekana wamekusanyika kushangaa tukio hilo, magari ya zimamoto yalikuwa yakiendelea kuuzima moto huo kwa bidii.

Leah na mumewe walikaa kimya wakisikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa na mtangazaji wa televisheni aliyekuwa akiwasiliana na makao makuu kutoka eneo hilo la tukio.

“Inaaminika watu wanne wamefia ndani ya moto huu! Mwanaume mmoja na mkewe pamoja na watoto wao wawili!”

“Hakuna njia yoyote ya kuwaokoa?”

“Inavyoonekana hakuna!”

“Chanzo cha moto ni nini?”

“Hakijajulikana bado ingawa kuna habari kuwa chanzo ni shoti ya umeme!”

Aliposikia maneno hayo mzee Shabir aliruka juu na kushangilia kwa furaha kwani mpango wake wa kudanganya ulikuwa umefanikiwa! Watu wote ndani ya hoteli hiyo walishangazwa na kitendo cha kushangilia ajali, hawakuelewa nini ilikuwa sababu ya mzee Shabir kufanya hivyo.

Muda mfupi baadaye waliondoka kwenda uwanja wa ndege ambako walipanda ndege kwenda zao Ottawa!

“Hawatakuja kufahamu siri hii, nipongeze basi mke wangu!”

“Hongera sana darling!”

“Hivi wewe una kitu ulichosahau Tanzania?”

“Hata kimoja, sina baba wala mama, nini cha kufuata tena bongo!” Alisema Leah, sababu alikuwa yatima aliamini asingerudi tena Tanzania.


Nicholaus, Tehran:

Uwanja wa ndege wa Al- Akiri ulijaa mamia ya wakazi wa jiji la Tehran, haukuwa mkusanyiko wa kawaida bali watu wote walikuwa pale kushuhudia kifo cha muuza madawa ya kulevya, biashara iliyochukiwa na karibu kila mtu nchini humo.

Watu walishangilia kifo cha binadamu mwenzao! Nicholaus alikuwa amefungwa kwenye mti mkubwa macho yake yakiwa yamefunikwa kwa kitambaa cheusi!Alikuwa amekata tamaa kabisa ya maisha na mwili wake wote ulikuwa umekufa ganzi! Picha ya dada yake Victoria iliendelea kumwijia kichwani mara kwa mara.

Machozi yalizidi kumbubujika Nicholaus, alisikitika kufa ugenini na kumwacha dada yake aliyempenda Victoria! Alijilaumu kwa kitendo chake cha kukubali kuongozana na wauza madawa ya kulevya!

“Sina hatia jamani! Sina hatia hata kidogo!” Aliendelea kulia Nicholaus wakati mkuu wa jeshi akihesabu maaskari walitegemea akifikisha tatu wafyatue bunduki zao na kummaliza Nicholaus aliyekuwa amefunika macho yake akisubiri kifo.

Ghafla kabla mkuu wa jeshi hajafikisha tatu katika kuhesabu tatu! Ardhi ilianza kupasuka, kutikisika na kudidimia! Maghorofa marefu yalianza kuanguka lilikuwa ni tetemeko la ardhi baya kuliko yote yaliyowahi kutokea nchini Iran.

Watu walisahau kilichowapeleka uwanjani na kuanza kukimbia huku na kule kuokoa maisha yao hata maaskari walizitupa bunduki zao na kuanza kukimbia mbio, hakuna aliyekumbuka kumuua Nicholaus tena. Alibaki peke yake akiwa amefungwa kwenye mti

Nicholaus aligeuza kichwa chake na kuanza kukisugua kitambaa alichofunguwa nacho usoni kwenye mti ili aweze kuona vizuri, ilikuwa kazi ngumu lakini alifanikiwa kukishusha hadi mashavuni na kuanza kuona mbele!

Hakuyaamini macho yake alipojikuta yu peke yake eneo hilo! Na alishuhudia maghorofa makubwa na marefu yakidondoka na kusambaa ardhini, watu wengi walirushwa na kutupwa mbali na mawe makubwa yaliviringika hadi eneo alilokuwa amefungwa mengi yalitaka kumponda na mengi yalipita pembeni! Hakuwa na uhakika wa kuokoka.

Pembeni yake kulikuwa na majengo marefu yaliyokuwa yakiyumba na kuashiria yangeanguka wakati wowote na kumpondaponda kabisa Nicholaus! Kwa mara nyingine tena aliiona sura ya dada yake Victoria na kulia kwa uchungu.

Aliendelea kujaribu kuzikata kamba zilizomfunga mikononi mwake kwa meno lakini alishindwa kwani zilikuwa kamba nene na ngumu! Kwa mbali aliona kisu lakini alishindwa kukifuata sababu alikuwa amefungwa.

“Mungu wangu ninusuru mie mwanao, nilifanya makosa makubwa kumkimbia ndugu yangu Victoria! Najua baba Mungu unaniadhibu kwa kosa hilo, napenda kusema nampenda Victoria hata wewe unajua! Nisingemwacha ila ni kwa sababu ya shida nilizokuwa nazo na kama nitakufa basi Mungu nisamehe makosa yangu!” Alisali Nicholaus na baadaye kuendeleza sala ya ‘baba yetu uliye mbinguni’

Alipofungua macho yake kuangalia mbele baada ya sala hiyo, alishangaa kumwona msichana wa Kitanzania aliyekutana naye uwanja wa ndege akija mbio kuelekea mahali alipokuwa, Nicholaus akajua alikuwa amempata Mwokozi wa maisha yake, aliamini Mungu amejibu maombi yake.

“Njoo unisaidie dada!”

“Nakuja usiwe na wasiwasi!” Alijibu msichana huyo huku akikimbia na alipomfikia alimfungua kamba zote mikono na baadaye miguuni.

“Haiwezekani Mtanzania mwenzangu ufe hapa peke yako ni heri nikuokoe kaka yangu! Nilikuwepo tangu mwanzo lakini nilishindwa kukusaidia, tetemeko lilipoanza nilikimbia lakini mbele zaidi nikakukumbuka nikaamua kurudi kuja kukusaidia!” Alisema msichana huyo baada ya kumfungua Nicholaus kutoka mtini.

“Sijui nikushukuru vipi dada? Kwa kweli sijui jinsi ya kukushukuru ila Mungu atakulipa kwanza unaitwa nani”

“Ninaitwa Neema Lucas ila hayo yaache kwanza tutaongea baadaye cha muhimu tujiokoe hebu nifuate!” Msichana huyo alisema huku akimvuta Nicholaus na wakaanza kukimbia kwenda upande wa pili kulikokuwa na maghorofa mafupi kidogo.

“Tukifika kwenye mnara wa Khomein tutakuwa tumeokoka!” Alisema msichana huyo.

Mnara wa Khomein ulikuwa ni mnara wa kiongozi wa nchi hiyo, uliheshimiwa na kila mtu na ulijengwa katika eneo la wazi ambalo halikuwa na ghorofa hata moja, kila lilipotokea tetemeko nchini humo watu walikimbilia kwenye mnara huo! Ulikuwa umbali wa kama mita mia tano kutoka maeneo hayo lakini kulionekana mbali kwa jinsi hali ilivyokuwa.

Walizidi kukimbia lakini ghafla kilitokea kitu ambacho hawakukitegemea! Ardhi mbele yao ilipasuka na ghorofa kubwa na refu lilikuwa likiporomoka juu yao, kila mtu alijua lingewaponda lakini kabla halijatua chini, ardhi iliyopasuka iliwameza wakawa wameingia ndani ya shimo likawa sawa na kaburi! Ghorofa lilianguka juu yao, pande kubwa kama jiwe la udongo lilitua juu yao lakini halikuwafikia baada ya kuzuiliwa na vipande vya ardhi. Walikaa humo kwa takribani masaa mawili bila kupata msaada wowote.

“Dada Neema samahani kwa kukusababishia matatizo ninajua nia yako ilikuwa ni kuokoa maisha yangu lakini kwa bahati mbaya imeshindikana na sasa hata wewe maisha yako yapo hatarini, thawabu yako utaikuta mbinguni!” Alisema Nicholaus huku akitokwa na machozi.

“Usijali Nicholaus yote ni mipango ya Mungu!”

“Heri ningebaki tu na Vicky wangu!” Aliwaza Nicholaus huku Neema akiwa amemkumbatia juu yake wote wawili walikuwa wakilia machozi.

“Dada wewe kwenu ni mkoa gani nchini Tanzania?”

“Kagera kijiji cha Kanyigo!”


Pande kubwa la udongo lililokuwa juu yao lilizidi kushuka kadri ardhi ilivyozidi kutingishwa na tetemeko hatimaye liliteremka kwa kasi na kumponda Neema kiuno, alijaribu kujinasua lakini alishindwa! Akaanza kulia kwa maumivu akimwomba Nicholaus amuokoe.

“Niokoe Nicholaus, nisaidie Nicholaus nakufa!”

NIcholaus alijaribu kuchimba kwa chini ili amtoe lakini pia ilishindikana,roho ilimuuma sana kushindwa kumsaidia mtu aliyejitoa ili kuokoa maisha yake. Machozi ya uchungu yalimtoka, kuumia kwa Neema ilikuwa ni sawa kuumia kwa Victoria dada yake.

Baadaye jiwe lilizidi kumgandamiza na hewa ilizidi kuwa nzito na hawakujua nini kingewaokoa kutoka katika mlango wa kaburi, kitu walichokuwa na uhakika nacho kwa wakati huo ni kifo sababu ya kukosa hewa safi.

“Nicholaus nisaidie nakufa!” Neema alizidi kulia.

“Sawa nifanye kitu gani dada?”

“Nivute!”

Nicholaus alijaribu kumvuta kwa nguvu zake zote lakini pia haikuwezekana Neema alizidi kulia hatimaye alinyamaza kimya kwa muda wa dakika kama kumi, aliporejea ni neno moja tu alilosema.

“Nisalimie Tanzania kama ukiokolewa!” Alisema Neema kisha akakaa kimya! Nicholaus alilia machozi ya uchungu na huruma!


Ndege iliingia katika uwanja wa ndege wa Ottawa masaa kumi na mawili baadaye, kila mtu alikuwa amechoka vibaya mno na safari lakini Victoria alichoka zaidi, pamoja na hali hiyo bado kipande cha noti alichoachiwa na kaka yake kilikuwa mkononi mwake! Mawazo yote yalikuwa kwa Nicholaus, alishindwa kuelewa yeye na kaka yake wangekuja kukutana vipi maishani mwao kwa umbali aliokuwa amekwenda! Lakini bado aliamini ipo siku wangeonana.

“Hapa ndio Ottawa, Canada! Tutaishi hapa maisha yetu yote!” Mzee Shabir alimwambia Leah baada ya kufika kwenye nyumba aliyonunua kwa pesa aliyopaa kwa ukwepaji wa kodi, alioufanya nchini Tanzania.

Jiwe hilo kubwa lilizidi kushuka na kumkandamiza Neema kifuani, alilia akimwomba Nicholaus msaada lakini alishindwa afanye nini kumsaidia Neema matokeo yake alianza kulia!

Neema hakusema kitu tena baada ya jiwe hilo kumgandamiza kifuani, tayari alikuwa amekufa! Nicholaus alimpapasa mdomoni na kugundua alikuwa hahemi tena, ingawa hata yeye alijua angekufa muda si mrefu sababu ya kukosa hewa au njaa bado aliumia moyoni kuona mtu aliyejitolea kuokoa maisha yake akifa! Alimshika kichwani na kuanza kumuombea akimshukuru Mungu kwa kazi aliyoifanya na bado alimuomba Mungu amnusuru na kifo kilichokuwa mbele yake ili siku moja aonane na dada yake Victoria.

Pamoja na kumuomba Mungu amuokoe na kifo kichwani mwake bado wazo la kusakwa liliendelea kuwemo! Alijua mpaka wakati huo bado alikuwa akitafutwa na ingawa alinusurika kifo cha risasi kimiujiza bado adhabu hiyo ilikuwa ikimsubiri kama tu angetiwa mikononi na serikali ya Iran iliyopiga vita madawa ya kulevya kwa nguvu zote.

Lawama zake nyingi alizitupa kwa Samwel na AbdulAzizi waliomdanganya na kutaka kumtumia kusafirisha madawa ya kulevya kwenda katika nchi hatari kama Iran, mpaka wakati huo hakuamini kama aliondoka Tanzania kumkimbia dada yake bali kwenda kutafuta maisha bora zaidi baada ya yeye na dada yake kudhulumiwa na ndugu mali zote walizoachiwa na marehemu wazazi wao.

“Kama si tetemeko la ardhi kutokea hivi sasa ningekuwa maiti, sijui Victoria angefahamu vipi kuwa nilikufa!” Aliwaza Nicholaus

Ghafla mawazo ya kijasiri yalimwijia kichwani mwake na kujikuta akipata nguvu za ajabu, hakuwa tayari kufa katika shimo hilo tena, alitaka kutoka nje lakini alishindwa angetoka vipi! Mawazo hayo yalimfanya ajikute akipiga kelele kwa nguvu kuomba msaada lakini sauti yake haikufika mbali kwa sababu ya kuzungukwa na udongo sehemu zote!

Hakuchoka kufanya hivyo bali aliendelea kupiga kelele zaidi na zaidi akiamini hatimaye sauti yake ingesikiwa na labda angejitokeza mtu akachimba juu na kumtoa ndani ya shimo alilokuwemo!


Hakuna msaada uliojitokeza na kwa siku nne mfululizo Nicholaus aliendelea kukaa ndani ya shimo hilo akisubiri kifo chake! Maiti ya ilikuwa pembeni mwake ikiendelea kuharibika! Ilivimba na kutoa harufu kali kupita kiasi, hewa yote iliyokuwemo ndani ya kishimo kidogo alichojificha ilijaa harufu lakini Nicholaus aliizoea harufu hiyo na kuna wakati hakuisikia kabisa.Ilikuwa si rahisi hata kidogo kuamini maiti iliyokuwa imevimba kiasi hicho ilikuwa ya msichana mrembo Neema.

Ilikuwa si rahisi kufahamu upi ulikuwa mchana na upi ulikuwa usiku ndani ya shimo alilokuwa, kwa siku zote nne aliendelea kupiga kelele bila kukoma akijua msaada ungepatikana, njaa kali pamoja na kiu ya maji ilimsumbua kiasi kwamba hadi siku ya tano ilipofika bila kunywa maji wala kula hakuweza tena kupiga kelele, nguvu zilimwishia akalala pembeni ya maiti ya Neema iliyovimba na kusubiri kifo chake! Alikuwa na uhakika asilimia mia moja angekufa.

Nicholaus aliendelea kukishika kipande cha noti mkononi mwake kilimkumbusha mengi kuhusu dada yake na hata nchi yake Tanzania! Ni fikra juu ya dada yake na pacha wake Victoria zilizomfanya azidi kulia machozi ya huzuni, Nicholaus alisikitika kufa akiwa mbali na Tanzania, kilichomuumiza zaidi ni kuwa dada yake asingeiona wala kuigusa maiti yake na angeendelea kuamini alikuwa hai!

Alitamani mambo yabadilike na arudi tena Tanzania kama ingetokea hivyo aliuahidi moyo wake kutofanya makosa kama aliyoyafanya maishani mwake, angeishi na dada yake siku zote za maisha yake. Mawazo juu ya dada yake yalimtia huzuni kupita kiasi na alijilaumu kwa kitendo cha kuondoka na kumwacha!

Kila kumbukumbu za siku ya mwisho uwanja wa ndege wa Kilimanjaro zilipomwijia alimwona dada yake akilia na kumwomba lakini alimpuuza akimwona ni msichana asiyejua kitu kumbe Mungu alishamuonyesha kila kitu kilichokuwa mbele ya kaka yake, Nicholaus alilia zaidi.

Mpaka wakati huo Nicholaus hakuwa jinsi yoyote ya kujiokoa zaidi ya kusubiri kifo chake mwili wake ulizidi kupoteza nguvu sababu ya njaa kali aliyokuwa nayo mpaka kiasi cha kushindwa hata kufungua macho na mdomo wake.


Nchi ya Iran ilikuwa imekumbwa na pigo kubwa, hapakuwahi kuwepo na tetemeko kubwa la ardhi kiasi hicho katika muda wa miaka ishirini kabla, idadi ya watu wasiopungua elfu moja waliaminika kufa na wengine zaidi ya elfu tatu walikuwa majeruhi.

Serikali ya nchi hiyo ilitangaza siku tatu za maombolezo wakati shughuli za uokoaji zikiendelea kwa nguvu zote. Hali ilishatulia na tetemeko halikuwepo tena, mashirika mbalimbali ya kupambana na majanga yalikuwa yakifukua ardhini kuondoa udongo na kuwaokoa watu waliofunikwa na udongo. Maiti nyingi zilitolewa na watu wachache walikuwa hai.

Shughuli ya uokoaji iliendelea usiku na mchana kwa siku nne, siku ya tano serikali iliamua kusitisha zoezi hilo kutoa nafasi kwa mazishi ya kitaifa kufanyika! Maiti nyingi zilizikwa katika makaburi ya pamoja, mamia kwa maelfu ya wananchi wa Iran walihudhuria mazishi hayo, watu ambao hawakuokolea katika siku hizo tano walihesabika kama wafu na kuhesabika wamezikwa hukohuko ardhini!


“Hawa hapaaaaa!” Alipiga kelele mmoja wa watu waliokuwa wakifukua chini ya ardhi kwa kutumia vijiko vya katapila baada ya kuona miili miwili ya watu! Mmoja ukiwa umevimba sana na uligandamizwa na jiwe kubwa. Watu wote wakiwemo mzee Mohamed walikimbia mbio hadi mahali kelele hizo zilipotokea.

“Sio wenyewe lakini hebu watoeni tu, huyo mmoja anaonekana amekufa lakini huyu mtoto bado hajafa mkimbizeni hospitali haraka ikiwezekanavyo!” Alisema mzee Mohamed na jambo hilo lilifanyika kwa haraka.

Maiti ilichukuliwa na kupelekwa chumba cha maiti cha hospitali ya Tehran Muslim Agency na mwili wa kijana ulipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi kwa matibabu!

“Huyu kijana hana tatizo jingine zaidi ya njaa! Lakini amewezaje kuishi huko chini bila hewa kwa siku zote hizi?”

“Hata mimi nashangaa sana au kulikuwa na matundu yaliyopitisha hewa?”

“Inawezekana!”

Waliendelea kuongea madaktari huku wakimwekea kijana huyo dripu za maji ya chakula katika mishipa yake na baada ya kugundua alikuwa ameishiwa sukari mwilini mwake pia aliwekewa mashine ya hewa safi ya oxygen li kumsaidia katika kupumua. Ngozi yake ilikuwa bluu kwa sababu ya kukosa hewa safi!

“Yuko cynotic kabisa!” Alisema daktari mmoja akimaanisha kuwa ngozi ya kijana huyo ilikuwa ya bluu sababu ya kukosa oxygen.

“Lakini hii oxygen anayopata itamsaidia!”

“Sijui huyo mtoto mwenyewe ni raia wa wapi? Anaonekana kama kuwa raia wa nchi ya Kiafrika!”

“Au ndiye alikuwa apigwe risasi sababu ya madawa ya kulevya kabla ya tetemeko?” alisema daktari mmoja huku akimwangalia kijana huyo usoni kwa makini!”

“Hapana si huyu!” Alisema daktari mwingine huku akimgusagusa kijana huyo usoni.

“Lakini anaonekana ni yeye subiri uvimbe ukipungua usoni kwake tutagundua sura tofauti na hii!”

“Inawezekana lakini sidhani kama ni huyu!”

“Hivi ingekuwa vipi kama mzee Mohamed asingejitolea kutafuta maiti za mke na mtoto wake?”

“Angekufa nasikia hata maiti ya mke na mtoto wake hajazipata ilikuwa bahati ya kijana peke yake!”


Kwa siku saba kamili kijana huyu aliendelea kulala kitandani bila kujitambua, maji ya dripu yaliendelea kuingia katika mishipa yake na kumtia nguvu mwilini taratibu, kila mtu alikuwa na matumaini angepona na kurejewa na fahamu lakini haikujulikana ni lini, madaktari walishasahau kumchunguza sura tena walibanwa na kazi nyingine.

Siku ya nane usiku wa manane kama namba yenyewe ilivyo kijana huyo alishtuka na kufumbua macho yake, alijikuta yu peke yake kitandani. Alikuwa ndani ya chumba ambacho hakukielewa, aliangaza macho yake huku na kule na kugundua mahali alipokuwa palikuwa ni hospitalini.

Alishindwa kuelewa alikuwa pale kwa sababu gani, dakika thelathini baadaye alipojaribu kuvuta kumbukumbu zake vizuri alikumbuka kila kitu kilichotokea na kufumba macho kwa woga! Kimbukumbu zilizomwijia zilionyesha picha yake akiwa amefunga kwa kamba kwenye mti na watu wenye bunduki walisimama mbele yake wakisubiri amri kutoka kwa mkuu wao ili wammalize kwa risasi.

Kumbukumbu zilizidi kumiminika akalikumbuka hata jina lake kuwa aliitwa Nicholaus na kumwona mkuu wao akihesabu namba na wenye bunduki walisubiri namba tatu itajwe ndipo wakamilishe kazi yao, kabla mkuu hajaifikia namba hiyo ardhini ilianza kutetemeka na maghorofa yalianza kuyumba na mengine kuanguka yakiwagandamiza watu.

Watu walikimbia huku na kule na kumwacha Nicholaus peke yake, baadae alimwona msichana mwafrika akija mbio na kufungua kamba walianza kukimbia naye lakini mbele ardhi ilipasuka na wakatumbukia!

“Wasalimie Tanzania ukiokolewa” Aliyakumbuka maneno ya mwisho ya msichana huyo kwake.

Nicholaus alilia machozi hapo hapo kitandani hakukumbuka ni namna gani alitolewa katika shimo alikokuwa amebanwa na kujikuta hospitali. Huo ulikuwau ni kama muujiza na alipousikiliza vizuri mwili wake aligundua ulikuwa na nguvu nyingi kuliko kawaida! Alikuwa na uwezo wa kujiokoa.

“Wakinikuta hapa ni lazima watanikamata na kunipiga risasi tena! Ni lazima niondoke!” aliwaza Nicholaus na kuanza kuangalia kila pembe ya chumba, watu wote ndani ya chumba hicho walikuwa wamelala fofofo! Hata muuguzi ofisini alikuwa amelala juu ya meza!

Aliuona huo kuwa wakati muafaka wa kuondoka na kuokoa maisha yake! Alipoangalia saa ya ukutani iliyokuwemo wodini ilionyesha saa tisa na nusu ya usiku ulikuwa ni usiku mkubwa mno kwake kutoroka kwani hakufahamu sehemu yoyote katika nchi ya Iran lakini hakuogopa.

Asingeweza kusubiri hadi asubuhi huku akijua angeingia mikononi mwa polisi na kuuawa kikatili! Alizichomoa sindano zilizokuwa katika mishipa yake na akaufyatua mfuniko wa mashine ya oxygen uliokuwa mdomoni mwake na taratibu alishuka na kuanza kutambaa chini kwa chini kuelekea mlangoni hakuna mtu aliyemwona alikuwa ameamua kuondoka hospitalini kwenda kusikojulikana.

Nje ya wodi alinyanyuka na kuanza kutembea akiiacha wodi na kupita chini ya miti mingi ya Misonobari iliyokuwepo katika mazingira ya hospitali hiyo, hali ilikuwa kimya na ya kiza! Katika muda huo wa usiku karibu kila mtu alikuwa usingizini, Nicholaus alimwomba Mungu asionekana mtu yoyote kwani kama jambo hilo lingetokea angekuwa amechungulia kaburi tena!

“Lakini kama Mungu ameniokoa na matatizo yote yaliyopita kwanini asininusuru na leo?” aliwaza Nicholaus huku akiingiza mkono mfukoni mwa suruali aliyovaa lengo likiwa ni kukitafuta kipande cha noti alichokwenda nacho kila mahali lakini hakukiona!

Hakutaka kupoteza muda wala kufikiria mara mbili, kwake kupoteza kipande hicho cha noti ilikuwa ni sawa na kifo cha dada yake, alianza kukimbia mbio kurudi wodini bila kuwaza angekamatwa au la! Alijua angeweza kukamatwa lakini hakujali, alipoikaribia wodi alianza kutambaa tena.

“Haiwezekani, siwezi kuondoka hapa bila Victoria wangu!” Alisema kwa sauti ya chini kwake kipande hicho cha noti kilikuwa ni sawa na dada yake mpendwa kukiona ilikuwa ni sawa na kumwona Victoria.

Nicholaus aliingia wodini na kuendelea kutambaa hadi kitandani kwake ingawa hakuwa na uhakika kama nguo zake zilikuwepo alijikuta akifungua kabati lililokuwepo pembeni mwa kitanda chake! Hakuamini alipoona suruali pamoja na shati lake vikiwa vimefungwa pamoja kwa kamba!

“Alhamdullilah” Alijikuta akitamka neno la Kiarabu bila kutegemea kwa furaha aliyoipata, alichukua nguo zake na kutambaa tena hadi nje bila kugundulika ambako alivua nguo za hospitali na kuvaa nguo zake.

Alipoingiza mkono ndani ya mfuko wa kulia ya suruali yake alikikuta kipande cha noti! Furaha aliyoipata ilikuwa haielezeki, ilikuwa ni kama kukutana na Victoria ana kwa ana, Nicholaus tayari kupoteza chochote katika maisha yake lakini si kipande hicho cha noti! Alikipiga busu na kuendelea na safari yake kutoka nje ya eneo la hospitali.

Hospitali ya Tehran Muslin Agency ilimilikiwa na shirika la Kiislam na ilikuwa na chuo kikuu cha mifugo na ilijishughulisha na utafiti mbalimbali wa wanyama, hasa mamba, ilikuwa na bwawa kubwa lililofuga mamba wengi pembeni mwa chuo hicho, watu walizuiliwa kupita katika maeneo hayo sababu ya usalama wao, watu zaidi ya kumi walishadumbukia katika bwawa hilo na kuliwa na Mamba katika kipindi cha miaka kumi na tano kabla! Nicholaus alitembea taratibu kuelekea lilikokuwa bwawa hilo kwa sababu ya giza hakukiona kibao kilichozuia watu kupita maeneo hayo!

Mita kama hamsini kulifikia bwawa alishtukia kundi kubwa la mbwa wakija huku wakibweka nyuma yake, walikuwa wakimfukuza yeye, aliogopa na kuanza kukimbia kwenda mbele bila kujua kulikuwa na bwawa la Mamba! Ghafla alishangaa mguu yake wa kulia ulibodumbukia ndani ya bwawa na kuanguka majini! Alisikia mlio wa maji ukija mbio kuelekea mahali alipokuwa, ni kama kitu kilikuwa kikimfuata lakini hakikutoa sauti! Suruali na shati lake vilikuwa kama vimenasa kwenye kitu kwa nyuma.

ITAENDELEA

Dimbwi la Damu Sehemu ya Tatu

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment