My Repentance (Kutubu Kwangu) Sehemu ya Nne
MAISHA

Ep 04: My Repentance (Kutubu Kwangu)

SIMULIZI My Repentance (Kutubu Kwangu)
My Repentance (Kutubu Kwangu) Sehemu ya Nne

IMEANDIKWA NA: AZIZ HASHIM

*********************************************************************************

Simulizi: My Repentance (Kutubu Kwangu)

Sehemu ya Nne (4)

Moyo ukashtuka kupita kiasi kwani nilijua muda mfupi baadaye, mume wangu atarudi na akimkuta akiwa katika hali ile, hawezi kunielewa. Ikabidi nivae ukauzu, nikabamiza mlango na kuufunga kwa ndani, nikafunga na funguo kabisa, jambo ambalo Evans hakulitegemea.

SASA ENDELEA…

“Wewe si unajifanya mjanja si ndiyo? Basi tutaona kati ya mimi na wewe nani mjanja zaidi. Ukimwaga mboga mi namwaga ugali,” alisema Evans kwa sauti ya kilevi. Sikutaka kurudi nyuma, nilishaamua kumtolea nje na huo ndiyo ulikuwa msimamo wangu.

Alipoona simjibu chochote, Evans aliondoka huku akiendelea kuporomosha kashfa nzitonzito. Nilijisikia vibaya sana ndani ya nafsi yangu, nikawa najiuliza kama mume wangu angefika na kumkuta rafiki yake akinitolea maneno makali kiasi kile, angeelewa kitu gani?

Ama kweli mchuma janga hula na wa kwao, kwa jinsi Evans alivyonigeuka, nilishindwa hata kumwambia kwamba nilikuwa kwenye matatizo makubwa, chanzo kikiwa ni yeye. Alipoondoka, nilishusha pumzi ndefu nikiwa bado nimesimama palepale mlangoni, machozi yakawa yananitoka kwa uchungu.

Yaani kama ni kujuta, mwenzenu nilikuwa naujutia sana moyo wangu, sijui ni shetani gani alikuwa ameingia kwenye ndoa yangu na kunishawishi kumsaliti mume wangu kipenzi. Niliuona mwisho wa ndoa yangu ukija kwa kasi kwa sababu ya ujinga wangu.

Nilienda chumbani na kujilaza kitandani, mawazo yakawa yanaendelea kupita ndani ya kichwa changu huku nikiendelea kujuta. Mara simu yangu ilianza kuita mfululizo, nilipotazama namba ya mpigaji, alikuwa ni Evans, moyo ukanilipuka kwa hofu.

Sikutaka kuipokea simu yake, ikaita mpaka ikakata. Akatuma meseji ya maneno ya vitisho lakini pia sikumjibu. Hakuchoka, akapiga tena na tena mpaka ikawa kero, ikabidi niipokee simu yake. Nilipopokea tu, alianza tena kunitolea maneno ya vitisho, eti akaniambia kama sitaki kuendelea kumpa mapenzi atahakikisha napewa talaka na mume wangu Ibra.

“Nitamtumia mtu ninayemjua mimi kumfikishia mumeo hii video ili ajionee mwenyewe usaliti wa mke wake, lazima uachike mwaka huu, wewe si unajifanya hujui kula na vipofu? Sasa nitakuonesha kazi,” alisema Ibra, kwa hasira nikakata simu na kuzima kabisa.

Yaani kadiri alivyokuwa anazidi kuniletea vitisho na kunilazimisha niendelee kuwa mpenzi wake, ndivyo nilivyokuwa nazidi kumchukia. Sikukubali vitisho vyake vinishinde nguvu, nikaamua kumpuuza ingawa kiukweli nilikosa mno amani ndani ya moyo wangu.

Sikuwa tayari kuachana na Ibra wangu, hasa ukizingatia kwamba hivi sasa nguvu zake zilikuwa zimerejea na kuanza kunipa kile kitu nilichokuwa nakikosa kwa muda mrefu. Wakati nikiendelea kuwaza kuhusu kilichotokea na hatima ya ndoa yangu, nilisikia mtu akigonga mlango.

Nilijifikiria mara mbili kama niende kufungua au niache lakini niliposikia kengele ya mlangoni ikipiga kelele, nilijua lazima atakuwa ni mume wangu. Nikaamka huku nikililazimisha tabasamu kwenye uso wangu, nikajifunga upande wa khanga na kwenda kufungua mlango.

Kweli alikuwa ni mume wangu, nikajitahidi kumchangamkia na kumkumbatia kwa mahaba, naye akafanya hivyohivyo, tukamwagiana mvua ya mabusu kisha tukaingia ndani na kwenda mpaka chumbani ambapo mume wangu alikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua maendeleo yangu.

“Naendelea vizuri mume wangu, ila bado nasikia kichwa kinaniuma,” nilimwambia mume wangu huku nikiendelea kumdanganya kwamba nilishakunywa dawa wakati haikuwa kweli.

Basi alianza kuniandalia chakula cha mchana na kunitaka nisifanye kazi yoyote. Nilibaki chumbani nimejilaza huku nikiendelea kuwaza majanga yangu, chakula kilipokuwa tayari, alikuja kunichukua na kunipeleka sebuleni. Hata hivyo, sikuweza kula kwani nilipotia chakula mdomoni tu, nilianza kutapika mfululizo.

Mume wangu alihisi labda bado ugonjwa haukuwa umeisha, akataka turudi hospitalini lakini nilimtuliza kwa kumwambia kuwa asiwe na wasiwasi kwa sababu natumia dawa nitapona tu. Moyoni nilikuwa natamani siku hiyo ipite haraka ili kesho yake niende kwa Dokta Twalipo kuchoropoa ujauzito huo kwani kama hali ingeendelea namna ile, mume wangu angenishtukia haraka kwani tayari nilishaanza kuchagua aina za vyakula, jambo ambalo halikuwa kawaida yangu. Mume wangu alinirudisha chumbani na kunilaza kitandani, akaenda kuoga na baada ya muda, alirudi na kushika simu yangu.

“Mbona simu yako imezimwa?” mume wangu alisema huku akijaribu kuiwasha, mapigo ya moyo yakanilipuka kuliko kawaida kwani nilijua lazima atakutana na meseji chafu za Evans, nikakurupuka pale nilipokuwa nimelala na kumpokonya simu, jambo ambalo lilimshangaza sana mume wangu.

Hata hivyo, nilipokumbuka kwamba niliweka ‘password’ kwenye simu yangu, kidogo roho yangu ilitulia.

Mume wangu aliiwasha ile simu lakini akashindwa kuendelea kufanya chochote, nikainua mkono kuonesha kwamba nilikuwa nataka anipe. Kwa kuwa mume wangu hakuwa na mazoea ya kupekuapekua simu yangu, aniponipa aliendelea kuwekaweka vitu sawa mle chumbani.

Harakaharaka nikaingiza namba za siri na kwenda kwenye meseji zilizoingia, nikabonyeza sehemu iliyoandikwa ‘delete all’ ikimaanisha futa zote. Meseji zote zikafutika kwenye simu yangu, nilienda na kwenye namba nilizopigiwa ambapo niliifuta ya Evans kisha nikaiweka simu mezani.

Angalau roho yangu sasa ilitulia, mume wangu akaendelea kunihudumia vizuri mpaka jioni ilipofika. Tulienda kulala lakini kiukweli nilikosa amani ndani ya moyo wangu. Hata usingizi haukuja kwa urahisi, mpaka saa tisa za usiku bado nilikuwa na kazi ya kujigeuzageuza tu kitandani.

Nilipopitiwa na usingizi, hakukuchelewa kupambazuka. Kulipokucha, mume wangu aliwahi kuamka kama kawaida yake, akaniandalia kifungua kinywa kisha na yeye akajiandaa, tayari kwa kuelekea kazini.

“Leo naendelea vizuri mume wangu, wewe kafanye tu kazi mpaka jioni,” nilimwambia mume wangu kwani sikutaka arudi mchana kwa sababu nilikuwa na safari ya kuelekea Kawe kwa Dokta Twalipo kuchoropoa ujauzito wa Evans, jambo nililotaka lifanyike kwa usiri mkubwa.

Mume wangu alikubaliana na nilichomwambia, akaniaga na kunitakia nipone haraka, akatoka na kuelekea kwenye maegesho ya magari ambako aliwasha gari lake na kuondoka kuelekea kazini. Alipotoka tu, sikutaka kupoteza muda, nilienda bafuni kuoga, nikavaa vizuri na kuchukua fedha za kutosha kwa ajili ya kazi ile ngumu na ya hatari iliyokuwa mbele yangu.

Dakika kadhaa tangu mume wangu alipoondoka, na mimi nilitoka na kuelekea mtaa wa pili kulipokuwa na maegesho ya teksi. Nikapanda kwenye moja niliyoichagua na kumueleza dereva kunipeleka Kawe, safari ikaanza.

Njia nzima nilikuwa nikitetemeka kwa hofu kwani sikuwahi hata mara moja kutoa ujauzito na kwa maneno niliyokuwa nayasikia kwa watu, kitendo hicho kilikuwa cha hatari mno, kinachoweza hata kukatisha maisha ya anayekifanya.

Hata hivyo, sikuwa na ujanja zaidi ya kufanya hivyo kwani bado nilikuwa naipenda ndoa yangu na sikutaka siri niliyokuwa naificha ifichuke. Dakika kadhaa baadaye niliwasili Kawe.

Baada ya kufika Kawe, nilifuata maelezo niliyokuwa nimepewa na rafiki yangu, nikamuelekeza dereva wa Bajaj kukata kushoto na kuiacha barabara ya lami, tukaendelea kukata mitaa mpaka tulipofika kwenye Mtaa wa Ukwamani.

Kwa kuwa sikutaka dereva huyo wa Bajaj aelewe nilikokuwa naelekea, tulipokaribia, nilimwambia asimame, nikamlipa kisha nikateremka na kuanza kutembea taratibu huku nikiwa bize kutafuta namba ya simu ya Dokta Twalipo.

“Nimefika Ukwamani, naomba nielekeze namna ya kufika kwenye zahanati yako,” nilimuuliza daktari huyo huku nikitetemeka. Akanielekeza kwamba niende mpaka jirani na serikali za mtaa huo, atamtuma mtu kuja kunichukua.

Niliulizia kwa wenyeji mahali zilipokuwa ofisi za serikali ya mtaa huo, kweli nilielekezwa na muda mfupi baadaye nilikuwa nimewasili. Nikamkuta dada mmoja akiwa amesimama kama anayemsubiri mtu.

Mara simu yangu ilianza kuita, nilipoisogeza sikioni ilikata kisha yule dada akanionesha ishara kwamba nimfuate. Kumbe ile ilikuwa ni namba yake na alipiga kwa lengo la kutaka kunitambua kwa urahisi kwani kulikuwa na watu wengi eneo hilo.

Nikaanza kumfuata ambapo tulipita kwenye uchochoro mrefu, tukiruka madimbwi ya maji machafu na kupita marundo ya takataka yaliyokuwa yamekusanywa kwenye vichochoro. Sifa kubwa ya mtaa huo ilikuwa ni uchafu uliokithiri. Viatu vyangu vya bei mbaya nilivyokuwa nimevaa vililowa matope lakini sikujali.

Baada ya kukatiza kwenye vichochoro kadhaa, hatimaye tulitokezea kwenye jengo moja chakavu ambalo kwa nje lilionesha kama hakukuwa na watu waliokuwa wakiishi ndani yake. Tukalizunguka jengo hilo mpaka upande wa pili.

Mlango mkubwa wa mbele ulikuwa umefungwa na hakukuwa na dalili zozote za kuwepo kwa watu kwenye jengo hilo. Tukaenda mpaka kwenye mlango mdogo uliokuwa upande wa nyuma ambao ili kuingia ilikuwa ni lazima uiname.

Yule dada alitangulia, akainama na kuingia ndani, na mimi nikafanya hivyohivyo, tukapita kwenye korido yenye giza na kutokezea ndani. Nilichokiona kiliufanya moyo wangu ushtuke mno kwani kulikuwa na watu wengi sana, tena wote wakiwa ni wanawake.

Kulikuwa na mabenchi huku na kule, wakawa wamejipanga kwa mistari, wote wakionesha kuwa wanasubiri kuingia kwa daktari. Nilipowatazama harakaharaka, niligundua kuwa kulikuwa na mchanganyiko, wanawake watu wazima, wasichana wakubwa na wengine wadogo kabisa ambao hata bila kuuliza nilijua kuwa ni wanafunzi.

“Kaa hapo usubiri zamu yako ya kuingia kwa daktari,” alisema yule msichana aliyenifuata huku akinionesha sehemu ya kukaa. Nikakaa kwenye benchi huku nikitetemeka kuliko kawaida, niliwasalimu niliokaa nao jirani ambao nao walionekana kunishangaa.

Nikawa nayachunguza mandhari ya eneo hilo kwa hofu kubwa, chumba kilikuwa kikubwa chenye dari lililochakaa, lenye michirizi mingi kuonesha kwamba mvua ikinyesha, paa lilikuwa likivuja.

Kulikuwa na utando wa buibui ulioshonana juu ya dari na mwanga hafifu wa taa ndogo. Pia hewa ilikuwa nzito sana. Hata kabla sijaingia kwa daktari, niliiona hatari iliyokuwa mbele yangu.

Nilitamani kuinuka na kuondoka lakini nilipofikiria majanga niliyokuwa nayo, nilijikuta nikipiga moyo konde na kuendelea kukaa. Nilipowahesabu watu waliokuwa ndani ya chumba hicho, walikuwa ni zaidi ya ishirini na tano.

Kwa hesabu za harakaharaka, ingenichukua muda mrefu sana mpaka kuingia kwenda kumuona daktari. Ikabidi nitumie ule usemi wa penye uzia penyeza rupia.

Nilitoa simu yangu ya gharama kwenye pochi, nikamtumia ujumbe Dokta Twalipo nikimwambia kwamba nilikuwa naomba kuonana naye kabla zamu yangu haijafika kwa sababu nilikuwa na dharura. Nikamtangazia dau kwamba nitamuongeza na fedha ya soda.

Dakika kadhaa baadaye, mlango wa chumba cha daktari ulifunguliwa, msichana mmoja mdogo akatoka huku akiwa amejiinamia, mikono ikiwa imeshikilia tumbo lake. Ilionesha kwamba ametoka kuchoropolewa mimba kwa jinsi alivyokuwa akiugulia maumivu makali.

Mwenzake mmoja akasimama na kumshika mkono, akawa anamuongoza kutoka nje. Yule dada aliyenifuata, alitoka na kufunga mlango kwa nje, akanifuata mpaka pale nilipokuwa nimekaa na kunishika mkono, akawa ananipeleka ndani kuonana na daktari.

Niliwasikia wale wenzangu niliowakuta wakianza kupiga kelele za kulalamika kwani niliingilia foleni lakini yule dada akawatuliza kwa kuwaambia kwamba mimi nilikuwa na appointment maalum na daktari Twalipo. Tukaingia ndani.

Chumba chote kilikuwa kikinuka harufu ya damu, kulikuwa na vifaa kama hospitali ingawa suala la usafi kidogo lilionekana kuwapiga chenga wahusika. Upande wa pili kulikuwa na meza yenye mafaili na baadhi ya vifaa juu yake, nyuma yake alikuwa amekaa mwanaume wa makamo, akiwa amevalia miwani na kuishusha chini kidogo.

Bila hata kuuliza, nilijua ndiye dokta Twalipo. Upande mwingine wa chumba hicho kulikuwa na vitanda viwili, kimoja juu yake kulikuwa na mtu amelala na kingine kilikuwa kitupu.

Daktari huyo ambaye muda wote tangu naingia alikuwa bize kuandikaandika, aliinua macho yake na kunitazama, akazidi kushusha miwani yake na kuachia tabasamu hafifu. Sikujua sababu iliyomfanya atabasamu kikware namna ile, nahisi alizuzuka na uzuri wangu.

“Karibu binti, karibu ukae,” alisema huku akiendelea kuniangalia kuanzia juu mpaka chini, nikakaa kwenye kochi chakavu lililokuwa pembeni ya meza yake. Siwezi kuficha, nilikuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu na sikuwahi kudhani ipo siku naweza kuingia kwenye mazingira ya kutisha kiasi hicho.

“Unaitwa nani binti,” aliniuliza Dokta Twalipo huku akijiweka vizuri pale kwenye kiti chake. Nilijitambulisha kisha nikaeleza tatizo langu ambapo aliniambia nisiwe na wasiwasi. Wakati tukiendelea kuzungumza, yule dada aliyekuja kunipokea alikuwa akiosha mikasi na vifaa vinavyotumika kutolea ujauzito.

Baada ya yule nesi kumaliza alichokuwa anakifanya, yule daktari alianza kunipima kwa kutumia kimashine kidogo kinachofanana na kompyuta kilichokuwa pale kwenye meza yake. Akaniambia kuwa ujauzito wangu haukuwa mkubwa hivyo kazi ingekuwa rahisi.

“Panda juu ya kile kitanda,” alisema Dokta Twalipo huku akinioneshea kwenye moja kati ya vile vitanda viwili, nikainuka huku nikitetemeka kuliko kawaida, nikaenda mpaka kwenye kile kitanda ambacho kusema ukweli kilikuwa kichafu sana, damu ikiwa imekaukia kwenye mashuka na kutoa harufu mbaya.

“Huyo mwingine mtoe ameshapumzika, na wewe nisubiri nje mpaka nitakapokuita,” Dokta Twalipo alimwambia yule nesi, kweli akaenda kumuamsha yule dada aliyekuwa amelala kwenye kitanda cha pembeni yangu na kumshika mkono, akawa anamsaidia kutembea kuelekea nje kwani ilionesha yupo kwenye maumivu makali kupindukia.

“Hivi na mimi nitakuwa kama huyu akishamaliza kunitoa mimba?” nilijiuliza huku nikitetemeka kuliko kawaida. Muda mfupi baadaye, baada ya yule nesi kutoka na yule mgonjwa na kufunga mlango, Dokta Twalipo alinifuata mpaka pale kwenye kile kitanda nilipokuwa nimelala.

“Vua nguo zote binti, unapanda na nguo nitafanyaje kazi?” alisema huku akisogeza vifaa vya kutolea mimba pembeni ya kitanda nilichokuwa nimelala juu yake. Nilijifikiria mara mbilimbili kama nivue nguo au nisivue lakini nilipofikiria matatizo makubwa niliyokuwa nayo, sikuwa na ujanja.

Nilishuka na kuanza kuvua nguo moja baada ya nyingine huku aibu tele zikiwa zimenijaa. Hatimaye nilimaliza zote, nikapanda kitandani huku nikiendelea kuona aibu ya hali ya juu. Nilimuona Dokta Twalipo akizidi kutabasamu huku macho ya udenda yakimtoka mithili ya fisi aliyeona mfupa.

“Hapo sawa, kazi inaweza kufanyika sasa,” alisema mwanaume huyo mtu mzima aliyekuwa na kila dalili ya ukware. Alinisogelea pale kitandani na kuanza kuliminyaminya tumbo langu. Alipomaliza alihamia kifuani kwangu na kujifanya ananipima mapigo ya moyo, nilifumba macho kwani sikutaka kuendelea kumtazama usoni.

Alikaa kwa muda mrefu kwenye kifua changu, akishika hapa, mara pale, nikajikuta nikizidi kuwa katika wakati mgumu kwani ilionesha alikuwa na ajenda nyingine tofauti na msaada niliokuwa nautaka kutoka kwake. Aliporidhika, alihamia ‘eneo la tukio’ ambapo alianza kunikaguakagua, nikafumbua macho kwa wizi na kumtazama, alionesha kuwa katika hali mbaya sana, hata sijui kwa nini.

“Binti! Binti,” alinipigapiga kuniamsha. Nikafumbua macho na kumtazama kwa ukamilifu.

“Njia yako inaonekana kuwa kavu sana, inabidi tuilainishe,” alisema daktari huyo huku akivua koti lake la kidaktari kisha akavua na ‘gloves’ alizokuwa amevaa mikononi. Nikashangaa kumuona anafungua mkanda wa suruali yake. Ikabidi nimuulize alikuwa anataka kunilainishaje?

“Inabidi tufanye mapenzi kidogo ili njia ifunguke,” alisema, nikainuka kwa mshtuko na kukaa juu ya kitanda huku mapigo ya moyo yakinienda mbio sana.

Nilimtazama daktari huyo usoni, hakuonesha masihara katika kile alichokuwa anakisema kwani tayari alishakuwa amejiandaa kwa kazi ya kunilainisha.

Japokuwa ni kweli nilikuwa na matatizo makubwa na nilidhamiria kuikoa ndoa yangu, sikuwa tayari kuudhalilisha utu wangu kiasi hicho. Nilikataa katakata huku nikiinuka pale kitandani nikiwa mtupu kabisa, nikakimbilia mahali nilipokuwa nimetundika nguo zangu.

“Vipi tena binti?”

“Dokta, hapana sipo tayari kwa hicho unachokitaka.”

“Sasa binti, mimi nafanya haya yote kwa ajili ya kukusaidia. Nikikutoa bila kukulainisha njia yako utaumia sana. Mbona wenzake wote huwa wanakubali?” alisema daktari huyo huku akiendelea kunibembeleza nikubali aniingilie kimwili eti kwa kisingizio cha kulainisha njia.

Bado niliendelea kushikilia msimamo wangu kwamba sikuwa tayari kwa hicho alichokuwa anakitaka. Alipoona nimeshikilia msimamo wangu na tayari nimeshaanza kuvaa nguo, alitoa wazo jingine.

“Basi nikuchome sindano ya usingizi ili usisikie maumivu,” alisema daktari huyo, nikafikiria kwa muda na kugundua kuwa hiyo ilikuwa ni njama nyingine ya kutaka kutimiza alichokuwa anakitaka kwangu.

Nilimgundua kuwa ameshapagawa na uzuri wa sura na umbo langu na sasa alikuwa akijaribu kufanya mbinu za kufanya mapenzi na mimi, jambo ambalo sikuwa tayari kuona linatokea.

“Hapana, sitaki unichome sindano ya usingizi, ni bora unichome ganzi,” nilimwambia daktari huyo, nikamuona akiishiwa nguvu na kupandisha suruali yake, akafunga mkanda na kunitaka nirudi kitandani. Nikarudi huku safari hii nikiwa makini zaidi kwani nilihisi nikimchekea anaweza kutimiza alichokuwa anakitaka.

Alivaa gloves zake na kusogeza vifaa vyake, akavuta dawa kutoka kwenye kichupa kwa kutumia bomba la sindano kisha akawa anajiandaa kunichoma, huku akiendelea kutabasamu mwenyewe kama mwendawazimu.

Kabla hajanichoma, tulishtuka kusikia mlango wa chumba tulichokuwemo ukigongwa kwa nguvu, huku kelele zikisikika pale koridoni nilipowaacha wanawake wengi waliokuwa wanasubiri zamu yao ya kuingia kwa Dokta Twalipo kutolewa ujauzito.

“Nani huyo anayegonga mlango kwa fujo kiasi hicho? Anafikiri hapa ni kwake?” alisema Dokta Twalipo huku akiacha kila alichokuwa anakifanya na kuusogelea mlango ambao bado ulikuwa ukiendelea kugongwa kwa nguvu. Kengele ya hatari ilishalia ndani ya kichwa changu hivyo niliwahi kwenda kuvaa nguo zangu.

Dokta Twalipo alipofungua mlango tu, alikutana na sura ambazo hakuzitegemea:

“Sisi ni maafisa wa jeshi la polisi, upo chini ya ulinzi,” alisema mwanaume mmoja mrefu mwenye mwili mkubwa, aliyeonekana kuwa kiongozi wa wenzake. Mwanaume huyo akaingia akiwa ameongozana na wenzake wanne, watatu kati yao wakiwa wamevalia sare za kipolisi.

Miongoni mwa siku ambazo nilipata mshtuko, basi ilikuwa ni siku hiyo. Mapigo ya moyo yalikuwa yakinienda mbio kuliko kawaida wakati wale askari waliokuwa na silaha wakimfunga pingu Dokta Twalipo, nikajua anayefuatia ni mimi kwani kisheria, anayetoa mimba na anayetolewa wote wana hatia

“Mchukueni na huyo akaunganishwe na wenzake hapo nje,” alisema yule mmoja aliyeonekana kuwa na mamlaka kuliko wenzake, nikatolewa msobemsobe mpaka pale koridoni ambapo nilikuta wale wanawake wote niliowapita pale, wakiwa wamekalishwa chini huku kukiwa na askari wengine kadhaa.

Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yakinidunda mno, nikawa najiuliza nitamwambia nini mume wangu atakaposikia nimekamatwa nikiwa nataka kutoa ujauzito. Nilianza kuuona mwisho wangu, nilijilaumu sana ndani ya moyo wangu kwa hatua niliyoichukua.

“Haya simameni na mjipange kwa mstari,” alisema askari mmoja wakati Dokta Twalipo akitolewa akiwa amefungwa pingu na kubebeshwa vitendea kazi vyake. Tukasimama huku kijasho kikinitoka, tukapangwa kwa mstari na kuanza kutolewa nje.

“Afande samahani naomba tuzungumze,” nilimnong’oneza yule askari aliyeonekana kuwa kiongozi wa wenzake alipopita karibu yangu lakini alinipita kama hajasikia nilichokisema, nikajua mwisho wangu umefika.

Tulianza kutolewa nje, tukakuta umati mkubwa wa watu ukiwa umesimama kwenye vichochoro vya kuingilia eneo hilo, kila mtu akitushangaa na wengine wakituzomea. Ilikuwa ni aibu ya mwaka ambayo haijawahi kutokea maishani mwangu.

“Ulikuwa unasemaje?” yule askari alinisogelea na kuniuliza wakati tukiendelea kukatiza kwenye vichochoro, nikamgeukia na kumtazama huku machozi yakiwa yameanza kunitoka.

“Nakuomba uniokoe afande, mimi ni mke wa mtu na mume wangu hajui chochote, nipo tayari kukupa chochote unachotaka,” nilisema huku nikiingiza mkono kwenye pochi yangu na kutoa fedha zote nilizokuwa nimezibeba na kutaka kumpa lakini alitingisha kichwa kuzikataa na kugeuka huku na kule kuwaangalia wenzake.

Akaondoka bila kusema chochote na kwenda mbele ya msafara ule wa wanawake zaidi ya thelathini tuliokutwa kwenye ofisi ya Dokta Twalipo. Baada ya kukatiza vichochoro hatimaye tulitokezea kwenye eneo lenye uwazi ambapo kulikuwa na difenda mbili za polisi zikiwa zinatusubiri.

Dokta Twalipo alikuwa wa kwanza kupakizwa, akafuatiwa na wanawake wengine waliopakizwa kwenye ile difenda ya kwanza mpaka ikajaa. Wengine wakaanza kupandishwa kwenye ile difenda ya pili, foleni ikasogea hadi ilipofika zamu yangu ya kupanda.

Nikiwa bado siamini kwamba ndiyo nimepatikana, nilishtuka nikiguswa begani, nilipogeuka alikuwa ni yule askari, akaniambia nisubiri pembeni kwanza. Huku nikiwa natetemeka nilisogea pembeni, wenzangu wakaendelea kupanda mpaka difenda ya pili nayo ikajaa.

Chini tukawa tumesalia wachache ambapo zile difenda mbili ziliondoka kwa kasi na kutuacha palepale, askari watatu wakiwa wamesalia kutulinda akiwemo yule niliyezungumza naye.

“Hebu wewe njoo huku,” alisema yule askari kwa sauti kali akinioneshea ishara mimi. Kwa jinsi alivyoongea kwa ukali, nilijua hawezi kukubali kuniachia kirahisi, tukasogea pembeni na kuwa kama tunarudi kule tulikotoka. Tulipoingia uchochoroni, tulisimama ambapo aliniambia nitoe nilichokuwa nataka kumpa muda ule.

Nilitoa fedha zote nilizokuwa nazo, kiasi cha kama laki moja na nusu nilizobeba na kumpa, akaziweka mfukoni bila hata kuzihesabu na kunipa simu yake nimuandikie namba yangu.

“Pita njia ya huku uondoke haraka na usirudie tena kujaribu kufanya ulichokuwa unataka kukifanya, ni makosa makubwa kisheria,” alisema yule askari huku akinionesha uchochoro mwingine wa kupita, akaniambia atanipigia simu baadaye.

Nilimshukuru mno, yaani mpaka naondoka nilikuwa bado siamini kama kweli nimesalimika, nilitembea harakaharaka huku muda mwingine nikitamani kuvua viatu na kuvishika mkononi kwani nilihisi vinanichelewesha.

Baada ya kukatiza sana kwenye vichochoro, hatimaye nilitokezea kwenye barabara ya lami, jirani na kambi ya jeshi. Ilibidi nitoe kitambaa na kuanza kujifuta jasho ambalo lilikuwa linanitoka kwa wingi mno.

Nikasimama barabarani kusubiri usafiri wowote wa kunikimbiza nyumbani kwani muda nao ulikuwa umeyoyoma na kulikuwa na uwezekano mkubwa mume wangu angeweza kurudi nyumbani na kunikosa.

Nikiwa nimesimama palepale barabarani, huku kichwa kikiendelea kunichemka, nikitafakari bila kupata majibu juu ya mimba haramu niliyokuwa nayo, nilisikia simu yangu ikiita mfululizo.

“Mungu wangu!” nilisema huku nikitetemeka kuliko kawaida baada ya kugundua kuwa aliyekuwa anapiga alikuwa ni mume wangu. Nilibaki nimeganda kama nimepigwa na shoti ya umeme, nikijiuliza kama nipokee au nisipokee. Nilishindwa kujua hata nikipokea nitamueleza nini mume wangu.

Nilichokifanya ilikuwa ni kuiacha simu iite mpaka ikatike. Muda mfupi baadaye, niliona bodaboda moja ikija kutokea upande wa Mwenge, nikamsimamisha dereva ambapo aliposimama tu, harakaharaka nilipanda na kumuelekeza kunipeleka Mikocheni haraka iwezekanavyo.

Hata sikukumbuka kumuuliza bei kwani mpaka muda huo, sikuwa hata na senti tano mfukoni baada ya kutoa hela zote kumhonga yule askari. Dereva wa bodaboda akatii nilichomwambia ambapo kweli alikimbia sana, muda mwingine akipita hata sehemu ambazo haziruhusiwi ili tu kuniwahisha.

Mara nyingi mimi huwa ni mwoga sana kupanda bodaboda kwenye lami lakini siku hiyo sikujali kitu, woga wote uliniisha. Wakati tukiendelea kuyoyoma na bodaboda kama mkuki, simu yangu ilikuwa ikiendelea kuita lakini sikuthubutu kuipokea.

Hatimaye tuliwasili Mikocheni, nikamuelekeza mitaa na dakika chache baadaye, tulikuwa kwenye geti la nyumba yetu ya kifahari. Nikamuelekeza dereva wa bodaboda kunisubiri palepale ili nikamchukulie fedha zake ndani.

Sikuwa najua nitamjibu nini mume wangu nikimkuta ndani kwani haikuwa kawaida yangu kuondoka bila kumuaga au kutopokea simu zake. Nilitoa funguo na kufungua mlango, harakaharaka nikaingia mpaka ndani. Nashukuru Mungu sikumkuta mume wangu, nikaenda mpaka chumbani ambapo nilitoa fedha kwenye droo na kwenda kumlipa yule dereva wa bodaboda.

“Zinakutosha?” nilimuuliza dereva wa bodaboda wakati nikimkabidhi noti mbili za shilingi elfu kumikumi, akazipokea na kushukuru kwani inaonekana hata yeye hakutegemea kama atapata fedha nyingi kiasi hicho. Alinishukuru kisha akawasha bodaboda yake na kuondoka.

Harakaharaka niliingia ndani na jambo la kwanza ilikuwa ni kukimbilia bafuni kuoga kwani pilikapilika za Kawe zilisababisha nichafuke mno, hasa miguuni. Nikaoga vizuri kisha nikarudi chumbani ambapo nilitoa simu na kuiangalia.

Kulikuwa na ‘missed calls’ nyingi sana za mume wangu, nikawa najiuliza sijui nitamjibu nini. Nikajikaza na kumpigia, akapokea harakaharaka na kuniuliza kama nipo salama.

“Nipo salama mume wangu, samahani nilikuwa nimelala sijaisikia simu wakati inaita,” nilimdanganya huku nikibana sauti ili ionekane kama kweli nilikuwa nimelala.

“Nipo njiani nakuja, nilipoona nakupigia simu hupokei nilifikiri umezidiwa ikabidi niombe ruhusa kazini,” alisema mume wangu, nikazidi kupatwa na hofu kwani kama angekuja, angegundua kwamba sikuwa nimelala. Alipokata simu tu, niliinuka na kuweka vitu sawa ili isiwe rahisi kwa mume wangu kugundua kwamba nilikuwa nimetoka. Nilipomaliza nilienda kujilaza kitandani na kujifunika huku nikiyafikicha macho yangu ili hata akirudi, aone kweli nilikuwa nimetoka usingizini.

Mawazo bado yaliendelea kukitesa kichwa changu, sikujua nini cha kufanya baada ya kushindikana kwa jaribio langu la kwanza la kutaka kutoa mimba ile bila mume wangu kujua. Sikuwa tayari kuzaa kwani kwa kufanya hivyo, lazima ukweli ungejulikana, jambo ambalo lingeisambaratisha kabisa ndoa yangu.

Kweli muda mfupi baadaye, mume wangu alirudi na kunikuta nimelala kitandani, huku nikijilazimisha kuonekana kwamba nimelala kwa muda mrefu. Akaingia na kuja mpaka kitandani ambapo alinibusu kisha akaanza kunipima joto la mwili kwa kutumia kiganja chake.

Maskini mume wangu, alikuwa akinionesha mapenzi mazito na kunijali sana bila kujua kilichokuwa ndani ya moyo wangu.

“Nimekuletea baga,” alisema na kunibembeleza niamke, kweli nikaamka na kujifanya najilazimisha kula baga aliyoniletea mume wangu. Hilo lilikuwa kosa kubwa kwani licha ya kwamba kweli nilikuwa mpenzi wa baga ambazo mume wangu ndiye aliyenifundisha, lakini hali yangu ya ujauzito ilikuwa ikikataa baadhi ya vyakula.

Nilipoonja kidogo tu, nilitapika mno, hali iliyozidi kumpa wasiwasi mume wangu. Akaniambia kwamba yeye anahisi nimepata ujauzito kwa sababu haikuwa kawaida yangu, hata kama ilikuwa ni homa mbona nilishatumia sana dawa!

“Inabidi nikanunue kipimo cha mimba nije kukupima mwenyewe,” alisema Ibra huku akiinuka na kutoka nje, mapigo ya moyo wangu yakawa yananienda mbio kuliko kawaida kwani hatimaye njia ya mwongo ilikuwa imefikia mwisho. Kwa kuwa duka la dawa halikuwa mbali, dakika kadhaa baadaye alirudi na kipimo hicho.

Akaniambia nikajisaidie haja ndogo na kuweka kwenye kichupa kidogo ili tupime kwa pamoja. Sikuwa na ujanja, kweli nilienda chooni huku nikitetemeka kuliko kawaida. Kuna wakati nilitamani niweke maji badala ya haja ndogo lakini moyo ukasita kwani nilihisi itakuwa rahisi kwa mume wangu kushtuka kwamba kuna kitu namficha.

Nikawa sina ujanja zaidi ya kufanya kama nilivyoambiwa, nikarudi chumbani nikiwa na kichupa kilichokuwa na haja ndogo. Nikampa mume wangu ambaye alichana karatasi lililokuwa na kile kipimo kisha akakiingiza kwenye kichupa kilichokuwa na haja ndogo.

Kwa jinsi nilivyokuwa natetemeka, nilijua lazima mume wangu anaweza kunishtukia, ikabidi nivunge kwamba naenda kuoga ili kutoa uchovu wa usingizi. Nikamuacha anaendelea kusubiri kile kipimo kibadilike.

Nilijichelewesha bafuni kwa makusudi kwani nilikuwa najua ni majibu gani mume wangu atayapata.

“Mke wangu, mke wangu,” nilisikia mume wangu akiniita kwa sauti kubwa, moyo wangu ukalipuka na mapigo ya moyo kuanza kunienda mbio kuliko kawaida. Nikaitikia kwa hofu kubwa.

“Njoo mke wangu,” alisema mume wangu akionesha kuwa na furaha kubwa. Nikajifunga taulo na kutoka huku nikiwa bado nimejawa na hofu kubwa ndani ya moyo wangu. Cha ajabu, mume wangu hakuwa vile ambavyo nilitegemea angekuwa baada ya kugundua kuwa nina ujauzito.

Alionesha kufurahi mno, akaja mwilini na kunikumbatia kwa nguvu huku akiniambia kwamba nimepata ujauzito.

“Unasema kweli?” nilimuuliza huku nikiwa bado siamini kwamba hajashtukia mchezo mzima.

“Angalia mwenyewe,” alisema huku akiniachia na kwenda kuchukua kile kipimo na kunionesha, kweli mistari miwili ya rangi nyekundu ilikuwa imetokea kuonesha kwamba nilikuwa na ujauzito.

Maskini mume wangu! Akawa anarukaruka huku na kule na kuimba kwa furaha kushangilia ujauzito wangu bila kujua kwamba rafiki yake Evans ndiye aliyekuwa mhusika wa mzigo huo. Akaja kunikumbatia tena huku akiendelea kufurahi, ikabidi na mimi nimuungie na kujifanya nina furaha kubwa.

Japokuwa mume wangu hakuwa akijua chochote, nilijisikia vibaya sana ndani ya nafsi yangu kwani nilikuwa na uwezo wa kuifanya furaha yake iwe ya kweli kama ningekuwa mwaminifu na kuwa na subira kidogo kwenye ndoa yangu.

“Mimi nilihisi tu, huku kuumwaumwa niliona kumezidi kumbe tayari mambo yamejipa,” alisema mume wangu na kunimwagia mvua ya mabusu. Akaendelea kufurahi huku akinishukuru sana kwa kumbebea ujauzito.

“Na mimi nitaanza kuitwa baba,” alisema akionesha kusuuzika sana ndani ya moyo wake. Siku hiyo ilipita huku mume wangu akiwa na furaha kubwa sana ndani ya moyo wake. Ilibidi niufute kabisa mpango wa kwenda kuutoa tena ujauzito wangu ingawa bado nilikuwa na mtihani mkubwa baadaye mtoto akizaliwa.

“Naomba Mungu akizaliwa asiwe amefanana na baba yake halisi,” niliwaza usiku baada ya kuzinduka kutoka usingizini. Mume wangu alikuwa amelala huku amenikumbatia kwa upendo.

Siku zilizidi kuyoyoma, ujauzito wangu ukazidi kukua huku mume wangu akizidisha mapenzi kwangu mpaka nikawa najishtukia. Kila siku ilikuwa ni lazima aniletee zawadi akitoka kazini. Kabla hajaondoka ilikuwa ni lazima alibusu tumbo langu na akirudi kazini ilikuwa ni lazima afanye hivyohivyo.

Nakiri kwamba mahaba aliyokuwa ananionesha mume wangu kipindi nikiwa mjamzito, yalikuwa makubwa mno. Kama wanaume wote wangekuwa wanajua kujali kama Ibra wangu, hakika wanawake tungekuwa tunapenda sana kubeba ujauzito na kuzaa.

Nilikuwa sikohoi, tayari mume wangu yuko pembeni yangu. Hata kazini hakuwa akikaa kama zamani tena, muda mwingi alikuwa anautumia kuwa na mimi. Siku nyingine akawa ananitoa kwenda kufanya mazoezi ya kutembea, siku nyingine tunaenda ufukweni, yaani ilikuwa raha mno.

Hata hivyo, moyo wangu ulikuwa unateketea ndani kwa ndani. Nilikuwa najilaumu sana kwa nilichomfanyia mume wangu kwani niligundua kuwa hata kama kipindi hicho alikuwa na udhaifu mkubwa katika suala zima la kumfurahisha mwanamke, bado hakustahili adhabu kali kama ile.

Siku zilizidi kusogea, kitumbo nacho kikawa kinazidi kuwa kikubwa, mtoto akaanza kucheza na kuzidi kumfurahisha mume wangu. Hakuna siku ambayo nilienda kliniki peke yangu, kila siku alikuwa akinipeleka na kunidekeza utafikiri mtoto mchanga.

Kwa kipindi chote hicho, Evans hakuwa akijua chochote kinachoendelea. Naye alipoona mahaba ambayo mume wangu alikuwa akinionesha, nadhani alianza kushikwa na wivu ndani ya nafsi yake kwani safari za kuja nyumbani kwetu zilipungua na baadaye zikaisha kabisa.

Hata vile vitisho alivyokuwa ananipa, navyo viliisha nadhani ni baada ya kuona hali niliyokuwa nayo. Hatimaye miezi tisa ilitimia, nikashikwa na uchungu wa kujifungua. Mume wangu alihangaika sana siku hiyo, tena bila msaada wa mtu yeyote. Akanikimbiza Hospitali ya Aga Khan ambako nilijifungua mtoto wa kiume kwa njia ya kawaida.

“Hongera dada, umejifungua dume la nguvu,” alisema nesi aliyenisaidia kujifungua, moyo wangu ukalipuka mno na kitu cha kwanza ambacho nilitaka kukithibitisha kabla hata mume wangu hajaenda kuitwa, ilikuwa ni kama mtoto huyo amefanana na nani?

Nikamuomba yule nesi aniletee mwanangu nimuone, kweli alifanya hivyo ambapo kitu cha kwanza ilikuwa ni kumtazama usoni. Mungu mkubwa, mtoto alikuwa amefanana sana na mimi kuliko mtu yeyote ila ilikuwa ukimchunguza sana, unagundua kuwa kuna baadhi ya vitu amefanana na baba yake halisi ambaye ni Evans.

Pua yake ilikuwa kama ya Evans na hata vidole vya mikononi vilikuwa vikifanana na baba yake. Nikashusha pumzi ndefu na kuanza kutunga uongo wa kuja kumdanganya mume wangu endapo atahoji kitu chochote kuhusu mtoto. Bado moyo wangu haukuwa na amani hata kidogo.

Muda mfupi baadaye, mume wangu alienda kuitwa na kuja kuoneshwa ‘mtoto wake’. Maskini, mume wangu alifurahi sana kumuona mtoto huyo, akambusu kwa furaha huku akinisifu kwamba nimekuwa kama mashine ya fotokopi kwa sababu nimezaa mtoto anayefanana na mimi kwa kila kitu.

“Ila pua na vidole vya mikono anafanana na marehemu babu mzaa baba,” nilimuwahi mume wangu, akakubali huku akiendelea kufurahi mno ndani ya moyo wake. Akaja kunikumbatia na kunibusu kwa furaha huku akinipongeza na kunipa pole kwa kazi kubwa niliyoifanya.

Wazazi wangu na ndugu zangu wengi walipopata taarifa, walifika kwa wingi hospitalini kuja kuniona. Kwa kuwa nilijifungua kwa njia ya kawaida, siku hiyohiyo jioni niliruhusiwa kutoka na safari ya kurudi nyumbani ikaanza ambapo tulipanda kwenye gari moja pamoja na ndugu zangu kila mmoja akiwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake.

“Naona baba hujataka kuchelewesha kazi, mwaka mmoja kwenye ndoa tayari kuna dume la nguvu limekuja,” mama alimtania mume wangu wakati akiendesha gari, wote wakacheka sana ndani ya gari. Ilibidi na mimi nicheke kinafiki kwani ukweli nilikuwa naujua.

Tulifika nyumbani ambapo tayari maandalizi yalishaanza kufanyika, wazazi wa mume wangu na ndugu zake nao walijaa pale nyumbani kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa. Ilikuwa siku ya kipekee sana kwa familia yetu, majirani, marafiki na ndugu wakawa wanamiminika kwa wingi.

Kesho yake asubuhi, mume wangu aliwahi kuamka na kuniomba aende kutoa taarifa kazini kwao kisha atarudi baada ya muda mfupi. Kwa kuwa kulikuwa na watu wengi waliolala pale nyumbani kusaidia kazi, wala hakukuwa na tatizo kwa yeye kuondoka.

Majira ya kama saa nne hivi, mume wangu alirejea akiwa na marafiki zake waliokuwa wakifanya kazi pamoja akiwemo Evans, mapigo ya moyo wangu yakaanza kunienda mbio baada ya kugundua kuwa Evans naye alikuwa amekuja kumuona mtoto, nikajua kunaweza kutokea tatizo kubwa kwani akimuangalia, atagundua kuwa ni wake kutokana na jinsi walivyofanana pua na vidole.

Hata hivyo, sikuwa na ujanja, mtoto akaandaliwa na wale wafanyakazi wenzake walioniletea zawadi nyingi, wakawa wanambeba mtoto na kupokezana. Hatimaye akafika kwenye mikono ya Evans.

Moyo ulinilipuka paah! Nikawa namuangalia Evans ataonesha hali gani baada ya kumshika mtoto. Nilichokihisi ndicho kilichotokea, baada ya kumshika mtoto huyo, Evans alimtazama kwa makini usoni halafu ghafla akaonesha kushtuka mno.

Kwa kuwa watu wengine walikuwa wakiendelea na stori za hapa na pale, kila mmoja akifurahia ujio wa mtoto katika familia yetu, hakuna aliyeuona mshtuko wa Evans zaidi ya mimi peke yangu.

Akiwa bado amepigwa na butwaa, Evans aliinua uso wake kunitazama, macho yetu yakagongana. Moyo ukanilipuka tena kwa mara nyingine, harakaharaka nikakwepesha macho yangu.

Ilibidi Evans azuge kwani tayari watu walishaanza kumuangalia, akajichekesha kidogo huku akimrusharusha mtoto mikononi mwake, mwisho akachomekea: “Amefanana sana na mama yake,” alisema huku akionesha ishara ya mtu mwingine naye ampokee mtoto.

Kwa kuwa watu walikuwa wengi sebuleni, mtoto alipokelewa na wageni wengine na kuendelea kumsifia kwamba alikuwa mzuri sana na alifanana na mimi kwa vitu vingi. Wakati sifa kedekede zikiendelea kumiminika, mimi akili zangu hazikuwepo kabisa, furaha yote ndani ya moyo wangu ilikuwa imeingia shubiri.

Hali ilikuwa hivyohivyo kwa Evans, ghafla naye alionekana kuzama kwenye dimbwi la mawazo, akawa wala hachangii tena kwenye stori alizokuwa anapiga na wenzake, akiwemo mume wangu.

Dakika chache baadaye, nilimuona akitoa simu yake mfukoni, akaibonyezabonyeza na kuiweka sikioni kisha akainuka huku akiwaoneshea ishara wenzake kwamba anaenda kuongea na simu nje lakini atarudi. Niligundua kuwa hiyo ilikuwa ni gia yake ya kuondokea kwani alishachanganyikiwa.

Nilichokihisi ndicho kilichotokea kwani tangu alipotoka, muda uliendelea kuyoyoma lakini hakurejea. Kwa kuwa mle ndani kulikuwa na watu wengi, haikuwa rahisi kuliona pengo lake. Maswali mengi yakawa yanaendelea kupita ndani ya kichwa changu, nikijiuliza nitamjibu nini mwanaume huyo ili asiendelee kunisumbua.

Muda uliyoyoma na hatimaye wageni wakaanza kuaga, wale wafanyakazi wenzake na mume wangu ndiyo waliokuwa wa kwanza kuondoka, mume wangu akawasindikiza wakati mimi nikiendelea kuhudumiwa na ndugu zangu wengine.

Wale ndugu nao baadaye walianza kupungua na mwisho tukabakia wachache tu, mimi, mume wangu, kachanga kangu na ndugu wawili kutoka upande wa mume wangu na mmoja kutoka upande wetu ambao kazi yao ilikuwa ni kunihudumia mimi pamoja na mtoto.

Tukiwa bado pale sebuleni, kuna ujumbe uliingia kwenye simu yangu, nikamuagiza ndugu mmoja anichukulie simu yangu kwani kwa muda wote huo ilikuwa imechomekwa kwenye chaji.

Simu ilipoletwa, nilitoa ‘password’ kwani siku hizi simu yangu ilikuwa ni lazima iwekwe password na ni mimi pekee ndiye niliyekuwa naijua. Nilipoufungua ujumbe huo, moyo wangu ulilipuka ‘paah’ baada ya kugundua kuwa ulikuwa umetoka kwa Evans.

“Nahitaji muda wa kuzungumza na wewe, ni muhimu sana,” ulisomeka ujumbe huo, nikashusha pumzi ndefu na kuufuta harakaharaka. Nikajua kwa vyovyote lazima atakuwa ameshtukia mchezo kwamba yule mtoto ni wake na si wa mume wangu kama kila mtu alivyokuwa akiamini.

Sikutaka kuonesha tofauti yoyote kwani mume wangu alikuwa karibu yangu, akiendelea kukafurahia kachanga. Muda wa kulala ulifika ambapo mume wangu alijitahidi kadiri ya uwezo wake kuniandalia kila kitu muhimu, huku wale ndugu wao wakifanya kazi ndogondogo.

Hata sikujua siku ambayo mume wangu ataujua ukweli itakuwaje kwani furaha aliyokuwa nayo ndani ya moyo wake, ilikuwa haielezeki. Tulienda kulala huku kichwa changu kikiwa na mawazo mengi mno.

Uamuzi ambao niliamua kuuchukua kuhusu Evans, ilikuwa ni kumkatalia kwamba mtoto huyo siyo wake na wala asiendelee kunisumbua.

Tulilala mpaka kesho yake huku mume wangu akiendelea kusherehekea kile alichokiita matunda ya ndoa yake. Kesho yake hakwenda kabisa kazini, tukashinda wote nyumbani huku kazi kubwa ikiwa ni kupokea wageni kutoka kila sehemu ambao walikuwa wakija kutupongeza kwa kupata mtoto.

Kitu cha kujivunia kwa mume wangu, alikuwa na marafiki na watu wa karibu aliokuwa anaheshimiana nao wengi sana kiasi kwamba tulipokea wageni mpaka tukaanza kuchoka. Kila mmoja alikuwa akileta zawadi, chumba chetu kikajaa zawadi kibao kwa ajili ya mtoto.

Siku hiyo nayo ilipita na kwa kuwa ruhusa aliyopewa mume wangu ilishaisha, ilibidi asubuhi ajiandae na kuondoka, akaniacha mimi, kachanga ketu ambako bado tulikuwa hatujakapa jina mpaka baada ya siku saba kama mila za kwao zinavyosema, pamoja na ndugu wa kike mmoja kwani wale wengine wawili walishaondoka.

Alipoondoka tu, simu yangu ilianza kuita. Nilipotazama namba ya mpigaji, alikuwa ni Evans, moyo ukanilipuka tena huku nikiandaa majibu ya kumpa.

“Nimemuona mumeo akiondoka kwenda kazini, nakuja hapohapo nyumbani tuzungumze,” alisema Evans kisha simu ikakatwa bila kunipa hata nafasi ya kuzungumza chochote.

ITAENDELEA

My Repentance (Kutubu Kwangu) Sehemu ya Tano

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment