Pasipoti Ya Gaidi Double Agent Sehemu ya Pili
NEW AUDIO

Ep 02: Pasipoti Ya Gaidi ‘Double Agent’

Pasipoti Ya Gaidi Double Agent Sehemu ya Pili

IMEANDIKWA NA : RICHARD MWAMBE


Simulizi : Pasipoti Ya Gaidi ‘Double Agent’

Sehemu Ya Pili (2)

“Samahani mama, bastola hatuwezi kukupa mpaka tuichunguze kama ina vibali, mji wa Arusha umeharibika sana siku hizi kwa ujambazi,” yule mkuu akaeleza.

“Zile bastola za Mererani mmezichunguza? Nipeni hiyo bastola sitaki maneno,” Madam akasimama, na yule mkuu akasimama, akatoka ofisini na dakika moja akarudi na ile bastola na kumkabidhi Madam pamoja na kile kisu. Akaipoke na kukamata sawasawa, akaislide pale juu na kuhakikisha ipo ok. Akamrushia Amata naye akaidaka na kuipachika kiunoni.

“Kwa herini,” akawaaga na kuondoka na kijana wake. Wale polisi wakabaki wanashangaa tu na ubabe wa yule mama. Walijikuta wakitii kila walichoambiwa na mama huyo pasi kuwa na jibu.

“Anajiamini kwa pesa zake siyo?” yule askari mwanamke akauliza.

“Mwache, tutambambikia kesi na hizo pesa zake tuone kama zitamsaidia. Ila sasa tutamweleza nini OCD juu ya hili?” Mkuu wa upelelezi akauliza kwa shaka.

“Aaaa sasa hapo nd’o pazuri, alikja mama yake akajifanya anajuana na viongozi kamtoa mwanae kibabe, mtiti unaanza upya,” yule dada akaeleza.

“Aaaaaa safi sana, hiyo pointi,” akajibiwa.


Madam S alimfikisha Amata katika hoteli ya Kundayo, “Vipi panakufaa hapa?” akamwuliza.

“Bila shaka, maadam umenileta wewe basi umejua kuwa panafaa,” Amata akajibu. Akateremka na kuchukua begi lake.

“Saa saba na nusu tukutane lunch pale Hoteli ya City Link,”

“Sawa!” akajibu na kupotelea ndani ya ile Kundayo Lodge.

Mwanadada wa kaunta alimkaribisha kwa bashasha kana kwamba anamjua siku nyingi.

“Kaibu mgeni,” akamkaribisha na kumpa funguo ya chumba.

“Asante sana, nimekaribia,” akajibu huku akipokea ufunguo ule na kuvuta hatua kuelekea ndani, lakini aligutushwa na sauti ile ya yule mwanadada kutoka pale kaunta.

“Samahani bro’ kuna mzigo wako hapa,” akatoka kaunta na kumkabidhi Amata boksi dogo lililofungwa barabara kabisa.

“Umetoka wapi?” akauliza.

“Umeletwa na kijana mmoja kama dakika kumi kabla hujafika,”

“Jina lake…!”

“Hapana hakutaja jina lake,” akamwambia huku akiondoka. Amata akamtazama yule mwanadada akitembea kurudi kaunta huku eneo la nyuma likichezacheza na kumfanya kijana huyu kumeza mate ya tamaa. Hii ndiyo Arusha, akawaza huku akigeuka na kuondoka alipohakikisha mwanadada huyo keshapotelea ndani ya ofisi yake.

Ndani ya chumba kipana, chenye kitanda kikubwa cha sita kwa tano, shuka safi jeupe lenye maua mazuri lililobeba blanketi zito ambalo lilikunjwa juu yake, kabati kubwa pembeni na meza ndogo yenye kiti kimoja kizuri. Akatua lile box kitandani, akachomoa kitu kama simu ndogo katika begi lake na kukiwasha, kisha akatembea nacho kila kona ya kile chumba ili aone kama kuna kitu chochote alichotegewa kiwe cha mlipuko au cha kunasa sauti, hakuna. Akaketi kitandani na kufungu lile boksi, ndani yake kulikuwa na miwani moja nyeusi kabisa, akaiinua na kuigeuzageuza, akaielewa. Taratibu akaipachika machoni pake na kuvuta kijiwaya kidogo chenye kifaa cha sikio akakipachika sikioni na kubofya kitufe kidogo pembeni yake.

“….TSA 01” sauti ilisikika kutoka kwenye ile miwani huku kwenye vioo vyake akiona picha tofauti zikibadilishana.

“…nilijua kuwa utafika hapa Arusha kwa kazi hii. Sikiliza, kazi hii ni ngumu kuliko inavyoonekana, Mwenyekiti wa Baraza la Usalama, Dr. Hamadou ameuawa na wauaji wenye taaluma hiyo ambao unawajua na uameshawahi kukutana nao. Walikuwa hapa Arusha tangu mwanzo wa mkutano. Bahati mbaya hivi sasa sijui wako wapi. Lakini unatakiwa kudeal na huyu (ikaonekana picha ya Kubrah Khaleb) huyu alikuwa hapa Arusha mpaka ninapokutengenezea ujumbe huu, naye ni mmoja wa mtandao huo, kisha jicho lako liweke kwa huyu (ikaonekana picha ya Benzilahagi) huyu naye alikuwepo hapa. TSA 01, nakuhakikishia hakuna mtu yeyote anayeweza kuwadhibiti watu hawa zaidi ya wewe tu, ukichelewa kuwadhibiti hawa kuna madhara makubwa yatakayolikumba Taifa ndani ya siku ishirini tu. Najua unawajua lakini najua kuwa hujui kwa sasa wako wapi. Walikuwa hapa Arusha lakini kwa sasa wamepotea kabisa, macho yangu yote hayawaoni, hivyo una kazi kubwa na kati ya hao wawili, mmoja wapo ndiye alifanya mauaji kule hotelini. Sina mengi ni mimi yuleyule…”

ile sauti ikakatika na vile vyoo vya ile miwani vikawa vya giza vizivyoonesha hata mbele kuna nini. Akaivua huku moyo wake ukiwa unadunda kwa nguvu.

Benzilahagi na Kubrah wapo hapa! Akashangaa moyoni huku kifua chake kikipanda na kushuka kwa hamu ya kukutana na hao watu. Nilijua hawawezi kwenda mbali, sasa tutaumana popote walipo, akawaza na kukunja ile miwani, mlipuko hafifu ukatokea na ile miwani ikaharibika kabisa. Akabaki ameketi pale kitandani huku akiwa hajui ni wapi ile miwani imetoka, ni mara kadhaa amepata ujumbe kwa mtindo huo bila kujua ni nani anayempatia, hilo halikumsumbua alijua tu kuwa wako wengi. Akakurupuka na kuingia bafuni ambako alioga na kurudi kuvaa nguo nyingine kabisa. Mara hii alitupia jinzi ya khaki, na fulani kaba shingo na jaketi moja juu yake ambalo ndani yake aliweka silaha zake kama kawaida na vifaa muhimu atakavyovihitaji. Vilivyobaki akaviweka vizuri kabisa katika begi lake na kulihifadhi kabatini. Bastola mbili alizipachika sawia katika jaketi lake na kutoka nje ya hoteli hiyo.

“He jamani hata upumziki?” yule mwanadada wa kaunta alimwuliza huku akimtupia jicho la wizi kijana huyo.

“Aaaa nimeshindwa kwa kuwa sina wa kupumzika naye, au…” Amata akaanza maneno yake ya uchokozi.

“Au nini? Malizia,”

“Labda wataka kunipumzisha!”

“Aaaa no we! Nina mume mimi isitodhe nipo kazini,” akajibu yule dada.

“Anhaaa kwa hiyo usingekuwa kazini ingewezekana? Ok!” Amata akajibu na kumpa kadi yake ya kibiashara kisha yeye akaondoka zake.


Ndani ya Hoteli ya City Link, kandokando ya barabara kuu ya Arusha – Himo, kulikuwako watu mbalimbali, weupe kwa weusi waliokuwa wakipata maakuli ya mchana huo. Kiti cha kona kabisa ambacho walikubaliana kukutana hapo, bado kilikuwa hakina mtu yeyote aliyekaa, akakiendea na kujiweka hapo.

“Nipe kisichana na Sprite baridi tafadhali,” akamwagiza mhudumu aliyekuwa tayari kasimama kando yake kusikiliza ombi la mhudumu, akimaanisha apewe konyagi ndogo na sprite. Akiwa kajiinamia akipitia gazeti lililokuwa mkononi mwake akisoma habari juu ya yale mauaji ya Arusha akahisi kama kuna mtu aliyeketi mbele yake. Akainua macho na kugongana na Madam S. Na muda uohuo tayari yule mhudumu alileta kile kinywaji.

“Madam S,” akatamka.

“Kamanda, Mheshimiwa yuko Arusha, na baadhi ya mawaziri wenye dhamana. Tukio hili limeitikisa sana serikali na Afrika mashariki kwa ujumla. Polisi, Usalama wote wapo kazini, lakini tunatakiwa kuifanya kazi hii kwa siri pasi na watru kutushtukia. Safari hii upo peke yako maana siwezi kukatisha mission za wale wengine kwa kuwa zina umuhimu wa kipekee. Kama kawaida, Mkuu wa nchi anatutegemea, ameomba tuiondoa hii aiu kwenye taifa letu kwa kuhakikisha muuaji anatiwa mbaroni,” akamwambia kisha katika mfuko wa koti lake akatoa picha tatu, akamwekea mezani, Amata akazitazama kwa makini, akachukua simu yake na kuipiga picha moja wapo kisha akatuma picha hiyo kwenye identification network.

“Huyu ni nani?” akauliza.

“Abiseilim,” akajibu Madam

“Abiseilim?” Amata akauliza.

“Yes, Abiseilim, jana nimekutana naye uso kwa uso usiku, nahisi anaweza kutupa mwanga kidogo kwa maana mi niliingia kwake kimakosa inaonekana ni mtu anayejua mengi, lakini ni mtu hatari sana, jana walitaka kuniua wajinga wale,” Madam akaeleza.

“Sasa walikuwachaje?”

“Waliniachaje, walichezea kichapo cha maana, mi ndiyo head of TSA” akaeleza huku wakiendelea kinywa taratibu.

“Sasa pale polisi kuna kijana namwitaji, atanifaa kwa kazi fulani hivi, anaitwa Winifred Kimario, yeye alikamatwa na wengine wote wafanyakazi wa hoteli wakawekwa ndani. Wenzake wamaechiwa lakini yeye hali yake ni mbaya sana na bado yuko ndani, si ajabu akafa wakati wowote,” Amata akeleza.

“Ok,” Madam S akainua simu yake na kubofya namba kadhaa kisha akiweka sikioni.

“Eee Mzee Simbeye upo?” akaiita upande wa pili kwa namna hiyo.

“Nipo nimejaa, sijui wewe mwanamama,”

“Nipo sawa, sasa kuna mtu namwitaji pale kituo kikuu cha polisi Arusha, aachiwe mara moja kama inawezekana, anaitwa Winfredi Kimario,” akamwambia.

“Unafikiri anafaa?” Simbeye akauliza.

“Anafaa sana tu, fanya hilo nasubiri,”

“Bila shaka!” akajibu na simu ikakatika. Baada ya simu hiyo akamgeukia Kamanda Amata “Enhe, mpango wako upo tayari?” akamuuliza.

“Yap, na nataka niuanze mara moja,” akajibu.

“Sawa sihitaji kujua, lakini kwa msaada zaidi wasiliana name kwa njia ileile,” Madam akamwambia.

“Yes Sir!” Amata akajibu na kumalizia kinywaji chake kisha akainuka na kuondoka katika mgahawa wa hoteli hiyo. Akiwa hatua kama tano hivi kutoka pale alipomuacha Madam S.

“Spark!” Madam akamwita, naye akasimama na kugeuka nyuma, wakatazamana kwa sekunde kadhaa, “Baki na roho yako, nakupenda sana,” akamwambia bila kutoa sauti ila kwa kutumia midomo yake tu, Amata akatabasamu na kuondoka eneo lile. Akainua funguo ya gari aliyopewa na Madam kwa siri na kuminya kitufe fulani, taa za Peugeot 405 vzikawaka mara mbili, akaiendea na kuingia ndani yake kisha akaondoka kwa kasi.


Winfred Kimario, mfanyakazi wa hoteli ya Mount Meru kitengo cha stoo na ufuaji (Laundry) aliachiwa huru mchana wa siku hiyo. Polisi walimwachia kijana huyo wakiwa bado wana hamu ya kumweka ndani ilhali hawapati ushahidi wowote kutoka kwake. Alikuwa hoi kwa kiminyo alichokipata ili kutoa siri yoyote kwa mauaji hayo, alitembea kwa tabu sana na mara nyingi alikuwa akiketi chini na kusikilizia maumivu. Alivuka barabara mbele ya kituo hicho na kukaa chini ng’ambo ya pili. Mara ghafla gari moja ikasimama mbele yake, ilikuwa Toyota Carina na mwanadada mrembo mrefu akashusha kioo cha kushoto.

“Winfred! Twende,” alimwita yule kijana. Win alimtazama huyo mwanamke kwa tabu kidogo, hakumjua ni nani lakini aliposisitizwa kuingia garini akafanya hivyo na ile gari ikaondoka eneo lile. Ndani ya gari kimya kilitawala hakuna aliyemwongelesha mwenzake isipokuwa sauti ya injini tu ilitawala, akaifuata barabara hiyo ya Makongoro mpaka round about akakunja kushoto na kuifuata barabara hiyo kubwa mpaka barabar ya Sanawari, akanyoosha mpaka Soko la Sanawari juu, akapita kama kilomita moja hivi na kukunja kushoto kwenye barabara mbovu yenye mashimo ya kutosha. Kwa jinsi gari ile ilivyokuwa ikrukaruka kwenye yale makorongo, Winfred alikuwa akihisi maumivu lakini hakuzungumza lolote.

Kati ya nyumba chache zilizojengwa kandokando ya njia hiyo kulikuwa na moja iliyokuwa na wigo wa michongoma mirefu kiasi kwamba ilifichwa kabisa, geti kubwa jesui likafunguliwa na ile gari ikpotelea ndani yake. Yule mwanadada akateremka na kumfungulia mlango Winfred.

“Karibu ndani, kasribu sana jisikie nyumbani,” akamwongoza mpaka kwenye sebule kubwa, pana iliyosheheni kila kitu cha thamani.

“Kwa nini umenileta huku, na we ni nani?” Winfred aliuliza kwa sauti iliyoonesha bado alikuwa na maumivu katika mwili wake.

“Usihofu, we tulia. Njoo upende huu,” yule mwanadada akamwongoza upande mwingine wa ile nyumba, akamwonesha chumba chenye kitanda cha wastani, bafu na choo ndani yake.

“Jihudumie, nitarudi baada ya muda,” akamuaga na kuurudisha mlango. Winfred alisikia gari ikiwashwa na kuondoka, akauendea mloango alipoufikia ndipo alipogundua kuwa ule mlango haukuwa na kitasa kwa ndani. Si kwamba kimeharibika bali hakikuwepo kabisa yaani hakikuwekwa na hilo lilimfanya mtu aliye ndani asiweze kutoka nje.

Ndani ya chumba kile kulikuwa na kila kitu, Winfred alikuta nguo za kubadilisha, chakula kikiwa katika meza ndogo na vinywaji kadhaa katika friji ndogo. Alipomaliza kuoga akabadilisha nguo kama alivyoelekezwa na kupata chakula hicho ambaco kilikuwa ni macaroni yaliyochanganywa na nyama ya kima, alipendelea soda badala ya pombe. Mwisho akaketi kitini akipitia magazeti haya na yale. Kilichomshangaza ni kuwa magazeti yale yalikuwa ni ya mwaka 1980 na siyo ya sasa lakini yalionekana bado mapya kabisa. Mwaka huu ndiyo mi nilizaliwa, aliwaza na mara akashtusha na mngurumo wa gari nje ya nyumba hiyo.

Mlango ulifunguliwa, hakusikia sauti ya mtu yeyote zaidi ya kishindo cha mlango huo kusikika ukifungwa kisha ukimya ukatawala. Dakika tano baadae akasikia mlango wa chumba chake na mtu mmoja akaingia na kuufunga ule mlango nyuma yake. Hakumjua ni nani kwani alikuwa ameuficha uso wake kwa sox nyeusi.

“Unaitwa nani?” yule mtu akamwuliza Win.

“Winfred Kimario,” akajibu huku akiwa amejawa na hofu kuu.

“Usiogope, hapa upo katika mikono salama, ninachotaka kujua tu ni juu ya uhusika wako wa mauaji ya kule hotelini,” yule mtu akasema.

“Mbona mi sihusiki?” akauliza huku akiwa kayatoa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango.

“Oh! Nimekosea, wewe unafanya kazi wapi?”

“Mount Meru Hotel, kitengo cha laundry” akajibu.

“Unaweza kunambia siku ya mauaji yale ulikuwa wapi?” yule mtu akauliza.

“Siku ile nilitoka kazini saa kumi za jioni kama kawaida yangu na kuelekea nyumbani,” akaeleza kwa kifupi.

“Ehne, baada ya kufika nyumbani nini kilitokea? Nieleze kila kitu ila kuficha hata kama ulifanya mapenzi na mtu, nieleze…” yule mtu aliomba zaidi, “Kuwa huru hii ni kwa usalama wako,” akamtoa hofu.

“Nilifika nyumbani saa nne usiku baada ya kupita kupata bia pale Masai bar. Kiukweli nilifika nyumbani na kulala usingizi mzito sana mpaka nilipoamshwa kwa mbisho wa hodi mlangoni kwangu, nilipotoka nilikutana na polisi, wakanifunga pingu na kuondoka nami mpaka kituoni,”

“Walikuhoji nini ukiwa kule?” akauliza huyo mtu.

“Walinihusisha na mauaji ya pale hotelini,”

“Kivipi?”

“Kwa sababu wanadai kuwa marehemu ameuawa kwa sumu ambayo ilikuwa kwenye shuka au folonya, na mimi ndiye mtunza stoo wa vitu hivyo na pia ndiye ninayefua mashuka yote ya hoteli hiyo,” akaeleza na kuinama chini.

“Je ulihusika au hukuhusika?”

“Sikuhusika kwani habari hiyo nimeisikia kulekule polisi,” Winfred akaeleza kinagaubaga.

“Hizo shuka au folonya ukiletewa unaweza kuzitambua kama ni za hapo hotelini au la?”

“Ndiyo! Kama ni za Mount Meru nitazijua na kama si za hapo nitazijua pia,” Win akaeleza.

“Ok, sasa utapumzika hapa hapa wakati uchunguzi unaendelea, na hizo shuka tutazileta uzitambue,” yule mtu akamwambia na kuinuka kisha akafunga mlango na kuondoka katika nyumba hiyo.


HOSPITALI YA MOUNT MERU

Kamanda Amata aliwasili katika hospitali hiyo na moja kwa moja akaomba kuonana na daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa Hamadou, haikumchukua miuda kumpata daktari huyo kijana. Wakaongozana mpaka ofisini, baada ya kujitambulisha kwake kama afisa wa polisi kutoka Makao Makuu Dar es salaam, mazungumzo yakaendelea.

“Unaweza kuniambia marehemu amekufaje?” Amata akauliza.

“Huyu bwana ameuawa kwa sumu ya Cyanide ambayo ilikuwa kwenye shuka na folonya la kitanda chake hivyo ameivuta kwa na sumu hiyo kuingia mwilini mwake…”

“Haiwezekani kuwa ameuawa kwa kitu kingine?” Kamanda Amata alimkatisha daktari huyo.

“Hapana, kwa sababu dalili au tafutishi zinazoonekana kwenye vipimo ni za sumu hiyo ninayokwambia. Niligundua kuwa seli zake zilishambuliwa sana kwa kukosa hewa safi na kumpelekea kufa, kifo cha cyanide ni kama kile cha mtu kubanwa pumzi, na hii sumu unapoivuta moja kwa moja inakuletea shida katika upumuaji na kukupelekea kifo haraka,” yule daktari akaeleza. Amata alibaki kinywa wazi akisikiliza maelezo ya daktari huyo kijana aliyependeza katika vazi lake la kidaktari.

“Ni sumu mbaya sana?” akauliza bila kutegemea.

“Ndiyo, ni mbaya sana; kijiko kimoja tu cha chai kinaua watu takribani thelethini na tisa kwa muda mfupi,” akaeleza.

“Ok, asante sana, labda swali la mwisho…”

“Ndiyo!”

“Unafikiri ni saa ngapi zilipita tangu afe mpaka ulipouchunguza mwili huo? Kama kuna kipimo cha kuionesha hilo,” Amata akarusha swali lililomfanya daktari huyo kuwa kimya kwa muda wa sekunde kama nne hivi.

“Mwili ulifika hapa saa tatu asubuhi jana, nilianza kazi hiyo saa nne na vipimo vyangu vilionesha kuwa marehemu alikutwa na mauti saa kumi na moja zilizopita…”

“Unamaanisha saa tano usiku?”

“Bila shaka,” akajibu daktari. Kamanda Amata akamshukuru kijana huyo na kuondoka katika jingo hilo la hospitali na kurudi katika ile gari alivyokuja nayo, Peugeot 405 aliyopewa na Madam S. Muda unakimbia kwelikweli, akawaza huku akiliacha lango la hospitali hiyo nakuelekea katikati ya jiji hilo.


Saa kumi na mbili jioni ya siku hiyo ilimkuta akiegesha gari katika megesho ya hoteli ya Mount Meru, akateremka na hatua kuziendea ngazi za hoteli hiyo, akazipanda na kuingia mapokezi, hakujali ofisi hiyo, alipitiliza na kuingia katika mlango mmoja uliofikisha kwenye korido ndogo ndefu. Mbele akakutana na mlango mwingine uliondikwa ‘No permission fo unauthorized person’ akautazama ulikuwa umefungwa kwa code maakum kutokana na aina ya kitasa hicho cha kielektroniki. Akachomoa kutoka mfukoni simu yake akabofya vitufe fulani na kioo chake akakielekeza kwenye kile kitasa kilichokuwa kikiwaka waka taa nyekundu, alipotazamisha tu akasikia sauti ya vitufe hivyo vya tarakimu fungushi, akabonya kwa kidole na ule mlango ukaachia na kufunguka, akaingia na kuufunga nyuma yake.

Ndani ya chumba hicho kulikuwa na runinga ndogondogo kama kumi hivi zikionesha picha mbalimbali za nje na ndani ya hoteli hiyo, akatazama na kuiona ile anayoitaka, inayopita picha mapokezi na mlango wa kuingilia. Akaiona ikifanya kazi sawasawa, akavuta droo lapembeni na kukuta cd nyingi zikiwa zimepangwa ndani yake, akapekua na kuipata ya tarehe ile aliyokuwa akiihitaji.

Akaichukua na kuitia katika kifaa maalum cha kusoma cd hiyo akawasha na kupeleka mbele mpaka saa ile, saa tano kamili na kuanza kuangalia mtu mmoja mmoja aliyeingia katika hoteli hiyo, hakuna aliyemtilia shaka isipokuwa kijana mmoja aliyeingia akiwa kava suti safi na briefcase ya rangi ya silva, akmwona akielekea kaunta na kuchukua kadi za kufungulia milango, akarudisha ile picha mara nne hivi, akaitazama kwa makini tena na tena. Alipomaliza kuitazama hiyo akahamia akasogeza mbele kidogo na kuangalia zile za koridoni, akamwona kijana yuleyule akifungua moja ya milango. Kilichomfanya amtilie shaka ni kuwa baada ya kutoka ndani ya chumba kile hakurudi kwenye lifti bali alitokea ngazi za nje, kwa nini? Alijiuliza. Kamera zote za nje hazikuonesha mtu huyo alipotelea wapi, Kamanda Amata hakulichukulia swala hilo kuwa ni la mzaa.

Alikuja na kuingialia mlango wa mbele kama kawaida lakini kutoka katokea mlango mlango wa dharula, kwa nini? Aliwaza huku akirudishia ile droo. Akatoka kwa tahadhari katika chumba hicho bila kuonekana na mtu, alipoufungua mlango akakutana na mhudumu wa usafi, yule mhudumu akamshangaa.

“Mkhh! Mkhh!” akajikooza kusuuza koo lake, “Samahani dada hivi choo ya jamii iko wapi?” akauliza. Kwa Kiswahili hicho yule mdhudumu alijua huyo ni Mkenya akamwelekeza na Amata akapotelea huko.


Meneja wa hoteli alikuwa ndani ya ofisi yake kimya akipitia kabrasha hili na lile, na kuangalia swala hili na lile, akagutushwa na hodi iliyofuatia mlango kufunguliwa. Kijana aliyeingia ndani ya ofisi yake na kujikaribisha hakumjua.

“Hauna haja ya kushtuka, kipindi hiki tegemea wageni wengi kukufikia, naitwa ACP Jafari,” Amata akajitambulisha kwa jina bandia na kumwonesha kitambulisho kilichomtambulisha vyema kwa jina na cheo hicho.

“Ndiyo afande!” yule meneja aliyeonekana wazi kuwa ni Mchaga bila kificho kutokana na lafudhi yake alijiweka sawa kitini.

“Nomba kumweka chini ya Ulinzi mtumishi wako wa mapokezi aliyekuwa kazini saa nne na dalika arobaini na tano usiku…”

“Kwa nini? Mbona swala hili limekwisha na polisi washamalizana na sisi kwa kuwa wamemchukua Winfred,” yule meneja akaeleza.

“Hao ni wao, mimi nimetoka Makao Makuu ya polisi Dar es salaam, yaani kesi inaanza upya kabisa,” Amata akaeleza.

“Sawa afande, fanya utakalo, nyie ndiyo dola bwana!” akamjibu huku akiinua simu kutaka kupiga mahali, Amata akamtoa mkono na kumrudisha pembeni.

“Huwa hatufanyi hivyo…” akamwambia huku akiinua simu yake na kupiga, kisha akaongeza machache na kuikata simu hiyo.

“Asante kwa ukarimu nitakuja tena kama utanikaribisha,” akanyanyuka kitini, “Aaaah samahani, naweza kuingia chumba alichofia marehemu?” akaongeza swali.

“Hapana, kwa kuwa hata kadi zake zipo kwa RPC wa mkoa mpaka uchunguzi ukikamilika,” akajibu yule meneja na wakati huo Amata ndipo akajua kuwa kuwa huyo bwana anaitwa Benson Moshi. Alipokuwa akitoka, kabla hjafungua mlango aliuona ukifunguka wenyewe, akatupa jicho huku na ukule kujua inakuwaje mlango huo kujifungia wenyewe; ndipo akatanabahi kuwa kuna mtu alikuwa akiingia, mwanadada aliyebana nywele zake nyuma, mfupi maji ya kunde aliyejazia vyema kifuani na sehemu za chini ya kiuno. Jinzi aliyovaa, mashaaalah ilimjenga vyema, macho yake yaliyokaa kama taa za mbele za Hyundai yalimfanya aonekane mrembo haswa. Hakuwa na mkoba isipokuwa alivalia kijikoti kidogo na ndani fulani ya kijana.

Aliivua miwani yake akaipachika katika V ya shingo ya fulani yake. Amata akatoka, na yule dada akaingia lakini kila mmoja akageuka kumtazama mwenzie, lakini ule mlango ukajifunga na kuwatenganisha. Lazima nimsubiri, akawaza huku akitoka nje ya hoteli ile. Alipofika mapokezi hakuongea na mtu, alimwona askari yule wa kike aliyemkata usiku uliopita akiwa na mwenzake mmoja pale kaunta, akajua ombi lake limefika mahali muafaka, naye asimtazame akapita kama hajamwona na kuelekea maegeshoni. Alitupa macho huku na kule, akabofya saa yake na kuizungusha ringi ya juu, hakuna chochote, akaingia na kuketi akitazama kinachoendelea…

Dakika ishirini baadae, alimuona yule mwanadada akitoka ndani ya hoteli ile, akamkodolea macho kumuona anapoelekea. Yule mwanadada akaingia ndani ya Vogue ya gharama sana na kuiondosha eneo lile. Kamanda Amata akawasha gari yake naye taratibu akaiondoa na kumfuata mwanadada huyo huku kati yake akiwa kaacha gari kama tatu hivi. Ile gari haikwenda mbali, ilipita mbele ya baa kubwa na kuegeshwa kati ya gari nyingi zilizokuwamo hapo, gari za gharama, nalo lilifanana kabisa na hayo. Ama akapita taratibu na kuegesha gari upande wa pili, akateremka na kufunga mlango huku jicho lake likiwa upande ule wa ile klabu. Baada ya kusubiri kwa muda mrefu simu yake ikamfinya kuashiria ujumbe uliokuwa ukiingia muda huo, akainua mkono na kuiruhusu kisha utepe wa plastiki ukajitokeza na yeye akuvuta taratibu akiusoma.

Moshono magari mabovu, ulisomeka. Akili ikamzunguka kijana huyo, akapata wakati mgumu kuamua asubiri kimwana au aende huko alikoambiwa? Ikawa ngumu kuamua akaamua kutuliza akili, akajumlisha moja na mbili na kupata tatu, akawasha gari na kuiondoa kwa kasi kuelekea eneo alilotajiwa.

Labda lina tija kwa kazi yangu, usiku huu usiishe mpaka nipate majibu, akawaza huku akiendesha gari ile kwa kasi ukizingatia usiku huo tayari gari nyingi hazikuwa barabarani hivyo alitamba atakavyo na gari hiyo ya Mfaransa. Alipoingia eneo hilo aliloambiwa, Moshono, alipunguza mwendo na kuendesha gari yake taratibu mpaka eneo lililokuwa likitumiwa kama dampo la magari mabovu kutokana na kujazana kwa screpa hizo. Akaegesha mahali fulani katikati ya yale magari mabovu na kuteremka bastola mkononi. Akavuta hatua fupi fupi huku akigeuka nyuma na mbele, kushoto na kulia akitazama kama kuna lolote la kutokea basi akabiliane nalo.

“Yes! Kamanda Amata,” Sauti kavu ikatokea nyuma yake, akageuka na bastola ikiwa tayari kufanya kazi yake, “No! No! No! kuwa mtulivu, rudisha bastola yako mkobani,” ile sauti ikaendelea na Amata akafanya hivyo kisha akasimama vyema kwa lolote. Kutoka ndani ya gari bovu moja wapo, mtu aliyevaa koti refu jeusi lililoanzia kichwani mpaka nyayoni aliibuka na kusimama kando tu. Amata akageuka na kukutana naye uso kwa uso lakini hakumtambua kutokana na giza na isitoshe mtu huyo alikuwa kavalia sox jeusi kichwani na kujifunika kwa kofia la koti hilo.

“Wewe ni nani?” akamuuliza.

“Amata Ric, TSA 01. Usihofu kuhusu mimi kwani mimi ni mfu hai. Najua ulilolifuata Arusha lakini una kazi ngumu kupambana na huu mtandao kwani hii si mara ya kwanza wewe kwa mkono wako kupambana nao,” yule mtu akaeleza.

“Ni mtandao gani huu?”akauliza.

“Hata mimi sijaujua, na hii ni kutokana na maisha yangu kwa miaka hii tangu nilipouawa,” yule mtu akazidi kueleza.

“Kwa hiyo…!”

“Nikupe mbinu ya kuushinda mtandao huu?”

“Ndiyo, kwani unasumbua akili sana…”

“Siyo akili yako tu, akili za wengi, wengi sana. Selina ni mwanamke shupavu na usiku wa jana ametoka kwenye makucha ya mtu mbaya kabisa,” yule mtu akamweleza jambo jipya Amata.

“Unasemaje hapo? Nahisi kama sijaelewa,” Amata akaonesha shaka.

“Nenda kwa Selina kamwulize usiku wa jana alikuwa wapi, atakueleza,” yule mtu akatembea kama hatua tano hivi na kusimama sehemu nyingine.

“Ina maana unaujua vyema mtandao huu?” Amata akauliza huku anye akibadilisha eneo la kusimama.

“Siujui lakini nataka kukupa mbinu ya kutumaliza…”

“Mbinu ya kutumaliza?”

“Ndiyo, mbinu ya kutumaliza,”

“Unapambana na watu unaowajua au uliowahi kufanya nao kazi ukitaka kutumaliza mtandao huu lazima uwe mmoja wao, nafikiri unaielewa vyema mbinu hiyo. Sasa hkikisha unapata kujua chanzo cha mauaji ya Hamadou kisha fanya uwezalo uingie ndani ya mtandao huo na kutoka hapo utaweza kutumaliza, ni wewe tu unayeweza hilo hakuna mwingine,” yule mtu akamweleza Amata mambo na kisha akarudi katika ile gari na kuingia ndani yake, akajifungia mlango. Amata akageuka na kuondoka eneo lile, akaingia kwenye gari yake na kuwasha, akatulia kama sekunde thelathini hivi na kuondoka.


Nusu saa baadae, kamanda Amata alikuwa amesimama mbele ya kioo kikubwa katika chumba kile alichopanga, akifunga vifungo vya shati lake jeusi la mikono mirefu. Akatulia na kujitazama. Kisha akageukia kitandani na kuchukua kijikoti chake kidogo amacho ndani yake kuna kila dhana anayoihitaji, akakivaa na kukifunga vyema. Bastola mbili na magazine za akiba akazipachika mahali pake, saa yake akaivaa sawia, simu yake akaifunga mlio na kuiweka mahali panapostahili, kisu kimoja chenye sindano, opener uzi na vitu vidogo vidogo akakipachika mahali pake. Kofia yake aina ya mzula akaitupia kichwani na kuchukua miwani yake inayomfaa gizani kisha akatoka kwa mlango wa nyuma wa lodge hiyo, akakwea ukuta kwa ustadi na kutua nje.

Akaitazama saa yake, ilikuwa ikikimbilia saa tisa za usiku. Akaondoka zake, uchochoro wa kwanza, wa pili akatokea barabarani na hapo akasikia kelele za ubishanaji kati ya mtu aliyeonekana kama mhalifu na polisi. Sauti ya kike aliyoisikia ikipayuka aliitambua kuwa ni yule mwanamke polisi aliyemkata jana yake. Hakujali, akajitokeza kuvuka ile barabara.

“Wewe! Simama!” akaamriwa naye akasimama hapohapo alipoambiwa, hakugeuka kumtazama mwanamke huyo, akatulia tuli huku miwani yake ikiwa usoni imemficha sura.

“Tena hili ndiyo jambazi kuu kabisa ona lilivovaa,” yule mwanamke akasema hayo huku akimwendea Amata. Leo nitakuonesha hiyo jeuri yako, akasema moyoni. Yule WP akamkaribia Amata, lakini kabla hajasema au kufanya lolote alijikuta akipigwa mtama mmoja maridadi, akarushwa hewani na kutua chini kama kifurushi. Wenzake walipozinduka kumsaidia mwenzao tayari Amata alishatoweka eneo lile.

HOTELI YA MOUNT MERU – Usiku huohuo

KUTOKA UPANDE WA PILI wa barabara Kamanda Amata alitulia kimywa chini ya mti wa Jacaranda akisoma mazingira na miendo ya watembea usiku. Hapo aliposimama hakuonekana na mtu yeyote isipokuwa yeye mwenyewe tu. Usiku kuna mambo, aliwaza baada ya kuona mwanadada mmoja kahaba akiwa nyuma ya gari na dume lililokuwa likigugumia kwa shughuli nzito. Kandokando tu ya hapo walikuwapo wadada wengine wakisubiri wateja, si kwamba hawakujua nini kinaendelea nyuma ya hiyo gari bali ilikuwa kazi yao, wenyewe huita vodafasta.

Kutoka baa ya jirani watu walimiminika nje, baa ile aliyoingia yule mrembo jioni ya siku hiyo. Kutokana na hilo wale wadada wakahama pale na kuhamia kule kwenye watu wengi kwa minajili ya kukamata mawindo zaidi.

Bingo! Akapiga kite na kuchomoka pale alipo, akavuka barabara kwa kasi na kuruka sarakasi moja matata sana akatua ndani ya wigo wa hoteli hiyo, na viatu vyake vilivyobeba uzito wake havikufanya kelele wala kishindo. Akatazama huku na kule, hakuona hata mlinzi lakini alijua kuwa kuna kamera nyingi zinazofanya kazi hiyo.

Akapita kando kando ya gari za wageni na kutokezea jirani kabisa na ukuta wa hoteli hiyo, akaizunguka mpaka kwenye ngazi za dharula, akazikamata kuzikwea, lakini kengele zake za hatari kichwani mwake zikalia, mlango wa sita wa fahamu ukafanya kazi na hii ndiyo sifa kubwa ya mwanausalama yeyote hasa wale wanaintelijensia kama Kamanda Amata. Alisimama kama sekunde mbili akiusikiliza moyo wake, akaiacha ngazi hiyo na kuambaaambaa mpaka usawa wa kile chumba anachokitaka. Kilikuwa juu kama mita tisa hivi. Akasimama na kuingia mkono ndani ya kikoti chake, akachomoa kitu mfano wa bastola lakini haikuwa bastola, akaikamata kwa mikono yake yenye gloves. Juu kabisa ya ghorofa hiyo kulikuwa na bomba za kumwaga maji endapo mvua inanyesha, akafyatua ile bastola yake na waya mrefu ukachomoka kwa kasi na kulinasa lile bomba, ukajiviriga sawia. Amata akatumia waya huo kwa kupanda huku akitembea ukutani kama atembeavyo barabarani.

Chumba namba 307, Amata alitua sakafuni kutokea dirisha kubwa la kioo, akatulia tuli.jicho lake likatua kitandani, shuka zilizojikusanya zikayalaki macho yake, bila kuchelewa na kwa hadhari kubwa akijua wazi kuwa shuka hizo ndizo zilimuua Hamadou, akazikusanya na kuzikunja taratibu kisha akazitia kwenye mfuko na kuubana vyema kwa mkanda wake wa suruali. Hili tu, akawaza. Alipotaka kufanya harakati za kutoka kwa njia ileile aliyoingilia alihisi kitasa cha mlango kikifyatuka, akatulia, akarudi karibu na dirisha na kujificha nyuma yake ili ashuhudie nini au nani anaingia. Giza lilijaa ndani ya chumba hicho, na kufanya mwanga wa nje kuwa hafifu sana na kutotosheleza mtu kuona vyema. Mlango ukafunguliwa na mkono wa mtu aliyevaa nguo nyeusi na gloves nyeusi mkononi mwake ukaoneka ukitangulia taratibu, kisha kiwiliwili chote kikaingia. Alikuwa mtu mfupi wa wastani aliyejaa nyama za mwili, alivaa nguo nyeusi chini mpaka juu.

Kamanda Amata alimtazama kwa makini, aligundua kuwa ni mwanamke kutokana na hips zake zilizojaa vyema. Yule mtu akasimama katikati ya chumba, akatupa jicho kitandani na mahali pengine asione akitakacho. Taratibu, alianza kukagua chumba kile kwa macho na mikono, akifungua hapa na pale, akakariia kabisa kwenye dirisha, akasita na kusimama. Akauzungusha mkono wake nyuma ya kiuno chake.

Bastola au kisu, Amata akawaza na kujichomoa kutoka pale alipo kwa kasi na guu moja la uzito ulioshiba likatua kifuani mwa yule mtu, akayumba na kujibamiza ukutani. Kabla hajakaa sawa, akapokea makonde mawili mazito, akaangukia kitandani. Amata akamwendea, lakini, la haula! Kabla hajafika yule mtu akajinyanyua kutoka kitandani na miguu yake mifupi ikiamtandika Amata shavuni, akashinda kustahimili, akayuma na kujigonga kabatini. Alipotazama vyema akamwona yule asiyemjua akichomoa kisu na kukirusha kwa ufundi, akaepa, kikachoma kwenye kabati na kubaki hapo, kisu kingine kikaja kasi akakidaka. Wakati huohuo, akajiondoa na kupeleka mapigo ya karate, yaliyomwishia huyo mtu sawasawa kwani hakuweza kupangua hata pigo moja.

Umekamatika! Akawaza Kamanda, lakini ghafla yule mtu akaja kama mbogo, ngumi ya kwanza Amata akaidaka na yapili vivyo hivyo, akamzungusha na kumbana kifuni kwake wote wakitazama mbele. Yule jamaa akamng’ata meno Amata mkononi na kutoboa shati mpaka ngozi.

“Aaaaaaigh!” Amata akapiga kelele na kumsukuma kwa nguvu, kisha akampa pigo moja la maana lililompeleka mbele, akajigonga kitandani na kuanguka huku akipigiza uso wake a sakafuni.

Dakika hiyohiyo, akasikia vishindo vya watu kuja upande ule, “Ni chumba hicho 307,” sauti ya mtu mmoja ikasikika. Amata akaona mambo yashaharibika, akamnyanyua yule mtu pale chini na kumbeba sawasawa, akalifungua dirisha na kuukamata ule waya ulikuwa umefungwa vyema kwenye lile bomba na muisho wake ambao ulikuwa na kitukama bastola ukiwa umebanwa na dirisha, akaukamata na kujitosa nje. Taratibu akatua kwenye bustani ya maua, akavuta hatua mpaka kwenye moja ya vibanda vilivyotumika kama stoo, akajificha nyuma yake na kumtua chini yule mtu, akavua kwa nguvu ile kofia iliyomficha uso wake.

“Stupid!” yule mtu akatukana, sauti ya kike ikapenya masikioni mwa Amata, “You are the killer!” akang’aka akimaanisha kuwa Amata ndiyo muuaji.

“Do you know the killer how he look like?” Amata akamuuliza kama anajua muuaji anafananaje, “Who are you?” wewe ni nani? Akamwuliza. Yule mwanamke akamsukuma Amata kwa nguvu.

“Get out from me!” nitokee hapa, akammwambia huku akiinuka. Amata akataka kumkamata lakini lo, yule mwanamke akatoa kitu kama pafyumu na kumpulizia Amata usoni.

“Shiiit!” macho yakaanza kumwasha na yule mwanamke akapotea. Akawahi kutoa kitambaa chake, na kibweta kidogo kilichokuwa na maji fulani ndani yake, akamwagia kwenye kile kitambaa na kujipangusa vyema. Mlio wa gari ukasikika kutoka nje ikiondoka.

“Vogue!” akajisemea kwa sauti ya chini kisha akavuta hatua na kutoka nje ya wigo ule kwa mtindo wa sarakasi. Akawahi upande wa pili wa barabara na kupotea vichochoronI.


Ndani ya nyumba ile aliyomwacha Winifred, mara hii kulikuwa na yule mwanamke wa Kimburu aliyempokea kutoka Uwanja wa Ndege, akisubiri kama alivyoamriwa kufanya hivyo. Pamoja naye alimleta mwanadada mfanyakazi wa kaunta katika hoteli ile na kumhifadhi ndani ya chumba tofauti na yule kijana.

Mara mlango ukafunguka na Amata akaingia ndani ya sebule ile ambayo hakukuta mtu yeyote.

“Simama ulipo!” sauti ya kike ikasikika kutoka asikokujua. Akatulia palepale lakini akajaribu kufikiri ni wapi amewahi kuisikia ile sauti. Mlango wa kushoto kwake ukafunguka, na yule mwanadada akajitokeza.

“We ni nani?” yule mwanamke akauliza. Amata akvua miwani, akatoa ile kofi na kubaki sura wazi.

“Mr. Spark!” akajitambulisha.

“Nimeshakutambua, naitwa Rose Kakai, ndiyo House Keeper wa hapa,” naye akajitambulisha na kumpa Amata kitambulisho chake.

“Yule mtumishi amefikishwa hapa?” akauliza Amata.

“Ndiyo, yuko huku,” Rose akamwelekeza Amata mahali alipo yule mhudumu wa hoteli.

“Ok, ngoja nimalize na Winifred kwanza,” akamwambia na kuvuta hatua pamoja naye mpaka katika kile chumba wakaingia wote huku Rose. Amata akaufungua ule mfuko kiunoni mwake na kutos zile shuka akazibwaga kochini. Rose akaliendea kabati na kuvuta droo akatoa gloves na barakoa za kuficha pua zao, wote watatu wakavaa.

“Winifred, hizi shuka nimezitoa kule hotelini, ndizo zilikuwa kitandani mwa marehemu mpaka anafariki. Bila kunificha nataka uniambie ni shuka zenu au siyo zenu kwa maana inawezekana kuwa huyu mtu aliziiba pale au ni kweli ulikula njama; kwa maelezo yako tu nitajua ukweli na uaongo,” Amata akamwambia Win. Yule kijana akaenda pale kochini na kuzichambua zile shuka, kwa kushika tu akatulia kwanza kama anayesikiliza kitu.

“Hapana Mkuu, hizi shuka si za hotelini kwetu, za kwetu hazitelezi, lakini hizi zinateleza, pia pindo zetu ni ndogo lakini hizi ni kubwa. Kama walijaribu kuiga basi wamefeli,” akaeleza.

“Ok,” Amata akazikusanya zile shuka na kutoka ndani ya kile chumba akaenda kule alikohifadhiwa yule mwanadada. Akamkuta amejikunyata kochini.

“Hujambo mrembo?” akamsabahi na kuziweka zile shuka mezani. Yule mwanadada akajiweka sawa akionekana ni mwenye woga.

“Stella Wanjala, unaweza kuniambia ni nani aliyefanya mauaji ya Hamadou pale hotelini?” Amata akaanza kwa swali.

“Ha-ha-pa-na!” akajibu huku chozi likiwa limeyameretesha mashavu yake mapana yaliyojaa kama mimba ya panya.

“Wewe umekula njama za mauaji yale kwa pesa ndefu na mimi najua,” Amata akazungumza kwa ukali kidogo.

“No, ha-ta si-ju-i…”

“Hujui! Wakati muuaji ulimkabidhi kadi ya mlango wewe mwenyewe! Utasemaje hujui, ina maana wewe huwajui wateja wako, hukumjua Hamadou?” Amata akawa mkali sasa.

“Mnanionea tu, mi hata sikumjua huyo muuaji,” akajibu.

“Siku ile, ulikuwa zamu ya usiku, na mida ya saa nne za usiku alikuja mtu huyo, ukampa kadi ile na hiyo ndiyo iliyotumika kuufungua ule mlango. Hebu nambie alipokuja Hamadou ulimpam kadi gani?” swali hilo likamgonga kichwa yule binti, akajaribu kuvuta hisia…

SIKU YA TUKIO…

STELLA WANJALA akiwa ametingwa na kazi katika ofisi ya mapokezi, aligutuliwa na sauti ya mtu akihitaji kadi ya kufungulia mlango. Mtu yule hakumtazama Stella usoni isipokuwa alikuwa akiangalia upande mwingine na mkono wake akiwa ameukinga juu ya kaunta ya mapokezi hiyo.

“307 please!” akamwambia Stella, mara moja mwanadada huyo aliacha kazi anayoifanya na kuivuta hiyo kadi kutoka mahali inapohifadhiwa na kumpatia, akijua ni moja ya wapambe wa Mwenyekiti huyo wa Baraza la Usalama. Yule kijana akaichukua na haraka akaondoka na kuiacha ile kaunta pasi na kurudi.

Nusu saa baadae, ulifika msafara wa Dr. Hamadou, moja kwa moja alifika kaunta na kijana wake mmoja. Suti walizovaa zilishahabiana kabisa na yule kijana wa kwanza. Bila kuuliza, Stella alivuta droo na kutoiona ile kadi, alipiga akili huku na kule lakini hakukumbuka sawasawa kadi ile iko wapi na hili lilitokana na mambo mengi aliyokuwa akiyafanya kwa wakati mmoja.

“Si uwape ile ya akiba!” ilisikika sauti ya msichana mwingine ikimwambia, naye bila kufikiri mara mbili, akabifya tarakimu fungushi za droo moja wapo kati ya nyingi na kuchomoa kadi akawapatia nao wakaondoka.

“Sir, the flight will be at 12 pm, and we shall start from here at 8 am,” kijana mmoja alimwambia hamadou walipokuwa wakiagana usiku huo baada ya kuhakikisha amefika salama hotelini. Alimwambia kuwa Ndege itaondoka saa sita kamili mchana na wao watatakiwa kuondoka hapo hotelini saa mbili asubuhi.

“Ok, see you tomorrow and sleep tight!” akamuaga huku wakipeana mikono na kukubaliana kuhusu safari ya asubuhi. Kijana yule anapoondoka, Dr. Hamadou akaingia chumbani mwake na kuufunga mlango, akalegeza na kuiondoa tai shingoni, akatoa kotinlake na kuliweka kwenye mkoba maalumu wa kubeba nguo za aina hiyo. Alipomaliza kuweka vitu vyake katika mabrgi, na kutoa suti ya kuvaa siku ya safari; aliingia maliwato na kuoga maji baridi yaliyomwondolea uchovu kisha akarudi kitandani kujipumzisha. Haimkumchukua hata dakika tatu alipoanza kusikia kifua kizito, pumzi inabana yaani anashindwa kupumua sawasawa, alijitahidi japo kujitoa kitandani lakini ilikuwa ngumu. Hamadou alijikuta ana-surfocate, akajibwaga chini kuiendea simu ya mezani ili kupata msaada lakini kila alipokuwa akiikaribia ile meza ndogo alijikuta anashindwa kabisa japo kuishika, akanyoosha mkono na kuukamata waya hata hivyo hakufanikiwa kutimiza lengo lake pale alipojikuta giza likimzidi na nguvu ikipotea, akajaribu tena tena kupigania roho yake lakini haikuwezekana, akabaki hivyo mpaka alipokutwa asubuhi iliyofuata.


Rejea KAMANDA na STELLA…

“Na hizi shuka je?” Amata akamwekea mezani, Stella akaziangalia kwa makini, “unaweza kuzitambua?” akaongeza swali.

“Bila shaka, zina nembo ya hoteli yetu lakini sisi hatutumii ghafi ya namna hii,” akajibu.

“Kwa hiyo unataka kuniambiaje?”

“Siyo zetu!” akajibu kwa mkato.

“Sasa msichana nisikilize kwa makini, kifo cha Hamadou kimesababishwa na shuka hizi unazoziona, zina sumu mbaya sana. Kwa hiyo kama hukufanya njama wewe wala Winfred basi ni yule ni mfanyakazi wenu anayeshughulika na vyumba, unakubaliana na mimi?” Amata akauliza.

“Hapana, kwa sababu, yule mhudumu alifanya kazi yake saa nne asubuhi, na mchana huo Hamadou airudi kupumzika kisha akatoka tena kwenda kwenye sherehe. Sasa kama angekuwa ni huyu mhudumu basi Hamadou angekufa mchana huo,” maneno hayo yakamwingia vyema Amata. Sasa akarudisha mawazo kwa yule mtu aliyekuwa kamhisi, ambaye aliingia usiku ule na briefcase ya rangi ya fedha. Atakuwa ni yeye! Akawaza, kwenye briefcase aliweka shuka hizi, akaendelea kuwaza huku kaduwaa kimya.

Taa nyekundu kwenye kichwa cha Amata iakawaka kuionesha kuwa kuna jambo kubwa na zito mbele yake. Mwanaume mwenye briefcase ya silver, akampa jina hilo kijana yule, kwa maana hata sura yake hakuiona sawasawa na hata Stella hakumkumbuka jinsi alivyo.

“Ok, asante!” akamgeukia Rose, “binti kama kawaida, nitarudi wakati mwingine,” akamwambia na kutoka katika nyumba ile, akiwa sebuleni kuelekea mlangoni.

“Spark!” Amata akageuka baada ya kuitwa na sauti hiyo aliitambua kuwa ni ya yule binti mtunza nyumba, Stella.

“Yes!” akaitika na kugeuka.

“Unahitaji msaada?” akauliza, swali hilo lilimvutia sana Amata.

“Aaanh msaada gani labda?”

“Wa kukufikisha kwako hivi,” akamweleza.

“Usijali, kwangu nitafika, labda kama kuna msaada mwingine,” Amata akaeleza na wakati huo tayari Rose alikuwa ameshafika pale alipo, wakatazamana usoni kwa nukta za kutosha. Macho ya binti huyo wa Kimburu yalitonwa na chozi la ndani, chozi la hamu ya kitu alichokosa muda mrefu. Lugha hiyo Kamanda Amata anaielewa vyema sana, akamkamata kwa mikono yake mabegani. Nyuso zao zikakaribiana taratibu, na mara ndimi zao zikabadilishana mawazo, wakakumbatiana kwa kubanana na hatimaye wakaangukia juu ya kochi. Wakasahau kabisa kama kuna watu wamewafungia kwenye vyumba vya siri ndani ya nyumba hiyo.


Ndani ya ofisi ndogo katika jingo la Ikulu ndani ya Jiji la Arusha kulikuwamo watu wawili tu, Madam S na Kamanda Amata. Baada ya kupata kikombe cha kahawa kila mmoja sasa ilikuwa ni uwasilishaji wa taarifa.

“Bado adui yetu yupo!” Amata akamwambia Madam S.

“Kivipi?” Mama huyo akauliza huku akiegemea vyema kiti chake.

“Muuaji wa Hamado mpaka sasa nimempa jina ‘mwanaume mwenyue briefcase ya Silver’ kwa kuwa bado sijapata jina kamilia la mtu huyo,” akaeleza. Wakati anataka kuendelea kuongea Madam S akamzuia kwa mkono wake na wote wawili wakabaki kimya kabisa. Sixth sense ikafanya kazi haraka na hii ndiyo ilikuwa sifa kubwa ya mtu anayefanya kazi ya usalama ndiyo maana akaitwa mwana – intelijensia kwa kuwa hutumia akili ya haraka, kuchanganua jambo, kulitazama na kujenga maana. Amata akatulia na kujua kuwa Madam ana jambo aliloliunganisha kwa nukta hiyo, naye akaona inabidi asubiri.

“Amata, kuna jambo sasa ndiyo limeleta maana kwangu,” akasema.

“Kitu gani?” akauliza.

“Siku nilipofika pale uwanja wa Ndege Arusha, kwenye tax moja aliteremka mwanaume aliyebeba briefcase ya silva, alikuwa na haraka sana ya kuwahi ndege, nilimtazama na akili yangu ilifanya yake, lakini sikuwa na haja kumfuatilia msafiri aliyechelewa ndege. Kwa habari hiyo Amata naye masikio yakanyanyuka kama mbwa aliyeona hatari.

“Anaweza kuwa yeye?” akauliza.

“Usijali, tax aliyoshuka ndiyo niliyopanda na namba yule dreva ninayo,” akajibu na kumwandikia Amata katika kijikaratasi kilichokuwa hapo mezani.

“Hiyo ndiyo namba yake huyo dereva,” Madam S akamwambia Amata hukuakimkabidhi kikaratasi chenye hiyo namba.

“Bingo!” akatamka kwa shauku na kusimama tayari kwa kuondoka.

“Hawa jamaa wamejiingiza kwenye mambo mengi sana! Hivyo kuwamaliza itakuwa tabu kidogo,” madam akaendelea na kauli hiyo ikamfanya Amata kugeuka na kurudi kwenye kiti.

“Tunafeli sana katika serikali yetu hasahasa juu ya hawa wahamiaji haramu, wanafanikiwa kuzaa na mabinti zetu kisha tunapata watu kama hawa. Kiukweli ishu ya Counterintelligency, naweza kusema ndiyo iliyotufikisha hapa leo,” Amata akaeleza.

“Sure…!”

“Inabidi kujiongeza katika hilo,” akaongezea Amata huku akiikata kauli ya Madam S.

“Sawa, fanya kuzi-tracy hizo nyayo za mbwa mwitu, ukizipata nipe habari,” akamaliza Madam na kufunga laptop yake iliyokuwa juu ya meza. Amata akapotelea njea ya ofisi hiyo na kuchukua ‘pijo’ yake kisha akapotelea katika viunga vya jiji hilo.


Kamanda Amata alirudi katika hoteli aliyofikia, Kundayo, maana tangu alipotoka hakurudi tena. Akaingia chumbani mwake na kujiweka sawa kwa mtoko mwingine. Alipohakikisha yuko tayari kwa kila kitu, akatoka zake na kuchukua pijo lake. Mwanamke yule wa jana ni nani? Akajiuliza swali ambalo lilikosa jibu kwa wakati huo.

Breki ya kwanza ilikuwa mbele ya mgahawa wa City Link ambapo ni jana yake tu aliketio hapo na Madam S. Akaegesha gari mahala pake na kuingia ndani. Alipoketi akaagiza kinywaji baridi huku akiibofya namba ile aliyopewa na Madam S.

“Hello!”

“Unaweza kunifuata hapa City Link? Nataka kwenda Mbauda.” Akamwambia dereva huyo ambye aliipokea simu hiyo upande wa pili.

“Ok, nipe dakika tano,” akajibiwa.

Kama alivyoahidi, dakika tano ile tax iliwasili katika mgahawa huo, Amata akatoka baada ya kuwasiliana kwa simu na mtu huyo.

“Mbauda, sehemu gani?” yule dereva aliuliza wakati akichukua barabara ya kuelekea pande hizo.

“We twende tu!” akamwambia. Yule dereva akaongeza mwendo na kuzidi kulikariia eneo hilo huku akikatiza kichochoro hiki na kile.

“Hivi, kutoka hapa mpaka Uwanja wa Ndege wa Arusha ni dakika ngapi?” Amata akauliza.

“Inategemea, lakini ni dakika kama ishirini hivi, una safari ya huko?” akauliza yule dereva.

“Hapana, kwani mara ya mwisho ulienda lini?”

“Juzi tu hapa,” akajieleza.

“Nikwambie kitu…”

“Enhe…”

“Unakumbuka nanai ulimbeba kwenye gari siku ile?” Amata akauliza.

“Wakati gani sasa? wa kwenda au wa kurudi?”

“Nyakati zote hizo,” akamwambia.

“Nilipokwenda nilimpeleka mteja mmoja tajiri sana, aaah yule jamaa alinipa dola tu, mi nilimwambia elfu kumi ya akanipa dola kumi,” akaeleza, “Na mi sikumwambia maana alikuwa na haraka kama anaenda chooni,” yule dereva aliongea huku akicheka.

“Ulimtoa wapi?” Amata akauliza.

“Yule bwege…”

“Mteja wako usimwite bwege wewe!” Amata akamkaripia.

“Yule nilimtoa pale Mererani Junction, yaania kuna baa nje haina jina halafu kwa ndani kuna kiwanja moja matata sana, humo wanaingia matajri bwana,” akaeleza.

“Panamilikiwa na nani?” akauliza.

“Hata simjui kwa kuwa hili jiji kuna watu wa kila aina, wezi, majangiri, Malaya, vicheche, wauza unga, wauza madini na wachimba jumlisha makahaba; wote wapo…”

“Wakristo na Waislam je?” Amata akadakia.

“Wote wapo.”

“Nipeleke,” Amata akamwambia huyo dereva.

“Enh?”

“Nipeleke?”

“Wapi?”

“Mererani Junction,” akamwambia.

ITAENDELEA

Pasipoti Ya Gaidi Double Agent Sehemu ya Tatu

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment