Ninah Sehemu ya Kwanza
IMEANDIKWA NA: CHANDE ABDALLAH
********************************************************************************
Chombezo: Ninah
Sehemu ya Kwanza (1)
Mimi ni msichana wa miaka 26, ni mrefu, mwembamba kidogo, rangi ya chungwa na cha zaidi sijisemei ila kwa mujibu wa watu mimi ni mzuri. Sasa hapo itategemea kila mtu anavyoniona, lakini ni mzuri kiasi kwamba watu wananifananisha na watu wengi maarufu tu.
Nimezaliwa na kukulia katika maisha ya kitajiri kidogo, nikipata kila ninachotaka kutoka kwa baba yangu ambaye tangu mama afariki ndiye yeye pekee aliyekuwa akinilea, lakini pia baba ana watoto wengine na mama yangu wa kambo na ni wadogo mno, hivyo mimi ndiye dada mkubwa.
Maisha yangu yalikuwa rahisi hivyo, nikiwa na marafiki wengi na wanaume wengi wanaotaka niwe nao kimapenzi. Uzuri wa kukulia kwenye maisha ya kitajiri, sibabaiki na mwanaume kwa ajili ya pesa zake. Naangalia moyo wake na mapenzi yangu kwake.
Cha zaidi ninaamini katika mapenzi ya dhati na sipendi kuumizwa, ninapenda sana na ninawivu mno. Nilishawahi kuumizwa mara kadhaa na watu niliowapenda mno na hiyo sikutaka ijirudie tena hivyo sikuwa na marafiki tena wakike kiasi cha kumuamini siri zangu.
Tofauti na wengi wanavyodai kuwa wanawake wazuri hawana akili za kimaisha na siyo makini, lakini si kwangu, sijajifunza kutegemea cha mzazi, ninahangaika kupata cha kwangu mwenyewe, tena hiyo pengine kutokana na baba ninavyomuona anavyopelekwapelekwa na mama yangu wa kambo.
Naogopa nisije kukosa hata kiurithi chenyewe.
Okey! Sasa nimemaliza kula na nimeingia chumbani kwangu kuchati na marafiki zangu kupitia simu yangu, ninafurahia nikiiona meseji kutoka kwa Brighton, mwanaume niliyetokea kumpenda tu, siyo kwa sura wala pesa bali ni kutokana na jinsi anavyoniheshimu na kunipenda pia na cha zaidi ni mcheshi sana.
Yaani hata ninune vipi, nitacheka tu nikiwa naye, na nikisema ananiheshimu jua ananiheshimu kiasi cha kutosha tu utajua huko mbele. Kabla hatujawa kwenye uhusiano nilimuona tu alivyokuwa akitamani kuniambia ananipenda lakini alikuwa anaogopa mno, nadhani alijitazama hadhi yake nakuona haiwezekani akawa na mimi, kwa kujua hilo nikamrahisishia na kuanza naye mahusiano; tuna miaka mitano hadi sasa na sijajuta kwa lolote.
NINAH 02
Huwezi amini, anajiona ana bahati kuwa na mimi, na mimi nafurahia hilo. Siyo unakuwa na mwanaume bitozi, hendsamu boy kiasi kwamba hajali hata ukikukosea ana uhakika atampata mwanaumke mkali zaidi yako. sitaki wanaume wa hivyo.
Kwa hiyo Brighton ndiye tulizo langu la moyo, lakini kama nilivyosema, hana kazi, kwa hiyo hana hela, japo ana elimu ya chuo kikuu na anatarajia sana kupata ajira.
Huko kipindi cha nyuma nilimpa mtaji tukafungua duka letu la vipodozi, biashara imekuwa mno. Tumehifadhi hela kiasi na anatarajia kunitolea posa kesho. Nina uhakika tukioana kipato chetu kitatuendesha kimaisha vizuri tu, na hatutayumba.
“Hallow my dia mithii you!” nilisema kwa kudeka fulani hivi nikiongea na Brighton, kwa sababu nilijua tu lazima atataka kunivunja mbavu kabla sijalala.
“My Ninah lakini unajua maana ya mithii you?” alisema Brighton.
“Mh si nimekukosa muda mrefu na ninatamani uwepo wako!”
“mh sasa hiyo my dia tunasemaga miss you, lakini ukiweka kithethe tu na kuwa mithii you hapo unachokimiss ni kingine sasa, n’takuita Centro sasa hivi shauri yako!” alisema Brighton nikacheka hadi nadhani huko sebuleni baba alinisikia, nikapunguza sauti kidogo.
“Hubby una vituko sana, enhee niambie, kesho ndiyo mtu wako anakuja kwa baba?”
“ndiyo, nimeshampanga kila kitu, yaani ujue namuogopa mzee wako, sijui atakubali maana uliona mwenyewe alivyosemaga kipindi kile alivyojua tunadate?” aliongea Brighton kwa masikitiko kidogo, uzuri wake akiongea mambo siriazi ucheshi anauweka pembeni.
Hapo alinikumbusha kipindi kile baba alipomuona Brighton ndani kwetu, akamsema mbele yangu kuwa hana kitu atanipotezea muda tu na maisha yangu.
“usijali akiona tupo siriazi kabisa tunataka kuoana atakubali mwenyewe!” nilisema na kumchumu kisimusimu. Akaonekana kufurahi kidogo halafu akaniambia: “Umeandaa cheti cha kuzaliwa? Mimi ninacho, Sitaki mambo madogomadogo yatukwamishe ndoa yetu,” alisema Brighton nikacheka mpaka nikapaliwa. Tukaagana na mimi nikalala ingawa kimoyo kikinidunda kwa ujio wa mshenga wa Brighton hapo kesho na jibu la baba litakuwaje.
NINAH 03
Basi kesho yake nikajifanya bize, sikukaa nyumbani nikaondoka zangu kwenye mihangaiko yangu nikipanga kurudi jioni ili baba anipe habari njema. Ooh sikukwambia kuwa nilikuwa pia nafanya dizaining ya mitindo mbalimbali ya mavazi kwasababu nilikuwa napenda sana.
Wakati wote nikiwa huko, nilikuwa nawasiliana na mpenzi wangu Brighton mara ya mwisho aliniambia kuwa mshenga wake alishaenda nyumbani kwetu, nikawa naombea tu muda wote baba akubali.
Jioni nikiwa narudi nyumbani nikampigia simu Brighton lakini hakuwa na furaha kabisa, aliniambia kuwa mshenga wake alifukuzwa na posa ilikataliwa baada ya baba yangu kujua kuwa mwanaume mwenyewe ni yeye.
Iliniumiza moyo kama vile mshale ulinichoma. Nilikasirika mno na kurudi nyumbani kwa hasira, nikamvaa baba na kuanza kumpandishia machozi yakinitoka kama mtoto mdogo.
“Baba, kwanini lakini, humpendi Brighton, miaka yote tumekuwa pamoja hajanifanyia chochote kibaya, kwanini lakini humpendi!” nilimuuliza baba akanitazama kwa ghadhabu.
“nini unajifanya umechetuka si ndiyo? Sikia mimi ni baba yako nitahakikisha unaolewa na mtu mwenye uwezo wa kukutunza kama ninavyokutunza mimi hapa, siyo holoipoloi fulani akataka kuwa na wewe ili umlelee, kwani sijui umemfungulia duka! funguka akili mpumbavu wewe!” alisema baba. lakini sikumsikiliza.
Nilikasirika mno, na sasa niliamua kufanya jambo ambalo nilijua kama nikifanya basi sitaweza kurudi nyuma tena. Kwa mdomo wangu nikafungua kinywa changu na kusema: “Baba, unaruhusa kunishauri na kuniamrisha chochote, lakini si kunipangia maisha yangu na eti niwe na nani? Nampenda Brighton na hakuna wa kututenganisha hata wewe hautaweza.”
Niliposema maneno hayo baba alinitazama kwa mshangao, mama yangu wa kambo naye alikuwepo pale na wadogo zangu, mama akanionya kuwa nimemkosea baba yangu nimuombe msamaha lakini sikujibu chochote zaidi nikaongeza kuharibu.
“Pengine mama yangu angekuwa hai, asingenipangia mambo haya kama wewe, baba wewe ni dikteta,” nilisema nikaingia ndani kwangu na kuchukua vitu vyangu nikaweka kwenye begi na kuondoka. Wakati napita sebuleni baba alisimama na kuniambia: “Ninah ukivuka huo mlango usirudi tena hapa!”
NINAH 04
Nikaenda mlangoni na kuvuka nikasonga mbele; “ndiyo sitaki kurudi tena.”
Niliposema hivyo nikasikia huko nyuma akinilaani; “tutaona! unawajua wanaume unawasikia, utarudi hapa wewe mpumbavu punguani.. kuanzia leo mimi siyo baba yako!”
Wakati huo Nikiwa na hasira kupita maelezo nikampigia simu Brighton, aliposikia nilichokifanya yeye mwenyewe alinipinga mno na kuniona nimekurupuka, lakini nilikuwa na kiburi cha ndani kwa ndani, nikamhakikisha kuwa laana ya baba ni sawa na debe tupu na haitatufika.
Basi nikaelekea alipopanga Brighton na hapo ndiyo nikaanza kuishi naye rasmi kama mume na mke, ndiyo ilikuwa hatari lakini hatari ndiyo ilikuwa utamu wa penzi letu.
Tukiwa pamoja sasa tulipanga kila kitu vizuri na maisha yalituendea, tena Brighton aliniona kama vile nimekuja na bahati maana siku mbili tu baada ya ujio wangu aliitwa kwenye interview ya kampuni ya DStv kwenye kitengo cha masoko, ‘Marketing’ na kupita, akipangiwa mshahara wa shilingi laki sita na allowances za kwa mkataba wa awali.
Ilikuwa ni furaha mno, na mimi nikawa sasa naenda kule dukani, yeye akiwa anaenda ofisini kwake.
Maisha yalikuwa ya furaha kiasi kwamba kwa miezi michache nasi tulikuwa watu katika watu, nilitamani baba anione sasa ninavyoishi, na pengine amuone mwanaume aliyemdharau kuwa na mimi akiwa mtu kati ya watu.
Kwa muda mfupi tulinunua kiwanja na kuanza kujenga nyumba yetu wenyewe huko Msata. Lakini wakati huohuo tulipanga mengi mno, ikiwemo kuoana hata bomani na kumzalia Brighton.
Lakini kabla ya hayo shetani alishuka na kutupima penzi letu kama anavyopima kila mapenzi ya watu wanaopendana. Maana huja na agenda ya uaminifu, magonjwa, migogoro ya kila mtu kutaka awe juu ya mwenzake, umasikini, kuchokana na mengineyo mengi.
Kwetu nadhani alitushindwa kwa vyote, lakini akaja na mtihani huu mdogo, uliohatarisha penzi letu na Brighton na kuniacha na somo kubwa mno ninalotaka na nyinyi wasichana wenzangu mjifunze kupitia mimi.
Tulia hapohapo stori ndiyo kwanza inaanza.. muite yule na yule..
NINAH 05
Nakumbuka siku hiyo ilikuwa kama kawaida, Brighton wangu alirudi kutoka kazini kwake, akionekana na furaha mno akiwa na habari njema, aliniambia kuwa kazini kwake amechaguliwa kama mfanyakazi bora wa mwezi. Tena akaniambia kulikuwa na sherehe ya kujipongeza ya wafanyakazi wote wikiendi ijayo, na uzuri sasa aliniambia kuwa kila mfanyakazi alitakiwa kufika na patna wake.
Nilifurahi mno kusikia hivyo, maana nakumbuka mara ya mwisho kutoka na Brighton kwenda kwenye sherehe sijui hata ni lini. Hiyo kutokana na maisha ya ubize na kukosa ndugu tulikokuwa nako. Maana mimi na baba yangu tulitofautiana na hata mashangazi nao hawakunishirikisha chochote, hivyo hata kwenye sherehe zao sikuwa nahudhuria labda kama misiba itatokea nitaenda.
Kwa Brighton naye ndiyo kama mimi tu, alikuwa na ndugu wachache mno, na wengi siyo wakazi wa Dar, kwa bahati mbaya zaidi hakuwa na baba wala mama wote walishafariki na mimi ndiyo alikuwa akiniita mama yake. Nafurahi kuwa tulizo lake.
Sasa hiyo sherehe ilinichanganya mno, kiasi kwamba nilipanga kuonekana nadhifu mno na katika ubora wangu, tena kwa kuwa nilijua kila vazi hapa mjini na bei yake kwa kuwa mimi mwenyewe ni mbunifu wa mavazi, nikajiapiza siku hiyo nitamfunika kila mtu kwenye hiyo sherehe yao. Labda nisiwe mzima.
SIku zikawa zinasogea taratibu na mimi nikawa nazidi kuisubiria kwa hamu hiyo sherehe, nikipangilia nguo zangu na kuzipangua kila siku, Brighton aliona hangaika yangu, akawa ananicheka tu.
Nakumbuka ilikuwa siku ya Alhamisi yaani siku moja tu kabla ya sherehe yenyewe iliyopangwa jumamosi pale Golden Tulip Hotel, Brighton akaniambia kuwa ofisini kwao yeye na rafiki yake Ali walikuwa na ubishani mzito kuwa couple gani ya wapenzi watafunika sherehe hiyo. Akanimambia rafiki yake mwingine ambaye ni mfanyakazi mwenzao Imelda alitamba kufunika kila mtu akiwa na bwana ake mnyanyua vyuma Geofrey.
Kusema kweli hao wote siwajui na Brighton hakuwahi kunitambulisha lakini nilijiamini kuwa hawataniweza nikiwa na Brighton wangu.
NINAH 06
Nilicheka kwa kebehi kwa sababu nilijijua mimi nikipendezaga ni habari ya mjini, nikamhakikishia mume wangu sisi ndiyo tutakaofunika. Basi nikamuandalia nguo zake kuanzia usiku huo hadi kesho yake kila kitu kilikuwa sawa.
Kumbe wakati napanga yangu na shetani naye alikuwa akiyapanga yake! Loh laiti kama ningejua nisingeenda kwenye sherehe ile.
Ngoja nikusimulie sasa. Siku hiyo niliwahi kwenda saluni kutengeneza rasta vizuri, nikarudi nyumbani nikiwa nimesafisha kucha zangu, nimepaka rangi na kufanya facial, nilihakikisha nimewaka kila kona.
Jioni hiyo mume wangu Brighton aliwahi kurudi kutoka kazini akanionesha na kadi ya mualiko, na alionekana ana furaha mno zaidi yangu.
Basi na mimi nikiwa na shauku nikaanza kumuonesha nguo zangu nilizoziandaa nikaingia chumbani na kumwambia anisubiri sebuleni, nikaingia chumbani nikaanza kuvaa lile gauni la nguva off sholder (mabega wazi) lililotengenezewa matirio ya Velvet lenye rangi machanganyiko tena nilizozidizaini mwenyewe kwa kuzifanya kama vile zina crazy colour, mabegani nikaweka staili ya Halter yaani vikamba vilivyopita mabegani na kufungia shingoni..
Nikajiangalia kwenye kioo aisee nikajiambia mwenyewe: “Ninah wewe mzuri,” nikatoka ili Brighton anione tena hapo sikuwa hata nimepaka lipstick yangu ya dola 30, wala kuvaa high heels zangu za Ruby slippers .
Tena sikupaka Make up, iasee we acha tu, nikatoka hivyohivyo nikaelekea sebuleni, Brighton alikuwa amekaa zake akiangalia tivii bila wasiwasi. Aliponiona alishtuka mno, nikageuka kuanzia mbele nikageuka nyuma nikajifanya natembea kimiss na kuweka pozi za Milen Magesa.
Nilipendeza hata yeye mwenyewe aliona hilo, akanitania: “Mh! waifu unataka uharibu sherehe sasa! Kwani ugomvi?” alisema. Nikacheka tu na kumvuta ndani, nikamjaribisha suti zake wote tukajiangalia kwenye kioo, mimi nilikuwa ni kama ua zuri yeye alikuwa akipata marashirashi kutoka kwangu, hivyo wote tulionekana tunapendeza.
Nikamkumbatia na kujifanya tunacheza bluuzi pamoja,yeye akanishika kiunoni na mimi nikamshika mabegani. Ilikuwa ni furaha mno, bado kizani shetani alikaa tu pembeni akituangalia, maana alipanga kunitumia baadaye. Najuta! Kaa hapohapo.
NINAH 07
Haya basi siku yenyewe ilifika nikiwa na kimuhemuhe balaa, mpenzi wangu Brighton siku hiyo akanionesha picha mtandaoni za huyo mfanyakazi mwenzake Imelda akiwa na nguo alizozinunua siku hiyo, nikazitazama zote nikaona ni za kawaida tu. Tena nilipooneshwa shepu yake ya epo yaani katikati mkubwa chini mdogo, nikaona hataniweza kwa chochote kwenye sekta ya mavazi.
Sasa nilipotazama vizuri ndiyo nikagundua katika nguo zake alikuwa na mkufu mzuri, mama yangu nilisahau. Na mimi nataka mkufu mzuri, tena unaoendana na rangi ya nguo yangu aidha uwe wa bluu au mwekundu.
Mh hapohapo nikamkumbuka mtoto wa shangazi yangu, Rose ambaye japo kuwa shangazi aliniwekea bifu kutokana na uamuzi wangu wa kugombana na baba kisa mwanaume, Rose alikuwa akipiga stori na mimi mara kadhaa.
Yeye kwa bahati nzuri aliolewa na mzee mmoja mwenye hela zake, kwa hiyo kwake kulikuwa poa, alikuwa na hela kuanzia kwao hadi kwa huyo bwana ake. Sasa nilijua tu atakuwa na kidani kizuri cha kuweza kuniazima kwa siku moja nikauzie sura na kufunika jioni ya siku hiyo kwenye hiyo sherehe ya akina Brighton.
Kama unakumbuka nilikwambia shetani muda wote huo alikuwa amejificha sasa alichomoka na kunishawishi niichukue simu yangu nimpigie Rose. Nikampigia na kumwambia shida yangu, tena nikamwambia nataka mkufu wa rangi gani.
“Mh Ninah necklace nzuri yenye rangi unayoitaka ni ya mama, na akijua nimekupa wewe itakuwa soo, lakini nitakuibia na ukimaliza tu kesho nirudishie, kwani unaenda shereheni saa ngapi?” aliuliza Rose.
“ni saa kumi na mbili ndiyo tunaondoka hapa nyumbani,” nilimjibu.
“oooh kama saa kumi na mbili basi nitakuwepo hapo hata usijali, maana hata mimi mwenyewe nitapita hapo kuelekea mjini” alisema Rose.
Muda ulipofika kweli Rose aliniletea ule mkufu, katikati ulikuwa na kijiwe kizuri chekundu, ilionekana ni Ruby halisi huku uzi wake ukiwa ni wa dhahabu. Rose alizungumza kidogo na Brighton kisha akaniaga na kuondoka zake akiwa na gari yake nzuri aina ya Rav 4.
NINAH 08
Basi nikaingia ndani na kuanza kuvaa, wakati huo Brighton yeye alikuwa tayari ameshamaliza zamani, si unajua wanaume tena, wanavaa kama wanakimbizwa, dakika moja tu kamaliza. Sasa mimi ndiyo nilikuwa navaa taratibu, nilipomaliza nikajimake up vizuri na kumzubaisha maana alikuwa akinipigia kelele kweli huko sebuleni akidai muda umefikia.
Nikajitazama kwenye kioo vizuri, na shetani akanisaidia kunivaa ule mkufu shingoni mwangu kisha akajigeuza mdogo akakaa shingoni mwangu, laiti ningejua.
Basi nikafungua pazia na kutokea sebuleni, Brighton aliponiona alinishangaa huyoo! Hakuamini. Akanisifia mno nilivyopendeza akauangalia ule mkufu na kushtuka, najua alimuona yule shetani sema alizibwa kinywa chake asiseme.
Tukatoka nje harakaharaka, tukapanda bajaji na kuelekea kwenye hoteli husika. Tukaingia pale tukiwa tumeshikana mikono bwana na bibi.
Getini tukaonesha kadi na kuingia ndani, tukipita kwenye bustani fulani. Sasa ndiyo niligundua kuwa tumechelewa kidogo maana tulipofika tu sisi sherehe ndiyo ilikuwa ikianza, lakini sasa cha kushangaza nilipoingia tu, ukumbi mzima ulizizima.
Macho yote yakawa kwangu, sasa nadhani walikuwa wakiniona kwa mara ya kwanza kuwa mimi ndiye Mrs Brighton mzuri wa sura na umbo. Nikatembea kwa mikogo huku nimeshika mkono mume wangu hadi kwenye siti fulani, ambayo ilikuwa ina watu wawili tu.
Nikaona sasa macho yamepungua kidogo, nikakaa pale ndiyo nikagundua kumbe tuliokaa nao mezani hapo ni huyo Imelda na bwana ake, ambaye mume wangu aliniambia kuwa ni mtu wa gym, kweli alikuwa na mwili wa mazoezi na alikuwa nadhifu mno, yaani kwa Imelda na huyo mwanaume walikuwa hawaendani kabisa, yaani bora mimi na Brighton. Loh!
Basi Brightona akanitambulisha pale, Imelda nikamuona akinitumbulia macho kuanzia juu hadi chini, akiwa ananitamani kweli, huyo bwana ake sasa ndiyo alikuwa akijichekeshachekesha hadi akawa anakera maana kila akizungusha shingo, aligeuka kwangu na kunitazama kwa sirisiri.
Shetani naye hakuwa mbali, alitulia vizuri pale kwenye mkufu akisubiri muda wake ufike aniumbue.
Loh! Ningejua njama zake ningeuvua na kuuweka kwenye begi na kumrudishia Rose haraka.
Itaendelea..
NINAH 09
Wakati huo nikamsikia emsii akitutaka tusimame ili mkurugenzi wao na Brighton, ni msauzi Africa aingie hapo ukumbini.
Tukasimama akaingia mtu mzima mmoja hivi, lakini alionekana nadhifu mno, yaani ananukia hela kuanzia utosini hadi unyayoni. Alikuwa na rangi ya kung’aa na alitembea kwa hatua za kukadiria na kujiamini hadi pale stejini kwenye meza kuu na kuungana na wengine.
Baada ya kukaa, yule emsii akawatambulisha meza kuu na kumpa kipaza sauti yule bosi, naye akaongea maneno yake kiswahili cha kugusagusa na kufungua sherehe, vinywaji vikazungushwa na tukaenda kwenye misosi, baadaye sasa ndiyo ilikuwa muda wa mume wangu kupokea nishani zake.
Tena hapo wakaanza kutaja wafanyakazi mbalimbali na sasa akatajwa mume wangu kwenye kipengele cha mfanyakazi bora wa mwezi, akasimama na kutembea harakaharaka akawapa mikono viongozi wake wote na kuchukua shahada iliyo kwenye kioo lakini pia alipewa bahasha iliyoonekana kuwa imenona.
Nilipiga makofi kwa nguvu kuliko watu wote humo ukumbini, sasa mume wangu akapewa nafasi ya kushukuru watu, basi Brighton alivyo na mapenzi ya dhati akaanza kumshukuru Mungu, kisha akasema:
“nishani hii pia ni kwa ajili ya mke wangu mpendwa, Ninah, umekuwa msaada mkubwa kwangu ukiniamini na kunipa moyo tangu mwanzoni. I Love u Ninah!” alisema, ikabidi emsii atake nisimame kulekule kwenye kiti, nikasimama kidogo nakukaa, nikiacha tafrani maana kila mtu alinizungumzia na mimi nikajishongondoa kwa kujifanya nazitupia rasta zangu upande mwingine wa uso.
Basi baada ya hayo yote, ukafika wakati wa kufungua muziki, eti emsii sasa akataka msichana aliyependeza kuliko wote humo ukumbini akafungue mziki na bosi wao akina Brighton, Mr Edgar, basi emsii alivyomchokozi akaacha wote akaja hadi kwenye meza yetu, akaninyanyua, nikamtazama Brighton. Brighton akatabasamu na kunipa ruhusa ya ishara.
Nikasimama na kutembea taratibu na viatu vyangu virefu na mwendo wangu na jinsi nilivyo, aisee najua wengi walijing’ata huko kwenye viti. Basi nilipofika pale dj akaweka wimbo wa Oliver Ngoma unaoitwa Adia (kama haujawahi kuusikia udownload maana ni fujo loh!).
NINAH 10
Akanivuruga mno, maana wimbo huu niliupenda kiasi kwamba nilishamwambia Brighton kuwa kwenye harusi yetu tutacheza wimbo huo.
Kwa uoga na aibu nikamsogelea yule bosi nikacheza naye kwa distansi tukitazamana maana niliogopa kumgeuzia wowowo. Tukacheza kidogo yule Mr Edgar akinitazama kama nini, lakini uzuri ilikuwa ni dakika chache tu emsii akawaita watu waje pale mbele kujiunga nasi.
Wakati huo nikamuacha yule bosi, japo alining’ang’ania kweli, akaniuliza kwa kiingereza eti kama kweli Brighton ni mume wangu, nikamjibu kuwa ni kweli, nadhani alishangaa kuona hatuendani, lakini sikujali.
Nikarudi na kumtafuta Brighton kwenye kundi la watu lakini kabla hata sijamfikia nikavutwa na yule mwanaume wa Imelda tena dijei kama alijua kunikomoa maana alipiga ngoma ya Joe Thomas. I believe. Maana yake ilikuwa lazima tucheze kwa karibu.
Mwanaume huyo mwenye misuli akanivuta na kunituliza kifuani kwake, sikuweza kujitoa haraka, nikaona ngoja nizuge naye dakika chache niachane naye nimtafute Brighton wangu, lakini na yeye alikuwa akitumia dakika hizo chache vizuri maana si kwa kunichambua kule.
Nilijitoa haraka na kumuona Brighton akiwa na glasi ya pombe akiibugia kuonekana amekasirika mno. Nikawa namfuata ili nimtoe hofu, lakini mara kundi la wakina mama wakiongozwa na Imelda wakawa wamekuja pale kuanza kunisifia nilivyovaa na kunitaka niwaelezee mavazi yangu wengine wakinikagua hadi rasta na kuziulizia, basi nikawalekeza duka langu lilipo na kugawa bizinezi kadi zangu.
“Brighton, amka twende nyumbani,” nilimuamsha Brighton aliyelala kwenye kiti, akionekana kukolea pombe. Wakati huo ukumbini watu walikuwa wakianza kutoka mmoja baada ya mwingine.
“saa ngapi?” aliniuliza, nikaangalia na kumwambia ni saa saba usiku.
Tukatoka kwa mguu hadi nje tukitafuta bajaji, lakini kwa bahati mbaya, zilikuwa zimejaa hivyo tutembee hadi kule mbele zaidi. Tukatembea hatua chache lakini shingo yangu nikaiona ikiwa nyepesi. Nikashtuka ule mkufu sikuwa nao.
Kumbe muda mrefu yule shetani, aliondoka na ule mkufu na kuchukua fimbo yake akanipiga nayo mapigo saba, Najuta
“Brighton, mkufu wangu siuoni?” nilisema nikianza kujisachi hadi kwenye mkoba.
“unasemaje?” alishtuka Brighton akinitazama vizuri shingoni.
“mkufu wangu siuoni?”
“Si ulikuwa umeuvaa wewe muda wote?”
“ndiyo sasa hivi nashangaa siuoni, naomba turudi tukaangalie mle ndani,” nilisema nikiwa nimeanza kuchanganyikiwa.
“si ulikuwa ukicheza sana, utakuwa umedondoka mle ndani labda,” alisema Brighton, tukiwa tunarudi nyuma huku tukitazama njia nzima tukimulika na vitochi vya simu yetu.
“ndiyo ule mkufu aliokuletea Rose?” aliuliza Brighton.
“ndiyo .. tena alimuibia shangazi Magreth, ili aniazime mara moja, na shangazi akijua sijui nitafanyaje, na Rose alisema ataupitia kesho, jamanii,” nilianza kulia lakini ilikuwa too late.
Tukaingia mle ukumbini tena, wakati huo tukaona wale wafanyakazi wa hoteli wanakunja viti na kusafisha fujo tuliyoifanya ikabidi Brighton awaulizie, wote wakaanza kutafuta mle ndani tena na mimi nikiwemo lakini hakuna chochote tulichoambulia.
Brighton akaacha na namba ya simu na kuchukua namba ya mkubwa wao ili mradi tu wakiuona watupe taarifa.
Sasa ilikuwa ikikaribia saa tisa usiku, tuliondoka tukiwa wote tumeshuka moyo, tulirudi nyumbani, sasa nikawa naanza kubabaika hovyo, nikimhisi pengine yule mume wa Imelda ndiyo alipocheza na mimi labda aliniibia. Lakini hapana nilivuta kumbukumbu kuwa nilipomaliza kucheza naye nikakutana na wale wakina mama nikiwa na ule mkufu.
“naona leo umeenjoi si ndiyo?” alisema Brighton akiwa ametoka kuoga akionekana hana wasiwasi, wakati mwenzie nilikuwa bado nimechanganyikiwa nikiuwaza ule mkufu.
“una maanisha nini!?” nilisema kwa hasira. Brighton akameza mate na kunifuata akanikumbatia kwa nyuma akinibembeleza kuwa nitoe wasiwasi kama umepotea ule mkufu tutaenda kuulizia dukani mapema kesho asubuhi ili Rose akija jioni tumpe mkufu ule tutakaoenda kumnunulia.
Basi nikaona ilikuwa sahihi zaidi, nikachukua picha za selfie kwenye simu nilizopiga tukiwa kule shereheni zikionesha ule mkufu na kuona ni rahisi kwenda nazo dukani hiyo kesho na kumuonesha muuzaji ili tuununue.
Basi nikaenda kuoga na mimi na kurudi kulala, ubaya wa Brighton akionja lazima usiku anisumbue.
NINAH 12
Nikampa kimoja cha kulalia, na alikuwa hata hivyo anastahili kupewa pongezi kutoka kwangu kwa kazi nzuri huko ofisini kwake.
Tulilala hadi saa tano asubuhi. Tulipoamka baada ya kunywa chai, zoezi la kwanza ni kwenda mjini kuulizia ule mkufu, tulienda Posta mtaa wa Aggrey kule kuna maduka ya vito mengi mno. Tulipofika kwenye duka moja tukamuonesha muuzaji ile picha yangu nikazoom hadi kwenye ule mkufu alipouona akashtuka na kutuitia sonara wa kihindi.
Alipoangalia akatuambia ule mkufu haupo kwenye showcase, zaidi alisema anaweza kuutengeneza, akapiga hesabu kuwa katikati una rubby na dhahabu kwenye uzi wake, bei yake ni shilingi milioni 78.8. aliposema hivi, tumbo la kuhara lilinishika. Brighton akaniinua na kuniweka kwenye kiti.
“unasema?” aliuliza Brighton jasho likimtoka.
“huo mkufu, dhahabu yake nakadiria ni gram 35 ni shilingi laki 8 na hiyo ruby kwa ukubwa huo itawakost shilingi milioni 69 na ufundi wangu kuuchonga huo mkufu kama ulivyo, hapo itakuwa ni shilingi laki moja na elfu themanini ndiyo maana nimesema shilingi milioni 78.8,” aliposema hivyo, Brighton alishtuka mno akaaga na kunivuta nje tukawa kama hatujamumini yule sonara maana alitaja milioni 78.8 kirahisi kama anataja bamia na kachumbari la mama Ndubikile.
Tukaingia duka jingine. Cha kustaajabisha naye alipishana na yule sonara kwa shilingi laki moja tu tena yeye akiwa zaidi.
Jasho lilitutoka, nikaanza kulia palepale makutanoni.
Tena kufanya mambo yakawa mabaya zaidi nilipoona simu ya Rose inaingia. Nikashindwa kupokea. Nikamtumia meseji kuwa nimepata dharula ya msiba wa ndugu yake Brighton. nikamuomba tuonane kesho kutwa ili nimpe ule mkufu. Maana nilijua tu hapo alikuwa akitaka kuupitia hiyo jioni.
“Ninah, tulia.. naomba utulie, sikia twende nyumbani kwanza, kesho nitaenda kuulizia tena kule ukumbini na wafanyakazi wenzangu wa ofisini, umesikiaeeh mama,” alinibembeleza Brighton tukapanda bajaji hadi nyumbani, sasa nikamuona wazi shetani mbele yangu akaniona na kunicheka mno.
Akasema: “nitakukomesha sasa!”
ITAENDELEA
Ninah Sehemu ya Pili
Also, read other stories from SIMULIZI;