Nyuma ya Machozi Sehemu ya Tatu
IMEANDIKWA NA: ALLY MBETU
*********************************************************************************
Simulizi: Nyuma ya Machozi
Sehemu ya Tatu (3)
ILIPOISHIA:
Kilole alijisemea moyoni kuwa asali ile aliyomlambisha ni chambo cha kumuingiza kwenye mtego wamlipue hakuwa na mapenzi tena na mumewe na kumuona shetani wa roho yake aliyetamani afe wakati wowote ili afaidi penzi tamu la Kinape.
SASA ENDELEA…
Siku ya pili Kinape alichelewa kutoka kwenda kazini kutokana na ishara aliyooneshwa na Kilole kuwa asiondoke ili wazungumze. Deusi aliondoka peke yake kuwahi kazini huku akijiona alichelewa kupata dili kubwa kama zile. Alipofika ofisini aliwasiliana moja kwa moja na Teddy mwanamke muuza unga. “Haloo Teddy.”
“Ooh! Brother za asubuhi?”
“Nzuri.”
“Nina imani una habari njema asubuhi hii?”
“Ni kweli, mimi nipo tayari kuifanya ile kazi.”
“Ooh! Vizuri sana, tena una bahati washirika wangu wote wapo hapa.”
“Kwa hiyo?”
“Basi jioni tukutane ili tuzungumze jinsi ya kufanya.”
“Hakuna tatizo.”
“Nakutakia kazi njema kaka yangu.”
Deus baada ya kukata simu alitabasamu kidogo kabla ya kuanza kazi. Wakati yeye anapanga mipango ya utajiri, nyumbani kwake pia kulikuwa na mipango ya kummaliza. Kinape baada ya kujiandaa kwenda kazini kabla ya kutoka chumbani Kilole alimfuata.
“Vipi mpenzi?”
“Safi.”
“Naona jana jamaa alikuita chemba alikuambia nini, au ndiyo anataka uwahi kumuoa Happy?”
“Walaa.”
“Alikuitia nini?”
“Jamaa anataka kututajirisha.”
“Kututajilisha una maana gani?” Kinape alimueleza yote aliyoelezwa na Deus pamoja na kukatazwa kuitoa siri ile nje. Pamoja na kusikia mpango ule wa mabiloni ya shilingi bado Kilole aliona wanamchelewesha.
“Kinape hiyo fedha itapatikana lini huoni kama tunachelewa, tuachane na mpango wake tummalize tufikiri mambo mengine.”
“Kilole zile ni fedha nyingi zitakazo tufanya tuishi kama peponi, tutakula mpaka tunakufa bila kufanya kazi.”
“Kwani huo mpango mwezi gani?”
“Wanamsubiri yeye tu watu waingine unga wakati wowote.”
“Mmh! Nitavumilia lakini kwa upande wangu naona zilizopo zinatutosha.”
“Ni kweli lakini tutafanya kosa kumbwa kuacha mabilioni ya fedha.”
“Mmh! Sawa.”
Wakati Kilole na Kinape wanapanga mipango ya kummaliza Deus, Jimmy mpiga picha naye alikuwa akipanga yake. Aliamini kupitia picha zile atajipatia fedha na penzi toka kwa Kilole mwanamke aliyempenda kupindukia. Aliamua kumtumia rafiki yake kumtisha ili wapate fedha. Kilole akiwa katika usafi wa kawaida wa nyumba simu yake iliita, namba ilikuwa ngeni kwake. Alibofya cha kupokelea na kusema:
“Haloo.”
“Haloo, nazungumza na Kilole.” “Ndiyo, nani mwenzangu?”
“Naitwa Simon, kumeokota picha zako ambazo zinaonesha unafanya uchafu kwa hiyo ili nisizisambaze nataka milioni tano.”
“Picha zangu?” Kilole alishtuka.
“Eeh, tena unafanya uchafu na ndugu wa mumeo, kabla picha hazijamfikia mumeo tunaomba huo mzigo.”
“Na..na..omba unipigie baada ya dakika tano,” Kilole alichanganyikiwa na kuona Jimmy amemgeuka. Kwa haraka alimpigia simu Jimmy kutaka kujua picha zake zimemfikiaje mtu mwingine. Alipopiga simu iliita kwa muda bila kupokelewa, hakukoma alirudia tena na kupokewa upande wa pili.
“Haloo Sister,” Jiimy alipokea upande wa pili. “Nazungumza na Jimmy?”
“Ndiyo Sister, lete stori.”
“Jimmy nilikueleza nini?”
“Kuhusu nini?”
“Kuhusu picha.”
“Kwani vipi?” “Kuna mtu kanipigia simu anasema ameokota picha zangu kwa hiyo anataka milioni tano la sivyo atazisambaza au kumpelekea mume wangu.”
“Ha!” Jimmy alijifanya kushtuka.
“Jimmy tulizungumza nini na umefanya nini?”
“Samahani Sister, wiki mbili zilizopita nilivamiwa ndani na kuibiwa vitu vingi, nina siku mbili tangu nitoke hospitali.”
“Taarifa ulifikisha polisi?”
“Niliogopa kwa vile kulikuwa na picha zako.” “Jimmy kwa nini umekaa na picha zangu, kama pesa yako nilikulipa yote?”
“Sister niliamini picha zile ulikuwa na umuhimu sana kwako hivyo ungeweza kuzipoteza ndiyo nikaamua kuzihifadhi nyingine kwangu.”
“Sasa umeona umenitia hasara?”
“Sikujua ingekuwa hivyo.”
“Sasa nitafanyaje, utawezaje kunisaidia?”
“Dada yangu kama fedha unayo ungempa kwa kweli picha zile siyo nzuri kuonwa na mumeo.” “Nampa lakini kumbuka umenifanyia kitu kibaya sana.”
“Najua lakini nia yangu ilikuwa nzuri tu.”
“Okay, imekwisha tokea sina jinsi, ila baadaye nitakupa kazi ya kunifanyia.”
“Hakuna tatizo dada yangu ila pole sana.”
“Bado sijapoa mpaka uifanye kazi yangu kwa asilimia mia.”
“Hakuna tatizo.”
“Basi baadaye.”
Kilole alikata simu na kumpigia aliyempa taarifa ya kuokotwa kwa picha zake. Baada ya kuita ilipokelewa upande wa pili.
“Ndiyo, sema.”
”Ulisema?” Kilole aliuliza.
“Kuhusu nini?”
“Si umesema una picha zangu?”
“Ndiyo.”
“Samahani kaka angu.”
“Samahani ya nini, fedha haipungui hata senti tano kama huna niifanye kazi yangu,” upande wa pili ulimtisha.
“Kaka yangu mbona unanifanyia ukatili kama huo, nimekukosea nini mpaka kushindwa kunisikiliza?” “Dada eeh, niambie utatoa mzigo au hutoi nijue moja sikuja kubembelezana.”
“Sio kwanza sitoi, nitatoa hata zaidi lakini nilitaka kujua hizo picha umeziokota wapi na zilikuwa kwenye nini?”
“Dada yangu eeh, sipo mahakamani kama mshiko upo nijulishe nina mambo mengi, hivi unafikiri nikimweleza mumeo kuwa nina picha hizo ningepata hata mara tatu ya fedha yako.”
“Basi naomba unielekeze nizilete wapi hizo fedha?”
“Unazo sasa hivi?”
“Hapana nakwenda kwenye mashine ya kutolea fedha.”
“Basi ukiisha kuwa nazo nijulishe nikuelekeze.”
“Nielekeze wala haichuki hata nusu saa.”
“Nitakujulisha baada ya dakika tano.” Jamaa baada ya kukata simu alimgeukia Jimmy aliyekuwa pembeni yake.
”Sasa mkuu fedha ndiyo hiyo atuletee wapi?”
“Mwambie Sea Green view hotel.”
“Poa.”
“Yule mwanamke anaonekana ana fedha za kuchezea lazima tumtumie kutengeneza maisha.” “Hakuna noma mkuu.”
Baada ya mazungumzo alimpigia simu Kilole. “Haloo Sister tukutane Sea Green view hotel.”
“Nje au ndani?”
“Aah! Jambo hili si la kitoto tunatakiwa tukabidhiane ndani.”
“Mmh! Sawa.”
“Mbona unaguna?”
”Si unajua mimi mke wa mtu naweza kuingia kwenye matatizo nikionekana katika mazingira ya kutatanisha.”
“Kuachika na kuonekana kipi kibaya?”
”Mmh! Sina jinsi kisu kimegusa mfupa.”
“Nikupe dakika ngapi?”
“Sidhani itachukua nusu saa, naomba basi nikukute kwani nina haraka.”
“Hakuna tatizo.”
Kilole alijikuta akiingia katika matatizo ambayo hakuyategemea, moyoni aliapa kumfanyia kitu kibaya Jimmy ambacho hatakisahau maishani mwake. Baada ya kutoka kwenye mashine ya kutolea fedha, alielekea Sea Green view hotel. Alipofika nje ya hoteli alimpigia simu mwenye picha zake.
“Haloo nimeisha fika upo wapi?”
“Njoo ndani ghorofa ya pili chumba namba 112.”
“Mmh! Mbona makabidhiano ndani ya chumba cha hotel?”
“Kwa vile wewe ni mke wa mtu.”
“Mmh! Sawa nakuja.
” Haikumpa shida kuingia ndani bila kujulikana kutokana na kujitanda kanga iliyomfunika kichwa na kujiziba na miwani nyeusi. Aliingia hadi ndani ya hoteli na kwenda moja kwa moja kwenye chumba namba 112, kabla ya kuingia alipumua kidogo na kugonga mlango.
“Pita mlango upo wazi,” sauti toka ndani ilimjibu.
Alizungusha kitasa na kusukuma mlango, mlango ulifunguka na kuingia ndani. Alimkuta kijana mmoja aliyekuwa amekaa kwenye sofa akinywa maji yaliyokuwa juu ya meza ndogo.
“Karibu,” alimkaribisha huku akitabasamu.
“Asante,” Kilole alijibu huku akikaa pembeni yake akiwa hajiamini. “Karibu soda.”
”Hapana nina haraka fedha hii hapa nipe picha zangu niondoke.” “Sikiliza dada yangu kufanya mambo yako kwa pupa utajikuta kila siku unarudia makosa.”
“Nimekuelewa kaka yangu ila naomba unipe kwanza hizo picha mambo mengine tutapanga siku nyingine.”
“Basi kunywa soda kidogo.”
“Hapana kaka yangu nina haraka.”
“Ina maana mimi ni mjinga kukununulia soda?” Jamaa alionesha kukasilishwa na kauli ya Kilole. “Basi wacha ninywe kidogo,“ Kilole alisema huku akichukua chupa ya soda iliyokuwa imekwisha funguliwa kabisa.
Alikunywa kidogo bila kujua alikuwa amepangiwa mchezo mwingine katika soda, aliona kama inamchelewesha alikunywa yote ili awahi kuondoka. Lakini hakufanya lolote baada ya kupatwa na kuzunguzungu na kujilaza kwenye kochi bila kujua. Joe alimpigia simu Jimmy aliyekuwa nje ya hoteli.
Jimmy aliingia ndani ya hoteli na kumkuta Kilole amejilaza kwenye kochi hakiwa hajitambui. “Ooh! Kazi nzuri sana,” alimpongeza mwenzake.
“Mmh! Nilikuwa kwenye wakati mgumu unajua kazi kama hujaifanya hata siku moja lazima utakuwa hujiamini, wasiwasi wangu anaweza kuja na polisi.”
“Aje na polisi hajitaki, vipi mzigo amekuja nao?”
“Huu hapo,” Joe alimpa bahasha lililokuwa na fedha. Kabla ya kufanya lolote walihesabu fedha na kukuta milioni tano taslimu, Jimmy alimkatia Joe milioni moja kama malipo ya kazi aliyompa.
“Mzee nafikiri zinakutosha.” “Asante mkuu, nini kinaendelea?”
“Bado sinema inaendelea, sasa hivi tutafanya naye mapenzi kwa zamu huku tukipiga picha ambazo naamini zitazidi kututengenezea fedha.”
“Hakuna tatizo.”
Walimbeba Kilole aliyekuwa hajitambui na kumlaza kitandani kisha walimvua nguo zate na kuanza kumbaka kwa zamu huku wakimpiga picha za aibu. Baada ya kumaliza zoezi la aibu waliondoka na kumwacha Kilole akiwa amelala hajitambui.
Majira ya mchana Teddy alimpigia simu Mr Deus kutaka kujua kama ana nafasi waonane kutokana na baadhi ya washirika wake jioni ya siku ile kuwa na safari kufuata mzigo. “Haloo brother za kazi?” “Nzuri, sijui zako.”
“Zangu ziko poa, samahani tunaweza kuonana mchana huu?”
“Hakuna tatizo.”
“Basi njoo mara moja nikukutanishe na jamaa zangu ili tuianze kazi mara moja.” “Hakuna tatizo, tutakutana wapi?”
”Njoo na gari mpaka sehemu uliyoniacha siku ile.”
“Hakuna tatizo ndani ya robo saa nitakuwa hapo.”
“Okay, baadaye.”
Deus alikata simu na kujiandaa kwenda kuonana na kundi la wauza madawa ya kulevya. Baada ya kupanga vitu katika hali nzuri alitoka na kumuaga msaidizi wake.
“Happy natoka kidogo.” “Hakuna tatizo bosi.” Mr Deus alielekea kwenye maegesho kuchukua gari lake na kuelekea kwenye wito, alipofika eneo aliloelezwa alilipaki gari pembeni ya barabara kusubiri maelekezo. Baada ya muda simu yake iliita, alipoitazama alikuta ni Teddy, alibofya cha kupokelea na kuweka sikioni.
“Haloo.” “Haloo nimekuona, teremka kwenye gari lako na kupanda kwenye gari litakalo simama mbele yako.”
“Na gari langu?” “Liache tu litakuwa katika usalama wa hali ya juu, kwa hilo usihofu.”
“Okay,” Mr Deus alikata simu na kuteremkana kulifunga gari lake na kufuata maelekezo. Kabla hajapiga hatua Range Rover Vogue nyeusi yenye vioo visivyoonesha ndani ilisimama mbele yake na kufunguliwa mlango.
Hakupoteza muda aliingia ndani ya gari na kufunga mlango na gari liliondoka. Ndani ya gari kulikuwa na watu watatu Teddy aliyekuwa akiendesha gari na wanaume wawili waliokuwa wamekaa siti za nyuma.
“Habari zenu?”
“Nzuri,” Walijibu kwa mkato.
“Samahani brother,” Teddy alisema huku akipaki gari pembeni. “Bila samahani.”
“Naomba ufuate utaratibu wetu kabla ya kufika kwetu.”
“Hakuna tatizo.” “Utafungwa kitambaa usoni mpaka tutakapofika.”
“Hakuna tatizo mnaweza kufanya.”
Baada ya kukubali alifungwa kitambaa cheusi usoni na safari iliendelea bila kujua anapelekwa wapi. Baada ya dakika tano gari lilisimama na kuombwa
Mr Deus aliteremke, alitii amri na kuteremka kisha alishikwa mkono na kuongozwa hadi sehemu na kufunguliwa kitambaa usoni.
Baada ya kufunguliwa alijikuta yupo mbele ya sebule lililokuwa na kila kitu cha thamani. Ndani ya sebule ile kulikuwa na watu zaidi ya nane ukijumlisha watatu aliokuja nao wakawa jumla watu kumi na mbili pamoja na yeye mwenyewe.
“Karibu Mr Deus jisikie huru, ila samahani kukuleta kama mateka.”
“Kawaida tu wala hakuna baya.”
“Karibu kwenye kochi.”
“Asante,” alijibu huku akikaa kwenye kochi, baada ya kuketi aliwasalimia aliowakuta.
“Habari zenu.”
“Nzuri,” Waliitikia kwa pamoja.
“Mr Deus hawa ndiyo washirika wangu, huyo hapo ni Mateez anayefuata Sopas, Natalie, Suzy, Moops, Sweet, Pako, Flog, JMS na Poona, nina imani mimi unanifahamu?”
Mr Deus alikubali kwa kutikisa kichwa. “Waungwana huyu ndiye mtu niliyewaeleza ana umuhimu mkubwa kwetu, nimeweza kumwelewesha na kanielewa. Kwa vile kazi hii haihitaji kupoteza muda nina imani kuanzia muda wowote biashara ifanyike.
“Mr Deus hawa ndiyo washirika wangu niliokueleza kwa bahati nzuri tumekutana sehemu kubwa ya kundi letu. Wengine watatu utawajua kwa vile wiki ijayo wanaingia nimezungumza nao ili wapitie katika mikono yako salama japo wawili wamesema wataanza baada ya sisi ila mmoja atakuja na mzigo ndogo kujaribu.”
“Hakuna tatizo kazi itafanyika vizuri kila mmoja ataifurahia,” alisema Mr Deus baada ya kumsikiliza Teddy.
“Kwa hiyo kazi rasmi inaanza mwezi ujao kwa mwezi una uhakika wa kutengeneza zaidi ya bilioni mbili.”
“Hakuna tatizo nina imani mtafurahia kufanya kazi pamoja japo ni ya hatari.”
“Baada ya makubaliano hayo, tunakuonya tena kosa lolote la kizembe litagharimu uhai wako,” Teddy alitoa onyo lingine.
“Najiamini kuliko mnavyonidhania,” Mr Deus aliwatoa wasi.
“Kumbuka nilikukataza usimwambie siri hii hata mkeo.”
“Siwezi kumwambia mtu.”
Baada ya mazungumzo Mr Deus aliagwa na kupewa asante wa kukubali kufanya kazi na kundi lile ya milioni 55 kwa kila mmoja kutoa milioni tano. Baada ya mazungumzo yale alifungwa tena kitambaa na kurudisha hadi kwenye gari lake na kumkabidhi huku wakimuacha Mr Deus akiwa hajui alikuwa wapi.
Kilole alishtuka na kujishangaa yupo wapi baada ya kushtushwa na mazingira aliyoyaona mbele yake. Alijiuliza pale amefikaje na anafanya nini, kingine kilichomshtua ni kujikuta kitandani akiwa mtupu na pembeni yake kulikuwa na kondomu zaidi ya nne zilizotumika.
Alishtuka na kujishika sehemu za siri na kukuta kweli amebakwa, pembeni yake kulikuwa na bahasha mbili zilizokuwa imeandikwa jina lake. Kabla ya kuichukua ile bahasha alitulia na kuvuta kumbukumbu ya kufika pale. Alikumbuka alipeleka milioni tano ili apewe picha alizipiga akifanya mapenzi na Kinape. Aliendelea kuvuta kumbukumbu na kukumbuka baada ya kuonana na yule kijana alikaribishwa soda lakini kilichoendelea hakujua mpaka aliposhtuka na kujikuta akiwa mtupu kitandani huku ikionesha amebakwa zaidi ya mara nne kutokana na mipira minne ya kiume iliyotumika.
Alijipa ujasiri na kunyanyuka hadi bafuni na kuoga kisha alirudi chumbani na kuvaa nguo zake kisha alichukua bahasha mbili zilizokuwa na jina lake na kuziweka katika mkoba wake na kutoka nje ya hoteli kurudi nyumbani kwake.
Alipofika nje ilionesha kiza kilikuwa kimeingia, alitoa simu yake kwenye mkoba na kuangalia saa ilimuonesha ni saa mbili usiku. Alijikuta akishtuka na kujiuliza utamueleza nini mume wake, katika simu yake kulionesha kuna simu zilizopigwa zaidi ya mara kumi za mume wake pamoja na Kinape.
Japo roho ilimuuma kwa kitendo cha kinyama alichofanyiwa na kuapa kulipa kisasi, lakini aliweka pembeni maumivu yale na kutafuta njia ya kukabiliana na mumewe nyumbani atakayetaka kujua alikuwa wapi. Lakini ilikuwa tofauti na alivyofikiria, alipofika nyumbani alishangaa kukuta mumewe hajarudi. Mfanyakazi wa ndani alipomuuliza alisema hajarudi, ile ilimpa nguvu na kumpigia simu mumewe. “Haloo sweet.”
“Ooh! Honey vipi mbona napiga simu hupokei mpenzi, kuna nini?”
“Nilikuwa nimelala kichwa kimeniuma ghafla.”
“Nilitaka kukujulisha kuwa nitachewa tuna kazi moja nzito.”
“Mmh! Mume wangu, siyo unanila kisogo,” Kilole alijifanya kulalamika.
“Mke wangu siwezi kutoka nje ya ndoa yangu nakupenda sana, hasa mwenetu ambaye ndiye mrithi wetu na yote nayafanya kwa ajili yenu.”
“Asante mume wangu, nashukuru kusikia hivyo.” “Nikimaliza tu narudi nyumbani.”
“Nakutakia kazi njema, nakusubiri kwa hamu,” Kilole alizidi kumtia ujinga mumewe. Baada ya kukata simu aliingia chumbani mwake na kuziangalia zile bahasha, bahasha ya kwanza ilikuwa na picha alizopiga akifanya mapenzi na Kinape. Bahasha ya pili kulikuwa na picha ambazo zilimmaliza nguvu lakini akijikaza na kuendelea kuzitazama.
Alijiona akibakwa na wanaume wawili, alishtuka na kukumbuka soda aliyokunywa ndiyo ilimfanya apoteze fahamu na kumfanya yule mwanaume na mwenzake wambake.
Roho ilimuuma kutoa milioni tano bado wamembaka na kumpiga picha chafu. Ndani ya bahasha kulikuwa na karatasi iliyokuwa na ujumbe usemao;
Kwa vile unapenda mchezo huo, baada ya kukupa picha zako na kutupa milioni tano, picha hizo zingine zinataka milioni kumi, la sivyo siri ilimfikia mumeo. Tutakupigia simu kujua utatupa lini na wapi?
Kilole jasho lilimtoka na kuona kama laana ya matendo yake ndiyo inayomtafuna, alijiuliza milioni kumi akiwapa lazima watatengeneza mpango mwingine. Wasiwasi wake huenda mpango ule Jimmy anaujua, lakini hakutaka kutumia pupa zaidi ya kutumia hata kishawishi cha fedha ili Jimmy amsaidie. Wazo lingine lilikuwa kumuwahi Deus kabla hajajua lolote kwa kumuua ili kuepusha aibu, lakini wazo la kuua bado hakulipa nafasi kutokana na Kinape kuweka pingamizi. Akiwa amechanganyikiwa simu yale iliita, aliipokea na kusema:
“Haloo.”
“Haloo, bahasha umeiona?”
”Wewe nani?” “Mdau wako, nina imani ujumbe umeuona nieleze hizo fedha nitapata lini?”
”Lakini kaka yangu nimekukosea nini mpaka kunifanyia unyama kama huo?” Kilole alilalamika huku akimwaga chozi. “Hujadhalilishwa na mtu, biashara umeianza wewe, sisi tunaiendeleza.”
“Kaka yangu milioni tano nimekupa leo, hizo kumi nitazipata vipi?”
“Kama huna pa kuzipata basi salamu utazikuta kwa mumeo,” sauti ya upande wa pili ilimtisha.
“Msifanye hivyo, nioneeni huruma.”
“Hukujionea huruma sisi tutakuonea vipi?”
“Basi nipunguzieni.”
“Tulikuwa tunataka milioni hamsini, lakini nimepunguza mpaka kumi bado huoni huruma yangu.”
“Basi nipeni muda wa muda ili nizikusanye.”
“Tutakupa siku mbili.”
“Mbona ndogo?”
“Kama ndogo utajuana na mumeo tena tuinampa na za mwanzo ulizopiga na shemeji yako.”
“Basi nitawapeni, nakuombeni msimpe mtu.”
“Hakuna tatizo timiza haja zetu.”
“Hakuna tatizo.”
“Kwa heri, usiku mwema.”
Baada ya kukata simu alijikuta akirudiwa na maneno ya mtu aliyetaka fedha kwa kusema alifanya mapenzi na shemeji yake ile ilionesha kabisa Jimmy huenda mpango mzima anaujua. Kilole pamoja na kutokewa na tukio zito la kumdhalilisha huku likizidi kumuingiza kwenye mazingira magumu. Lakini hakutaka kuyumba kwani aliamini vita ile ni yake na yeye ndiye anayetakiwa kupambana mpaka tone la mwisho.
Alizirudia zile picha na kuuona unyama aliofanyiwa ikiwa pamoja na kuingiliwa kinyume na maumbile. Moyo ulimuuma sana na kujikuta akidondokwa na machozi kutokana na udhalilishwaji kama ule. Aliapa kupigana nayo mpaka hatua ya mwisho hata kwa mtutu kwani alikuwa anajua kutumia vizuri chombo cha moto baada ya kufundishwa na mumewe na kujua kuitumia vizuri.
Alikumbuka visasi vingi ambavyo ameviona kwenye sinema hutendeka usiku kwa mtu kuingia sehemu na kufanya mauaji kisha kutokomea bila mtu kujua.
Wazo lake lilikuwa kwenda kumbana Jimmy ili amtaje mtu mwenye picha zake na alipanga kuhakikisha anamuua Jimmy na kijana anayemtumia kama mtaji. Wakati akiwaza vile alishtuka kusikia mlango ukigongwa, alificha picha kwenye kabati na kwenda kufungua mlango.
Alifuta machozi na kujirudisha katika hali ya kawaida kisha alipofungua akijua mumewe karudi, lakini kumbe alikuwa Kinape ambaye alionekana mwenye jambo zito kichwani mwake kutokana na mwonekano wake. Kilole alizidi kuchanganyikiwa na hali ile ambayo aliona huenda inafanana na yake.
“Kilole mbona hivyo?” alimuuliza kwa mshangao. “Kilole umeniweka katika wakati mgumu sana,” Kinape alisema huku akikuna kichwa.
“Mungu wangu! Amejua? Kwa nini tusimmalizie mbali?”
“Tummalizie mbali nani?”
“Si Deus.”
“Kwa kosa gani?”
“Si amejua.”
“Wala si hilo.”
“Picha ameziona?”
“Kilole hebu acha papala, yote unayouliza siyo.”
“Sasa nimekuweka kwenye wakati mgumu kivipi?”
”Happy hanielewi kabisa, kila kukicha naitwa na familia yake naichenga, nikienda nitawaelezea nini wanielewe.”
“Kinape unakuwa kama siyo mwanaume, mwambie kuwa humtaki kwani mapenzi ni lazima.”
“Si rahisi kiasi hicho, kuvunjika kwa penzi kuna sababu huwezi kuzima chuma cha moto na maji baridi lazima kitapinda na Deus nitamwambia nini mtu niliyempeleka kwa wazazi wa Happy kumtambulisha kama kaka yangu?”
“Yote uliyataka wewe, kwa nini hukuniuliza kabla ya kwenda huko?”
”Kilole, wewe ni mke wa mtu na Happy ni mchumba wangu hivyo nilikuwa na haki ya kufanya vile.”
“Sasa Deus atakulazimishaje umpende Happy wakati humtaki?”
“Nitaanzia wapi ikiwa nilimweleza mengi juu ya mapenzi yangu ya dhati kwa Happy huku akiniahidi kusimamia harusi yangu. Kibaya zaidi Happy na wazazi wake watakuja hapa jioni ya leo ili kujua hatima ya ndoa.”
“Kwani wewe ulimjibu nini Happy?”
“Nilimueleza asubiri kidogo mzazi wangu mmoja alikuwa na matatizo.”
“Sasa yeye anataka nini na ulikwisha mweleza ukweli?”
“Anataka kwenda kumuona kwa vile anajua na yeye ni mzazi wake, pia muda wa kuwa naye umepungua si kama zamani. Kingine majibu yako ya mkato yamemshtua kitu ambacho kimemetia wasiwasi huenda tuna uhusiano wa kimapenzi.”
“Sasa akijua atafanya nini? Tena mweke wazi ili ajue hana chake.”
“Kilole acha kujisahau wewe ni mke wa mtu, kibaya kosa tunalifanya ndani ya kinywa cha simba. Hivi wakija hapa nitamwambia nini Deus na kwa vile huu ni mwisho wa wiki huenda akasema kesho tunakwenda kijijini. Siyo siri tabia ya Happy ilimvutia sana Deus na kusema atanipigania hata kwa fedha kuhakikisha namuoa, hivi niseme simtaki Happy nitaanzia wapi?”
“Kinape, Deus hawezi kukulazimisha kuoa mwanamke usiyempenda.”
“Unasema tu lakini kauli hiyo kwa mtu mwenye akili timamu hawezi kuitamka.”
“Kwa hiyo unamuogopa Deus?” “Ndiyo.”
“Kwa nini tusimpoteze?”
“Kilole acha papara nimekueleza tutajipanga.” “Nataka kukueleza kitu kimoja Deus ni kikwazo kwa nini mnamlea?”
“Tukifanya kwa pupa tutakosa mwana na maji ya moto.”
“Sasa tutafanyaje?”
“Nimekueleza niache niangalie tufanye nini?”
“Na kuhusu Happy najua ndiye anayeweza kuharibu kila kitu kama ataonekana kijijini?”
“Kwa kweli la Happy ndilo linalonichanganya nashindwa nifanye nini, nilipokutana naye leo nimechanganyikiwa jinsi alivyokonda kwa muda mfupi niliokuwa karibu yako na amenitishia nikimuacha lazima atajiua.” “Sasa akijiua wewe utapungukiwa nini, kwanza ndiyo itakuwa safi tunakuwa na nafasi ya kuishi wawili baada ya kumpoteza na Deus.”
“Siwezi kufanya hivyo, kama Happy atafariki basi nitakuwa na dhambi kubwa sana ambayo itakuwa kama tone la rangi nyekundu kwenye nguo nyeupe haitanitoka mpaka nitakapo ingia chini ya udongo.”
“Mmh! Sasa tutafanya nini?”
“Ndiyo maana nikasema umenipa mtihani mzito ambao sikuwahi kuusoma hata siku moja kwangu naona kiza. Kwa nini tusiachane na wazo kama hili?” ”Wazo gani?”
“Ukaniachana nioane na Happy na wewe unakie na Deus?”
“Kinape huwezi kunivisha kitanzi kisha uniweke juu ya donge la barafu likiyenyuka lazima nitakufa. Heri nife mimi kuliko kuendelea kuishi kwani naamini maisha yangu baada ya zile picha hayana thamani.
Kwa hiyo ulitaka kunidhalilisha ili ufurahi kwa vile nimeolewa na Deus kama kweli ulitaka niishi na Deus kwa nini ulinitendea unyama kama ule?”
“Happy..Ooh! Sorry Kilole mbona umekosa subira.”
“Nimekuelewa Kinape, tutazungumza kesho.”
Waliachana na Kilole alirudi chumbani akiwa amechanganyikiwa na kushindwa afanye nini juu ya picha mpya na habari za Happy.
Kilole baada ya kuachana na Kinape alirudi chumbani kwake na kujifungia kwa ndani, kila dakika iliyokuja mbele yake ilikuwa na maumivu makali yaliyomfanya akose jibu la haraka afanye nini. Kubakwa hakuona tatizo zaidi ya kusikia habari za Happy kupigania penzi lake ambalo ndilo lililomfikisha katika maumivu yale makali.
Alijiona mtu mmoja ambaye alikuwa akipigana na watu wengi bila msaada wa mtu mwingine, alijiuliza atawezaje kumdhibiti Happy kuhakikisha anampata Kinape mwanaume ambaye aliamini ndiye wa maisha yake.
Alichukua bahasha na kurudia kuangalia picha alizopigwa akibakwa na wanaume wawili kwa mpigo ambao hawakuonesha sura zao zaidi ya yeye peke yake.
Picha zile zilimchanganya sana na kuamini kama zitamfikia Kinape zitamweka katika mazingira magumu ambao utakuwa kama fimbo ya kumpigia ili kumuoa Happy.
Alipiga ngumi kwenye godoro kwa hasira baada ya kujiona yupo njia panda asijue aanze na kitu gani ili aweze kuyazima yote na mwisho wa siku awe na Kinape.
Akiwa katikati ya mawazo mlango uligongwa, alijua ni Kinape amekuja na wazo jipya, alikwenda hadi mlangoni na kufungua lakini alikuta ni mumewe ambaye alimchanulia tabasamu pana.
Kwa mshtuko aliufunga mlango haraka na kufunga na komeo, kwa haraka alichukua picha zake na kuzificha kisha alitoka hadi mlango ambako mumewe alikuwa bado amepigwa na butwaa.
“Ha! Kumbe ni mume wangu?” Alijifanya kushtuka.
“Unaniona sasa mwanzo ulifikiria nani?”
“Mmh! Hata sijui niseme nini, wakati unagonga mlango nilikuwa nimejinyoosha kitandani na kupitiwa na usingizi na kuota nimevamiwa na majambazi. Ulipogonga nilikuwa bado na usingizi nilipofungua na kukuona nilifikiri ni jambazi mpaka uliponiita na kuitambua sauti yako nisamehe mume wangu.”
“Kawaida, pole kwa ndoto mbaya.”
“Asante mume wangu.”
“Vipi mbona kama haupo sawa?”
“Mume wangu si nimekueleza naumwa, hata ndoto zangu zilikuwa za kutisha.” “Ooh! Pole sana.”
Kilole alijikuta akiangua kilio kilichomshtua mumewe.
“Vipi tena?” alimuuliza.
“Aah! Basi tu.”
“Basi tu nini! Au umezidiwa?”
“Walaa, hata sijiui nalia nini.”
”Niambie kama umezidiwa nikuwahishe hospitali, utalia bila kujua unalia nini?”
“Nimemeza dawa naomba kitu kimoja.”
“Kipi hicho mke wangu?”
“Uniache nipumzike nisiamshwe na mtu yeyote na mtoto alale kwa msichana wa kazi.”
“Hakuna tatizo mke wangu.” Deus hakutaka kumsumbua mkewe alifanya yote aliyoelekezwa, alitumia nafasi ile ya mkewe kutotaka usumbufu kuzungumza na rafiki yake juu ya mpango aliozungumza na Teddy na wauza unga wenzake.
Baada ya kuoga na kupata chakula cha usiku kilichopikwa na msichana wa kazi alikwenda chumba cha rafiki yake. Alimkuta amejipumzisha, alipomuona rafiki yake alimkaribisha kwa furaha.
“Ooh! Best karibu.”
“Naona umejipumzisha.” “Nifanye nini baada ya mihangaiko ya siku nzima.”
“Basi leo tulikuwa na kazi moja nzito ya kukamata gari lililokuwa na madawa kutokana na taarifa za watoa habari. Wenye gari waligoma kufungua mpaka walipokuja wakubwa zetu ambao waliliruhusu bila hata kuuliza. Lakini taarifa zilisema gari lile lina dawa za kulevya.”
“Basi hapo kuna rushwa imetembea kwa wakubwa.”
“Umeona eeh!”
“Ukweli ni huo unafikiri ndani ya gari kulikuwa na mzigo kiasi gani, ndiyo maana walikuwa wabishi kuwafungulia gari kwa vile kuna watu wanawategemea.” “Kitendo kile kimenivunja nguvu kweli, siwezi mkupote muda wangu kwa upuuzi kama ule.”
“Nawe kula sehemu yako.”
“Sasa kuna dili moja nimeingia leo si mchezo.”
“Mmh! Dili gani tena mzee?”
“Si nilikueleza yule mwanamke alisema atanikutanisha na wenzake?” “Eeh, ndiyo.”
”Basi leo mchana alinipigia simu na kunikutanisha nao.”
“Acha utani! Ehe ikawaje?”
“Tumekubaliana kuinza mwezi ujao kwa hiyo mpaka mwezi ukikatika nitakuwa nimetengeneza bilioni mbili.” “Acha utani!”
“Ukweli sasa hivi najiona nimekwisha uaga umasikini, kweli! Umefikia wapi mambo yako na Happy?”
Swali lilikuwa kama pigo zito moyoni mwa Kinape hakuwa na jibu la haraka, Deus hakujua rafiki yake anawaza nini baada ya kumuuliza na kukaa kimya. “Ni hivi nina fedha kidogo nitakupa ili kuhakikisha unakamilisha harusi yako.”
“Kiasi gani?”
“Milioni ishirini ambazo nitakupa sasa hivi ufanye maandalizi yako na shemeji, umekwisha mpeleka kwa wazazi kijijini?”
“Bado.”
“Unasubiri nini? Fanya hivi kesho kutwa hakikisha unakwenda na Happy kwa wazazi ili tupange nipango mingine. Utatumia gari langu sawa pia tafuta nyumba ya milioni hamsini ili nikununulie kwa siri ili shemeji yako asijue kitu.”
“Hakuna tatizo nimekuelewa mkuu.”
“Mbona kama upo mbali au umechoka?”
Deus alimuuliza Kinape aliyeonekana yupo mbali kimawazo. “Ni kweli leo nimefanya kazi kama mbwa, hapa nilipo natamani kulala tu si kitu kingine.”
“Basi pumzika tutaonana kesho.”
“Usiku mwema.”
“Na kwako pia.”
Deus alitoka na kwenda sebuleni kutafuta mkanda wa filamu ili kuvuta muda kabla ya kupanda kitandani huku akiwa anaisikia harufu ya utajiri. Alipiga mahesabu hata kama wataingiza mara moja kwa miezi miwili kwa mwaka aliziona bilioni kumi na mbili mbele yake.
Alijikuta akicheka peke yake huku akisema kwa sauti ya chini: “Kumbe utajiri hauna njia ndefu.”
Wakati akiwaza yale chumbani mkewe alikuwa akigaagaa kitandani kama nyoka aliyemwagiwa mafuta ya taa kutokana na kuwa na maswali yasiyo na majibu juu vitu vilivyopo mbele yake alijiuliza aanze na lipi la Jimmy au la Happy.
Alipanga usiku atoroke na kwenda kwa Jimmy kumbembeleza kwa njia yoyote ili tu amjue nani aliyemfanyia mchezo mchafu kama ule tena kujua picha za awali akifanya mapenzi na shemeji yake. Pamoja hakuwa na usingizi alitulia kitandani akisubiri mumewe akilala atumie nafasi hiyo kwenda kwa Jimmy.
Naye Kinape baada ya kutoka Deus alijikuta kwenye mtihani mzito wa kutoa uamuzi sahihi ambao hautaleta madhara kati ya Happy na Kilole. Lakini Happy kwake alikuwa muhimu kuliko Kilole ambaye tayari alikuwa mke wa mtu.
Swali ambalo kila kukicha lililokuwa likimla akili lilikuwa kuhusu picha alizopigwa akifanya mapenzi na Kilole nani aliyezipiga, alipata wazo la kumtafuta ili kupata ukweli wasiwasi wake huenda mtego ule ulipangwa na Deus.
Kingine kilichomkosesha raha kama picha zile zikivuja na kumfikia Deus angekuwa kwenye wakati gani. Wazo la kuua Deus au kumfanyia baya lolote alilipinga kwa nguvu zote japo hakuweza kumweleza ukweli Kilole. Taarifa za siku ya tatu kwenda kijijini kumtambulisha Happy zilizidi kumchanga kwa kujiuliza habari zile akimweleza Kilole atazipokea vipi.
Aliamua liwalo na lile lazima amweleze ukweli na hiyo kesho kutwa lazima ampeleke kijijini mengine yatakayotokea atakuwa tayari kukabiriana nayo. Alipuuza mkwara wa Kilole na kujilaza kuitafuta siku ya pili.
Majira ya saa saba usiku baada ya kuona mumewe amelala na kukoroma, Kilole alijinyanyua kitandani na kumtazama mumewe aliyekuwa amepitiwa na usingizi hajitambui. Alinyanyuka taratibu kwa kunyata hadi pembeni ya kitanda na kuunyanyua mto aliokuwa amelalia mumewe taratibu na kutoa bastola ya mumewe.
Alikwenda hadi kwenye kabati na kuvaa kaptura na fulana, aliichomeka bastora kiunoni kisha alijifunga kanga zilizomziba mwili mzima na kutoka taratibu bila kumshtua mtu yeyote. Aliegesha mlango na kutoka kwa kunyata hadi nje ya geti na kuchepua mwendo kupitia barabara kubwa kuelekea kwa mpiga picha Jimmy ambako hapakuwa mbali sana na kwake.
Baada ya mwendo mfupi aliacha barabara ya rami na kuingia kwenye uchochoro ambao ungemfanya atokee nyuma ya nyumba anayoishi Jimmy pia ndipo palipokuwa na dirisha lake. Alishukuru Mungu muda wote hakupata kizuizi chochote alitembea kwa taadhari kubwa, shida yake kwenda kugonga dirisha la Jimmy ili azungumze naye na kutaka msaada wake. Alipokaribia alitembea kwa kunyata ili mtu wa ndani asijue nje ya nyumba kuna mtu anapita. Aliporikaribia dirisha la Jimmy alisikia sauti za watu wawili mwanaume na mwanamke.
Mwanaume alimtambua ni Jimmy lakini mwanamke hakujua ni nani, lakini alijua ni mwanamke wake japo Jimmy hakuwa ameoa. Alitulia akijifikiria amwite au afanyeje kwani wasiwasi wake huenda pakatokea tatizo kwa muda ule mwanamke wake akajua yeye ni hawala yake. Wakati akiwaza afanye nini, aliendelea kusikia mazungumzo yaliyokuwa yakizunguzwa ndani.
“Sasa mpenzi hiyo fedha utanipa lini?”
“Kuna dili moja litatiki muda si mrefu nitakupatia.”
“Kumbuka na mimi ninataka kuendesha gari.” “Nimekueleza nitakupatia hiyo fedha baada ya wiki kila kitu kitakuwa tayari.”
“Najua unanidanganya.”
“Mbona laki nane za kupangia nyumba nilikupa kisha laki nane zingine za kununulia sofa nimekupa nitashindwa vipi milioni nne?”
Kauli ile ilimshtua sana Kilole na kujiuliza Jimmy uwezo ya kutoa fedha kiasi kile ameutoa wapi, wakati maisha yake yalikuwa ya kubahatisha mpaka apige picha na muda mwingi alishinda kijiweni.
Wakati akijiuliza maswali yasiyo na majibu ndani mazungumzo yaliendelea.
“Ha..ha..lafu mpenzi siku hizi unafanya kazi gani maana fedha zimeibuka kama uyoga?”
“Maisha kama kalata ukijua kuzichanga kila kitu kina kwenda kilivyopangwa.”
“Au unauza dawa za kulevywa?” “Kwani dia tatizo lako nini?”
“Naogopa nisije kukupoteza wakati nakuhitaji.” “Ungekuwa unanihitaji ungeridhika na nilivyokupa.”
“Sawa, hata kama unauza unga kuwa makini.”
Kilole alijikuta akijawa na maswali juu ya maneno ya Jimmy kuonesha ndani ya wiki ile atampatia yule mwanamke milioni tatu. Pia siku ile alimpa milioni moja na laki sita. Akili ya haraka aliamini fedha hizo huenda ndipo aliziombwa azitoe ili azipate picha zake.
Alikubaliana na wazo lake la awali kuwa Jimmy ndiye mhusika mkuu wa mipango yote. Wakati akiwaza vile alisikia simu ya Jimmy ikiita, alimsikia Jimmy akimwambia mwanamke wake.
“Samahani nakuja.” “Unakwenda wapi?”
“Sipendi maswali ya kijinga nimekueleza nakuja,” Jimmy alijibu kwa ukali.
“Najua na wanawake zako tu, “ alimsikia mwanamke akilia wivu.
“Wewe si unataka gari sasa kwa nini unapenda kufuatilia mambo yangu?”
“Sawa, basi nenda.”
Kilole alisikia mlango ukifunguliwa kuonesha Jimmy alikuwa akitoka nje kusikiliza simu. Kilole akiwa ametulia pembeni ya ukuta kwenye choo cha nyumba ya jirani.
Alisikia sauti za viatu zikielekea nyuma ya nyumba, kwa haraka alijificha nyuma ya choo. Jimmy bila kujua kuna mtu alisimama pembeni ya choo na kupiga simu iliyopokelewa upande wa pili.
“Sema Rich mbona usiku?”
“Aisee nina tatizo kubwa ya fedha,” kutokana na utulivu wa hali ya hewa Kilole alisikia mtu aliyekuwa akizungumza upande wa pili.
“Shida gani mzee, si leo nimekupatia mgao wa milioni?” “Ni kweli, si unajua nyumba za uswahili baada ya leo kununua sofa nimepandishiwa kodi ghafla na kutakiwa nilipe mwaka mzima na fedha yake anataka kesho. Sasa sijui utanisaidia vipi naomba basi unikope milioni ili kesho kama tukilipwa ile fedha nitakurudishia.”
“Sikiliza Rich leo nimempa shemeji yako milioni mbili kwa ajili ya sofa na kulipia nyumba, kwa sasa sina kitu ila jitahidi kumtisha yule mwanamke ili tupate hiyo fedha ikiwezekana hata kesho saa tano asubuhi.”
“Okay, nitajaribu kumsomesha.”
“Atakuelewa tu, jitahidi kesho tuzipate zote milioni kumi sawa?”
“Sawa nimekuelewa.”
“Basi usiku mwema, unajua umenitisha sana, wasiwasi wangu yule mwanamke kujua kama ni mimi ndiye namchezea mchezo huu.” “Walaa, nawe usiku mwema.”
Baada ya kukata simu Jimmy alirudi ndani na kumuacha Kilole akiwa amepata kitu ambacho mwanzo alikidhania lakini siku ile ukweli ulijulikana. Aliona hakuna haja ya kuendelea kuwa pale. Aliondoka na kurudi nyumbani huku moyo ukimuuma kwa kitendo alichotendewa na Jimmy.
Alifika kwake na kuingia ndani bila mtu yeyote kujua kama alitoka, alipanda kitandani na kujilaza. Kutokana na kutingwa na mawazo muda mwingi alifikiria jinsi ya kumuadabisha Jimmy. Moyoni aliapa kabla ya kuwapa hizo milioni kumi lazima wote wawe wamelamba udongo.
Teddy mwanamke hatari muuza unga baada ya kumaliza kuuza mzigo wake alimuaga Deus na kumweleza kila kitu kitakavyoendelea atamjulisha. Muda wote alikuwa na maswali juu ya mtu aliyemchoma katika kitengo cha madawa ya kilevya.
Alijiuliza nani aliyekuwa akijua kuondoka kwake zaidi ya mdogo wa marehemu mumewe ambaye alinyongwa China baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya. Tokea kifo cha mumewe mdogo wa mumewe alikuwa akimfuatilia na kumtaka kimapenzi. Lakini hakuwa tayari kutembea na familia moja kwa vile alikuwa na uamuzi wa kumchagua nani awe mpenzi wake. Muda mwingi kulikuwepo na kutoelewana kwa shemeji yake kulazimisha mapenzi na yeye kumkatalia. Mwanzoni alifanya kazi na mumewe ya uuzaji wa madawa na ndiye aliyemfundisha kuifanya kazi ile. Baada ya kifo cha mumewe alimshirikisha mdogo wa mumewe ambaye baada ya kupata fedha alianza nyodo na kuendelea kumtaka kimapenzi huku akimuahidi kumfanyia kitu kibaya kama ataendelee kumtolea nje.
Teddy bado hakutishwa na vitisho vya shemeji yake ambaye bado aliendelea kufanya naye kazi ya kusambaza dawa za kulevya kila kona ya dunia. Hata siku ya kuondoka mara ya mwisho aliyekuwa akijua safari ile ni yeye na washirika ambao wote walikula kiapo cha kuficha siri ya kazi yao na kuwa tayari kumsaidia mwenzao kwa gharama yoyote anapopatwa na tatizo. Wazo lake lilimpekeka huenda ni shemeji yake ndiye aliyefanya mchezo ule ili kumkomoa baada ya kumkataa kimapenzi.
Aliapa kumfanyia kitu kibaya kama ni yeye na adhabu yake ilikuwa ni kifo kwa vile nia yake ilikuwa ni kumpoteza. Teddy alipofika Italia alikwenda moja kwa moja kwenye nyumba aliyokuwa akiishi pamoja na shemeji yake.
Mara zote alipokuwa akisafiri na kurudi alikuwa akiwasiliana naye hata kumpokea, lakini siku ile alirudi kimya kimya. Alipofika nyumbani kwake aliingia ndani bila hodi, shemeji yake aliyekuwa na rafiki zake wakinywa na kujiachia na wanawake na muziki mkubwa alipomuona alishtuka sana.
“Ha! Teddy wewe si ulikamatwa?” “Wapi?” “Si..si.nilisikia umeshikwa Tanzania?” “Nani aliyekuambia?”
“Au alinidanganya?” “Nani mbona sikuelewi nani amekwambia mimi nimeshikwa?”
“Au umetoa rushwa?” “Ili?” Teddy alimuuliza huku akimtazama usoni kutafuta ukweli. “Tu..tu..achane na hayo, na..na mbona umekuja bila taarifa.” “Tatizo nini? kwa nini umegeuza nyumba yangu club?”
“Kwani tatizo nini?” “Mose unanitafuta huwezi kuigeuza nyumba yangu kama kilabu cha pombe ya kienyeji zinazouzwa Afrika.”
“Oya washikaji tutimke mambo yamekwisha haribika.”
“Sasa sherehe tunaihamishia wapi?” Mwanamke mmoja aliyekuwa amelewa sana na kuvaa nusu uchi aliuliza.
“Oya Rose, hii tunakwenda kuimalizia club Royal clasic.”
“Sasa kuna faida gani ya kupoteza muda, na huyu nani?” “Shemeji yangu.”
“Si ulisema umenyongwa au kafufuka?”
“Sitaki maswali hebu tuondokeni.”
Mose aliondoka na washikaji wake waliokuwa wamelewa na kwenda kumalizia starehe zao club.
Teddy alianza kufanya usafi ili kuirudisha nyumba katika hali nzuri. Macho yake yaliona simu kwenye kochi, aliacha kufanya usafi kuichukua simu ile na kuanza kuipekea kwenye sehemu ya ujumbe.
Jicho lake lilikutana na ujumbe ulioonesha shemeji yake alimtumia mtu aje kwenye sherehe ya kupotezwa kwake. Ilisomeka: yule fala nimemmaliza njoo tusherehekee njoo na demu wako. Palepale alipata picha kuwa shemeji yake ndiye aliyemtengenezea mtego ule. Aliapa kummaliza na kutoroka Italia na kwenda kuishi nchi yoyote kutokana na uwezo ya kifedha.
Siku ya pili Kilole aliwahi kuamka ili aweze kuzungumza na Kinape kuwa asiondoke ili wazungumze. Kama kawaida Kinape alijichelewesha kwenda kazini. Baada ya Deus kuondoka alimfuata chumbani kwake ili apate muafaka wa jambo walilozungumza jana yake. “Mhu! Umefikia wapi?” Kilole alimuuliza Kinape.
“Kuhusu nini?” “Kuhusu huyo mwanamke wako.”
“Kwa kweli bado sijapata jibu, tena jana Deus ndio kaniachanganya zaidi.”
“Kivipi?”
“Amesema kesho niende na Happy kijijini.”
“Eti nini?” Kilole alishtuka kusikia habari zile.
“Mumeo kasema kesho niende na gari kanipa ili kuhakikisha sina cha kujitetea.”
“Wewe ulimjibu nini?”
“We unafikiri ningemjibu nini?”
“Si ungemwambia umebadili umamuzi kuwa hutamuoa tena Happy.”
“Ningeanzia wapi wakati kila siku nimekuwa nikiomba msaada wake kufanikisha ndoa yangu.” “Mmh! Kumbuka akiishafika kijijini mimi sina changu.”
“Lakini kwa nini tulazimishe mambo wakati yamekwisha onesha vikwazo?” “Kinape hunielezi lolote nikakuelewa, nimejitoa kwako sitarudi nyuma.”
“Sasa nitafanyaje maana leo jioni happy na mama yake watakuja kujua hatima ya uchumba wetu.”
“Lakini kwa nini tusimfutilie mbali Deus, huoni anatuwekea kivingu?”
“ Ni haraka sana kufanya mambo hayo, kuna kitu kimoja kizuri tukifanya haraka tutakipoteza.”
“Kitu gani?”
“Mwezi ujao kuna bilioni kama mbili hivi zinaingia kwa hiyo tukizipata tutakuwa na uwezo wa kuishi nchi yoyote tuitakayo.”
“Lakini kumbuka kila siku unaongeza siku mwisho wake picha zitamfikia na kuharibu kila kitu.” “Kilole tutakuwa wajinga kuziacha hizo bilioni mbili za bure.” “Tutazitoa wapi?”
Kinape alimueleza yote aliyoelezwa na Deus juu ya mpango wa kuhongwa na wauza dawa za kulevya. “Nimekuelewa.”
Alimkubalia ili kumaliza mazungumzo lakini moyoni alipanga wiki ile lazima afanye kitu ambacho kitakuwa simulizi midomoni mwa watu. Baada ya Kinape kuondoka kwenda kazini, Kilole alijikuta akizidi kuchanganyikiwa na kujiuliza aanze na nani kati wa watu wote watatu, mumewe, Jimmy na Happy mchumba wa Kinape.
Aliamini mtu wa kuanza naye alifaa kuwa Happy kwa kumzima usiku wa siku ile ili kuzuia safari ya kwenda kijiji, kisha Jimmy na mwisho alipanga kummaliza mumewe. Mpango ule aliufanya kwa siri ili mtu yeyote asijue kwa kuamini kama angemshirikisha Kinape angemuharibia kila kitu.
Wazo alilopata la kummaliza mumewe aliona anahitaji msaada wa mtu, na mtu wa karibu alikuwa Jimmy. Aliamini msaada wake ulikuwa muhimu lakini mwisho wa yote na yeye angemmalizia mbali. Baada ya kukubaliana na mawazo yake aliamua kumpigia simu Jimmy ili mpaka jioni mpango wake wa kummaliza mumewe ukamilike ibakie kuutekeleza. Baada ya kupiga simu ya Jimmy iliita upande wa pili na kupokelewa. “Haloo.” “Haloo Jimmy.” “Ndiyo sister.” “Samahani Jimmy nina shida na wewe.”
“Shida gani?” Sauti ya upande wa pili ilionesha kushtuka.
“Nitakueleza tukionana, sema tuonane wapi.”
“Njoo nyumbani kwangu.”
“Sawa nakuja.” “Nitakuwa nyumbani baada ya nusu saa.”
“Hakuna tatizo nitafika kwa muda huo.” Dakika tano baada ya kumaliza mazungumzo na Jimmy, simu ya Kilole iliita alipoitazama ilikuwa namba ngeni. Aliipokea. “Haloo.”
“Eeh! Umefikia wapi?”
“Kuhusu nini?” Japo sauti iliijua alijifanya kuuliza. “Hiyo milioni kumi ipo tayari?”
“Kesho itakuwa tayari.”
“Sihitaji kesho nataka leo.” “Okay, hakuna tatizo jioni ya leo nitatimiza kila kitu.”
“Na ufanye hivyo, kinyume na kauli yako kila kitu hadharani.”
“Wala usihofu, itanibidi nichukue fedha ya ujenzi wa nyumba nitazirudisha kesho.”
“Nakutakia siku njema.”
“Na wewe pia.”
Kilole baada ya kukata simu alishusha pumzi ndefu na kujikuta akili yake ikifanya kazi kama kompyuta kwa kupata jibu. Ilionesha muda alioweka Jimmy ulikuwa ni kuwasiliana na jamaa yake ili kutaka kujua fedha yao.
Alicheka kwa uchungu na kuamini siku ile mpaka inakatika itabaki kumbukumbu akilini mwake. Alikwenda kujiandaa kisha alitoka hadi kwenye mashine ya kuchukulia fedha na kuchukua milioni ishirini ambazo aliamini zingemsaidia kuifanya kazi yake vizuri.
Baada ya kuziweka vizuri fedha zake aliingia kwenye gari na kwenda moja kwa moja kwa Jimmy. Alimkuta Jimmy yupo nyumbani, kwa vile chumba alikuwa akikijua alikwenda kugonga mlango.
“Karibu,” Jimmy alitoka akiwa kifua wazi.
“Ooh! Sister karibu.”
“Asante nimekaribia,” Kilole alijibu huku akiingia ndani.
Ndani ya chumba cha Jimmy hakukuta mabadiliko makubwa zaidi ya tivii ya flati na friji ndogo. Alikaa kwenye kochi wakati huo Jimmy alikuwa akielekea chumbani kuchukua fulana. Macho ya Kilole yaliona kitu kilichomshtua, kiuoni kwa Jimmy kulikuwa na mchoro ambao ulifanana na mchoro aliouona kwenye kiuno cha mtu wa kwenye picha ya watu waliombaka.
Moja kwa moja ushahidi wake ulikamilika alijua Jimmy ni mmoja ya watu waliombaka, alijilaumu kwa kuondoka bila siraha ambayo ingemsaidia kumaliza kazi kwani ushahidi wa kutosha kuwa Jimmy ndiye mbaya wake ulikuwa umetimia. Lakini bado aliamini Jimmy alikuwa kiungo muhimu wa kufanikisha mpango wake kabambe utakaomuwezesha kutimiza lengo lake.
Baada ya Jimmy kutoka chumbani akiwa amevaa fulana alikaa pembeni kidogo na Kilole.
“Ndiyo sister karibu sana.”
“Asante sana, mbona ndugu yangu umenitupa?” Kilole alijifanya kuchangamka japo moyoni alikuwa na hasira za kuua mtu. “Nikutupe wapi wakati kila kukicha mambo afadhari ya jana.” “Samahani sister unatumia kinywaji gani?” Jimmy aliuliza huku akinyanyuka kuelekea kwenye friji. “Walaa usisumbuke nashukuru.”
Jimmy alirudi kukaa kumsikiliza Kilole aliyeonekana na haraka.
“Sasa ni hivi nahitaji msaada wako wenye malipo mazuri sana.”
“Kazi gani tena sister?”
“Nina imani michongo ya mjini unaiju vizuri nilikuwa nahitaji unga.”
“Unga! Upi?” Jimmy alishindwa kumuelewa. “Kokeni.”
“Ha! Wa nini?” alizidi kushtuka.
“Dada yako najidunga muda mrefu lakini mtu aliyekuwa akiniletea amesafiri hivyo napata shida sana kubembea.”
“Mmh! Wa shilingi ngapi?”
“Kwa vile kuna watu wangu nao wana shida nilikuwa nahitaji wa milioni kumi.”
“Ha! Mbona mwingi?” “Tatizo mwingi au niupate, mbona kila kitu unashangaa.”
“Mmh! Ulikuwa unautaka lini?” “Leo hii na fedha ipo.”
“Na kamishina yangu kiasi gani?” “Wewe unataka shilingi ngapi?”
“Si unajua kazi za hatari hata laki mbili siyo mbaya.”
“Nitakupa milioni.”
“Ooh! Asante sana.” “Samahani Jimmy simu yako ina salio nataka nimpigie mtu wa tigo,” Kilole ambaye siku zote alijengwa uwezo wa kufanya mambo na mumewe Deus hata kumfundisha jinsi ya kutumia siraha kwa utimilifu tena kwa uhakika mkubwa.
Aliamini kupitia simu ya Jimmy ataweza kuipata namba ya mwenzake ambayo ingemsaidia kumfahamu na kuweza kumtia mikononi. Jimmy bila kujua alimpa simu yake, Kilole aliichukua na kujifanya anaingiza namba, kila alilofanya alimuangalia Jimmy ambaye hakuwa na habari naye.
Aliangalia simu iliyoingia jana yake usiku muda ambao yeye alikuwepo pale, baada ya kuiona ili kujiridhisha aliangalia iliyopigwa muda mchache baada ya Jimmy kutoka nje. Jina lilikuwa moja la Rich.
Baada ya kunukuu akilini ile namba alimrudishia simu yake, Jimmy naye bila kuhoji aliipokea simu yake. Kilole alinyanyuka kwenye kochi na kuanza kutoka nje. “Basi twende kwenye gari nikakupe hiyo fedha ili jioni nije niuchukue mzigo.”
Baada ya kusema vile Kilole alitangulia kwenye gari na kumsubiri Jimmy alipokuja alimuhesabia milioni kumi na moja kisha waliagana.
“Jimmy nakutegemea, basi usiniangushe kama zile picha ambazo ninanitia wazimu.”
“Ooh! Ina maana bado wanakusumbua?”
“Hawana lolote shida yao fedha sina jinsi nitawapa.”
“Ooh! Pole sana.”
“Ya kawaida, la muhimu nifanyie kazi yangu vizuri.”
“Hakuna tatizo sister kazi yako nitaifanya vizuri.”
Kilole baada ya kuondoka njiani aliwaza mengi huku hasira zikumpanda kichwani na kutamani kuwafanyia kitu kibaya. Lakini alikumbuka upumbavu wote anaoufanya ni kwa ajili ya kutetea penzi lake kwa Kinape. Hivyo alitakiwa kuwa makini kutekeleza mipango yake bila kumshirikisha mtu moja kwa moja hasa ya mauaji.
Kilole alirudi nyumbani kujipanga kuhakikisha kazi yake ya usiku wa siku ile anaifanya kwa umakini mkubwa japo moyo mwingine ulimshauri aachane na mpango ule wa hatari. Lakini upande wingine aliamini maji kaisha yavulia nguo lazima ayaoge na liwalo na liwe.
Wakati Kilole akipanga mkakati wa kummaliza Happy mchumba wa Kinape ili kuhakikisha haendi kijijini. Kinape naye alikuwa na mazungumzo na mpenzi wake sehemu tulivu waliyochagua, ambaye alikuwa akiteseka na mabadiliko ya mpenzi wake yaliyoonekana kutishia uhusiano wao.
Kinape pamoja na kujitahidi kuwa karibu na Happy lakini muda mwingi alibanwa na Kilole ambaye nia yake ilikuwa kuuvunja uhusiano ule.
“Kinape pamoja na kusema kesho unakwenda kunitambulisha kwenu bado siamini najua ni kunipoza moyo lakini hunipendi tena.”
“Happy kama kusingekuwa na umuhimu wa kwenda kukutambulisha kwetu ningekaa kimya usingejua nini kinaendelea?”
“Kinape lakini umegeuka kiasi hiki, nini nimekukosea?” Happy aliuliza kwa sauti ya kilio.
“Mambo yameingiliana tu lakini muda si mrefu kila kitu kitakuwa sawa,” Kinape alijitetea.
“Kuna kitu unanificha, Kinape una mwanamke mwingine.”
“Sina mwanamke mwingine zaidi yako.”
Kinape alijitetea japo alijua ana mtihani mzito kwa Kilole, moyoni mwake hakuwa tayari kumsaliti Deus rafiki yake kwa ajili ya mpenzi wake wa zamani.
Kilichomuumiza kichwa kilikuwa ni picha za kufanya mapenzi na Kilole ambazo kwake aliamini zilikuwa bomu ambalo kama lingepasuka kusingekuwa na usalama. Moyo alijipanga kuhakikisha anamfahamu aliyefanya mchezo ule, akiwa katikati ya mawazo Happy alimshtua.
“Ha..ha..lafu mbona simuelewi shemeji yako?”
“Umuelewi kivipi? Kinape alishtuka kidogo.
“Asingekuwa mke wa kaka yako ningesema mwanamke wako.” “Kwa nini unasema hivyo?”
“Kuna kila dalili za kuwepo siri nisiyojua kuhusu mustakabali wa penzi langu kwako. Mimi si wa kukatazwa kuingia ndani kwenu, hata kama haupo bado nina haki ya kuja kwenu.”
“Nimekuelewa lakini kila kitu kitakwenda vizuri, naomba uniamini na kesho ndiyo siku yako ya kuamini kuwa penzi letu lipo hai.”
“Mmh! Nitaamini mpaka nitakapokuwa mbele ya wazazi wako na kunitambulisha kuwa mimi ni mpenzi wako mkeo mtalajiwa.”
“Tena tumepewa lile lexus kwenda nayo kwa raha zetu.” “Usiniambie!” Happy alifurahi kwa kumkumbatia Kinape na kujisahau kama muda mfupi alikuwa akilaumu.
“Hii yote kukuonesha jinsi gani ninavyo kujali na ahadi niliyokuahidi ni ya kweli.” “Asante sana mpenzi wangu.”
“Si hilo tu, brother amenipa jana milioni 50 kwa ajili ya maandalizi ya harusi yetu.” “Jamani yaani matamani siku ifike niwe nisimame pembeni yako nikiulizwa: Happy Kinape unakubali kuolewa na Kinape kama mumeo?”
“Mmh! Utajibu nini?”
“Ndiyooooooo, tena mara mia.”
“Basi nikuache akajiandae na safari, kesho alfajiri nakupitia.”
“Sawa mpenzi wangu, katika siku ambayo nitakula chakula kiteremke sehemu zake ni leo, na siku tukifunga ndoa sijui itakuwaje bado naona ndoto ya mchana.”
“Nina imani kuanzia kesho utakula na kunywa kwa furaha baada ya kukuvisha pete ya milioni kumi.” “Haaaa!” Happy alishika mikono kifuani asiamini masikio yake.
“Nataka uamini ile ahadi niliyokuahidi inatimia.” “Kinape amini usiamini mabadiko yako kama yangeendelea kidogo nilikuwa nimewaza kufanya kitu kibaya.”
“Kipi tena mpenzi wangu?”
“Haki ya nani, leo isingepita salama nilipanga kunywa sumu nifilie mbali.”
“Aah! Happy mawazo gani tena hayo mpenzi wangu?”
“Hujui tu, nimeteseka sana, nimeumia sana, hebu nitezame mimi ndiye Happy unayemfahamu nimekuwa kama mti uliokauka.”
Happy alizungumza huku akiangua kilio ambacho kilikuwa sawa na kukamua uchungu wa moyo kutokana kuteswa na penzi la Kinape baada ya kutekwa na Kilole.
“Happy mpenzi wangu yote hayo yatakwisha hata mimi najua kosa langu lilikuwa wapi.” “Naomba usinitende nakupenda sana Kinape, sioni sisikii juu yako, bila wewe mimi sipo,” Happy aliendelea kusema huku akibubujikwa na machozi. “Basi mpenzi nimekuelewa nina imani nilikuumiza lakini nakuahidi kutuliza maumivu yako yote.”
Kinape alimpeleka Happy kwao na kuamua kwenda club ili aingie nyumbani usiku sana asionane na Kilole na alfajiri awahi kuamka na kuondoka ili kumkwepa.
Majira ya jioni akiwa amejipumzisha nyumbani kwake alipokea simu ikiulizia mzigo wao.
“Vipi umefikia wapi?” “Kila kitu kipo sawa ila sasa hivi nina wageni muhimu naomba univumilie kidogo.”
“Mpaka saa ngapi?”
“Sijajua ila lazima usiku huu nikupe mzigo wako wote kwa vile nimekwisha uandaa kabisa.” “Sasa tuambie saa ngapi?”
“Nimepanga baada ya mume wangu kulala nitoke mara moja, ila nilikuwa naomba uje karibu na nyumbani ili nikikukabidhi nirudi haraka kabla mume wangu hajashtuka kama nimetoka.”
“Kwa hiyo saa ngapi?” “Kuanzia saa sita usiku ila uhakika saa saba.”
“Hakikisha muda huo unatupa mzigo wetu ukifanya ujanja wowote picha zako zitasambaa kila kona ya jiji.” “Walaa usitie hofu nilichowaeleza kitakwenda kama nilivyopanga, naomba usikae mbali na simu yako ili nikikupigia utokee na kuchukua.”
“Nimekuelewa baadaye.”
Kilole baada ya kukata simu alicheka na kuuapia moyo wake usiku wa siku ile utabakia historia nzito moyoni mwake. Majira ya saa moja na nusu usiku Kilole alipigiwa simu ya Jimmy kumjulisha kupatikana kwa mzigo, walielekezana pa kuonana.
Alikwenda eneo la tukio na kupewa unga wake wa shilingi milioni moja. Baada ya kuupata aliamini kabisa utamsaidia kuifanya kazi yake kwa uhakika mkubwa. Aliagana na Jimmy na kurudi zake nyumbani na kuuficha sehemu ambayo mumewe hawezi kuiona.
Baada ya kuweka mzigo vizuri alichukua bastola ya mumewe na kuichunguza kama risasi, alikuta za kutosha aliamini zitafanya kazi yake ya usiku ule aliiweka vizuri kwa kazi ya usiku ule. Alichota unga kidogo na kuuweka kwenye chakula cha mumewe ili akila alale na yeye aweze kutoka usiku ili akafanye kazi yake nzito ambayo ilimpa mtihani mzito. Baada ya kuipanga mipango yake vizuri, alitulia kusubiri muda. Mumewe baada ya kutoka kazini alimuandalia chakula.
Baada ya kula alimuomba waende wakazungumzie chumbani. Waliingia chumbani huku Deus akikisikia kichwa kizito. Hata wakuwahi kuzungumza usingizi mzito ulimpitia. **** Ndani ya jiji Sicily nchini Italia, jiji linalosifika kwa uuzwaji wa dawa za kulevywa,Teddy bado alikuwa na hasira baada ya kugundua shemeji yake ndiye aliyemchoma kwa kitengo cha kuzuia dawa za kulevya Tanzania. Kwake alimuona ni adui mkubwa asiyefaa kuendelea kuishi.
Alipanga usiku wa siku ile amuulie mbali na yeye kutimka zake kwenda mji mwingine wa Turin kuanzisha maisha mapya kwa kuamini uwezo wa kifedha ungemwezesha kuishi sehemu yoyote duniani bila tatizo.
Baada ya kugundua kuwa shemeji yake ndiye mbaya wake hakutaka kumuonesha kukasilishwa na kitendo kile. Ili kumvuta adui yake alijifanya kubadilisha msimamo kuwa amemkubali kimapenzi. Asubuhi ya siku ile baada ya kifungua kinywa alimwita Mose na kumweleza kitu:
“Mose my sweet.”
“Teddy kauli hiyo imeanza lini?” Mose alishtuka kusikia anaitwa vile.
“Leo mpenzi, nimetafakari na kuona hakuna umuhimu wa kulikataa penzi lako kwa vile wewe ni mwanaume kama wanaume wengine pia kuwa na wewe sawa na kuwa na marehemu kaka yako.”
“Umeona eeeh,” Mose alifurahi kusikia vile bila kujua aliyekuwa anazungumza naye si Teddy aliyemzoea bali malaika wa kifo.
“Unajua Mose nimekuwa sipati jibu kila nilipojiuliza kwa nini nisikukubalie uwe mpenzi wangu, lakini ujio wa safari yangu Italy ilikuwa kuja kukueleza nimekufungulia moyo wangu kwako.”
“Ooh! Asante sana, siamini kwa kweli lazima nikueleze ukweli Teddy nimeteseka kwa muda mrefu juu yako. Nina imani sasa hivi moyo wangu utapoa.”
“Najua umeumia kwa muda mrefu, nina imani kama uliteseka juu yangu basi penzi letu litakuwa lenye upendo wa dhati. Mose mpenzi naomba usinitende.”
“Teddy amini nitakupa mapenzi zaidi ya kaka, hutajutia kunikubali kuwa mpenzi wako.”
Siku ile ilikuwa yenye furaha kwa Mose lakini moyoni kwa Teddy ilikuwa ngumu sana kwake kwa kujipanga kuhakikisha kujirahisi kule kutamlahisishia kummaliza kwa urahisi. Teddy hakuona hiyana kuutoa mwili wake kwa Mose japo alikwisha muapia labda atafanya naye mapenzi akiwa marehemu asiye na fahamu.
Siku ile alijitoa ili kumvuta karibu na kuamini kabisa anachokitafuta muda mrefu atakipata. Majira ya mchana Teddy alibuku tiketi ya ndege ya kuelekea Turin saa tatu usiku, baada ya kurudishiwa taarifa ya kupatikana kwa nafasi katika ndege ya usiku ule.
Alijipanga kuhakikisha mipango yake inakwenda kama alivyopanga na saa tatu awe kwenye kiti cha ndege akihamia jiji wa Turin kuanza maisha mapya baada ya kummalizia mbali shemeji yake Mose aliyetaka kumpoteza kwenye ramani ya dunia.
Baada ya mambo yake kwenda alivyopanga alirudi kwa Mose na kuendelea kunywa katika mahaba mazito. Mose baada ya kulewa sana Teddy alitumia nafasi ile kumpeleleza kupata ukweli. “Mose mpenzi wangu kwa nini ulinichoma?” Teddy alijifanya kulalamika katika mahaba mazito.
“Teddy ulinichanganya kimapenzi kwa kweli nilichokifanya hata sielewi nilifanya nini, nilikuwa sawa na mfa maji.”
“Lakini usirudie tena, ona sasa kama ningefungwa penzi tamu kama hili ungelipata wapi?”
“Nisamehe mpenzi wangu.”
Kauli ya Mose ilizidisha machungu moyoni kwa Teddy na kuamini wazo lake na ushahidi aliopata lilikuwa sahihi.
Alijitahidi kutengeneza tabasamu la uongo ili kuvuta muda wa kummaliza Mose. Muda wote alionesha mapenzi mazito yaliyomziba masikio asijue nini kilichokuwa kikiendelea.
Majira ya saa moja na nusu Teddy aliamini ule ulikuwa muda muafaka kwake kufanya alichokikusudia, hakutaka kumuua Mose kwa bastora kwa kuhofia sauti yake unaweza kufika mbali.
Kwa vile alikuwa amefunga dirisha la chumbani na kuamini sauti haitatoka nje aliona kisu kingefanya kazi yake vizuri kutokana na Mose kulewa sana asingeweza kushindana naye. Wakiwa watupu kitandani Teddy alisema kwa sauti ya mahaba: “Samahani mpenzi.”
“Bila samahani,” Mose alijibu kwa sauti ya kilevi.
“Nakuja mara moja,” Teddy alisema huku akinyanyuka kitandani.
“Basi usichelewe mpenzi, leo moyo wangu una furaha ya ajabu.” “Usihofu leo mimi na wewe mpaka lyamba.”
Teddy alikwenda hadi kwenye kabati na kuchukua kisu kikubwa na kurudi nacho kitandani. Wakati huo Mose alikuwa amejilaza chali akiwa amefumba macho kutokana na kunywa kiasi kikubwa cha pombe. Teddy alimkalia tumboni kama anataka kumuandaa kimahaba. Kwa sauti iliyojaa ukatili isiyo na chembe ya huruma alisema: “Wee mbwa Sali sala yako ya mwisho.”
“Vipi tena mpenzi?” Mose aliuliza huku alijitahidi kufumbua macho yaliyokuwa mazito kutokana kunywa pombe nyingi kupita kiasi. Macho yake hayakuamini kuona Teddy amemshikia kisu.
“Ha! Nini tena?” “Unauliza jibu, nilikueleza nini siku moja?”
“Mpenzi mbona sikuelewi.”
“Nilikueleza toka mwanzo kuwa hutaugusa mwili wangu labda maiti yangu, lakini leo umeugusa nikiwa mzima ni ishara ya kifo chako.” “Kwa hiyo unataka kuniua?”
“Si ulitaka kunipoteza? Sasa nakupoteza wewe.”
“Si..si..nimekueleza sa..sa..babu yake,” Mose alijitetea akiwa bado amelala chali mwili haukuwa na nguvu kutokana na kulewa sana.
“Fedha yote niliyopoteza baada ya kukamatwa itanunua kifo chako,”
Teddy alisema huku akikipunga kisu hewani.
“U..u..usi..ni..”
hakumalizia alikutana na mapigo ya kisu mfululizo yaliyompiga bila mpangilio.
Teddy alimshambulia Mose kwa visu mfululizo kama anatengeneza chujio la nazi. Mose kutokana na ulevi wa kupindukia hakuweza kujitetea.
Baada ya kupiga kelele za maumivu kwa muda bila msaada sauti ilizidi kupungua mpaka aliponyamaza kabisa, wakati huo kitanda kizima kilikuwa kimejaa damu kama kachinjwa ng’ombe ambazo zilizomrukia Teddy mwilini.
Teddy baada ya kuamini amemaliza kazi, alinyanyuka na kukimbilia bafuni kuoga kisha alibadili nguo na kuchukua vitu vya muhimu na kuhakikisha picha zake zote ameondoka nazo. Baada ya kubeba mizigo yake alikodi gari hadi uwanja wa ndege.
Alifika ikiwa imebakia nusu saa ndege iondoke, baada ya kupima mizigo alielekea kwenye ndege na kuketi huku akiomba Mungu aondoke kabla ishu haijashtukiwa. Hakujiamini mpaka ndege alipoondoka katika jiji la Sicily, safari yake ilikwenda vizuri mpaka alipotua katika jiji la Turin salama salimini. Alitafuta hotel yenye hadhi ya nyota tano iitwayo Principi di Piemonte.
Baada ya kupata chumba aliagiza chakula na kula kidogo kwani bado picha ya kitendo cha kinyama alichomfanyia shemeji yake ilijirudia akilini mwake. Aliamua kuagiza pombe kali ambayo alikunywa mpaka alipopoteza mawasiliano na kulala alipokuwa amekaa. Alishtushwa siku ya pili na hodi iliyokuwa ikigongwa.
Alishangaa kujikuta amelala pembeni ya kitanda kwenye zulia. Aliponyanyuka alizidi kujishangaa kukuta haja ndogo aliimalizia pale bila kujielewa kutokana na kunywa pombe nyingi kupita kiasi.
Alinyanyuka na kukimbilia bafuni na kuchukua cha kufutia kisha alifungua mlango.
“Za saizi?” mhudumu alimsalimia. “Nzu..nzuri, karibu.”
“Asante, nilikua naomba kufanya usafi.”
“Kwani sasa hivi ni saa ngapi?”
“Saa tano.” “Ooh! Kumbe nimelala sana.”
“Inaonesha ulikunywa sana.”
“Okay, fanya haraka usafi nataka kupumzika.”
Teddy alimwacha mhudumu afanye usafi, baada ya kufanya usafi alioga na kuagiza kifungua kinywa kisha alizimua kidogo. Akiwa amejipumzisha kwenye sofa huku akinywa whisky taratibu, tukio la jana yake lilimjibu kwenye akili na kujikuta akiwasha luninga labda habari za kifo cha Moze kitatangazwa.
Alifungua luninga ya taifa, alikuta kuna matangazo ya magazeti na moja ya habari iliyotawala kwenye ukurasa wa mbele ilikuwa yake. Kichwa cha habari kilisomeka unyama wa kutisha, juu kulikuwa na picha ya Mose akiwa amelala kitandani mwili wote ukiwa katika dimbwi la damu.
Picha ile ilimtisha alijikuta akifumba macho kwa woga na kuchukua chupa ya whisky na kuipeleka mdomoni kwake na kujaza kiasi kikubwa na kukimeza chote kwa shida huku amefumba macho mpaka mishipa ya kichwa ikamsimama, baada ya kutikisa kichwa alisema kwa sauti ya chini.
“Ooh! Mungu wangu, nimemuua Mose kifo kibaya sana.”
Akiwa ameinamisha kichwa huku akisikitika na machozi kumtoka kutokana na unyama aliofanya, alinyanyua macho na kushtuka kuona Mose hakufa yupo hospitali ila katika chumba cha wagonjwa mahututi. Akiwa bado anatumbulia macho habari za Mose ambaye alionekana mfu.
Alimuona mkuu wa makosa ya jinai akitoa taarifa kuwa mpaka muda ule upelelezi ulikuwa unaendelea ili kujua nani aliyefanya tukio la kikatili kama lile baada ya kukosa ushirikiano wa mgonjwa ambaye alikutwa katika hali mbaya mpaka wakati ule alikuwa akipumua kwa mashine. Taarifa za daktari zilisema mgonjwa kutokana na kupoteza damu nyingi kutokana na kutobolewa na kitu chenye ncha kali aliongezwa damu zaidi ya chupa kumi.
Habari zile hazikumfurahisha hata kidogo Teddy na kuamini kama Mose atapona na kutoa ushahidi basi atamtia kwenye matatizo makubwa na akishikwa adhabu yake ni kifo. Wazo la haraka lilikuwa kuondoka ndani ya nchi ya Italy na kwenda kuishi Afrika kati ya nchi ya Tanzania au Kenya. Aliamini upelelezi lazima utajua kuwa ni yeye mhusika aliwasiliana na washirika wake na kukubaliana akajifiche Kenya mpaka hapo mambo yatakapojulikana yamefikia wapi.
Bila kupoteza muda alipanda ndege moja kwa moja mpaka Kenya na kwenye kujificha katika jiji la Nairobi katika jumba moja la mshirika wao lililokuwa na kila kitu ndani maeneo ya Kasalani. Mwezi mmoja akiwa anaishi kwa kificho katika jiji la Nairobi aliziona habari na picha yake za kutafutwa kwake kuhusiana na jaribio la kutaka kumuua Mose.
Baadhi ya vyombo vya habari na luninga alitoa kila siku sura ya Teddy kutafutwa huku donge nono likitangazwa kwa mtu atakayetoa habari zake na kufanikisha kukamatwa. Taarifa zile zilizidi kumficha Teddy ambaye alikuwa akitoka usiku tu kwenda club za usiku na baada ya hapo alishinda ndani tu. Aliweza kumuona Mose katika hali ya umajeruhi kutokana na shambulio kali la kutaka kumuua.
Mwili wake ilionesha kuharibika vibaya hata kuzungumza kwake alizungumza kwa shida. Katika mahojiano na mwandishi wa habari mmoja alimsikia akisema kuwa akipona atamtafuta popote hata kaburini ili kulipa kisasi.
****
Majira ya saa sita za usiku Kinape alijirudisha nyumbani kwa kuamini muda ule Kilole atakuwa amelala. Alipokaribia nyumbani aliona teksi ikisimama mbele kidogo na nyumbani kwao. Aliendelea kusogea kwa vile alikuwa upande wa giza aliweza kuliona lile gari ambalo hata namba zake hazikuwa ngumu kuzinakili kichwani.
Kabla ya kupiga hatua alishangaa kumuona mwanamke aliyevaa hijabu na nikabu iliyomziba uso wake akitelemka kwenye teksi na kuelekea kwenye geti la nyumba yao na gari ile kuondoka. Alijuliza ni nani aliyevaa vazi lile kuelekea kwao muda kama ule. Ilibidi atembee kwa taadhari ili kujua yule mwanamke anakwenda kufanya nini kwao muda ule.
Alisimama nje ya uzio na kuweza kumuona yule mwanamke akifungua mlango kwa taadhari kubwa, alijiuliza yule mwanamke ni nani au mwizi. Hakutaka kumshtua alitulia kutaka kuona mwisho wake, lakini kilichomshangaza kilikuwa kufungwa mlango kwa ndani. Moja kwa moja alijua yule ni Kilole, lakini swali lilikuwa usiku ule anatoka wapi na katika vazi lile ambalo hakuwahi kuliona hata siku moja.
Hakutaka kupitia mlango wa mbale alizunguka nyuma na kuingia chumbani kwake kwa kutumia dirisha. Mara zote anapojua anachelewa kurudi alilitegesha dirisha na aliporudi aliingilia kupitia dirishani.
Baada ya kuingia ndani alibadili nguo na kwenda kuoga na kurudi kulala ili alfajiri awahi kuamka kabla Kilole hajaamka. Alikumbuka muda wote alizima simu ili kumkwepa Kilole asimsumbue, alipowasha haikuchukua muda simu iliita. Ilikuwa simu ya dada ya mchumba wake, aliipokea. “Haloo shemu.”
“She..she..mu,” hakuendelea kuzungumza alivuta kamasi za kilio kitu kilichomshtua Kinape na kutaka kujua kuna nini, kwani simu ilikuwa hewani kwa mbali alisikia sauti kama za vilio.
“Haloo shemu,” aliita lakini upande wa pili haukupokea zaidi ya kuendelea kusikia vilio vya upande wa pili.
Aliamua kukata simu na kupiga, iliitaka kwa muda mfupi ilipokelewa upande wa pili na dada ya mchumba wake.
“Shemu upo wapi?” aliulizwa.
“Nyumbani.”
“Una habari gani za Happy?” “Sina! Amefanya nini?” alishtuka.
“Amefariki.”
“Nini?” Kinape alishtuka. “Amefariki,” kauli ile ilirudiwa. “Muongo acha kunirusha roho shemeji.”
“Si kukurusha roho ukweli ni huo mchumba wake ameuawa saa mbili zilizopita.”
“Hapana sikubali Happy hawezi kufa kirahisi namna hiyo nimeachana naye jioni akiwa na mzima wa afya.”
“Hakufa kwa ugonjwa.”
“Nini kimemuua mpenzi wangu?” “Ameuawa.”
“Nini?”
“Ameuawa.”
“Na nani?”
“Hatujajua ile sasa hivi tunaupeleka mwili wa Happy hospitali.”
“Nakuja sasa hivi.”
Kinape alikata simu na kujikuta akichanganyikiwa kwa kuvaa fulana na taulo. Alikwenda moja kwa moja kugonga katika mlango wa Deus kumjulisha taarifa za mchumba wake Happy.
Aligonga mlango kwa muda, Deus aliyekuwa kama yupo ndotoni alishtuka na kunyanyuka hadi mlango. Alipofungua alikutana na Kinape aliyekuwa akitokwa na mchozi na macho yalikuwa mekundu kuonesha ana tatizo zito.
Deus alishtuka na kutaka kujua rafiki yake kipi kimemsibu usiku mkubwa kama ule.
“Best vipi?” Kinape alishindwa kuzungumza alijitupa kifuani kwa Deus na kuangua kilio bila kusema neno.
“Best kuna nini?”
“Happy.”
“Happy amefanya nini?”
“Amefariki.”
“Wewe! Acha utani, si leo asubuhi mnakwenda kijijini?” Deus alishtuka na kumshika Kinape mabegani na kumsogeza mbele yake ili kumtazama vizuri.
“Ndiyo, lakini nimepigiwa simu muda huu amefariki.”
“Alikuwa akiumwa?” “Hapana.”
“Nini kimemuua?”
“Na..na..sikia.. ameuawa.” “Ameuawa! Na nani?”
“Hata wao hawajui.”
“Mwili wa marehemu upo wapi?” “Wameniambia ndiyo wapo njiani kuupeleka hospitali.”
“Unasema kauawa, kivipi?”
“Hata najua, nakwenda kujua huko huko.”
“Nisubiri basi tuongozane.”
Deus alirudi chumbani kumjulisha mkewe habari za Happy.
“Mke wangu,” alimwita huku akimtikisa.
“A.aa..bee mume wangu.” “Kuna tatizo limetokea.” “Tatizo gani tena?” Kilole aliuliza huku akifikicha macho. “Happy amefariki.”
“Nini?” Kilole aliuliza kwa mshtuko. “Happy amefariki.”
“Acha utani, Happy mchumba wa shemeji Kinape?”
“Ndiyo.”
“Muongo, si kesho wanakwenda kijijini kumtambulisha?”
“Ndiyo.”
“Nini kimemuua?”
“Nasikia ameuawa saa mbili zilizopita.”
“Sasa inatakuwaje, kwani Kinape yupo wapi?” “Yupo ananisubiri twende hospitali.”
“Sasa hospitali kufanya nini ikiwa mnasema amekwisha kufa?”
“Wamesema wanaupeleka mwili wa marehemu.”
“Kwa hiyo twende wote?”
”Hapana nilikuwa nakutaarifu tu.”
Wakati Deus akibadili nguo ili awahi hospitali, Kilole alitoka nje na kilio hadi kwa Kinape na kujitupa kifuani kwake.
“Maskini shemeji yangu nini kimemsibu mke mwenzangu?”
“Ha..ha..ta sijui.”
“Kinape tuwahi nipo tayari,” Deus alisema huku akimtoa Kilole kifuani kwa Kinape.
“Okay twende.”
“Mbona hujabadili nguo?”
“Mbona nipo sawa.”
“Sasa utakwenda na taulo?”
Kinape alipojiangalia akijikuta amejifunga taulo, alikimbilia ndani kubadili kisha walitoka kuwahi hospitali.
Walipofika walikuta mwili wa Happy ndiyo umefikishwa muda mfupi ukiwa bado upo katika gari la polisi, dada yake Happy alipomuona Kinape alimkimbilia na kujitupa kifuani kwake na kuangua kilio cha sauti.
“Ooh! Shemeji mdogo wangu wamemuua.”
“Hapana si kweli Happy hawezi kufa kirahisi namna hiyo,” Kinape alisema kwa sauti ya juu huku akimkumbatia shemeji yake.
“Kweli mdogo wangu amekufa, yaani wamemuua kama jambaziii…amewakosea nini mdogo wangu mimiii,” dada yake Happy aliendelea kulia akiwa bado amejilaza kifuani.
Wakati huo kitanda cha kuuchukulia mwili wa Happy uliokuwa umefunikwa shuka kilikuwa kimesogezwa karibu kabisa na gari la polisi.
Kinape alijitoa kwenye mikono ya dada yake Happy na kwenda kwenye gari la polisi wakati huo askari walikuwa wakiushusha mwili wa Happy uliokuwa ulifunikwa na shuka jeupe lililojaa damu.
Baada ya kuulaza mwili juu ya kitanda cha magurudumu, Kinape alisogea karibu kabisa akiwa bado haamini kama kweli mpenzi wake Happy amekufa. Aliishika shuka upande wa kichwani na kuanza kuifunua huku mikono ikimtetemeka. Macho yake yalikutana na uso wa Happy aliyeonekana kama umelala.
“Happy mpenzi wangu amka,” alimwita kwa sauti huku akimtikisa taratibu.
“Shemeji amekufa mdogo wangu,” dada Happy ambaye alikuwa akilia kuliko watu wote waliokuwa pale alikwenda kuungana na shemeji yake ambaye alikuwa bado akiona kama kiini macho kilichokuwa mbele yake.
“Happy mpenzi wangu amka huwezi kufa kirahisi mpenzi wangu, huwezi kuniacha peke yangu, leo asubuhi tunakwenda kwa wazazi wangu wakakutambue. Hata kaka Deus yupo hapa ametoa gari ili lake la kifahari ili nikupeleke kijijini…Amka mpenzi amka ni wewe peke yako niliyekuchagua… Hapiiiiiiiiii,” Kinape alimtikisa kwa nguvu ili aamke lakini mwili ule haukuwa na uhai. Kinape alilia kwa uchungu, Deus alimchukua na kumuondoa kwenye kitanda na kumpeleka pembeni kumbembeleza.
“Deus niache huu ni unyama wa hali ya juu, inaniuma kwa nini wamuue mpenzi wangu nimewakosea nini?” alisema huku akipiga chini. “Pole rafiki yangu, kazi ya Mungu haina makosa.” “Noooo, hapana hii si kazi ya Mungu ni mashetani wasiopenda kuona Kinape na Happy wanaoana.”
“Basi…basi, wewe mwanaume unatakiwa kuyashinda maumivu ya moyo wako,” Deus aliendelea kumbembeleza. “Yaani Happy…hata siamini haiwezekani Happy hajafa,” Kinape alimponyoka Deus na kukifuata kitanda kilichokuwa kikielekea chumba cha uchunguzi kabla ya kupelekwa Mochwali. Alichepua mwendo huku akimwita kwa sauti kama anamsikia, lilikuwa pigo mujalabu ambalo hakulitegemea kipindi kile.
“Jamani mnampeleka wapi mpenzi wangu, Happy hajafa amelala mwambieni aamke leo asubuhi nakwenda kumtambulisha kwa wazazi,” kifo cha ghafla cha Happy kilimchanganya Kinape na kuonekana kama chizi. Lakini Deus alimuwahi na kumketisha chini rafiki yake.
“Kinape hebu kuna kuwa na moyo wa kiume.”
“Siwezi, siwezi Deus inauma sana.” “Najua inauma lakini imekwisha tokea kinachotakiwa kutafuta chanzo cha kifo chake.”
Baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wa Happy alipelekwa mochwali kwa ajili ya kusubiri kuchukuliwa na kwenda kuzikwa.
Kilole alijikuta akijigeuzageuza kitandani akiyakumbuka matukio yote aliyoyafanya usiku ule. Moyo ulimuuma kwa kitendo cha kikatili lakini hakuwa na jinsi ilikuwa lazima afanye vile ili kupata anachokitaka. Matukio yalipokuwa yakijirudia kichwani alikwenda hadi kwenye friji ndogo ya chumbani na kuchukua chupa ya pombe kali na kunywa glasi nzima.
Baada ya kunywa alijikuta akipitiwa na usingizi na kujilaza nusu ya kitanda, Deus aliporudi toka hospitali alishangaa kumkuta mkewe aliyemwacha amelala akiwa katika hali ya ulevi. Alimshtua toka usingizini kwa kumwita na kumtikisa ili alale vizuri.
“Mke wangu.”
“Tafadhali, mimi sijamuua Happy,” Kilole alikurupuka usingizini baada ya kumuona mumewe amemsimamia mbele yake. “Nani kakuambia umemuua?”
“Sa..sa mahani mume wangu,” Kilole alijibu kwa sauti ya kilevi. “Mbona umekunywa pombe?”
“Hivi kweli Happy amekufa?”
“Kweli amekufa.”
“Basi kila dakika ananijia ndotoni, nikaamua bora ninywe pombe kali nilale fofofo.”
“Ooh! Pole sana.”
“Umefikia wapi?”
“Tumerudi kila kitu kitakuwa asubuhi ya leo.”
Siku ya pili asubuhi wakiwa sebuleni Kilole na Deus wakimsubiri Kinape atoke chumbani ili wawahi msibani huku macho yao yalikuwa kwenye runinga katika taarifa ya habari ya asubuhi ile. Katika taarifa ile ya habari vilitangazwa vifo vya watu watatu vilivyotokea usiku wa kuamkia siku ile waliouawa kwa risasi.
Mmoja wa maiti hizo alikuwemo mchumba wa Kinape, Happy, wengine waliouawa ni Jimmy mpiga picha na rafiki yake Rich. Deus alishtuka kuona na Jimmy amekufa mtu aliyekuwa akimfahamu kwa kumpiga picha nyingi zikiwemo za birthday na mkewe.
Taarifa ya habari ilielezea kwa ufasaha vifo vile kuwa mwili wa Happy ilikutwa nje ya geti la nyuma yao na miili mingine ya wanaume wawili Jimmy na Rich ilikutwa katika chumba cha Jimmy wote wakiwa wameuawa kwa risasi.
Pia taarifa iliongeza kupitia mashahidi majirani wa nyumba ile kuwa usiku wa saa sita walimuona mwanamke mmoja aliyekuwa amevaa hijabu iliyomziba mwili wote aliyeingia mule ndani.
Kwa vile hawakuwa na wasiwasi naye hawakujishughulisha naye lakini baadaye katikati ya usiku waligundua Jimmy hajafunga mlango kitu ambacho hakikuwa kawaida yake. Walipokwenda ndani ndipo walipokuta tukio lile la kutisha. Zilioneshwa picha za Jimmy na Rich zilivyokuwa zimelala kwenye kochi na sakafuni.
Lakini maiti ya Happy haikuonekana kutokana na kuchelewa kwa taarifa kufika kwenye vyombo vya habari. Kinape aliyekuwa ndiyo anafika sebuleni aliliona tukio lile. Kilichomshtua ni picha ya Jimmy.
“Jamani huyu si Jimmy mpiga picha?”
“Ndiye mwenyewe.”
“Mungu wangu na yeye kafanya nini?”
“Tena nasikia muuaji ni mwanamke,” Deus alimwambia Kinape aliyekuwa amesimama nyuma ya kochi waliokalia. “Mwanamke!” Kinape alishtuka.
“Ndiyo, tena alikuwa amevaa hijabu iliyomzima mwili wote.”
“Unataka kuniambia ndiye aliyemuua Happy?”
“Walaa, mume wangu hawakusema yule mwanamke ni muuaji bali ndiye aliyeingia chumbani kwa Jimmy,” Kilole alipinga kauli ya mumewe.
“Kwa nini ujifiche lazima atakuwa muuaji.”
“Jamani tuachane na hayo tuwahi msibani tukajue nini kinaendelea,” Kinape alikatisha ubishani wa mtu na mkewe.
Wote walinyanyuka kuelea nje kwenye gari, njiani wakiwa ndani ya gari kauli ya Deus kuhusiana na msichana aliyemshtumu kuvaa hijabu ilimshtua na kukumbuka jinsi alivyo mshangaa Kilole aliyekuwa amevaa usiku ule. Alijiuliza kama ni yeye aliyefanya mauaji yale alifanya kwa lengo gani. Alizidi kujiuliza kuhusu kifo cha Happy anaweza kuwa pia ni yeye?
Msibani watu walikuwa wengi huku kila mmoja akizungumza la kwake, wengi walikuwa walionekana na huzuni hasa familia ya Happy baba, mama na dada yake ambaye alilia mpaka kupoteza fahamu. Mashoga zake nao walichanganyikiwa kwani walikuwa katika maandalizi ya harusi ambayo walipanga iwe ya kukata na shoka baada ya kuelezwa siku ile ndiyo ilikuwa ya kwenda kutambulishwa kijijini kwa mchumba wake. Kinape naye muda mwingi alikuwa amekaa chini kutokana na kutokuwa na nguvu za kusimama.
Deus alitumia muda wake mwingi kuwa karibu ya rafiki yake kumfariji kwani kila rafiki na ndugu wa Happy walipolia naye aliporomokwa na machozi. Kila aliyekuwepo msibani uso wake ulijaa simanzi nzito kutokana na kifo Happy msichana aliyekuwa bado mbichi pia mwenye malengo mazito katika maisha yake. Lakini ilikuwa tofauti kwa Kilole na wote waliokuwepo msibani, moyo wake ulijaa furaha kwa kutimiza lengo lake la kuweza kuuvunja uchumba wa Kinape na Happy ambao aliamini hautaunganika mpaka mwisho wa dunia.
Wakati watu wakiendelea kulia huku ibada ikiendelea kabla ya kuuchukua mwili wa Happy haujaenda kupumzishwa Kilole alijikuta akivuta kumbukumbu ya matukio ya kikatili aliyoyafanya jana.
Aliamini kabisa kwa Happy alifanya unyama wa hali ya juu, lakini kwa Jimmy na rafiki yake ilikuwa ni kulipa kisasi cha kubakwa kwani aliamini adhabu ya mbakaji Uarabuni au China ni kifo. Pia alikuwa kutimiza kile alichomuahidi Jimmy kama picha zake zitavuja basi angemfanyia kitu kibaya. Aliamini vifo vyao vilibakia simulizi ndani ya vinywa vya watu.
Alianza kukumbuka jinsi alivyotoka nyumbani baada ya kuhakikisha mume wake amelala fofofo baada ya kumwekea madawa kwenye chakula. Kwanza alimpigia simu Kinape ajue yupo wapi kwani alipanga na yeye siku ile naye angelishwa chakula kile na kulala fofofo ili aweze kutoka bila kutiliwa wasiwasi na mtu.
Lakini simu ya Kinape haikuwa hewani ile haikumsumbua sana japo wasiwasi wake aliwaza huenda wapo pamoja na Happy. Baada ya kuvaa vazi lake lililomziba mwili mzima, alichukua bastora ya mume ambayo aliikagua na kukuta risasi za kutosha.
Alichukua na kiwambo cha kuzuia sauti. (bomba linalowekwa mbele ya bastora au bunduki kuzuia sauti) Baada ya kuviweka vitu vyake vizuri alikwenda hadi kwenye bodaboda na kukodi. “Samahani kaka angu, Masaki shilingi ngapi?”
“Masaki ipi?”
“Mwanzoni kutokea Salenda?”
“Kwa vile usiku buku ishirini.”
“Naomba uniwahishe.”
Baada ya kupanda dereva aliondoa pikipiki kwa mwendo wa kasi kidogo, Alipokaribia nyumba ya kina Happy aliomba ashushwe mbali kidogo. Kwa vile muda ule magari hayakuwa mengi alitumia dakika kumi tu.
“Nina imani umewahi?” dereva wa bodaboda alimuuliza huku akipaki pikipiki. “Ndiyo ila naomba unisubiri hapa.”
“Dada mbona unanitisha?” aliogopa kukabwa.
“Hapana kaka yangu, bado kuna sehemu nakwenda, nafika nyumbani mara moja narudi sasa hivi.”
“Na fedha yangu?” “Chuku hii nikirudi tutapatana tena,” Kilole alipa dereva elfu arobaini.
“Poa wahi basi.”
Kilole alichepua mwendo kuwahi nyumbani kwao na Happy ambapo palikuwa na kipande chenye giza kutokana na nyumba za sehemu ile kuachana eneo kubwa. Alipokaribia alitoa simu yake ambayo aliiseti sauti ambayo muongeaji huwezi kuijua sauti yake mara moja hata laini alikuwa ameinunua siku ileile ambayo ilikuwa haijasajiliwa.
Baada ya kujipanga alipiga simu ya Happy ambaye alikuwa amejilaza kitandani akiwaza safari ya kesho yake ambayo alijiuliza sijui itakuwaje atakapo kutana na wazazi wa Kinape mwanaume aliyemkabidhi moyo wake. Happy aliichukua simu yake na kuitazama namba ambayo ilikuwa ngeni kwake, aliipokea. “Haloo.”
“Haloo Happy hongera shosti.”
“Ya nini?”
“Yaani kumbe kesho unakwenda kutambulishwa ukweni hujanijulisha.”
“Lakini hiyo si kwenda kutambulishwa lakini mambo bado, nikirudi kila kitu kitakuwa wazi, lakini mazungumza na wewe bado asijakufahamu sauti yako?”
“Mimi Betha,” Kilole alimdanganya.
“Betha yupi?”
“Happy hilo si muhimu kama hili ninalotaka kukueleza?”
“Lipi tena hilo?” Happy alishtuka na kujiweka vizuri kitandani. “Najua
naweza kuonekana mbeya lakini lazima niseme juu ya tabia za mchumba wako Kinape.”
“Tabia gani?”
“Japo kweli ni mchumba wako lakini si muaminifu, hivi ninavyozungumza yupo nje ya gari tulilokuja nalo na shoga yangu wakilana denda kibaya zaidi ni jirani na nyumba yenu kweli huu ni ustaarabu?” “U..u..unasema?” Happy aliingia kigugumizi.
“Tena kama unaweza wahi uwafumanie ‘live’ ukichelewa hata dakika kumi Kinape ataondoka.”
“Okay, nakuja.”
Happy bila kumweleza mtu alikurupuka kuwahi kumfumania Kinape, wakati huo Kilole alijiandaa kummaliza baada ya kujua anakuja.
Alitoa bastora na kufunga kiwambo na kumsubiri. Mara alimuona akitokeza kwao akiwa na gauni la kulalia bila hata ya viatu kwani aliamini angevaa kiatu angechelewa kufumania.
Kwa vile alikuwa kwenye giza alimuona Happy akisogea upande ule akipepesa macho, alitumia nafasi ile kumpiga risasi mbili za kifuani upande wa kushoto kama alivyoelekezwa na mumewe Deus jinsi ya kuua adui kwa risasi.
Alimuona Happy akiruka kwa nyuma hakutaka kuona kinachoendelea alichepua kwendo huku akiiweka bastora ndani ya hijabu. Alipofika alimwambia dereva wa bodaboda: “Tuondoke.”
“Tunaelekea wapi?”
“Mikocheni B.”
Baada ya msiba Kinape alibakia kwenye kaburi na mpenzi wake ambaye usiku wa jana yake alikuwa naye kabla ya kuagana kuonana alfajiri ya siku ile kwa ajili ya safari ya kijijini. Alibakia ameliinamia kaburi huku msiba kwake ukianza upya.
Deus na ndugu na jamaa walimbembeleza sana mpaka alipokubali kuondoka makaburini. Moyoni aliapa lazima atamshikisha adabu aliyehusika na kifo cha Happ. Mwanzo alikuwa na wasiwasi na Kilole, lakini kilio alicholia kumlilia mchumba wake aliamini kabisa hausiki kabisa.
Usiku wakiwa nyumbani Deus katika kutafuta vitu kwenye kabati alishtuka kuona kiwambo cha bastola yake kipo kwenye nguo. Alishtuka kwani siku zote hukiweka mbali kutokana na kutotumia sana kutokana na matukio ya kijibizana kwa risasi na wauza madawa ya kulevya kupungua.
Alikichukua na kukinusa kilionesha kimetumika, alijiuliza mbona kinanuka baruti kama kimetumika. Wazo la haraka lilikuwa kuikagua bastola, alipofungua droo alishtuka kuona haipo kama alivyoiweka.
Aliitoa na kuifungua upande wa risasi, alizidi kushangaa baada ya kuzikuta pungufu ya risasi sita. Alijiuliza bila kupata jibu kuwa risasi zile zimekwenda wapi, alinusa mdomo wa mtutu wa bastora na kukuta umetumika.
Alijikuta akipata wasiwasi na kumwita mkewe aliyekuwa sebuleni akizungumza na Kinape ili amulize. Kilole aliingia chumbani bila kujua anaitiwa nini.
Alishtuka baada ya kumuona mumewe ameshikilia bastora na kiwambo chake. Mshtuko wake ulikuwa dhahili ambao ulionekana wazi kwa mumewe.
Mshtuko ule aliuona na kujua kuna kitu anachokijua mkewe kuhusiana na matumizi ya bastola ile. “U..unasemaje mume wangu?” alisita kidogo.
“Nani katumia hii bastola?” alimuuliza kwa sauti ya kiaskari.
Kilole aliamini kabisa akibabaika lazima atakuwa swali la kujibu, alitulia kwa muda akipanga la kujibu mume wake ambaye alionekana amekunja uso alilirudia swali lake la mwanzo.
“Nakuuliza mbona hunijibu nani katumia siraha yangu?”
“Si..si..jui.”
“Hujui ina maana mimi ndiye niliyetumia?”
“Kama hujatumi wewea nani mwingine anaweza kuitumia hiyo bastora, mimi niitumie kwa kazi gani?”
“Hujanijibu nani katumia hii bastola na kiwambo chake pia risasi zangu sita hazipo?”
“Sijui.”
“Mke wangu sitaki utani nieleze ukweli la sivyo leo utanitambua mimi nani, unaweza kuikodisha kwa watu wafanye uharifu ili mimi niingie matatizoni.”
“Mume wangu hiyo imeanza lini, niikodishe ili iweje, nina shida gani mimi?”
“Kama huna shida nani kaitumia, kumbuka vitu vyote vinakaa sehemu ya siri tunayojua mimi na wewe.”
“Kama unataka kufanya lolote juu yangu fanya lakini mimi sijui lolote.”
Kauli ile ilimuudhi sana Deus na kuamini kabisa mke wake anajua kila kitu juu ya matumizi ya bastola ile kutokana na kushtuka alipoingia ndani na kumuona ameshika ile silaha.
Alimsogelea mkewe kumpa kipigo ili aseme ukweli juu ya matumizi ya silaha ile kwa kuamini kabisa kama silaha ile ikikamatwa inatumika vibaya basi lazima yeye ndiye atakaye julikana anafanya mchezo ule na kufia gerezani. Wakati anamsogelea amzabe makofi, simu yake iliita, aliipokea na kuzungumza
“Haloo,” alizungumza huku akitoka nje kutokana na simu kuwa ya kikazi.
Taarifa iliyomfikia alitakiwa uwanja wa ndege mara moja kuna ndege iliyosemekana kuna mtu ana madawa ya kulevya hivyo ilitakiwa akamatwe. Taarifa ile ilikuwa inatoka kwa mkuu wake, alibadili nguo harakaharaka na kupitia vifaa vya kazi na kuelekea mlangoni, kabla ya kutoka alisema:
“Nakwenda nikirudi nikute jibu la sivyo leo humu ndani patachimbika.”
Deus alitoka kutokana na kuchanganywa na matukio ya ndani, alijikuta akimsahau hata Kinape aliyekuwa amejilaza kwenye kochi, alipofika mlangoni alikumbuka hajamuaga rafiki yake aligeuka na kumsemesha Kinape aliyekuwa kwenye dimwi la mawazo mikono kichwani.
“Besti…Besti,” alimwita zaidi ya mara mbili ndipo aliposhtuka. “E..ee.eeh,” Kinape alikuwa kama umeamshwa usingizini. “Unaonekana upo mbali sana?”
“Wee acha tu, hata sielewi kama nitaweza kuidhibiti hali hii mpaka napata mawazo ya kijinga.” “Mawazo gani tena rafiki yangu.”
“Eti nami nijiue nimfuate mpenzi wangu.”
“Wewee! Mawazo gani hayo rafiki yangu, baada ya Happy kuna maisha mengine na farijiko lingine.”
“Ni kweli, siamini kama nitampata kama Happy, Deus yule mwanamke alinipenda mapenzi ya dhati toka moyoni mwake. Nina imani hata kifo chake kinatokana na kulilinda penzi letu.”
“Besti hebu tuache sheria ichukue mkondo wake.”
”Watamkamataje mtu ambaye hajulikani?”
“Mkono wa sheria ni mrefu atashikwa tu amini hilo best.”
Kauli ile ilimtisha Kilole aliyekuwa kwenye mlango wa chumbani akifuatilia mazungumzo. Wasiwasi kumjaa na kuamini kabisa mumewe kutokana na kazi yake ya kijeshi anajua siri nyingi, pengine hata tukio lile anajua yeye ndiye aliyefanya.
Alijikuta akitetemea na kujiona atafia gerezani au kinyongwa, lakini aliendelea kusikiliza kwa kuijificha. Alimuona mume akitoka nje na baada ya muda alisikia gari lake likiondoka.
Alirudi chumbani na kukaa kwenye kitanda kutafuta majibu ya maneno ya mume wake. Aliamini ile ni vita alitakiwa kumuwahi mumewe kabla hajafanya jambo lolote baya, wazo la haraka lilikuwa kwenda kwa wakuu wake hasa yule alimweleza hailewani naye baada ya kuzurumiana fedha za rushwa ya madawa ya kulevya.
Aliamini kupitia yule bwana atafanikisha mpango wake, kwa vile mumewe alisema akirudi akute jibu na yeye aliamini kabisa hakuwa na jibu la kumjibu hasa akizingatia siraha ile anayejua ni yeye na mumewe tu. Aliona kujiepusha na maswali yasiyo na majibu na mwisho wake kujulikana yeye ndiye muuaji ni kutoroka.
Aliamua kutoroka na kwenda kulala nyumba ya wageni ile kesho amtafute yule mkuu wa mumewe na kumweleza kuwa mumewe anajihusisha na dawa za kulevya.
Alijua yule bwana atataka kumkomoa na kuja kufanya upekuzi kwa vile atakuwa amwelekeza lazima atatiwa hatiani. Alichukua baadhi ya nguo za kuvaa kesho na kuziweka kwenye mkoba alimuaga mfanyakazi kwa kumwambia siri ile asimwambie mtu. “Marry hakikisha mtoto amekula vizuri.”
“Hakuna tatizo dada.”
“Na hizi utanunua chochote,” alimpa elfu ishirini.
“Asante dada.” Alitoka hadi sebuleni kumuaga Kinape.
“Shemu nakuja mara moja.” “Hakuna tatizo, wacha na mimi nikalale,” Kinape alijibu huku akielekea chumbani bila kuuliza safari ile ya wapi.
Siku ya pili Kilole alifika makao makuu ya kitengo cha kuzuia dawa za kulevya, alimuulizia yule mzee ambaye jina lake alikuwa analijua moja. Baada ya kuingia getini alikwenda mapokezi na kuulizia. “Samahani dada mzee Shamo yupo?”
“Wewe nani yake?”
“Mtu wake wa karibu.”
“Ameingia sasa hivi.”
“Naomba nimuone.” “Subiri,” yule dada alisema huku akinyanyua simu, baada ya kuzungumza alisema:
“ Nenda chumba namba sita.”
Kwa vile hakuwa mgeni sehemu ile alikwenda moja kwa moja chumba namba sita na kugonga mlango.
“Ingia,” sauti nzito toka ndani ilisema. Alizungusha kitasa na kuingia ndani, mbele ya meza kubwa kulikuwa na mzee mmoja aliyekuwa na mvi nyingi kichwani zilizompendeza.
“Karibu mrembo.”
“Asante, shikamoo.”
“Asante, nikusaidie nini?” Kilole alitengeneza uongo huku akiusema hata ugomvi wao, baada ya kumsiliza alimuuliza:
“Una uhakika na usemacho?”
“Mimi si ndiye mkewe sasa unataka uhakika gani zaidi ya huu?”
“Okay, muda si mrefu tunakuja kwako.”
“Asante mzee wangu.”
Kilole aliondoka moyo wake ukiwa mweupe kama seluji, moyoni alijisemea akuanzae mmalize.
Baada ya kuhakikisha kila kitu kimekwenda kama alivyopanga alirudi aliamua kurudi nyumbani kwake akiamini muda ule mumewe atakuwa kazini mpaka arudi jioni angekuwa amekwisha wekwa chini ya ulinzi.
Alipofika nyumbani alishangaa kumkuta mumewe nyumbani kumbe naye hakurudi jana alipoondoka na kurudi asubuhi ile. Japo alipatwa na mshtuko uliofanya haja ndogo imtoke kidogo alijitahidi kuuficha.
“Karibu mke wangu,” Kilole alishangazwa na hali ya mumewe ambaye hakuonesha hasira. Kilole hakujibu alikimbilia chumbani na kuangua kilio kitu kilicho mfanya mumewe amfuate na kumbembeleza.
“Mke wangu bado una yaleyale ya jana?” Deus alimuuliza mkewe kwa sauti ya upole. “Siku hizi hunipendi, nimekuwa mke mwema na muaminifu siku zote za ndoa yetu, lakini bado umekuwa huoneshi nina umuhimu kwako,” Kilole alisema kwa sauti ya kilio cha uongo.
“Mke wangu, kama kimetokea kitu cha tofauti ndani nimuulize nani kama si wewe mke wangu?”
“Ni kweli, lakini kama sijui mimi nitajibu nini, tena ulitaka kunipiga.”
“Ni hasira za mpito lakini baada ya kujua kosa langu niliamua kuliacha, lakini muhimu kuwa na uangalizi mzuri wa vitu vyetu usipovitunza wewe nani avitunze…Halafu lile gari lako linaingia mwisho wa wiki.”
“Usiniambie! Asante mpenzi wangu.”
Kilole alinyanyuka na kumkumbatia mumewe huku akiamini bado ni mshindi na muda si mrefu Deus ataionja joto ya jiwe. Wakati wao wanabembeleza kikosi maalumu cha kupambana na dawa za kulevya kilikuwa nje ya nyumba ya Deus na kugonga hodi. Deus alitoka nje kuwakaribisha alishtuka kumuona mkuu wake mzee Shamo:
“Ooh! Mzee karibu naona leo mmenitembelea.”
Waliingia wote ndani na kuketi kwenye kochi wakati huo Deus alimwita mkewe awahudumie wageni.
“Mke wangu kuna wageni hebu njoo uwasikilize wanatumia nini.” “Tunashukuru, hatuna muda tumekuja kufanya kazi moja hapa kwako.”
“Kazi moja! Ipi hiyo?” Deus alishtuka.
“Nina imani unaelewa vizuri kazi yetu ni nini?”
“Naijua, ndiyo maana hata mimi nimerudi alfajiri kufuatilia mtu mmoja aliyeingiza dawa za kulevya.” “Ni kweli, lakini huwezi kuwa msafi bila kujisafisha.”
“Una maana gani?”
“Kuna msamalia mwema mmoja amesema kuwa wewe unajishughulisha na uuzaji wa dawa za kulevya.” “Mimi?” Deus alishtuka kusikia vile.
“Unashtuka nini, sasa hivi upo chini ya ulinzi na kutuachia kufanya upekuzi.”
“Fanyeni tu, hizi ni njama za kuchafuana lakini kila kitu kitafahamika.”
Deus aliwekwa chini ya ulinzi na upekuzi ulianza mara moja, Kilole alijifanya kushtuka na kuuliza:
“Jamani kuna nini tena?”
“Siyo kazi yako,” Mzee Shamo alijibu kwa sauti kali.
“Jamani mume wangu kafanya nini?” Kilole aliendeleza usanii. “Wee waache, naona kila siku wananichokonoa lakini ukweli utajulikana,” Deus alisema bila kujua bomu lipo ndani litalipuka muda wowote.
“Hebu njoo hapa,” mzee Shamo alimwita Kilole kwa sauti ya ukali. Kilole alimfuata nakumwacha mumewe amekalishwa chini ya ulinzi, alipofika karibu alimuuliza kwa sauti ya chini.
“Kuna mabadiliko?”
“Hakuna kila kitu kipo vilevile.”
“Ipo sehemu gani?”
“Ndani ya kabati.” “Okay,” baada ya kusema vile alisema kwa sauti kali kupoteza lengo.
“Haya na wewe rudi kwa mwendawazimu mwenzako.
” Kilole alishikwa na askari mmoja na kwenda kukalishwa pembeni ya mumewe, upekuzi uliendelea huku Deus akisema kwa hasira: “Yaani mkikosa hicho mnachokitafuta walahi nitazaa na mtu.” “Mume wangu mbona wanakufuatafuata?” Kilole aliendelea kulalamika kiuongo.
“Wee waache, mwaka huu nitakufa mimi au mtu, nimechoka kuchezewa kama mpira,” Deus aliendelea kulalamika kwa hasira.
“Wee piga kelele utanyamaza muda si mrefu,” mzee Shamo alisema huku akiendelea kufanya upekezi wa uongo kabla hawajafanya kilichowapeleka pale.
Baada kutafuta sehemu nyingine mwisho waliingia chumbani na kufungua kila sehemu na mwisho walichukua briefcase iliyokuwa ndani ya kabati na kuifungua. Ndani ya briefcase kulikuwa na dawa za kulevya zilizokuwa ndani ya mifuko, mzee Shamo alisema kwa furaha:
“Amekwisha, hapa hata ateremke masihi kumtetea hatoki.”
Waliibeba na kutoka nayo hadi sebuleni na kuifungua mbele ya Deus.
“Nilikueleza mapema kuwa huwezi kuwa msafi bila kujisafisha.”
“Hiyo nini?” Deus alitaka kunyanyuka kwa hasira lakini alitulizwa na siraha zilizokuwa zimemtazama. “Deus umekwisha, nilikueleza toka zamani kuwa wewe mtoto mdogo huwezi kushindani na mimi, kwa hili utafia gerezani.” “Muongo mkubwa huwezi kuja kuniwekea madawa ili kunitia hatiani, lakini nikitoka nitakuua nakuapia,” Deus alipagawa kuona ndani briefcase yake kuna madawa ya kulevya.
ITAENDELEA
Nyuma ya Machozi Sehemu ya Nne
Also, read other stories from SIMULIZI;