Najisikia Kuua Tena Sehemu ya Tano
NEW AUDIO

Ep 05: Najisikia Kuua Tena

Najisikia Kuua Tena Sehemu ya Tano

IMEANDIKWA NA : BEN R. MTOBWA


Simulizi : Najisikia Kuua Tena

Sehemu ya Tano (5)

“Fungua,” Kombora alifoka tena. “Polisi hapa,” aliongeza akiitazama saa yake. Dakika tatu zilikuwa zimepita tangu alipowasili hapo na kuwakuta askari wa doria wakiendelea kuugonga mlango wa ofisi ya Kwame
“Mnadhani kuna nini kinachofanyika humo ndani?” aliwahijo.
“Hatujui mzee. Hatusikii chochote.”
“Msichana anayekaa hapa mmemkuta?”
“Hatukumkuta.”
“Okay, tutavunja mlango. Nitaita kwa mara ya mwisho… FUNGUA!” akafoka.
“Mara mlango ukafunguka polepole. Kwame alitokeza akitetemeka mwili mzima isipokuwa macho yake tu. Kombora hakuyaona kuwa na dalili yoyote ya hofu. Aliwatazama kwa mshangao na shukrani.
“Karibu,” aliwaambia akiwapisha mlangoni.
Walipoingia macho yao yalidakwa na mizoga ya binadamu wawili waliolala juu ya sakafu. Mmoja akiwa kalala chali bastola mkononi. Wa pili ambaye ilikuwa dhahiri alikuwa marehemu alikuwa chali, sura yake ikitazama angani. Kombora na wasaidizi wake sita walimtazama marehemu huyo mara moja na kisha kutazamana.

“Bazile Ramadhani!” mmoja wao akajaliwa kutamka.
“Ni Bazile siyo? Ule muuaji anayeua ovyo? Basi Mola asifiwe kwa kufa kwake. Angeweza kuniua au kumuua huyo kijana hapo,” alitamka Kwame kwa namna ya furaha.
“Kombora alimtazama kijana huyo na kumwona akipumua polepole. Akainama na kumgeuza uso. Mara alijikuta kashtuka akiwageukia wenzake kwa macho ya kutokuamini.
“Kati yenu hakuna anayemfahamu mtu huyu?” aliwahoji.
Watu hao walimtazama mtu huyo na kumrudushia Kombora macho ya mshangao. “Huyu si Joram Kiango mzee?” mmoja wao alijibu.
“Joram Kiango!” Kwame alifoka tena. “Yule kijna wa C.I.D? La haula! Angeweza kufa mbele ya macho yangu kama asingeweza kutumia vyema bastola yake.”
“Joram sio C.I.D,” Kwame aliambiwa. “ Ni kijana mwenye ofisi yake ya upelelezi, ambaye amefanya mengi kulisaidia taifa.” Kombora alisita, kisha akamgeukia Kwame, “Ndiyo ndugu Kwame. Nadhani waweza kutufunua macho na kutueleza kinachotokea katika ofisi hii.”
Kwame akiwa katika hali ile ile ya kuchanganyikiwa ingawa macho yake yakiwa maangavukinyume cha hali yake, alisema kwa sauti ya utulivu, “Sidhani kama kuna mengi ya kueleza bwana inspekta. Nilikuwa nikiendelea na shughuli zangu kama kawaida, dakika chache tu zilizopita, mara akatokea bwana huyo mmnayemwita Joram na kuingia huku mbio. Kabla sijamuuliza lolote marehemu huyo naye akaingia. Wakavaana na kupigana kwa muda. Joram alipoelekea kuzidiwa aliitoa bastola na kuifyatua. Muda mfupi nanyi mnaingia.” Alipoona Kombora hajaridhika aliongeza, “Ni hayo tu bwana Kombora.”
“Hayo tu? Hujasema lolote juu ya simu. Umepiga baada au kabla? Kombora alihoji.
“Simu! Simu ipi?”
“Simu iliyotuleta hapa.”
“Siifahamu simu hiyo. Yaani mmepata simu? Basi bila shaka hyo ni katibu wangu. Nadhani aliona pindi wakiingia ndipo akakupigia.
“Yuko wapi?”
“Sijamwona tangu alipoanza haya. Nadhani mara tu baada ya simu hiyo kukufikia amekimbia. Nakuambia bwana ilikuwa hali ya kutisha kweli. Nilichanganyikiwa…”

Kombora akamkatiza kwa kuuliza, “ Wakati wote wa mapambano wewe hukuweza kufanya lolote? Umeshindwa walao kuinua simu kama alivyofanya karani wako?”
Haikuwa hali ya kawaida inspekta. Nakuambia nilichanganyikiwa…”
Huonekani kama mtu uliyechanganyiokiwa kiasi hicho! Kombora aliwaza, nusura ayatamke. Wala hakuona kama Kwame alikuwa mtu mwenye asili ya kushtushwa na jambo lolote kiasi cha kushindwa kujua la kufanya. Hata hivyo, hayo hayakuwa na nafasikubwa katika fikra za Kombora. Alikufa na mengi kichwani.
Sana alilitazama suala la mauaji hatimaye kifo cha muuaji na kuhisi tamati yake haimridhishi kama alivyotegemea. Hakuna alichopenda zaidi ya kifo cha Bazile. Na angependa zaidi kama fursa ya kukifumua chake kwa risasi angekuwa kaipata yeye. Lakini bado angeridhika zaidi kama tukio hilo lingetukia kwa namna nyingine. Namna iliyoridhisha zaidi.
Jana tu alikuwa kaanza kupata mawazo mapya juu ya mauaji hayo. Ilikuwa baada ya kuufuata ushauri wa msaidizi wake na kuikusanya pamoja akili yake katika kulishughulikia suala hilo. Alikuwa amemfikiria Bazile Ramadhani kama alivyo: kijana mwandishi chipukizi asiye na mengi ya ajabu, vipi aondokee kuwa hodari wa kuua kiasi cha kumkabili askari mwenye silaha na kumjeruhi? Zaidi, vipia askari huyo baada ya kuhojiwa sana bado anang’ang’ania kuwa alipoteza fahamu zake pindi akifanyiwa ukatili? Ingawa askari huyo alithibitisha kuwa mtu huyo alikuwa Bazile, bado Kombora alisisitiza hata alama za vidole zikachukuliwa kutoka katia uso huo ili zilinganishwe na alama nyingine. Lakini matokeo yalikuwa ya kutatanisha zaidi. Hazikupatikana alama zozote katika sehemu zote ambazo askari huyo alistahili kuwa ameguswa na Bazile. Yaelekea zilifutwa kwa uangalifu na alikuwa kavaa glovu. Hilo lilimshangaza Kombora. Kwa nini afiche alama hizo naye alikuwa akijitangaza mara kwa mara kwa simu? Mara Kombora akawa na mawazo mapya juu ya mauaji hayo. Alihisi kuwa kuna jambo zaidi ya wazimu wa mwandishi huyu. Vinginevyo, Kombora hakuona vipi kijana huyo angeendelea kutaabisha jiji huku akiepuka kila kikwazo ambacho polisi walijaribu kumwekea.
Hayo yalikuwa mawazo tu. Lakini yaligeuka kuwa mashaka. Mashaka ambayo yalijiimarisha kichwani mwake hata akiziruhusu fikra zake kutambaa huku na huko akitafuta uwezekano wa Bazile kushirikiana na watu wengine. Kwa nini? Ni ipi sababu ya mauaji hayo? Kuna uhusiano gani baina ya marehemu wote? Mara akapata wazo ambalo lilimshtua sana. yawezekana lipo jambazi au majambazi ambayo yalikuwa yakiitumia sura ya kivuli cha Bazile? Alijiuliza.
Yawezekana kabisa katika dunia hii iliyopiga hatua ndefu katika ndefu katika sayansi na teknolojia, lolote lawez kufanyika. Bazile aweza kuwa kofia tu ambayo imefunika mengi.
Mengi? Yepi? Kombora akajiuliza kwa hofu. Mara moja akamwita msaidizi wake na kumtaka achukue jukumu la haraka kujaribu kupata habari, mienendo, vitendo na uhusiano baina ya marehemu wote. Alisisitiza kuwa kazi hiyo ni muhimu na ipewe umuhimu zaidi ya lile jukumu la kumsaka Bazile.
Pindi Kombora akiwa ofisini kuisubiri taarifa hiyo ndipo ikamfikia simu hii ambayo ilimwita hadi hapa na kumkuta Bazile akiwa marehemu. Ni Bazile yuleyule. Si sura ya bandia wala mtu mwingine zaidi yake. Na inasemekana kafa pindi akikusudia kuua tena. Kumuua Joram Kiango. Joram ambaye mchango wake ni mkubwa mno katika harakati za kijambazi. Yawezekana kuwa Joram pia alikuwa akimsaka muuaji huyu? Na yawezekana huu ukawa mwisho wa kisa hiki cha kikatili? Hakutakuwepo na kusimama mahakamani kumsikia Bazile akikiri au kukanusha mauaji haya.?
Kombora angeweza kuwaza mengi zaidi. Lakini hakuiona sababu yoyote ya kuendelea kuusumbua ubongo wake pindi Joram alikuwa hai. Baada ya sindano moja tu ya daktari atazinduka na kutoa maelezo kamili.
“Well!”
“Well?” Kwame alihoji.
Kombora akagundua kuwa alikuwa ameropoka. Akamtazama Kwame kwa macho yenye maswali mengi lakini hakuuliza chochote.
Na awaze apendavyo! Kwame alijinong’oneza kimoyomoyo. Awaze anavyotaka. Asingeweza kuutengua ushahidi aliouandaa hata kama ni askari mwenye shahada ngapi.
Hadithi nzuri ilioje. Hadithi isiyopingika kabisa…. Kwame aliendelea kuwaza. Bazile Ramadhani, mwandishi, kapata wazimu. Kamuua mchapishaji wake. Damu ikampanda kichwani, akachemka kuua ovyo. Mara kupambana na Joram Kiango. Ramadhani kazidiwa na kuuawa na Joram. Polisi wenyewe ni mashahidi. Wamemkuta muuaji anakufa. Nani aikatae hadithi. Na ataikataa kwa misingi ipi pindi hakuna anayejua ukweli?


Ukweli ulikuwa siri yake Kwame na wachache ambao hawawezi kufunua midomo yao na kuitoa. Hakuna mwingine anayefahamu kuwa muuaji si Bazile ila hilo kundi lake ambalo dakika chache tu limetoweka na kumwachia yeye, Kwame fursa ya kutia risasi katika mwili wa Bazile. Wala hakuna atakayefahamu kuwa mauaji ya Kitenge, mchapishaji, yalipangwa ili kuwapotezea askari lengo la kuwafanya polisi wazidi kuamini kuwa muuaji ni Bazile Ramadhani. Na kwamba Fambo Wamangi na Jugeni Kawamba walikuwa wameuawa bila hatia yoyote. Kosa lao kubwa ilikuwa kusafiri katika ndege moja na Kwame alipotoka visiwani kukamilisha mipango ya kuuza kisiwa. Ilionekana kuwa wao wangeweza kuwa daraja la kuwafanya wapelelezi kumfikia Kwame au walao kushuku jambo endapo kifo cha Dismas Komba kingetukia.
Ni Komba tu aliyetakwa. Na ni yeye aliyekuwa na hatia ingawa yeye pia alipata hatia hiyo kwa ajali. Akiwa uwanja wa ndege baada ya kutua kutoka Zanzibar, alikosea na kuchukua suitcase ya Kwame badala ya yake. Alipofika nyumbani aliifungua na kukutana na kile ambacho macho yake hayakutakiwa kuona. Kabla hajajua la kufanya kwa siri hiyo, wafuasi walishapeleleza anakoishi na kumwandama kwa hadhari huku wakimtesa kwa mbinu aina aina ili arejeshe bahashahiyo yenye siri. Naye akijua mara tu aitoapo watamuua ndipo akaing’ang’ania kwa udi na uvumba. Jambo ambalo halikuyaokoa maisha yake, kwani Bon alikuwa ametimiza wajibu wake.
Nani atayajua yote hayo? Kwame alijiuliza kwa kiburi. Zaidi, nani atayajua katika muda mfupi uliosalia?
Huyu askari mkuu hapa haonekani mjinga, lakini hana nafasi ya kuunga vipande vyote vya matukio na kupata pande zima la kisa na ushahidi wake wakati unaofaa. Joram? Joram yuko usingizini na ataendelea kulala hadi kesho. Atakapoamka kujua hakutamsaidia yeye wala mtu yeyote, itakuwa….
Kwame alilazimika kusita alipomsikia Kombora akitoa amri ambayo hakuitegemea.
“Unasemaje inspekta? Apelekwe Muhimbili? Ya nini kusumbuka. Nimekwisha mpigia daktari wa kampuni yangu aje mara moja kumpa huduma ya kwanza,” Kwame alisema.
“Daktari wako?” Kombora akauliza akitazama, “Umempigia lini simu hiyo?”
Muda mfupi kabla yenu.”
“Nadhani ulisema kuwa hujapiga simu yoyote.”
“Nilipiga. Atafika wakati wowote, kama una msaada wa haja bwana inspekta nadhani msaada huo ungekuwa kuiondoa maiti hii mbele yangu. Ofisi hii si jumba la maiti. Suala la Joram niachie mimi. Ameyaokoa maisha yangu. Ningeweza kufa.”
“Joram hatatibiwa hapa,” sauti kali ya kike ilitamka ghafla. Wote wakageuka kumtazama msemaji. Alikuwa msichana mwenye umo na sura nzuri ambaye aliingia ghafla baada ya kubishana sana na askari wa mlangoni.
Kombora alimfahamu kwa sura na jina. “Neema!” akaita.
“Ni mimi inspekta. Ni mimi niliyekupigia simu kama nilivyoelekezwa na Joram,” akaongeza akiinama kumgusa Joram ambaye alilala kwa utulivu mkubwa. “Inspekta, Joram hawezi kutibiwa hapa. Tena ningeomba apelekwe Muhimbili mapema iwezekanavyo.”
“Kwa nini? Daktari wangui…” Kwame alijaribu kusema. Alikatizwa na Kombora ambaye alifoka kwa Kiingereza.
“Shut up!” akawageukia wasaidizi wake na kuwaamuru wamchukue Joram mara moja.


Fahamu zilipomrejea, Joram alifumbua macho polepole na kuyafumba mara moja kwa kushindwa kustahimilinuru ambayo aliona kali mno. Alipoyafumbua tena, alifaulu kutazama pande zote. Kitu cha kwanza alichokiona ilikuwa kofia ya kipolisi, ilikuwa juu ya kichwa cha mtu mwenye mavazi ya kipolisi aliyesimama kando akimtazama. Huyo alikuwa mmoja kati ya polisi wane waliokuwa chumbani humo silaha mikononi. Kisha, Joram aliweza kuwaona daktari na nesi ambao walikuwa wakimhudumia.
Baada ya kutazama sana aligundua kuwa alikuwa katika chumba maalumu katika hospitali ya Muhimbili. Joram akiwa mtu asiye na mazoea ya kufika hospitali kwa miaka, hilo lilimshangaza sana.
“Nini kinatokea? Niko hapa kwa nini?” akauliza.
“Pole sana bwana Kiango,” daktari alimjibu. “Pumzika kidogo umsubiri inspekta Kombora ambaye yuko nje akisubiri kuzungumza nawe. Kabla hajafika huruhusiwi kuzungumza lolote.”
“Kwa nini?” Joram alihoji. Lakini mara akarudiwa na matukio yote ya muda mfupi uliopita. Akakumbuka kuwa alikuwa mbele ya umati wa wauaji wenye dhamira ya kumwaga damu na kupoteza uhuru wa wananchi usiku wa leo. Akakumbuka pia kuwa katika juhudi zake za kuwazuia ndipo alinusa harufu ambayo bila shaka ilitoka katika mitambo ya Kwame, ikamtia usingizi. Baada ya hapo, hakusikia lolote isipokuwa hisia tu, kama ndoto alisikia majadiliano ya haraka haraka kwa sauti za hofu baina ya watu hao waliochanganyikiwa. Yaliyofuata hakuyafahamu.
“Ndiyo!” akafoka ghafla akiitazam saa yake na kuona ikikaribia saa nane mchana. “Yuko wapi Kombora?” akawageukia askari, “Mwiteni haraka.”
Haikuwepo haja ya kumwita. Wakatri huo huo, Kombora aliingia. Baada ya kupokea saluti kutoka kwa askari hao akawataka wasubiri nje. Daktari na msaidizi wake pia waliombwa kutoka.
“Ndiyo bwana Joram. Kwanza nikupe pole kwa yote yaliyokupata. Kisha nitakuomba unifafanulie kwa niaba ya jeshi zima la polisi kitu gani kinachotokea,” alisema akiketi kitandani.
“Kitu kinachotokea? Nadhani sijakuelewa vizuri inspekta,” Joram alimjibu. Alipoona upinzani katika macho ya Kombora aliongeza haraka, “Sivyo. Nina maana kuwa nitapenda kufahamu yepi unafahamu na yepi yamenifanya niwe hapa Muhimbili chini ya ulinzi mkali wa polisi badala ya kuwa mahala fulani huko ahera au peponi. Ilikuaje hata ukafaulu kuniokoa.
“Yametokea mengi zaidi ya kukuokoa Joram,” Kombora alisema akitoa sigara na kumpa Joram moja. “Mengi mno. Nikianza mwanzo ni kwamba nilipokea simu kutoka kwa msichana wako, kama alivyodai yeye, kuwa mtu anauawa katika ofisi ya Kwame. Nikaenda mara moja na kukuta wewe umezirai na bastola ambayo imemuua yule mtu tuliyekuwa tukimsaka kama kunguni, Bazile Ramadhani.”

Bazile amekufa! Umemwona!…” Joram alihoji kwa mshangao.
“Ndiyo. Kwani hukumuua wewe?”
“Mimi!”
Kombora akatikisa kichwa na kuendelea, “Hilo ni lingine katika mengi ya kutatanisha katika mkasa huu. Lingine ni matokeo yaliyotokea pindi tukikuleta hapa. Ulikuwa kwenye gari aina ya Landrover iliyokuwa ikiendeshwa na askari wangu. Msichana wako alikuwa katika hiyo gari pia. Gari hiyo ilipokuwa imalize barabara ya Morogoro iingie mtaa wa Umoja wa Mataifa iligongwa makusudi kabisa na gari nyingine aina ya Landrover. Wewe kwa kuwa ulikuwa umelazwa kwenye kiti hukudhurika. Dereva wangu ameumia kidogo. Lakini msichana wako….”
“Neema! Tafadhali Inspekta! Usiniambie kuwa Neema amekufa!” Joram alidakia.
“Hakufa, ila…”
“Ila?”
“Ametoweka.”
“metoweka? Sijakuelewa Inspekta.”
“Kwa kweli ni tukio la kutatanisha. Mimi nimefika katika eneo la dakika nne tu baada. Nimekuta watu wakishughulika. Nikaambiwa kuwa teksi moja imejitolea kumchukua Neema na dereva wa gari iliyogonga ambaye hakuumia sana. kwamba imewaleta hapa hospitali. Lakini tumeshakagua hospitali nzima bila dalili yoyote ya Neema wala huyo dereva.
“Jambo la kutisha zaidi ni barua hii fupi ambayo imeokotwa katika chumba hiki pindi ukitibiwa. Imeandikwa jina lako.”
Joram akaipokea na kuifunua. Iliandikwa kwa mashine, wino mwekundu ikisema;

Mpendwa Joram,
Nakuonya usifunue mdomo kwa yeyote kusema lolote. Vinginevyo kesho utaamka hapo kitandani na maiti ya mpenzi wako.
Rafikio Joe Kileo.

Baada ya kuisoma Joram alimgeukia Kombora. Ingawa alijitahidi kuficha mshtuko alioupata kwa habari hiyo, hakufanikiwa kumfanya Inspekta Kombora asihisi mteremo katika sauti yake aliposema, “Endelea mzee.”
“Nadhani sina zaidi,” Kombora alimjibu. “Labda naweza kusema kuwa nina mashaka na mtu anayeitwa Kwame. Vitendo na maneno yake vinaonyesha kuwa anajua mengi kuhusu mkasa huu. Kifo cha Bazile bado kinatatanisha. Barua hiyo kwako inaongeza uzito katika mashaka yangu.kwa ajili hiyo, nimewapa wapelelezi kadhaa kazi ya kuchunguza mienendo ya Kwame na kuniletea taarifa mara kwa mara. Inashangaza ripoti zote zinaposema yuko katika hali ya kawaida na anaendelea n shughuli zake kama kawaida baada ya kutoka mara moja kwenda Salamander ambapo amepata kahawa na kuzungumza na watu wachache juu ya ‘mkasa’ katika ofisi yake. Sasa hivi inasemekana yuko ofisini mwake kama kawaida ingawa katibu wake hajapatikana.”
Hayo yalizidi kumfumbua Joram macho. Akaipata picha kamili ya yote yaliyokuwa yametukia. Akaelewa kuwa baada ya jaribio la Kwame la kumuua kwa gari kukwama, aliona hatari ya Joram kueleza polisi ukweli na ndipo akamteka Neema na kuleta waraka huu ili kumtisha asiendelee na mipango yake hatari.
“Hivyo ndugu Joram,” Kombora alikuwa akiendelea kueleza, “Kadri n inavyokufahamu, natumaini hutakuwa tayari kutii waraka huo ambao unakusudia kuwaweka mapenzi mbele ya jambo la hatari kama hili. Utakkuwa mwanamume kama ulivyo na kueleza kwangu yote unayofahamu ili tushirikiane kuyaokoa maisha ya mpenzi wako pamoja na…”
“Neema si mpenzi wangu,” Joram alitamani kufoka hivyo, lakini alijizzuia. Ingemchukua muda mrefu mno kumfanya Kombora na watu wengine waelewe kuwa uhusiano wake na Neema ulikuwa wa kikazi tu. Muda ambao hakuwa nao kabisa. Kwa sasa, alifikiria jinsi Kwame alivyokuwa akiendelea na mipango yake bila hofu yoyote akiamini kuwa iwapo majasusi wake walifaulu kuleta barua hiyo kwa siri wasingeshindwa kumuua. Bila shaka walidharau wakijua kuwa muda waliokuwa nao ungetosha kuwawezesha kutawala nchi. Aliwaza pia kuwa huenda wameacha vifaa vyao ambavyo sasa vinapeperusha kila neno linalotamkwa chumbani humu hadi masikioni mwa Kwame kama alivyowafanyia polisi. Hivyo, Joram alimkatiza Kombora kwa kumjibu akisema , “siwezi kutishwa na kijibarua kama hicho Inspekta. Wewe wanifahamu vyema. Kwa bahati mbaya sifahamu lolote kinyume cha ukweli ulivyo.”
“Ukweli upi?” Kombora alihoji kwa mshangao. “Unataka kusema kuwa ni wewe uliyemuua Bazile?”
“Oh, Yes,” Joram alidakia.
“Hatukufahamu kama muuaji Jopram.”
“Kwa hiyo tangu leo mmenifahamu kuwa sishindi kutumia bastola yangu kwa muuaji kama yule. Kama unataka kunitia kizimbani kwa kosa hili niambie.”
Kombora akaonekana kuchanganyikiwa, “Acha uoga Joram. Mapenzi…”
“Tafadhali Inspekta. Suala la mapenzi yangu na Neema halikuhusu,” alijitia mkali.
Wakati huo mikono ya Joram ilitambaa polepole mwilini mwake akipapasa alikoficha silaha zake za siri, kamera ndogo pamoja na kanda ya kunasia sauti. Akatabasamu kwa furaha kuona vitu hivyo pamoja na misukosuko yote, vilikuwa salama katika mifuko yake ya siri.
Akavitoa na kumpa Kombora huku akimfanyia ishara ya kutokusema lolote. Kombora alivitazama kwa mshangao, lakini akavifahamu mara moja na kuvidaka kwa furaha.
“Kwa hivyo bwana Kombora maadamu nimepata nafuu naomba uniruhusu nijipumzishe. Kama maswali nitayajibu kesho. Siwezi kuihama nchi usiku mmoja.”
Kombora , akiwa kamwelewa Joram, alijitia kubisha kidogo.
“Mpenzi wako?”
“Suala lake niachie mwenyewe. Kesho nitampata.”
“Sikujua kuwa u mwoga hivyo Joram. Lakini sina budi kukwambia kwamba tuna mashaka. Polisi itafanya kila njia kupata ukweli. Nawe utahesabiwa kuwa mwenye hatia kwa kuficha habari.”
“Kesho Inspekta, tafadhali,” Joram alijibu akiinuka na kutoka. Ndiyo kwanza akagundua alivyodhoofika. Mwendo wake ulikuwa wa kujikongoja hadi nje ya chumba ambapo alisimama kwa muda akikusnya nguvu.


“Umesikia?” Kwame alitabasamu, macho yake ambayo dakika chache nyuma yalimtazama mwezi wake kwa hasira ya kutisha kidoo yalikuwa yameisahau hasira hiyo, ingawa yaliendelea kutoa nuru ya kuogofya. “Umesikia mwenyewe Joram akikiri kuwa amemuua Bazile. Hawezi kuwa mjinga na kukubali kumpoteza msichana mzuri kama yule kwa ajili ya mabadiliko tu ya serikali. Atakachoofanya ni kuwazungusha hadi kesho. Na kesho hiyo…”
“Simwamini hata chembe kijana yule. Ana akili za ajabuajabu,” mwezi wake alikanusha. “Aweza kuwa sasa hivi anabuni jambo lingine la kututia mikononi.”
Kwame akaukunja uso wake, “Uoga wa aina hiyo siupendi kabisa bwana Matata,” alifoka. “Kama huniamini wala kuwaamini wataalamu, matajiri na watu mashuhuri walioandaa mipango yote hii, tamka mara moja ili tukuondoe katika mipango yetu. Na nafikiri sina haja ya kukumbusha adhabu ya mtu anayevunja kiapo cha hatari kama hiki.”
“Siyo hivyo bwana Kileo. Ila…”
“Ila nini?” alifoka tena. Kisha akaishusha sauti yake akisema, “Joram yumo mikononi mwetu. I kwa kuwa tunaye msichana wake, bali pia makachero kadhaa wako nyuma yake. Wakati wowote watakapoarifu kuwa anaelekea kwenda kinyume cha matakwa yangu atakula risasi. Kumwachia hadi sasa ni pamoja na hamu yangu ya kutaka kuona hayo machachari yake hapo kesho wakati tutakapokuwa Ikulu, nchi itakapokuwa chini ya miguu yetu.”
Kimya kifupi kikafuata.
“Kwa hiyo, bwana Matata, sikuiona kabisa sababu yaw ewe kurejea hapa kwa ajili ya kule kusita tu ati Joram amenusurika katika ajali ya gari. Nakupa amri ya mwisho kuondoka hapa. Na nakuomba tusionane tena hadi kesho tutakapokutana Ikulukuapishwa kama baraza lipya la mawaziri na baadaye katika ukumbi wa Karimjee au Kilimanjaro Hoteli kwa tafrija maalumu. Sawa?”
“Sawa bwana…”


MOTO Matata alipowasili katika jengo la wizara yake, alilisahau mara moja jina hilo na kuendelea katika jina lake halisi na hadhi yake katika wizara hii. Kama mtu mkubwa, alitumia lifti maalumu ambayo ilimfikisha ghorofa ya nane ilikokuwa ofisi yake.

Akautumia mlango wa pili kuingia ofisini mwake ambamo alijibwatika juu ya kiti na kuitazama saa yake. Ilisema saa nane na dakika ishirini. Saa kadha wa kadha zilisalia kabla ya kutokea jambo ambalo lingebadili historia ya nchi.

Matata alihofia sana muda huo wa kusubiri. Hakuwa na hakika kama anastahili kuendelea na mipango yake au atoroke nchini mara moja kama roho ilivyokuwa ikimshawishi. “Utajiri hauji kwa starehe”… alijikumbusha kwa taabu maneno ya Kwame.

Kuyakumbuka huko kukamtia moyo hata kicheko kikamtoka na akasahau ndoto mbaya zilizomwandama usiku wa jana akijiona yuko kitanzini huku umati wa watu ukimcheka na kumsimanga.

“Ndoto au woga tu,” aliwaza. “Kesho ni siku nyingine. Nitakuwa mtu mwingine; tajiri na mwenye matumaini na nafasi ya kuwa tajiri na tajiri tena..”

Simu iliyomuunga na katibu wake ikakoroma ghafla. Akaiinua na kulitaja jina lake.

“Umerudi mzee?”

“Ndiyo Salome, lakini sijisikii vizuri, hivyo sitapenda kusumbuliwa kwa matatizo madogo madogo.”

“Nimeelewa mzee, ila kuna huyu kijana hapa. Anadai kuwa ni lazima akuone kwa hali yoyote. Anasema mnafahamiana na kwamba ana hakika utafurahi kumwona.”

“Amekutajia jina lake?”

“Ndiyo. Anajiita Joram Kiango.”

“Nani?” Bwana mkubwa alinguruma katika simu kiasi cha kuyaumiza masikio ya katibu wake. Hakujua afanye nini. Hakujua kama alistahili kumwona au la. Akabaki kaduwaa na simu mkononi hana uwezo wa kumjibu Salome ambaye aliendelea kuongea upande wa pili.

Joram alimkuta katika hali hiyo.

“Nadhani nitasamehewa kwa kuingia kabla ya kibali chako mzee,” Joram alisema kwa sauti yake tulivu akijiweka kitini bila kusubiri kukaribishwa. Nimeona nikutembelee mapema ili nishirikiane nawe kujadili maisha yako ya baadaye. Unasemaje mzee?”

Jibu halikusikika hivyo Joram aliendelea, “Kitendo chako na wachache wenye nyadhifa kadha wa kadha serikalini, ambao mmethubutu kula njama dhidi ya taifa lenu, taifa changa, ambalo linakutegemeeni ninyi kuliokoa, ni kitendo cha aibu kubwa mno. Ni kitendo ambacho hakistahili kuyafikia masikio ya taifa hili ambalo lilikutegemea sana hata likakupa wadhifa muhimu kama huu.

Hivyo nilichofuata hapa ni kukushauri tuondoke pamoja hadi Ikulu kwa mtukufu Rais ambako utakiri madhambi yako yote na kumwachia jukumu la kuamua.

“Usijidanganye kuwa ndoto yenu yaweza kuwa kweli,” Joram aliendelea. “Orodha yenu, picha zenu, maongezi yenu ya asubuhi ya leo na njama zenu zote sasa hivi ziko mikononi mwa wanaohusika. Kuchelewa kujitoa kutakufanya uaibike zaidi. La muhimu ni kwenda mwenyewe mbele ya Baba wa Taifa ambako utatubu na kukiri yote bila kusahau kuwa unahusika kwa kila hali katika mauaji ya watu wengi wasio na hatia.”

Bwana mkubwa huyo alishindwa kujibu lolote, walao kumtazama Joram usoni. Baada ya muda mrefu alinong’ona kwa sauti ya aibu akisema, “Siwezi. Siwezi kumtazama Rais wala raia yeyote usoni. Tafadhali nenda zako nifikirie la kufanya.”

“Fikiria bila kusahau kwamba mpango umeharibika,” Joram alisema akiinuka na kutoka nje. Akamuaga katibu na kutoka hadi mbele ya lifti ambapo alibonyeza kidude cha kuteremkia. Lifti ilipofika, aliteremka hadi chini.

Mlango wa lifti ulipofunguka masikio ya Joram na abiria wote waliotoka ndani ya lifti hiyo yalidakwa na kelele za ghafla zilizotoka katika umati uliokuwa ukijaa haraka haraka chini ya jengo hilo la wizara. Joram akawa mmoja kati ya watu waliokimbilia sehemu hiyo kutazama kinachotokea. Lilikuwa jambo la kutisha kuliko alivyotarajia. ‘Bwana mkubwa’ ambaye alikuwa akiongea naye muda mfupi tu uliopita alikuwa kalala chali akivuja damu nzito kutoka katika majeraha ya kutisha ya kichwa kilichoonekana kufumuka, miguu iliyovunjika na kiuno ambacho kilionekana kuvunjika kabisa.

“Nimemwona akijitupa mwenyewe toka dirishani,” alidai mtu mmoja.

“Mimi pia…”

Joram akaitazama saa yake na kuondoka mahala hapo kwa mwendo wa haraka. Mbele kidogo, alipungia teksi na kumweleza dereva wapi alihitaji kupelekwa. Ilimfikisha kwa muda mzuri. Joram akateremka na kuiendea ofisi aliyoihitaji ambamo aliomba kuonana na ‘Afande mkubwa zaidi’.

Akaelekezwa ofisi yake.

Alimkuta afande huyo kabadilika kabisa kwa magwanda ya kijeshi yenye nyota nyingi mabegani kinyume kabisa cha yale ya kiraia aliyovaa katika mkutano wao wa siri. Afande huyo alimtazama Joram mara moja na kujikuta akishikwa na hofu kubwa.

Ghafla, akasahau furaha aliyokuwa nayo muda mfupi alipokuwa akiwaza kesho itakavyokuwa siku tofauti mno kwake. Siku ambayo itamkaribisha katika dunia ya kutumia bila hofu ya kuishiwa, dunia ya kumchukua msichana yeyote amtakaye bila kuogopa sheria wala wazazi wake, dunia ya yeye kuwa na amri juu ya kuishi na kufa kwa mtu yeyote katika nchi hii. Naam, dunia itakayomweka hadharani, kila mtu akimtetemekea. Alikuwa akisubiri saa zitimie ili atimize wajibu wake kuikaribisha dunia hiyo.

Katika muda huo wa kusubiri, hakutarajia kabisa kuonana na
kijana huyu aliyeketi mbele yake akivuta sigara na kutabasamu kisirisiri.
“Nani wewe? Na wataka nini hapa?” akajitia kuuliza.

“Tunafahamiana sana afande. Nadhani huwezi kusahau kuwa muda mfupi uliopita tulikuwa wote katika mkutano fulani. Kwa jina naitwa Joram Kiango.”

“Sikufahamu wala siufahamu mkutano huo.”

Labda,” Joram alijibu. “Lakini naamini utaufahamu vizuri. Baada ya muda mfupi polisi watakapokutia pingu na kukuhifadhi hadi kesho ambapo picha yako na wenzako mkiwa mkutanoni zitakapotolewa gazetini na maongezi yenu kusikika katika Redio Tanzania. Ama hufahamu kilichonileta mbele yenu ilikuwa kupata picha hizo?

“U mtu hatari usiye na shukrani hata chembe,” Joram alifoka. “Wadhifa ulionao ni mzito. Mamilioni ya Watanzania wangeweza kuumudu wadhifa huo lakini taifa limekukabidhi wewe. Ili ulilinde. Ili uwe mstari wa mbele kulinda silaha na masilahi yake. Lakini wewe unageuza silaha walizokupa wao kuwaangamiza. Unashiriki katika mikataba ya kupokonya masilahi yao. Huoni aibu kuuza wananchi. Aibu ilioje! Kwa kweli hustahili kuishi.”

Afande huyo akainua uso kumtazama Joram kwa hasira, “Toka nje bwana mdogo,” akafoka. “Toka, vinginevyo nitakudhuru!”

“Lazima nikueleze kwanza nilichokusudia…”

“Toka. Toka!” akafoka.

“… Kwamba taifa hili si zizi la ng’ombe ambalo mtu yeyote anaweza kuligeuza rasilimali yake kwa faida yake binafsi na mabwana zake.”

“Toka!”

“Na…”

“Toka!” Safari hii ‘afande’ alikuwa na bastola mkononi. Bastola aliyotoa ndani ya mtoto wa meza. Ilimwelekea Joram kifuani. “Toka vinginevyo nitakuua!”

Sauti yake iliwavuta wengi. Wakaja na kuduwaa mlangoni wakiwa hawayaamini macho yao mkubwa kaielekeza bastola kwa raia ambaye alionekana hana hatia wala hofu.

“Kifo change kitaongeza uzito wa madhambi yenu juu ya damu
nyingi zisizo na hatia ambazo mmemwaga. Hakitaleta mabadiliko yoyote wala kufanikisha mipango yenu ya kishetani…”

Mara mlipuko wa bastola ukasikika. Kila mtu alifumba macho kwa miali ya mlipuko huo. Walipoyafunua, walimwona bwana mkubwa kasahau kiti chake na kukaa chini, kainamisha kichwa ambacho kilikuwa kimefumuka kwa risasi hiyo. Bado, mkono wake uliishikilia bastola hiyo iliyotimiza wajibu.

Umati ulipiga kelele za hofu na mshangao. Joram aliacha umati huo katika hali hiyo na kutoka nje ambako alipata shida kidogo kupata usafiri. Watu wote walikuwa wakikimbilia kufuata mlipuko huo. Joram akapishana nao hadi nje ya jengo hilo ambako alijipatia usafiri.

Safari ilimfikisha katika wizara nyingine. Akaifuata ofisi ya mtu mkubwa moja kwa moja na kuomba kumwona.

“Huwezi kumwona mtu,” katibu alidai. “Amepata habari mbaya. Hana hali nzuri kuweza kuonana na mtu yeyote.”

“Habari ipi?”

“Ya kifo. Bwana mkubwa serikalini kafa na alikuwa rafiki yake mkubwa.”

Joram akashangaa habari zinavyosafiri haraka haraka. Ni hicho alichohitaji. Genge hilo hatari lifahamu kuwa limefahamika na limevunjika. Mipango yao isiweze kuendelea. Joram akatabasamu huku huku akigeuka ili aondoke zake. Lakini mara hamu ya kuuona uso wa mtu mkubwa baada ya habari njema kama hiyo ikamshika.
Akamgeukia katibu wake na kumwambia: “Nataka kumwona. Ni lazima nimwone. Siwezi kuondoka bila kumfariji. Mimi ni rafiki yake pia.”

Alipoona achelewa kuruhusiwa, alijielekeza mlangoni na kuuendea. Akagonga mara moja na kuufungua. Alimkuta bwana mkubwa kasimama nyuma ya meza mkono wake ukizungusha namba za simu, mkono wa pili ukiwa umeshika shavu. Mkono uliokuwa kwenye simu ulisita ghafla mara macho yake yalipokutana na yale ya Joram ambaye alikuwa akitabasamu.

“Pole mzee.”

“Nani wewe? Joram!” mtu mkubwa alifoka. “Tafadhali toka nje ya ofisi yangu.”

“Ndiyo,” Joram alijibu. “Lakini si kabla ya kukumbusha kuwa wenzako wametangulia kwa heshima kidogo. Hawatawajibika kutazamana na umati ambao utajaa mahakamani kukutazama kwa mshangao wewe na wenzako pindi mkijibu maswali ya Jaji Mkuu. Wala hawataning’inia juu ya kitanzi na kufa polepole huku wakijutia uroho wao na utovu wa shukrani ambao wamekufanyeni kuwa fisi mbele ya kondoo badala ya wachungaji. Aibu iliyoje kuwa na kiu ya utajiri kiasi hicho, pole tena mtu mkubwa.”

Mtu huyo alimtazama Joram kwa macho yenye mchanganyiko wa hasira na aibu. Kisha aliutia mkono wake katika mfuko wa koti na kutoa pakiti ya vidonge vidogo vidogo vya usingizi ambavyo alivimimina mkononi na kuvitupia kinywani. Alivyohakikisha amevimeza alimtazama tena Joram na kusema, “Siwezi kukubali kuitazama jamii….siwezi…” macho yake yakaanza kubadilika.

Akajibwatika chini akisahau kiti na kuketi sakafuni huku akijaribu kuyafumbua macho yake kwa juhudi kubwa. Hakufaulu. Mara akayafumba na kutulia.

Joram alifahamu kuwa huo ulikuwa usingizi ambao usingeisha. “Kifo cha amani kuliko alivyostahili,” aliwaza akitoka zake polepole na kumtupia katibu ‘kwa heri’ bila kumtazama usoni.

Nje ya jengo hilo Joram alisita na kuwaza kwa furaha. Nusu ya kazi ilikuwa imekwisha. Mizizi mingi ilikwishang’olewa. Uliosalia ni ule mzizi wa shina; mzizi wa fitina; Kwame au Joe Kileo. Huyu alikuwa mtu hatari na bado alikuwa na Neema tayari kumdhuru endapo angejua mambo yanamwendea kombo.

Hivyo, alihitajiwa kupatikana haraka, katika hali ya uangalifu zaidi. Hali ambayo Joram alihitajika kuwa mkamilifu kwa kila hali. Kwa bahati baya hakuwa na silaha zozote za haja mfukoni zaidi ya visu kadhaa vilivyohifadhiwa katika mfuko wa siri. Lakini kwa ajili ya haja kubwa ya kumpota Neema akiwa hai bado, Joram alijikuta ndani ya teksi akielekea jengo la Snow Fund.

Gari liliposimama, Joram alijikuta akiruka nje na kutazamana na Inspekta Mkwaju Kombora ana kwa ana. Kombora alikuwa na bastola wazi mkononi, nyuma yake, askari sita wenye bunduki aina ya Sub-Mashine Gun wakimfuata kwa uangalifu.

“Joram,” Kombora alimwita kwa nguvu alipomwona. “Umekuwa wapi muda wote huu? Kijana, nasikitika muda hautoshi kuweza kuzungumza mengi. Lakini kwa ufupi tu safari hii ulichogundua ni kitu kizito ambacho kingeifanya nchi hii igeuke dimbwi la damu ama iwe zizi ambalo mchungaji ni fisi mwenye njaa.”

“Nami nasikitika pia Inspekta kuwa umegundua mapema kuliko nilivyotaka,” Joram akamjibu. “Ningependa kukamilisha kazi hii peke yangu kwa faida ya watu ambao wengi wao wana vyeo vikubwa serikalini. Nilikuwa nikiwaonea aibu au huruma kuwafanya wasimame mbele ya wananchi waliowaamini madaraka hayo na kukiri madhambi yao. Kwa bahati umeniwahi.
Hata hivyo, wengi wameshafuata njia inayowastahili. Wamejiua wenyewe. Utapata taarifa kamili baada ya muda mfupi.

“Kadhalika, huko Kigamboni iko nyumba moja ambamo amelala marehemu asiye na hatia, Komba ambaye ndiye hasa aliyesaidia siri hii ya hatari kutoka nje. Ameuawa na jambazi hatari ambalo bado liko hai katika nyumba hiyohiyo. Nimelifunga vizuri. Halina nafasi ya kutoroka. Mara tu upatapo nafasi, nitapenda kupata askari ambao nitawaelekeza katika nyumba hiyo. Napenda Bon afe kwa kitanzi.”

“Kwa nini Joram?” Komba alifoka. “Kwa nini hukusema mapema? Anaweza kutoroka!” Kisha akajisahihisha kwa kusema polepole, “Kweli haikuwepo nafasi. Tuombe Mungu nimkute hai. Atajuta kuzaliwa. Sasa ni kumwingilia huyu kiongozi wao, Kwame.”

“Kwame ni mtu hatari sana,” Joram alikumbusha tena. “Na bado anaye Neema mikononi mwake. Bila shaka yuko katika jengo hilihili. Nadhani utahakikisha usalama wa Neema Inspekta.”

“Usitie shaka.”

“Wakaanza kuingia ndani wakiwapita wafanyakazi wa ofisi hiyo ambao kwa muda mrefu, walikuwa wamechanganyikiwa kwa matukio ya kutisha ambayo yalikuwa yakiitokea ofisi hii kutwa nzima. Waliduwaa juu ya viti vyao au wima wakimtazama Kombora, Joram na askari wote ambao waliingia na kuiendea ofisi ya mkurugenzi mtendaji.

“Hana nafasi ya kutoroka,” Kombora alimnong’oneza Joram. “Jumba hili limezingirwa kila upande. Askari wengine wako juu ya paa. Sijui atatokea wapi.”

“Usisahau usalama wa Neema Inspekta,” Joram aliasa tena. “Kwa kweli kazi hii ningependa kuifanya mwenyewe. Sina imani sana na askari wako…”

Kombota alimkatiza Joram kwa kumwambia, “Neema atatoka salama. Askari wote wameonywa waangalie sana risasi zao zisimguse msichana wako walao unywele. Natumaini watafanya kazi nzuri. Nimechagua wale ambao ni hodari kwa shabaha tu.”

Wakaifikia ofisi ya Kwame. Waligonga mara kadhaa bila jibu. Kombora akaita kwa nguvu ingawa alijua mlango huo ulikuwa maalumu kwa kutokuruhusu sauti kutoka nje. Alipochoka alielekeza bastola yake katika kitasa na kuifyatua. Risasi ya .45 maalumu kwa polisi haikusita kutimiza wajibu.

Chumba walikikuta kitupu, Kombora akatoa macho ya mshangao. Lakini Joram alizunguka nyuma ya meza na kuchungulia hapa kisha pale, mara sakafu ikafunguka na kuacha mwanya wenye ngazi iliyoelekea chini. Kombora akawa wa kwanza kuifuata. Joram alifuatia akifuatiwa na askari.

Huko chini walijikuta katika ukumbi wenye vyumba vingi vyumba vyote vilikuwa vimefungwa. Risasi ya bastola ya Kombora ikavifungua vyote. Waligundua mengi; akiba ya silaha, nyaraka za siri na dawa aina aina. Ni katika chumba cha mwisho ndimo walipopata kitu walichokuwa wakihitaji. Walimkuta Kwame kashika bastola mkononi mbele ya msichana aliyeketishwa sakafuni, nusu uchi kwa jinsi mavazi yake yalivyotatuka katika hali ya kuadhibiwa sana.

“Neema!” Joram alipiga kelele.

“Neema, ndiyo,” Kwame aliwajibu akitabasamu kifedhuli. “Ni mpenzi wako. Lakini endapo unampenda, waambie rafiki zako wote pamoja na mkubwa wao anayejiita Inspekta warudi walipotoka haraka. Mimi na wewe pamoja na mpenzi wetu tutaondoka pamoja hadi nje ya jiji ambapo nitawapeni uhuru wenu nami nichukue uhuru wangu.”

Kwame alichukua uamuzi huo baada ya kupata taarifa ikimfahamisha kuwa Joram alikuwa ametoweka machoni mwa walinzi wake. Taarifa hiyo ilifuatwa na vifo vya washiriki wenzake pamoja na kuambiwa kuwa askari walikuwa wakiizingira ofisi yake ndipo akawa hana njia zaidi ya hiyo.

Kombora akamgeukia Joram kwa mshangao. Alitarajia madhara, lakini hakutarajia madhara hayo yawe katika hali hiyo. Hakutarajia kumkuta Kwame akiwa na bastola mkononi akimtazama msichana asiye na hatia na ambaye ametoa mchango madhubuti kuiokoa nchi katika madhara ya mtu huyo. Msichana mzuri, Neema Iddi. Wakati huohuo, hakuwa tayari kuacha mtu huyo anusurike mbele ya macho yake mwenyewe hasa baada ya kuziona picha alizofotoa Joram pamoja na kusikiliza kanda ambayo ilinasa mengi yanayotosha kuwa ushahidi kamili dhidi ya watu hawa waovu.

“Labda hunifahamu vyema Inspekta,” Kwame alimjibu baada ya tabasamu lingine la kebehi. “Mwambie, Joram. Mwambie mimi ni nani. Nadhani wewe wanifahamu zaidi yake.”

“Nakufahamu sana,” Kombora alijibu. “Wewe ni jasusi mkubwa uliyepewa jukumu la kuharibu siasa na uchumi wa nchi kwa njia yoyote. Umefanikiwa kuwalaghai watu kadhaa kwa vishawishi vya kishetani na kupanga kuangusha utawala halali wa nchi hii usiku wa leo.”

“Kumbe wafahamu…” Kwame alijibu.

“Kwa bahati mbaya bwana Kwame au Joe Kileo mipango yako yote imeharibika. Utakachofanya ni kujitoa kwetu ili uwekwe mahabusu kusubiri hukumu kwa makosa yako yasiyohesabika. Umemwaga damu zisizo na hatia umethubutu kula njama dhidi ya nchi na wananchi. Umesababisha fujo na ghasia. Kwa kweli unastahili kula kitanzi Kwame. Ni hapo mabwana zako watakapofahamu kuwa nchi hii si uwanja wa mpira ambapo wanaweza kutegemea wapendavyo,” Kombora aliendelea kufoka.

“Kumbe wanifahamu Kombora!” Kwame alijibu akitabasamu kifedhuli. “Kwa bahati mbaya siwezi kushikwa nanyi. Nitaondoka na msichana huyu hadi nje ambako nitaamua wapi nielekee. Mkinilazimisha nitakubali kufa, lakini si kabla ya kuhakikisha bastola hii inaifumua sura nzuri ya msichana huyu. Nadhani hutapenda kushuhudia hilo mtakatifu Inspekta Kombora. Na Joram? Utafurahi mpenzi wako asulubiwe mbele yako?”

Wote walikubali kuchanganyikiwa. Joram alisaga meno kwa hasira. Lakini hakuona lipi afanye lipi aseme katika hali hiyo. Ingawa bastola ya Kwame ilikuwa ikimwelekea Neema, lakini macho na mawazo yake yalikuwa kwa umati huo uliomzunguka silaha zao zikimtazama kwa uchu.

Hivyo, hakuona wala kutarajia pindi Neema alipoinuka na kuachia pigo kali ka karate ambalo lilifanya bastola hiyo ipae angani. Wakati huo bastola zote zilifyatuka na risasi saba kuuteketeza uso na kifua cha Kwame. Alikufa kabla hajatua chini. Hakuwa na haja ya kupapatika!

“Neema!” Joram aliita kwa nguvu akimkimbilia na kumwinua pindi alipoanguka kwa mshindo wa bastola. Alikuwa hai… hakuwa na jeraha….

“Neema!” Joram aliita tena akimkumbatia kwa nguvu.

MWISHO
*HUO NDIO MWISHO WA RIWAYA YA MAREHEMU BEN R. MTOBWA ILIYOCHAPWA KITABU KWA MARA YA KWANZA MWAKA 1984. IMECHAPWA HAPA ‘KICHWAHITS’ KATIKA KUUENZI MCHANGO WAKE MKUBWA WA FASIHI KWA JAMII YA KITANZANIA NA HATA AFRIKA MASHARIKI KWA JUMLA. TAREHE 9, NOVEMBA, 2008 NDIPO GWIJI HUYU ALIPOIAGA DUNIA.

TUNASHUKURU KWA KUWA PAMOJA TANGU MWANZO HADI MWISHO.****

Isikupite Hii: Jinsi Ya Kumfanya Mwanamke Akupende Kwa Mara Ya Pili

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment