Pasipoti Ya Gaidi Double Agent Sehemu ya Kwanza
NEW AUDIO

Ep 01: Pasipoti Ya Gaidi ‘Double Agent’

Pasipoti Ya Gaidi ‘Double Agent’ Sehemu ya Kwanza

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE


Simulizi : Pasipoti Ya Gaidi ‘Double Agent’

Sehemu Ya Kwanza (1)

KIKAO CHA SIRI

KATIKA MOJA YA OFISI NYETI za serikali, Rais Robert Sekawa alikutana na wadau wa Baraza la Usalama la Taifa, hoja kubwa ikiwa ni jinsi ya kuimarisha na kujipanga upya katika medani nzima ya usalama nchini ili kuepusha uzandiki na hujuma kama zilizotokea.

“Ningeshangaa, mpaka watu wavamie Ikulu, kweli ilikuwa ni hujuma lakini hatutakiwi kuiruhusu itokee tena,” mmoja wa wadau aliwaasa wenzi wake waliokuwa katika kikao hicho.

“Lakini mi bado haingii akilini kwa vipi hawa jamaa walipenya mpaka ndani na kuvikwaa vyeo vya juu kabisa katika usalama? Hii kweli ni hatari, hata sisi hatuna budi kujikagua upya tusije kuwa bado tunao kwenye ofisi zetu,” mwingine aliongeza kusema.

“Ewaaaaa, hapo ndipo nilitaka kugusa, ni kwamba haya mapandikizi si ajabu bado yapo katika majeshi yetu, kumbuka hatukatazi mtu kuhamia nchini na kuomba uraia lakini wakati mwingine hivi vitu vinatugharimu, tunapokea majasusi bila kujua,” Rais aliongea huku sura yake ikionesha hamasa ya kutoa uamuzi.

“Mheshimiwa uemelo ni sahihi, katika tafiti zetu zilizofanywa na MI tumegundua kuwa huyu Benzilahagi aliingia jeshi kupitia Kigoma, zaidi ya hapo kituo chake cha kwanza kufanyia kazi kilikuwa ni Ngara kule mpakani kabla ya kumhamishi mahali pengine, yeye alijiunga akiwa tayari na shahada ya TEHAMA, ikaonekana ni vizuri aje kwenye kitengo hicho hapa Makao Makuu…”

“Unaona!” Rais akadakia, “Umakini unahitajika kuanzia udahili wa wanajeshi, polisi, magereza, JKT na kila kunakohusika na usalama wa nchi, hii ni hatari, siku unaweza kukuta wanatugeuka na kutumaliza sote,” akaongeza kwa masikitiko.

Kikao hicho kilichukua zaidi ya saa nne mengi yakajadiliwa na kupangwa na jioni ya siku hiyo mambo kadhaa yaliwekwa sawa, maamuzi ya nini cha kufanya yakapitishwa na kila mmoja akapewa kazi ya kufanya kwenye kikosi chake.

Rais Robert Sekawa alitoka katika kikao hicho na kuondoka kwa siri kama alivyokuja, gari iliyombeba ilikuwa ni ya kawaida kabisa yenye vyoo vya giza vizivyoruhusu mtu wa nje kuona kilichomo ndani yake.

Siku hii kwa Rais huyu ilikuwa ni siku iliyojaa kazi nyingi hasa vikao mbalimbali, alikuwa akiweka sawa mambo kwa kushirikiana na wadau wa usalama nchini. Jioni ya saa kumi na moja aliwasili Ikulu na moja kwa moja aliingia katika chumba chake cha kazi za siri na kujifungia akichambua hili na lile.

Juu ya meza yake kulikuwa na kabrasha kadhaa zilizokuwa na maelezo mbalimbali ya tafutishi zilizofanywa na vijana wa MI (Wana intelijensia wa Jeshi) pamoja na zile za TISS (Idara ya Usalama wa Taifa), aliyasoma moja baada ya jingine na kujiridhisha na kazi nzito ambayo ilifanywa na vijana hao. Hakusita kufurahi moyoni kila alipoona hatua mpya ya kimaandishi na mafanikio yake.

Kazi kubwa imefanywa lakini vipi kuhusu hawa watu waliotutoroka, lazima wapatikane maana wana information za kutosha juu ya hii nchi na hatari kwetu, aliwaza akiwa analifunga moja ya kabrasha alilokuwa akiliperuzi. Akavuta karatasi tupu iliyokuwa na kuandika vitu fulani kisha akainua simu yake na kubofya tarakimu kadhaa na kuiweka sikioni.

Dakika chache baadae, ugeni mwingine ukafika katika ofisi hiyo nyeti, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa aliwasili kutimiza miadi yake kwa Rais kwa kuwa yeye aliwajibika moja kwa moja kwake.

“Karibu sana Bwana Hosea! Unaendeleaje lakini?” akamsabahi na kumuuliza.

“Naendelea vyema Mheshimiwa, matibabu niliyoyapata ni makubwa,” Hosea akajibu.

“Unaweza kufanya kazi au nikuongezee likizo?”

“Hata kama unataka kuniongezea likizo lakini sina budi kulikamilisha hili kwanza ambalo linatukabili kama taifa, kishapo, kwa matakwa yako, utaliona hilo kama linafaa,” Hosea akaeleza huku akilitua kabrasha moja lililokuwa mkononi mwake juu ya meza.

“Ok, tusipoteze muda, sasa nafikiri tunaweza kuingia awamu ya pili ya kazi yetu, baada ya tafutishi hizi ambazo vijana wako wamezileta, nataka tuamue nini tunafanya kwa kuwa hali ya taifa ndiyo hii uliyoiona,” Rais akaanzisha mada.

“Yeah ni kweli, sasa hata mimi nimeipitia na nimeongea na wale vijana mmoja baada ya mwingine kwa nyakati tofauti. Inonekana baada ya mapinduzi yale ya Nduruta mwaka uleee, na Rais Sebutunva kuingia madarakani hii ilikuwa ajenda kubwa, na ndipo alipoingiza watu wake ndani ya mipaka yetu kwa minajiri ya; siku moja washike silaha na kutuangusha. Zaidi ya hapo aliwatumia watu wenye nasaba na Nduruta ambao tunao nchini hasa kwenye Idara zetu na kuwarubuni kwa pesa nyingi sana na wao kuweza kuiba information za kiusalama na kumpelekea huyu bwana.”

“Unataka kuniambia Sebutunva anatujua vizuri sana?” Rais akauliza akiwa ameiegemea meza tena kwa sauti ndogo ya kunong’ona.

“Hawezi kutujua kiundani, bali anajua kile anachokijua. By the way, wapo wengine kwenye Baraza lako la mawaziri, na wapo kwenye Bunge letu tukufu,” akaeleza.

“Hosea, unataka kunambia kuwa ndani ya Cabinet yangu kuna funza?” Rais akauliza.

“Nini funza! Kuna minyoo…” Hosea akasisitiza. Mheshimiwa akashusha pumzi kwa nguvu na kujituliza huku fikra kadhaa zikimtambaa ubongoni, “Lazima kufanya maamuzi magumu,” akaongeza.

“Nimekuelewa vizuri, tena vizuri sana,” Mkuu wa nchi akajibu huku akitikisa kichwa.

“Majambazi wanaoteka mabasi kila mara huko Bihalamuro, wana ubia mkubwa na huyu jamaa. Unafikiri silaha zile nzito za kivita wanazitoa wapi? Kuna makahaba pale Ngara, Kigoma na hapa mjini Dar es salaam, hawa makahaba si makahaba wa kawaida, ni wanajeshi wanaotafuta information mbalimbali za nchi yetu, na wanazipata kiurahisi kwakuwa kuna watu wanaowalenga na kwa uzuri na urembo wao wanawanasa na walengwa ubwabwaja kila wanalojua,” Hosea alizidi kudadavua juu ya hilo.

Kikao chao kizito kilichukua saa moja tu; na mikakati ikapangwa, Mheshimiwa akaona mikakati hiyo na Bwana Hosea na ile ya Baraza la usalama inashahabisna vyema, wakaagana huku tayari kifuani mwake kahifadhi lile linalopaswa kufanya.


SIKU MBILI BAADAE

AICC – ARUSHA TANZANIA

WAJUMBE WA BARAZA la Usalama la Umoja wa Afrika (AU) lilikuwa na kikao ndani ya ukumbi huo wa kimataifa huko Arusha. Mkutano huo uliwakutanisha wajumbe kutoka kila nchi zinazounda umoja huo. Kwa upande wa Tanzania Waziri wa Ulinzi na wajumbe wake kadhaa walihudhuria. Agenda kubwa iliyotawala kikao hicho ni kuhusu kukomesha kabisa uwasi na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea katika nchi nyingi za Afrika. Vita hivyo vimekuwa kama donda ndugu katika ardhi ya mtu mweusi. Maghalibi, Mashariki, Kusini, Kaskazini kote damu ilikuwa ikimwagika na tatizo kubwa lilikuwa ni madaraka. Viongozi wa nchi nyingi za Afrika hawataki kuachia madaraka na kuwapisha wenzao kutawala hii imepelekea wenye mioyo migumu kuingia msituni na kufanya mapinduzi ya damu.

“Kwa sababu kampeni yetu imeamzia huko Ngoko na tunashukuru jeshi lililosambaratisha wale waasi. Hata hivyo bado kuna magugu ya uasi huo yamebaki, lazima tuhakikishe kuwa kila gugu linang’olewa na kuteketezwa kabisa. Hatuwezi kuiruhusu damu ya Waafrika imwagike ilhali nasi tupo, nasi ambao ni chombo cha kulinda usalama wao, lazima hatua stahiki ichukuliwe,” Mwenyekiti wa Baraza hilo alisema na wote waliobaki wakapiga makofi ya kumpongeza kwa hilo. Katika kikao hicho kulipitishwa maazimio magumu, mojawapo lilikuwa ni kuendelea kuyakalia kijeshi maeneo yaliyokuwa na waasi huko Kusini mwa Ngoko wakati huo wale wote waliokuwa na mahusiano na waasi hao kusakwa kokote waliko.

Baada ya kikao hicho kufungwa wajumbe walirudi katika mahoteli yao kujipumzisha na wengine kuendelea kubadilisha klabu za usiku ilimradi wale maisha.

HOTELI YA MOUNT MERU-Saa 4:05 usiku

MAZDA CELICA ilisimama mbele ya lango kuu la hoteli hiyo, kijana shababi, mweusi wa rangi, aliyevalia suti safi ya gharama aliteremka katika gari hiyo mkononi akiwa na briefcase iliyomfanya aonekane mwenye nazo hasa. Alimnongo’oneza kitu dereva wake kisha akaingia ndani ya ukumbi wa hoteli hiyo ambao ulitumika kama sehemu ya mapokezi na pia mahali pa kupumzika wakati ukisubiri huduma. Kijana Yule aliielekea meza ya mapokezi na alipoifikia tu, mhudumu wa sehemu hiyo akampatia kadi maalumu iliyokuwa ikitumika kufungulia milango ya vyumba vya hoteli hiyo ya kimataifa.

Ulinzi uliimarishwa ndani na nje ya hoteli hiyo kwa kuwa viongozi wengi walipanga vyumba hapo. Yule kijana akaingia katika lifti na kujifungia, akabonyeza kitufe ‘namba 3’ nayo ikampandisha haraka mpaka hapo alipopataka. Alipoteremka alijikuta peke yake kwenye korido ndefu iliyotenganisha vyumba upande huu na ule, akaitazama ile kadi mkononi mwake.

37, akasoma kimoyomoyo na kuuendea mlango uliondika namba hiyo, akapachika katika mashine fulani iliyobandikwa hapo mlangoni, akabofya tarakimu kadhaa kisha akachanja kwa ile kadi, mlango ukafunguka, akajitoma ndani. Chumba kilikuwa kitupu, kitanda kikubwa kilikuwa pweke kabisa na shuka nyeupe nzuri za kupendeza zilikuwa zimetulia juu yake. Yule jamaa akapekua hapa na pale, hakuonesha dalili ya kuchukua chochote, akakiendea kitanda na kuondoka mashuka yote pamoja na folonya za mito ya kulalia, akayaweka pembani na kuacha kitanda kikiwa tupu, akaingiza mkono mfukoni mwake na kutoa gloves za plastiki akavaa mikononi mwake kisha akafungua ile briefcase yake na kutoa shuka nyingine kama zilezile tena zilikuwa na nembo ya hoteli ile, kwa ujumla hazikuwa tofauti na zile alizoziondoa kitandani. Akatandika kwa ustadi wa hali ya juu na ile mito akavika folonya zake na kuirudisha pale kitandani kama ilivyokuwa. Hakika husingeweza kugundua kama shuka hizo ni nyingine. Alipojiridhisha na zoezi hilo, akazichukua zile alizoziondoa na kuzitia katika ile briefcase kisha akatoka ndani ya chumba kile huku akihakikisha kuwa hagusi kitu kingine chochote.


Baada ya hafla fupi iliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto viongozi hao walirudi kwenye mahotyeli yao waliyofikia kwa mapumziko ya usiku ambapo siku iliyofuata kila mmoja alitakiwa kurudi nchini kwake. Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Dkt. Hamadou Hussein kutoka Namibia, moja kwa moja alirudi katika hoteli aliyofikia, Mount Meru, akachukua kadi yake kutoka mapokezi na kukiendea chumba chake.

Ilikuwa saa sita karibu na nusu usiku wakati kiongozi huyo akijipumzisha kitandani mwake kuikabili siku nyingine inayokuja.

Saa 2:30 Asubuhi

MSAFARA wa gari unaotakiwa kumchukua Mwenyekiti huyo uliwasili pale hotelini, Ndege ya kuelekea Namibia ilitakiwa kuondoka saa tano na nusu katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro. Dakika kumi zikapita mtu huyo hakuonekana, kutoka Mapokezi walipiga simu kwenda chumba namba 307, chumba cha Dkt. Hamadou Hussein lakini haikupokelewa. Watu wa usalama walipopewa habari hiyo wakajaribu kupiga simu ya mkononi, ikaita pasi na kupokelewa. Hakuna jinsi ikabidi kupanda kuelekea chumbani kwa mtu huyo, walipoufikia mlango ukimya ulitawala, wakaanza kubisa kwa fujo lakini hakukuwa na majibu yoyote. Wanausalama wale wakatazamana, kuna tatizo, wakawaza vichwani mwao na kupeleka taarifa mapokezi ambapo kadi ya akiba ikaletwa na kuufungua ule mlango chini ya uangalizi wa meneja wa hoteli.

Mlango ulipofunguliwa, macho ya wote yakatua sakafuni ambako mwili wa Hamadou ulikuwako, huku mkono wake mmoja ukiwa umeshika waya wa simu ilihali yenyewe ikiwa juu ya kitako chake.

Kila mmoja alipigwa na butwaa, mashuka yalionekana kutupwa huku na huko.

“Amekufa?” mmoja wa wanausalama akauliza huku akiwahi pale ulipo ule mwili, hakuugusa, aliutazama kwa ukaribu na kuuona umauti katika mwili huo. Akageuka taratibu na kuwatazama wenzake.

“Man down!” akawaambia na kila mmoja akaonekana kushangazwa na kifo hicho. Ndani ya muda mfupi tu, simu zikatawanywa kila upande uliohusika na ugeni huo na mshikemshike wa kiusalama ukaanza.


Wachunguzi wa jeshi la polisi walikuwa ndani ya chumba hicho wakikagua hiki na kile kwa Umakini wa hali ya juu. Walipohakikisha uchunguzi umekamilika, waliondosha ule mwili na kwenda kuuhifadhi hospitalini.

Katika ofisi ya Usalama wa Taifa mkoa wa Arusha, Mkurugenzi alikutana na mtu mmoja na kujaribu kuliangalia swala hilo kwa undani.

“Amekufa au ameuawa?” akawauliza vijana wake ambao walikuwa katika msafara wa kwenda kumchukua mtu huyo.

“Kwa uchunguzi wa macho, visual inspection, yule bwana ameuawa, si kwa kukabwa au kupigwa bali kwa njia nyingine isiyo na maumivu lakini yenye ukatili zaidi,” akajibu aliyekuwa kiongoza wa msafara huo.

“Wahusika wanasemaje?”

“Hawana jibu la uhakika katika hilo,” akajibiwa.

“Ok, nataka ukakusanye taarifa zote zinazotuhusu juu ya kifo hiki na ikiwezekana fuata nyayo za muuaji ili tumtie mbaroni,” Mkurugenzi akaagiza.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha alikuwa akiumiza kichwa juu ya tukio hilo, vijana wake walipomletea ripoti juu ya kifo hicho alihisi mwili kufa ganzi ukizingatia aliweka Ulinzi mkali nje ya hoteli hiyo kuhakikisha kuwa hakuna baya lolote linaloweza kutokea kwa vipongozi hao. Lakini kifo cha Hamadou kilimwachia maswali mengi yasiyo na majibu.

Aliyemuua atakuwa alikuwa ndani ya hoteli hiyo ama ah! Aliwaza na kutikisa kichwa chake huku kalamu ikizunguka katika vidole vya mkono wake wa kulia.

“Ngoh! Ngoh! Ngoh!” mbisho wa mlango ulimkurupua kutoka katika lindi la mawazo, akajiweka sawa na kumkaribisha huyo alaiyekuwa akibisha hodi. Mtu mzima aliyekuwa na mvi kiasi kichwani mwake, akiwa ndani ya suruali ya cadeti na fulani ya mistari mchanganyiko wa rangi, miwani yake ndogo ya giza ilimfanya aonekane kuwa ni mtu mmoja mwenye pesa sana, alisimama mbele ya Kamanda huyo kwa ukakamavu akiwa kaibana mikono yake sawia. Hakuwa mwingine bali Mkuu wa kitengo cha upelelezi katika jeshi la polisi Mkoa wa Arusha.

“Afadhali umekuja, hapa kichwa kinanizunguka…” RPC akaanzisha mazungumzo bila hata kusalimia.

“Ndiyo afande nimeitika wito wako,” akajibu.

“Nipe ripoti, upelelezi umefika wapi?” akauliza RPC

“Upelelezi mkali unaendelea, vijana wametawanyika mji mzima na kupekuwa kila gesti na loji wakiwachunguza wageni wote waliongia na waliotoka leo hii kwenda nje ya mji, alkadhalika tumeweka barrier barabara kuu ya Moshi, Namanga, Singida, Dodoma na zile zote ambazo zinaweza kumtoa mtu nje ya mkoa na vijana wanakagua kila gari inayotoka,” akaeleza.

“Pale tumewatia mbaroni wahudumu wote wa vyumbani pamoja na mtunza kabati yaani stoo,” akaeleza.

“Kwa nini mmewakamata, uhusika wao unaingiaje hapo?” kamanda wa polisi alizidi.

“Majibu ya awali ambayo tumepewa na daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili ule ni kwamba kifo chake kimetokana na sumu aina ya Cyanide, na kwa vyovyote sumu hiyo ilikuwa ndani ya chumba hicho, sasa nani anahusika na kazi za ndani za vyumbani? Ni wao. Hivyo tunao kwa mahojiano,” ACP Karama, Mkuu wa upelelezi mkoa alieleza.

“Ok!”

“Kwa hiyo taarifa zetu tunaanza kuzikusanyia hapo. Askari waliokuwa nje wanasema hawakuona mtu yeyote wa kumshuku katika wageni walioingia ndani ya hoteli hiyo, hivyo tunapata hofu kuwa mhusika anaweza kuwa mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo,” akaeleza.

“Sawa hapo nimekuelewa na ninaamini ni starting point nzuri. Hili swala ni zito sana Karama, hivyo hakikisha kwa any means unalipatia mwanga mapema, aliyekufa ni mtu mkubwa sana na macho ya AU yanatutazamaje sisi, hebu fikiria!” RPC akaonesha shaka la wazi juu ya hilo.

“Najua, na nakuhakikishia tutamtia mbaroni mhusika, njgoja tuwaminye hawa wafanyakazi watasema tu,”

“Kazi njema, nipe taarifa ya kila hatua unayopiga, nataka wewe mwenyewe uingie kazini na ushirikiane na watu wenye uwezo mkubwa katika hili, kama utahitaji msaada wowote, tafadhali moja kwa moja wasiliana na mimi au ofisi yangu”.


Jiji la Arusha lilikuwa katika msukomsuko mkubwa sana siku hiyo, vijana wa polisi wakishirikiana na wale wa Jeshi la Kujenga Taifa walitawanyika kona zote za mji huo, kwenye baa, vilabu vya pombe za kienyeji, vilabu vya usiku, casino, kwenye nyumba zote za kulala wageni na sehemu ambazo waliona zinaweza kuwapa jibu la swali lao. Wote hao hakuna aliyevaa kikazi isipokuwa nguo za nyumbani tu ili kuwafanya wapate fununu hizo kirahisi.

Bila vijana hao kujua, hawakuwa peke yao, Idara ya Usalama wa Taifa nao walikuwa kazini, kama kawaida na vita yao ya kimya kimya, walihakikisha wanapita kona zilezile ambazo vijana wa poilisi wapo, wao waliwagundua kirahisi sana lakini vijana hawa hawakuwagundua shushushu waliokuwa miongoni mwao kwenye nyato zao.

Ndani ya baa moja kubwa maeneo ya Unga Limitedi, watu walifurika wakipata vinywaji na wengine vyakula aina aina. Mazungumzo ya hapa na pale yalikuwa yakiendelea kama ujuavyo pombe zikifika mahali pake. Katika luninga kubwa zilizofungwa pande tofauti katika baa hiyo kulikuwa kukioneshwa habari na kubwa iliyovuta wateja ni ile ya kukamatwa hao wafanyakazi wa hoteli.

“…aidha wafanyakazi hao wamekamatwa kuisaidia polisi…”

Ilimalizia habari ile.

“Aaaaaggh ndiyo shida ya vipolisi vyetu hii, yaani unawakamata wafanyakazi kwa kuwahoji, unapoteza muda wewe, tafuta mhalifu…” mmoja wa watu waliokuwa ndani ya baa hiyo aliropoka, mtu huyo aliyeonekana mchafu, suruali yake aliifunga kwa kamba ya katani, jaketi la Malboro lililochoka lilikuwa mwilini wake huku mkononi akiwa ameshika boksi dogo la pipi mpira aina ya Batook akizungusha na kuwauzia wateja wake. Nywele zake kichwani zilikuwa timu-timu.

“We Manchester… sasa ungekuwa we ungefanyaje?” mmoja wa vijana waliokuwa wakicheza pool alimtupia swali kwani alionesha kumjua sana mtu huyo.

“Aa wanapoteza muda, kwanza muuaji hawezi kuwa hapa Arusha saa hii wewe, kumbuka hajaua paka wala nyau kaua mtu tena kiongozi. Ala! We vipi!” akabwabwaja kwa sauti lake la kilevi.

Majibizano kati ya wawili hao yalichangiwa na wengi waliokuwamo katika baa ile kila mtu akionesha wazi kulaumu vyombo vya usalama nchini.

“Huu uzembe, hoteli inalindwa mtu anauawa vipi bwana!” mwingine alidakiza.

“We usiseme hivyo, watu ni profesheno kwenye kuua kaka, wanajipanga,” mwingine akamjibu huku akisimama na kumfuata kijana huyo palepale. Miongoni mwa watu waliokuwa mo katika baa hiyo wapo waliotega masikio na kusikiliza kipi pumba na kipi mchele.

Dar es salaam – Masaki

MADAM S ALIZIMA luninga yake na kuitupia rimoti katika kochi alilokalia, akainua bilauli yake na kupiga mafunda kadhaa ya kinywaji kilichokuwa ndani yake. Siku hii ilimkuta akiwa nyumbani, likizo fupi aliyopewa na Mheshimiwa Rais aliamua kuitumia kwa kukaa ndani na kufanya mapumziko ya nguvu. Hakumwambia mtu yeyote kuwa yuko wapi, alichofanya ni kuacha tu maagizo ya kazi kwa kila mtu wa Idara yake. Akashusha pumzi ndefu na kuinua miguu yake mpaka juu ya meza moja ndogo iliyokuwa mbele yake, akajiegemeza kochini. Simu zake zote zilikuwa offline. Hakuna mtu ambaye angeweza kumpata zaidi ya watu wa Idara yake tu ambao wangemtafuta kwa njia nyingine wanayoijua wao.

Sasa ni wakati wa kustahafu, akawaza huku akiwa kafumba macho yake na mikonmo kaikusanya kifuani mwake. Lakini Mkuu wa nchi anataka nifie kazini lo! Akazidi kuwaza. Mwanamama huyu aliyekuwa amefikisha miaka sitini na nane mpaka siku hiyo akiwa juu ya kocho hilo, aliitumikia serikali katika Idara ya Usalama wa Taifa kwa kipindi kirefu ndani na nje ya nchi. Muda wake wa kustahafu ulipita kwa kuwa alirudishwa kazini ili kushika kitengo muhimu cha ukachero wa kimataifa TSA, aliaminiwa. Kwenye Idara yake ya Usalama wa Taifa barua ya kustahafu kwake ilisainiwa na sherehe ya kumuaga ilikwishafanyika lakini Ikulu kwa siri ikamrudisha kazini na kwa kisingizio cha yeye kufungua ofisi yake binafsi iliyokuwa ikifanya kazi za kisheria. Yote hiyo ilikuwa ni ‘changa la macho’ lakini ndani yake kulikuwa na Idara hii nyeti iliyowajibika kwa Rais mwenyewe, hawa waliitwa invisible, kwa kuwa walijificha kwenye miamvuli mbalimbali ‘covers’ au tungesema wapo ‘undercover’. Kazi zao zilificha kazi halisi.

Akayafumbua macho yake, na kuyazungusha kuitalii ile sebule safi iliyotulia, ambayo hata ungeisafisha mara moja kwa mwezi isingechafuka kwa kuwa hakukuwa na mtoto wa kufanya hayo. Ni mara chache alipotembelewa na wageni ama kaka na dada zake au ndugu na jamaa ukiacha marafiki ambao hupenda kuja kupiga ulevi nyakati fulanifulani au kamanda Amata aliyewahi kutumia nyumba hiyo kama ficho lake na kulala hapo kwa siku kadhaa.

Macho yake yakatua ukutani katika picha kubwa iliyomuonesha akiwa msichana mbichi umri kama wa miaka thelathini na tano hivi, akatabasamu, nilikuwa mrembo sana jamani, akawaza. Akiwa kazama katika kuitazama picha hiyo, mlango wa sita wa fahamu ukachukua uhai, alihisi mwili kusisimka, akili yake ikamwonesha rimoti, akaichukua na kuwasha luninga, moja kwa moja akapambana na habari hiyo ya mauaji yaliyotukia huko Arusha usiku uliotangulia, masikio yake yakatulia na kumtazama mtangazaji aliyekuwa akiitangaza habari hiyo. Ilipomalizika akapitisha tafakuri ya sekunde kadhaa, akaana kuhisi damu ikichemka. Hizi kazi hazina likizo, aliwaza kwa kuwa alishaona kuwa hawezi kuliacha hilo swali hivyohivyo. Akainua simu yake na kutaka kuiwasha, akakumbuka alikuwa likizo, akaiacha. Nafsi yake haikutulia hata kidogo, moyo wake ulihangaika.

Hii ni aibu kwa taifa, mtu anakufaje na usalama wapo? Akajiuliza. Lakini baadae akaona wazi kuwa ni swali la kijinga, hakupaswa kujiuliza hasa mtu kama yeye anayejua mbinu za adui.

Hakufikiri mara mbili alijiinua pale alipo na kufuata ujia un aoelekea katika chumba chake cha kulala, kiapo changu ni kulilinda taifa, natakiwa kulilinda na kuhakikisha liko katika usalama, akawaza huku akifungua mlango wa chumbani kwake, akaingia na kusimama mbele ya kabati kubwa, akaufungua mlango na kuvuta droo la ndani, akatupa macho na kuzitazama bastola zake zilizolala kimya, nazo ziko likizo, akajisemea moyoni. Bila kuchelewa akaiendea simu iliyo pembeni mwa kitanda chake akaiinua na kubofya tarakimu kadhaa kisha akaiweka sikioni.

“Hello! Nandumbili Travel Agencies, tukusaidie nini tafadhali” sauti ya upande wa pili ikaijibu simu hiyo.

“Yeah, eee kuna Ndege ya kufika Arusha mchana huu?” akauliza.

“Aaaa hapana kwa leo hatuna kabisa…”

“Sikiliza nahitaji Ndege ya kufika Arusha iwe hata ya kukodi, niko njiani kuja uwanja wa ndege” Madam S akamaliza kauli yake na kutaja namba za kadi yake ya viza kwa malipo kisha akajianda harakaharaka.

Mtu mmoja hawezi kuliaibisha taifa zima, akawaza huku akiinua begi lake dogo na kulikamata sawia. Alikuwa kikazi, likizo imekwisha, safari ikaanza.


ARUSHA

SAA KUMI NA NUSU alasiri, Ndege ya kukodi ya shirika la Coastal Travel ilimfikisha Madam S jijini Arusha katika uwanja mdogo ambao hutumiwa na ndege ndogo tu. Uwanja huu unatumiwa zaidi na watalii wanaoingia na kutoka jijini humo ili kutembelea maeneo mengine ya utalii kama mbuga za wanyama. Nje ya jingo la uwanja huo kulikuwa na tax chache sana, kwa haraka haraka hazikuzidi tano. Bila kuangalia hii ni ya nani na ile ni ya nani, taxi moja ikaingia kwa kasi katika maegesho mita chache tu kutoka aliposimama Madam S. ikasimama ghafla na kijana mmoja mwenye mwili uliojengeka kimazoezi, akateremka na briefcase yake mkononi akivuta hatua za haraka haraka na kuingia ndani ya Uwanja ule. Madam S alimgeuzia macho na kumtazama kijana huyo mwenye haraka akipotelea, kisha tax ileile akauvuta mlango wa nyuma na kuketi.

“Sanawari Hoteli tafadhali,” akamwambia dereva naye akaiondoa ile gari mara moja na kuelekea mjini.


Hoteli ya Sanawari ilikuwa ni ya kawaida kwa watu wa kawaida, Madam S alifika na kupata chumba katilka nyumba hiyo ya ghorofa mbili. Akaingia chumbani na kuutua mkoba wake kitandani, kabla ya yote akawasha simu ambayo aliifunga kwa siku kadhaa, alijua wazi kuwa anafanya kosa kwa kuifunga lakini hakuwa na jinsi, alihitaji kupumzika. Simu ile ilipowaka tu haikupita dakika moja ikapata uhai na kupiga kelele, akaitazama, Olduvai, ilijiandika katika kioo. Kumekucha! Akawaza na kuipokea akaiweka sikioni.

“TSA…” akatamka neno hilo tu na kusikiliza ujumbe utakaofuatia.

“Olduvai… fika Ikulu ndogo Mara moja. Ova!” ile simu ikakatwa.

Akiweka vifaa vyake vyema, akabeba kila alichokihitaji, zaidi ya mkoba wenye nguo aliouacha ndani ya chumba kile, Madam S hakuacha kingine, akaondoka zake.

Wakati mwanamama huyo alikuwa akisubiriwa katika Ikuku hiyo baada ya saa mbili zitakazofuata, walishtushwa kumwona akiingia langoni ndani ya dalkika kumi na tano tu. Alitenbea kwenye bustani nzui ya maua mpaka akafika kwenye nyumba ndogo iliyo pembeni ya jingo la Ikulu, akaingia na kuketi ndani yake. Dakika mbili tu Rais Robert Sekawa aliungana naye katika chumba hicho, walikuwa wawili tu.

“Selina, nilikutegemea saa mbili usiku…”

“Najua, lakini nipo hapa likizo wiki sasa,” akamjibu.

“Unajua nilichiokuitia?” Rais akauliza.

“Bila shaka, ni kifo cha Hamadou,” akajibu Madam S.

“Upo sawa, Selina kuna harakati nyingi zinaendele, lakini nataka muuaji apatikane ili tuweze kuondokana na hii aibu, mimi nimekuja hapa kwa siri tu, wanaojua nipo hapa ni wachache sana. Nitakuwa hapa kwa siku tatu, na nataka ufanye juu chini unipe mrejesho wa maana, samahani kwa kuvunja likizo yako lakini ukimaliza kazi hii utaendelea likizo yako, kazi njema!” Rais Robert Sekawa akamaliza kutoa maagizo kwa Selina.


Akiwa ndani ya chumba chake kidogo katika hoteli ile ya Sanawari, Madam S aliweka sawa vitu fulani tayari kwa kazi hiyo naliyokabidhiwa jioni hiyo. Alipanga kuja kuona harakati za kumsaka muuaji huyo lakini alipokabidhiwa sasa haikuwa kuona bali kuingia katika sakata hilo na kuhakikisha anamtia mbaroni kiumbe huyo. Kazi ya kwanza kuifanya katika hilo, mara tu alipopata kazi hiyo rasmi ilikuwa ni kuinua saa yake iliyokuwa mkobani, akaitazama na kuibofya hapa na pale kisha akaonge maneno fulani juu ya kioo cha saa hiyo na kumaliza kwa kubofya kudubwasha kingine, akaivaa mkononi mwake na kuondoka ndani ya chumba hicho.

Nje ya hoteli hiyo tayari aliikuta tax ile iliyomleta hapo ikimsubiri kwani aliita impe huduma hiyo.

“Nipeleke hoteli ya Mount Meru,” akamwambia dereva wakati akiufunga ule mlango baada ya yeye kuingia.

“Hotelini palepale au?” Yule dereva akauliza.

“Ndiyo, vipi kwani?”

“Aaaa hamna tabu, ila tu leo kuna Ulinzi taiti sana pale haturuhusiwi kuingia,” akajibu dereva huku akikunja usukani kuingia barabara kuu.

“Ulinzi! Ulinzi mbona kila siku upo?” Madam akauliza.

“Ni kweli mama upo, lakini leo umebana sana si unajua jana kuna kiongozi kakutwa amededi chumbani, hivyo muuaji anasakwa huku na kule kwa hiyo da! Tunapata shida sana. Kama upo radhi nitakushusha kwa nje basi,” akaeleza na kumaliza.

“Sasa wao wanafikiri muuajai watampata kwa hivo? Je kama ni hawara yake ndiyo kamuua inakuwaje…”

“Na hapo ndipo swali lililpo mama ‘angu,”

“Poleni sana, utaniacha nje tu hapo nitampigia mwenyeji wangu atanifuata,” Madam akaongopa.

Haikuwachukua hata nusu saa, Yule dereva akaegesha gari jirani kabisa na hoteli hiyo lakini upande wa pili wa barabara hiyo iendayo Nairobi. Madam S akatoa noti mbili za elfu tano tano, akamkabidhi yule kijana.

“Nitakupigia… Keep change!” akamwambia huku akiiacha ile tax na kuendele mbele kwa mwendo wa miguu, akipotelea kwenye vivuli vya miti vilivyofanyizwa na taa za majengo ya kuvutia. Hatua kama mia sita na ishirini hivi zikamfikisha katika moja ya baa kubwa ambayo ndani yake kulipatikana kila huduma unayoijua wewe. Magari ya kifahari yaliegeshwa nje ya baa hiyo, watu walioingia na kutoka walikuwa ni wenye pesa zao kimwonekano tu. Suti za dukani za gharama, minyororo ya madini ghali ilining’inia shingoni mwao na kuwafanya waonekane mashababi haswa. Hayo yote hayakumfanya mwanamama huyu wa makamo kuchanganyikiwa nao, kwani alijua nini anapaswa kufanya. Hatua nyingine kama ishirini na saba hivi zikamfikisha ndani ya baa hiyo ya kisasa, akapita moja kwa moja mpaka kaunta, kabla hajaifikia kaunta hiyo mbele yake akakabiliwa na mlango uliondikwa VIP. Akauendea na kuusukuma ndani, mlango ule ulipojifunga akatanabahi watu wawili wamesimama mbele yake, wakubwa waumbo, wanaume wenye nguvu. Akataka kupita katikati yao wakamzuia.

“Bibi umesoma hapo nje?” mmoja akauliza.

“Ndiyo maana nikaingia kwa sababu hata mimi sistahili kukaa huko nje, au ninyi mnanionaje?” akawauliza.

“Huku ni kwa watu maalumu, si kima mmoja anaingia,” mwingine akadakia.

“Najua, hata mimi ni maalum, sio?”

“Umaarufu wako nini nchi hii? Huku ndani watu wanauza madini, ndiyo wanaingia, bia tu shilingi 5000…”

“Wanauza madini, yana faida gani kwa Watanzania? Mimi naishi Keko, hakuna mwanamke anayenizidi kwa kuuza maandazi Keko nzima, mi nikumwa watu wengi Keko hawanywi chai, umeuaona umuhimu wangu? Haya shilingi ngapi kuingia kama kuna kiingilio,” Madam S akadakiza kusema, na mara hiyo mmoja wa wale vijana akasogea pembeni huku akiwa mkono mmoja wapo kainua upindo wa koti lake.

“Yes Sir! (…) Sawa sawa,” akaongeza na kuliweka koti lake vyema. Kisha akampa ishara mwenzake na wote wakamruhusu Madam S kuingia ndani. Ujumbe wa kumruhusu ulitoka kwa bosi wao baada ya kuona mabishano yale kupitia kamera zake za CCTV zilizofungwa kwa siri katika eneo hilo la mlango.


Ndani ya ukumbi huo mkubwa wenye vikolombwezo vingi, Madam S alilakiwa na mataa ya rangi rangi yaliyokuwa yakizunguka huku na kule na kubadilisha kabisa mandhari ya ndani humo. Upande wa mbele juu kulikuwa na maandishi makubwa yaliyosomeka Mererani huku yakijibadilisha rangi, mara hii na mara ile.

“Karibu Mererani!” sauti nyororo ya kike ilimkaribisha, alipogeuka alikutana uso na mwanadada mrembo, aliyevalia nguo nyepesi ya kutepeta iliyouoneshwa mwili wake sawia kabisa. Umagharibi umetuaharibu, Madam akawaza.

“Asante sana!” akaitikia.

“This way please…” Yule mwanadada akamwambia na kumwonesha kwa ishara ya mkono huku yeye mwenyewe akitangulia. Madam S hakuona tatizo, akamfuata Yule dada na kuzipita sehemu kadhaa ambazo aliona watu walioketi kwenye masofa ya gharama, wakinywa mapombe makali, wengine wakikumbatia na kupigana mabusu na wasichana waliokuwa ndani humo.

Mlango wa kioo kizito ukafunguliwa, Madam S akaingia ndani yake na kumwacha Yule msichana palepale nje.

“Ingia paleee!” sauti ya kijana mmoja ikamwambia, akaongeza na kuingia ndani ya mlango wa pili ambao ulimfikisha kwenye sebule kubwa na ya kisasa, iliyosheheni samani za hali ya juu na kila kitu ambazho mwanadamu angepaswa kuwa nacho ndani.

“Naitwa Abiseilim, wewe ni nani?” mtu mmoja mwenye ngozi nyeupe kidogo, hudhurungi kidogo, aliyekuwa na sigga kinywani mwake alimwuliza.

“Naitwa Kadogo!” Madam S akajibu.

“Kadogo! Aaaa ha ha ha, Kadogo kanini sasa? wakati we zee zima. Hivi hebu nitazame, we una akili hauna, umekosa cha kufanya, nani aliyekwambia uje humu ndani? Hii ni sehemu ya wenyewe, watu wa umri wako mwende vilabu umiza mkanywe wanzuki. Tazama umezeeka halafu huku kufanya nini” Abiseilim alimwambia Madam S huku akimzungukazunguka.

“Mh! Sikiliza bi kizee, hapa huwa wanaingia mabinti wabichi, tunawafanyia usahili kama wanafaa kuwa humu kisha wanabaki humu na kulipwa pesa nyingi. Mabinti sio vi bi kizee kama wewe. Sasa wewe kwa kuwa umeingia mwenyewe hutatoka mzima,” akaendelea kusema.

“Ina maana mnaua watu?” Madam akauliza.

“Ndiyo, mtu yeyote asiyestahili kuingia humu akaingia anauawa, sisi kuua ni kazi kama ya kuua mbu tu. Yeyote tunayetaka kumuua sisi tunamuaa tu ilimradi iwe faida kwetu, awe Waziri, awe Rais, awe Balozi, tunauwa tu,” Abiseilim akaendelea kumwambia.

“Kwa hiyo na mi mnaniua?”

“Ndiyo tunakuua vizuri kabisa, hata hutosikia maumivu,” akajibiwa.

“Mnaniua kama mlivyomuua Hamadou?” swali hilo la Madam S lilimfanya Abiseilim kusimama badala ya kuendelea kumzunguka mama huyo.

“Inaonekana unajua mengi ee? Umejuaje kama sisi ndiyo tumemuua Hamadou?” akauliza.

“Si umesema ninyi mnaweza kuua mtu yeyote, sasa nilifikiri ndiyo ninyi mliomuua Hamadou,” Madam S akaendelea kudadavua.

“Ha! Ha! Ha! Ha! Hatuwezi kuua kimburu kama yule, hana faida kwetu, wamemuua wenyewe viongozi wenu wa serikali yenu. Ulikuja kuuliza hilo tu au kuna lingine?” Abiseilim akauliza.

“Ni hilo tu nilitaka kujua, kumbe sio ninyi, ok, asanteni naomba niende,” aliposema hilo akageuka na kuvuta hatua lakini alizuiwa na kifua kipana cha dume lililosimama hapo mlangoni. Lile jamaa likamwonesha ishara kuwa anatakiwa aende upande mwingine na sio huo. Alipgeuka kuotoka akakutana na wengine wawili huku Abiseilim akiwa kando. Amadam S akajishika kiuno.

“Mnataka nini kwangu?” akauliza. Lakiniw ale jamaa ndiyo kwanza kila mmoja wao akakusanya mikono yake iliyoshiba mazoezi kifuani mwake.

“Nilishakwambia, kila aingiaye hapa kwa kukosea huwa hatoki akiwa hai,” Abiseilim akadakia kujibu kisha akawapa ishara wale jamaa wafanye kazi yao. Mmoja wao alipokuwa anataka kumvamia Madam S, tayari mwanamama huyo kwa wepesi wa ajabu alichomo bastola zake mikono yote miwili. Kwa shabaha nzuri, alimfumua kifua Yule wa mbele kisha akaruka na kujitupa upande wa pili nyuma ya kochi. Wale jamaa nao wakachomoa bastola zao na kukimbilia upande ule alikotua Madam S.

“Kill her!” Abiseilim alipiga makelele huku akibofya kengele ya dharula. Kutoka nyuma ya kochi Madam S alijiviringa chini na kuingia ubungu wa meza, wale jamaa walipofika nyuma ya kochi, yeye akaibukia upande wa meza kubwa ya chakula, akamwaga risasi na kuwaangusha wote wawili. Mlango ukafunguliwa na vijana wengine kama watano hivi wenye silaha wakaingia. Madam akainuka na kukimbia kwa kupita kwenye korido ndefu, huku risasi zikimkosa kosa hupa na pale. Kwenye korido hyo kulikuwa na dirisha pembeni yake, dirisha la kioo lililoshikwa na nguzo za aluminium, akafuatua risasi moja litawanyika, akachumpa na kutua upande wa pili, akaingiza mkono ndani ya koti lake na kutoa, smoke grenade ndogo, akaifyatua kijizibo chake na kulirusha kwenye ile korido kisha yeye akakimbia juu ya huo ubaraza ndipo alipogundua kuwa kwa upande huu jingo hilo lina ghorofa kwa kuwa lilijengwa mlimani, hakujali alitazama huku na kule kulikuwa na kamba ya kuanikia nguo, akaifyatua upande mmoja na kuteremka nayo mpaka chini kabisa.

Ule moshi mzito uliojaa muwasho uliwasumbua wale vijana wakakohoa na kutoa machozi huku wengine wakivujwa na makamasi mazito. Vifaa maalumu vya kusafisha hewa vikawashwa na ule moshi ukaondolewa mara moja lakini wale jamaa walibaki hoi.

IRINGA

RIVERSIDE CAMP

GIZA LILIZIDI UZITO baada ya miti mingi katika eneo hilo kuinyima uhuru mbala mwezi wa kuling’aza eneo hilo. Akiwa kaegemea ukingo wa kibaraza kwa nje akichezea simu yake hapa na pale akahisi mgongo wake ukipapaswa kimahaba. Ulaini wa mkono ule wala haukumpa taabu kujua ni nani alikuwa akifanya hivyo.

“Umeamka?” akauliza bila kugeuka.

“Ulitaka nilale moja kwa moja au?”

“Hapana, sasa wewe ukilala moja kwa moja nani atanipapasa mgongo kama hivi?” akageuka na kumtazama mwanadada huyo, mfupi, kibonge wa wastani, vazi lake jespesi la usiku alilizungush mwilini na kulikusanya katika kifua chake. Macho yake madogo yalijizungusha kama kinyonga ijapokuwa yalikuwa mazito kama mtu mwenye usingizi lakini sasa analazimisha kuyafungua.

“Twende tukalale dear!” yule mwanadada akamwambia mwandani wake.

“Mbona mapema? Saa nne sasa kwa nini tusiende kutazama sinema hapo ukumbini?” akamwuliza.

“Aaaaa no Mr. Spark, nahitaji joto lako bebi wangu, si unajua huku Iringa baridi sana,” mremboa akalalamika mara hii akiwa tayari kifuani mwa bebi wake, Mr. Spark.

“Mmmm! Kisa, una maneno sana binti wewe, haya twen’zetu,” Kamanda Amata akamnyanyua Kisa kwa mikono yake yenye nguvu na kuingia naye ndani ya chumba hicho cha kuvutia kilichoezekwa kwa nyasi na kujengwa kwa miti.katika eneo hilo kulikuwa na vibanda vingi vya mtindo huo ambavyo watalii wengi walipenda kupumzikia hapo na wazawa wengi walipenda kuja kufanya picnic katika uwanda mzuri wa nyasi ulio kandokando ya mto Ruaha.

Amata akamtupia Kisa kitandani kisha akatua juu yake na kuanza kubingirishana, mitekenyo na vicheko vya mahaba vikatawala huku taa ya chemli iikiwaka kando yao.

Ni wakati wakiwa katikati ya starehe hiyo ndipo Amata aliposikia ukulele wa saa yake ambao kama si mzoefu wa saa hiyo unaweza kufikiri ni mlio wa mdudu fulani. Akasitisha manjonjo juu ya mwanadada huyo mrembo, na kuinyakua ile simu, akabofya katika kinobu fuloani na kuiruhusu iingize ujumbe huo uingie.

“Mama anaumwa sana, fika hospitali ya Mount Meru haraka. Tena Sana Aisee!”

Ujumbe ule ulimalizika na kile kijimkanda kikakatika. Kamanda Amata akashusha pumzi ndefu na kujitoa kifuani mwa Kisa.

“Bebi vipi tena, mbona waniachia njiani mwenzio ah!” Kisa, alilalamika huku akijigeuza kitandani na kulala kifudifudi akilia kwa vikwifukwifu. Amata aliingia maliwato haraka haraka na kujimwagia maji, akatoka na kutafuta jinzi lake safi na fulani iliyomkaa vyema mwilini.

“Mbona sikuelewi we mwanaume, unavaa mijinzi yako unaenda wapi?” Kisa akauliza.

“Kisa mpenzi, nimepata dharula, yaani mama anaumwa na mimi ndiyo mtoto pekee ninayetegemewa, wacha niende…”

“Aah masikini mzaa chema, mpe pole au twende wote,”

“Hapana, mpaka hapo upendo wako kwa mama umeonekana, nitampa salamu za mka mwana na akipona nitakuita uje umsalimu,” akamjibu huku akipaki begi lake la mgongoni tayari kwa safari.

“Sasa basi gani saa hii mpenzi? Kama za Arusha zinaondoka saa kumi na mbili asubuhi,” Kisa akauliza.

“Aaaa usihofu, ukiwa mwanaume ujifunze kupiga kambi popote na kuondoka muda wowote hata kama hakuna usafiri,” akamjibu na simu yake ikaita hapohapo, akainyanyua na kuiweka sikioni.

“Hello Mr. Spark, Auric Air hapa tunaongea,”

“Ndiyo!”

“Ndege imeshaondoka hapa Dar, itakuchukua na kukupeleka Arusha usiku huu, asante na usiku mwema,” ile simu ikakatika.

“Kisa, amka twende!” akamwamuru mrembo huyo.

“Aaaa mi nna usingizi,” aliajiu huku akiamka na kuingia bafuni wakati Amata yuko nje akipanga hili na lile.

Nililitegemea hili, akawaza. Na wakati huohuo Kisa akawa tayari, wakakiacha kibanda

hicho na kukuta gari ikiwasuiri.

“Pole sana Mr. gari hii itakufukisha uwanja wa Ndege, karibu tena Riverside Camp,”

kijana mmoja wa kizungu aliongea Kiswahili safi na Amata akamwelewa vyema. Usiku huo safari ya kuelekea Nduli, uwanja wa ndege wa mkoa wa Iringa ikaanza. Walitoka kule porini na kukunja kushoto kuingia barabara ya Mbeya, kilomita kadhaa mbele waliiacha barabara hiyo na kupanda mlima mkubwa mpaka Iringa mjini ambako waliongoza na barabara ya Dodoma kuelekea Nduli Airport.

Ulikuwa mwendo wa nusu saa tu waliwasili uwanja wa ndege.

“Kisa, nakupenda sana, ngoja nione hali ya mama kisha nitakujulisha,” Amata alimkubatia Kisa na kumpa maneno hayo ya kumuaga, akachomoa noti ya dola mia moja, “Hii utachenji pale benki, ya kwako,” akamaliza kusema na kumwachia mrembo huyo.

“Nitakumiss Spark, maana sparks zako zimeniwasha moto wa mapenzi, bye bebi, salamia mzaa chema!” Kisa alimuaga Amata huku chozi likimdondoka, akarudi kwenye gari na kuondoka eneo lile. Auric Air ilikuwa ikiweka magurudumu yake ardhini tayari kwa kazi iliyopewa ya kumfikisha Kamanda Amata katika jiji la Arusha.

ARUSHA – saa 6 usiku

BARIDI KALI LILIZIZIMA katika jiji la Arusha, Kamanda Amata alipokuwa akiteremka katika Ndege hiyo ndogo ya kukodi. Akavuta hatua chache na kulifikia jingo linalotumiwa na watu wa uwanja huo. Alipomaliza itifaki za uwanjani hapo, alitoka nje na kuangaza angaza macho yake. Akaliweka begi lake chini na kutazama saa, kisha akarudisha tena mkono mahali pake na kunyanyua lile begi.

“Karibu Arusha!” sauti ya kike ilimkaribisha, alipotupa macho upande huo alikutana na binti mrefu, sio mnene sio mwembamba, kwa harakaharaka alikuwa na sura ya Ki-mburu.

“Asante sana! Wapi gari?’ akaitika na kuuliza.

“Gari kule!” akajibiwa na yule binti, kisha wakafuatana kimya mpka kwenye gari moja ndogo, Nissan Sunny, wakaingia.

“Pole kwa safari!”

“Asante,” akajibu wakati ile gari ikiingia barabarani na kuondoka. Kimya kilichukua nafasi, hakuna aliyekuwa akiongea na mtu kwenye gari hiyo, mpaka walipolipoingia katikati ya jiji hilo.

“Leopard Hotel yatakuwa makazi yako kwa muda wote uwapo hapa Arusha,” Yule binti akamwambia Amata wakati akikunja kona kuingia katika hoteli hiyo maeneo ya Njiro.

“Asante sana, nani kanichagulia hoteli nzuri kama hii?” akauliza wakati akishuka.

“Mimi,” akajibu yule binti.

“Asante, inaonekana unajua kuchagua hoteli, bila shaka utakuwa mwenyeji wangu pia,” akamwambia akiwa ameinama ili kuchungulia ndani maana gari ile ilikuwa fupi mno.

“Yeah! Una lingine?”

“Na utaniburudisha pia…”

“Mxiuuuuuuuiy!” yule binti akasonya na kuondoka gari akimwacha Amata akitabasamu. Kamanda Amata, aliweka begi lake vyema kabisa mgongoni, akaitazama ile hoteli kisha akageuka na kuuelekea lango la kuingilia hoteli ile. Akatoka nje, utulivu wa mji huo ulifanya usiku uonekane. Akaiendea moja ya gari iliyoonekana kama tax hivi, akagonga kwenye kioo na kijana aliyekuwa amelala ndani yake akakurupuka.

“Kaniache Sakina tafadhali,” akamwambia huku akiketi katika kiti cha nyuma na ile gari ikaondoka katika eneo lile.

Dakika chache wakawasili Sakina, kitongoji chenye kila aina ya uswahili japokuwa waishio hapo si waswahili.

“Panatosha!” akamwambia dereva naye akaegesha gari kando ya barabara. Baada ya malipo, Amata alisubiri kuhakikisha ile gari imeondoka eneo lile, akavuta hatua ndefundefu na kupotelea vichochoroni.

“Hey!” sauti ilitokea vichochoroni katika lindi la giza, Amata akajifanya hakusikia akaendelea na safari yake.

“Oya, unasikia au husikii?” sauti nyingine ikamfikie, lakini Amata akaendelea na safari. Nyuma yake akasikia vishindo vya watu kama wawili wanamfuata, akasimama na kugeuka. Mng’aro wa panga lililopungwa hewani ukamfikia Amata machoni, kwa wepesi wa ajabu akaudaka mkono wa Yule kijana na kuuzungusha kwa nguvu.

“Aaaaaaiiggghhh!” akapiga kelele. Amata akamwachia na kumdaka mwingine akampiga kichwa cha maana yule kijana akaenda chini na mmoja aliyebakia akaona ‘isiwe tabu’ akatimua mbio. Akawaacha pale chini, mmoja kavunjika mkono na mwingine kapoteza fahamu. Katika pitapita usiku huo akakutana na doria ya polisi.

“Polisi! Simama,” akaamuriwa naye akasimama. Vijana wawili waliokuwa na makoti marefu na bunduki mikononi mwao wakamwendea.

“Nyie ndio wazururaji tunaowatafuta! Chuchumaa chini…”

“Fanya haraka wewe, ala!” mwingine akadakia na kumtandika mbata ya maana, Amata akachuchumaa.

“Enhe haya, unakwenda wapi usiku huu?” akauliza polisi mwingine wa kike aliyeonekana kajaa nyama za mwili maana jinzi aliyovaa ilikuwa imembana haswa na kuiruhusu hipsi za matamanisho kuonekana wazi pasi na kujificha. Fulani iliyoandikwa ‘FUBU’ iliubamba vyema mwili wake na kuionesha maziwa yaliyojaa sawia kifuani pake.

“Natafuta pa kulala afande!”

“Unatoka wapi?”

“Natoka Iringa, nimeingia na basi la Hood usiku huu,” akawaeleza.

“Ok, vyema, haya usiku saa hizi, kila atembeaye usiku ni mkora. Afande Juma, mpekue huyo!” afande mmoja akiweka bunduki yake mgongoni na kumsogelea Amata, akamgusagusa sehemu za mbavuni, kiunoni, mapajani na alipofika kwenye soksi alihisi kitu kigumu, alipovuta ile jinzi, akatoa macho.

“Vipi afande mbona umepoa?” Yule mwanamke akauliza.

“Asee hili ni rijambazi, lina bastola,” kauli ile ikawafanya wale wenye bunduki kuziweka sawia.

“Si ajabu na hilo begi lina silaha nyingine hebu pekua,” amri ya Yule mwanamke ikasikika, huku akiwasha redio kolu yake na kuisogeza kinywani.

“Maeneo ya Sakina, operesheni konokono, ova!”

“Umesomeka afande, lete habari, ova!”

“Tumemkamata mtu mwenye silaha, akiwa kama msafiri, tuna wasiwasi anaweza kuwa tunayemtafuta, ova!”

“Mlete haraka kituoni, watu tunaumiza vichwa na wenyewe wakaura maisha, lirete haraka, ova and out!”

Amata akafungwa pingu na kupakiwa kwenye Land Cruiser, na kupelekwa kituo kikuu cha polisi.

***

Usiku uleule, Amata alifikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, barabara ya Makongoro. Alipoteremshwa tu moja kwa moja akaswekwa rumande.

“Asee hili jamaa ni rijambazi kweli, ona, bastola hii, kisu hiki umekiona, du! Hapana taarifa yake ifike panapohusika mara moja,” mmoja wa askari aliyekuwa doria aliwaambia wenzake wakati akiweka mahali salama vifaa vya Amata kwani ndani ya selo hile hakuruhusiwa kuingia na mkanda, viatu wala saa, vyote aliviacha kaunta pamoja na begi lake.

Dakika kumi baadae, mkuu wa upelelezi mkoa alifika akiongozana na Kamanda wa polisi kwa tofauti ya dakika chache.

“Yuko wapi huyo mtu?” Mkuu wa upelelezi akauliza.

“Yuko selo afande!” kijana wa kaunta akajibu huku akiwa kakakamaa kama muogo wa kukausha.

“Mtoe umlete maelezo,” akatoa amri na kuingia katika chumba fulani kitupu kilichokuwa na meza moja pamoja na viti viwili vya chuma. Dakika moja tu kama sio mbili Amata aliletwa pale na kuketishwa kitini akiwa kafungwa pingu mikono yake na miguuni minyororo. Akaketishwa kwa kusukumwa tu. Yule mkuu wa upelelezi akasogea mbele ya Amata huku pembeni kukiwa na Kamanda wa mkoa pamoja na askari mwingine aliyekuwa akiandika maelezo hayo.

“Wewe ni jambazi sivyo?” akulizwa.

“Hapana afande mi siyo jamabazi na wala siujui,” akajibu Amata.

“Wewe ni jambazi, kwa nini unatembea na bastola kama hii? Na hiki kisu tazama, isitodhe kumekutwa vitu visivyoeleweka katika begi lako. Kama sio jambazi we nani?” akang’aka yule mkuu wa upelelezi.

“Afande nimeshakwambia mi sio jambazi, sasa unanilazimisha kuwa mi ni jambazi?” Amata naye akaja juu huku mishipa imemtoka.

“Sasa wewe ni nani?”

“Mimi ni mfanyabiashara, mkurugenzi wa AGI Investment ipo Dar es salaam, na huku nipo katika biashara zangu, nimetoka Iringa usiku huu kwa Ndege nimekuja Arusha, vijana wako wamenikamata,” akaeleza.

“Aaaaa ha ha ha ha sikia wewe bwege jambazi, mfanyabiashara gani anamiliki bastola kama hii. Unaitwa nani?” akauliza.

“Mr. Spark,”

“Spark? Yaani hilo ndilo jina lako?”

“Ndiyo!”

“Ok, huyu ni jambazi na inawezekana anahusika na mauaji ya kule hotelini, naomba mumbane mpaka aseme yote,” Kamanda wa Polisi wa mkoa akatoa amri. Amata akapewa mateso na wale vijana lakini hakuna maelezo ya zaidi waliyoyapata kutoka kwake.

“Sasa utaseme au hutosema?” akaulizwa.

“Yaani hata mkinikata kichwa, mi sio jambazi na wala sijui hayo mnayoyaongea ya mauaji ya hotelini.

“Lirudishe sero, kesho kuna watu watakuja labda wao atawajibu”. Amata akarudishwa selo akiwa kifua wazi kwani shati lake lilivuliwa wakati wa kile kibano. Akasukumiwa ndani huku mlango ule wa chuma ukifungwa kwa nguvu.

Chumba kidogo, chenye joto na harufu mbaya na kali, hakikuwa na taa ila kidirisha kidogo sana kilionekana juu karibu na paa.

“Sorry man!” alimwomba msamaha jamaa aliyemwangukia baada ya kusukumwa.

“Usijali kaka, ndiyo nyumba yetu hii, tutafanyaje sasa…” yule jamaa alimjibu kwa sauti mbaya ya kukwaruza.

“Vipi man, naona jamaa walikutaiti kinoma, mpaka RPC mwenye we katia timu! Jomba we piganaji nini!” jamaa mwingine aliyejilaza sakafuni akaongeza kwa utulivu.

“A achana nao hao, wanadai mi nimehusika na ishu ya kule hoteli,” Amata akaeleza.

“Kule, aaaaah! Wanajisumbua hao, na watatafuta mpaka wakome, jamaa kishapaa kitambio Yule, kapiga kaunta attack zake kasepa, watu washakula hela,” akaeleza yule kijana huku akiinuka na kuketi, “Unasikia chalii, wale wakimataifa, we ulinzi wote na mtu katoboa, hapohapo mlipo mtu shaaaaa anafanya yake, tuna polisi sisi au takataka,” akajilaza tena.

“Ah nd’o hivo si unajua juya likizama majini kila kitu linabeba, nyoka mtasema samaki…” Amata akaongeza.

“Yule jamaa kwenye kona yule pale yule, Yule anafanya kazi palepale hotelini, wamemtesaaaa we sasa kijana wa watu yuko hoi, leo kesho tunaimba ‘tumpeleke baba huyu’…” yule kijana akaendelea kubwabwaja, Kamanda Amata akatupa jicho kwenye ile kona na kumwona mtu kalala kimya bila kujitikisa.

“Anaongea?” Amata akauliza.

“Anaongea hivohivo kwa tabu ka’ anakata roho vile, mcheki umsikie”.

Amata akajivuta na kuwaruka wengine watatu waliokuwa wamejilaza kwenye hiyo sakafu chafu, akamfikia yule kijana pale kwenye kona, alimtazama haraka haraka na kumgeuza upande wa pili, yule jamaa akashituka.

“Vipi?” Amata akauliza.

“Vipi nini! Hebu toka zako huko,” yule kijana akaonge kwa taabu sana. Amata akamwinamia sikioni na kumnong’oneza, “Ukiongea na mimi kesho tu utatoka humu!” yule kijana akaonekana kama kapata uhai hivi akamtazama Amata lakini asimwone sawasawa kutokana na giza lile.

“Kwa nini wamekuweka humu?” akaanza kuongea naye kwa kunong’ona.

“Aaaa tulikuwa wengi, wenzangu wametoka nimebaki mimi,” akajibu.

“Unaitwa nani?”

“Winifredi Kimario,” akajibu kisha akakohoa sana mpaka akatema kitu kama damu pembeni ya ukuta. Baada ya hapo walizungumza mengi kwa kunong’ona hivyohivyo huku mara kwa mara afande akiwapigia kelelel kuwa asisikie hiyo minong’ono.

SIKU ILOFUATA

MADAM S ALISHANGAZWA kwa ukimya wa Amata, ina maana hakusafiri au ilikuwaje? Akajiuliza lakini moyoni mwake akiweka mambo mawili, ama hajasafiri au ametekwa pindi tu alipokanyaga Arusha kwani mara nyingi hizo ni mbinu ambazo hutumiwa na adui hasa akiweza kunasa mawasiliano yenu. Alichukua simu yake na kuwasiliana na watu wa shirika la Auric Air wakamwambia kuwa kijana huyo alitua Arusha saa sita za usiku jijini hapo. Atakuwa ametekwa? Mh! Sasa kazi inaanza, akawaza tena na kuchukua uamuzai wa kwenda Ikulu ndogo ambako itifaki zote zinatakiwa kufanyika huko.

Aliwasili kwa kutumia tax, alipofika katika moja ya ofisi aliyokuwa akiihitaji akaomba kujua kama Mr. Spark alipokelewa au la, jibu alilopewa ni kuwa alipokelewa na kufukishwa Hoteli ya Leopard saa saba na dakika arobaini na tano usiku. Akaaga na kuondoka zake, akachukua tax mpaka katika kampuni ya kukodisha magari, akakodi Peugeot 405 ya kizamanai kidogo, na taratibu akaelekea huko Leopard.

Ktika hoteli hiyo ndiko alikoshtushwa zaidi kwani hakukuta taarifa yoyote ya kijana huyo, isitoshe aliambiwa kuwa hata chumba chake funguo bado zipo pale kaunta. Madam S alirudi ndani ya ile gari, akainua mkono wake na kuitazama saa yake ilimwonesha kuwa ni saa tatu asubuhi. Ooooh Kamanda uko wapi? Akajisemea moyoni huku akiwasha gari na kuiondoa mahali hapo, akiwa njiani, simu yake ikaita, hii ilikuwa ile simu anayoitumia kuwasiliana na kila mtu. Akaitazama, namba ngeni, ikakatika. Sekunde kadhaa ikaita tena, mara hii akaegesha gari pembeni na kuipokea.

“Mama, unaongea na mwanao wa kwanza hapa, nipo kituo cha polisi cha kati Arusha, nimekamatwa,” sauti ya Amata ilimfikia Madam S moja kwa moja.

“Ok, nakuja sasa hivi!” kisha akakata simu. Akawasha indiketa ya kulia na kuingia barabarani, akaendesha kilomita kama tatu hivi akakunja kushoto na kuchukua barabara ya kuelekea Njiro, lakini aliiacha na kuingia barabara ya Makongoro mpaka katika kituo hicho. Akaiacha gari maegeshoni na kuelekea kaunta ya kituo hicho.

“Karibu mama, karibu sana,” mmoja wa polisi pale kaunta akamkaribisha.

“Asante, eee nimekuja kuna kijana wangu amekamatwa na yuko hapa,”

“Anaitwa Spark,” akaeleza.

“Aaa ok, Spark jambazi? Haya pita hapa ingia mlango namba nne pale,” akaelekezwa naye akauendea mlango huo, alipoufungua akakutana na Mkuu wa upelelezi wa mkoa akiwa na vijana wawili mmoja wa kike na mwingine wa kiume, wote walionekana ni polisi kwa jinsi tu walivyo, Madam S alitanabahi hayo kwa haraka haraka.

“Karibu mama, karibu kiti,” yule mkuu akamkaribisha, “bila shaka ni mzazi wa Spark!”

“Ndiyo, mwanangu yuko wapi?”

“Mwanao tumemkamata jana, ni jambazi anayetumia silaha,” yule mkuu wa upelelezi akamwambia Madam S.

“Una uhakika na hicho unachokisema?” Madam akatupa swali.

“Ndiyo, hawa hapa ndiyo waliomkamata jana usiku,” akasema. Madam S akawaangalia wale askari wawili.

“Mlimkamata mwanangu akiwa anavunja nyumba?” akawauliza.

“Hapana mama, mwanao anatembea usiku na silaha ya moto, na kisu, huyu ni jambazi!” yule askari wa kike akaongeza kwa kujiamini.

“Mimi ni jambazi?” Madam akauliza, “Niangalie…”

“Mama we labda hujanielewa…, nimesema mwanao tumemkamata akiwa na silaha ya moto usiku wa manane…”

“Mlipomhoji aliwaambiaje?” akadakiza swali.

“Alijitetea kuwa yeye ni mfanyabiashara…”

“Na usiku huo alikuwa akitoka wapi?” akaongeza swali.

“Alijitetea anatoka sijui wapi…”

“Iringa!” akadakia yule askari wa kiume.

“Sasa mlichukua hatua gani kujua ukweli kuwa anatoka Irimga au la?” kimya kikapita kila mmoja ana jibu.

“Mkuu wa upelelezi mkoa, niambie mmechukua hatua gani kuhakiki kuwa yeye ni mfanyabiashara, na alikuwa anatoka Iringa?” akauliza tena, mara hii kwa Mkuu wa upelelezi, kimya kikabaki palepale.

“Nifungulieni mwanangu! Tena msiniuzi! Nani anayewapa vitengo hivi ilhali hamjui kazi mnayotakiwa kufanya? Mfungulieni namtaka hapa, kakamateni majambazi sio watoto wa watu,” Madam akamaliza kusema na wote wakabaki kimya.

“Afande Tuli,” yule Mkuu wakaita kwa upole, “Kamlete,” akamwambia.

Kamanda Amata akaletwa katika kile chumba na kusimamishwa kando akiwa amechoka.

“Pole son!” Madam akamwambia Amata, kisha akawageukia wale polisi, “Nipeni vitu vyake,” akawaambia. Vifaa vikaletwa, begi, waleti, mkanda, viatu, vikawekwa mezani.

“Son, ndo hivi tu?” akaumuuliza Amata.

“Hapana, kisu na bastola yangu havipo,” akasema.

“Haya, kisu na bastola leteni,” Madam akaomba.

ITAENDELEA

Pasipoti Ya Gaidi Double Agent Sehemu ya Pili

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment