Aziza wa Facebook Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA: NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Chombezo: Aziza wa Facebok
Sehemu ya Nne (4)
Gari lile likaendelea kuja, lilipofika karibu na pale tulipokaa, nikasimama na kisha kulisimamisha kwa kupunga mkono. Kwanza washikaji wakaonekana kunishangaa, hawakuwa wakifahamu kitu chochote kile kilichokuwa kikiendelea mahali hapo. Nilibaki nikiwa nimesimama nje ya mlango hasa baada ya Aziza kusimamisha gari, sikuweza kumuona kwa sababu vioo vilikuwa tinted. Aliposhusha kioo…MUNGU WANGU!
Ngoja nikwambie kitu rafiki yangu. Kati ya majini wote wanaojigeuza kuwa warembo na kuua wanaume nyakati za usiku umewahi kuwaona? Kabla sijaendelea, ngoja nikwambie kitu fulani. Mimi kama mimi nilikwishawahi kukutana na msichana ambaye alikuwa jini nyakati za usiku, tena nakumbuka ilikuwa mkoani Kilimanjaro katika kipindi ambacho kulikuwa na tetesi nyingi kuhusiana na majini ambao walikuwa wakiua watu nyakati za usiku, bila shaka ilikuwa 2006 au 2007.
Usijiulize nilijuaje kwamba huyo mwanamke alikuwa jini. Nilikutana nae usiku katika kipindi ambacho nilikuwa nikielekea Majengo katika kipindi cha likizo, nakumbuka ilikuwa saa mbili usiku, tulifunga shule na kuja Dar es Salaam niliona ningetumia gharama kubwa.
Nilikutana na huyo msichana, asikwambie mtu, alikuwa mrembo mkali sana, ukali wa msichana yule jini sikuwahi kuuona kwa msichana yeyote yule toka nizaliwe, hata mrembo wangu alikuwa haingii ndani.
Nilipopishana nae, alikuwa akinukia manukato mazuri sana, nywele zake zilikuwa ndefu, nilitamani kumsalimia, ila nilikuwa dogo, nadhani kama ningekuwa mkubwa, siku hiyo na mimi lazima ningeuliwa tu…yaani ni LAZIMA. Unamwacha vipi msichana mrembo unayepishana nae? Ukimwangalia, mwarabu si mwarabu, mzungu si mzungu na mtu mweusi si mtu mweusi. Nilipopishana nae, nilipiga kama hatua tano, nilipogeuka nyuma ili niangalie umbo lake la nyuma, kajazia vipi, sikumuona, kilichofuata…ni kutoka nduki tu huku nikipiga kelele.
Nilipokuwa nikiwangalia Aziza katika kipindi hicho nilikuwa nikimfikiria yule mwanamke jini wa kule Kilimanjaro. Aziza, aisee Aziza….Mhh! Nadhani Eduado alikuwa mchoyo, hakutoa sifa ambazo alistahili kuwa nazo Aziza, Aziza alikuwa msichana mzuri sana, msichana ambaye….dah! Sijui nizungumze vipi.
Hahaha! Kwanza kwa washikaji. Walipoona kwamba nimelisimamisha gari lile, wakataka kuangalia ndani kujua kuna nani, nilikuwa nimewapa mgongo, mlango ulipofunguliwa, Aziza akatoka nje…aiseeee. Si kwa watoto, watu wazima, mababu, wala warembo wengine, wote wakabaki wakimshangaa Aziza, alikuwa mkali mpaka mtu mzima nikawa najipa mapungufu.
Ukiachana na zile sifa za uchoyo ambazo alikuwa amezitoa Eduado juu ya Aziza, acha nikwambie jinsi alivyo, umtengeneze Aziza wako kichwani mwako na uone ni jinsi gani alikuwa mrembo.
Kwanza Aziza alikuwa Mpemba, kwa hapo sitaki nizungumze sana kwa kuwa wote mnaamini kwamba wapemba wamebarikiwa kwa urembo, mtoto alionekana kuwa baba yake alikuwa mwarabu, tena wa Dubai, mama yake alikuwa Mlangi, vuta picha mtu mzima. Mtoto alikuwa na nywele nyingi sana, hapo ndipo nilipogundua mapungufu ya sifa za Eduado. Mtoto hakuwa na nywele zilizoishia kwenye mabega, mtoto minywele ilikuwa hiyooo mpaka mgongoni huku zikiwa zinang’aa sana. Uso wake ulikuwa mwembamba ambao ulikuwa ukizungukwa na tabasamu pana ambalo lilikuwa likiyafanya meno yake meupeeee kuonekana. Ukiachana na hayo, huyu mtoto alikuwa na kidoti aisee, tena kile kidoto kilichokuwa karibu na pua, kilimfanya kupendeza sana.
Ukiachana na uso wake uliomfanya kuonekana kama malaika, umbo lake lilikuwa zuri sana. Huwa wapemba ni kama waarabu au wachina, hawana makalio hayoooo tofauti na wanawake wetu weusi, yeye alikuwa mwembamba wa wastani, kifua chake kilikuwa kimesimama. Kwa sababu alikuwa amevaa sketi fupi kiasi, miguu yake haikuwa miguu ya bia, ilikuwa miguu ya wastani kidogo. Kila nilipokuwa nikimwangalia, mtoto hakuwa na kovu lolote lile, yaani alionekana kama katengenezwa kupitia Adobe Photoshop na kisha kuja kwangu.
AZIZA: Wao Ibraaaaaa.
Aliniambia kwa furaha na kisha kunikumbatia. Watu wote ambao walikuwa wakimwangalia Aziza wakaanza kutushangaa, Aziza alionekana kama mzungu, nilionekana kuokota embe katika mti wa mlimao au kujenga nyumba kubwa angani. Aziza alikuwa akinukia vizuri sana, harufu ya manukato yake ikanifanya nifall inlove zaidi na zaidi. Nilitamani kumbeba juu juu. Warembo wa pale mtaani ambao walikuwa wakiniringia sanaaaaaa, katika kipindi hiki walionekana kushikwa na wivu huku mioyo yao ikiukubali uzuri wa Aziza.
MIMI: Mzima wewe cheupe?
AZIZA: Mimi mzima.
MIMI: kweli nilipatia, sikutoka nje hata mara moja.
AZIZA: Ulipatia nini?
MIMI: Wanawake mnaoweka picha za midoli na maua huwa mnakuwa wakali sana.
AZIZA: Kwani mimi mzuri?
MIMI: Nilikuwa najiuliza kwamba hivi umezaliwa hapa duniani au umeshushwa kutoka hukooooo.
AZIZA: Hahaha! Acha hizo Ibra.
MIMI: Mtoto unaonekana kuwa mrembo sana, mtoto una mvuto wa ajabu, mtoto unaonekana zaidi ya malkia Cleopatra aiseee…dah! Ulivyonikazia kuwa na mimi sawasawa tu manake ungenisababishia kifo.
AZIZA: Kivipi?
MIMI: Mmh! Hapa kifo nje nje aiseee. Tena bora ulivyokuwa na gari manake ungekuwa unatembea kwa miguu, utawafanya hata wale wanaokwenda msikitini kuswali wakatishe safari zao, utawafanya mpaka wale wanaokwenda kanisani kusali wakatishe safari zao kwa muda wakuangalie wewe. Kama vitabu vya dini vinavyosema kwamba ukimwangalia mwanamke na kumtani utakuwa umeshazini nae, haki ya Mungu nina uhakika wewe umeshazini na watu wengi maishani mwako. Umeshazini na mimi, umezini na wale marafiki zangu, umezini na wale mababu waliokaa pale chini wakicheza bao, mbaya zaidi, umezini mpaka na wasichana wenzako….hahahaha! Wamekusaga.
AZIZA: Yaani yote hiyo kwa sababu wamenitamani?
MIMI: Ndio. Hebu jiangalie, hivi unaweza kujilinganisha na nani? Hata Beyonce haingiii, labda Alicia Keys ndiye anaweza kuifikia nusu yako.
AZIZA: Hahaha! Ibra una maneno matamu. Hebu nisubiri kidogo niende hapo dukani.
AZIZA: Unakwenda kununua nini? Hakuna pizza wala baga hapa Tandale.
AZIZA: Hahaha! Hebu acha utani.
Huyu Aziza. Aisee bora alivyoweka picha ya mdoli katika akaunti yake ya facebook manake kama angeweka picha yake basi ingekuwa balaa. Mwendo wake ulikuwa ni wa mapozi kupita kawaida, alionekana kutembea kwa tahadhali ardhini. Nilichokifanya nikayapeleka macho yangu kwa washikaji waliokuwa pale kijiweni, nilijua tu kwamba walikuwa na dukuduku mioyoni mwao.
JAFARI: Kaka heshima. Kaka heshima yako…kuanzia leo…hauna mpinzani hapa mtaani aiseeee…duh!
MIMI: Hahaha! Mtoto umemuonaje.
JAFARI: Kwanza huyu mtoto umemtoa wapi?
MIMI: Facebook.
JAFARI: Duh! Kaka naomba na mimi uniunganishe manake dah!
MIMI: Kaka mambo hayapo rahisi kama unavyofikiri. Mpaka nimempata huyu mtoto, nimepitia kwenye mabonde, mito majabari mpaka wewe kumuona hapa. Usifikiri ukijiunga leo kesho unampata, unaweza ukawa babu hujaambulia chochote.
ALLY: Kwani huyu ni wa facebook?
MIMI: Yeah! Tena yupo mpaka Twitter…yupo kotekote.
HUSSENI: Ila huyu mrembo sio mgeni machoni mwangu, nadhani nilishawahi kumuona sehemu.
MIMI: Acha uongo. Wapi?
ALLY: Daah! Nshajichanganya. Kumbe kichwani mwangu ilikuwa inakuja picha ya Kajool, yule mrembo muigizaji wa Kihindi.
MIMI: Hahaha!
JAFARI: Ila Ibra. Daah! Unapokuwa na mtoto kama huyu, hivi kweli unaweza kutembea nje ya ndoa?
MIMI: Kaka, sisi wanaume hatufai, hata upewe mrembo mzuri kama malaika, kesho unalala na rafiki yake…hahaha!
AZIZA: Ibra.
MIMI: Niambie (Huku nikimfuata)
AZIZA: Tuondoke.
MIMI: Bila ya kukanyaga nyumbani? Hebu acha zako, twende home.
AZIZA: Ibra…nataka tuwahi nyumbani.
MIMI: Hata kama. Twende mara moja tu.
Lengo kubwa la kumtaka Aziza twende nyumbani lilikuwa moja tu, kutaka kuwaonyeshea wale wasichana ambao walikuwa wakileta mapozi kwamba huyu msichana alikuja kwa ajili yangu kwani kama nisingefanya hivyo, wangejua kwamba alikuwa mpita njia ambaye alikuwa amesimama kutaka kuulizia kitu fulani. Kwa sababu alikuwa amelipaki gari pembeni, nikawaambia washikaji waliangalie na mimi kuanza kuondoka na Aziza kwenda nyumbani.
Watu walikuwa wakinitolea macho, wengine walikuwa wakiniangalia kisiri na kunipigia saluti. Aziza alionekana kukimbiza kupita kawaida, urembo wake ulikuwa ni mkubwa kiasi ambacho hakukuwa na mtu aliyefikiria kama ningeweza kuja na msichana mzuri kiasi kile.
AZIZA: Mazingira ya huku nimeyapenda.
MIMI: Umeyapendea nini?
AZIZA: Yametulia sana. Halafu kumechangamka.
MIMI: Hahaha! Nyie si mmezoea mazingira ya kwenu yapo kimya utafikiri jangwani.
AZIZA: Yeah! Unajua kule sijui kupo vipi, huwa kunaboa kweli.
Katika kipindi chote ambacho tulikuwa tukiongea huku tukielekea nyumbani, kichwa changu kilikuwa kikimfikiria baba. Nilijua kabisa kwamba katika kipindi hicho alikuwa nyumbani, kichwa changu kilikuwa kikifikiria uongo ambao nilitakiwa kumpa, uongo ambao ungeendana na ukweli. Nilipofikiria kwa kipindi fulani, nikapata jibu, nikapata kile nilichotakiwa kumwambia baba.
Kweli tukafika home, majirani wote wakawa wananiangalia kwa macho ya kunishangaa, Aziza, kwao alionekana kuwa tofauti sana, uzuri ambao alikuwa nao ulionekana kuwa wa kipekee sana. Nikaufungua mlango, tulipoingia ndani tu, kizaazaa, baba alikuwa kwenye kochi akiangalia televisheni.
Nikamkaribisha Aziza, akamsalimia baba na kutulia kochini. Nikamwangalia baba huku lengo langu likiwa ni kutaka kumsoma, hiyo ndio ilikuwa tabia ya nyumbani, muda mwingi watu huwa tunasomana kabla ya kuongea kitu chochote kile. Baba akaonekana kufahamu nilichokuwa nikikifikiria. Akaniwahi.
BABA: Unaonekana unataka kuniambia jambo, halafu hilo jambo la uongo, hebu niambie sasa nikusikilize.
MIMI: Hahaha! Tatizo mzee Akilimia una presha sana. Wewe subiri kwanza, mbona unakuwa na wasiwasi?
BABA: Huo mtazamo wako unaoutumia kunitazama. Ok! Karibu mgeni. Sijui unatumia kinywaji gani?
AZIZA: Hapana. Nimeshiba.
BABA: Kwani ukinywa kinywaji chochote utavimbiwa?
AZIZ: Hapana. Nimekwishakunywa.
BABA: Ibra, ni kweli anayoyasema?
MIMI: Hapana. Hapo kakupiga fix.
AZIZA: Hahaha!
BABA: Jisikie huru. Uletewe kinywaji gani?
AZIZA: Maji tu yanatosha.
MIMI: Ok! Ila kuna maji ya chumvi…utakunywa?
AZIZA: Mmmh! Maji ya chumvi?
MIMI: Sasa unashangaa nini? Au haujui kama Dar es Salaam kuna bahari ya Indi?
AZIZA: Niletee hata hayo nitakunywa tu.
Mtu mzima nikanyanyuka, kumbuka hapo bado sikuanza kumtambulisha Aziza kwa mzee kwamba alikuwa nani na alifuata nini nyumbani. Juu ya hilo, sikuwa na wasiwasi sana kwani kwa umri ambao nilikuwa nimefikia, mzee hakuwa muongeaji sana zaidi ya kunitaka kuwa makini kila siku kwa kila nikifanyacho. Nilipochukua maji, nikamletea, tena kwa makusudi, nikamletea kwenye kikombe cha plastiki, nilichokuwa nikikihitaji ni kumuonyeshea maisha fulani ya tofauti sana, maisha ambayo alikuwa akiyaamini kichwani mwake kwamba yalikuwa yakiishiwa na watu waliokuwa wakikaa Tandale uswahilini.
MIMI: Baba huyu ni rafiki yangu anaitwa Judith. Nilisomanae Faraja Seminari ila nilimuacha darasa moja. Kwa sasa yupo hapo I.F.M anasomea sheria.
BABA: Asante kwa kumfahamu. Karibu Judith na jisikie huru.
AZIZA: Asante.
MIMI: Judith, huyu ndio mzee Akilimia. Huyu ndiye ambaye nimemuibia hiki kipaji cha kuandikaandika.
AZIZA: Nashukuru kumfahamu.
Kwa sababu tulikuwa na safari, hatukutaka kukaa sana mahali hapo, tukasimama na kisha kuaga na kuondoka. Njiani, Aziza alionekana kushangaa sana, hakuamini kama nilikuwa na uhuru mkubwa wa kuongea na mzazi kwa kiasi kile.
AZIZA: Mbona baba yako unaongea nae namna ile?
MIMI: Kivipi?
AZIZA: Ulivyokuwa ukiongea. Yaani kama unaongea na vijana wenzako.
MIMI: Nisikilize Aziza, mzazi ni rafiki, hautakiwi kumuogopa sana mzazi mpaka kukosa uhuru, wazazi wetu hawakutulea katika mazingira hayo, walitulea katika mazingira ya kirafiki zaidi, mazingira ambayo yametufanya kuwa huru kwao.
AZIZA: Basi hongereni. Mzee wangu ukae chini na kuongea nae namna ile, mh! Mtu hujiamini. Kwanza akirudi tu, amani nakosa, muda wote utasikia Azizaaaa.
MIMI: Hahaha! Ila hao wazee ndio fresh. Mzee unakuwa bandidu kama hivyo, hakuna utani, hakuna masihala…hahaha!
AZIZA: Kuna uzuri gani? Baba akirudi unajificha chooni. Ngoja nikuulize swali.
MIMI: Uliza.
AZIZA: Kwa nini umemdanganya jina langu na kila kitu kuhusu mimi?
MIMI: Pale ningemwambia unaitwa Aziza, angeshtukia mchezo.
AZIZA: Kivipi?
MIMI: Unajua nimesoma seminari, sasa niliposema kwamba nimesoma na wewe, kidogo angetilia mashaka. Nilichokifanya ni kucheza na akili yake kabla ya yeye kucheza na akili yangu, nikamuwahi. Hahaha!
AZIZA: Ibra una visa sana.
Tuliendelea kwenda mtaa wa juu, tulipofika, watu wengine bado walikuwa wakishangaa, wala sikutaka kuwa na wasiwasi, kama kuuza tayari nilikuwa nimeuza sana, nilichokifanya ni kushukuru kwa niaba yake kwa washikaji waliokuwa wakililinda gari na kisha kuingia garini.
AZIZA: Sasa hapa safari ni kwenda nyumbani. Unatakiwa kuwa huru, baba yangu ni mkali sana ila kwa sasa hayupo. Jiamini, usiwe na wasiwasi. Umenisikia.
MIMI: Ooopsss…nimekuelewa. Sasa kama akirudi ghafla?
AZIZA: Usiwe na wasiwasi. Kila kitu kipo under control.
MIMI: Mmmh! Aya bhana japokuwa huwa ninahofia sana kwenda nyumbani kwa mwanamke.
AZIZA: Hahaha! Kwa nini unaogopa?
MIMI: Unaweza kugeuzwa mwanamke….hahaha
AZIZA: Usijali Ibra. Hakuna mtu anayeishi nyumbani ambaye ametokea Mombasa. Kuwa na amani.
MIMI: Aya (Nilisema na Aziza kuwasha gari na kuondoka mahali hapo huku nikiwa nimezoa maksi nyingi sana kwa kila aliyeniona na Aziza).
Ila pamoja na hayo yote yaliyokuwa yakiendelea, nadhani sikutakiwa kwenda kwa kina Aziza. Mungu ametufumba macho kutojua mambo yanayotokea mbele yetu, kama angetupa uwezo, nadhani nisinge kwenda kwa kina Aziza kwani hali ilikuwa ni balaa tofauti na uhakika ambao alikuwa amenipa…..chezea wazee wa kiarabu kwa mabinti zao
MIMI: Mmmh! Mbona mapigo ya moyo yananidunda hivi?
AZIZA: Hahaha! Uoga wako tu. Au una BP?
MIMI: Hapana. Yaani kama kuna jambo baya linakwenda kunitokea.
AZIZA: Jambo gani na wakati nimekwishakwambia kwamba baba hayupo, nipo peke yangu.
MIMI: Na mama je?
AZIZA: Nae hayupo. Yaani kurudi kwao mpaka saa mbili usiku.
MIMI: Hapo mwakemwake.
Kiukweli nilikuwa na wasiwasi sana ila Aziza alijitahidi sana kuniondoa wasiwasi. Ngoja nikwambie kitu kimoja, hakuna wazee ambao ninawaogopa kwa mabinti zao kama wazee wa Kiarabu. Huwa hawataki utani kabisa, huwa hawataki ulete masihala kwa mabinti zao hata mara moja.
Kukutoa roho kwa sababu umemfuata binti yake wala haoni tatizo hata mara moja. Kwa Aziza, akajitahidi sana kuniondoa wasiwasi lakini sikufichi rafiki yangu, hofu bado ilikuwa ikiendelea moyoni mwangu.
Nikaona haina noma, mzee wa Kiarabu angenitishaje mimi mtoto wa Tandale na wakati kama fujo nimekwishazizoea? Mzee wa Kiarabu angenitishaje mtoto wa Tandale na wakati kama ugomvi tushazoea ? Nilikuwa nikijipa moyo ila nilipofikiria kwamba wazee wa Kiarabu walikuwa wakitumia hata bunduki kukudedisha, nikaona mweeeee…kazi ipo.
AZIZA: Tumekwishafika nyumbani. Karibu.
MIMI: Asante.
ITAENDELEA
Aziza wa Facebook Sehemu ya Tano
Also, read other stories from SIMULIZI;