Utata wa 9/12 Sehemu ya Nne
KIJASUSI

Ep 04: Utata wa 9/12

SIMULIZI Utata wa 9/12
Utata wa 9/12 Sehemu ya Nne

IMEANDIKWA NA: HUSSEIN ISSA TUWA

*********************************************************************************

Simulizi: Utata Wa 9/12

Sehemu ya Nne (4)


Waliingia ndani ya wodi ile kwa kiherehere na papara kubwa, lakini walijikuta wakisita kwa muda wakiwa hatua chache ndani ya wodi ile, macho yao yakiwa pale kwenye kitanda alicholalalia Chambuso.

Manesi wawili walikuwa wamesimama mbele ya kitanda kile wakimtazama Chambuso kwa mshangao mkubwa. Nao wakajikuta wakipeleka macho yao pale kitandani.

Chambuso Mwagala alikuwa amelala chali akiwa amefumbua macho na akitazama mbele kwa macho yasiyokuwa na hisia yeyote. Yaani hukuweza kuona mshangao, hasira au fadhaa kwenye macho yale. Ni kwamba alikuwa amefumbua macho tu, ambayo safari hii hakuwa ametumbua kwa mshangao au woga kama ilivyokuwa hapo mwanzo.

Dokta Nigel Smith alikisogelea kile kitanda huku akimtazama Chambuso kwa makini, Inspekta Dilunga akiwa hatua chache nyuma yake, naye akimtazama yule kijana kwa udadisi mkubwa.

“Nini kimetokea…? Imekuwaje hata ameamka…?” Dokta Nigel aliwauliza wale manesi

“Na amesema kitu chochote baada ya kuamka….?” Inspekta Dilunga naye akadakakia kabla hata wale manesi hawajaweza kumjibu Dokta Nigel.

“Jamaa kaamka tu, yaani kafumbua macho tu, basi!” Brian Koba alidakia kutoka kwenye kitanda alichokuwa amelalia kwenye kona moja ya wodi ile, na ndipo kwa mara ya kwanza Dokta Nigel na

Inspekta Dilunga walipokumbuka kuwa naye alikuwamo mle ndani.

“Kwamba…?” Dilunga aliuliza huku akimgeukia Brian ambaye alikuwa amelalia ubavu kugeukia kule kilipokuwa kitanda cha Chambuso, sehemu yote ya ubavu wake ikiwa imepakwa rojo la plasta maalumu aina ya hogo, au P.O.P., mkono wake ukiwa umeinuliwa juu na ukiwa umeshikiliwa huko juu kwa kamba maalumu iliyokuwa imefungwa kwenye chuma kilichochomoza kwa juu ya kitanda kile.

“Sisi tulikuwa tunamgeuza afande hapa kutoka kulala chali na kulalia ubavu huu…” Mmoja wa wale manesi alisema, na kuendelea, “…sasa alipogeukia ubavu huu ndipo alipomuona kuwa ameamka.”

“Kwa hiyo ni hivyo tu…hakukuwa na jambo lolote alilofanya kuwajulisha kuwa ameamka?” Dokta Nigel alimuuliza Brian.

“Yaani kwa jinsi nionavyo, jamaa atakuwa aliamka kitambo akabaki kimya tu…mi’ nilivyogeuka ndipo nilipomuona…” Brian alijibu kwa taabu, sauti yake ikibainisha maumivu makali aliyokuwa nayo.

“Mmnh…naona mambo ni yale yale tu Dokta.” Dilunga alisema kwa wasiwasi. Badala ya kumjibu, Dokta Nigel alimuinamia Chambuso na kumtazama kwa karibu. Chambuso aliendelea tu kutazama alipokuwa akitazama bila ya kuonesha kutambua uwepo wa watu wengine kando ya kitanda chake. Dokta Nigel alipeleka kidole chake cha shahada moja kwa moja usawa wa jicho la Chambuso, ambaye alibaki vile vile bila ya kukwepua wala kupepesa jicho.

Dokta Nigel akazidi kukisogeza kile kidole kwenye lile jicho taratibu, na kilipofika karibu sana na jicho lile, Chambuso alipepesa jicho kama jinsi watu wote wafanyavyo pindi wakihisi kuwa kuna kitu kilikuwa kikielekea kuwaingia jichoni.

“Good! Hii ni safi sana…kuna mabadiliko sasa. Inspekta …ingawa kidogo,” Dokta Nigel alisema kwa kuridhika.

“Oh…vizuri…” Inspekta Dilunga alisema, kisha akamgeukia Chambuso, “Ongea na sisi sasa Chambuso, ni nini kilichotokea kule barabarani…?”Alimuuliza kwa kiherehere.

“Aan-Aaah…hatuendi hivyo bwana…” Dokta Nigel alimkatisha, kisha akamwambia, “…hebu naomba utupishe kwanza, tufanye uchunguzi zaidi…”

“Siwezi kusubiri hapa hapa…?” Dilunga alisaili.

“Hapana…afterall, Inspekta Brian naye si yumo humu humu…?”

“Okay…lakini nitahitaji matokeo yoyote haraka iwezekanavyo.”

Baada ya kujibu hivyo Inspekta Dilunga alitoka mle ndani na kwenda kushughulikia msako wa yule mtu aliyeamsha kizaazaa pale hospitalini asubuhi ile.

Ni nani huyu…na anahusika vipi na suala hili zima la mauji ya ajabu kule katikati ya barabara pweke ya Kazimzumbwi?

Njiani alipishana na Mzee Mwagala Kifyagi akikimbilia kule ilipokuwa wodi ya Chambuso Mwagala. Wala hakutaka kumsemesha, kwani naye alikuwa na yake yaliyokuwa yamemzonga kichwani wakati ule.


Saa nne baadaye Inspekta Dilunga alirudi tena pale hospitali, akiacha msako wa hali ya juu ukiendelea huko mitaani, msako ambao hadi muda ule haukuwa umezaa matunda yoyote, ingawa bado siku ilikuwa mbichi. Alienda moja kwa moja hadi kwenye wodi ya Chambuso Mwagala, na alipigwa na mshituko alipokuta kitanda alichokuwa amelalia yule kijana hapo awali kikiwa kitupu.

“Vipi… imekuwaje tena…?” Aliuliza huku akimtumbulia macho Inspekta Brian Koba aliyekuwa amelalia ubavu pale kitandani kwake.

“Wamempeleka kwenye chumba kingine kwa utafiti zaidi…kwenye mitambo maalumu ihitajikayo kwa tiba yake…” Brian alimjibu.

“Kwa hiyo hapa hawakuweza kupata chochote…?” Dilunga aliuliza.

“Ah, Inspekta….mbona hii hali ni ngumu! Zaidi ya kupepesa yale macho yule kijana hakuwa akitoa dalili yoyote nyingine kuwa yuko nasi hapa duniani…akiitwa jina lake haitiki wala haoneshi kuwa analitambua jina lake!”

“Ebwana we!”

“Ndio bwana…mara nyingine alipoonesha hisia ni pale alipochomwa sindano naye akakunja uso kwa muda, lakini zaidi ya hapo ni bure kabisa…baba yake analia kama mtoto huko…” Brian alizidi kumpasha habari. Inspekta Dilunga alikunja uso kwa taarifa ile ya kukatisha tamaa.

“Sasa tutajuaje kilichotokea kule barabarani iwapo huyu kijana hataweza kuongea…?” Alisema kwa fadhaa.

“Mi’ nadhani huyu kijana tumtoe kabisa mawazoni mwetu kwa sasa Inspekta. Atatupotezea muda tu. Chochote alichokiona usiku ule, kitakuwa kimemvuruga akili yake moja kwa moja…” Brian alisema.

“Akh, sasa…!”

“Sasa tuhamishie nguvu zetu kwenye kumsaka huyu mtu aliyeibuka leo…tukimpata huenda tukajua mengi juu ya kadhia hii kuliko jinsi ambavyo tungetarajia…”

Kimya kilichukua nafasi mle ndani wakati Dilunga akilitafakari lile wazo.

“Hebu na sasa nieleze ni kitu gani hasa kilikuchotokea, maana hii nayo ni pembe nyingine katika kesi hii inayoongezea ugumu kwenye kitendawili tulichonacho…” Hatimaye Dilunga alisema huku akiketi kwenye kona ya kitanda cha Brian.

Ndipo Brian Koba alipomsimulia mkasa wote uliomkuta wakati akikabiliana na yule mtu wa ajabu na mwenye nguvu zisizo za kibinadamu hata kidogo. Inspekta Dilunga alibaki kinywa wazi.

“Yaani unasema kuwa aliweza kujua ni nini kilikuwa kinapita kichwani mwako?” Aliuliza baada ya Brian kumaliza maelezo yake.

“Kabisa Inspekta! Kama mara mbili hivi amekuwa akitamka mawazo ambayo yalikuwa yakipita kichwani mwangu…tena alikuwa akinitazama kwa udadisi wa ajabu, lakini sasa baada ya kutafakari hali yote ile, nadhani alichokuwa akikifanya ni kusoma mawazo yangu…”

“Mnh, we’ Brian we’…unajua unachokisema lakini?”

“Najua. Na ni kwa sababu ni mimi mwenyewe ndiye niliyetokewa na mambo hayo Inspekta. Ingekuwa nami nasimuliwa kama wewe hivi sasa, hakika nisingeikubali kabisa hadithi hii.”

Kimya kilitanda tena, kisha Dilunga akaongea, “Kwa hiyo unataka kuniambia kwamba yule mtu hakuwa wa kawaida…”

“Naye mwenyewe kanithibitishia hilo kwa maneo yake! Yule si mtu bosi wangu, hebu nitazame nilivyo sasa Inspekta…ngumi moja tu ndio imenifanya hivi, nusura anivunje mbavu…na lile jambo lililotokea nilipompiga risasi! Sijawhi kutarajia kuona kitu kama kile maishani mwangu! Yaani ni shoti kubwa sana ya umeme Inspekta, na wala ile risasi haikumdhuru kitu….”

“Doh…!” Dilunga aliguna bila kupenda.

“Na aliniambia…kwamba nikijaribu tu kumpiga risasi kitakachotokea sitakuwa hata na uhai wa kujutia, nami nikadhani anavunga tu…”

Inspekta Dilunga alitikisa kichwa kwa mastaajabu.

“Mnh, ila safari hii tumekutana na kesi ya aina yake….naanza kuyatilia maanani mawazo ya Dokta Nigel sasa…kwamba labda haya mambo yote ni uchawi wa aina fulani…” Alisema huku akiendelea kutikisa kichwa.

“Na kama Chambuso ndio amekutana na mtu yule, basi sitashangaa kabisa iwapo yule kijana atapata wazimu wa milele. Yule mtu anatisha afande!”

“Na bado unataka tumsake…unadhani tutakabiliana naye vipi sasa, kwani kwa mujibu wa maelezo yako, huyu ni mtu ambaye hadhuriwi na risasi wala ngumi.”

“Yeah…lakini lazima kutakuwa na namna ya kummudu. Sisi hatuna jinsi Inspekta, lazima tumsake, vinginevyo ni kukiri kuwa hii kazi imetushinda, kitu ambacho siko tayari kabisa kukiafiki…”

“Ndiyo…”

“Na pia mimi binafsi nina hasira naye sana yule mtu. Kunifanya hivi mimi! Lazima nimsakame mpaka mwisho ujulikane!” Brian alisema kwa hasira iliyochanganyika na uchungu.

“Aaan-Aaah, sasa hii usiifanye ni kitu binafsi Brian, hii ni kazi, na inahitaji utendaji kazi na si visasi vya binafsi, unaweza kufanya kosa la kutumia jazba zaidi kuliko tafakuri….”

“Ah, sawa Inspekta…lakini ni lazima nimpate huyu mtu…”

“Na unadhani yeye ndiye anayehusika? Kwani kwa mujibu wa maelezo yako ni kwamba na yeye alikuwa akimuuliza Dokta Shabbir ni nini alichogundua alipoichunguza miili ile, ikimaanisha kuwa na yeye pia, kama sisi, hajui ni nini kilichotokea…” Dilunga alimuambia.

“Ni kweli. Nadhani yule mtu alikuwa akitafuta taarifa fulani kutoka kwa Dokta Shabbir. Kama ukiongea na Shabbir mwenyewe huenda ukapata picha kamili ni nini hasa alikuwa akitafuta…” Brian alijibu huku akionekana kuchoka.

“Okay Inspekta. We’ pumzika. Mi’ n’tajaribu kuongea na Dokta Shabbir…” Dilunga alimuambia na kutoka nje ya wodi ile. Mlangoni akakutana na Bruno Mgimba, mwandishi wa gazeti la Ngurumo.

“Heeey, Inspekta! Ndiwe hasa niliyekuwa nikikutafuta. Nimesikia kulikuwa kuna taarifa ya moto, ambayo kumbe haikuwa sahihi, una lolote la kuongea juu ya hilo…?” Bruno alisema na kumtupia swali huku tabasamu pana likiwa limemtapakaa usoni.

Inspekta Dilunga alimtazama kwa hasira yule mwandishi mdaku. Alibandika usoni miwani yake ya jua na kuondoka kuelekea ofisini kwa Dokta Nigel Smith bila ya kumjibu kitu. Bruno Mgimba alibaki akimtazama huku bado uso wake ukiwa na lile tabasamu lake pana.


Haikuwa mpaka saa moja kasoro robo za usiku ndipo Inspekta Dilunga alipopata fursa ya kuongea na Dokta Shabbir aliyekuwa amelazwa pale hospitali. Na ndipo alipopata habari zaidi kuhusu yule mtu aliyezusha kizaazaa kikubwa pale hospitalini siku ile.

Dokta Shabbir alimueleza kila kitu kwa ufasaha sana, na aliongezea taarifa ambayo Inspekta Dilunga hakuipata kutoka kwa Brian Koba. Alimuambia kuwa yule mtu baada ya kumpiga kwa kiganja chake kifuani na kumtupa hadi ukutani, alirudi na kuutazama ule mwili wa yule marehemu wa kike, kisha akaenda kuitazama ile miili mingine miwili iliyokuwa ndani ya kile chumba na kurudi tena kwenye ule mwili wa yule binti. Kisha akamuendea Dokta Shabbir pale alipokuwa ameangukia akigumia kwa uchungu na kukosa pumzi kwa lile pigo zito, na kumsukasuka kwa nguvu huku akimuuliza kwa hasira.

“Ni nani aliyefanya mambo haya, eenh? Ni nani…?”

Dokta Shabbir alibaki akiwa amekodoa macho kwa woga na mshangao, akilini mwake akijiuliza kwa nini yule mtu alikuwa akimuuliza swali lile wakati ni yeye ndiye aliyefanya yale mauaji…

“Na hapo Inspekta yule mtu alinishangaza kuliko kawaida…” Dokta Shabbir alisema katika maelezo yake.

“Kwa vipi…?”

“Akanijibu bwana…!” Alimuambia, lakini Dilunga hakuelewa, hivyo Dokta Shabbir akaendelea, “…yaani akanijibu swali ambalo bado lilikuwa kichwani mwangu Inspekta…kabla hata sijalitamka, akaniambia, “Nini…? Unadhani mimi ndiye niliyewaua hawa watoto? Bloody Fool! Sasa kwa nini tena nije hapa kukuuliza haya maswali…?”

“Hah…?” Dilunga alimaka, akikumbuka maelezo aliyopewa na Brian juu ya jinsi yule mtu alivyoweza kusoma mawazo yaliyokuwa yakipita kichwani mwake wakati alipokabiliana naye.

“Ndiyo Inspekta…ni bora nikusimulie tu hivi hivi, lakini kukutana na hali hiyo uso kwa uso kunatisha sana…niliishiwa nguvu.”

Inspekta Dilunga alikunja uso kwa mawazo.

“Sasa…ina maana huyu mtu naye anatafuta watu waliofanya uhalifu huu…?” Alisema kwa sauti ya kunong’ona, akijiwazia mwenyewe kwa sauti.

“Hivyo ndivyo ilivyonifunukia mimi Inspekta…” Dokta Shabbir aliingilia.

“Kwa nini…?” Dilunga aliendelea kujiwazia, safari hii Dokta Shabbir alibaki kimya, wazi kuwa hakuwa na jibu, na akijua kuwa ile ndiyo ilikuwa kazi ya Dilunga kuifanya, si kazi yake.

Baada ya kimya kifupi, Dilunga alimuuliza Dokta Shabbir iwapo kuna kitu kingine chochote anachoweza kukumbuka juu ya yule mtu.

“Ndio bwana…nakumbuka kitu kingine cha ajabu zaidi, pale Inspekta Brian alipoubamiza mlango wa kuingilia mle ndani tulimokuwamo na kushindwa kuuvunja…yule mtu aliniambia kwa sauti ya chini kuwa bado alikuwa na shida na mimi, na kwamba atanituliza kwa muda, kisha…kisha akaniwekea kidole chake cha shahada kwenye upande wa shingo yangu na nikahisi kupigwa na kitu kama shoti ya umeme hivi, ambayo bila shaka ilinilegeza nguvu kabisa!”

“Aaanh…?”

“Kabisa Inspekta…!” Dokta Shabbir alithibitisha kauli yake, na kuendelea, “…Inspekta Brian alipovamia mle ndani alinikuta nikiwa ninaning’inia tu kwenye kabali ya yule mtu…Lah, Inspekta, yule ni kiumbe hatari sana bwana…si mtu yule…sijui ni kitu gani, lakini kwenye utu hayuko kabisa…!”

E bwana we!

Inspekta Dilunga aliishiwa namna. Ni kitu gani hiki tunachopambana nacho hivi sasa lakini…?

“Unadhani unaweza kuikumbuka sura ya huyo mtu Dokta?” Hatimaye alimuuliza.

“Kabisa…siwezi kuisahau asilani…”

Nusu saa baadaye, Inspekta Dilunga alikuwa na mchoro ulioonesha wajihi wa mtu yule wa ajabu aliyeanzisha kimuhemuhe mle hospitalini asubuhi ya siku ile. Aliupata mchoro huu baada ya kuita wachoraji wa polisi walio mahiri katika kazi yao, ambao walichukua maelezo ya jinsi yule mtu alivyo kutoka kwa Dokta Shabbir na kwa Inspekta Brian Koba, na hatimaye kupata mchoro wa sura ya yule mtu.

Brian alipooneshwa mchoro ule aliafiki moja kwa moja kuwa yule hasa ndiye mtu aliyekabiliana naye mle ndani. Na Dokta Shabbir naye halikadhalika aliafiki kuwa wale wachoraji wa polisi walikuwa wamemtoa yule mtu kama jinsi alivyomuelezea.

Inspekta Dilunga aliutazama mchoro wa sura ya yule mtu wa ajabu kwa muda mrefu, na alipokuwa akiitazama, aliona mshabihiano wa wazi na yule mtu aliyekutana naye kwenye lango kuu la kuingilia ndani ya hospitali ile. Mtu aliyekuwa akipiga kelele za moto…moto…

Ghadhabu zilimpanda.

“Okay wewe mtu…sasa tumeshapata sura yako, bado jina lako na kukutia mbaroni tu…” Alijisemea peke yake akiwa ameketi nyuma ya meza yake, ofisini kwake.

Watu watano walikuwa wamekamatwa katika msako wa yule mtu kutokana na maagizo yake ya asubuhi ile. Alipoenda kuwatazama, hakukuwa na hata mmoja kati ya watano wale aliyefanana japo kidogo tu na sura ile iliyochorwa kutokana na maelezo ya Dokta Shabbir na Inspekta Brian Koba. Siku iliisha bila ya kuwa na mafanikio yoyote. Jadu Mfaume bado alikuwa huru akiendelea na msako wake, na akijua fika kuwa sasa na yeye alikuwa akisakwa na polisi…


Asubuhi ya siku iliyofuata gazeti la Ngurumo lilisheheni habari za jinsi mtu mmoja asiyejulikana alivyozusha tafrani ndani ya jengo la Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, na kisha kufanikiwa “kirahisi mno” kuwatoroka polisi waliokuwa wamezatiti ulinzi pale hospitali “kuzuia waandishi wa habari wasiingie kupata ukweli wa kilichokuwa kikiendelea”, na wakati huo huo akiacha polisi mmoja na tabibu mmoja muhimu sana pale hospitali wakiwa mahututi kwa kipigo.

Inspekta Dilunga aliingia wodini alimolazwa Inspekta Brian Koba akiwa amefura kwa hasira, macho yake madogo yakionekana madogo zaidi, na weusi wake ukiwa umekoza mara dufu. Brian Koba alimtazama kwa macho ya kuuliza akiwa amelala kitandani kwake. Dilunga alimtupia lile gazeti huku akimwambia kwa hasira.

“Hebu tazama upuuzi wa Bruno Mgimba…Pumbavu!”

Brian Koba alimtazma kwa mshangao, kisha akaliinua lile gazeti kwa mkono wake uliobaki huru na kuanza kusoma ile habari. Inspekta Dilunga alikuwa akitembea huku na huko mle ndani huku akimumng’unya midomo yake kwa hasira, akisubiri Brian amalize kusoma habari ile ikerayo.

“Khah! Sasa hii si sawa na kutukashifu tu…?” Brian alisema huku akiwa amekunja uso kwa mshangao na kutoamini.

“Sio kama…ni kwamba katukashifu kweli kweli! Ye’ anadhani haya mambo yote ni masikhara eenh?” Dilunga alisema kwa hasira na kuishia kusonya. Muda huo nesi mmoja aliingia mle ndani na kumuarifu kuwa alikuwa anahitajika kwenye simu iliyokuwa ofisini kwa Dokta Shabbir. Alitoka kwa hasira mle ndani kuelekea ofisini kwa Shabbir. Huku nyuma, Inspekta Brian Koba alibaki akiwa amelishika lile gazeti huku uso wake ukiwa na mawazo mazito…


“Ni upuuzi gani huu niusomao kwenye hili gazeti asubuhi hii Inspekta?” Tib Haggard alifoka kwenye simu. Dilunga alibaki ameduwaa.

“Khah….sasa unaniuliza mimi Super?”

“Wewe si ndio niliyekukabidhi hii kesi huko Kisarawe?”

Inspekta Dilunga akamuelezea kwa kirefu mambo aliyoelezwa na Brian na yale aliyoelezwa na Dokta Shabbir, hususan juu ya uajabu wa yule mtu.

“Mnh! Hii ni nini sasa Inspekta…inakuwa kama Science Fiction…?” Tib Haggard alisema, akifananisha matukio yale na kisa cha kubuni cha kisayansi.

“Tatizo ni kwamba kinatokea kweli afande…na unaweza kuona ni kwa nini hatuwezi kutoa taarifa kama hizi kwenye vyombo vya habari, kwani sisi wenyewe hatuna ufafanuzi sahihi juu ya kinachotokea…”

“Ni kweli…lakini sasa kadiri hii kesi inavyozidi kuchelewa kutatuliwa ndivyo wapuuzi-puuzi kama hawa wanavyozidi kupata muda wa kuandika ujinga dhidi ya jeshi la polisi….au ndio maana ya kupata uhuru hii…?”

Inspekt Dilunga aliuma meno kwa hasira na akabaki kimya, akiubinya kwa nguvu mkono wa ile simu aliyoibandika sikioni kwake.

“Anyway…tuache hilo, nipe mikakati yako kwa sasa, ni nini kinachofuata, na iwapo unahitaji askari zaidi…” Hatimaye Tib Haggard alimuuliza.

“Kwa sasa mkakati uliopo ni kumsaka yule mtu aliyezusha hii tafrani inayotutukanisha kwenye magazeti, na kwa hilo nitahitaji msaada wote utakaoweza kupatikana…mkakati wa pili ni kusubiri matokeo ya uchunguzi wa kijana Chambuso Mwagala na baba wa yule binti aliyeuawa, iwapo wataweza kuongea na kutuelezea kilichowatokea hata wakawa vile. Na wakati tunaendelea na msako wa huyu mtu, ambaye kwa sasa tutamwita John Smith mpaka hapo jina lake halisi litakapojulikana, nashauri lile jopo la matabibu liendelee na uchunguzi wa ile miili ili tuone kama kutakuwa na matokeo yoyote tofauti…” Inspekta Dilunga alijibu kwa kirefu.

“Okay…Good. Nitaangalia nitaweza kuongeza askari wangapi katika huo msako wa huyo John Smith…kuna utambulisho wowote juu ya kumtambua mtu huyo?”

Inspekta Dilunga alimueleza juu ya ule mchoro wa sura ya mtu wamtafutaye.

“Good…Good…lakini nadhani kabla hiyo picha haijatangazwa hadharani, ingebaki kwa askari wetu tu kwanza na kuendesha msako wa chini kwa chini, kwani naamini huyo mtu…John Smith…atakuwa akiamini kuwa polisi haina sura yake, na asiposikia lolote kuhusu kutafutwa kwake, atafanya kosa jingine tu na tutamtia mbaroni…” Tib Haggard alitoa hoja.

“Nakubaliana nawe afande…”

“Okay, nitakutaarifu juu ya ujio wa jopo la matabibu kwa ajili ya uchunguzi wa hiyo miili…”

Inspekta Dilunga aliafiki na kukata simu. Alienda moja kwa moja hadi ofisini kwa Dokta Nigel Smith na kutaka kujua hali za Chambuso Mwagala na Mzee Malambi.

“Hali si nzuri na si mbaya…” Dokta Nigel alimjibu, na Inspekta Dilunga akamtupia swali hapo hapo.

“Sasa hiyo ndiyo hali gani…?”

“Mzee Malambi ameamka na ana fahamu nzuri tu sasa. Anafahamu jina lake na anajua kuwa yuko hospitali na pia anajua kuwa ana mke na wana binti aitwaye Huba…”

“Oooh, habari nzuri sana hiyo!”

“Lakini…”

“Lakini nini tena…?”

“…hana kumbukumbu yoyote ya mambo yaliyomtokea hata akajikuta akiwa katika ile hali ya kushangaza hapo awali, na hatimaye kuwepo kwake hapa hospitali. Kwa mujibu wa kumbukumbu yake, bintiye Huba bado yu hai, na anatarajia kufunga ndoa karibuni…”

“Hah, sasa…Dah!” Dilunga alichanganyikiwa.

“Ataendelea kupata tiba maalumu kwa muda, lakini kwa upande wako hatakuwa na msaada wowote…angalau kwa muda mrefu ujao.”

“Kwa hiyo ndio basi tena? Kumbukumbu haiwezi kumrudia kabisa?”

“Hakuna garantii Inspekta. Inaweza ikarudi kesho, au ikarudi mwaka kesho…au isirudi kabisa. Vyovyote iwavyo, sidhani kama utataka kukaa na kusubiri tu mpaka hiyo kumbukumbu irudi ndio uendelee na kazi yako Dilunga.” Nigel alimjibu kwa kirefu. Dilunga aliona ukweli wa maneno yale. “Oh…Oh…na…vipi kuhusu Chambuso Mwagala?” Dilunga aliuliza, tayari akiwa amekata tamaa.

“Chambuso Mwagala….” Dokta Nigel alisema taratibu huku akionekana kujishauri aseme nini juu ya Chambuso, kisha akaguna na kutikisa kichwa.

“Niambie Dokta, ni nini?” Inspekta Dilunga aliuliza kwa wahka.

Dokta Nigel alimtazama kwa muda, kisha akamuambia, “Nadhani ni bora uje ujionee mwenyewe Inspekta…”

Waliongozana hadi kwenye chumba alichohamishiwa Chambuso huku Dilunga akichemkwa akili.

Chambuso alikuwa ameketi kitandani akiwa ameegemeza mgongo wake kwenye vyuma vya kitanda kile na miguu yake akiwa ameikunja mbele yake na kuikunyata pamoja kwa mikono yake, kidevu chake akiwa amekiegesha juu ya magoti yake yaliyoinuliwa mbele yake. Alikuwa amekodoa macho yaliyokuwa yakitiririkwa machozi mfululizo. Inspekta Dilunga aliguna kwa mshangao na kumsogelea karibu yule kijana.

“Amekuwa katika hali hiyo tangu alfajiri hii…” Dokta Nigel alimwambia, na Dilunga aliguna tena kwa mshangao.

“Ati…?”

Alimtazama yule kijana kwa makini huku akimuita jina lake, lakini Chambuso hakumuitika wala kumtazama. Dilunga alimgeukia Dokta Nigel.

“Sasa hii ndio nini…analia nini huyu sasa?”

Dokta Nigel alimtazama yule askari kwa macho yaliyohamanika.

“Hatujui Inspekta! Yaani amekuwa hivyo tangu alfjiri hii, na kib…”

“Na yeye pia hana kumbukumbu yoyote ya yaliyotokea huko nyuma kama Mzee Malambi?” Dilunga alimkatisha, mishipa ya kichwa ikimpiga na akiwa makini sana.

“Hapana…”

“Hapana…? Kwa hiyo anakumbuka…?” Dilunga aliuliza kwa kiherehere huku akimtupia macho yule kijana na kuyarudisha tena kwa Dokta Nigel, ambaye aliguna kabla ya kuongea.

“Vipimo vya hali yake vinaonesha kuwa huyu mtu ana kumbukumbu fulani kichwani mwake ambayo imejificha…yaani ipo, naye nadhani hajajifahamu kuwa ni Chambuso Mwagala, ila amepata athari katika mfumo wake wa fahamu au akili kwa ujumla, na huenda asiwe kama alivyokuwa hapo awali…”

“Hujaniambia kutu Dokta…ana kumbukumbu kichwani mwake au hana..?” “Kumbukumbu anayo…ila akili yake imeathirika, hivyo hakuna garantii kuwa kilicho kichwani mwake kinaweza kutoka kama jinsi kilivyo, au kitatoka kikiwa kimevurugwa na athari iliyokuwa akilini mwake…huyu kijana ameona, au amefanya, au amefanyiwa…vitu vibaya sana. Vitu ambavyo mimi naona zaidi ni hizi mila zenu waafrika au kitu kama hicho…”

Inspekta Dilunga alipagawa.

“Sasa una maana gani kuwa ana kumbukumbu wakati huo huo akili yake imeathirika…?”

Dokta Nigel alimtazama kwa muda, kisha akamjibu taratibu. “Ndio hivyo nikwambiavyo…uchunguzi wetu uko wazi kabisa juu ya athari katika akili ya huyu kijana, na ama katika kumbukumbu zilizokuwa kichwani mwake, matokeo ya vipimo yanaonesha kitu kiitwacho kitaalam kama pseudo–amnesiac syndrome…hii ni hali ya mtu kuwa kwenye hali ya kukaribia kupoteza kumbukumbu, lakini bado amebaki na sehemu ya kumbukumbu zake za zamani…”

“Nazitaka hizo kumbukumbu zilizobaki Dokta! Lazima ufanye namna ya sisi kuweza kujua anachoweza kukumbuka kuhusu tukio la yale mauji ya kutisha…” Inspekta Dilunga alidakia kwa wahka, na Dokta Nigel akatikisa kichwa kumfahamisha kuwa hilo lilikuwa haliwezekani.

“Huyu kijana hajaongea neno hata moja Inspekta, tumejaribu kila namna ya kumsemesha lakini wapi! Kwa hiyo lolote lililo kichwani mwake hatuwezi kulijua mpaka yeye afungue mdomo na aongee…”

Dilunga alipigiza upande wa ngumi yake kwenye chuma la kitanda kile na kulaani hali ile.

“Shiit, Dokta Nigel! Hunisaidii asilani!” Alilalamika.

“Sio kosa langu Inspekta, lakini pia kuna hii nilitaka uione…” Dokta Nigel alisema na kumkabidhi karatasi iliyoonekana kuwa ilikuwa imekunjwa kunjwa ovyo kabla ya kunyooshwa na kuwekwa sawa.

Inspekta aliipokea ile karatasi na kuitazama.

“Ish..Hii…Vipi Dokta, im…imetoka wapi?” Alimuuliza kwa wahka, akiwa amemkamata ukosi wa koti lake jeupe la utabibu, kiherehere kikiwa kimemjaa pasina kiwango. Dokta Nigel aliutoa mkono wa Dilunga kwenye koti lake taratibu, kisha akamwambia, “Imetoka kwa Chambuso Mwagala.”

“WHAAAAAT…?” Inspekta Dilunga alimaka huku akitutumua macho mara dufu na kuikodoea tena macho ile karatasi, akamgeukia Chambuso Mwagala, akairudia tena ile katatasi iliyokuwa mikononi mwake, na alihisi moyo ukimyong’onyea pale alipoona mikono yake ikimtetemeka kwa nguvu.

Aliikamata kwa nguvu ile karatasi ili isimtoke, alipepesa macho na kuitazama tena kile kilichokuwa kwenye ile karatasi.

Alikuwa akilitazama tena lile jereha la ajabu lililokuwa kifuani kwa hayati Huba binti Malambi…likiwa limechorwa kwenye ile karatasi iliyokuwa mkononi mwake!

Kwa muda mrefu Dilunga alibaki akiutazama ule mchoro uliomkumbusha moja kwa moja lile jeraha la ajabu lililokuwa kifuani kwa hayati Huba binti Malambi. Ingawa haukuwa fasaha kama jinsi ulivyokuwa ule aliouona kifuani kwa yule marehemu wa kike, haikuwa na shaka kabisa kuwa kilichokuwa kwenye ile katatasi kilikuwa ni taswira halisi ya lile jeraha la ajabu. Kwa jinsi mchoro ule ulivyokuwa ukionekana kwenye karatasi ile, alipata hisia kuwa mkono uliokuwa ukiuchora mchoro ule ulikuwa ukitetemeka vibaya sana.

“Un…una maana gani kuwa umetoka kwa Chambuso Mwagala…?” Hatimaye alipata akili ya kumuuliza yule tabibu wa kiingereza ambaye muda wote alikuwa akimtazama kwa makini.

“Ni ajabu sana Inspekta…hili jambo limetokea leo asubuhi wakati mmoja wa manesi wangu alipokuwa akimpima msukumo wake wa damu. Baada ya yule nesi kumpima, alianza kuandika vipimo alivyosoma kutoka kwenye msukumo wake wa damu kwenye karatasi iliyokuwa kwenye faili alilokuwa nalo, ndipo ghafla sana Chambuso alipokurupuka na kumpora lile faili…”

“Eeeeh?”

“Ndio…nesi aliruka kwa mshtuko na kalamu ikamtoka. Na kwa mshangao mkubwa alimuona Chambuso akiiokota ile kalamu na kuanza kuchora-chora haraka na kwa kitetemeshi kikubwa kwenye hiyo karatasi iliyokuwa ndani ya lile faili, kisha akalitupa sakafuni na kubaki akiwa anabubujikwa na machozi huku amejikunyata kama hivyo unavyomwona…” Dokata Nigel alimueleza Makubwa!

“Kwa hiyo…Chambuso ndiye aliyechora huu mchoro…?”

“Ndivyo nikwambiavyo Inspekta…”

“Na hajasema lolote baada ya hapo?”

“Hata neno moja…!”

“Na mlijaribu kumfanya aongee mkashindwa?”

“Yes Sir…kijana kapiga kimya moja kwa moja!”

“Sasa…sasa mbona mambo kama haya yanatokea na sipewi taarifa mara moja?” Dilunga alilalama.

“Mara kilipotokea kitendo hiki nilipiga simu ofisini kwako, nikaambiwa umeshatoka kuelekea huku…”

“Sasa mbona nilipofika hapa hukuniambia mara moja?”

“Umeingia hapa na maswali mfululizo Dilunga…hukutoa muda wa kuelezwa kitu ambacho hukuuliza…” Dokta Nigel alizidi kujitetea.

Inspekta Dilunga alimgeukia Chambuso na kumtazama kwa macho makali.

“Basi anajua huyu! Anajua kila kilichotokea…na bila shaka ni yeye ndiye aliyefanya mauaji yale…ndiye aliyemfanyia kitendo kile kibaya yule binti!” Dilunga alisema kwa jazba huku akimsogelea Chambuso pale kitandani na kuanza kumsuka-suka kwa nguvu huku akimkemea.

“Unajua nini kuhusu huu mchoro wewe, eenh? Unajua nini juu ya…”

Chambuso hakuwa akionesha kushitushwa wala kujali hali ile, alibaki vile vile alivyokuwa ameketi hapo awali, akikodoa macho yake mbele.

“Inspekta!” Dokta Nigel alimwita kwa ukali huku akimvuta kutoka pale kwa yule kijana.

“Hii sio namna ya kumfanya mgonjwa wangu hata kidogo!” Alimkemea kwa hasira.

“Hilo kwangu si tatizo…kama huyu ndiye muuaji wangu ni lazima nim…”

“Hawezi kuwa muuaji wako huyu Inspekta! Kumbuka kuwa jeraha lililokuwa kifuani kwa yule binti limetokea ndani ya mwili wake na si nje…sasa huyu kijana aliwezaje kuingia ndani ya mwili wa yule dada na kulichora, na kisha akatoka tena nje? Hebu tuliza jazba bwana!” Mzungu alimjia juu. Dilunga alitupa mikono yake hewani kwa kuchanganyikiwa na kutazama pembeni kwa hasira akiwa amejishika kiuno.

“Na sasa nakuomba unipishe niendelee kutafuta namna ya kumfanya huyu kijana aongee, na nasema nijaribu, kwani njia zote nilitumia mpaka sasa hazijazaa matunda!” Dokta Nigel aliongezea huku akimsukuma pembeni yule Inspekta mwenye jazba.

Inspekta Dilunga alimtazama yule tabibu kwa muda, na akaona kuwa maneno yake yalikuwa na ukweli.

“Okay Dokta…sawa. Nitarudi baadaye…” Alisema na kutoka nje ya chumba kile kwa mwendo wa haraka, ile karatasi iliyochorwa na Chambuso Mwagala ikiwa mkononi mwake.


Siku tatu baadaye Brian Koba alikuwa wima na tayari kurudi kazini, na Chambuso Mwagala hakuwa ametamka lolote. Hali yake ilibadilika kutoka kuwa ya kukatisha tamaa na kutia moyo kidogo, ingawa tayari ilishathibitika kuwa atakuwa na athari ya akili. Msako wa siri wa kumsaka Jadu Mfaume, au John Smith kama jinsi akina Brian walivyombatiza, bado haukuwa umezaa matunda yoyote.

Jopo la matibabu lilikuwa limefanikiwa kufanya kazi yake na kutoa ripoti ya mauaji ya barabara ya Kazimzumbwi, na ripoti yao ilikuwa ikithibitisha tu kile kilichobainishwa na uchunguzi wa Dokta Nigel Smith na Dokta Shabbir.

Inspekta Dilunga alikuwa ofisini kwake akiikodolea macho ile ripoti ya jopo la matibabu asubuhi ya ile siku ya tatu baada ya kile kituko cha Chambuso, akili ikimzunguka wakati Brian Koba alipoingia mle ofisini akiwa amevalia mavazi yake ya kiaskari.

“Heh…u”shapona wewe?” Dilunga alimuuliza kwa mshangao.

“Niko tayari kuimaliza hii kesi sasa Inspekta…naomba twende tukamuone Chambuso.” Brian Koba alimwambia huku akimsogelea pale mezani kwa mwendo wa kuchechemea kidogo. Inspekta Dilunga alishamuelezea juu ya kile kituko cha mwisho cha Chambuso, na Brian alikuwa na hamu sana ya kujaribu kumhoji yule kijana.

“Una hakika na hali yako Brian?” Alimuuliza.

“Sio mbaya kiasi cha kuendelea kuniweka kitandani…nahitaji kuonana na Chambuso.”

Wale askari wawili waliingia hadi kwenye wodi aliyowekwa Chambuso Mwagala na kumkuta akiwa amejikunyata kwenye kona ya kitanda chake, macho yake akiwa ameyatuliza kwenye kona moja ya dari la wodi ile.

“Chambuso…” Brian alimwita, na yule kijana aliendelea tu kutazama alipokuwa akitazama pasina kujali uwepo wa wale askari wawili mle ndani. Brian aliikunjua ile karatasi iliyokuwa na ule mchoro wa ajabu na kumuwekea mbele ya uso wake.

“Unaukumbuka huu mchoro Chambuso…?” Alimuuliza taratibu huku akimtazama usoni. Chambuso alizungusha jicho lake na kuutazama kidogo ule mchoro, kisha akarudia kutazama tena kule alipokuwa akiangalia hapo awali bila kujibu kitu.

“Wale askari walitazamana, na Brian alimtikisa kidogo yule kijana kabla ya kumuuliza tena, lakini Chambuso hakujibu wala kumtazama tena. Brian alijaribu kila namna lakini ilikuwa ni sawa na kulisemesha gogo.

Inspekta Dilunga aliishiwa subira. Alimkamata mabega yule kijana na kumtikisa kwa nguvu.

“Hebu ongea na sisi we’ mtoto…kwa nini unajitia hujui wakati unaj…” Alianza kumkemea kwa hasira, lakini kabla hajamaliza Chambuso aliwashangaza wote wawili.

Kwa wepesi usitarajiwa alirusha mikono yake na kuipangua kwa nguvu mikono ya yule askari iliyomshika mabega, na hapo hapo akamdaka koo yule askari kwa mkono wake mmoja huku akimtazama moja kwa moja usoni kwa macho yaliyojaa ghadhabu.

“Hey…! Heeeeeey…!” Brian alipiga kelele wakati Dilunga akikukuruka kujinasua kutoka kwenye kabali ile bila mafanikio. Chambuso alikuwa amembana koo kwa nguvu sana naye hakuweza kujinasua kabisa. Pumzi zilimbana na macho yalimtoka pima.

Brian Koba alimrukia Chambuso pale kitandani na kujaribu kumuokoa mwenzake, lakini ilikuwa ni kama anayejaribu kumnasua kutoka kwenye mkono wa chuma.

“Neeees… Nesiiiii…!” Brian aliita kwa nguvu, na muda huo manesi wawili waliingia mbio mle ndani na walipoona kile kituko wakatoka mbio tena kurudi walipotoka na waliporudi walikuja mbio na Dokta Nigel nyuma yao, wakiwa na sindano tayari kumdunga yule kijana.

“What the…?” Dokta Nigel aliropoka alipoona ile hali. Inspekta Dilunga alikuwa ametumbua macho pima, mishipa ya kichwa ikiwa imemtutumka vibaya sana, huku Chambuso akiwa amemkodolea macho yaliyodhamiria kuua.

“Mtoeni hapo Dokta…Upesi…! Atamuua…” Brian alisema kwa jazba. Haraka wale manesi waliiandaa ile sindano kumchoma Chambuso lakini hapo hapo Chambuso alimsukuma kwa nguvu yule askari na kumwacha akigaagaa sakafuni naye akawageukia wale manesi kwa macho yaliyojaa wazimu.

Manesi waligwaya.

“Chambuso…tulia baba. Hakuna haja ya kuwa mkali, okay? Dokta Nigel alimsemesha kwa upole.

Taratibu Chambuso alimgeukia yule tabibu na kumtazama kwa muda, kisha akajiegemeza pale kitandani na kurudia kutazama pale juu ya dari kama kwamba hakuna kitu chochote cha ajau kilichotokea mle ndani.

Brian Koba alimuinua Dilunga kutoka pale sakafuni na kumsaidia kusimama. Dilunga alibaki akikohoa kwa taabu huku macho yamemwiva, na kumtupia macho yule kijana kwa taharuki kuu.

“He is crazy alright…ana wazimu kabisa huyu sasa…” Alisema kwa sauti iliyotaharuki.

“Mmemfanya nini huyu nyinyi, eeenh….” Dokta Nigel aliwauliza wale askari kwa ukali.

“Tulikuwa tukijaribu kumuuliza maswali tu Dokta…” Brian alijibu.

“Mimi najua uulizaji wa Dilunga, na hiyo ndiyo hasara yake…huyu kijana hakuwa mkorofi hata kidogo!” Nigel alisema kwa jazba.

Wale askari walianza kutoka mle ndani taratibu, Inspekta Dilunga akijishika koo huku akikohoa kidogo kidogo.

“Inspekta…”

Wote walisimama hatua chache kabla ya kuufikia mlango, na kugeuka taratibu kuelekea kule sauti ilipotokea, wote wakiwa na hakika kabisa kuwa ilikuwa ni sauti ya Chambuso Mwagala.

Walimtazama yule kijana aliyeita kwa sauti ya chini, wale manesi na Dokta Nigel wakiwa wamepigwa na butwaa. Chambuso Mwagala alimtazama Inspekta Dilunga kwa muda mrefu, kisha akasema tena kwa sauti ile ile ya chini, lakini iliyosikika na kila aliyekuwemo mle wodini, kauli yake akiielekeza kwa Inspekta Dilunga.

“Amesema niwaambie kuwa sio yeye…”

“What…?” Dilunga aliuliza kwa mshangao na kutoamini.

“Na…nani amesema kuwa…” Brian alianza kuuliza, lakini Chambuso aliwashangaza tena kwa kujibu.

“Huba…sio…yeye…”

Walibaki wakiwa wamepigwa na butwaa kwa muda, na Inspekta Brian Koba ndiye alikuwa wa kwanza kuzinduka kutoka katika mshituko ule wa mwaka. Alimkimbilia Chambuso pale alipokuwa na kumuuliza kwa macho yaliyojaa umakini na upole ili kutomtia hofu yule kijana.

“Huba…? Huba amekutuma utuambie kuwa sio yeye? Kwa nini Chambuso, kwa nini…ni nini kingine alichosema Chambuso?”

Chambuso alimtazama yule Inspekta kwa macho yaliyojaa wazimu, tena kwa muda mrefu, bila ya kumjibu.

“Ana maana gani…mbona inakuwa kama…” Inspekta Dilunga aliuliza kwa mshangao. Brian Koba akamkatisha kwa kiherehere. “Inakuwa kama anamaanisha kuwa Huba siye aliyefanya mauaji yale…!”

“Hah…sasa ina…inawezekana vipi hii? Amejuaje haya…au ndio wazimu?” Inspekta Dilunga aliuliza kwa wahka.

“Mmmn-mmnh, huu sio wazimu huu…lakini haileti maana hata kidogo! Hii ni ajabu kubwa…” Brian alisema kwa kuchanganyikiwa.

Wote walitazamana, na kuishia kutikisa vichwa kwa kuchanganyikiwa.

“Jamani hakika huu ni utata…!” Dilunga alisema kwa kukata tamaa kukubwa kabisa.

Brian Koba alimtazama mwenzake, na kumgeukia tena Chambuso, ambaye alikuwa ameketi pale kitandani akimkodolea macho nzi aliyekuwa ametua kwenye chuma la kile kitanda.

“Chambuso…umesema…Huba kakutuma utuambie kuwa sio yeye…?” Alimuuliza, kisha akaendelea, “…ni nani sasa kama sio Huba…na sio yeye kwenye nini?”

Chambuso alibaki vile vile alivyokuwa, sasa akili yake, kama ilikuwa ni akili, ilikuwa imehamia kwa yule nzi. Dokta Nigel alisogea pale kando ya kitanda na kumtazama Chambuso kwa makini.

“What…unaweza kutuelezea zaidi juu ya Huba, Chambuso…?” Dokta Nigel alidakia na kumuuliza yule kijana. Chambuso alihamishia macho yake kwa Dokta Nigel, na muda huo macho yake yalionekana kama kwamba hakuwa akielewa ni nini kilichokuwa kikiongelewa na yule tabibu, kisha midomo ikaanza kumtetemeka.

“Chambuso…” Brian alianza kumuita tena, lakini Dokta Nigel alimuashiria kuwa anyamaze. Brian alinyamaza na kumgeukia yule tabibu, na kuona kuwa yule tabibu alikuwa akimtazama Chambuso kwa makini sana, naye akamgeukia Chambuso.

Sasa Chambuso alikuwa amekaza macho mbele, machozi yakimbubujika ilhali uso wake ukionesha hofu kubwa sana, midomo ikimtetemeka hadi meno yake yakisikika yakigongana kinywani mwake. Kama kuna kitu kilikuwa kikipita kichwani mwa yule kijana wakati ule, hakika kitu kile kilikuwa ni cha kutisha sana.

Wote waliokuwamo mle ndani walibaki wakimtazama yule kijana kwa mshangao na maswali mengi vichwani.

“Nadhani itabidi tumuache apumzike…” Hatimaye Dokta Nigel alisema, na kumgeukia mmoja wale manesi wake, “…hebu leteni ile sindano tumchome apumzike.”

Yule nesi alianza kutekeleza.

“Hapana! Ngoja kwanza…” Inspekta Brian aliropoka, na wote walimgeukia.

“Nini Inspekta…” Dokta Nigel aliuliza, na bila ya kumjibu, Inspekta Brian Koba aliiendea meza iliyokuwa kwenye kona ya wodi ile ndogo na kuchukua faili lililokuwa juu yake. Haraka alichomoa karatasi kutoka kwenye lile faili na kumsogelea Chambuso huku akichomoa kalamu kutoka kwenye mfuko wa shati lake.

Alimpa yule kijana ile karatasi na kalamu.

Chambuso aliendelea kubaki katika hali ile ile, wakati Brian akiwa amemnyooshea mkono wenye ile karatasi na kalamu.

“Unafanya nini…?” Dokta Nigel aliuliza.

“Muache…anajua anachofanya…” Inspekta Dilunga alisema kwa sauti ya kunong’ona huku akitazama kwa makini kilichokuwa kikiendelea pale. Hatimaye Brian aliviweka kitandani vile vitu alivyokuwa akijaribu kumpa Chambuso, karibu sana na alipokuwa ameketi. Alimpiga-piga begani kwa namna ya kumuaga, kisha bila ya kusema neno, alitoka mle ndani, akifuatiwa na Inspekta Dilunga ambaye baada ya ile kabali kali aliyokuwa amekabwa na Chambuso muda mfupi uliopita, alikuwa na hamu sana ya kutoka nje ya chumba kile…


Siku ile ile, idhini ilitolewa kwa ndugu wa wale marehemu waliouawa kwenye kituko kile cha barabara ya Kazimzumbwi kuchukua miili ya wapendwa wao na kwenda kuzika. Miili ya marehemu Uwesu Shaame na Esmund Bwaira ilichukuliwa na jamaa zao kwa ajili ya maziko.

Kiasi cha saa mbili baada ya kutoka pale hospitali, wale askari wawili walikuwa ofisini kwa Inspekta Dilunga wakiitathmini hali iliyotokea kule hospitali.

“Una mawazo gani juu ya hali ile Inspekta?” Brian alimuliza Dilunga.

“Kijana anajua mambo, ila akili yake si murua, si umeona jinsi alivyonikaba pale? Angeweza kuniua yule…!”

“Nakubaliana na wewe…lakini…kama alikuwa anamaanisha kwamba Huba siye aliyefanya yale mauaji kama uchunguzi wa kitaalamu unavyoonesha, ni nani basi?” Brian alijibu na kuuliza.

“Na sio tu kwamba kasema kuwa siye Huba, bali ni kwamba Huba ndiye aliyemtuma yeye, Chambuso Mwagala, atuambie sisi kuwa muuaji si Huba…unaona mchanganyiko wa habari huu lakini?” Dilunga alisema kwa hamaniko.

“Duh, ila hapa kweli kuna utata afande…tena utata mzito…” Brian aliafiki uzito wa kazi iliyokuwa mikononi mwao.

“Sasa bwana mdogo bado una mawazo ya kuitatua hii kesi?” Dilunga alimuuliza yule askari kutoka mjini huku akijipapasa koo lake pale alipokabwa na Chambuso.

Brian alimtazama kwa muda huku uso wake ukionesha mawazo mengi, kisha akaguna kabla ya kumjibu, “Hii kesi ni ngumu mzee…lakini tutaitatua tu. Na ili tuitatue, ni lazima tumpate yule jamaa…John Smith…”

“Hudhani kuwa Chambuso anaweza kuwa na msaada kwetu tena?”

“Anaweza…lakini yuko very unpredictable…tunaloweza kulipata kutoka kwake, na likatuingia akilini, tutalichukua, vinginevyo sisi tucheze na John Smith tu kwa sasa, Chambuso iwe kama by the way tu”

“Sasa na John Smith ndio amekuwa kama ndoto tu…hakuna hata dalili…sijui kapotelea wapi! Vijana wanasaka kutwa kucha, patupu!”

Brian alikaa kimya kwa muda, kisha akasema.

“Unajua siku ile uliponiletea lile gazeti na kunionesha ile habari ya kashfa iliyoandikwa na Bruno Mgimba, nilipata muda wa kuwaza sana juu ya hali hii…”

“Na…?”

“Na…nadhani tunaweza kuwa na namna ya kukutana tena na John Smith, ila itabidi tuwe tumejiandaa vilivyo kabla ya kukutana naye tena.”

“Ni nini unachoongelea Brian, sikuelewi…”

“Nadhani itabidi tuonane na Bruno Mgimba…”

“Yule Shaitwani…? Kwa minajili gani? Mbona na wewe unataka kunichanganya?” Inspekta Dilunga alimaka, na kwa ufasaha wa hali ya juu, Inspekta Brian Koba akamuelewesha kilichokuwa kichwani mwake.


Asubuhi ya siku iliyofuata ilikuja na matukio makubwa mawili. Kwanza Bruno Mgimba aliandika kwa undani juu ya habari za Chambuso Mwagala, akiueleza umma wa watanganyika kwamba kuna shahidi mpya aliyejitokeza katika lile sakata la mauaji ya barabara ya kazimzumbwi. Aliandika kuwa baada ya kuwa kwenye hali ya kuduwaa mfululizo tangu siku alipokutwa kwenye eneo la maafa kando ya maiti waliouawa kwa namna ya kutisha kabisa, kijana Chambuso Mwagala alirejewa na fahamu zake na kuweza kutoa habari muhimu kwa jeshi la polisi, ambalo kama kawaida yake liliendelea kuficha ugunduzi ule kwa madai kuwa “eti uchunguzi bado haujakamilika.”

“Sasa wakati Chambuso Mwagala akipigania kurejesha fahamu zake ndani ya wodi namba mbili ya hospitali ile ya wilaya, na hatimaye akafanikiwa kutoa japo mwanga wa kuweza kuikoa jamii yetu na balaa jingine kama lile la kule Kazimzumbwi, jeshi letu adhimu la polisi bado linayaweka maisha ya wananchi wa Kisarawe kwenye mashaka kwa kukaa na taarifa muhimu kama hiyo kwa madai yao ya kawaida ya kukamilisha uchunguzi…” Habari ya Bruno Mgimba ilimalizia katika gazeti lile.

“The bastard has done it again…!” Inspekta Dilunga alijisemea peke yake akiwa na gazeti la Ngurumo ofisini kwake asubuhi ile, na mara simu yake iliita. Aliinyakua na kuikoromea.

“Inspekta Gezza Dilunga!”

“Inspekta…inabidi uje huku haraka!” Dokta Nigel aliongea kwa wahka kwenye ile simu.

“Nini tena Dokta…?”

“Ni Chambuso…” Dokta Nigel alimjibu na mara moja Dilunga alilitupa pembeni lile gazeti na kutimua mbio kuliendea gari lake. Alipofika pale hospitali alienda moja kwa moja hadi ofisini kwa Dokta Nigel, ambaye kwa mkono uliokuwa ukitetemeka, alimkabidhi karatasi ambayo Dilunga aliinyakua haraka na kuitazama, mguno mzito ulimtoka na macho yakimtumbuka.

Kwenye ile karatasi kulikuwa kumechorwa picha ya kiumbe wa ajabu na kutisha sana. Ilikuwa ni picha ya kiumbe chenye mwili mrefu na mwembamba, miguu, mikono na vidole vyake vyote vilikuwa virefu na vyembamba. Kichwa chake kikubwa chenye umbo la yai kilikuwa kimebebwa na shingo ndefu na nyembamba. Sehemu ambapo macho yalitakiwa yawepo kwenye kile kichwa kikubwa cha kile kiumbe cha ajabu, kulikuwa kumechorwa matobo mawili makubwa.

Inspekta Dilunga aliinua uso wake taratibu kumtazama yule tabibu.

“Un…una maana hii kachora Chambuso…?” Alimuuliza huku akihisi koo likimkauka.

“Tumemkuta akiwa amelala ilhali ameishikilia hiyo karatasi pamoja na ile kalamu aliyoachiwa na Brian pale jana…ni wazi kuwa ni yeye ndiye aliyechora hiyo picha…”

“Oh, My God…Brian alifikiria jambo la maana sana…” Dilunga aliwaza, kisha akamuuliza yule tabibu.

“Sasa hii ina maanisha nini Dokta?”

“Ni wazi kuwa akili yake inatema vile vitu ambavyo vimeacha athari kubwa kwake…na kwa mujibu wa mchoro huo, ni kwamba Chambuso alionana…au alikiona…hicho kiumbe. Na nadhani hicho kiumbe ndicho kilichohusika na vifo vile…”

“Whaaat…?”

“Yes…sasa ukitaka ushahidi wa kisayansi juu hilo sitakua nao, lakini ukitaka maoni yangu binafsi, na kumbuka kuwa mimi nimekuwa hapa duniani kwa muda mrefu kuliko wewe, basi hayo ndio maoni yangu, nini unafanya juu ya maoni yangu hayo ni juu yako mwenyewe.” Dokta Nigel alimjibu.

Huku akili ikimzunguka, Inspekta Dilunga alitoka mle ndani akiwa na ile karatasi mkononi mwake.

Hatua chache nje ya mlango wa ofisi ya Dokta Nigel alisimama ghafla, kisha akarudi kasi ndani ya ofisi ile.

“Dokta…kuna kitu unasahau…iweje huyu…” Alimtikisia ile karatasi iliyokuwa na mchoro wa kile kiumbe cha ajabu uliochorwa na Chambuso Mwagala, “…hiki…kiumbe, kiwe ndicho kilichofanya mauaji haya wakati tayari uchunguzi umeonesha kuwa ni Huba ndiye aliyewaua wale vijana.?” Alimuuliza yule tabibu, ambaye alimtazama kwa muda, kisha akamjibu taratibu.

“Inspekta, naona hii kesi itakutia wazimu…unakumbuka maneno ya Chambuso, kuwa Huba siye aliyeua? Halafu kumbuka na ule mchoro wa ajabu kifuani kwa yule binti…unadhani ni nani anayeweza kufanya kitu kama kile kama si kiumbe kama hicho…?”

Dilunga alimkodolea macho yule tabibu. “Ah, sasa…ina maana sasa unaupinga ugunduzi wako na wa jopo la matabibu kuwa ni Huba ndiye…” “Hapana! Kisayansi imeonesha hivyo, lakini kimazingira ambayo nadhani ndiyo yaliyoizunguka hii kesi yote, alichosema Chambuso huenda ndicho kikawa sahihi, ingawa hatuwezi kukithibitisha kisayansi…”

“Na iweje sasa Chambuso aweze kuchora vitu namna hii…? Sidhani kama alikuwa na fani ya uchoraji…na…”

“Aaaanh, sasa hii ni hali ambayo huwa inatokea kwa watu waliokumbwa na hali kama hii ya pseudo-amnesiac syndrome….kila mtu huwa anatokewa na namna ya kuelezea kumbukumbu zake, wengine huwa wanakuwa na uwezo wa kutabiri vitu vitakavyotokea, wengine huwa na uwezo wa kusikia vitu ambayo watu wengine hawavisikii…mradi kila mja huja na uwezo fulani ambao binadamu wengine hawana. Na hali kama hii hudumu kwa muda mfupi sana, kisha aidha wanapoteza kabisa kumbukumbu, au wanakuwa wehu moja kwa moja. Sasa kwa Chambuso hii ndio namna yake ya kuonesha vilivyokuwa kichwani mwake, hivyo si lazima iwe alikuwa na kipaji cha uchoraji tangu awali.” Nigel alifafanua kwa kirefu.

“Dah, hii sasa imekuwa too much…”

“Ndiyo, lakini ndivyo nionavyo mimi, hasa ukizingatia kuwa kisayansi tumeshindwa kabisa kuelewa ni katika mazingira gani ule mchoro wa ajabu ulifika au uliwekwa kifuani kwa yule binti…ukiongeza na ushahidi wa kisayansi kuwa hali ya Chambuso inatokana na kuona jambo la kutisha sana, nadhani hata mimi kama ningekutana uso kwa uso na kiumbe kama hicho, na mazingira yote yaliyofichika kwetu ambayo tunadhani Chambuso aliyaona, ningekuwa kama Chambuso hivi sasa…”

“Kwa hiyo unadhani kuwa haya anayotuchorea Chambuso si vitu vya wazimu wake tu…?”

“Inspekta, si umeona ule mchoro wa kwanza?”

“Ndiyo, lakini…”

“Sasa kuna sababu yoyote ya kuutilia mashaka huu mchoro aliokuja nao sasa? Hii ni namna ya Chambuso, na watu wote wanaokumbwa na hali kama yake, ya kuelezea kinachobaki akilini mwao, na mara nyingi hivyo huwa ndivyo vitu vilivyofyatua au kuharibu akili za watu kama hao…ningekuwa wewe ningetilia maanani sana kila kitu kinachotoka kwa Chambuso Mwagala sasa hivi, halafu ningetafuta namna yangu mwenyewe ya kuleta maana katika vitu hivyo…kumbuka kuwa mimi nimekuwa hapa duniani muda mrefu kuliko wewe Inspekta…” Dokta Nigel alimjibu huku akimtazama kwa macho yaliyomaanisha kuwa yeye alikuwa akijua mambo mengi kuhusiana na mazingira yale.

Inspekta Dilunga alimtazama kwa muda, kisha akatoka tena nje ya chumba kile bila ya kuongea neno zaidi, akili ikimzunguka maradufu.

Nje ya ofisi ya yule tabibu, Inspekta Dilunga alitembea taratibu kwenye korido ndefu ya hospitali ile, akiona kuwa kulikuwa kuna sura nyingi ngeni kati ya manesi na wahudumu wa hospitali ile, lakini hilo halikumshtua asilani. Saa yake ilimuambia kuwa muda ulikuwa ni saa mbili kasoro robo za asubuhi.

Nje ya mlango wa wodi namba mbili kulikuwa kuna askari wawili wakiweka ulinzi, na akili yake ikarudi kwa mwandishi Bruno Mgimba na makala yake ya asubuhi ile…


Kiasi cha saa tatu asubuhi, mhudumu mmoja mtu mzima alijisogeza taratibu kuelekea kwenye mlango wa wodi namba mbili, ambamo ndani yake Chambuso Mwagala alikuwa amelazwa. Alikuwa amevaa mavazi rasmi ya wahudumu wa hospitali ile na miguuni alikuwa amevaa viatu vya raba. Usoni alikuwa amevaa miwani pana ya macho iliyokuwa na lensi nzito, hali iliyoonesha kuwa macho yake yalikuwa mabovu sana. Yule mzee mwenye kibyongo alikuwa akitembea kwa taabu kidogo huku akisukuma toroli maalumu la vyakula kwa wagonjwa, likiwa na vinywaji kama uji na matunda kadhaa ilhali akiwa amejiegemeza kwenye lile toroli kama kwamba ndilo lililokuwa likimsaidia kutembea.

Wale askari waliokuwa nje ya wodi ile walimtazama kwa muda wakati akiusogelea mlango wa wodi ile, kisha wakageuza nyuso zao mbele, wakimuacha yule mhudumu mzee aendeleee na taratibu zake.

Mhudumu aliingia kwenye wodi moja kabla ya kuifikia ile wodi namba mbili, na dakika chache baadaye alitoka na kuielekea wodi namba mbili ambayo kando ya kila upande wa mlango wake kulikuwa kuna askari mwenye silaha.

“Assalaam Alaykhum mabwana.” Yule mhudumu alisalimia alipoufikia ule mlango, na wale askari walimtazama bila ya kujibu. Sauti yake ilikuwa ikitoka kwa kukauka-kauka, na ilikuwa kama kwamba alikuwa na kohozi lililomkwama kooni.

“Kuna nini hapo?” Mmoja wa wale askari alimuuliza huku akimtazama kwa makini, wakati yule mwingine akitazama kile kilichokuwa kwenye lile toroli lake.

“Staftahi tu kwa ajili ya mgonjwa humo ndani afande…” Mhudumu alijibu huku akijitahidi kusimama wima, na akionekana kupata maumivu fulani kwa kufanya hivyo.

Walitazamana uso kwa uso na yule askari, mhudumu akiwa amefinya uso kwa maumivu aliyokuwa akiyapata kwa kusimama wima. Alikuwa na sunzua kubwa chini ya jicho lake la kushoto, na hapo alianza kukohoa kwa nguvu, akiinamisha uso wake huku akijiziba mdomo wake kwa kiganja chake.

“Mzee kwa nini usistaafu kazi tu? Namna hii si utaweza hata kuambukiza wagonjwa magonjwa mengine…?” Yule askari alimuuliza, huku akimuashiria yule mwenzake kwa kichwa kuwa hakuwa na tatizo lolote.

“Maisha mwanangu, maisha…” Yule mhudumu alijibu kwa sauti yake ya kizee.

“Oke…endelea mzee.” Yule askari mwingine aliruhusu, na yule mzee akasukuma toroli lake kuingia ndani ya wodi ya Chambuso Mwagala.

Akiwa ndani ya ile wodi yule mzee alirudisha mlango taratibu na kutembeza macho yake mle ndani. Ilikuwa ni wodi ndogo, hatua chache mbele yake kulikuwa kuna kitanda ambacho juu yake alimuona yule mgonjwa aliyekuwa amemkusudia akiwa amejifunika mashuka pale kitandani na akiwa amelalia ubavu, mgongo wake ukiwa umeelekea kule mlangoni.

Taratibu yule mhudumu mtu mzima aligeuka na kuubana kwa komeo ule mlango kwa usiri mkubwa kiasi cha wale askari kule nje kutoweza kusikia, kisha kugeuka taratibu na kujinyoosha wima.

Aliiweka ile miwani iliyokuwa usoni kwake juu ya kile kitoroli cha kusukumia chakula na kuangaza kwa macho yake makali mle ndani.

Kwenye kona moja ya wodi ile kulikuwa kuna makabati maalumu ya kuhifadhia nguo na bila shaka dawa mbali mbali, na upande mwingine kulikuwa kuna mlango ulioelekea kwenye chumba kingine. Akiwa makini ghafla, na akitembea kikakamavu, ule u-goigoi wa hapo awali wote ukiwa umetoweka, yule mhudumu aliuendea ule mlango mwingine na kuufungua kwa tahadhari kubwa, kisha akachugnulia ndani yake.

Kilikuwa ni choo.

Alirudi haraka katikati ya chumba kile na kukisogelea kile kitanda, akili yake sasa ikiwa kwa yule mgonjwa aliyelala pale kitandani, ambaye asubuhi ile alisoma habari zake kwenye gazeti la Ngurumo.

Kwa mkupuo mmoja alizifunua zile shuka alizojigubika yule mgonjwa na kumgeuza chali kwa nguvu, akimtazama kwa macho yake makali.

“Tulia kama ulivyo John Smith…” Brian Koba alifoka huku akimnyooshea mtutu wa bastola yule mzee, na hapo uso ukambadilika alipoona sura tofauti na ile aliyoitarajia, na hapo hapo akaongezea, “…au yeyote awaye!”

E bwana we!

Jadu Mfaume alipigwa butwaa wakati alipojikuta uso kwa uso na yule askari aliyepambana naye mara ya mwisho alipotembelea ile hospitali na kuzusha tafrani ile ya moto wa uongo, akiwa amemuelekezea bastola moja kwa moja usoni.

Binadamu wamenihadaa…!

Alimtazama yule askari kwa ghadhabu kubwa, na ndipo Brian alipoona ule mng’ao wa ajabu kwenye yale macho yake, na akajua kuwa hakika alikuwa akikabiliana na John Smith, ingawa sura ilikuwa tofauti.

Kabla Jadu hajajua achukue hatua gani, alisikia vishindo vikitokea nyuma yake, na milango ya yale makabati yaliyokuwa upande mmoja wa chumba kile ikijibamiza kwa nguvu. Alianza kugeuka kutazama kilichokuwa kikitokea nyuma yake, lakini Inspekta Brian Koba aliruka kutoka pale kitandani alipokuwa amejilaza kama chambo, bastola ikiwa imara mkononi mwake na kumkemea kwa ukali.

“Uko chini ya ulinzi John Smith!”

“Tulia hapa hapo mhalifu! Umezingirwa na askari wenye silaha nzito!” Sauti nyingine kali ilimfokea Jadu Mfaume kutokea nyuma yake, ambapo askari wengine wanne waliokuwa wamejificha ndani ya yale makabati yaliyokuwa upande mmoja wa chumba kile walikuwa wametoka na wote walikuwa wamemuelekezea bunduki zao yule mtu wa ajabu.

Taratibu Jadu Mfaume aligeuka huku akirudi nyuma na kuwatazama wale askari waliomzingira. Wawili walikuwa wamemuelekezea bastola kama ile iliyokuwa mkononi kwa Brian Koba moja kwa moja kichwani kwake, na wawili walikuwa wamemuelekezea bunduki ndefu na kubwa zilizokuwa na vitu kama ncha za mikuki vilivyochomoza mbele. Hawa wawili waliokuwa na bunduki ndefu walikuwa wamepiga goti moja kila mmoja, na walikuwa wamemuelekezea bunduki zao kifuani kwake.

Kwa mkono wake wa kushoto, Inspekta Brian Koba alitoa kifaa maalumu cha mawasiliano, na kuongea.

“Inspekta Brian Koba anaripoti. John Smith mbaroni, narudia…John Smith mbaroni…over!”

Sauti ya mkoromo ilisikika kutoka kwenye ile redio maalumu, na kisha sauti ya Inspekta Dilunga ilisikika.

“Safi sana Inspekta…tumekupata vilivyo. Hakika mtego wako ulikuwa mzuri…tupe hali halisi, over!”

“Hali imedhibitiwa…kaeni tayari kwa kutoa msaada iwapo itahijika, over and out!” Brian Koba alimjibu huku bado akiwa amemkazia macho yule mtu wa ajabu aliyekuwa amemkamia kwa muda mrefu.

Jadu Mfaume alikuwa amepatikana.

Jadu Mfaume alikuwa amepatikana.

Alimtazama Brian kwa uso uliojaa ghadhabu na kumwambia, “Hivi mpaka sasa bado hujajifunza tu wewe kuwa mimi hamniwezi?”

“Shut Up weweee! Uko chini ya ulinzi…bastola iliyokuwa mkononi mwangu, na zilizokuwa mikononi mwa askari wawili walio nyuma yako, zimesheheni risasi maalumu ambazo zinalipuka pindi zikipiga mahali zilipokusudiwa…they explode on impact…! Kwa hiyo hata kama unajitia kuwa hudhuriki na risasi, ujue kuwa ikikupiga kichwani inalipuka na bichwa lako!”

Jadu Mfaume, alitikisa kichwa kusikitikia upotofu wa maneno ya yule askari.

“Na hivyo vyuma vinavyochomoza kutoka kwenye bunduki zilizokuwa mikononi mwa hao askari wengine wawili vina uwezo wa kuupenya mwili wako, na kubaki humo humo…vina nguvu hasi za umeme, na sasa kama mwili wako una umeme utakumbuna na nguvu hasi za hivyo vyuma na matokeo yake ni kwamba vitapiga shoti ya umeme…ndani ya mwili wako! Sasa sidhani kama nina haja ya kukueleza ni nini kitakachotokea baada ya hapo…!” Brian alizidi kumpa habari mbaya yule mtu wa ajabu.

Jadu Mfaume alimtazama yule askari kwa ghadhabu, na pamoja na uwezo wake, alijua kuwa iwapo yale yaliyosemwa na yule kijana yalikuwa ya ukweli, basi alikuwa na kibarua kizito.

Alimkazia macho yake na kumtazama kwa makini yule kijana huku akiinua juu mikono yake taratibu.

“Kwa hiyo unataka nini kutoka kwangu Inspekta…?” Alimuuliza yule askari huku akimtazama kwa makini.

Oh, Mungu wangu! Anajaribu kusoma mawazo yangu…

Jadu Mfaume alitabasamu huku akizidi kumtazama kwa makini yule askari, Brian Koba akajua kuwa ameshajua ni nini kilichopita kichwani mwake muda ule, lakini naye pia alikuwa amejiandaa kwa hali ile.

Kimoyo-moyo alianza kuimba wimbo aliokuwa akiupenda sana wakati akiwa shuleni.

Kuna mapera jama, njooni muyaone…

Kuna mapera jama, njooni muyaone….

Jadu Mfaume alikunja uso na kumtazama kwa uso wa kuuliza, hakuelewa ni nini kilikuwa kikipita hakuelewa ni vipi ule wimbo ulikuwa ukihisiana na hali yote iliyokuwapo.

Jadu Mfaume alifinya macho na kumtazama kwa uso wa kuuliza. Hakuelewa, ni vipi ule wimbo ulikuwa ukihusiana na hali yote ile iliyokuwapo wakati ule.

Alichanganyikiwa.

Muda huo mlango wa kuingilia mle ndani ulipigwa kwa nguvu kutokea nje na askari wengine wawili waliingia, mmoja akiwa na pingu mkononi, mwingine akiwa na bunduki.

“Mfungeni pingu haraka!” Inspekta Brian Koba alisema kuwaambia wale askari, huku bado macho yake yakiwa yamemganda yule mtu aliyemtambua kwa jina la kubuni la John Smith, na kumuambia, “Nakushauri utulie hivyo hivyo John Smith, kuna bunduki tatu zilizoelekea kichwani kwako, na kuna tatu zilizouelekea mwili wako…”

“Huwezi kuthubutu kuniua…au kujaribu kuniua…” Jadu Mfaume alimuambia huku akizidi kujaribu kumsoma mawazo ya yule kijana, haraka Brian alianza tena kuimba ule wimbo wake kichwani mwake, na kwa mara nyingine Jadu Mfaume alichanganyikiwa.

Anafanya nini huyu binadamu, akh…shit! Ananichezea eeenh…?

Askari mwenye pingu alimsogelea Jadu huku wale wengine wote wakiwa makini na bunduki zao. Askari alimshika mkono na kuanza kuiweka pingu mkononi mwa Jadu Mfaume, na hapo kilitokea kitu ambacho hakuna yeyote kati ya wale askari aliyekitegemea.

Kitendo cha yule askari kuigusanisha tu ile pingu na mkono wa Jadu kilimsababishia kupigwa shoti moja kubwa sana ya umeme. Mlipuko mkubwa ulisikika na yule askari alitupwa nyuma kwa nguvu huku yowe likimtoka.

Sambamba na mlipuko ule, taa ya balbu iliyokuwa ikining’inia kwenye dari ya wodi ile ilipasuka na kutoa mlipuko mkubwa uliowachanganya baadhi ya wale askari waliokuwemo mle ndani, wakidhani ni mlipuko wa bastola, huku ikitupa vipande vya vioo huku na huko.

Jadu Mfaume alitawanya shoti za umeme wodi nzima, na tafrani iliyoamka hapo haikuwa ndogo.

“Ayyaaaarrgh…anashambulia!” Mmoja wa askari alisikika akipiga kelele kwa taharuki kubwa.

“Piga risasi…!”

Sekunde hiyo hiyo balbu nyingine iliyokuwa kule chooni nayo ilipasuka na kutoa mlipuko mwingine kama ule wa kwanza. Si kizaa zaa hicho!

“Acchaaa….!”

Mambo yote yalitokea ndani ya sekunde chache sana.

Yule askari aliyepigwa shoti alitupwa na kujipigiza kwenye kile kitoroli alichoingia nacho Jadu mle ndani na kusambaratika pamoja nacho hadi kando ya mlango wa kuingilia mle ndani. Muda huo huo Jadu Mfaume a.k.a. John Smith, alipiga msamba na kubonyea chini, wakati wale askari wengine wakikumbwa na taharuki na kupiga mayowe, na mwingine kwa kuchangayikiwa akifyatua risasi.

Brian Koba aliona vitendo vile kwa mkupuo mmoja uliojaa mshituko mkubwa. Haraka sana alijitupa pembeni na kujibiringisha juu ya kile kitanda alichokuwa amelalia hapo awali, na kudondokea upande wa pili, risasi iliyofyatuliwa na yule askari mmoja aliyekuwa nyuma ya Jadu Mfaume ikimkosa Jadu na kumpitia Brian kwa umbali mdogo sana na kwenda kujikita ukutani.

“Tulieni askariiiii!!” Brian alipiga kelele huku akiangukia upande wa pili wa kile kitanda, macho yake yakiwa makini kwa yule mhalifu wake.

Akiwa pale sakafuni Jadu alijibiringisha kwa kasi kuwaendea wale askari waliokuwa nyuma yake hapo awali na kuzungusha mguu wake kwa ngwala kali iliyomkumba mmoja wa wale askari na kumpeleka chini kwa kishindo ilhali bunduki yake ikimtoka mkononi.

Askari mwingine aliona tendo lile na alianza kugeuza silaha yake kumuelekea yule mhalifu mahiri, lakini kwa wepesi wa ajabu Jadu Mfaume alijirusha na kusimama wima mbele yake, na kabla yule askari hajafyatua silaha yake, Jadu alishazungusha mkono wake na kuikamata ile bunduki huku naye akijigeuza kistadi, mtutu wa ile bunduki ukipita chini ya kwapa lake, yule askari aliyeishika ile bunduki akiwa nyuma yake.

Askari wa tatu aliyekuwa jirani na yule aliyedhibitiwa na Jadu aligeuka na bastola yake kumuelekea Jadu lakini hapo hapo Jadu alifyatua ile bunduki bado ikiwa mkononi mwa yule askari aliyemdhibiti na kile chuma kilichokuwa kimechomoza kwenye mtutu wa ile bunduki kilichomoka kwa kasi na kujikita ubavuni kwa yule askari ambaye aliachia yowe kubwa huku bastola ikimtoka naye akitupwa nyuma kwa msukumo wa risasi ile iliyokuwa imekusudiwa Jadu Mfaume.

Brian Koba alipiga ukelele wa ghadhabu huku akimuelekezea bastola yake yule mhalifu, lakini hapo alimshuhudia Jadu akizungusha kiwiko chake na kumbamiza kwa nguvu usoni yule askari aliyembana nyuma yake, ambaye alibweka kwa maumivu huku akipepesuka nyuma, ile bunduki iliyokuwa mkononi mwake ikibaki mikononi mwa Jadu.

“Uko chini ya ulinzi weweeee…!”

Jadu alimtupia ile bunduki yule askari aliyeingia pamoja na yule aliyekuja na pingu, yule askari alijirusha pembeni kuikwepa ile bunduki wakati Jadu akiruka kwa hatua moja kubwa hadi juu ya kile kitanda, kisha akajirusha kulielekea dirisha lililokuwa upande mmoja wa wodi ile. Brian Koba aliona kitendo kile na alijua kuwa ile ndio ilikuwa nafasi pekee ya kumpata yule mhalifu. Alitaka kumtupia risasi lakini alibadili mawazo dakika ya mwisho kabisa, kwani alihofia huenda ile risasi yenye kulipuka ipigapo ipokusudiwa ingeweza kumlipua kabisa yule mtu ambaye yeye alikuwa akimtaka akiwa hai.

“Pumm-Bbaaaavvvvv…!”

Alimpiga ukelele na kumrukia mzima mzima. Walikumbana hewani na wote wawili wakaenda chini kwa kishindo hatua chache kutoka dirishani. Jadu alikuwa wa kwanza kuinuka na kumsukumia teke zito Brian, lakini Brian aliliona na kuruka nyuma na lile teke likamkosa. Kwa pembe ya jicho lake Brian aliona askari wawili waliobaki wakiinua bastola zao kumlenga yule mhalifu.

“Piga miguuni…!” Aliwapigia kelele kisha naye akajitupa pembeni kujiepusha asidhuriwe na zile risasi.

Askari waliachia risasi kwa pamoja na milipuko ya bastola zao ilirindima mle ndani, lakini Jadu alijirusha kwa namna ambayo kama tungejaribu kujirusha mimi na wewe lazima tungetegua viuno.

Lakini Jadu sio mimi wala wewe.

Alijirusha kwa kujipindia nyuma, miguu yake ikiiacha sakafu na kujibiringisha hewani. Akaruka juu, risasi zikapiga ukuta na kulipuka kwa kishindo mithili ya bomu dogo, zikichimba tundu kubwa pale ukutani na zikitawanya vipande vya plasta ya ukuta kila kona.

Ukelele wa fadhaa ulimtoka Brian na wale askari, na Jadu akatumia mfadhaiko wao kuwazidi kete nyingine. Alijigeuza haraka na kutoka kasi kuwaelekea wale askari, akikikumba kile kitanda kilichokuwa mle ndani na kuwavugumizia wale askari kwa nguvu za ajabu.

Askari walitupwa chini na kile kitanda huku wakipayuka mayowe ya taharuki, wakimuacha Jadu akitoka mbio kuuendea mlango wa kutokea nje ya chumba kile.

Brian alijibiringisha chini na kuiwahi haraka bastola yake na akiwa bado amelala chini na bastola yake ameikamata kwa mikono yake yote miwili, alimtupia risasi yule mhalifu.

Risasi ilimpiga Jadu mguuni, na kulipuka kwa kishido, cheche za umeme zikitawanyika kila upande na Jadu akianguka chini akitanguliza mbele mikono yake na kuupamia ule mlango, ambao ulitawanyika naye akaangukia nje ya chumba kile kwenye korido ndefu ya hospitali ile.

Kule ndani Brian alijiinua na kutoka mbio kumuwahi yule mtu aliyemtambua kama John Smith na ambaye alidhamiria kumtia mbaroni.

Nje ya ile wodi, Jadu alijiinua na kuutazama mguu wake uliodhurika kwa risasi ya yule askari jeuri, lakini aliona kuwa ile athari isingemzuia kujiokoa. Aligeuka na kuanza kuifuata ile korido lakini hapo tena alikutana na hali ambayo hakuitegemea.

Kutokea kule alipokuwa akitaka kukimbilia aliona wahudumu wote wa ile hospitali wakifunua makoti yao meupe ya utabibu na kutoa bastola na wengine bunduki na kumuelekezea kule alipokuwako.

“Simama! Uko chini ya ulizi! Umezingirwa kila upande…!”

Shit…!

Aligeuka nyuma na kuona hali kama ile ile, tena huko akamuona na Inspekta Dilunga naye akiwa katika mavazi yake ya kiaskari akiwa na bastola kila mkono, akielekea mbio eneo lile, akifuatwa na wahudumu wengine wa hospitali ile wenye silaha.

Kumbe wote hawa ni askari! Pumbavu…leo wanadamu wamenitega!

Alijirusha kwenye chumba kilichokuwa karibu yake na muda huo huo Brian Koba naye akatokeza pale kwenye korido na kumfuata mbio. Ndani ya chumba kile Jadu alikwenda mbio moja kwa moja na kujitupa kwa nguvu kulirukia dirisha la chumba kile.

Brian aliona tendo lile na alipiga ukelele wa kutoamini pale alipomshuhudia yule mtu akijipigiza kwa nguvu kwenye lile dirisha la luva ngumu za mbao, na kutoka nalo mzima mzima hadi nje ya chumba kile.

E bwana we!

Nje ya dirisha lile Jadu alijibwaga kwenye bustani ya maua na kujibiringisha chini kwa kasi, kabla ya kujiinua na kugeuka kule alipotokea, na muda huo alimshuhudia yule askari mbishi akiruka nje ya chumba kile kupitia kwenye uwazi aliouacha baada ya kuruka na dirisha lililokuwa pale ukutani. Aligeuka na kuanza kutimua mbio kuyaendea maGari la polisi na ya pale hospitali yaliyokuwa yameegeshwa nje ya jengo lile.

“Simama…!”

Jadu alizidi kutimua mbio, wakati ghafla mbele yake ilipotokeza gari iliyokuwa ikiendeshwa na askari wa jeshi la polisi aliyemkatishia mbele kwa nia ya kumzuia kukimbia na hatimaye akamatwe.

Jadu alipiga ukelele wa ghadhabu huku akijitahidi kusimama na kulikwepa lile gari, lakini alishindwa na badala yake alienda kujibamiza kwenye ubavu wa lile gari lililotikisika kama kwamba limegongwa na kifaru, kisha naye akaanguka chini kwa kishindo.

“Well done Corporal!” Brian Koba alipiga ukelele kumpongeza yule askari huku akikimbilia pale alipoangukia Jadu Mfaume.

Na hapo yule askari aliyemkatizia Jadu na kumdhibiti alifanya kosa kubwa sana maishani mwake…


Kule ndani ya jengo la hospitali, Inspekta Dilunga alimuona Jadu akikimbilia ndani ya kile chumba, na kisha akamuona Inspekta Brian akimfuata mbio nyuma yake. Alikimbia kuelekea kwenye kile chumba akifuatwa mbio na askari wake waliokuwa wamejivisha nguo za wahudumu wa ile hospitali kama mtego walioujadili na Brian, sasa wote silaha zao zikiwa wazi mikononi mwao.

Alisikia ukelele wa hamaniko wa Inspekta Brian Koba, na aliongeza kasi huku akili ikimuenda mbio na mapigo ya moyo yakiongezeka maradufu. Aliserereka na kujipigiza kwenye ukingo wa mlango wa kuingilia mle ndani wakati ambapo ndio Jadu Mfaume, kwake John Smith, akipotelea nje ya chumba kile na lile dirisha.

“Ayyaaaarrgh….!” Alipiga ukelele wa taharuki, na hapo hapo alimuona Inspekta Brian naye akijitupa nje ya uwazi uliobaki pale ukutani, wakati baadhi ya wale askari wake, wengine wakiwa wameletwa maalumu kwa kazi ile kutoka Dar es Salaam, wakimpita na kukimbilia mle ndani huku kila mmoja akipiga ukelele wake wa mshangao.

Inspekta Dilunga aligeuza kasi na kutoka nje ya chumba kile, akikimbia kuelekea kwenye lango kuu la kutokea nje ya hospitali ile, njiani akipishana na Dokta Nigel Smith aliyetumbua macho kwa woga na kutoelewa kilichokuwa kikiendelea, ingawa alikuwa akijua juu ya mtego ule ambao polisi walikuwa wamemtegea yule mhalifu wa ajabu, kwa kutumia ushirikiano wa mwandishi Bruno Mgimba.

“Amekamatwa…?” Alimuuliza yule askari aliyekuwa akimpita mbio.

Inspekta Dilunga hakuwa na muda wa kumjibu.

“Wengine zungukieni mlango wa nyumaaaa!” Aliwapigia kelele askari wake, huku akiendelea kutimua mbio, nao wakatawanyika, wengine wakimfuata kule alipokuwa akikimbilia, ihlali wengine wakitimua mbio kueleka mlango wa nyuma wa jengo lie, wakati wengine tayari walikuwa wamesharuka kwenye lile dirisha alilotokea Jadu na Brian Koba kujaribu kumfukuza yule mhalifu….

  • * *

Koplo aliyemkatishia Jadu kwa gari na kumdhibiti, alimuona yule mhalifu akiwa aliyeanguka chini akijizoazoa kwa taabu, mguu wake ukiwa na jeraha kubwa na ukionekana kuwa hauna nguvu. Alimtupia jicho Inspekta Brian Koba na alimuona kuwa bado alikuwa mbali kidogo na pale alipokuwa yule mhalifu, nyuma yake akifuatwa na askari wanne wenye silaha waliokuwa wamevaa mavazi ya wahudumu wa ile hospitali. Wote bado walikuwa mbali, hivyo aliruka nje ya gari ile akiwa na bastola yake mkononi. Alimkuta Jadu akiwa amepiga goti moja na akitikisa kichwa kujaribu kuweka akili yake sawa baada ya mtikisiko alioupata kwa kujibamiza kwenye lile gari.

Alimuwekea bastola kichwani akiwa amesimama mbele yake na kumshika ukosi wa shati huku akimkemea kwa ukali. “Uko chini ya ulinzi…Tulia, bazazi mkubwa…!”

Lilikuwa kosa kubwa sana.

Brian Koba aliona kitendo alichofanya yule askari na hapo hapo moyo ukamuingia baridi. Aliongeza kasi huku akimpigia ukelele yule koplo.

“Kuwa makini Kopl-AAAAARRRGHHHH!”

Hakumalizia kauli yake, na badala yake aliishia kupiga ukelele wa fadhaa pale alipomshuhudia Jadu Mfaume, kwake John Smith, akimpiga ngumi nzito ya kwenye korodani yule askari, na wakati huo huo akiinua mkono wake wa pili na kuipangusa ile bastola iliyokuwa mkononi mwa yule koplo huku akipeleka kichwa chake pembeni naye akiinuka kutoka pale chini.

Koplo aliachia yowe kubwa la uchungu na wakati huo huo ile bastola iliyokuwa mkononi mwake ikafyatuka, risasi iliyokuwa ndani yake ikichimba ardhi hatua chache kando ya pale alipokuwa amesimama Jadu…

Na ni katika muda huu, hatua kadhaa kutoka pale walipokuwa, ndipo Inspekta Dilunga naye alitoka kasi nje ya lango kuu la hospitali ile, bastola ikiwa wazi mkononi mwake, akiwashitua wananchi waliokuwa wakiingia ndani ya jengo lile kutafuta tiba, na kufuata kule ulipotokea ule mlio wa bastola, ambako aliona lile gari likiwa limesimama kwa namna isiyo sawa, na harakati za Jadu na yule koplo zikiwa zikiendelea upande wa pili wa gari ile. Askari waliokuwa wakimfuata nyuma yake walimfikia na kwa pamoja walianza kulisogelea lile gari kwa tahadhari kubwa.

“Toa raia eneo hili…haraka!” Alimwambia mmoja wa askari waliokuwa karibu yake huku akiwa makini sana na kilichokuwa kikiendelea upande wa pili wa gari lile.

Askari wawili walianza kuwaondoa raia eneo lile haraka haraka.

“Inspekta Dilunga amefika…tumemzingira!” Mmoja wa asakri waliokuwa nyuma ya Brian alisema, na ingawa Brian aliisikia kauli ile, akili yake ilikuwa makini sana kwa yule mtu aliyekuwa mbele yao, ambaye hakutaka kumuacha awatoroke kwa mara nyngine.

Alielekeza bastola yake kwa Jadu huku akipiga kelele za kumtahadharisha kuwa atulie kama alivyokuwa, lakini Jadu hakuwa amemaliza mambo yake na wala hakuwa na nia ya kuyamaliza muda ule.

Aliupigiza mkono wa yule koplo uliokuwa umekamata ile bastola kwenye upande wa lile gari na ile bastoka ikamtoka yule askari huku akipiga ukelele mwingine wa uchungu. Jadu alipitisha mkono wake shingoni kwa yule koplo na kumpiga kabali kali huku akimuweka mbele yake, sasa akimfanya ngao, na kumtazama yule Inspekta kijana kwa macho yaliyowiva kwa ghadhabu. Alirudi nyuma hatua moja na kujiegemeza kwenye lile gari.

“Tulia hapo hapo Inspekta! One more step and I break his neck!”

Brian alisimama, na kuwainulia mkono wake askari waliokuwa nyuma yake kuwa nao wasimame, bastola yake bado ikiwa imemuelekea yule mtu wa ajabu, na wakati huo huo aliona kuwa yule mtu alikuwa hawezi kusimama sawasawa kutokana na risasi aliyompiga.

“Just give your self up John Smith! Tumekuzingira kila upande…tayari umejeruhiwa na huna pa kukimb-” Brian Koba alimuambia, lakini kwa mara nyingine tena hakufanikiwa kumaliza kauli yake, kwani ghafla sana, yule mtu aliyembatiza jina la John Smith alimsukuma mbele kwa nguvu yule koplo naye akajitupa ndani ya lile gari, akimuacha yule koplo akipiga ukelele huku akipepesuka ovyo kuelekea kule alipokuwa Brian.

“Bloody fooo….lll!”

Brian Koba alipiga ukelele na kuruka pembeni kumkwepa yule koplo, na wakati huo huo akatupa risasi kuelekea kwenye lile gari. Risasi ilipiga mlango wa upande wa abiria na hapo hapo ililipuka, na kuuchanachana ule mlango. Lile gari lilichomoka kwa kasi kutoka eneo lile, Jadu Mfaume, a.k.a. John Smith, akiwa nyuma ya usukani, likiacha vumbi kubwa nyuma yake, na kwa mara ya kwanza, ukimya, amani na utulivu wa mji wa Kisarawe vilikatishwa na milio ya risasi za mfululizo wakati Brian Koba na wale askari waliokuwa nyuma yake walipolimiminia risasi lile gari lililokuwa likiondoka kwa kasi kutoka eneo lile.

Mayowe yalitawala kila upande pale wananchi waliokuwa wamefika pale hospitali kupata tiba mbali mbali walipohamanishwa na tafrani ile, wengine wakikimbia ovyo huku na huko.

Ulikuwa ni mtafutano si mdogo.

Gari liliyumba kulia na kushoto, tairi zilipiga kelele wakati zikichubuana na ardhi, risasi zikilitoboatoboa lile gari na kupasua vioo na kutupa vipande vya vioo kila upande ndani ya lile gari, Jadu Mfaume mpya akiwa amejikunja nyuma ya usukani, Brian na askari wenzake wakilikimbiza lile gari liliyokuwa likiwaacha kwa kasi sana.

Inspekta Dilunga aliliona gari alilokuwa akiendesha mhalifu John Smith likielekea kwa kasi kule alipokuwa ameweka ukuta na askari wake kadhaa, na aliona lile gari likija kwa mwendo wa kona-kona na wakati huo huo risasi zilizokuwa zikitupwa na akina Brian waliokuwa nyuma ya gari ile zikipita juu na pembeni ya gari lile na kuhatarisha maisha yao.

“Take cover Dammit!” Alipiga ukelele huku akijitupa pembeni wakati ile gari ikiwaendea kwa kasi na kuwatawanya wale askari kila upande, muda huo huo Inspekta Dilunga akiwa amejilaza chini, alimimina risasi za mfululizo kulielekea lile gari, na aliona taa ya mbele ya gari ile ikitawanywa vipande vipande na moja ya risasi zake, gari liliyumba vibaya, likamgonga mmoja wa askari waliokuwa eneo lile ambaye alitupwa hewani huku akiachia yowe kubwa, na kisha lile gari likawa limewaacha na wao, likitimua vumbi kuliendea geti la kutokea nje kabisa ya uzio wa hospitali ile.

Dilunga hakuuweka.

Aliiinuka na kutimua mbio bastola ikiwa juu mkononi mwake na kuikimbilia pikipiki maalumu ya polisi, ambayo ilikuwa na matairi matatu huku ikiwa imeunganishwa na kitoroli kando yake ambacho kiliweza kubeba abiria. Ni aina ya pikipiki ambazo zilitumika sana na jeshi la Ujerumani katika vita kuu ya pili, na ambazo baada ya vita ile, zilikuwa zikitumika sana na majeshi ya waingereza.

“Nipe ufunguo askari….upesi!” Alimkemea askari aliyekuwa kwenye ile pikipiki ambaye mpaka muda ule hakuwa akijua afanye nini. Dilunga aliupokea kwa fujo ule ufunguo, na huku jasho likimtiririka, vumbi likiwa limemtapakaa, aliiparamia ile pikipiki na kutoka kasi eneo lile kulifukuza lile gari lililokuwa likipotelea nje ya geti la hospitali ile.

“Inspektaaaaaaaaa…!” Brian alimpigia ukelele mwenzake huku akijitupa hewani na kuidandia ile pikipiki. Mikono yake ikikamata ile sehemu ya kitoroli cha ile pikipiki na kubururwa kwa sekunde kadhaa kabla Dilunga hajaelewa kilichotokea.

“Whaaaaaat…?” Dilunga alimaka na kukamata breki ghafla. Brian alitupwa mbele kwa msukumo wa breki ile na kutumbukia ndani ya kile kitoroli.

“TWENDEEEEEE…!” Alimpigia ukelele kwa mara nyingine huku akijiweka sawa ndani ya kile kitoroli, na Inspekta Dilunga aliachia klachi na kuvuta mafuta. Pikipiki ikaruka mbele mithili ya jiwe kutoka kwenye manati.

“Kimbiza yuleeee…!” Brian aliwapigia kelele askari waliokuwa wameduwazwa na matukio yake ya haraka, na mara moja wakaanza kuparamia maGari la polisi yaliyokuwapo pale na kuondoka kwa kasi kumfukuza yule mhalifu wao, wale viongozi wao wawili wakiwa kwenye ile pikipiki.

Sasa mji wa Kisarawe ulishuhudia tafrani ya kufukuzana magari katika barabara zake, ving”ora vya gari za polisi vikirindima kwa kelele kubwa, risasi zikifyatuliwa kulielekea lile gari alilokuwa akitorokea Jadu Mfaume mpya, vumbi likizagaa kila upande. Kwa muda wa kama nusu saa maGari lale yalikuwa yakipigana chenga katika mitaa ya Kisarawe wakati Jadu akitafuta uelekeo wa kwenda, na kila alipoelekea ile pikipiki ilikuwa nyuma yake, ikifuatwa na msururu wa magari manne ya polisi. Alipofika njia panda ya kuelekea jijini Dar na ile ielekeayo Kazimzumbwi, alikunja kona kali na kuchukua uelekeo wa Kazimzumbwi, akijua kuwa kuelekea Dar hakukuwa salama kabisa kwake, kwani huko ndiko serikali ilipokuwako.

Alielekea kwa kasi kwenye ile barabara, akisikia ving’ora vikizidi kumfuata nyuma yake. Alipita lile eneo yalipotokea maafa ya kutisha na kuendelea mbele. Kiasi cha kilometa mbili mbele aliona njia ya kuchepuka kutoka kwenye ile barabara kuongia porini, naye akakunja kuifuata ile njia, akijua kuwa atawapoteza tu porini wale askari wajinga.

“Ah…kaenda kule, tumempata…!” Dilunga alimaka, na wakati huo huo akiongeza kasi akipita moja kwa moja kuifuata ile barabara ya Kazimzumbwi, akiacha kufuata ile njia ya vumbi aliyochokua yule mhalifu mahiri.

“Whaaat…sasa mbona unapitiliza…?” Brian alimaka kwa mshangao.

“Waashirie wenzetu wamfuate! Sisi tunamkatishia denge …tunaye this time, mwanaharamu…tunaye!” Inspekta Dilunga alisema kwa kelele. Brian Koba aligeuka na kumwashiria dereva wa gari iliyokuwa nyuma yao afuate kule alipoelekea Jadu a.k.a. John Smith.

Msururu wa gari za polisi ulifuata kule alipokimbilia Jadu, wakati Dilunga na Brian wakifuata ile njia ya Kazimzumbwi, kumzungukia kwa mbele mhalifu wao.

Hakika sasa Jadu atapatikana.

Alitupa macho mbele na kuona kuwa njia ilikuwa inaekea kwenye muinuko mkali. Alikanyaga mafuta na gari ikakwea ule muinuko kwa kasi huku ving’ora vya gari za polisi vikizidi kumkera masikioni mwake. Alifika juu ya ule muinuko na kuanza kushusha kwa kasi, na hapo kwa mshangao mkubwa mbele yake aliiona pikipiki ya Inspekta Dilunga ikiwa na Brian Koba kwenye kitoroli cha pembeni ikiiinga kwenye ile barabara kutokea kwenye njia moja ya msituni.

“Pumbaaaavu….!” Alimaka kwa ghadhabu na kupeleka macho yake kulia na kushoto. Kila upande wa njia ile kulikuwa na mporomoko mkali na ile njia nyembamba ilikuwa ikielekea kwenye korongo refu, ambalo sasa lilikuwa nyuma ya wale askari wawili waliokuwa wakija kutokea mbele yake.

“SHIT WANADAMU! SHIT…SHIT…SHIIIIIIIIIT…!” Alimaka tena huku akikanyaga breki na kugeuka nyuma. Huko aliona msururu wa maGari la polisi ukishuka kilima kwa kasi huku vingo’ora vikitawala eneo lote lile. Aligeuka mbele na kuwaona wale askari wawili wakiteremka kutoka kwenye pikipiki yao wakiwa na bastola zao mikononi, ile pikipiki ikiwa katikati ya ile njia nyembamba ya vumbi iliyozingirwa na maporoko makali kila upande.

Jadu alibaki ndani ya lile gari, sasa akiwa amechanganyikiwa vibaya sana.


Inspekta Dilunga na Inspekta Brian walisimama bega kwa bega katikati ya ile barabara nyembamba, ile pikipiki ikiwa hatua zipatazo tatu mbele yao, ikiwa imeegeshwa kuikata ile njia kama aina ya kizuizi mbele ya lile gari alilokuwamo yule mhalifu mkorofi.

Walikuwa wakitazama kule lilipokuwa lile gari, wakiwa wamefinya nyuso zao kutokana na jua la asubuhi lililokuwa likiwapiga usoni, bastola zao zikiwa mikononi mwao.

Nyuma ya gari la yule mhalifu waliyekuwa wakimsaka kwa udi na uvumba kwa siku kadhaa sasa, waliyaona yale magari mengine ya polisi wenzao yakiwa yameegeshwa kwa msururu mmoja pale barabarani, kwani ile barabara ilikuwa nyembamba sana kiasi cha kutoweza kuegesha magari mawili ubavu kwa ubavu. Wale askari wenzao walikuwa wameteremka kutoka kwenye maGari lale na walikuwa wameelekeza bunduki na bastola zao kwenye lile gari lililokuwa limembeba yule mhalifu mgumu.

“Tumempata huyu mwanaharamu safari hii…tumempata!” Inspekta Dilunga alisema huku akitazama kwa makini kule lilipokuwa gari la Jadu Mfaume, kwake John Smith.

“Mnh, Inspekta, huyu jmaaa mjinga sana ujue…? Si umeona jinsi alivyotutoka kule hospitali? Lazima tuwe makini kuliko kawaida, na tutarajie lolote…”

“Sio sasa hivi Brian. Mimi simuachi huyu mbwa hata iweje. Kwani n”na hakika asilimia mia moja kuwa tukimpata na kumdhibithi hii kesi tunaimaliza…”

“Sasa mbona hatoki…na wala hafanyi lolote…?” Brian Koba aliuliza kwa mashaka, huku akitazama kwa makini kule lilipokuwa gari la Jadu Mfaume.

“Hana ujanja tena…kajiingiza mwenyewe kwenye mtego, na sasa hajui afanyeje…”

“Mnh, I doubt Inspekta…mjinga anaweza akawa anatusoma mawazo yetu kutokea kule kule…” Brian alisema.

Sasa zilikuwa zimepita kama dakika tatu tangu lile gari la yule mhalifu lisimame hatua kadhaa mbele yao na wao wateremke kutoka kwenye pikipiki yao.

Akiwa ndani ya lile gari aliloteka, Jadu Mfaume mpya alikuwa ametulia tuli, akisikiliza maongezi ya wale askari kwa kutumia akili yake ya ajabu, na baada ya ile kauli ya mwisho ya Brian Koba alikenua meno kwa ghadhabu.

Kwa nini huyu binadamu anajifanya mjanja sana…? Yaani anajitia kujua kila ninachoto\aka kukifanya!

“UKO CHINI YA ULINZI! JISALIMISHE KWA AMANI MHALIFU! TOKA HUMO NDANI YA GARI TARATIBU, MIKONO YAKO IWE JUU!” Inspekta Dilunga alimpigia kelele yule mhalifu huku bastola yake ikiwa imeelekea kule kwenye lile gari.

“Unadhani atakusikia kwa umbali huu Inspekta?” Brian alimuuliza mwenzake huku bado akitazama kwa umakini uliojaa mashaka kule kwenye lile gari.

“Amenisikia tena vizuri sana mpumbavu mkubwa yule…ikiwa anaweza kusoma mawazo ya watu yakiwa vichwani atashindwa kunisikia kwa kelele zote hizi Brian?” Dilunga alimjibu huku macho yake yakiwa bado kwenye gari la Jadu.

“Yeah…uko sahihi Inspekta…nadhani sasa anatusubiri sisi tuanze kufanya makeke…anatutegea…” Brian alisema huku akizidi kulitazama lile gari na jasho likimtiririka. Aliweza kumuona yule mtu akiwa ndani ya lile gari, mikono yake ikiwa kwenye usukani.

Akiwa mle ndani ya gari, Jadu Mfaume mpya alisikia ile amri ya yule askari, na kwa kutumia hisia zake kali na zenye nguvu, aliweza kusikia yale majibizano baina ya wale askari akiwa pale pale nyuma ya usukani, na kwa mara nyingine ghadhabu zake zilimuelekea Brain Koba kwa kumuotea mipango yake, kwani hakika kile ndicho alichokuwa akikifanya; kuwategea wale askari kuona ni hatua gani watachukua baada ya kumuweka kati kati ya mtego ule aliojitegea mwenyewe kwa kutojua njia sahihi.

“Basi na si’ n’do tu’shamtega hapa, tunaye tu leo!” Inspekta Dilunga alijibu na wakati huo huo Inspekta Brian Koba aliamua cha kufanya.

Aliwaashiria wale askari waliokuwa nyuma ya gari la mhalifu Jadu Mfaume a.k.a. John Smith, waanze kulizingira lile gari. Kwa tahadhari kubwa wale askari walianza kulisogelea lile gari huku bunduki na bastola zao zikiwa imara mikononi mwao, wakilinzungukia kutokea nyuma, kulia na kushoto.

Na hata pale alipokuwa akifura kwa hasira mle ndani ya gari, alimsikia tena Inspekta Dilunga akimpigia kelele kumuamuru atoke nje ya gari lile akiwa ameweka mikono yake juu.

“Wajinga sana binadamu…hivi mnadhani mtaniweza mimi…?” Alisema kwa hasira, na muda huo huo, kwa kupitia kwenye kioo cha kuonea nyuma kilichokuwa ndani ya lile gari aliwaona wale askari wengine wakilizingira taratibu lile gari kutokea nyuma.

“Akh…Pumbavu…” Alimaka na kupeleka macho kwenye vioo vingine vya kuonea nyuma vilivyokuwa kila upande wa lile gari, nako akaona askari wakilizingira taratibu kutokea kila upande.

“Ebbo…hivi hawa….(Alisonya) Pumbavu!” Aliinua macho yake kule mbele, na kuwaona wale askari wawili wakiwa bado bega kwa bega nyuma ya pikipiki yao waliyoiweka katikati ya barabara kama kuzuizi. Hatua kama tatu mbele ya yule Inspekta ambaye mpaka sasa alishamjua kuwa alikuwa akiitwa Dilunga, na kushoto kwake kidogo kando ya barabara ile nyembamba, kulikuwa na mti mkubwa uloning”niza tawi kubwa pale barabarani.

Ghadhabu zilimpanda.

“Nyi’ hamnijui mimi, eeenh…?” Alisema kwa sauti, na hapo hapo aliwashangaza wale askari wote waliokuwepo pale. Alikanyaga mafuta kwa nguvu na gari lilivuma, kisha akaachia klachi ghafla. Gari liliruka mbele na kuchomoka kwa kasi sana, likiwaelekea wale askari wawili waliokuwa mbele yake huku likitimua vumbi kubwa sana nyuma yake, ambalo lililowachanganya na kuwaziba macho wale askari waliokuwa wakilinyatia lile gari kutokea nyuma na pembezoni mwake.

Kilichofuata hapo kilikuwa ni kizaazaa kikubwa!

Askari waliokuwa nyuma na kando ya lile gari walipiga mayowe ya kiwewe, wengine wakijitupa chini bila sababu, wakiamini kuwa ndio walikuwa wakijiokoa, ilhali wengine wakigeuka walikotoka na kutimua mbio, wakidhani kuwa lile gari lilikuwa likitimua vumbi na kuwarudia wao kule nyuma, wengine wakipiga mayowe tu bila kujua ni kwa nini walikuwa wakifanya hivyo.

Wawili walifyatua risasi kulielekea lile gari, milio ya bunduki zao ikizidi kuwachanganya wale askari wenzao waliohamanika pasina kiwango.

Inspekta Brian Koba na Gezza Dilunga walilishuhudia lile tendo la yule mhalifu majinuni kwa mshtuko mkubwa. Dakika moja walikuwa wamesimama wakilitazama lile gari likiwa na yule mtu aliyeonekana kuwa amezidiwa kete, sekunde ya pili walilishuhudia lile gari likiwachomokea kasi pale walipokuwa.

Lakini wote wawili waliikabili ile hali kwa wepesi usiopatikana popote pengine ila kwa askari makini na mashujaa.

“Bloody Fooooooolll…!” Brian Koba alipiga ukelele huku akilishudhudia lile gari likiwatimkia kwa kasi ya kuua, na badala ya kukumbia aliinua bastola yake na kutupa risasi tatu za mfulululizo. Katika sekunde moja ile alishuhudia sehemu ya paa la gari lile ikitawanyika vibaya sana baada ya moja ya rasasi zake kupiga sehemu ya mbele ya paa la gari lile na kulipuka pale pale, kisha akajitupa pembeni ya ile barabara, akijivuruga kwenye vumbi na kusererekea ukingoni mwa ile barabara kulikokuwa na mporomoko mkali. Alijikamata kwenye mawe makubwa yaliyokuwa yametawanyika huku na huko kando ya barabara ile na kubaki akiwa amelalia tumbo kando ya barabara ile, miguu yake ikining’inia upande wa korongoni ilhali kiwiliwili na mikono yake ikibaki juu ya mporomoko ule, akilishuhudia lile gari likimuendea Inspekta Dilunga kwa kasi ya ajabu, huku sehemu yote ya juu ya gari lile ikiwa imefumuliwa kabisa na ile risasi yake na yule mhalifu akionekana waziwazi akiwa ameuma meno kwa ghadhabu huku amelielekeza gari kwa Inspekta Dilunga.


Muda lile gari lilipochomoka ghafla na kuwaendea kasi pale walipokuwa wamesimama, Inspekta Dilunga aliachia tusi kubwa sana la nguoni kwa mshangao, lakini hapo hapo umakini wa kiaskari ukamrudia. Alitanua miguu yake na kuikamata vizuri zaidi bastola yake kubwa aina ya Snub Nosed Smith & Wesson kwa mikono yake yote miwili, alibana jicho moja na kumuweka kwenye shabaha yule mhalifu mwenye wazimu aliyekuwa nyuma ya usukani wa lile gari lililokuwa likimuendea kwa kasi, moyo ukimwenda mbio. Alisikia mlipuko wa bastola ya Brian, na akajizuia kutupa risasi zake kwani bado hakuwa amemuweka kwenye shabaha aitakayo yule mhalifu, na hapo alishuhudia paa la lile gari likitawanywa vipande vipande na risasi zenye kulipuka za Brian, na alishuhudia vipande vya ile paa vikitupwa hewani ilhali yule mhalifu akiwa wazi nyuma ya usukani huku ameuma meno na uso ameukunja kwa dhadhabu.

“Ama zako ama zangu, shaitwaani-L-Rrajiim we!”

Alifyatua risasi.

Risasi ilijikita kwenye bega la kulia la yule mhalifu, na Dilunga alimuona yule mtu akitupwa nyuma na kujipigiza kwenye mgongo wa kiti alichokalia, mikono yake iliuacha usukani na gari likayumba kulia na kushoto, sasa likiwa karibu sana na pale alipokuwapo, kisha kwa kihoro alimuona yule mtu akiukamata tena ule usukani na kumuelekezea lile gari kwa kasi ile ile.

“Inspektaaa…!” Brian alipiga ukelele kwa fadhaa huku akilishuhudia lile gari likimuendea Dilunga. Dilunga aliachia risasi ya pili, na aliishuhudia ile risasi ikijishindilia kwenye bega la mkono wa pili wa yule mtu asiye na jina rasmi, ambaye alitupwa nyuma kwa mara ya pili, akiachia usukani na gari ikiyumba vibaya sana huku ikielekea kumkumba na yeye.

“AYYYAAAAAHHH INSPEKTAAAAAAAAAAA…!” Brian Koba alipiga ukelele wa kukata tamaa huku akishuhudia kiwetewete kilichokuwa kikitokea, kwani alijua kuwa Dilunga alikuwa anaelekea kugongwa vibaya sana na lile gari.

Lakini Inspekta Dilunga alikuwa amepiga mahesabu makali. Pale pale alipiga hatua moja kubwa sana mbele kuliendea lile gari kisha akaruka juu, akiiachia ile bastola yake na kudandia lile tawi la ule mti uliokuwa kando ya barabara ambalo lilikuwa likining’inia juu ya barabara ile.

Na ni muda huo huo ambapo lile gari lilipopinduka huku likiruka hewani chini yake. Alikunja miguu yake ili kulikwepa lile gari, lakini gari lilikuwa limetupwa juu sana kutokana na kasi ililotoka nayo, na Inspekta Dilunga alihisi akipigwa na kitu kigumu na kizito miguuni, maumivu makali sana yakitambaa kutokea magotini mwake na kupanda kwenye uti wake wa mgongo, mikono yake ikiligea na kuliachia lile tawi alilolikamata, naye akitupwa hewani…


Brian Koba alilishuhudia lile gari likitupwa hewani na kupinduka ubavu-ubavu, na hapo alimuona Inspekta Dilunga akiruka juu na kudandia lile tawi kulikwepa lile gari, na aliona lile gari kwanza likiikumba ile pikipiki yao waliyoiegesha katikati ya barabara na kuitupa hewani, likimkosa Inspekta Dilunga na kupita chini yake, kisha likaanza kurudi tena ardhini kwa kuinamisha ile sehemu yake ya mbele kuelekea mwisho wa ile barabara ambako kulikuwa kuna korongo refu sana, ilihali ile sehemu ya nyuma ya lile gari ikiinuka juu zaidi.

Na ndipo aliposhuhudia ile sehemu ya nyuma ya gari iliyoinuka juu wakati lile gari likirudi tena ardhini ikimpiga Dilunga miguuni, naye akitupwa hewani mikono yake ikiachia lile tawi alilokuwa amelishika.

“DILUNGAAAAAAAA…!”

Alipiga kelele huku akijisotesha juu ya ile barabara kutoka kule kongoroni alipokuwa akiinig”nia, na hapo alisikia kishindo kizito kushoto kwake. Aligeuka na kuona lile gari lilikuwa limejipigiza ardhini kwa kishindo, kabla ya kuanza kusererekea ukingoni mwa lile korongo refu, yule mhalifu mkorofi akiwa ameshikiliwa na mkanda wa dereva ndani yake.

“Nnnoooooo…!” Brian alipiga kelele huku akijaribu kulikimbila lile gari ili angalau amuokoe yule mtu ambaye alikuwa na imani kuwa ndiye angeweza kuwaongoza katika ufumbuzi wa ile kesi, lakini lile gari likaporomokea korongoni kabla hajalifikia.

Brian alikimbia hadi kwenye ukingo wa lile korongo, na aliwahi kulishuhudia lile gari likianguka kuelekea chini kwenye lile korongo, likizidi kuwa dogo kadiri lilivyozidi kupotea korongoni, kisha akasikia kishido hafifu wakati lile gari ilipojikita mwisho wa lile korongo, kiasi cha mita mia mbili kwenda chini.

“Oh my God…!”

Alirudi mbio kuelekea kule alipoangukia Inspekta Dilunga, akili ikimzunguka. Aliwakuta askari wenzao wakiwa wamejirundika kando ya ile barabara.

“Dilunga…?” Aliwauliza kwa kiherere, jasho likimtoka na mishipa ya shingo ikiwa imemtutumka

“Tunasikitika afande…Inspekta Dilunga ameangukia kwenye mporomoko mrefu kando ya barabara…”

“Whaat…?”

“Ndio afande…”

“Sasa ndio kusema…?” Aliwauliza kwa jazba.

“Itabidi tupate msaada maalumu wa waokoaji wa kwenda huko chini afande. Ni korongo refu sana hili…na hatari…!”

“Oh, My God…OH, MY GOD…!” Inspekta Brian Koba alihamanika vibaya sana.

Alitupa macho kule kwenye korongo alipopotelea Jadu Mfaume, kisha akatazama tena kule alipoangukia Inspekta Dilunga. Akawageukia wale askari waliojirundika pale kando ya mporomoko ule.

“Sasa…ni wateremkaji gani mnaowaongelea nyinyi? Nahitaji waanze kuteremka huko chini sasa hivi…na sasa hivi kwangu maana yake ni sasa hivi!” Alifoka huku jasho likimbubujika, pua, mishipa ya shingo imemtutumka, na macho yamemuiva.

“Afande…tatizo la hapa ni kwamba mawe yaliyokuwa kwenye miporomoko hii hayajajishika kabisa na udongo, ukiweka mguu tu unakwenda nayo, sasa tunahofia kuwa huenda tukaishia kuokoa watu wengi zaidi kutoka huko chini badala ya mmoja…” Mmoja wa wale askari, ambaye alikuwa mtu mzima kuliko wengine, alisema.

“Ndiyo…kwani kila atakayejaribu kushuka huko chini naye ataporomoka tu!” Mwingine alidakia.

Briani alizidi kuchanganikiwa.

“Tunapoteza muda, sasa ni wateremkaji gani hao mnaowazungumzia ambao hawataanguka huko chini?”

“Nimeshaagiza waitwe kwa redio ya kwenye gari afande…ni kikosi cha kuzima moto…” Yule askari mtu mzima alimjibu na Brian alimtazama kwa mastaajabu.Yule askari aliuelewa vibaya ule mtazamo wa Brian, na akaongezea haraka haraka,“…aam, nilipooona tu kuwa Dilunga ameanguka kule bondeni, na yule mhalifu amepotelea korongoni, nilijua kuwa hatutaweza kufanya lolote zaidi, hivyo nikachukua jukumu afande la kuwasiliana na kikosi cha waokoaji kabla sijaja hapa kutazama kilichotokea…najua sikusubiri maelekezo lakini…”

“Usijali afande umefanya vizuri sana… sasa sijui kama umewapa maelekezo ya kutosha kuhusu hali ya hapa, kwani kwa jinsi ilivyo ni kwamba panahitajika vikosi viwili vya uokoaji, kimoja hapa na kingine kule alipotumbukia yule mhalifu…”

“Nimewaleza hali yote kama ilivyokuwa ikitokea afande…”

“Nenda kaongee tena afande…uwasisitizie juu ya hilo!” Brian aliamrisha, na yule askari alikimbia tena kule yalipoegeshwa yale maGari la polisi yaliyokuwa yakilifukuza lile gari alilokuwa akilitumia yule mhalifu wa ajabu.

Dakika tatu baadaye yake askari alirudi na kuarifu kuwa gari mbili za uokoaji zilikuwa zimeondoka kitambo kuelekea eneo lile.

“Good…very good…” Brian alisema huku akitembea huku na huko, akili ikimzunguka, kisha akasimama ghafla na kumwita tena yule askari mtu mzima.

“Sasa hii njia ni nyembamba sana afande…waambie madereva wetu waanze kurudi nyuma na kuyaondoa kabisa eneo hili magari yetu, ili kutoa njia kwa maGari la waokozi pindi yatakapofika, sawa?”

“Ndiyo afande, mara moja afande!” Yule askari alijibu kikakamavu, na wakati huo huo akiwageukia wenzanke, tayari akiwa na mamlaka mapya juu yao, na kuanza kutoa maelekezo yale kwao.

Brian alirudia kuzunguka-zunguka huku na huko eneo lile, wakati yale maGari lakianza kuondolewa eneo lile moja baada ya jingine. Aliona kuwa muda mwingi ulikuwa ukipotea, huku maswali mengi yamkimzingira kichwani mwake.

Kuna uwezakano wa kumpata yule mhalifu kutoka kule chini akiwa hai?

Ingawa yule alikuwa ni mtu wa ajabu kwa namna yake, lakini ule mporomoko ulikuwa mkali na mrefu…hakuna aliyejua ni uwezo gani alikuwa nao yule mtu, lakini kwa binadamu wa kawaida, kuporomoka kutoka pale juu hadi kule chini kilikuwa ni kifo kisicho shaka hata kidogo!

Sasa na Dilunga naye…sijui itakuwaje huko…

Alirudi tena kwenye ukingo wa barabara, sehemu ambapo Dilunga aliangukia, na kutazama tena kule chini.

Hakuona kitu chochote, ingawa aliona kuwa mporomoko ule japo ulikuwa mrefu, haukuwa mkali kama ule wa kule alipoangukia John Smith mtukutu.

Sasa wako wapi hao waokoaji God Damn it?

Na kadri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo alivyozidi kupoteza subira, lakini hakuwa na la kufanya zaidi ya kusubiri. Na wakati akiendelea kusubiri, alienda kule yalipohamishiwa yale maGari lao na kwa kutumia redio ya mawasiliano iliyokuwa kwenye moja ya maGari lake, aliongea na ofisi ya Inspekta Dilunga na kumuomba opareta wa polisi amuunganishe na ofisi ya Superintendent Tib Haggard.

Dakika mbili baadaye alikuwa akimpa habari mkuu wake wa kazi juu ya mambo yote yaliyotokea hadi kufikia muda ule.

“Holy shit, Brian! Ina maana huyo mtu ameangukia kwenye korongo la urefu wa zaidi ya mita mia mbili? Tib Haggard alimaka kwa mshangao.

“Ndivyo nikwambivyo afande…” Brian alimthibitishia mkuu wake wa kazi.

“Basi tumempoteza…hamna namna mtu huyo atakuwa hai, lazima atakuwa amekufa. Lakini hata kama hivyo ndivyo, ni lazima tuthibitishe kwa macho yetu…kwa maana hiyo uthibitishe kwa macho yako lnspekta…” Tib Haggard alisema. Muda huo Brian alisikia ving’ora vya maGari la uokozi yakielekea eneo lile. Aligeuka na kuona yale maGari lakiwasili kwa kasi huku yakitimua vumbi kubwa.

“Kwa jinsi yule mtu alivyonionyesha maajabu, sitashangaa kabisa iwapo tutamkuta bado hai, na ndicho ninachokitaka sasa…sasa afande, naona kikosi cha uokozi ndio kinaingia…naomba nikuache sasa.” Alimuambia mkuu wake wa kazi.

“Okay my boy…endelea. Na…umefanya kazi nzuri sana mpaka sasa, najivunia sana utendaji wako, pamoja na Dilunga pia, natumai hatakuwa ameumia sana au kukutwa na jambo baya zaidi…”

Dakika tatu baadaye, magari matatu yalikuwa yamesimama moja baada ya jingine, katika barabara ile. Mawili yalikuwa ya kikosi cha zimamoto yenye uwezo wa kuokoa watu walionasa juu ya majengo marefu, au kwenye vina virefu, na moja lilikuwa ni la hospitali ya wilaya, likiwa na wahudumu wanne wa hospitali ile, pamoja na tabibu mmoja.

Kwa dakika kumi na tano zilizofuata, eneo lote lile lilicharuka kwa harakati za uokozi. Moja kwa moja Brian Koba alichukua majukumu ya uongozi wa kampeni ile ya uongozi kwa umakini na msimamo wa hali ya juu, akimfanya yule askari mtu mzima kuwa msaidizi wake katika kampeni ile.

Aligawanya ile kampeni katika makundi mawili, kundi la kwanza ambalo ndilo lililokabidhiwa lile gari la kwanza la kikosi cha zima moto, alilielekeza kwenye uongozi wa Inspekta Dilunga, na aliliweka chini ya uongozi wa yule askari mtu mzima, ambaye alikuwa na cheo cha Kostebo.

Kundi la pili la ile kampeni lilipewa jukumu la kwenda kumuokoa yule mhalifu, na kundi hili lilikuwa chini ya uongozi wake yeye mwenyewe.

Wakati lile gari la kwanza likijirudisha kinyuma-nyuma na kuelekeza mkonga mrefu uliokuwa nyuma ya gari lile kule alipopotelea Dilunga, Brian aligeuka na kumuongoza dereva wa gari la pili la uokozi kule alipoangukia mtu ambaye mpaka muda ule alikuwa akimtambua kama John Smith.

Ule mkonga, au “kijiko” kama wenyewe walivyokuwa wakiuita, wa lile gari la kwanza, ulioteremshwa kule kwenye korongo alipoangukia Inspekta Dilunga ukiwa na waokozi wawili waliokuwa wamejifunga kamba maalumuu na ndefu viunoni mwao ndani yake, kamba ambazo zilikuwa zimefungwa kitaalamu kwenye sehemu maalumuu kwenye gari ile ya uokozi.

Kampeni ya kumuokoa Inspekta Dilunga ilikuwa imeanza, na Konstebo Mwakalinga alikuwa amesimama kando ya mporomoko ule pamoja na askari wengine akifuatilia kwa makini kila kilichokuwa kikitokea, kando yake, wahudumu wawili kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe wakiwa tayari kutoa msaada wowote wa kitabibu utakaohitajika.


Gari la pili lilikuwa tayari kuteremsha “kijiko” chake kule chini alipopotelea yule mhalifu mbaya. Kiongozi wa msafara ule kutoka kwenye kikosi cha Zimamoto, aliteua askari wawili wa kikosi chake na kuwaamrisha kuingia ndani ya kile kijiko, ambacho kingewashusha hadi umbali fulani, kwani kule chini kulikuwa ni mbali sana kuliko uwezo wa kile kijiko cha zima moto kufika. Na kutokea hapo kitakapoishia kile kijiko, wale askari walitakiwa waendelee kushuka wenyewe kule chini kwa kutumia kamba maalumu watakazofungwa viunoni mwao.

“Hapana komredi…na mimi nitakwenda huko chini.” Inspekta Brian Koba alimwambia yule kiongozi wa Zimamoto.

“Eti nini afande?” Yule kiongozi wa zimamoto aliuliza kwa mshangao, kisha hapo hapo akaendelea, “Hiyo haimo kabisa afande, wewe huna ujuzi wa kufanya kazi hizi…ni hatari sana kushuka huko chini. Hii tuachie sisi, wewe kaa pembeni…”

“Komredi, sina muda wa kubishana nawe saa hizi. Si wewe wala hao watu wako, ambaye ana ujuzi wa namna ya kukabiliana na mhalifu aliyeko huko chini, kwa hiyo nakuagiza wewe ukae pembeni na unitazame jinsi ninavyoteremka huko chini na mmoja wa vijana wako, tumeelewana?” Brian alimjibu huku akimtazama kwa macho makali.

Yule jamaa alimkodolea macho kwa mshangao.

“Yaani we’ unategemea kukuta mtu akiwa hai huko chini afande…?” Alimuuliza huku akimtazama kama kwamba alikuwa ana wazimu. Badala ya kumjibu, Brian alianza kujifunga mwenyewe kiunoni mwake ile kamba ya kuteremkia kule chini, huku bastola yake ikiwa imewekwa thabiti kwenye mfuko wa suruali yake iliyojaa vumbi na iliyochanika magotini.

“Basi angalau acha tukusaidie kufunga hiyo kamba afande…” Hatimaye yule jamaa alisema na kuanza kumsaidia kumfunga ile kamba kiunoni.

Brian alitulia kimya huku macho yake yakitoa mng’ao wa dhamira isiyoyumba katika alilokusudia kulifanya.

Dakika tano baadaye, Brian Koba na askari mmoja wa kikosi cha zima moto waliteremshwa taratibu kule kwenye korongo, wakiwa katika kampeni ya kwenda kumuopoa yule mhalifu wa aina yake kutoka kule chini.

Okay John Smith…nakuja kukabilina nawe tena sasa, na safari hii kutakuwa na mshindi mmoja tu baina yetu, na nitahakikisha kuwa mshindi huyo si wewe! Brian Koba aliwaza huku akiwa ameuweka mkono wake juu ya mfuko wa suruali yake ambao ndani yake kulikuwa kuna ile bastola yake.

Dakika kumi baada ya Inspekta Brian Koba kuteremshwa kule kwenye lile korongo refu, kiongozi wa wale makamanda wa kikosi cha kuzima moto alipata mawasiliano na wale vijana wake wawili walioteremka kule alipoangukia Inspekta Gezza Dilunga, kuwa wamefanikiwa kumuona yule Inspekta.

Yule kiongozi alimsogelea Konstebo Mwakalinga, kiongozi wa kampeni ya uokozi wa Inspekta Dilunga, huku akiendelea kuongea na wale vijana wake waliokuwa kule chini kwa kutumia redio yao ya mawasiliano.

“…kwa hiyo mtam-mudu wenyewe au mtahitaji msaada zaidi?” Aliwauliza huku akiwa amemkazia macho Kostebo Mwakalinga.

“Nini…kuna taarifa gani…?” Konstebo Mwakalinga aliuliza huku akiwa makini sana, kama jinsi walivyokuwa wale askari wenzake waliojirundika pale kando ya barabara ile nyembamba.

“Inspekta Dilunga ameonekana huko chini. Anaonekana kuwa kwenye hali mbaya…hana fahamu, na vijana wanahofia kumnyanyua wakichelea kumuumiza zaidi…” Yule kiongozi wa kikosi cha uokozi cha zimamoto alimuambia kwa kirefu. Konstebo alionekana kutoielewa ile hali, lakini hapo yule tabibu aliyekuja na wahudumu wa hospitali alidakia.

“Nipe redio niongee nao…” Alimuambia yule kiongozi ambaye bila kusita alimpatia, na kwa kutumia redio ile, yule tabibu aliongea na wale waokozi waliokuwa kule chini.

“Nadhani itanibidi niteremke kule chini wazee…” Hatimaye tabibu alisema. “Kulikoni…?” Konstebo Mwakalinga aliuliza kwa wahka.

“Kwa mujibu wa maelezo yao, Inspekta hana fahamu. Miguu yake imejikunja katika namna ambayo si ya kawaida, na inavuja damu nyingi. Sasa katika hali kama hiyo, ni hatari sana kwa mtu asiye na taaluma ya utabibu kujaribu kumnyanyua majeruhi…” Tabibu alijibu kwa kirefu.

Dakika tano baadaye naye aliteremshwa kule chini, na dakika kumi nyingine, kile “kijiko” cha lile gari maalumu la uokozi la kikosi cha zimamoto kiliibuka taratibu kutoka kule chini, kikiwa na yule tabibu pamoja na mwili usio na fahamu wa Inspekta Gezza Dilunga ndani yake.

Ilifuata pilika-pilika kubwa wakati wale askari na wahudumu wa hospitali waliokuja na yule tabibu wakisaidiana kwa tahadhari kubwa, chini ya usimamizi wa yule tabibu, kumtoa Inspekta Dilunga kwenye kile “kijiko” na hatimaye kumlaza kwenye machela kando ya ile barabara.

Miguu yake ilikuwa imepata majeraha makubwa sana sehemu juu kidogo ya magoti yake na damu nyingi ilikuwa imemtapakaa miguuni na kulowesha suruali yake. Aidha alikuwa na majeraha mengine mengi mwilini na usoni yaliyotokana na kubingirika kwenye ule mporomoko mrefu uliojaa mawe makubwa.

“Oh, Mungu wangu! hii miguu yake vipi Dokta…?” Konstebo Mwakalinga aliuliza kwa fadhaa. Ile miguu ilikuwa imejikunja kwa namna ambayo si sahihi kwa binadamu kuikunja.

“Nadhani imevunjika vibaya sana…” Tabibu alijibu huku akijishughulisha kutoa huduma ya kwanza kwa yule askari jasiri, akisaidiwa na wale wahudumu wake.

“Huyu anatakiwa afikishwe hospitali haraka sana…” Hatimaye yule tabibu alisema akiwa na mashaka makubwa usoni. Ni wazi kwa wale askari wote waliokuwapo pale, kuwa kiongozi wao alikuwa kwenye hali mbaya sana.

“Basi hakuna cha kusubiri hapa…apelekwe hospitali haraka sana…” Konstebo Mwakalinga alisema, na wakati wale wahudumu wakiubeba mwili wa Inspekta Dilunga kuelekea kwenye gari lao, ile redio ya kiongozi wa kikosi cha zimamoto iliita tena, safari hii alikuwa ni yule askari wa zimamoto aliyeteremka korongoni na Inspekta Brian Koba.

“Nakusoma kamanda…nipe hali halisi huko chini!” Aliongea kwenye ile redio huku macho na masikio yote ya wale askari waliokuwapo eneo lile vikiwa kwake.

“Hali ya huku ni utata mtupu kamanda!” Jibu kutoka kule chini lilisikika, sauti ya yule kamanda wa zimamoto ikiwa imejaa wahka na kitetemeshi kikubwa. Wote waliokuwa pale karibu walilisikia jibu lile na kila mmoja akaachia mguno wa mshangao kwa namna aliyoizoea.

“Kwamba…?” Ndio ilikuwa namna ya mshangao aliyoizoea yule kiongozi wa kile kikosi cha kuzima moto, akiwa kinywa wazi.


Inspekta Brian Koba na yule kamanda wa kikosi cha zimamoto waliteremshwa taratibu kule korongoni wakiwa ndani ya boksi kubwa la chuma lililounganishwa mwisho wa ule mkono mrefu wa lile gari la uokozi la kikosi cha zimamoto.

Muda wote wakati wakiteremshwa kule chini, yule kamanda wa zimamoto alikuwa akiwasiliana na dereva wa kile “kijiko” aliyekuwa kule juu kwa redio yake maalumu, akimuelekeza uelekeo wa kukishushia kile “kijiko”, mara akimuelekeza apeleke kulia zaidi au arudishe kushoto kidogo, alimuradi wapate kuteremshwa sehemu iliyo muafaka.

Na wakati yule kamanda akiwa amezama kwenye kuelekezana na yule mwenzake, Inspekta Brian Koba alikuwa akitembeza macho yake kule chini walipokuwa wakielekea kwa makini akijaribu kulitafuta lile gari pale lilipoangukia, lakini bado walikuwa juu sana kiasi cha kutoweza kuona vizuri kule chini, hasa ikichangiwa na baadhi ya miti iliyokuwa huko chini, ambayo kutokea pale alipokuwa, alikuwa akiiona kutokea juu.

Hatimaye walifika sehemu ambapo ule mkono wa lile gari ulikuwa umefika kikomo, na kutokana na maelekezo ambayo yule dereva alikuwa akipewa na yule mwenzake, kile kijiko kiliishia kikiwa kimejiegesha kwenye mgongo wa lile korongo refu.

Na wakiwa wamejiegesha pale kwenye mgongo wa lile korongo, Brian aliweza kuliona lile gari alilokuwa akitumia yule mhalifu majinuni aliyemtambua kwa jina la kubuni la John Smith, likiwa limeanguka kiasi cha kama mita sitini hivi kutoka mwisho wa lile korongo kule chini, ambako kutoka pale walipokomea, bado kulikua mbali sana

“Sasa yatupasa tuteremke kule chini kwa miguu afande, na kitakachotusaidia tusibiringike kama maboga huko chini ni hizi kamba tulizojifunga viunoni…kwa hiyo…” Yule kamanda alianza kumwabia Brian huku akimtazama kwa mashaka, kwani akilini mwake alikuwa na imani kuwa yule askari hatoweza kuteremka kule chini.

Kabla hajamaliza maelezo yake Brian alikuwa ameshateremka kutoka kwenye kile kijiboksi walichokuwa wamesimama ndani na kujiegemeza kwenye ule mgongo wenye mporomoko mkali.

Na hata pale alipokuwa amejiegemeza, mawe yaliyokuwa kwenye ule mporomoko yalianza kuporomoka naye akawa anateleza.

“Heh…afande…angalia bwana!” Yule kamanda alifoka kwa wahka. Brian alimtupia jicho kali, kisha akajiweka sawa. Akakamata ile kamba aliyofungwa kiunoni na kugeuka kule juu ilipopotelea, ambako ilikuwa imefungwa kwenye lile gari lililokuwa likiwatelemsha kule chini.

“Tulia wewe…hizi kamba si ziko imara…?” Alimuambia huku jasho likimtiririka.

“Ziko imara sana, lakini pia zinataka uzoefu na mafunzo…sasa wewe…”

Mara moja Inspekta Brian Koba alianza kuteremka kule chini, akimuacha yule kamanda akiendelea na maelezo yake.

Aliserereka huku na huko kuelekea kule chini, mawe yakiachia chini ya miguu yake, naye akijitahidi kujizatiti huku akiwa ameishika ile kamba ndefu na ngumu.

Nyuma yake, yule kamanda naye alianza kuteremka taratibu na kwa tahadhari kubwa.

Brian ndio alikuwa wa mwanzo kufika kule chini.

Alijifungua haraka haraka ile kamba iliyokuwa kiuononi mwake, macho yake yakiwa kule kwenye lile gari lililolalia ubavu umbali wa mita kama sitini kutoka pale alipokuwapo, likiwa limejipachika baina ya mti mmoja mkubwa na jiwe moja kubwa.

Hatua chache kutoka pale alipokuwa amesimama, aliona vipande vingi sana vya vioo vya gari lile vikiwa vimetawanyika kila upande, na sehemu kubwa ya ardhi kutoka pale vilipotapakaa vile vioo hadi pale lile gari ilipoenda kujikita baina ya mti na jiwe, ikiwa imetifuliwa na mawe yaliyotapakaa eneo lile yakiwa yamechimbuliwa kutokana na msoto wa gari lile baada ya kujipigiza pale chini kutoka kule juu.

“Oh, Mungu wangu, hapa hakuna dalili za uhai kabisa hapa…” Brian aliwaza kwa wasiwasi, moyo ukimuenda mbio.

Kule lilipokuwa lile gari kulikuwa kimya kabisa. Hakukuwa na mtikisiko wala purukushani yoyote,na hii ilizidi kumthibitishia kile alichokuwa akikihofia.

Kwake John Smith alikuwa na faida kubwa akiwa hai kuliko mfu, na hata kama yule mtu alikuwa wa maajabu, kwa umbali ule lilipotoka lile gari hadi kufika pale chini, alitarajia kumkuta akiwa ameumia vibaya sana, na si mfu.

Lakini sasa mbona ukimya huu unakuwa kama huyu mtu wa ajabu naye amekufa…? Amezirai… Au …?

Alianza kulikimbilia lile gari, bastola yake ikiwa mkononi mwake. Na alipofika kiasi cha kama mita nne hivi kutoka pale lilipokuwa lile gari, alipunguza kasi na kuanza kulisogelea kwa tahadhari kubwa, hisia zake zote zikiwa makini, moyo ukimpiga kwa nguvu ndani ya kifua chake. Kwa pale karibu aliweza kuona jinsi lile gari lilivyobondeka na kujifinyanga kiasi cha kukatisha tamaa kabisa.

Jambo la kwanza lililomletea hofu ni pale alipoona, kupitia kwenye dirisha la nyuma la gari lile ambalo lilikuwa limepasuka kioo chote na kuacha uwazi mkubwa mahala ambapo awali palikuwa na kioo, kuwa mle ndani ya gari hakukuwa na mtu…

Mnh! Ni nini hii sasa…?

Alisogea hadi kwenye lile gari akiwa makini mno, akiwa tayari kwa purukushani yoyote itakayotokea, na kuchungulia ndani yake. Jadu Mfaume, kwake John Smith, hakuwemo ndani ya lile gari.

E bwana we!

Inspekta Brian Koba alichanganyikiwa si kidogo.

Itakuwaje huyu mtu atoweke namna hii? Ni kweli walikuwa wamepoteza muda mwingi kule juu wakisubiri yale maGari la kuwawezesha kuteremka kule chini, lakini kwa hali ambayo aliijua kuwa alikuwa nayo yule mtu, asingeweza kuwa ametoka mzima kwenye gari ile na kutoweka. Kwa macho yake alishuhudia risasi mbili za Inspekta Dilunga zikijikita mwilini mwa yule mtu wakati akiwa ndani ya lile gari kabla hajatumbukia kule korongoni, na wakati huo huo yeye mwenyewe alishamjeruhi mguuni kwa risasi yake yenye kulipuka. Sasa ukichangia na kuanguka kutoka kule juu hadi pale chini, na jinsi lile gari lilivyobondeka, suala la yule mtu kutojeruhiwa kiasi kwamba aweze kutoka ndani ya lile gari na kutoweka kwake lilikuwa haliwezekani kabisa.

Lakini ukweli mchungu aliokuwa akiushuhudia ni kwamba yule mtu hakuwemo ndani ya lile gari.

“Afande…” Yule kamanda wa zimamoto alifika huku akitweta.

“Jamaa hayumo humu ndani bwana!” Brian alimwambia kwa mshangao.

“Aaa bwana we…!”

“Kabisa bwana…” Brian alijibu huku akilichunguza lile gari, na eneo lililoizunguka, kwa makini. Hakukuwa na alama zozote za kuonesha ni wapi yule mtu alikuwa ameelekea. Hakuona michirizi ya damu, wala alama za miguu.

Mnh, hii kali…

Ndipo yule kamanda wa zimamoto, alipowasiliana na mkuu wao aliyekuwa kule juu ya lile korongo kumpasha habari juu ya utata uliojitokeza kule chini…


Inspekta Brian Koba alilipekua lile gari kwa muda, na katika upekuzi wake alibaini vitu viwili. Kwanza, ni hakika kuwa John Smith alikuwa amejeruhiwa, kwani sehemu kubwa ya kile kiti kilichokuwa nyuma ya usukani wa gari lile ilikuwa imetapakaa damu nyingi. Hiki kilikuwa kitu kipya kidogo kwake, kwani katika mara mbili alizowahi kumpiga risasi yule mtu, hakuwahi kumuona akitokwa damu na badala yake zilikuwa zikitoka cheche kubwa za umeme zile sehemu ambapo risasi iliupiga mwili wake. Lakini safari hii ametokwa damu…nini maana yake hii? Brian alichekecha akili kujaribu kung’amua juu ya jambo lile.

Yumkini yule mtu alikuwa ameanza kuishiwa zile nguvu zake za kimaajabu pale alipokuwa ameelemewa na yale mashambulizi yao dhidi yake…na hivyo kupoteza kinga iliyokuwa ikizidhibiti risasi zao hapo awali, na kuruhusu risasi za Inspekta Dilunga kumdhuru kama jinsi ambavyo zingeweza kumdhuru binadamu mwingine yoyote.

Mnh, lakini pale hakika Dilunga alicheza…natumai hatakuwa ameumia vibaya kule alikoangukia.

Akarudisha mawazo yake kwenye ile hali iliyokuwapo pale chini. Na kwa mara nyngine ile hisia kuwa yule mtu alikuwa ameanza kuishiwa zile nguvu zake za ajabu, au wakati alipokuwa amewekwa mtu-kati na wale maaskari wawili, alichanganyikiwa kiasi cha kupoteza umakini katika hizo kinga zake za kimaajabu na hivyo kumuwezesha Dilunga kumjeruhi namna ile. Lakini kama hivyo ndivyo, kwa nini sasa hayupo hapa?

Utata mtupu!

Kitu cha pili alichogundua ni kwamba ule mkanda ambao ndio ulikuwa umemshikilia yule mhalifu kwenye kiti wakati alipokuwa akiporomoka kule korongoni, ulikuwa umekatwa kwa kuunguzwa bila shaka na kitu kama mwale wa umeme, kwani ncha ya mkanda ule sehemu ulipokatikia, ilikuwa imeungua na kujifinyanga kama jinsi ambavyo vitambaa vyenye mchanganyiko wa nailoni ndani yake vinavyokuwa pindi viunguzwapo.

Hii ilimaanisha kuwa John Smith alikuwa amejeruhiwa kiasi kwamba hakuweza kuufungua ule mkanda na kujitoa mle ndani ya gari, ndio maana akatumia uwezo wake wa ajabu kuunguza ule mkanda na kujitoa pale kwenye kiti.

Lakini sasa hii pia iliongezea utata kwenye hali ile, kwani sasa ilimaanisha kuwa kama zile nguvu zilitetereka kidogo wakati wa mashambulizi yaliyokuwa yakimuandama, ni wazi kuwa zilirudi tena, na ndio maana akaweza kuukata ule mkanda kwa moto, bila shaka wa umeme…

Utata mtupu!

Jambo moja lilibaki wazi akilini mwa Brian; John Smith alikuwa ameumia sana, lakini yu hai.

Na kama hivyo ndivyo, basi hawezi kuwa ameenda mbali na pale walipokuwa, pamoja na muda waliopoteza kule juu kabla ya wao kufika pale chini.

Na hata wakati wazo lile likipita kichwani mwake, aliona kitu kingine mle ndani ya gari. Kwenye mlango wa dereva uliobondeka, ambao hata hivyo haukuwa umefunguliwa na usingeweza kufunguka kwa jinsi ulivyojifinyanga kutokana na kupigizwa chini kwa lile gari kutoka kule juu, kulikuwa kuna alama ya kiganja cha mkono uliotapakaa damu, bila shaka kabisa kuwa ni wa yule mhalifu balaa. Brian aliitazama kwa makini ile alama na akapata mwanga mpya. Ilikuwa ni alama iliyoonesha alama zote za vidole vya mtu yule, na hapa alijua kuwa iwapo wataweza kubahatisha kuzitambua alama zile, wataweza kupata utambulisho wa mtu yule.

Pia hii ilimjulisha kuwa yule mtu alitoka nje ya gari lile kwa kutumia ule uwazi wa juu ya gari lile uliotokana na yeye kulitawanya paa la lile gari kwa zile risasi zake zenye kulipuka.

Aliinua uso wake na kutembeza macho yake eneo lile walilokuwepo. Mbele yake aliweza kuona mbuga kubwa, ikiwa na majani makavu yaliyoweza kumfikia kwenye magoti, ilhali sehemu kadhaa za mbuga ile zikiwa zimetapakaa mawe makubwa-makubwa, na miti mikubwa iliyotawanyika huku na kule. Hali hiyo ilikuwa hivyo hivyo kulia na kushoto kwake.

Kwa hali ile, kama kungekua kuna mtu akikimbia au kutembea tu umbali fulani mbele, kulia au kushoto kwake, angeweza kumuona hata akiwa umbali mkubwa kutoka pale alipokuwapo, kwani ile mbuga haikuwa na majani marefu kiasi cha kumfunika mtu akiwa wima, labda mtu huyo aamue kutambaa mle mbugani.

“Uko wapi sasa John Smith, eenh…? Where are you, muoga mkubwa wewe?” Alijisemea peke yake kwa sauti ya chini, uso akiwa ameukunja kwa tafakuri, macho yake yakiiangaza ile mbuga iliyotambaa mbele yake, kulia na kushoto, bila mafanikio ya kuona kitu chochote cha kumjulisha juu ya uelekeo wa yule mhalifu aliyeelekea kushindikana. Alimgeukia yule kamanda wa zimamoto, ambaye alikuwa akiendelea kutoa maelezo kwa wale waliokuwa kule juu ya korongo juu ya ule mtihani waliokuta kule chini.

“Komredi…” Alimuita, na yule kamanda alimgeukia, akiacha kuogea na ile redio yake.

“Wewe ni mwenyeji Kisarawe hii, hakuna namna nyingine ya kuweza kufika hapa tulipo tofauti na njia tuliyotumia sisi?”

“Mnh, eeenh…ndio, na…nadhani ipo, unajua hii mbuga yote iliyo mbele yetu ni kama eneo lisilotumika, hakuna watu wanaokuja huku kabisa, ila kutokea ile barabara ya Kazimzumbwi, kuna kijiji kimoja ambacho nyuma yake kuna milima midogo, na nyuma ya milima hiyo ndio inaanzia mbuga hii, na kutambaa mpaka hapa tulipo…”

“Ni kijiji gani hicho kamanda, sema upesi, hatuna muda wa kuendelea kupoteza…”

“Aaam, Chakenge…kijiji cha Chakenge.”

“Una hakika?”

“Come on Inspekta, mi’ nimezaliwa, nimesoma na nimeoa Kisarawe hii hii, najua kila kijiji cha wilaya hii…”

“Okay, mwambie huyo kamanda wako huko juu ampatie Konstebo Mwakalinga redio yake, nataka kuongea naye…” Brian alimuambia huku akinyoosha mkono wake kuipokea ile redio kutoka kwa yule afisa wa kikosi cha kuzima moto.

“Nakusoma Afande…” Sauti ya Konstebo Mwakalinga ilisikika kutoka kwenye ile redio, na mara moja Brian aliuliza juu ya Inspekta Dilunga, Mwakalinga akamueleza kwa kifupi kuwa ameshapelekwa hospitali.

“Oh, vizuri sana…sasa hali ya huku si nzuri, bazazi ametoweka, lakini nadhani yuko kwenye hii mbuga iliyotawanyika hapa chini, na kwa kuwa ameumia, naamini hatakuwa mbali…” Brian alimuambia, na yule Konstebo aliendelea kumsikiliza akiwa kimya, hivyo Brian akaendelea; “…Komredi hapa ameniambia kuwa kuna namna ya kufika huku chini kutokea kule kwenye milima iliyokuwa nyuma ya kijiji cha…” Jina la kile kijiji likamtoka, na haraka yule komredi wa kikosi cha zimamoto akamkumbusha.

“…Chakenge…”

“Enh, Kijiji cha Chakenge…”

“Ni kweli afande…” Mwakalinga alithibitisha.

“Okay, sasa nataka askari watumwe haraka kutokea kwenye hicho kijiji na nyuma ya milima hiyo, waanze kuichambua hii mbuga kutokea huko kuja huku, na wateremshwe askari wengine huku chini, nao waanze kuichambua mbuga hii kwenda huko kwenye hiyo milima, tutakutana katikati…na wakati tunakutana, tutakuwa tumeshamkuta huyu jamaa, hatakuwa mbali…”

“Wateremke huko chini afande…?” Mwakalinga aliuliza kwa mshangao.

“Sasa ulitaka wateremke wapi…? Waje huku chini kama tulivyokuja sisi, tena waanze kushuka sasa hivi!”

“Ndio afande!Mara moja afande…!”

“Mara moja haitoshi afande! Hapo ni kitendo bila kuchelewa! Nataka ufanye mawasiliano na makao makuu ya wilaya ili watume vikosi vya askari kuelekea Chakenge…faster…na vikosi hivyo viwe na mbwa wa kutosha…huu sasa ni msako mkubwa na kabambe…ni manhunt hii sasa…lazima huyu mtu apatikane na lazima apatikane leo hii, upo?” Brian Koba alifoka kwenye ile redio.

“Ndio afande…”

“Na nataka vijana wa kuchukua alama za vidole wafike hapa…wateremke huku chini na wachukue alama za vidole kutoka kwenye hili gari kwa uchunguzi zaidi, okay?”

“Okay…yaani…Yes Sir afande…mara moja afan…” Konstebo Mwakalinga alijibu kwa wahka, lakini Brian alimjia juu.

“Mara moja haitoshi askari…! Changamkia utekelezaji wa maelekezo sasa hivi, na ulete taarifa ya maendeleo upesi!”

“Sir…!” Konstebo Mwakalinga alibweka kutii amri na kumaliza mawasiliano na mkuu wake wa kazi kwa wakati ule, jasho likimvuja na macho yakimuwiva kadiri sekunde zilivyokuwa zikipita.

Dakika kumi baadaye, askari wengine wawili waliteremshwa kule chini kwa kutumia kile kijiko kama jinsi walivyoshuka akina Brian, na mara moja Brian aliwapanga upande mmoja wa mbuga ile, akiwaambia wasubiri askari wengine watakaoshushwa kule chini ili waungane nao na waanze msako kuelekea kulia kwa mbuga ile kwa kama kilometa mbili, kisha waanze kupanda kuelekea kule mbele kwenye kijiji cha Chakenge.

“Wengine watatawanyikia upande wa kushoto na wengine wataanzia hapa na kwenda moja kwa moja mbele yetu hadi huko kwenye kijiji cha Chakenge.” Brian alimalizia.

Dakika kumi nyingine, wakati askari wengine wawili walishushwa kule chini, Brian alipokea mawasiliano kutoka kwa Konstebo Mwakalinga.

“Askari wataalamu wa alama za vidole wako njiani kuelekea eneo la tukio afande…”

“Safi, endelea…”

“Vikosi vitatu vya askari sita kila kimoja vimeondoka wilayani kuelekea Chakenge, kila kikosi kina mbwa wakubwa wawili…”

“Safi…”

“Kwa maelezo niliyopata kutoka makao makuu ya wilaya, ni kwamba vikosi viwili vitaingia mbugani kutokea kulia kwa milima iliyokuwa nyuma ya kijiji kile, wakati viwili vitaiingia mbuga kutokea kushoto, na viwili vitaiingia mbuga kutokea katikati …”

“Good…very good, namna hiyo tunamzingira mhalifu kutokea kila upande, kama jinsi nilivyoelekeza huku chini. Good work afande. Sasa kama huko hakuna la zaidi, na najua hakuna la zaidi, nakuhitaji na wewe huku chini, quickly…!”

“Mara moj…Ndi-ndio afande, nashuka sasa hivi afande!”

Ndani ya saa moja iliyofuata, wataalamu wa kuchukua alama za vidole walikuwa wamewasili eneo lile na kufika kule chini.

Brian aliwaelekeza sehemu alizotaka watilie maanani katika uchunguzi wao kwenye gari ile, na askari wengine walioteremshwa kule chini walikuwa wameshatawanywa mle mbugani kutokea chini ya lile korongo kuelekea kule ilipoaminika kuwa mhalifu John Smith alikuwa amekimbilia, akiwa amejeruhiwa, kutoka pale lilipoangukia lile gari.

Mawasiliano ya redio yalikuwa yakiendelea baina ya vile vikosi vilivyotokea pale chini ya lile korongo, na vile vilivyokuwa vikitokea kule kwenye kijiji cha Chakenge.

Msako mkali dhini ya mhalifu aliyebatizwa jina la John Smith ulikuwa umeanza, na Inspekta Brian Koba alikuwa katikati ya msako ule, dhamira yake ya kumtia tena mbaroni mtu yule wa ajabu ikiwa moto moyoni mwake.

Bado niko na wewe tu John Smith, au yeyote uwaye…na nitakupata tu, bloody fool!

Aliwaza huku akisonga mbele taratibu baina ya askari wenzake katika mbuga ile, jua kali la mchana mchanga likimchoma, jasho likimtiririka.

Msako uliendelea mpaka saa kumi alasiri, wakati vile vikosi vya askari kutokea kule kijijini Chakenge na kule chini ya lile korongo la maafa vilipokutana katikati ya mbuga ile.

Jadu Mfaume, a.k.a. John Smith, hakuonekana, na Brian Koba alizidi kuchanganyikiwa.

Inayumkini vipi hii…?

Ndani kabisa ya moyo wake, Brian Koba alijua kuwa kwa John Smith, hilo lilikuwa linayumkini kabisa.

Vikosi vyote vilirejea hadi kijiji cha Chakenge vikiwa mikono mitupu, askari na mbwa wao wakiwa wamechoka taabani. Kumsaka Jadu Mfaume, kwao John Smith, ilikuwa ni sawa na kujaribu kutafuta sindano kwenye mbuga ile kubwa.

Jua lilikuwa likizama wakati Brian Koba na askari wenzake, wakiwa hoi na wenye njaa, walipoparamia maGari laliyokuja na vile vikosi kule Chakenge, na kuanza safari ya kurudi wilayani Kisarawe.

John Smith alikuwa ametoweka mithili ya vumbi katika upepo mkali.


ITAENDELEA

Utata wa 9/12 Sehemu ya Tano

Also, read other stories from SIMULIZI;

Leave a Comment