Hii ni Dunia au Kuzimu Sehemu ya Nne
IMEANDIKWA NA: AHMED JIRIWA
*********************************************************************************
Simulizi: Hii Ni Dunia Au Kuzimu?
Sehemu ya Nne (4)
Inspekta Bogo alikuwa akifuata kila hatua ya Don Philipo kwani huyo ndiye pekee aliyekuwa akihitaji kujua machache kutoka kwake. Hivyo wakati Don akiwa anatoka maegeshoni, Bogo aliacha gari moja tu pekee ambayo ndiyo alitaka iwe ngao yake huku Petii akiwa ametanguliwa na gari nne hadi kuifikia gari ya Don. Yaani ukiachilia gari ya Insp. Bogo, kulikuwa kuna gari tatu, mbele ya Bogo gari moja na nyuma ya Bogo tena gari mbili lakini alihakikisha gari hiyo haipotei machoni pake. Safari hiyo ilikuwa ni ya taratibu sana kutokana na Don Philipo kuendesha gari hiyo kwa mawazo makubwa sana. Msafara huo ulichukua barabara ya Bambuu way, ukanyoosha moja kwa moja hadi kwenye makutano ya barabara ya Tulizo. Hapa gari ya Don iliifuata barabara ya King John. Magari yale mawili yakapungua sasa msafara ule ukawa ni wa magari matatu tu pamoja na la Don mwenyewe. Walipofika kwenye makatisho ya maduka ya wahindi (Hindi Shops). Gari mbili zikapita ambayo ilikuwa ni ya Don Philipo na ya Insp. Bogo lakini gari ya Petii ilipata ukinzani kidogo baada ya kusubiri gari ya mizigo ipite ambayo ilikuwa ikitaka kuingia kwenye godauni moja la wahindi maeneo hayo. Petii alichukia sana kwa kitendo kile lakini hakukuwa na njia nyinge hivyo ikambidi kuwa mpole. Hata gari hiyo ilivyopisha njia, tayari Petii alishapoteza gari aliyokuwa akiifuatilia.
“Shit!” akang’aka kwa hasira lakini haikuwa dawa. Akaamua kukisia tu huku akiongeza kasi.
Huko mbele, Don aliingiza gari yake kwenye jumba moja kubwa lililoonekana kutulia sana. Lilikuwa limejitenga sana. Insp. Bogo alipita kwa mwendo wa taratibu hadi mbele kwenye nyumba nyingine, akapita mbele kidogo kisha akaiacha gari yake kwenye Super market kubwa iliyopo ndani ya mtaa huo kisha akarudi kwa miguu hadi kwenye nyumba ya Don Philipo. Jumba hili lilikuwa la kisasa sana lakini halikuwa na uzio wa aina yoyote ile, ukimya ulikuwa umetawala. Gari ya Don ilikuwa imeegeshwa mahali penye gari nyingine mbili za kifahari sana. Insp. Bogo aliikamata bastola yake vizuri kisha akapiga hatua hadi kwenye mlango wa jumba hilo. Akatekenya kitasa, kitasa kikatekenyeka akasukuma mlango taratibu sana hadi akafanikiwa kuingia ndani, hakukuwa na mtu yoyote sebuleni kimya. Bogo akavuta mlango na kusimama nyuma yake. Don Philipo alipoingia hapo ndani, moja kwa moja alielekea chumbani kwake. Hakuwa Philipo yule mwenye majivuno ya pesa tena hapo alikuwa ni Philipo mwingine aliyekuwa akiumiza kichwa juu ya kujua ni nani aliyethubutu kuigusa ngome yake kwa kidole kati, hizo zilikuwa ni dharau kubwa kama siyo matusi. Simu yake iliita akaitoa mfukoni na kuipokea
“Nataka hadi ikifika saa mbili usiku niwe nimepata ripoti kamili na nzuri” sauti kutoka upande wa pili wa simu iliunguruma.
“Kijazi, nipo nalishughulikia hilo hata mimi hili jambo limenikera sana usione hivi” alisema Don lakini simu ilikuwa kimya kabisa kuonesha kuwa mtu aliyepiga hiyo simu, ameshaikata tayari. Alizidi kuchanganyikiwa Don akajua kuwa amefanya kosa kubwa sana na yeye ndiye anayeonekana mzembe kwenye hilo na si vinginevyo. Alitoka sebuleni akiwa si yeye kifikira, alichanganyikiwa sana. Alilielekea Friji lililopo hapo sebuleni akatoka na kinywaji kikali kisha akatwaa gilasi ndefu na kujimiminia kinywaji hicho bila kujua kama ndani ya nyumba yake kulikuwa na mgeni tayari. Wakati anataka kunywa, akagutushwa na kitu cha baridi kikiligusa shingo lake.
“Freezy Don!” sauti kutoka kwa Insp. Bogo ikamwambia.
“Ni nani wewe unayethubutu?” akauliza Don Philipo akiwa anajigeuza taratibu.
“Naitwa Inspekta Bogo kutokea ndani ya nchi hii, nipo hapa kwa ajili ya kufuatilia ile kesi ya wapelelezi wawili waliouwawa nje kidogo ya uwanja wa ndege, kifo cha Mr. Ndungai pamoja na kutekwa kwa waziri mstaafu na binti yake. Nataka kujua hii Nyororo inaurefu gani na ni nani na nani wamehusika humo?”
“Ha ha ha haaaaa! Kweli wewe ni mwenda wazimu, nani kakudanganya kuwa huwa tunapelelezwa hivyo. Najua aliyekutuma najua, wewe umetumwa na Rais wewe na yule mjinga sisi tulishampa onyo asithubutu kutia mpelelezi humu ila ameonesha ni jinsi gani alivyo kiburi” alibwata Don Philipo mara baada ya kuisha kwa cheko lake kubwa la dharau na majigambo. Bogo alirudi hatua moja nyuma kisha kuitoa usalama silaha yake. Akasema.
“Kujibu nilichokuuliza ndiyo usalama wa pekee kwako, kinyume na hapo ni sheria ya kazi tu ndiyo itatendeka” Don hakujibu kitu akataka kuleta janja ya Nyani kutishia kurukia majani ya miwa akidhanisha ni matawi ya mkarambati. Baada ya kuona ni mgonjwa wa sasa ama baadae na hata uji haupiti kooni. Akadondosha ile gilasi ya kinywaji aliyokuwa ameikamata kisha wakati gilasi ile ikiwa inatoa mlio wa kupasuka, yeye akataka kuchomoa bastola kwa haraka kubwa. Alichelewa. Risasi moja ikaruhusiwa kutoka kwa Bogo ikazama mgongoni mwake na kuchana kifua chake kwa mbele, akaganda kama anasubiri picha ya mnato kisha akanyong’onyea magoti na kurudi chini pasipo kupenda. Bogo aliichukua ile simu kisha akaitia mfukoni na kutoweka mule ndani. Wakati Bogo akiwa anatoka kwenye ile njia inayotokea kwenye lile jumba, Petii ndiyo alikuwa akipita pale barabarani. Akamuona Bogo akiwa anatembea kwa mwendo wa haraka kidogo kule kule kwenye ile Super market ambapo ndipo gari yake ilipo. Petii alimjengea mashaka huyo kijana kwani alishawahi kumuona kule kwenye Hoteli ya New. Hapo alikuwa amefuata nini? akajiuliza lakini hakutaka kulipuuzia hata kidogo jambo hilo akasogea hadi mbele ya ile Super Market akaegesha gari pembeni kidogo akatulia na kumfuatilia huyo kijana kupitia kioo cha side mirrow huku akimuiba ki aina kwa picha kadhaa kwa kutumia simu yake ya kisasa. Alitulia hapo hadi alipomuona huyo kijana akiingia garini kisha kuondoka ndipo yeye alipoliondoa gari lake, akaligeuza akarudi kule ambako yule kijana alitoka hadi kwenye lile jumba. Akashuka garini baada ya kusimama mbali kidogo ya lile jumba. Akagusa kiunoni kuangalia kama silaha yake ipo kisha akatembea kwa mwendo wa haraka hadi kwenye mlango wa lile jumba.
Safari ya Roi kuwafuatilia wale vijana iliishia kwenye nyumba moja pembeni kidogo ya mji wa Muavengero. Kisha vijana wale wakawa kama wanabishana juu ya jambo fulani huku mmoja akionekana akishikilia neno uzembe. Alisema kuwa ni uzembe wa mwenzake kwani wakati akiwa amemuona Romy kuwa amelewa kwanini asingeondoka nae au wakalala wote.
“Lazima kutakuwa na siri amezitoa Romy” alisema huyo kijana mmoja lakini huyo mwingine alisema kuwa Romy alikuwa mbishi sana na alitaka kulala peke yake hakutaka kubaki na mtu hivyo ikambidi amuache na yeye aondoke. Wakabaki wameshika vichwa bila kuingia ndani walionekana ni wenye mawazo makuu sana vijana hao. Roi alikuwa akifuatilia hayo yote kupitia kwenye kibanda kimoja cha mama aliyekuwa akiuza maembe mabivu na muda huo alikuwa akimenyewa embe moja na mama huyo. Baada ya Embe lake kuwa tayari na wale vijana walikuwa wanaingia ndani.
“Ngoja niwape usabahi wale jamaa zangu pale” alisema Roi baada ya kulipa pesa halali ya gharama ya tunda hilo.
“Ahaa hakuna shida” alijibu huyo mama huku akiwa anaendelea na hamsini zake. Roi alitembea kwa mwendo wa haraka huku akiomba wale vijana wasitoke haraka ndani ya ile nyumba. Akaelekea moja kwa moja kwenye mlango wa nyumba ile akaukumba kwa kishindo kikubwa kisha hakuwa na muda wa kuwauliza aliwamininia risasi wale vijana kisha akaufuata mwili wa kijana mmoja akaweka kile kikadi chenye ramani ya Tanzania.
“Hii ni salamu kwa mabosi wenu nataka kujua nani ni kiongozi wa hili” alisema Roi kisha akatoka ndani ya lile jingo na kurusha bomu dogo la masaa kwenye viti vya mbele vya ile gari waliyofika nayo hao vijana mahali hapo lakini alihakikisha hata kama bomu hilo likilipuka haliwezi kuleta madhara kwenye ile nyumba kisha akarudi kwenye gari yake akamuaga yule mama kwa kumpungia mkono akaondoka hapo kwa mwendo wa kawaida. Hajafika mbali mlipuko mkubwa ukatokea kwenye ile gari.
“Nipe habari huko kwa Don Petii?” aliuliza Roi baada ya kuwa garini na hapo alikuwa akiingia Muavengero kati kwa mwendo wa taratibu.
“Kuna mtu mwingine bila shaka yuko nyuma ya huu mchezo Roi” alijibu Petii, jibu ambalo ilikuwa ni lazima muulizaji aulize tena Kivipi? na ndivyo Roi alivyouliza. Petii akajibu kuwa amemkuta Don akiwa ameuwawa. Hii ikawa ni habari ya kuchanganya kidogo. Ni nani ambaye amefanya haya? Kwanini? akajiuliza lakini akaona haitosaidia kitu.
“una utambuzi wa huyo aliyeuwa?” akauliza Roi.
“Yaa, ninapicha kadhaa nilizompiga kwa simu yangu”
“Ok, inatosha, umeweka utambuzi?”
“Yea, nimeweka”
“Ok, tukutane nyumbani” akasema Roi kisha akaongeza kasi kuitafuta Hoteli ya Bi Rozi ambayo ndiyo makazi yao tangu wameingi ndani ya Taifa hilo la Ungamo.
Kichaa mwenye machungu makubwa ya kuuliwa kwa wazazi wake miaka kama mitano ama sita iliyopita, kichaa aliyepania kuhakikisha machozi aliyoyamwaga kipindi kile yalikuwa yakirudi kwa watu wengine, alikuwa yupo kwenye jumba moja bovu sana jumba lililoonekana ni la siku nyingi sana na lilikuwa halikukamilika ujenzi wake. M.Y.S. Kichaa au Frank Kichaa, alikuwa amelaza mgongo wake kwenye ubao mmoja uliokuwa umechoka kiasi. Nywele zake chafu za rasta zilikuwa zimeuficha vema uso wake na alikuwa ameyafumba macho yake. Alionekana kuwa amelala usingizi kabisa. Simu yake iliita kwa mara ya kwanza, pili na tatu pasipo kujishughulisha kuipokea kutokana na usingizi aliokuwa amelala. Sauti nyingine ya kuashiria kuwa kunaujumbe ulikuwa umeingia kwenye simu yake ikasika. Ulipita muda wa kama dakika ishirini hivi ndipo Frank akainuka kutokea usingizi, alionekana kuwa mchovu sana kwa jinsi alivyoinuka kivivu. Alianza kufumbua jicho moja baada ya jingine kisha yote kuwa wazi. Akageuka pembeni akaona simu yake ya kisasa sana na yenye uwezo mkubwa mno ikiwa pembeni yake. Ajabu hiyo. Simu na mmiliki wa simu hiyo vilikuwa havishabihiani kabisa. Simu mpya na ya kisasa lakini mmiliki alionekana kuwa wa zamani.
“KAKA NIMESHINDWA KUWASAIDIA WAZAZI WANGU KUTOKA KWENYE KIFO CHA KINYAMA LAKINI NAENDA MBALI KABISA NA MJI HUU, NIKIRUDI NITALIPA HAYA…………..Muda unakimbia Frank na watu wanazidi kutanua kwa maisha ya furaha kwanini?” Machozi mazito yalimtoka Frank baada ya kumaliza kuusoma ujumbe huo ambao ulikuwa ni ujumbe aliowahi kuutuma zamani sana kisha mwisho ukamuuliza muda wa ahadi yake ambayo aliwahi kuwaahidi wazazi wake kuwa akirudi atalipa. Aliyaacha machozi yamwagike kisha tabasamu lile alipendalo likakaa usoni. Tabasamu lile la kulazimisha, tabasamu linalobeba sura ya kilio lakini kinywa na macho yakionesha tabasamu hilo. Akakaa kitako na kuyafuta yale machozi kwa mkono wake mchafu kisha akishika vema simu yake na kujibu ujumbe huo.
“Sasa, nd’o nimerudi” akautuma. Muda mfupi tu baada ya kutuma akapigiwa simu iliyomchanganya sana baada ya kuipokea. Simu hiyo ilimtoa macho kweli hadi ilipokata bado alikuwa haamini kama kweli hicho alichokuwa akikisikia hapo ni kweli. Don Philipo ameuwawa kwa kupigwa risasi ya kifua baada ya kupenya mgongoni kisha kuwekewa kadi ndogo yenye bendera ya Tanzania na si hivyo tu, hata vijana wawili nao wamekutwa na jinamizi hilo la kifo mahali tofauti. Mh! aliguna Frank baada ya kukatika kwa ile simu.
“Ni nani kutokea Tanzania ambaye anafanya mauwaji hayo?” akajiuliza lakini akaona haitosaidia, akatuma ujumbe kwenye namba iliyompigia na kuuliza ni nani aliyeuwa na kwa nini Don Philipo auwawe na wakati alikuwa ni mfanyabiashara pendwa sana ndani ya Taifa hili. Ujumbe ukaja kuwa Habari zinaufigisufigisu mwingi na haijulikani sababu ya mauwaji hayo na jeshi la polisi halijaongea chochote kuhusiana na jambo hilo.
“Mzimu anazidi kulitafuna Taifa la Ungamo masikini” alisema Frank kichaa kisha akatulia. Akiwa anazidi kuwaza akapokea tena ujumbe uliokuwa ukisomeka.
“Inabidi hata hii tuitoe kwenye Gazeti ili watu wasome lakini si kwa jinsi ilivyotoka, yaani inabidi sisi tuingie kwenye chimbuko la sababu ya vifo hivyo maana haiwezekani Don afe kisha vijana wawili pia wafe huku nao wakiwekewa kadi ya namna hiyo na gari yao ikilipuliwa kwa moto”
“Mgh!” Frank akajikuta akiguna kwa mtindo wa aina yake kisha akafikiri kwa muda kidogo na kuujibu huo ujumbe kuwa sasa anaingia mtaani rasmi na hatarudi porini tena hadi ashinde au ashindwe.
Ni nani huyo aliyekuwa akichati na Frank Kichaa na nini maana ya M.Y.S? Ni kwanini huyo aliyekuwa akichati na Frank Kichaa amwambie kuwa aichunguze habari hiyo kwa undani na waitoe kwenye gazeti? Kubwa zaidi ni kukumbushwa ujumbe wa miaka kama sita iliyopita hii ni nini? Hatari ama?
Hasira kali ziliwamba kwa wakuu, Dr. Lee na Bencov baada ya Dr. Tereza kusita kumalizia kuchanganya mchanganyo wa mwisho kutoka kwenye viambatanishi vya Brainaptic kuchanganya na viambatanishi vya Diet pills ili kuweza kupatikana kwa dawa iliyokuwa ikikusudiwa. Kila walivyokuwa wakimlazimisha hakukubali hata kidogo. Dr. Henry daktari mwenye roho mbaya akamshushia kipigo cha nguvu sana kutokana na kukataa kwake huko. Dokta huyo alifanya hivyo kutokana na kazi ya kufanikisha hilo kukabidhiwa yeye na wakuu wake.
“amesema kuwa ni hatari sana na inaweza kusababisha maafa makubwa sana kwenye nchi zake za kiafrika” alisema muuguzi mmoja kati ya wawili ambao walikuwa wakiwasiliana kwa ishara na wakiwa ni watu wa karibu sana na Dr. Tereza ambao ndio aliwachagua kufanya nao kazi.
“Nani kamwambia kuwa hapa anaweza kupinga amri yetu” aliongea Dr. Henry huku akitoka kwa kasi hadi kwenye baraza kubwa aliyokuwa amesimama Tereza huku macho yake yakiutazama msitu mkubwa uliokuwa uko pembezoni mwa Bahari.
“Hey binti, nini unafikiria sasa” aliongea kwa sauti kubwa Daktari huyo huku akiwa anamsogelea Tereza kwa hatua za taratibu. Hapo Tereza alikuwa amegeuka tu mwenyewe bila kujua kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akimfuata hapo alipo ndipo akakutana na maneno hayo ambayo yeye aliyaelewa kwa kutazama kinywa cha muongeaji.
“Siwezi kuchanganya mchanganyo wa mwisho uliobakia ni hatari sana kwa bara langu maana ndilo mnalolilenga” aliongea moyoni lakini sauti yake haikuweza kutoka nje kutokana na hali yake ya sasa ilivyo kitu pekee ambacho Dr. Henry alikiona ni kichwa kilichokuwa kikitikiswa kushoto kulia kuashiria kuwa alikataa. Kofi zito likatua kwenye shavu la Tereza, maumivu makali yakaambaa kwenye shavu lake. Alivyotaka kujishika shavu, kofi jingine, jingine na jingine yakalichabanga shavu lake hilo hilo moja lililotoka kuumia muda huo mfupi. Machozi yalimmwagika Tereza kuonesha kuwa alikuwa akiumia sana. Maneno makali aliyatoa Dr. Henry, Tereza akawa anayaelewa maneno hayo kupitia muinuka na mshuko wa kinywa cha Daktari huyo. Pamoja na kipigo hicho lakini Tereza alizidi kuwa mkaidi juu ya jambo hilo, alizidi kukataa. Mara sauti kali ikatokea ndani, ilikuwa ni sauti ya maumivu makali sana. Sauti hiyo ilitokea kwenye chumba cha jirani tu na eneo hilo. Kumbe hapo walipo na mahali alipokuwa amehifadhiwa Backa Ramson Backa, palikuwa karibu sana. Sauti hizo zilimshtua Dr. Henry akajua kuwa kwa kipindi hicho ndiyo baba wa huyo binti alikuwa akipitia kwenye maumivu ya majira yaliyokuwa yakimrudia kila baada ya masaa nane na kudumu kwa dakika mbili ama tatu. Henry alibonyeza ukutani mahali hapo hapo walipo, luninga kubwa ikawaka na kuonesha chumba hicho alicholazwa Backa. Mwili wa Backa ulikuwa ikizidi kutisha saa baada ya saa. Mishipa ya kijani ilikuwa imejitokeza mwilini mwa mzee huyo hadi akawa hatazamiki.
Ni hali ambayo ilikuwa ikijirudia mara kwa mara lakini hata kama kila kipindi ambacho anapitia maumivu hayo ungewekwa humo, usingeweza kuyazoesha macho yako kwa kumtazama mara zote. Ulikuwa huwezi kumlinganisha na binadamu wa kawaida akifikiwa na hali hiyo. Tereza alipoiona picha ya baba yake si kama alikuwa haikumbuki la! Aliikumbuka sana na alikuwa akimpenda bado na kila akimuona akiwa katika maumivu hayo alikuwa akiumia sana ila tu ni kwamba alikuwa hana jinsi ya kufanya. Machozi yalizidi kumtoka huku akiwa anaifinya mikono yake na macho kana kwamba maumivu yale anayapitia yeye. Dr. Henry alimkamata kichwa na kumgeuza ili waweze kutazamana, akamwambia kwa sauti nzito.
“Kama hutaki kumalizia mchanganyo wa mwisho nakwenda kumuongeza baba yako sumu ili abadilike kabisa na kuwa kiumbe cha ajabu zaidi ya pale alivyo, kubali ili niache kufanya hivyo?” pamoja na sauti hiyo nzito ambayo yeye hakuisikia zaidi ya kufuatisha midomo lakini alizidi kutikisa kichwa chake kukataa. Hasa akikumbuka maneno ya baba yake yaliyokuwa yakimuonya tangu awali. Ilikuwa ni bora baba yake afe lakini siyo kumalizia kuchanganya michanganyo ya mwisho. Dr. Henry alichukia maradufu akamsukuma binti huyo kwa hasira hadi Tereza akapepesuka. Kipigo cha Mbwa mwizi kikafuatia. Alipigwa sana, kipigo kilimshukia. Alikuwa akiruhusu kupigwa kila pande ya mwili wake lakini siyo tumboni, alikuwa makini sana kulilinda tumbo na hakuruhusu hata pigo moja kupiga tumbo lake. Hali hii haikueleweka hata kidogo na daktari huyo na laiti angejua sijui ingekuwaje. Alivyoona amechoka kutoa dozi hiyo na bado msimamo wa binti huyo uko palepale, akaona liwalo na liwe sasa anauwa.
“Nakuuwa sasa potelea mbali” alisema Henry huku akitoa bomba la sindano lenye dawa yenye rangi ya nyekundu ndani akataka kutoa kile kifuniko kinachokinga sindano isilete madhara. Tereza akageuka haraka sana upande ule ulioko msitu kisha akaanza kuziba masikio yake, ilikuwa ni kama kuna sauti alikuwa akiisikia ikitokea ndani ya ule msitu mzito. Dr. Henry akashangaa lakini hakuelewa kitu alijua ni uoga tu wa kifo lakini hakujua na kama angejua ni bora angejitoa hapo na kuondoka kabisa ndani ya ngome hiyo maana madhara ya baadaye sijui. Tereza aligeuka haraka sana kisha akamgeukia Dr. Henry akamwambia kwa ishara kuwa yuko tayari kuchanganya mchanyo huo. Dokta huyo alifurahi sana akalirudisha lile bomba la sindano kwenye mfuko wa koti kisha akamuongoza binti huyo ambaye alikuwa akivuja damu sehemu kadhaa za mwili wake kutokana na kipigo alichokipokea. Aliwapa taarifa mabosi wake kuwa kazi imekamilika na muda huo ndiyo binti huyo alikuwa akienda kuchanganya hiyo michanganyo miwili ili kuunda dawa moja ambayo itazalisha kiasi kingi ambacho kitakwenda kuiangamiza Afrika hasa kwenye nchi mbili pekee moja ikiwa ni ungamo huku nyingine ikiwa bado haijajulikana hadi muda huo japo Dr. Lee alisema kuwa hata yeye ana nchi anayoichukia sana kwenye maisha yake yote. Hiyo ndiyo ambayo haijajulikana ni ipi. Tereza aliingia kwenye chumba cha maabara kilicho na mchanganyo mmoja tu. hiki ndicho kilichokuwa kikimchanganya Dr. Henry kwani kila akitafuta viambatanishi vingine alikuwa havioni, yeye alikuwa akiona sumu moja tu ya Brainaptic lakini viambatanishi vya Diet pills alikuwa havioni. Jopo zima la madaktari lilikuwa limejaa kwenye chumba hicho cha maabara wakishuhudia hatua ya mwisho ya kazi hiyo iliyochukua muda mwingi hadi kumalizika kwake. Kundi kubwa la viongozi wote wa kambi hiyo walikuwa nyuma ya kioo kigumu kwani hawakuwa na imani na Tereza hata kidogo. Walijua mtu huyo anaweza kuwageuka kisha akaunda bomu kubwa la kisayasi ambalo lingeweza kuwaangamiza wote hivyo walikaa humo kwa kuamini kuwa hata kungetokea moto wa aina gani, hicho kioo kisingepasuka wala kusababisha joto na jumba lote lingeungua na kubaki hicho kioo tu. Kila kitu kilikuwa kikifuatiliwa Mubashara kabisa kwenye mitambo na wengine wakiwa wanashuhudia kabisa. Tereza alikisogelea chungu ambacho ndicho kilichoandaliwa maalumu kwa ajili ya kuchanganya michanganyo hiyo miwili. Alikifunua chungu hicho kisha akachukua Tube iliyokuwa imebeba kimiminika chekundu cha Brainaptic kisha akakimimina chote kwenye chungu kile kisha akachukua kikopo kidogo sana na kuchanganya mule ndani. Ukimya ulikuwa umetawala humo ndani. Alipofanya hivyo, akageuka na kulitazama jopo zima la madaktari ambo walianza kupata hofu. Akaitazama kamera kisha akatazama upande ule wenye kioo kigumu. Hofu kubwa ikatanda mule maabara kila mmoja haja kubwa na ndogo zilikuwa zinataka kugonga nguo ya ndani. Akagusa kinobu cha kijani kuashiria kuwa sasa anawasha.
Frank kichaa alikuwa katikati ya mji akipita kona hii na ile akiwa katika zilezile nguo zake chafu zinazomtambulisha mjini pale. Alikuwa ni mtu mwenye vituko sana hasa akiamua kuleta vituko lakini pia alikuwa mpole sana kipindi akiamua kuwa mpole. Siku hii alikuwa mpole sana lakini pia alikuwa makini kuliko siku zote. Alikunja kona moja akiwa na fuko lake kubwa begani lililochanika na kuchakaa, alipita vibanda na masikani kadhaa za vijana ambao hawakuacha kumtania huku wengine wakisema kuwa ni muda hajaonekana tangu siku ile aliyofukuzwa na silaha za moto. Alipita kwenye uchochoro mmoja hivi ambao ulimtoa kwenye kilabu cha pombe za kienyeji kisha kukatiza kwenye Saluni ya kike. Wadada waliomuona hawakusita kumuita kwa jina la heshima, ‘We kaka!, we kakaaa!’ hii yote ilitokana na kufahamika kwake kwa kiasi kikubwa kutokana na vituko vyake mjini pale lakini hakuwa akiitwa hivyo tangu awali, kilichofanywa aitwe ni siku ambayo alikoswa koswa kuuwawa kwa kupigwa risasi siku ambayo alizuia magari barabarani.
“Masikini wangemuuwa siku ile, sijua amewafanya nini wale?” walisikika wanawake wawili aliokuwa akipishana nao, hapa akiwa kwenye kibanda cha fundi baiskeli huku pembeni kukiwa na banda kubwa la mama ntilie ambalo ndilo alilokuwa akipewa chakula. Aisee! Alijiweka kama chizi kweli na alikuwa ni chizi kamili kwa anavyotambulika na wengi. Hapo alikwenda kwenye gogo moja ambalo lilikuwa na kivuli kizuri sana akaketi. Hii ndiyo ilikuwa maskani yake na mara nyingi hupenda kukaa hapa kwa sababu zake za msingi. Pembeni kidogo ya fundi baiskeli kulikuwa na kibanda cha muuza magazeti na hapo alikuwa akifuatilia magazeti kwa siri sana bila mtu yoyote kujua. Macho yake yalitua kwenye kichwa cha habari cha gazeti moja kilichokuwa kikisomeka. ‘VIFO TATA VYAANZA TENA’ kingine kilisomeka ‘MFANYA BIASHARA MKUBWA AUWAWA KWA RISASI NDANI YA JINGO LAKE JIPYA’ kisha chini maandishi madogo meusi yaliyokolezwa wino yakasomeka. ‘Mzimu huyo huyo awakumba vijana wawili, ungamo yatatanisha!’
Frank kichaa akapeleka macho yake pale kwa fundi Baiskeli akaona kuna gazeti moja lilikuwa chini ilimaanisha kuwa mnunuzi au wanunuzi wa gazeti hilo walisoma halafu wakashindwa kulipa thamani yake na badala yake wakalipa shukurani ya Punda. Akafikiria jinsi ya kuweza kulipata gazeti lile, si kama alikuwa hana pesa ya kununulia la! Bali alitaka kuwa msiri na maisha yake. Alikaa pale hadi muda wa fundi yule kuhitaji kulihudumia tumbo lake kwa kulipa kula kufika, akaenda kula kwenye kile kibanda cha mama lishe lakini lile gazeti halikujaliwa wala kuulizwa kuwa nini shida yake, likaachwa palepale likiwataza wezi na vibaka wataotaka kudokoa masikerepa ya fundi huyo huku lingali halina kinywa cha kutoa ushuhuda wake. Frank akataka kulipa hifadhi ya aina yake lile gazeti kwa kulipitia mithili ya mwewe kwani kuna habari alitaka kuisoma ili ajue ni wapi anaweza kuitafutia chanzo cha mauwaji hayo ili kuanika ukweli maana hiyo ndiyo kazi aliyopewa na mtu tusiyemjua. Kweli alilipitia kisha akatoweka kabisa lile eneo na kurudi chimbo kwake. alipofika chimbo, akalifunua lile gazeti kisha akaanza kuisoma kwa kina ile habari hadi mwisho. Hakuna cha maana sana kama utakuwa unasoma tu ili kujua huyo mfanyabiashara ni nani kwa majina yake matatu na alikuwa akimiliki biashara gani lakini kama ni mtu kama Frank, ni lazima utajua habari hiyo inamaana gani kwanza kabisa ni kuhusu kadi zenye bendera ya Tanzani, hii ilikuwa ni sababu ya muhimu ya kwanza. Pili ilikuwa ni mahali vifo hivyo vilipotokea. Vilikuwa vimetokea mahali tofauti. Moja ikiwa ni mji mpya kwenye makazi ya baadhi ya vigogo pili ikiwa ni nje kidogo ya mji wa Muavengero.
“Kwanza ni leo kwenye jumba la huyu kiongozi kisha kwenye nyumba ya hao vijana” alijisemea Frank.
(Paaaaah!) sauti ya kofi zito lililopiga meza ilisikika kisha sauti ya mtu kuongea ikafuatia.
“Sielewi hii ni nini maana yake!” alisema Bande Sir kwa ghadhabu kuu mara baada ya kupiga kofi zito kwenye meza safi na kubwa iliyokuwa imezungukwa na watu wane. Kimya kilikuwa kizito baada ya kuongea maneno hayo.
“Watu wanauwawa kikondoo halafu eti, tunaoneshwa kadi yenye bendera ya Tanzania. Acheni ujinga nawaambia hii ni kadi ya mualiko na mualiko huu ni mualiko wa kifo” aliongea Bande Sir huku akiwa amewatazama kwa makini na ukaribu sana watu waliyopo pale. Kimya kikachukua nafasi yake tena hadi Bwana huyo alipoendelea kwa mtindo wa maswali.
“Inamaana huyu muuwaji anatoka Tanzania? Sasa kama anatoka Tanzania ameingiaje? Inamaana hakukuwa na ulinzi wa kutosha?” akatulia, jibu halikutoka kila mmoja alikuwa katumbua macho. Bande Sir akameza mate, akajua maswali yote aliyouliza hapo yalikuwa si levo yao bali maswali hayo alitakiwa kuyauliza ngazi ya juu zaidi. Akahema kwa nguvu sana kisha akanyanyua gilasi ya maji na kuileta hadi mdomoni hakuinywa, akahisi maji yote yalikuwa yakinuka harufu ya damu ya kunguni, akairudisha gilasi mezani akiwa kakunjua pua kama kuna harufu mbaya ya kinyesi. Akasema.
“Kijazi, hapa hakuna wa kumpa lawama yule tuliyetakiwa kumpa lawama muda huu anatabasamu kwa hewa safi ya baridi aipatayo Monchwari. Sambaza vijana makini huku wewe ukiwa unawapa ‘direction’ nzuri, waambie wakachukue mkanda uliorekodi matukio kwenye nyumba ya Don Philipo kupitia kamera za ulinzi zilizotegwa, nataka majibu saa mbili na robo usiku huu nataka kupeleka hizi ripoti ngazi ya juu” aliongea hivyo waziri huyo aliyepewa dhamana ya ulinzi lakini matokeo yake kumbe kuna mengi yamejificha ndani yake. Kijazi akajibu hakuna shaka. Kikao kikavunjwa watu wakatawanyika. Kijazi akaita vijana makini wa kazi. Akawasha sigara yake/bangi na kupiga pafu zake huku akiwapa vijana hao majukumu huku akihitaji ripoti kamili kabla ya saa mbili na robo.
Vijana wakatawanyika.
“nimeshatoa ripoti nchini kwangu kuwa jambazi moja limekwenda na maji” Petii alianzisha maongezi.
“Wakajibu nini?” Roi akahoji.
“Wamenipa pole kwa kazi nzito kwani taarifa wanazozipata ni za ajabu sana hivyo wanajua kuwa ninakazi nzito, nashukuru kwa sasa wanaimani na mimi na wako radhi sasa kunipa msaada wowote nitakao uhitaji maana walikuwa wamesitisha msaada kwangu kabisa” aliongea Petii.
“Usijali nitahakikisha namaliza kwanza kazi yako kisha ndiyo, nafanya yangu kwani naamini kazi yako inashabihiana kwa asilimia mia moja na yangu” alijibu Roi. Petii akasema kuwa atashukuru sana. kisha akauliza.
“Uliniambia kuwa kesi hii ni ngumu sana na ni ya ajabu, hebu niambie uajabu wake ni nini?” akachomekea Petii huku akimuangalia kijana huyo usoni. Roi hakujibu kitu alivuta karatasi mbili kutoka kwenye kabati ambazo zilitoka Tanzania kwa wataamu wa ofisi yake ndogo ya siri iliyopo Morogoro, sehemu ya siri pia. Akaziweka juu ya meza kisha yeye akafungua kompyuta yake mpakato na kuanza kusoma ripoti za muuwaji wa Mr. Ndungai sambamba na kufuatilia maongezi ya kwenye ile simu ambayo yako ‘recorded’. Zilikuwa ni ripoti za kutisha kweli kila alipokuwa akisoma macho yalikuwa yakipata hofu juu ya kile yalichokuwa yakikisoma. Aliwahi kusikia kupitia vyombo vya habari mauwaji hayo na pia wakati yupo hapo Muavengero, aliwahi kusoma kwenye magazeti taarifa hiyo lakini hakujua kuwa mambo hayo yapo kitaalamu namna ile. Aliogopa sana Petii. Mawazo yakaanza kumzonga ni vipi kama atakutana na mauwaji ya aina hiyo? ni vipi atajua kuwa hiyo silaha ilivyo? Hakutaka kuendelea kusoma alizisogeza hizo karatasi pembeni kisha akabaki kimya akitetemeka. Alikuwa ni mpelelezi kweli wa kuaminiwa nchini kwake na alitumwa kwasababu aliaminiwa lakini hakujua kama ndani ya Taifa hilo dogo kuna mambo makubwa hivyo. Ni wazi kabisa kama siyo kukutana na huyo mwanaume, kazi kwake ingekuwa ngumu tena ngumu, ngumu kupindukia.
“Vipi kuhusu hizi silaha Mpenzi mbona mimi damu zinanikimbia mwilini?” aliuliza Petii. Roi akatulia kimya alikuwa kuna kitu cha mwisho alikuwa akikimalizia kusoma. Alipomaliza akakaa vizuri kitini na kusema.
“Sikutaka ujue mimi ni nani yaani nikiwa na maana ya kuwa, sikutaka ujue kazi yangu hapa Ungamo lakini kupitia hizo ripoti umeweza kujua mimi ni mpelele kutokea wapi pia kupitia zile kadi ambazo nilikupa moja na kukwambia uiweke kwenye mwili wa Don Philipo akishakufa. Natokea Tanzania na ni Jasusi wa siri sana kutokea Tanzania, wao wataniita mimi Jasusi ila wewe ni vema ukinitambua kama mpelelezi kutokea nchi niliyokuambia. Kuhusiana na ripoti hiyo.” akaweka kituo kikuu kisha akanywa maji kidogo kulegeza koo na kuendelea.
“Nilichukua mifupa kadhaa kutoka kwenye moja ya miili ile ya wahanga wa mauwaji yale ya ajabu kisha nikaituma Tanzania siku moja ilipokuwa ikisafiriswa miili ya wapelelezi waliouwawa hapa nchini. Mifupa hiyo imefanyiwa uchunguzi kwenye kitengo fulani kinachohusiana na uchunguzi wa masuala haya ya silaha za kibaolojia kilichopo pale muhimbili kinachoongozwa na dokta mzuri tu wa mambo hayo. Kiukweli silaha hiyo ni silaha mbaya kama ulivyoisoma hapo na imetengenezwa nchini urusi kama umefika hadi chini utaligundua hilo…..!”
“Imetengenezwa nchini Urusi?” akauliza kwa mshangao Petii.
“Ndiyo,” akajibu Roi.
“Hii inakuwaje sasa kama imetengenezwa nchini Urusi inamaana utakuwa unapambana na Warusi kwenye vita hii huoni kama utakuwa unaingilia ugomvi usiokuhusu kwenye hilo?” akauliza tena Petii.
“Inavyoonekana Petii ni kwamba. Kama mrusi yumo humu ndani basi kwa namna moja au nyingine, anahusika kwenye yale mauwaji ya wapelelezi na kama vilevile mrusi yumo humu, basi anahusika pia kwenye mauwaji ya Mtoto wa waziri mkuu nchini kwako”
“Kivipi?” akahoji zaidi Petii.
“Nyororo ni moja. Huwezi kumuuwa Bande Sir halafu mrusi akuache, lazima atahakikisha humuuwi Bande Sir au hukutani naye kwani anaamini kukutana naye au kumuuwa ni sawa na kuzuia mipango yake, ni nani anayekubali mipango yake isitimie?”
“Hakuna labda mnyonge” alijibu Petii.
“Basi hii vita siyo ya Bande Sir, hii inaweza ikawa ni ya mrusi na huyo Bande Sir akawa ni kibaraka tu wa kuwafikisha wakubwa kwenye lengo lao” alijibu vizuri tu Roi, Petii alishusha pumzi nyingi kisha akauliza tena.
“Sasa tutawezaje kupambana na silaha hizo wakati sisi hatuna silaha hizo?”
“Itawezekana tu kwani hii siyo ‘mission’ yangu ya kwanza nimepambana na mambo kama haya kwenye harakati zile za SEX MACHINE seuse hii”
“Wewe ile ya Sex machine ulikuwa ni wewe?”
“Ndiyo, nilikuwa ni mimi”
“Mungu wangu!” alistaajabu Petii, Roi akaona huyo mtoto anataka kuleta balaa sasa akabadili mada.
“Nisikilize vizuri mwanamke, Kuna taarifa ya kiuchunguzi hapa nilikuwa naipitia, taarifa hii inahusiana na kifo cha baba yake Tamimu yule kijana niliyekuwa nimemsaidia siku ile kwenye mashindano ya magari. Sasa nataka kuingia kwenye sababu ya kifo cha baba yake ili nijue hii inauhusiano gani na kazi yangu. Mtu aliyesababisha mauwaji anakwenda kwa jina la Kijazi, huyu bwana aliwahi kuwa mbunge wa nchi hii ila akaachia ngazi bila sababu za kueleweka, mtu huyu hana historia yoyote ile ya mauwaji ila anaonekana ni muuwaji mbaya sana wa chinichini. Kwa maana hiyo basi, mimi itanibidi nielekee kwa IGP jioni hii ili kwenda kumuuliza mambo machache tu najua pia kuna vitu naweza kung’amua ndani ya ofisi yake” akasema Kijana huyo. Petii akakubali lakini huwa si mbakiji hovyohovyo huyo. Roi akaondoka hapo kwa ajili ya kuelekea kwenye ofisi ya IGP jioni hiyo baada ya kuomba kuonana na mkuu huyo wa jeshi la polisi. Wakati yeye anatoka, nyuma Petii naye akatoka hiyo ndiyo kawaida yake. Na wakati Roi anaegesha gari kwenye maegesho ya magari ya makao makuu ya polisi hapo, yeye alikuwa amepaki pikipiki kwenye mgahawa mdogo uliopo mkabala na ofisi hizo akipata kinywaji huku macho yake yote yakiwa kwenye mlango wa kuingilia ndani ya ofisi zile. Roi alipita moja kwa moja akiwa anajiamini kabisa. alikuwa amepiga mawani ya giza na hakuna aliyemzuia, huku kichwani akiwa ametupia kofia ya kapelo. Macho ya baadhi ya askari yalimtazama hadi anaingia kwenye ofisi ya mkuu huyo wa polisi. Roi alipoingia tu ndani ya ofisi hiyo, alisimama karibu kabisa na meza aliyokuwa amekaa mwenyeji wake, akakaribishwa lakini hakuitikia ukaribisho na wala hakukaa. IGP akabaki akimtazama machoni. Baada ya dakika moja akarudi mlangoni na kuufungua mlango kwa kushtukiza kisha akatoka pale kwenye korido iliyokuwa inaanzia hapo kwenye ofisi hiyo, akamuona kijana mmoja akiwa kwenye miwani ya macho akijifanya kutokea kwenye chumba kilichoandikwa kwa herufi kubwa MAHOJIANO. Yule kijana alipofika mbali kidogo, Roi akakamata kitasa cha mlango huo akagundua kuwa ulikuwa umefungwa kwa kufuli kabisa. Akatabasamu na kurudi ndani. Wakati anataka kuufungua mlango ule wa ofisi ya IGP tena, akaona kinasa sauti kidogo kikiwa kimepachikwa mlangoni. Alikichukua akakiharibu kisha akaingia ndani kichwani akiwa na yake. Akakaa kitini kisha akaomba radhi lakini kabla ya maongezi akamwambia kuwa ofisini kwake pia siyo pazuri kuna mamluki amewekwa hivyo huyo atadili na yeye lakini pia hata yeye asishangae anaweza akapokea ugeni muda wowote hivyo asisite kumpa taarifa. Hapo kijana huyo akaamka na kutoka. Alishajua mahali ambapo yule kijana anapatikana hivyo alivyotoka pale moja kwa moja ni kwenye Compute Room. Alipoofika huko akakuta watu wakiwa harakati za utendaji kazi lakini kiti kimoja kilikuwa hakina mtu. Akatoka, alipokuwa anakaribia nje akamuona yule kijana akiwa kwenye gari moja nyeusi akiongea na mtu fulani hivyo wakati anatoka alijifanya kutowaona, mara simu yake ikaita alipoitoa mfukoni alikuwa ni Peti. Anashida gani naye huyu? akawaza huku akiipokea na kuiweka sikioni.
“Huyo mtu wa kwenye gari ameingia muda huu na inavyoonekana kuna kidudu mtu wao humo” alimaliza kuongea Petii, Roi akajua kama huyo mtoto wa kike yupo hapo basi kazi ipo. Akaielekea gari yake akaingia ndani kisha akatulia huku akiifuatilia ile gari alipoona haiondoki akajua si bure, hapo anategwa hivyo umakini unatakiwa uwepo. Akiwa anazidi kuwaza, mara gari hiyo ikatoka hapo maegeshoni kisha ikapita hapo karibu, ilikuwa ni ya vioo vya giza hivyo ikawa ni ngumu kumuona wa ndani. Roi akaisubiri hiyo gari ifike barabarani halafu na yeye ndiyo akatoka akapita njia nyingine kabisa hakuwasiliana tena na Petii bali alijua kuna mitego yake atakuwa ameitega. Walivyodhani sivyo, walidhani labda watafuatiliwa lakini kumbe haikuwa hivyo na wala hawakumuona mtu wala gari yoyote iliyokuwa ikifuatilia. Petii naye akaondoka mahali hapo bila kujua kama kuna mwewe hatari sana alikuwa makini na mviziaji mbaya ailiyekuwa akiwafuatilia kwa mbali mno, Petii hakujulikana lakini Roi alijulikana picha kadhaa zikapigwa.
Kigiza cha saa 7:08 usiku. Kilimkuta Frank kwenye viunga vya jumba la Don Philipo akiwa makini zaidi kufuatilia kilichomfanya yeye kufika maoeneo hayo. Taa zenye mwanga mkali sana ambazo huwa zinajiwasha zenyewe zionapo giza, zilikuwa zikiwaka sana, Frank akajua tu hizo zitakuwa zimewekwa hapo kwa maaana maalumu. Alizama ndani kwa njia zake mwenyewe, alipofika ndani pia, alikuta taa zikiwa zinawaka. Hakukwa na kiumbe cha aina yoyote ile kwa macho ya haraka haraka akajua kuwa hiyo nyumba ilikuwa si ya kukaliwa na watu na pengine labda Don Philipo alifika hapo kwa kupumzika au kwa lolote lile lakini si kwa kukaa ndani ya jumba hilo. Kila kitu cha humo ndani kilikuwa kipya kabisa na havikuonesha kama vilianza kutumika. Vitu hivyo baadhi vilikuwa ni Makochi na vingine vidogo vidogo. Macho ya Frank yote mawili yalikuwa makini kuangalia kila kona ya nyumba hiyo. Hakuna alichoambulia ndani ya Jingo hilo ila kabla hajachukua maamuzi ya kutoka, kuna kitu kilimsukuma aangalie kwenye kona moja. Hapo akatazamana sura kwa macho na kamera moja ya ulinzi akatabasamu. Akazunguka mule ndani hadi akakipata chumba kilichokuwa kikiongoza zile kamera. akachomoa mikanda miwili mmoja ukiwa ni wa kamera ya nje nyingine ikiwa ni ya ndani kisha akaharibu mfumo mzima wa uchukuaji wa picha akatoka kwa njia azijuazo yeye.
Kwahiyo hata wakati vijana waliotumwa na Kijazi wakiwa wanaingia hapo yeye hakuwaona wala wao hawakumuona. Alipotoka hapo moja kwa moja ilikuwa ni chimboni kwake. Alipofika aliwasiliana na mtu wake ambaye walipanga wakutane usiku huo huo ili wakabidhiane hicho kimoja alichokigundua kisha wakijengee matukio ili wajue ni nini chanzo cha mauwaji hayo na muuwaji ni nani.
Mioyo yao ilikuwa ikiwakimbia sana, walikuwa na hofu kuu lakini Dr. Tereza alikiachia kile kinobu cha kuwashia akainama chini kwenye vungu za ile meza ya kimaabara akatoa chupa moja ya saizi ya kati ambayo ilikuwa ya rangi nyekundu kisha akamimina ule mchanganyiko kwenye kile chungu kwa uangalifu mkubwa sana huku machozi yakiwa yanamtoka, alijua fika alikuwa akitengeneza dawa moja hatari sana ambayo ilikuwa hakuna mtu yoyote anayejua madhara yake zaidi ya yeye pekee. Baada ya kuuchanganya mchanganyiko ule, akawasha kitufe cha kijani, mtambo ukawaka. chungu kile kikaanza kazi ya kuichemsha pamoja michanganyiko ile ambayo haikusubiriwa hadi ichemke, ilipopata joto kidogo ikatolewa na kuingizwa kwenye mtambo wa kupoozea kisha kugandishwa kabisa. Baada ya hatua hiyo hatua ya mwisho ikawa ni kusaga na hatimae kukatoka vitu mfano wa chumvi ya madongemadonge madogomadogo meupe pee. Alipo maliza akakaa kwenye kiti kimoja kilichokuwa nyuma ya ule mtambo ambapo kulikuwa na kompyuta, akaandaa ripoti ambayo ilichukua muda wa masaa mawili kukamilika kisha akaiprinti na kumkabidhi Dr. Henry, kazi ya kutengeneza kitu hatari ikawa imekamilika. Dr. Tereza akachukuliwa na kuwekwa kwenye chumba maalumu ambacho alikuwa akipata huduma zote muhimu, aliwekwa hapo kwa muda maalumu wa kuhakiki kitu alichokitengeneza ambacho kilikuwa kikifahamika kwa jina la kitaalamu Diebrainaphine. sumu hatari iliyokuwa inauwezo wa kuotesha mimea au magugu hatari yanayofahamika kwa jina la Partathenum. Magugu haya huota sambamba na mmea uliyopokea sumu hiyo ambayo wao wenyewe walikuwa na mpango wa kuhakikisha wanaipeleka afrika hasa ndani ya nchi ya Ungamo na moja ambayo bado ilikuwa kwenye mabano ndani ya vichwa vya Bencov na vijana wake. Kwanza ilikuwa ni lazima sumu hiyo ya aina yake ifanyiwe majaribio kisha wakishaona madhara yake ndiyo waitangaze kwa kutanguliza mbolea ya kweli ambayo inafahamika kwa jina la Diet pills ambayo ilitengenezwa na Dr. Tereza kwa lengo la kuhakikisha nchi zenye ukame zinaondokana na balaa la kukosa chakula kutokana na ukame kupitia dawa hiyo ambayo mwenyewe aliita mbolea yenye kuleta msaada kwa wakulima. Sasa Mbolea hiyo ilikuwa ikitangulia kisha nyingine mbaya na yenye lengo baya pia kufuatia. Watu wote waliokuwa wakiishi ndani ya himaya hiyo ya Dr. Lee walikuwa ni watu wenye furaha kubwa sana kwani walikuwa wakinywa na kula tu muda wote hadi pale watakapopata majibu kutoka kwa Dr. Henry kuhusu ukweli wa sumu hiyo.
Mtu aliyekuwa akimfuatilia Roi bila ya Roi mwenyewe kujua, alikuwa ameshafika hadi kwenye hoteli ya Bi Rozi lakini Roi hakuingia kwenye chumba chake bali aliingia kwenye chumba cha Petii ambacho walikuwa hawakitumii sana, akaweka vitu sawa kisha akatoka na kuelekea nje ya hoteli ile kisha akaelekea mgahawani. Alipofika akampigia simu Petii na kumwambia asiingie ndani kwani hali ya hewa ya siku hiyo ameshaiharibu kule makao makuu ya polisi. Petii akafanya kama alivyoagizwa, akaelekea mahali ambako Roi yupo huko wakapata chakula cha usiku pamoja kisha wakarudi hotelini.
“Kila nikipiga hatua nahisi kama kuna hatari mbele yetu” aliongea Roi.
“Kwanini?” akauliza Petii.
“Sijui ila nahisi hivyo tu maana naona mwili wangu hautaki kabisa kuingia humu ndani” alijibu. Walipofika kwenye chumba cha Petii kilipo, Petii akataka kuingia kichwa kichwa, Roi akamzuia na kumwambia aingie kwenye chumba chake kisha yeye akatulia hapo nje ya mlango wa chumba cha Petii huku Petii akiwa anazidi kutokomea kwenye ngazi za kupanda floow ya juu ambako ndiko chumba cha Roi kilipo. Akiwa ametulia hapo nje hivyo, akahisi damu zikimkimbia mwilini akajua bila shaka si kwema humo ndani. Akacheki silaha yake akaikuta ipo salama. Akafungua mlango ule kwa kadi maalumu kisha akausukuma mlango kwa nguvu na kujirusha kando, risasi tatu zikapiga mlangoni. Roi haraka sana akachomoa bastola akaishika mkononi sasa akawa anasubiri adui yake afanye makosa. Wakabaki kuviziana, yule mvamizi alikuwa ameshikilia kamba ambayo ilikuwa ipo tayari kumtoa nje muda wowote ule atakapomaliza kazi. Dirisha la kioo lilikuwa wazi kabisa mahali hapo. Adui alikuwa akimsubiri Roi anyanyuke ili ammiminie njugu na Roi alikuwa akimsubiria Adui akanyage kwenye sakafu atoke pale juu aliponing’inia, hapo ndipo palipokuwa patamu. Yule mvamizi akapiga risasi moja kumchanganya Roi kisha akaruka kutoka pale juu na kutua chini, hakujua kuwa mtu aliyeko hapo yuko makini zaidi kuliko alivyotarajia, kupitia uvungu wa kitanda Roi aliiona miguu ya huyo bwege. Akauchapa risasi mguu mmoja, jamaa akabweka kwa ukelele mkali huku silaha ile akiiachia na kwa kuwa dirisha lilikuwa uchi, silaha ile ikadondokea dirishani. Roi akachomoka pale alipojificha huku akiwa amemnyooshea huyo jamaa bastola.
“nani amekwambia njia ya kufika huku?” akauliza Roi.
“Mama yako mzazi bwege wewe aaaghr…..!” alisema huyo jamaa huku akiugulia maumivu kutokana na mfupa wa mguu kuvunjwa vibaya sana.
“Basi amekudanganya sana maana utakufa kama huta sema ukweli” aliongea Roi huku akiikoki tena silaha yake kisha akapiga risasi nyingine ya paja, huyo bwana akalia kwa maumivu makali akashuka chini na kujibwaga sakafuni. Roi akamsogelea na kumuuliza tena kwa utaratibu akiwa amelikanyaga lile jeraha la risasi, jamaa akalia sana huku akisema kuwa atasema. Roi akalegeza jamaa akasema kuwa ametumwa na Kijazi kazi hiyo.
“Anapatikana wapi?” akauliza tena, jamaa akaleta kujua, akaongeza kukanyaga akasema kuwa anapatikana mjini Haika The most Casino. Baada ya kujibu hivyo huyo kijana akamsukuma Roi kwa guu lake kisha akaikamata kamba akiwa na lengo la kutoweka. Roi akiwa palepale chini, aliilenga ile kamba na jamaa huyo akashuka kupitia pale dirishani na kutua chini ya ile ghorofa kama mzigo. Roi alisimama pale dirishani akamuona huyo jamaa alivyo tua huko chini.
“Pumzika kwa amani” akasema kisha akachukua kilicho chake huku akihakikisha haachi ushahidi humo ndani akatoka hadi chumbani kwake alipofika, alivua nguo na kuelekea bafuni kisha akabadili nguo, zile za awali alizitia kwenye mfuko wa nailoni na kunyanyua kabati akaweka. Wakati anamaliza kufanya hivyo tu mlango ukagongwa. Akaelekea kwenda kufungua.
“Ooh! samahani kwa usumbufu si wewe” alisema dada wa mapokezi akiwa na askari bila kueleweka vizuri.
Asubuhi kulipokucha Mambo ndiyo yalikuwa yanazidi kuwa magumu kwa upande wa kina Kijazi, Mauwaji ya watu wao yalizidi kuongezeka hali ikawa tete. Mezani alikuwa na picha ya mtu aliyesadikika kuwa ni msumbufu. Eti, huyu ndiyo anatuchanganya akili zetu. Aliwaza Kijazi kisha akatuma zile picha kwa Bande Sir kupitia mtandao akimwambia kuwa huyo ndiye muuwaji wa vijana wetu. Taarifa hizo hazikuwa ndogo, zikamfikia na Raisi wa zamani, Rais akaita kikao kizito kikao ambacho majibu yake yalitakiwa kutumwa kwa mkuu wake wa kazi, kijana mdogo wa Kirusi anayekwenda kwa jina la Bencov.
Watu walikutana Mjini Pande nje ya mji wa Muavengero kwenye jumba kubwa la Raisi huyo wa zamani. Walikuwa ni watu watano. Alikuwamo Rais Mobande Julio, alikuwepo Kitema, kijazi, Bande Sir na Alikuwepo na Jalome.
“Si sahihi sisi kukutana hapa na kuzungumzia jambo hili asubuhi lakini kitu kilichonishtua ni hawa watanzania kuanza kuleta shida…wameingiaje hapa nchini kwetu kirahisi hivi?” akauliza Mh. Julio.
“Hata mimi ninamashaka mkuu lakini tukumbuke kuwa ulinzi wote wa mipaka ya kuingia humu nchini kwa watu kama hao hatukupewa sisi, Mkuu alisema hii kazi atawapa vijana wake sasa nashangaa kusikia kuna watanzania” aliongea Bander Sir.
“Don ameuwawa lakini pia mtu aliyetumwa kumfuatilia huyo kiumbe, ameuwawa bila kusema chochote kwetu, naiona hatari kama tusipokuwa makini zaidi” aliongea Jarome mtu mnene makini asiyeonekana mara kwa mara. Huyu alikuwa ni mnene kuliko hata Kijazi. Rais Julio alitulia kidogo akajikohoza kisha akawatazama wale mabwana kabla ya kuzungumza. Lazima leo hii niwasiliane na Bencov lakini vile vile lazima hata sisi tuwe makini zaidi huku mkisubiria kauli ya mkuu” kikao hicho kikavunjwa na kila mmoja akaelekea kwake. Kijazi alipotoka hapo moja kwa moja alihitaji kwenda kupumzisha akili alikuwa amechoka sana akili kutokana na matukio yalivyopandana. Wakati anaingia nyumbani kwake huko Haika, Roi mzee wa kunusa alikuwa ameshaingia hapo ndani, kwani maelezo aliyopewa na yule kijana aliyemsafirisha kuzimu, yalitosha kabisa. Huyu alitaka kumuondoa mapema sana kwani alijua fika kuwa huyo ndiye waliyekuwa wakimtumia mara nyingi. Na tayari ripoti kamili za mtu huyo alikuwa nazo. Kijazi alipofika ndani kwake, aliingia chumbani akachukua Taulo na kuelekea bafuni, alikuwa akiishi peke yake huyo jamaa. Wakati yeye akiwa anaelekea bafuni, Roi alikuwa tayari ameshajikaribisha ndani zamani tu na alikuwa yupo sebuleni amekaa akinywa pombe kali aliyoichomoa kutoka kwenye Friji kama vile ni mwenyeji wa siku nyingi ndani ya nyumba hiyo. Kijazi aliporudi chumbani akahisi kitu, moja kwa moja akakimbilia kwenye kioo cha kompyuta akawasha. Macho yake yakamshuhudia huyo kijana waliyekuwa wakimzungumzia tu kule kwa Rais Mobande.
Akanyanyua mkonga wa simu akauweka sikioni kisha akabofya namba kadhaa.
“Ndiyo mkuu, yule kijana tuliyekuwa tunamzungumzia yuko hapa nyumbani kwangu amejileta mwenyewe, wacha nimuuwe kwa kifo kibaya ninyi mtaishuhudia maiti yake chumba cha kuhifadhia maiti au niichome moto isionekane kabisa?” aliongea kwa tambo kubwa Kijazi huku akiyafinya macho yake makubwa kwa hasira kisha akaacha swali.
“Aah! Uwa kabisa huyo na hata maiti yake hatutaki kuiona choma wape mbwa wako wale” alisema Bande Sir huku akijua kuwa kazi imekwisha.
Kijazi akawasha Bangi yake kubwa akapuliza moshi mwingi kwa hamu kubwa na mara nyingi akifanya hivyo yeye huamini anauwa kifo kibaya sana. Akakamata kisu mkononi mwake akatoka huku akiwa anavuta.
“Karibu sana kwenye kifo mgeni, umekuja muda muafaka sana nafikiri hukusahau sanda yako?” alikaribirisha Kijazi huku akiwa anachezea kisu chake.
“ohoo kumbe uliniona, kumbe uko vizuri sana, nataka kukuuwa wewe kisha uniambie ni nani anayemiongoza ninyi”
“ha ha ha hahaaaa!” alicheka kicheko kikali sana Kijazi kisha akanyamaza ghafla, akavuta moshi mwingi kwenye mapafu yake halafu akatulia kama kakabwa. Ule moshi wa bangi ulikuwa unaingia ubongoni sawia na kumletea maisha ya kufanya kazi kwa ari kubwa akijiona ni mithili ya malaika atumwapo kazi na Mola wake. Akaachia tena cheko huku akiruka hewani na kuachia mateke mawili mazito kumuendea Roi, Roi akahama pale alipo na kuhamia kochi jingine.
“Ohooo! Kumbe uko vizuri sana nilikuwa nakujaribu sasa inabidi nikushughulikie vizuri” alisema huku akirusha kisu ambacho kama si ushapu wa Roi basi kile kisu kingezama kifuani, kilichoma kwenye kochi. Roi akiwa anashangaa, Kijazi alisharuka na kukichomoa kile kisu kisha akaanza kucheza nacho kwa ustadi mkubwa. Roi akawa na kazi ya kukwepa kile kisu lakini hakuweza kukwepa kila kitu, alipokea ngumi safi ya kifua iliyomrudisha nyuma.
“Kumbe mdebwedo, nilidhani mkakamavu” alijitapa Kijazi baada ya kumuona Roi akihema kwa pumzi ya kutanua kifua.
“Pambana basi usiongee shoga wewe, mwanaume tangu lini akawa na mwili kama huo uliojaa mijinyama mtepweto” alikejeli Roi. Kama kuna mambo ambayo Kijazi aliyachukia ni matusi. Alichukia sana kutukanwa hivyo akapandisha hasira kali akawa anakuja kwa lengo la kuleta madhara. Alikizungusha kisu chake kwa aina ya pekee sana. Roi akabonyea na kupiga ngumi ya tumbo nzito sana, Kijazi akagumia mh! Hajakaa sawa alikula ngumi nyingine mbili za mdomo damu zikamwagika. Kijazi sasa akawa Mbogo, akawa anakuja kwa maguvuguvu hilo likawa kosa kwake. Alichezea kichapo cha dakika tatu tu akalegea kama Mgomba uliochomwa na jua la kiangazi. Akashuka chini.
“Nani mdebwedo kati yangu na yako?” aliuliza Roi lakini Kijazi hakuwa na uwezo wa kujibu alikuwa hoi. Roi akatoa kadi ndogo yenye bendera ya Tanzania kama ada.
“No, no, noooo!” alipiga kelele Kijazi kwani alijua nini maana ya hiyo kadi, hawezi kukuachia hiyo kadi ya mualiko bila kukuuwa. Roi akaiachia ile Kadi sambamba na pigo moja baya sana la kwenye koo. Kijazi akahama dunia hii tuishio mimi na wewe na kuivuta hewa safi ya Mungu muumba bila malipo na kwenda kuliko na haki ya milele. Simu iliunguruma kwa muda sana, Roi akaiwahi na kuipokea kisha akaiweka sikioni.
“Nipe habari Kijazi umesha……!”
“Bahati mbaya mkuu nimekufa mimi, mtakuta kadi ya mualiko nanyi pia msikawie” Roi aliikata sentensi ya Bande Sir kisha kuongea maneno makali yenye kuumiza, simu ikakatika hewani, akaachia tabasamu kisha akaitazama kamera iliyopo hapo. Akachomoa bastola yake ndogo akaichapa ile kamera kwa risasi kisha akaingia chumbani akachukua mkanda uliokuwa ukimrekodi kisha akatoweka. Kitu cha kwanza baada ya kutoka pale Roi, alimkumbuka yule binti aliyempa kadi ya biashara siku ambayo alikuwa katika kombozi ya kumkomboa Petii. Aliivuta taswira ya yule binti, urembo wake wa sura mwili na ngozi, vikamfanya ameze mate ya uchu, akatamani kumtafuna kama kuku wa kisasa. Pia alifikiri mengi kuhusu binti huyo, moja na kubwa likiwa ni kupata siri nyingi kutoka kwake. Nikimkunja mkao wa Paka kashiba yule mrembo lazima anitemee siri zote. Aliwaza akiwa garini mwake kisha akafungua Dash board na kuitoa hiyo kadi ya biashara. Akanukuu zile namba kutoka kadini na kuziingiza kwenye kitabu cha namba simuni mwake. Akisha akabonyeza kitufe cha kupigia na kuiweka sikioni. ‘Namba ya simu ya mteja unayempigia, haipo’ sauti ya kike kutoka simuni ikamjibu. Au nimekosea? Akawaza kasha akajaribu tena, majibu yakawa si ya kubadilika, akapiga kite cha hasira na kuitupia simu kitini upande wa pembeni wa gari yake akasema.
“Wamemshtukia huyu binti au pengine wameona kitu siku ile. Bila shaka wamemuuwa huyu”
Mida fulani ya saa sita mchana ilimkuta Frank kichaa/M.Y.S, akiwa maeneo ya mjini. alikuwa ni tofauti na alivyozoeleka, siku hii alikuwa amepiga ‘Prover’ lililomfunika kichwa kizima. Hapa hakuwa na ule muenekano wake zoelefu. Alitembea mwendo wa haraka akipita mitaa hii na ile, kona hii na ile hadi akaja kutokea kwenye mti mmoja mkubwa nyuma ya Grossary moja. Hapa alikutana na mtu aliyekuwa amevaa kama yeye. Wakatazamana usoni kwa muda kidogo kisha yule mtu aliyekutana na Frank mahali hapo akatoa picha mbili za mnato akamkabidhi Frank.
“Nenda kamuangalie huyo vizuri kisha utanijulisha kama utakuwa unamfahamu” akasema huyo mtu halafu akageuka kutaka kuondoka lakini akasita akasimama hivyo hivyo bila kugeuka akasema.
“Nilitaka kusahau, leo saa 12:08 mchana huu, kuna mtu mwingine ameuwawa huko Haika. Hizi taarifa ni nyeti sana na nilipigiwa simu na jirani wa huyo aliyeuwawa anafahamika kwa jina la Kijazi, unalifahamu hilo jina?”
“Hapana silifahamu na sijawahi kulisikia kabisa” alijibu Frank baada ya kufikiri.
“Ok, nenda kamtambue huyo kwanza kisha utanijuza ili tujue nini cha kufanya” alihitimisha huyo mtu ambaye ilikuwa si rahisi kumjua kisha akaondoka mahali hapo na Frank nae akaondoka kwa mtindo huo huo.
Kiti kilikuwa hakikaliki, sebule aliiona kubwa na pana sana kwa jinsi alivyokuwa haimalizi kila akiizunguuka. Alikikuna kichwa chake kilichokuwa na nywele nyeusi tii! Tofauti na umri wake. Mzunguuko ule ulikomea katikati ya sebule akashika kiuno na kulitazama dari la hapo sebuleni.
“Kijazi, Kijazi, Kijaziii! Hata wewe? Haa! Siamini” alisema Bande Sir huku chozi likiwa linamtoka. Akapiga hatua nyingine za kujisukuma hadi mahali kiti kilipo akakaa mbwaa! kama kavunjwa miguu utotoni au Kama kasukumwa, akatulia tuli. Bado alishindwa kuyazuia machozi yake yasimtoke tena.
“Huyu mwendawazimu anayeuwa hata wanaouwa ni nani? Nani huyu asiyejipenda nauliza?” aliuliza kwa sauti kubwa kama kulikuwa na mtu mwingine mule ndani kisha akanyanyuka kwa kasi kubwa na kusogea mahali ilipo simu ya ofisi akabonyeza namba mbili tatu akavuta mkonga wa simu hiyo na kuipachika sikioni mwake.
“Habari za asubuhi Bande?” Sauti nzito ilisikika kwenye simu.
“Habari za asubuhi ni mbaya sana Muheshimiwa”
“Unataka kuniambia nini Bande?”
“Kijazi pia ameingia kwenye listi ya waliouwawa na yule anayetumia kadi yenye bendera ya Tanzania” aliweka kituo Bande Sir lakini kituo alichoweka yeye, kilikuwa si kituo cha kumtuliza aliyepigiwa simu. Mshtuko mkubwa kupitiliza ulimkumba muheshimiwa Mobande. Tumbo lilimcheza vibaya sana ni wazi sasa hali ilikuwa si ya kupuuzia tena, hali ilikuwa tete na utete wa hali hiyo unaweza kuleta methali mbaya yenye kunadi kuwa, Mdharau mwiba………!
“Bande!” aliita kwa sauti kavu Mh. Mobande. Bande Sir akaitikia kwa utulivu ili kujua nini mkuu wake anamuitia.
“Kijazi alikufa kabla hatujakaa kile kikao cha asubuhi au?” swali hili aliloliuliza mtu mkubwa mwenye kupewa heshima laiti kama ungeulizwa mtu anayependa kucheka kama wewe, ungepasuka mbavu, lilikuwa ni swali la kijinga kweli, kwa namna nyingine lilikuwa ni swali la mtu aliyechanganyikiwa kuliko mtu wa kawaida achanganyikiwavyo.
“Baada ya kikao kile mkuu”
“Fu*k!” akatukana. Kimya kikatanda, hakukuwa na aliyekuwa akiongea, ni wazi hali ilikuwa imeanza kutisha na mambo yanakwenda kuwa magumu kwao. Lazima niwapigie wakuu waniambie vizuri wameweka walinzi gani wa kukaa kwenye viwanja vya ndege. Aliwaza Mobande baada ya kukata simu. Akairudisha hiyo simu mahali inapokaa akakamata nyingine akaweka namba na kusikiliza.
MADAGASCAR.
Kila siku iliyokuwa inaitwa leo watu wa himaya ya Dr. Lee walikuwa wakinywa na kula vizuri, hiyo ilikuwa ni katika harakati za kusubiri majibu ya tafiti za uhakiki wa dawa iliyotengenezwa ndipo waingie kazini. Asubuhi ya siku hiyo, wengi walikuwa wameamka nazo za siku iliyopita lakini bado meza za vinywaji zilikuwa zikiwahitaji wao tu. Ilikuwa ni starehe kweli, kila kileo kilikuwepo. Wapenzi wa madawa mengine ya kulevya kama Bangi, unga wa kila aina na madawa mengine yafananayo na hayo pia yalikuwepo. Walikuwepo wanawake wazuri wa kuvutia ambao ulikuwa ukijichukulia yule umtakaye na kwenda kumbanjua kwa hiyari yake wala si kwa kumlazimisha. Meza zote ndani ya ukumbi huo zilikuwa zimejaa jinsia tofauti, walikuwapo wanawake kwa wanaume kwa lugha nyepesi ni kwamba kila mtu alikuwa na wake ila wenye kuhitaji zaidi ya mrembo mmoja pia iliwezekana.
“Sijisikii kunywa leo kabisa” ilisikika sauti moja ya kike ikisema.
“Unataka nini sasa kama kunywa hujisikii?” sauti ya kiume iliuliza huku mwanaume huyo akichezesha mikono yake kwenye maungo ya mrembo huyo.
“Nataka tukafanye mapenzi tu leo maana siku zote huwa unalewa sana kiasi kwamba nashindwa kukufaidi vizuri” alisema huyo mwanamke. Wakati hayo yakiwa yanaendelea kwenye ukumbi huo, pembeni kwenye kijichumba kimoja kwenye kona fulani hivi, kulikuwa na meza iliyokuwa imezunguukwa na watu wane. Hapa alikuwapo Bencov, Merina/Lady Devil, Lonto pamoja na Kijana mmoja aliyekuwa amevaa mawani ya giza ambaye muda wote alikuwa hajui kucheka wala kutabasamu na huyu alikuwa hata hagusi pombe zilizopo maeneo hayo, huyu muda wote alikuwa amepozi karibu na Bencov. Walikuwa wakiokota nyama iliyochomwa vizuri kabisa, wakitia mdomoni, pombe ilikuwa ikifuatia baada ya kuitafuna nyama hiyo. Soga na tashtiti za hapa na pale zilikuwa zikiendelea bila kupiga kelele lakini wakiwa wanaendelea na unywaji huo, Simu iliyopo pembeni kidogo na hapo walipo iliita. Watu wakatulia, Bencov akaagiza simu hiyo iletwe kwake. Akakamata mkonga akaiweka sikioni. Kimya kilitanda ghafla, mshangao wa waziwazi ulimkumba huyo bwana. Watu wote pale wakaacha kunywa na kumtazama huyo mkuu wao mahali hapo ili kujua kinachomshangaza. Bencov aliirudisha ile simu kwenye kikalio chake ambacho kilikuwa kimeshikiliwa na mletaji wa simu hiyo bila kutazama anapoweka hiyo simu.
“Kuna nchi inaitwa Tanzania sijui Tanzia!” akasema hivyo kisha akanyanyuka. Wote waliobaki pale hawakuelewa ila Lady Devil hili jina Tanzania lilianza kumpa mchafuko wa tumbo. Hakupenda kulisikia hili jina wakati mipango yao bado. Bencov na mtu wake wa karibu waliponyanyuka na kuondoka, Merina nae akakung’uta makalio kufuata mkia. Safari yao iliishia kwenye chumba cha mapumziko ya Dr. Lee kisha wakatwaa nafasi wakaketi. Ujio ule haukuwa wa miadi wala ahadi hivyo ukampa mashaka Dr. Lee kidogo akageuka kuwatazama kwa mtazamo wa kuuliza kulikoni.
“Dr. Lee, Unakumbuka kuwa tuliwaangamiza wapelelezi wawili kutokea Tanzania ambao walikuwa wanakuja Ungamo kwa ajili ya kumsaidia Backa juu ya kupotea kwa binti yake?” alianza kwa kuuliza Bencov. Dr. Lee akakubali kwa kutingisha kichwa huku akiwa makini kujua nini zaidi.
“Basi kuna mshenzi mwingine ameshaingia ndani ya Ungamo kutokea Tanzania huko huko, huyu hakuonekana na vijana wangu bila shaka na yuko tofauti na binaadamu wa kawaida maana anaakili ya kujua kuuwa na kuacha taharuki. Akiuwa anaacha kadi ya mualiko yaani anaacha kadi yenye bendera ya nchi hiyo ya Tanzania” alitulia hapo Bencov akapiga kimya. Lady Devil na Dr. Lee wakatazamana bila kuongea chochote. Ukimya ule haukudumu sana. Dr. Lee alikamata kichwa chake kilichokuwa kimelegea na kulalia kwenye bega la kulia akakiweka sawa kisha akaegamia kitini akauliza.
“Hajafahamika ni nani?” swali hilo likamgutua Bencov, akanyanyua simu hapohapo na kumpigia Rais wa zamani Mh. Mobande ambaye ndiye aliyempa taarifa hizo. Simu hiyo haikuita sana ikapokelewa.
“Eti, hamjaijua hata sura yake?” akaanza kwa kuuliza. Jibu alilolipewa ni kwamba asubiri baada ya muda mfupi anatumiwa kwenye mtandao. Akakata simu. Kweli baada ya kama dakika tatu Kompyuta moja iliyoletwa hapo ikapokea ujumbe. Harakaharaka wakaufungua. Zilikuwa ni picha mbili ambazo Bencov alizitazama lakini hakuzielewa akazipasi kwa Dr. Lee. Mungu wangu! Ulikuwa sio mshtuko wa kawaida.
Dr. Lee aliiangusha ile kompyuta mpakato hapo chini halafu akatulia kimya. Mapigo ya moyo yakawa yanakimbia kwa kasi sana. Merina akaiokota hiyo kompyuta na kuitupia macho. Hakuamini kwenye Kompyuta ile kile kilichokuwa kikitazamwa na macho yake.
“Roi!” alilitamka jina hilo kwa sauti ya mshangao.
“Huyo mtoto ni jini hana ubinaadamu hata kidogo na kama ameingia ungamo basi kazi ipo. Sidhani kama yupo wa kumzima huyo kijana” alisema kwa sauti ya upole sana Dr. Lee. Bencov akaiomba hiyo kompyuta kisha akaitazama tena picha ya huyo mtu anayeambiwa ni moto wa kuotea mbali lakini yeye alimuona ni wa kawaida sana hivyo hakushtuka sana.
“Tunafanyaje!” akauliza. Merina alipotaka kujibu, akagutushwa na sauti za mtu aliyekuwa akiingia mahali hapo. walipogeuka kuangalia, alikuwa ni Dr. Henry. Henry alikuwa akiingia kwa tambo kubwa mahali hapo. Macho ya kuuliza yakamtazama yeye. vipi? Kila mmoja akauliza.
“Mchezo umekwisha, ile sumu ni yenyewe na inatisha vibaya sana” akasema. Watu wakasahau habari za Roi wakageukia kwa huyo dokta. Tambua kuwa zilishapita wiki tatu tangu Dr. Henry aanze kuifanyia utafiti dawa ya maangamizi ya Diebrainaphine. ambayo ni kama mbolea ya chumvichumvi ukiitazama ila hiyo ilikuwa na uwezo wa kukuza mimea ya chakula inayodumu kwa muda wa wiki tatu ama nne, waliamua kuathiri na mbegu kabisa ambazo zitakuwa zikitumia mbolea hiyo kwa muda mfupi kabisa. Dr. Henry alikuwa tayari ameshaifanyia utafiti hiyo dawa na alikiwa na ‘information nzima ya tafiti yake. Alimtuma msaidizi wake atoe CD ambayo walitumia kuchukua maendeleo mazima ya Tafiti hiyo. CD ile ilipowekwa, ilianza kwa kuonesha jinsi ambavyo watu watakaotumia dawa hiyo, watakavyoelekezwa uandaaji wa mashamba yao kisha upandaji na utumiaji wa mbolea hiyo ambayo ni sumu ya kutisha sana. Ilikwenda ikapandwa na ilipokwisha kupandwa ukafuata wakati ambao mkulima atatakiwa amwagilie au hata kutegemea mvua ambayo si lazima inyeshe kwa wingi. Mazao hayo yatakuwa. hapo yalioneshwa Mahindi ambayo ndiyo kilimo kikubwa na uti wa mgongo kwa nchi nyingi za Afrika. Wakati mahindi hayo yanakuwa kwa kasi kubwa, kuna magugu mengine ambayo haya yalikuwa membamba sana na yaliota sambamba na shina la mmea husika. Ilikuwa vigumu sana kuliondoa gugu hilo kutokana na wembamba wake na jinsi lilivyoshikamana na mmea.
“Sumu inaanza kusambaa hapo” alisema Dr. Henry, watu wakawa makini zaidi kutazama CD ile huku wakimsikiliza Daktari huyo.
“Pindi kinapofikia kipindi hicho cha uchavushaji, hapo ndipo sumu hiyo inapoanza kutoka kwenye mmea gugu na kuingia kwenye mmea pandwa. Uchavushaji huo haufanywi na wadudu wala ndege. Hakuna mdudu anayeweza kuukabili mmea gugu huo na akithubutu kugusa hapo naye hana maisha. Ni hatari sana, harufu yake kwanza si rafiki kwa ndege wala wadudu. Uchavushaji wa mmea gugu na mmea pandwa, hufanywa na upepo. Tazama hapo kiooni” alitulia Dr. Henry na watu wakawa makini kutazama kioo cha mbele yao. baada ya kutazama sehemu hiyo, ikaja sasa sehemu ya madhara baada ya chakula kuvunwa kutoka kondeni hadi kufika likoni na kuwa tayari mezani. Madhara yalikuwa ni makubwa sana,
“kwanza mtu anapokula chakula kilichoingia sumu hiyo ya mmea gugu, huanza kuwashwa mwili baada ya masaa thelathini na sita (36). Siku mbili na masaa mawili kama sikosei” alisema huyo Dokta. kisha akaendelea huku akifuatana na ile picha kiooni.
“Muwasho anaoupata muhanga wa sumu hiyo huongezeka kila baada ya muda na haupungui wala kuwa na afadhali. Baada ya muwasho huo ambao hudumu kwa siku tatu ama nne, mtu huyu anapoteza nguvu mwilini, analegea kisha huanza kutoka damu puani na mdomoni, hali ikiwa hivi basi ujue hakuna tiba tena lakini kabla ya hapo kama muhanga atakimbizwa hospitali na kupewa dawa, siku hizi nilizozitaja hazitafika. Muhanga atapatwa na umauti kabla hata siku tatu hazija fika endapo atapewa dawa ya aina yoyote ile ya kutumia. Tazameni picha hiyo na mtazame kati ya mtu aliyepewa dawa za kihospitali na mtu ambaye hajatumia dawa ya aina yoyote ile” akahitimisha Dr. Henry, daktari katili mwenye asili ya kiingereza. Matabasamu yalikuwa makubwa sana kwenye nyuso zao kisha wakaachana na ile CD baada ya kuwa imefika mwisho, wakageukia kwenye lile la mwanzo. Walikuwa na furaha kubwa kwani waliamini kuwa hata huyo wanayemuita Roi huwenda akapoteza maisha kwa kula hiyo sumu ambayo hutoka kwenye mmea gugu unaofahamika kwa jina la Partathunum.
“Inabidi leo hii uende Ungamo Bencov ukapange vijana makini ambao watamsambaratisha huyo mtazania hata kabla hajaleta madhara zaidi. Naamini vijana wako na kama hali itakuwa ngumu basi nitakupa vijana wangu ambao wataingia kazini na kujua mbinu za kumuondoa huyo Jini kwenye himaya ya Ibilisi. Ili sisi tufike kileleni mwa mipango yetu” aliongea Dr. Lee akiwa ameweka furaha kando. Aliujua mziki wa huyo mtoto anayejiita Roi japo wengine walimuona ni kama kupe tu ambaye unaweza kumuuwa kwa poison spray. Bencov akasema kuwa hilo ndilo hasa alilokuwa akilifikiria. Wakatawanyika maeneo hayo huku Dr. Lee akihitaji mazungumzo na Merina pamoja na Lonto. Bencov akachukua gari akiwa na Mtu wake wa karibu, wakielekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Antananarivo. Wakati Bencov akiwa anaondoka maeneo hayo, huku nyuma aliacha kikao kizito sana cha watu watatu. Kikao kilichokaliwa kwa siri kubwa tena kilikuwa ni kikao ambacho kilifanyika kwenye chumba chenye giza kali sana. Sauti pekee ndizo zilizokuwa zikisikika lakini watu waliokuwa wakiongea hawakuonekana.
“Wasaa umefika, wasaa ule ambao tulikuwa tukiusubiria ndiyo huu. Lonto, utaungana na Dr. Henry kuelekea ungamo kisha Tanzania baada ya Bencov kuleta taarifa ya kinachoendelea huko” sauti ya mtu aliyeonekana ni kiongozi wa kikao hicho. Baada ya maelezo hayo, yalifuata maswali kutoka kwa kila mmoja aliyepo pale kwenda kwa huyo aliyeonekana ni kiongozi.
“mkuu, pamoja na hayo ambayo umeyaongea hapa lakini bado kuna jambo moja ambalo ni muhimu sana mkuu nalo ndilo nguzo kuu ya kila jambo ambalo tunataka kulitenda, nalo ni kafara, vipi kuhusu Bencov, hata husishwa kwenye hili?”
“Hata mimi nilikuwa na swali hilo mkuu” akaongeza Merina. Kimya kifupi kikapita kabla ya Dr. Lee ambaye ndiye kiongozi haswa wa kikao hicho hajaongea chochote.
“Hakuna njia atakayopita, hawezi kwenda kinyume na sisi hata kidogo nadhani mnajua kuwa hili ndilo linalonifanya mimi kuwa hai hadi leo na mkumbuke pia bado sijawa mkamilifu. Hapa nilipo ni sawa na mashine ya gari au mtambo wowote unaoishi kwenye bodi chakavu. Mwili wangu haujawa mkamilifu na pia vilevile maisha yangu yapo mikononi mwa King Bondo, kiumbe kilichoamua kuyabeba maisha yangu kwa makubaliano maalumu. Yeye ndiye anayehakikisha kuwa naishi na huku mimi, nikihakikisha na yeye anaishi. Hatua ya kwanza niliyokuwa naihitaji nimeshaikamilisha, bado hatua ya pili lakini hiki ndicho kipindi ambacho nasi tunatakiwa kuhakikisha naye anapata fuaraha kwa kila wiki ama milele” alizungumza Dr. Lee.
“Akikataa kushiriki nasi?” akauliza Merina.
“Atakuwa kafara ya kwanza kwa King Bondo na hakutakuwa na mjadala kwa hilo. Maisha yangu ni muhimu zaidi kuliko kitu kingine Lady Devil, kwenye kuutafuta ukamilifu wa maisha yangu niko radhi kuuwa kila anayekwenda kinyume na mimi. Nataka kuwa kamili na nataka kuwa mmiliki mkubwa wa dunia hii kwa kuwa na nguvu kubwa kwa ajili ya King Bondo nitamuuwa!” aliongea kwa kumaanisha Dr. Lee. Kimya kikarudi tena mahali hapo, Dr. Lee akasimamisha ukimya huo na kumalizia kile alichokuwa anahitaji kukimalizia.
“Lonto, fikisha taarifa kwa Henry mwambie ni wiki moja imebaki ama mbili za kufanya maandalizi ya kuondoka ndani ya ardhi hii” kikao hicho kikafungwa wakatawanyika.
Ndege kubwa ya shirika la ndege la Ethiopia, lilikanyaga ndani ya ardhi ya Ungamo kwenye uwanja mkubwa wa kimataifa wa Tao De. Dege hilo lilikuwa kubwa sana na lilikuwa limebeba abiria wengi mno. Baada ya kusimama mahali lilipopaswa kusimama, gari nyeusi ilisogea taratibu kuifuata ndege hiyo kisha kusimama umbali kidogo na ndege hiyo. Abiria wa kwanza kutoka ndani ya ndege hiyo alikuwa ni Bencov pamoja na msaidizi wale au mlinzi wake, moja kwa moja walielekea kwenye ile gari bila kupita mahali pa ukaguzi. Hii ndiyo ilikiwa desturi yake. Nchi hiyo ya Ungamo aliifanya kama ni himaya ya baba yake mzazi. Gari hiyo nyeusi iliyondolewa uwanjani hapo kwa kasi kubwa sana kutoka nje ya uwanja huo. Saa moja mbele, gari ile ilifunguliwa lango lile kuukuu la kizamani kisha ikazama ndani na kwenda kuegeshwa kwenye maegesho ya humo ndani. Bencov alishuka kwa kasi kubwa na kuelekea ndani ya jingo lile pasipo kutazama popote, alielekea hadi ndani ya chumba kimoja ambacho ndani yake alimkuta Bacon akiwa anavuta marijuana kama ilivyo ada yake.
“Ita kikao haraka sana” alisema kisha akatoka kwa kasi hiyohiyo. Watu wote walikutana kwenye ukumbi mkubwa sana wa mikutano. Makundi yote yalikutana hapo kisha yakaweka ukimya kusikiliza wito huo. Bencov alikuwa kwenye hasira zisizo kipimo na haikuwa kawaida ya kijana huyo hata mara moja kwenye maisha yake.
“Mnaijua kazi yenu ninyi ama ni nini? Mnajua sababu hasa ya kuwaweka hapa?” akatulia baada ya kuuliza maswali hayo kisha akamgeukia Bacon na kumuuliza swali jingine bila kusubiri majibu ya maswali tangulizi.
“Bacon jibu kwa niaba ya wenzako au huna cha kujibu?”
“Ndiyo, tunajua Boss!”
“Hamjui nyinyi, hamjui hata kidogo na laiti kama mngekuwa mnajua yasingetokea haya. Nimewaweka hapa kwa sababu ya kazi moja pekee ya kuhakikisha hakuna kiumbe anaingia kutoka nchi ya aina yoyote ile. Tazama huyu” akatupa picha moja juu ya meza. Picha hiyo ilikuwa ni ya Roi ambayo alipigwa na kijana mmoja ambaye alikuwa akimfuatilia kutokea Makao makuu ya polisi bila ya yeye mwenyewe kujua kisha kijana huyo kuzawadiwa kifo kabla ya kurudisha majibu mengine baada ya zile picha ambazo alizipiga angali bado yu makao makuu ya jeshi la polisi. Huyu ndiye alimpiga picha kijana huyo. Akaendelea.
“Mtazameni huyo, huyo ni Jasusi kutokea Tanzania. Nadhani mmeshasikia baadhi ya matukio yaliyokuwa yanaendelea hapa nchini” akaweka tuo. Bacon akatikisa kichwa kuafiki kuwa anajua hayo matukio yanayoendele. Hilo likawa kosa kubwa sana kwa kijana huyo.
alifoka vibaya sana hakutegemea uzembe wa namna hiyo kama ungekuja kutokea kwa vijana hao. Akawapa sifa ya huyo kijana kisha akawageukia Mbega ambao ndiyo kikundi pekee alichokuwa akitegemea wangeweza kumuona kijana huyo mahali popote wakati anaingia. Mbega wakasema kuwa pamoja na kuangaza macho yao hewani mara zote lakini sura ya binadamu huyo hawakufanikiwa kuiona. Bencov akasema anatoa masaa Arobaini na nane, anataka kuona mzoga wa huyo kijana mbele yake. Hatari kubwa sasa, Roi anatafutwa kila kona ya mji huo kama almasi.
Macho yalikuwa makini sana kila alipokuwa akitazama picha alizokuwa amepewa na yule mtu kule katikati ya mji. Frank kicha hakuamini kama huyo anayemuona kwenye macho yake ndiye aliyesababisha mauwaji ya Don Philipo. Picha hizo kumbuka kuwa zimerudi kwake baada ya yeye kutoa ile mikanda aliyoichukua kwa Don Philipo. Kulikuwa na picha mbili, moja hakuielewa, huyu alikuwa ni mwanaume aliyevaa prova lililokuwa limefunika hadi kichwa. Ni nani huyu? Alijiuliza huku akiirudia ile picha ya mwanamke ambaye alimfahamu. Kunamahali aliwahi kumuona huyo mwanamke. Ni wapi? Akajiuliza, jibu hakulipata akafikiri kwa muda akiwa palepale chimbo kwake. Akakumbuka. Aliwahi kukutana na huyo mwanamke mjini siku ambayo aliamua kuyazuia magari, huyu alimsaidia kumuokoa na kifo.
“Ninani huyu? Nimemkumbuka sasa, aliniokoa kutoka kwenye kifo mbele ya wale watu washenzi waliotumwa na J.M.J. Aliwajuaje wale kuwa si watu wazuri kwangu? Nakumbuka alikuwa yuko mbali sana na mimi lakini ile kasi aliyokimbia na kunikumba ilikuwa si ya kawaida, yule ni nani?” alizidi kujiuliza Frank akiwa anazidi kuitazama picha hiyo. Alifikiri kwa muda mrefu sana ndipo akakumbuka kitu. Petii, ndiyo, aliniambia anaitwa Petii. aliwaza kisha akasema.
“nimemkumbuka sasa, huyu mwingine je, ni nani? Ngoja” akajishauri. Akatoa simu yake ya mkononi akabonyeza namba fulani akaiweka sikioni.
“huyu mmoja wa kike niliwahi kukutana nae mahali (akamkumbusha ni wapi alikutana nae pamoja na kumtajia jina la huyo mwanamke). Huyu mwingine wa kiume bado sijamfahamu lakini nadhani kupitia kwa huyu nitamjua” akakata simu baada ya kutoa maelezo hayo kisha akajinyanyua akatazama saa kupitia simu yake, ilikuwa tayari ni saa kumi na mbili za jioni. Akaitazama simu yake ile ambayo aliifananisha na ile ya awali ambayo aliwahi kuchukulia matukio ya wazazi wake pindi walipokuwa wakiuwawa. Simu ile aliipoteza mtoni wakati akiwa anawakimbia askari waliokuwa na hamu ya kumtia mikononi baada ya kumuangamiza binti wa Rais Julio. Akayafinya macho yake kwa hasira kisha akajisahaulisha ile kumbukumbu mbaya kabisa. Muda umekwenda, usiku huu lazima kieleweke na lazima nijue huyu dada ni nani na kwanini anauwa. aliwaza kisha akatoka lile eneo na kuingia upande mwingine wa ile nyumba.
Wakati Frank akiwa anajiuliza, kwa upande wa Inspekta Bogo nako kulikuwa na mawazo ya aina yake. Yeye alikuwa akijiuliza kuhusiana na matukio ya vifo vilivyokuwa vikiendelea na aina ya mauwaji yafanywayo na muuwaji huyo. Kuuwa kisha kuweka kadi yenye bendera ya Tanzania, hili lilikuwa ni tukio jipya kwenye maisha yake na hakuwahi kulitegemea wala kulifikiria. Nani anayefanya haya? Alijiuliza tena mbaya zaidi ni mtu yule aliyekuwa kule kwenye mkutano na wale vijana ambao hata nao waliuwawa kwa mtindo huo. Kitu kilichomuacha hoi zaidi na kujua kuwa nyuma ya kila analolitenda kuna mtu nyuma yake, ni kitendo cha kukutwa kadi hiyo kwenye mwili wa Don Philipo ambao yeye ndiye aliyehusika kuuangamiza. Kichwa kilimuuma sana lakini akaona asijiumize kichwa, alifikiri jambo na kung’amua kuwa hakuwezi kufanyika harakati zenye mafanikio pasipo serikali kujua. Aliamini kuwa kama kuna mtu mwenye harakati kama zake basi huyo yupo kwenye haki lakini hakuna haki bila kuwashirikisha unaowatafutia haki. Baada ya kuwaza hilo, alinyanyua simu yake ya mkononi na kusaka jina fulani alipolipata, akapiga akasikiliza.
“Habari yako kijana?” Ilisikika sauti upande wa pili wa simu hiyo.
“Habari yangu ni nzuri mkuu” alijibu Insp. Bogo kisha akamalizia pasipo kutoa nafasi ya msikilizaji kuongea.
“Nitakuwa mgeni wako leo muda kama ule” akakata simu baada ya kupokea mrejesho wa ruhusa kisha akaigeukia Kompyuta yake mpakato kuchambua mambo kadha wa kadha ya dunia na mengi yakiwa yahusuyo kazi yake.
Hatuwezi kuyafuta machozi yaliopo miyoni mwetu, tunaweza kuyafuta yale yatokayo tu ndani ya mioyo yetu na kupitia kwenye milango ya mboni za macho yetu lakini ya ndani ya mioyo yetu, katu hatuwezi. Unapolia na kulia na ukalia zaidi, unapunguza machungu tu lakini si kuyamaliza machungu ya kweli hasa pale upatapo kidonda chenye kuuma hasa. Usiombe ukakutana na maumivu ya aina hiyo kwenye maisha yako, usiombe ukakutana na maumivu ya kupoteza sehemu ya wale unaowapenda. Hakuna wa kuziba pengo hilo hata iweje, hakuna wa kuweza kuziba nafasi ya uliyempoteza hata thumni. Wa awali ni wa awali tu hakuna awali mbovu asikudanganye mtu. Kwanini muandishi nasema haya?
Martan aliingia na warembo wawili ndani ya sebule kubwa waliyokuwa wakiitumia kufanyia starehe zao. Mbele ya Martan kulikuwa na Morde, fundi mkuu na muundaji au mtaalamu wa kuunda magari yenye uwezo mkubwa. Morde alikuwa na mrembo mmoja mrefu mwenye shingo ndefu kama ya Twiga. Alikuwa ni mrembo haswa kama tutamuweka kwenye kundi la urembo lakini kwenye meza hiyo ya pembeni kidogo, alikuwapo Tamimu ambaye hakuwa katika hali ya kawaida hata kidogo. Alikuwa akinywa pombe mithili ya Ng’ombe mwenye kiu anywavyo maji. Chupa kadhaa za pombe kali zilikuwa zimemzunguuka mahali alipo na nyingi kati ya hizo zikiwa tupu. Alionekana kuwa ni mwingi wa mawazo sana, muda mwingine machozi yalikuwa yakimtoka waziwazi kabisa na kuyafuta kwa kitanga chake cha mkono kwa kujishtukia. Alimpoteza baba tena kwa kifo kibaya sana, alimpoteza mpenzi tena mbaya zaidi alimpoteza akiwa katika hatua za mwisho za kutaka kukamilisha ndoa. Alikuwa akisubiri Tereza amalize shughuli zake za kufanya majaribio ya dawa aliyoitengeneza ambayo ilikuwa ni muhimu kwa maisha ya waafrika wote kisha afunge naye ndoa lakini haikuwa hivyo, Tereza aliondoka machoni mwake kabla, Tereza alizifunika ndoto za Tamimu kama upepo usambaratishavyo vumbi angani. Hali hiyo ilikuwa ikimuathiri moyoni mwake, hali hiyo ilikuwa ikifanya machozi mazito yatiririke ndani ya moyo wake huku yakikosa mfutaji. Moyo wa Tamimu ulilia, machozi yaliyobahatika kutoka nje ya moyo, ndiyo yaliyojenga maisha mapya ya kijana huyo. Akawa ni wa kulia kila wakati, akawa ni wa kutoa machozi kila anapomkumbuka baba wa Tereza, Mh. Backa, akawa ni wa kulia tu. Kibao kimoja cha ‘maumivu niache’ kilichoimbwa na msanii kutokea nchi jirani ya Tanzania, kikawa ndicho pekee anachokumbuka kuyanyonga mashairi yake hata awapo mahali pa kustahereka kama hapo. Vijana wake muda wote walikuwa ni watu wanaomhurumia sana bosi wao, maisha ya bosi wao huyo yalibadilika kwa asilimia kubwa sana. Walijaribu kwa kila hatua kuhakikisha wanamrudisha kijana huyo katika maisha yake halisi lakini bado ilikuwa ngumu mno. Siku hiyo Martan aliamua kumletea mwanamke mrembo sana bosi wake ili kujaribu karata nyingine kama inaweza kuzaa matunda baada ya nyingi kuwa garasa. Alikuwa mrembo kweli mwenye umbo, sura hata haiba yake ilionekena kuwa ya upole sana. Hicho ndicho kilichomfanya Martan kuingia ndani ya chumba hicho akiwa na wanawake wawili.
“Anaitwa Zayona ni msichana mrembo sana boss” alisema Martan. Tamimu alikinyanyua kichwa chake na kumtazama huyo mrembo anayesemekana ni mrembo sana. Kweli alikuwa mrembo na hadhi ya urembo ilimstahiki yeye kwa wakati huo.
“Karibu Zayona, karibu vinywaji, kunywa na ujisikie huru kufanya uwezalo. Nimekuwa kwenye furaha hii kwa muda sasa sina furaha nyingine mimi, nimepoteza watu wangu muhimu sana kwenye maisha haya, nimempoteza baba, nimempoteza mpenzi wangu niliyekuwa nampenda zaidi ya kila kitu kwenye maisha yangu amekwenda na upendo wangu wote, sasa sina upendo tena zaidi ya ufariji tu wa watu wangu wa karibu na pombe” alisema mengi Tamimu, alipomaliza kueleza kila kitu akionacho sawa, akabaki kutulia kisha akanyanyua chupa ya pombe na kumimina kwenye gilasi yote.
“Yote haya niliyaona boss” alisema Martan na kumfanya Tamimu anyanyue kichwa chake na kumtazama. Akaendelea.
“Najua ni vigumu kuurudisha upendo uliopotea lakini acha sisi wafariji wako tuliobakia, tutafute mbinu ya kuifanya furaha yako irudi japo robo, mtazamame Zayona usoni” Tamimu akainua sura yake akamtazama Zayona kisha akairudisha kwa Martan.
“ni msichana mrembo sana, huyo ndiye niliyekuchagulia na ndiye atakayeirudisha furaha yako taratibu” baada ya kuongea hayo Martan, mshtuko mkubwa sana ukamkumba Tamimu, mshtuko ambao ulimshangaza kila mmoja mahala hapo na ni mshtuko uliomtia hofu kubwa Martan.
“Martan!” aliita kwa sauti kubwa Tamimu. Martan akajibu naam Boss.
“Huwezi kuwa kuwadi kwenye maisha yangu. Pombe haiwezi kunitoa akili hadi kusahau nafasi yangu. Nani kakuambia pengo la jino linazibwa na jino kutoka kwenye kinywa cha mwanadamu mwingine? Martan umenikosea sana, umenikose kiasi cha kukufanya nikuone huna huruma nami” alifoka Tamimu tena kwa sauti kubwa sana, alifoka kiasi kwamba hata ule muziki uliokuwa ukiwaburudisha wafanyakazi wote wa T.N. RACE, uzimwe.
“Si kama sina huruma na wewe Boss, nakuhurumia sana na ndiyo maana nimeamua kufanya haya….!”
“Nyamaza wewe, mapenzi unayajua wewe, wewe huyajui mapenzi na ndiyo maana unafanya mambo kirahisirahisi kama unatitika debe tupu. Hakuna mwanamke anayeweza kukaa nafasi ya yule mwanamke niliyempoteza au wewe unaniona mjinga kwa kutokumtafuta” alisema kwa hasira kiasi cha kubadilika hata sura. Martan alipotaka kutia neno, alishtukia akipokea ngumi nzito sana ya kifua, Martan akabingilia na kiujipigiza kwenye meza moja nyuma yake.
Tamimu alimfuata kama Faru aliyejeruhiwa akakamata ukosi wa shati na kumshushia kipondo kama si ujanja wa Martan kuziba sura kwa mikono yake, uso ungechafuliwa vibaya sana. Wafanyakazi wengine walikuja na kumuamulia. Walitumia nguvu sana kumtoa japo alikuwa anataka aendelee kutoa adhabu kwa kijana huyo. Morde na wafanyakazi wengine wakasimama na kusema kwa pamoja huku wakiwa wamemkinga Martan.
“Si mpango wa yeye pekee, huu ni mpango wetu sote tulioupanga kwa utashi wetu. Boss, tumeona mwenendo wa maisha yako ulivyobadilika ghafla, hivyo tukajua ni mapenzi yalisababisha yote hayo. Tukamteuwa Martan afanye hii kazi lakini kumbe hukupenda. Sisi tulijenga hofu baada ya kuona uko mbali na mwenendo mzima wa kampuni na kwa sasa umekuwa ni mlevi kupindukia, hii ni hatari sana bosi na hatungependa kuacha hali hiyo ijenge mazoea mwilini mwako” maneno hayo yaliyotolewa na Morde, yalimuingia sana Tamimu, aligeuza macho yake kwa kila mfanyakazi aliyekuwepo mahala hapo akaona jinsi walivyokuwa wakikubaliana na maneno ya mwenzao. Aliumia sana moyo wake Tamimu, alikuwa na hasira kali mno alikosa kujielewa kwa asilimia kubwa mno. Aliondoka hapo mbele ya vijana wake akiwa na hasira kubwa sana.
Asubuhi kulipokucha Tamimu alikuwa mchovu sana na aliamka akiwa mnyonge kupitiliza. Alikuwa yupo nje kwenye bustani yake kubwa aliwa anatazama mandhari ya eneo hilo, alipoteza uwezo wa kufanya kazi, alipoteza nguvu ya mwili pia alipoteza uwezo mkubwa wa kufikiria. Hapo alipo hakujua chochote kuhusiana na maendeleo ya kampuni yake kila siku kijana huyo alikuwa ni yeye na ulabu ulabu na yeye, kifupi ni kwamba alipoteza muelekeo mzima wa maisha yake.
“Boss!” aliita Morde akiwa anapiga hatua ndogondogo kumkaribia Tamimu. Kijana huyo mdogo mwenye utajiri mkubwa, aligeuka na kumtazama huyo aliyeemuita.
“samahani sana Boss kwa lile ambalo lilifanyika jana, najua kuwa tulikukwaza sana. Ni wazi binaadamu anapokosa, anastahili kuomba msamaha kwa kile alichokikosea, tumekosa na ndiyo maana leo niko hapa kuhakikisha nasimama kwa niaba ya wenzangu” alizungumza Morde.
“Haujanikosea wewe wala hawajanikosea wenzako, nashindwa kuelewa ni kwanini niko hivi Morde, nimekuwa wa ajabu sana nimebadilika najiona, nahisi mimi ndiyo niliowakosea ninyi” aliongea Tamimu.
“Hapana Boss hujatukosea hata kidogo bali sisi ndiyo tuliokurupuka na kupanga mambo amabayo ni kero kwako, tulipanga ujinga ambao ni kero kubwa sana kwako na laiti kama kweli hatukukukera jana kamwe usingethubutu kutoa adhabu kwa Martan” Tamimu akarudisha nyuma tukio akakumbuka jinsi alivyomshushia kipigo Martan, aliumia sana Tamimu, aliumia kupitiliza hakuwahi kugombana na wafanyakazi wake hata siku moja hiyo ilikuwa ni mara yake ya kwanza. Kwanini amefanya yote yale? Kwanini alimvamia na kumpiga Martan? Kwanini?
“Nahitaji kuonana na Martan sasa hivi” aliongea Tamimu.
“Boss, Martan ameniagiza kwako, ameniambia nije nikuambie kuwa amekosa sana na anakutaka msamaha, amekiri kosa pia amesema haitakuja kutokea ukapata maumivu tena sababu yake”
“Kwanini umsemee wewe, nipeleke alipo Martan sasa hivi” alisema Tamimu.
“Amesema hutomuona tena Boss, Martan ameamua kuondoka ndani ya himaya hii”
“Whaat?” aling’aka kwa kiasi kikubwa sana Tamimu, kitendo cha kuambiwa kuwa Martan anaondoka, kilikuwa ni kibaya sana na hakukitegemea. Tamimu hakutaka kusikia habari za kuondoka kwa kijana huyo hata kidogo. Nilikosea sana, nilivuka mipaka sasa nakiri. alijiwazia Tamimu kisha akauliza ni muda gani tangu kuondoka kwa kijana huyo. Morde akajibu kuwa si muda mrefu sana na kwa muda huo hata getini atakuwa hajatoka bado.
“Kwanini msimzuie sasa? Kwanini mmeruhusu aondoke” alifoka Tamimu huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Tumejaribu kumsihi sana lakini hakutaka kutuelewa hata kidogo” Morde alijibu. Tamimu alitoka mahali hapo mbio sana hadi upande wa mbele wa jingo lile. Alipofika langoni, akasogea hadi mahali alipo mlinzi.
“Wapi Martan alipo Kakaaa!” alifoka Tamimu.
“Martan!” mlinzi akashaangaa lakini muda huohuo, Martan akatokea langoni hapo akiwa amebeba begi lake dogo mgongoni huku kubwa kiasi akiwa amelishika mkononi.
“Nini unafanya Martan, unafanya nini sasa?”
“Nimeamua kuondoka Boss, sioni sababu ya kuendelea kuwepo mahala hapa wacha niende nikaendelee na maisha yangu” alijibu Martan.
“Najua kuwa nimefanya kosa, najua kuwa nimekukosea Martan lakini……!”
“Hapana mimi ndiye mkosaji mkuu Boss, hakuna jambo jema na la maana ambalo nimewahi kulifanya likakufurahisha hata moja. Nimekuwa ni mtu wa kukukwaza kila wakati wacha niondoke, wacha niirejeshe furaha yako maana hakutakuwa na atakaye kukosea tena. Mimi ndiye niliyepanga upuuzi wote ule wa jana baada ya kuona haukuwa na furaha na nilitaka kuirudisha furaha yako iliyopotea lakini kumbe nilikosea. Naomba unisamehe sana” aliongea Martan akiwa anauchungu mkubwa Machozi yalimtoka lakini alijitahidi kuyafuta.
“Martan!” aliita Tamimu.
“Wewe na mimi ni binaadamu, ukamilifu wetu ni siku tunaingia kaburini, hakuna mwandamu aliyekamilika kiasi cha kila anachokitenda kiwe na thamani kuishinda dhahabu. Nakiri kuwa ulinikosea sana jana niwe muwazi lakini hata mimi nilikukosea sana, sikustahili kufanya yale niliyoyafanya” aliongea Tamimu.
“Kwanini mimi kila siku sasa, kwanini mimi ndiwe mwenye kukukosea kila wakati. Kumbuka kuwa mimi ndiye niliyesababisha mashindano yale akashiriki mtu mwingine nawe ukajua ni mimi. Hata kama alishinda lakini lile lilikuwa ni kosa kubwa sana inamaana kama angelikuwa ni mtu mbaya, mimi ndiye ningekuwa msababishi mkubwa. Nisamehe sana Boss”
“Martan kumbuka kuwa wewe ndiye ulikuwa msaada kwangu na laiti kama labda asingelikuwa yule aliyetumia mavazi yako kushindana siku ile, Serikali isingemtia mikononi bwana Don Dou. Kumbuka wewe umekuwa msaada mkubwa kuirejesha Sami Ado ambayo ilikuwa chini ya yule bwana, wewe ni mtu wa pekee sana tafadhali usiondoke naomba urudishe maamuzi yako nyuma kwani hakuna binadamu mkamilifu hata mmoja” alisema Tamimu huku akikazia kwa kumalizia.
“kumbuka mimi nilifanya maamuzi ya kuhakikisha wote mnakuwa karibu nami baada ya kujua kumbe ninamaadui wengi nisiowajua kama lile jambo lingenichukiza nisingefanya maamuzi yale” baada ya kusema hayo, Tamimu alitaka kuzidi kuomba msamaha zaidi lakini Martan akadondosha begi alilokuwa amelishika mkononi akamkumbatia bosi wake huku akizidi kuomba radhi kutokana na maamuzi magumu aliyotaka kuyachukua. Tamimu akamsihi na kumuambia asijali wote walikoseana na hawakuwa na budi kufuta yaliyopita.
“Boss!” sauti nzuri ya kike ikawashtua kutokea nyuma. Wakaachiana kukumbatiana na kumtazama huyo aliyeita hakuwa mwingine alikuwa ni Zayona. Tamimu akameza funda kubwa la mate na kumtazama binti huyo.
“Kuna simu yako imeingia sasa hivi” akasema huyo binti. Tamimu akatoka hapo na kuelekea huko kulikokuwa na simu, akachukua mkonga wa simu na kuuweka sikioni. kisha hakuongea chochote alibaki kuwa msikilizaji hadi simu hiyo ilipokatwa. Akauliza.
“Morde yuko wapi?”
“Hayupo Boss ameondoka muda tu”
“ok, nifuateni hadi garini, sote watatu tunahitajika kwenye ofisi ndogo. Wakatoka hapo hadi mahali gari ilipo walipofika huko mahali gari zinapopaki, hakuiona gari yake anayoitumia muda wote, alipotaka kuuliza akazuiwa kisha kuoneshwa gari nyingine.
“Karibu kwenye gari yako mkuu, hii ndiyo gari utakayoitumia kuanzia sasa” alisema Zayona. Tamimu hakuongea kitu alikaa kwenye usukani na kuindoa gari hiyo taratibu hadi langoni. Kakaa hakuwepo. Kila alivyopiga honi hali ilikuwa ni kimya tu hakukuwepo kakaa wala kivuli chake. Mule ndani ukimya ulikuwa umechukua nafasi kubwa sana.
“Wapi kakaa alipo?” akauliza.
“Kakaa amepangiwa kazi nyingine na kiongozi hivyo hatakuwa mtu wa getini tena na unasubiriwa wewe umpe majukumu mapya lakini si ya kukaa getini” alijibiwa hivyo na Zayona.
“Mnawazimu ninyi eeenh! Kwahiyo ni nani atahusika na hapa getini?” alifoka.
“bonyeza kinobu chekundu hapo kwenye usukani” alielekeza Zayona, Tamimu akafanya kama alivyoelekezwa mara akaona lango likifunguka lenyewe, hali hiyo ilimstaajabisha sana lakini hakuuliza kitu akaliondoa gari kwa kasi kubwa huku nyuma lango likijifunga lenyewe baada ya kubonyeza tena kile kinobu. Walifika nje ya ofisi ndogo ambayo ndiyo walikuwa wakiitumia kwa ajili ya mikutano yao. Waliposhuka garini, Tamimu alimfuata Zayona na kumwambia kwa sauti ya chini.
“Utazidi kuwa mtendaji mzuri wa kazi na napenda utendaji wako lakini mapenzi yaliyojiunda moyoni mwako futa na sahau” kisha akaondoka kwa mwendo wa haraka akimuacha Zayona akiwa kwenye tabasamu kubwa.
Ofisi hiyo ilikuwa imejaa wafanyakazi wengi sana wa kampuni hiyo ya TN RACE. Kila mmoja alikuwa kwenye suti safi ya kuvutia sana. Nafasi zilikuwa zimetendewa haki mahali hapo hata hao waliongia muda huo walitwaa nafasi zao huku Tamimu akienda mbele kwenye meza ya viongozi.
“Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kuwa wote tulionza tuko hapa na tumekutana tena kwa ajili ya maendeleo ya kampuni yetu” alisema Morde ambaye ndiye fundi mkuu wa kampuni hiyo. Watu wote walikuwa kimya mahali hapo akasema tena.
“ni faraja yangu tumekutana tena lakini dhumuni na dhima kuu ya kikao hiki ni kwa mambo mawili makuu, jambo la kwanza likiwa ni kujuzana kuhusu mfumo mpya ambao tumeugunduwa wa kuhakikisha hakuna gari yetu hata moja itakayohitaji mfunga wala mfungua lango.
Mfumo huu mpya na wa kipekee utatumiwa kama ifuatavyo. Gari yako itakapoingia kwa mara ya kwanza kwenye lango letu, utabonyeza kinobu chekundu na ukishalipita lango hilo utafanya kama ulivyofanya awali. Baada ya hapo hutotakiwa tena kubonyeza kinobu hicho abadani kwani tayari gari hiyo itakuwa imeingia kwenye huo mfumo milele. Hii ni kwa gari za ndani lakini si kwa zile ambazo zinatoka nje ya Kampuni hii nikiwa na maana si zile ambazo zitauzwa. Wafanyakazi wote walipiga makofi kwa kufanikiwa hilo lakini hapohapo Morde akaendelea kwa sababu ya pili.
“Sababu ya pili ya kukutana hapa ni hii. Ni furaha kubwa na niseme ni jambo kubwa mno ambalo mwisho wa hapa inabidi nimuombe radhi Boss kwa kutokumuambia hili. Kampuni ya TN RACE, imeingia kwenye mashindano ya magari Afrika ambayo yatafanyika huko Nairobi kenya lakini kabla ya hapo tunatakiwa tutoe sampuli ya gari moja ambayo itakwenda kufanyiwa uchunguzi na wataalamu wa kimataifa ili kujua kama gari hizi zimekidhi ubora wa kimataifa, nadhani kwenye hili hakuna shida” wakati Morde anamaliza kuongea, Tamimu alikuwa mdomo wazi asiamini kile ambacho anakisikia mahali hapo. Inamaana hadi kampuni yake inachaguliwa kuingia kwenye mashindano hayo yeye hajui chochote. Ama kwa hakika alikubali kuwa alifikia pabaya mno.
“Mungu wangu!” alihamaki Tamimu.
“Kabla ya mashindano hayo ambayo yataanza wiki mbili zijazo, tunatakiwa kuwa na madereva wawili ambao watakwenda kushiriki katika mashindano hayo. Tukumbuke tu kwamba mashindano hayo yatakuwa yakioneshwa kwenye vyombo vikubwa vya habari duniani kote” alisema Morde. Tamimu kusikia kuwa mashindano hayo yataoneshwa kwenye vyombo vya habari vya dunia, alijikuta akipata nguvu kubwa na kuamini kupitia mashindano hayo anajua ni wapi mchumba wake alipo. Hakutaka kuamini kuwa eti, Tereza amepoteza maisha, aliamini asilimia mia moja kuwa mpenzi wake bado alikuwa hai hivyo alitaka kuhakikisha hiyo ndiyo inakuwa njia ya pekee ya kumuona mpenzi wake au yeye kuonwa na mpenzi wake. Mwisho kabisa wa kikao hicho ambacho kilikuwa na umuhimu mkubwa, Morde alichukua jukumu la kuomba radhi kwa bosi wake mara baada ya kusisitiza mazoezi. Tamimu alisimama na kuzungumza machache huku akisema kuwa hakuwahi kuamini jambo hilo kama lingekuja kutokea. Alisema amekuwa na imani kubwa na vijana hao katika utendaji na kujitoa kwao huku wakionesha uzalendo mkubwa sana kwenye kampuni hiyo. Hakuamini kama wangeweza kuzidi kusimama na kupigania kuhakikisha kampuni yake inaingia kwenye mashindano ya Afrika ambayo ni tiketi pekee ya kuingia kwenye mashindano ya dunia na hatimae kujitangaza kimataifa kuwa kuna kampuni inayotengeneza magari yaendayo kasi ipo Afrika tena kwenye nchi changa kabisa kimaendeleo. Akasema kuanzia muda huo hadi siku husika inafika, ni mazoezi kwenda mbele na anataka yeye awe ni mmoja wapo kati ya watakaoshiriki kwenye mashindano hayo. Alitaka kuwa na kijana mmoja tu ambaye atakuwa naye ili kuweza kushiriki kwa gari mbili kutoka kwenye kampuni yake.
“Nani yuko tayari kushiriki nami kwenye mashindano hayo?” aliuliza Tamimu. Wa kwanza kusimama alikuwa ni Martan kijana mdogo mwenye uzalendo na uchungu mkubwa. kijana aliyesaidiwa kimaisha na Tamimu kisha kumuingiza kwenye udereva wa magari yake na kuwa kinara kabisa katika uendeshaji wa magari, alikuwa ni tishio sana kwa vijana wenzake ndani ya kampuni hiyo katika kukimbiza gari na ndiyo maana hata siku ile alipopokonywa gari na Roi baada ya kufungiwa kule nyumbani kwake, watu wengi hasa vijana wenzake walijua ni yeye kwani walikuwa wanamjua vizuri tu. Vijana wengine watano wakasimama kumuunga mkono bosi wao. Tamimu akatabasamu kisha akasema.
“Kuanzia kesho ni mashindano, tutashindana sisi wenyewe hadi tufikie watatu kisha nitatangaza mashindano makubwa ambayo yatashuhudiwa na watu wengi huku nikiwatangazia kuwa hiyo ni kwa ajili ya kushiriki kwenye mashindano ya Afrika kwani kampuni yake imepata bahati ya kushiriki kwenye mashindano hayo. Kikao hicho kikafungwa na kila mmoja akiwa na ari ya kuanza mazoezi hayo yatakayofanyika siku hiyo iliyopangwa.
Wakati hayo yanaendelea uraiani, kule mahabusu ambako Don Dou alikokuwa amehifadhiwa akisubiri mashtaka yake kusikilizwa baada ya kusomewa mashtaka matatu moja likiwa ni kuuwa watu wengi wasio na hatia, pili ikiwa ni kutaka kufanya mapinduzi baridi na tatu ikiwa ni kujipa mamlaka kinyume na taratibu za nchi za kutaka kukitawala kipande kimoja cha Taifa hilo kifalme. Don Dou aliweza kuona taarifa ile ya kuingia kwa kampuni ya hasimu wake kwenye mashindano ya Afrika. Alijua fika baada ya pale ni mashindano ya dunia. Hilo lilimuuma sana moyo Don dou aliumia kupita kawaida. Alisimama kwa hasira na kupiga ngumi nzito ukutani kisha akazikamata nywele zake nyeupe na kuzilaza kwa nyuma kabla ya kuanza kukizunguuka kile chumba kwa hasira kuu.
“haiwezekani, haiwezekaniiiii!” alipiga kelele nyingi Dou kisha akarudi kwenye kitanda kidogo cha mule mahabusu. Alikuwa amewekwa kwenye chumba cha peke yake huyu mzee kutokana na ukatili alionao. Kuuwa kwake ilikuwa ni kama kuvuta mtepa kwa Sultani. Alipenda kuuwa kuliko anavyopenda kitanda wakati wa ngono. Dou kwenye swala la kuuwa huwa hana undugu hata chembe kama alithubutu kusema kuwa anauwezo wa kumuuwa mama yake mzazi unafikiri angeshindwa kuuwa mjinga mwingine yeyote. Wanao mfahamu kama aliyetaka kuwa mfalme wao wa Sami Ado, walimtukuza kwa kumuita Don, Don Dou.
“Don, Don Dou!” Sauti nzito iliita dirishani ndani ya chumba alichomo yeye. Dou akageuka kutazama kwenye kidirisha cha kuongelea na mtu, vidirisha hivyo mara nyingi wamekuwa wakivitumia maaskari magereza kutoa chakula kwa watu watukutu na wenye historia mbaya kama ya Dou ambao hawakutakiwa kutoka nje ya vyumba vyao kihasara hasara. Dou aligeuka na kutazama kwenye kile kidirisha, hakuwahi kuitwa hata siku moja mara nyingi amekuwa akipokea chakula tu na si kuitwa. Mwili wake ulikuwa umejaa majeraha makubwa baada ya kupinduka na gari siku ya tukio alipotaka kutoroka, Alitisha sana Don Dou. Hakujibu kitu alishika ndevu zake nyingi kisha akasogea hadi hapo dirishani.
“nani wewe uliyefika hapa muda huu?” aliuliza Dou.
“unajua ni ngumu sana mahabusu mwenye mashtaka makubwa na ya uhaini kama wewe, ni vigumu kutembelewa na mtu lakini hakuna kigumu mbele ya pesa na ukuu. Dou, usiku wa leo ndiyo mwisho wa wewe kuwepo hapa mahabusu, utatoroshwa na kuingia kwenye mpango kabambe wa kutimiza ndoto zako na za wengine” alisema mtu huyo aliyefika mahali hapo. Alikuwa ni mwenye sura pana, kwa mtazamo wa sura tu ungeweza kugundua kuwa mtu huyo alikuwa ni bonge.
“Mbona sikuelewi wewe unasema nini?” alistaajabu Dou.
“Utanielewa tu Dou subiri” alisema mtu huyo kisha akatoweka. Dou alicheka cheko kubwa sana Cheko lake lile alipendalo kisha akazikamata nywele zake na kuzirudisha nyuma akatulia kimya akitafakari na kumfikiria mtu aliyemjia.
MASAA MAWILI NYUMA NDANI YA JINGO LA RAIS JULIO.
“Mkuu nini unawaza hadi ukasema hivyo?” aliuliza mjumbe mmoja. Rais wa zamani bwana Julio Mobande alikuwa kimya kama si yeye vile mahali hapo lakini ndani ya kichwa chake kulikuwa na wazo kuu na aliloliona linatija sana kwake. Hilo ndilo aliloliwasilisha kwa watu wake hapo lakini hawakuwa wamemuelewa vizuri. Julio alivuta gilasi ya mvinyo akaufinya wote na kutoa sauti za kuupenda mvinyo huo kisha akawageukia watu wake akasema.
“Hatuwezi kuwa wajinga wa kuona wenzetu wanakufa ni lazima kuna jambo kubwa hapa litakuwa limejificha na kupitia hili nililoliongea kwenu, tunaweza kuzalisha matunda yenye mafanikio kwetu. Tambueni kuwa hii nchi inatakiwa kuingia mikononi mwetu kwa haraka kubwa mno sasa hatuwezi kuwategemea wazungu watusaidie kila kitu hata sisi wenyewe tunapaswa tujitume na tuoneshe tunauhitaji na hii nchi” alisema Julio lakini bado ilikuwa ni sintofahamu kwa wajumbe walioko maeneo yale, kulikuwa hakuna mjumbe asiyejua kama hapo walipo walikuwa wanaitaka Ungamo kwa udi na uvumba lakini hawakuitaka kwa kuanzisha vita na kusababisha mataifa kujua kuwa sasa Ungamo kuna vita ya kimapinduzi kama ilivyo kwa baadhi ya nchi ambazo zinaendesha vita vya namna hiyo. walichotaka kujua hapo ni kipi mkuu wao anafikiri au anataka kufanya. Hawakusita kuuliza lakini Julio akatamka jina moja tu nalo ni Dou akimaanisha Don Dou. Watu macho yakawatoka hawakuamini kusikia hilo jina likitajwa hapo mbele yao.
“mkuu si unakumbuka kuwa huyu alikupokonya jimbo moja lililojitenga, jimbo la Sami Ado akalitawala kifalme na kuuwa kila aliyeleta chokochoko juu ya jimbo lile, sasa iweje leo awe kwenye mipango yako ya kuirudisha ungamo kwenye mikono yako je, inamaana utakuwa tayari kumuachia tena ule mji wa Sami Ado, mji wenye utajiri mkubwa wa madini mengi?” mjumbe mmoja aliuliza swali. Julio akatulia kabla ya kusema.
“Nisikilizeni vizuri, najua ni lazima muwe na mashaka kwa hili lakini nataka mjue kuwa mwanzo tulichaguliwa na wananchi lakini leo hii tunataka kurudi kwa kutumia mabavu hivyo namtumia huyu kwa sababu maalumu nayo ni hii,” akaweka koma kisha akamimina kinywaji na kunyanyua macho yake tena.
“Don Dou alitaka kushinda kwenye mashindano yale ya kuitangaza kampuni yake hapa Africa mashariki, Afrika na kidunia ili baadae aje kushindana kwenye mashindano haya ya Afrika kwenda dunia yatakayofanyika wiki moja ama mbili zijazo huko nchini Kenya. Kumbukeni kuwa alikuja na hila nyingi sana za kutaka kushinda mashindano yale moja ikiwa ni hata kuuwa ili tu ashinde lakini hakuweza. Kuna mtu alimzidi nguvu na mtu huyo hajulikani ni nani, mtu huyo alisababisha hadi kifo cha kijana wake wa karibu sana hivyo hamuoni kama yeye atakuwa anamjua muuwaji na anaweza akatusaidia sisi, yeye kama yeye kutokana na kuwa ni mtu hatari mwenye mbinu nyingi za kumtambua mtu mbaya?”
“Je, kama sisi tungeamua kuvamia kwenye kampuni ya yule kijana na kufanya vitisho ili watutajie ni nani aliyefanya yale siku ile, si ingekuwa rahisi kuliko kumrudisha huyu muuwaji mtaani anaweza kuja kutugeuka huyu akawa mwiba kama mwanzo” aliuliza mjumbe mwingine.
“Najua kinachowachanganya ninyi ni woga na hofu hakuna kitu kingine lakini kwa kuwa nimeamua na hakuna wa kupinga nilichokiamua mimi, lazima Dou akatoroshwe mahabusu iwe kwa namna yoyote ile, iwe kwa kuuwa au kwa mazingara lakini lazima atoke. Si kama njia mnayoifikiria ninyi mimi siijui, naijua sana lakini hamuoni watu wetu wanavyouwawa hovyo, tulieni tujaribu na mbinu hii” alisema Julio kisha akamteuwa Jalome kuwa ndiye atayesimamia suala zima la kumtorosha mbabe huyo. Hivyo kitendo chake cha kwenda kule mahabusu ilikuwa ni njia tu ya kuangalia njia ya kuweza kujua jinsi ya kumtorosha mtu huyo. Ilikuwa ni ngumu kuweza kumuona Dou lakini pesa aliyotumia Jalome kuwahonga askari magereza waliokuwa lindo zililipelekea kupata wepesi mkubwa wa kuweza kupenyeza shilingi kwenye tundu la sindano.
Vikosi vyote hatari vilikuwa mitaani kimya kimya vikimsaka mtu ambaye anadaiwa kuwa ni muuwaji, kila kijana alikuwa na picha ya mtu huyo. Hawakujua tu kuwa hata hapo walipofikia Roi alishajua kuwa kwa kazi ndogo tu aliyoifanya, atakuwa anatafutwa kwa udi na uvumba. Mtindo alioutumia siku ile alikuwa amebadili kabisa, sasa alikuwa kwenye suti nzito huku ile mawani yake aipendayo ambayo alipewa na Hussein Babu akiitumia sasa kuanzia hapo na kwa muda huo ndiyo alikuwa akiingia kazini kikwelikweli. Ndani ya klabu moja kubwa ya mjini hapo, kulikuwa kukirindima muziki mkubwa na uliokuwa ukiwapa wazimu watu wote waliokuwa ndani ya ukumbi huo wa burudani. Ulikuwa ni ukumbi maarufu sana uliokuwa ukimeza kila aina ya rika bora tu awe ni mpenzi wa anasa. Watu wenye suti hata wenye vitambi walithubutu. Gari aina ya Mercides Benz new model ilipiga break mbele ya ukumbi huo wa starehe, wakashuka watu wawili mmoja alikuwa mwanaume na mwingine alikuwa ni wa kike, wakazama ndani ya ukumbi huo uliokuwa ukitoa hamasa kubwa sana ya kuweza kumpenda ibilisi kwa jinsi muziki ulivyokuwa ikitumbuizwa na wachezesha Santuri kwenye mashine zao. Watu wale walipoingia ndani ya ukumbi ule, nyuma ya kama dakika tano kutoka kwa wale walioingia mule ndani, gari nyingine aina ya SSC Tuatara iliingiia mahali hapo. Mtu aliyekuwa akiiendesha gari hiyo ya kukodi alikuwa ni Roi ambaye alichukua gari hiyo mahususi ili kuendana na muonekano aliokuwa nao. Alikuwa ametinga suti safi sana nyeupe inayowaka huku akiwa ametundika udevu wa kunyurutika kwa rangi yake nyeusi pamoja na sharafa alizozishusha kwa kupendeza. Ama kwa hakika alionekana ni kijana mwenye kujijali sana. Alivaa four angle safi nyeupe miguuni mwake zilizozidi kumpa daraja la kijana anayejijali. Muziki ulikuwa ukivuma na kuleta raha kwa kila aliyemo humo ndani, hata kama hukuwa na dhamira ya kucheza ni lazima ungejaribu hata kujitingisha kichwa ama miguu. Roi alipita moja kwa moja hadi kwenye kiti kirefu kilichopo kaunta. Akaagiza awekewe mvinyo mkali kwenye gilasi. Mvinyo ukamiminwa na taratibu akaanza kuunyonya. Alipiga gilasi ya kwanza pili na tatu akatulia huku ya nne ikiwa kwenye gilasi tayari. Macho yake yakageukia kule ambako watu walikuwa wakikata ngoma. Macho yake yakakutana na binti mmoja mrembo sana ambaye alikuwa akijua kwenda na mtindo wa mdundo wa muziki huo. Hakuonekana kuhitaji kucheza na mtu yeyote yule japo wanaume walikuwa wakitamani sana kumsogelea. Roi alizidi kumtazama binti yule ambaye alikuwa amejichora usoni lakini sura yake haikupoteza mvuto bado. Mh! Mbona amejichora vile?
“Nakuja tena kwa mara ya mwisho, ukinizidi nakuruhusu uniuwe” alisema Frank. Akasimama, Kitema akajipanga kisha akaja kwa mapigo ya kumaliza kazi hiyo aliyotumwa, alikosea. Pigo lake lilikwepwa kwa utaratibu maalumu na wenye lengo maalumu, kwani Kitema akiwa anakuja kwa pigo la kijanja na kushangaza, Frank alidanda kuta moja iliyopo hapo na kujigeuza, pigo hilo likapita kisha kuachia pigo baya sana la kwenye mbavu za kushoto. Kitema akashidwa kijihimili akaenda chini, hata kuamka ikawa shida kwake. Frank akaamua kuja kwa lengo la kumaliza lakini ghafla bin vuu! Kukasikika milio ya ving’ora vya gari za polisi vikija maeneo hayo na walikuwa tayari wameshakaribia eneo hilo. Frank alimkamata mkono Petii kisha wakatoweka hapo kwa njia nyingine.
NAYO INASONGA HIVI
“Tulia bwana, we unafikiri kila wakati mimi ni wa kuvuliwa nguo hovyo, ni kwa kazi maalumu na hata ulivyokuwa ukianzisha mahusiano na mimi nilikuambia kuwa usiwe na wivu wa kijinga kwani nipo kazini na mwili wangu pia ni moja ya silaha” alisema kwa sauti ya juu Dede akiwa ndani ya jingo la BBD, hiyo ikiwa ni baada ya kufika mahali hapo akitoka anakokujua yeye.
“Msipende kubishana kijinga hapa kwanza mnatakiwa mjue kuwa hapa tulipo tupo kazini na muda tuliopewa ni mdogo sana wa kuhakikisha huyo anayejiita jasusi anauwawa. Kuna lipi au kipi kipya katika harakati zenu?” aliongea Bacon akiwa amekunja ndita. Alisogelea meza iliyopo hapo kisha akavuta kiti na kukaa. Wale vijana Benson na Dede wakamgeukia kiongozi wao huku wakiwa wamenuniana.
“Si huyu nae anayeniita mimi malaya, hajui kuwa ni malaya kweli niwapo kazini” alisema akatulia kidogo kisha akaendelea.
“Jana kuna mtu nililala nae lakini nikamtilia shaka mtu huyo. Hebu tazameni hizi picha mbili za awali na hizi mpya kisha muitafute tofauti”
“Picha hii na hii ni tofauti sana hazifanani wewe huoni kwani?” aliongea Bacon.
“Sawa hiyo ni tofauti kwa sababu umeona sura lakini ukumbuke sura ya picha ya kwanza ilikuwa haionekani vizuri. Tazama upande wa nyuma sasa” hapo watu wote wakawa makini kutazama tofauti ya picha hizo kwa nyuma.
“zinafanana, huyu na huyu ni kitu kimoja. Kwaiyo unataka kuniambia umelala na adui kitanda kimoja na kumpa mwili wako hadi asubuhi?” aliuliza Bacon baada ya kugundua kuwa huyo mtu ni mmoja.
“Kazi yangu hainifungi kwenye hilo, nisingefanya hivyo ningejuaje sasa” alijibu Dede.
“Ok, sawa kwa hiyo huyu mtu anapatikana wapi na sisi tutampata vipi?” alihoji tena Bacon.
“Anaonekana ni mtu anayependa sana anasa hivyo sehemu nzuri za kumkamatia ni kwenye nyumba za anasa tu na si vinginevyo” alijibu Dede. Muda wote huo Ben alikuwa ametulia kimya kama si yeye vile.
“Hakikisheni tunakuwa walinzi kwenye kila kona ya baa yoyote hapa mjini na pia kwenye majumba ya kulala wageni na mahoteli. Kila kona huyu Kunguni asakwe nadhani tumeelewana nataka ikifika kesho nisikie habari za maiti yake” alihitimisha Bacon. Ben akaahidi kabla ya kesho huyo bwege atakuwa marehemu. Wivu dhidi ya penzi lake vilikuwa vikimtafuna sana kuliko kitu kingine, kitendo cha Dede kulala na Roi, kilimuumiza sana Benson.
Bugatti Veyron ilikuwa ikiingia taratibu kwenye uzio wa jumba kubwa linalobeba uchafu wa kila chenye ubaya ndani yake. Himaya ya Dr. Lee. Gari hiyo ya kifahari ilitoka Line one, two kisha kuingia kwenye lango la mwisho ambalo lilikuwa imara zaidi. Ndani ya gari hiyo aliteremka kijana mdogo wa kirusi Bencov pamoja na mtu wake wa karibu aliyekuwa akifahamika kwa jina moja tu la Beda. Baada ya wao kushuka kutokea garini, gari hiyo iliondoka hapo na kwenda kupaki mahali pengine kisha wao wakaingia ndani ya jingo hilo kubwa. Walipofika ndani ya jingo hilo, kikao kikaitwa kwa haraka kubwa kuonesha kuwa yeye pekee ndiye aliyekuwa akisubiriwa mahali hapo. Hiyo ilionesha ni jinsi gani uwepo wake ni wa muhimu sana mahali hapo.
“Utekelezaji” Alisema Dr. Lee kwa sauti yake ya kukwaruza. Akameza funda la mate lililoonekana kupita kwa shida kooni mwake kisha akaendelea.
“Nataka kuiangamiza Tanzania lakini wakati mimi naiangamiza Tanzania, wewe Bencov kwa muda huohuo unaiangamiza Ungamo”
“Tanzania!” Bencov na baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wakahamaki. Si Bencov tu kumbe hata watu wengine wengi walikuwa hawajui sababu za Dr. Lee kutafuta dawa ambayo itakuwa angamizo kwa maisha ya watu.
“Ndiyo, Tanzania” akasisitiza zaidi. Swali likaja kutoka kwa Bencov. Kwanini Tanzania. Kimya kikatanda hadi watu wote hapo wakapatwa na mshangao.
“Ni miaka kadhaa imepita sasa, tangu nikumbwe na maisha haya ya kuto kuwa na furaha” akaanza.
“Nilijijenga nikiwa inchini Tanzania ndani ya mkoa wa Morogoro lakini kabla ya hapo nilikuwa kama muwekezaji ndani ya Taifa hilo kipindi cha nyuma lakini ikaja chokoachokoa kuwa nilikuwa nawekeza kinyume cha taratibu” alianza kwa namna hiyo Dr. Lee. Alieleza kila kitu kuhusiana na chuki yake dhidi ya Tanzania. (ukitaka kujua anaeleza nini, simulizi nzima imejaa kwenye mkasa wa SEX MACHINE. Tafuta Riwaya hiyo ujisomee mengi ya kutisha). Akafikia mahali ambapo alitaka kuiangamiza Tanzania na mkoa mzima wa Morogoro. Akakumbuka.
KUMBUKIZI.
“Nifungue mjinga wewe, nifungue nasema au unataka nife na huu mlipuko?” yalikuwa ni malalamiko yake.
” Merina kimbiaa, kimbia Merina, anataka kuuwa huyo mshenzi hilo pigo ni la maangamizi” bado yalikuwa ni malalamiko yake pindi kijana Roi alipolitaja jina la D.A ambaye ndani ya mkasa huu unamfahamu kama Hussein Babu ambalo ndilo jina lake kabisa. Mlipuko mkubwa ukaibuka, moto wa kutisha mno.
“Aaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaghr” kelele hizo zilizotoka kwenye kumbukumbu, zilimfanya Dr. Lee kushtuka kidogo.
“Nilipiga kelele za muda mfupi tu kisha nikapoteza fahamu na sikuwa nikijua kitu chocho kilichokuwa kikiendelea” alimaliza kutoa simulizi hiyo Dr. Lee kisha akatulia tuli huku machozi yakimtoka.
“uliponaje sasa mbele ya moto wa kemikali Dr. Lee?” aliuliza Bencov. Dr. Lee akamgeukia Lady Devil, binti huyo baada ya kutazamwa akajua kuwa alitakiwa kufanya nini. Ikabidi achukue jukumu la kueleza jinsi ambavyo mzee huyo wa kikorea aliweza kuokoka na ule moto wa kemikali.
KUMBUKUMBU INAENDELEA.
“Baada ya mimi kukimbia pale na kupasua vioo ili kulikwepa lile pigo, sikuwa nimeangukia nje ya lile jingo bali niliangukia kwenye chumba cha upande wa pili kisha nikajibana kimya nikisubiri nini kitafanyika. baada ya kama dakika moja, nikawaona wale maadui zetu wakirukia dirishani kwa kuvunja vioo kisha kuangukia nje kabisa ya jingo lile. Mimi nilishajua kuwa mtambo ule ulikuwa umebakisha muda mdogo sana kuweza kulipuka, zilisalia sekunde za kuhesabia tu kwa kweli. Nilirudi kule ndani kwa haraka kubwa sana nikiwa na nyaya mbili ngumu. Nikamfunga miguu yote miwili kisha nikazichomoa zile cheni ambazo zilikuwa zimemfunga kwa juu. Muda ulikuwa umekwisha tayari na kutokana na kipigo kizito cha tumboni alichokuwa amekipata kutoka kwa yule mshenzi Roi, Kim hakuweza kutembea hivyo akaanguka chini mazima na kukita magoti chini, miguu yote miwili ikavunjika kutokana na uzito na muanguko alioangukia ambao ulisababishwa na mning’inio aliokuwa amening’inizwa nao. Mtambo ulifika mwisho wa alarm tayari. Mlipuko mkubwa ukaibuka, maumivu makali yakanitambaa kwenye mkono wangu baada ya kufikiwa na moto lakini niliweza kujivuta na kujirusha kwenye dirisha la upande wa nyuma ambalo halikuwa kubwa na lilikuwa limeanzia kweye sakafu. Kitendo kile cha kujirusha kwa nguvu, kiliweza kumburuza Dr. Lee lakini tayari moto ulikuwa umemharibu maeneo ya kifuani kuja juu. Nikatoka nae na kutokana na urefu kidogo wa lile jingo na kwa vile sisi tulikuwa ghorofa ya pili, Dr. Lee akatanguliza tena miguu ile hapo ndipo ilipovunjikavunjika vibaya sana na si kuvunjika pekee bali ilipasuka kabisa mifupa yake. Nilijua amekufa lakini nilipomkagua vuzuri nikagundua bado anahema. Nikambeba na kumuingiza kwenye Chopa ya tahadhari ambayo ilikuwapo sehemu ya siri na kufanikiwa kumtorosha kuja nae huku Madagascar baada ya kuwasiliana na rafiki yangu ambaye niliwahi kusoma nae chuo kimoja huko china nilipopelekwa kimafunzo na Kim.” akaweka kituo Lady Devil. Macho ya Bencov yakatua kwenye mkono wa Binti huyo kweli kulikuwa na kovu kubwa la moto. Si Bencov pekee bali hata Beda alishtuka na kuona kumbe hapo walipo wapo na binti hatari sana tofauti na wanavyofahamu wao. Kumbukumbu ile ikawafanya wawe radhi kushuhudia Tanzania ikiangamizwa pia lakini hofu ya Bencov ikahamia kwa Roi, kijana ambaye yeye binafsi alimfanananisha kijana huyo na Ruba ama Kupe lakini kumbe alikuwa ni mwiba kweli. Alijipa imani kuwa alikuwa na vijana makini na wanaoweza kuifanya hiyo kazi kwa muda mfupi tu. Kikao kile kikaendelea pale kilipokuwa kimekomea.
“Kesho jopo la madaktari linaelekea ungamo na jingine linaelekea Tanzania. Hili la Tanzania litaongozwa na Dr. Henry mwenyewe huku la Ungamo likiongozwa na madokta wengine. Tumeshafanya mawasiliano na mamlaka husika kuwa tunatokea Uingereza na tuko nyuma ya shirika la chakula na dawa duniani. Hii haitakuwa na shida yoyote kwetu kwani huwa tunapoamua kufanya kazi zetu huwa umakini unakuwa wa kwanza kuliko kitu kingine chochote. Tume hack mawasiliano na mamlaka husika hivyo hata kama wakitaka uthibitisho kutoka kwa shirika hilo, watakutana na sauti za watu wetu ambazo zitawatoa wasiwasi.” akaweka kituo kikubwa kisha akaweka kichwa chake vizuri na kuzunguusha jicho lake moja lenye nguvu huku akiwa bado ana ile maski iliyoziba sura yake sambamba na nguo ndefu iliyokuja hadi maeneo ya kichwani. Akaendelea.
“Madaktari wetu watakuwa kwenye nchi hizo kwa muda wa miezi sita, mitatu ya mwanzo ni mafunzo maalumu ya kutumia mbolea hiyo ambayo wataanza na Diet pills. Hii itafaa zaidi kuwashawishi wajinga hao kisha mitatu ya mwisho, hii ya pili ndiyo itasambazwa kwenye mikoa mbalimbali ya Nchi hiyo. Hakuta kuwa na hofu yoyote kwani hata kama watataka kupima watapima Diet Pills na siyo Diebrainaphine” Makofi yakapigwa baada ya Dr. Lee kutoa maelezo hayo marefu lakini yenye faida kubwa kwao.
“Kwa Tanzania watafikia Arusha na kwa Ungamo watafikiaaaaaa…..
“Pande” akamalizia Bencov baada ya kumuona Dr. Lee anakwama.
“Lakini kuna jambo moja la muhimu na la msingi sana inabidi lifanyike ndipo kesho watu hawa waruhusiwe kusafiri na jambo hilo ni Kafara ya damu” akaweka tuo hapo kisha akawatazama kila mmoja. Wote walikuwa kimya kuonesha kuwa jambo hilo lilikuwa geni kwao. Kati ya hao wote watu watatu tu ndiyo ambao hawakuwa na mashaka na kauli hiyo ya Dr. Lee.
“Kafara ya damu?” akauliza Bencov.
“Ndiyo”
“Ya nini sasa na inahusiana vipi na hili jambo?”
“Maisha yangu Bencov, maisha yangu yanaongozwa na nguvu za ziada na ziko kwenye mamlaka ya viumbe wengine” alijibu kwa msisitizo Dr. Lee.
“Sijakuelewa Dokta unamaanisha nini!” alizidi kuonesha wasiwasi wake kutoka kwenye maneno hayo Bencov.
“Maisha yangu ni nusu nusu, niko na nusu uhai na nusu mfu hivyo ili niishi ni lazima niwasaidie wengine na ili nifanikiwe malengo yangu ni lazima nisaidiwe na wengine. Kuna vimbe au kiumbe wa ajabu anani-contral anafahamika kwa jina la King Bondo. Kiumbe hiki kinatoka kwenye kipande cha dunia kisichoonekana na macho ya mwanadamu wa aina yoyote ile, kiumbe anayeishi kwa kunywa damu” akaeleza. Bado ulikuwa ni mtihani mkubwa sana kwa Bencov na aliwataka watu hao wamueleze sababu za kuweza kuongozwa na nguvu hizo ambazo kwa asilimia kubwa ni za kishetani. Merina akasimama akiwa amelitoa tabasamu kwenye uso wake kwa mara ya kwanza kabisa kisha akabadilika ghafla na kuikunja sura yake kwa kiasi cha kuogopesha, hofu zilikuwa kwa kila mmoja aliopo eneo hilo.
“Hali ya kiafya ya Dr. Lee ilikuwa si ya mtu wa kuendelea kuishi tena japo alikuwa akiendelea kupumua kwa shida. Nisingeweza kumuacha afe wakati bado anapua. Dr. Lee, moto ulimuathiri sana kiasi cha kushindwa kuivuta pumzi yake kwa hali ya kawaida. Alikuwa akipumua kwa kutumia machine ya Oxyge. Alikaa hospitali kwa muda wa mwaka mzima bila mafanikio. Madaktari wa hospitali moja ya binafsi ambayo ilikuwa ikisifika kwa kuwa na wataalamu wengi na wenye uwezo mkubwa, pia walinyanyua mikono wakasema kuwa mgonjwa wangu hawezi kupona tena kwani ameharibika ubongo, yaani ubongo wake ulipatwa na madhara ya moto ule pia alipoteza mawasiliano kwa karibu viungo vyote vya mwili wake. Mishipa yote ilikuwa haiwezi kupitisha damu vizuri na hata misuli ya shingo ililegea na kuifanya shingo yake isiweze kusimama na badala yake ilale kama mnavyoiona hivi sasa” alieleza yote hayo Merina akiwa amekunja sura yake kabisa.
“Binti, mgonjwa wako hawezi kupona tena, hadi hapa tumeshindwa kumtibu na leo ndiyo siku ya mwisho kuweza kumuweka hapa kwenye hospitali yetu. Tunaitoa mashine ya kumsaidia kupumua kwani kila siku hali yake inazidi kuwa mbaya” nayakumbuka maneno haya, alinimbia dokta mfawidhi wa hospitali hiyo. Kiukweli sikuvumilia nilikamatwa na hasira mbaya sana. Nikamvunja shingo yule daktari kisha nikaondoka na Lee huku nikiwa nimekata tamaa kabisa ya kupona kwake. Kwanini madaktari bingwa wa magonjwa ya binadamu kama wale wenye sifa kubwa, washindwe kumtibia? Watakuwa wanenifanyia kusudi tu lakini si kushindwa, wanashindwaje sasa? Nilikuwa nikiwaza tu mambo mengi huku nikiwa sielewi kabisa cha kufanya lakini sikuwa radhi kuona anakufa mikononi mwangu.
Nilimpakiza kwenye gari kisha nikaongoza naye hadi kwenye msitu mkubwa huko nilikuwa na lengo la kwenda kumzika ama kumuacha huko msituni” akakomea hapo Merina kuhadithia kilichosababisha hadi Dr. Lee akakutana na kiumbe cha ajabu sana. Sasa akaingia kwenye kumbukumbu nyingine.
KUMBUKUMBU INAENDELEA.
Merina alikuwa amechanganyikiwa sana hata uendeshaji wake wa gari ulikuwa wa kuto kujielewa. Alikuwa amemzoea sana Dr. Lee kwani alimfunza mambo mengi sana, hata kama alikuwa akimtumia kwa kumuingilia kinyume na maumbile lakini kitendo cha kumtoa ndani ya lile jingo na kuanza kumpa mafunzo ya kujilinda mwenyewe (self difens). Aliona ni uthamini mkubwa sana kwa mzee huyo. Akasahau udhalili aliokuwa akifanyiwa akamchukulia Dr. Lee kama mzazi wake kwani alikuwa hana mzazi hata mmoja kwenye maisha yake. Aliendesha gari kwa hasira kubwa hadi akachoka na kujikuta akiacha kuendesha hiyo gari. Aligeuka nyuma alikokuwa amemlaza Lee akamuangalia jinsi alivyokuwa amelala kwa kukatisha tamaa. Akaupiga usukani kwa nguvu hadi akajikuta anapiga honi. Alikuwa tayari yupo katikati ya msitu mkubwa. Njia aliyokuwa akiitumia hadi kufikia hapo ni zile ambazo walikuwa wakitumia watalii kwenda kwenye misitu hiyo. Giza lilikuwa nene sana ndani ya msitu ule. Kitendo kile cha kupiga honi maeneo yale, hali ikabadilika, msitu ule ukaanza kutikisika kwa upepo mkubwa. Upepo ule ukaanza kumtisha Merina hadi akapandisha vioo vya gari yake. Akawa anashuhudia miti ilivyokuwa ikiyumba kwa nguvu kubwa, woga ukamkamata. Wakati akiwa anatetemeka na kuzidi kushangaa, vioo vyote vya gari yake vikapasuka kwa kishindo kikubwa tena kwa pamoja. Merina alipiga kelele kali mara ghafla upepo ule ukatulia. Hali ikawa shwari kabisa, hapo ndipo Merina alipoanza kuhangaika kuwasha gari ili aondoke eneo hilo, gari haikuwaka iligoma kabisa kuwaka. Kila alivyojitahidi kugusa hapa na pale patupu. Alikuja kushtuka sauti za kuvunjika kwa vijiti vikavu na harufu kali yenye kuumiza pua zake ambazo hakuwahi kuzihisi kabla, alivyogeuka, alimuona kiumbe wa ajabu asiye na umbo linaloeleweka kwa mtazamo kiumbe hicho kilitisha sana na kilikuwa kikivuja damu mwili mzima. Kile kiumbe ambacho kilikuwa na pembe moja kubwa kichwani, hakikuongea neno lolote bali kilivunja mlango wa gari na kutoweka na Dr. Lee. Sifa ya kiumbe huyo tokea kumuona kwangu hakuwahi kuongea bali nilikuja kujua kuwa anaongea kwa njia tofauti nayo ni njia ya ndoto. Hapo hapo nilipokuwa nimejikunyata, nilipitiwa na usingizi. Hapo ndipo nikaanza kuongea na yule kiumbe ndotoni ndipo akaniambia kuwa ile ni karata tunacheza kwani hadi pale ilipofikia mgonjwa wangu alikuwa amebakisha muda mfupi tu kufariki dunia. Akaniambia damu mbichi ndiyo maisha yake na anahitaji damu kwa wingi ili aweze kuishi muda mrefu bila kuhitaji damu tena na aweze kuwa na nguvu ya kurudi kwenye maisha ya dunia aliyotoka. Makubaliano ya kucheza karara hiyo yakapita lakini hata alivyomrudisha Dr. Lee, alikuwa katika hali hiyo ya kukaa kwenye baiskeli maisha yake yote hadi pale atakapofanikisha kupatikana kwa damu hiyo nyingi ndipo anarudishwa katika maisha yake ya zamani lakini ikishindikana inamaana anakufa kabisa na ataacha balaa kubwa nyuma” alimaliza kusimulia Merina au Lady Devil kisha akasema.
“Ni nani kati yenu angeikataa ofa hiyo ya kuishi tena ukiwa umekata matumaini ya kuishi?” Jibu likatoka kuwa hakuna atakaye kubali kuikosa.
“Sasa kwa majibu hayo kafara ni lazima na itafanyika leo usiku” akasisitiza kisha makubaliano yakapita kuwa kafara hiyo itafanyika japo kafara yenyewe haijajulikana kupatikana kwake. Bencov alitulia kwa muda kidogo kisha akasema,
“Damu hiyo nyingi ya kuweza kukifanya hicho kiumbe kipate nguvu mpya ya kurudi kilipotoka bila kuleta madhara itatoka wapi?” Merina alimgeukia kijana huyo mdogo lakini mwenye mamlaka na pesa nyingi kisha akamjibu.
“dawa hii iliyotengenezwa ndiyo itakayo leta ushindi kwetu sote” baada ya jibu hilo wote wakatikisa vichwa kuashiria kuwa wamekubaliana.
USIKU WA KAFARA.
Giza lilikuwa limetanda kila kona ya jumba hilo hakukuwa na taa hata moja ambayo ilikuwa ikiwaka mahali hapo. Giza hilo lilikuwa ni kero kubwa kwa watu wengine ambao hawakujua nini maana hasa ya giza hilo lakini kwa watu wengine hilo wala halikuwaathiri hata kidogo. Taa zote za jumba hilo zilizimwa. Kila mtu wa jumba lile alikuwa katika mavazi ya ajabu na hakujulikana yupi ni yupi na nani ni nani, walikuwa wamevaa nguo ndefu zenye kofia zilizofunika vichwa vyao huku sura zao wakiwa wamezielekezea chini kiasi cha kufanya iwe ngumu kidogo kuwafahamu. Kimya kilikuwa kimetanda, hakuna wa kuongea kilichosikika hapo ni hatua zao ambazo walikuwa wakizipiga kwa kuburuza miguu. Safari hiyo waliyokuwa wakiitembea, ambayo ilikuwa ikiongozwa na mwanga hafifu wa muenge wa moto ulioshikwa na mtu mmoja aliyopo mbele ya msafara huo, uliishia kwenye chumba kimoja kikubwa na cha ajabu sana. Chumba hicho kilikuwa cheusi kilicho na giza la kutisha sana. Watu wale walijipanga mstari na kutengeneza umbo la herufu ‘V’. Kiongozi alikuwa amekaa katikati ya ile ‘V’ akiwa kwenye baiskeli yake. Hakuwa mwingine bali ni Dr. Lee. Alianza kuongea maneno ya ajabu kwa sauti ya chini sana lakini kila alivyokuwa akizidi kuongea ndivyo sauti yake ilivyokuwa inazidi kuongezeka hadi kufikia kwenye ile hali yake ya kawaida. Yalikuwa ni maneno ambayo hakuna mtu mwenye kuweza kuyaelewa hata mara moja. Watu wawili tu ndiyo walikuwa wakijua hicho kilichokuwa kikizungumzwa mahali hapo. Maneno yalizidi kwa takribani masaa mawili kisha kimya kikakita tena. Kilikuwa ni kimya kizito sana. Baada ya kimya hicho, mlango wa hicho chumba ukafunguliwa, vijana wawili wakaingia ambao walikuwa wamefunika sura zao huku wakiwa wameongozana na vijana wengine wawili hawa walikuwa wamefunikwa sura zao kwa nguo ngumu na nyeusi ambazo ziliwafanya wasijue kabisa mahali walipokuwa wakipelekwa. Walipofikishwa ndani ya chumba hicho kikubwa, Merina akanyanyua shingo yake na kumtazama mkuu wake.
“wakague wote kama wako sawa?” ilitoka kauli hiyo kwa sauti ya chini sana. Merina akawatoa nguo wale watu waliokuwa wamefunikwa usoni kisha akaagiza na wengine waletwe mahali hapo. Walipoletwa hali ilikuwa ni hiyo hiyo ya kukaguliwa kwa kutumia ule mwanga hafifu wa muenge wa moto kisha maneno ya ajabu yakaanza upya huku Lonto akitoka mbele mahali ambapo wale vijana wapo. Akatoa amri wafungwe kamba imara kabisa, amri ikatekelezwa. Akakamata Jisu kubwa na kulipitisha shingoni mwa kijana mmoja kisha akamsukuma yule kijana hadi akaangukia kwenye mtaro mmoja uliokuwapo mahali hapo kisha akakanyagiwa na miguu yenye nguvu nyingi, damu ikawa inachuruzikia kwenye ule mtaro. Hali iliyomtokea yule kijana, ikamkuta kila aliyekusudiwa hadi wote wane walipokwisha. Dr. Lee akapiga kimya kingine kizito kisha akatulia kama si yeye aliyekuwa akiongea kwa sauti yake kubwa na mbaya. Hali ya hewa mule ndani ikaanza kubadilika, harufu mbaya ya kuziba pua ikaaza kuhisiwa na kila mmoja aliyopo maeneo hayo lakini amri waliyopewa ni kwamba hawakutakiwa kufanya jambo lolote lile zaidi ya kutulia tuli. Harufu ikazidi kuwa kali sana kiasi kwamba kama ungelikuwa na moyo mwepesi ungeweza kutapika. Harufu ile ilizidi kuzisumbua pua za kila mja aliyekuwepo mahala pale kisha muenge ule uliokuwa ukiwaka ukazima pasipo mtu yoyote kujua ni nani wa kuuzima ule muenge wa moto.
Wakati Muenge ule ukiwa unazima, kwenye chumba cha ndani alichokuwa amelala Tereza hali ilikuwa tofauti kabisa. Tereza alianza kuhangaika pale kitandani kisha akatulia kimya baada ya kuhangaika kwa muda wa dakika kama tatu. Nafsi yake ikaamka taratibu kisha ikatoka kabisa kwenye mwili ule usioelewa kitu na kutoka kabisa ndani ya chumba kile na kuvamia chumba kilichokuwa kikifanyika kafara. Tereza alishuhudia kila kitu kilichokuwa kikiendelea na alishuhudia hadi vile ambavyo watu waliokuwepo pale walikuwa hawavioni. Tabasamu pana likakivaa kinywa chake ilihali kilichokuwa kikifanyika mahali hapo si kitu cha kumfanya mtu atabasamu. Alishuhudia mambo ya ajabu yaliyokuwa yakifanywa na kile kiumbe chenye harufu mbaya ambacho kilikuwa kikitisha mno. Kiumbe kilichokuwa kikitembea kingali kinaoza mwili, Kiumbe kilicho na roho ya ajabu sana. Hata taa ilipokuja kuwaka tayari Tereza nafsi alisharudi kwenye mwili wake. Kiumbe kile kikatoka mule chumbani kikiamini hakikuonekana na binadamu wa aina yoyote ile lakini bila kujua kuwa kuna binadamu wa ajabu na mwenye nguvu nyingi kuliko hata yeye alishamuona. Kiumbe kile kilipopotea kule kwenye chumba cha kafara, kilikuja kutokea kwenye chumba cha Tereza. Kumbuka kuwa hii ni mara ya pili kiumbe huyu anakuja kwenye maisha ya Tereza, mara ya kwanza ilikuwa ni kipindi Tereza ni mgonjwa akiwa hajitambui kitandani na mara ya pili ni hiyo. Ajabu ni kwamba kiumbe hicho hakikukuta mtu kitandani bali kilikuta kitanda kikiwa kitupu kabisa tena kikiwa kimetandikwa vizuri kabisa kuonesha kuwa hakikuwa kikitumiwa na mtu. Kuna kitu alikihisi mule ndani nayo ni harufu ya kiumbe kisichoeleweka. Kiumbe nyama kilicho na harufu ya kushangaza, kiumbe hicho ndicho kilichokuwa kikimkosesha amani kabisa katika akili yake. Alitafuta kwa hisia kali lakini bado hali ilikuwa ileile. Kitanda kilikuwa kitupu na kilikuwa kitupu kweli.
Swali la kujiuliza ni kwamba Tereza alikwenda wapi? Ikiwa muda mfupi tu uliopita, mwili wake uliachwa huku nafsi yake ikitoka. Nafsi yake iliporudi kwa mara ya pili ilikwenda wapi na mwili ule uko wapi. Akili ya kile kiumbe bado haikumpa. Kila muda alikuwa akibadilika na kutisha zaidi. Mwili wake ulianza kutoa damu nyeusi damu ambayo kama utafanikiwa kuiona, ungeweza kuhisi ni sharubati ya zabibu iliyokamuliwa. Pembe yake ya juu ilianza kupotea kwa kudidimia kichwani huku damu ikizidi kumwagika kwa wingi na kuchafua sakafu ile ya pale chumbani. Pembe ile ilipopotea kabisa, macho ya kile kiumbe yakaanza kuwaka na kuleta moto wa ajabu. Sasa alianza kuitafuta harufu aliyokuwa akiihisi kwa nguvu za ajabu lakini wapi. Harufu hiyo haikuonekana.
Kiumbe kile kilipandisha hasira kali sana kikalia kwa mlio wa kutisha hakikujali kama kilikuwa ndani ya kile chumba kisha kikatoweka ghafka na kupotea mule ndani ukabaki mwangwi wa sauti yake ya kutisha. Wakati kiumbe kile kikipiga kelele, mlinzi wa karibu wa Bencov alikuwa akipita karibu na chumba hicho cha Tereza akiwa anaelekea kwenye chumba chake kwa ajili ya kwenda kujipumzisha baada ya kafara kwisha. Aliisikia sauti hiyo ambayo ilipasua ngoma zake za masikio kutokana na ukali wake. Hali ile ikaleta hofu kubwa sana kwenye moyo wake. Haikuwa ni sauti ya kiumbe cha kawaida hiyo na hakuwahi kuisikia kwenye maisha yake yote. Akajiuliza ni sauti ya kiumbe gani iliyokuwa ikitokea humo ndani. Pamoja na kujiuliza kwake lakini pia alipata msukumo wa kuingia ndani ya kile chumba. Akafungua mlango akazama ndani kwa uangalifu wa hali ya juu sana. Alipata mshtuko mkubwa sana baada ya kutupa macho yake ndani ya kile chumba. Maji ya rangi nyeusi yalikuwa yakisambaa chini huku harufu mbaya kama ile iliyojitokeza kule kwenye chumba cha kafara akiihisi mule ndani. Alipopiga macho kwenye kitanda anacholala Tereza kilikuwa kitupu.
“Mungu wangu!” akatamka maneno hayo huku akifumba macho na kugeuzia shingo ukutani. Hali ile ilimpa woga wa ajabu sana kwani tayari maisha ya himaya hiyo yalishaanza kumtisha. Akawa anairudisha shingo yake taratibu mno hapo ndipo alipojikuta akitoka mbio sana ndani ya kile chunba na kukimbilia chumbani kwake kisha kujifungia. Alishuhudia sakafu ikiwa kavu haina chochote lakini mbaya zaidi kitanda kilikuwa na mtu tena aliyelala kihasarahasara kabisa huku akionekana kutopea kwenye usingizi mzito.
“Mungu wangu nini kile ambacho nimekiona pale, inamaana Tereza ndiyo kiumbe cha ajabu kilichokuwa kikizungumziwa pale ama?” alijiuliza huyo kijana kisha akajikuta akikosa majibu sahihi ya kuweza kujibu mahali hapo. Akajilaza kitandani lakini mwili ulikuwa ukitetemeka sana, Pamoja na hayo, moyoni akajiapiza kuwa hataruhusu kinywa chake kuachama kumwambia mtu kile alichokiona pale. Alitishwa na imani za kishetani. Hofu yaanza kutanda sasa, kazi nzito.
Usiku huohuo kama masaa mane yaliyopita, Petii na Frank walifika kwenye maficho ya kijana huyo aliyekuwa amejiweka mithili ya kichaa. Akamuleza kuwa hapo ndipo anapoishi na anaishi hapo kwa sababu maalumu. Kwa ufupi ni kwamba kijana huyo alieleza kila kitu kilichopita katika maisha yake mwanzo hadi pale huku akificha baadhi ya mambo kama mahali alipojifunzia mapigano na kadhalika. Wakati yeye akiwa anahadithia hivyo, kitu ambacho hakukijua ni kuhusu kurekodiwa, Petii alikuwa akimrekodi kijana huyo mwanzo mwisho kwa kutumia simu yake yenye uwezo mkubwa. Waliongea mambo mengi kisha wakaagana na kupanga mahali pa kukutana kwa siku inayofuata. Kwa muda huo ilikuwa tayari yapata saa mbili au tatu usiku. Petii alivyotoka kule mafichoni kwa Frank kichaa, moja kwa moja ilikuwa ni hotelini lakini wakati anafika tu kwenye maegesho ya magari ya hoteli waliyokuwa wamefikia, simu yake ikaita, akaipokea na kuiweka sikioni baada ya kujua mtu aliyempigia.
“rudi nyuma kisha ingia kwenye gari nyekundu” aliyepiga simu alitoa maelekezo hayo. Petii hakubisha wala kutetereka, alifanya kama alivyoelekezwa. Alipoingia tu kwenye gari hiyo nyekundu gari ikawashwa na kuondolewa maegeshoni hapo kwa mwendo wa kawaida sana.
“Wapi tunaelekea sasa Roi?” akauliza Petii.
“Hakuna hoteli iliyo na usalama hata moja kwa sasa Petii, kila hoteli imewekwa kunguni wa kuweza kunusa damu za watu maalumu”
“Kwahiyo wapi tunakwenda?” akahoji tena Petii.
“Kazi nd’o imeanza sasa, timu yangu imeingia na imenielekeza mahali salama ambapo naweza kuishi kwa muda mfupi wa kumaliza hili”
“Timu yako? Kwahiyo naweza kuiona na mimi?”
“Sahau Petii, umeniona mimi na huwezi kuiona timu yangu hadi unaondoka ndani ya udongo huu wa Ungamo?” alijibu Roi kisha akakaa kimya kwa muda mfupi akasema.
“Kuanzia sasa sitajali wewe ni mpelelezi au jasusi, sitaki kukuona unakuwa mbele zaidi yangu tena bali utafuata kile nitakachokuelekeza mimi”
“Whaaat! sasa ndyo…..!” alihamaki Petii.
“Kwa kawaida huwa sipendi kubishiwa ninapoongea kaa kimya, hii vita siyo ya maneno wala risasi za chuma, utapotea ukijifanya mbishi…narudia tena, Utafuata nitakacho mimi” akahitimisha Roi kisha akakanyaga mafuta na kubadilisha gia na kufanya kasi ya gari kuwa maradufu. Msafara ulikuwa mrefu kidogo, gari yao iliingia kwenye nyumba moja iliyokuwa imejificha sana lakini ilikuwa ni nyumba ya maana sana yenye kila kitu ndani. Walipoingia tu ndani ya nyumba hiyo, Roi akazama chumbani kisha kujifungia. Petii akabaki akishangaa akajua sasa kazi kweli imeanza maana kijana huyo alikuwa si yule aliyemzoea. Roi alipofika chumbani alikuta kifaa kidogo kilichopo kitandani akakichukua na kubonyeza kinobu cha kijani, sauti ikaanza kusikika. ‘fungua kabati mlango wa kushoto kutoka hapo uliposimama, utaona mlango mwingine ambao ni vigumu kujua kama kuna mlango ukitazama. Gusa kwenye kona ya kulia kwa juu kwenye usawa huo wa mlango wa kabati kisha mlango huo utazama ardhini, hapo utakuwa kwenye chumba kingine ambacho ukikikanyaga tu kitakupeleka kwenye chumba kilichopo chini ya ardhi huko utakutana na kila zana unayoipenda pamoja na mambo mengine ya Tahadhari ambayo utatakiwa kutembea navyo ili pindi utakapobanwa basi utujulishe. Toka ndani ya hicho chumba kwa kugusa kinobu kilichopo nyuma ya ukuta wa nguo za kujikinga na risasi za kila aina. Hapo utakuwa juu baada ya muda mfupi tu kisha utatoka nje kabisa. Nyuma ya nyumba utakuta gari kali na yenye kila kitu pia kwa ajili yako. Ni mahususi kwa ajili yako, ndugu yako Zomba amekutunukia. Kazi kwako nami niko ndani ya mji huu na nipo kila baada ya hatua mia moja ulizoniacha. Kuwa makini tafadhali na hakikisha husahau elekezo hata moja kwani baada ya kumaliza kuisikia sauti hii, nitakutaka ubonyeze kinobu chekundu, naomba ufanye hivyo tafanyali’ sauti hiyo ikakata kisha kile kinobu kilichokuwa kinawaka taa ya kijani sasa kikabadilika na kuwaka nyekundu. Roi akabonyeza na kukiweka chini. Kikawaka moto. Akafanya kama alivyotakiwa kufanya. Akafungua Kabati na kugusa mahali alipoelekezwa, akatokea mahali kwenye chumba kidogo na chenye vioo hapo alishangaa tu akipelekwa chini ya ardhi. Alipofika huko chini, nusura achanganyikiwe kwa furaha, alikutana na zana za kila namna hadi zile ambazo alizitumia kwenye mkasa uliopita. Alitabasamu na kufurahi kupita kiasi kisha akazikaribia nguo ambazo zilikuwa hapo mbele kwenye enga maalumu. Nyingi zilikuwa ni full suti ambazo zilikuwa ni za gharama kubwa kwa mtazamo wake lakini zilikuwa ni maalumu kwa kazi ya kuzuia risasi tu. Hakutaka kupoteza muda mahali hapo kwani alikuwa amemuacha Petii katika sintofahamu kubwa. Alitoka kwa njia ile aliyoelekezwa kisha kutoka sebuleni. Akamkuta Petii akiwa amejikalisha kwenye kochi moja wapo sebuleni hapo.
“niambie nini kimejiri katika mizunguuko yako maana nataka kutoka sasa hivi” alisema Roi huku akikaa karibu kabisa na binti huyo.
“Unataka kutoka usiku huu na siyo kupumzika?” aliuliza Petii.
“Nilikuwambia kuwa sasa kazi nd’o iko rasmi” alijibu. Petii muda huo huo akajipekua kwenye kijibegi chake akatoa simu ambayo ilikuwa na ile rekodi aliyomrekodi Frank, akaenda sehemu husika kisha akaiweka mezani. Maongezi yote yakasikika hadi mwisho.
“Huyo kijana nitahitaji kuonana nae kesho ninaimani atatusaidia kwenye hili na tutapiga hatua” alisema Roi huku akiwa anavaa fulana nyingine ya rangi nyeupe kisha akapiga na kapelo huku chini akipiga raba safi nyeupe.
“sitachelewa kurudi mpenzi isitoshe nimekumbuka utamu wako sana” alisema Roi akachukua bastola ndogo kutoka kwenye zana mpya za kazi pamoja na vitu muhimu vya siri alivyotakiwa kutoka navyo pamoja na visu kadhaa, akampiga busu huyo binti na kutoweka.
Insp. Bogo alikuwa akizichambua habari alizopewa na IGP wakati wa giza lililopita alipokuwa amekwenda kumuuliza juu ya mtu ambaye naye anasababisha mauwaji tena akiwa anaweka kadi yenye bendera ya Tanzania. Alitaka kujua juu ya huyo mtu ambaye hata kwenye mwili wa Don Philipo ambao aliusababishia kifo yeye uliwekwa hiyo kadi. Majibu aliyopewa ndiyo yaliyokuwa yakimchanganya sana usiku huo upatao kama saaa nne hivi na ushee.
“Harakati za mtu huingiliwa na mtu pia, kama hana madhara kwako na anafanya kile unachokifanya wewe hata kama ni kwa sababu zake ambazo ni tofauti na zako basi huyo hana madhara. Fanya kwa kuicheza nafasi yako, acha na yeye aicheze nafasi yake. Inaweza kuwa wote ni wamoja na mtakuja kukutana” majibu haya yalikuwa tata sana lakini kwenye kichwa chake akajipa imani kuwa labda pengine IGP ameamua kumuweka mtu mwingine baada ya kuhisi cheni hiyo ni ndefu. Alipoikumbuka kadi yenye bendera kutoka Taifa jingine, akajikosoa na kuondoa kabisa mawazo yake. Akapiga moyo konde huku akijisemea kuwa hakuna marefu yasiyo na ncha.
Usiku huo ulikuwa ni usiku wenye mambo sana kwani pia Bogo alikuwa akitafakari uvamizi wa mahabusu ya gereza kuu la Pande iliyokuwa imevamiwa na kisha mtuhumiwa mwenye makosa makubwa ya mauwaji kutoroshwa. Nani kafanya hivi? alijiuliza Bogo swali ambalo si chini ya mara sita, alishajiuliza na bado jibu lilimkwepa. Swali hilo ndilo pekee lililomfanya afunge safari hadi kwenye magereza hayo punde tu alipozipata taarifa za mauwaji hayo ya askari waliokuwa lindo kisha mtuhumiwa kutoroshwa. Alipofika huko aliambiwa kuwa kuna askari mmoja tu ambaye ndiye aliyefanikiwa kutoroka baada ya kuzidiwa nguvu na huyo ndiye aliyeshuhudia kila kitu lakini hali yake si shwari, kwani alijeruhiwa vibaya kwa risasi na amelazwa kwenye hospitali ya rufani ya Muavengero. Inasemekana kuwa huyo ndiye aliyemuona mtu aliyekuja mchana kumtazama mtuhumiwa na haikujulika aliruhusiwa vipi wakati haikutakiwa mtuhumiwa huyo kuonana au kutembelewa na mtu wa aina yoyote ile. Habari hizo zikampa hofu na mashaka.
Kama askari huyo aliyepona anaijua sura ya mtu aliyekuja mchana au hata jina basi huyo ni muhimu zaidi. Aliwaza namna hiyo. Alipofika hapo aliifikiria hali aliyomkuta nayo huyo shuhuda, akapoa kidogo. Hali yake haikuwa mbaya sana lakini alipigwa risasi ya mbavu ambayo ilimpotezea damu nyingi kabla ya kukutwa na msaada.
SONFA NAYO
Kwa matibabu aliyopewa, madaktari wakamwambia kuwa ifikapo siku inayofuata anaweza kupata mawili matatu kutoka kwa mgonjwa huyo. Akatabasamu, pia akakumbuka staili aliyoitumia kwenda nayo hospitali na kwenye tukio, akacheka kabisa huku akijiona ni mtu mbaya sana lakini hakujua. Nasema hakujua kwa sababu hakujua kuwa muda huo wakati yeye anawaza, kuna watu walikuwa wanapanga mipango ya kuharibu na kumuingiza huyo wanayemuita mtuhumiwa kazini.
“Sijakataa kushirikiana nanyi na pia siko kinyume nanyi ila jambo moja tu la msingi ni kwamba, kazi yangu huwa haiingiliwi na mtu na hilo naomba sana mlifahamu kinyume na hapo sitaangalia kama mmefanya jambo la muhimu sana kunitoa mahabusu” alikuwa akiongea kwa tambo kubwa na kiburi kilichochumpa mipaka Don Dou. Rais wa zamani Mh. Julio alikuwa akimsikiliza huyo mtu kwa umakini mkubwa sana mahali hapo. Kimya chake kilikuwa na mafikirio makubwa mawili kichwani mwake. Kwanza ilikuwa ni kukubaliana na matakwa ya huyo mbabe, pili ni kuja kumgeuka baada ya kukamilika kwa misheni hiyo nzima. Watu tuko kwenye mipangilio yetu ya kimaisha na tunahitaji kutawala hii nchi vile tutakavyo, huyu wacha atambe tu na kujiona mjanja lakini atajuta kunifahamu. Aliwaza Julio kisha akasema.
“Kila kitu kiko kwenye maamuzi yako Dou na wewe ndiye mwenye kujua nini ufanye na…..!” kabla haja malizia kauli yake, mule ndani ya chumba cha mikutano kama ile ya siri, kukaingia mtu.
“Taarifa zilizopo ni kweli mkuu, kuna askari alipona kwenye lile tukio la kumtorosha Dou na yuko hospitali kwa sasa. Kwa hali yake kesho anaweza kutapika kila alichokila maana alimuona Jarome mchana wa leo” alitoa taarifa huyo mtu. Macho yakawatoka watu wote walipo hapo.
“Inamaana kuna wapelelezi wa kimya kimya wapo ndani ya nchi hii?” akauliza wajumbe wake Rais Julio huku akisahau kuwa hata kama hakuna wapelelezi wa siri waliowekwa na serikali lakini yupo anaezitafuna roho za wenzao na kuwaachia kadi. Kitema na wengine wakabaki kimya lakini Yule mtu akajibu.
“Hilo nalipa uhakika mkuu kwani Kuna mtu anaonekana si mgeni, kuna taarifa alizifuata kwa dokta mfawidhi wa ile hospitali na kuangalia hali ya mgonjwa. Nasi tukataka kujua mgonjwa anavyoendelea na jinsi unafuu wake utakavyo kuwa, tukaambiwa kuwa kesho anaweza kumtambua anayeingia na anayetoka na si hivyo tu bali anaweza kuongea pia” majibu yale yakazidi kumshtua rais Julio akatoa macho kwa hasira kali kisha akasema.
“Mabandu anakwenda kinyume na amri zetu, kwanini aweke mpelelezi na sisi tulimuonya?” akaweka alama ya kuuliza ambayo hakuna aliyetilia maanani miongoni mwa walio pale. Baada ya kuona kimya kile akamgeukia kila mjumbe kisha akatoa agizo.
“Jarome, hakikisha vijana wanamleta yule binti hapa hata Kitema tuma vijana wakamwambie mke wa Rais kuwa ahakikishe kuwa Rais anamtoa mpelelezi alioko kazini haraka sana kabla binti yake hatuja mkata kichwa” hiyo ilikuwa ni mri kali ambayo hakuna aliyetakiwa kupinga mahali hapo isipokuwa ni matekelezo na majibu mazuri yamfikie kwa muda maalumu. Alisahau ulinzi mkali wa chuo anachosoma binti huyo wa Rais. Wakati vijana wale wakiwa wanaamka, big na kimbaumbau, Don Dou naye akaamka.
“Vipi?” akauliza Mh. Julio.
“Sitaki njia ninayopita mimi iwe na miiba, nakwenda kuuwa huyo kirusi huko hospitali usiku huu. Kikao kile kilifungwa kwa kila mjumbe kuondoka kwa muda wake, Rais alibaki mwisho kabisa kisha akajilaza kitini kwake akiwa mwingi wa tafakari nzito. Tafakari za kuwa kiongozi mkubwa sana siku moja, kiongozi atakayeishi madarakani kwa muda autakao yeye bila kutolewa na mtu yoyote. Rais Julio Mobande Julio, alikuwa ni Nyoka mbaya mwenye sumu kali mno, sumu ya kuuwa bila anayeuwawa kujua kama anauwawa. Huyu ndiye aliyepanda chuki mbaya kwa waziri mkuu Backa, waziri aliyekuwa ni mtenda kazi na mwenye kujitoa kwa hali na mali. Julio alijipendekeza kwa wageni wa kirusi huku akiwaangamiza warusi hao na kutega mtego mbaya sana kwa Backa hadi kuonekana kuwa yeye ndiye muuwaji wa warusi wale, kumbe yeye ndiye aliyeyafanya yote yale. Alikaa hapo na kukumbuka siku aliyowatuma vijana ambao walikuwa wamevaa mavazi ya kiraia huku wakiwa wamejificha sura zao. Aliwaambia kuwa wasiuwe mtu wa aina yeyote ile zaidi ya warusi tu. Siku ambayo Backa alikuwa akitoka kuwatia mbaroni warusi wale baada ya kuagizwa yeye akiwa kama waziri mkuu huku akipewa dhamana na waziri wa ulinzi na kiongozi wake mkuu wa kazi kuwa watu wale ni lazima wawekwe chini ya ulinzi na wajibu tuhuma juu ya kuwekeza nchini pasipo kufuata taratibu stahiki za kiuwekezaji. Hakujua Backa kama alikuwa akiingizwa kwenye mtego wa kumtia matatizoni baadaye. Warusi wale wakauwawa wote huku Backa akishangaa kundi la vijana wa kiaskari wakipambana kwa weledi lakini hakuna adui aliyepata madhara wala askari aliyejeruhiwa.
“Ha ha ha ha! Aha ha ha haaa! Backa, wema wako na kujifanya ni mwenye utajiri na mpenda kutoa misaada kwa raia. Ulikuwa ukifanya yale ili ujekuwa Rais baadae mimi najua. Ulitaka kuja kukikalia kiti cha uraisi baada ya huyu mpuuzi Mabandu kutoka madarakani. Na kwa jinsi wananchi walivyokuwa na imani na wewe ni wazi wangekuchagua lakini hukujua kuwa hakuna mtu yoyote anayejifanya kujua akapita anga zangu bila kupata matatizo. Kumbuka kuwa mimi ndiye niliyeharibu maisha ya yule mtoto Frank, kwa kujifanya anaakili sana. Watu kama wale ni mwiba sana na kwakuwa yule kijana alinipa kidonda cha maisha kwa kuniulia binti yangu kwa kujifanya kichaa, nitamu…..wa” alipaliwa na mate baada ya kuwa akijisemea kwa muda mrefu baada ya kumaliza kuwaza. Akakohoa sana kwa ufirauni wake hadi akayatafuta maji yalipo.
Gari nyekundu ilipaki kwenye ukumbi mkubwa wa starehe huu ukijulikana kwa jina la NO STRESS CLUB. Club kubwa ambayo nayo ilikuwa ni tishio kwa namna yake japo si kama ile ya awali ambayo ndiyo vijana wengi waipendayo. Siku kama hiyo ya mapumziko ya wiki, vijana wengi wa kileo walipenda kujiachia hapo kwa kucheza muziki na kunywa pombe vile watakavyo huku wakifurahishwa zaidi na huduma zingine za anasa. Roi alitaka kuianza kazi yake usiku huo ndani ya Cub hiyo pendwa kwa siku kama hiyo. Siku hii ndiyo siku ambayo Benson alitoka pamoja na Dede kuhakikisha kijana Roi hatoki na walikuja kwenye jumba hilo la starehe baada ya kujua kuwa Roi ni mtu anayehusudu sana mambo hayo na anapenda kumbi kubwa kubwa na maarufu kama hizo. Watu walikuwa wengi mno siku hiyo, usipokuwa makini unaweza hata kuserebuka juu ya miguu ya watu kwa jinsi umati wa watu ulivyoshikamana.
“Unanikanyaga boya wewe huoni nini?” alisema kijana mmoja aliyekuwa akicheza na binti mmoja mrembo sana mwenye umbo gomvi kwa vijana au kijana kama Roi. Jicho lake lilikuwa limeganda kwenye bogi la mwanamke huyo hadi kujikuta akimpamia mtu aliyekuwa akicheza na huyo mrembo.
“samahani bro” akaomba radhi Roi kwa sauti ambayo kijana aliisikia.
“Acha usng kuwa makini bwana, we km nini” alitukana huyo kijana Roi akajua huyo kijana ni mkorofi na hajui kuwa hapo anacheza na mtu wa aina gani. Alichokifanya ni kmvutia yule mrembo kwake na kumlaza kifuani huku akiwa amemgeukia yule jamaa lakini nyuma ya yule jamaa akakutanisha macho yake na Dede. Roi akatabasamu, Dede akakunja sura kwa wivu wa mambo matamu kutoka kwa Roi. Aliona kama yule mwanamke mwenzie anakwenda kufaidi. Akasahau kazi na laiti angelikuwa pekee hapo, angeharibu kazi iliyofikisha mahali hapo lakini huku mbele, yule jamaa akarusha konde ambalo halikuwa na maana yoyote kwani liliishia kwenye mkono wenye nguvu wa Roi kisha akanyongwa mkono wake hadi ukageuka. Jamaa akatoa sauti za maumivu makali sana lakini Roi alikuwa akitabasamu na sura ya Dede ambayo ilikuwa imekasirika baada ya kumuona Roi akicheza na Mwanamke mrembo pengine aliyemzidi yeye. Dede hakufanya kosa alimgeuza Benson na kumuelekeza mahali Roi alipo kisha akajichanganya na watu. Dede alikuwa tayari anawivu na hasira kwa wakati mmoja hivyo aliamua kuacha vita ambavyo alijua fika Roi asingefua dafu kwa Ben. Roi baada ya kuona kidume kikija upande wake, alimsukuma yule kijana aliyekuwa kaunyonga mkono wake huku akimsindikiza na maneno ya kiungwana.
“Mtu akiomba samahani siku nyingine uwe muelewa bwege wewe” jamaa alianguka kwa kishindo huku akiugulia maumivu ya mkono. Roi akakimbilia upande wa nyuma, kitendo cha Roi kukimbia pale, Ben akatoa bastola yake na kuishika mkononi akawa anapiga risasi juu huku akipiga kelele watu watulie. Hofu ikatanda mule ndani. Roi alipofika nyuma tu ya ule ukumbi, alibana kwenye mlango akimsubiri hasimu wake. Ben alikuja kichwa kichwa pasipokujua kama ametegwa. Alipotokea tu, silaha yake ilitolewa mkononi kwa teke maridadi huku akizawadiwa mateke mawili ya juu juu, Ben akaserereka lakini hakufika chini.
“Hongera kwa kunigusa” alisema Ben pamoja na kuruka juu na kuzunguuka kwa mtindo mtamu na wa kuvutia, Roi pasipo kutarajia alijikuta akipoke mateke matamu matatu na ngumi iliyopigwa kistadi sana ambayo ilimpita sentimita chache baada ya kuikwepa. Mapigo yale yakampotezea umakini kidogo na mpigaji hakuwa mtu wa kungoja. Ben alimfuata Roi kwa kasi kubwa ambayo ilikuwa ikimchanganya sana.
“Kasi hii si kasi ya kawaida hata kidogo natakiwa kuwa makini zaidi, huyu jamaa anapumzi sana anaonekana” alisema Roi huku akiyumba kadiri awezavyo kuhakikisha anazikwepa ngumi zinazomjia. Alipigwa kwa ngumi nyingi japo chache ndizo zilizofanikiwa kuingia mwilini. Ben akatabasamu baada ya kuona kuwa mtu anayepambana naye hakuwa mzuri, hilo ndilo kosa alilolifanya mahali hapo. Kitendo cha kutokuijua tabia ya Roi, hilo lilimgharimu sana. Roi alikuwa ni mgumu sana kusomeka wakati wa kupambana naye, huyo alikuwa ni mtu mwenye tabia nyingi sana kwaza ni kujifanya goigoi, asiyejitambua na nyingine nyingi zaidi. Ukizubaa hapo ndiyo huwa anakuja kama popo nyakati za usiku kwenye Stafeli bivu.
Ben alijinyoosha viungo vyake na kukaa tenge, Roi hakuja mbele kumfuata bali alikuwa akijiweka sawa na kusoma mitindo na kujua ni jinsi gani huyo boya atakaa. Ben alijisogeza kwa kasi sana pasipokujua kuwa kasi yake ilikuwa tofauti na jinsi alivyokuwa kajiweka. Alikuja akajisukuma hewani kwa mtindo wa Pakuwela, Roi akakunja magoti kidogo kisha akanyanyuka kwa kasi baada ya guu moja kupita. Alipiga ngumi kavu moja nzito sana iliyopiga kwenye mbavu za mwanzo wa kiuno. Ben aliguna akarudishwa chini kwa kishindo baada ya kushindwa kujigeuza kwa guu jingine. Pale chini akataka kujipindua akashindwa, akachomoa kisu lakini alichelewa kwani alipokea ngumi tatu kavu na kutazamana na giza ghafla. Hata alipowekewa kadi yenye bendera hakujua. Pigo lile lilimkata pumzi na ngumi zile zikasimamisha kazi ya moyo kabisa. Wakati Roi akiwa anataka kutoka eneo lile, akaguswa na kitu cha baridi kichwani.
“Wewe ni nani unayeuwa kwa mtindo huu wa kuacha kadi kwa mfu?” aliuliza hivyo mtu huyo mwenye silaha. Roi akajua kuwa huyo hakuwa mtu mbaya pengine lakini kwanini ajiaminishe hivyo sasa wakati anachuma kisicho na huruma kichwani mwake. Kitendo cha kujiuliza mawazoni, kikamfanya achelewe kujibu. Silaha ile iliyowekwa kichwani ikatolewa usalama lakini kabla kitu au jambo jingine halijafanyika, mlio mkali wa risasi ulisikika kisha silaha iliyokuwa imeshikwa na yule kijama ikirushwa mbali, Roi akajirusha kwenye mauwa ambayo yalikuwa yakitoa harufu mbaya ya mkojo kuonesha kuwa watu walikosa ustaarabu kabisa eneo hilo lakini alipogeuka kutazama risasi ilipotokea, akamuona Dede akiwa anakuja kama mzimu huku akiwa anawahaka mkubwa sana machoni mwake. Haraka sana Roi akafikiria jinsi ya kufanya akagundua kuwa hapo alipo huwenda pakawa na maadui wawili tofauti ambao wanahitaji roho yake zaidi. Hakupoteza muda alijirusha kwenye upande wenye mauwa marefu huko akakutana na harufu ya kinyesi kabisa na hata kukishika na mikono yake, akatoa tusi kubwa la nguoni kwa mtu huyo aliyepageuza hapo ni mahala pa kumalizia haja zake kubwa na ndogo kisha akadandia ukuta na kuchumpia upande wa nje. Yule aliyekuwa amemuwekea silaha Roi kichwani hakuwa mtu mwingine bali alikuwa ni Insp. Bogo ambaye alishuhudia mchezo mzima ule tangu Roi akiwa ndani ya ukumbi ule hadi mapigano yale. Hata alivyomuweka chini ya ulinzi na silaha ile, alijua kuwa mtu huyo hakuwa wa kawaida hata kidogo. Naye pia alitoka kwa njia kama ambayo aliitumia Roi akapotelea gizani.
Uchungu mkubwa ulimkamata Dede baada ya kuukuta mwili wa Ben ukiwa chini pasipo uhai. Roho ilimuuma sana mbaya zaidi ni kadi yenye bendera ambayo Roi mwenyewe aliita kadi ya mualiko wa kifo kwa anayehusika na ujinga wowote ule. Alinyanyua simu na kumpigia kiongozi wao kuwa Ben si wa kwao tena. Aiseei! Ilikuwa ni huzuni na pigo kubwa sana kwa vijana wale watatu na haikuwahi kutokea wakafikiria kuwa ipo siku BBD ingekuja kukatika kirahisi namna hiyo. B moja ililamba mchanga sasa zilibakia B na D. Dede alilia lakini haikusaidia. Vijana walikuja kwa njia wazijuazo wao wenyewe na kuuchukua mwili wa Kijana wao.
Usiku wa saa nane, ndani ya wodi maalumu ambayo alikuwa amelazwa askari aliyepona kwenye uvamizi, kulikuwa kuna mtu alikuwa akikaribia hapo. Huyo alikuwa ni Don Dou mwenyewe ambaye aliapa kuwa hatoweza kutuma mtu tena kwani vijana wote aliwaona ni wazembe tu sasa huo mchezo alitaka aufanye mwenyewe na awaoneshe kuwa yeye hakuwa mtu wa kutania hata kidogo. Alijitia ndani ya mavazi ya kidaktari, ndevu zake nyingi nyeupe zilizokuwa zikishabihiana na nywele kwa rangi yake, zilimfanya aonekane ni dokta kweli kulingana na vazi lile lenye heshima kwa daktari yoyote alivaapo, kwa jinsi lilivyokuwa limejenga nasaba naye. Mwendo wake wa hatua za kuto kumpa maumivu hata Sisimizi endapo akimkanyaga, zilikuwa zikikita kwenye sakafu hiyo ya hospitali pasipo kuleta kelele. Alitembea kwa haraka kidogo huku akiwa makini hadi kilipo chumba hicho maalumu ambacho nje kulikuwa na askari wawili wenye silaha. Akawakaribia kisha akawaambia.
“huwenda mgonjwa akawa kwenye maumivu zaidi baada ya kushtuka kutoka usingizini kutokana na baridi hivyo natakiwa kumchoma sindano ya kumpa afueni na aweze kulala pasipo shida. Kumbukeni kuwa ni mtu muhimu sana” askari wale wakajiuliza, Daktari au muuguzi, ndiye mwenye kazi hii? Mbona muda si mrefu alifika muuguzi mahali hapa na kumpa dawa tena alisema kuwa yupo macho tu ila bado anahisi maumivu kwa mbali? Lakini yawezekana ni mtu muhimu ndiyo maana. Hapa ndipo walipo haribu. Wakampa nafasi. Kwa kuwaaminisha zaidi, akawataka waingie wote humo ndani ya hicho chumba, wakakubali, midomo ya silaha zao wakazielekezea sakafuni na kuzipachika begani. Ile wanazama tu ndani ya chumba kile, visu viwili vikazama vifuani mwao kwa nguvu kubwa wakahamaki na kutoa macho huku wakitia huruma. Yule mgonjwa ambaye alikuwa macho kweli akaona lile tukio, akahisi kama maumivu yamekimbia na mwili wake ukipata ganzi ya nguvu mno. Akataka kunyanyuka kwa nguvu ili aiokoe nafsi yake. akashindwa kwa jinsi alivyojitonesa kidonda akarudi huku akiomba dua moyoni yule muuwaji asimuone pale kitandani. Nani kasema na muuwaji alikuwa pale kwa ajili yake. Kabla haja tamka neno, kisu kikazama kifuani.
“Naomba uitunze siri hii ya kuwa hujaniona milele kwenye maisha yako ila kama kuzimu wakikuuliza waambie ni Don Dou mr. Visu kazini” alisema Dou kwa kunong’ona kisha akafuta damu kwenye zana zake akazirudisha zilipotoka kisha akafungua mlango na kutoweka.
MADAGASKAR
Asubuhi jopo la madaktari sita kutokea mataifa tofauti kwa jinsi muonekano wao ulivyokuwa. Walikuwa uwanja wa ndege wa nchi hiyo wakiwa wanasafiri kuelekea Tanzania jijini Arusha na Ungamo jijini Pande. Msafara huo ulikuwa ukiongozwa na dokta msaidizi wa Dr. Lee, dokta Henry. Walikuwa wamejipanga kwa kila kitu tayari lakini wakati wao wakiwa angani wanaiacha ardhi ya kisiwa hicho. Bencov alikuwa akipokea simu yenye habari mbaya kupata kusikia kwenye maisha yake. Habari ya kwamba kijana wake mmoja kati ya watatu alikuwa ameuwawa na mtu mwenye kuacha jumbe ya kadi kutokea Tanzania. Bencov alipiga ngumi nzito kwenye meza aliyopo akanyanyuka na kukaa kwa dakika kadhaa kabla haja nyanyua mkonga wa simu na kuwataka vijana wake waufanyie mwili huo mazishi kisha vijana wote wasambae mtaani wahakikishe huyo kiumbe anaingia kwenye mikono yao akiwa amekufa tayari.
Majira ya saa 11:39 asubuhi. vijana sita wakiwa mbele ya mwili wa Benson ambaye amekufa akiwa na wivu, ambao ulikuwa juu ya kuni kubwa huku ukiwa umelala juu ya Toroli lenye magurudumu mane ya chuma. Walikuwa kwenye huzuni kubwa sana vijana hao. Bacon alipiga alama ya msalaba akiwa anamwaga machozi sana huku akisema. Damu yako italipwa, kapumzike kwa amani. Dede akawa ni mtu wa mwisho kabisa kufanya hivyo. Yeye alimpiga busu Ben kisha akasema.
“Sitakusahau mpenzi, ulikuwa ukinipa raha na kunitoa upweke, penzi lako nitalikumbuka daima, nenda kwa amani” alikomea hapo kisha akachukua muenge wa moto na kuuchoma ule mwili ambao ulianza kuungua kwa kasi kubwa. Hawakutoka hapo hadi ulipoteketea kabisa ndipo Bacon alisukuma lile Toroli ambalo lilibingilia korongoni na kwenda kuzama majini. Wakapotelea ndani wakiwa si wale waliokuwa na huzuni muda mfupi uliokuwa umepita.
“Ita wote tukutane” aliongea Bacon. Vijana wakaitwa na kupangiwa majukumu mapya kabisa na walitakiwa kuhakikisha huyo kiumbe anasakwa hata kama amepotea tayari. Maagizo yale yakapokewa na kazi ikaanza rasmi.
Taarifa mbaya ilimkuta Insp. Bogo ya kuwa mgojwa pamoja na askari waliokuwa wakimlinda mgonjwa huyo wamepoteza maisha. akatanabahi kwa muda kisha akakosa jinsi. Akawaza mengi na alipokuja kutulia akapata jibu na kujua nini afanye. Alipotaka kuinuka pale kitini alipokuwa amekaa, moyo ulisita kabisa hasa alipokuwa akilikumbuka tukio lililopita. Tukio la usiku ambalo pengine lilikuwa likienda kuondoka na roho yake. Risasi iliyopiga silaha yake ndiyo iliyokuwa ikimpa mawazo sana na hakujua nini lengo la mpigaji kwani kwa usawa aliokuwepo, kama alikuwa na dhamira thabiti ya kulenga, pale ilikuwa ni kifo bila uwongo. Hatari yake ilikuwa kubwa zaidi kwake na alipaswa kuwa makini zaidi na pia aliona kuwa huo ndiyo muda wa kufanya kazi kwa nguvu kubwa. Lakini Hali ilikuwa si shwari kwenye uongozi wa juu, kwani baada ya Bencov kupigiwa simu kuwa kijana wake amekufa, alinyanyua mkonga wa simu kisha aliikuruza kwa Rais Julio na kumwambia kuwa hataki uzembe kwenye kazi na mipango waliyokubaliana ili itimie ni lazima ahakikishe anaubana uongozi ulioko madarakani hata kwa vitisho ili mradi tu mambo yao yaende na yafanikiwe. Bencov alichokuwa akikifanya ni kumpiga na kumuuwa nyoka kwa gamba lake mwenyewe yaani alikuwa akiwatumia wazawa kuuwana kwa makubaliano kuwa baada ya hapo, Julio angekamata dola yeye lakini kumbe kwenye kichwa cha Bencov kulikuwa na maangamizi makubwa mno. Maangamizi ambayo yalikukuwa hayana macho na yapo kwa ajili ya malipizi makubwa ya kupotea au kuwawa kwa familia yake yote kipindi hicho cha nyuma. Hakukuwa na kiumbe aliyetakiwa kupona hata mmoja ndani ya Taifa hilo kwani Bencov hakumuamini kiumbe hata mmoja mwenye ngozi nyeusi. Julio hakujua kuwa alikuwa akicheza patapotea mbele ya kijana wa kirusi mwenye hasira na chuki kubwa dhidi ya Taifa la Ungamo na mpango ukiwa ni kuuwa kila mtu ndani ya Taifa hilo. Alizidi kutabasamu na kujihakikishia ukuu wa nchi usio na kelele pindi tu atakapo upiga chini uongozi wa Mabandu kwa kutumia akili kuliko nguvu.
Asubuhi na mapema kabisa geni mbili zilitua ndani ya ofisi mbili tofauti lakini pia kulikuwa kuna makutano ya siri ambayo nayo yalikuwa na lengo moja. Geni moja ilitua ndani ya ofisi ya IGP ndani ya makao makuu ya jeshi la polisi, geni ya pili ilitua ndani ya ofisi maalumu ya Rais Mbandu. Wote hawa walikuwa ni watu wa siri waliokuwa wametumwa na Mh. Julio ambao walikuwa na jumbe moja ya kuhakikisha eidha Rais au IGP Liyambo, anamsimamisha mtu ambaye walimuweka kwa siri kwenye upelelezi. Haikuwa hivihivi bali ilikuwa ni kwa vitisho maalumu vilivyoandaliwa.
“binti yako kwa sasa yupo kwenye mikono yetu na muda si mrefu unaweza kumkosa maana tutamuuwa kwa kifo kibaya sana huku wewe ukipatiwa zawadi ya kichwa tu kwa ajili ya kukifanyia mazishi” alisema mtu huyo wa siri aliyetumwa na Mh. Julio.
“Mnataka nini tena kwangu jamani?” alihoji Rais Mabandu huku akiwa na hasira kali sana dhidi ya watu hao.
“Mtoe mtu uliyemuweka kutupeleleza kwenye njia tunazopita”
“Mimi mbona sijaagiza mpelelezi yeyote, hakuna mpelelezi ambaye mimi nilimuagiza afanye upelelezi juu ya hili”
“Huyu anayepeleleza na kuuwa watu wetu ni nani sasa, Jini? Shetani? Au nani?”
“Sijui!”
“Unaonekana kweli hujui ila kwa hili utajua” akasema mtu huyo kisha akachomeka flashi kwenye kompyuta iliopo mahali hapo, sauti kali ya kilio cha binti yake ikasikika, ilionesha kuwa binti yake yupo katika maumivu makali mno. Baada ya sauti hiyo, picha ya binti yake akiomba msaada na kumsisitizia baba yake awape hao jamaa kitu wanachokitaka, ilikuwa ni picha ambayo haikuonesha kuwa binti huyo alikuwa kwenye mazingira ya chuoni bali alikuwepo kwenye shida iliyokuwa ikihitaji msaada wa hali ya juu mno.
“Nakupa giza la leo tu la kuamua na kufanya maamuzi kinyume na hapo kifo cha binti yako hauto kizuia. Usifanye kitu chochote kile kwani hapo ulipo wanatuona tazama binti yako mashine aliyowekewa kichwani hiyo ni kabla ya hapa lakini hata hapa, mashine hiyo iko kichwani, endapo utafanya lolote kuhusu mimi, unekiruhusu kifo cha binti yako mpendwa” alimaliza huyo bwana kisha akanyanyuka kitini na kutoka mule ndani. Rais akajua kweli huwenda ile ilikuwa ni sura ya binti yake wa pekee. Ki ukweli Rais alibaki akimtazama mtu huyo pasipo kummaliza. Alichanganyikiwa kupita maelezo. Mtu yule alipotoka, Rais Mabandu alikimbia kwenye meza iliyokuwa imejaa simu tofauti tofauti. akapiga namba ya mlinzi maalumu wa kumlinda binti yake huko chuoni, namba hiyo ikasema kuwa mteja hapatikani labda aache ujumbe ili akirudi hewani aukute. Akahamaki. Inamaana itakuwa kweli?” akajiuliza, kabla hajajipa jibu akaweka simu nyingine sikioni. Hii ilikuwa ni ya Lecture ambaye alikuwa karibu zaidi na binti yake nayo ikampa majibu chukizi. Alibutwalika zaidi. Akaamua sasa aipige namba ya binti yake moja kwa moja. Hii nayo ilikuwa hivyo hivyo haipatikani. Akataka kulia Rais, akajua kweli binti yake yupo mashakani, hali kama hiyo haijawahi kutokea kwenye maisha ya masomo ya binti yake huyo sasa iweje. akafikiri kwa muda kisha akapata wazo la kupiga kwenye vyombo vya usalama vya nchi ambayo binti yake anasoma ili aseme kuwa binti yake amepotea. Akakumbuka maneno ya kumtaka asithubutu kufanya kitu chochote kile kama anahitaji uhai wa binti yake uendelee kuwa huru. Akakata shauri na kuamua kumpigia IGP Liyambo. Hawa jamaa ni kweli walifanikiwa kumtisha Raisi kwa video ya kutengeneza huku wakitumia janja za kitaalamu kuzuia mawasiliano yote kwa Rais huyo ili kumtia kimuhemuhe, afanye walitakalo lakini kumbe hakuna lolote la kweli na walifanya hivyo baada ya kugundua ulinzi uliopo kwenye chuo anachosoma binti huyo huko China haukuwa wa daraja dogo.
NUSU SAA NYUMA.
Liyambo alikuwa akikosa la kufanya juu ya ugeni ulioingia ndani ya ofisi yake kwani tangu kuingia kwa ugeni huo, hakukuwa na salamu wala maongezi yoyote bali kilikuwa ni kitendo cha kutazamana tu mwanzo mwisho kama majogoo. IGP alishindwa kuutafsiri ugeni huo mtata kwani kikubwa cha ugeni huo kilichokuwa kikifanyika hapo ni tabasamu baya pekee. Walizidi kukaa kimya kwa namna ile kwani hata Inspekta Jenerali alipojitoa sadaka na kuuliza sababu za kuja kwake hapo, mgeni huyo alizidisha tabasamu hadi Kiongozi huyo wa jeshi la polisi akahisi huenda mtu huyo ni bubu. Baada ya kuwa hivyo kwa muda mrefu, simu ya IGP ambayo ilikuwa ikileta taarifa moja kwa moja kutoka Ikulu ikaita. IGP akanyanyua mkonga wa simu kisha kumtaka mtu huyo ampishe aweze kuongea na simu hiyo, mtu huyo akaliondoa tabasamu na kubaki akishangaa. IGP akajua pengine ni kichaa mtu huyo lakini kila alivyoitafakari simu hiyo, akajua fika huwenda si kichaa kwani kama ni kichaa asingeruhusiwa kupita kote huko hadi kuifikia ofisi yake. Akaziba spika ya simu hiyo ili Mtu yule asiyeeleweka, asisikie.
“kama kuna mpelelezi yoyote yule Kijana wangu naomba umsimamishe haraka sana sielewi mimi!” ilikuwa ikilalama sauti hiyo.
“M….pe….ngoja mbona siku……..?”
“Liyambo nini tatizo, huelewi nini?” ilizidi kufoka sauti ya upande wa pili, Liyambo kuongea chochote alishindwa kwani ugeni uliyopo mbele yake ulikuwa ukimtazama kwa mtazamo wa ajabu sana ambao ulionesha fika kuna kitu cha msingi ulitaka kusikia.
“Kama si mkeo atakuwa ni binti yako au huwenda pia akawa mama yako mzazi kama hutamtoa mpelelezi uliyemuweka atupeleleze” alisema mtu huyo kwa sauti ya kunong’ona kisha akanyanyuka na kutoka mule ndani. Liyambo akapigwa na butwaa hata maamuzi hakuwa nayo, simu aliyokuwa akiongea na mkuu wa nchi ni kama hakuisikia. Simu ile ikakatika. Liyambo akajua hali pengine ni mbaya zaidi kwa Rais hivyo alichokifnya ni kupiga simu kwa Insp. Bogo na kumtaka asitishe zoezi la kuacha kupeleleza haraka iwezekanavyo. Potelea mbali, wa kwanza alimsimamisha baada ya kifo cha baba yake, acha na huyo amsimamishe yasije kuzaliwa mapya bure. Hakupewa muda wa kuhoji hiyo ilikuwa ni amri na si ombi. Akachoka Bogo lakini moyoni alikiri kukiuka maneno ya mkuu wake wa kazi na kuamua liwalo na liwe hawezi kurudi nyuma japo atafanya kwa siri kubwa. Yote hayo wakati yanafanyika, geni nyingine ambayo ilikutana na mtu faragha, ilikuwa ni geni iliyokuwa imemlenga First Lady. Mke wa Rais Mabandu. Geni hii ilikuwa ya pekee na ilikuja kwa mke huyo wa kiongozi wa nchi kwa maneno kadhaa. Kwanza ni kumwambia juu ya mpango wa binti yake kuwa yupo mahali wamemuweka lakini ni salama, jingine lilikuwa ni kuhakikisha anampeleleza mume wake ili kujua mipango yote ikiwemo mikutano, safari za nje ya nchi na hata simu anazopiga. Ujumbe huo ukapokelewa kwa nguvu kubwa lakini kubwa zaidi ni kujulishwa kikao kikubwa cha kuingia au kukaribia kwenye ushindi. Hivyo kuna mipango na mikakati mipya ya kimaangamizi alitakiwa aijue. Wakakubaliana kwa kupeana mikono kisha wakaagana kwa namna hiyo hiyo. Geni ile ikaondoka.
Gari ya kibuluu ilipiga breki makao makuu ya polisi punde tu baada ya ugeni ule kutoka mule ndani ya ofisi ya IGP na eneo lile. Gari hiyo ilikuwa ikiwaka sana na ilikuwa ni mpya bado ukiitazama, ilikuwa ni gari maalumu ilyotengenezwa kwa niaba ya Roi na hapo Ungamo ilikuja kwa kazi maalumu. Kijana huyo alimtazama Petii akiwa garini bado kisha akamwambia ahakikishe anafuatilia kiumbe yoyote yule atakayetoka baada ya yeye kuingia ndani ya ofisi ile kubwa na yenye kila kitu kifaacho kwa kazi ya kipolisi. Roi alishuka kutoka ndani ya gari ile yenye jina MT. Hatua za haraka alizopiga zilimfikisha kwenye mlango wa kuingilia ndani ya ofisi zile. Mawani ya giza ilikuwa machoni pake na kumfanya atokelezee, alinyuka suti safi ya gharama sana. Moja kwa moja aliingia kwenye chumba kinachoongoza kamera za ulinzi za pale ndani. Alipofika humo akaagiza aoneshwe matukio yote yaliyofanikiwa kurekodiwa siku hiyo. vijana wale wakataka kuhoji lakini wakasita baada ya kuona kitambulisho maalumu cha kazi kinachomtambulisha kama askari maalumu wa usalama wa Taifa wa nchi hiyo. Matukio yote akaoneshwa yeye akavutiwa na mtu aliyeingia kwenye ofisi ya IGP asubuhi hiyo.
“Simamisha hiyo, vuta picha yake mbele, ok….mnamjua huyu namaanisha kama ni mtu zoelefu kufika eneo hili?” akauliza. Vijana wale wakajibu kuwa hawamfahamu.
Akatoa flashi akatumbukiza kwenye kompyuta iliyokuwa ikionesha video hiyo na kuomba anyonyewe video ile yote kisha baada ya kuhakikisha ameipata, akaomba ile video ifutwe. Ikafutwa mbele yake akiwa anashuhudia. Akatoka mule ndani akiwa na kitu alichokitaka hadi kwenye ofisi ya IGP.
“Afadhali umekuja” alisema IGP. Kisha bila kutoa nafasi akaendelea.
“Mambo yamekuwa magumu sana na kila kitu kinatishia usalama wa nchi na uongozi kwa ujumla hivi ninavyosema mkuu wa nchi hii amenipa taarifa ya kusitishwa kwa kila kitu”
“Najua na najua hawa watu ni hatari na wamewakalia shingoni lakini niwape tu taarifa kuwa kuanzia sasa sitamuonea haya mtu yoyote yule kwani nimejua kuwa hili jambo lina vibaraka ambao kama si viongozi basi walishawahi kuwa viongozi na wanafanya haya kwa mpango maalumu. Nikupe tu taarifa ndogo Afande, nimeianza kazi ya kuwatafuta walioniulia ndugu zangu kutokea Tanzani na hii itagusa uhalifu wa kila namna” akakoma hapo Roi huku akiwa amemkazia macho IGP. Pumzi nzito sana zikamtoka bwana huyo kisha akauliza.
“Hali ya usala wa Rais ukoje sasa?”
“Hali ya usalama wa Rais hauna tatizo kwani naanza na huyu aliyekuja kwako leo kisha napiga kwa walengwa” akamaliza na kutoka humo ndani. IGP alibaki akiduwaa asijue nini afanye lakini hapo aliona ni afadhali kidogo maana tayari ameshamtoa mpelelezi wake wa siri kazini japo hakujua kama itasaidia ama la! Roi alipotoka mule na kurudi garini. alioneshwa kijana mmoja ambaye alikuwa akiongea na simu huku akiwa makini na lile gari. Hapo hapo akatoa bastola yake ya siri ambayo inauwa kwa siri pia na yenye nguvu kubwa. Akashusha kioo kidogo akalenga shabaha kisha akaachia risasi ikafanye yake pasipo kufanya kelele yoyote, risasi ya kifua ilitosha kubadili mfumo mzima wa maisha wa kijana yule. Petii alishangazwa sana na maamuzi ya Roi, hakuwahi kumuona akiwa na maamuzi ya haraka kiasi hicho na mbaya zaidi kila baada ya muda huwa anabadilika.
“alikuwa pale kwa muda gani?” alihoji Roi akiwa anaigeuza hiyo gari taratibu kisha kuiondosha eneo lile.
“Ni kama dakika tano baada ya wewe kuingia ndani” alijibu Petii.
“Ok, sasa tunakwenda kwa huyo kijana anayeitwa Frank kisha tunarudi hotelini, najua kuna watu wamewekwa kila kona kwa ajili yangu” alisema Roi.
“Hotelini tena?” alishtuka Petii.
“Ndiyo” akajibu kifupi tu kisha akaondoa gari kwa kuongeza kasi kubwa sana. Wakati akiwa ndani ya gari ile alikuwa akifanya mambo mawili kwa wakati mmoja, alikuwa akiendesha huku akiwa anafanya kazi nyingine. Alifungua mfuniko mmoja kwenye dashboard kisha akabonyeza kinobu fulani na kuichomeka ile flash baada ya kompyuta ndogo kutokea kwa juu. Akafungua ile picha ya mtu aliyemtilia mashaka na aliyepanga kuanza nae ambaye aliingia ofisini kwa IGP asubuhi hiyo. Akaituma mahali na kuandika na ujumbe fulani kisha akairudisha ile kompyuta mahali pake kwa mtindo uleule. Kasi ya gari ilikuwa kubwa sana kiasi cha kufanya safari yao isiwe ndefu na ya kuchosha. Muda mfupi tu wakawa wapo kwenye maskani ya Frank kichaa.
“Huyo kijana anaishi hapa?” akahoji Roi.
“Ndiyo, anaishi hapa” Petii alijibu huku akiwa ni wa kwanza kushuka na kuelekea mahali jengo baya la kijana Frank lilipo, aliita sana lakini hakukuwa na dalili kuonesha kuwa kijana huyo alikuwa mahali hapo. Wakati akiwa anazidi kuita, akasikia sauti ya chuma kisogoni mwake kikitolewa usalama pamoja na sauti ndogo ya kunong’ona.
“Umeamua kunivamia huku na watu wako, hebu niambie umekuja na nani hapa?” alikoroma mtu aliyoko nyuma.
“Ni salamu tu M.Y.S, hakuna shida nyingine” aliweka sawa Petii kisha akataka kugeuka lakini akazuiwa kwa mkono mzito wenye nguvu.
“Freeezz kijana kuna usalama wa kutosha!” sauti kali ya Roi ikamshtua Frank, kijana huyo akagwaya na kupoteza lengo, hapo hapo Petii akageuka na kuchukua ile silaha huku akimwambia aache uchuro wake.
“Kuna nini mbona siwaelewi, Petii shida nini sasa!”
“Kama nilivyokuambia kuwa leo nitahitaji kuonana nawe, huu ni ujio wangu sasa huelewi nini?”
“Ujio wako si ndani ya makubaliano yetu”
“Ondoa hofu hapa ni amani sana, huyu ndiye mwenye utambulisho wa kadi yenye bendera ya Tanzania kila anapouwa nadhani kwenye harakati zako umesikia au kuona hilo” alizungumza Petii, Frank kichaa akamgeukia Roi kwa kumshangaa kisha akarudisha macho kwa Petii ambaye alikuwa akiendelea.
“Kwa utambulisho huo nadhani kuna kitu umegundua? Yuko hapa kwa kazi maalumu na anahitaji umpe kile ambacho wewe unakifahamu ama unacho na pengine tunaweza kuwa tumesaidiana wote kwa namna tofauti” ndivyo aivyozungumza Petii. Frank hakutaka kujibu wala kusema kitu chochote bali alichokifanya ni kuwa mkimya huku akiwa na tafakuri nzito kichwani mwake. Hakuamini kukutana na mtu ambaye ni msababishi wa mauwaji ya watu ambao ni gumzo ndani ya Ungamo lakini hakujua kama wale wanaokufa walikuwa ni watu wa namna gani, alijua ni watu maarufu tu kwa biashara zao au vinginevyo lakini hakujua kama nao walikuwa ni watu wabaya, akataka kujua mengi kupitia huyo kijana.
“Naitwa Frank, au kwa utambulisho mwingine waweza kuniita Frank kichaa. Nadhani mengi kuhusu mimi unayajua, nami nadhani ingekuwa busara sana kama ningejua mengi kukuhusu…..!” hata Frank hakufika mwisho wa sentensi yake, muungurumo wa gari na risasi kadhaa zilizopunyua gari na kuwakosa, ndizo zilizokatisha maongezi yale. Vijana wale watatu wakajirusha chini na kuanza kupambana na jinsi ya kukwepa risasi zilizokuwa zikipigwa kwa ufundi mkubwa huku kwa namna ya pekee wakibingilia ili kutafuta pa kujificha. Kila mmoja pale chini alikuwa na bastola yake mkononi akiwa tayari kufanya shambulio la aina yoyote ile. Wanatoka wapi hawa? Akajiuliza Frank. Au ni mtego? Akaongeza huku akiwa amejibanza mahali. Kimya kilikuwa kimetanda sana baada ya wale jamaa kukosa kuwaona maadui zao. Frank alikuwa ametulia tuli pale chini huku akiwa anatafakari juu ya uvamizi ule ambao hakuutegemea, uvamizi ambao unekuja kuharibu chimbo lake pengine.
“Tokeni basi kama nyinyi ni wanaume mlio kamilika, kinachowafanya mjifiche nini. Huu ndiyo mwisho wenu wapuuzi nyinyi” sauti ya mmoja ilikuwa ikibwata eneo hilo na huyo ndiye yule aliyemvamia IGP asubuhi. Frank alikuwa akiilia taiming hiyo sauti kwa hisia kali sana na hapo alikuwa na imani kuwa wote aliokuwa nao walikuwa wakitaka kumuuwa au kumtia mbaroni ikibidi hivyo alitakiwa kuwa makini na kujitoa zaidi.
“Cheza na sauti pindi tu unapokuwa unapambana na mtu mwenye silaha yaani namaanisha kuwa wewe unapokuwa na silaha na adui anasilaha. Ni ngumu sana kupambana na adui ambaye haongei, hapo inabidi utumie hisia zaidi kuliko masikio lakini kama adui ni muongeaji basi ni rahisi sana kwani milango yako ya fahamu ya kimapigano inatumika yote, yaani hisia na masikio. Sikiliza sauti inapotoke kisha hisi mkao aliokaa adui yako, ukishajua mkao aliokaa adui yako, fanya udanganyifu ambao utamgharimu maisha yake” aliyakumbuka maneno ya mwalimu wake Frank alipokuwa ndani ya msitu mnene akipokea mafunzo ya lala salama ya kulenga shabaha na mapambano ya silaha. Hisia zake zikamwambia kuwa adui zake wapo hatua ishirini na tano kutoka alipo na wote wakiwa wanavuta hatua kumfuata alipo. Akaona ugumu lakini hakubaki kuona wanamkaribia. Alifikiria gari walilokuja nalo akina Petii lilipo kisha akachukua kijiwe kidogo akakirusha kwa nguvu sana, sauti ya kijiwe kile ilienda sambamba na mruko wa sarakasi moja kisha akalala kama nyoka silaha yake ikiwa mbele lakini pia sauti ya kijiwe kile ilienda sambamba na risasi kutoka kwa Roi hivyo wakati Frank akiwa anashambulia, kuna vijana kama wawili walikuwa wamedondoka. Frank akafuta dhana kuwa ametegwa. Risasi zake alizozipiga kwa ufundi mkubwa zikasafiri na maisha ya vijana watano. Kasi yake ya upigaji rasasi ikamshtusha Roi kwa kiasi kibwa sana, akajua kuwa huyo kijana ni hatari zaidi kwenye matumiza ya silaha.
“Hongera sana Frank kwa kuwa na kasi kubwa ya kutumia silaha, sijawahi kuona mtu dizaini yako” alitoa shumbe Roi akiwa anamsogelea kijana huyo.
“Hongera nawe kwa kucheza na hisia zangu kwani kama usingewashtua upili na kuwachanganya, ingekuwa ngumu kidogo mimi kulenga shabaha kwa haraka ile.
“Ok, sasa hapa si rafiki tena ni vema tukaondoka chukua kila chenye umuhimu kwako Frank tuondoke eneo hili” alisema Roi, Kijana huyo aliingia ndani ya jingo lile baya baada ya dakika tatu akatoka na bag moja dogo la kuvaa mgongoni.
“Petii wewe utangoza gari hadi Hoteli ya Bi. Rozi” akatoa agizo, wakapanda garini. Kijana huyo alitoa maelekezo madogo ya jinsi ya kuendesha gari hiyo maalumu, wakaondoka hapo. Walipokuwa njiani, kuna ujumbe uliingia kwenye simu ndogo ya Roi.
Ujumbe huo ulikuwa ukimpa majibu ya ile picha aliyoituma wakati akiwa anatoka kituoni. Roi akaitoa simu nyingine nayo ilikuwa na umbo kama la ile iliyoingia ujumbe kisha akabonyeza vitufe kama viwili vitatu akaiweka sikioni akasubiri.
“Nitahitaji unipe location ifikapo kesho kwani kwa muda huu kuna kazi ndogo naenda kuifanya” alisema Roi baada ya mtu aliyempigia kupokea simu.
“niko nyuma ya kila tukio, kazi nzuri kiongozi” ulijibu upande wa pili kisha sinu hiyo ikakatika. Safari ilikuwa bado inaendelea huku ukimya ukiwa mkubwa kiasi ndani ya gari ile. Si Frank, Roi wala Petii aliyekuwa akiongea kwa muda huo kila mtu alikuwa kimya kabisa. Walipokuwa wamebakisha umbali wa mwendo mfupi, Roi akaelekeza mahali ambapo gari ile iegeshwe, ilikuwa ni sehemu ambayo mtu akiwa garini angeweza kuona tukio zima likifanyika kwenye eneo la mbele la hoteli ile.
“Petii unaiona hiyo gari iliyosimama hatua chache tu kuingia kwenye lango la hoteli” alisema Roi. Petii akajibu kuwa ameliona, Roi akaendelea.
“Ujinga wanaoufanya ni kutokubadili gari, hiyo inasiku ya nne sasa tangu iwe hapo na kila sekunde inakuwa na watu ndani wanaongalia anayeingia na anayetoka hadi watakapomuona adui yao. Mimi nitapita hapo wakati wa kutoka hotelini lakini wewe nitataka ubaki hapo utazame atakayekimbia kisha ummalize sitaki hata Kunguni mmoja a escap kwenye huu mchezo, tunauwa wote ili liwe pigo kwao na kuzidi kuzionesha hasira zao. Frank utapita mbele ya hiyo hoteli baada ya dakika kumi, nadhani mimi nitakuwa nimeshatoka ndani ya chumba changu baada ya kuingia kwa njia nizijuazo” aliweka tuo hapo, wote wakajibu kwa kutikisa vichwa. Roi akashuka garini na kupitia upande wa nyuma wa hoteli ile kubwa kisha akapita kwenye mlango wa jikoni wanaoutumia wapishi na baadhi ya wahudumu wa hoteli hiyo kwa kila mapokezano ya kuingia kazini na kutoka. Alipita jikoni na kuwafanya wapishi wamshangae lakini yeye hakujali, alitokea upande wa ngazi ndogo ambazo zilikuwa zikifika hadi ghorofa ya pili akazipanda huku akitazama saaa yake. Alipofika ghorofa ya pili aliingia kwenye kikorido fulani akatoke kwenye ngazi kubwa, hapa akazipanda hadi kwenye korido ya floo ya tatu. akapiga hatua za haraka hadi ulipo mlango wa chumbani kwake. Kuna vitu aliviacha humo japo havikuwa na umuhimu sana kwake lakini ukiwa kama mtego kwa namna nyingine. Kwa akili zao lazima watege na humu. Aliwaza kisha akafungua mlago kwa kadi yake ya kijajusi akausukuma mlango kwa nguvu kisha akajirusha kavu hadi katikati ya chumba kile mikono yake ikiwa imekamata silaha imara. Hakuwa ameongopwa na mawazo yake kwani nyuma ya mlango kulikuwa na mtu, kitendo kile cha kufungua mlango kwa nguvu kikamyumbisha mtu huyo nyuma ya mlango. Roi pasipo kupoteza wakati, risasi mbili zikatoka kwenye domo la bunduki yake, zikazama kwenye kifua cha kijana yule uhai ukawa si mali yake halali, akadongoka chini akiwa mfu. Akafungua kabati akakuta limechanguliwa, akaona hakuna cha umuhimu kwani vingi vya msingi alishabeba baada ya kumuondosha yule boya wa kwanza aliyevamia chumba cha Petii. Kwakuwa hakurudisha chumba wakajua kuwa iwe isiwe ni lazima kijana huyo angerudi na kweli amerudi lakini akiwa ameacha madhara makubwa. Akatazama saa yake ilikuwa imebaki dakika moja tu kutimia dakika kumi. Akatoka mule ndani na kuielekea lifti kisha kushuka kuelekea chini. Wakati yeye akiwa anashuka, Frank alikuwa tayari yupo ndani ya hoteli ile kwenye kiti kimoja kilichopo mahali ambapo alikuwa akiona upande wa nje. Roi alielekea upande wa mapokezi akakabidhi chumba na kuaga kabisa kuwa hatorejea tena kwa kipindi cha karibuni. Akatoka na kumpita Frank kama hawakuwahi kuonana kisha akafika eneo ambalo aliamini halina usalama. Wakati anatoka, mule ndani kulikuwa na mtu mwingine ambaye aliiweka simu yake sikioni mara tu Roi alipopita. Akasema machache na kuishusha kisha akatoa bastola kwa siri sana bila kujua kama kila hatua aliyokua akiichukua, kuna mtu alikuwa akimuona. Mtu yule aliyekuwa ametoka kuongea na simu muda mfupi alipompita tu Frank, Frank naye akanyanyuka kisha akamkaribi akiwa na kisu mkononi. Akamkamata bega la kulia na kukizamisha kile kisu mgongoni kwa nguvu nyingi kisha akamkumbatia na kumpandishia kile kisu. Mtu yule alipata maumivu makali sana kisha akasukumiwa pembeni akiachwa apambane na uhai. Nje Roi alishtukia vijana watatu wakimtokea kwa mbele wakiwa na mitutu ya bunduki.
“Dooownn!” Frank alipiga kelele huku akiachia risasi tatu zilizofanya kweli lakini bila mategemeo alipigwa moja ya bega ambayo ilimpa maumivu makali sana. kitendo cha yeye kupigwa risasi ile, bastola yake ikamtoka mikononi akajitupa chini huku akibingilia kupoteza shabaha za maadui lakini Roi alishacheka nao na kufanikiwa kuwaangusha wawili waliobakia.
“hali ngumu huku kiongozi wenzangu wote wameuwawa!” alisema mtu mmoja aliyoko kwenye gari ambayo ilikuwa nje ya lango la hoteli ile kisha mtu yule aligeuza gari na kuiweka sawa lakini kabla hajaitoa pale, tairi za mbele zikalala zikiwa hazina upepo. Kijana akajua kuwa hata yeye yuko kwenye hatari ya kupoteza maisha. Akiwa anashangaa asijue la kufanya, akakoswa na risasi iliyodhamiria kumkosa akachomoa bastola na kutoka nje ya gari ile, alikosea. Mateke mawili mazito yakambabatiza na vioo vya gari ile. Vioo vikapasuka silaha ikamtoka mikononi kabla ya kujiuliza ni shetani gani aliyekuwa na kasi ya kushambulia kiasi kile, alichezea ngumi mbili za kifua zilizo mpunguza makali akalegea. Hapo hapo Roi na Frank wakatoke huku Frank akiwa anavuja damu kwenye bega lililopata madhara. Roi alimpekua yule kijana kwa upekuzi maalumu kisha wakamzimisha na kumapakiza garini. Petii ambaye ndiye aliyeleta shuruba kwa kijana yule aliyetaka kutoroka baada ya mambo kumuwia ugumu alichana fulana ya Frank na kutumia kulifunga lile jeraha ili lisizidi kutoa damu kisha wakaingia garini na kuondoka wakiwa na mateka wao.
Shangwe, nderemo, mbinja na vifijo, vilikuwa vimelipamba jiji zima la pande. Watu wengi walikuwa wakiandamana kwenye kila barabara na maeneo mengine ya wazi wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali zilizokuwa zikinadi na kuleta jambo moja kuu kabisa. ‘TN. RACE, KATUWAKILISHE KIMATAIFA. HATA MIMI NI MZALENDO. TUJUMUIKE WOTE KWENDA KUTOA NGUVU KUBWA YA KUHAKIKISHA WANAPATIKANA WATU WAWILI WA KWENDA KUSHINDANA. TN. RACE, BABA LAO’ hayo na mengine mengi yalikuwa ni mabango yaliyokuwa yakining’inia juu ya vichwa vya watu yakiwa na jumbe hizo. Hakuna ambaye alikubali kubaki nyumbani, kama yupo aliyebaki nyumbani basi alikuwa eidha ni mgonjwa au mtoto lakini kila mwenye kujitambua alikuwa katika kuhamasisha huko watu wajitokeze kwa wingi kwenda kujionea anavyopatikana au wanavyopatikana madereva wawili makini.
“Lazima tajiri mtoto awepo kwenye list hiyo”
“Yule hawezi kukosa wewe, mwenyewe anapenda ule mchezo mbaya mbovu”
“Mi nawaza yule jamaa aliyemuangusha Don Dou na kampuni yake”
“yule si Martan?”
“Oooh! Wewe, hakuwa Martan yule, yule alikuwa ni mgeni kabisa, aliamua tu kumpa msaada mshkaji. Asingekuwa yule, Tajiri mtoto angeshindwa wale jamaa walikuwa makini sana ujue na waliutaka ushindi”
“Sasa alikuwa ni nani yule? Hata mimi nakubali hilo kwani hata tajiri mtoto mwenyewe alibaki akimshangaa yule jamaa ujue”
“ni nani yule?”
“Hakuna anayejua kati yetu ujue halafu hilo shindano la kesho ninamashaka nalo sana ujue”
“Kivipi?”
“Si yule Dou ametoroka mahabusu tena baada ya kusikia kuwa jamaa anaingia kwenye mashindano ya Afrika kama bingwa wa Afrika mashariki kisha anaelekea kidunia?”
Mh! hao walikuwa ni vijana ambao walikuwa wamekaa kijiweni baada ya kutoka kuandamana kwa amani. Hapo walikuwa wakijadili jinsi ya mambo yatakavyokuwa siku inayofuata huku wakitaka kujua ni nani na nani atakayeweza kuchuana na bosi mwenye Kampuni ya TN. RACE, Tamimu, ili kupata watu wawili watakaoweza kwenda nchini kenya. Waliongea mengi sambamba na kuonesha shauku yao lakini vijana hao hawakujua kama kwenye hilo kundi alikuwapo Ispekta wa polisi, Insp. Bogo ambaye mara baada ya kutolewa kwenye upelelezi, akaamua kutafuta njia nyingine ya kuweza kuendelea na kazi ile kwa siri sana huku wakuu wake wakiwa hawajui. Yeye ndiye aliyechomekea kuhusu kijana aliyeweza kumpa ushindi Tamimu wakati kampuni mbili pinzani zilipokuwa zikikinzana. Alitaka kumjua yule kijana ni nani kwani? Akili yake kila ilivyomfikiria mtu aliyekutana naye Club siku za usoni na kuilinganisha na sura ya kijana aliyetoa msaada kwa Tamimu, sura zilikuwa hazitofautiani sana. Akajua tu yule aliyemkamatisha Don Dou baada ya kuleta vurugu lazima atakuwa ndiye yule anayeuwa kwa kuacha kadi ya mualiko wa kifo. Aliapa ni lazima akutane naye na afanye jambo ambalo kwake aliamini ni msaada tosha wa kumfanya yeye awemo ndani ya upelelezi pasipo kung’amuliwa.
Chumba kilikuwa kipana si kwa Bacon wala Rais Julio, mambo kwao wote yalikuwa magumu na ya kutisha mno. Alikuwa akienda huku na huko kama mtu aliyekosa amuzi sahihi la kufanya. Kichwani alikuwa na zaidi ya hasira dhidi ya kiumbe asiyeeleweka ni jini au mzimu. Hakutaka kuamini kama kiunbe huyo yuko peke yake. Vijana saba amba nane ambao walitumwa kumuangamiza mara baada ya kupewa taarifa na shushu wao ambaye walimuweka pale kwenye makao makuu ya polisi, leo wafe wote kwa muda mfupi tena bila hata ya mmoja kukimbia kwa ajili ya kutoa taarifa ya idadi yao. Shushu wao pia amemuawa wakati akitoa hiyo taarifa. Akakumbuka sauti ya Bande Sir ilivyomwambia kuwa wana kazi nzito ya kupambana na huyo mtu asiyetabirika. Rais Julio akaiona hatari ikiwa inataka kubomoa kama sio kuharibu kabisa mipango yake. Alikaa kwenye kiti chake cha gharama kilichopo hapo ndani kisha akanyanyua simu na kumpigia mtu amtakaye akaiweka sikioni.
“Hebu tusileteane mchezo wa kuigiza bwana, unataka kuniambia mipango ya mumeo juu ya watu wanaotishia mipango yetu hujaidaka?” alisema Julio Mobande.
“Nisikilize mkuu, usidhani labda mimi siko upande wenu nop, niko kwenu na napenda kuwa bilionea mkubwa sana baadaye si kuwa chini ya huyu na kupewa kijicheo kidogo cha first Lady, nataka kuwa na pesa zangu, makampuni yangu, biashara zangu na maamuzi yangu juu ya matumizi yangu pia. Hadi sasa ninavyokuambia huyu mjinga anasema hajui. Jana nimempa penzi hadi la siku ananitongoza lakini amesema hajui. Nimeshindwa jinsi ya kufanya ninachowaomba ni kwamba munipe nafasi ya mwisho nadhani habari za huyu mtu kutoka Tanzani anaweza kuwa nazo. Nitahakikisha nazipata usiku wa leo kisha niwape taarifa kesho. Chonde chonde binti yangu akifa huyo mtakuwa mmenikosea sana, huyo ni binti yangu mimi na siyo mtoto wa Rais, uchungu nimeupata mimi” alitoa maelezo First Lady huyo anayekwenda kwa jina la Salama kisha akamalizia kwa kusema kuwa ujumbe wa asubuhi aliupata hivyo ataufanyia kazi kwa haraka ya kupitiliza. Rais Julio akashusha pumzi kisha akamuita Kitema na kumpa maagizo ikiwemo na kujua nini amefanya kwa kichaa yule. Kitema hakuna jipya aliloliongea bali alisema kuwa kichaa yule hayuko mwenyewe yuko na binti ambaye ni mzuri wa mapigano na anaakili kubwa sana ya kufanya kazi yake kama ambavyo alimpa taarifa.
“Hatujui amuzi la Bencov hadi sasa kwani naye pia amepata pigo kwa kijana/vijana wake kuuwawa na huyu jini. Tusuburi tuone kitakachoamuliwa sisi tutafanya hata kama akisema tuilipue Ikulu tutailipua kisha kujenga nyingine” alisema Julio kisha akavuta chupa kubwa ya mvinyo akagida kwa hasira na shonde zito lililomkaa kooni dhidi ya Mabandu.. Huku nako Bacon alikuwa kama si yeye kwa jinsi naye alivyopatwa na shock kubwa baada ya kupigiwa simu na kijana mmoja kati ya sita aliokuwa amewaweka kwenye hoteli ya Bi. Rozi lakini kitu kilichomchanganya ni kuto kumpata hewani mazima kijana aliyempa taarifa, hiyo ilimaanisha kuwa hata huyo atakuwa ameuwawa.
“Nini tunafanya kiongozi, Boss amechanganyikiwa sana baada ya hili najua” aliongea Dede akiwa ameghadhibika mara zaidi ya mbili, mtu aliyemvulia nguo na kumpa penzi lake, anawapa maumivu makali sana. Kwanini nilishindwa kumuuwa pale Club, nilikuwa ninanafasi nzuri sana ya kukifumua kichwa chake kuliko yule aliyekuwa amemuwekea bastola kichwani, eti, nimelenga bastola. Inamaana ninemuokoa adui kwenye kifo mara mbili. Aliwaza Dede. Alisahau kuwa kuna mmea unaoitwa mapenzi dhidi ya Roi, ulikuwa umemea moyoni mwake na huo ndio uliopelekea amuache hai.
“Boss amesema kunampango upo unatokota kwenye jiko la gesi, huo ndiyo utakaoleta majibu ya kufa kwa kila Kima aliyepo ndani ya shamba hili” alijibu Bacon. Dede alikuwa bado yu mawazoni hata hilo jibu hakulisikia kabisa. Mambo yalizidi kuwa mambo lakini Dede hajui sababu za kumuacha Roi ni nini. Mambo hayo. Chezea Afrika Dede!
NDANI YA JINGO LA SIRI LA ROI. Hiyo ikiwa ni baada ya Frank kupewa matibabu na kutolewa risasi.
“Nani alikutuma/alimituma mkae pale hotelini?” aliuliza Petii akiwa mbele ya mateka waliyemteka kule hotelini. Alikuwa amechoka vibaya sana kutokana na kipigo alichokuwa amekipata baada ya kuwa mbishi kusema, kipigo kilimnyang’anyaza vya kutosha sana hadi akawa amelegea na bado kilikuwa kikimshukia kila alipoonesha kutokuwa tayari kusema.
“hutaki kusema siyo?” Petii alikuwa katili sana mbele ya watu ambao wanamnyima usingizi na mara nyingi huwa hapendi kubembelezana nao kwa muda mrefu. Alimunamia hadi karibu ya sura yake kisha akamnong’oneza.
“niambie basi maana umepata bahati ya upendeleo” pamoja na hayo lakini yule mtu alikuwa akikoroma tu kuonesha kuwa hata uwezo wa kusema hakuwa nao hapo ni kama alikuwa akifanya mawasiliano ya mwisho na Malaika wa mauti kwa jinsi alivyokuwa akikoroma kwa kipigo kitakatifu kutoka kwa huyo mpelelezi wa Malawi. Petii alirudi juu ghafla kisha akabonyea chini na kupiga ngumi nzito ya kifua, yule mateka akagoa na kunyoosha shingo, hapo Petii alipiga ngumi nyingine ya shingo mateka akakohoa damu na kutulia kimya miguu ikiwa inajinyoosha kwa mara ya mwisho. Petii akatoka mule chumbani akiwa anahasira bado.
“Vipi?” akahoji Roi.
“Labda ukamuhoji wewe anaweza kusema mimi nimeona ananisumbua tu hivyo nimempa mapumziko ya amani” akasema Petii huku akijikalisha kitini. Roi na Frank wakatabasamu tu. Mtu amemuuwa halafu anataka akahojiwe na wengine, lazima hata kama ni wewe utabasamu.
“nilifanya makusudi kukuambia ukamuhoji wewe kwani nilijua kuwa hukawizi” aliongea Roi, Petii akamuangalia kijana huyo usoni kwa muda kisha akayageuzia macho yake luningani na kutazama habari za jiji kuhusiana na mashindano ya mwisho ya kumpata dereva atakaye kwenda Kenya kushiriki mashindano.
“Tunakula luninga leo mrembo?” alihoji Roi.
“Si tunaelekea wote jikoni kuandaa chakula au?”
“Au unayo wewe mimi sijui, waafrika hatuko hivyo”
“Acha kuendekeza tamaduni mwanaume”
“Hebu acha uvivu nenda kapike bwana kwanza ukumbuke leo nataka kula chakula cha kimalawi”
“Umeshakila sijui unataka chakula gani tena” alijibu Petii huku akiwa anacheka na kunyanyuka kuelekea zake jikoni. Roi akamsindikiza na utani wa kumwambia, hata leo pia nakitaka” wakacheka wote watatu. Ilikuwa ni furaha sana baada ya kuwa wameelewana wote. Frank aliahidi kuwa bega kwa bega hata kama ni kufa kwani kuna jambo zito aliota kwenye ndoto moja alipokuwa amelala na alipomuuliza mwalimu wake kuhusiana na ndoto hiyo kipindi bado yupo mafunzoni, jibu alilopewa ni kwamba ndoto aliyoota ni ngumu sana kuitafsiri na ndoto ngumu kama ile huwa hujirudia kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ni hiyo aliyokuwa nayo lakini awamu ya pili ni pale atakapokuwa amekutana na mambo ya awali basi huja hiyo kuleta majibu.
“kama kweli umeota basi jua kazi ni ngumu na inaendana na kile nilichokiota mimi kama mtaalamu wa maisha ya roho za viumbe wa kale, ndoto hiyo huwenda ikawa na maana kubwa sana, siku tukija kukutana tena nitakupa maana” Frank alikumbuka maneno ya mwalimu wake pindi alipokuwa akimuahidi Roi kuwa hatakubali awe mbali naye kivyovyote vile afe yeye ndipo afe Roi.
“Frank nini tena mbona anatuchanganya tena? Roho za viumbe wa kale tena Haya?” alihoji Petii lakini Frank akamwambia kuwa bado ni mapema ila atajua.
Chakula kilikuwa tayari kimeshaandaliwa, vijana hao wakaikaribia meza kwa ajili ya kupata chakula hicho cha jioni. Walikula kwa furaha kubwa wakakisifia chakula sambamba na mpikaji wa chakula hicho. Walikula wakashiba wakaridhika kisha kila mmoja akachukua kinywaji akipendacho kwa ajili ya kukisukuma chakula hicho kifike mahala kinapostahiki kukaa. Simu ya Roi ikaita muda huo huo. Roi aliitazama simu hiyo kwa muda kisha akatoka kwenye meza ya chakula na kuifuata. Namba hakuwa akiifahamu, akasita kidogo kuipokea lakini hakungoja ikatike.
“Brother isingekuwa busara kama shughuli hii isingepata uwepo wako. Tamimu hapa naongea, karibu sana kesho kaka kwenye mashindano ya kumpata kijana atakayeongozana nami kwenye mashindano ya Afrika kwa ujumla” aliongea mtu wa upande wa pili kisha akatulia kumpa nafasi Roi ya kujibu.
“Hata kama usingenialika lazima ningefika, ilikuwa ni lazina nifike kwani kuna kitu cha msingi sana ninakihitaji hapo” akajibu Roi. Wakaongea mambo mengine kisha akakata simu.
Giza lilikuwa tayari limechukua mamlaka yake ya kulifunika anga, ndani ya jumba moja la mafichoni, jumba ambalo lilikuwa limetulia kulikuwapo kimya sana. Sebule ya wastani ambayo ilikuwa imetulia sana, ilikuwa imekusanya meza moja ya kioo pamoja na kiti kimoja cha thamani ya kawaida huku kukiwa na Jokofu moja la kugandishia chakula na vitu vingine vinavyostahili kuganda lakini pembeni ya Jokofu hilo kulikuwa na friji la vinywaji ambalo mlango wake ulikuwa wazi kuashiria kuwa kuna mtu alilifungua muda mfupi uliopita na kusahau kulifunga au kuliacha kwa makusudi. Baada ya dakika moja kupita, mlango wa chumbani ulifunguliwa akatokea mtu mmoja mwenye ndevu nyingi nyeupe sambamba na nywele zenye mshabihio wa ndevu hizo kwa rangi. Alikuwa amevaa nguo ndefu ya moja kwa moja mfano wa Kanzu yenye rangi nyeusi. Alifika kwenye lile friji ambalo lilikuwa wazi akachukua chupa kubwa ya mvinyo akaenda nao hadi kwenye kile kiti ambacho kiko nyuma ya meza ile ya kioo akaketi huku ule mvinyo akiuketisha juu ya ile meza. Akaokota kijimkoba fulani kilichopo chini ya meza akakiweka juu mezani pale kisha akakifungua na kutoa visu vidogo vidogo sita pamoja na vikububwa viwili.
“Tamimu!” akataja jina hilo huku akiwa amelitazama dari akiwa amekamata kisu kikubwa mkononi mwake. Akasema.
“Hawa viumbe wapo kwa ajili yako, nikikukosa hata kwa kimoja basi utakuwa unabahati ya kuzaliwa” alipokwisha kusema hayo akakirudisha kile kisu mezani na kupiga tarumbeta ya kile kinywaji kisha akairudisha chini, akashika nywele zake na kuzirudisha nyuma.
“Siwezi kufeli kipumbavu halafu nikakuacha utambe, nafasi hii ilikuwa ni yangu mtoto mdogo wewe, ushukuru yule kiumbe mjinga kama wewe ambaye alijitahidi kukupa msaada. Mimi lazima nitakukalisha milele na hiyo nafasi ya kwenda Kenya iwe ndoto kwako. Nitakuuwa kwa mikono yangu umfuate baba yako kuzimu” aliongea kwa sauti kubwa Don Dou akiwa amezimakata nywele zake nyeupe akizisukasuka kwa hasira. Asubuhi ya siku iliyofuata kila mwana jiji hilo alikuwa akiisubiria saa kumi kwa hamu kubwa ili kuweza kujionea mashindano. Kila mtu alikuwa na shauku sana ya kuweza kuona maufundi ya vijana makini wa TN. RACE wakifanya vitu vyao. Wakati mambo hayo yakiwa yanasuburiwa, huku Dou alikuwa akipanga zana zake kwa uangalifu mkubwa sana, alihakikisha kila zana inakuwa kwenye nafasi yake. Huyo ndiyo alikuwa Dou mtu mwenye uzoefu mkubwa wa kutumia Visu kuliko zana za aina yoyote ile. Wakati akiwa anapanga mambo yake, alikuja mtu mmoja hapo ndani kisha akampa taarifa Dou kuwa alikuwa akihitajika kwa waziri Bande Sir. Dou alisimama kwa hasira kuu kisha akasema.
“Bande Sir ni nani kwangu? Nilishawaambia mapema kuwa sauti ninayoisikiliza mimi ni ya Rais Julio pekee, sitaki kupokea amri ya Kunguni wa aina yoyote ileeeee” alifoka Dou kisha akarusha kisu kwa ufundi wa hali ya juu na kwenda kuzama kwenye kifua cha mleta taarifa, upande ambao kulikuwa na Moyo. Mtu yule akabaki kuachama mdomo kama mtu anayehamaki. Mruko wa kitaalamu kabisa ulirukwa na Dou kisha akamzawadia huyo mtu mateke ya namna yake hadi mtu huyo akasambaratikia sakafuni akiwa kimya.
“Fu*k” akatukana na kutoka mule ndani kwa hasira akafunga mlango na kutoka akiwa juu ya pikipiki kubwa ambalo ndilo alilolihitaji kwa kazi na safari zake.
ARUSHA TANZANI.
Pembeni ya jiji la Arusha nchini Tanzania, watu waliofahamika na kutambulika kama wataalamu wa madawa na watoa mafunzo ya kuhusiana na masuala ya kilimo. Wazungu ambao vitambulisho vyao vilionesha kuwa wametokea Uingereza kwenye shirika moja la utafiti wa masuala ya kilimo huku wakiwa ndani ya koti la shirika la chakula na afya duniani. Watafiti hao walikuwa ndani ya jiji hilo kwa ajili ya kutoa elimu ya Mbolea mpya ya kukuzia mazao ya kila aina hususani mazao ya muda mfupi. Serikali ya Tanzania iliwapokea wageni hao ambao kwa muda huo walikuwa tayari wamemaliza siku tatu tangu kuingia nchini na tayari walishatoa somo kubwa ambalo lilikuwa likisambaa kwa kasi kubwa kupitia vyombo vya habari hususani Luninga. Tayari mashamba ya muda mfupi yalikuwa yameshakuandaliwa kwa ajili ya mfano dhidi ya mafunzo hayo. Elimu hiyo iliyokuwa ikitolewa si kwa watanzania pekee bali hata kwa watu wa nchi ya Ungamo walilipata hilo somo na mambo yalikuwa yakienda kwa mpango maalumu. Huku kikifanyika hiki na kule kulifanyika hichohicho hakukuwa na mapishano hata robo. Ulikuwa ni mpango wa maangamizi makubwa sana kwa nchi hizo mbili za kiafrika. Tanzania ilikuwa ikienda kuangamia kwa ajili ya malipizi ya Dr. Lee ambayo yalikuwa yakifanyika kwa sababu ya kukoswakoswa kuuwawa na vijana makini kutoka ndani ya Taifa hilo. Kitendo cha Lee ambaye mwanzo alikuwa akitumia jina la Lee Kim na sasa Dr. Lee. Huyu aliapa kuionesha Tanzania kuwa yeye ni kiumbe wa aina gani na hilo ndilo lililopelekea hayo yote yafanyike. Haya mambo yalikuwa yakisababishwa na visasi na si vinginevyo.
“Leo tutawaonesha njia nyepesi ya kupanda mazao kwa kutumia mfumo mpya ambao huufanya mmea uweza kujipatia chakula chake vizuri na wenyewe uweze kujizalishia chakula kwa wingi sana. Kwa kutumia dawa au mbolea hii ambayo inafahamika kama Diet Pills, Tutaweza kupata mavuno mengi sana kwa siku za usoni” alikuwa akitoa maelekezo kwa lugha safi ya kigeni Dr. Henry ambaye alikuwa ni Daktari mwandamizi wa msafara huo. Mazao yakapandwa kwa utaalamu mkubwa na kufuata misingi yote ya kitaalamu. Wakulima wakubwa walikuwa hawatoki kwenye Luninga zao kwa ajili ya kuangalia matangazo ya hiyo mbolea mpya ambayo inasemekana kuleta mapinduzi makubwa ya Mbolea zote ambazo zilishawahi kuingia nchini. Wengine ambao walikuwa hawana majukumu mengi ya kikazi, waliamua kujumuika na wataalamu hao ili kuweza kupata mambo mazuri hatua kwa hatua.
“Weweeeeeeeeee! Hureeeeeeeee! Weweiyaaaaaa!!” Kelele zilikuwa zikisikika ndani ya Uwanja mkubwa sana wa Tajiri mtoto kama wananchi wengi wa Pande walivyopenda kumuita Tamimu. Gari mpya kabisa zilizokuwa na nembo ya Moto ubavuni na maandishi mekundu chini ya nembo ya moto ule yaliyosomeka TN. RACE. Gari hizo zilikuwa zimebeba rangi ya kibuluu zote. Zilikuwa ni gari mpya tupu ambazo ni maalumu kwa kazi hiyo. Morde na wataalamu wenzie walikuwa wamekaa juu sana kwenye jukwaa la peke yake wakitazama uwezo wao wa kufanikisha kuzifanya gari hizo ziweze kutembea hadi kufika hapo. zilikuwa ni gari nne tu ambazo zilikuwa uwanjani hapo.
“Inapendeza, inapendeza tena inapendeza sana. Gari zipo tayari kabisa kwa ajili ya kuanza mashindano haya ya kukata na shoka. Kumbuka kuwa haikuwa kazi ngumu sana kwa Tajiri mtoto kuchagua kijana mmoja kwa ajili ya kuelekea naye nchini Kenya kwa ajili ya kwenda kupambana. Ilikuwa ni kazi ndogo sana lakini kwanini achague yeye? Kwanini ajipe maamuzi mwenyewe wakati kuna raia ama wanachi wengi wanaompa sapoti kubwa na wanaomkubali. Ametaka ninyi ndiyo mchague kwa macho yenu mtu ambaye atashiriki mashindano hayo huku mkiwa hamna mashaka miyoni mwenu. Hata kama yeye atapigwa chini na vijana wake, yuko radhi kuwakabidhi bendera ya nchi hii atakayotunukiwa na serikali usiku wa leo na yeye akawa mtazamaji. Zimesalia dakika tano tu kwa kuanza kwa mashindano haya ya kukata na shoka, vijana wanaingia kwenye gari zao kwa tambo kubwa, kumbuka mashindano haya ni mubashara kabisa” shangwe kubwa liliibuka, zilikuwa ni kelele kali sana hakuna ambaye alikaa, kila mmoja alijinyanyua kitini na kushangilia baada ya vijana hao kutoka kwenye chumba maalumu walichokuwa wamekaa kisha kupita kwenye njia nyembamba ambayo iliwatoa juu ya uwanja huo mkubwa. Walikuwa wapo kwenye sare zao maalumu kwa ajili ya mashindano hayo. Vijana hao wane waliingia kwenye gari zao kila mmoja kisha wakaanza majigambo ya kuziungurumisha injini zao zilizokuwa zikiunguruma kwa sauti ya simba dume. Walikuwa wapo katika majigambo makubwa ya kutambiana wenyewe kwa wenyewe. Ndani ya ule uwanja kulikuwa na Luninga kubwa sana ambazo zilikuwa zikionesha njia zote ambazo gari hizo zitapitia. Kila barabara ilikuwa imewekwa kamera maalumu kwa ajili ya kuweza kuwapa watu haki ya kile walichopaswa kukiona mahala hapo. Sauti ile ya mshehereshaji wa mashindano hayo, ilisikika tena ikisema kuwa kwa muda huo zilikuwa zimesalia dakika mbili pekee.
“Boss, leo niko mwenyewe hakuna udanganyifu, hushindi leo” alijitapa Martan akiwa anagusa hiki na kile kwenye dashboard ya gari yake huku akiwa amekiweka kisafirisha sauti mdomoni mwake na yeye akiwa amepachika kinasa sauti masikioni. Alisema kwa kujiamini sana na huyo ndiye alikuwa mpinzani mkubwa wa Tamimu.
“Ukishinda nakupa Bendera wewe na nitakupa kazi maalumu ya kumfanya mpenzi wangu popote alipo duniani ajue kuwa mimi nipo na namkumbuka kila siku, si unajua kuwa haya mashindano ni kwa ajili ya kumtafuta na yeye pia” alisema Tamimu huku akitazama nje ambako kulikuwa na watu wengi sana, ile anageuka tu, alipigwa na mwanga mkali sana machoni. Alipotazama vizuri, alikutana na alama ya dole gumba kutoka kwa Roi ambaye alikuwa kwa mbali kidogo. Kijana huyo alikuwa amepiga mawani ya giza, mawani maalumu ambayo akivaa basi humkumbuka mpenzi wake aliyemuacha nyumbani, Catherine. Mawani ambayo inauwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, Mawani ambayo ndiyo aliyoitumia Catherine, wakati wa kulivamia jingo kubwa la Lee Kim mjini Morogoro kwenye mkasa wa Sex machine. Mawani hiyo ikivaliwa ujue hata ukiwa umeweka shilingi mia ya sarafu kwenye buti na ukavaa na soksi lazima itaonekana. Ilikuwa inauwezo wa kuona kitu chochote chenye madini ya chuma ama shaba mwilini mwako. Tamimu alivua kofia kisha akafinya jicho moja na kulivaa tena lile kofia hapo alikuwa na imani kuwa hata kama Dou ametoroka mahabusu lakini ulinzi kwake ulikuwa mkubwa. Hakuna ambaye aliligundua hilo pia hakuna ambaye p alijua kuwa kuna pikipiki kubwa lilikuwa limeingia uwanjani hapo kwa muda mfupi tu uliopita, zaidi Roi pekee baada ya kuona mtu huyo akiwa amepanga visu vyake kiunoni kama miiba ya Nungunungu.
Dou alijua tayari ameharibu eneo lile huku akiamini shabaha yake imekwenda alipoiagiza kumbe haikuwa hivyo. Aliruka kwa kasi kama Ngedere ama Nyani, alijizunguusha hewani kama Popo na kuja kutua juu ya pikipiki lake. Roi alipiga risasi kwa lengo la kumdondosha pale juu ya lile lipikipiki lakini Dou hakuwa mzembe kiasi hicho, alivuta mafuta kwa nguvu kisha akapachika gia kisha akachia clachi kwa haraka sana. Gurudumu ya mbele akanyanyua juu na kuondoka eneo lile kwa kasi kubwa huku akiwa anatembea na gurudumu ya nyuma. Risasi ile ya Roi ikapiga maboya na kwenda kukita kwenye boneti ya gari moja iliyokuwa imesimama pembeni. Dou alishaacha vumbi mahali hapo hata polisi walipounga waliambulia patupu, mnyama Dou alishatoweka kama mzimu. Vijana wa Roi wakataka waunge, Roi akawazuia na kuwaambia hapo si mahala pao tena.
WIKI MBILI MBELE.
Mafanikio yalikuwa yameshaonekana tayari, Mashamba makubwa yalikuwa yameshaandaliwa karibia mikoa yote ya Tanzania na Ungamo. Pamoja na vitisho vya matukio ya mauwaji yaliyokuwa yakiendelea ndani ya Ungamo lakini serikali haikuacha kuhimiza wananchi wake juu ya kulima mazao ya chakula na ya mda mfupi yanayoweza kustahimili ukame ili kuweza kuepukana na baa la njaa siku za usoni. Hivyo wakulima wengi wakatumia fursa hiyo waliyoipata kutoka kwa wataalamu kutoka nchini Uingereza mara baada ya kuona mazao yakistawi sana kupitia mbolea mpya ya Diet Pills ambayo wamekuja nayo wataalamu hao. Wakati wa kupanda ukafika sasa wakapewa mbolea ambayo waliamini ni ile waitakayo kumbe tayari mbolea iliyotumika kwa ajili ya somo na kuleta mazao yenye kupendeza na kuzalisha chakula kwa wingi huku chakula hicho kikiwa hakina madhara kwenye maisha ya wananchi baada ya kupimwa na mkemia mkuu wa serikali, badala yake walisambaziwa mbolea inayofanana na Diet Pills kwa kila kitu na kupewa jina hilo lakini kumbe ilikuwa si Diet Pills bali ilikiwa ni Diebrainaphine. Mbolea mbaya yenye mpango mbaya kwenye maisha ya wananchi wa mataifa haya mawili kwa ujumla. Mbegu wakati zinapandwa kwa kutumia mbolea hiyo na baada ya muda kuota na kukua kwa kasi kubwa. Wananchi hususani wakulima wakiwa wanashangilia kwa kuweza kupata mbadala wa kuondokana na umasikini, huku watu wengine walikuwa wakishangilia na kujipa ushindi mkubwa. Wakati wanapalilia. Wataalamu wale walitembelea baadhi ya mashamba makubwa ambayo yalikuwa na uwezo wa kulisha nchi kama chakula chake kikisambazwa nchi nzima. Wakapiga picha. Wakulima wakadhani ni utaratibu tu wa maisha ya wazungu/watu weupe lakini kumbe walikuwa wakikusanya data na ushahidi wa mimea mipya ambayo mingi haikuweza kuondoka kwa upalizi uliokuwa umefanyika. Mimea itakayokuja kuuwa Watanzania wengi kwa wakati mmoja na wana Ungamo wengi. Kwani asiyekula ugali basi angekula matunda ya mbogamboga kama nyanya, nyanya chungu, mabilinganya na mengine mengi yanayofanana na hayo. Mimea hiyo mipya inayokwenda kwa jina la Partathunumu iliyoshikamana na mazao ndiyo itayoleta ushindi mkubwa kwenye kazi ya maangamizi ya Dr. Lee, Bencov na watu wao.
Wiki moja mbele, huko kisiwani Madagascar baada ya madaktari wote kurudi wakiwa wanasikilizia majibu kutoka kwenye mabomu yao waliyokuwa wameyatega. Walikuwa wapo kwenye ukumbi mkubwa wakifuatilia mashindano makubwa ya magari yaendayo kasi ambayo yalikuwa yakifanyika nchini Kenya. Walikuwa wakiangalia utaalamu mkubwa uliokuwa ukifanywa na vijana kutoka nchi ya Ungamo ambao walikuwa wakiongoza kundi lao. Vinara wengi kutoka mataifa mengine ambao walikuwa ni wazoefu wa mashindano hayo, walishaingia baridi miyoni mwao. Kampuni ya TN. RACE, ilikuwa ni tishio sana kwenye mashindano hayo na kila shabiki wa mchezo huo alipokuwa akihojiwa alisema kuwa nafasi mbili lazima zichukuliwe na kampuni hiyo ya TN.
“Unayaonaje mashindano hasa katika hatua hii ya lala salama?” alikuwa ni mtangazaji kutoka kwenye chombo kimoja cha habari cha nchini hapo alikuwa akimuhoji Tamimu ambaye ndiye aliyekuwa akioneka kinara wa mchezo huo.
“Kiukweli….?”
“Jitambulishe tafadhali” alikatisha muandishi huyo wa habari.
“Kwa majina naitwa Tamimu Ndungai, ni mshiriki namba TN 956/02.A. Kutoka kwenye kampuni ya TN. RACE. Kiukweli mashindano ni magumu sana na kila mmoja ana moyo na ari kubwa ya kutaka kuibuka mshindi. Hakuna ambaye hapendi kampuni anayoshiriki isifike kwenye mashindano ya Dunia. (akacheka kidogo). Kila mshiriki anataka kuifikisha kampuni yake mbali hivyo hata kama ni magumu kiasi gani lakini niwahakikishie tu wana Ungamo kuwa mimi ni mzalendo nisiyekubali kushindwa lazima niibuke kinara. Kati ya kampuni tatu zitakazokwenda duniani basi hii ya TN ipo” aliongea Tamimu huku akiwa makini na kamera ili kama mpenzi wake yupo hai, basi amuone kwenye luninga au magazeti.
“Ndugu mpenzi mtazamaji wa matangazo haya Mubashara unayoyapata popote duniani, huyo alikuwa……..!” ndivyo alivyokuwa akiongea muandishi huyo wa habari.
“Ha ha hahaaaa! Eti, anauhakika wa kufika kwenye mashindano ya dunia huyu mpumbavu!” aliongea Bencov huku akiangua kicheko cha kushiba kwa ukwasi mkubwa alionao. Kilikuwa ni kicheko kilichojaa kejeli, dharau na kashifa kubwa. Kwa imani yake alijua fika hakuna mwananchi wa Ungamo au Tanzania, atakaye fikisha miezi miwili kuanzia muda huo labda kama hatakaa ndani ya nchi hizo. Kwa chumba kingine cha mtu asiye na uhuru, matangazo hayo yalikuwa pia yakionekana. Mtu huyu ambaye alikuwa ni Tereza, habari hiyo ya kuwa yule aliyekuwa akihojiwa pale alikuwa ni Tamimu, ziliulipua moyo wake kwa kiasi kikubwa sana na kuyafanya mapigo ya moyo huo yaanze kwenda mrama. Mh. Backa pia aliona lakini alishindwa kufanya kitu chochote aliachia tu tabasamu. Mwili wake haukuwa umekonda sana kwani alikuwa akipata chakula ambacho kilikuwa kikiingia mwilini mwake kwa njia ya mipira. Muda huo yale maumivu yalikuwa yameshapita, yalikuwa yakisubiri tena masaa mengine manane ndipo yaweze kurudi tena kama ratiba ya maisha yake inavyosema.
“My, love, my love, my love Tamimu!” nafsi ya Tereza iliongea hivyo kwa kurudia rudia, machozi yalianza kumtoka lakini ghafla alianza kutabasamu na kucheka pasipo kutoa sauti yoyote japo kicheko kilionesha kuwa ni kikubwa sana. Akazima ile kuninga.
“Siamini kama ni hivi, nitaishi hivi kwa muda gani sasa? Nakupenda Tamimu, ishi ukiamini kuwa nakupenda lakini usiishi ukiamini tutaonana tena. Maisha yangu na baba yangu yapo kwenye gereza lisilo na matumaini ya kutoka tena. Gereza hili ni la ajabu sana My love, unaona mwanga, unakula chakula ukitakacho lakini uhuru wa kuongea kusikia ndiyo nimenyimwa, nimekuona tu sura yako lakini sijajua umeongea nini. Hata kama umenitaja watakuwa wamesikia wengine si mimi. Nakupenda sana na nakupenda kuliko nilivyokuwa nikikupenda hapo mwanzo” nafsi ya Tereza ndivyo ilivyokuwa ikiimba kwa namna hiyo. Kwakuwa giza lilikuwa lineshaingia tayari na ilikuwa yapata saa 10:05. Usiku. Akajilaza mtoto huyo wa kike, kuusubiri usingizi kama utakuja. Usingizi ulipokuja kumchukua pia hakujua hata umemchukua muda gani.
“Hutakiwi tena kuishi hapo wewe na mwili wako?”
“Niende wapi sasa?”
“Utakwenda kwenye maisha ya roho ya mwili ulioubeba”
“Roho ya mwili nilioubeba?”
“Ndiyo, kwani hujui kuwa tulipokutana kwenye jumba la roho ya mkombozi wa Dunia yetu inayoteseka, nilikuingilia kimwili?”
“Nakumbuka”
“Basi ulikuwa katika siku za hatari na ndiyo maana nikawahi kufanya vile kwani kama ningechelewa tungezidiwa na maadui zetu wanaotaka kuingamiza nusu ya Dunia yetu, na nidingefanya vile, Malikia wa Dunia yetu asingeweza kupandikiza makuzi na nguvu za kuweza kumbeba mkombozi tumboni mwako”
“sikuelewi ujue”
“Utanielewa siku moja na kwa hili utateseka sana, naomba unisamehe sana maana umebeba kiumbe cheche sura mbili ambacho roho yake inaishi kwenye lile jumba kule msituni jumba ambalo halionekani kwenye rada ya adui yetu yoyote yule. Hata siku ambayo wale viumbe walimuweka baba yako na wewe kifungoni ambao wanamuabudu King Bondo, kiumbe ambaye ni adui wa dunia yetu, siku ambayo kulikuwa kukifanyika ibada kwa ajili ya damu ili ajipatie nguvu, mimi ndiye niliyekuhamisha na kuja kukuficha huku ili asikuone alipokuja kule chumbani kwako. Kwanini alikuja? Hilo utalijua baadae kwa sasa ni wewe kukubali kuhama hapo na wasikuone tena”
“Naondoka na baba yangu?”
“Hapana kwenye jumba la roho ni mimi na wewe ndiyo tutakaoishi, kule hakuna kiumbe mwingine anayetakiwa kwani kila baada ya siku saba ninatakiwa nikuingilie kimwili kuupa chakula mwili ulioubeba”
“kama baba haendi nami siendi”
“Baba yako atabaki salama na mwisho wa siku atakuwa mzima, usihofu ulinzi utakuwa ni wa kwetu kwasababu umeyakubali mateso ya kuishi na kiumbe kitakachokufanya uchukie kuzaliwa mwanamke lakini kwa muda maalumu kisha amani ya maisha yako na baba yako inarudi”
“Sitakiiii. mnanidanganya na kwanini mnitese sasa, nasema kama baba yangu haendi nami siendi mahaliiiii!”
“Utakwenda kwa ulinzi wa mkombozi wetu utakwendaaaaaaaa!”
“Baba yanguuuuuu!!!”
Vuuuuuuuuummmmmmm!!! Baada ya majibizano hayo ya nafsi ya Dr. Tereza na kiumbe cha ajabu ambacho hadi muda huu bado hatujakifahamu ni kiumbe cha aina gani. Kiumbe kinachoitaja nusu ya dunia ambayo wanasema kuwa inaweza kuangamia kama mkombozi wao ambaye mwili wake ndiyo unaoshi tumboni mwa Dr. Tereza, hautapata usalama. Ni kiumbe gani huyo na hiyo nusu dunia ni ipi?” Inamaana Tereza ataishi kwenye mateso makali zaidi ya hayo aishio sasa? Mungu wangu?
Vuuuummmm! Puuuuh!
“Zumbeeeee Mghoshiiii!” Baada ya mvumo ule ambao ulikuja baada ya majibizano ya Tereza na hicho kiumbe kutopata muafaka, kukasikika kishindo kikubwa sana, kishindo hicho kilileta ukimya mazima kwa majibizano yale ya Tereza na kile kiumbe lakini katikati ya msitu mkubwa uliopo kati ya mkoa wa Sami Ado na Pande. Kuna babu mmoja mwenye nywele chafu sana babu huyu alikuwa akiishi ndani ya msitu huo peke yake hakukuwa na kijana wala mke au binti yeyote aliyekuwa akiishi nae ndani ya msitu huo. Ulikuwa ni msitu wa kutisha sana na wenye kuhifadhi nyoka na wanyama wakubwa lakini mzee huyo alikuwa hakaribiwi na wanyama hao na badala yake wanyama hao ndiyo waliokuwa wakimlinda na kumpa taarifa ya mgeni au wageni watakaokuwa wanaikaribia ngome yake. Babu huyu alikumbwa na mshtuko mkubwa sana, mshtuko ambao ulimtoa kwenye ndoto mbaya aliyokuwa ameiota na ndoto hiyo yalikuwa ni yale majibizano ya nafsi ya Tereza na kiumbe cha ajabu.
“Nyumba ya roho ya ukombozi!” hili neno alilitamka kwa sababu alilisikia likitajwa kwenye ndoto hiyo aliyoiota na kumfanya ashtuke huku akimtaja Mungu kwa lugha anayoijua mwenyewe. Babu yule ambaye anafahamika kwa jina la Seki Lonzo ambaye alikuwa ameamua kuweka makazi ndani ya msitu huo wa Dabaa Lonzo. Msitu wenye sifa na maajabu ya kushtusha mioyo ya watu lakini haukuwa kwenye kundi la misitu yoyote ile ya kihistolia ila Seki Lonzo alikuwa na historia nao na andiyo maana hakutoka ndani ya Dabaa Lonzo.
“Maajabu yanazidi kuwa makubwa, huyu biti atakwenda kuifuta Ungamo kabisa. Mbona ndoto niliyoota mwanzo na hii haziendani?” alijiuliza huyo babu mwenye mywele chafu huku akiwa na Gagulo kuu kuu lililokuwa limeufunika mwili wake kwa mtindo wa lubega kama vazi la kimasai livaliwavyo.
“Lakini hebu ngoja!” akasema kisha akajinyanyua kutoka kwenye uchaga uliokuwa umesitiri mgongo wake kisha akatoka pangoni mule akiwa na muenge wa moto. Akajikongoja kwa hatua za taratibu kisha akapanda juu ya jiwe na kusema.
“Zuuumbeee na Mulungu!” tena akasema.
“Zuuumbeee na Mulungu! Muliniweka hapa, nikaishi hapa na niliapa kuwa siku moja nitakufa nikiwa hapa labda ije kauli yenu ya kunitoa upweke. Njozi mbili na moja ya pekee kutoka kwa mtiifu aliyeishi nami kwa miaka mitatu akiwa na shida zilizohitaji msaada wangu lakini mbona kama ni kubwa nikitazama kwenye fasiri zangu. Naona binaadamu wengi watakufa, naona damu itakavyofanywa ni maji ya kunywa ya kupoza kiu cha waabudu mashetani na ninaona Taifa mliloishi ninyi linavyokwenda kuangamia looooote. Zuuumbeee na Mulungu!” alisema mzee huyo ambaye kwa mtazamo alionekana kuwa ni kikongwe sana. Upepo wa wastani ukapuliza na kunyanyua lile gagulo aliolivaa yule babu. Babu yule akatokwa na cheko moja la mshangao. Enheeee! Kisha akainama na kuinuka mara tatu. Upepo ukazidi kuwa mkali hatimaye ukatulia.
“Bado, badoooo!!” akakema kwa sauti ya juu kisha kimya kizito kikatanda kwa muda fulani. Mara akapiga mkongojo wake chini mara ya kwanza, pili. Akatokwa na mguno wa mfadhaiko kisha akaupiga mara ya tatu. Jiwe alilopo likatoa moto wenye cheche. Akaweka mkongojo chini akachukua kuni kutoka chini ya lile jiwe kisha akaukoleza ule moto.
Jarome alipotoka hapo aliondoka moja kwa moja hadi kwenye ofisi ya Fisrt Lady akakaribishwa na kupewa nafasi ya kukaa. Salama hakuwa na amani moyoni mwake baada ya kumuona mtu huyo kwani haikuwa kawaida kwa Jarome kufika kwenye ofisi hiyo. Tabasamu kwa mtu huyo lilikuwa adimu sana, hakuwahi kutabasamu hata siku moja mbele ya kiumbe hai huyo jamaa, labda kama huwa anatabasamu mbele ya taswira yake ya kiooni.
“Karibu sana kiongozi?” alikaribisha tena Salama akiwa na hofu kuu sasa. Alisahau kabisa kuwa yeye na huyo mtu aliyeko mbele yake, yeye ndiye mwenye cheo kikubwa kuliko huyo jamaa lakini kwa jinsi alivyokuwa akiogopa ujio wa mtu huyo akajikuta anajipa udogo.
“Ni siku tatu tu nazitoa kwako za kuhakikisha, Rais anatoa majibu sahihi kuhusu mpelelezi kutoka Tanzania. Tumekuwa hatuna raha, tumekuwa tukiwapoteza wenzetu kwa ajili yake halafu bado tusubiri tu hadi tukutanenae wenyewe. Kumbuka kuwa hata nyaraka za utajiri wa Backa hatuzijui zilipo na hatujui ni nani ametuwahi. Siku tatu kinyume na hapo Binti yako utaipokea maiti yake kutokea nchini huko mbali aliko masomoni na nitamuuwa mimi. Nadhani hujui jinsi ninavyouwa kwa ghadhabu….tatu tu kumbuka sana hilo” akamaliza kuongea kisha akanyanyuka hata ikiwa bado hajapata mrejesho kutoka kwa Salama. Macho ya first Lady yakapepesa kwa hasira kali. Eti, binti yake atauwawa kama mumewe hatasema alipomuweka mpelelezi kutokea Tanzania. Nani kasema kuwa alichokizaa hakina thamani, alichokizaa yeye kinathamani kubwa kuliko vizazi vya kadamnasi yote duniani. Mtoto wa pekee aliyempata kwa bahati nasibu leo aambiwe anasiku tatu tu za kukilinda kifo cha bahati nasibu hiyo. Au nimrejeshe nyumbani na nikae nae karibu? maana naona mwenendo wa mapigo yangu ya moyo si sawa kabisa? aliwaza Salama kisha akaamka na kusimama wima pale kwenye meza ya thamani kubwa kutokea duniani. Mabandu utakuwa unamtoto mwingine nje ya huyu binti yetu wewe? kama hauna sasa kwanini unathamini mijiwatu ambayo si damu yako na kuiacha damu yako ikiwa kwenye alama ya hatari? Alijiuliza tena mawazoni kisha akatoka kibubububu bila hata kumuaga mtu, mlinzi wake ilibidi anyanyuke haraka sana na kumkimbilia kutokana na kushtuliwa na safari isiyo rasmi.
“Atanitambua hukohuko” akasema kwa sauti hadi mlinzi wake akatamani kuuliza lakini haikuwa ndani ya kazi yake akabaki kufunga mlango wa gari baada ya kumfungulia na yeye kuzunguuka upande wa pili kisha gari ikaondolewa na dereva wake ambaye huwa hatoki garini kizembe maana anazijua safari za bosi wake zilivyo hazina kichwa wala miguu. Alipofika kwenye viunga vya Ikulu, alitoka garini hadi kwenye ofisi ya Rais. Akasimama mbele ya muheshimiwa huyo kama kizuka cha jini Subiani. Ilibidi wote waliokuwa humo ndani watoke maana walijua kuwa kinachofuata hawakupaswa kukisikia hata kwa bahati mbaya. Mlango ukafungwa kwa namba maalumu wakabaki wenyewe tu ndani ya ofisi hiyo.
“Wapi mpelelezi kutokea Tanzania umemuweka?” likawa ni swali la kwanza kutoka kwa Salama. Rais Mabandu akashtuka kwa nguvu, swali kama hilo la siri ambalo halikupaswa kuulizwa kizembe hivyo ni vipi mkewe aulize tena kishari na si mara moja wala mbili?
“Unawazimu wewe?” akasema Rais Mabandu.
“Ni sawa ninawazimu, nitukane tu hii yote najua ni jeuri ya kulewa kwa haya madaraka lakini ukumbuke wewe si wa kunitukana na hukuwahi kunitukana” akabwata Salama. Mabandu akazidi kuchanganyikiwa. Kulewa kwa madaraka? Mimi? Kwanini sasa? Na tangu lini huyu mwanamke kuongea haya? Akajiuliza Rais Mabandu kichwani mwake harakaharaka kabla hajamtazama mkewe na kusema.
“sijakuelewa mke wangu nini tatizo na haya mambo ya kuhusu mpelelezi kutokea Tanzania wewe umeyajuaje na unayatakia nini?”
“Kama firs Lady, kama mke wa Raisi, nina haki ya kujua haya yote” akasema Salama.
“Huna haki ya kujua mambo ya kiusalama, haya mambo ni ya usalama wa nchi tena unakosea sana na umenikosea sana kuingia kwenye ofisi yangu kama unaingia chumbani kwako. Umeharibu kikao cha muhimu sana kwa ajili ya mambo yako ya kipuuzi…”
“Mambo ya kipuuzi!” akaja juu kwa mshangao Salama.
“Toka ndani ya ofisi yangu kuna kikao kinatakiwa kuendelea, toka unanitafunia muda wangu bwanaaa!” akasema Rais Mabandu huku akionesha ishara ya kumtoa mkewe ambaye hakutumia utaratibu mzuri kuingia ndani mule, utaratibu wa kishenzi na yeye kama Rais ilikuwa ni aibu tupu.
“Binti yangu Vone amepewa siku tatu za kuuwawa kama hutosema kuwa huyo Jasusi wenu yuko wapi” akashtuka Mabandu lakini haukuwa mshtuko mkubwa sana wa kumuonesha mkewe. Vone amepewa siku tatu za kuuwawa kama hatatoa siri za ni wapi mpelelezi kutokea Tanzania yupo. Akawaza kisha akauliza.
“Aliyekupa haya maneno ni nani?”
“Siyo mara ya kwanza hii napewa onyo, ni mara ya pili. Sasa basi tambua kuwa binti yangu akifa, sitataka kuona ukiniletea vitoto vya pembeni, nitavikanyagakanyaga ni…..!”
“Tokaa njeee Salama, tokaaaa!” alifoka Rais Mabandu, alikuwa katika hali ya sinto fahamu hata kidogo na ukimya wake aliouweka aliona jinsi ambavyo mkewe anampanda kichwani. Salama alitoka kwa hasira sana. Rais Mabandu akabofya batani kuruhusu mlango kufunguka kisha akakaa chini kwa nguvu na kujimwaga kitini. Akashika kichwa chake kwa kuchanganyikiwa sana. Kimya kingi kinamshindo, nimekaa kimya wakaona ni mjinga nilitaka kuona kwanini huyu mwanamke hayuko upande wangu, mimi nakumbwa na matatizo lakini wala haoneshi kuguswa kwa hili? Nimegundua kitu na natakiwa kukifanyia kazi. Aliwaza kwa kina kisha akaufunga mlango kwa namba na kutulia, hakutaka kumruhusu mtu tena kwa muda huo. Aliwasha mashine fulani ndogo iliyopo pale mezani kisha akatulia. Taa ya manjano iliwaka karibia chumba kizima kwa kuzunguuka kila upande kisha ikawaka taa ya kijani. Mashine ile ikaandika kuwa Scan Complete. Hakukuwa na kitu chochote kilichokuwa kikipeleka siri nje.
Akavuta simu moja yenye rangi nyeusi kisha akabonyeza namba kadhaa na kuweka mkonga wa simu sikioni akasikiliza, baada ya muda simu ikapokelewa.
“Muheshimiwa!” sauti nzito kutokea upande wa pili wa simu ikaita.
“Mr!” Rais Mabandu naye akaita.
“Kunatatizo?” akauliza wa upande wa pili wa simu.
“Lipo ila ni la uangalizi, hakikisha binti yangu anakatisha masomo na unamuhamisha kutoka China hadi Marekani, awe chini ya ulinzi wako kuanzia sasa hadi siku nakupigia tena, sitawasiliana na wewe na siku ukiiona simu yangu, ujue ni kumrudisha tena shule si kinyume na hapo” alisema Rais Mabandu lakini moyoni mwake akigundua kuwa alifanywa mjinga siku nyingi. Walisema wamemuweka binti yake chini ya ulinzi wao lakini sasa mbona mlinzi wa binti yake leo anapokea na hakuna taarifa mbaya. Moyo wake ukamcheka sana, akaona haya kwa kutokuwa makini.
“Nakwenda kutekeleza sasa” ukajibu upande wa pili wa simu bila kuuliza kitu chochote kisha simu ikakatika. Mabandu alishusha pumzi nzito akatulia kidogo kisha akavuta simu nyingine, hii ilikuwa na rangi nyekundu na ni nadra sana kutumika simu hiyo. akagusa namba mbili tu kisha akasikiliza kwa kuiweka sikioni.
“Kuanzia leo mfuatilie first Lady hadi saluni kasoro akienda msalani tu” alitoa amri Rais Mabandu kisha akatulia kidogo na kusema kwa ukali.
“Fuata oda na si kutoa hoja” kisha akakata simu. Huu ni mtego kwao, wakijitusu tu wameumia sitajali mke wala nini sasa naingia kwenye azimio langu mwenyewe sitamhusisha mtu tena. aliwaza Mkuu huyo wa nchi kisha akaruhusu mlango uwe wazi baada ya kuhakikisha hakuwa na suala jingine tena. Binti yake alimuwekea usalama na mkewe yupo kwenye uchunguzi na hiyo ni baada ya kujikanyaga mwenyewe kwa kusema kuwa kuna watu wanampa onyo kila siku, alitaka kuwajua hao watu ni akina nani. Baada ya kuwaza sana mlango ukapiga alarm kuashiria kuwa kuna kiumbe alikuwa mlangoni.
Mitego ilitegwa na kila mmoja alikuwa katika mtego wake, Roi akitegwa kwa namna yake lakini pia yeye na kikosi chake wakiwa wanatafutwa kwa kasi kubwa sana. Dou alikuwa tayari ameshapewa jukumu zito la kuhakikisha Jasusi la kitanzania kama wao wenyewe walivyomuita, linaingia mikononi mwao.
ITAENDELEA
Hii ni Dunia au Kuzimu Sehemu ya Tano
Also, read other stories from SIMULIZI;