Taaluma Iliyopotea Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA: FRANK MUSHI
*********************************************************************************
Simulizi: Taaluma Iliyopotea
Sehemu ya Tatu (3)
“Frank pesa zinatafutwa na zinapatikana. Historia ya baba yangu ni ndefu lakini kiufupi alikuwa ni mtoto wa masikini sana, alisoma kwa shida sana na alikuwa kwa shida, lakini alipofika kidato cha sita alijiunga na jeshi, akachaguliwa kwenda Cuba kusomea ukomandoo, ila karibu na kumaliza mafunzo akapigana wakamfukuza ndo akarudishwa Tanzania, baadaye alipelekwa tena kusoma shahada ya Military science huko Izrael, na aliporudi alipandishwa cheo, alikuwa ni mchapakazi sana wakateuliwa watu wa kwenda kusoma na yeye akawepo tena, akaenda kusoma shahada ya pili ya Sheria za kivita na uhusiano wa kimataifa, ndipo alipokuja akafanya kazi tena mpaka kufikia cheo cha Brigedia na ndipo alipoamua kuachana na mambo ya jeshi na akapewa tenda ya kusambaza silaha za kijeshi na vyakula kwenye makambi ya jeshi, baadaye alikuwa tajiri na kufungua hotel Malawi na Afrika ya kusini pia alikuwa na Ukumbi mkubwa wa mikutano katikati ya jiji la Nairob, kwahiyo kila mtu anaweza kuwa mtu Fulani kama ataamua, baba yangu alitoka kuanzia chini na mpaka sasa amefikia kuwa balozi baada ya kutoka kwenye uwaziri, japo najua baba yangu hataki niijue shida lakini kwako Frank mimi ni tajiri sana, tutasaidiana mpaka tutafikia pale tunapopataka sisi, tuna nia, uwezo na nguvu za kufanya kazi kwa bidii,,cha msingi tujifunze nidhamu ya fedha na tutazame tunapotaka kufika, kisha tuandae minguu na nyonga zetu” hayo ni maneno ya kunifariji aliyowahi kuniambia Natasha enzi za uhai wa penzi letu wakati bado tukiwa Zanzibar.
“lakini pamoja na hayo bado safari ni ndefu sana kufikia pale tunapopataka, tunachangamoto nyingi sana za kimaisha ambazo lazima tuzikabili” nilimwambia siku hiyo kwasauti iliyojaa matumaini na woga wa maisha.
“Ujue Frank, maisha ni kama mpira uliowekwa katikati ya uwanja mkubwa,,sisi binadamu ndio wachezaji wa mpira huu, na kwenye maisha hakuna mpira wa kugombaniana ila ni penalt tu, unapiga ya kwako ukikosa ndo basi tena, hivyo kila binadamu hupiga mpira akiwa na lengo la kufunga ila kuna ambao waliufikisha mpira karibu na goli ila haukuingia golini, hawa ni wale ambao waliyakaribia mafanikio ila hawakuwa wamejipanga wakashindwa kufika, wapo waliopiga mpira ukatoka nje, hawa ndio wale ambao maisha yako hayana kesho imara, ila wapo waliopiga wakafunga mpaka nyavu zikachanika, hawa walifanikiwa sana. Katika kuupiga huu mpira Frank ni lazima tukusanye pumzi kwa pamoja, tushikamane kama wapenzi, tulindane, tuhakikishe miguu yetu ni imara, tuangalie umbali wa goli na tupange tutapiga kwa kasi gani ili tufunge na zaidi tumuombe mungu na ninahakika tutakuwa na familia yenye mafanikio mpenzi wangu” nilimtazama mara mbilimbili siku aliponiambia maneno haya na nilimuambia mungu asante kwa kunipa mwanamke kichwa.
Tayari nilifanikiwa kuingia jijini Dar na nilipanga chumba maeneo ya Mbagala na tayari nilianza maisha mapya, haikuwa rahisi sana kusahau yaliyonitokea lakini kwasasa nilikuwa nafikiria ni nini cha kufanya. Kwa pesa kidogo niliyokuwa nayo nilianzisha biashara ya kuuza maji na nilifanikiwa kutengeneza mkokoteni wangu kwaajili ya kazi hiyo, nilikuwa nikiuza maji kwa shilingi mia 5 kwa dumu na niliridhika na kazi hiyo, huku sasa nilijulikana kwa jina la Athuman, sikutaka tena mtu yeyote afahamu jina langu halisi.
Niliendelea na biashara hiyo na ndani ya wiki tatu nilifanikiwa kupata fedha za kuanzisha kitu kingine na ule mkokoteni nilimkabidhi kijana mwingine kwa masharti kuwa awe analeta shilingi elf 3 kwa siku. Kiherehere cha kumsaidia mtu jambo lolote hata kama nalifahamu kiliniishia na sasa niliishi kama mtu wa hovyo tu.
Nilianza biashara ya kuuza maji ya chupa kwenye barabara ndani ya jiji la Dar na maji yalikuwa yanatoka kweli, nilikuwa nikitembeza kwenye foleni za tabata na ubungo na muda mwingine nilifika hata katikati kabisa ya jiji na maeneo mengine, nilifanya kazi hiyo kwa kipindi kirefu cha mwezi mzima na sikunyoa zile ndefu ndefu zilizoning’inia kiduvuni mwangu, sikutaka kutafuta kazi kwa yeyote yule.
Ilikuwa Alhamis tulivu nikiwa katika bar ya Songambele baada ya mizunguko ya kutwa nzima ndipo nilipopata mshtuko kuona mtu niliyemfahamu akiwa kwenye Tv, alikuwa ni Natasha katika kipindi cha UCHAGUZI NA CHANGAMOTO kilichokuwa kikirushwa na TTV. Alikuwa akiongelea changamoto za kampeni za urais yeye akiwa kama mkurugenzi wa kampeni za baba yake, alikuwa ni mjamzito kitu ambacho kilinichosha kabisa, alikuwa amebadilika na amezidi kuwa mzuri.
“Natasha” nilijikuta nikishangaa na kutaja jina lake.
“vipi unamfahamu nini” aliniuliza mzee aliyekuwa ameketi karibu na mimi.
“Hapana, namfananisha na mtu Fulani niliyewahi kumjua kabla” nilijibu kwa hali ya kumkana kwa kuwa hata kama ningemueleza yule mzee kuwa nilimfahamu angeona najisifia.
“Huyu msichana ni mchapakazi bhana, hakuna mfano, na inasemekana kama ikitokea baba yake akishinda uchaguzi tena yeye anaweza kuteuliwa kuwa waziri” aliongea yule mzee na kuendelea kumsifia.
“Kwani kwasasa yeye ni nani” niliuliza katika namna ya kidadisi.
“kwasasa yeye ni mkurugenzi wa uchaguzi, ila kabla ya hapo yeye ndo alikuwa katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nje baada tu ya baba yake kushika urais, yani kasaidia kweli, alipofika pale wizarani akabadilisha mambo na wale walioingia pale kimagumashi akafukuza wote” aliongea yule mzee huku akionekana kufurahishwa sana na kazi ya Natasha.
“inaonekana ni mchapakazi kweli mzee” niliongea huku nikimuunga mkono yule mzee kwa yale maneno yake ila moyoni nilikuwa nikiwaza ile mimba ni ya nani.
“alipitia magumu sana huyu binti ila mungu kamjalia sasa hivi ametulia” aliongezea yule mzee na mimi nilimgeukia ili kutaka kujua ni magumu gani hayo.
“magumu gani mzee” nilimuuliza.
“huyu binti alikuwa na mchumba wake, muhuni Fulani tu hivi, huyu msichana alikuwa anampenda sana huyo kijana lakini kumbe kale kajamaa ni kahuni tu kakataka kumuua, ili tapakaa sana iyo story mwaka ule baba yake akiwa anagombea urais, kuna hiki chama hiki, hiki sijui wanakiitaje ndo inasemekana walikuwa wanamtumia yule jamaa, sasa kesi ilipoenda mahakamani yule jamaa akaachiwa, taharuki ikatanda ikasemekana kuwa wale wa kile chama ndo walienda kuhonga aachiwe japo wao walikana kumjua huyo mtu, mungu mkubwa msichana wawatu akavumilia, baadaye bhana yule msichana nasikia baba yake akamtafutia mtu wa kumuoa, ndo unaona sasa hivi anakatoto kake tumboni” huyu mzee niliona kama katumwa vile lakini aliyoyaongea yalianza kunipa taarifa ya mambo yalivyokuwa wakati sipo Tanzania.
“kwahiyo huyo mtu wake mwingine yuko wapi sasa hivi na huyo aliyemuoa ni nani?” nilimuuliza yule mzee na kumuagizia kiroba kingine.
“yule jamaa alishafariki nasikia aliumwaga akafa,, sasa hivi kaolewa na huyu kijana mmiliki wa hii Kampuni ya Afrika kusini inayofanya kazi hata hapa nchini, (akiwa anajaribu kukumbuka), huifahamu hii Kampuni ya Usafirishaji hii, inaitwa 2N Transport Ltd, jamaa flani anaitwa Nicholas ni mtoto wa rais aliyepita huyu mzee, ni tajiri kweli kweli huyo jamaa,,wamefunga ndoa mwaka juzi hapa dar ilikuwa hapakaliki, kila gazeti liliandika nakwambia, yani siku hiyo ingetokea mtu alipue huo ukumbi aisee watu wakubwa sana wangekufa, nakwambia kulikuwa na watu toka nchi mbalimbali na baadhi ya marais wa nje walikuja, sasa naskia baada ya kampeni hii ya baba yake ameamua kutoka kule wizani na kuja kumsaidia baba yake kuratibu shughuli zake” maneno yale yaliuchoma na kuuzunisha moyo wangu sana, lakini nilijua hata iweje bado Natasha alikuwa akinipenda, na hata kama ikitokea leo hii akaujua ukweli basi angemwacha alieyenae na kunifuata. Nilimuacha yule mzee pale na tayari nilishika njia ya kuelekea kwangu.
MWEZI MMOJA MBELE
“….katika taarifa hiyo aliyoitoa kwenye vyombo vya mawasiliano, kurugenzi ya mawasiliano ikulu imesema kuwa rais ameamua kutangaza baraza lake hilo la mawaziri ili kuanza rasmi kufanya kazi zake ikiwa ni safari yake ya mwisho ya kuleta mabadiliko aliyoahidi, taarifa hiyo pia imetaja baraza lililo na mfanano ule wazamani lakini hivi sasa likiwa na sura mpya ya mtoto wa rais ambaye aliteuliwa jana kuwa mbunge wa kuchaguliwa na rais na kupewa uwaziri wa Wanawake jinsia na watoto. Taarifa ya ndani ya ikulu inasema rais amefikia uamuzi wa kumteua Natasha Nicholas ambaye aliwahi kuwa Katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nje kwakuwa utendaji wake katika wizara ya mambo ya nje haukuwa na shaka na ni dhahiri kuwa alikuwa ni mtu makini, Natasha ambaye atakuwa ni waziri wa kwanza mdogo kuliko wote aliwahi pia kuwa mfanyakazi wa wizara ya mambo ya nje kabla ya kuhamia wizara ya mambo ya ndani na baadaye aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nje, hata hivyo duru za kisiasa na wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema kuwa hatua ya kumchagua mtoto wake katika nafasi hiyo isipimwe kwa mahusiano ya kifamilia ya wawili hao ila kwa utendaji kazi wa mteuliwa….”
Hiyo ilikuwa habari iliyonishtua toka usingizini.
“naota au?” nilijiuliza moyoni lakini sikuwa naota wala nini ilikuwa ni kweli, nilikaa pale chini nikiwaza mambo mengi lakini nilijua kabisa kilichokuwa kikinisumbua si kitu kingine bali ni jina Natasha Nicholas badala ya Natasha Rweikaza.
“Natasha ni mke wa mtu na ni mtu mkubwa sana Tanzania kwaiyo achana nae Frank” nilijisemea moyoni na machozi yalianza kunitoka, Natasha kwangu alikuwa si waziri, alikuwa ni mpenzi wangu niliyenyang’anywa kwa hila, nilifahamu kuwa angekuwa ananichukia lakini niliamini siku moja atakuja kuufahamu ukweli ingawaje kwasasa kulikuwa na wingu kubwa katikati yetu, sikuwa mtu yeyote kwake na ninafahamu hakuwa kuniwaza pengine toka azaliwe.
Nilichukua maji kwa mangi sikuiyo na kuanza kutembeza kwenye foleni ya buguruni na kwenye mida ya saa 7 mzigo uliniishia hivyo nililazimika kwenda mpaka ubungo ili nikafunge mzigo mkubwa zaidi. Baada ya kujiweka sawa sasa nilirudi tena barabarani huku nikipita katikati ya magari yaliyokuwa yamepanga foleni pale ubungo mataa, nilifanikiwa kuuza chupa mbili na kwa mbali nilisikia mtu akiita muuza magazeti, niliipenda sauti ile na nilipogeuka nilikutana na VX V8 nyeusi iliyokuwa hatua mbili toka pale nilipokuwa, ilikuwa ni gari ya mbele kabisa, nilitamani sana kumuona aliyekuwa anaiita japo mimi sikuwa nauza magazeti, niliposogea kidogo nilidondosha fedha zangu na kuinama ili kuokota ndipo niliposhtushwa na sauti ile tena:
“Frank” ilikuwa sauti ya kike iliyotoka kwenye yale magari yaliyokuwa kwenye foleni, niligeuka na nikaisikia tena sasa nilipopeleka macho yangu mbele nilikutana uso kwa uso na Natasha, hakuwa na lile tumbo kubwa nililoliona kwenye TV siku ile na pembeni kwa mbali niliona mtoto mchanga akiwa amewekwa pembeni, nilimtazama na yeye alinitazama kisha niliona kama sura yake ilianza kubadilika na hasira zilianza kumshika, nilitupa maji chini na hapo foleni ilikuwa imesharuhusu, nilichomoka mbio lakini watu walidhani nimemuibia, walianza kunikimbiza na wakati huo magari yalisharuhusiwa, nilifika mbele nikakutana na jamaa mmoja aliyenipiga teke na kunifanya nianguke chini, kilichofata kilikuwa kichapo kikali sana lakini nilikuja kuokolewa na mgambo wa jiji baada ya kuwa nimeshachakaa kwa kipigo, nilichukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi ambapo niliandikishwa maelezo na kupewa PF3 (Police form no. 3) nikapelekwa hospitali, nilichoshukuru ni kwamba polisi walinielewa kuwa sikuiba lakini mgambo mmoja alisema alimtaja dada ninayesemekana kuwa nimemuibia kuwa ni waziri mteule, polisi walipiga simu kadhaa na niliachiliwa baada ya matibabu kwa sharti la kwamba niripot kesho pale kituo cha polisi, nilikubali lakini niliona kujipeleka pale ndio ulikuwa mwanzo wa kifo changu, baada ya kutoka hospiali nilijikongoja kuelekea nyumbani huku nikiwa nimevunjika mkono mmoja na majeraha mengine kichwani na miguuni, lakini nilikuwa na nguvu ya kutembea. Nilifahamu kabisa Natasha angeweza hata kufikiria kuwa nilitaka tena kumuua ndo mana labda nilienda kumvizia pale,,nilifahamu kuwa huo ndio ulikuwa mwanzo wa mauti yangu. Kesho yake sikwenda polisi na kesho kutwa yake asubuhi saa 12:00 alikuja yule jamaa wa mkokoteni na kunionyesha gazeti lililokuwa na picha yangu kuwa nilikuwa nikitafutwa na jeshi la polisi. Nilitoka pale nyumbani nikavaa vizuri, ndevu nilikuwa nimenyoa na sasa nilionekana kama binadamu, nilichukua paspot yangu ya kusafiri na pesa kiasi cha laki 3 nilichokuwa nimebakiwa nacho kisha nilipanda daladala mpaka ubungo na kufanikiwa kuikuta Chakito Long way bus iliyokuwa inakwenda monduli, nililipa shilingi elfu 18 na nilipatiwa siti ya nyuma kabisa.
Safari ya kuelekea Monduli ilianza na kila mara kwenye basi nilikuwa nawaza tu nini kitanitokea, kwakasi ya lile basi saa 10 jioni nilikuwa tayari nimefika maeneo ya kisongo katika wilaya ya monduli na hapo nilishuka na kununua bushori nilivaa na kukaa pale nikisubiri gari lakini sikuona, saa kumi na moja jioni nilipata gari ndogo ya IT iliyokuwa ikielekea Nairob Kenya na walikubali kunichukua kwa shilingi elfu 25,,,Saa 7 Usiku nilikuwa jijini Nairob na pale boda nilifanikiwa kupita bila matatizo.
“Ili ufanikiwe lazima ujue wewe ni nani, ni wa aina gani na hadhi ipi, lazima ujiamini na utafute kitu cha kukutofautisha na mwingine (sense of uniqueness), lazima ufahamu unachotaka lakini zaidi unachostahili. Unaweza kutaka kumi kumbe wewe ni wa mbili, hii haimaanishi kuwa wewe huwezi kupata kumi uitakayo bali inamaanisha juhudi zako hazijafikia kumi hivyo ukijitahidi utapata,,kila mtu amezaliwa masikini kwakuwa wote tulizaliwa uchi lakini kila mtu alizaliwa tajiri pale alipoanza kuvuta pumzi. Usikubali mtu akusaidie kufikiri, amua leo kwani wewe ni KIRANJA WA AKILI YAKO MWENYEWE, WEWE NI BUNGE,SERIKALI NA MAHAKAMA YA AKILI YAKO, utajitungia sheria na mipango ikiwa ni pamoja na bajeti yako, utatekeleza sheria zako na mipango yako na kujiletea kipato na ukikosea utajihakiki mwenyewe na kujirekebisha, FIKIRIA KWA KADRI UPENDAVYO KUFANIKIWA” ,,HII NI SEHEMU YA SABA,,,ANDIKA HIVI…
BEATRICE ANASIMULIA
Nilisafiri salama na kutua uwanja wa ndege wa kimataifa wa JK Nyerere jijini Dar es Salaam, nilipokuwa kwenye ndege nilikuwa nikisali mda wote ili mungu aniongoze kwani sikuwahi kufika Tanzania na hiyo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza, lakini pia ilikuwa mara yangu ya kwanza kabisa kwenda sehemu nisiyoijua kumtafuta mtu nisiyejua nitampata wapi, lakini nilikuwa nina uhakika wa kumpata kwa uweza wa mungu, nilipotua uwanjani pale nilipokelewa na msichana mmoja mrembo sana aliyejitambulisha kwangu kama Brenda na ndiye niliyeelekezwa kuwa atakuwa mwenyeji wangu nchini Tanzania. Baada ya kufika na kufanya taratibu zote nilimpigia simu baba na alinitumia kiasi Fulani cha pesa, tulitoka na Bredha na kwenda kuzichukua kwenye tawi la Western Union na kuzibadili kwa fedha za kitanzania nilipatiwa shilingi milioni 15 na kuziamishia kwenye akaunti yangu na kwakuwa nilikuwa na ‘master card’ haikunisumbua kutoa fedha pale nilipopahitaji. Eneo alilokuwa akikaa Brenda ni Masaki, sehemu ambayo niliisoma kama sehemu iliyotulia sana na waliishi watu ambao walionekana mida ya asubuhi wakitoka na magari yao kuelekea makazini na jioni wakirudi. Sikuwa nimemweleza Brenda ukweli wa kila jambo zaidi ya kumwambia kuwa nilikuja kumtafuta rafiki yangu, nilimtajia maeneo miwili ambayo Frank aliyaandika kwenye kitabu chake na yeye aliniambia alikuwa akiyafahamu na mimi nilipanga vitu vyangu sawia nikakaa chumbani usiku kucha nikipanga kwa makini na kusoma kile kitabu alichoandika Frank, nilijiona mwenye bahati kwakuwa Brenda alikuwa yukpo likizo ya miezi mitatu hivyo niliamini kuwa angekuwa msaada mkubwa sana kwangu ingawaje nilijua nitamchosha lakini sikujali kwa hilo.
Asubuhi na mapema siku moja mbele niliamka na kujitayarisha vizuri, nilipotoka chumbani nilikuta Brenda ameshajitayarisha na mfanyakazi wake wa ndani alitutengea chai tukanywa na kisha tuliondoka, Brenda ndiye alikuwa dereva na tulipofika sheli alitoa fedha ili aweke mafuta lakini nilimzuia na kuagiza yule kijana ajaze ‘full tank’ na baada ya hapo tulikamata njia kuelekea alikosema yeye kuwa ndio Tandale, tulipofika lile eneo tuliegesha gari sehemu na kuanza kutembea kwa mguu kidogo kuelekea huko ambako Frank alikuwa amepaandika kwenye kitabu chake, lakini nilipofika pale nilikutana na dada mmoja aliyeniambia kuwa Frank hajawahi kuonekana hapo;
“(akiongea kwa lugha ya Kiswahili na mimi nikitafsiriwa na Brenda) huyu mtu hajawahi kuonekana huku toka kipindi alipohama” alinieleza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“hey, usiwe na wasiwasi sisi ni marafiki zake tuna mtafuta ndo mana tumekuja hapa” Brenda alimwambia na yule dada alionekana kuonyesha sura ya kukubaliana na alichoambiwa;
“nani unahisi anaweza kutusaidia kujua alipo?” nilimuuliza yule dada na Brenda alimtafsiria.
“kuna jamaa anaitwa Juma ni fundi radio pale barabarani ndo alikuwaga rafiki yake kipindi yupo huku” alijibu akionyesha kidole kuelekea kwa fundi aliyekuwa mita hamsini toka pale tulipo.
“asante sana dada na mungu akubariki” nilimshukuru na kumkabidhi noti ya shilling elfu 10 kama zawadi kwakunisaidia, kisha tuliondoka na kwenda kwa yule fundi tulipofika pale Brenda aliongea nae kwa muda wa dakika kumi na ilionekana kama vile walikuwa hawaelewani, nilimuuliza Brenda na kuniambia kuwa yule fundi anaonekana anajua kitu lakini hataki kusema, nilianza kuongea nae mimi huku akitafsiriwa na Brenda ila hakusema chochote zaidi ya kusema kuwa hafahamu chochote, nilimuambia Brenda tumuache na nilimpatia noti ya shilingi elfu 5 na namba yangu ya simu ili anitafute kama atajisikia kuongea.
Safari ya kuondoka kuelekea kimara ilianza na baada ya mwendo na foleni tulifika katika lile eneo na nilifanikiwa kuongea na majirani wapale lakini sikufanikiwa kupata lolote lile, kila mtu alionekana kuogopa kuongea na hivyo tuliamua kurudi nyumbani kwenye mida ya saa 9 jioni, foleni ya jiji hili kwakweli ilinichosha, jua kali lilikuwa likiwaka na kila mtu alionekana kuchoka, watu walikuwa wakipita huku na kule kuhakikisha usiku hauingii bila wao kupata chochote.
SIKU MBILI MBELE.
Nilikuwa bado nikihangaika huku na kule lakini sikufanikiwa kitu, saa 6 usiku nilipokea ujumbe wa simu uliokuwa ukisomeka ‘TOMMOROW AT 10:30 AM, UBUNGO BUS TERMINAL, ALONE..SHOE SHINER’ , niliwasha simu yangu nyingine na kuangalia ramani ya kwenda hapo aliposema nikitokea pale nyumbani, nilifanikiwa kuipata na kwenda sebuleni usiku uleule kuichapisha, kisha nilirudi tena kulala, usingizi haukuja kabisa. Ilipofika saa nane nilipitiwa na usingizi kabisa.
Saa 4:00 ulisomeka mshale wa saa iliyokuwa mbele yangu, nilitazama huku na huku sikuona yeyote anayekuja. Nilikaa pale chini nikisubiri na hapo simu yangu ilianza kuita, nilipotazama ilikuwa ni Brenda anapiga simu,
“Hey upo wapi mbona chumbani sikuoni” aliuliza kwasauti yenye wasiwasi.
“nimeondoka mara moja kuna fedha kiasi Fulani nilikuja kutuma kwa mtu wa kwetu” nilimdanganya ili kumuondoa wasiwasi.
“umejuaje huko” aliuliza.
“nimechukua tax, ila usijali nitawahi kurudi” nilimjibu na kabla sijamaliza niliguswa bega na nilipogeuka nilikutana na ngumi iliyonifanya nipoteze fahamu palepale. Nilikuja kushtuka nikajikuta niko kwenye jumba ambalo linaonekana halikai mtu.
“kwanini unamtafuta Frank” aliniuliza yule kijana aliyekuwa amevalia suti nyeusi na miwani nyeusi, aliniuliza kwa lugha ya kingereza kana kwamba alifahamu kuwa mimi sijui lugha ya Kiswahili.
“kwasababu nataka kumuomba msamaha” nilimjibu kwa sauti ya upole lakini iliyojaa ujasiri.
“hiyo tu?” aliuliza tena.
“hapana si hilo tu, hilo ni dogo ambalo tayari Alishasamehe, lipo kubwa zaidi ya hilo” nilimwambia huku nikifuta ile damu iliyokuwa ikitoka mdomoni.
“ni lipi hilo” aliniuliza huku akinisogelea.
“Ya kuwa nina mpenda na niko tayari kumuonyesha mwanzo mpya” nilimwambia huku nikimtazama moja kwa moja kwenye macho yake, alinipika kofi moja takatifu na nilihisi kichwa kupasuka lakini niliona ni bora niumie ili majuto ya tulichomfanya Frank yanipungue.
“Mimi kumpenda yeye ni kosa kwenu?” nilimuuliza tena huku nikilia.
“sio kosa, ila hatutaki kusikia kuhusu huyo mtu wala yeyote anayemfahamu” aliniambia tena huku akinitazama.
“una maana gani” niliuliza na hapo ghafla niligundua kuwa wale watu ndio watakao kuwa walimtesa na kumpeleka Frank Madagascar, akili yangu ilirudi harakaharaka nyuma na kukumbuka maandishi ya kile kitabu yalivyokuwa yakielezea aina ya watu waliokuja kumpiga Frank siku ile alipokuwa kwake na sasa nilipata picha kamili kuwa watu hawa ndio walewale.
“unaelewa nini kuhusu maisha ya Frank” lilikuwa swali lililofata na mimi sikujibu chochote.
“huwa tunauliza mara mbili tu kwa kukubembeleza, na haizidi hapo” aliniambia maneno hayo na ndipo niliponyanyua mdomo wangu.
“naelewa Frank ni kijana aliyedhulumiwa kila alichokipigania kwenye maisha, nafahamu alikuwa na mahusiano na binti anaitwa Natasha lakini wewe na wengine mlimnyang’anya furaha ambayo leo hii hanayo tena” niliongea kwa sauti iliyojaa kilio lakini nilikuwa na uhakika kuwa ujumbe umefika.
“unajua nini kingine” aliniuliza huku akicheka.
“najua yote ambayo wewe unayajua na yale usiyoyajua” nilimjibu kwa sauti ya kiburi na kilichofuata hapo kilikuwa ni kipigo kama vile niliiba, kisha nilisikia wakielekezana kitu kilichofata, nilichukuliwa na kuingizwa kwenye chumba kingine kisha walinining’iniza kichwa chini miguu juu, sikuwa na la kufanya zaidi ya kulia tu;
“Tunataka kujua Frank yuko wapi na tunahitaji kila kitu ulichokuja nacho Tanzania chenye taarifa yoyote ya Frank” aliongea tena yule kijana.
“Sina chochote cha kukupa wewe, sina na nina maanisha sina” niliongea kwa hasira huku niking’ata meno.
“tutakuua binti tunahitaji hizo taarifa” alinipiga teke la kifua na kunifanya niteme damu.
“ni bora mniue, nitajisikia faraja sana kufa kwaajili ya mtu nimpendae hasa baada ya kuacha ateseke kutokana na uzembe wangu wa kufikiri, hichi mnachonifanyie nastahili kwakuwa malipo ni hapahapa duniani na sasa nalipwa kwa kusababisha Frank ateseke akiwa Madagascar, itakuja zamu yenu na nyie kulipa, kwaiyo nawashauri wala msihangaike na mimi mkijua nitawapa chochote” niliwaambia huku nikiliza lakini nikiwa namaanisha.
Walinishusha chini na sasa hapa walimleta mtu mwingine akiwa amefunikwa nilipomtazama alikuwa Brenda na hapo hapo nilisikia mlio wa risasi kulekea kwa Brenda.
“utatoa au nimfumue risasi ya kichwa” alinisemesha kwa sauti ya juu.
“sikupiiiiiiiiiiiiiiii” nilitoa sauti ya juu na hapo nikasikia mlango umefunguliwa.
“Beatrice una tatizo gani” nilisikia sauti na kushtuka, alikuwa ni Brenda.
“ooh mungu wangu” nilijisemea kwa uchovu.
“njoo hapa” aliniita Brenda kwa sauti ya kubembeleza na kunikumbatia.
“nimeota ndoto mbaya” nilimwambia kwa sauti ya chini kabla sijajikurupusha pale kitandani na kukimbilia simu yangu chini ya mto, kuitazama ilikuwa ni saa 3: 45. Nilivuta pumzi na kufungua sehemu ya ujumbe kisha nilimuonyesha Brenda ule ujumbe wa simu, aliniambia nisiende lakini nilimwambia sikuwa na namna nyingine, nilimwomba aniitie tax lakini alisema atanipeleka yeye.
****
Saa 4 kama ule ujumbe ulivyoelekeza nilikuwa pale, nilikuwa nina wasiwasi hasa kwakuwa nilikuwa na ndoto mbaya siku hiyo lakini sikuwa na njia nyingine. Nilienda kusimama sehemu ya wazi huku nikiangalia huku na kule, na kwa mbali mbele yangu Brenda alikuwa akiniangalia kwa tahadhari ili baya lolote lisinipate.
“Hey how you doing” (habari yako) aliniongelesha kijana aliyekuwa pembeni yangu huku na yeye akitazama mbele kama vile alikuwa akimsubiri mtu.
“am cool”(niko poa) nilimjibu lakini sikuwa na mpango nae, niliendelea kutazama huku na kule.
“follow me” (nifuate) aliniambia hivyo na nilipogeuka alikuwa ameshaanza kuondoka kuelekea kwenye ‘super market’ iliyokuwa pale karibu. Nilimtumia ujumbe Brenda ili aendelee kunifatilia na hapo nilianza kumfata yule kijana mpaka ndani ya ile ‘supermarket’. Nilifika kule ndani na kukutana na yule fundi viatu. Cha ajabu kumbe alikuwa akifahamu kingereza.
“Dada kitu unachokifatilia ni hatari sana, mi nafahamu fika yaliyomkuta Frank lakini ni kitu kilichofanywa na watu wakubwa na wenye nguvu sana, toka Frank aondoke kule mtaani sijawahi kumuona tena, ingawaje juzi alikuja kule na kuniambia kuwa amerudi lakini asingependa mtu yeyote afahamu, hakuniambia namba yake ya simu wala anakoishi, lakini alisema leo atakwenda kuangalia makaburi ya wazazi wake na ndio maana nilikuambia uwe hapa leo” alinieleza kwa ukarimu sana.
“Kwahiyo tunafanyaje kaka” nilimuuliza
“umekuja na gari?” aliniuliza na nikashindwa cha kumjibu ila nikamwambia tu ukweli.
“mimi ni mgeni na sijui huu mji kwaiyo nimeletwa na rafiki yangu na gari yake yupo kule mbele nimemwacha” nilimjibu.
“mpigie simu aje hapa” nilinyanyua simu yangu na kumpigia Brenda na yeye alifika pale.
“sasa bila kupoteza muda, mtaondoka hapa mpaka kimara baruti kule upande wa kushoto kuna njia flani inateremka bondeni pale kuna kiwanda cha kuranda mbao, nyoosheni na ile njia mpaka mbele mtaona makaburi, kaeni mbali ili asije akaja alaf asifike pale. Mimi natangulia mtanikuta.
Tuliondoka na gari pale kwa haraka na muda wala haukuwa mrefu sana tulifika pale, tulikaa na wale vijana kwa karibu nusu saa nzima, na kwa mbali tulianza kusikia sauti ya pikipiki ikija, ilikuja mpaka pale makaburini na baada ya kushuka pale nilihakikisha kabisa kuwa alikuwa ni Frank, ndipo tulipotoka pale na kuanza kuelekea kule ila baada ya yeye kugeuka na kuona wale vijana kwakuwa ilikuwa kwa mbali hakuweza kuwatambua na hivyo alikimbia na yule mwenye pikipiki aliondoka tulijitahidi kumuita lakini walitokomea vichochoroni na hatukuwa na la kufanya, nilisogea mpaka pale kwenye yale makaburi na kuanza kulia, hii ndiyo ilikuwa nafasi yangu ya kumuona Frank lakini ilishashindikana.
MWEZI MMOJA MBELE
Asubuhi na mapema niliondoka kwenda kumalizia kuwasimamia mafundi waliokuwa wakijenga makaburi ya wazazi wa Frank, kwakuwa baada ya kukata tama ya kumpata niliona japo niache makaburi ya wazazi wake yakiwa yamewekwa katika hali nzuri. Wakati nipo njiani na sasa nilikuwa nikiendesha gari mwenyewe niliona picha ya Frank kwenye gazeti na kuegesha gari pembeni kisha nilimuita yule mwenye magazeti nikanunua lile gazeti na kugeuza gari kurudi nyumbani lakini sikumkuta Brenda nilimpigia simu na alinielekeza alipokuwa hivyo nilimfata na kumuomba anitafsirie kilichoandikwa, alinieleza kila kitu na mimi ilibidi nimueleze sehemu ya ukweli kuhusu Frank iliyokuwa imebaki. Baada ya hapo niliondoka mpaka wizarani na kuingia nikaomba kuonana na Natasha lakini nilikataliwa, nilimpa katibu muktasi wake kikaratasi ampelekee na ndipo niliporuhusiwa kuingia.
“Habari yako” alinisalimu na kunikaribisha kiti.
“asante sana habari ya majukumu” alinimuuliza huku nikimtazama, alikuwa ni mrembo sana na kila alipoongea midomo yake na sura yake vilikuwa vikisadifu uzuri wake, niliongea kwa lugha ya Kiswahili lakini ilikuwa dhahiri kabisa kuwa sikuiweza na hivyo ilibidi nimwambie ukweli ili kufupisha maongezi. Nilijitambulisha kama rafiki wa Frank na nilikuja pale ili kuongea nae kuhusu Frank.
“ I don’t wanna talk any shit about Frank, not even in a second, so I gues we are done here, am a minister I have alot of works to do, and not sitting here talking about that rude guy. he hard his time but he ruined it and now am a married woman with a kid, and he know because just a day before yesterday he saw me at the traffic lights with my baby so tell him his days are numbered” (sitaki kuongelea upuuzi kuhusu Frank hata kwa sekunde, na nadhani tumemalizana,mimi ni waziri nina kazi nyingi za kufanya na sio kukaa hapa kumuongelea yule katili. Alikuwa na muda wake ila aliuharibu na kwasasa mimi nimeolewa na nina mtoto, na anajua kwakuwa juzi aliniona nikiwa kwenye mataa na mtoto wangu, kwaiyo muambie siku zake zinahesabika. Aliyaongea hayo huku akitokwa na machozi,, ni kweli alikuwa akimchukia lakini niliona jinsi ambavyo alikuwa anampenda Frank,,alinyanyuka na kuanza kunifukuza lakini kabla sijanyanyuka pale nilimpatia CD ambayo nilinakili ile hadithi ya Frank,,nilimuachia pia na kikaratasi kilichokuwa na namba yangu lakini hakupokea na badala yake niliweka pale mezani.
“Don’t ignore the CD, and that is my number your honour, don’t throw it away cause you might need to talk to me” (Usidharau iyo CD, na ile pale ni namba yangu muheshimiwa, usiitupe kwakuwa unaweza kuhitaji kuongea na mimi). Nilinyanyuka na kuondoka.
“Bahari tulivu haimpimi nahodha wa meli na kisichokuua kitakukomaza, kuna muda tunakutana na changamoto za kimaisha na kukata tama lakini tunasahau kuwa juhudi binafsi ni muhimu katika kutuletea maendeleo chanya kwenye maisha yetu, tunataka kutembea masaa yote bila kuliona giza na kuula mua bila kukutana na pingili, maisha yana changamoto na ukubwa wa fikra pevu zitawalazo nafsi na ufikiri wako ndio mtaji wako katika changamoto zikukumbatiazo,,,kila mtu anaweza ila tunatofautiana uwezo na namna ya kuitendesha kazi akili yetu na fikra zetu, kila kizuri umeumbiwa wewe ila kukipata ni juhudi yako,,,tulikuja duniani peku ila kuvaa ndala ni juhudi yako,,,UKISUBIRI UNUNULIWE KIATU,,UTATEMBEA PEKU MJINI”….HII NI SEHEMU YA NANE…ANDIKA HIVI.
NATASHA ANAHADITHIA
MIAKA 10 ILIYOPITA.
Nilifurahi sana kukutana na Frank kwakuwa alikuwa na muonekano na fikra pevu kama kijana na kama mtu anayejitambua. Jioni ya wiki ya pili toka nitoke likizo na ikiwa ni baada ya mi kuwa nimefahamiana na Frank kwa muda mrefu nilikuwa nikiongea nae kwa njia ya ujumbe wa simu na kesho yake aliniomba tukutane kesho yake nyumbani kwake, nakumbuka hii ilikuwa ni baada ya kifo cha Janeth ambaye ni mdogo wake. Mazungumzo ya siku hiyo ndo yalizidi kunivuta nitamani kuwa na Frank, chanzo ilikuwa picha yake akiwa mdogo;
“hahaa ulikuwa na mashavu” nilimwambia kwa kumtania huku nikicheka, nilikuwa nimeshikilia ile picha na yeye hakutaka niichukue.
“Acha utani bhana,,njoo basi nipe iyo picha mana mimi siipendi” aliniambia huku akinifata, alianza kunishika ili aninyang’anye lakini ghafla wote tulikaa kimya pale tulipojikuta katika kunyang’anyana akawa kama amenikumbatia kwa nyuma.
“samahani sikumaanisha…” aliniambia huku akiniachia na kwenda kuketi pale kwenye kochi, lakini kabla hajamaliza nilimkatisha.
“hujakosea chochote” nilimtazama kwa makini usoni kitu kilichomfanya aone aibu, nilimfata mpaka pale kwenye kochi na kumrukia, kisha nilimlalia kifuani bila ya aibu kwakuwa nilijua tunajaribu kuzikimbia hisia zetu tu ila ukweli ni kwamba tulipendana.
“Frank niambie unachokwepa kuniambia” nilimwambia huku nikivishika vidole vyake na yeye mkono wake ukiwa kwenye nywele zangu.
“Unamaana gani” aliniuliza kana kwamba hakufahamu nilichokuwa nikiongea, lakini nilimuacha na kumtazama tena machoni, kisha bila haya nilimbusu shavuni, aliona kama miujiza lakini hisia zake hazikumdanganya kuwa hata mimi nilikuwa na hisia juu yake
“Namaanisha nini unasikia unaponitazama na nini unawaza nikiwa mbali na wewe” nilimwambia huku nikimpa tabasamu anitazame vizuri.
“Nakupenda Natasha, nakupenda sana, wewe ndio kitu cha thamani nilichobakiwa nacho kwenye maisha, wewe ni msichana wa furaha yangu, wewe ni maisha kwangu Natasha” haya yalikuwa meneno machache sana yaliyoanzisha mwanzo wa mapenzi yangu na Frank, kila mara nilipoyawaza na kuyakumbuka maneno haya nilizidi kumpenda Frank.
“Nakupenda pia Frank, sijui tutafika wapi katika maisha lakini sitaki tuachane, kwangu wewe ni zaidi ya bustani nzuri inipayo faraja na upepo mwanana”,,nilimtazama Frank chozi likanidondoka, nilimpenda sana Frank na sikuwa tayari kuona akiteseka, kila alichokitaka kwangu nilimsaidia kwakuwa nilikuwa na pesa za kumsaidia, alikuwa na heshima.
Katika mahusiano yangu na Frank alikuwa na heshima sana kwangu kila alipoona amekosea aliomba msamaha, alikuwa mpole sana, alijali furaha yangu kuliko kitu chochote, kila mara alitaka kujua nilipo na kama niko salama, hiyo ilikuwa ni inatosha sana kunionyesha kiasi gani anajali.
MIAKA MITATU BAADA YA FRANK KUONDOKA
Sikuwa natamani hata kusikia jina la Frank. Licha tu ya kumuona,alinitendea kitu ambacho sikuwahi kukifikiri, na baada ya yeye kuondoka kwenye maisha yangu japo sikumsahau kabisa lakini wazazi wangu na ndugu walinishauri sasa niwe na maisha mapya, sikuwahi kumwamini mwanaume yeyote kabisa katika maisha yangu kwakuwa nilikuwa na nafasi ya kumuamini Frank ambaye pamoja na yote aliishia kutaka kuniua, nilikubaliana nao japo ilikuwa kishingo upande.
Wiki tatu mbele toka nilipoambiwa kuwa nianze maisha mapya nilikutana na Nicholas katika tafrija ya kumpongeza baba yangu kwa kufikisha miaka sitini na moja, alitambulishwa na baba yangu kwangu kama mmoja wa vijana wenye mafanikio makubwa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, alikuwa mtanashati na mwenye kujiamini. Mbali na utajiri aliokuwa nao alikuwa na msimamo na mambo yake, kila aliposema hapana alimaanisha, alicheka mda wote hata pale alipokasirika. Sikuwa na hisia nae mara ya kwanza nilipomuona pale ikulu ila nilianza kumpenda siku aliponialika kwenye sherehe ya kumshukuru mungu kwa mafanikio makubwa aliyoyapata kwenye Kampuni zake tatu kwa muda wa miaka miwili, sherehe hiyo ilifanyika kwenye jumba lake la kifahari lililoko pembezoni mwa bahari ya hindi jijini Dar, nakumbuka siku hiyo usiku wakati tukiendelea na ile sherehe, mimi na yeye tulitoka nje na kuanza kuzunguka kwenye bustani iliyopo pale nyumbani kwake, ilikuwa ni bustani ya kupendeza hasa kwakuwa ilikuwa na mwanga hafifu lakini usimamapo kwenye bustani hiyo unaweza kuliona jiji la dar lilivyo kwa uzuri na mataa yake;
“Kwanini hujaolewa mpaka sasa na unakila kitu Natasha?” lilikuwa swali la kichokozi toka kwa Nicholas.
“hahaa,, kwanini we huajoa mpaka sasa na unakila kitu?” nilimuuliza tena lile swali huku nikitabasamu, tulikuwa tukitembea lakini alisimama na kunitazama huku akitabasamu kisha alitembea taratibu hadi mbele kidogo akanipita na kunigeukia;
“Nitazame vyema, kwanini sijaoa unadhani” aliniambia huku akinitazama kama mtu aliyetaka kuisoma akili yangu, nilijaribu kumkazia macho lakini nilishindwa.
“Hujataka kuoa, au muda bado” nilimjibu huku nikiangalia pembeni, tulienda mpka sehemu ya juu ya ile bustani na wote tulikuwa tukiangalia mataa ya majumba ya mjini yalivyoung’arisha mji, kimya kilitanda kwa muda na maongezi yalirudi tena;
“sababu za kutokuolewa kwako ndo ndo sababu za kutokuoa kwangu” aliniambia huku akiangalia zile taa.
“sababu zipi” nilimuuliza huku nikigeuka na kumtazama lakini hata hivyo hakunitazama aliendelea kuongea.
“Kila msichana katika jiji na dunia hii anawaza kuishi maisha mazuri, na kila mvulana anawaza na anandoto za kuwa na maisha bora, ila maisha bora hayapatikani kirahisi sana, lazima uteseke, unyanyasike ndipo uanze kufaidi, sasa kwakuwa njia ya mafanikio ni ngumu wengi hutumia mkato, ikiwa ni pamoja na kuigiza mambo yasiyo halisi, nilishawahi kuwa na wasichana wengi sana lakini wengi walifata pesa, walikuwa na mapenzi ya kunatisha na mate na upepo kidogo ulivyokuja yale mapenzi yalidondoka, walifanikiwa kupata walichotaka kwangu ila sikufanikiwa kupata nilichotaka kwao” alinieleza kwa sauti iliyoonyesha ni namna gani aliumizwa na jambo hilo.
“kitu gani ulitaka kwao” nilimuuliza huku nikigeuka na kutazama nyumba yake na wakati huo yeye alikuwa bado akitazama zile taa mbele yake.
“nilitaka kitu kidogo tu toka kwao ambacho kingeza mengine, nilihitaji upendo wa kweli tu ambao ungepelekea ndo na familia bora, hiyo ilikuwa ndiyo ndoto yangu kubwa, nina pesa na kila kitu lakini sina familia, sina mtoto, niko mimi kama mimi,” aliongea na kukaa kimya kwa muda, machozi yalinitoka kwani alinikumbusha jinsi ambavyo nilikuwa nikipanga na Frank lakini ilishindikana kwa kuwa hakufata mapenzi kwangu bali pesa na njama zake za kijasusi.
“hatutofautiani sana Nicholas,,,,”nilimueleza japo alinikatisha.
“ndio najua” alinijibu na kugeuka.
“unajua nini” nilimuuliza huku nikimtazama.
“najua kila kitu kilichokutokea kwenye maisha yako, nilimuona yule kijana na niliwahi kuongea nae” aliniambia na hapo nilibadilika na kutaka kujua ilikuwaje.
“sikuelewi” nilimuambia na kuonyesha sura ya kutaka kufahamu.
“ujue Natasha baba yako ni mtu wangu wa karibu sana, nilikutana nae kwenye mambo ya kibiashara kipindi hiko mimi nikiwa mdogo, kwaiyo pamoja na kwamba alikuwa ni kama baba yangu lakini kila mara alinihitaji kumpa ushauri na hata kampeni zake za urais nilishiriki katika kutafuta pesa ya kumuwezesha kufanya kampeni zake, na hata kipindi yule kijana anapanga ujinga wake tulimshughulikia sawia” alinieleza hayo na kunifanya nikae kimya kwa muda.
“kwaiyo ulinifahamu toka kipindi hicho” nilimuuliza kwa shauku.
“nimekujua toka ukiwa chuo kikuu” alinijibu na kunishika mkono, tuliondoka mpaka mbele zaidi ya eneo la nyumba yake kisha tuliketi kwenye viti vilivyokuwa kwenye kiunga cha maua.
“Natasha, naomba uwe mke wangu” ni sauti iliyonishtua na kuninyima neno lolote la kusema.
“lakini….Nico..lakii,,,,”sikuweza kumaliziakusema kile ambacho hata sikujua ni nini nilitaka kusema, lakini kabla sijaendelea nilikatishwa na maneno mengine ya Nico.
“Yeah I know this is difficult after what you have gone through, but take some times to think”(ndio najua hii ni ngumu kwako, hasa kwa yote yaliyokutokea, lakini nakupa muda wa kufikiria), yalikuwa ni maneno ya kiume ambayo hayakuonyesha tone la kusitasita wala kulazimisha kukubaliwa,,ilikuwa ni chukua ukakae nalo utafakari. Alinivuta mkono wakati nikiendelea kushangaa pale na kunipeleka mbele kidogo ya ile bustani ambapo kulikuwa na bwawa zuri la kuogelea. Aliniambia nisubiri pale, kisha alitoka na kurudi na taulo nyeupe mbili na mfuko uliokuwa na nguo mpya za kuogelea alinionyesha mlango uliokuwa mbele kidogo ambapo kulikuwa na chumba cha kubadilishia nguo, ni kama aliniondoa ufahamu vile kwakuwa alifanya mambo mfululizo nikakosa la kusema, nilienda nikabadilisha zile nguo na kurudi pale nikakuta yeye ameshabadili nguo na alikuwa sasa akiogelea. Nilijitupa kwenye maji na kuanza kuogelea huku kichwani nikiwaza kila kilichotokea pale, ghafla tu alinishika na mimi nilishindwa kujizuia, nilimtazama na yeye alinikumbatia pale kwenye maji, mara zote aliponitazama alikuwa akitabasamu tu kitu ambacho kilininyima uhuru wa nafsi na kujikuta nikizama kwenye penzi lake.
MIEZI MINNE MBELE
Baada ya miezi minne niliingia rasmi kwenye mahusiano na Nicholas, ilichukua muda mimi kumsahau Frank lakini baada ya kufungwa ndoa nilianza kujitoa kwa Nicholas, alikuwa mpole na mtu mwema sana kwangu, tuliishi kwa furaha na kila mara alikuwa akihakikisha sipati tabu tena,,nilianza kusahau tabu na manyanyaso ya dunia hii,,na sasa sikuwa tu nafurahia kuwa nilikuwa mtoto wa rais la nilikuwa nafurahi zaidi kuwa mke wa Nicholas.
SASA
Nilikaa pale ofisi nikitafakari juu ya kile yule msichana Beatrice alichoniambia, alikuwa amenivuruga akili kwa kuwa sikutaka kabisa kuongelea kuhusu Frank. Nilinyanyuka baada ya yeye kuondoka na nilikwenda mpaka kwa katibu muktasi wangu na kumkataza kabisa kumruhusu yule dada siku nyingine.
“iwe mwanzo leo na mwisho kumruhusu yule dada akija hapa, la sivyo utaondoka nae” nilimuambia maneno makali japo nilijua kuwa hakuwa na kosa lakini nilihisi kama ametumwa kunivuruga. Siku hiyo nilikuwa na kikao na kamati ya bunge, hivyo muda mfupi baada ya Beatrice kuondoka niliondoka kuelekea Dodoma.
Baada ya kufika Dodoma nilikuwa nina shughuli nyingi na mida ya usiku saa 7 tulikuwa tumemaliza kabisa na mimi nilikwenda kwenye hoteli niliyofikia kwaajili ya kupumzika, nikiwa pale chumbani yale mawazo yalinijia tena ya yule msichana lakini nilijitahidi kupambana nayo. Asubuhi na mapema nilianza safari ya kurudi Dar na kwenye majira ya saa sita mchana nilifika nyumbani na kumtazama mtoto wangu kisha nilijiandaa tena na kwenda ofisini kwa Nicholas kisha nilienda ofisini kwangu, nilipofika nilikumbuka kuhusu ile CD nikaichukua na kuiweka kwenye laptop yangu ilifunguka vizuri na niliona kitu kimeandikwa huko, niliitoa na kuiweka pembeni kisha niliendelea na kazi za kiofisi. Jioni ya siku iyo nikairudia tena ile CD na kuisoma yote yaliyokuwa yameandikwa kule ndani, nililia sana lakini sikuwa na uhakika wa mambo kama ni kweli yale yaliyoandikwa ndiyo yaliyo tokea, nilinyanyua simu yangu ya mkononi na kumpigia kijana mmoja niliyemfahamu;
“hello, habari yako Haleed” nilimsalimia kwa sauti iliyoonyesha kuna jambo la dharura.
“salama muheshimiwa, za kazi” alinisalimu na bila kupoteza muda niliamua kumuambia shida yangu.
“nataka kuonana na wewe mda huu” nilimuambia huku nikikusanya funguo zangu pale mezani.
“wapi muheshimiwa” aliuliza kwa shahuku,
“we uko wapi sasa hivi” nilimuuliza tena na kuanza kutoka nje.
“niko maeneo ya hapa exim tower”
“rudi njoo hapa wizarani kuna sehemu nataka unipeleke maana dereva wangu hayupo” nilikata simu na baada ya dakika kama 10 hivi Haleed aliwasili, huyu alikuwa kijana wa usalama wa taifa ambaye mara nyingi yeye ndiye amekuwa mpelelezi wangu na mlinzi wangu, namuamini kuliko kitu chochote kwakuwa huwa ni mkweli. Alifika pale na nilimuambia kuwa tunaelekea Mbweni na safari ilianza, tulipofika mbele kidogo eneo la jeshi nilimuambia asimamishe gari na kwakuwa nilikuwa nikitumia gari langu binafsi haikuwa rahisi kujulikana.
“Haleed mimi nina shida ndugu yangu, nataka unambie kitu kimoja na kwa ukweli na nitakupa zawadi kubwa sana” nilimuongelesha huku nikimtazama usoni.
“kitu gani muheshimiwa” aliniuliza huku akijiweka sawa, nilitazama chini kwa muda kidogo na kukumbuka jambo.
“unakumbuka kipindi nahangaika na yule kijana kuna siku ulikataa kunipeleka kule walikokuwa wamemshikilia na kuniambia kuwa hauko tayari? Nilimuuliza na kumkumbusha jambo lililtokea miaka miaka mingi iliyopita.
“nakumbuka madam” alijibu huku akionanekana kutaka kujua kinachoendelea.
“nataka kujua kila kitu kuhusu yule kijana, nataka kujua kwanini uliniambia siku ya mimi kufumbua macho nitalia” nilimkazia macho
“aaahh mada,,,” aliongea kwa kung’atang’ata maneno.
“hey, hey namaanisha Haleed, umekuwa mtu wa upande wangu kwa muda mrefu sana, tafadhali niambie kila kitu” niliendelea kumsisitizia. Alinizungusha kwa muda wa nusu saa nzima lakini mwishowe alikuja kunieleza ukweli;
“madam nahatarisha kazi yangu na maisha yangu, lakini iko hivi, yule kijana hakuwa hivyo ulivyoambiwa, na hatuwezi kuongelea hapa” aligeuza kari kwa kasi na tulikamata njia ya nisikokujua, mwendo kama wa nusu saa tulifika kwake na geti lilifunguliwa kisha tuliingia ndani, alinikaribisha mpaka ndani na nilipoingia aliondoka na kuja na laptop yake kisha aliigeuza na kufungua upande wa betri akatoa ‘memory card’ kisha aliirudisha ile betri na kuiwasha laptop yake, alifanya vitu kwa haraka na tahadhari kubwa sana, baada ya ile laptop kuwaka aliingiza ile ‘memory card’, kisha alianza maelezo.
“hii unayoiona hapa ni siku ya kwanza tumeitwa na mzee wako kuhusu huyo jamaa yako,tukapewa kazi ya kumfatilia na kukufatilia wewe, na ndipo tulipogundua mambo yote ya wewe kumpangia chumba na mambo ya ada, taarifa zote tulikuwa tunakabidhi kwa mtu anayeitwa Reuben ambaye kwasasa ni mkuu wa kitengo cha usalama wa raia, lengo lilikuwa ni mzee wako kukutenganisha na huyu kijana kwakuwa hakuwa wa hadhi yako hasa kwakuwa alitegemea kuwa rais mda mfupi mbele” alinielezea hivyo na kuichezesha ile video iliyoonekana kuchukuliwa kwa siri, mwili wangu ulisikia baridi na nilianza kutetemeka taratibu.
“alaf hiki kipande hapa ni siku wanapanga mbinu za kumfutia vyeti vyake vyote, utaona hapo mbele itaonyesha mtu anaongea kwenye ‘skype’,,(huku akionyesha kidole, na kisha kuisimamisha), huyu hapa ni mkuu wa chuo cha Mzumbe wa wakati huo, alikuwa akielezwa juu ya mchakato wa kumfutia vyeti Frank na yeye alikubali kwa sharti la kuletwa wizarani, lakini hata hivyo kwakuwa hakuwa na uzoefu lakini alikuwa ashaangizwa kwenye mchakato basi alivyokuja kuletwa wizarani akauliwa kimtindo, hapa mbele (akaichezesha tena ile video), hapa,,,,huyu ni msajili wa law skul nae alipewa hiyo kazi na huyo mdada unaemsikia anaongea kingereza hapo ni msajili mkuu wa chuo upande wa taaluma wa Pretoria University, wote hawa walipewa zaidi ya milioni 60 kufanikisha hilo” nilikuwa tayari nimesha nyong’onyea na mwili mzima ulijaa hofu na fikra zilikuwa haziko sawa,.
“Nani alichukua hii video” aliuliza.
“nilichukua mimi na ndio maana kwenye tukio zima hujaniona, nilikuwa na saa niliyokuwa nimeiweka kamera ndogo sana, kwaiyo kila kikao nilikuwa nikichukua kwakuwa nilikuwa nasimama” alinijibu kwa ufupi huku akiendelea na ile video.
“kwanini uliichukua ile video” nilimuuliza swali lililomfanya aache kufanya afanyacho.
“Frank ni kijana niliyemfahamu alipokuwa Mzumbe, alikuwa ni mtu safi sana, sikuweza kuyazuia haya kwakuwa nilitaka kuendelea kuishi, lakini niliamini ipo siku naweza kukutana nae na kumpa ushahidi huu” aliendelea kuongea lakini mbeleni kidogo aliisimamisha ile video.
“mchezo mzima ulikuwa ni kumsambaratisha Frank, watu walioshiriki ni wengi sana, lakini kama baba yako hakufanya hivyo basi wapinzani wake wa kisiasa wangeweza kuzua lolote la kuzua, sasa angalia hapa” nilisogea tena kwa makini nikiangalia hiyo video.
“hapa kilikuwa kikao cha mwisho kabisa na kilifanyika Cris Hotel iko Boko, huyu hapa mwenye upara ni mstaafu sasa hivi na ndiye alikuwa mwendesha mashitaka kipindi kile, hapo utasikia maneno kwa sauti ya chini na ni kwakuwa nilikuwa mbali na yeye ila alikuwa anaeleza kuwa pale wataongea na yule hakimu ili afute lile shitaka ili ionekane kuwa Peter Pronto yule mgombea wa chama kingine ndiye aliyetoa hongo yule jamaa aachiwe, hii ingekuaminisha kuwa yule jamaa si mtu mzuri, lakini lengo hapa ni kupata ‘people’s sympathy’(huruma ya wananchi)” nilimkatisha kwa swali.
“hiyo huruma ingemsaidia nini” nilimuuliza
“huruma inakuja pale ambapo kuna watu hawakukubali sasa kwa kuonyesha kuwa wewe unaonewa na kufatiliwa basi wananchi wanakuonea huruma na hiyo inammaliza nguvu mpinzani wako kwakuwa yeye atatumia muda mwingi kujitetea kuliko kunadi sera zake” alimaliza kunielezea hapo na kuendelea mbele zaidi.
“sasa baada ya hapo ndio tulikaa tukapanga kumuua lakini kwakuwa hatukutaka kumuua tulikubaliana kumchoma sindano ya kumvuruga na kwenda kumtupa mbali, na hapo ilikamilika” alivuta pumzi na mimi nilichomoa ile memory kadi na kufungua mlango ili niondoke;
“Muheshimiwa bado hatujamaliza” alinifanya nisimame.
“bado nini” nilikuwa ninalia kama mtoto.
“leta iyo ‘memory card’” nilirudi nakumpatia kisha aliingiza tena kwenye laptop na ilipofunguka aliipeleka ile video mbele kisha aliisimamisha na kuniambia nisogee, niliposogea aliichezesha na hapo niliishiwa nguvu.
“nini icho” nilimuuliza.
“NICHOLAS NDIYE ALIYETOA FEDHA ZOTE ZA KUMSHUGHULIKIA FRANK ILI AJE AKUOE BAADAE” aliniambia Haleed.
“Huwezi kuwa makini zaidi ya makini yenyewe, kuna muda si kila kilicho muhimu basi kina weza kuwa muhimu muda wote, kuna wakati wa kuachia hisia zako zitembee kwenye mirija ya fikra zako. Mwambie usiogope.” HII NI SEHEMU YA TISA ANDIKA HIVI.
NATASHA ANASIMULIA
Niliweka kila kitu pale na kuvua viatu kwakuwa nilihisi kama viliniwekea mzigo, niliitazama ili video vizuri na kuanza upya kuisikiliza.
“Muheshimiwa..”aliniongelesha Haleed lakini nilimkatisha.
“Sistahili kuitwa muheshimiwa, niite Natasha, huu ni unyama mkubwa ambao nimeshiriki, Frank alikuwa ni zaidi ya vyeo nilivyonavyo sasa na sio kama ambavyo mlifikiri” niliongea huku nikilia mfululizo.
“Inabidi uwe na uvumilivu wa hali ya juu, unaenda kupambana na watu wengi na sio baba yako tu, katika njia hiyo mengi yanaweza kutokea, nimefanya kazi na usalama kwa zaidi ya miaka nane naelewa mbinu na kila namna ya watu hao, hili jambo lina mlolongo mrefu sana na huweza kuumaliza wote ukawa salama kama hautakuwa makini Natasha” aliniambia Haleed huku akinitazama kana kwamba alikuwa na njia aliyotaka kuniambia niitumie.
“kwaiyo wewe unashauri nini” nilimuuliza huku nikimtazama.
“Kuwa mpole kwa muda, usimuonyeshe Nicholas utofauti wowote wala mtu yoyote, nenda kwako sasa hivi kisha ukifika utaniambia nitakuelekeza cha kufanya” , sikuelewa alichotaka kufanya lakini sikuwa na cha kufanya zaidi ya kumkubalia.
ITAENDE;EA
Taaluma Iliyoptea Sehemu ya Nne
Also, read other stories from SIMULIZI;