Ninah Sehemu ya Pili
IMEANDIKWA NA: CHANDE ABDALLAH
********************************************************************************
Chombezo: Ninah
Sehemu ya Pili(2)
Loh ungekuwa wewe Ninah ungekuwa katika hali gani?
Itaendelea.
NINAH 13
Tulienda nyumbani, Brighton akajitahidi kunibembeleza kwa kadri alivyoweza, lakini nilikuwa nimechanganyikiwa mno, kilanga chote kiliniisha, tena nilikonda kwa siku moja tu.
Nikawa najiuliza mwenyewe kila siku; “Hivi ningekosa nini kama nisingeazima ule mkufu?” lakini sikupata jibu zaidi ya kuamini kabisa kulikuwa na nguvu za kishetani zilizonipelekea mimi kufanya kila kitu nilichokifanya hadi kuazima ule mkufu.
Basi nikawa naombea tu Brighton akienda kazini kwake apate taarifa kuwa ule mkufu umepatikana, la sivyo hali yangu itakuwa mbaya zaidi.
Asubuhi Brighton alijiandaa kwenda kazini kwake, tena palepale alianza kwa kuwapigia wale watu wa hotelini waliosema kuwa hajaona chochote, sasa tumaini likawa ofisini kwa wafanyakazi wenzake. Najua tu huko ofisini kwao nitakuwa ndiyo habari ya mjini na watamsifia Brighton kuwa na mke mzuri kama mimi, lakini sitajali kuhsuu hayo nitajali kuhusu ule mkufu maana bei yake ilinizungusha kichwa mno.
Nikiwa hapo nimekaa natafakari, mara simu ya Rose ikaingia tena, sasa sikuwa na sababu ya kutopokea, nikaiweka sikioni na kusikilizia.
“Hallow, cousin vipi msiba?” aliuliza Rose nikajikuta nakumbuka sasa maana hata nilishasahau kama jana nilimdanganya kuwa Brighton amefiwa.
“Ooh tumemaliza vizuri ndo tunarudi leo nyumbani, niambie?” nilisema kwa wasiwasi.
“Okey nimepatwa na dhalura, mimi na shemeji yako tunataka kwenda Dubai jumatatu, sasa kesho nitakuwa shopping, sijui kama nitaweza kuja kuichukua ile necklace? Lakini kama nitashindwa itabidi niifate jumamosi, si umeona ilivyo nzuri eeh..” alisema Rose. Nikaitikia kiunyonge nikimlaani na kumtukana kimoyomoyo kama alinilazimisha anipe ule mkufu kumbe kiherehere changu, hata hivyo nikaona afadhali hizo siku tatu nipate nafasi ya kuutafuta.
“Mh huko Dubai ukienda njoo basi hata na baibui, na mimi niingilie shughuli za Kiislamu,” nilisema kwa kujilazimisha. Rose akacheka na kuahidi ataniletea kisha akakata simu.
NINAH 14
Nilizunguka ndani kwangu kichwa kikiniuma, nikaona Brighton anachelewa nikampigia simu kumuuliza kulikoni?
“Mke wangu nimeuliza lakini hakuna hata mmoja aliyeuona, tutakuja kuyaongea hukohuko nyumbani,” alisema na kuzidi kunikata maini.
Nitafanya nini? nilijiuliza lakini nikaona nyumbani siyo suluhisho, nikaenda dukani kwangu siku hiyo sikuwa na mudi hata kidogo, nikamuwazia shangazi yangu alivyo na gubu, loh halafu ajue eti nimechukua mkufu wake halafu nimeupoteza. Nitakoma.
Nikajiapiza nitafanya chochote niurudishe. Sijui niende kwa mganga? Mh nasikiaga tu sijawahi kwenda naogopa, ngoja tu nimsubiri Brighton.
Kweli jioni Brighton alirudi na kuniulizia kuhusu Rose, nikamtaarifu kuwa atafika kesho kutwa kuuchukua huo mkufu kwa kuwa jumatatu ana safari ya kwenda Dubai.
Brighton naye akaonekana kuchanganyikiwa kama mimi.
“Sasa tufanye maamuzi magumu, maana hata mimi sitaki kupata aibu kwa kushindwa kurudisha huo mkufu, cha msingi tuingie hasara ya mali zetu, Mungu alitupa, atatupa tena,” alisema Brighton akitazama chini kwa uchungu.
Loh! nilikataa katakata, maana nilianza kupiga hesabu, duka langu mtaji wangu wa milioni 6, nikajumlisha hela zetu benki nadhani hazizidi milioni15, nikajumlisha na kile kibanda chetu tunachomalizia kule saiti, kinachogharimu kama milioni 32, na hizo zote bado, maana jumla yake ni milioni 53 tu hapo bado kumalizia hizo milioni 25.8 . Mungu wangu, tunafanyaje, tena malengo yetu! maisha yetu yatakuwaje? Halafu mimi ndiyo nimesababisha yote hayo. Nililia mno Brighton akaja kunibembeleza.
“mke wangu, usijali, tutafight tutapata kila kitu kama awali, Mungu ana makusudi yake, kumnyanyua shetani atujaribu, tunatakiwa kushinda, tukiupita mtihani huu tumeshinda kila kitu,” alisema Brighton, nikajifuta machozi nikamkumbuka baba laiti kama nisingegombana naye, angenipa hela zaidi ya hiyo, lakini kwa kuwa niliamua kufanya nilichokifanya siwezi na ni aibu kurudi kwake tena.
“Sasa, itabidi nikubali kuuza vitu vyetu vyote kama Brighton alivyoshauri, kisa mkufu tu. Shetani mfyuuuuuu! Na kama una mama. **mamko!”
NINAH 15
“Yote hii kwa sababu yangu Brighton, naomba nisamehe sana, mpenzi wangu, nisamehe,” niliomba radhi na kupiga magoti, lakini Brighton alikuwa jasiri, alikuwa akinitazama kama vile hakuna kitu kilichotokea. Ama kweli Mungu ana kusudi lake kuwafanya wanaume kuwa majasiri kiasi hicho, na hiyo ilinipa matumaini nikajiegesha kwa Brighton kwa lolote maana ndiye alikuwa mhimili wangu.
Tukaanza kupiga hesabu, mali zetu, tukapata jumla hiyo milioni 53, akafungua ile bahasha aliyopewa jana, ilikuwa imeandikwa cheque ya milioni tatu, akatazama balansi yake ya Benki kupitia simu akaniambia alikuwa ameanza kuweka kihela cha kutaka kununua gari la sapraizi kwa ajili yetu, ilikuwa ni milioni 6 na pointi hivi.
Yote haya alikuwa akiyafanya bila kujuta bila kupepesa macho, akaingia kwenye begi lake akafungua na kutoa bahasha na kuweka mezani, ilikuwa ni ya mkopo benki akitaraji kukopa kiasi chochote kitakachokuwa kimebakia kwa dhamana ya ofisi yake.
Tena sasa tukaitazama hata nyumba tuliyokuwa tumepanga, kwa ule upande wetu chumba na sebule tulikuwa tunalipa laki moja na nusu kwa mwezi kama kodi, na mwezi ujao tulitakiwa tulipe kodi ya mwaka mzima ujao. Hapo maana yake palikuwa hatupawezi tena. Ilikuwa lazima twende uswazi, kwenye kodi ya elfu hamsini hadi arobaini.
Brighton alifanya hesabu zake vizuri mbele yangu huku kila anachokisema kikiniumiza na kuninyong’onyesha, lakini ili kulinda hadhi yetu, ilitupasa tufanye haraka mno kesho ikifika tayari tuwe na la kufanya.
Basi wakati huohuo, Brighton akapiga simu kwenye zile ofisi za sonara, tulioonana nao jana, kwa kutumia namba zilizokuwa kwenye bizinezi kadi yao aliyotupa na kuwasiliana nao moja kwa moja. Akawaambia waanze na kazi ya kuchonga ule mkufu na kuwaambia kuwa tunataka huo mkufu siku gani, tena akatuma na picha zangu nilizoonekana nimevaa ule mkufu ili aigilizie bila kukosea kitu.
Katika maongezi yao yule Mhindi alitaka atumiwe advansi ili aanze kazi hiyo haraka mno ili mpaka kesho kutwa iwe tayari.
NINAH 16
Hapo ndiyo wakawa wamekwazana kidogona Brighton aliyekuwa akilazimisha yule Mhindi aanze jioni hiyohiyo ili yeye ampitishie fedha kesho.
Wakashindana kwa muda lakini hatimaye Brighton akaamua jioni hiyohiyo zege lisilale akaondoka pale na pikipiki hadi Posta na kumpa yule sonara advansi ambayo ilikuwa ni robo ya fedha na kumwambia aanze kazi.
Nilikwambia Brighton ni mcheshi, lakini siku hizo zilikuwa ngumu mno kwake nikawa najitahidi kama mwanamke nicheze sehemu yangu, hasa kumpetipeti na kuhakikisha hawi chizi kwa ajili yangu.
Basi haraka ndani ya siku mbili, alipata mkopo kazini tena kwa kusingizia mimi naumwa, nahitaji kufanyiwa oparesheni, tukafoji na mavyeti ya kansa na ushenzi kibao. Wakati huo duka langu na nyumba vyote vilikuwa rehani, kwa yule sonara,. Tuliyempa tayari nusu nzima ya hela na nusu nyingine ikiwa katika mfumo wa mali zisizohamishika yaani hiyo nyumba yetu na duka langu.
Hadi hapo, yule sonara alifanya kazi kweli ndani ya siku mbli alitupa mkufu yaani ukiwa kama kaupiga copy na paste. Tena alifanya tu ile kazi kwa kutuonea huruma, wakati anatukabidhi alimuuliza mume wangu kilichotukuta hadi kufikia hatua ya kumuwekea dhamana vitu vile, lakini Brighton alikuwa hawezi kuongea.
Tuliondoka dukani kwa sonara, yeye akiwa ameubeba ule mkufu, tukiwa makini mno. Mimi niliogopa hata kuushika maana usije ukadondoka tena halafu mimi ndiyo nikaonekana nimeupoteza tena.
Tulirudi nyumbani sasa nikampigia simu Rose aliyekuja nikamkabidhi akaondoka nao, ingawa alikuwa akiniuliza maswali mengi baada ya kuona hali yangu nikiwa kama nimechanganyikiwa hivi.
Sio siri niliumwa, na Brighton aliumwa zaidi. Tulirudisha mkufu wa watu, sasa tulilitua zigo, lakini tulikuwa na mzigo mwingine, maana Brighton alikuwa na mkopo aliotakiwa kuulipa na tulitakiwa wakati huohuo tukomboe mali zetu, japo kuwa haikuwa hela ndefu sana kama tungekuwa nayo, maana tulipiga hesabu na kugundua tulitakiwa kulipa kama milioni 12 hivi kila kitu kirudi kwetu, lakini wakati huo hatukuwa na hela hata kidogo.
Itaendelea..
NINAH 17
Sasa mbaya zaidi, tulikuwa na baki ya shilingi laki tatu tu, tena kwenye tigopesa yangu, hiyo sasa ndiyo ilitakiwa kutuendeshea maisha. Asikwambie mtu, siku iliyofuata nikaenda mwenyewe kutafuta chumba Tandale. Tukapata chumba cha giza. Yaani ambacho hakina umeme kwa shilingi elfu 35 kwa mwezi. Nikalipia miezi sita.
Tukaanda kuchukua mizigo yetu na kuelekea huko uswazi. Maisha yalikuwa magumu mno hadi ikabidi niuze baadhi ya vitu vyangu, ikiwemo Iphone 6 yangu, dressing table, cheni zangu na heleni za dhahabu, nguo zangu baadhi. Nikaishia kuvaa madela tu, ama kweli sikutarajia kuishi maisha hayo hata siku moja.
Tena kwa huko uswazi ni ngumu kuishi kwa kunata kama nilivyokuwa nikiishi mwanzoni, ili kuishi kirahisi lazima uwe na marafiki, uzuri nikawapata wengi tu tena micharuko ya kufa mtu, lakini nikajitahidi kuishi kwa adabu na kuweka heshima kwa mume wangu.
Hapo nikapata akili ya kuwa na choma vitumbua asubuhi na jioni nikawa nakaanga miguu ya kuku. Yaani kihivyo nikawa tayari mwanamke wa uswahilini. Wakati huo mume wangu, akawa akirudi kazini anapitia kuchoma chipsi barabarani kwenye kibanda alichokifungua hadi usiku mnene, akirudi analala kidogo na asubuhi anapaswa kwenda kazini tena.
Wakati huo pale nyumbani tuliandaa kibubu kikubwa. Ikawa kila tukipata hela za biashara tunatumbukiza tukijitahidi zifike hizo milioni 12, ilikuwa ni kichekesho maana siku nyingine tukawa tunapigika mno hadi tunavunja kibubu na kuchukua hela hizohizo kwa ajili ya matumizi.
Yaani kusema kweli nilizeeka, uzuri wangu nikashuhudia ukiwa unapotea taratibu. Nilipigika asikwambie mtu na kila siku ijayo ilikuwa afadhali ya jana. Kuna kipindi tulikula mkate siku tatu na maji lakini sikusema kwa baba wala kuomba poo kwa ndugu zangu maana ni aibu.
Kwa maisha hayo si mimi wala Brighton aliyekuwa hata akikumbuka kuna kitu kinaitwa mapenzi. Tulikuwa tu kama mtu na dada yake. Akirudi kivyake na mimi kivyangu na yeye anapolala mimi naamka.
NINAH 18
Siku moja isiyokuwa na jina, nilipokea simu kutoka kwa mtu fulani nisiyemjua, aliongea kwa Kiingereza fulani hivi, akijitambulisha kuwa ni bosi wa Mume wangu, Mr Edgar. Haraka nikamkumbuka kuwa ndiyo yule niliyechezaga naye siku ile shetani ananipiga. Nikashangaa namba yangu aliipata wapi?
Alinitoa hofu na kusema anahisi mume wangu hayupo sawa kazini, nilipouliza kivipi, alifafanua tu kuwa amekuwa akilala ofisini na kukosea mahesabu mengi mno. Akahisi pengine kuna jambo limetokea nyumbani kwetu ambalo labda limemtoa kwenye umakini Brighton. lakini bosi huyo alienda mbali zaidi akataka tuonane eti tuzungumze sisi wawili tu kuhusu mustakbari wa mume wangu.
Nilimkubali tukapanga siku, lakini nilipanga kumyeyusha huyo bosi maana alinitisha pale aliponiambia kuwa nisimwambie mume wangu na kuahidi kuwa atanifurahisha pindi nikienda.
Usiku Brighton aliporudi nilijitahidi kumtaka awe anapumzika na mimi kwenda kukesha kwenye kibanda chake cha chipsi, lakini alikataa katakata na kunitaka nitulie akiamini yeye ni mwanaume na hilo ni jukumu lake.
Alfajiri nikiwa bize na pilikapilika zangu sokoni, simu yangu ya tochi iliita nikapokea na kukumbuka kumbe ni namba ya bosi wake mume wangu; nikaipokea na kuongea naye ndiyo nikakumbuka kuwa ni siku ile aliyotaka nikaonane naye. Akanitajia sehemu ya kukutana naye na muda, kama nilivyohisi, eti aliniambia tukutane hotelini na alitaka kama kawaida nisimwambie mume wangu.
“Huyu mpuuzi, ngoja akae zake huko peke yake,” nilijisemea kimoyomoyo nikaendelea kugombania utumbo na miguu ya kuku sokoni nikiwa sambamba na wakina mama wengine maana nikiikosa asubuhi hiyo sitaipata tena.
Nikiwa nyumbani jioni nampikia Brighton, nilipokea meseji kutoka kwa yule bosi, ikiwa imeandikwa: “Okey let us see!” yaani “Sawa tutaona” nikaipuuzia na kuendelea na mapishi yangu.
Siku ikapita, nakumbuka Brighton alienda kazini lakini, alirudi mchana akiwa amechanganyikiwa na bahasha yake mkononi. Akisema amefukuzwa kazi. Kwa mara ya kwanza, Brighton nikamuona anatokwa na machozi. Tena akaniambia stahiki zake zote zimekatwa kufidia mkopo aliouchukua. Hivyo kifuta jasho pekee kilikuwa ni NSSFna hakizidi hata shilingi laki nne.
NINAH 19
Nikajiuliza, hapo tu alivyokuwa na kazi, maisha yalikuwa magumu hivyo, sembuse akiwa nyumbani! Nikajiongeza kuwa lazima bosi wake amemfukuza kazi kisa niligoma kuonana naye. Loh nimefanya nini!
Nililia tena kwa uchungu, shetani akinipiga kwa fimbo yake tena, lakini yote kisa ni ule mkufu. Nilimtazama Brighton kila siku nikamuona matumaini yake yakimuisha na akikaribia kuchanganyikiwa mbele yangu maana alianza kutojipenda na kuwa rafu mno.
Punde akaingia kwenye ulevi wa pombe chafu, akaanza kuwa mgomvi ndani ya nyumba hadi kufikia hatua ya kuropoka mbele za watu kuwa nimemsababishia mikosi.
Nyumba ilikuwa chungu, maisha yalikuwa magumu na mume alikuwa hashikiki akaanza kuwa na visichana vichafuchafu huko mtaani. Sikumlaumu Brighton kwa lolote, maana kiukweli akili yake iligota kufikiria na mimi ndiye mwenye makosa yote hayo.
Siku hiyo jioni nilikuwa nimetoka kwenye biashara zangu za kuuza miguu ya kuku, nilirudi nyumbani nikiwa nimechanganywa na mengi mno, sasa nilipotokea mtaani kwetu tu nikawaona wakina mama kila mmoja ananikimbilia na kunifuata kwa nyuma.
Nikawa sielewi, lakini sikujali, nilipofika nyumbani nikashangaa pale mlangoni kuona viatu vya kike, moyo ukawa unanidundadunda, nikafungua mlango ndani, huwezi amini nikamuona Brighton amelala na mwanamke kitandani. Huyo mdada aliponiona alishtuka na kutaka kukimbia.
Nikamshikilia na kumbamiza kwenye ukuta kama mara mbili, nikamlaza chini na kuanza kumpiga kwa hasira ambazo sijui zilitokea wapi. Wakati huo Brighton alikuwa akinigombelezea na kutaka nisubiri kwanza anielezee. Nikajua anataka tu kujitetea.
Huko nje watu walikuwa wakipiga makelele kushangilia ugomvi, yule dada alitoka mbio nikamkimbiza na kushindwa kujua alipoelekea.
Nikamgeukia Brighton aliyeonekana kulewa bwii.
“Yaani Brighton umefikia kunidharau kiasi hiki cha kuniletea wanawake ndani kwangu! Hapana, hivi wanaume wangapi wenye hela nawakataa pamoja na umasikini wetu huu kwa ajili yako? kumbuka tulipotoka Brighton!” nilisema huku nikiangusha kilio, sikuamini kama Brighton angeniumiza kiasi hicho.
Tatizo ni nini? kisa nimemfilisi? Mbona mimi ndiye niliyemnyanyua mpaka tulipokuwa enzi zile? Kwanini hathamini kujitoa kwangu? “ nilijiuliza maswali yote hayo, sasa nikaona laana ya baba waziwazi ikiniandama.
NINAH 20
Nilikosa cha kufanya na mara hii nikaona ngoja nikapige magoti kwa baba, nipate radhi angalau nirudie maisha yangu ya awali, sikuwa na jinsi wala jinsia.
Nikabeba vitu vyangu, Brighton akiwa ananipigia makelele ya kilevi, eti amekoma ananiomba msamaha mkewe. Mara ooh amenizoea, eti na pombe zake akaanza kulia. Nikamsukumia pembeni huko.
Siku hiyo nakumbuka nilipanda gari hadi Mbezi Jogoo na kuelekea kwa baba, nafsi yangu ikiwa imegota kwa shida, nakawa radhi hata nikiambiwa nipige magoti nitapiga na kumlamba baba miguu, hakika asiyesikia la mkuu huvunjika guu. nikashika njia. Nilifika nyumbani, lakini nilipogonga kengele getini, alitoka mlinzi ambaye sikuwa namfahamu.
“Sema shida yako!” alisema.
“Namuulizia mzee Ernest,” nilisema.
“anhaa mzee Ernest, hayupo amesafiri ameenda kwenye harusi ya mpwa wake, Dubai, wewe ni nani?” aliniuliza yule mlinzi.
“Niaitwa Ninah ni mwanaye, kwa hiyo ndani kuna nani niweze kuongea naye.”
“ooh Ninah nimekuwa nasikia kuhusu wewe, ndiyo wewe mrembo mtukutu! Uliyegombana na wazazi wako kisa mwanaume? Hahaaa. Jamaa alipata zari aiseee!” alisema yule mlinzi akinichungulia vizuri nikajisikia vibaya na kumkazia macho akajishtukia na kusema: “Aah, hapa ndani hakuna mtu hata mmoja, sista hapo itabidi usubiri hadi warudi, au unaweza kusema shida yako nikakusaidia,” alisema yule mlinzi nikatafsiri kama dharau anazonionesha nikaondoka kwa hasira, nikajisemea kimoyomoyo laiti nikirudi nitamfukuza kazi.
Nikajaribu kumpigia Shangazi, naye hakupatikana na ilionekana naye amesafiri pia kuelekea huko huko kumbe ni harusi ya mdogo wake Rose, Magreth.
Nikiwa na mabegi yangu nikatafuta pa kwenda lakini kote sikuwa na msaada, usiku huo nilikuwa naadhirika. Sasa nikaamua kufanya jambo la mwisho ambalo mwanamke anafanya akili yake ikigoma.
Nikanyanyua simu yangu mwenyewe na kutafuta namba za wanaume wote waliokuwa wakinitakaga nikawa nawakataa. Loh nikamkumbuka Mr Edgar nikampigia midomo ikinitetema. “Hallow nakuja tuonane unapotaka.”
“Kama ni kwa ajili ya mumeo, umechelewa!” alisema kwa ukali Mr Edgar.
“Hapana, ni mimi na wewe hotelini.”nilisema nikiwa sielewi ninachofanya.
“Tukutane Protea sasa hivi, chukua teksi nitalipa!” alisema Mr Edgar.
Nilichofanya haraka nikapanda teksi nikafuta machozi yangu na kuelekea Oysterbay huko kwenye hoteli ya Protea kama nilivyoelekezwa na Mr Edgar. Nilipofika nje nikampigia simu alipokuja akashtuka kuniona. Akalipa hela ya teksi na kunichukua hadi ndani, chumbani.
Akanitazama tena, “Ninah nini kimetokea mbona upo hivyo,” Alisema Mr Edgar.
Sasa nikaanza kujishtukia, nikajitazama kwenye kioo cha kabati na kujiona nilivyochunjuka, nimekondeana, vinywele vya mabutu venye vumbi kichwani, kucha zikiwa zimekatikakatika kwa pirikapirika. Ngozi imefifia. Macho mekundu kwa kilio, mashavu yameingia ndani kwa dhiki. Loh nilikuwa nimekomaa! Nikaanza kulia palepale, Mr Edgar akanibembeleza na kuniomba nimuelezee tatizo langu.
Nikamhadithia kila kitu kilichotokea kuanzia mkufu hadi nilivyomfumania Brighton na mwanamke mwingine siku hiyo.
Mr Edgar akaguna tu. Nikafuta machozi, nikaingia bafuni kuoga nikarudi pale kitandani nikiwa sina nguo yoyote. Nikamwambia Mr Edgar: “ulikuwa ukinitaka, nimekuja,” nilisema roho ikiniuma mno sikuamini kama siku hiyo nilikuwa radhi kuutumia mwili wangu kisa hela, lakini kwa kuwa Brighton alinisaliti nikapata nguvu ya kusema ngoja na mimi nilipize.
Basi Mr Edgar akanisogelea nikafumba macho, lakini nikaona anachukua shuka na kunisitiri. Nikashangaa mno. Na kujiuliza ina maana simvutii tena kama zamani au?
“Ninah, naitwa Edgar Khumalo. Nina familia yangu pia huko nyumbani kwetu Kwazulu naipenda sana familia yangu na nimekuwa mume bora na mwaminifu mno kwa mke wangu miaka yote hiyo, lakini nilikuja kugundua kuwa yeye hakuwa muaminifu. Nilifikiria kumuacha lakini alikuwa akiniomba sana msamaha. Nikaona kitu cha kufanya nimpe adhabu lakini siwezi kumuacha mke wangu kwasababu nilijiuliza nikiachana naye wanangu watajifunza nini? lakini pia nitampata nani atakayenivumilia madhaifu yangu kama yeye? Ona tumetoka mbali sana, lakini hiyo haitoshi mimi kumuacha yeye hata siku moja kwa ajili ya mwanamke mwingine,”alisema Mr Edgar na kuendelea.
“Nilimfukuza kazi, Brighton kwa sababu aliharibu mno kazi. Hilo halihusiani na wewe. niseme tu ukweli, nilitokea kuvutiwa na jinsi ulivyo tangu siku ya kwanza nilipokuona kule hotelini. Nilipenda tu ulivyolivyo mzuri.
NINAH 22
“Siku nilipokupigia na kukwambia nataka kuonana na wewe, nilikuwa nimelewa sana na mke wangu na ndiyo niligundua mke wangu ananisaliti. Niliona na mimi nimsaliti pia. Ndiyo nikakutafuta nikiwa sina akili vizuri. Sitaki uwe kama mimi, kufanya maamuzi ya haraka, naamini Brighton aliteleza kutokana na mambo aliyopitia baada ya kupoteza huo mkufu.
“All in all, nataka ujue mwanaume akifikia mwisho wa kufikiri hukimbilia kwenye pombe kama faraja yake, kwenye pombe ndiyo kunazaa matatizo hayo ya usaliti. Usikasirike sana na sitaki hiyo iwe sababu ya wewe kuachana naye, ningependa ujue hivyo kwanza,” alisema Mr Edgar nikashangaa mno sikujua kama alikuwa na busara hivyo.
“sawa, nimekusikia.” Niliitikia kwa aibu na kujikunja pembeni ya kitanda nikitamani kuvaa nguo zangu na kukaa kiheshima.
“Ninah, sisemi Brighton hapaswi kuadhibiwa hapana, lazima apate adhabu yake. Na utamsamehe ukiamua hapo baadaye. Lakini kwanza ngoja tukurudishe kwenye hali yako ya kawaida, nataka kuona uzuri wako ukirudi na sura yako ikijaa furaha tena, Okey!” alisema Mr Edgar hapo ndiyo sikujua alikuwa amepanga kufanya nini? baada ya kunisusa pale kitandani, huyu mwanaume ananitaka au hanitaki? Bado nilikuwa na kisebusebu.
Basi nikavaa kiabuaibu tukaenda restaurant tukala na kunywa hadi nikavimbiwa kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu nikafurahi kwa kweli.
Mr Edgar mwenyewe akacheka na kuniambia: “Unaona? Tabasamu limeanza kurudi. For sure wewe ni mzuri kama nisingeoa mapema ningekuoa malaika.”
Nikaangalia chini kwa aibu.
Tulirudi chumbani tukalala, huwezi amini hakunigusa hata kidogo. Nikawaza kuwa huenda alitaka kulila tunda likiwa limeiva vizuri au pengine alikuwa akinitega kwa kunionesha kuwa yeye si kama wanaume wengine.
Nilikuwa na wasiwasi mno. Nikijua pengine usiku ataniua au lah lakini baba wa watu aliamka tu vizuri.
Basi asubuhi baada ya kuoga, alivaa nguo na kujiandaa kwenda kazini, mimi akaniachia shilingi laki tano, akanitaka nikanunue nguo na kujiweka safi. Nikashukuru mno nusura nilie.
NINAH 23
Basi alipoondoka tu Mr Edgar mimi nikaenda saluni zangu za laki moja, tena saa hiyo kwa kuwa nilivyoijua shida, nilikuwa makini kweli na hela. Niliitunza laki nne, kwenye tigopesa na kutulia.
Nilirudi pale hotelini kama kwangu, tena niligundua kumbe Mr Edgar kwa jeuri ya fedha aliyokuwa nayo alikuwa akiishi palepale hotelini. Na nilipata kila huduma, kuanzia breakfast, lunch, dinner, nikazunguka kwenye swimming pool, gym na kufanya kila kitu free.
Wiki mbili tu zilipoisha nilikuwa Ninah yuleyule wa zamani. Mzuri, mrembo niliyesifiwa kila nilipopita. Lakini moyo wangu ulikuwa na hofu, maana bado Mr Edgar hakunigusa. Sikuwa na amani, nilimuwazia mambo mengi mno.
We mwanaume gani, mnalala chumba kimoja, kitanda kimoja, tena analala kwa kunikumbatia kabisa lakini hata kunisumbua hakuwa akinisumbua. Mara ya kwanza nilipokuja nilidhania ni ubaya wangu kwa sababu nilikosa mvuto tena. Lakini sasa hivi mbona navutia tena nilinawiri zaidi lakini bado hakuwa na habari na mimi?
Sikuombea anisumbue lakini angalau angefanya hivyo ningekuwa na amani kuwa ananisaidia vyote hivyo kwa ajili ya mapenzi, lakini sasa msaada wake wote huu kwangu ni kwa malipo gani? Sikupata jibu.
Basi na mimi nikaanza kuwa namkumbuka Brighton wangu. Nilijizuia sana hata kumpigia simu, kwa sababu nilifuata ushauri wa Mr Edgar kuwa Brighton alipaswa kuadhibiwa, lakini si kumuacha.
Kweli kila nilipomfikiria nikajua pengine alifanya yote hayo baada ya kukata tamaa, na kweli wanaume wengi matatizo yakiwazidia hawafanyi kitu kingine zaidi ya kukimbilia kwenye ulevi na kujisusa. Wakati wanawake matatizo ya kizidi wanakuwa kama mimi yaani wanajirahisisha kwa wanaume wowote wenye vihela waliowakataa mwanzoni.
Nilifikiria lakini kweli hata nikimuacha Brighton, nitampata nani mwenye moyo kama wake. Basi mawazo hayo yakanipelekea siku iliyofuatia kumpigia shoga wangu wa Tandale kupeleleza tu Brighton alikuwa anaendeleaje.
“Hallow shoga upo wapi siku hizi? vipi ndiyo umemuacha mumeo kwa visichana vya Tandale?” alisema Mama Sele.
NINAH 24
“kwanza niambie vipi hapo? bado anawaleta hao wanawake zake?” niliuliza kwa wivu.
“Mh hapana, yaani tangu siku ile mwenzio amekuwa kama vile amedata, tunamsikiaga akiwa amelewa anakuliliaga weee akichoka analala. kawa mchafu balaa kama chizi vile, nani atamtaka.”
“Mh aya!” niliitikia na kukata simu. Nikafurahi angalau sasa nilijua Brighton alikuwa akiumia kwa alichonifanyia. Lakini je, nimpe adhabu hii hadi lini, ndiyo nimsaheme, mbona kama ndiyo hivyo anateseka sana? Nilitaka kuomba ushauri kwa Mr Edgar.
Siku hiyo usiku Mr Edgar aliporudi na kuniona alifurahi mno, akanikumbatia na kunibusu shavuni, akaniambia: “Naona sasa umekuwa kwenye ubora zaidi!”
ITAENDELEA
Ninah Sehemu ya Tatu
Also, read other stories from SIMULIZI;