Noti Bandia Sehemu ya Kwanza
KIJASUSI

Ep 01: Noti Bandia

SIMULIZI Noti Bandia
Noti Bandia Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA: BEN R. MTOBWA

*********************************************************************************

Simulizi: Noti Bandia

Sehemu Ya Kwanza (1)

JIJI la Dar es Salaam linatingishika, wezi sugu wanaingiza noti bandia, watu wanaibiwa. Baadhi wanauza majumba, magari na viwanja. Wafanyabiashara hatari wa dawa za kulevya nao wanacharuka, wanatangaza hali ya hatari kwa atakayeonesha kuwaingilia. Patashika linatokea, Dar es Salaam inakumbwa na misukosuko na mauaji ya kutisha.

“Kama unayathamini maisha yako jiweke pembeni”. Amri inatolewa, “Vinginevyo yatakupata makubwa”. Onyo linatolewa kila pembe ya jiji. Polisi wanagwaya, mauaji ya kutisha yanatokea, tishio linakuwa kubwa zaidi. Rais anapaza sauti, “Lazima hali hiyo ikomeshwe vinginevyo, hatuwezi kuvumilia…”.

Mashujaa kadhaa wanajitokeza kuikabiri hali hiyo. Maiti zao ziokotwa kando ya bahari. Teacher anatua uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kukabiliwa na mtihani mkubwa, gari lake linashambuliwa, anaponea chupuchupu. Lakini anaapa kuikabibiri hali hiyo ngumu. SASA ENDELEA.

NDEGE ndogo ya kukodi ya Kampuni ya ndege za Coastal ilishuka taratibu kwenye uwanja wa ndege wa mjini Musoma, baada ya kuwa angani kwa takribani dakika ishirini na tano hivi ikitoka katika Jiji la Mwanza. Mara baada ya ndege hii kutua kwenye uwanja huu, ulioko karibu kabisa na ukingo wa Ziwa Victoria, eneo maarufu la Makoko, nilikuwa miongoni mwa abiria watatu tuliosafiri kwa ndege hii kutoka Mwanza ambako tulibadilishiwa ndege.

Hii ilitokana na uwanja wa ndege wa Musoma kutokuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa kwa sasa. Baada ya ndege hii kutua, nilitwaa mfuko wangu mdogo uliosheheni vifaa vyangu muhimu vya safari, taratibu nikavuta hatua kutoka ndani ya ndege hii nikiwa tayari kuelekea nje.

Sikuwa na sababu ya kwenda haraka kutokana na hali ya ndege hii kuwa ndogo, hivyo nilisubiri wenzangu watoke kwanza ndipo nami niweze kutoka. Baada ya kukanyaga ardhi ya mji wa Musoma nilitembea taratibu, mkoba wangu begani, nilipita mapokezi na sehemu ya mapumziko ya wageni mashuhuri, nikaelekea kwenye maegesho ya magari ya kukodi nje ya uzio wa uwanja.

Hali ya hewa ya mji wa Musoma ilikuwa ya kuvutia sana, wingu zito lilitanda angani, kuashiria dalili ya mvua. Hali kama hii pia tuliikuta tuliposhuka kwenye uwanja wa Mwanza ambako tulikuta mvua ya kutosha. Kiasi fulani nilivutiwa na hali hii ya ubadiridi hususan kutokana na joto kali nililoliacha Jijini Dar es Salaam.

“Haraka, nipeleke Mkendo tafadhali”, nilimwambia dereva teksi, baada tu ya kuingia na kuketi ndani ya gari yake iliyokuwa imeegeshwa karibu na sehemu niliyotoke.

“Sawa mzee”, alisema dereva huyo huku akiwasha gari na kufunga mkanda, nami nikafanya hivyo. Wakati anaanza kuondoka aliuliza, “Mkendo ipi?”, alihoji dereva huyo huku akiondoa gari taratibu kutoka kwenye maegesho ya uwanja wa ndege.

“Mkendo… Nadhani utaniacha baada ya njia panda ya mtaa wa Iringo”, nilimwambia.

“Nadhani dakika tano”, alisema huku akiingia kwenye barabara kuu ya Majita, akaongeza mwendo tukaelekea katikati ya mji. Baada ya kuzipita ofisi za Shirika la Umeme Tanzania Tanesco, nilivunja ukimya uliodumu kwa dakika kadhaa.

“Vipi hali ya samaki katika mji huu, wanapatikana?”, nilimuuliza, taratibu akageuza shingo kunitazama, kiasi fulani alionekana kushangazwa na swali langu.

“Samaki!… alihoji kwa mshangao.

“Ndio… Mbona kama imekushituawa sana, wanapatikana?”.

“Samaki bwana ni wengi sana. tatizo ni bei. Samaki kama Sato wanauzwa kwa bei mbaya sana, viwanda vimeleta shida, minofu ya samaki katika mji huu ni lulu, inasafirishwwa nje ya nchi, wakazi wa hapa tunaachiwa mifupa”, alisema kwa utani huku akinitazama usoni akicheka.

“Mifupa ya samaki?”, nilimuuliza. Niliwahi kusikia kuwa idadi kubwa ya samaki wanaovuliwa Ziwa Victoria wanapelekwa viwandani na kusafirishwa nje ya nchi, wenyeji wanaambulia mfupa mkubwa wa katikati na kichwa. Maelezo yake yalinifanya nihamasike kuuliza maswali mengine zaidi.

“Hiyo mifupa unayodai kuwa ndiyo inauzwa kwa wananchi, inafaa kuwa chakula?”.

“Samahani kaka, wewe ni mgeni katika mji huu?”, alihoji kijana huyu ambaye umri wake haukutofautiana sana na wangu.

“Mgeni mwenyeji, ni mzaliwa halisi wa mkoa huu, nimeishi sana mjini hapa, enzi zetu tulipokuwa wadogo samaki walikuwa wengi sana, sato, sangara, nembe ilikuwa usiseme, ukishuka Mwigonero samaki wa kumwaga, nasikia siku hizi hawapatikani ndiyo nashangaa”, nilimwambia wakati anaingia kwenye mzunguko wa barabara za Nyerere na kuacha ile ya Sokoni.

“Umewahi kuona mabaki ya samaki yaliyoondolewa minofu ikabaki mifupa, hapa mkoani yanaitwa mapanki. Umewahi kuyaona?”, aliniuliza.

“Hapana?”.

“Basi labda nikudokeze, mapanki ni sehemu ya samaki waliotolewa minofu kwa ustadi mkubwa na kubaki kichwa na mfupa mkubwa wa katikati, mabaki ambayo huuzwa tema kwa watu wa kipato cha chini, hii inatokana na bei ya samaki kuwa juu sana. Ndiyo hali halisi ndugu yangu, samaki tunawasikia kwenye bomba tu huko viwandani”, alifafanua kijana huyu.

“Aisee, sasa nimekupata. Kumbe ndivyo ilivyo…”, nilinyamaza kidogo nikitafakari kisha nikamuuliza. “Kwanini serikali isiingilie kati, kuwasaidia wananchi wapate maisha bora, nina maana kuwa yatengwe maeneo ya wavuvi wa samaki kwa ajili ya wananchi wenye kipato cha chini, viwanda navyo vinunue kwa bei ya juu kidogo ili kuweka usawa”.

“Nchi hii kaka, wananchi hawana maamuzi, tumewapa wenzetu dhamana wanaitumia kujinufaisha wao na matumbo yao, tatizo pia liko kwetu wabongo, tunajua kulalamika tu lakini hatuna maamzi ya kukataa jambo”, alisema, baadaa ya kunyamaza kwa sekunde kadhaa, akageuka kunitazama. Labda hii serikali mpya italeta maisha bora”.

“Labda, tusubiri tuone, maana watendaji ni walewale walioshindwa”, nilimwambia akacheka.

Baada ya kupita kwenye mzunguko wa Barabara ya Nyerere, tukauacha mtaa wa Sokoni, tukaingia kwenye Barabara ya Nyerere, baada ya kituo cha mafuta cha GAPCO karibu na ilipokuwa karakana ya mabasi ya United. Sambamba na uwanja wa shule ya msingi Mkendo, tukaingia kushoto ulipo mtaa mdogo wa Rutiginga, moja mitaa yenye historia kubwa mjini Musoma. Inasemekana mtaa huu ndiyo wa kwanza kuwa na kinadada wanaouza miili yako. Baada ya kuuacha mtaa huu wa Rutiginga, moja kwa moja tukatokea barabara kuu ya Mkendo.

“Nimelazimika kupita njia hii kukwepa msongamano wa magari eneo la standi ya mabasi, muda huu kunakuwa na foleni kidogo”, alisema wakati akisubiri kuingia mtaa wa Mkendo.

“Usijali, mitaa hii naifahamu vizuri pengine zaidi kuliko wewe, hata tungepita barabara ya Uhuru bado ilikuwa sawa tu”, nilimwambia akatabasamu wakati akisimama mbele ya studio ya Issa Mkate, nilitoa kiasi cha pesa nikampatia akashukru na kuondoka.

Nilikuwa nimewasili mkoani hapa kwa likizo fupi ya upendeleo, niliyopewa na Mkuu wangu wa kazi, Kanali Benny Emilly, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi. Lakini kabla ya kuondoka Dar es Salaam nilipanga ratiba fupi ya kuonana na watu kadhaa. akiwemo rafiki yangu kipenzi Luteni Kanali Charles Matumbi anayeishi mtaa huu wa Mkendo.

Kwa mjibu wa ratiba yangu mjini Musoma sikuwa tayari kuonana na mtu zaidi na Luteni Kanali Matumbi, nikihofia kuharibu ratiba yangu, kwani nilipanga pia kufika kijijini kwetu Nyamuswa, Wilayani Bunda ambako nilipanga kukutana na mama yangu mzazi niliyempenda sana. Baba yangu niliyempenda sana alikwisha tangulia mbele ya haki. Nimekuwa nikijiuliza maswali maswali mengi kwa nini Baba yetu tuliyempenda alikataa kula chakula hata akadhoofu na kupoteza maisha. Hii ni siri ya Mungu aliyetuumba na kutufanya tuishi kwa muda katika ulimwengu.

Likizo hii fupi ilitolewa na Mkuu wangu wa kazi Kanali Emilly kwa upendeleo, baada ya ofisi yake kupokea hati ya utambulisho wa kimataifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutambua mchango wa utendaji kazi wangu nikiwa mlinzi wa amani wa umoja huo. Baada ya kushiriki kazi za ulinzi wa amani katika mipaka mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania. Kazi niliyofanya kwa uaminifu mkubwa, nikiwa mkuu wa operesheni za kijeshi kwenye baadhi ya mipaka.

Kwa takriban miaka miwili nilihudhuria kozi na masomo mbalimbali ndani na nje ya nchi yetu na kutunukiwa vyeti na shahada mbalimbali, katika ngazi za Ukamanda, Utawala na Ukufunzi katika Shule na Vyuo vya Kijeshi vya ndani na nje ya nchi. Uangalizi wa Amani katika kituo cha SADC Regional Peacekeeping Training Centre, kilichopo Harare Zimbabwe, ambako nilirudi kufundisha kozi fupi za ‘UNITED NATIONAL MILITARY OBSERVARS’ na ‘UNITED NATIONAL STAFF OFFICES’ kwa nyakati tofauti.

Nikiwa nimeshiriki kazi za uangalizi wa amani katika mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea, kwa miezi saba nilifanya kazi hiyo nikipewa dhamana ya mkuu wa operesheni, nikishirikiana na baadhi ya maofisa kutoka katika nchi za Marekani, Norway, Poland, Romania, Kenya, Zambia, Nigeria, India, China na Ukraine. Waliofanya kazi chini yangu kwa nyakati tofauti.

Kutokana na utendaji wangu kama mlinzi wa amani ‘Observer’ wa UN kwenye mpaka wa Ethiopia na Eritrea, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alinitunuku Medali ya amani, ambayo ilimfanya Kanali Emilly afurahishwe sana. Kutokana na utashi wake ameweza kuiongoza Idara hii nyeti kwa ufanisi mkubwa, kutokana na umri wake kufikia wakati wa kustaafu, serikali iliona kuwa bado anaweza kuhimili mikikimikiki ya kazi aliyoizoea wakamuongezea mkataba wa miaka miwili.

Kutokana na uwezo na msimamo wake huo Kanali Emiily amekuwa akishiriki katika kazi za hatari, ambazo zimemjengea heshima. wakati serikali inaangalia nani atakuwa mrithi wa Kanali Emilly, ilimuongezea mkataba wa miaka hiyo miwili, kitendo ambacho kiliungwa mkono na kila mpenda amani duniani.

Baada ya kumaliza kazi na kupewa medali hiyo kama ilivyo kwa wahitimu wengine kutoka mataifa mbali mbali duniani, nilirejea Dar es Salaam nikiwa na matumaini ya kupata hati ya heshima ambayo ni zawadi kwa jeshi na serikali ya Tanzania.

Kama kawaida hati hiyo ilitumwa kwa Jeshi la Tanzania na kupokelewa na Kanali Emilly, ikinielezea kuwa, nimehitimu vizuri na kupata alama B, alama ambayo ni ya juu kutolewa na Chuo hicho, kilichoko kaskazini mwa Jiji la Moscow, nchini Urusi.

Kanali Emilly alifurahishwa sana mimi kupata alama hiyo ya juu, aliniita ofisini kwake na kunikebehi kwa maneno ya utani kiasi kwamba nami niliamini kuwa ndoto zangu zilikuwa ndoto za Kimweri.

Kanali Emilly alitania, “Yawezekana mambo yalikuwa mazito Teacher, sikutarajia, kijana shupavu kama wewe kuchemka, pole sana mwanangu”, alisema Kanali Emilly mimi nikimwangalia usoni kwa makini.

“Yawezekana mambo yalikuwa magumu, sikutarajia kupata matokeo ya kushangaza kama unavyosema, nilijipanga vizuri, kama imetokea hivyo sina jinsi”, nakumbuka jinsi nilivyomwambia Kanali Emilly akacheka.

“Umejisikiaje kufanya vibaya, Teacher?”, alihoji tena.

“Nimejisikia vibaya sana, sidhani kama yupo anayependa kufanya vibaya”, nilimwambia.

“Taarifa yako itatoka ubaoni mchana leo, ni taarifa mbaya sana, sina njia nyingine lazima itoke kama ilivyo kawaida”, aliniambia huku akionesha tabasamu, lililonishangaza.

“Naomba isiwekwe kwenye ubao”, nilijaribu kumshawishi akakataa.

“Hapana, unataka niharibu kazi ili nikufurahishe wewe, sikukutuma kufanya madudu”, Kanali Emilly alisema kwa hasira sura yake ilibadilika, nilitoka ndani ya ofisi yake nikitafakari aibu itakayonipata baada ya taarifa hiyo kutolewa.

Nilijiuliza nini nimefanya wakati wa kozi sikupata jibu, nilitembea huku moyo wangu ukisononeka, nikaelekea Kantini, ambako nilikunywa chai na chapati moja tena kwa shida, kisha nikaelekea ofisini kwangu.

Tofauti na jinsi nilivyotarajia, kidogo nipoteze maisha kwa furaha, ubao wa matangazo ulisomeka kuwa nilifaulu vizuri na kupata alama B, alama ambayo ukiipata katika chuo hicho, unatunukiwa cheti cha heshima na Rais wa nchi yako kwa niaba ya Mkuu wa Chuo.

Nilimtafakari Kanali Emilly sikupata jibu, niliporejea mazungumzo yetu ya awali kuwa nimemfedhehesha, nikabaini kuwa Mzee huyu alikuwa akinitania kama ilivyokuwa kawaida yake.

Sikupoteza muda, nilimpigia simu kumfahamisha nilivyofaulu kwa kupata alama B, ambayo tuliipata maofisa wawili, mimi kutoka Tanzania na Meja Charles Katasi wa Jeshi la Uganda.

Kanali Emilly aliniita ofisini kwake na kunifahamisha kuwa, yaliyotokea ni sababu ya furaha aliyokuwa nayo baada ya kupokea hati hiyo. “Unatakiwa Ikulu saa nne ya asubuhi kesho, faili lako limepelekwa kwa Rais, atakubabidhi hati hiyo yeye mwenyewe, maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi watakuwepo, inafurahisha sana Teacher”, Kanali Benny alisema huku nikijisikia mwenye furaha ya ajabu kuonana na Rais kesho.

Nilivaa vizuri, nikajipanga pamoja na familia yangu, baada ya kujiweka sawa tulielekea Ikulu, Kanali Emilly na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Jeshi walifika kushuhudia tukio hili la aina yake.

Baada ya Rais kunikabidhi hati yangu ya heshima alisema maneno machache, akitoa maagizo kwa maofisa na makamanda wangu kuhakikisha wanathamini mchango wangu na kuongeza vijana na kuwahamasisha kufuata nyayo zangu.

Kutokana na heshima hiyo, nilipewa nafasi ya kutoa neno la shukrani, baada ya kusema niliitwa kupiga picha za kumbukumbu na Rais, maofisa wa Jeshi, familia yangu, wakiwepo watoto wangu wapendwa, Masey, Changasi na Warioba ambaye alibebwa na Rais.

“Karibu Teacher”, mawazo yangu yaliingiliwa na sauti nzito ya Luteni Kanali Matumbi.

“Asante Kamanda”, niliitika huku tukashikana mikono, tukakumbatiana kwa furaha.

“Ni Afande Matumbi?”, nilimuuliza kwa utani na bashasha.

“Hakika ni mimi, wewe ni Teacher?”, yeye pia aliuliza.

“Mwili huu unakula nini Kamanda?”, nilimtania.

“Samaki na viazi”, alijibu kwa utani.

Luteni Kanali Matumbi alinipokea mkoba wangu, kisha mkono wake wa kushoto akaushika mkono wangu wa kuume, tukatembea kuelekea ndani.

“Umenikumbusha mambo ya zamani Teacher, bahati mbaya sana historia hazijirudii, ingekuwa hivyo tungefanya maandalizi ya kutosha kuzirudia historia”, alisema tukacheka.

“Kweli kabisa, unakumbuka opereseni ya kula chakula cha wanafunzi wenzetu kule chuoni Nachingwea”, nilimkumbusha.

“Operesheni ipi hiyo Teacher, maana tumefanya mambo mengi?”, aliuliza wakati tunaingia kwenye sebule ya nyumba yake.

“Wakati wa mafunzo ya awali kule Fam seven teen Nachingwea, tulianzisha operesheni ya kula chakula cha wenzetu, unamkumbuka yule Bahati kutoka Kigoma?”, nilimuuliza.

“Bahati…, Bahatiiii, mbona simkumbuki, alitoka Kigoma?”, aliuliza.

“Unamkumbuka bwana, alikuwa kijana mchafu sana, alipenda kuiba mchele stoo wakati wa fatiki na kujipikia vichochoroni”, nilimkubusha.

“Bahati… namfahamu sana, alikuwa Kombania C, una kumbukumbu sana Teacher, njaa bwana ni baraa, sikujuwa operesheni ile iliendeshwa na nani?”, alisema akitabasamu.

“Niliifanya mimi”, nilimwambia tukacheka tena. “Maana Bahati alivunja rekodi kwa kukimbia na kofia ya chuma la moto lililokuwa na ubwabwa.

“Ni kweli alitoka Kigoma”.

“Huwezi kuamini, tulijiandaa kama kawaida yetu, baada ya kuwazingira na kuwaachia upenyo ili aweze kukimbia, huku tukiwa tumefunga makaratasi meupe miguuno na upande wa kulia wa mkono mfano wa Military Polisi, tulimkurupusha bwana…”, nilisema huku Meja Matumbi akishika tumbo kwa kucheka. “Lakini ilikuwa kama abiria chunga mzigo wako, akakimbia na mzigo, tukaambulia patupu”.

“Eheee, alikuwa makini sana katika masuala ya misiso”.

“Siwezi kumsahau, tulipomkurupusha tu, kitendo cha haraka, tena bila kuchelewa, alibeba kofia ya chuma, tena likiwa la moto…, aisee alimudu kukimbia nalo”, nilimwambia huku tukicheka sana.

Baada ya kucheka sana, huku tukikumbushana mambo yaliyotokea wakati tukiwa chuoni, chakula na vinywaji vililetwa tukaanza kula huku tukiulizana hili na lile.

“Teacher”, Luteni Kanali Matumbi aliniita.

“Ndio Kamanda”.

“Kulikuwa na uvumi kuwa Rais wa Sudani Omari al Bashir anatafutwa ili akamatwe na kufikishwa kwenye Mahakama ya kimatafa ya uhalifu wa kivita, kujibu tuhuma za mauaji, uvumi huo uliishia wapi, naamini wewe kiasi fulani unafahamu kinachoendelea”.

Nilivuta pumuzi nikazishusha, nilitafakari kuhusu swali la Meja Matumbi, nikaamini kuwa hata yeye mizozo na migogoro katika nchi za kiafrika inamsumbua sana akilini.

“Ni kweli, mwaka jana mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, ilitoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi huyo wa Sudani, niliwahi kumwambia hata Kanali Emilly kuwa ni vigumu mno kwa kiongozi wa nchi kama Bashir kukamatwa na kufikishwa kwenye mahakama hiyo wakati bado anaongoza nchi, ni vigumu sana”.

“Hakika ni vigumu Teacher, lakiniiii…, wakidhamiria kabisa kabisa wanaweza kufanikiwa”.

“Wampate wapi, ni vigumu sana Bashir kukamatwa”, nilisisitiza.

“Kuna ugumu gani, kwani huyu Bashir hafanyi ziara nje ya Sudani… Wanamvizia akitoka tu, wanamtiwa mikononi, sidhani kama inashindikana”, alishauri Luteni Kanali Matumbi.

“Wewe unaona rahisi, nikwambie sasa, huyu Mzee pamoja na kuwepo hati ya mahakama ya uhalifu wa kivita, amefanya safari zaidi ya kumi nje ya nchi yake, tena bila woga, ni vigumu mno”, nilimwambia akabaki amekodoa macho.

Nilichukuwa glasi ya maji nikanywa kidogo, nilimwangalia kama ana la kusema, nilipoona ananiangalia bila kusema kitu nikatambua kuwa jambo hili limemgusa mno, maana ni mmoja wa maofisa wapenda amani wenye msimamo usioyumbishwa.

“Mbona umenyamaza Mkuu, kama vile umegushwa mno na jambo hili”.

“Teacher, kama ungeweza kujua moyo wangu ulivyo, hakika ungeelewa nini natafakari, viongozi wa aina ya Bashir ndiyo wanaochangia machafuko barani Afrika, mtu mmoja anasababisha mauaji ya mamilioni ya watu, haipendezi Teacher”, alisema kwa uchungu.

“Ni kweli, lakini utafanyaje, migogoro imekuwa migogoro, watu wanauana kama wanyama, hii yote inatokana na udhaifu wetu, angalia mfano mtu kama Jonas Savimbi, aliumiza watu wengi nchini Angola, amewaachia watu vilema vya maisha, ICC haikuwa na ubavu, iliishia kusema na kulaani tu, mpaka alipouawa. Kwanini walishindwa kumtia mikononi?”, nilimwambia.

“Wewe unadhani nini kifanyike kukomesha mauaji ya waafrika, maana kwa takwimu za haraka nchi zaidi ya 30 zinakabiliwa na migogoro mikubwa, inayotishia amani ya dunia, na kati ya nchi hizo zaidi ya ishirini ziko barani Afrika”, alihoji.

“Cha kufanya ni kumuomba Mungu, kwa sababu kila siku mataifa makubwa yanatengeneza silaha, na silaha hizi hazitengenezwi kwa ajili ya wanyama, zinatengenezwa kwa ajili yetu, ili uweze kuwa na nguvu kijeshi, lazima uwe na silaha za kisasa, kila taifa linatamba dhidi ya taifa lingine, unadhani amani itapatikana?”, nilimuuliza akakuna kichwa.

“Azimio la Umoja wa mataifa la kupiga marufuku mapinduzi ya kijeshi duniani linatekelezwa kweli?”, alihoji.

“Hata kama linatekelezwa, mbona halina meno, toka azimio hilo lipitishwe na Umoja wa Mataifa ni nchi ngapi zimepinduliwa na kuongozwa kijeshi, tumeshuhudia baadhi ya nchi Umoja wa Mataifa ukiingilia kati, na sehemu zingine wakisita kufanya hivyo eti ni kuingilia mambo yao ya ndani”.

“Kweli Teacher, ni nyingi”, Luteni Kanali Matumbi alisema kwa sauti ya upole.

“Aisee, tutafute siku nyingine tutaongea zaidi, muda wangu wa kuwepo hapa Musoma umekwisha, labda tuonane Jumamosi wakati narudi Dar es Salaam, nitajitahidi kuwahi ili tuongee zaidi”, nilimuomba Luteni Kanali Matumbi baada ya kuona muda unayoyoma.

“Nilitegemea utalala Musoma, nimekufanyia maandalizi ya kila aina, hebu lala Musoma leo nikutembeze kidogo uone mji”, alishauri nikatingisha kichwa kutokubaliana naye.

“Usijali, lazima niondoke leo, nina shauku kubwa ya kumuona mama yangu mzazi, wajuwa tena Afande, baba na mama ni mungu wa dunia, pamoja na kwamba baba alikwisha tangulia mbele ya haki, tafadhali tuonane siku nyingine”, nilisema nikisimama kutoka sehemu niliyoketi, maana nilikuwa nimekula na kunywa vizuri.

“Ok, sina jinsi Teacher, nilitegemea kuvuna uhondo zaidi kutoka kwako, basi bwana, ngoja nikutowe”, akabeba mkoba wangu tukaelekea nje.

“Usisahau kupita hapa hiyo Jumamosi, nitafanya maandalizi ili usafiri Jumapili”, aliongeza, huku nikitingisha kichwa kukubaliana na mawazo yake, japokuwa haitawezekana kurudi hapa kutokana na ratiba yangu niliyojiwekea. Baada ya kuagana na Luteni Kanali Matumbi nilitafuta usafiri wangu binafsi nikaelekea Nyamuswa.

Jijini Dar es Salaam, kilifanyika kikao cha siri katika nyumba moja ya mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya. Mfanyabiashara huyu alifahamika kila pembe la Jiji, akiitwa Mzungu Carlos Dimera, Umbo lake lilitosha kabisa kuogopwa na wapinzani wake. Asili ya mzungu huyu ilikuwa ni Corombia. Kutokana na uwezo wake wa kushawishi, Carlos aliweka matawi kadhaa katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Ndiye aliyeitisha kikao hiki kwa siri kubwa.

Kutokana na uwezo wake wa fedha na ushawishi aliokuwa nao kwa baadhi ya viongozi wa serikali kadhaa za Afrika, Carlos Dimera aliweza kuanzisha vikosi kadhaa vya uhalifu ndani ya nchi kadhaa, mojawapo ya vikosi hivyo ni usafirishaji wa shehena kubwa ya dawa za kulevya, kikosi cha wizi kutumia noti bandia na kikosi maalumu cha mauaji dhidi ya watu aliowaita vihelehele. Vihelehele ni wale walioonekana kuingia mambo yake.

Kikao hiki ambacho yeye Carlso Dimera aliwa Mwenyekiti wake, kiliwakutanisha watu wachache, akiwemo mwanamke mmoja tu, Mwana mama huyu aliitwa Hawa Msimbazi, ambaye kutokana na uwezo wake wa kupanga mambo yakawa, wenzake walimfananisha na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Condoliza Rice. Hawa alifananishwa kwa mambo mengi na Mmarekani huyo mwenye asili ya Afrika. Tofauti yao ni kwamba yule alikuwa mtendaji katika Serikali ya Marekani, huyu alikuwa mfanyabiashara wa dawa haramu za kulevya Tanzania.

“Mambo yote yamekamilika kwa asilimia tisini na tisa, vijana wamejipanga vizuri kufanikisha kazi hii, kama itakwenda salama kama tulivyojipanga, nawahakikishia kila mmoja atachagua nchi gani atapenda kuishi pamoja na familia yake”, alisema Hamis Nombo, mmoja wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambaye kiutendaji ni mtaalam wa mipango katika kikosi.

“Sijui hata niahidi nini, jambo hili si gumu kama mnavyodhania, mambo yote yamefanyika, kama alivyosema Nombo hii ni nafasi yenu kuamua wapi mtapenda kuishi, baada ya kazi hii kumalizika kila mmoja ataihama nchi hii akatumbue raha huko atakapopenda kwenda”, alirudia Dimera.

“Bosi, hakuna sababu ya kuumiza vichwa, vijana wamejipanga vizuri, bahati nzuri ni kwamba muda mfupi uliopita wana spoti wetu wametuletea taarifa kuwa serikali imewatuma vijana wawili kutoka Jeshi la ulinzi kuangalia mambo fulani fulani, watoa taarifa wetu wanasema, vijana hao wametumwa kwa siri, baada ya kuona polisi wanasuasua”, alisema Hawa.

“Safi sana, aliyekuita Condoliza Rice hakukosea, kazi unazofanya ni kielelezo kuwa jambo hili litafanikiwa, cha msingi sasa, watume vujana wako waonane na askari hao, ili wapewe ahadi zao kabisa, lakini pia wasiwaendee mikono mitupu, nadhani pia waingizwe kwenye orodha ya malipo yetu na wafahamishwe”, alishauri Carlos Dimera.

“Jambo hilo limefanyika hata kabla sijasema katika kikao hiki. Mambo ameleta taarifa. Amesema askari hao ni miongoni mwa Makomandoo mahili sana, wana uwezo mkubwa mno, tayari tumeingia nao mkataba. Wako upande wetu sasa”, alisema Hawa Carlos akitabasamu.

“Ni jambo zuri sana Hawa, lazima muelewe kuwa kufanya ishu na watu hatari kama hao lazima tuwe tumejiandaa vizuri pia, tuwe makini nao isije ikawa tunamalizana nao halafu wanaanza kutusumbua”, anashauri Nombo.

“Kweli, lakini niwaambie jambo moja, hebu tumalize kazi kwanza, mengineyo yatakuja baadaye”, Dimera alishauri.

Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, kila mmoja akitafakari hili na lile, Carlos aligonga meza, akatoa angalizo, “Cha msingi tuwe makini na kila hatua tunayopita na kutoka, ahadi yangu kwenu ni malipo mazuri mara dufu, jiandaeni kuishi vizuri.

“Lakini pia tusimsahau Teacher, maana waswahili wanasema usipoziba ufa utajenga ukuta”, alikumbusha Aloyce Jackina, aliyekuwa kimya kwa muda mrefu.

“Hana chochote huyu Teacher, jambo hili likiisha tukafanikiwa kuvuka vikwazo, Teacher atakuwa na nafasi gani?”, alihoji Dimera.

“Ni tahadhali tu natoa bosi”, aliongeza Jackina.

“Umefanya vizuri, ili tuongeze nguvu na umakini”, alisema Hawa.

“Kwa maana hiyo tunaachana baada ya kikao hiki, nawatakia mafanikio mema, tufahamishane kila hatua tutakayokuwa, cha msingi ni kutunza midomo yetu. Tukionana kila mmoja awe na jibu la nchi gani atakwenda kuweka makazi yake ya kudumu” alisema akisimama.

Baada ya kikao hicho, Carlos Dimera alikuwa na kikosi kingine chumba cha pili, watu wawili nadhifu sana walikuwa wakimsubiri. Watu hawa walikuwa wamemaliza kazi waliyotumwa na sasa walikuja kupata maelezo ya kazi nyingine.

“Nimesikia kilio mitaani, watu wanalia, tamaa zao zimewafanya walie, kazi yenu ni nzuri sana, nimefarijika, rafiki yangu mmoja kutoka polisi kituo cha kati amenidokeza kuwa kesi zilizofunguliwa hapo ni waliobiwa kwa mpango wetu, wakati hao bado wanalia na kusaga meno wapo wengine wenye tamaa ya kupata utajiri wa haraka. Wewe Oliver Mapunda hakikisha unaingia Chuo Kikuu Mlimani. Maprofesa pamoja na elimu yao katika dunia, ni wepesi kuingia katika kipindi, wakiingia usifanye makosa”, aliagiza Carlos Dimera.

“Naam, nimekusoma bosi”, anadakia Oliver Mapunda aliyekuwa kimya akiwa amefunga mikono yake kifuani.

“Kuna wastaafu waliolipwa mapesa yao baada ya kustaafu, wakati bado wanatafakari nini wazifanyie pesa hizo, sisi tunazitaka. Wewe Masta Bolendile, kazi yako ni hiyo, lakini usiishie hapo, tafuta mahusiano ya karibu na watendaji wa mashirika ya umma, hawa wana mapesa mengi, lakini ni wagumu kuzitoa, tukijipanga vizuri tutazichukua”.

“Naam bosi”, anasema Bolendile.

“Dakika chache zilizopita nimetoka kuzungumza na wenzenu upande wa pili, nimesema baada ya kazi ngumu na nzito iliyo mbele yao, kila mmoja apendekeze nchi gani atapenda kuweka makazi yake ya kudumu, kazi yao ni nzito, kazi ya hatari zaidi ya hii yenu”.

“Kazi zote zina hatari bosi”, Bolendile aliingilia mazungumzo.

“Sawa, lakini hii kazi yenu tunatumia sayansi na teknolojia zaidi, hata ukikamatwa na polisi haina uzito sana. Lakini ‘nga’, umekutwa na unga, lazima yatoke mawe ya uhakika. Naamini kila mmoja amepata mgawo wake sawa. Mtaniletea taarifa za kazi hii baadae. Kila mbinu itumike Teacher auawe, iwe kwa risasi, kisu au hata akitumiwa msichana ammalize kwa sumu, Kwaherini”. Akafunga kikao na kuondoka.

Nyamuswa kama ilivyo kwa miji mingine midogo, iliyoko Bunda, mkoani Mara, ulikuwa umechangamka kwa kiasi, wananchi kutoka sehemu mbalimbali zinazouzunguja mji huu walipishana huku na huku wakifanya mahitaji. Ilikuwa Jumapili ya mwisho wa mwezi. Siku ambayo kila inapowadia wenyewe huiita SIKU YA MTERA NYAMUSWA.

Nilikuwa nimewasili kijijini hapa dakika chache zilizopita, lakini barabara iendayo nyumbani kwa wazazi wangu ilikuwa imefungwa na wafanyabiashara waliokuwa wakiuza bidhaa mbalimbali. Kama ilivyo kawaida yangu, niliutwaa mkoba wangu nikaunjika begani, kisha nikamruhusu dereva aliyenileta aondoke, kwani hakukuwa na njia ya kupita.

Haikupita sekunde mkoba wangu ulipokelewa na Taabu dadangu kipenzi, sikumuona jinsi alivyotokea, alionekana mwenye furaha kupita kiasi, labda alifutahi kuniona tena baada ya kuwa mbali nae kwa muda.

“Pole na safari”, alisema Taabu.

“Mungu amesaidia, habari ya nyumbani?” nilimuuliza wakati tunapita kwenye kundi la watu kuelekea nyumbani.

“Mama pia nilimuona”. alisema akaangaza macho kumtafuta.

“Mwache, mwache asafishe macho. Atanikuta nyumbani”. nilisema huku tukitembea na baadhi ya watu wakitusindikiza kwa macho.

Dakika kadhaa mama naye alifika, hakufanya ajizi moja kwa moja alikuja na kunikumbatia. “Pole na safari mwanangu”, Akaanza kulia, “Ulizoea kutukuta na baba yako, sasa hayupo tena”, alisema mama huku machozi yakianza kumtoka. “Ametuachia ukiwa”, alilala.

Machozi ya mama yalinifanya niwe kimya kwa sekunde kadhaa nikitafakari hili na lile, “Nyamaza mama, kilichotokea ni kazi ya Mungu, baba yatu ametutangulia tu, siku moja tutamuona. Siku zote baba alikuwa akisema hatapenda tumtangulie sisi, alitaka atangulie yeye, kwa kuwa siku yake ilifika, mapenzi ya Mungu yalitimizwa, alihitajika kutoka miongoni mwetu”, nilisema huku nikimuacha mama na kuliendea kaburi la baba kwa ajili yakufanya maombi mafupi.

Baada ya kumuombea mama, tulianza kuzungumza habari nyingine, mama alitaka kujua habari ya safari zangu nje ya nchi, nilimweleza kifupi kuhusu mafanikio ya safari hizo kwa nchi yetu na jinsi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alivyonizawadia tuzo maalum nilipokuwa katika kazi ya ulinzi wa amani. Alionyesha kufurahishwa sana na maelezo yangu, japokuwa hakujua nini heshima ya tuzo hiyo.

Kwa vile nilikuwa nimetoa taarifa mapema niko njiani, mama na dada waliniandalia chakula nikipendacho, ugali na samaki aina ya ningu na nembe. Nimetokea kupenda aina hii ya samaki, ambao hupatikana sana Ziwa Victoria.

Ilipofika saa tisa mchana, nilipita mitaa kadhaa nikiangalia mji, nilivutiwa na maendeleo yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya vijana. Watu walikuwa wengi, na sehemu za starehe kama baa na hoteli zilikuwa zimejaa watu huku wengine wakicheza pool, karata na bao la solo. Nililazimika kumtembelea shemeji yangu mpendwa Mama Feka, ambaye kwa muda mrefu alikuwa na shauku ya kuniona.

“Ah, karibu sana molamu”, alisema Mama Feka akinikumbatia.

“Nafasi ya upendeleo molamu, nina muda mchache sana wa kuwa hapa Nyamuswa, nimehofia jambo moja, nimeogopa usijesikia nilikuwepo na sikukutafuta, sidhani kama ungenielewa?”, nilimuuliza.

“Nisingekuelewa kabisa, habari ya Dar… Nadhani umeingia leo”.

“Yes, nimeingia leo na ratiba yangu imebana mno, lakini nitajitahidi kuwepo hapa kwa siku mbili tatu hivi”, nilimwambia.

“Naamini utakuwa umekula, twende maduka saba nikupe japo bia mbili molamu”, alisema. Kabla sijasema kitu haraka aliingia ndani. Hakuchukua hata dakika moja akatoka ameshika kitenge mkononi. “Haya togende molamu”, akatangulia, nikamfuata, tukaelekea hapo maduka saba.

Sehemu hii ilikuwa imechangamka kiasi, vijana ninaowafahamu na nisiowafahamu walikuwa hapa wakiangusha moja moto moja baridi, nilipungiana mikono na vijana hao waliokuwa wakibisha kuhusu mchezo wa mpira, Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kati ya Yanga na Simba. Mmoja wa vijana hawa alionekana mwenye jazba sana. “Mwamuzi alichangia kuharibu radha ya mchezo, huwezi kutoa kadi nyekundu dakika za mwanzo kama vile”, alisema kijana huyo kwa ghadhabu.

“Ulitaka aachwe aendelee kufanya makosa uwanjani?”, alihoji kijana mwingine ambaye pia alisimama kuonyesha msisitizo.

“Molamu, huwezi kuamini baada ya mchezo wa Yanga na Simba, ngumi zilipigwa hapa, wengine wakilalamikia kadi nyekundu iliyotolewa na mwamuzi, wengine walidai eti mwamuzi alikuwa sahihi kutoa kadi hiyo, yaani ni vurugu tupu”, alisema Mama Feka nikimwangalia kwa makini.

“Molamu, wewe ni shabiki wa timu gani?”, nilimuuliza.

“Aaah molamu… Mabingwa watetezi Yanga Afrika, nikuletee kadi yangu ya uanachama, usije kusema mimi ni shabiki kishoka”.

“Umesema, nimekuelewa molamu”, nikasimamam kuelekea mahali vijana hao walikuwa wakibishana bila mpangilio.

“Mimi nilijua kabisa kuwa mwanamke hawezi kuchezesha mchezo kama ule”, alirukia kijana mwingine.

“Sikilizeni”, niliwahadhalisha.

“Tumsikilize mzee, naamini alikuwa uwanjani, sisi tunabishana kwa kuona mchezo katika luninga”, alisema Adul Light, mmoja wa vijana hao.

“Kwani luninga ina tofauti gani na kuwa uwanjani, si kila kitu kinaonyeshwa laivu”, alidakia kijana mwingine.

“Ndio maana nikaomba mnisikilize… Lazima mtambue kuwa mchezo wa soka unaendeshwa kwa kanuni na sheria za mchezo, mnaweza kumlaumu mwamuzi wa mchezo huo kuwa alimtoa mchezaji wa Simba kwa kadi nyekundu, lakini ukweli ni kwamba mwamuzi hakutoa kadi nyekundu…”

“Unaona sasa. Inaonekana hukufika hata uwanjani, maana hujui kama mwamuzi alitoa kadi nyekundu, eti jamani mwamuzi hakutoa kadi nyekundu?” alihoji kijana huyo akionyesha kuwa na jazba.

“Ungenisikiliza kwanza”, nilimsihi kijana huyo.” akakubaliana nami. Haraka nikamuomba mtoa huduma awapatie vinywaji. “Kama nilivyotangulia kusema, mchezo wa soka unaendeshwa kwa kanuni na taratibu. Dakika chache baada ya mchezo huo kuanza, mwamuzi alitoa kadi ya njano, kimsingi mchezaji alipaswa kujihami, asifanye makosa. Lakini kabla hata dakika kumi hazijapita akafanya kosa lililostahili kadi ya njano, akapewa yelow card ya pili. Kanuni za soka zinasema, mchezaji akizawadiwa kadi mbili za njano, atapewa kadi nyekundu ili aende nje. Ndiyo maana nikasema hakupewa kadi nyekundu, ila kadi mbili za njano zilimfanya mwamuzi kutoa kadi nyekundu. Si matakwa yake, ni kanuni za mchezo”, nilifafanua.

Vinywaji vikaletwa tukaanza kunywa,

“Hali hii iliwahi kuwakuta hata Yanga, wachezaji wake wawili walitolewa uwanjani kwa nyekundu, na hii si kwa Yanga na Simba tu, tumeshudia hata ligi za Ulaya”, anabaisha Abdul.

“Yes, kadi nyekundu ni sehemu ya mchezo, ndiyo maana mwamuzi anakuwa nazo mfukoni. Lakini pia yafaa mfahamu kuwa mwamuzi anapowajibika pale uwanjani, kuna mamlaka zingine juu yake, kama atakuwa amekwenda kinyume na kanuni anaadhibiwa”, niliwadokeza, wakaonekana kunielewa.

Mara ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu yangu, Ujumbe ulisema. “UMEZUKA MOTO NA KUUNGUZA JENGO LA OFISI ZETU ZILIZOKO MTAA WA AZIKIWE, VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA HUSUSAN KIKOSI CHA ZIMA MOTO NA UOKOAJI KINAENDELEA NA KAZI YA KUZIMA MOTO HUO, UNATAKIWA KUREJEA HARAKA KWA AJILI YA TAtHIMINI”, Col. Ben. Kwanza nilicheka, mapigo ya moyo wangu yakaongezeka.

“Molamu, nimepata ujumbe wa kushtua kidogo, natakiwa kurejea haraka Dar, es Salaam, hivi tunavyozungumza, moto umezuka ghafla unateketeza jengo la ofisi zetu mtaa wa Azikiwe, kwa hiyo nalazimika kuondoka sasa hivi”, nilisema wote wakaonekana kushangazwa.

Aaah molamu, sina bahati na wewe, jitahidi kuvumilia uondoke kesho mapema”.

“Muda huu utapata usafiri gani kaka?” alihoji Abdul Light.

“Kama nitaweza kufika Mwanza mapema, saa tatu usiku kuna ndege, bahati nzuri rubani wa ndege hii ni mtu wangu wa karibu, nitamjurisha aniwekee nafasi, nilipenda kuwa nanyi, lakini hali ndiyo kama mlivyoona”, nikasimama na kuwaaga kwa mara nyingine nikaondoka.

Ilikuwa saa mbili na dakika arobaini hivi usiku, nilipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Jijini Mwanza, niliwahi kufika uwanjani hapa kama ambavyo inatakiwa abiria wasichelewe kufika kwa ajili ya ukaguzi. Baadhi ya abiria walikuwa wakilalamikia kuachwa na ndege ya saa tisa kwa sababu tu walichelewa kufika uwanjani hapo kwa wakati.

“Nitawashitaki mahakamani, haiwezekani nilipe nauli mara mbili, huu ni wizi”, alisema kijana mmoja aliyekuwa karibu yangu, “Tena niliwahi nusu saa kabla, lakini wakanigomea”, alisisitiza kijana huyo.

“Hata mimi nimewahi nusu saa kabla lakini nikazuiwa kuingia ndani, sasa natakiwa kulipa tenai inashangaza”, alisema mama mmoja kwa jazba. “Haiwezekani, haiwezekani…” aliongeza.

Akili yangu ilikuwa juu ya kuungua kwa jengo la ofisi zetu Dar es Salaam. Lakini nilishangazwa vipi vyombo vya habari kama Televishen na redio havikuwa vimeripoti habari ya tukio hilo kubwa. Labda lilikuwa agizo kutokana na unyeti wa ofisi hizi, Nilijiuliza mambo mengi, baada ya kutafakari kwa kina nikijiuliza hili na lile, wazo likanijia. Nikapiga simu kwa Peter Twite, Dar es Salaam.

“Sikiliza Peter, kwanza habari ya saa hizi… Una taarifa zozote kuhusu ofisi zetu Dar es Salaam?. Niko Mwanza” nilimuuliza baada ya salaam.

“Habari si nzuri Mkuu, moto umezuka ghafla na kuteketeza kabisa ofisi zetu, ninavyoongea niko sehemu ya tukio na kazi ya kuzima moto inaendelea, Kanali Emilly anakusubiri kwa shauku kubwa”, alisema Peter Twite nikashangaa.

“Ananisubiri… kwanini anisubiri kwa shauku… Nitasaidia nini mimi wakati tayari maji yamekwisha kumwagika?”, nilimuuliza akacheka.

“Ukubwa dawa, labda ana jambo lingine la ziada, linapotokea tatizo kubwa kama hili, kila mtu huwa na mtazamo wake, utamsikia ukifika Dar”.

Abiria walikuwa wengi. Ili niweze kusafiri usiku huu, nilikuwa nimewasiliana mapema na rubani wa bdege hii, Mapambano Mussa, kumfahamisha kuhusu umuhimu wa safari yangu, akanihakikishia kuwa nitasafiri na ndege ya saa tatu na nusu.

Mawazo yangu yalikuwa juu ya tukio la kuungua kwa ofisi zetu Dar es Salaam. Sasa akili yangu ilikuwa imeamini baada ya Peter Twite naye kunithibitishia hivyo. Nilipita sehemu ya ukaguzi, baadhi ya abiria walikuwa wakilalamikia gharama kubwa ya kulipia ndoo zenye samaki. Papo hapo pia kulikuwa na malipo ya karatasi laini ya kuzuia harufu. Niliumizwa gharama hizi zilizobuniwa na watu kwa ajili ya kuwaongezea mzigo abiria.

Chumba cha abiria kilikuwa kimejaa, waliobahatika kukaa walikaa na waliokuwa na bahati mbaya kama mimi tulisimama. Ndege ndogo zilikuwa zikiruka na kutua, bila shaka zilikuwa za kukodi. Mara nikamuona abiria mmoja anasimama na kukiacha kiti chake, nilinyata taratibu nikaketi.

“Samahani kaka, usikae pana mwenyewe hapa”, alisemama mama mmoja.

“Pana mwenyewe!”, nilimuuliza kwa mshangao. “Mama, sehemu kama hizi huwa hazina mwenyewe, hizi ni sehemu za huduma, kila mmoja ana haki ya kuketi, mbaya ni kumuondoa mtu kwenye kiti alichowahi kuketi, lakini kama amesimama mwenyewe na mimi nikakaa kuna tatizo”, nilijaribu kufafanua.

“Lakini kama mwenzio amewahi tayari ana haki ya kuwa sehemu yake”. alisema.

“Si kusudio langu kulumbana na wewe, hebu angalia tiketi yako”, akaifungua ili kuangalia, “Angalia namba yako utakayoketi”, akafanya hivyo, baada ya kuangalia kwa sekunde kadhaa akageuka kuniangalia. “Namba iliyoandikwa kwenye tiketi hii ndiyo abiria mwingine hawezi kuingilia, hata mahakamani utakwenda kifua mbele”, nilisema huku nikisimama kumpisha asijeniona mkorofi.

“Keti tu kaka, wajamaa hawabanani, sote ni abiria, tusikosane kwa sababu ya kiti”, alisema mama huyu, nikatabasamu.

“Usijali mamangu, samahani kwa maneno yangu ya utani, usiyachukulie kama ndivyo nilivyo, ni katika kutania tu, tunaposafiri katika chombo kimoja, tumekuwa ndugu katika safari, nikianguka hapa nyote mtaacha kazi zenu kunisaidia, vivyo hivyo na wewe, ukianguka hapa nitakuwa wa kwanza kukusaidia”.

“Shetani apishie mbali, tena ashindwe kabisa kwa jina la yesu”, alidakia mama huyu, mimi nikacheka na baadhi ya abiria pia wakacheka.

Foker 27, ndege ya abiria ya shirika la ndege Tanzania iliruka kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza saa tatu na dakika arobaini usiku, tayari kwa safari ya kuelekea Dar es Salaam. Abiria wote ndani ya ndege tulikaa kimya tukisubiri hatma yetu. Maana kutoka Mwanza. Ukanda wa Ziwa ViCtoria hadi Dar es Salaam ilipo Bahari ya Hindi ni mwendo wa saa moja na nusu hivi.

“Wewe ni mwenyeji kidogo Dar es Salaam?” Mzee mmoja wa makamo aliniuliza baada ya ndege kuruka na kukaa sawa.

Kwa sababu ambazo sizijui nikamjibu, “Hapana. Leo itakuwa mara yangu ya pili kuingia Dar es Salaam. Una tatizo mzee wangu?”, nilimuuliza.

“Nimeitwa kwenye kikao cha wafanyabiashara. Kikao kimepangwa kufanyika kesho saa tatu asubuhi, eneo la Sinza. Hii ni mara yangu ya kwanza kuingia katika jiji hili”, alisema mzee huyu.

“Kikao kuhusu nini?” nilihoji.

“Ni mambo ya biashara tu. Kuna watu wanatoka nje kwa ajili ya mazungumzo, tumekuwa tukiwasiliana nao kwa njia simu na email, sasa kesho tunakutana rasmi”, alifafanua.

“Vizuri, siku hizi dunia imekuwa kijiji, kila aina ya mawasiliano, usafiri na mambo mengine huwezi kupotea, hata mimi tukishuka nachukua taksi kuelekea Kigamboni waliko ndugu zangu. Wewe unahusika na biashara gani?”.

“Biashara ya nyumba za kulaza wageni Mwanza na Shinyanga, pia nasafirisha abiria kati ya Mwanza na Bariadi, mkoani Simiyu. Kwetu kabisa ni Simiyu”.

“Oh hongera sana, nilikuwa na ndoto ya kuwa mfanyabiashara mkubwa kama wewe lakini ndoto yangu haikutimia, nikaishia kuwa Mwalimu wa shule ya msingi huko Bunda, mkoani Mara”, niliongopa.

“Ualimu si kazi mbaya, sasa hivi waalimu ndiyo wanaangaliwa na serikali kama kioo. Rais wetu hataki mchezo, naamini baada ya mwaka mmoja waliokuwa wanachukia kazi ya ualimu sasa wataitafuta wasiipate”, alisema mzee huyu, pamoja na matamshi yake kuwa ya kiswahili chenye rafudhi ya Kisukuma, nikaanza kuelewa kuwa ni mzungumzaji mzuri.

“Nimefurahi sana kusikia maneno hayo, zamani kazi ya walimu ilikuwa nzuri sana, sijui kilipita nini walimu wakaonekana si lolote, binafsi namshukru sana Rais wetu, kama hali itaendelea hivi heshima yetu itarudi. Nitakupa namba yangu ya simu, pia utanipa namba ya simu yako ili tutafutane kesho baada ya wewe kumaliza kikao”, nilimwambia akaonekana kufurahishwa na maneno yangu.

“Umefuata nini Dar es Salaam?”, alihoji.

“Mdogo wangu ni askari polisi, yuko kituo cha kati”. Baada ya kupeana namba za simu mazungumzo yakaendelea. Tuliongea mambo mengi kuhusu biashara hizi na zile. Nilianza kumpenda mzee huyu, alionekana muungwana sana, labda ndiyo siri ya mafanikio yake.

“Nitakutafuta kesho tukimaliza kikao, nitakuelekeza mahali nilipo, utakuja tutaongea mawili matatu”, alisema wakati ndege inashuka taratibu kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere, Dar es Salaam.

“Naitwa Julius, Mungu akitujaalia tukionana tena tutafahamiana zaidi, nitakuita Bunda siku moja, japokuwa si rahisi masikini kama mimi mwalimu kumuita tajiri kama wewe na ukaja kunitembelea, kama unavyojua masikini kwenda kwa tajiri mara kwa mara ni sawa, lakini tajiri kwenda kwa masikini, akafuate nini?”, nilimwambia.

“Hiyo inategemea na aina ya mtu. Sikiliza Mwalimu Julius, kwanza mimi naitwa Paul Mwifa, nina hoteli Mwanza inaitwa New Rehema, nyingine iko Shinyanga kwa jina hilo na Baria pia. Lakini sina majigambo, uliza wanaonifahamu, nitakukaribisha siku moja utaamini maneno yangu”, alisema huku tukianza kutoka ndani ya ndege hii.

Nilichukua mkoba wangu mdogo nikauvaa, kwa kuwa nilikuwa karibu na mlango wa kutokea wa nyuma nilimuaga mzee Mwifa nikatoka taratibu kuelekea nje. Nilipita sehemu ambayo abiria husubiri mizigo, kwa vile sikuwa na mzigo wa kusubiri nikapita moja kwa moja kuelekea nje. Watu wengi walifika uwanjani hapo kusubiri wageni, baadhi walibeba mabango yenye majina ya watu. Nilipita kimya kimya nikisumbuliwa na baadhi ya madereva taksi, hatmaye nikavutiwa na maelezo ya dereva mmoja nikaingia kwenye gari lake tukaondoka kuelekea mjini.

Wakati dereva wa gari hii anaanza kuondoka uwanja wa ndege, kupitia kwenye kioo cha kushoto, niliweza kuwaona vijana wawili wakikimbia na kuingia kwenye gari iliyokuwa imeegeshwa karibu na sehemu ya malipo ya gharama za uwanja.

“Jitahidi nina haraka kidogo”, nilimwambia dereva akaongeza mwendo. Tulipofika kwenye kizuizi cha kukagua tiketi za malipo, gari hiyo ilisimama nyuma yetu, dereva wangu aliingiza kadi ya malipo, kizuizi kikafungua kuashiria kuwa tumeruhusiwa kupita. Gari hilo pia likafuata taratibu kama tulivyofanya nalo likapita. Ilikuwa BMW nyeusi, ndani kulikuwa na vijana wawili, ambao hata hivyo sikuweza kuwaona vizuri.

Haraka nilifungua mkoba wangu nikatoa lens yangu ndogo ambayo hunisaidia kuona vitu vya mbali. Kulikuwa na vijana wanne, kila mmoja alionekana kuwa majukumu yake kama wenyewe walivyokuwa wamepangiana. “Ingia kituo cha mafuta”, nilimwambia dereva wa gari hii akanishangaa.

“Gari yangu ina mafuta ya kutosha, sisi huwa tunajaza full kwa ajili ya kuepuka usumbufu kwa abiria wetu, ni agizo la uwanja, kwa hilo usihofu”, alisema.

“Nataka kuingia Super Market kidogo”, nilidanganya.

“Hapa wanafunga saa nne usiku, sasa ni saa tano na nusu, labda tujaribu Super Market ya Uchumi”, alishauri kijana huyu aliyekuwa akiendesha Toyota Carina muundo wa TI.

Mbele yetu nikaliona gari lingine aina ile ile ya BMW, rangi ya blue, nilipovuta lens yangu kulikuwa na vijana wawili nao wakiwa tayari kutimiza kazi waliyotumwa. Nilijilaumu kwa kutokuweka tahadhari, lakini kwa vile nilikuwa nimegundua hali hii mapema nikajiweka tayari kwa lolote ambalo lingetokea.

Mara ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu yangu, ‘KUWA MAKINI BOSI, NYOKA MWENYE SUMU KALI ANATEMBEA KARIBU NA MIGUU YAKO, AKIKUNG’ATA UMEKWISHA’. Wakati tunavuka kwenye taa za kuongoza magari za uwanja wa ndege. Gari lililokuwa mbele yangu lilipungua mwendo ili kuruhusu gari letu lianze kupita kwenye taa hizi.

Ghafla nilisikia kelele za risasi, wakati huo nilikuwa tayari nimejitupa nje na kuliacha gari likiseleleka kuelekea mtaroni. Mara lilitokea Lori lililobeba takataka na kuigonga BMW iliyopunguza mwendo ili kuturuhusu sisi tupite, Vijana wawili waliovalia mavazi yaliyoficha nyuso zao waliruka kutoka kwenye lori na kurusha risasi kuyashambulia magari hayo.

Ilikuwa asubuhi ya misukosuko, vurugu na jitimai, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walikimbia bila mpangilio. Kila mmoja akijaribu kuitetea roho yake, wakati askari kutoka Kikosi Maalum cha Polisi wa Kutuliza Ghasia walipokuwa wakitekeleza moja ya majuku yao ya kuzuia fujo katikati ya Jiji.

Wakitumia magari yao ya kazi aina ya Landrover Defender TDI za jeshi la polisi Tanzania, zikiwa na rangi ya blue, bunduki maalum za kurushia mabomu ya moshi zikiwa mikononi mwao. Askari hawa walipita mitaani kifua mbele, wakirusha mabomu ya machozi huku na huku ili kutimiza wajibu wao huo.

Magari haya yaligawanyika katika pande mbili mengine yalielekea upande wa Mnazi Mmoja. Mengine yakaelekea upande wa Ilala, ili kuwakabili vyema wananchi hawa waliodaiwa kukaidi agizo la serikali lililowakataza kufanyabiashara katikati ya jiji. Askari hawa waliendelea kurusha mabomu kila mahali palipoonekana kuwa na mkusanyiko wa watu kuanzia wawili.

Hali hii ilionekana sawa na mchezo wa kuigiza. Sikufurahishwa na kitendo hiki cha askari kurusha mabomu bila mpangilio, wananchi sasa walikimbia huku na huku mfano wa Pundamilia waishio kwenye mbuga za wanyama za Serengeti, wanapofukuzwa na mnyama mwenye njaa kali Simba.

Hata hivyo kulikuwa na ukaidi wa wazi kutoka kwa raia hawa, ambao walionekana wazi kukaidi amri hii iliyotolewa na polisi kupitia chombo maalum cha kukuza sauti. “Amri ya Jeshi la Polisi, mnatakiwa kutawanyika haraka, vinginevyo tutatumia nguvu kuwatawanya”, sauti ilisikika kutoka katika chombo hicho maalum.

Wakati huo mimi nilikuwa nimesimama kwenye ukuta wa Shule ya Msingi Uhuru, karibu na makutano ya Barabara ya Uhuru na Msimbazi, nikifuatilia kwa karibu kasheshe hilo, ambalo kwa kiasi fulani lilibadili sura nzuri ya Jiji la Dar es Salaam, hali ya utulivu ikatoweka na hofu ikachukua sehemu yake. Kumbukumbu za mauaji yaliyosababisha kuwa na wakimbizi wengi katika nchi za Congo, Rwanda na Burundi ikanirudia kichwani.

“Hali hii ikiachwa iendelee hivi kama ilivyo sasa, itatuletea matatizo siku za usoni”, nilijisemea moyoni. Nilikumbuka somo la usalama wa ndani, nilifundishwa somo hili na Luteni John John, wakati huo nikiwa mwanafunzi huko Monduli, mkoani Arusha, kuwa askari wanapashwa kufuata taratibu zilizowekwa wakati wa kukabiliana na hali kama hii, kukaidi amri halali.

Kila mahali ambapo askari hao waliona kuna mkusanyiko wa watu, walisogea na kurusha kombora, hali ilikuwa mbaya, karibu kila upande kilio kikubwa kilikuwa ni kuwashwa macho, kutokana na moshi huo kuwaingia machoni. Ili hali hii isikupate lazima ufumbe macho, jambo ambalo ni vigumu kukwepa.

Mimi pia nilikumbwa na kadhia hii, baada ya bomu lililorushwa kuanguka na kulipuka karibu kabisa na mahali nilipokuwa nimesimama. Kutokana na uzoefu wangu katika majanga kama haya, nilifanikiwa kutoka eneo hilo haraka bila kupatwa na madhara makubwa. Kila kikubwa cha watu ilikuwa ni kuwashwa macho, wengine walikimbilia maji ili kusafisha nyuso zao, lakini wakabaki kutetea kile walichoona kinafaa.

Kiasi nilibaini kuwa askari hawa hawakuwa makini katika kutekeleza majukumu yao, nilibaini kuwa iwapo wananchi hawa wakipata silaha zenye ubora kama walizonazo wao huenda wangesalimu amri kutokana na mpangilio wao kuwa mbovu, “Mmmh mfano hali hii ingetokea katika nchi za wenzetu na askari hawa wakafanya mchezo kama hivi, itakuwaje?” nilijiuliza.

“Mabomu haya yanayorushwa hovyo, hivi askari hawa hawaoni kuwa wanaitia hasara serikali”, alisema mama mmoja wa makamo alisimama karibu yangu akiyahaha kuyasafisha macho yake.

“Hakuna hasara mama, mabomu haya yamenunuliwa na serikali kwa kazi hii, lakini hayakupaswa kutumika sasa, sioni sababu ya tembo kupigana na sungura, polisi wanatumia nguvu kubwa kupambana na adui ambaye hana silaha yoyote ya hatari, nikisema silaha nina maana hata wembe sidhani kama wamebeba hawa”, nilisema.

“Kwanini wasitumie silaha kama hizi kukomesha matukio ya ujambazi yaliyokithiri nchini, au kuwakamata maharamia wanaosumbua wanachi katika maeneo ya mipaka na sehemu ya bahari, ambako kila siku tunasikia meli zinatekwa”, alishauri mama huyu.

“Kuhusu suala la ujamnazi ni kweli silaha hizi zingesaidia sana mama, lakini hili na kukabiliana na maharamia wanaoteka meli hapa, polisi hawahusiki, hilo ni jukumu la wanajeshi, majukumu ya polisi ni kukabiliana na raia wakorofi, kama hawa waliogoma kutia amri ya serikali”, nilimwambia mama huyu akaonekana kutabasamu.

“Nimejifunza kitu kutoka kwako kijana wangu, kumbe mipakani ni jukumu la wanajeshi? Nimeelewa sasa mwanangu”, aliongeza mama huyu aliyekuwa na rafidhi ya mkoa wa Mtwara.

Pamoja na rafidhi yake kuwa ya kimakonde, alionekana mama mwenye busara nyingi, baada ya kumtafakari nikabaini kuwa huenda ni mmoja wa viongozi wa taasisi za wanawake ama mjasiriamali. “Kuwasumbua wananchi kwa kuwapiga mabomu kama hivi wewe kwa mtazamo wako unaona sawa?”, aliniuliza.

“Si sawa kabisa, lakini pia lazima uangalia chanzo nini? Serikali imetenga bajeti ya kuagiza silaha kama hizi, kwa ajili ya kazi kama hii, lakini busara ilihitajika kwanza, sijui kama wamefuata njia hizo, pengine inatafutwa sababu ili kupunguza masalia ya silaha hizo”, nilimwambia akanikazia macho halafu akacheka.

“Kuwachokoza wananchi ili uwarushie mabomu?, hilo umejaribu kuweka chumvi, sijui, labda kwenye Serikali za Kidikteta”, alisema tukacheka huku nikimuaga baada ya hali ya vurugu kutulia kidogo.

Gari langu dogo aina ya VW Golf, lenye muundo wa polisi ambalo wengi hawalijui, nililiegesha ndani ya uzio wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, nilifanya hivyo kuepuka hali hii, ambayo baadhi ya watu huitumia kuwaibia wengine kwa mgongo wa watu wenye msimamo mkali.

Kilichonifikisha katika eneo hili ni kamba maalum niliyokuwa nikihitaji kuinunua, kamba hii ilikuwa na maana kubwa katika kazi zangu za hatari. Nilikuja kuinunua kamba hii baada ya kutokea shambulizi la kushitukiza wakati niliposhuka Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere. Sikujua walionishambulia walikusudia nini. Lakini pia taarifa ya kuteketea kwa jengo la ofisi zetu iliyotolewa na Kanali Emilly, ambayo si kweli iliniongezea tahadhari.

Nilijikuta nikitafakari hili na lile, nikiwaza na kuwazua, nilibaini kuwa kuna tukio la hatari limetokea hivyo, Kanali Emilly alinihitaji haraka ofisi kwake, akalazimika kugeuza lugha, kuwa ofisi zetu tunateketea kwa moto. Hata nilipofuatilia tukio hilo kwenye vyombo vya habari, taarifa hiyo haikuwepo. Hata nilipoongea na Peter Twite, ilionekana hakuna tukio la kuungua jengo la ofisi zetu barabara ya Azikiwe.

Baada ya kupata kitendea kazi kilichonileta eneo hili. Yaani, kamba nyembamba lakini madhubuti kwa ajili ya mambo yangu, nilijiondoa taratibu, nikatembea kwa tahadhari kubwa kuelekea lilipo gari langu, kila mtu karibu yangu alionekana kuwa adui yangu, waswahili wanasema uking’atwa na nyota, ukiguswa na ujani unashtuka, ndiyo hali niliyokuwa nayo, nililikagua gari hilo vizuri, baada ya kujiridhisha nikaingia na kuliodoka taratibu kuelekea Posta, ofisini kwa Kanali Emilly.

Niliendesha gari taratibu kuelekea kwenye ofisi zetu zilizoko Barabara ya Azikiwe. Kichwa changu kilishika hili na lile, nilijiuliza maswali mengi ambayo hata hivyo nilikosa maelezo yake. Nilijilaumu kwa kutozima simu yangu ya mkononi nilipokuwa kijijini kwetu Nyamuswa, ningefanya hivyo, pengine sasa ningekuwa nafaidi samaki, kuku wa kienyeji na maziwa ya mtindi.

Kutoka Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, nilipokuwa nimeegesha gari, nilipita kwenye Barabara za Shauri Moyo na Uhuru nikaibukia kwenye taa za kuongoza magari za Karume, ambapo nilisimama kusubiri ruhusa ya taa hizi. Nilipoingia kwenye Barabara ya Rashid Kawawa, niliongeza mwendo kidogo ili kuwafanya madereva wa magari ya nyuma yangu yasipate usumbufu. Nilipolipita eneo la Msimbazi Centre, niliiacha barabara hii nikaingia kulia halafu kulia tena nikaupita Uwanja wa mpira wa Kaunda, unaomilikiwa na Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.

Shambulizi la usiku uwanja wa ndege liliniongezea hofu na umakini katika kufanya maamuzi, nilijiweka tayari kwa lolote, kila mtu alionekana kuwa adui yangu, nilijiuliza maswali mengi, ningekuwa wapi muda huu iwapo shambulizi lile lingefanikiwa, sikujua sababu za watu hao kufanya shambulizi hilo lililolenga kuniondolea maisha, moyo wangu haukuwa na amani tena, nililitilia shaka kila gari lililoonekana kuwa nyuma au mbele yangu.

Ilikuwa vigumu sana kwa mtu asiye na uwezo wa ziada kama wangu kulibaini gari ninaloendesha, nililazimika kutumia gari hii Toyota Brevis ya rafiki yangu Tigani, ili kukwepa shambulizi lingine, japokuwa dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia hakuna jambo la siri, lolote laweza kutokea.

Shambulizi hilo lilinithibitishia kuwa watu hawa hawana mchezo na wamejipanga vizuri katika mipango yao ya kazi, nilimtafuta Luteni Fred Libaba kwenye simu yake, baada ya kumpata nilimuuliza mahali alipo akanijulisha kuwa yuko Wizara ya Mambo ya Nje kwa kazi maalum nikamtaka asirudi ofisini mpaka nitakapomjulisha ili baadaye tuonane juu kwa juu nje ya ofisi.


Wakati huo, kikao cha dharura kilifanyika nyumbani kwa mzungu Carlos Dimera. Kikosi maalumu cha matapeli wa kisasa kabisa kikiongozwa na mzungu huyu kilikutana kwa siri kujadili hatua za kuchukua baada ya shambulizi la kumuua Teacher kutofanikiwa.

“Nani aliongoza mpango wa mashambulizi ya usiku kule uwanja wa ndege?” akiwa amechukizwa sana Carlos Dimera aliuliza baada ya wajumbe wote muhimu kufika kwenye kikao hiki.

Tofauti na kikao cha awali kilichofanyika juzi, ambapo Carlos alifanya mazungumza na washiriki pande mbili, kila upande aliupangia majukumu yake, safari hii aliwakutanisha wote, kilikuwa kikao cha pamoja, kikiwahusisha wataalam wa wizi madini feki, watakatishaji wa noti bandia na wasafirishaji wa dawa za kulevya.

“Bosi Carlos… Vijana walijipanga vizuri mno, tulikuwa na asilimia zaidi ya mia kumaliza kazi hii, kwa hili tusitafute mchawi, lazima ufahamu katika mawindo, kuna kuwindwa pia, ndicho kilichotokea usiku. Lakini tukuhakikishie kuwa kutenda kosa siyo kosa, kosa ni kulirudia hilo kosa, leo itakuwa mwisho wa maisha ya Teacher, popote atakapoonekana amekwisha”, alisema Nombo.

“Sitaki kusikiliza hadithi za Abunuasi hapa, natoa nafasi ya mwisho, kama Nombo alivyosema kazi hii iishe leo mapema ili tupate uhuru wa kufanya mambo yetu, tukionana kesho tusizungumzie habari ya Teacher tena, nimetenga kiasi cha pesa kwa ajili ya sherehe kubwa, mkimaliza kazi hii vizuri tukutane tupongezane kwa kazi nzuri”, Carlos Dimeta alieleza.

“Pamoja na kikao hiki cha dharura, Nyati, Simba na Chui wako katika mawindo, tunawasiliana kila baada ya dakika tano au kumi, kama unavyowajua vijana hawa bosi, jua la kesho Teacher hawezi kuliona kabisa, hasa nikimfikiria Nyati alivyo Teacher amekwisha”, alieleza Jackina.

ITAENDELEA

Noti Bandia Sehemu ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment