Kitisho Sehemu ya Tatu
KIJASUSI

Ep 03: Kitisho

Kitisho Sehemu ya Tatu

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE


Simulizi : Kitisho

Sehemu ya Tatu (3)

KEREGE

“SASA mtataja password au hamtaji? Tunajua kama ninyi mnaijua ofisi nzima na sisi tunataka kuwasha hii kompyuta,” John the Killer ‘JoKi’ akiwa na mjeledi mkononi mwake alikuwa akimuhoji Chiba aliyekuwa hoi kwa kipigo huku mikono na miguu yake ikiwa imefungwa kwa minyororo imara. Kila alipoiangalia ile kompyuta Chiba alshikwa na woga wa kutaja password, kwa maana alijua wazi kuwa akitaja tu basi siri za za idara zimemwagika.

Upande wa pili Madam S alikuwa amerudiwa na fahamu lakini bado akajifanya amepoteza fahamu akiskiliza kila kinachoendelea, damu iliyoganda usoni kwa majeraha ya vioo, maumivu makali ya mkono na mguu yalimfanya ajikute anashindwa kustahimili hali ile, aliwaza sana alipogundua kuwa wale jamaa wameikamata ile kompyuta na vijana wake wote alishawaambia ni heri kufa kuliko kutaja hiyo password.

“Anhaaa! Bibi ameamka, verygood!” JoKi akavuta hatua mpaka kwa Madam S, akatikisa kichwa chake, kisha akamkanyaga kwa nguvu kwenye mguu wake ulioonesha kila dalili ya kuwa umevunjika kwa jinsi ulivyovimba.

“Aaaaaiiiiggghhhh! Ms**ge wewe!” Madam akapiga yowe la uchungu na kutoa tusi, JoKi akamtandika teke la usoni, Madam S akajigonga ukutani kwa kisogo na kutulia bado kwenye ile minyororo, kwa kuwa alikuwa hajafungwa miguu yake na alijiinua kwa kutumia nguvu ya mikono kwa kujiegemeza na ile minyororo, alijisungusha hewani na kumtandika teke JoKi, lililomsukuma na ye akajibamiza ukutani na kupasuka kwenye paji la uso.

Mtesi mwingine akampiga na shoti ya umeme Madam S akapiga kelele na kutulia.

JoKi akajipapasa usoni na kukuta damu zikimwagika, akamtazama Madam S kwa hasira sana, “Umefanya jambo baya sana mwanamke! Utajuta leo nakwambia!” JoKi akauzungusha mjeledi wake na kumcharaza vibaya Madam. Chiba alishindwa la kufanya.

“Mwachee!” akapiga kelele kutoka pale chini. Wale jamaa wakaanza kucheka kwa kejeli, “Ipo saa yenu, na haiku mbali, mtajuta kuiona siku ya leo,” akaongea huku akiuma meno.

“Tutajuta saa ngapi ilhali alfajiri hii nyote mnauawa?” mmoja wao akasema.

“Hata kama mkituua, nawaapia mtajuta kuiona siku ya leo!” Chiba aliendelea kusisitiza.

“Kelele wewe, nguruwe jike we!” JoKi akafoka. Na wakati huo huo watu wane wakaingia ndani ya chumba kile wote wakiwa wamevaa maguo meusi na soksi usoni; ni macho tu yaliyokuwa yakionekana.

“Karibuni wazee!” JoKi akakaribisha.

“Madam S, na kikosi chako, serikali ilkutuma kufuatilia nyendo za watu au kulinda usalama wa Taifa dhidi ya hila za Mabeberu?” mmoja wao akauliza.

“Beberu lenyewe ndio wewe!” Madam S akajibu kwa taabu kidogo lakini waliayaelewa maneno yake.

“Unajibu utumbo! Madam ! unakitaka kifo kabla ya wakati wake sio, subiri subiri bado nusu saa ya kukuua kwanza utimize haja yetu moja tu kisha tunakuua ili upumzike na mateso haya,” mwingine akadakia.

“Inaonekana mnanifahamu vema sio? Mimi siogopi kifo, nishakutana na kifo zaidi ya mara mia tano sasa hicho unachosema wewe wala sikiogopi, lakini naomba mniue kabla sijawaua ninyi,” akaongea kijeuri.

Kosi kali likatua shavuni, la pili, la tatu, la nne, kisha sonyo kali likafuata, “Acha ujeuri, usibishane na Mkuu!” Yule mtu wa pili akamaliza alilolifanya.

“Yote yatarudi kama usiponiua sasa!” madam akamwambia Yule bwana.

Jasmine akaletwa ndani akiwa na kamba mikononi na tambala chafu lililoshindiliwa kinywani, akasukumiziwa mle chumbani.

“Wawili wameshakufa,” Yule bwana aliyezungumza mwanzo akamwonesha picha ya mwili wa Scoba. Madam S akaangusha chozi, “Hakika mtalipa roho ya huyo mtu kwa gharama kubwa!” akalalama.

“Never!” Yule bwana akajibu.

Madam S akamtemea mate usoni, “Never say never again!”.

“Huyu mwanamke jeuri mpeni disprini kwanza!” amri ikatolewa, umeme ukawashwa na shoti zikamchapa Madam S takriban sekunde thelethini.

“Stop!” ikatolewa amri ya pili, umeme ukazimwa,

“Nilishawaambia, ukifuata nyayo zap aka utapotea, sasa ninyi ni manunda na sasa mtapotea hakika,” sauti yenye lafudhi ya kihindi kwa mbali ikasikika kutoka kwenye soksi jeusi lililomfunika mtu huyo.

“Haya nataka password ya hii kompyuta!” ile sauti ya kihindi ikaendelea. Alipoichukua ile kompyuta kutoka kwa kijana mmoja ndipo Chiba alipoiona kwa uvunguni na kugundua kuwa kompyuta ile si yenyewe, akamtazama Madam S, akajikohoza mara tatu kwa mtindo wa pekee, Madam akaelewa kuwa ule ni wito akamtazama Chiba, Chiba akayazungusha macho yake kwa namna ya ajabu huku akibana na kuachia kope zake, Madam S akaelewa anachoambiwa kuwa kompyuta ile ni feki.

Akawatajia password ya hiyo kompyuta, wale jamaa wakaanza kuifungua, ilipoanza kufunguka wakafurahi sana na kuondoka zao.

“Tunarudi muda si mrefu kuwaua!” mmoja wao akasema.

Wakaondoka zao.

KITUO CHA POLISI KATI –saa 11 alfajiri.

KIPIGO alichokipata Ravi Kumar kutoka katika mikono ya vijana wataalam wa kazi hiyo alitapika kila alichokijua juu ya sakata hilo, ingawaje alionekana vingi hafahamu lakini alimtaja mshirika wake mkubwa aliyekuwa akimpa maagizo ya kupeleka Gerezani au kuchukua na kuleta kwake, huyu hakuwa mwingine ni Pancho Panchilio.

“Kwa hiyo Pancho ndiye alikuwa anakutuma?” kamanda akauliza.

“Ndiyo kabisa yaani, ni jeje huyo, lakini mimi sijui nini alikuwa anaadika,” akajieleza.

“Pancho anaishi wapi?” akauliza Kamanda.

“Mimi mtaniua, sijui naishi wapi najua ofisi yake tu,” Ravi akajibu huku akilia na damu zikimtoka kinywani na puani.

“Na huyu Mke wa Mahmoud umemjuaje?” kamanda akauliza.

“Huyu manamuke bana, nilikutanishwa na jeje tu,” akaeleza.

“Sasa yuko wapi?” swali linguine.

“Aliniaga anaenda Zanzibar na atarudi jumamosi hii,” akajibu.

“Zanziba sehemu gani?”

“Mimi hapana jua jamani, mambo ya familia hayo!” akaanza kulia.

Kamanda Amata akaanza kupekuwa simu moja baada ya nyingine za wale wafanyakazi, ndipo katika simu ya msichana wa kazi alipokuta ujumbe mfupi wenye maagizo Fulani kuwa mtu yeyote akiuliza aseme mama huyo kaenda Zanzibar lakini alipochunguza haraka kwa makampuni ya simu aliambiwa namba hiyo mara ya mwisho ilikuwa ikisoma eneo la Laskazoni Tanga.

Kamanda Amata akaagiza kwa Inspekta Simbeye kuwa huyo mama akamatwe mara moja, simu ikapigwa Tanga, kituo kikuucha polisi, masako wa panya wa kimya kimya ukaanza.

“Kamanda Amata,” Simbeye akaita, kisha akampa ishara ya mkono kumwita pembeni.

“Vijana wangu wawili wameuawa eneo la Klabu ya Mbowe! Masaa matatu yaliyopita,” akamnong’oneza.

“Pole sana Inspekta, walikuwa kazini, wamekufa kishujaa, na muuaji atapatikana tu!” kamanda Amata akajibu na kutoka kituoni hapo.

4

JOKI alitulia mezani kupokea taarifa zote za vikosi kazi walivyovituma kuwasaka watu hao, vikosi vinavyoongozwa na wapiganaji hodari kuanzia makabiliano ya ana kwa ana na hata yale ya silaha za kila aina. Alishangaa tu kuwa muda unakwenda lakini hapati jibu lolote juu ya kupatikana au kuonekana kwa Kamanda Amata ambaye nguvu zote walikuwa wameelekeza kwake, isitoshe ilikwisha amuriwa kuwa akipatikana wala haina haja kumleta na uhai wake bali ni kumuua kwa vyovyote vile.

Aliitazama saa yake, pambazuko lilikuwa kwenye miimo ya mlango ulio mbele yake. Wamepatwa nini hawa? Mbona muda umetutupa mkono! Alijisemea kwa sauti ndogo iliyotosha kujisikia yeye mwenyewe. Kichwa kilikuwa kikimzunguka kila mara alitamanai kuinua simu awapigie kuliza lakini alikumbuka kuwa makubaliano yao hayakuwa hivyo bai wao wakikamilisha kazi watampigia simu kama walivyofanya kwa wengine wote.

Akiwa katika kuwaza, simu yake iliita, akaiinua na kuiweka sikioni akiwa na shauku ya kujua nini kimetokea katika msakao huo.

“JoKi !” sauti iliita kisha ikakata.

“Sema, mmekamlisha kazi?” akauliza.

“Hapana JoKi, muda tulioupanga kukamilisha kazi umepita, lakini hatujafanikiwa kumpata Yule hayawani, tufanyeje?” Mkuu wa kikosi cha kwanza akajieleza.

JoKi akatulia kimya kwa fungu la sekunde, akashusha pumzi na kuitoa simu sikioni; tayari alikuwa amesahau anaongea na nani, akakumbuka, akajicheka na kurudisha simu sikioni.

“Subiri kidogo, nitakupa jibu,” JoKi akajibu. Akaitua simu chini na kuhisi kuchanganyikiwa, akabofya namba Fulani na kusikiliza. Naima alikuwa upande wa pili.

“Yes JoKi!” akaitikia.

“Niambie mmefikia wapi na harakati?” JoKi akauliza.

“Bad! Very bad! Huyu jamaa kwanza keshaua mtu mmoja, nimepambana naye lakini Polisi wameharibu muvi, kanitoroka,” akaeleza.

JoKi akapiga ngumi mezani baada ya kujua uwa keshapoteza watu wane katika harakati zake.

“Shiit!” akang’aka, “Unamwonaje?” akauliza.

“Mtepetevu, simshindwi hata kidogo, nab ado namsaka kwani amenijeruhi,” Naima akajigamba. Baada ya kuongea na Naima akapigia kikosi cha tatu nacho majibu ni yaleyale kuwa mtu huyo hajaonekana. Ni Naima peke yake aliweza kumwona na kupambana naye japo kwa sekunde chache. JoKi akatoa maagizo kuwa vikosi viwili vibaki kazini na kikosi kimoja kirudi kambini kwa ajili ya kutekeleza majukumu mengine. Kati ya vikosi viwili vilivyobaki kumsaka Amata kikosi cha Naima nacho kilikuwamo.

Tayari giza lilianza kuuachia mwanga nafasi ya utawala, kwa pande zote mbili huo haukuwa muda rafiki kufanya makeke yoyote lakini haikuwa na jinsi. Pande zote mbili zilikuwa kazini kwa umakini zaidi.

JoKi aliwapanga watu wake vyema katika jiji la Dar es salaam kuwa popote watakapomuona Kamanda Amata wasifanye lolote bali waitaarifu ofisi nayo itajua nini cha kufanya ili kumaliza kijana huyo shababi.

§§§§§

KATIKATI YA JIJI LA DAR ES SALAAM-saa 1:02 asubuhi.

MITEGO MIWILI ilitegwa mahsusi kwa ajili ya Kamanda Amata, wakati huu wa jua hawakutakiwa kumuua ila walipewa amri moja tu ya kutoa taarifa kwamba kaonekana sehemu Fulani kisha kazi ya kummaliza ifanyike bila tabu.

Kikosi cha kwanza chenye watu wane kilikuwa jirani kabisa na jingo la JM Mall ambapo ndani yake, juu; ghorofa ya sita kuna ofisi ya AGI Investiment inayomilikiwa na Kamanda Amata kama Mkurugenza huku Gina akiwa kama Katibu wake, hapo ndipo hupangia mipango yote migumu na kuigeuza kuwa myepesi, nani afe na nani hasife, nani aokolewe na nani atoswe yote yalijadiliwa hapo kwa usiri mkubwa wakati leseni ya kampuni hiyo ni ya ufaulishaji mizigo bandarini.

Watu waliaanza kulijaza jiji, mishemishe za hapa na pale zilianza kuzikumba kona za jiji la Dar es salaam, jua nalo lilipanda angani taratibu likitokea pande zile za Kigamboni. Naima alikuwa ametulia katika moja ya mbao za magazeti akitazama habari nzito iliyobeba magazeti mengi ya siku hiyo.

…Mbunge wa Miroroso auawa kikatili nyumbani kwake Msasani…

Moja ya gazeti liliandika hivyo kwa wino mzito, watu walijazana kusoma habari hiyo, kila kona ya jiji liliongelewa hilo.

“Washamuua huyo! Nchi hii utaiweza!” mmoja wa madereva Tax aliropoka

“Ndiyo hivyo, hii nchi ya wenyewe hii, alikuwa anaongea sana huyu, washamtengeneza!” mwingine alidakia.

“Badala msikitike wapigania haki wanapotezwa nyie mnashabikia kwa maneno ya ajabu,” mara hii mshona viatu alimalizia.

Mazungumzo juu ya hilo yakatawala kila kona ya eneo lile, kufumba na kufumbua gazeti la Mbiu ya Mnyonge likapotea mbaoni, likaisha kabisa kwa kuwa liliandika vizuri habari hiyo.

Naima alisikiliza yote hayo, akakitazama kidole chake cha shahada cha mkono wa kuume akatabasamu na kusogea pembeni ya eneo hilo, aliwatazama vijana wake wawili aliobaki nao katika kikosi chake akawapa ishara kuwa mambo yako sawa.

Kamanda Amata alikuwa akisubiriwa katika maeneo yake muhimu ya kujidai, yeye hakuwa na habari ya lolote katika kuwindwa huko. Asubuhi hiyo alirudi nyumbani kwake japo kujiweka sawa na kuanza awamu mpya ya mapambano ya mchana, muda ulimpiga kikumbo, alipenda kuibuka kidedea kabla ya jogoo kuwika lakini akajikuta akikabiliwa na mambo mengi ya kiupelelzi ili kuwajua adui zake walivyo, lakini hakujuwa bado wamejipanga vipi, kitu kilichompa ujasiri siku hiyo, ni kule kuwa peke yake katika uwanja wa mapambano, kumbe hakuhitaji kutumia akili ya pili kumlinda mwingine; lakini pia alijua wazi kuwa nalo ni hatari ubwa kwani macho ya adui yake yatakuwa na kazi moja tu ya kumtazama yeye kila anaponyanyua wayo wa mguu wake. Aliegesha pikipiki lake mahala pake na kulizima, akatulia kusikiliza lolote kama lipo, ukimya ulitawala, hakuna jipya, akavua kofia lake na kulipachika juu ya kioo cha pikipiki hilo kisha yeye kujitoma ndani huku mkono mmoja ukiwa ndani ya jaketi lake.

Alipohakikisha kila kitu ni salama, akaingia chumbani mwake na kujiweka sawa kivingine.

Alipotoka ndani; alikuwa ndani ya suti ya kijivu iliyotanguliwa na shati la buluu bahari, akalielekea jokofu na kuchukua dumu la maziwa, akamimina kwenye kikombe kikubwa, soseji tatu nene pamoja na slesi kadhaa za mkate, vikapashwa kwa microwave na toaster.

Nje ya nyumba ya Amata kulikuwa na pub ya kisasa ambayo iliendesha shughuli zake saa saa ishirini na nne, asubuhi hiyo iliyokuwa na hali ya mawingu, bado watu wachache walionekana kuwapo eneo hilo ama wakiongea hiki na kile au wakipata supu ya kongolo. Hilo halikuwa tatizo kwa Amata, aliitoa gari yake nje na kuiweka sawa tayari kwa safari, akafunga geti lake kwa kutumia rimoti maalum kwa kazi hiyo.

Huku macho yake yakifanya kazi ya ziada ya kuatzama huku na kule akili yake ilipisha uamuzi wa kuhamisha tiba za Gina na Scoba kwenda shamba ili kuepusha lolote ambalo adui yake anaweza kulifanya, kwa maana kama ni watu aliyoawategemea basi ni hao tu. Aliingia kwenye gari yake aina ya Volks Wagen, au wengi mngependa kuiita Golf, akashusha kioo taratibu na kumtazama binti aliyekuwa akipita mbele ya gari yake. “Duniani kuna viumbe mwe!” akajisemea na kisha akaingiza gia namba moja na kuondoka taratibu, alipoumaliza wigo wa ile Pub, akatupa jicho kutazama kijia kile alichoingilia Yule mwanadada, akalisanifu umbo la msichana huyo kwa nyuma, lo; akashindwa afanye nini, akaodoa gari yake na kuikamata barabara ya KInondoni kuelekea daraja la Salenda, alipoikanyaga tu barabara ile na kwenda mwendo wa mita kama 200 hivi, akatazama kioo chake cha ndani na kuona gari nyingine nyeupe ikiingia barabarani kutokea njia ileile. Hakuitilia shaka lakini alitaka kupata uhakika kama gari hiyo ana nasaba nayo au la.

Kabla hajafika kwenye makutano, akakunja kulia na kuingia ofisi za ubalozi wa Uswizz, akaweka gari katika maegesho yake, hakushuka. Akaiona ile gari ikipitiliza, hapo nay eye akatoa gari yake na kurudi barabarani, alipokunja kulia hakuiona ile gari, akajua hisia zake hazikuwa sawasawa, akaingia barabarani na kuifuata barabara ya Bagamoyo mpaka Salenda na kukunja kushoto kuingia barabara ya Ocean kisha akaegesha gari yake kwa mbele kidogo akitazama kama kunayeyote anayefuatilia nyendo hizo. Alipohakikisha hakuna jipya, akakodi Tax na kuelekea Sea View.

“Nishushe hapa!” akamwamuru dereva Tax kisha akamtupia not ya 5000 na kutokomea zake.

§§§§§

DR. KHADRAI ALIKUWA BIZE NA MGONJWA WAKE, kama Mzuka Kamanda Amata akasimama katika mlango wa chumba hicho.

“Karibu Amata,” akamkaribisha kitini.

“Asante nimekaribia, anaendeleaje huyo?” akauliza mara baada ya kuketi kitini.

“Anaendelea vyema, ameamka ila bado fahamu hazijamrudia, lakini si muda mrefu atakuwa sawa, lakini, Amata, huyu atatakiwa kupumzika kama miezi mitatu hivi asifanye shughuli za mikiki mikiki,” akaeleza.

“Ok, umeeleweka kabisa. Sasa Khadrai ipo hivi, hali ya kiusalama sio nzuri sana, na nimekuja hapa kwa jambo moja tu,” Kamanda akainuka kitini, na kuliendea dirisha kubwa la aluminium na kuchungulia nje, akaiona ile gari ikiegeshwa mahala Fulani jirani kabisa na lile jumba la Khadrai, akarudi na kusimama karibu kabisa na daktari huyo, “Sikiliza, wewe na huyu Gina nitawapeleka Safe House, leo hii, kila kitu kipo kule utatumia ofisi ya Dr. Jasmine”.

“Ni wapi huko?” Khadrai akauliza.

“We jua ni Safe House, iko wapi hilo sio swali kwa sasa, haya mwandae mgonjwa wako kwa safari, ukiwa tayari unambie, nitatumia gari yako pia,” akamwambia huku akitokea sebuleni, ukimya wa jumba hilo ulibaki hivyo hivyo, akatzama huku na huko, akachomoa bastola yake ndogo kabisa na kuiweka sawa, akavuta hatua kuuelekea mlango wa kutokea nje, akabana dirishani kutazama.

Mlinzi wa geti aliliendea kufungua baada ya kusikia mbisho, Kamanda akatulia palepale akitazama huku bastola yake ikiwa tayari kutekeleza itakaloamuriwa. Yule mlinzi akafungua geti, mtu mmoja akaingia ndani akifuatiwa na wengine wawili, alikuwa amevalia suti nyeupe kabisa na wale wenzake vivyo hivyo, hakuwa Mtanzania, wala hakuwa Mwafrika, kutoka pale dirishani Kamanda Amata akajihisi kupata ubaridi wa ghafla.

“Smart Killer!” akajisemea, kisha akarudi ndani kwa Daktari Khadrai.

“Kaeni humu, msitoke nje wala kuchungulia,” akarudi sebuleni, na kukuta wageni wake wakiujia mlango mkubwa wa nyumba ilhali mlinzi anagalagala chini pale getini.

“Haina haja ya kutukaribisha,” Yule mtu aliongea kwa Kifaransa safi huku wale wenzake wakiwa kimya na mikono yao wameifumbata ndani ya makoti yao, Yule bwana mkubwa alijishika kiuno na kuyaachia mabastola yake waziwazi yakining’inia.

“Karibuni, karibuni viti,” akawakaribisha huku yeye akikiendea kimoja ya viti hivyo.

“Hatuna haja ya kukaa! Tumeshakaa sana kwenye ndege tuliyokuja nayo!” tunataka kitu kimoja tu hapa na tunaondoka na ndege ya saa tano,” Yule bwana akajibu kijeuri huku akichomoa bastola moja na kuifunga kiwambo cha sauti.

“Kitu gani?” Amata akauliza.

“Roho, roho yako inayokutia ujeuri ndiyo tunayoitaka sisi!” Yule bwana akaeleza, huku akiwa tayari kainua bastola yake na kuielekezea katika paji la uso la Amata. Uongo wa Amata ulikuwa ukifanya kazi kwa kasi ya ajabu kuliko kawaida yake akitazama huku na kule kwa kuzungusha macho, akiwatazama wote watatu na kuuona kwa haraka haraka uhatari wa viumbe hao waliovalia sare mpaka mtindo wa viatu vyao ulikuwa wa kipiganaji kabisa. “Kazi ipo, hapa ni kufa nakupona,” Kamanda akawaza.

§§§§§

KANAYO O. KANAYO ALIKETI KATIKA NUSU UKUTA akiangali mechi ya mpira wa miguu kati ya afungwa mashabiki wa Yanga na Simba. Nywele zilianza kupoteza mng’ao wake, ndevu zilizokosa mnyoaji mzuri anayeijua kazi yake nazo zilikuwa hoi, uzee ulinyemelea mwili huo ambao ulikuwa wa kupendeza kwa mafuta na unyunyu wa gharama. Akiwa ametingwa katika kutazama mechi hiyo ambayo upande wa Yanga ulishinda 3-0 kama kawaida, alihisi kitu kikipenyeshwa kwenye kiganja cha mkono wake.

Ilikuwa kijikaratasi kidogo, akamtazama huyo aliyeifanya kazi hiyo, akamwona na kumbania jicho kisha akaifungua ile karatasi na kuisoma, alipomaliza, akaikunja na kuondoka zake.

Ndani ya chumba chao cha kulala chake cha kulala kilichokuwa na kitanda kimoja kidogo chenye tandiko tu bila godoro, aliketi kwa utulivu na kuingiza mkono uvunguni akachomoa bahasha ndogo na kuifungua ndani.

“…Kazi imeanza mtaani, tumekamata watatu, tumewaweka kwenye hali mbaya wawili, bado mmoja, Kamanda Amata.

Tumeleta Smart Killer kama mlivyoagiza, tukimmaliza yeye ndipo tutafanya plan B, kaa tayari kwa taarifa ya mapinduzi.

Mafisadi; kama wanavyotuita, tutaendelea kuwapo tu na tutaiburuza nchi kwa noti zetu.

Cheers!…”

Akaikunja ile karatasi na kuitia kinywani huku akitabasamu.

§§§§§

MAHMOUD ZEBAKI alitema karatasi iliyokuwa kinywani mwake na kuipachika uvunguni mwa kitanda chake, akatabasamu kwa tabasamu pana. Ijapokua ngozi yake ilikuwa kavu kwa kukosa japo Vaseline lakini bado ilionesha afya kwa mbali, jela ni jela tu. “Hawatuwezi hawa, tutaendelea kutafuna pesa tu, fisadi sio peke yangu kuna Magurubembe huko nje hawayajui, na kesi yetu tutashinda,” akajipa moyo huku akisimama na kutembea hapa na pale.

Kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na pesa za umma waliyoshitakiwa Mahmoud Zebaki, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uswizz na Kanayo O. Kanayo aliyekuwa Waziri katia Wizara nyeti ya Serikali ilikuwa ikiunguruma katika Mahakama ya Kisutu, kila mara iliposomwa iliahirishwa na watu hao kurudisha lumande. Wananchi wengi walilalamika kwani hawakuelewa kwanini kesi hiyo inapigwa danadana kiasi hicho, wakati Wananchi wakilalama kuwa watu hao ‘wasulibiwe’, walioshika mpini wanasema ‘uchunguzi unaendelea’.

§§§§§§

Kama kuna kitu kilimuuzi Pancho Panchilio alipokuwa ofisini kwake ni kitendo cha kudanganywa juu ya ile kompyuta, alipoifungua akiwa ofisini mwake ilifunguka na kumuonesha picha moja tu ya fuvu lenye ujumbe chini yake ‘Ni zamu yako kufa’. “Kama wao ni wajanja basi mimi ni zaidi, na ile kompyuta lazima niipate leo hii,” akajiwazia huku mwili wake ukitetemeka kwa hasira. Aliinuka na kuliendea dirisha kubwa la kioo na kuitazama mandhari ya jiji la Dar es salaam, akasonya na kuichomoa bastola yake, alipogeuka alifyatua na kuisambaratisha ile kompyuta pale mezani, akairudisha bastola yake na kurudi kitini. “Fanya nililokuagiza, kumbuka sisi ndiyo tunaokulinda hapa nchini na hata nchi yako haijui kama upo hapa kutokana na makosa uliyoyafanya huko,” aliyakumbuka maneno ya Kanayo O. kanayo siku alipokwenda kumtembelea gerezani.

“Lazima ufe leo Kamanda,” akajisemea na kujibwaga kitini. Aliinamisha kichwa chake mezani huku mikono yake ikizitimua nywele zake za Kihindi kama anayetafuta kitu Fulani humo, kisha akakiinua ghafla na kutazama mlangoni. Akapiga ngumi mezani, akanyanyuka na kuibeba briefcase yake, akatoka mpaka kwenye ofisi ndogo ya katibu wake.

“Boss, mbona mapema?” Yule binti akauliza.

“Usijali, natoka, kuna kazi naenda kuifanya, nitarudi hapa kesho, aaah no hapana, naweza kuchukua hata siku mbili nje ya ofisi, nitakupigia baadaye,” alikuwa akiongea huku akibabaika hapa na pale. Akatoka ofisini na kuiendea gari yake kabla hajapotelea mjini.

KITUO CHA POLISI CHA KATI- muda huohuo

INSPEKTA SIMBEYE hakujua nini la kufanya asubuhi hiyo, wingu jeusi lilikuwa limekigubika kichwa chake, alijua la kufanya lakini alishindwa kulifanya. Hapo ndipo moyo wake uliporudisha uamuzi wa kustahafu kazi hiyo, uamuzi ambao ulikataliwa pindi ulipowafikia wakubwa, ulikataliwa kwa sababu ya utendaji kazi wa kiumbe huyo alijulikana kwa cheo kama jina, Inspekta. Aliipenda kazi yake sana, hata baadaye akafanya kazi nyingi kwa kushirikiana na Idara nyeti za Usalama wa Taifa, alikuwa mpole, mnyeyekevu, msiri, mwenye huruma, lakini makini katika kazi na hakufanya makosa. Hakupenda kukumbatia ujinga wala upumbavu. Alikuwa mkufunzi wa mafunzo ya polisi wapya pale CCP na ndipo alipokuatana na Kijana Amata alipoingia mafunzoni.

Mara kwa mara alikuwa akimtazama kijana huyo mchangamfu kwa jicho la pekee, “Anafaa,” alijisemea huku akitikisa kichwa alipokuwa akishuhudia shabaha ya aina yake iliyokuwa ikilengwa mazoezini, wepesi wa kufanya michezo ya karate na kungfu, alivutiwa. Alimjua vema, vema sana na alimwamini kuliko unavyofikiria.

Alijiinua kichwa chake na kuitazama picha kubwa ya Mwl. Nyerere iliyokuwa imening’inia ukutani, “Tutakumbatia waovu mpaka lini ilhali wanajulikana walipo?” alijikuta akiiuliza ile picha bila kujua kuwa haiwezi kumjibu, akatikisa kichwa. “Usifanye lolote juu ya mtu huyo! Mwache kama alivyo mpaka oda ya juu itakapotoka,” aliikumbuka sauti hiyo iliyomfikia kupitia simu yake ya ofisini pale alipoomba kumkamata bwanyenye huyo aliyezaliwa India na kutarajia kufia Tanganyika.

Akasonya, akaisogeza kofia yake pembeni na kuinyanyua simu yake, akabofya zile namba unazozifahamu, akaiweka sikioni, tayari moyo wake ulipitisha maamuzi, kifua chake kilikuwa kikipanda na kushuka, “Nitajua la kumfanya!” alijiambia.

§§§§§

§§§§§

NYUMBANI KWA DR. KHADRAI

SIMU ya Kamanda Amata ikaita kutoka mfukoni mwake, Yule bwana aliyekuwa amemlenga sawia Kamanda Amata akijiongelesha kwa Kifaransa chake safi, akayumbisha jicho kidogo. Kama kuna kosa ambalo Kamanda Amata alikuwa akilisubiri lifanyike basi hilo lilikuwa haswa, ndilo lenyewe.

Aliipiga ile bastola kwa pigo la nguvu, ikachomoka mikononi mwa Yule bwana, kisha akamsukuma kwa nguvu na kuwapamia wale wawili wa nyuma, wakati huo Kamanda tayari hakuwepo eneo lile, alijirusha na kuviringika na kochi kubwa. Risasi takribani tano zilifumua kochi lile kisha utulivu ukafuata. Wale mabwana wakiwa na bastola zao mikononi mwao walitulia kama masanamu, hawakutikisika, Yule kiongozi wao alikuwa akihema, hakuamini anachokiona. Ni sekunde mbili hadi tatu tukio hilo lilikuwa limekamilika, akawapa ishara vijana wake waende kuangali upande wa pili wa kochi kama mtu huyo yuko hai au la.

Walitawanyika mmoja upande huu na mwingine upande wa kule, wakaenda mbali na kochi lile huku wakitembea bila kufanya ukelele wowote kwa miguu yao kutokana na viatu walivyovivaa.

Kamanda Amata alikuwa ametulia kimya huku lile kochi likiwa limemfunika nusu na miguu yake ikiwa nje ya kochi lile, lakini kiwiliwili kilifunikwa ndani yake, hakujitikisa alitulia tuli kabisa. Wale mabwana walipoona hali ile wakasimama kila mmoja upande wake, mmoja akashusha bastola yake na kuipachika mahala pake, kisha akachomoa kisu kidogo na kukirusha sawia kwenye mguu wa Amata, kikachoma kwenye ‘kigimbi’ kikatulia palepale. Kamanda hakutikisika japo maumivu makali yalimwingia moyoni. Akatulia tuli akiwacheza shere akisubiri wasogee kabisa eneo lile.

“Amekufa huyo!” Yule aliyerusha kisu aliwaambia wenzake kisha kila mmoja aliteremsha bastola yake na kukaribia eneo hilo. Ni nukta hiyo hiyo Kamanda alitumia nguvu zake zote akanyanyuka kwa kasi na aliuzungusha mguu na kumchapa ngwala mmoja wao, naye akajibwaga kama gunia la chumvi ya Uvinza, chali sakafuni, alipotaka kujiinua kiufundi alichelewa, kwani kwa jinsi alivyojizungusha Amata aliipiga tena mikono yake Yule bwana akarudi chini.

Yule kiongozi wao aliruka sarakasi ‘back’ baada ya kuona lile kochi likija kwake, kabla hajajipanga alisuhudia kijana wake aliyebaki akijishika koromeo, tayari kisu kikali kilichomolewa na Amata katika mguu wake na kurushwa kwa ustadi. Yule Kiongozi alipandwa na hasira, akaichomoa tena bastola yake na kuiweka sawa kuua. Kama umeme Amata alijirusha na kuinuka kumuwahi Yule aliyeanguka, alipoona ile bastola inafyatuliwa alijikusanya chini na Yule jamaa kisha akamweka ngao na risasi tatu zilimfumua mgongo wake akabaki hana uhai.

Kitendo hicho kilimchukiza Yule Kiongozi wao, kwani alijiona bwege kwa kuuawa mbele ya macho yake watu wake anaowategemea kwenye kazi kama hizi. Aliilegeza tai yake na kuruka hewani kumwendea Kamanda Amata. Amata akajiweka sawa na kuandaa pigo la maana ambalo kusudio lake lilikuwa ni kupasua korodani lakini Yule bwana alikuwa mjuvi wa mambo, alijigeuza hewani na kutanguliza mikono, pigo alilolitoa hapo, lilimpeleka Kamanda Amata kwenye kabati la vioo na kujibamizapo. Vioo vilitawanyika eneo lote na vingine vilimwachia michuno ya hapa na pale. Hakupotea muda alijichomoa na kujiweka sawa. Yule mjinga alikuwa hafai, alitembeza kichapo kwa Amata na kuhakikisha kamnyongonyesha katika kila kona ya mwili.

“Shenzi sana, umeniulia watu wangu!” aliongea kwa ukali kwa lugha ya Kifaransa.

“Hata wewe utakufa!” Kamanda Amata aliongea kwa shida huku akijivuta kujiinua kutoka pale alipojibwaga.

“Nani wa kuniua? Nimetumwa kukuua wewe tu!” akaendelea kuongea kwa sauti lake baya la kukwaruza.

§§§§§

Dr. Khadrai aliposikia kishindo cha kabati kuvunjika na vyombo vyake kumwagika, alijikunyata kwenye moja ya kona ya chumba hicho, kisha vishindo vya kipigo kizito vilifuatia. Kishindo kile cha kabati ndicho kilichomshtua Gina na fahamu zake zikamrudia upya, akatzama huku na kule kwa mshangao.

Alipomtupia jicho Yule daktari hakuwa anamfahamu.

“Kuna nini? Hapa ni wapi?” akauliza haraka haraka, akajaribu kujinyanyua lakini maumivu yake makali yakamrudisha kitandani.

Dr. Khadrai akasimama huku machozi yakimtoka.

“Amata anauawa!” akajibu.

“What?” Gina akauliza kwa mshangao. Akatazama huku na kule kwenye trey ya daktari huyo akaona vikorokoro kadhaa vimejaa. Akateremka kitandani huku mkono wake mmoja ukiwa umejishika eneo lile alilopigwa risasi.

“Ah aaaaa! Tulia kitandani, wewe hali yako hii haitaki mikiki mikiki, utajiumiza Gina!” Dr. Khadrai alimsihi Gina huku akijaribu kumrudisha kitandani. Gina hakukubali.

“Wacha nife, lakini bosi wangu hawezi kufa ndani ya mita tano toka kwangu,” akajivuta mpaka kwenye kabati kubwa.

“Gina unataka kufanya nini?” Dr. Khadrai akauliza alipomwona Gina akipekua boksi na kutoa bomba la sindano, kisha akasogeza sogeza vitu vingine na kulifumania boksi lililokuwa na dawa za ganzi.

“Gina acha!” Khadrai alimwambia kwa sauti ya chini lakini ya ukali. Gina akamchana lile bomba la sindano, akaipachika sindano bombani na kuchoma kile kizibo cha ile dawa akafyonza yote na bomba likajaa, kisha akamkabidhi Khadrai.

“Nichome haraka sana!” aliamuru.

Dr. Khadrai hakujua la kufanya.

“Nyingi hii tuipunguze!” akasihi.

“We! Nataka yote hiyo, choma, muda unakwenda!” Gina aliamuru, Dr. Khadrai huku akijua kuwa afanyacho si sahihi kwani ile dawa ilikuwa nyingi sana, lakini afanye nini, akamdunga Gina katika eneo la jirani kabisa na lile jeraha lililokuwa limefunikwa kwa bandeji. Gina alitulia kama dakika moja tu na kuhisi eneo la jereha lake ni pazito na hapaeleweki, hakusikia maumivu tena.

Kishindo kikubwa cha mtu kujibamiza ukutani kilimshtua Gina, akachukua forceps na kuufungua mlango kwa nguvu, akajitokeza msambweni, kwa mbali alimuona Kamanda Amata akigalagala chini huku lile jamaa likiwa linajinadi kummaliza. Kishindo cha mlango kufunguliwa kilimgutusha mtu huyo, lakini alipogeuka tu forceps ilizama kwenye shavu lake. Kwa hasira, alimpiga ngumi mbili Gina na kumtupa upande wa pili, alimwendea alimnyayua na kumtupa chini, Gina hakuweza kujitetea, aliruka kiutaalamu na kusimama, pigo la kwanza alilipangua vizuri, la pili na la tatu, lakini la nne lilimchanganya na kupata kipigo cha mbwa mwizi.

Kamanda Amata akanyanyuka kwa hasira na kumwendea mtu huyo.

“Geuka huku mjinga wewe unaonea wanawake sio!” Kamanda akampa maneno ya kejeli. Yule bwana akageuka na kukumbana na makonde mazito ya Amata yasiyo na idadi, Yule bwana alijitahidi kuyapangua mapigo hayo lakini alijikuta anaelemewa. akaanguka sakafuni na mara akajiinua na kwa wepesi w ajabu akajirusha hewani akatawanya miguu yake kwa kufanya shambulio a ghafla lakini Kamanda Amata alikwisha iona hiyo, naye akajirusha juu kisha wote wawili wakakutana hewani. Guu la Amata likatua tumboni kwa Yule jamaa alipoanguka akafikia juu ya meza ya kioo na kuitawanya vipande vipande, Kamanda Amata akasimama kwa miguu yake miwili huku tayari akijipanga kimapigano, akavua koti lake na kulitupa pembeni, Yule bwana naye akafanya vivyo hivyo. Kamanda akafyatua vifungo vya mikono ya shati, na Yule bwana akafanya vivyo hivyo, Amata akajiweka sawa kwa Karate na yyule bwana naye akajiweka tayari, wakabaki wakitazamana.

Mchezo ukaanza, mapigo takribani kumi na tano kutoka kwa Kamanda Amata yalipanguliwa kitaalamu na hakuna hata pigo moja lililomfikia Yule muuaji. “Napambana na mjuvi,” akajisemea. Akajiweka tena sawa na kupeleka mashambulizi ya kasi na haraka, Yule bwana alikuwa mwepesi ajabu, aliyakinga kwa kasi ileile na kumnyima Kamanda hata nafasi ya pigo moja, wakatulia tena kimya.

“Come baby, sasa namaliza kazi yangu!” Yule muuaji alijigamba kwa KIfaransa chake, kisha akajitutumua na kumfuata Kamanda Amata kwa namna ya ajabu, pigo moja lilitua lilitua kifuani mwa Kamanda Amata, akayumba nyuma na kujibamiza ukutani, nukta hiyohiyo Yule bwana alikuwa akileta wayo wa guu lake kukanyaga ama kifua au koromeo, Amata akasubiri kucheza na sekunde ya mwisho, akabonyea chini na kujizungusha, akamchota ngwala moja maridadi, Yule muuaji badala ya kuanguka akaruka sarakasi na kusimama tena lakini kabla hajatulia alikutana na mapigo matatu ya karate kutoka kwa Gina yaliyotua sawia tumboni, Gina akaruka ‘shufan’ na kutua nyuma yake, pigo lingine maridadi likatua kweny uti wa mgongo. Yule bwana akasukumwa kwenda mbele na akajikuta akikumbana na Kamanda Amata kwa kichapo cha maana, shughuli nzito.

Alipoona anazidiwa kwa mapigo na mbinu aliamua uamuzi wa ajabu kidogo, “Llive today fight tomorrow!” alijisemea na kujirusha kwenye dirisha la kioo, akatua nje na kuruka sarakasi akauruka ukuta mrefu na kutua nje yake, akapotea.

Amata akatoka kasi ndani ya ile nyumba, akasikia gari ikiwashwa na kupigwa norinda, akatazama huku na kule, akaona Toyota Duet iliyokuwa pembeni, akaingia haraka kisha akampigia kelele Gina aliyekuwa nje hapo afungue geti, akatoka kasi na kukunja kulia kuifuata ile gari.

§§§§§

JoKi alichanganyikiwa kwa maana kila alipopiga simu kwa wageni wake simu yake haikujibiwa kabisa, alikuwa akizunguka huku na kule na simu yake mkononi. Baadae akapiga kwa Naima na kumpa taarifa ya watu hao, akamwomba Naima akae tayari kwa lolote litakaloamuriwa. “Kazi hii iishe mapema kabla serikali haijaamka,” aliyakumbuka maneno ya bosi wake, akajikuta akiuma meno kwa hasira na uchungu.

Akiwa kasimama nje, akitazama walinzi waliokuwa wakiendelea kuweka ulinzi wa ngome hiyo, alijikuta hana uamuzi, “Ina mana huyu mshenzi katuzidi kete? Maana muda wa kuwasiliana umefika lakini kimya,” aliwasiwasika moyoni mwake, moyo wake ukapiga kite kwa ukimya huo.

Kutoka katka mitego yake hakukuwa na taarifa ya Kamanda kuonekana mjini, taarifa alokuwa nayo ilikuwa ni kamanda kuonekana nyumbani kwake na kisha maeneo ya Sea View, akaelekeza nguvu huko kwa kukituma kikosi namba mbili kikiambatana na Smart Killer aliyekodiwa kutoka nchi za mbali akakamilishe kazi hiyo pa si na fujo.

Mara simu yake ikaita, akainyanyua na moja kwa moja alijua ni huyo jamaa yake akaiteguwa na kuitia sikioni huku akiingia ndani.

“Hello!” akaita.

“Hey JoKi, ile kazi imekuwa ngumu, vijana wangu wawili wameuawa na Yule mjinga ndani ya sekunde tatu tu, nimebaki peke yangu,” Yule muuaji akaongea harakaharaka akihema.

“Sasa uko wapi?” JoKi akauliza.

“Nimetoroka na gari nipo barabara ya Ocean, Yule jamaa hafai ni shetani,” akaeleza.

“Jitahidi umpotee urudi kisha tujipange kummaliza kwa shambulio moja hata kama itabidi kukodi B-52 itabidi,” JoKi aliongea kwa hasira na kuiendea simu ya mezani.

§§§§§

CHIBA aliendelea kulala palepale chini, fahamu zake zilikuwa zimerudi sawasawa lakini alijikuta nguvu za kufanya lolote hana, alimtazama Madam S, bado mnyororo uliotumika kumfunga ulimshika sawasawa, alionekana kachoka sana na mwili wake ulikuwa umetona damu hapa na pale. Chumba kilifungwa, lakini kwa nje kulikuwa na ulinzi mkali bila shaka. Alijaribu kujigeuza; bado alikuwa na hali mbaya alishindwa, akaendelea kulala pale chini huku akili yake ikianza kufanya mapambano na kufikiri jinsi ya kujiokoa kwani mpaka muda huo hakujua Kamanda ana hali gani na yuko wapi, kitendawili.

Ndani ya chumba hicho kulikuwa na kamera moja ya usalama iliyokuwa inaonesha matukio yote ya ndani ya chumba hicho na kusafirisha picha hizo moja kwa moja kwenye chumba cha usalama chenye luninga zinazoonesha jumba lote ndani na nje, hata sisimizi akipita wanajua na moja kwa moja mlinzi wa eneo husika hupigiwa simu ya upepo kuulizwa juu ya hilo. Kiujumla kulikuwa na ulinzi wa uhakika si wa kubabaisha.

Chiba aliitazama ile kamera kwa jicho upande, ilikuwa imetazama upande mmoja kwa muda mrefu, upande ambao Madam S alikuwa amefungwa. Mara nyingi kamera hiyo ilikuwa ikizunguka huku na kule kutazama chumba kizima. “Au opereta amelala?” akajiuliza moyoni na kutokuwa na jibu.

Aliitazama minyororo aliyofungwa nayo Madam S, akabaki kusonya kwa maana ilikuwa imefungwa kwa kufuli madhubuti kabisa, linalofungwa kwa tarakimu maalum; ujanja hakuna. Aliuma meno kwa hasira na uchungu, aliona wazi watu hao jinsi walivyowadhalilisha kwa kuwanyanyasa namna hiyo.

Mara akasikia mlango ukifunguliwa na vijana wawili wenye silaha wakaingia huku nyuso zao zikiwa zimefichwa kwa soksi nyeusi, kisha akafuatia mtu mwingine, yeye hakuwa na silaha yoyote lakini mwili wake uliositiriwa na fulana iliyombana ulionekana wazi jinsi gani mtu huyo alivyokuwa mwanamazoezi. Hakuongea, alionesha ishara ya kidole kwa Chiba, wale vijana wawili wakaweka silaha zao migongoni na kumfunika kwa mfuko mweusi kisha kumnyanyua Chiba kumtowa nje ya chumba kile huku wakimwacha Madam S akiwatazama bila kusema neno.

§§§§§

Kilikuwa ni chumba kingine chini ya ardhi, chumba ambacho kilikuwa kikitisha zaidi ya kile cha kuhifadhia maiti, damu zilikuwa zimefanya maua ya ajabu kwenye kuta zake nyeupe na hakuna aliyezisafisha, vitu kama vining’inizio na vitanzi vilikuwepo upande mmoja wa chumba kile. Chiba akatolewa ule mfuko usoni mwake na macho yake yakapambana na hali hiyo ya kuogofya ya chumba hicho.

Hewa nzito ilikijaza chumba hicho kilichokuwa na kila dalili za umauti.

“Karibu sana Kuzimu,” JoKi alimwambia Chiba mara tu walipomfunua lile limfuko, “Unaweza kukitalii chumba hiki ambacho kamwe huwezi kukiona mahala pengine zaidi ya hapa ulipo,” akamwonesha kwa mkono chumba hicho, “Na sasa utaona demo ya kazi ya chumba hichi kama ifuatavyo,” kisha akapiga kidole chake hewani.

Watu wengine wawili wakaingia na mtu aliyefungwa mithili ileile ya Chiba, akafungwa katika moja ya zile kamba karibu na ukuta, nyuma tu ya kichwa chake, ukutani, kulikuwa na damu iliyoganda, Yule mtu akavuliwa lile limfuko kama ilivyokuwa kwa Chiba, Chiba akamwona, akashtuka na kukodoa macho, hakuamini anachokiona.

“Usishangae! Na demo yetu itaanzia hapa!” JoKi akamwambia Chiba aliyekuwa kabaki kimya akitetemeka kwa hasira lakini bado kamba zilimdhibiti na hakujua la kufanya.

§§§§§

SCOBA alifumbua macho, akili ikamrudia na kujikuta kwenye kitanda cha hospitalini, linga ikiwa pembeni na chupa ya maji ikiyatiririsha kwa matone madogo madogo yaliyokuwa yakitembea ndani ya mrija mrefu wa plastiki na kuingia mwilini mwake kupitia sindano iliyochomwa kwa ufundi kabisa katika mshipa wa mkono wake. Macho yake yakanyanyuka na kutamtazama huyo aliyesimama jirani yake ambaye alimwona miguu tu pindi alipokuwa akiangalia ule mrija wa maji ulioingia mwilini mwake.

Mubah alikuwa amesimama akiwa ndani ya suti yake nyeusi ya mikono mifupi au mimi hupenda kuziita ‘suti za mbao’.

“Scoba!” Mubah akaita. Muba akamtazama usoni hakuwa anamjua mtu huyo, “Usihofu, akampoza na kumwonesha kitambulisho chake, “Niko upande wako, nimekuja kukuchukua, vipi una nguvu za kutosha?”

“Yeah! Niko fiti, hawa washenzi hawajaniumiza ila tu walinipiga na kitu gani sijui kichwani wakanipotezea network,” Scoba akajibu. Mara muuguzi mmoja waliyevalia mavazi rasmi ya kiuguzi akiongozana na daktari aliyevalia kijeshi na juu yake kujitupia koti kubwa jeupe, walikifikia kitanda cha Scoba.

“Hauna majeraha, wala hakuna mfupa wako uliovunjika, hatuna budi kukuruhusu ila unatakiwa utumie dawa kali za maumivu,” Yule daktari akamwambia Scoba huku akiwa anaandika andika vitu Fulani, kisha akararua ile karatasi kutoka kwenye faili lake na kumpa Mubah. Muuguzi akaondoa ile sindano mkononi mwa Scoba.

“Simama!” akamwambia.

Scoba akasimama kwa tabu kidogo alipokuwa wima, akashika kichwa, akayumba kidogo kisha akasimama imara, akajinyoosha mwili; uko fiti. Akapiga push up kama kumi na tano hivi kisha akasimama imara, akachukua vidonge viwili kutoka kwa Yule Muuguzi na kuvimeza.

“Baada ya dakika thelethini waweza kufanya lolote, utakuwa poa!” Yule Muuguzi akamwambia huku akiondoka.

“Asante kwa ukarimu wako mrembo,” akamshukuru huku akimwangalia na jicho lake kutua kwenye nyama za nyuma za binti huyo aliyejaliwa shepu, “Mwe!” akajikuna kichwa, kisha wakaondoka.

ITAENDELEA

Kitisho Sehemu ya Nne

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment