Aziza wa Facebook Sehemu ya Tano
CHOMBEZO

Ep 05: Aziza wa Facebook

SIMULIZI Aziza wa Facebook
Aziza wa Facebook Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA: NYEMO CHILONGANI

*********************************************************************************

Chombezo: Aziza wa Facebok

Sehemu ya Tano (5)

Mlinzi akafungua geti na kisha Aziza kuliingiza gari ndani. Nikabaki nikishangaa tu, sikuamini kama hapa Tanzania kulikuwa na watu ambao walikuwa wakiishi katika majumba makubwa kama ule mjengo aisee. Kulikuwa na bonge la bwawa la kuogelea, bustani kubwa ya maua pamoja na sehemu ya kuegesha magari. Mazingira ya nyumba yakanivutia sana, tukateremka na kisha kuanza kuangalia huku na kule, nilitaka kuyazoea mazingira japokuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kwangu.

AZIZA: Mbona unaangalia hivyo.

MIMI: Lazima niyazoee mazingira, naangalia vichochoro vya kufanyia uninja wangu mara mzee wako atakapotokea ghafla.

AZIZA: Acha hizo bwana. Mzee harudi sasa hivi, mpaka saa mbili usiku.

MIMI: Basi hakuna noma. Kuna nani mwingine ndani ya nyumba?

AZIZA: Mfanyakazi wa ndani. Wadogo zangu wote wapo shule nchini Kenya.

MIMI: Hakuna noma.

Tukaingia ndani na kisha kutulia. Macho yangu hayakutulia sehemu moja, yalikuwa yakiangalia huku na kule kama mtu ambaye nilikuwa natafuta jambo fulani. Sebule ilikuwa nzuri, ilivutia na kupendesha macho ya kila aliyekuwa akiiangalia. Nikakaribishwa katika mkochi mmoja mkubwaaaa, ile kukaa tu, nikayahisi makalio yakiingia ndani kabisa na kuzama kochini.

AZIZA: Hapa ndipo nyumbani. Karibu

MIMI: Asante

AZIZA: Nikuletee nini?

MIMI: Kwani kuna nini na nini?

AZIZA: Kuna juisi, soda, maziwa na maji.

MIMI: Kwa sababu nyumbani ni ngumu sana kunywa maziwa, hebu niletee maziwa.

AZIZA: Hahaha! Aya. Kuna kingine unachokitaka?

MIMI: Kama kuna vitafunio itakuwa full mzuka.

AZIZA: Unataka vitafunio gani?

MIMI:Kwani kuna nini na nini?

AZIZA: Kuna keki, mandazi, baga, pizza, chapati

MIMI: Duh! Utafikiri nimeingia hotelini. Fanya hivi. Kwa sababu sijawahi kula baga zaidi ya kuisikia kwa watu, hebu niletee hiyo na kwa sababu nasikia sikia watu wakitamba facebook sijui pizza tamu, nami niletee kwanza.

AZIZA: Utamaliza vyote Ibra?

MIMI: Kwani vikibaki si nitabeba! Au hairuhusiwi kubeba?

AZIZA: Inaruhusiwa.

MIMI: Basi niletee.

Usinishangae aiseee, hivi ndivyo nilivyo na nilikwishazoea kuishi maisha ya namna hiyo. Tandale hakukuwa na sehemu inayouza baga wala pizza, kwa hiyo kwa nini nisiagize baga na pizza nami nitoe ushamba mdomoni mwangu? Nikaletewa vitu nilivyovitaka, aiseee, kwanza nikajifanya kutokujua baga ipi pizza ipi, ikanibidi niulize.

MIMI: Pizza ipi na baga ipi?

AZIZA: Pizza hiyo ya duara na baga ni huo mkate wenye vitu mbalimbali.

MIMI: Mweee…kazi ipo. Nahisi leo nitaumwa sana tumbo.

AZIZA: Kwa nini?

MIMI: Tumbo langu halijazoea kula vitu hivi Aziza.

AZIZA: Usiogope, vitu vya kawaida tu.

Nikaanza kula buana, vilikuwa vitamu sana, tofauti na Aziza alivyofikiria kwamba ningebakisha, haikuwa hivyo, nikala vyote na kushushia na maziwa. Muda wote Aziza alikuwa akiniangalia, sijui alinionaje, sikutaka kujali, nilichokijali ni kupiga msosi tu.

Hayo ndio yalikuwa matukio ambayo niliyafanya mahali hapo, bado nilikuwa nikitaka kumuonyeshea Aziza kwamba mimi nilikuwa mtoto wa uswahili. Najua wale masharobaro wangeomba maji na pia kama wangeambiwa kuhusu chakula wangesema wameshiba, ila kwangu mimi mtu nisiyekuwa sharobaro, hahaha! Nikaagiza vitu ambavyo vilikuwa adimu kupatikana Tandale.

Nilichokuwa nikikifanya ni kucheza na akili ya Aziza tu, unajua unapoona umekuwa na msichana wa matawi ya juu halafu wewe unatoka uswahilini, usijifanye matawi sana na wakati kwenu ni wababaishaji tu. Nilitaka kumtia kipofu Aziza, nikajifanya sijawahi kula pizza na wakati mara nyingi nilikuwa nakwenda kuzinunua Magomeni karibu na msikiti wa Kichangani. Nikajifanya kwamba hata baga sijawahi kula na wakati nilikuwa nikipenda kuzinunua pale Kijitonyama katika sheli ya mafuta karibu kabisa na jengo la TTCL. Aziza akaniona kwamba kweli nilikuwa mtoto wa uswahilini

MIMI: Nashukuru kwa chakula chako na kinywaji chako. Nadhani sasa ni wakati.

AZIZA: Asante kwa kushukuru. Wakati gani?

MIMI: Wa kuniambia kile ambacho kila siku nilikuwa nikikihitaji sana kwako.

AZIZA: Kipi?

MIMI: Kuwa msichana wangu wa dhati.

AZIZA: Hahaha! Hausahau?

MIMI: Nitasahau vipi na wakati ninakupenda. Then ukiona nakumbuka basi jua kwamba wewe ni mtu muhimu sana kwangu. Kama usingekuwa muhimu, nisingekumbuka.

AZIZA: Hahaha! Nisikilize Ibra, najua kwamba unanipenda ila…

MIMI: Ila nini tena?

AZIZA: Nahofia.

MIMI: Unahofia nini?

AZIZA: Kuwa na wewe. Naweza kufa kwa presha.

MIMI: Haha! Hakuna kitu kama hicho. Nahitaji kuwa na wewe tu. Hebu fikiria muda wote ambao nimeupoteza kwa ajili yako Aziza, umekuwa rafiki yangu mkubwa, rafiki ambaye sikutaka kumpoteza katika maisha yangu yote.

AZIZA: Najua. Tuendelee kuwa marafiki.

MIMI: Nisikilize Aziza. Kila kitu kinakwenda na nyakati pamoja na mabadiliko. Najua kabisa kwamba kabla ya baba yako kumuoa mama yako walikuwa marafiki, si ndio?

AZIZA: Ndio.

MIMI: Baadae wakabadilika na kuwa wapenzi, si ndio?

AZIZA: Ndio.

MIMIl Na mwisho kabisa wakawa mke na mume. Nimekosea?

AZIZA: Haujakosea.

MIMI: Yeah! Hayo ndio maisha yalivyo. Tumekuwa marafiki kwa kipindi kirefu, inatupasa tubadilishe kila kitu kwa wakati huu, kutoka kwenye urafiki mpaka kuwa wapenzi, tukitoka hapo, itatupasa tubadilike pia, tuje kuwa wachumba na hatimae mke na mume.

AZIZA: Mmmh! Ibra una malego ya mbali.

MIMI: Yeah! Hayo ndio maisha yanavyotakiwa kuwa. Hatutakiwi kila siku tufikirie kuhusu hapa tulipo, yatupasa tufikirie kule tutakapokuwa kesho. Ukiona mtu anafikiria zaidi hapa, kidogo atakuwa na matatizo fulani kichwani.

AZIZA: Naomba nikuulize swali. Unanipenda?

MIMI: Nadhani macho yangu yanaelezea kila kitu. Siku zote mapenzi ya msichana huonekana katika tabasamu lake ila mapenzi ya mvulana huonekana machoni mwake. Unaona nini machoni mwangu?

AZIZA: Mapenzi.

MIMI: Yeah! Hicho ndicho kitu kilichomo moyoni mwako juu yako. Nakupenda sana.

AZIZA: Najua.

MIMI: Naomba kitu kimoja Aziza.

AZIZA: Kitu gani?

MIMI: Lipsi zako.

AZIZA: Zimefanyaje?

MIMI: Nataka kuona ni jinsi gani zilivyo laini.

MIMI: Unamaanisha nini?

MIMI: Haujajua namaanisha nini? Subiri.

Nikainuka pale nilipokuwa na kisha kumsogelea. Lengo langu kubwa mahali hapo lilikuwa ni moja tu, kubadilishana mate na kisha nione lipsi zake zilikuwa laini kiasi gani. Hakuonekana kuwa mchoyo, akanipokea, huku lipsi zetu zikiwa zinatamaniana tu, ghaflaaaaa….tukasikia honi ya gari getini. Kwa haraka sana Aziza akainuka na kisha kuchungulia dirishani, geti lilipofunguliwa, alikuwa baba yake.

AZIZA: Mungu wangu! Baba!

MIMI: Unasemaje?

AZIZA: Baba. Baba amerudi.

MIMI: Amerudi (Nikainuka na kwenda kuchungulia dirishani, gari aina ya Range la baba yake lilikuwa linaingia)

AZIZA: Mungu wangu! Sijui nifanye nini.

MIMI: Wewe si ulisema baba yako anarudi saa mbili usiku?

AZIZA: Ndio. Sijui leo imekuwaje.

MIMI: Mmmh! Hiki kifo (Nilijisemea moyoni huku nikitetemeka na haja ndogo ikitaka kunitoka)

Aziza alionekana kama kupigwa ganzi, hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya kwa wakati huo, nilimuona akianza kutetemeka huku kwa mbali kijasho chembamba kikianza kumtoka. Hakuonekana kuamini kile ambacho alikuwa akikiona mahali pale.

MIMI: Kwa hiyo?

AZIZA: Sijui nifanye nini.

MIMI: Chumba chako kipo wapi?

AZIZA: Njoo.

Nikaanza kumfuata kule aliponiambia nimfuate, chumbani. Nilijua fika kwamba katika kipindi hicho akili yake haikuwa sawa, mimi kama ninja nikatakiwa kufanya manuva. Tukaenda mpaka chumbani kwake, alikuwa akiendelea kutetemeka tu. Baada ya kufika chumbani, mtu mzima nikabaki nikikiangalia chumba kile, kilionekana kuwa na mvuto sana.

AZIZA: Kwa hiyo.

MIMI: Daah! Ngoja nizame chini ya kitanda (Sikutaka kuchelewa hata sekunde kumi, mtu mzima nikazama chini ya kitanda)

Huko chini kulionekana kusafi ajabu, kitanda kile kikubwa cha chuma kilikuwa na nafasi ya kutosha kabisa. Kitu cha kwanza nilichokifanya ni kuichukua simu yangu na kisha kuiweka katika silent. Nilibaki nikijiuliza sana kwamba kwa nini jambo kama lile lilikuwa likinitokea? Kwa nini Aziza alikuwa ameniaminisha sana mimi kwenda kwao mpaka kutaka kuniletea msala? Kila nilichojiuliza nikakosa jibu. Kule chini ya kitanda nikaanza kuchati na Eduado kupitia sms za kawaida.

EDUADO: Ibra umefikia wapi?

MIMI: Kaka acha. Nipo kwao.

EDUADO: Du! Upo kwao? Wewe noma. Ilikuwaje kuwaje hadi umefika kwao?

MIMI: Alikuja kunichukua home.

EDUADO: Sikupatii picha mtu mzima. Leo malovee hapo hapo chumbani kwake.

MIMI: Haha! Kaka acha, huku msala. Nipo uvunguni.

EDUADO: Uvunguni! Kivipi tena?

MIMI: Baba yake amefika na wakati dogo alisema kwamba anarudi saa mbili usiku. Karudi kwa kushtukiza, yaani hapa nimeingia chumbani kwake na kujificha uvunguni.

EDUADO: Hahaha! Kaka hiyo kweli noma, sikupatii picha aisee ulivyojipinda huko mtu mzima, kama dawa ya mbu.

MIMI: Kaka wewe acha tu, huku ni noma. Ukisikia nimepigwa risasi, usishangae.

EDUADO: Dah! Ngoja nikuombee Mungu akuokoe.

MIMI: Wewe unafikiri Mungu atanisaidia hapa?

EDUADO: Atakusaidia tu.

MIMI: Kunisaidia anaweza ila dah! Kaka mimi ni mwenye dhambi. Nafikiri atataka nikamatwe ili nisirudie mchezo wangu wa kusalandia watoto wa watu.

EDUADO: Kaka pole sana. Sasa mtoto anasemaje?

MIMI: Yaani hapa ni kujiokoa mwenyewe. Aziza anazingua, anaonekana kuogopa sana.

EDUADO: Kwa hiyo utatokaje humo uvunguni?

MIMI: Ngoja kwanza giza liingie manake huku mtu unaweza kufa.

Mtu mzima nilikuwa nazidi kutetemeka chini ya uvungu wa kitanda, Aziza hakuwa akitulia, mara aingie, mara atokea hali ambayo ikanionyeshea angetoa boko muda wowote ule. Nilichokifanya nikachukua simu yangu na kisha kuanza kumtumia meseji.

MIMI: Nini kinaendelea hapo?

AZIZA: Baba amekaa sebuleni, amekuja na wageni. Tena wageni ambao watalala hapa hapa nyumbani.

MIMI: Hilo sio tatizo sana. Wa kike au wa kiume?

AZIZA: Wa kike.

MIMI: Duuh! Ila si watalala chumba cha wageni?

AZIZA: Yeah! Ila wengine watalala katika chumba changu. Mbaya zaidi baba ameniambia nije kusogeza kitanda ili kiingizwe kitanda cha pili.

MIMI: Duuuh! Leo kazi ipo.

AZIZA: Mbaya kuliko zote amemwambia mdogo wangu aje kufagia chumbani.

MIMI: Wewe si ulisema wadogo zako wapo shule bording?

AZIZA: Nilikuwa nimekudanganya.

MIMI: Mungu wangu! Nimekwisha.

AZIZA: Naomba uniambie nifanye nini Ibra.

MIMI: Kwanza kabla ya yote punguza presha.

AZIZA: Sawa.

MIMI: Najua kwamba leo nakwenda kukamatwa, kabla sijakamatwa naomba uniambie kitu kimoja.

AZIZA: Kitu gani?

MIMI: Unanipenda?

AZIZA: Nakupenda Ibra.

MIMI: Upo tayari tuingie katika mahusiano kwa muda mchache uliobakia kabla sijauawa na baba yako?

AZIZA: Ibra usiseme hivyo.

MIMI: Wewe unafikiri nitasemaje? Naomba unijibu. Upo tayari?

AZIZA: Nipo tayari lakini jua hautokwenda kuuawa.

MIMI: Nimefanya kila kitu kwa ajili yako, nilihisi mambo haya yatatokea tu toka tulipokuwa tukija. Ila usijali. Ngoja nikuonyeshe jinsi mchezo unavyofanyika Aziza. Nataka nikuonyeshe kwamba huwa sikamatwi kijinga jinga.

AZIZA: Utafanya nini sasa?

MIMI: Cha kwanza hakikisha mdogo wako haji kusafisha chumba, akifika chumbani mpokonye fagio, ng’ang’ania kusafisha chumba chako.

AZIZA: Sawa. Cha pili?

MIMI: Hakikisha kila unapotoka chumbani, unafunga mlango kwa ufunguo, cha tatu, uache mlango wa jikoni wazi, cha nne mpe taarifa baba yako kwamba kuna mtu alikuja kumuulizia.

AZIZA: Mmmh! Huyo mtu nani?

MIMI: Ibra…ila leo niite jina la Ahmed.

AZIZA: Akisema yupo vipi?

MIMI: Mwambie kama jinsi nilivyo. Usitie shaka.

AZIZA: Kingine nisemeje?

MIMI: Mwambie kwamba ningekuja baadae kumuulizia tena.

AZIZA: Mhh!

MIMI: Usijali. Kila kitu kipo under control.

AZIZA: Sawa.

Baada ya dakika kadhaa, nikasikia mlango ukifunguliwa, nikasikia vishindo vikija kwa kasi, alikuwa mdogo wake ambaye alitaka kusafisha chumba kwa kukifagia, Aziza akafika na kisha kumpokonya ufagio kwa kutaka kufagia yeye mwenyewe. Mdogo wake alipoondoka, akakiinamisha kichwa na kisha kukutana nami.

MIMI: Vipi huko?

AZIZA: Bado hali ni ngumu.

MIMI: Daah! Sikamatwi kijinga hapa. Fanya kama nilivyokwambia, umesikia?

AZIZA: Sawa.

MIMI: Nakupenda mpenzi.

AZIZA: Nakupenda pia (Tukafanya kile tulichotaka kukifanya pale sebuleni….lol)

Aziza akaondoka, nikaona sio ishu, niliendelea kukaa uvunguni mule. Nazo dakika zilikuwa zikisogea tu, zilisogea zaidi na zaidi, mpaka saa moja usiku inaingia, mtu mzima nilikuwa mule mule ndani, chini ya uvungu. Saa mbili kasoro nikaona ungekuwa ujinga, nikamtumia Aziza meseji.

MIMI: Njoo uvunguni kwanza.

AZIZA: Sawa.

MIMI: Ila kabla ya kuja, cheki kuna nani jikoni.

AZIZA: Yupo mama.

MIMI: Vizuri sana

AZIZA: Vizuri?

MIMI: Yeah! Njoo kwanza huku uvunguni.

Baada ya muda, Aziza akafika, hakuonekana kuwa na amani.

AZIZA: Unasemaje baby?

MIMI: Hapa naondoka na kuelekea jikoni, cha msingi kamtoe mama yako jikoni.

AZIZA: Mmmh! Nitamtoa vipi?

MIMI: Kamwambie kwamba baba yako anamuita.

AZIZA: Eeeh!

MIMI: Fanya hivyo. Una dakika moja ya kufanya hivyo. Nakwenda na muda.

AZIZA: Halafu?

MIMI: Wewe kamwambie hivyo. Akija sebuleni mimi utanikuta nje ambapo huko sebuleni utamwambia baba yako kwamba kulikuwa na mtu alikuja kumuulizia. Umesikia

AZIZA: Na mama akifika sebuleni na kusema kwamba kaitwa kumbe hajaitwa?

MIMI: Mwambie uliskia vibaya.

AZIZA: Sawa. Umeifungua

MIMI: Kwenye ile dakika moja, umebakisha sekunde arobaini. Nenda, ukitoka zima taa ya humu chumbani na uuache mlango wazi kidogo

AZIZA: Sawa.

Aziza akaondoka mahali hapo, na kweli akaelekea jikoni na kumwambia mama yake kwamba alikuwa akiitwa na baba yake, nilipomuona mama yake akipita ukumbini kueleka sebuleni, nikaufungua mlango na kupita kuelekea jikoni kwa kasi huku nikihakikisha sisikiki, nikaufungua mlango na kutoka nje kwa nyuma, nikaanza kuambaa ambaa mpaka pembeni ya gari lao.

MAMA AZIZA: Nimekuja mume wangu.

BABA AZIZA: Kuna nini?

MAMA AZIZA: Aziza amekuja na kuniambia unaniita.

BABA AZIZA: Mimi! Hapana, labda kasikia vibaya.

AZIZA: Si nimesikia unamuita mama.

BABA AZIZA: Hapana.

AZIZA: Basi samahani nilisikia vibaya

MAMA AZIZA: Usijali. Nipo jikoni naandaa chakula kwa sababu dada wa kazi anaumwa, amelala na huyu Aziza asije akatoa chakula kibichi

BABA AZIZA: Sawa. Aziza, wapeleke chumbani wageni hawa.

AZIZA: Sawa. Ila leo kuna mtu alikuja kukuulizia.

BABA AZIZA: Nani?

AZIZA: Sijui, ila alisema atarudi usiku.

BABA AZIZA: Yupo vipi?

AZIZA: Mrefu kidogo, maji ya kunde halafu ana………!

MLANGO: Ngo ngo ngo ngo (Nilikuwa nikipiga hodi huku mlinzi akionekana kunishangaa kwani aliniona ninavyoingia na Aziza, alikuwa hajui sababu kwa nini nilikuwa nimetokea nyuma ya nyumba na kuanza kugonga mlango. Mlango ukafunguliwa, alikuwa Aziza, kama vile sterring, nikaingia ndani, Baba yake Aziza akabaki akiniangalia, sikufichi, nilijiamini kama Van Damme)

Baba yake Aziza alikuwa amenitolea macho pamoja na wageni wote ambao walikuwa sebuleni, mtu mzima sikutaka kuteteleka hata kidogo, nilionyesha uso wa kujiamini kupita kawaida. Kwa Aziza, kwa mbali alionekana kuwa na hofu kwani alidhani kwamba nisingekuwa na ujasiri wa kusimama na kuzungumza.

MIMI: Samahani mzee. Shikamoo.

BABA AZIZA: Marahaba.

MIMI: Nilikuja katika kipindi kilichopita lakini sikukuta.

BABA YAKE AZIZA: Sikuwepo. Sawa, umeshanikuta. Kuna nini?

MIMI: Niliagizwa na mzee Badour wa kule Msasani, ameniambia kwamba leo utatakiwa kufika katika kikao kile cha harusi kinachoendelea (Baba Aziza akaonekana kushtuka)

BABA AZIZA: Kikao gani?

MIMI: Kile cha mtoto wake, Farhia.

BABA AZIZA: Huyo mzee ndiye nani?

MIMI: Mfanyabiashara mwenzako.

BABA AZIZA: (Huku akionekana kushangaa zaidi) Alikutuma uje kwangu?

MIMI: Ndio (Nilijibu huku nikiwa serious)

BABA AZIZA: Una uhakika ni mimi?

MIMI: Ndio.

BABA AZIZA: Yeye alikwambia uende kwa nani?

MIMI: Kwako.

BABA AZIZA: Nani?

MIMI: Mzee Mahmoud.

BABA AZIZA: Hapana. Mimi sio mzee Mahmoud. Mimi ni mzee Mansour.

MIMI: Mmmh! Mbona unanichanganya? Hii si nyumba namba 315?

BABA AZIZA: Hapana. Hii ni nyumba namba 511. Nyumba kuanzia namba 300 zipo kule mbele.

MIMI: Ok! Basi samahani kwa usumbufu mzee wangu. Nikosea namba, ila nilipomuuliza mlinzi alijibu hapa ni kwa mzee Mansour ila jina likanichanganya, si unajua sisi wengine majina ya kiarabu hatuyajui vizuri.

BABA AZIZA: Usijali kijana. Najua vijana wa sasa hivi mnakuwa na mambo mengi vichwani. Sawa. Nenda.

MIMI: Usijali (Nikageuka na kisha kuufungua mlango huku Aziza akibaki kutetemeka tu)

MLINZI: Ebwanaa vipi tena, mbona sikuelewielewi?

MIMI: Hakuna tatizo. Nilikuwa nataka kuonana na mzee Mansour tu, kuna uninja nilikuwa nakamilisha mara moja.

MLINZI: Uninja gani?

MIMI: Wa kucheza na akili za watu

MLINZI: Kivipi?

MIMI: Usijali, hili liko nje ya uwezo wako, ukitaka kulifahamu, utachanganyikiwa.

MLINZI: Mmmh! Sawa! Karibu.

MIMI: Asante.

Nikashusha pumzi ndefu, sikuamini kama niliweza kutoka katika mikono ya mzee yule aliyeonekana kuwa na hasira kupita kawaida. Nilitembea kwa mwendo wa haraka haraka mpaka kituoni ambapo nikapanda gari na kisha kuelekea nyumbani. Garini, mawazo yangu yalikuwa juu ya ule msala ambao nilikuwa nimenusurika, ulikuwa msala mkubwa ambao ungeweza kunitoa roho kama ningeleta ishu za Kisharobaro kama Eduado. Nilipofika nyumbani, nikaanza kuchati na Aziza.

AZIZA: Hakuna kama wewe. Umeshindikana mpenzi. Wewe ni genius.

MIMI: Hahaha! Tena ana bahati leo sikutaka kuleta usanii mkubwa zaidi.

AZIZA: Mmh! Kwani ungeweza kuleta zaidi ya ule?

MIMI: Yeah! Yaani mngenibeba pale.

AZIZAl: Hahaha! Hapana chezea wewe mtoto wa Tandale, umeshindikana aisee.

MIMI: Hahaha! Usijali. Kokote kunapokuwa na ishu zinazohitaji mafunzo ya kininja wewe niite tu, usiogope. Hata ukitaka kuingia Ikulu, wewe niite tu na kila kitu kitakuwa poa.

AZIZA: Mmmh! Unajiamini wewe.

MIMI: Acha masihala na mimi.

AZIZA: Ok! Leo sichati sana ila ningependa kuonana na wewe kesho.

MIMI: Wapi?

AZIZA: Popote upendapo.

MIMI: Poa. Tuonane gesti.

AZIZA: Hahaha! Acha masihala.

MIMI: Ndio maana nimekwambia sema wapi. Yaani ni sawa na kuja Tandale halafu nikuulize unakunywa kinywaji gani, je ukisema unataka maziwa, nitayatoa wapi? Ukija huku sikuulizi unakunywa kinywaji gani, nakuuliza unakunywa soda gani.

AZIZA: Hahah! Wewe mtoto wewe. Najivunia kuwa na mtu kama wewe.

MIMI: Usijali. Kuwa serious, tuonane wapi?

AZIZA: Njoo chuo.

MIMI: Saa ngapi?

AZIZA: Muda wowote ule.

MIMI: Poa. Nitakuja saa nne usiku.

AZIZA: Nini?

MIMI: Hebu kuwa serious, nije saa ngapi?

AZIZA: Njoo saa tisa. Unalijua lile jengo la Biashara la UDBS?

MIMI: Yeah! Si pale karibu na kituo cha polisi, opposite na mini-super market?

AZIZA: Yeah!

MIMI: Poa nitakuja.

AZIZA: Usichelewe, kuna bonge la sapraizi nataka kukuonyeshea.

MIMI: Mmmh! Lipi hilo?

AZIZA: Nikikwambia haitokuwa sapraizi. Wewe njoo tu.

MIMI: Poa.

Kuanzia kipindi hicho sikuonekana kuwa na furaha tena, muda wote nilikuwa nafikiria kuhusiana na sapraizi hiyo ambayo Aziza alikuwa ameniahidi. Sikufichi rafiki yangu, usiku ulikuwa mrefu kwangu. Sikutaka kuchati na Aziza, nililala moja kwa moja mkpaka kesho ambapo nikaamka. Kutokana na ubize wa hapa na pale, nikaenda chuo saa tisa na kisha kumuita aje nje ya jengo lile la UDBS, haukuchukua muda, akatoka huku akiwa na Eduado, wote walikuwa wakicheka jambo lililonichanganya.

AZIZA: Karibu mpenzi.

MIMI: Asante. Mbona mnacheka hivyo mtafikiri mnamwangalia Mr Bean?

EDUADO: Ungekufa. Watoto wa Waarabu si wa kwenda kuwavaminia kwao. Matokeo yake ukajificha uvunguni, sikupatii picha, ulijikunja kama dawa ya mbu.

MIMI: Hahaha! Aisee ni noma. Kweli nimeamini mtu akifumaniwa, acha awe mdogo kama panadol.

AZIZA: Kwanza twendeni tukapate lunch, au Ibra umeshiba?

MIMI: Nimekula home ila sijashiba wala nini. Wazo ulilolitoa liko poa. Msosi wapi?

AZIZA: Kule bondeni.

MIMI: Wanapakua kingi au nao wababaishaji.

AZIZA: Kikiwa kidogo utaongeza.

MIMI: Namna hiyo, hayo ndio maneno. Ila hapa nina 400 ya nauli tu.

AZIZA: Usijali. Nitakurudisha na gari.

MIMI: Hapo mzuka zaidi. Itakubidi uniongezee shilingi mia ninunue vocha ya 500 ili niingie facebook baadae.

AZIZA: Usijali. Nitakutumia elfu kumi kabisa.

MIMI: Duh! Sasa simu yangu si itazima

AZIZA: Kwa nini?

MIMI: Haijazoea kuingiza kiasi kikubwa cha hivyo. Sawa na mgonjwa wa Tandale ukampelekea juisi ya shilingi elfu kumi. Anaweza kufa.

AZIZA: Hahaha! Kwa nini?

MIMI: Tumbo limeingiza kitu kigeni kwa hiyo inaweza kuonekana kama asidi.

AZIZA/EDUADO: Hahaha.

MIMI: Huo ndio ukweli. Ila nina swali.

AZIZA: Swali lipi?

MIMI: Nahisi kama mnanificha. Kuna ishu inayoendelea hapa?

AZIZA: Muulize Eduado.

MIMI: Eti kaka kuna nini?

EDUADO: Aziza anakupenda. Alikuwa akikuhitaji toka zamani ila alikuwa akiogopa kukwambia, akaniambia nifanye juu chini mpaka anakupata.

MIMI: Unasemaje?

EDUADO: Ndio hivyo. Anapenda kusoma kila unachokiandika facebook, amekuwa rafiki yako mkubwa, akavutiwa na wewe ila alikuwa akikuhitaji, alichokifanya, akakuunfriend na kisha kujifanya mtu mpya kwako.

MIMI: Aiseee…duh! kwa hiyo kila kilichokuwa kikiendelea kilikuwa kikijulikana?

EDUADO: Yeah! Huo ndio ukweli.

MIMI: Sasa na wewe Aziza ulikuwa unaogopa nini kuniambia?

AZIZA: Maadili.

MIMI: Kivipi?

AZIZA: Msichana hatakiwi kumuanza mvulana.

MIMI: Hahaha! Ningekuwa na girl mwingine je?

AZIZA: Ningepigana mpaka nikupate.

MIMI: Hahaha! Aya buana. Mchezo wenu umefanikiwa na wote mmeshinda. Hebu kwanza ongezeni mwendo washikaji, unajua hapa nina ubao ile mbaya mpaka tumbo linasikia kizunguzungu.

AZIZA: Mmmh! Kwani tunatembea taratibu?

MIMI: Mnatembea kama mnamsindikiza Bibi Harusi.

Hicho ndicho kitu ambacho nilitaka kukwambia kila siku katika maisha yangu. Aziza ndiye alikuwa msichna wangu, nilimpenda na kumthamini sana. Japokuwa alikuwa msichana mwenye uwezo lakini kila alipokuwa pamoja nami alikuwa akionyesha heshima ya hali ya juu japokuwa nilikuwa nikiishi Tandale. Aziza alinipenda, nilimpenda pia, tulifanya mengi sana hasa yale ambayo wapenzi huyafanya faragha. Mpaka leo hii, bado ninampenda mtoto huyu ila cha ajabu….hahaha! hata kwao sitamani kukanyaga.

MWISHO.

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment