Siku ya Utakaso Sehemu ya Pili
KIJASUSI

Ep 02: Siku ya Utakaso

SIMULIZI Siku ya Utakaso
Siku ya Utakaso Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA: BEKA MFAUME

Simulizi: Siku ya Utakaso

Sehemu ya Pili (2)

Taarifa za kukamatwa kwa Beda zikamfikia Husna, naye akawasiliana na maafisa wa jeshi la polisi aliokuwa akijuana nao, wakamthibitishia kuwa ni kweli Beda amekamatwa na akatajiwa kituo kimoja cha polisi ambako kwa muda huo angeweza kuwepo. Lakini wakamshauri kuwa, asipate tabu ya kumtafuta kwani asingeweza kumwona kwa vile bado yuko chini ya uchunguzi. Ushauri mwingine wa kumwumiza aliopewa ni kuwa, isingekuwa vyema kwa muda huo kujishughulisha kabisa na suala la Beda, kwani lingeweza kumletea matatizo kutokana na uzito wa shitaka lenyewe lilivyo.

Husna naye akachanganyikiwa na ushauri huo wenye vitisho vya kumtisha. Alikuwa na uhakika kuwa, Beda hakuhusika kabisa na kumwua Himidu, na amekamatwa kama kafara kutokana na kutapatapa kwa jeshi la polisi. Uhakika aliokuwa nao kuwa, Beda hahusiki na mauaji ya Himidu ni kutokana na jinsi Beda alivyokuwa akimwongoza vizuri katika mbinu za kumdhibiti Himidu kimapenzi kuhakikisha anamtumia mheshimiwa Waziri huyo kugawa sehemu ya utajiri wake kwa Husna. Ni yeye Beda aliyemshauri kuukataa ushauri wa Himidu wa kutaka kumnunulia nyumba, badala yake Beda akamshauri amwambie Himidu amjengee nyumba. Himidu akakubali kumjengea nyumba, Husna akatafuta kiwanja cha ekari nne eneo la Bunju, Himidu akapelekwa kwenye kiwanja hicho na kukubali kukinunua kwa jina la umiliki wa Husna. Beda huyo huyo tena akamshauri kuwa, Himidu atumike kukisajili kiwanja hicho kipate hati baada ya kununuliwa kikiwa ni shamba. Himidu akaambiwa, kiwanja kikapata hati.

Ni Beda ndiye aliyehangaika kuutafuta mchoro wa nyumba itakayojengwa. Akaupata mchoro wa nyumba iliyokwisha jengwa huko nchini Spain kwenye fukwe ya bahari na kumtaka Husna autumie kuijenga nyumba hiyo ya kifahari huku gharama za mchoro huo na gharama za ujenzi vikimuangukia mheshimiwa Himidu. Isitoshe, Beda ndiye aliyemshauri Husna ahakikishe Himidu anamfungulia akaunti kwenye benki tofauti zenye pesa lukuki, jambo ambalo lilifanikiwa. Kitu pekee ambacho Husna alikitoa kwenye mawazo yake kumshauri Himidu ni wazo la kufunguliwa biashara ya duka la nguo ambalo liko katikati ya jiji.

Beda akiwa ni mshauri wake mkuu kwenye masuala yake kimaisha na namna ya kumdhibiti Himidu kimapenzi na wakati huo huo licha ya Beda kufaidika kwa kumpa penzi lake kwa njia ya siri, bado Beda huyo huyo alikuwa akifaidika mno na kukirimiwa kwa kila gharama ya kilichomgharimu kwa kulipiwa na Husna. Siku chache tu kabla ya kifo kumkuta Himidu, Beda alimwomba Husna amnunulie gari dogo la kutembelea. Husna akamwomba Beda afanye subira ili atafute mbinu ya kumwingia Himidu anunue gari hilo, hakuona sababu ya yeye kutumia fedha zake kununua gari hilo wakati buzi Himidu yupo. Kabla ya Husna hajaliingiza ombi hilo kwa Himidu, Himidu akauawa kwa kupigwa risasi!

Beda atahusika vipi kumwua Himidu wakati alikuwa akisubiri kununuliwa gari? Husna alijiuliza kwa lengo la kupingana na kitendo cha Beda kukamatwa na kuhusishwa na mauaji ya Himidu. Akaapa kumwokoa Beda kwa kila hali! Naye akamtafuta wakili wake na kumpigia simu ili aifuatilie kesi ya Beda!

**HUSNA anamtafuta wakili ili kumwokoa Beda kitanzini…… je? Atafanikiwa na ni nani aliyefanya mauaji na kwa nini???

Siku ya pili asubuhi, Beda hakupelekwa hospitali kama ilivyostahili iwe kutokana na afya yake ilivyokuwa. Badala yake alihamishwa kutoka kituo cha polisi cha darajani na kupelekwa kituo cha polisi cha Chambuzi huku ikitumika timu ya Nunda kumuhamisha. Hali yake ya afya ilizidi kudorora kadri ya muda ulivyokuwa ukienda na mateso aliyoyapata yalimfanya ashindwe kutembea mwenyewe, uso na macho vilimvimba na kushindwa kuona vizuri. Sehemu ya mgongoni kulikuwa na alama za vichapo zilizoacha vidonda na kufuatiwa na vidonda vingine vilivyokuwa bado vibichi kwenye ugoko wa miguu yake yote miwili. Nyayo zake zote mbili zilikuwa na uvimbe uliotakana na kipigo.

Alipofikishwa kituo cha Chambuzi, hakupelekwa kwenye mahabusu ya wote, badala yake alichukuliwa na kuingizwa kwenye chumba maalumu cha mahojiano. Chumba hiki kilikuwa tofauti na vya awali, humo kulikuwa na meza pamoja na viti viwili vitatu. Beda akakalishwa kwenye kiti kilichokuwa karibu na meza kwa ajili ya kupata mhimili wa kuuegemeza mwili wake.

“Tutajie wenzako ulioshirikiana nao,” Nunda alimwambia Beda mara baada ya kukalishwa kwenye kiti.

Hoja hiyo ya Nunda ikawa imemchanganya Beda. Alijua akisema hana washiriki alioshirikiana nao, kichapo kitamrudia tena; na akisema anao; hajui atawataja akina nani! Badala ya kuifikiria kuijibu hoja ya Nunda, Beda akaanza kuwafikiria walioko nje kama wanazo taarifa za kukamatwa kwake. Pamoja na kulifikiria hilo, bado aliuona ugumu kwa ndugu na jamaa zake kuweza kumfuatilia kwa haraka kabla hajafa kwenye mikono ya polisi kutokana na mateso anayopewa kwa kosa ambalo hakuhusika nalo kwa njia moja au nyingine. Akatamani Mungu aweke uwezo wake ili taarifa za kukamatwa kwake ziweze kumfikia Husna haraka. Alijua kuwa, endapo Husna atazipata taarifa za kukamatwa kwake, Husna lazima angelazimika kufanya juhudi zote za kuhakikisha anaachiwa au aendelee kukaa ndani kusubiri upelelezi bila ya kupewa mateso mengine!

Akiwa katikati ya fikra hizo, Nunda akamshitua tena kwa kumuita, “Wewe!”

Beda akashituka, akamwangalia Nunda kwa macho yaliyojaa uwoga na kudhihirisha alikuwa akimwogopa Nunda kwa wakati huo kuliko hata Mungu! Alikwisha kumsahau Mungu, akawa anamwona Nunda ndiye aliyeikamata roho ya uhai wake.

“Nimekwambia nitajie majina ya wenzako ulioshirikiana nao!” Nunda alimkumbusha kwa kuikaza sauti yake.

Beda hakujua aanze kwa kumtaja yupi. “Afande,” alisema kwa sauti iliyopwaya huku akionyesha kwa dalili zote kutaka aaminiwe na aonewe huruma. “Kweli mimi sihusiki na mauaji ya mheshimiwa Himidu.”

Jibu hilo likaonyesha dhahiri kumwudhi Nunda ambaye kwa sekunde kadhaa aliganda akimwangalia Beda kama vile alikuwa akitamani aikamate shingo ya kijana huyo na kuisokota! “Nataka nikwambie kitu kimoja,” Nunda alisema huku akionekana kuidhibiti hasira yake. Aliyatoa matamshi yake kwa umakini kama sehemu ya msisitizo wa kumtaka Beda aitulize akili yake na asikilize vizuri anachoambiwa. “Rais wa nchi ameturuhusu kuua! Achana na propoganda za tume za kimataifa za haki za binaadamu zinazowadanganya kuwa, polisi hawaruhusiwi kutesa au kuua! Na ndiyo maana husikii tukashitakiwa kwa mauaji ya watuhumiwa wanaokufa kutokana na mateso wakiwa kwenye mikono ya polisi, labda kutokee kuwe na ushahidi mzito ambao utathibitisha kuwa, polisi walihusika na mauaji. Vinginevyo, hakuna kitu kama hicho! Mnapokataa kukiri tuhuma mnazotuhumiwa mkiwa chini ya ulinzi wa polisi, huwa tunawatesa mpaka mkiri, bila ya kujali kama unahusika. Lakini nataka utambue kuwa, yoyote anayekamatwa kwa tuhuma na kuletwa kituoni akawa chini ya ulinzi wa polisi kwa ajili ya kufanyiwa upelelezi, kwetu sisi tunamchukulia kuwa, anahusika na tuhuma anazotuhumiwa. Kutopatikana kwa ushahidi kwamba mtuhumiwa hahusiki na kosa alilotuhumiwa, mara nyingi huwa si kazi yetu. Kazi hiyo hufanywa na ndugu zenu walioko nje ambao hututafuta na kukata kitu kidogo kwetu, kitu hicho kidogo ndicho kinachoandika kuwa, mtuhumiwa hahusiki na makosa aliyotuhumiwa na tunamwachia huru, vinginevyo unakufa! Hakuna askari mwenye huruma na hiyo ndiyo maana ya kuitwa askari au kwa jina jingine, mpiganaji! Kwa hiyo, sisi kazi yetu huwa ni moja, nayo ni kutesa mpaka ukiri kuhusika na tuhuma zinazokukabili na ikitokea bahati mbaya ukifa kwenye mikono yetu huwa tunaandika ripoti yoyote ya uwongo. Tunaweza hata kukusingizia ulikuwa unaumwa na ripoti yako huwa inathibitishwa na daktari kuwa, umekufa kwa ugonjwa fulani! Ndiyo maana hatushitakiwi!” Nunda alinyamaza na kumwangalia Beda kwa utulivu. Kisha kwa upole akasema, “Naomba unitajie wenzako ulioshirikiana nao. Ukinitajia, nakuahidi kukuachia huru. Uamuzi ni wako!”

Kimya kikakita kati yao, Nunda akimwangalia Beda, Beda akiwa amekiinamisha kichwa chini, akijiuliza awataje akina nani ili ayaokoe maisha yake!

“Muhsin..!” Beda alianza kuwataja marafiki zake mmoja baada ya mwingine na kufikia wanne huku akijua fika kuwa anawaingiza kwenye matatizo makubwa! Lakini angefanya nini na yeye anataka kuyaokoa maisha yake!


Kukamatwa kwa Muhsin na wenzake wengine waliotajwa na Beda kukawa kumewashitua watu wanaowafahamu. Wengi wao walisema wazi wazi kuwa, waliokamatwa wameonewa na wakatoa sababu za kuonewa kwao. Moja ya sababu walizozitoa zilifanana kimazingira kwa kila upande ukidai kwamba, muda aliouawa mheshimiwa Himidu kati ya mmoja wa waliokamatwa au wawili wao hawakuwa katika eneo la mauaji na ushahidi huo ulikuwepo! Lakini kutokana na taratibu za polisi au pengine kwa kanuni zao au sheria walizonazo, hawafanyi taratibu za kufuatilia mahojiano wanayoyafanya na watuhumiwa wao pale swanapolalamika kuwa, muda wanaotuhumiwa kuyatenda makosa wanayotuhumiwa nayo wao hawakuwa kwenye eneo husika kwa muda huo na wakati mwingine hutaja hata watu waliokuwa nao ili ikiwezekana polisi wawafuatilie kuwahoji watu hao, lakini katu huwaoni polisi wakihangaika kuifanya kazi hiyo ambayo ingewasaidia angalau kupata picha halisi ya mtuhumiwa waliyemkamata kama angekuwa anahusika na tuhuma, badala yake wao hutumia njia ya mkato kwa kumpa kisago mtuhumiwa mpaka akiri kuhusika kama inavyomtokea Beda chini ya kachero Nunda!

Mmoja wa walioupata mshituko huo wa kukamatwa kwa Muhsin ni Husna! Hali hiyo ikamtia kigugumizi cha kufikiri na kujikuta akitaka kuamini kuwa, mauaji ya Himidu yangeweza kufanywa kwa ushirikiano wa Beda na Muhsin. Lakini wazo hilo halikuweza kumwingia kirahisi. Akaanza kwa kujiuliza; Kwa nini wamwue Himidu? Kwa kutaka nini? Beda atakuwa alikuwa akimwonea wivu Himidu? Ndio akamshauri Muhsin wamwue? Husna akaamua tukio hilo alifanyie kazi ili azipate habari za uhakika. Akaanza kuwatafuta maofisa wa polisi waliomwonya kuhusu kukamatwa kwa Beda ili wampe taarifa za ndani kuhusu sakata hilo linalomchanganya akili.

Husna akazipata taarifa zilizomchanganya kutoka kwa maafisa hao, taarifa ambazo zilimrudisha nyumbani kwake na kukita kilio kilichoendana na kusema peke yake, “Beda nilikupa kila kitu ulichokitaka si kwenye mwili wangu tu, hata ulichokuwa ukiomba nikununulie, nilikununulia bila ya kujali uzito wa gharama. Kumbe mwenzangu ulikuwa na lako jambo…leo unakuja kuniulia Himidu wangu..!”

Alikuwa bado akizikumbuka taarifa alizokuwa amepewa na maofisa wa polisi, taarifa zilizomjulisha kuwa, Beda alikuwa amekiri kuhusika na mauaji ya mheshimiwa Himidu kwa maelezo yake mwenyewe kimaandishi aliyoyawekea saini yake na alama ya dole gumba. Husna akathibitishiwa tukio hilo kwa kuonyeshwa stetimenti aliyoisaini Beda kuhusika na mauaji hayo. Pia, akataarifiwa kuwa, kukamatwa kwa Muhsin na wenzake wengine kumetokana na Beda kuwataja watu alioshirikiana nao kumwua Himidu!

Husna alijikusanya tena na kuivuta pumzi kwa nguvu kisha, akaitoa kama mtu aliyeutua mzigo kutoka kichwani. Akaiangalia simu iliyokuwa ipo kando yake kwenye kitanda alichokalia. Akaichukua na kuanza kulitafuta jina la Wakili aliyempa kazi ya kufuatilia suala la Beda, akampata na kumpigia.

“Usiendelee na kesi ya Beda, nimeamua kujitoa!” Husna alisema.


Siku moja baada ya kumwarifu Wakili wake ajiondoe kwenye kesi ya kukamatwa kwa Beda, asubuhi iliyofuata Husna akiwa amevaa mavazi meusi yanayoashiria kuwa, yupo kwenye msiba na akiwa anajiandaa kutoka, aliisikia simu yake ya mkononi ikiita. Aliitoa simu kutoka kwenye mkoba wake wa begani wakati ikiendelea kuiita, akaitazama kwenye kioo na kuliona jina la Pius ambaye ni kaka yake Beda.

“Nataka kukuona shemeji,” Pius alisema kwenye simu.

“Asubuhi hii hii?” Husna aliuliza.

“Ndiyo.”

“Basi tuonane kwenye mgahawa wa Fernandies kuanzia saa nne.”

“Nitakuja.”

Wote wakakata simu zao.

Mgahawa wa Fernandies upo katikati ya jiji na una umaarufu wa kuwa na wateja wenye kufanana kimapato ambao fikra zao hutawaliwa kwa kujiona ni wabora fulani kijamii, wengi wao wakiwa kama watumishi wa benki, watumishi wa kwenye makampuni makubwa yenye kulipa mishahara minono na wafanya biashara wenye kujua kuhangaika. Mgahawa huo ambao muda wote hutumia kiyoyozi chenye kufanyiwa huduma kwa muda wake maalumu na kutopoteza nguvu yake ya kupuliza ubaridi ulikuwa ukitumika kama eneo la kukutana kwa watu wa jamii hiyo na kuzungumza mambo yao. Wengi wao walipenda kuzungumza kwa kuchanganya kiswahili na kingereza au kuzungumza kingereza kitupu. Watu wengine ambao hawamo kwenye kundi hilo la wenye uwezo hawakutaka kabisa kuingia kwenye mgahawa huo kununua chochote kutokana na bei zake kuwa ghali. Ukawa ni mgahawa wa watu maalumu.

Husna aliingia kwenye mgahawa huo akiwa amechelewa dakika kumi. Na mara alivyoingia aliyazungusha macho yake kwenye meza zilizomo humo huku akitarajia kumwona Pius kwa kuamini kuwa, muda aliokwisha kuchelewa ungekuwa umemfanya Pius awe amekwishafika. Alimwona Pius akimnyooshea mkono kumwonyesha alipokaa. Husna akaenda alipokuwa amekaa Pius.

“Utakula au kunywa nini?” Pius alimwuliza Husna huku yeye mwenyewe akiwa na glasi kubwa ya juisi iliyotumbukizwa mrija.

“Bado sijanywa chai,” Husna alisema. Akamwita mhudumu na kumwagizia alivyovihitaji ambavyo vilikuwa ni fried eggs, slice of cheese, toast, sausage, glasi ya juisi na chai.

Pius ambaye sura yake ilishabihiana kwa kiasi fulani na mdogo wake, naye alikuwa ni jamali wa sura kama alivyo Beda. Yeye alikuwa ni mrefu kidogo kuliko Beda na alikuwa na kitambi kisichomchukiza. Alikuwa mtanashati kama Beda na alifuga sharubu zilizompendeza na mwenyewe alipenda kuziita kwa jina la diplamatic moustache kutokana na kuzipa huduma ya kila wiki kwa kwenda kwa kinyozi wake aliyemchagua. Kinyozi huyo ndiye aliyekuwa akizinyoa nywele zake ambazo nazo pia alizikata kwa kila wiki na kuonekana kuwa ndogo wakati wote. Pius alikuwa ni mkaguzi wa mahesabu kitaaluma na ni mwajiriwa kwenye kampuni ya kigeni yenye matawi yake Nairobi na Kampala. Wakati mdogo wake akikamatwa, yeye alikuwa yuko Kampala na alipewa taarifa za kukamatwa kwa mdogo akiwa huko.

Akiwa amewasili jijini Dar es Salaam siku moja nyuma, Pius alikuwa aende Tanga siku iliyofuata ili akaonane na wazazi wake pamoja na ndugu zake wengine ili kuujua mkasa mzima wa kukamatwa kwa Beda ulivyokuwa pamoja na kwamba alivyokuwa Kampala aliweza kuwasiliana nao kwa simu kuhusiana na tukio hilo.

Ingawa aliipanga safari ya kwenda mjini Tanga siku hii ambayo anaonana na Husna, aliamua kuichelewesha kwa kubadilisha muda ili aweze kuonana na Husna waweze kulizungumzia tatizo la kukamatwa kwa Beda ili angalau apate mwanga wa kuyalinganisha atakayoyasema Husna na yale aliyoambiwa na ndugu zake kwenye simu.

Pius hakuwa karibu sana na Husna pamoja na kwamba alikuwa akiujua uhusiano wa mapenzi kati ya mdogo wake na yeye Husna. Uhusiano huo ndio uliofanya kuwe na dosari kati yao kutokana na yeye kumshawishi mdogo wake aachane na Husna baada ya kugundua kuwa, wakati Husna akitembea na mdogo wake, lakini pia wakati huo huo alikuwa na uhusiano mwingine wa kimapenzi na mheshimiwa Himidu. Pius alihofia maisha ya mdogo wake yangekuwa hatarini endapo kama mheshimiwa huyo angeugundua uhusiano ulioko kati ya Husna na Beda. Hata hivyo, baadaye aligundua kuwa, Beda alikuwa haufuati ushauri wake. Aligundua hivyo baada ya Beda kuanzisha tabia ya kumkwepa mara kwa mara kila alivyotaka kuonana naye na kutambua kuwa, kilichokuwa kinamfanyisha awe hivyo ni kule kuendelea kwake kufanya mapenzi na Husna.

Husna alimfahamu Pius kwa kufahamishwa na Beda siku ambayo walikwenda nyumbani kwa Pius eneo la Upanga kwa ajili ya kumtembelea. Baada ya utambulishi huo, Beda na Husna wakaanza kumtembelea Pius mara kwa mara na wakati mwingine kula chakula cha pamoja hasa cha jioni. Lakini baada ya muda, Pius akatambua kuwa, Husna ni kimada wa Waziri wa Miundo Mbinu mheshimiwa Himidu na hapo hapo akampa onyo mdogo wake kuwa aachane na Husna! Kuanzia hapo mawasiliano yao yakaanza kupotea na wakawa wanaonana mara moja moja katika mitaa ya katikati ya jiji na kila walivyokuwa wakionana, Husna alimpa Pius heshima inayostahili na Pius aliipokea na kuijali. Pamoja na hilo kuendelea kuwepo, lakini Pius hakugusia lolote kuhusu kuadimika kwao. Ingawa Pius hakutokea kuligusia hilo, lakini kila mmoja kati yao alikuwa akiifahamu sababu ya kuadimika huo. Ufahamu huo ulikuja kutokana na macho yao yalivyokuwa yakizungumza kila walivyokuwa wakikutana, macho ya Husna yakimwambia Pius kuwa, ‘Najua kama unamkataza mdogo wako asiwe na uhusiano na mimi!’ Hali kadhalika macho ya Pius nayo yalikuwa yakimwambia Husna kuwa, ‘Najua kama unajua kwamba, ninamkataza mdogo wangu asiwe na wewe.’ Kila mmoja akaamua kubaki na uelewa wake huo huku Pius akiwa mwangalifu wa kutozidadisi habari za Beda kila walivyokutana.

Lakini kwa suala hili la kukamatwa kwa Beda, Pius alijiona akiuvunja mwiko huo wa kutozidadisi habari za Beda kutoka kwa Husna kwa kuamua kuchukua hatua hiyo ya kumwomba waonane!

“Pole na matatizo,” Pius alimwambia Husna aliyekuwa ameanza kujikorogea chai.

“Nimeshapoa. Na wewe pole,” Husna alijibu.

“Ahsante,” Pius alisema na kuamua kwenda moja kwa moja kwenye lengo alilokusudia kumwona nalo Husna. “Husna, nataka moja kwa moja tuzungumzie suala la kukamatwa kwa Beda. Alikuwepo hapa dar siku aliyouawa mheshimiwa Himidu?”

“Hakuwepo. Aliniaga siku tatu nyuma kuwa, anakwenda Tanga.”

“Akiwa yuko Tanga mlikuwa mkiwasiliana kwa simu?”

“Mara nyingi tulifanya hivyo.”

“Lakini bado amekamatwa kwa kuhusika na kifo cha mheshimiwa Himidu!” Pius alisema na kusikitika peke yake. “Wewe unalichukuaje hilo?”

“Hata mimi lilinishangaza mara ya kwanza.”

“Mara ya kwanza? Una maana gani?”

“Niliamini Beda hahusiki na kumwua Himidu,” Husna alisema wakati akikata sausage, akakitia mdomoni kipande alichokikata na kutafuna. Hakuonekana kutaka kuongeza neno.

“Uliamini hahusiki?” Pius aliuliza baada ya kumwona Husna kutomalizia alichokuwa anataka kukizungumza.

Husna alitingisha kichwa kulikubali swali Pius kisha, asiseme neno.

“Baadaye ikawaje?

“Niliamini.”

“Kwamba?” Pius aliuliza huku akionyesha udadisi wa kuichunguza tabia ngeni yenye kiburi iliyokuwa ikifanywa na Husna. Hakujua kwa nini Husna alikuwa akiifanya tabia hiyo kwake. Labda ni kwa ajili ya kumkataza Beda… aliwaza.

“Amehusika na kumwua Himidu!” Husna alisema.

Pius akapaliwa na juisi aliyokuwa anakunywa! Akakohoa na kuonekana kuitafuta pumzi.

“Pole,” Husna alisema huku akimwangalia Pius aliyekuwa akiendelea kukohoa.

“Ahsan..te,” Pius alijibu na kukohoa tena. Hatimaye akajiweka sawa na kujifuta machozi kwa leso huku macho yake yakiwa yameanza kuwa mekundu. Akamwangalia Husna. “Una uhakika na unalolisema?” aliuliza na kujikohoza tena kusafisha koo lake.

“Ninao uhakika,” Husna alisema kwa kujiamini.

“Upi?”

“Ni Beda mwenyewe ndiye aliyekubali kuhusika na mauaji…”

“Umejuaje?” Pius aliuliza kwa haraka na kumkatisha Husna.

“Nimeshuhudia kwa kuiona stetimenti yake aliyokiri na ina saini yake pamoja na alama ya dole gumba lake!”

Pius hakujibu. Akaonekana kuvuta fikra. “Haya mambo yanachanganya,” hatimaye alisema. “Nimezungumza na mtoto wa dada yangu kwenye simu wakati nikiwa Kampala, ameniambia kuwa, siku na muda ambao mheshimiwa Himidu ameuawa, yeye na Beda walikuwa kwenye sherehe ya harusi ya rafiki wa mtoto wa dada yangu iliyofanyika barabara ya saba na amenihakikishia kuwa hata picha walizopiga wakiwa pamoja anazo! Sasa na wewe hapa unaniambia kuwa Beda amekiri kuhusika na mauaji ya Himidu! Sielewi!”

Kauli ya Pius ikamfanya Husna asite kuendelea na kifungua kinywa alichokuwa anakula, akamwangalia Pius huku sura yake ikipigwa na butwaa. “Anasema na picha walizopiga pamoja anazo?” aliuliza.

“Hivyo ndivyo alivyoniambia. Na huyu mtoto wa dada yangu hawezi hata kidogo kunidanganya!” Pius alisema huku akionyesha msisitizo kwenye kauli yake. Kisha kwa sauti ya taratibu akasema, “Nina wasiwasi Beda atakuwa ameteswa na atakuwa amekiri kwa sababu ya kipigo. Ndivyo walivyo polisi wetu, mbinu yao kubwa ya kuhoji ni kuwatesa watuhumiwa na mtuhumiwa akiendelea kukana anaweza akafa kwa kipigo. Kwa vyovyote, Beda atakuwa amekiri kwa kuhofia kipigo. Ni nani ambaye amekwisha kumwona Beda tokea alivyokamatwa?”

“Polisi walikuwa hawaruhusu kumwona,” Husna alijibu. Kiburi alichokuwa akikionyesha awali kilianza kutoweka. “Leo asubuhi Wakili wangu alikuwa amepanga kwenda kumwona kwenye mahabusu aliyowekwa, hata hivyo nilimzuia asiende.”

“Kwa nini?”

“Baada ya kuiona stetimenti hiyo nikaona hakuna haja kwa Wakili kuendelea na kesi!”

Pius akaziparaza nywele zake kwa kupitisha mkono juu ya kichwa huku akiwa ameuinamisha uso. Alionekana kuchanganyikiwa! Hatimaye aliuinua uso wake na kumwangalia Husna. “Naona stetimenti uliyoiona ilikufanya umchukie ghafla Beda?” alisema.

Akiwa anamwangalia Pius usoni, Husna alitingisha kichwa kukubali bila kutamka lolote. Alikuwa akilengwalengwa na machozi na sura yake akiwa ameikunja kujizuia asilie.

“Naomba uendelee kumwekea Beda, Wakili wa kumsimamia kesi yake. Tunaweza tukampoteza kama masihara!” Pius alisema.

“Nitaongea na Wakili aendelee na kesi,” Husna alisema na kuonekana akiwa ameishiwa hamu ya kuendelea na kifungua kinywa chake huku mayai aliyoyaagiza yakionekana kutokuguswa kabisa.

“Fanya haraka kumpigia na leo hii hii aende mahabusu akamwone. Nina wasi wasi Beda anaweza akawa yuko kenye hali mbaya kiafya. Ni Wakili pekee ndiye anayeweza kulazimisha amwone na ni yeye pekee ndiye anayeweza kulazimisha Beda apelekwe mahakamani. Akipelekwa mahakamani itasaidia kwani hatarudi tena kwenye mahabusu za vituo vya polisi, hilo litamsaidia kutoendelea kuteswa. Akipelekwa mahakamani atasomewa shitaka lake, kesi yake itaahirishwa na atapelekwa kwenye mahabusu za magereza ambako watuhumiwa hawateswi na atakuwa ameokoka na kipigo. Tutakapolifanikisha hilo itabidi tushughulike na upande wa pili ambao ni kucheza na mahakama ili kesi iweze kuzungumzwa haraka, vinginevyo atasahaulika kwa kusota mahabusu. Naujua urasimu wa mahakimu wetu na naujua ukatili wa polisi wetu, hakuna hata mmoja atakayejali muda wa kusota kwa Beda gerezani!”

“Nampigia sasa hivi!” Husna alisema na kuitoa simu yake.

“Wewe endelea kumpigia simu, mimi niache niondoke. Nakwenda Tanga sasa hivi ili kesho nirudi nikiwa na picha walizopiga kwenye harusi, huu utakuwa ni ushahidi mzuri wa kumpelekea hakimu. Nina imani hakimu atachukua hatua ya kumwachia huru Beda. Vinginevyo, kama hakimu naye ataleta gozi gozi nitakuwa tayari kumvaa hata DPP na kumpelekea ushahidi huo!” Baada ya kusema hivyo, Pius alikivuta kiti nyuma na kusimama. Akatoa pochi na kuchomoa noti zinazotosha kufidia gharama za matumizi ya vitu walivyotumia na kuziacha juu ya meza kisha, akaondoka na kuahidi kuwasiliana na Husna kabla ya siku inayofuata.


Wakati Pius akiingia kwenye basi linalosafiri kwenda Tanga ambalo ilibidi akate tiketi muda mfupi kabla ya kupanda, Husna alikuwa bado hajapata mawasiliano na Wakili wa kuisimamia kesi ya Beda. Mara zote alizokuwa akimpigia, alikuwa akipata majibu yanayomwelewesha kuwa, simu anayoitaka haipatikani. Husna akaiweka dhana huenda Wakili huyo atakuwa yupo mahakamani akiwa anaendesha kesi au atakuwa yuko kwenye kikao na imemlazimu aizime simu yake.

Husna alimpata Wakili huyo wakati Pius akiwa kilomita kadhaa akielekea mkoani Tanga na ilikuwa imeshapita saa nane mchana. Alichokifanya Husna baada ya kumpata Wakili aliyekuwa akimtafuta ni kumwomba msamaha kwa uamuzi aliompa jana na kujaribu kumshawishi kumrudisha tena kwenye kesi ya Beda.

Mwanasheria ni Mwanasheria, mara Wakili huyo alipoombwa kurudi tena kwenye kesi hiyo ya Beda, akaamua kumpa adhabu Husna kwa usumbufu aliompa. Akaongeza kima cha ada, tofauti na kile kilichokuwa awali. Husna akakubaliana nacho baada ya juhudi zake za kulalamika kutokana na kupandishiwa huko kugonga mwamba. Husna akamtaka Wakili huyo aende kwenye kituo cha polisi alichowekwa mahabusu Beda ili akamwone baada ya kuonyesha wasiwasi kuwa, huenda akawa ameteswa na pengine yuko kwenye hali mbaya.

Jina kamili la wakili huyo ni Mustapha Feruzi, lakini alijulikana sana kwa kuitwa, Wakili Feruzi. Ni mrefu wa kimo na mwenye mwili mwembamba. Kwa yeyote mwenye kujua kukadiria umri asingesita kumkadiria miaka yake baada ya kumwona. Alionekana kuwa na umri wa miaka hamsini, ingawa umri wake halali ni miaka hamsini moja. Alikuwa ni mmoja wa mawakili wenye tabia ya ujivuni kutokana na kujiamini kwake, tabia hiyo ilikuwa ikidhihirisha umuhimu wake wa kufuatwa na wateja wengi kutokana na kesi nyingi alizokuwa akiziendesha mahakamani, wenye kufikiri mambo wakamwekea mashaka huenda anakula na mahakimu.

Ilikuwa jioni ya saa kumi na moja wakati Feruzi alipojiunga na misururu mirefu ya magari yaliyopo barabarani akielekea kwenye kituo cha polisi alichokuwa amewekwa Beda mahabusu. Aliwasili kituoni hapo saa kumi na mbili na ushehe baada ya kusota kwenye foleni kwa kipindi chote hicho.

Alijitambulisha kwa askari aliowakuta kituoni kisha, akaomba kuonana na mteja wake.

“Hutoweza kumwona,” Mkuu wa zamu wa kituo alimwambia.

“Nadhani nimejitambulisha kwenu mimi ni nani. Kisheria ninayo haki ya kumwona mteja wangu. Unaweza ukanipa sababu yoyote ya kuniridhisha nisimwone mteja wangu?” Feruzi alisema.

“Njoo kesho asubuhi utamwona.”

“Kwa nini isiwe sasa hivi?”

“Mkuu wa kituo ametoa maagizo kuwa yeyote atakayetaka kuonana na mtuhumiwa inabidi amwone yeye. Hayo ni maagizo yake na siwezi kwenda kinyume na maagizo yake, kama angekuwepo ningekuruhusu ukamwone kwanza, lakini hayupo. Kesho asubuhi atakuwepo, ndio maana nimekushauri uje asubuhi.”

“Siwezi kukuahidi muda ambao ningeweza kuja kwa hiyo kesho kutokana na kutakiwa mahakamani. Ni nani mwenye jalada la kesi?”

Mkuu huyo wa zamu akavunga kuangalia kwenye jalada lenye kumbukumbu za watuhumiwa lililokuwa juu ya meza ya kaunta. Aliporidhika akalifunga na kumwangalia Feruzi. “Kesi yake anayo afande Benardicto wa Central polisi.”

“Namfahamu,” Feruzi alisema. “Nitakwenda kumwona, nataka mteja wangu apelekwe mahakamani haraka iwezekanavyo!” Baada ya kusema hivyo, Feruzi alitoka bila ya kuaga.

Ilikuwa ni jeuri ya uanasheria!


Husna aliwasiliana na Feruzi na kufahamishwa ilivyoshindikana kumwona Beda. Akaondolewa wasiwasi kuwa asiwe na mashaka na aweke uvumilivu mpaka siku inayofuata na Feruzi kumuhakikishia kuwa atahakikisha anafanikiwa kumwona Beda na kuweka msukumo wa Beda kupelekwa mahakamani ndani ya siku mbili zijazo, vinginevyo atachukua hatua za kisheria dhidi ya polisi kwa kuendelea kumuweka mteja wake mahabusu bila ya kumfikisha mahakamani. Husna akaridhika na juhudi zilizofanywa na ahadi aliyopewa na Feruzi na kukubaliana wawasiliane siku ya pili.

Usiku Husna alipigiwa simu na Pius.

“Nimezipata picha alizopiga Beda akiwa kwenye harusi,” Pius alisema kwa sauti iliyochangamka. “Isitoshe nimepata ushahidi mwingine unaothibitisha zaidi kuwa, bwana mdogo hakuwepo Dar es Salaam wakati Himidu akiuawa. Kesho asubuhi narudi Dar es Salaam nikiwa na ushahidi wote. Washenzi hawa wanataka kumbambikia bwana mdogo kesi ya mauaji!

Husna naye akionekana kufurahishwa na habari hizo, akamwelezea Pius kuhusu juhudi zifanywazo na wakili Feruzi na hatua alizofikia.

“Tutampa ushahidi wote ili aufanyie kazi. Nina imani hata yeye ataridhika na juhudi zetu. Isitoshe na huku nako walikwisha kumtafuta wakili wa kuisimamia kesi ya Beda, lakini kwa bahati nzuri walikuwa bado hawajampa malipo ya awali kwa ajili ya kunisubiri mimi. Nimewaomba wafanye subira kwanza ili tumwache Wakili wako aendelee yeye na kama kutakuwa na ulazima wa kumwongezea Wakili mwingine basi tutafanya hivyo. Wamenikubalia kwa hilo.”

“Uliwafahamisha kuhusu utiaji saini wa Beda kwenye stetimenti ya polisi?” Husna aliuliza.

“Hapana, hilo sikuwaeleza. Lingewachanganya!”

“Umefanya vizuri.”

“Kwa hiyo kesho…nikifika nitakujulisha.”

“Sawa shem. Safari njema.”

“Nawe usiku mwema.”

“Nawe pia.”

Saa 5:25 asubuhi, Husna akiwa dukani kwake alipigiwa simu na Feruzi.

“Nataka tuonane haraka iwezekanavyo!” Feruzi alisema.

Kitu cha kwanza kilichomshitua Husna ni sauti ya Feruzi. Haikuwa sauti yenye kujiamini kama alivyoizowea kuisikia kila walivyokuwa wakiwasiliana. Ilikuwa ni sauti iliyoonyesha kukosa furaha na iliyopwaya. Kuna nini? alijiuliza.

“Kuna lolote lililotokea?” Husna aliuliza huku akijaribu kuifanya sauti yake ionekane ni ya kawaida. Hata naye alikwishaingiwa na wasiwasi.

“Unaweza ukaja hapa mahakama ya Kisutu sasa hivi?” Feruzi alisema na sauti yake ilionyesha msisitizo.

Msisitizo huo ukanaswa na Husna! Beda atakuwa amekiri ameua mbele ya Feruzi? Husna alijiuliza. “Nakuja sasa hivi!” alimwambia Feruzi na hapo hapo kuanza kumwachia maagizo msaidizi wake wa dukani.

Ilimchukua dakika chache kufika mahakama ya Kisutu. Mara baada ya kufika alimpigia simu Feruzi kumjulisha kuwa amekwisha wasili. Feruzi alimwendea Husna sehemu aliyokuwepo na wakati alipomkaribia, Husna akajaribu kuusoma uso wa Feruzi, lakini kitendo chake hicho kikashitukiwa na Feruzi. Feruzi akamkabili Husna kwa kuuweka uso wake katika hali ya kawaida.

“Twende tukazungumzie ofisini,” Feruzi alisema na kumwongoza Husna kwenye ofisi zilizomo kwenye mahakama hiyo.

Husna ndiye aliyeanza kukaa kwenye kiti alichokaribishwa na Feruzi kisha, Feruzi akatoka na kumuacha humo ofisini kwa takribani dakika tano ndipo aliporudi.

“Samahani kwa kukuacha peke yako,” Feruzi alisema na kukaa kwenye kiti, akamkabili Husna.

“Usijali,” Husna alisema na kujaribu kuonyesha yuko hapo mustarehe.

“Habari siyo nzuri!” Feruzi alisema huku akimwangalia Husna machoni.

Husna alishusha pumzi za nguvu baada ya kuambiwa hivyo kisha, asiseme neno. Beda atakuwa amemwua kweli Himidu! aliwaza.

“Uhusiano wako na Beda upo karibu kwa kiasi gani?” Feruzi aliuliza huku akiendelea kumwangalia Husna.

Ni swali ambalo halikumfurahisha Husna. Kwa sekunde kadhaa hakujibu, alionekana kama aliyekuwa akitafakari namna ya kujibu.

“Kama ulivyokuwa umenieleza awali kuwa, kesi inayomkabili Beda ni kesi ambayo hata wewe itakuhusisha,” Feruzi alisema kwa upole. “Na ndiyo sababu ukawa umenitaka isijulikane kuwa, umeniajiri kwa ajili ya kumtetea Beda, lakini bado nataka kujua ukweli ulivyo kuhusu uhusiano wako na Beda.”

“Nadhani nilikwisha kukwambia uhusiano wetu ulivyo,” Husna alisema na kujaribu kuyakabili macho ya Feruzi.

“Uliniambia kuwa Beda ni mtoto wa mama yako mdogo,” Feruzi alimkumbusha Husna.

“Kwa hiyo tatizo liko wapi?”

“Inasemekana ni hawara yako?”

“Polisi ndio waliyokwambia?”

“Ndiyo.” Feruzi alijibu na kuendelea kumwangalia Husna machoni.

“Kwa hiyo wanajua nimekuajiri ili umtetee Beda?”

“Hawajui.”

“Ilikuwaje wakakwambia Beda ni hawara yangu?”

“Kwa sababu wanajua!”

Husna akakiinamisha chini kichwa chake.

“Ni kweli?” Feruzi aliuliza.

Husna akatingisha kichwa kukubali bila ya kutamka.

“Lakini wao hawataki ijulikane hivyo,” Feruzi alisema tena.

Husna akakiinua kichwa chake na kumwangalia Feruzi. “Nani hawataki?” aliuliza.

“Polisi. Hawataki itoke kwenye vyombo vya habari kwa mtazamo huo. Na pia wanakutaka ukane mahusiano yaliyokuwepo kati yako na mheshimiwa Himidu. Huo ndio usalama wako!”

Husna akapigwa na butwaa, akamkodelea macho Feruzi. Kisha, akajivuta kitini kama kuonyesha kuitafuta nguvu ya kutaka kusema. “Wamekutuma uje uniambie hivyo?” aliuliza.

Ikawa ni zamu ya Feruzi kuitikia kwa kutingisha kichwa bila ya kutamka huku akimwangalia Husna.

“Kwa hiyo wanajua?”

“Kujua nini?”

“Kwamba ni mimi ndiye niliyekuajiri kuisimamia kesi ya Beda!”

“Nimekwisha kukwambia kuwa hawajui.”

“Kwa nini wakuchague wewe kukutuma kwangu?”

“Kwa sababu wana uhakika Wakili yeyote angeisimamia kesi ya Beda, ungekuwa unawasiliana naye kwa njia moja au nyingine kutokana na uhusiano wa mapenzi kati yako na Beda.”

Husna akaonyesha kutafakari. “Endapo nitakataa kutekeleza wanavyotaka nifanye, itakuwaje?” hatimaye aliuliza.

“Kama utashindwa kuufumba mdomo wako, wao wataufumba!”

“Kivipi?”

“Usiulize maswali ya kijinga!”

Husna akashusha pumzi za nguvu na kuonekana kuuelewa ujumbe aliopewa. “Nina ombi,” alisema.

“Kwangu au kwao?”

“Kwao.”

“Sema.”

“Wakikubali kumwachia Beda, nami nitakana kujihusisha nao kimapenzi.”

“Huna haja ya kutoa ombi hilo.”

“Kwa nini?”

Ikawa zamu ya Feruzi kushusha pumzi kwa nguvu. Akayakaza macho na kumwangalia Husna machoni. Akashusha tena pumzi kisha, asiseme lolote.

“Vipi?” Husna aliuliza na kumwangalia Feruzi machoni.

“Beda amefariki dunia tokea jana jioni!” Feruzi alisema huku akiangalia pembeni.


Akina mama waliokuwa wima wakiwa hawatulii sehemu moja, wengine wakiwa wamejishika sehemu ya kizazi, wengine wakiwa wameipachika mikono juu ya vichwa vyao, wote kwa pamoja walikuwa wakilia wakizunguka huku na kule, mmoja wao akiomboleza kwa huzuni akisema, “Beda uliniaga unakwenda mjini kisha, utarudi… kumbe ndio ulikuwa ukienda moja kwa moja…” Mwingine aliomboleza kwa kusema, “Kaka umetutoka! Kaka ulikuwa kipenzi cha wengi, leo wamekuua!”

Eneo hilo likawa la kuomboleza kwa kila mmoja akitamka lake, likawa eneo la huzuni huku likizidi kuwapokea waombolezaji wengine wa kike waliozidisha vilio kila walivyoingia ndani na wengine walivianzisha vilio kabla hata ya kukigusa kizingiti cha mlango.

Kwenye chumba kilichokuwa kimeondolewa samani zote na kutandikwa majamvi, mama yake Beda alikuwa amekaa upande wa ukutani akiwa amekaa katikati ya akina mama watu wazima kama alivyokuwa yeye waliomzunguka. Alikuwa akitikisika kama aliyepandwa na ruhani huku uso wake akiwa ameuelekeza juu na kukiyumbisha kichwa pande zote za kulia na kushoto, akijaribu kujizuia kulia kwa kelele, alikuwa analalamika kwa maneno ya kuomboleza huku wanawake waliokaa ubavuni mwake wakijaribu kumbembeleza kwa kauli za kumfariji kutokana na taarifa za kifo cha mwanae zilizowasili hapo nyumbani muda mfupi uliopita.

Baba yake Beda, yeye alikuwa amekaa kwenye viti vilivyokuwa vimewekwa nje kulikofungwa turubai, alikuwa amekaa na wazee wenzake karibu na mlango wa mbele wa kuingilia nyumba kubwa ambao ulikuwa wazi kwa kufunguliwa sehemu zote mbili, wakimsikiliza. Alikuwa akizungumza kwa sauti ya chini iliyoonyesha akikabiliana na maumivu yaliyokuwa yakimwumiza moyo. Alikuwa akijaribu kuwaeleza wazee wenzake mambo yaliyojitokeza kwa mwanae mpaka kufa kwake.

Vijana wa kiume waliokuwa wamesimama nje ya turubai ambao walionekana kutokimbilia kuvijaza viti, walikuwa wakizungumza kwa sauti za chini kwa kila mmoja akijaribu kueleza alivyokuwa na Beda kwa mara ya mwisho na jinsi walivyositushwa na habari za kukamatwa kwake na polisi kabla ya kufa.

Muda mfupi, kabla ya kuwasili kwenye stendi ya Ubungo ya mabasi yanayokwenda na kuja kutoka mikoani, Pius akiwa ndani ya basi akitokea Tanga, kifamilia yeye alikuwa wa kwanza kupewa taarifa za kifo cha mdogo wake kwa njia ya simu. Simu hiyo alikuwa amepigiwa na Husna. Habari hiyo ilimchanganya na kumweka kwenye jitimai, akajikaza kwa kutulia kimya ndani ya basi na kujenga mzubao uliomwondoa kwenye kufuatilia mwelekeo wa basi alilopanda. Upande wa dirishani alikokuwa amekaa ulimsaidia kukiegemeza kichwa chake kwenye kioo cha dirisha alilolifungua kidogo na kadri alivyokuwa akiikaribia stendi ya Ubungo kwa kuyapita maeneo kama ya Kibamba, Mbezi na hatimaye Kimara, uliirudisha kichwani picha yote jiji la Dar es Salaam na kuanza kurejewa na kumbukumbu za mdogo wake kwa matukio ya uhai wao wakati wakiwa pamoja.

Hatimaye Pius alijikuta akiijenga picha aliyoiunda mwenyewe kichwani kwa kuitengeneza taswira ya kumwona Beda akiwa mikononi mwa polisi akiteswa kwa kipigo chenye kila aina ya uonevu, akamwona jinsi alivyokuwa akikana kuhusika na kifo alichotuhumiwa nacho, akaiona sura ya mdogo wake ilivyokuwa ikilia huku akiiomba toba kutoka kwa polisi hao akiwa amepiga magoti kuwaomba wasiendelee kumtesa… Machozi yakaanza kumtoka, yakapeperushwa nchani mwa macho yake na upepo uliokuwa ukiingia kupitia kwenye dirisha lake lililokuwa wazi!

Alishangaa alipojiona tayari yuko ndani ya kituo cha mkoa cha Ubungo! Aliwaangalia abiria wenzake walioonyesha kufarijika na kufika kwao salama wakiitoa mizigo yao kutoka eneo la ndani ya basi la kuhifadhi mizigo midogo. Hakufanya haraka ya kuteremka, bado alikuwa na maswali lukuki aliyokuwa akijiuliza. Kila jambo lilitakiwa lifanyike kwa wakati mmoja; Aliahidi kumpigia simu Husna mara akishafika Ubungo, lakini pia alitaka kuwajulisha walioko mjini Tanga kuhusu kifo hicho ambako alikuwa na uhakika wangekuwa hawajazipata taarifa zake. Alijiuliza kama angeanzia kwa kwenda moja kwa moja kwenye hospitali ya Mwananyamala ambako alikwishaambiwa na Husna ndiko ulikohifadhiwa mwili wa mdogo wake. Alitaka kuhakikisha kwa kuuona kisha, ndiyo aanze taratibu nyingine za kuwasiliana na marafiki zake ili washirikiane kwa ajili ya kwenda pamoja kituo cha polisi kupata kibali cha kuuchukua mwili wa Beda.

Lakini yote aliyokuwa ameyapanga na kujiuliza aanze na lipi, hatimaye alikata shauri kwa kuanza kwenda kumwona Husna, baada ya kuwasiliana naye ndiyo angejua lipi lianze mapema na lipi lianze baadaye. Aliwaangalia abiria wenzake wakiwa wanamalizia kutoka kwenye basi, ndipo naye akainuka. Akauchukua mzigo wake na kuteremka kutoka kwenye basi.

Akiwa ndani ya teksi, Pius alimpigia simu Husna na kumwambia azma yake ya kutaka kuusafirisha mwili wa mdogo wake siku inayofuata.

“Itabidi uonane na wakili Feruzi,” Husna alisema. “Taratibu zote za kupata kibali cha kuuchukua mwili wa Beda atazifanya yeye.”

“Sifahamu iliko ofisi ya Feruzi,” Pius alisema.

“Mimi ndiyo nawasili nyumbani sasa hivi na ameniahidi atakuwa ofisini kwake baada ya kutoka mahakamani. Kwa nini usije nyumbani kwangu, tunaweza tukaenda pamoja.”

“Nipo kwenye teksi, nakuja.”

“Sawa. Mambo yote tutayazunguza ukifika.”


Ripoti ya Polisi ilibainisha kuwa, kifo cha Beda kilisababishwa na ugonjwa wa kipindupindu uliompata akiwa mahabusu, ripoti ambayo ilithibitishwa na mganga Mkuu wa hospitali ya serikali aliyokuwa amepelekwa Beda wakati akiugua.

“Nina wasiwasi na ripoti hii. Hii siyo ripoti ya kweli!” Pius alilalamika wakati akiwa na Feruzi ndani ya gari.

“Unao ushahidi wa kuipinga hii ripoti?” Feruzi aliuliza bila ya kumwangalia Pius aliyekuwa amekaa kushoto kwake kwenye kiti cha mbele cha abiria.

“Nina uhakika mdogo wangu atakuwa aliteswa!”

“Inawezekana. Lakini kesi ya namna hii haiko kwako peke yako, wengi wamekutana na mkasa kama wako na walipojaribu kuipeleka kesi ya namna hii mahakamani, walishindwa!”

“Kwa nini walishindwa?”

“Walikosa ushahidi wa kuthibitisha.”

“Chukua mfano, nikiukuta mwili wa mdogo wangu una majeraha ya kipigo, huo hauwezi kuwa ni ushahidi wa kutosha wa kuwashitaki Polisi mahakamani?”

“Kesi kama hizi Polisi hujipanga na kuwa kitu kimoja. Na kibaya zaidi watatumika mashahidi watakaokuwa wameshuhudia wakati mdogo wako alivyokuwa akiumwa, na mashahidi hao ni mahabusu ambao ni rahisi kutumiwa na polisi kwa kuhaidiwa uhuru wao endapo watasema uwongo kwa kukubali kuwa ndugu yako alikuwa na ugonjwa wa kipindupindu. Na halitakuwa jambo la ajabu kuwaona mahabusu wanaokuja kutoa ushahidi wakiwa hawaijui hata sura ya mdogo wako, lakini watadai walikuwa naye. Wewe utakuwa na ushahidi gani wa kuwakataa kuwa hawakuwa kwenye mahabusu moja na mdogo wako? Wa kukanusha hilo ni yeye mwenyewe. Atakanushaje wakati akiwa ni marehemu?”

“Nitaithibitishia mahakama kuwa, mdogo wangu aliteswa endapo mwili wake utakuwa na majeraha. Nitapiga picha majeraha hayo na kuzitumia picha hizo kama kielelezo cha ushahidi.”

“Mahabusu hao hao watatumika kudai kuwa, majeraha hayo yalitokana na ugomvi uliokuwepo kati ya mdogo wako na mahabusu wenziwe. Utakuwa na ushahidi wowote wa kuyapinga madai hayo?”

“Sasa nifanyeje kama mdogo wangu nitamkuta na majeraha ya kuteswa?”

“Ni kwenda kumzika na kumshukuru Mungu. Kesi za kuzifungua dhidi ya Polisi zinatakiwa ziwe na ushahidi uliokamilika hasa kutoka kwa watu walioshuhudia na kuwa tayari kuutoa ushahidi wenyewe. Vinginevyo utapigwa chini tu. Kibaya zaidi, kesi yenyewe inaweza ikafanyiwa hukumu hiyo ya kukupiga chini baada ya miaka mitano ya kuwepo kwake mahakamani!”

Pius akakosa la kusema. Akajisogeza vizuri kwenye kiti na kukiegemea kwa ukamilifu. Akaanza kupanga namna ya kuwasiliana na viongozi wake wa kazi kwa ajili ya utaratibu wa kuusafirisha mwili wa Beda kuupeleka mjini Tanga kwa mazishi. Uonevu wa aina hii utaisha lini? alijiuliza na kukiegemeza kichwa chake kwenye shingo ya kiti na kufumba macho. Kisha,akapiga kite cha hasira ambacho hakikuwa na msaada wowote kwake!


Msiba kwa wakazi wa Dar es Salaam ulifanyika nyumbani kwa Pius kabla ya mwili wa Beda kusafirishwa kwa siku inayofuata. Mmoja kati ya waliohudhuria msiba huo ni Husna ambaye alikaa mpaka usiku, na ilipofika saa 5:30 ndipo alipoondoka na kurudi nyumbani ili ajiandae kwa siku ya pili kuusindikiza mwili huo ambao msafara wa kuusafirisha ulipangwa uwe saa tano asubuhi.

Mlinzi wa usiku anayemlindia nyumba yake ndiye aliyemfungulia geti na Husna kuliingiza gari lake. Baada ya kuliegesha aliteremka na kusalimiana na mlinzi aliyekuwa tayari amekwisha kulifunga geti.

“Alikuja yeyote kuniulizia?” Husna alimwuliza mlinzi.

“Hakuna,” mlinzi alijibu.

Husna akamuaga mlinzi na kuondoka huku mlinzi akimtakia usiku mwema.

Mshituko na mshangao ulimpata Husna alivyoingia sebuleni. Kulikuwa na mvurugano wa kupanguliwa kwa vitu vilivyokuwemo humo na baadhi ya vitu vingine vikiwa vimeanguka chini. Butwaa likiwa limempata, Husna aliangalia kwa haraka haraka kuchanguliwa na kutawanywa kwa vitu uliofanywa hapo sebuleni na kuonekana kama kwamba kulikuwa na vurugu za watu waliokuwa wamepigana, tena wenye ujuzi wa kucheza karate. Hali hiyo ikamfanya ageuze kama vile aliyeona chatu aliyejitokeza ghafla, akatoka kwa kasi na kurudi nje aliko mlinzi.

Mlinzi alishangaa alipomwona tajiri yake akitoka nje kwa kasi kubwa akiwa ametaharuki mno. Alishangaa alivyomwona akiwa anahema kama aliyetoka kukimbia umbali wa mita mia!

“Vipi?” mlinzi aliuliza baada ya kuwa, yuko ana kwa ana na Husna.

“Kuna mtu aliyeingia humu ndani?” Husna aliuliza huku akiendelea kuhema na uso wake kujengwa na taharuki isiyomilithika.

Mlinzi akaangalia upande ulipo mlango wa nyumba kama kwamba alikuwa akihakikisha kabla hajatoa jibu. “Hajaingia mtu yoyote tokea nimefika,” alisema.

“Wewe ulifika saa ngapi hapa nyumbani?” Husna aliuliza na kuonyesha bayana kuwa, alikuwa hajamwelewa kabisa mlinzi.

“Niliwasili muda wa kawaida,” mlinzi alijibu huku naye akionyesha kutaka kukijua kinachomfanya tajiri yake awe kwenye taharuki ya aina hiyo.

“Kawaida! Kawaida ndio saa ngapi?” Husna aling’aka.

“Saa moja.”

“Ulipofika ulimkuta nani?”

“Sikumkuta mtu yoyote. Kwani vipi?”

“Ulivyofika uliikutaje hali ya nyumba?” Husna aliendelea kushusha maswali bila ya kuelewa kuwa, hata naye aliulizwa swali.

“Nilivyofika nilifungua geti kama kawaida kwa ufunguo, nikaingia ndani na kuizunguka nyumba yote na kuiona ni salama.”

“Mlango wa mbele wa nyumba uliukuta ukiwa wazi au umefungwa?”

“Niliukuta ukiwa umefungwa. Wewe umeukuta vipi?”

Husna akajikuna kichwani na kuonekana kuchanganyikiwa zaidi. Lakini safari hii alilisikia swali la mlinzi. “Hata mimi niliukuta ukiwa umefungwa na nimeufungua kwa kutumia funguo,” alisema.

“Kwani vipi?”

“Kuna mtu au watu waliokuwa wameingia ndani!”

“Watu waliingia? Unawajua?” mlinzi naye aliuliza kwa kutaharuki.

“Siwajui,” Husna alisema na kuonekana kuchoka ghafla.

“Labda waliingia kabla ya mimi sijafika,” mlinzi alisema na kuonekana kujitetea. “Wameiba?”

“Bado sijajua.”

“Twende tukaangalie!” mlinzi aliamuru.

Wakafuatana.

ITAENDELEA

Siku ya Utakaso Sehemu ya Tatu

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment